HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU 0%

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU Mwandishi:
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi: Tarehe

 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi: Jopo La Waandishi Wa Vitabu Vya Kiada
: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI
Kundi:

Matembeleo: 8633
Pakua: 2661

Maelezo zaidi:

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 8633 / Pakua: 2661
Kiwango Kiwango Kiwango
 HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

HISTORIA NA SIRA ZA VIONGOZI WAONGOFU

Mwandishi:
Swahili

SOMO LA KUMI NA MBILI: SIFA ZA IMAM ALI (A.S) NA MWONEKANO WAKE

URAFIKI

Laiti kama si mafuriko makubwa ya urafiki wa kweli na huruma iliy- ojaa na kumwagika ndani ya nafsi yake basi Ali(a.s ) asingechagua urafiki penye uadui. Kwa ajili hiyo wanahabari waaminifu kuanzia wafuasi wake hadi adui zake wamepokea kuwa: Pindi Zubayri na Talha walipong’ang’ania kumpiga vita, wakakataa kumtii huku wakimtuhumu katika tukio mashuhuri la vita vya ngamia (Jamal) Ali(a.s ) aliwaendea akiwa hajajiandaa kwa vita, hana ngao wala silaha huku akiwaonyesha amani aliyodhamiria, kisha akanadi:

“Ewe Zubayri! Njoo kwangu”. Zubayri akatoka akiwa amejiandaa kwa vita akiwa na silaha. Aisha alipomsikia Ali(a.s ) akapiga kelele akisema: “Eee vita.”

Alipiga ukulele huo kwa kuwa kwa uchache alikuwa hana shaka kuwa hakuna kipingamizi isipokuwa ni Zubayri kuuawa, kwani anayepambana na Ali(a.s ) bila kizuizi huuawa hata kama atakuwa ni shujaa mkubwa wa namna yoyote ile au akawa na ujuzi wa juu wa kivita wa kiwango chochote kile.

Lililomshangaza sana Aisha na waliomzunguka ni wao kumwona Ali bin Abu Talib(a .s ) akimkumbatia Zubayri kwa muda mrefu, kwa kuwa sababu za mapenzi ya kweli haziishi ndani ya moyo mkubwa kama huu. Imam Ali(a.s ) akaanza kumuuliza Zubayri kwa lugha ya urafiki wao wa zamani akisema:

“Jihurumie ewe Zubayri, hivi ni kitu gani kilichokutoa uje kunipiga vita?” Akajibu: “Damu ya Uthman.” Imam akasema: “Mwenyezi Mungu amuuwe aliyetuchonganisha kwa damu ya Uthman.” Hapo Imam akaanza kumkumbusha ahadi zao, urafiki wao na siku za undugu wao wa zamani. Na huenda Ali(a.s ) alilia sehemu kama hii, lakini Zubayri aliendelea kumpiga vita Imam Ali(a.s ) mpaka Zubayri alipouawa huku kifo chake kikimkarahisha yule aliyemuuwa mwenye kujali upendo Ali bin Abu Talib(a.s ) .[181]

HURUMA YA ALI (A.S)

Imam Ali(a.s ) alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu laiti nikipewa mbingu saba na vyote vilivyo chini yake eti ili tu nimwasi Mwenyezi Mungu kwa kumnyang’anya mdudu chungu punje ya shairi, sitofanya, na hakika dunia yenu hii ni dhalili kwangu kuliko jani lililomo mdomoni mwa nzige.”[182]

Ali(a.s ) ndiye mwenye maagizo mazuri aliyoyatuma kwa Al-Ashtar An-Nakhaiy gavana wake wa Misri na watu wake. Ndani ya maagizo hayo amesema: “Usiwe mnyama mkali mwenye kushambulia unayetumia fursa kwa ajili ya kuwala wao. Kwani hakika wao wako katika makundi mawili: Ima ni ndugu yako katika dini au ni kiumbe mwenzako, hivyo wape msamaha wako kama unavyopenda upewe msamaha na Mwenyezi Mungu. Wala usijute kwa msamaha wowote utakaotoa, wala usijivune kwa adhabu yoyote utakayotoa.” Kisha akamwambia: “Jizuie kujilimbikizia.”[183]

Hakika ukali wa Ali(a.s ) katika kuzuwia kujilimbikizia ulikuwa ni sababu kubwa ambayo ilipelekea kutokea yaliyotokea kati yake na Muawiya na jamaa zake, kwani hakika hawa walitaka ufalme, mali na utajiri kwa ajili ya nafsi zao huku Ali(a.s ) akitaka hayo yote yawe kwa ajili ya raia wote.

Huruma iliwafikia watu wote akawasamehe dhidi ya yale wanayoya- tenda, hivyo watu wa Basra walimpiga vita, wakaupiga kwa mapanga uso wake na nyuso za wanae, wakamtukana na kumlaani, lakini alipowashinda hakuwauwa na akawa kawaingiza katika amani yake. Na aliusia kutendewa wema yule mwovu muuaji wa nafsi yake Ibnu Muljim.

UADILIFU WA ALI (A.S)

Si ajabu Ali(a.s ) kuwa mwadilifu kuliko watu wote bali ajabu ni kama hatokuwa hivyo. Kati ya mambo yanayoelezea uadilifu wake ni kuwa alikuta ngao yake kwa mkiristo mmoja wa kawaida, hivyo akampeleka kwa Kadhi ambaye jina lake ni Sharihu ili aweze kumhukumu na kumtolea maamuzi, hivyo waliposimama wote waw- ili mbele ya Kadhi, Imam Ali(a.s ) alisema: “Hakika ni ngao yangu sijaiuza wala sijaitoa zawadi.”

Hapo Kadhi akamuuliza yule mkiristo: “Unasemaje kuhusu aliyoyasema kiongozi wa waumini?” Akajibu: “Hakuna ngao isipokuwa ni ngao yangu, na kiongozi wa waumini kwangu si mwongo”. Hapa Kadhi Sharihu akamuelekea Ali(a.s ) na kumuuliza: “Je una mashahidi watakaothibitisha kuwa hii ni ngao yako?” Ali(a.s ) akatabasamu na kusema: “Sharihu umepatia, sina mashahidi.”

Hivyo Sharihu akahukumu kuwa ngao ni ya yule mkiristo na hapo akaichukua yule mkiristo na kuondoka huku kiongozi wa waumini akimtazama.

Isipokuwa baada ya hatua chache yule mkiristo akarudi huku akise- ma: “Hakika mimi nakiri kuwa haya ni maadili ya manabii, yaani kiongozi wa waumini ananipeleka kwa Kadhi ili ahukumiwe yeye!” Kisha akasema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu hakika ngao hii ni ngao yako ewe kiongozi wa waumini, na mimi nilisema uongo katika madai yangu.” Baada ya muda watu walimwona mtu huyu akiwa pembeni mwa Imam Ali(a.s ) akiwa ni askari wake mwaminifu na komandoo wake mkubwa akipambana vikali katika vita vya Nahruwani dhidi ya waasi (Khawariji).[184]

Usia wa Imam Ali(a.s ) na barua zake kwa magavana wake, zote zinakaribia kulenga lengo moja nalo ni uadilifu, hivyo watu wote wa mbali na karibu hawakumkubali isipokuwa ni kwa sababu alikuwa ni kipimo cha uadilifu, kipimo ambacho hakikuelemea kwa mtu wa karibu wala hakikumpendelea mtawala, hakikuhukumu isipokuwa haki tupu.

Ama Uthman bin Affan ambaye alitawala dola kabla yake hakika aliachia huru mikono ya ndugu zake wa karibu, wasaidizi wake na swahiba zake wafanye watakavyo katika kila sekta ya vyeo na mali huku akiongozwa na mawazo mabaya ya siri, na hasa Mar’wan ndiye aliyemuathiri sana katika mawazo. Hivyo ilipofika dola mikononi mwa Imam Ali(a.s ) hakutaka chochote isipokuwa ni kuwafanyia uadilifu, akawavua utawala baadhi yao akawaondoa kwenye vyeo na kuwatenga dhidi ya ujilimbikiziaji wa mali huku akipambana na kila aliyetaka kugeuza dini kwa lengo la kujimiminia mali, vyeo na mamlaka nyumbani kwake kwa kuitoa dini kwenye msitari wake.

Mara kwa mara alikariri kauli yake nzuri masikioni mwa watu hawa akisema: “Mimi ninajua litakalowafaa na kunyoosha mapindo yenu, lakini haifai niwatengenezee hali zenu kwa kuiharibu nafsi yangu.”[185]

UKARIMU WA IMAM ALI (A.S)

Imam Ali(a.s ) alikuwa mkarimu sana na mwenye mkono mkunjufu kuliko watu wote, kwani alikuwa akifunga na inapofika wakati wa kuftari anachukua chakula chake na kumpa mtu huku akibaki na njaa, hivyo Aya hizi zikamshukia yeye na familia yake: “Na huwalisha chakula masikini na yatima na mfungwa hali ya kuwa wanakipenda.* Tunakulisheni kwa ajili ya radhi ya Mwenyezi Mungu tu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani.”[186]

Wafasiri wamepokea kuwa alikuwa hamiliki isipokuwa dirhamu nne, hivyo akatoa sadaka dirhamu moja usiku na nyingine mchana, na dirhamu nyingine kwa siri na ya nne kwa dhahiri hapo ikateremshwa Aya: “Wale watoao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, basi wana malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.”[187]

Imepokewa kuwa alikuwa akimwagilia maji mitende ya mayahudi huko Madina mpaka mkono wake unatoa uvimbe lakini apatapo malipo huyatoa sadaka huku akibakia na njaa akifunga jiwe juu ya tumbo lake.

UKWELI NA NIA NJEMA YA IMAM ALI (A.S)

Alifikia kiwango cha juu cha nia njema, kiasi kwamba kutokana na nia hiyo njema akapoteza utawala wa dola, na laiti kama katika hali fulani angebadili nia yake njema basi asingepata adui, wala rafiki zake wasingegeuka adui dhidi yake.

Kuna kipindi maswahaba wakubwa muhajirina walijikusanya kwake kwa lengo la kutaka kumkinaisha kwa kumpa njia ya kumwondoa Muawiya, amuundie jambo la ghafla litakalommaliza, lakini aliwakatalia wote akijiepusha dhidi ya njama hiyo.

Baada ya Imam Ali(a.s ) kupewa kiapo cha utii cha kuongoza dola alikuja Al-Mughira bin Shu’bah ambaye alijulikana kwa ujanja, njama na mitego, akamwambia Ali(a.s ) : “Hakika wewe una haki ya kutiiwa na kunasihiwa, na mawazo ya leo huzaa yatakayokuja kesho, na upotovu wa leo hupoteza yaliyotakiwa kesho, hivyo mwache Ibnu Amir katika kazi yake, na Muawiya katika kazi yake na watumishi wengine katika kazi zao ili watakapokutii na askari wao wakakupa kiapo cha utii basi ndipo ubadili utakayembadili na umwache unayemtaka.” Imam akanyamaza kwa muda kisha akatangaza kuikataa njama hiyo akisema: “Sidanganyi katika dini yangu wala sifanyi la udhalili katika jambo langu.”[188]

Pindi njama na ujanja wa Muawiya ulipodhihiri Imam alitoa ibara ifuatayo ambayo inafaa kuwa mfano bora wa maadili mema ya hali ya juu, alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakika Muawiya si mjanja kuliko mimi, lakini yeye anadanganya na kutenda maovu, hivyo laiti kama si kuchukia udanganyifu basi mimi ningekuwa mjanja kuliko wote.”[189]

Amehimiza kukazania nia njema katika hali yoyote ile akasema: “Alama ya imani ni kutanguliza ukweli japo unakudhuru, na kuuacha uwongo japo unakunufaisha.”[190]

KUJIAMINI KWA IMAM ALI (A.S)

Sifa zote hizi nzuri ziliungana na sifa nyingine ya kupendeza ya kujiamini, ambayo Imam alifahamika kwayo. Bali kujiamini ni kitu kinachoshikamana na sifa hizi, hivyo Imam anatenda huku akiwa na matumaini na uzuri wa matendo yake, huku akidhihirisha haki wazi wazi, kiasi kwamba hata shujaa wa Bara la Uarabu Amru bin Abdul Wuddi hakumzuia kudhihirisha haki huku Mtume(s.a.w.w ) na maswahaba wakimtahadharisha dhidi ya Amru. Hiyo ni dalili inayoonyesha kujiamini kwake na ushujaa wake mbele ya haki, vitu ambavyo vilijaa ndani ya nafsi yake.

Mara nyingi amekuwa akitoka kuelekea kwenye swala bila ya kusindikizwa na mtu atakayezuia hatari za maadui mpaka Ibnu Muljimu alipomkuta na kumpiga kwa upanga wenye sumu. Je, huu si ushahidi juu ya kujiamini kwake mbele ya haki, kujiamini ambako kunaendesha viungo vyake vyote na mwenendo wake wote.

Kutokana na kujiamini huku kuzuri ndio maana anamwambia swahaba wake na gavana wake huko Madina Sahlu bin Hunayfa Al-Answariy kuwa: “Ama baada, zimenifikia habari kuwa watu kati ya wale waliokuwa kabla yako wanakwenda kwa Muawiya kwa siri, hivyo usihuzunike kwa idadi yao itakayokupita wala kwa mchango wao utakaokutoka, kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu wao hawa- jakimbia toka kwenye ujeuri wala hawajajiunga na uadilifu.”[191]

MUHTASARI

Huruma ya kutekeleza ahadi ni huruma ya kina kwa Imam Ali(a.s ) , huruma ambayo ilikuwa imejenga moyo wake huku ikidhihirika katika matendo na mienendo yake, hiyo ni hata mbele ya adui yake.

Akitarajia kuwaongoza waliopotea na kuwarudisha katika njia sahihi wale waliokengeuka.

Ama kuhusu uadilifu ni kuwa laiti kama ungejitokeza kwa mtu basi angekuwa ni Ali bin Abu Talib(a.s ) na wala si mwingine, kwani alikuwa ni nguvu kali ya kutekeleza uadilifu kwa watu wote. Alikuwa ni mjuzi anayemjua mwanadamu, jamii na kanuni za Mwenyezi Mungu, hivyo kidole chake hakikuacha haki na uadilifu kwa maana yote ya uadilifu na vipengele vyake vyote katika maisha.

Kila kitu katika utu wa Imam Ali(a.s ) kimekamilika na chenye muundo mmoja, kwani hatupati tofauti yoyote katika sifa zake na mwonekano halisi wa utu wake, hivyo akastahiki kuwa alama kati ya alama za utukufu wa Mwenyezi Mungu na mfano bora kwa wanadamu wote katika kumtii Mwenyezi Mungu, na kujenga imani ya Mwenyezi Mungu, kifikira, kimwenendo na kihuruma, hivyo yeye ni mfano mwema wa mtawala shupavu na mtawaliwa mwaminifu mtiifu, na yeye ni sura halisi ya nia njema, utiifu, ibada na nguvu ya haki.

Imam Ali(a.s ) alikuwa mkarimu sana kuliko watu wote huku akiwa na mkono mkunjufu. Alikuwa na ukarimu wa hali ya juu huku akijitofautisha kwa kuwa na moyo salama usiokuwa na chuki hata kwa maadui zake, hivyo hakuridhia jambo mbadala lichukue nafasi ya ukweli, kikauli au kivitendo.

Sifa zote hizi ziliungana na sifa ya kujiamini mbele ya haki kwa kiwango cha juu.

Mwana wa Abu Talib alijitofautisha na wengine kwa jihadi iliyoende lea katika vipindi vyote vya maisha yake yote huku akiwa na maadili bora na mtazamo wa ndani wa makini uliyonyooka, akiwa na ubainifu safi na utambuzi wa haraka na nguvu za kupambana, hivyo akawa ni kiongozi bora na mfano wa juu baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) katika kila sifa bora.

SOMO LA KUMI NA TATU: URITHI WA IMAM ALI (A.S)

Baada ya Mtume Muhammad(s.a.w.w ) hatupati hazina kubwa yenye rutuba iliyokamilika na iliyo maarufu kama hazina aliyoiacha Imam Ali bin Abu Talib(a.s ) . Na ya kwanza ni hazina inayojulikana kwa jina la kilele cha fasaha, yaani Nahjul-balaghah. Ya pili ni ijulikanayo kwa jina la hekima bora na makusudio ya maneno, yaani Ghurarul- Hikam wa Durarul-Kalim.

Kamusi za maudhui ya vitabu hivi viwili vya thamani zimetupa sura ya wazi na halisi kuhusu ukubwa na upana wa hazina hii. Kuanzia ujazo wake, kina chake hadi mjumuisho wake uliojumuisha sekta mbalimbali za maisha ya mwanadamu, kuanzia kijamii hadi mtu mmoja mmoja.

Sisi hapa tumechagua toka kwenye hazina hii kubwa maudhui mbili muhimu zenye uhusiano wa karibu na mtu mmoja mmoja hadi jamii nzima.

HALI HALISI YA WEMA NA UOVU

AKHERA NDIO KUFAULU KWA WATU WEMA

Tutakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu ndipo wema na uovu utabainika. Utamu wa Akhera huondoa makali ya uchungu wa mateso ya dunia.

MTU MWEMA

Mwema ni yule anapoogopa adhabu hujisalimisha, na anapotarajia thawabu hutenda mema. Inatosha mtu kuwa mwema kwa kuaminiwa katika mambo ya dini na dunia.

Ni mwema wa hali ya juu sana yule ambaye moyo wake umekutanishwa na ubaridi wa yakini. Hawi mwema ambaye ndugu zake ni waovu. Mwema ni yule anayedharau asichokipata.

VINAVYOPELEKEA MTU KUWA MWEMA

AKILI NA MAARIFA

Atakayeuwa ujinga wake kwa kutumia elimu yake basi amefaulu kwa kupata hadhi ya juu ya wema. Atakayemfahamu vizuri Mwenyezi Mungu basi daima hatokuwa muovu.

IKHLASI NA UTIIFU KWA MWENYEZI MUNGU

Atakayemtii Mwenyezi Mungu milele hatokuwa muovu. Mtu huwa hawi mwema isipokuwa kwa kumtii Mwenyezi Mungu. Mwema ni yule ambaye utiifu wake una ikhlasi.

Harakisha kutii utakuwa mwema. Mtu yeyote hawi mwema isipokuwa kwa kusimamisha sheria za Mmwenyezi Mungu.

Kukesha usiku katika hali ya kumtii Mwenyezi Mungu ni mavuno ya mawalii na ni bustani ya watu wema. Mkesho wa macho kwa kumtaja Mwenyezi Mungu ni fursa ya watu wema na utakaso wa mawalii.

BIDII KATIKA KUITENGENEZA NAFSI

Atakayepiga vita nafsi yake katika kutafuta wema wake basi atakuwa mwema.Hakika nafsi ambayo inajitahidi kung’oa mabaki ya matakwa itapata inalolitafuta na itapata wema katika marejeo yake.

JIHADI KATIKA NJIA YA MWENYEZI MUNGU

JIHADI NI NGUZO YA DINI NA NJIA YA WATU WEMA

Utawa Dhidi Ya Dunia Isiyodumu

Hakika dunia hutolewa na hukataliwa, hivyo watu wema huachana nayo, huku waovu huitamani. Jiepushe na dunia utapata wema katika marejeo yako na yatakuwa mema mafikio yako.

WATAKAOPATA WEMA WA DUNIA KESHO NI WALE WANAOIKIMBIA LEO.

Ikiwa kweli mnatafuta neema basi ziacheni huru nafsi zenu toka nyumba ya uovu.

UZURI WA KUJIANDAA NA KIFO

Jitahadhari na mauti, yaandalie maandalizi mazuri utapata wema kati- ka marejeo yako.

KIFO KINA RAHA KWA WATU WEMA

KUITATHMINI NAFSI

Atakayeitathmini nafsi yake atakuwa mwema.

KUKITAFUTA KILICHOKUPOTEA

Kutafuta mwishoni mwa umri wako kile ulichokipoteza mwanzoni mwa umri wako hukufanya uwe mwema katika marejeo yako.

KUKAA NA WANAVYUONI

KAA NA WANAVYUONI UWE MWEMA

Kutoa Katika Njia Ya Mwenyezi Mungu

Mkarimu husifiwa hapa duniani na hupata mema huko Akhera. Ukitoa mali yako kwa ajili ya Akhera yako kisha ukamwachia Mwenyezi Mungu yule aliyekuja baada yako, utakuwa umepata wema kwa yale uliyotoa na umeutendea wema urithi wako kwa yule uliyemwachia.

Aliye Mwema Kuliko Wengine

Ukitamani kuwa mwema kuliko wengine basi yafanyie kazi yale uliyoyajua.

Mwema zaidi kwenye kheri ni yule anayetenda kheri.

Mwema zaidi kuliko watu wengine ni yule muumini mwenye akili. Mwema kuliko watu wengine ni yule mwenye kujihukumu mwenyewe kwa kumtii Mwenyezi Mungu.

Mwema zaidi kuliko watu wote duniani ni yule mwenye kuiacha dunia, na mwema zaidi huko Akhera ni mwenye kutenda kwa ajili ya Akhera.

Mwema zaidi kuliko watu wote ni yule atakayejua fadhila zetu na akajikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kupitia sisi. Akawa na mapenzi ya dhati kwetu, akatenda yale tuliyohimiza na kuamrisha, akaacha yale tuliyokataza, basi mtu kama huyo ni katika sisi na yeye atakuwa pamoja nasi katika nyumba ya kudumu.

MTU MWOVU

Atakayetegemea dunia ndio mwovu asiye na kitu.

ALAMA ZA MWOVU

Miongoni mwa uovu ni mtu kuzuia dini yake kupitia dunia yake. Miongoni mwa alama za uovu ni kuwatendea ubaya watu wema. Miongoni mwa alama za uovu ni kumlaghai rafiki.

VINAVYOSABABISHA UOVU

Upumbavu ni uovu. Nia mbaya ni uovu. Kulimbikiza haramu ni uovu.

Mtu hawi mwovu isipokuwa kwa kumwasi Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa uovu wa mtu ni shaka kuharibu yakini yake. Sababu ya uovu ni kuipenda mno dunia.

Yule ambaye lengo lake ni dunia basi Siku ya Kiyama uovu wake utarefuka.

Matokeo ya husda ni uovu wa dunia na Akhera. Kupenda mali na shari husababisha uovu na udhalili.

Kitendo cha mtu kudhulumu hapa duniani ni anwani ya uovu wake huko Akhera.[192]

MUHTSARI

Qur’ani imetilia umuhimu mambo yote yanayohusu maisha na mus- takabali wa mwanadamu, hivyo Mtume(s.a.w.w ) na kizazi chake nao wakafuata njia hiyo ya Qur’ani, wakisimama imara kutafsiri makusudio ya Qur’ani na kubainisha ishara na alama zake.

Suala la wema na uovu ni suala la mwanzo kabisa walilotilia umuhimu na kuliashiria, hivyo wakafafanua kipimo cha wema na uovu huku wakifafanua alama na mwonekano wa mtu mwema na mtu mwovu. Waligusia vinavyosababisha wema na uovu, hivyo kwa maelezo hayo wakatoa mfumo kamili wa ukamilifu wa mwanadamu katika maisha.

SOMO LA KUMI NA NNE: URITHI WA IMAM ALI (A.S)

FALSAFA YA UTAWALA NA NIDHAMU YAKE

KWANZA: UTAWALA NI DHARURA YA KIJAMII

Uimamu ni mpangilio wa umma.

Lazima watu wawe na kiongozi, awe mwema au mwovu.

PILI: FALSAFA YA UTAWALA

Utawala Ni Jambo Linalokuja Na Kutoweka

Dola kama inavyokuja ndivyo inavyorudi.

Utawala wenye kuhama wenye kuondoka ni jambo dhalili jepesi.

UTAWALA NI NJIA SI LENGO

Ewe Mwenyezi Mungu, hakika wewe unafahamu kuwa yale yaliyoto- ka kwetu hayakuwa kwa ajili ya kugombania utawala wala kupata chochote kati ya mabaki ya kinachosagika. Lakini yalitoka kwa ajili ya kuhami mafunzo ya dini Yako na kudhihirisha wema katika nchi yako, ili wasalimike wale waliyodhulumiwa miongoni mwa waja Wako na zifanyiwe kazi hukumu Zako zilizoachwa.

Utawala Ni Sehemu Ya Kutahinia Maisha

Akili za watu hutahiniwa kwa mambo sita: Urafiki, mahusiano, utawala, kuvuliwa cheo, utajiri na ufakiri. Uwezo hudhihirisha sifa njema na mbaya.

TATU: MAJUKUMU YA DOLA YA KIISLAMU

Kuuelimisha Umma

Ni wajibu wa Imam kuwaelimisha anaowatawala sheria ya Uislamu na imani yake.

Kusimamia Uadilifu

Uadilifu ni nguzo ya raia. Uadilifu ni nidhamu ya utawala.

Hakuna kinachowapa hali nzuri raia isipokuwa ni uadilifu tu.

Kwa uadilifu hufuatwa sunna za Mwenyezi Mungu na dola huimarika.

Kuihami Dini

Kila dola inayozungukwa na dini huwa haishindwi. Watawala ni watetezi wa dini.

Atakayefanya utawala wake ni kutoa huduma kwa ajili ya dini yake basi kila kitu kitamnyookea.

Kutekeleza Sheria

Kuwalazimisha waja wa Mwenyezi Mungu kutekeleza hukumu za Mwenyezi Mungu ni kutekeleza haki na kila chenye manufaa. Kati ya majukumu aliyobebeshwa Imamu na Mwenyezi Mungu ni kutekeleza adhabu kwa yule anayestahiki.

Kujitahidi Kutoa Nasaha

Imam hana jukumu lolote isipokuwa lile alilobebeshwa toka kwenye amri ya Mola Wake nalo ni kuzidisha mawaidha na kujitahidi kutoa nasaha.

Kuhakikisha Kipato Na Kuboresha Maisha

Ama haki yenu iliyopo kwangu ni kuwanasihi na kuwahakikishieni kipato chenu. Watawala wenye hali nzuri sana ni wale ambao maisha ya watu yan- aboreka wanapoishi nao.

Kulea Umma

Ama haki yenu iliyopo kwangu ni kuwanasihi…..kuwafunza ili msiwe wajinga na kuwaadabisha kama mlivyojifunza.

Kutetea Uhuru Wa Nchi Na Heshima Ya Taifa

Katika mafunzo ya Imamu kwa magavana wake ni kauli hii: “Hifadhini mipaka yao na pembe za nchi zao.” Pia akasema: “Lazima watu wawe na kiongozi…..watakayemtumia kumpiga adui.”

Kuleta Usalama Wa Ndani

Lazima watu wawe na kiongozi…….ambaye kupitia yeye njia zote zitakuwa na amani.

Kuwasaidia Wasiyojiweza

Zaka ya mtawala ni kumsaidia asiyejiweza.

Kujali Ujenzi Wa Nchi

Ubora wa mtawala ni kujenga nchi.

Kuwatetea Madhaifu

Dhaifu huendelea kutetewa dhidi ya mwenye nguvu mpaka mwema atakapostarehe na dhaifu akastarehe dhidi ya muovu.

NNE: SABABU ZA KUDUMU DOLA NA SIFA YA MTAWALA WA KUIGWA

Kufahamu Mambo

Imam anahitaji moyo wenye akili.

Akili iliyojiepusha na machafu huamrisha mema.

Kuifuata Haki Na Kuidhihirisha Vitendoni

Atakayeifanya haki kuwa ndio dira basi watu watamfanya mtawala. Atakayeitawala nafsi yake atapata utawala.

Utawala wako ukipenya hadi ndani ya nafsi yako basi nafsi za watu zitajikusanya kuelekea kwenye uadilifu wako.

Kiongozi bora ni yule ambaye matamanio yake hayamwongozi. Kiongozi mwenye akili sana ni yule anayeitawala nafsi yake kwa ajili ya raia kupitia yale yanayoangusha hoja za raia dhidi yake, Na akawatawala raia kupitia yale yanayothibitisha hoja yake dhidi yao.

Ushujaa Katika Kutekeleza Haki Na Kusimamisha Uadilifu

Imam anahitaji moyo wenye akili na ulimi wenye kauli na moyo mpana ili asimamishe haki nzito.

Nia Njema

Mtawala bora ni yule mwenye vitendo na nia njema, mwadilifu kwa askari wake na raia wake.

Ufasaha Wa Maneno

Imam anahitaji….ulimi wenye kauli.

Ihsani Kwa Raia

Atakayewafanyia ihsani raia wake Mwenyezi Mungu humtandazia mbawa za rehema zake na humwingiza katika msamaha wake. Atakayewafanyia ihsani watu wake anastahiki utawala.

Kueneza Uadilifu Kwa Watu Wote

Nguzo ya utawala ni uadilifu.

Atakayefanya uadilifu utawala wake hupenya.

Aliye mwadilifu katika utawala wake hatohitajia wasaidizi wake. Atakayetenda kwa uadilifu Mwenyezi Mungu atalinda utawala wake. Mwenye kuzidi uadilifu wake siku zake husifika.

Mtawala mwenye maadili bora ni yule anayewajumuisha watu kwa uadilifu wake.

Utawa Wa Nafsi

Mtawala bora ni yule mwenye kuizuia sana nafsi yake.

Mbora ni yule asiyebabaishwa wala kudanganywa huku tamaa hazimlaghai.

Uchumi Na Kuratibu Maisha

Hatoangamia yule mwenye kufanya iktiswadi. Siasa nzuri hudumisha utawala.

Uratibu mzuri na kujiepusha na ubadhirifu ni utawala bora.

Uadilifu Wa Nafsi

Uadilifu dhidi ya nafsi ni pambo la utawala. Zaka ya nguvu ni uadilifu dhidi ya nafsi.

Upole

Msingi wa utawala ni kutumia upole. Siasa nzuri ni upole.

Uvumilivu

Uvumilivu ni msingi wa utawala.

Nguzo ya utawala ni kifua kipana (uvumilivu). Msamaha ni Zaka ya uwezo.

Muadhibu mtumwa wako amwasipo Mwenyezi Mungu lakini msamehe akuasipo wewe.

Utawala wa uadilifu hupatikana katika mambo matatu: Kulainika katika jambo ulilo na uhakika nalo, kulipiza kisasi katika jambo la uadilifu na kumpendelea mwenzio katika jambo ulilokusudia.

Kutetea Dini

Ifanye dini kinga ya dola yako, na shukurani kinga ya neema yako, hivyo kila dola inayozungukwa na dini haishindwi, na kila neema inayokingwa na shukurani hainyang’anywi.

Kujizuia Kwa Bidii

Omba msaada wa uadilifu kwa kuwa na nia njema kwa raia, kupun- guza tamaa na kuzidi kujizuia dhidi ya maasi.

Kuhisi Kuwa Mamlaka Ni Amana Ya Mwenyezi Mungu Iliyo Juu Yako

Hakika mtawala ni muhazini wa Mwenyezi Mungu hapa ardhini. Hakika mamlaka yako si wito wa chakula kwa ajili yako.

Kuwa Macho

Ambaye hayajamdhihirikia akiwa macho hawatomnufaisha chochote walinzi wake.

Miongoni mwa alama za dola ni kuwa macho (kuwa chonjo) ili kulin-da mambo.

Kutojivunia Nguvu

Mwenye hadhi hajivunii cheo alichopata hata kama ni kikubwa namna gani, na dhalili hujivunia cheo chake.

Kuamrisha Yanayowezekana

Ukitaka utiiwe omba yanayowezekana.

Mgao Sahihi Wa Kazi Na Kuainisha Majukumu Ya Kila Mmoja Kila mwanadamu kati ya watumishi wako mpe kazi yake ambayo utamwajibisha kwayo, kufanya hivyo ni bora ili wasitegeane.

Kugawa Wema

Atakayetoa wema wake atastahiki uraisi. Ukarimu ni utawala.

Anayetoa cheo chake husifika. Pambo la utawala ni kuwapendelea watu (kabla ya nafsi yako).[193]

MUHTASARI

Uislamu ulikuja kuanzisha dola ya Mwenyezi Mungu yenye mpangilio wa Mwenyezi Mungu na utawala wa kuigwa ambao utamhakikishia mwanadamu wema wa sasa na wa baadaye. Mtume (s.a.w.w.) kiongozi aliasisi dola na kusimamisha nguzo zake. Ama wasii wake mlinzi wa ujumbe wake alibainisha mafunzo ya dola ya kuigwa baada ya kufukuza uovu baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w ) .

Akabainisha sababu za kudumu dola, kukamilika na kuendelea. Akabainisha sababu za kuporomoka dola, ustaarabu wake na utamaduni wake. Ujumbe wake wa kuigwa aliyoutuma kwa gavana wake wa Misri Malik Al-Ashtar unatoa taswira halisi timilifu ya utaratibu wa utawala wa kiislamu.

SOMO LA KUMI NA TANO: FATIMA AZ-ZAHRAU MAMA WA MAIMAM WATAKASIFU

NASABA YAKE TUKUFU

Hakika kiungo kati ya uimamu na utume ni Fatima binti Muhammad, mama wa Maimam maasumina na mbora wa wanawake wote wa ulimwenguni. Mama yake ni mbora wa wanawake wa kikuraishi, Khadija binti Khuwaylid bin Asad bin Abdul-Uzza bin Quswayy, na yeye ndiye mke wa kwanza wa Mtume(s.a.w.w ) na yeye alitokana na nyumba yenye elimu na sharafu. Hakika kumzaa mtu kama Fatima Az-Zahrah mkweli, mtakasifu na maasumu kunatosha kabisa kuwa utukufu mkubwa kwake.

MAZAZI YAKE MATUKUFU

Tabarasiy ndani ya kitabu Iilamul-Waraa amesema: “Linalodhihiri katika riwaya za wapokezi wetu ni kuwa alizaliwa Makka siku ya ishirini ya mfungo tisa mwaka wa tano tangu Mtume(s.a.w.w ) kukabidhiwa utume, na Mtume(s.a.w.w) alifariki Fatima akiwa na umri wa miaka kumi na nane na miezi saba.”[194]

Imepokewa kutoka kwa Jabir bin Yazid kuwa alisema: “Imam Al- Baqir(a.s) aliulizwa: Fatima aliishi muda gani tangu kufariki kwa Mtume(s.a.w.w) ? Akajibu: “Miezi minne na akafariki akiwa na umri wa miaka ishirini na tatu.”[195]

Hakika hili linakaribiana sana na yale waliyoyapokea wasiokuwa Imamiya kuwa alizaliwa mwaka wa arubaini na moja tangu kuzaliwa Mtume(s.a.w.w) , hivyo atakuwa kazaliwa mwaka mmoja tangu Mtume(s.a.w.w) kukabidhiwa utume.[196]

Mwalimu wetu Abu Said Al-Waidhiy ndani ya kitabu Sharafun-Nabii amesema: “Watoto wote wa Mtume(s.a.w.w) walizaliwa kabla ya Uislamu isipokuwa Fatima na Ibrahim hakika wao wawili walizaliwa ndani ya Uislamu.”[197]

MAJINA YAKE NA LAKABU ZAKE

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar As-Sadiq(a.s) kuwa alisema: “Fatima ana majina tisa mbele ya Mwenyezi Mungu: Fatima, As- Siddiqah, Al-Mubarakah, At-Tahirah, Az-Zakiyyah, Ar-Radhiyah, Al- Mardhiyyah, Al-Muhaddathah na Az-Zahrau.”[198]

Imepokewa kutoka kwa Imam Ridha(a.s) kuwa Mtume(s.a.w.w) alisema: “Hakika binti yangu amepewa jina la Fatima kwa sababu Mwenyezi Mungu amemtenga mbali na moto yeye na yule atakayempenda.”[199]

Mtume(s.a.w.w) alimpa jina la Batul7 kisha akamwambia Aisha: “Ewe mwenye macho mekundu, hakika Fatima si kama wanawake wa kibinadamu yeye hapatwi na siku kama mnavyopatwa na siku .”[200]

Alikuwa akichuruzika maji ya Peponi kwa sababu pindi Mtume(s.a.w.w) alipopelekwa miraji aliingia Peponi akala na kunywa chakula na maji ya Peponi kisha usiku huo huo akarudi na kumwingilia mkewe Khadija na akawa kashika mimba ya Fatima, hivyo mimba ya Fatima ikatokana na maji ya Peponi.[201]

MAKUZI YAKE

Fatima amezaliwa na kutokana na wazazi wawili watukufu, kwani hakuna mtu yeyote ambaye ana baba mwenye athari kama za baba yake, athari ambazo zilibadili sura nzima ya historia, huku ndani ya muda mfupi zikimpeleka mwanadamu hatua za mbali kuelekea mbele. Wala historia haijatusimulia kuhusu mama kama mama yake ambaye alimpa mume wake na dini yake tukufu kila alicho nacho kwa malipo ya kupata uongofu na nuru.

Chini ya kivuli cha wazazi hawa wawili watukufu ndipo alipokulia Fatima Al-Batul, akakulia ndani ya nyumba ambayo imezungukwa na mapenzi ya baba yake ambaye alibeba joho la utume na akavumilia yale ambayo majabali yalishindwa kuvumilia.

VIPINDI VYA MAISHA YAKE

Fatima Az-Zahrau(a.s) aliishi ndani ya misukosuko ya kufikisha ujumbe tangu utotoni mwake, akawekewa vikwazo yeye, baba yake, mama yake na Bani Hashim wengine katika bonde maarufu ilihali wakati vikwazo vinaanza alikuwa hana umri isipokuwa miaka miwili tu.

Vilipoondolewa tu vikwazo baada ya miaka mitatu migumu akakum- bana na msukosuko mwingine nao ni kufiwa na mama yake kisha kufariki ami yake huku akiwa mwanzoni mwa mwaka wake wa sita, hivyo akabakia kama kifuta machozi cha baba yake akimliwaza wakati wa upweke huku akimsaidia dhidi ya majeuri na mabeberu ya kikurayshi.

Mtume akahama kuelekea Madina yeye na Fatima mwingine akiwa ni mtoto wa ami yake Ali(a.s) huku akiwa na umri wa miaka minane, hivyo akabakia na baba yake mpaka alipokutanishwa na mtoto wa ami yake, Ali bin Abu Twalib, hapo ikaanzishwa nyumba tukufu ndani ya Uislamu kwani Fatima aligeuka chombo safi cha kuendeleza kizazi kitakatifu cha Mtume(s.a.w.w) na kheri nyingi waliyopewa kizazi kitakasifu cha Mtume(s.a.w.w) .

Az-Zahrau alitoa mfano bora wa mke na mama ndani ya kipindi kigumu cha historia ya Uislamu, kipindi ambacho Uislamu ulikuwa unataka kuweka njia ya kudumu ya utukufu wa juu lakini ndani ya mazin- gira ya kijahiliya na mila za kikabila zinazokataa uwanadamu wa mwanamke huku zikimhesabu mwanamke kuwa ni aibu. Hivyo ikawajibika kwa Az-Zahrau kutumia mwenendo wake binafsi na wa kijamii ili kuwa mfano halisi wa kivitendo unaojenga mjengo halisi wa mafunzo na hadhi ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu.

Az-Zahrau ameuthibitishia ulimwengu wa wanadamu kuwa yeye ni mwanadamu timilifu ambaye ameweza kuwa alama ya uwezo wa juu wa Mwenyezi Mungu na muujiza wake wa ajabu, hiyo ni kutokana na hadhi, heshima na utukufu aliokuwa nao. Az-Zahrau Al-Batul alimzalia Ali(a.s) watoto wawili watukufu wa kiume nao ni mabwana wa vijana wa Peponi na watoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu: Hasan na Husein Maimam watakasifu, pia alimzalia mabinti wawili watukufu: Zaynabu mkubwa na Ummu Kulthum wapiganaji wawili wenye subira.

Az-Zahrau alimporomosha mwanae wa tano Muhsin baada ya kifo cha baba yake kutokana na matukio ya uadui dhidi ya nyumba yake, nyumba ya utume na uimamu, hapo zikatimia habari za Qur’ani ili- posema:

“Hakika sisi tumekupa kheri nyingi.* Basi swali kwa ajili ya Mola wako na uchinje.* Hakika adui yako atakuwa mkiwa.”

Hivyo yeye Zahrau ndio kheri nyingi ya utume ambayo Mwenyezi Mungu alimpa Mtume wake(s.a.w.w) , isipokuwa Mtume(s.a.w.w) alikuwa anahitaji wenye kujitolea atakaowatoa kwa ajili ya mti wake wenye kustawi ili kuwazima maadui zake ambao tangu mwanzo walisimama kidete kuuwa Uislamu na alama zake.

KIFO CHAKE NA KUOSHWA KWAKE

Az-Zahrau(a.s) alifariki Madina siku ya tatu ya mfunguo tisa mwaka wa kumi na moja. Aliishi siku tisini na tano tangu kufariki kwa Mtume(s.a.w.w) .[202] Wengine wamepokea kuwa aliishi miezi minne. Wengine wakasema siku arubaini. Pia imepokewa kuwa aliishi siku sabini na tano huku wengine wakidai aliishi miezi sita au minane.[203]

Imam Ali(a.s) ndiye aliyemwosha.[204] Imepokewa kuwa Asmaa binti Umays ndiye aliyemsaidia Imam Ali(a.s) kumwosha. Az-Zahrau alikuwa kaacha usia kuwa atakapofariki asioshwe na yeyote yule isipokuwa Ali(a.s) na Asmaa.[205]

MAZISHI YAKE NA ENEO LA KABURI LAKE

Aliswaliwa usiku, na waliomswalia ni Ali(a.s) , Hasan, Husein, Ammar, Mikdad, Aqil, Zubeyr, Salman, Baridah na kundi dogo la Bani Hashim. Kisha kiongozi wa waumini Ali(a.s) akaenda kumzi- ka kwa siri ikiwa ni kutekeleza usia wake kuhusu hilo.[206]

Watu wametofautiana kuhusu eneo la kaburi lake, yupo anayesema kuwa alizikwa Baqii.15 Yupo anayesema alizikwa nyumbani kwake. Bani Umaiyya walipozidi msikitini ikawa ni msikitini.[207]

Yupo anayesema kuwa alizikwa kati ya kaburi la Mtume(s.a.w.w) na mimbari yake.[208] Huenda hili ndilo lililoashiriwa na Mtume(s.a.w.w) aliposema: “Kati ya kaburi langu na mimbari yangu kuna kiunga kati ya viunga vya peponi.”[209] Isipokuwa Tabarasiy amesema: “Kauli ya kwanza iko mbali na usahihi, na kauli mbili za mwisho zinakaribia usahihi, hivyo anayechukua tahadhari katika kumzuru humzuru mae- neo yote matatu.”[210]

MUHTASARI

Fatima Az-Zahrau(a.s) mbora wa wanawake wote na binti wa mbora wa viumbe amekulia chini ya kivuli cha nabii wa rehema na mlezi wa wanadamu, hivyo Mwenyezi Mungu akampenda kutokana na sifa zake bora. Mama yake alifariki huku akipambana na misukosuko kwa ajili ya ujumbe wa Mwenyezi Mungu, hivyo Fatima(a.s) akawa kifuta machozi na liwazo la baba yake.

Alihama kutoka Makka akiwa na mtoto wa ami yake ili aungane na baba yake ambaye alikuwa ameanza kujenga misingi ya dola ya kiislamu iliyobarikiwa.

Mwenyezi Mungu alimteua awe mke wa Ali bin Abu Twalib, hivyo akatoa mfano bora wa mwanamke wa kiislamu, huku akiwa ni chombo safi cha kuendeleza kizazi cha Mtume(s.a.w.w) ambacho kiliendelea kupitia wanae wa kiume mabwana wa vijana wa Peponi, hivyo yeye akawa ni makutano ya utume na uimamu.

Aliishi na baba yake na mumewe ndani ya matatizo yote ya ulinganio wa Uislamu akashirikiana nao katika jukumu la kujenga Uislamu.

Baada ya baba yake alikumbana na dhulma toka kundi lililoacha njia, hivyo akaporomosha (kuharibika mimba) mwanae wa tano kutokana na tukio la uadui alilofanyiwa yeye pamoja na mumewe. Baada ya tukio hilo hakuishi muda mrefu akawa ameungana na baba yake huku akiwa mwenye subira mvumilivu wa maudhi yote yaliyomfika kwa ajili ya ujumbe wa milele wa Muhammad(s.a.w.w) .