NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI0%

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Mwandishi:
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi: VITABU VYA HADITHI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

Mwandishi: SAYYIDI SHARIFU RADHIY
: Sheikh Haruna Pingili
Kundi:

Matembeleo: 7714
Pakua: 2904


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 15 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 7714 / Pakua: 2904
Kiwango Kiwango Kiwango
NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI

NAHJULBALAGHAH JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

101 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

NAYO NI KHUTBA MOJAWAPO AMBAYO NDANI YAKE KUNA MAELEZO YA MAPAMBANO YA KIVITA

“Mstahiki wa sifa ni Mungu ambaye ni wa mwanzo kabla ya chochote. Na wa mwisho baada ya kila kitu. Na kwa umwanzo Wake imelazimu iwe hakuna kilichomtangulia. Na kwa umwisho wake imelazimu iwe hakuna wa mwisho ila ni Yeye. Ninashuhudia kuwa hapana mungu ila ni Allah (tu) wazi wazi na kwa siri, kwa moyo na kwa ulimi.

“Enyi watu! Kunikhalifu kwenu na kuniasi kusiwafanye mnikadhibishe, wala msishawishike kuniasi, wala msikonyezane kwa macho mnaponisikiliza.

Ninaapa kwa ambaye ameipasua mbegu na kumuumba mwanadamu kuwa ambayo nimewaambieni ni kutoka kwa Nabii Al’ummiyyi(s.a.w.w) , Wallahi mfikishaji hakusema uwongo, wala msikilizaji hakuwa mjinga[235] .

Kana kwamba namuona na namuangalia mpotovu mno[236] amepiga kelele Sham (Syria) na amesimika bendera zake mpakani mwa Kuufani - (ni jina la mji wa Kufa) - afunguapo kinywa chake na kushika kasi ukaidi wake na ujeuri (yaani dhulma) wake ardhini kuwa nzito, fitna itawang’ata watu kwa meno yake, na vita mawimbi yake yatachafuka, na siku zitadhihirisha kisir- ani chake, (zitakuwa ngumu) na usiku taabu zake.

Matunda yake yakipevuka, na akianza kuyachuma, na ngamia kuunguruma, na mikuki na panga kumwetuka, fitna korofi itachukuwa nafasi, na itakuwa kama usiku wa giza, na bahari yenye kupigapiga mawimbi yake.

“Hii ni mara ngapi mji wa Kufa unaharibiwa na dhoruba, na kupitiwa na kimbunga. Hivi punde karne itapambana na karne[237] , mazao yaliyosimama yatavunwa na yaliyovunwa yataharibiwa![238] ”.

102 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU MAUDHUI ILEILE YA SIKU YA KIYAMA

“Hiyo ni siku ambayo Mungu atawakusanya waliokuwa kwanza na wa mwisho ili kudodosa hesabu, na kulipwa aamali, wakiwa wanyenyekevu, wamesimama, jasho limewafunga hatamu[239] .

Na ardhi ikawatetemesha[240] , basi mwenye hali nzuri katika wao ni mwenye kuipata nafasi kwa ajili ya nyayo zake, na wasaa kwa yeye kuweza kupumua.”

NA SEHEMU YA KHUTBA HIIHII KUHUSU TAABU ZA SIKU YA KIYAMA

“Ni fitna kama giza la usiku, hakuna kikundi kitachosimama kupambana nayo wala bendera zao kurudishwa nyuma. Atakujieni (hiyo saa) mfano wa ngamia aliyetayari akiwa na hatamu yake na zana zake, muongozi wake yuamhamasisha[241] , na mpandaji wake anambidiisha[242] , watu wake wachocheao vita - mashambulizi yao ni makali, uporaji wao ndio kidogo[243] . Wanaopigana vita katika njia ya Mungu ni kaumu dhalili mbele ya wenye kiburi[244] , wasiojulikana aridhini, na maarufu mbinguni. Ole wako ewe Basrah, pindi kipigo cha adhabu ya Mungu kitapokuangukia! Hakina vumbi wala sauti, watu wako watakabiliwa na umauti mwekundu na njaa yenye rangi ya vumbi.[245] ”.

103 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU KUJIEPUSHA NA TAMAA ZA DUNIA

“Enyi watu! Itazameni dunia mtizamo wa watawa wanaojiepusha nayo, wenye kuigeuzia uso, kwa kweli Wallahi ni punde tu itawaondoa wakazi walioifanya maskani, na kumfadhaisha anayeishi kwa anasa na mwenye kujiamini, kilichogeuka na kiendacho kuzimu hakitorudi, na ambacho kinatarajiwa kuja hakina uhakika, furaha yake ni mchanganyiko na huzuni, na watu imara wenye nguvu wanaelekea kwenye ulegevu na udhoofu. Hivyo basi msighurike na mengi yanayokufurahisheni humo kwa sababu ya uchache wa yatakayofuatana na nyinyi kutokana nayo.

“Mungu amrehemu mtu ambaye ametafakari na kujifunza humo, amejinfunza na kufanikiwa mwangaza. Kana kwamba ambacho kipo katika dunia hii kwa muda mfupi kitakuwa kama hakijakuwa. Kama kwamba ambacho kipo katika akhera baada ya muda mfupi kitaonekana kama kwamba hakijakosa kuwa. Kila kihesabiwacho kitatoweka, na kila kitazamiwacho kinakuja. Na kila kinachokuja kimekurubia.”

SEHEMU YA KHUTBA HII HII KUHUSU SIFA ZA MWANACHUONI

“Mwanachuoni hasa ni yule mwenye kuitambua thamani yake, yatosha kwa mtu kuwa yu-mjinga kwa kutoijua thamani yake. Kwa hakika miongoni mwa watu awachukiao mno Mwenyeezi Mungu ni yule mja aliyemuachia mambo yake yeye mwenyewe. Anakwenda kombo mbali na njia iliyo sawa, anakwenda bila ya dalili, aitwapo kwenye shamba la dunia atafanya, na aitwapo kwenye shamba la akhera atakuwa mvivu, kana kwamba alilofanya ni wajibu juu yake, na kana kwamba alilolifanyia uvivu si wajibu juu yake.”

SEHEMU YA KHUTBA HII HII KUHUSU WAKATI WA BAADAYE

“Huo ni wakati ambao hatookoka kutoka humo isipokuwa aliye na usingizi sana[246] , akiwa yupo hatambuliki, na akighibu, hakosekani, hao ndio taa za mwongozo na alama za misafara ya usiku, si wasambazaji wa masingizio wala si watoboa siri.

Hao Mungu atawafungulia milango ya rehema Zake, na atawaondolea madhara ya adhabu Zake[247] . “Enyi watu! Zitakujieni zama uislamu utapinduliwa juu chini kama ambavyo chombo kifunikwavyo pamwe na kilicho ndani yake.

Enyi watu! Kwa hakika Mungu amekulindeni kwa maana ya kuwa hatowadhulumu, wala hakuwalindeni kwamba hatowafanyieni mtihani[248] , na amesema Mtukufu katika wasemaji:[249] “Hakika katika hayo yapo mazingatio. Na kwa yakini. Sisi ni wenye kuwafanyia mitihani.” (23:30).

Ar–Radhiy (r.a) amesema: Ama kuhusu kauli yake(a.s) : “Kullu mu’minin nuwamatin” Kila muumini mwenye kulala sana, amekusudia kwa hilo: yaani yule muumini asiye kumbukwa au asiyetajika, na si mtu wa shari.

Na al-Masayiihu: Ni wingi wa neno misyahun, naye ni chakubimbi aendaye kwa huyu na kwa huyu ili kufanya ufisadi (umbea). Al-Madhayyiiu: Ni wingi wa midh’yaun, naye ni ambaye asikiapo baya la mwenzake analitangaza na kulieneza.

Ufafanuzi

Usemi wake(a.s) : “Mwanachuoni ni yule ambaye ameijua Qadiri yake,” ni miongoni mwa mithali mashuhuri kutokana naye(a.s) na wamesema watu baada yake na wamekithirisha, mfano wa kauli yao: ‘Ikiwa hutoijua Qadiri ya nafsi yako, kwa hiyo Qadiri ya mwingine hautoijua kabisa.’

Na mfano wa kauli yao: ‘Ambaye hajui Qadiri ya nafsi yake, watu watakuwa hawana kosa endapo watakuwa hawamjui.’

Na miongoni mwa maneno yaliyoelezwa kutoka kwa Abi Abdillah as-Sadiq(a.s) katika riwaya marfu’u: “Ma halakamru’u arifa Qadrahu” yaani hatohiliki mtu aliyeijua Qadiri yake - riwaya hii ni ya Abul’Abbas kutoka kwake katika Al’Kaamil. Na katika Hadithil-Marfu’u:

104 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s)

MWANZO WA KHOTUBA HII UMETANGULIA KATIKA NAMBA 33.

“Sasa basi! Kwa kweli Allah (s.w.t) alimtuma Muhammad(s.a.w.w) wakati hapakuwa na yeyote katika waarabu aliyekuwa akisoma kitabu, wala kudai unabii wala wahyi (ufunuo).

Na alimpiga vita aliyemuasi akisaidiwa na wanaomtii, akiwaongoza kwenye uokovu wao, na anawaharakishia saa isije kuwashukia[250] , anashindwa mwenye kushindwa, na anasimama aliyevunjika[251] anamsimamia mpaka amfikishe kwenye lengo lake[252] .

Isipokuwa aliyeangamia asiye na kheri, mpaka alipowaonesha uokovu wao, na aliwakalisha mahali mwao, mambo yao yakaenda sawa, na yalitengenea.

Naapa Mungu, kwa kweli nilikuwa miongoni mwa waswagaji wake[253] - mpaka walirudi nyuma wote, na kujikusanya kwenye kamba yao, sikuonyesha udhaifu au kutokuwa na hima, au kuhini wala sikuonyesha unyonge, namuapa Mungu nitaitumbua batili mpaka niitoe haki kutoka kiunoni mwake!”

Sayyid Ar-Radhiy (r.a) amesema: Yaliyoteuliwa katika khutba hii yametangulia, ila tu mimi nimeikuta katika riwaya hii kukiwa na tofauti na iliyotangulia, kati ya ziada na upungufu, kwa hiyo hali imewajibisha kuithibitisha tena.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

105 - MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

KUHUSU BAADHI YA SIFA ZA NABII MTUKUFU NA KEMEO KWA BANI UMAYYAH NA MAWAIDHA KWA WATU

“Kisha Mungu alimtuma Muhammad(s.a.w.w) ili awe shahid[254] na mbashiri na muonyaji, ni mbora katika viumbe akiwa mdogo, na mwenye heshima mno akiwa mtu mzima, na msafi mno katika wasafi wa tabia, na ni mkarimu mno kwa wenye kumuomba[255] .

Dunia haikuwa tamu katika ladha yake kwenu. Wala hamkuweza kunyonya chuchu zake ila mlipokuta hatamu zake zimelegea.

“Kisha alisema kuwa wao wameikuta dunia kwa bahati imekwisha kuwa ngumu kwa atakayeitawalia utawala wa haki kama anavyokuwa mgumu ngamia kwa mpandaji wake endapo hatamu yake itajikusanya, haudaji yake haitulii kwa mpandaji, haramu zake zapatikana kiurakhisi kwa aipendaye.

Ni mfano wa mti wa msidiri uliokatwa miba yake, kwa hiyo ukawa laini wateleza; na halali zake hazipo tena kwa kushindwa na haramu; na kwa kuwa umezagaa umechukua nafasi kulingana naye; na hii ni ishara kwenye aliyokuwa akiyasema daima kwa kujitwalia kwao binafsi suala la ukhilafa makhalifa waliomtangulia mbali naye, kuwa yeye alikuwa msitahiki.

“Kunyonya kiwele chake ila baada ya kumkuta kwa bahati hatamu yake ya puani inajiburura na ukanda wake wa ngozi umelegea. Uharamu wake umekuwa kwa kaumu ya watu kama msidiri ulionepa (kwa uzito wa matunda) hali ikiwa uhalali wake ni mbali, haupo.

Wallahi, mngeikuta kama kivuli kirefu, mpaka muda uliopangwa.

Kwa hiyo ardhi kwenu ni tupu[256] , na mikono yenu humo imekunjuka, na mikono ya viongozi imefungwa mbali nanyi. Panga zenu zimewadhibiti[257] na panga zao zimezuilika dhidi yenu[258] .

Jueni kuwa kwa kila damu iliyomwagwa ina kisasi, na kila haki ina mdai, na mdai kisasi wa damu yetu ni sawa na hakimu anayetoa hukumu kuihusu haki yake binafsi[259] , huyo ni Mungu ambaye hamshindwi amtakaye, wala hamkosi atakayemkimbia.

Namuapa Mungu Enyi Banii Umayyah! baada ya muda mfupi mtaiona nafasi yenu ikiwa mikononi mwa wengine, na nyumbani mwa adui yenu! Jueni kuwa macho yaonayo sana miongoni mwa macho ni yale yaliyopenya kuiona kheri! Jueni kuwa masikio sikivu ni yale yaliyoelewa mawaidha na kuyakubali![260] ”.

KUHUSU SHUGHULI ZA IMAM

“Enyi watu, chukueni mwanga kutoka mwenge wa taa ya muwaidhi mwenye kuwaidhika[261] ,kunyweni na chukueni maji kutoka chemchemi iliyohifadhiwa na kusafishwa bila uchafu[262] .

“Enyi waja wa Mungu! Msiutegemee ujahili wenu, wala msiutii utashi (mbaya) wa nafsi zenu kwa kuwa yule mwenye kuwasili kwenye nyumba hii[263] yupo kwenye ukingo wa kuzolewa na maji yazoayo kila uchafu[264] ananakili[265] maangamizi mgongoni kwake kutoka sehemu (ya mgongo) mpaka sehemu, kwa rai aizushayo baada ya rai; anataka kuambatanisha kisichoweza kuambatana, na kukisogeza karibu kisicho weza kusogea! Ala ala muogopeni Mungu msimlalamikie huzuni zenu yule asiyeweza kuzitanzua, wala hawezi kutangua kwa rai yake lililo lazima juu yenu.

Na kwamba si juu ya Imam isipokuwa alilobidiishwa miongoni mwa amri za Mola Wake Mlezi: Kufikisha mawaidha, na kujitahidi kutoa nasaha, na kuihuisha Sunnah, na kuitekeleza adhabu kwa wanaostahili, na kuzirudisha hisa kwa wenye kustahiki. Hivyo basi harakishieni elimu kabla ya mmea wake haujakauka, na kabla hamjashughulishwa na nafsi zenu mbali na wenye kuwa nazo. Katazeni maovu na wenyewe muwe mmejikataza, mlichoamriwa ni kukataza baada ya kujikataza!.

106 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

HUMO ANABAINISHA UBORA WA UISLAMU, NA AMTAJA MTUKUFU MTUME(S.A.W.W) KISHA ANAWALAUMU SAHABA ZAKE:

“Shukrani zote anastahiki Allah (s.w.t), ambaye ameifanya sharia ya kiisla- mu na kuifanya nyepesi kwa mwenye kuiendea, na ameziimarisha nguzo zake dhidi ya mwenye kutaka kuushinda, na akaufanya kuwa ni amani kwa wenye kujiambatanisha nao, na salama kwa mwenye kuingia – (yaani hapigwi vita akishaingia uislamu), na hoja kwa mwenye kuueleza, na ni shahidi kwa mwenye kugombana kwa ajili yake, na ni nuru kwa mwenye kujiangaza nao, na ni fahamu kwa mwenye kutumia akili, na ni busara kwa mwenye kuzingatia, na ni alama kwa mwenye kuchunguza, na ni uelewa kwa mwenye kuazimia, na ni funzo kwa mwenye kuwaidhika, na ni uokovu kwa mwenye kusadiki, na ni ithibati kwa mwenye kutegemea, na ni raha kwa mwenye kuitumainia, na ni kinga kwa mwenye kusubiri.

Ni njia maarufu iliyo wazi mno na maingilio yaliyo wazi na ni mnara wa juu, na ni njia iliyo dhahiri, ni taa ziwakazo, ni mahali pa kujivunia, bendera iliyoinuka, yenye kukusanya farasi, ni pa kushindania washindani, mtukufu wa washindi wa farasi.

Wapandaji wake ni wenye kuheshimiwa, kusadiki (Mungu, Mtume…) ndio njia yake, vitendo vyema ndio minara yake, umauti ndio lengo lake[266] , na dunia ni kiwanja chake cha mafunzo, na kiyama ni farasi wake, na pepo ni malipo yake ya mashindano.

NA SEHEMU YA KHUTBA NI KUMUELEZA NABII (S.A.W.W):

“Mpaka aliwasha mwenge kwa autakaye[267] , na aliangaza mwanga kwa mahabusi[268] , hivyo basi yeye ni muaminifu wako wa kuaminika, na shahidi wako siku ya malipo, na ni muwakilishi wako akiwa neema, na ni Mtume wako wa kweli akiwa ni rehema.

“Oh Allah! Umgawiye fungu katika uadilifu Wako, na umpe jazaa ya kheri nyingi katika fadhila Zako. Oh Allah! Lirefushe jengo lake zaidi kuliko majengo ya wajengao, na umkirimu mafikio yake Kwako.

Itukuze kwako daraja yake, mtunukie wasila na heshima maalumu na ubora, na tukusanye sisi katika kundi lake, bila ya fedheha wala wenye kujuta, wala wenye kupetuka njia, wala wenye kutengua ahadi, wala wenye kupotea wala wenye kupoteza, wala walioshawishika kwa maovu!”

Ar-Radhiy (R.A) Amesema:

Maneno haya yamepita katika habari zilizotangulia, isipokuwa sisi tumeyakariri hapa kwa sababu ya tofauti iliyopo kati ya riwaya hizi mbili.

MIONGONI MWAYO AKIWAHUTUBIA SAHIBA ZAKE

“Kwa ukarimu Wake Mungu (s.w.t) mmefikia daraja ambayo wanahishimiwa hata vijakazi wenu, na majirani zenu wanatendewa vyema, na anakuheshimuni ambaye hamna fadhila yeyote juu yake, wala hamna hisani juu yake. Na anawahofuni asiyekuwa na maalumati ya kuwa mmepata kumshambulia, wala kuwa na mamlaka juu yake.

Mnaziona ahadi za Mungu zinatenguliwa wala hamkasiriki, hali ninyi mwasumbuka kwa kutanguliwa mila za babu zenu. Na mambo ya Mungu yalikuwa yanakuja kwenu, na yanatokea kwenu, na kwenu yanarejea[269] .

Mmewawezesha madhalimu sehemu zenu, na kuwaachia majukumu yenu, na mmeweka mambo ya Mungu mikononi mwao. Wanatenda kwa shaka, na wanakwenda katika utashi mbaya wa nafsi. Naapa Mungu hata wangekutawanyeni chini ya kila nyota, Mungu angewakusanyeni katika siku mbaya mno kwao!”.

107 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

At-Tabari ameieleza katika Ta’arikh yake katika matukio ya mwaka wa 37 H.A., na Ibn Muzahim katika Swifiin, uk. 256.

BAADHI YA SIKU ZA SIFFIIN

“Kwa kweli nimeona kukimbia kwenu na kutawanyika kwenu mbali na safu zenu za vita, mkizungukwa na watu fedhuli na duni, na mabedui wa (Shaam) Syiria, ingawaje ninyi ni watangulizi katika waarabu na ni kilele cha utukufu na kilele cha ubora, na mna daraja ya juu mfano wa ile ya pua, na ule wa nundu kubwa ya ngamia.

Uhemaji wa moyo wangu utapoa tu niwaonapo mnawazunguka kama walivyokuwa wamewazungukeni, na mnawaondoa mahali mwao kama walivyokuondoeni, mkiwauwa kwa mishale na kuwachoma kwa mikuki, hivyo msitari wao wa mbele uangukie juu ya msitari wao wa nyuma, kama ngamia walioshikwa na kiu waliofukuzwa kutoka kwenye manyweo yao, na kuzuiliwa maendeo yao ya kunywea maji!”.

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

108 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Zamakhshari ameieleza katika Rabi’ul-Abrar, Jz. 1, mlango wa ‘kubadilika kwa hali’.

NAYO NI KHUTBA YA HALI YA MABADILIKO, YAANI MATUKIO MAKUBWA VITANI

“Mstahiki wa sifa njema ni Mungu Aliye dhahiri kwa viumbe Wake kupitia viumbe wake[270] , na mwenye kudhihiri nyoyoni mwao kwa hoja Zake[271] , ameumba viumbe bila ya kufikiri, kwa kuwa kufikiri hakumfalii isipokuwa wenye kuwa na dhamiri[272] , naye si mwenye dhamiri[273] , elimu yake imepenya mpaka ndani ya siri zisizojulikana, na kuzingira itikadi za ndani za siri.”

NA SEHEMU YA KHUTBA HII NI MAELEZO KUHUSU NABII (S.A.W.W)

“Mungu (s.w.t) amemchagua kutoka mti wa nasaba ya manabii[274] , na kutoka mwale wa mwanga, na ni miongoni mwa nywele za utukufu wa kipaji cha uso, kutoka sehemu bora mno katikati ya bonde la Bat’ha’a[275] , na taa za kuangazia gizani, na chemchemi za siri za hekima.”

Miongoni mwayo: “Yeye - yaani Nabii(s.a.w.w) alikuwa mfano wa tabibu anayezunguka na tiba yake, aliyeimarisha marhamu yake, azungukaye na aliye tayari na dawa zake, na amekwisha koleza mawasimu zake[276] . Anazitumia mahali ambapo ipo haja, ili kuziponya nyoyo za vipofu, na masikio ya viziwi na ndimi za mabubu, kwa dawa zake hufu- atilia mahali ulipotawala mghafala na mahali penye mashaka na matata.

Hawakufaidika na mwanga wa hekima zake, na wala hawakuwasha moto kutoka jiwe la elimu litoalo cheche; Hivyo basi wao katika hilo ni kama wanyama watafunao nyasi, na mawe magumu. Siri zimefichuka kwa wenye kufahamu[277] njia ya kweli imekuwa wazi kwa wale wasiokuwa na mwongozo na saa ikurubiayo imeondoa kifuniko usoni pake, na alama zimeonekana kwa wanaoangalia kwa makini.

Nimekuwaje mimi! Nawaoneni (mko) miili isiyokuwa na roho, na roho bila ya miili[278] , wafanya ibada bila wema[279] , na wafanyibiashara bila ya faida[280] , wako macho hali wamelala[281] ,wanatazama hali ni vipofu, wanasikia hali ni viziwi na wanaongea hali ni mabubu!.

MIONGONI MWAYO

“(Nimegundua kuwa) Kuna bendera ya upotovu imejiimarisha katikati, na imetawanyika na watu wa kabila lake, inakupimieni kwa kilo yake[282] , na kuwachanganyeni na uzito wake.

Kiongozi wake yuko nje ya mila (ya kiislaamu) yupo katika upotovu, siku hiyo hatobaki miongoni mwenu ila ni kama mabaki ya chungu[283] au vumbi kama vumbi lililokung’utwa kutoka kwenye kipeto[284] . Hivyo basi itakusugueni kama isuguliwavyo ngozi, na itakukanyageni mkanyago wa mazao yaliyovunwa, na itamdonoa muumini kati yenu kama anavyodonoa ndege punje nene kati ya punje nyembamba.

Madhehebu yanawapelekeni wapi, na giza linawafanya mtangetangie wapi! Na mnapelekwa wapi na matarajio! Kutoka wapi mwaletwa, na mwadanganyiwa wapi? Kila muda una maelezo ya maandishi, na kila aliyetoweka ni lazima arudi, hivyo basi wasikilizeni viongozi wenu wa kiungu, na zihudhurisheni nyoyo zenu, na amkeni atakapowapigieni kelele. Mtangulizi inambidi aongee la ukweli kwa watu wake.

Yampasa azikusanye azma zake na fikra zake ili aangalie, fahamu zake aziweke hadhiri, suala ameliatua uatuaji wa tundu la kizuizi cha vazi, na ameliparua uparuaji wa ulimbo[285] (kutoka kwenye kijiti cha mti na kuondolewa). Wakati huo batili itachukuwa nafasi yake, na ujahili utapanda kipando chake, utovu wa nidhamu utakuwa mkubwa, na wito utakuwa mdogo, na wakati utavamia uvamiaji wa mnyama mkali, na dume la ngamia litakoroma baada ya ukimya, na watu watakuwa ndugu katika maovu, watahamana kwa dini[286] . Watapendana katika uwongo, na watachukiana kwa sababu ya ukweli.

Hali ikiwa ni hivyo mtoto atakuwa chukizo[287] - (yaani atakuwa sababu ya kuchukiza badala ya kuwa kitulizo cha jicho kwa wazazi wake) na mvua - (sababu ya joto), uovu utajaa mno, na maadili mema yatatoweka, na watu wa zama hizo watakuwa mbwa mwitu, na masultani wao ni kama wanyama wavamizi, na watu wao wa hali ya kati watakuwa walafi, na mafakiri wao ni maiti, ukweli umedidimia, na uwongo umefurika, na upendo utakuwa wa maneno, hali watu wakiwa wanagombana kimoyo, na uzinzi ni nasaba, na usafi wa kutozini ni ajabu[288] , na uislamu utavaliwa kama ngozi juu chini.[289] ”.

109 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Az-Zamakhshariy ameieleza katika Rabi’ul-Abrar katika mlango wa Malaika, na ibn Abdi-Rabih katika al-Iqdu al-Farid, jalada la 4, uk. 76.

Katika kubainisha Qudra ya Mungu (s.w.t) na kuwa Yeye ni wa pekee katika utukufu na wa pekee katika suala la kuwarejesha hai viumbe Wake: “Kila kitu chamnyenyekea Yeye, na kila kitu huwa kwa kupitia kwake Yeye: Yeye ni toshelezo la kila fakiri, na hadhi kwa kila mnyonge, na nguvu ya kila dhaifu, na kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo.

Mwenye kuongea anamsikia tamko lake, na mwenye kunyamaza anajua siri yake, na kwa anayeishi riziki ni juu yake, na anayekufa Kwake ndio marejeo.

“Macho hayajakuona hata yawe na uwezo wa kueleza habari zako, na ulikuwa kabla ya waelezaji miongoni mwa viumbe Wako.

Hukuwaumba viumbe kwa ukiwa, wala haukuwafanya wafanye kazi kwa ajili ya manu- faa, hautomtaka yeyote na akukose, wala hakuponyoki umshikae[290] , wala hapunguzi mamlaka yako anayekuasi, wala hazidishi ufalme wako anayekutii, wala hawezi kuirudisha amri yako mwenye kukasirikia maamuzi yako, na wala hajitoshelezi bila wewe mwenye kugeuka mbali na amri yako. Kila siri Kwako ni dhahiri shahiri, na kila cha ghaibu Kwako kipo mbele yako.

Wewe ni wa milele hauna mwisho, Wewe ndio lengo hakuna jinsi ya kukuepuka, na Wewe ndio mahali pa ahadi ya marejeo ambapo hakuna jinsi ya kuokoka kwa kukuepuka Wewe ila Kwako Wewe. Mkononi mwako kuna shungi la nywele la kila kiumbe, na Kwako ni marejeo ya kila kiumbe.

Utukufu ni wako adhama ilioje ya mambo yako! Utukufu ni wako adhama ilioje tuyaonayo kwa viumbe wako! Na udogo ulioje kwa kila adhama pembeni mwa uwezo Wako! Kutisha kulikoje kwa tuyaonayo katika ufalme wako! Unyonge ulioje kwenye yale ambayo yameghibu kwetu miongoni mwa mamlaka Yako! Wingi ulioje wa neema yako duniani, ni ndogo ilioje kwa kuilinganisha na neema ya akhera!”

UFAFANUZI

Amesema: Kila kitu ni chenye kuinyenyekea adhama ya Mungu (s.w.t), na kila kitu huwa kwa kumtegemea Yeye, na hii ndio sifa Yake makh’susi. Yaani: Kuwa Yu ajitosha si muhitaji kutoka kwa chochote, wala hakuna kitu miongoni mwa vitu kinachojitosha bila Yeye asilan.

Imekuja (khabari) katika athari kuwa: Mwenye kujitukuza kupitia asiyekuwa Mungu huwa dhalili. Na mwenye kujikithirisha kupitia asiyekuwa Mungu huwa mchache; Na ilikuwa inasemwa: ‘Si fakiri mwenye kujitosheleza kwa Mungu.’

Na Al-Hasan amesema: ‘Ajabu ilioje kwa Lutu Nabii wa Mungu! Amesema: “Laiti ningelikuwa na nguvu juu yenu, au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu”. (11:80) (kwa kujiun- ga na mtu mwenye nguvu aninusuru dhidi yenu) (au nikimbilie kwenye sehemu yenye nguvu). Je wamuona ametaka uimara zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko wa Mungu!?

Na wanachuoni wametolea dalili kuthibiti kuwepo kwa Muumba (s.w.t) kutokana na yaliojulishwa na maana ya kauli yake(a.s) : “Ni kimbilio la kila mwenye kuvunjika moyo,” hiyo ni kwa sababu nyoyo katika hali yake ya dhahiri hukimbilia kurejea kwa muumba wao wakati wa shida na majanga.

Je humuoni mpanda chombo pindi mawimbi yanapochafuka ni vipi anavyomsihi Yeye (swt): “Na inapokufikieni taabu katika bahari, hao mnaowaomba wanapotea, isipokuwa Yeye tu”. (17:67).

Kisha akasema(a.s) : “Mweye kusema hulisikia tamko lake, na mwenye kunyamaza yuajua siri yake,” yaani yeye hujua yaliyo dhahiri na yaliyojificha.

Kisha akasema: ‘wa man aasha fa alayhi rizquhu, waman maata fa ilayhi munqalabuhu,’ yaani Yeye ndiye mratibu wa ya duniani na ya akhera, na Ndiye Mtoa hukumu wa sehemu zote mbili.

Amesema(a.s) : “Macho hayajapata kukuona hata yaweze kueleza khabari zako, kama ambavyo mtu huelezea kuhusu aliyoyaona, lakini Wewe huna mwanzo wala mwisho, Ulikuwapo kabla ya waelezaji wa kueleza habari Zako”.

SWALI : Kuna kupingana kati ya haya mambo mawili, je haiwezekani awe yupo (s.w.t) kabla ya wasifiaji wa kueleza khabari zake, pamwe na hali hiyo awe aonwa na macho akishawaumba viumbe, kisha wawe wanamsifu au kumuelezea hali wakimuona wazi wazi kwa macho!

JIBU : Kuna kupingana kwa dhahiri, nako ni: Ikiwa Yeye (s.w.t) ni wa milele na sio wa kimwili, yaani Mungu dhati yake sio kitu cha kimwili na wala sio mfano wa kiwa au kiumbe miongoni mwa viumbe visivyokuwa mwili – incorporeal - (mfano wa akili wepesi na uzito) na ambacho si mwili wala- incorporeal, ni muhali kuonwa, kwa hiyo ni muhali kueleza kumhusu kwa njia ya kumuona.

NA SEHEMU YA KHUTBA KUHUSU MALAIKA

“Ewe Allah! Umewafanya malaika wakae ndani ya mbingu Zako, na ume- wanyanyua juu mbali na ardhi Yako, wao ndio wakujuao mno katika viumbe Wako, na wakuogopao mno, na walio karibu mno na Wewe; Wao hawajakaa viunoni, wala kubebwa na matumbo ya uzazi, na hawakuumbwa kwa maji duni.

Na wala hawakutawanywa na shaka ya matukio ya wakati, na wao wana nafasi na daraja Kwako, na mkusanyiko wa upendo wao ni kwa ajili Yako, na kukithiri utii wao Kwako, na kutokughafilika na amri Yako. Lau wangeainisha uhalisi wa yaliyofichika kwao kutoka Kwako, wangezihakiri aamali zao, na wangejibeza wenyewe, na wangetambua kuwa hawajakuabudu ukweli wa kukuabudu, na hawajakutii ukweli wa kukutii Wewe.

Utukufu ni Wako, Muumba na mwabudiwa! Kwa uzuri wa balaa lako ulipoumba[291] , umeumba nyumba (Jannah) na umejaalia humo dhifa: kinywaji na chakula, wanawake na wahudumu, makasri na mito, mashamba na matunda; hatimaye ulimtuma mlinganiaji analingania huko (Yaani Nabii).

Mlinganiaji hakuitikiwa wala uliyo wapendezesha hawakuyapenda wala hawakuwa na shauku na uliyowatia shauku. Waliuelekea mzoga (mzoga hapa yakusudia dunia), ambao walifedheheshwa kwa kuula.

Na waliungana kuupenda, mwenye kukiashki kitu hupofusha macho yake, na kuufanya moyo wake uwe mgonjwa, kwa hiyo yuangalia kwa jicho ele, na yuasikia kwa sikio lisilosikia, kupenda kumeirarua akili yake, na dunia imeufisha moyo wake, hali nafsi yake imehuzunika kwa ajili yake, kwa hiyo yeye ni mtumwa wa dunia, na mtumwa wa ambaye mkononi mwake mna kitu kutokana nayo, itelezeako naye yuatelezea, ielekeako naye yuaelekea. Haonyeki na muonyaji kwa amri yeyote kutoka kwa Mungu, na wala hawaidhiki na mtoa waadhi yeyote, naye awaona waliochukuliwa na ghururi, kuwa hawana batilisho wala rejea.”

KUHUSU KIFO

“Limewafika walilokuwa wakilipuuza, nalo ni kuiacha dunia kumewajia (dunia) ambayo waliifanya iko salama kwao, na wamekifikia akhera kile ambacho walikuwa wanaahidiwa, yaliyowafika hayaelezeki, yamejikusanya kwao mawili: Uchungu wa kifo, na huzuni ya kuiacha (dunia), viungo vyao vya miili vimelegea kwa (mauti), rangi zao zimebadilika (kwa mauti), hatimae kifo kilizidi kuwaingia, mtu anazuilika mbali na uwezo wake wa kutamka, naye yupo kati ya ahali yake akiangaza kwa macho yake, na asikia kwa masikio yake, akili yake ikiwa sahihi, uelewa wake umebaki, anafikiri katika ambayo umri wake ameumaliza, na katika alivyoupeleka muda wake! Yu-akumbuka mali alizozikusanya, aliufumbia macho utafutaji wake[292] .

Ameyachukuwa (mali) kwa njia ya halali na kwa njia yenye utata[293] hivyo sasa imemkabili dhambi ya jinsi alivyoikusanya, na amekaribia kuiacha, nayo (mali) yabaki kwa watakaobakia nyuma yake wananeemeka nayo na kustarehe nayo, kwa hiyo kheri na anasa (ya alichochuma) itakuwa ya wengine si yake yeye, na uzito (wa dhambi) utakuwa juu ya mgongo wake.

Mtu amekuwa rehani[294] , hivyo yeye anauma vidole vyake akijuta kwa yaliyomdhihirikia wakati wa mauti miongo- ni mwa mambo yake, na atakuwa hapendi ambalo alikuwa analipenda siku za umri wake, na atakuwa anatamani kuwa ambaye alikuwa akimhusudu kwa ajili ya mali na kumuonea wivu, angeihodhi yeye badala yake yeye mwenyewe.

Mauti yangali yanamwingia kwa kasi mwilini mwake, mpaka ulimi wake uwe umechukuliwa na umauti kama masikio yake, yupo kati ya ahali zake hawezi kuongea kwa ulimi wake, wala kusikia kwa masikio yake, yuazungusha macho yake nyusoni mwao, akiona mtikisiko wa ndimi zao, lakini hasikii wanayojibishana. Kisha umauti utazidi kumkaba na kuyashika macho yake kama ulivyoshika masikio yake, na roho itatoka mwilini mwake, na kuwa mzoga mbele ya Ah’li zake, na ahali zake wameingiwa na ukiwa, wakiwa wamefadhaishwa naye, na wanajiweka mbali naye, hamfurahishi mliaji, wala kumjibu mwitaji. Kisha watambeba mpaka kwenye mwanandani ardhini, na kumkabidhi humo kwenye matendo yake, na kukata ziyara yake (kuwa hawaendi kumzuru).”.

KIYAMA

“Mpaka Kitabu kifikie muda wake, na amri makadirio yake, na kukutan- ishwa viumbe wa mwisho na wa mwanzo, na itakuja amri ya Mungu apendavyo katika kuwafanya upya viumbe Wake, ataiyumbisha mbingu na kuichana, na ataitikisa ardhi na kuitetemesha, na kuin’goa milima yake na kuivunja vunja, na kwa haiba ya utukufu Wake itagongana yenyewe kwa yenyewe, na kwa hofu ya ukali wake, na atawatoa nje walio ndani yake (ya makaburi), na atawafanya upya baada ya kwisha kwao (kuchakaa kwao).

Na kuwakusanya baada ya kutawanyika kwao, kisha atawapambanua[295] kwa ajili ya kutaka kuwauliza kuhusu amali zilizojficha, na matendo yaliyofichikana, na amewafanya makundi mawili: Hili moja alineemesha na hili la pili analiadhibu.

Ama watiifu atawalipa thawabu ya kuwa karibu Yake, na kuwafanya wa kudumu ndani ya nyumba yake, kiasi kwamba wafikao humo hawatotoka, wala hali haitowabadilisha, wala hawatofikiwa na hofu, wala hawatopatwa na magonjwa, wala hawatopatwa na hatari, wala kusumbuliwa na safari kwa kuwatowa sehemu hadi nyingine.

Ama watenda maasi atawakaribisha kwenye nyumba ya shari mno, na kuwafunga mikono shingoni, na kuzifunga nywele za utosi na nyayo za miguu, na kuwavisha kanzu za lami na vazi la moto, watakuwa katika adhabu ya moto uliokolea, na mlango uliowagubika wahusika wake, katika moto wenye ukali na sauti, na mwale umulikao, na wenye ukelele wa nguvu na wa kutisha, wakaao humo hawatoki, mateka wake hawakom- bolewi kwa fidia, pingu zake hazikatwi. Ile nyumba haina muda kiasi cha kuwa muda ukifika itakwisha, wala muda uliopangwa kwa wale watu hata ufikie mwisho.”

SEHEMU YA KHUTBA IMUELEZAYO NABII (S.A.W.W)

“Aliidharau dunia na kuiona duni na kuidogesha, aliona dunia haina thamani na akaidharau, na alijua kuwa Mungu (s.w.t) amemuepusha nayo kwa hiyari yake(s.a.w.w) na ameikunjua kwa wengine ili kuwadharau. Hivyo basi alijiepusha nayo kwa moyo wake, na kufisha utajo wake katika nafsi yake, na alipenda mapambo yake yatoweke mbali na macho yake, ili asichukue kutoka humo vazi la fakhari, au awe anatarajia humo nafasi, amefikisha kwa niaba ya Mola wake Mlezi akitoa udhuru[296] , na alitoa nasaha kwa umma wake akionya, na alilingania pepo akibashiri, na alihofisha moto kwa kuhadharisha.”

AHLUL-BAYT

“Sisi ni mti wa unabii, na mashukio ya risala, na mapishano ya malaika[297] , na chimbuko la elimu[298] , na chemchemu za hukumu, mwenye kutunusuru na kutupenda atakuwa anangoja rehema, na adui yetu mwenye kutuchukia anangojea adhabu[299] .

NAHJUL BALAGHA

JUZUU YA PILI

MTARJUMI: HARUNA PINGILI

110 - NA MIONGONI MWA KHUTBA ZAKE(A.S)

Na Miongoni Mwa Khutba Zake(a.s) - Ibn Shu’ba ameieleza katika Tuhful-Uqul, uk. 104. Na al-Barqi katika al-Mahasin, uk. 233.

HUMO ANAELEZEA FARADHI ZA UISLAMU:

“Kwa hakika jambo bora ambalo wanaweza kulifanya wasila kwa Mungu (s.w.t), wafanyao wasila ni kumwamini Yeye na Mjumbe Wake, na jihadi katika njia Yake, kwa kweli hicho ni kilele cha uislamu.

Na neno la ikhlasi kwa kuwa hiyo ni fit’ra; na kutekeleza wajibu wa sala kwa kuwa hiyo ni mila; na kutoa Zaka kwa kuwa hiyo ni faradhi ya wajibu, na kufunga mwezi wa Ramadhani hiyo ni kinga ya kutoadhibiwa; na kuhiji Nyumba na kuiendea kwa ibada ya Umra kwa kuwa mawili hayo yanaondoa ufakiri na yanaosha dhambi; na kuunga udugu kwa kuwa hilo lakithirisha mali na linarefusha umri. Na sadaka ya siri kwa kuwa hilo lasitiri kosa[300] .

Na sadaka ya wazi wazi kwa kuwa hilo linazuia kifo kiovu; na matendo mema kwa kuwa yanazuia kuangukia kwenye fedheha.

Kithirisheni kumtaja Mungu kwa kuwa ni utajo mwema, na yafanyieni raghba ambayo (s.w.t) amewaahidi wachamungu kwa kuwa ahadi Yake ni ahadi ya kweli mno, na ongokeni kwa kufuata mwongozo wa Nabii wenu kwa kuwa hiyo ni sera iliyo bora[301] .

Fuateni Sunna zake kwa kuwa ni mwongozo bora mno, na jielimisheni Qur’ani kwa kuwa hayo ni maongezi mema mno, na jitahidini kuifahamu kwa kuwa ni kheri ya nyoyo, na jitibuni kwa nuru yake kwa kuwa Qur’ani ni tiba ya vifua, na isomeni vyema kwa kuwa hiyo ni visa vyenye manufaa mno.

Kwa hakika mjuzi atendaye kinyume na ujuzi wake ni kama jahili aliyechanganyikiwa ambaye hang’amui kutokana na ujahili wake, bali hoja dhidi yake ni kubwa mno, na majuto yatamlazimu mno[302] , na yeye kwa Mungu ni mlaumiwa mno[303] .

MAELEZO

Ametaja(a.s) vitu vinane vyote ni wajibu.Cha kwanza: Kumwamini Mungu na Mtume Wake. Na anakusudia neno imani hapa ni: Kusadiki kutupu moyoni, kwa kuweka kando yasiyokuwa hayo kwa mfano kutam- ka shahada, na matendo ya wajibu, na kuacha mabaya. Na madhehebu ya kundi miongoni mwa wanafalsafa wa itikadi za Kiislamu wamesema kuwa: Kiini cha imani ni: Kusadiki moyoni pekee; na hilo ijapokuwa si madhehebu ya sahibu zetu, wao wangesema: Kuwa Amirul-Mu’minina(a.s) amelileta tamko hili kwa mujibu wa asli ya uwekaji wa kilugha; kwa kuwa imani katika asili ya lugha ni kusadiki. Amesema (s.w.t):

“Wa maa anta bimuuminin Lana walaw kunnaa sadiqiina” - Na wewe hutuamini ijapokuwa tunasema kweli; (12:17), yaani hautotusadiki; tuwe waongo au wakweli. Na kuleta kwake (a.s) tamko hili kwa mujibu wa uwekaji wake kilugha hakubatilishi madhehebu yetu kuhusiana na kinachoitwa imani; kwa kuwa sisi madhehebu yetu ni kuwa sheria imepanua maana ya tamko hili kwa tamko lingine, kama ambavyo madhehebu yetu kuhusu Sala na Zaka na yasiyokuwa hayo mawili, hivyo basi hakuna kinachopingana kati ya madhehebu yetu na alilolileta Amirul- Mu’miniina(a.s) .

La pili ni: Jihadi katika njia ya Mungu.

Tatu; Tamko la ikhlasi; yaani: Ash’hadu an laa ilaaha illa llahu wa ash’hadu ana Muhammadar-Rasulu’llah.

Na amesema: Hilo ni umbo; yaani ndilo ambalo watu amewaumba kwalo; na asili yake ni neno la kwanza, kwa kuwa ni tawhiid, na kwa hilo ndio watu wameumbwa kwalo.

Nne: Kudumisha Swala.

Tano: Kutoa zaka.

Sita: Kufunga saumu ya mwezi wa Ramadhani

Saba: Hija na Umra,

Nane: Kuunga udugu, nako ni wajibu, na kuutelekeza ni haramu, amese- ma: “Kwa leta mali na kuikithirisha.”.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s) Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU