• Anza
  • Iliyopita
  • 9 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 13998 / Pakua: 2371
Kiwango Kiwango Kiwango
USUULID DIIN

USUULID DIIN

Mwandishi:
Swahili

2

USUULID DIIN

UIMAMU

IMAM WA TISA

MUHAMMAD BIN ALI(a.s)

Ni maarufu kwa lakabu ya "Al-jawad" na "Attaqii". Alizali-wa kwenye mji wa Madina katika mwezi wa Ramadhan mwaka 195 H.

Aliishi mwanzoni mwa utoto wake katika zama za utawala wa khalifa Maamun, ambae pamoja na mambo yote yaliyo uzunguka utawala wake, alikuwa akionyesha kuwa na mapenzi na kuwatawalisha Ahlul Bayti(a.s) . Naye Imamu Ridhwa(a.s) alipo fariki na watu kuzielekeza tuhuma za kifo cha Imam kwa Maamun, na mazungumzo hayo kuenea kwenye vinywa vya watu kuwa yeye ndie aliemuua Imam, Khalifa alijaribu kukanusha suala hilo na kutoa dalili ya kivitendo ili kuyabatilisha hayo, na hima zake zote kuzielekeza kwa mwana wa Imamu Ridhwa, kwa kumpenda na kujikaribisha kwake, hadi kufikia kuchukua uamuzi wa kumuoza Imamu binti yake na kuimarisha mahusiano kati ya familia mbili hizo.

Nao bani Abbasi wakamchukia Maamun kwa kufanya hivyo na wakamwambia wazi kutoridhishwa kwao, na kumsisitizia kua-chana na jambo hilo analo taka kulifanya, huku wakimtaka awatendee wana wa Ali na kuwa pamoja nao kama walivyo kuwa wakiwatendea na kuwa nao makhalifa walio tangulia, waki-kusudia kuwafanyia chuki na kukata mawasiliano na kuwafanyia uadui.

Maamun akalikataa hilo na kuwaeleza wazi ulazima wa kuondoa hali yiho ya dhuluma na uadui iliyo rithiwa, kwa sababu kufanya hivyo ni kukata udugu na kuwafanyia uadui wana wa Ali bila sababu na bila ya dalili, na akawawekea wazi na kuwabaini-shia kuwa kumchagua Imam ili amuozeshe binti yake hakikuwa ni kitendo cha kuathirika kwa hisia au kitendo kisicho na faida, bali alifanya hivyo kutokana na kuona sifa au hali tofauti ambayo inamtofautisha na kumpambanua na watu wote wenye elimu na wenye sifa bora akiwa bado ni mdogo.

Walipo muona Maamun harudi nyuma na kuacha msimamo wake ule wakamtaka ampe muda Imamu hadi akasome elimu ya fiqhi vizuri na aweze kujifunza. Maamun akawaambia "Hakika huyu ni katika watu wa nyumba ya Mtume, elimu yao hutoka kwa Mwenyezi Mungu, na mkitaka mfanyieni majaribio ili muweze kufahamu jambo hili. Watu wale wakakubali kufanya hivyo, na wakafanya maandalizi yenye kufaa, na wakamuomba Qadhil-Qudhati (hakimu wa mahakimu) alie kuwa akiitwa Yahya bin Aktham amuandalie Imam maswali ambayo yatadhihirisha kuto-kuwa na uwezo na kushindwa kwake kuyajibu.

Na mtihani ule ukafanyika kwenye siku yake iliyo pangwa, na matokeo yake ilikuwa ni kadhi yule kushindwa kwenye majaribio yake na Imamu kudhihirisha kiwango cha juu zaidi na kikubwa kwenye fiqhi ya kiislamu jambo ambalo hatuna nafasi ya kulie-lezea kwa upana. Kisha ndoa ikafanyika na kukawa na mahu-siano ya kina kati ya Imam na Maamun.

Ukhalifa ulipomfikia Muutaswim alimuita Imamu kwenda Baghdaad na kumuweka kwenye nyumba maalum, kisha Imam hakubakia kwa muda mrefu, kwani alifariki haraka sana baada ya kufika huko na alikufa kwenye mazingira yasiyo eleweka ambayo yalielekewa na vidole vya tuhuma, vikimtuhumu Muuta-swim kuwa yeye ndie alie muwekea sumu Imamu kupitia mkewe Umulfadhli.

Hata ingawa utawala ulikuwa umembana Imam na hasa kipindi alicho kaa Baghdad, zimebaki kutoka kwake athari za kielimu zenye thamani zilizomo kwenye vyanzo vikubwa (vitabu) na mashuhuri vya kiislamu.

Alifariki (rehema na amani ziwe juu yake) katika mwezi wa dhulqaada mwaka 220H, na kuzikwa pembezoni mwa babu yake Imam Kadhim Kwenye makaburi ya makuraishi "Al-kadhimiyya".

IMAMU WA KUMI

ALI BIN MUHAMMAD(a.s)

Alie maarufu kwa lakabu zake "Al-haad"na "Annaqi".

Alizaliwa Madina katikati ya mwezi wa dhul-hijja, mwaka wa 212 H Aliishi miaka kadhaa kwenye zama za utawala wa Muutaswim, nazo ni zama za kuanzishwa mji wa Surra man ra'a (Samarra) na Khalifa kushughulikia matatizo ya waturuki waliokuwa watumwa na walio kuwa wakilitawala jeshi na dola. Kisha zikaja zama za utawala wa Waathiq, na ni zama ambazo hapakuwa na tukio lolote isipokuwa hali ya kupendana kati ya Khalifa na Imam. Kisha zikafuatia zama za Mutawakil, nazo ni zama za utawala ulio kuwa ukienda kinyume na Ahlulbait(a.s) na kutangaza wazi uadui wao na kuwapiga vita kwao.

Mtumishi wa Mutawakil aliekuwa Madina alipofahamu malengo ya Khalifa, akawa akituma ripoti kwenda mji mkuu wa utawala, na ripoti zote zikimtuhumu Imamu kwa kuandaa mapinduzi na kusisitiza juu ya hatari ya Imamu huyu kwa dola.

Na ripoti hizo zilipo kithiri Mutawakil akamuandikia Imamu barua akimpa pendekezo ndani ya barua hiyo kuwa aende Samarra pamoja na yeyote atakae taka kufuatana nae katika familia yake na watu wa nyumbani kwake, ili kujadidisha uhusiano wao (kuufanya upya) na ili kuzima joto ya hamu na shauku ya kukutana naye kama ambavyo Mutawakili alivyo muandikia pia mtumishi wake wa Madina na kumueleza, ikiwa Imamu ataazimia kusafiri awatume walinzi na watu watakao fuatana nae ili kuonyesha zaidi umuhimu na heshima nyingi aliyokuwa nayo Khalifa kwa Imam.

Kutokana na yote hayo Imamu akaona kuwa yeye ni lazima asafiri, na baada ya kutulia kwa muda kiasi kwenye nyumba ya pekee aliyo tayarishiwa na Mutawakil, akahamia kwenye nyumba aliyo inunua yeye mwenyewe kwa mali yake ili kuepuka kuwa mgeni wa Khalifa, nayo ni nyumba ambayo baada ya kufariki kwake ilikuwa ni sehemu yake ya kuzikwa na ni sehemu ambayo watu huifanyia ziara.

Na Imamu akabakia Samarra akiwa mateka na kukaa pale kwa lazima (kifungo cha nyumbani) hadi alipo fariki. Na pamoja na yote hayo uchunguzi ulikuwa ukiendelea wa kumchunguza Imamu, na wachochezi wakiendelea na kazi yao kwa bidii zote, na nyenzo zote za kumfanyia maudhi Imamu zikifanya kazi, ikiwemo kuvamiwa nyumba ya Imamu usiku kwa madai ya kutafuta mali na silaha anazo ziandaa kwa ajili ya mapinduzi dhidi ya utawala wa Mutawakili.

Pamoja na uchokozi wote huo na usumbuaji, khalifa wakati mwingine alikuwa akilazimika kumkimbilia Imamu anapo patwa na masuala magumu na mazito ya sheria ambayo kwenye serikali au watu wa karibu wa khalifa, hakuna alie kuwa akiyafahamu vizuri na mwenye uwezo mzuri wa kuyajibu.

Na katika urithi wa Imamu wa kielimu kilibakia kwetu kitu cha thamani sana, na miongoni mwa urithi huo ni kitabu madhu-buti kilicho tilia mkazo maudhui ya "Al-jabri wa Tafwidh", kwani alielezea kwenye kitabu hicho mas'ala haya pande zake zote, na kubainisha mielekeo yake, na kuyabainisha mambo yake yaliyo fichika na matatizo yake, na kutoa ufafanuzi kamili wa yale aliyo yakusudia babu yake Jaafar bin Muhammad(a.s) alipo sema "Hakuna kutenzwa nguvu wala kuachiliwa huru, bali jambo hilo ni kati kwa kati.[62]

Alifariki kwenye mji wa Samarra katika mwezi wa Rajab mwaka 254 H.[63] na kuzikwa kwenye nyumba yake huko, sehemu ambayo ndiyo ifanyiwapo ziara yake kwa hivi sasa.

IMAMU WA KUMI NA MOJA

ASSAN BIN ALI(a.s)

Ajulikanae kwa lakabu maarufu ya "Askari" na hilo ni jina moja wapo kati ya majina ya mji wa Samarra.

Alizaliwa kwenye mji wa Madina katika mwezi wa Rabiiul-akhir, mwaka wa 232 H, aliishi katika siku za uhai wake, kwenye zama za watawala na zama hizo kuanzia kwa Khalifa Al-muutazzu, na hapakumtokea Imamu kwenye zama hizo pamoja na Muutazzu suala lolote kama kuwa na msimamo wa aina yoyote wenye sura ya kumfanyia uchunguzi wa karibu Imamu.

Na hilo lilitokana na Khalifa kujishughulisha na matatizo ya askari jeshi wa kituruki walio kuwa wakilidhibiti dola na serikali na kueneza fujo na uharibifu kwenye sehemu za dola hilo, hadi kufikia hatua ya kumshika mateka, kumtia kizuwizini khalifa na kumvua madaraka.

Khalifa Al-Muhtadi, mahusiano yake na Imamu yalikuwa mazuri, kutokana na kufahamika kwake khalifa huyu kuwa ni mwenye kujiepusha na unywaji pombe na vikao vya taarabu na ngoma, na kujiweka kando, na kujidhihirisha kwenye madh'hari ya wema na upole.

Khalifa Al-Muutamad alikuwa ni mkali na mwenye kutumia nguvu kwa Ahlulbaiti, na Imamu aliwekwa jela kwenye utawala wa khalifa huyu Muutamad kwa muda kadhaa, kisha khalifa akalazimika kumuachia huru Imamu pale walipo mtatiza viongozi wa kikristo katika tukio lililo tokea baina yao nayeye, na kisa chake kime simuliwa na baadhi ya wanahistoria. Khalifa akakimbilia kwa Imamu ili awape majibu ya kuwaziba midomo na kudhihirisha uongo na udhaifu wao mbele ya halaiki ya waislamu.

Na Muutamad alikuwa na dauru isiyo njema na isiyotukufu pale alipo fikiwa na habari za kufariki kwa Imamu, kwani aliwaamuru askari wake kumtafuta "Muhammad Almahdi", mtoto wa Imamu Askari, huku akimtumia katika tukio hilo Jaafar bin Ali, ami yake Almahdi, kwa kumlimbikizia mali na kumpatia cheo, ili amsaidie kumtafuta mtoto wa nduguye.

Lakini pande hizo mbili hazikufaulu katika matakwa yao. Imamu Al-mahdi akatoweka kwenye macho ya maadui zake na Mwenyezi Mungu akamuokoa kutokana na vitimbi vya watu hao wafanyao vitimbi.

Pamoja na kuwa mazingira ya Imamu yalikuwa ni magumu na yenye matatizo, wapokezi wa riwaya wamesimulia na kupokea kutoka kwake mambo mengi ya kielimu na yenye manufaa na muelekeo wa uongofu na ujuzi wenye kueleweka na wa kweli.

Alifariki (rehema na amani ziwe juu yake) katika mji wa Samarra tarehe 8 mwezi wa Rabiul awwal mwaka 260 H.[64] na kuzikwa kwenye mji huo karibu na baba yake, kwenye nyumba yao makhsusi.

IMAMU WA KUMI NA MBILI

MUHAMMAD BIN HASSAN(a.s)

Alie maarufu kwa lakabu ya "Al-mahdi" na "Al-qaa'im-Al-Muntadhwar".

Alizaliwa kwenye mji wa Samarra wakati wa Alfajiri, tarehe 15 ya mwezi wa Sha'aban mwaka 255 H. Alitoweka kwenye macho ya Serikali ya wakati huo pale walipo taka na kufanya juhudi kubwa za kumtafuta, kufuatia kufariki kwa baba yake.

Kipindi cha mwanzo cha kughibu kwake aliteuwa wawaki-lishi maalumu watakao kuwa wakiwasiliana nae na kumpelekea barua za mashia na masuali yao, na pia kupokea majibu ya maswali yao, na kuyafikisha kwa wenyewe. Na mawasiliano haya yalipo onekana kuwa ni hatari vilevile, pamoja na kuwa yalikuwa yakifanywa kwa tahadhari na siri, Imamu akayamaliza mawasi-liano yale na uwakilishi ule, na mawasiliano ya moja kwa moja yakakatika, kwa pande zote, kati yake na wafuasi wake.

Na Mwenyezi Mungu atamdhihirisha baada ya kutoonekana (kughibu) kwa muda mrefu. Na atakapo dhihiri ataijaza ardhi kwa uadilifu na usawa kama ulivyo jazwa dhuluma na ujeuri. Kufuatana na bishara aliyo itowa babu yake Mtume(s.a.w.w) kwenye hadithi nyingi kama kauli yake isemayo:

"Hakika Ali ni wasii wangu na katika kizazi chake atatoka Al-qaa'im Almuntadhwar Mahdi " (Mwenye kufanya mapinduzi mwenye kusubiriwa kuja kwake alieongozwa), ambae ataijaza ardhi uadilifu na usawa kama ilivyo jazwa ujeuri na dhulma".

Pia kauli yake Mtume(s.a.w.w) :

"Mfurahieni Mahdi, (au pokeeni bishara ya mahdi) ni mtu atokanae na kabila la kikuraishi, ni mtu atokanae na kizazi changu. Atatoka wakati watu watakapo tofautiana na kuwepo mtetemeko, na ataujaza ulimwengu na ardhi kwa uadilifu na usawa kama ulivyo jazwa dhuluma na ujeuri ".[65]

Na kutokana na umuhimu wa maudhui ya Mahdi tumeyawekea kitabu makhsusi na tumegawanya mazungumzo yake katika sehemu tatu:

Sehemu ya kwanza ina husu kuitoa na kuiweka wazi fikra ya "Al-mahdi" na kiwango cha mahusiano na maungano yake na uislamu.

Na sehemu ya pili, inaelekea kwenye suala la kumbainisha na kumu ainisha "Mahdi" kutokana na dalili za hadithi za Mtume zilizokubaliwa kati ya waislamu wote.

Na sehemu ya tatu, inazungumzia uwezekano wa kughibu kwa Imamu na dalili zake. Na mwenye kutaka ufafanuzi zaidi arejee kwenye vitabu tulivyo viashiria hapo kabla.

Na baada ya hayo: Huu ndio "uimamu" kama ambavyo akili ilivyo tuongoza na kama dalili zilizo nukuliwa zilivyo eleza wazi. Na hizi ndio "dalili" zikiwa wazi na zikiainisha na kupambanua. Na hawa ndio "maimamu" na urithi wao ulio mkubwa, na historia yao yenye kutoa marashi (yaani nzuri) na mienendo yao yenye kupendeza na kuvutia. Je msomaji anaona ya kuwa kuwa-fuata na kupitia kwenye miongozo yao na kufuata nyayo zao ni kutoka kwenye uislamu na kuwafuata mayahudi?

Na je inafaa kusemwa, kutokana na yote yaliyo tangulia, ya kuwa ushia umedhihiri kwenye zama za khalifa Othumani binil Afan na kufuatia mapinduzi dhidi yake yaliyo fanywa na waislamu kupitia kwa yahudi alie ingia kwenye Uislamu kwa ajili ya kuubomoa uislamu aitwae Abdallah bin Sabai?!

Je Abdallah bin Sabai, ana uhakika wowote wa kuwepo kwenye historia ili awe atanasibishiwa kuanzisha Ushia na kuweka misingi yake?! Hakika Dr.Barnado Luise alilizingatia Suala la kuwepo Abdallah bin Sabai kuwa ni suala au picha iliyo simama kwenye msingi wa khayali na dhana, na akasisitiza kuwa mambo aliyo husishwa nayo ni mambo yaliyo undwa na watu walio kuja mwishoni.[66]

Naye Dr Twaha Hussen ameyatilia shaka mambo yote yaliyo nasibishwa kwa Ibnu Sabai miongoni mwa matukio mbali mbali na akaweka maelezo yake juu ya riwaya za wanahistoria kwa kusema:"Ni uovu ulioje wa masingizio waliyoyasingizia maadui wa mashia kwa mashia!.[67]

Naye Dr. Jawad Ali amezitilia shaka habari zinazo husiana na Ibnu Sabai kwa sababu riwaya zote zimetoka kwa Saifu bin Omar, na hazitoki kwa mwenginewe.Na Saifu huyu ametuhumiwa kuhusu ukweli wake na riwaya zake.[68]

Naye Dr. Ali Al-ward, ameonelea kuwa Ibnu Sabai ni jina la umashuhuri walilo litoa bani umayya na kulitumia kwa sahaba mtukufu Ammar bin Yaasir, na akatoa dalili kadhaa zinazo unga mkono maneno yake juu ya rai yake hiyo.[69]

Kisha akaja Ustadh Ahmad Abbas Swaleh mwishoni na kutilia mkazo kuwa "Ni ukosefu wa akili kufikiria kuwa huenda yupo kweli mtu kama huyu". Na akasema katika mazungumzo yake kuhusiana na Ibnu Sabai yafuatayo:

"Na Abdallah bin Sabai ni mtu wa kupandikizwa bila shaka yoyote..na fikra yenye kuelekea kuunda mtu kama huyu wa kupandikizwa asie na ukweli wowote ni fikra finyu na potovu bila shaka yoyote, ili aipe athari katika matukio yaliyo tokea" na "visa vyote vilivyo undwa kuhusiana na Abdallah bin Sabai ni mambo yaliyo wekwa (kutungwa) na watu walio kuja nyuma wala hakuna dalili juu ya kuwepo kwake kwenye vitabu mama vya zamani ukiachilia mbali ubovu wa fikra hiyo ya kutarajia kuwa na asili ya kuwepo kwake".[70]

Na ikiwa Ibnu Sabai, kama tulivyo tangulia kusema, ni mtu wa kupandikizwa, na historia haikupata habari zake wala kumjua, basi ni nani alianzisha Ushia? Na ni nani alikuwa wa mwanzo kulitumia neno hilo?

Jawabu :

Hakika ni Muhammad bin Abdillah(s.a.w.w) mwenyewe. Twabari na Al-haafidh bin Hajari wametoa kwa mashekhe wao ambao ni mahufadhi walio mashuhuri, kwamba Mtume(s.a.w.w) siku moja alisoma kauli ya Mwenyezi Mungu:"Hakika wale ambao wameamini, na wakafanya matendo mema, hao ndio viumbe bora zaidi". Kisha akamgeukia Ali bin Abi Twalib (a.s) na kusema: "Watu hao ni wewe na mashia wako (wafuasi wako).[71]

Na ikiwa Muhammad bin Abdillah(s.a.w.w) ndie wa mwanzo kutumia neno hili na akawakusudia kwa kutumia wafuasi wa Ali kwa dhati, basi Ushia hautadhurika na maneno au uzushi wa wazushao maneno ya uongo, na shaka za wenye kuutilia shaka na kauli za wasemao.

Na sifa zote ni za Mwenyezi Mungu ambae ametuongoza kwa hili na hatukuwa ni wenye kuongoka kama si Mwenyezi Mungu kutuongoza, na amani ziwe juu ya mitume wote na himidi zote ni za Mola wa viumbe wote.

Na huwenda mwenye kufanya utafiti na mdadisi wa hali iliyokuwa wakati wa kufariki Mtume(s.a.w.w) atafahamu kiukamilifu hali hiyo na mambo mengine yaliyo kuwa yakitarajiwa kutokea. Na alifahamu hivyo kwa hukumu ya ufahamu wake wa ukweli wa mambo, na kwa hukumu ya kupewa habari na Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya hayo yatakayo tokea kama Mwenyezi Mungu alivyo sema: "Je ikiwa atafariki au kuuwawa mtageuka na kurudi kwenye visigino vyenu ".

Sasa kwa nini Mtume hakumteua na mtu mwengine akateua? Je Muhammad alikuwa ana ufahamu mdogo zaidi wa kuijua hatari na kuhis i majukumu juu ya umma huu kuliko walioteua?

Ili kujua kuwa Fatima ndie binti pekee wa Mtume rejea kwenye bahthi yetu kuhusu "Utume"katika ukurasa wa 45-55-chapa ya Baghdad 1392 H.

Mtume alimpa habari kwamba yeye atapigana vita na watu hawa, rejea Taarikhu Baghdaad Juzuu 8/340 na 13/187 na Al-istiaab 3/53.Ili kujua usiku alio kufa rejea Muruju Adhahabi:2/291,na al-kaafi 1/452, na pia Irshaad-6 na Twabari, kwenye historia yake amesema katika juzuu 5/143 kuwa pigo la Abdurrahman bin Muljim alilo mpiga Ali lilikuwa usiku wa 17 au 19 na kutokana na kuwa alibakia hai kwa muda wa siku mbili baada ya pigo hilo kifo chake kinakuwa usiku wa 21 kulingana na mojawapo kati ya riwaya mbili za Twabari.

MAHDI MTARAJIWA KATI YA TASWAWWUR NA TASDIQ

KUMFAHAMU NA KUMSADIKI

"Na hakika yeye ni alama ya Kiama ". Suratu-Zukhruf:61

Muqaatil bin Sulaiman amesema na mufasirina wengine walio mfuata: "Hakika aya hii imeteremka kumhusu Almahdi".

Ibn Hajar Al-haitami As-shaafii: Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Ili aidhihirishe juu ya dini zote, hata kama washirikina watachukia". Surat Aswaf:9.

Said bin Jubair amesema: "Ni Mahdi atokanae na kizazi cha Fatima(a.s) ".

Al-haafidh Al-Kanjiy As-shaafii.

UTANGULIZI

Kwa jinala Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema

Mwenye kurehemu.

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu kwa neema alizotoa na kutupa ilhaam. Na rehma za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad na Ali zake wema.

Zilitolewa na kuzalishwa shub'ha na shaka kuhusu maudhui ya Mahdi mtarajiwa na kutawaliwa na majibizano, kati ya viku-ndi vya waislamu, hata baadhi ya waandishi na watunzi wa vitabu kufikia hatua ya kusema na kuona kuwa kumuamini Mahdi au fikra ya Mahdi ni sawa na kuamini mambo yaliyo pandikizwa yasiyo na ukweli au kuamini visa vya watu wa kale.

Kwa hivyo ilikuwa ni lazima kwa watafiti walio jihusisha na masomo ya kiislam, kutokana na hali hii, kuyaelekea na kuyafanyia utafiti maudhui haya, kwa kiwango kikubwa na kuyapa umuhimu mkubwa, na kuziandaa kalamu zao kwa ajili ya utafiti kuhusu masuala haya kwa uhuru kamili na uwazi, ili waweze kuondoa shub'ha zenye kutokea, na kuzibatilisha shaka zitokanazo na dhana, na kuyabatilisha madai yaliyo zuiliwa, na kuondoa pazia kwenye ukweli ulio wazi ili uweze kuonekana mbele ya watu wote kwa uhakika wake wa Uislamu au kama yalivyo kiuhakika wake ndani ya Uislamu wenye kumeremeta na kutoa mwanga.

Na huenda kati ya watu kuna wanao dhania kwamba kuyazungumziya maudhui haya na mengine mfano wake ni miongoni mwa mas'ala ambayo yanaweka kizuwizi cha kuleta ukaribu na kuelewana kati ya waislamu na kuchochea moto wa tofauti kati yao uzidi kuwaka na kulindima, na kwamba kuweka na kubakiza sitara au pazia kwenye mambo haya ni vizuri na ni jambo lenye manufaa zaidi, lakini kufikiria hivyo, kama ninavyo amini, ni dhana zisizo kuwa na ukweli na zisizo ufikia ukweli kwa aina yoyote, kwa sababu kuficha jambo haijawahi kuwa ni utatuzi wa matatizo kama haya, bali kufanya hivyo hakutatoa athari yoyote isipokuwa ni kuandaa mazingira mapana ya kupatikana dhana mbaya na kubobea hali ya kutofautiana na kuyachanganya mambo tofauti, kwa sababu hii kufanya utafiti wa makusudi kabisa kwa uwazi na ukweli ni jambo lenye athari ya upeo wa juu na lenye faida nyingi, kwani ukweli utadhihiri (uliokua haufaha-miki) na uongo wa kuunda na ulio zuliwa utakuwa wazi, na madirisha au nafasi za kutia shaka na kutoamini zitajifunga.

Na kutokana na haya, matarajio yangu kwenye kurasa hizi yalikuwa ni kwamba hizi kurasa ziwe hatua tuzifanyazo kwenye njia hii kuelekea kwenye lengo kubwa na ziweze kuwa juhudi zenye nia safi katika kujaribu kuleta mtazamo ulio salama na mafundisho yaliyo wazi na kuziba nyufa.

Na katika kijitabu hiki sintakuwa na nafasi kubwa -kwani kinaandikwa kwa msukumo huu mtukufu na kutaka kulithibi-tisha lengo hilo la juu kabisa- isipokuwa ni kuyadhihirisha kwa ukweli na kutoa hukumu iliyo salama, na kufanya utafiti ulio epukana na matamanio na mapenzi ya upande fulani.

Na matarajio yangu yote ni kuwa msomaji mtukufu apate ndani yake dalili zitakazo ondoa wingu jeusi ambalo limetanda juu ya maudhui haya kwa karne zote zilizo pita na apate dalili zinazo weka wazi msimamo wa Shia Imamiyya kuhusu mas'ala ya Mahdi na (kuhusu) fikira ya Mahdi.

Na himidi zote ni za Mwenyezi Mungu ambae alituongoza kwa hili, na hatukuwa ni wenye kuongoka lau kama si Mwenyezi Mungu kutuongoza.

MUHAMMAD HASSAN AALU-YAASIN

Muhtasari wa maudhui tuliyo yamaliza kwenye utafiti wa "Uimamu"[72] ni kuwa Uimamu kwa hukumu ya Hadithi, Qur'an na Akili ni sehemu ikamilishayo ujumbe, na ni sehemu iufanyayo ujumbe wa kiislamu uendelee kuwepo, na kwamba dalili zote zilizo julisha ulazima wa kuwepo utume na uwajibu wake zinafaa kuzinukulu na kuzitumia kutolea dalili juu ya ulazima wa kuwepo uimamu, kwa sababu kuwepo kwa utume bila ya uimamu ni kuwepo kuliko katika kusiko endelea, na hali hiyo inapingana na jengo la Uislamu lililo simama juu ya msingi wa kuendelea ujumbe hadi siku ya mwisho.

Kwa hivyo basi utume ni mwanzo wa uhai, na uimamu ni kuendelea kwa uhai ule na lau kama ingefaa kwetu kusema na kukubali utume bila uimamu, ingefaa kusema kuwa ujumbe wa Mtume una mtazamo finyu na wenye mipaka maalumu, hauku-weza wenyewe kujikadiria umri wa kuendelea kuwepo baada ya uhai wa Mtume wake, na haukuweka akiba kwa ajili ya kuyathi-bitisha malengo yake kwa kumteua Wasii ili aendeleze kazi na kuwepo kwa ujumbe wake.

Na ukweli ni kwamba, lau kama usia usingethibiti kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwa njia ya riwaya na habari zilizo nukuliwa, hakika akili pekee ni yenye kuhukumu ulazima wa kuwepo usia na kuwa ulifanyika, na kwamba mtu yeyote miongoni mwetu haridhii kughibu na kuacha mali zake ziwezazo kutoweka au kufa na kuacha vitu mbali mbali hata kama ni vichache, bila kuzikabidhi mali hizi au zile kwa mtu alie muusia na muaminifu aziendeshe na kuzipangilia na kuzilinda.

Basi je ina juzu kwa Mtume wa Uislamu kuuacha urithi wake mkubwa, urithi ambao ni wa watu au wanadamu kwa zama zote, bila kumuweka wasii atakae uchunga na kuulinda urithi huu na kuuangalia kama inavyo stahili?!

Hakika mazingira yote yaliyo uzunguka Uislamu siku au wakati alipo fariki Mtume(s.a.w.w) yanatuita na kutulingania kuamini kuwa Mtume aliusia, na kwamba hakuliacha pandikizo lake lenye baraka jangwani, lipigwe na upepo mkali au joto kali lenye kuunguza au tukio lenye kulitokea, na kulifanya litoweke. Na hivyohivyo ina dhihiri wazi kuwa Shia Imamiyya hawakutoa maneno yahusianayo na kupinga kwao uchaguzi kutokana na hisia ya chuki kwa mtu fulani, au kutokana na rai yao ya kisiasa kwa maana ifahamikayo na yenye kuenea ya siasa, bali waliona kwenye Qur'an na Hadith dhamana sahihi ya maisha na nyenzo ya ujenzi iliyo salama, na basi wakawa wamevutiwa katika kuunga mkono rai hii kwa roho ya imani juu ya Uislamu na ikhlasi kwa ajili ya malengo na kuhisi maslahi ya Uislamu.

Ali bin Abi Twalib(a.s) alikuwa ni Imamu wa kwanza alie thibitishwa kwa dalili kwani riwaya za Mtume(s.a.w.w) ni nyingi sana nani "mutawaatiri" kumhusu yeye, baadhi zikimuelezea wazi na zingine zikimuashiria. Na riwaya zote hizo pamoja na kutofautiana matukio yake na minasaba yake na mifumo yake zinalenga, kama tulivyo tangulia kusema, kwenye kitu kimoja nacho ni kumteua mwenye cheo cha uimamu na ukhalifa baada ya kufa kwake Mtume(s.a.w.w) .

Na imamu wa pili alikuwa ni Hassan bin Ali Na watatu ni Hussen bin Ali. Na wa nne ni Ali bin Hussen Assajad. Na wa tano Muhammad bin Ali Albaaqir. Na wa sita ni Jaafar bin Muhammad Asswadiq. Na wa saba Mussa bin Jaafar Al-kaadhim. Na wa nane Ali bin Mussa Al-ridhaa. Na wa tisa Muhammad bin Ali Al-jawaad. Na wa kumi ni Ali bin Muhammad Alhaadi. Na wa kumi na moja ni Al-Hassani bin Ali Al-askari. Kisha alikuwa Muhammad binil-Hassan al mahdi ndie Imamu wa kumi na mbili[73] , na alighibu kwenye macho ya watu hadi Mwenyezi Mungu atakapo toa idhini ya kudhihiri kwake na "kuujaza ulimwengu kutokana na yeye, uadilifu na usawa kama ulivyo jawa na dhuluma na ujeuri"[74] .

Na mishale ya kutuhumu na kupinga ikamuelekea Almahdy kwa nguvu zote na kwa kutia mkazo na kusisitiza, na maneno yakawa mengi kwenye maudhui haya ya ghaiba (kufichika na kutoonekana) hadi kufunikwa na mawingu mazito ambayo hayakuwezeshi kuona na kufahamu na kukupa uwezo wa kudadisi na kupambanua lililo sahihi, na watafiti wengi ambao ni wenye ikhlasi wakajiweka kando na maudhui haya kwa kuyakimbia matatizo yake na ugunu wake, na sauti za wapingaji zikaja juu na kusikika kwa kudhalilisha na kufanya istihizaa nazo zikidhania kuwa silaha yake iliyo simama kwenye msingi wa kufanya maskhara na kutoa hila kuwa ni silaha kali yenye kukata isiyo katwa na wala haishindwi.

Na hivyo ndivyo utafiti wa "Almahdi na fikra ya kuwepo Almahdi" ulivyo jitenga na kuwa mbali na mfumo wa kielimu ulio salama. Na ukawa si utafiti wa kimaudhui wenye amani na ikhlasi, na ukawa chini ya msukumo wa mapenzi ya nafsi yaliyo mbali na akili na mantiki.

Na kutokana na hayo ilikuwa mfumo wetu kwenye kijitabu hiki ni lazima ufuate upande na mfumo usiofuata mapenzi na uwe ni mfumo wa kimaudhui, ili tujiepushe na tofauti ambazo wengi walizitumbukia. Na mfumo huu utasimama juu ya msingi wa kuyagawa mazungumzo hayo sehemu tatu

Sehemu ya kwanza inakusudia kuitoa fikra yenyewe ya (Mahdi) na jinsi mahusiano yake na Uislamu yalivyo, na sehemu ya pili inaelekea kumuonyesha na kumuainisha (Mahdi) kwenye dalili zilizo pokelewa za Mtume, na sehemu ya tatu inazungumzia maudhui ya uwezekano wa kughibu na kutoonekana, na dalili zake.

Na mwendo huu ulioandaliwa na ufanyao uchunguzi, kama ninavyo itakidi, utachukuwa dhamana ya kutoa ufafanuzi na kuweka wazi kiukamilifu mambo yatakavyo gundulika na kupatikana kwenye mwendo huu na matokeo yake, na kutoa ufahamu makini wa matatizo yake kwa uhakika wake na ukweli wake wa asili ulio mbali na mapenzi na matamanio na malengo mengine.