• Anza
  • Iliyopita
  • 21 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 10406 / Pakua: 967
Kiwango Kiwango Kiwango
MAISHA YA ABU DHARR

MAISHA YA ABU DHARR

Mwandishi:
Swahili

5

MAISHA YA ABU DHARR

Kwa mujibu wa hadithi ya Mtukufu Mtume, Abu Dharr aliona ndoa ni jambo la muhimu. Alioa lakini kwake ndoa kamwe haikuwa na maana ya starehe na furaha. Alidhani kwamba ndoa ilikuwa ni jina la kufuata Hadith ya Mtukufu Mtume. Inaeleweka kwamba alifuatana na mke wake popote alipokwenda.

Kwa kuwa mke wake alitoka Afrika, wakati fulani watu walisema, "wewe unaye mke mweusi?" Alijibu, "Nafikiri ni bora zaidi kuwa na mke mweusi na mwenye sura mbaya kuliko mke wenye sura inayopendeza na watu wanitembelee kwa sababu tu ya uzuri wa sura ya mke wangu." Abu Dharr alikuwa anamjali sana mkewe.

Ukarimu si tu ndio mojawapo ya sifa bora sana, lakini ni kiini cha ubinadamu. Jinsi mtu anavyozidi kutambua kanuni za Uislamu ndivyo anayozidi kujaa moyo wa huruma.

Naim Bin Qanat Riyath anasema, "Siku moja nilikwenda kumtembelea Abu Dharr na nikamwambia kwamba ninampenda na ninamdharau wakati huo huo." Abu Dharr akasema, "Inawezekanaje hali hizi mbili zije pamoja?" Nilisema, "Nimekuwa nikiwaua watoto wangu. Sasa nimetambua kwamba hicho ni kitendo kiovu. Kwa hiyo, kila mara ninapofikiria kuja kwako kukuuliza kuhusu vipi nitaokolewa na kusamehewa, hisia hizi kubwa zinapanda pamoja. Nilipofikiria kwamba ingekuwa bora kama ungeniambia kuhusu ufumbuzi wake hisia za mapenzi zilipanda juu sana, lakini nilipofikiria kwamba ningeumia daima milele endapo ungetangaza kwamba dhambi hiyo haisameheki, chuki dhidi yako ilizidi kuongezeka. Sasa nimekuja kutaka kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili."

Abu Dharr alisema, Sawa! Niambie endapo umefanya yote haya mnamo siku za ujahilia au baada ya kuingia kwenye Uislamu?

Nilisema, "Wakati wa ujahilia." Abu Dharr akasema, "Dhambi yako imesamehewa. Uislamu ni ukombozi wa uchafu wa aina hiyo yote na dhambi zote."

Niliposikia hivi niliridhika. Baadae nilitaka kuondoka akasema, "Ngoja!" Na nilifuata maelekezo yake.

"Baadaye alimwambia mkewe kwa alama alete chakula ambaye alikwenda ndani na akarudi akiwa na chakula. Abu Dharr alisema, "Naim, Bismillah (maana yake kula katika jina la Mwenyezi Mungu).

Kabla sijaanza kula nilimwambia tule wote. Akasema, "Mimi nimo kwenye Swaumu." Aliposema hivi akaanza kuswali. Mimi nikaanza kula na nilipokaribia kumaliza, naye akamaliza Swala na akaanza kula.

Nilisema, "kusema uongo ni dhambi kubwa katika Uislamu na hata kama nikimdhania mtu fulani kuwa ni mwongo inawezekana kwamba anaweza kuwa mwongo, lakini nikufikirie vipi wewe?"

Abu Dharr alisema, "Umekaa muda mrefu na mimi. Jambo gani limekufanya unifikirie mimi kuwa ni mwongo?" Nikasema, "Muda mfupi uiliopita uliniambia kwamba unafunga Swaumu na sasa unakula na mimi."

Aliniambia, "Sijakuambia uongo. Nimefunga Swaumu na wakati huo huo ninakula na wewe."

Akasema, Mtukufu Mtume amesema kwamba yeyote anayefunga Swaumu terehe 13, 14, na 15 ya mwezi huu wa Shabani, kwa namna nyingine ni sawa kama amefunga Swaumu ya mwezi mzima. Kwa maneno mengine, atapata thawabu ya kufunga Swaumu ya siku thelathini yaani kila Saumu ya siku moja inabeba uzito wa Swaumu ya siku kumi. Kwa kuwa nimefunga Swaumu katika siku hizi ninayo haki ya kusema kwamba ninafunga Swaumu ya mwezi mzima." (Musnad Ahmad bin Hanbal na Hayatul Qulubi-Allamah Majlis).

Alamah Bayhaqi pia amesimulia tukio la aina hiyo hiyo. Muhtasari wake ni kama ifuatavyo:

Siku moja Abu Dharr na Abdullah bin Shafiq Uqaili walikwenda nyumbani kwa mtu kama wageni. Abu Dharr alikwisha sema kwamba yeye anafunga Saumu na chakula kilipoletwa alianza kula. Abdullah alidokeza, "Wewe unafunga Saumu." Abu Dharr alisema, "Ninaikumbuka Swaumu yangu. Sijaisahau Saumu yangu. Kila mara nipo makini kufunga Swaumu katika hizo siku tatu za kila mwezi ambazo huitwa "Ayyam al-Beydh." na kwa mujibu wa hadithi ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , uelewe kwamba mimi ninafunga Saumu (Sunan Bayhaqi).

SURA YA SITA

Shahidi Thalit Allamah Nurullah Shustari ameandika: Abu Dharr alikuwa mmoja wa masahaba mashuhuri sana na anahesabiwa miongoni mwa masahaba wa mwanzo kabisa walioingia kwenye Uislamu. Katika kuukubali Uislamu alikuwa mtu wa tatu, hivyo kwamba, aliingia kwenye Uislamu baada ya mama wa Waumini Khadijahtul Kubra na Amiri wa Waumini Ali. Kwa mujibu wa mwandishi wa kitabu cha 'Isti'ab' alikuwa na sifa ya juu katika ujuzi, kushikilia maadili, uchaji Mungu na kuwa mkweli, miongoni mwa masahaba wote. Ali amesema kwamba, Abu Dharr alifanikiwa nafasi hiyo katika kupata na kuelewa mafundisho ya kidini ambayo hakuna mwingine ambaye angeyafikia. Mtukufu Mtume alikuwa anasema, "Abu Dharr yu kama Mtume Isa katika umma wangu. Abu Dharr anashikilia maadili kama alivyofanya Mtume Isa."

Kwa mujibu wa hadithi, mtu anayetaka kuona mfano wa Mtume Isa amuone Abu Dharr. Shaykh Saduq katika kitabu chake Uyumul Akhbar al-Ridha ameandika kwamba Imamu Ali al-Ridha amesema kutoka kwa mamlaka ya wahenga wake kwamba kwa mujibu wa Hadith ya Mtume, "Abu Dharr ni mtu mkweli wa umma huu."

Ali anasema kwamba Abu Dharr ndiye mtu peke yake asiye jali kamwe kushutumiwa kwa sababu ya Mwenyezi Mungu maamrisho na maagizo yake, ni kwamba, yeye alisema lolote ambalo ni haki na atatekeleza kwa vitendo, na wala hatajali vitisho vyovyote kuhusu jambo hili, ama kuogopeshwa na uwezo wa serikali.

Wanavyuoni wameandika kwamba Abu Dharr alitoa kiapo cha uaminifu kwa Mtume kwa ahadi kwamba katika imani ya Mwenyezi Mungu hangejali mtu yeyote anaye mshutumu na kwamba angesema ukweli hata ungelikuwa na athari ya aina yoyote ile.

Ukweli na ujasiri ni sifa ambazo hata watu mashuhuri sana hushindwa kushikilia. Mtukufu Mtume ameitabiri sifa hii ya Abu Dharr na akasema kwamba Abu Dharr angetoa mchango mkubwa katika jambo hili na ataendelea kushikilia hata katika mateso makali ambayo angeyavumulia.

Mtume alisema: "Hapana mtu mkweli zaidi ya Abu Dharr kati ya utando wa anga na ardhi ." [3] .

Katika ufafanuzi wa hadithi hii Allamah Subaiti ameandika: "Mtukufu Mtume aliwahutubia masahaba wake alisema: "Enyi masahaba wangu! Ni nani miongoni mwenu ambaye atakutana na mimi mnamo siku ya Hesabu katika hali hiyo hiyo ambayo nitamwacha nayo hapa duniani? "

Waliposikia hivi, kila mmoja wao alinyamanza kimya isipokuwa Abu Dharr aliyesema kuwa mtu huyo ni yeye. Mtukufu Mtume akasema: "Bila shaka! umesema kweli ."

Baada ya hapo, aliongeza, "Enyi masahaba wangu! kumbukeni ninayowaambieni. Hakuna mtu kati ya mbingu na dunia ambaye ni mkweli zaidi kuliko Abu Dharr ."[4] .

Allamah Majlis ameandika maelezo baada ya kunukuu hadithi hiyo hapo juu kwenye kitabu chake (Hayatul Qulub).

Bin Babwayh ameeleza kupitia mamlaka ya kuaminika kwamba mtu fulani alimuuliza Imamu al-Sadiq endapo Abu Dharr alikuwa bora zaidi ya Ahlul -Bait wa Mtukufu Mtume au vinginevyo. Imamu Alisema, "Mwaka mmoja una miezi mingapi?" Alijibu, "Kumi na miwili." Imamu akasema, "Miongoni mwa miezi hiyo mingapi

inaheshimika na kutakaswa?" Akasema, "Miezi minne," Imamu aliuliza, "Mwezi wa Ramadhani umejumuishwa katika miezi hii minne?" Akasema, "Hapana." Imamu aliuliza, "Mwezi wa Ramadhani ni bora zaidi au miezi hiyo ni bora zaidi."

Akajibu, Mwezi wa Ramadhani ni bora zaidi." Imamu Akasema, "Ndivyo ilivyo na sisi, Ahlul-Bait. Huwezi kumlinganisha yeyote na sisi."

Siku moja Abu Dharr alikuwa ameketi katika kundi la watu ambao walikuwa wanaeleza maadili ya taifa hili. Abu Dharr alisema, "Ali ni bora kuliko wote katika taifa hili, na yeye ni mpaka wa Pepo na Jahanamu, ni Siddiq na Farooq wa Umma na utibitisho wa ujuzi wa mambo ya dini wa taifa hili." Waliposikia maelezo haya kutoka kwake wanafiki hao waligeuza nyuso zao na kutazama upande mwingine na kukanusha tamko lake na kumwita muongo. Haraka Abu Amamah alinyanyuka na akaenda kwa Mtukufu Mtume na kumwambia alichosema Abu Dharr, na jinsi kundi hilo lilivyokataa kukubali. Mtukufu Mtume akasema, "Hapana mtu kati ya ardhi na mbingu ambaye ni mkweli kuliko Abu Dharr."

Kitabu hiki hiki kimeeleza kupitia mamlaka nyingine kwamba mtu mmoja alimuuliza Imamu Jafar al-Saqiq endapo hadhithi hiyo ilikuwa sahihi ambamo Mtukufu Mtume ametangaza hivyo. Imamu alisema, "Ndio." Akasema, "Kama ndio hivyo, Mtukufu Mtume, Ali, Imamu Hasan, na Imamu Husein na nafasi yao ni ipi?"

Imamu akajibu, "Sisi ni kama mwezi wa Ramadhani ambao ndani mwake upo usiku huo ambao ibada yake ni sawa na ile ya miezi elfu moja ambapo masahaba ni sawa na mwezi unao heshimika

ikilinganishwa na miezi mingine, na hapana mtu anayeweza kulinganishwa na sisi, Ahlul-Bait."

Ni dhahiri kama mwanga wa mchana kutoka kwenye hadithi hiyo hapo juu ya Mtukufu Mtume kwamba Abu Dharr alikuwa hana wa kumlinganisha naye katika ukweli.

Maelezo na ufafanuzi wa hadithi hii hii kama yalivyotolewa na Subaiti inaeleza kwamba Abu Dharr ataondoka hapa duniani akiwa katika hali ile ile ambayo Mtume alimwacha nayo, na atamuona akiwa katika hali hiyo hiyo huko Peponi.

Kama hadithi hii ikitazamwa kwa umakini zaidi, msimamo imara wa Abu Dharr kwenye njia ambayo iliimarishwa na Mtukufu Mtume unadhihirisha uadilifu wake. Wanavyuo wanakubaliana kwenye mtazamo huu kwamba Abu Dharr hakutetereka hata nchi moja kutoka katika njia ya Mtukufu Mtume. Baada ya Mtume, hata sabaha kama Salman alilazimishwa kutoa kiapo cha utii na siku moja alipigwa sana ndani ya msikiti hadi shingo yake ikavimba. Lakini Abu Dharr kamwe hakunyamaza.

Allamah Subaiti ameandika: "Abu Dharr alikuwa mmojawapo wa wafuasi wa Mtukufu Mtume ambao walishika njia yao na walisimama imara kuhusu agano lao walilofanya na Mwenyezi Mungu. Ali mtu Mtukufu Mtume kwa uaminifu, alifuata nyayo zake na kuiga mwenendo wake. Hakuachana na Imamu Ali hata kidogo, alimfuata hdi mwisho na akapata faida ya nuru ya ujuzi wake.

Allamah Majlis ameandika: "Bin Babwayh anaeleza kupitia kwa mamlaka ya kuaminika kutoka kwa Imamu Ja'far al-Sadiq kwamba siku moja Abu Dharr alikuwa anapita karibu na Mtume wakati Jibril alikuwa anazungumza naye katika faragha katika

umbile la 'Dahyah Kalbi.' Abu Dharr alirudi nyuma kwa kudhani kwamba Dahyah Kalbi alikuwa anazungumza na Mtume kwenye faragha. Aliporudi Jibril alimwambia Mtume, "Ewe Muhammad! Abu Dharr alikuja muda mfupi uliopita na akarudi bila kunisalimia. Amini kwamba endapo angenisalimia, hakika ningejibu salamu yake. Ewe Muhammad! Abu Dharr anayo dua yake ambayo inajulikana kwa watu wa Peponi. Tazama! Nitakapoandoka kwenda mbinguzi muulize kuhusu taarifa hii. Akasema, "Vema."

Jibril alipoondoka na Abu Dharr akarudi kwa Mtume, Mtume akasema; "Ewe Abu Dharr! Kwa nini hukutusalimia ulipokuja hapa muda mfupi uliopita? Abu Dharr alijibu, Nilipokuja, Dahyah Kalbi alikuwa ameketi na wewe na mlikuwa na mazungumzo. Nilidhani mnazungumza kuhusu mambo fulani ya siri na mimi sikuona vema kuingilia kati.

Kwa hiyo nikarudi. Mtukufu Mtume akasema, "Huyo hakuwa Dahyah Kalbi lakini huyo alikuwa Jibrili aliyenijia katika umbile la Dahyah Kalbi. Ewe Abu Dharr! Alikuwa ananiambia kwamba endapo ungemsalimia naye angejibu salamu yako. Pia aliniambia kwamba unayo dua ambayo inajulikana sana miongoni mwa watu wa Peponi." Abu Dharr aliondoka akiwa na haya sana na akaonyesha kujutia kitendo chake.

Halafu Mtukufu Mtume akasema, "Ewe Abu Dharr! Niambie dua unayosoma na ambalo linazungumziwa sana mbinguni" Abu Dharr akamwambia Mtume "Dua hiyo ni hii ifuatayo: Allahumma inni Asalukal Amna wal Imana bika wat tasdiqa bi nabiyyika wal 'Aafiyata min jami'il blaa'i' washukra 'alal 'afiyat wal ghina'an shirarin naasi."[5]

Zipo hadithi nyingi sana upande wa madhehebu ya Shia na Suni ambamo maagizo maalum yametolewa kuwapenda masahaba wanne. Wanavyuo wanasema kwamba masahaba hao wane ni Ali, Abu Dharr, Miqdad na Salman.

Umar Kashi ameandika kwenye Rijal yake, Abu Jafar Qummi kwenye Khasail, Abdullah Humayri kwenye Qurbul Asnad, Shaykh Mufid kwenye Iktisas, Ayashi kwenye maelezo yake, Sadiqu kwenye Uyun Akhbar al-Riza, Abdul Barr kwenye Istiab, Bin Sad kwenye Tabaqat na mwandishi wa Usudul Ghabah kwenye kitabu chake:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema kwamba Mwenyezi Mungu amemuagiza kuwaweka masahaba wangu wanne kuwa marafiki zangu na niwapende, na pia nimeambiwa kwamba Yeye pia amewafanya marafiki masahaba hao majina yao ni haya: Ali bin Abi Talib, Abu Dharr Al-Ghifari, Miqdad bin Al-Aswad na Salman Farsi[6] .

Hadithi inasema kwamba hao masahaba wanne ni Salman, Abu Dharr, Miqdad na Ammar. Wanachuo wanafikiria kwamba hawa masahaba wanne ambao Pepo na wakazi wa Pepo wanawapenda sana. Inasimuliwa kwenye hadithi kwamba ambapo mtangazaji atatangaza mnamo siku ya Hukumu, "Wako wapi hao masahaba wa Muhammad bin Abdullah ambao hawakuvunja ahadi yao ya kuwapenda Ahlul Bait al-Risalah, lakini walikuwa imara kuendelea nayo?" Salman, Miqdadi, na Abu Dharr watasimama.

Allamah Nuri ameandika kwa kumnukuu Raudhatul Waidhin cha Shaykh Shahia Muhammad bin Ahmad bin Ali bin Fital Naishapuri

kwamba Imamu Muhammad al-Baqir amesema, zimo daraja kumi za imani. Miqdad amepata daraja nane, Abu Dharr amepata daraja tisa na Salman amepata zote kumi.

Dhamana ya udugu inakumbusha hilo tukio la kihistoria ambalo Mtukufu Mtume aliasisi udugu katika jozi moja ya masahaba wake kabla na baada ya kuhamia Madina.

Kabla ya Hijiriya aliasisi dhamana ya udugu baina ya kila masahaba wawili ili kwamba waweze kuhurumiana kwenye udugu huu alifikiria mfanano wa tabia wa masahaba wawili. Aliwafanya hao masahaba wawili kuwa ndugu wa kila mmoja kwa kua tabia zao zilikuwa zinafanana na kulingana kwa mwenendo. Kwa njia hii alitangaza udugu kati ya Abu Bakr na Umar, Talhah na Zubayr, Uthman na Abdur Rahman bin Auf, Hamza na Zayd bin Harith, Salman na Abu Dharr na Ali na yeye Mtume.

Halafu baada ya miezi mitano au minane, baada ya Hijiriya, Mtume(s.a.w.w) kwa mara nyingine aliasisi dhamana ya udugu kwa njia ile ile. Ilikuwa muhimu kuanzisha udugu baina ya wahamiaji na wenyeji wa Madina kwa lengo la kujenga misingi ya kuhurumiana baina yao. Mtume alianzisha udugu miongoni mwa masahaba hamsini.

Allamah Sahibli Nomani ameandika: "Kwenye himaya ya Uislamu yapo maadili na tabia safi sana. Ilikuwa ilizingatiwa kwamba masahaba ambao walipewa dhamana ya udugu baina yao walikuwa na mfanano wa upendeleo. Muungano huu wa upendeleo baina ya mwalimu na mwanafunzi ni muhimu kwa lengo la usilimishaji wa ujuzi. Baada ya kuuliza kupima ilionekana kwamba muungano huu wa upendeleo wa hao wawili waliofanywa ndugu ulizingatiwa na tunapoona kwamba ni kama vile haiwezekani kuamua kikamilifu na

kwa usahihi mienendo na upendeleo wa mamia ya watu kwa muda mfupi hivyo, lazima ikubalike kwamba uamuzi wa Mtukufu Mtume ulikuwa mfano wa sifa maalumu ya Utume[7] .

Juu ya hayo, hili pia linafaa kukumbukwa kwamba Mtume hakupata mtu mwenye upendeleo unaofanana na ule wa Ali ama miongoni mwa Muhajirina (wahamiaji au Ansari). Ali akasema, "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu umeniunganisha na nani?" Akasema, "Wewe ni ndugu yangu hapa duniani na baada ya hapa duniani (Peponi)" Ndio maana ya Ali alitangaza mara kwa mara kwenye mimbari ya Msikiti wa Kufa, "Mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu na ndugu yake Mtume wa Mwenyezi Mungu."[8]

Mtukufu Mtume pia alisema kuhusu Salman, "Salman ni mmoja wetu sisi Ahlul Bait ."

Kwa maoni yangu hii pia ni mojawapo ya sifa bora za Abu Dharr kwamba mtu mwenye uamuzi ulio komaa kama Mtukufu Mtume alimtangaza kuwa ndugu yake Salman. Allamah Subaiti amenukuu usemi wa Saleh al-Ahwal ambaye alimsikia Imamu Jafar al-Sadiq akisema kwamba Mtukufu Mtume alianzisha dhamana ya udugu baina ya Salman na Abu Dharr na alimwambia Abu Dharr asije akampinga Salman.[9]

Hadith ya Abu Dharr ni ya juu sana hivyo kwamba aya za Quran Tukufu zimeteremshwa kwa ajili ya kumsifu yeye. Moja ya Aya hizo ni kama ilivyonukuliwa hapa chini:

"Hakika wale walioamini na wakatenda mema mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo ya Firdausi ." (Surah 18:107).

Imamu Jafar al-Sadiq anasema kwamba Aya hii imeteremshwa kuhusu Abu Dharr, Miqdadi, Ammar na Salman.

Kwa mujibu wa hadithi, Mtume alisema kwamba Mwenyezi Mungu alimuamuru ampende Salman, Abu Dharr, Miqdadi na Ammar na akaongeza zaidi kwamba yeye mwenyewe aliwafanya hao marafiki zake. Kwa mujibu wa hadithi nyingine Mtume alisema: "Pepo inayo shauku na watu hawa. "[10] .

Allamah Gilani ameandika kwamba heshima ya Abu Dharr na hadhi yake ni hali zilizoongezeka sana siku hadi siku katika mazingira ya Mtume, hivyo kwamba, Mtukufu Mtume alipokwenda kwenye Vita ya Zaat al-Ruqa1 alimfanya yeye kuwa mtemi wa Madina, na si yeye tu kuwa mtemi lakini kwa ajili yake wakati fulani Ghifari wengine pia walipata cheo hiki. Mathalani, Mtukufu Mtume alimteua Saya' bin Urfah al-Ghifari kama Mtemi wa Madina wakati wa Vita ya Daumatul jandal, (Zaadul Ma'ad).

Ilikuwa kawaida ya huko Arabuni kwamba wakati wowote ilipotokea mtu anapanda ngamia alimfanya mtu wake maalumu kuwa 'sanjari' wake. Sanjari alipoketi nyuma, alikuwa akishika hatamu kwa kuzungusha kiunoni. Kwa mujibu wa hadith hii ya hawaida Mtukufu Mtume pia alimfanya mtu kuwa Sanjari wake.

Wakati wa hija ya mwisho, Sanjari wake alikuwa Fazal bin Abbas bin Abdul Muttalib.

Masahaba waliona kuwa ni heshima kuwa Sanjari. Sanjari wa Mtume aliitwa'Radifun Nabi.' Wasomi wanasema kwamba Mtume zaidi alimpa heshima hii Abu Dharr. Mtume alikuwa na desturi ya kupanda wanyama wengine wadogo.

Punda pia mara nyingi walitumika kumbeba Mtume. Alikuwa na tabia ya kumruhusu Abu Dharr kukaa nyuma yake na waliendelea na safari huku wanazungumza. (Tabaqat Ibn Sa'd).

Shah Walyullah Dehlavi, anapoelezea ghasia kwenye Uislamu, ameandika kuhusu tukio la Harrah. Abu Dawudi amemnukuu Abu Dharr ambaye alisema, "Siku moja niliketi nyuma ya Mtukufu Mtume tukiwa tumepanda punda.

Tulipokuwa nje ya Madina- sehemu isiyokaliwa na watu, aliniuliza hali yangu ingekuwaje wakati njaa itakapoikumba Madina, na ningeshindwa kuvumilia kabla ya kufika msikitini baada ya kutoka kitandani mwangu." Nikasema, "Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi."

Akasema, "Ewe Abu Dharr! Usije ukaenda kuomba wakati huo." Halafu akasema, "Hali yako itakuwaje ambapo bei ya kaburi italingana na ile ya mtumwa kwa sababu ya kiasi kikubwa cha vifo?" Nikasema. "Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi." Akasema, "Ewe Abu Dharr! Jizoeze uvumilivu."

6

MAISHA YA ABU DHARR

Halafu aliuliza tena, "Ewe Abu Dharr! Hali yako itakuwaje ambapo patatokea mauaji ya haliaiki hapa Madina hivyo kwamba mawe na

mchanga vitaloa damu?" Nikajibu, "Mwenyezi Mungu na Mtume Wake wanajua zaidi." Alisema, "Wakati huo utatakiwa ukae nyumbani kwako."

Nilimuuliza, "Itabidi nishike upanga wakati huo?" Alijibu, "Kama ukifanya hivyo utafikiriwa kuwa ni mshirika wao." Halafu nilimuuliza, "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Nifanye nini wakati huo?" Alisema, "Hata kama unaogopa kwamba mng'ao wa upanga utafanya macho yako yasione vizuri, funika uso wako tu kwa kipande cha nguo yako na usipigane, lakini nyamaza kimya."

Maelezo haya yapo ukurasa wa 176 kwenye Juzuu ya 5 ya Musnad Ahmad bin Hanbal iliyochapishwa Misri. Kwamba Mtukufu Mtume alikuwa na kawaida ya kumdokeza Abu Dharr siri zake na akasema kwamba alikuwa anamwamini sana. Abu Dharr naye pia, alikuwa mwangalifu sana kuficha siri zake. Wakati wowote alipoulizwa kuhusu Hadith, alisema, "Isipokuwa mambo yale ambayo Mtukufu Mtume ameniambia kuwa ni siri, nipo tayari kukueleza kila kitu. Unaweza kuniuliza chochote unachotaka."

SURA YA SABA

Zipo nasaha nyingi ambazo Mtume alimpa Abu Dharr. Hapa tunadokeza kuhusu chache miongoni mwazo. Muhammad Harun Zangipuri ameandika ka mujibu ya mamlaka ya 'Amali' ya Shaykh Tusi kwamba Mtume alimwambia Abu Dharr: "Ewe Abu Dharr! Muabudu Mwenyezi Mungu kama vile unamuona Yeye, na Yeye Anakuona wewe na hata kama humuoni wewe." Tambua kwamba kwanza kabisa ibada Yake ni kumtambua yaani kuelewa kwamba Yeye ni wa kwanza kabla ya chochote. Yeye hana mshirika. Yeye ni wa Milele hana mwisho.

Yeye ni Muumbaji wa vitu baina ya ardhi na mbingu. Yeye Ametakasika na yumo kila mahali. Yeye hahusiki na dosari yoyote, na ni Muumbaji wa vitu vyote.

Baada ya kuelewa Upweke wa Mwenyezi Mungu ni muhimu kukubali Utume wangu na kuamini, kwamba Mwenyezi Mungu amenituma kama mjumbe wa habari njema, mwonyaji na taa nyeye nuru ya mwongozo kuwaita watu kwa Mwenyezi Mungu.

Baada ya kukubali Utume wangu, ni wajibu na muhimu kuwapenda Ahlil-Bait wangu ambao Mwenyezi Mungu ameweatakasa kutokana na uovu wote.

Zingatia kwamba vimo vitu viwili vyenye neema: Afya njema na fursa ya kufanya ibada.

Vithamini vitu vitano kabla ya vitu vitano: Thamini ujana kabla hujazeeka, afya njema kabla ya kuugua maradhi, utajiri kabla ya umaskini, starehe kabla ya kazi na uhai kabla ya kifo. Ishi duniani kama mgeni au pitisha siku zako kama mpita njia.

Unapoamka asubuhi, usiwe na matumaini ya kuiona jioni, na baada ya kupitisha siku usiwe na tegemeo la kuiona asubuhi. Chukua nafuu ya afya yako njema (kwa ajili ya kuabudu kabla hujaugua na tumia maisha (katika njia ya Mwenyezi Mungu) kabla hujafa, kwa sababu hatujui watu watatuitaje kesho tukiwa hai au tumekufa; maana yake ni kwamba hatujui endapo kesho tutakuwa hai au hapana.

Uwe bahili kuhusu maisha yako kuliko pesa zako. Kwa maneno mengine, kama vile unavyotumia fedha zako kwa kujinyima na unajaribu hutaki kutumia kitu chochote isivyofaa kwa njia ile ile,

unatakiwa kuwa bahili kuhusu maisha yako na jaribu kutokufuja katika matendo ya uovu.

Mnamo siku ya Hesabu, Mwenyezi Mungu atawapia jicho baya kupita kiasi la kutoridhika hao Maulamaa ambao ujuzi wao haukuwanufaisha watu, au ambao wamepata ujuzi kwa lengo la kupata heshima ya kidunia bila kumnufaisha yeyote. Maulamaa wa aina hiyo, hawatanusa manukato ya Pepo.

Wakati wowote unapoulizwa kuhusu kitu ambacho hukijui, kiri ujinga wako wazi wazi. Tazama usitoe uamuzi kuhusu jambo usilolijua.

Siku inakuja ambapo baadhi ya wakazi wa Peponi watawaambia baadhi ya wakazi wa Jahanamu, "Kwa sababu gani tumeingia Peponi kwa sababu ya mafundisho yako na nasaha, lakini wewe umeingia Jahanamu?" Watajibu kwa kusema, "Tuliwaagiza wengine kufanya wema lakini sisi hatukufanya hivyo sisi."

Mwenyezi Mungu anazo haki nyingi juu yako. Ili iweze kuzitambua unatakiwa kuomba msamaha wake wakati wa kulala na unapoamka asubuhi.

Kifo kinakutafuta wewe na kinaweza kuja wakati wowote. Kwa hiyo, inatakiwa kufanya mambo mema na uharakie kufanya hivyo, na sikiliza! Mtu huvuna anachokipanda. Ngano huzaa ngano na shairi huzaa shairi. Usisahau adhabu ya matendo yako.

Watu wanaojihini ni makamanda na wanasheria ni viongozi, kuna manufaa yasiyo na mwisho kuwa karibu nao.

Muumini anafikiria dhambi kuwa mzigo mkubwa kama mlima. Anahisi kama vile anakandamizwa na mlima.

Lakini asiye muumini anafikiria dhambi kama inzi kwenye pua yake.

Usiangalie udogo wa dhambi lakini angalia unafanya dhambi hiyo kinyume cha matakwa ya nani.

Mtu ambaye ni muumini anao wasiwasi zaidi katika dunia hii kuliko ndege aliye nasa kwenye mtego wako. Anataka aondoke duniani haraka iwezekanavyo.

Si vema kuingilia katika kila jambo na unatakiwa kudhibiti ulimi wako kwa namna ile ile unavyo linda chakula chako.

Mwenyezi Mungu amezifanya Swala kuwa utulivu wa macho yako. Ewe Abu Dharr! Mtu mwenye njaa hula chakula hadi anashiba na mwenye kiu hunywa maji hadi anatosheka, lakini mimi sitosheki na Swala.

Almuradi unaswali, wewe ni kama vile unagonga mlango wa Mfalme kamili, unatakiwa utambue kwamba, kwa kugonga mlango huo mfululizo, hatimaye mlango huo hufunguka.

Usiifanye nyumba yako kama kaburi. Nyumba ambamo haisaliwi Swala imeenea giza kama kaburi. Unatakiwa kufanya mpango wa kuweka nuru kwenye kaburi lako kwa kusali ndani ya nyumba yako kwani unaposali ndani ya nyumba yako, unatia nuru kwenye kaburi lako.

Sala ni nguzo ya imani na sadaka hutakasa dhambi, lakini kudhibiti ulimi wako ni jambo la muhimu zaidi kuliko hayo mawili yaliyo tangulia kutajwa.

Mtu mwenye moyo mgumu hawezi kumkaribia Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, unatakiwa kuwa na moyo wa huruma.

Mkumbuke Mwenyezi Mungu Katika hali ya Khumul (faragha) Nilimuuliza yeye, "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Khumul ni nini?" akajibu, "Maana yake ni kumkumbuka mwenyezi Mungu katika faragha."

Mwenyezi Mungu anasema: "Mja wangu ni yule anayeniogopa. Nitamfanya mtu wa aina hii asiogope mnamo siku ya Hukumu, ikiwa ananiogopa Mimi. Hatakuwa na fadhaiko siku ya ufufuo badala yake atakuwa na amani."

Mwenye akili ni yule ambaye hunyenyekea na kufanya matendo kwa ajili ya kuingia Peponi; "Na asiye na msaada na mpumbavu ni yule anayefuata matamanio ya kidunia na hajali Pepo. Dunia na watu wa dunia wamelaaniwa. Ni vitu hivyo tu ambavyo vimetumika katika njia ya Mwenyezi Mungu, vinaweza kuwanufaisha watu wa dunia.

Mwenyezi Mungu alimfunulia ndugu yangu, Mtume Isa, "Ewe Isa! Usiipende dunia kwa sababu ni mahali pa marejeo. Kila mtu atarejea hapo na atatakiwa kutoa maelezo ya matendo yake hapo. Thawabu za matendo mazuri zitakuwa nzuri na adhabu itatolewa kwa matendo maovu.

Mwenyezi Mungu ataujaza busara moyo wa mtu anayejinyima. Ataupatia ulimi wake uwezo wa kujieleza kwa ufasaha, atamwonyesha maovu ya dunia na jinsi ya kuyaepuka na atamnyanyua kutoka hapa duniani kwa namna ambayo kwamba atafika kwenye nyumba ya amani (Darus-Salaam) kwa jinsi inayostahili.

Mwenyezi Mungu kamwe hakuamuru kukusanya utajiri. Badala yake Ameagiza Aabudiwe Yeye. Kwa hiyo, unatakiwa kuwa mchaji

Mungu, rukuu mbele Yake na uendelee kumuabudu Yeye hadi mwisho wa uhai wako.

Mimi huvaa nguo za kawaida, huketi kwenye ardhi na hupanda punda asiye na mito ya kukalia. Sikiliza! Unatakiwa kuwa mfuasi wangu na ufuate Sunna zangu. Mtu anayekataa Sunna zangu, hata hesabiwa miongoni mwa watu wangu.

Nawapongeza watu wanao hiji ni ambao hawajali mambo ya dunia na wanaielekea Pepo; ambao hukaa chini kwenye ardhi, na huifanya ardhi kuwa zulia na maji yake kuwa safi; watu ambao wanacho kitabu cha Mwenyezi mungu, Qurani Tukufu kuwa kigezo chao na maombi kuwa heshima yao, na hujitenga na dunia.

Bidhaa za dunia ni watoto na utajiri na bidhaa za Peponi ni matendo mema.

Muogope Mwenyezi Mungu na usiwajali watu. Watu watakuheshimu wewe pia ikiwa utamuogopa Mwenyezi Mungu.

Nyamaza kimya unapoona maiti imebebwa, au unapokuwa na maiti. Pia nyamaza mapigano yanapoendelea na pia unyamaze wakati Quran Tukufu inaposomwa.

Chumvi huhifadhi kila kitu kisioze, lakini chumvi ikiharibika, hakuna marekebisho (Hadith hii inahusu wanavyuo na maana yake ni kwamba imani huharibika pale ambapo wanavyuo kuwa waovu). Swala mbili fupi zikisaliwa kwa uaminifu na tafakuri ni bora zaidi kuliko Swala za usiku moja zilizosaliwa bila uaminifu.

Jiite na ujifanye unahesabiwa matendo yako mnamo Siku ya Hesabu. Kusali bila matendo mema ni sawa na kutupa mshale bila lengo.

Mtu anaposali angalipo porini, Mwenyezi Mungu huwaamuru Malaika kusimama katika safu na kusali nyuma yake na kusema Amin baada ya Swala yake alimuradi Adhan imeadhiniwa na Swala imekimiwa kabla ya Swala.

Endapo mtu anasali Swala bila ya wito huo uliotajwa hapo juu, malaika wawili tu kuamuriwa kushiriki katika Swala hiyo.

Kumkumbuka Mwenyezi Mungu miongoni mwa watu wazembe ni sawa na kupigana kwenye uwanja wa vita. Kuwa na watu wazuri ni bora zaidi kuliko kukaa katika upweke na upweke ni bora zaidi kuliko kuwa miongoni mwa watu wabaya.

Kila wakati fanya urafiki na waumini, kula na kunywa na watu wanao

jinyima.

Mwenyezi Mungu yu karibu na ulimi wa kila msemaji kila wakati.

Kwa hiyo mfikirie Mwenyezi Mungu unaposema.

Kwa uwongo inatosha kwamba mtu husema chochote asikiacho. Ni muhimu kudhibiti ulimi moja kwa moja.

Mwenyezi Mungu humpenda mtu anayeheshimu ujuzi, wanavyuo, Waislamu wakongwe, wafuasi wa Qurani Tukufu, na mtawala mwenye haki.

Zilinde na uzifuate amri za Mwenyezi Mungu. Naye atakulinda na utamuona Yeye yu mbele yako. Mkumbuke Yeye wakati wa furaha naye atakukumbuka wakati wa shida na atakukomboa kutoka humo. Kama unahitaji kitu, omba kutoka kwake tu. Hakuna atakaye kudhuru hata kama dunia yote itakuwa adui yako, almuradi Mwenyezi Mungu hana ugomvi na wewe. Hutaweza kunufaika hata kama watu wote kwa kuungana pamoja wanataka kukunufaisha

wewe isipokuwa Mwenyezi Mungu aridhie hivyo. Mwenyezi Mungu hukusaidia wewe ukiwa kwenye uvumilivu. Ni Yeye ndiye anayekuondolea maumivu yako. Kila mara kuna faraja baada ya shida.

Mwenyezi Mungu haangalii nyuso zenu au utajiri wenu; Yeye hutazama nia zenu na matendo yenu.

Sifa za muumini ni kuwa na amani, kuonyesha staha na kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika hali yoyote ile. Aliyelaaniwa ni yule anayesema uwongo kwa watu kwa madhumuni ya kuchekesha tu.

Epukana na usengenyi kwa sababu hilo ni tendo ovu zaidi ya zinaa. Nikauliza, "Vipi Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?" Mtume alijibu, "Mzinzi akitubu, Mwenyezi Mungu hukubali toba yake lakini dhambi ya kuteta (kusenyenya) haisameheki hadi mtu ambaye ametetwa (amesengenywa) anaisamehe."

Mtu anayemtukana muumini ni mwovu na mtu anayepigana na muumini ni kafiri, na akimsengenya muumini maana yake ni kwamba anakula nyama ya anayemsengenya na kwa hivyo ni mwovu mkubwa; na mtu anaye linda mali ya muumini ni sawa kama vile analinda maisha yake."

Mimi nilisema, "ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Kusengenya ni nani?" Akasema, "Kumtaja ndugu yako kwa mabaya yake ambayo hangependa kutajwa kwayo." Mimi nikasema, "Hata kama anazo sifa hizo?" Akasema, "Hiyo ni kusengenya, kwa kweli; lakini, kama ukimsingizia mambo asiyo kuwa nayo, hiyo ni usingiziaji ambao adhabu yake ni tofauti."

Mwenyezi Mungu atamzawadia thawabu ya kwenda Peponi endapo anamwondolea shida ndugu yake katika imani.

Qatat, hawataingia Peponi." niliuliza, "Ni nani hawa Qatat?" Alijibu, "Hawa ni wasengenyaji."

Mtetaji hataweza kukwepa adhabu ya Mwenyezi Mungu huko Akhera."

"Msaliti atakwenda Jahanamu." kutoa siri ya rafiki yako ni usaliti.

Endapo mtu anakufa kabla ya kuhisi toba baada ya kuonyesha majivuno hata mara moja tu, hatanusa harufu ya Pepo. Mtume mwenye mashati mawili, yeye atumie moja na la pili ampe ndugu yake ambaye hana shati.

Mtu anayeacha kuvaa nguo za gharama, pamoja na yeye kuwa tajiri, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huko Peponi atapewa majoho kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kabla ya majilio ya Mahdi.[11] watatokea watu watakaovaa nguo za sufi wakati majira ya joto na baridi, kuonyesha ubora wao kwa watu wengine. Mwenyezi Mungu atawalaani.

Dunia hii ni jela kwa muumini na Pepo kwa kafiri. Nia yako katika hali yoyote lazima iwe uaminifu. Hata kula na kulala kwako ni mambo ambayo unatakiwa uyafanye kwa makusudio ya uamifu.

Kwa mujibu wa Hafidh Abu Naim, Kama inavyoelezwa kwenye kitabu chake, Huyatul Awlita Abu Dharr anasema: "Siku moja nilikwenda kwa Mtukufu Mtume alipokuwa amekaa msikitini. Nilikuwa hata bado sijaketi sawasawa, akiniambia, "Bado hujatoa heshima yako kwa msikiti."

Nilimuuliza, "Kitu gani hicho bwana wangu!" Alijibu, "Rakaa mbili za Swala. Ewe Abu Dharr! Unapoingia msikitini haraka sana lazima swali Swala ya raka mbili." Kufuatana na amri yake, mara moja nilisali Swala ya rakaa mbili.

Halafu niliuliza, "Nini msingi na dhamira ya Swala?" Alijibu, "Ni ibada bora kuliko zote."

Halafu niliuliza, "Ni amali gani iliyo bora kuliko zote." Alijibu, "kumwamini Mwenyezi Mungu na kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu hizi ni amali kuzidi zote."

Nikauliza, "Ewe bwana! Ni waumini gani ambao imani yao inafikiriwa kuwa kamili?" Alijibu, "Ni hao ambao matendo yao ni mema na tabia zao ni nzuri." akasema, "Ni hao ambao ndimi zao haziwasemi kwa ubaya na mikono yao haiwashambulii Waislamu wenzao" Niliuliza, "Ni mambo gani mtu anatakiwa ayaepuke?" Alijibu, "Kujinyima na kuepuka kufanya dhambi." Nikauliza. "Ni Swala zipi zilizo bora kuliko zote?" Alijibu, "Ni Swala zile ambazo dua ndefu hukaririwa katika Qunuti," Nikauliza, "Ewe bwana! Kufunga swaumu ni nini?" Akajibu, "Ni ibada ya faradhi ambayo thawabu yake ni kubwa sana" Niliuliza, "Ni jihadi ipi iliyo bora zaidi?" akajibu, "Ni hiyo ambayo miguu ya mnyama aliyepandwa hukatwa na aliyempanda mnyama huyo kuuawa." Niliuliza, "Ni sadaka ipi iliyo bora zaid?"

Alijibu, Ni sadaka ile iliyotolewa kutokana na malipo ya kazi ngumu." Niliuliza, "Ewe bwana ni Aya gani miongoni mwa zile zilizofunuliwa na Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuzidi zingine?" Alijibu, "Ayat al-Kursi (aya za kiti cha enzi) Nikasema, Ewe bwana! Nipe nasaha zako." Akasema, "Nina kushauri umwogope Mwenyezi Mungu kwa sababu huo ndio msingi wa amali njema."

Kariri Qurani Tukufu ambayo ni chanzo cha nuru kwako hapa duniani, na utajo wa upendeleo wako huko mbinguni. Usicheke sana, ukicheka sana moyo hukosa uhai na uso husinyaa. Uwe kimya kwa muda mrefu zaidi, kwani hali hii itakuepusha kwenye matatizo mengi.

Uwe kipenzi cha watu fukara na uwe nao.

Waangalie watu hao ambao kipato chao ni cha chini zaidi na usijilinganishe na watu ambao kiuchumi wapo juu zaidi.

Wafanyie wema ahali zako, hata kama wanakudharau. Usijali lawama yoyote endapo tendo lako ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Sema ukweli hata kama unauma.

Kwa kuwa Mtukufu Mtume alikuwa na uwezo wa kubashiri mara kwa mara alitamka matukio na matatizo ambayo yangempata Abu Dharr katika maisha yake ya baadaye.

Imeandikwa kwenye Musnadya Ahmad bin Hanbali kwamba siku moja Abu Dharr alikwenda msikitini na kulala baada ya mchoko wa mahubiri. Mtume alikwenda msikitini kumliwaza na akaona kwamba alikuwa amelala. Mtume alimwambia kwa ishara ya kidole gumba chake na alisema: "Ewe Abu Dharr! Utafanya nini utakapofukuzwa kwenye msikiti?" Abu Dharr alijibu, "Ewe bwana! Endapo hali inakuwa hiyo, nitachomoa upanga wangu na nitamkata kichwa chake mtu atakayefanya hivyo." Mtume akasema, "Ewe Abu Dharr! Usije ukafanya hivyo lakini uwe mvumilivu wakati huo; nenda popote utakapo pelekwa na uondoke uende huko utakapopelekwa."

Allamah Muhammad Baqir Majlis ameandika kwamba siku moja Mtume alimwambia Abu Dharr, "Ewe Abu Dharr! Utaishi maisha ya

upweke, na utakufa ukiwa peke yako. Utafufuka mnamo siku ya Ufufuo ukiwa peke yako. Utafariki dunia ukiwa peke yako katika nchi ya ugenini. Baadhi ya watu wa Iraq wataikafini maiti yako, wataivisha sanda, na kukuzika." (Anwarul Qulub).

Aidha ameandika kwamba siku moja Uthman na Abu Dharr walingia kwenye msikiti wa Mtume huku wakizungumza.

Hapo walimuona Mtume ameketi akiwa ameegemea kwenye mto. Wote wawili walikwenda kwake. Baada ya muda mfupi Uthman aliondoka hapo. Baadaye Mtume akasema, "Ewe Abu Dharr! Ulikuwa unazunguma nini na Uthman?" Abu Dharr alisema, "Tulikuwa tunazungumza kuhusu aya fulani ya Quran Tukufu." Mtume akasema, Ewe Abu Dharr! Haiko mbali siku ambapo wewe na Uthman mtatofautiana sana na wote nyinyi wawili mtakuwa wahasimu wakubwa. Wakati huo mmoja wenu atakandamizwa na mwingine atakuwa mkandamizaji. Abu Dharr! Usiache kusema kweli, hata kama ukifanyiwa udhalimu wa aina yoyote ile" (Hayatul Qulub).

Ilielekea zaidi kwamba aya iliyotajwa kwenye fungu la maneno hapo juu lilihusu suala la Zaka kwa sababu Allamah Subaiti akidokeza kwenye kitabu chake ameandika kwamba palitokea mazungumzo baina ya Uthman na Abu Dharr kuhusu suala la Zaka, ambalo lilisuluhishwa na Mtukufu Mtume (Hayatul Qulubi).

Waandishi wa historia na wahadithi wanakubaliana kwamba Abu Dharr alikuwa kwenye upeo wa uchaji Mungu. Alitumia maisha yake yote katika kuhubiri, na sababu ni kwamba alitoa kiapo cha utii kwa Mtukufu Mtume katika kipindi hicho hicho. alisema kwamba hangemjali mtu yeyote mwenye kumshutumu kwa sababu inayohusiana na amri za Mwenyezi Mungu. Hotuba zake ni nyingi sana, baadhi ya hizo zimeatajwa hapa chini:

Kwa mujibu wa maneno ya Allamah Turayhi, Abu Dharr amesema mara nyingi kwenye mahubiri yake, "Enyi watu! Hata kama migongo yenu itajikunja na miguu yenu kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya kusali sana na huduma zingine za dini, haitawapeni manufaa isipokuwa muwapende Ahlul-Bait katika mioyo yenu. Kwa hiyo mnatakiwa kwanza, muwapenhe watu wa nyumba ya Muhammad kwenye nyoyo zenu (kwa maelezo zaidi kuhusu "kuwapenda Ndugu" [12]

Allamah Subaiti ameandika kwamba siku moja Abu Dharr aliita kwa sauti kwenye mlango wa Al-Kaaba, "Enyi ndugu zangu! Njooni karibu yangu na msikileze kwa uangalifu."

Waliposikia hivi watu walikusanyika karibu naye. Abu Dharr alisema, kila mmoja wenu hukusanya mahitaji kwa ajili ya safari yake na huanza safari yake baaada ya kukusanya mahitaji. Si rahisi kumuona mtu miongoni mwetu ambaye ataanza safari bila mahitaji. "Enyi ndugu zangu! Safari yenu kwenye siku ya Ufufuo ipo mbele yenu. Kwa hiyo, ni muhimu kwenu kukusanya mahitaji kwa ajili ya safari."

Watu wakasema, "Ewe ndugu hapana shaka kuhusu safari ya kwenye Ufufuo, lakini hatujui tuchukue mahitaji gani?" Abu Dharr akasema, "Jambo linalohitajiwa katika safari hii ni Hija ya kutembelea Kaabah. Mahitaji yake ni kufunga Swaumu wakati wa siku za joto sana na kusali Swala ya rakaa mbili ili kuondoa hofu ya kaburi kwenye usiku wa giza, "Enyi ndugu zangu! Fanyeni amali njema. Chunga ulimi wako usitamke maneno mabaya. Tumia utajiri wako katika kutoa Sadaka. Tumia siku za uhai wako katika kuitafuta Pepo, na tafuta njia za halali za kupata riziki. Ukipata dinari mbili, tumia moja kwa kumpa nduguyo na nyingine toa sadaka kwa ajili ya ustawi wa Pepo.