• Anza
  • Iliyopita
  • 2 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 3808 / Pakua: 1787
Kiwango Kiwango Kiwango
MAWAHABI NA MAUWAJI YA IMAM HUSEN (A.S)

MAWAHABI NA MAUWAJI YA IMAM HUSEN (A.S)

Mwandishi:
Swahili

MAWAHABI NA MAUWAJI YA IMAM HUSEN (A.S)

KIMEANDIKWA NA: SAYYID SAEED AKHTAR RIZVI

KIMETAFSIRIWA NA: MAALIM DHIKIRI OMARI KIONDO

Kimetolewa juu ya web na timu ya: Ahlul Bayt Digital Islamic Library Project

SWALI LA KWANZA

Hebu na tufikirie ni madhahebu ipi yenye kumtukuza yule mtu Mtukufu ambaye yu Shahidi wa Karbala na inayozifuata nyayo zake, na ni ipi isiofanya hivyo. Bila ya kusema mengi, ni madhehebu ya Shia yenye kumwamini Imamu Husayn(a.s) kuwa yu mtu aliyeteuliwa na aliyewekwa na Allah (s.w.t) na yu mrithi wa haki wa nafasi ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Shia wanaamini kwamba kila neno na kitendo cha Imamu(a.s) ni katika kumtii Allah, vita yake na amani yake ni kioo cha amali chenye kufaa, na msimamo wake ndio mapenzi ya Allah. Kwa Shia, Imamu ni sehemu ya Nuru (Nuur) ya Mtukufu Mtume Muhammad(s.a.w.w) , Nyama na damu ya Imamu ni nyama na damu ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Kujitoa kwa ajili ya Imamu ni jukumu kuu. Kumtii kuna maana ya kuikamilisha imani yake mtu, na kwanza yeye Imamu katakasika kutokana na kukosea na makosa. Kumpenda Imamu ni kutimiza malipo ya Utume wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Allah (s.w.t) anasema:

"...Sema (ewe Rasuli Wetu Muhammad): kwa hayo, siombi ujira wowote kwenu ila mapenzi (yenu) kwa karibu (zangu)... "(Qur'ani, 42:23).

Imamu katakasika kutokana na kila aina ya uchafu, uwe wa kimwili au wa kiroho. Allah (s.w.t) anasema:

"...Hakika Allah anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Ahlul Bayt (wa Rasuli Wetu Muhammad) na kukutoharisheni kwa tohara kamili ." (Qur'ani 33:33)

Imamu ni mwana wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Allah (s.w.t) anasema:

"...Lakini atakayekuhoji kuhusiana na hayo baada ya kukufikia elimu, basi sema: "Njooni tuwaite wana wetu na wana wenu, na wanawake wetu na wanawake wenu na nafsi zetu na nafsi zenu.. ."(Qur'ani 3:61) Imamu yu ua la Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na anatokana na Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , kama alivyosema Mtukufu Mtume(s.a.w.w) mwenyewe, pale aliposema: "Husayn anatokana na mimi, na mimi ninatokana na Husayn." Imamat (Uimamu) wake hautegemeani na upatano wa watu wala kiapo cha utii cha watu. "Yeye yu kiongozi wa vijana wa Peponi." Yu mtakatifu (kutokana na dhambi na kukosea) tangu kuzaliwa kwake hadi kufariki dunia kwake. Itikadi hii juu ya Umaasum (Utakatifu wa Maimamu) ni maalumu kwa Mashia tu, na wasiokuwa Mashia hawashiriki kwenye itikadi hii. (Ingawa wanavyuoni wakuu wasio Shia wanaweza kuthibitisha Uma'sum wa Maimamu). Waislamu wasio Shia, hasa wale wa madhehebu ya Hanafii na Shafii wote, na wengi wa Hambali (Wafuasi wa Imamu Ahmad Ibn Hambal) wanamtambua Imamu Husayn (a.s) kuwa na haki na Yazid kuwa yu mwenye makosa. Kuzitaja rejea zote hapa kutaifanya orodha hiyo kuwa ndefu sana. Hivyo nitazitaja baadhi tu ya rejea hizo, nilizozichagua miongoni mwa waandishi walioandika juu ya jambo hili:

1. Allamah Shahabuddin Abul Abbas Ahmad bin Muhammad Qastalani, aliyefariki kwenye mwaka wa 923 Hijiria, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Irshad Alsari Sharh Sahih Bukhari", Juzuu 2, ukurasa wa 139.

2. Bwana Ibn Jawzi (aliyefariki mnamo mwaka 1200 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Al-Radd Alal Mutaassib Alanidil Man 'Min Dhulm Yazid."

3. Bwana Sibt Ibn Jawzi (aliyefariki mnamo mwaka wa 1257 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Tazkiratu Khawassil Ummam".

4. Allama Ibn Hajar Al-Haitami (aliyefariki mnamo mwaka wa 974 Hijiriya), mwenye kitabu chake kiitwacho: As-Sawa'iq al-Muhriqah, ukurasa wa 132-134.

5. Imamu Jalaluddin Abdul-Rahman Ibn Abi Bakr Al-Suyuti (aliyefariki mnamo mwaka 911 Hijiriya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Tarikhul Khulafaa".

6. Shaikh Muhammad bin Ali Sabban (aliyefariki mnamo mwaka 1792 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Is'afur Raghbiin".

7. Allama Sa'duddin Mas'ud bin 'Umar Taftazani (aliyefariki mnamo mwaka 1389 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Sharh Aqaid Nasafi".

8. Shah Abdulaziz Dehlawi (aliyefariki mnamo mwaka 1824 Masihiya) mwenye kitabu chake kiitwacho "Sirrul Shahadatain".

9. Shah Abdulhaqq Dehlawi (aliyefariki mnamo mwaka 1642 Masihiya), mwenye vitabu vyake "Mada-rijun Nubuwwat" na "Ja-adhbul Qulub".

10. Maulana Abdulhai Firangi Mahali, mwenye kitabu chake kiitwacho "Fatawi," Juzuu 3, ukurasa wa 7.

11. Nawwab Siddiq Hassan Khan Bhopali (aliyefariki mnamo mwaka 1889 Masihiya), mwenye kitabu chake kiitwacho: "Bughyatul Raid Fi Sharhil Aqaid".

12. Maulana Muhammad Matin Firangi Mahali, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Wasilatun Najat", ukurasa wa 290.

13. Mufti Muhammad Akramuddin, mwenye kitabu chake kiitwacho: "Sa'adatun Kawnain Fi Fadhailil Hassanain."

14. Qadhi Muhammad Sulaiman, mwenye kitabu chake kiitwacho:

15. "Rahmatuh-Lil- 'Alamiin". Majina haya machache ni mifano michache tu yenye kuwajumlisha wanachuoni wa kihanafiyah, Kishafi'i na Kihambaliya ambao wameweka sehemu ya Imamu Husayn kuwa ilikuwa ya haki na kwamba alikufa akiwa shahidi aliyedhulumiwa. Kinyume na hivyo, wako Mahambaliya wanaoamini kuwa Ibn Taimiya ni kiongozi wao; na hivyo ndivyo waaminivyo Nasibi na Kharji, ambao ili kuwahadaa Masunni, hujitokeza kama Masunni. Watu hawa humchukulia Yazid kuwa ni khalifa wa kweli na hivyo, Mwenyezi Mungu na atusamehe, humchukulia Imamu Husayn(a.s) kuwa yu mwenye makosa aliyestahili kuuawa. Siku hizi, maoni ya namna hii yanatolewa na Mahmud Ahmad Abbasi, ambaye kitabu chake kiitwacho "Khilafat Muawiya wa Yazid" kimeziumiza hisia za Waislamu wengi. Kwenye siku za awali, kabla ya Ibn Taimiya (aliyefariki mnamo mwaka 728 Hijiriya), mtu mmoja aliyeitwa Abu Bakr Muhammad bin Abdullah bin al-Arabi (aliyefariki mnamo mwaka 543 Hijiriya) alijitokeza kwenye itikadi hiyo hiyo. Mtu huyo aliandika hivi: "Husayn hakuuawa ila kwa upanga wa babu yake mwenyewe (yaani kwa mujibu wa kanuni za shari'ah), kwa sababu kililiwa kiapo cha utii kwa Yazid na hivyo Husayn alikuwa mwasi". Maelezo ya huba yake kwa Yazid yaliyomo kwenye kitabu kiitwacho "Tazkiratul Huffaz" yanatosha kuwa utangulizi: "Hafidh, Allama, Qadhi, Faqihi, alifikia daraja la Ijtihad". Abu Bakr bin Al-Arabi alikuwa mwanafunzi wa Imamu Ghazali (aliyefariki mnamo mwaka 505 Hijiriya). Imamu Ghazali huyu ndie yule yule aliye maarufu kwa jina la Hujjatul Islam na anaaminiwa kuwa yu nguzo ya kanuni za kidini (za Kisunni) na mmoja wa wale ambao Fat'wa (hukumu ya Kiislamu) zao zilikuwa: "Ni haramu kuhadithia juu ya Husayn na wafuasi wake kwenye hotuba, kwa sababu kufanya hivyo kunazaa chuki juu ya masahaba". Ni dhahiri kwamba, kama Imamu Ghazali aliifikiria sehemu ya Imamu Husayn(a.s) kuwa ni ya haki, asingeharimisha kuihadithia. Tukiyafikiria yote haya, mtu hatakuwa na jingine la kufanya ila kuamua kuwa, Ulama kama hawa hawamfikirii Imamu Husayn(a.s) kuwa yu mtu mtukufu na kwamba, kwa mujibu wa mauni yao, kukataa kwa Imamu Husayn(a.s) kula kiapo cha utii kwa Yazid kulikuwa ni kosa kubwa mno kiasi kwamba hadi hivi leo wanaandika kuwa, Mwenyezi Mungu na atusamehe Imamu(a.s) alikuwa na dalili za ukaidi. Kabla ya Muhammad Abbasi, mtu mwingine aliandika kitabu kiitwacho "Shahidi A'zam" kilichojaribu kuonyesha kuwa "Yazid alikuwa khalifia wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na kwamba Husayn alimwasi Yazid bila ya haki wala sababu kwa kulilia madaraka. Nduguze walimshauri kutofanya hivyo, lakini hakuwasikiliza. Mwishowe, Gavana wa Yazid aliyeitwa Ibn Ziad, akimzuia Husayn na kutoleta mfarakano na baada ya kushindwa katika kuzitumia njia nyinginezo, kwa shingo upande, alimwua ili kuidumisha amani na umoja." Mwandishi aliyeandikwa kwenye ukurasa wa mbele wa kitabu hicho alikuwa ni Abdul Kalam Asad, kwa mujibu wa umaarufu na cheo cha mwandishi huyo, kiwanda cha uchapishaji wa vitabu kiitwacho: "Islah Publication, Kujhwa (Bihar, India) kiliona kuwa ni muhimu kukijibu kitabu hicho na kikatoa kitabu kiitwacho "Shahadat 'Uzma", ambacho hadi hivi sasa kinapatikana. Baada ya Uhuru wa India, mtu fulani alimtahadharisha Maulana Abdul Kalam Asad (Waziri wa Elimu wa India wa wakati ule) kuhusiana na kitabu kilichochapishwa kwa jina lake. Maulana huyu hakuwa na taarifa zozote juu ya kitabu hiki na hivyo akatoa tamshi rasmi la kutojihusisha na kitabu hicho. Kukikana kwake kitabu hiki kulikuwa kwa haki kwa sababu huyo marehemu Abdul Kalam Asad angeweza kuandika juu ya Imamu Husayn(a.s) akikirejea kitabu hiki. Kwa mfano, hebu itazame makala yake ndefu iliyoandikwa kwenye gazeti liitwalo "Al-Hilal" lililotoka mwezi wa Muharram (Mfunguo Nne) iliyochapishwa tena neno hadi neno kwenye gazeti la mjini Lahore (Pakistan), liitwalo "Inqilab", toleo la Shaban, 1927, na ambayo Sayyid Muhammad Hashim Marhum Patlavi aliinakili tena kwenye sehemu ya pili ya kitabu chake kiitwacho "Namoose-Islam", kwenye ukurasa wa 274 - 278. Hata hivyo, wale wanaomfuata Ibn Taimiya na Ibn Al-Arabi na Manasibi wamesema moja kwa moja au kwa mifano tu kuwa Imamu Husayn (a.s) hakuwa na haki. Maelezo: Muhammad bin Abdullah bin Al-Arabi alimfunza itikadi hii mwanawe aliyeitwa Muhyuddin Ibn Al-Arabi, aliyeandika kitabu kiitwacho "Al-Futahatul Makkiyah", na aliyefariki mnamo mwaka 638 Hijiriya.

SWALI LA PILI

Hebu sasa natuligeukie lile swali la upande wa pili na tuone ni madhehebu ipi inayomchukulia Yazid mwenye nuru ipi. Baada ya kulielezea lile swali la kwanza waziwazi, haipo haja tena ya kueleza kwa kirefu hapa, lakini ili kuzi-imarisha zaidi thibitisho hizo, hapa chini tunatoa maelezo zaidi. Mashia wanamchukulia mtu huyu aliyelaaniwa (Yazid) kuwa yu adui na kila mtoto wa Kishia humwona Yazid na jadi zake wote kuwa ni kizazi kilicholaaniwa Al-Shajaratul Mal-'unnah kilichotajwa kwenye Qur'ani (kwenye aya isemayo: "...Na hatukuifanya ile ndoto tuliyokuonyesha ila kuwa ni mtihani kwa watu, na (pia) ule Mti uliolaaniwa (Ash-Shajarata Mal'uunat) kwenye Qur'ani na tunawahofisha lakini haiwazidishii (chochote) ila uasi mkubwa." (Sura Bani Israil, 17:60) Kinyume na hivyo, Mawahhabi ambao ni wafuasi wa Ibn Taimiya humwona Yazid kuwa ni Khalifa wa haki. Hapo juu tumekwisha kumtaja Abu Bakr Ibn Al-Arabi. Mullah Ali Qari, kwenye kitabu chake kiitwacho "Sharh Fiqh Akbar", kwenye ukurasa wa 84, na lbn Hajr Haithami (ambaye pia tumemtaja hapo juu) kwenye kitabu chake kiitwacho: "Sawa'iqul Muhriqah, kwenye ukurasa wa 11 na wa 12 wameonyesha hisia zao zenye nyuso mbili (huku na huku) kwa kumwingiza Yazid miongoni mwa Maimamu kumi na wawili ambao kuhusiana nao imepokewa Hadith ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) isemayo kwamba dini itabakia kuwa imara madamu wako Maimamu kumi na wawili. Ibn Taimiyya na wafuasi wake Mawahhabi wamefanya kila walichokiweza kumwokoa Yazid kutokana na kulaaniwa: wakitoa Fatwa isemayo kuwa yeye alikuwa ni Mwislamu na Mwislamu ameharimishwa kumlaani Mwislamu mwenzie: au kumwekea lawama yote ya mauaji ya lmamu Husayn(a.s) Ibn Ziad; au kuzusha Hadithi isemayo kuwa Imamu Husayn(a.s) atamsamehe Yazid kwenye siku ya Kiyama. Kwa ufupi ni kwamba, kila hila iliyowezekana inatumiwa katika kumwokoa Yazid kutokana na laana. Mshairi mmoja amejaribu kuzijibu hila hizi akisema: "Enyi msemao kuwa tusimlaani Yazid au majeshi yake kwa sababu yawezekana kwamba Allah akamrehemu. Kama Allah atamsamehe, ingawa kawatendea yote hayo Dhuria wa Mtukufu Mtume, basi hakika Allah Atakusameheni nyie nanyi kwa kumlaani Yazid ".

Ukweli uliopo ni kwamba Mashia, Mahanafiya, Mashafi na Mahambaliya wenye kuipenda haki (akiwemo Imamu Ahmad bin Hambal mwenyewe) humchukia Yazid ambapo Manasibi na Mawahhabiya (wengi wao huwaghilibu watu kwa kujiita Mahambaliya) sio tu kwamba hawamlaani Yazid bali vile vile hujaribu kuwazuia watu wasimlaani.

SWALI LA TATU

Kwa Mashia, Yazid na wauaji wengine wa Imamu Husayn(a.s) ni Kafir na hivyo wamejitakia laana ya Allah iwe juu yao na juu ya wote wenye kuyafurahia matendo yao; na huwahesabu wote hao kuwa ni watu wa motoni. Mahanafiya, Mashafii na Mahambaliya wapenda haki nao humchukia Yazid na wauaji wengine wenye kustahili karipio kali zaidi. Lakini Mawahhabiya na Manasibi huwapinga Mashia waziwazi kwa kuwa wanawahesabu wauaji wa Imamu Husayn(a.s) kuwa ni wenye kustahili sifa. Miongoni mwa wauaji hawa, baadhi yao waliweza hata kujinyakulia Ukhalifa na wengine wakapewa majina ya heshima kama vile "Saduq" (Mkweli zaidi) na "Thiqah" (Mwaminifu), na watu kadhaa miongoni mwao wamekuwa wapokeaji wa Ahadith za Mtukufu Mtume(s.a.w.w) kwenye "Sihah Sitta" na kutokana na maelezo yao watu hujichukulia hukumu za kidini. Sasa tutawataja hapa chini kila mmoja wao kwa jina na kumwonyesha alikuwa ni mtu wa aina gani.

1. 'Umr Ibn Sa'd Ibn Abi Waqqas

Huyu ndie aliyekuwa amiri jeshi wa majeshi ya Yazid. Baada ya Yazid na Ibn Ziad, yeye anahusika moja kwa moja na matendo maovu mno yaliyotendwa dhidi ya Imamu Husayn(a.s) . Aliviambia vikosi vyake vishuhudie kwamba yeye anamtupia Imamu Husayn(a.s) mshale wa kwanza. Mwandishi wa kitabu kiitwacho "Tahdhi'b al-Tahdhib" anamwelezea mtu huyu kama ifuatavyo:- "Yeye (Umar Ibn Sa'd) alizipokea Ahadithi za Mtukufu Mtume(s.a.w.w) kutoka kwa baba yake na kutoka kwa Abu Sa'id al-Khudri, masahaba wawili wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na mapokezi yake yalitolewa na mwanawe (aliyeitwa) Ibrahim na mjukuu wake aliyeitwa Abu Bakr Ibn Hafs Ibn Hurith, na Yazid Ibn Abi Maryam, na Qatadah, na Zuhri, na Yazid Ibn Habib na wengineo." "Mwana wa mtu huyu aitwaye Ijli amehadithia kwamba alikuwa na kawaida ya kuzihadithia Ahadith alizozipokea kutoka kwa baba yake na watu wengi wamezihadithia Hadithi walizozipokea kutoka kwake na yeye yu "Tabi'i" (Mwanafunzi wa Sahaba) na Thiqah (mwaminifu)". Kwenye kitabu kiitwacho Taqribul Tahdhib imeelezwa hivi:- "Umar Ibn Sa'd Ibn Abi Waqqas wa Madina, mkazi wa mjini Kufah, alikuwa ni Saduq (Mkweli). Lakini watu walimtweza kwa sababu alikuwa amiri jeshi wa jeshi lililomwua Husayn." Kumbuka kwa, hii ni kauli ya Shaikhul Islam wa mawahhabiya, Ibn Hajar. Ifuatayo hapa chini ni orodha ya wale waliozihadithia Ahadith zilizopokewa na 'Umar Ibn Sa'd: i. Abu Ishaq Sabi'i ii. Qatadah, na iii. Imamu Zuhri. Hawa ndio wale watu watatu ambao Mawahhabiya huwategemea kwa Ahadith zao na huwahesabu kuwa ni mabwana wa uhadithiaji wa Ahadith. Kutokana na hawa watu wote watatu kuyakubali mapokezi ya 'Umar Ibn Sa'd, kunamfanya mtu huyu kuwa msema kweli na mwenye madaraka. Zaidi ya hapo, uthibitisho zaidi unaotolewa ni kwamba Imamu Nasai, Ibn Majah na Bukhari wamezihukumu Ahadithi alizozihadithia. Kwenye hali hii, hakuna umuhimu wowote uwezao kupewa wale watu wa kawaida wanaojificha au yale maneno ya Ibn Mu'in pale aliposema: "Ni vipi mwuaji wa Husayn aweza kuwa mwaminifu?" Kwenye Sharhi yake ya kitabu kiitwacho "Mishkat", Mullah Ali Qari anayehesabiwa kuwa yu miongoni mwa waandishi wakweli juu ya tabia za wapokeaji wa Ahadithi) anafafanua, akisema: "'Umar Ibn Sa'd yeye mwenyewe hakumwua Husayn na inawezekana kwamba kushiriki kwake kwenye jeshi lile kulitokana na ujuzi wake halisi (ijtihad) na inawezekana kutokana na kuteleza au kutenda dhambi? Hivyo basi, iwapo malango ya lawama yanafunguliwa kwa hasira, kwa ajili ya vitu kama hivi, basi wanachuoni watajikuta kwenye mashaka". Kwetiye kitabu kingine kiitwacho "Mizanul-I'tidal" zaidi ya kuyaandika hayo kuwa Umar alishiriki kwenye vita dhidi ya Imamu Husayn (a.s) , aliongezea kusema: "Utu wake ni mwema kiasi cha kutokana kabisa na lawama. Mpokeaji wa Ahadithi (aitwaye) Su'ba (kwa kutokana na mabwana wake) amepokea Ahadithi kutoka kwake na wamefanya vivyo hivyo watu wengineo nao."

2. Shimr Ibn Dhil-Jaushan

Huyu ndiye mchinjaji hasa wa Imamu Husayn(a.s) . Ibn Ziad alimfanya mtu huyu kuwa kapteni wa jeshi madhubuti la watu elfu nne, na akampa maagizo ya kwamba iwapo 'Umar Ibn Sa'd atasitasita kumshambulia Imamu Husayn(a.s) basi amnyang'anye uamiri-jeshi wa jeshi hilo na auchukue yeye. Huyu naye yu kiongozi wa wapokeaji wa Ahadithi wa Mawahhabiya. Kwenye kitabu kiitwacho "Tahdibut Tahdhib" imeandikwa hivi: "Shimr ibn Dhil-Jaushan Abu Nabighah Dhubyani amepokea Ahadithi kutoka kwa baba yake, na kutoka kwa Shamr amepokea (Ahadithi hizo) Abu Ishaq Sabi'i." Hayo yameandikwa kwenye kitabu kiitwacho Mizanul I'tidal na kwenye kitabu kingine kiitwacho Isti'ab. Kwenye Tadhkiratul Hufadh inaelezwa zaidi hivi: "Na kutoka kwake amepokea A'mash na Shu'bah na Thawri na Israil na Abul Ahwas na Abu Bakr Ibn Ayyash na Sufyan bin Ayniyah." Maelezo ya Abu Ishaq Sabi'i (ambayo ndani yake ameeleza udhuru wa kutomlaumu Shimr) ni haya yafuatayo:- "Shimr alikuwa akisali pamoja nasi, na alikuwa kila mara akisema: Ee Allah! Unajua kuwa mimi ni mtu mtukufu, basi unisamehe." Abu Ishaq anasema: "Nilimwuliza: Ni vipi Allah Angeweza kukusamehe wakati wewe umeyasaidia mauaji ya mwana wa Mtume? Shimr akajibu: Ole wako! Ningefanyaje? Viongozi wetu wametuamrisha kufanya hivyo nasi hatukuwaasi! Kama tungewaasi, hali zetu zingekuwa mbaya zaidi kuliko kumwua Husayn."

3. Hasin ibn Numayr

Mlaaniwa huyu aliongoza jeshi la askari elfu nne huko Karbala. Baada ya kuuawa kwa Bwana Muslim Ibn Aqiil, Ibn Ziad alimfanya Hasin ibn Numayr kuwa kiongozi wa jeshi la kufunga mipaka ya Kufah ili kuweza kumkamata Imamu Husayn(a.s) atakapokuja huko. Hurr alikuwa na afisa wa chini yake. Baada ya masaibu ya Karbala, wakati wa kuzingirwa kwa mji wa Madina na Harram, alikuwa kiongozi wa Jeshi sababu kiongozi wa jeshi hilo aliyeitwa Muslim ibn Uqbah alikuwa mgonjwa; baada ya kuuteka mji wa Madina Muslim ibn Uqbah alipofariki, akawa kiongozi hasa wa jeshi lililouzingira mji wa Makkah. Yeye nae yu mpokeaji wa Ahadith kwenye Sihah. Kwenye kitabu kiitwacho Tahdhibat Tahdib imeelezwa hivi: "Mwenye mazingira ya mji wa Madina alikuwa mmoja wa maamiri-jeshi wa Yazid ibn Mu'awiyah. Kisha mwenye kumzingira Ibn Zubair alikuwa amiri jeshi wa jeshi la Yazid. Yeye yu mtu maarufu". Kwenye Mizanul-Itidal imeandikwa kuwa yeye kapokea Ahadithi chache tu, lakini halaumiwi kwa kuwa mmoja wa wauaji wa Imam Husayn(a.s) . Zaidi ya hapo, Bukhari, Abu Dawuud, Tirmidhi, na Nasai wapokeaji wanne maarufu sana wamezinukuu kwa uhakika Ahadithi zake kwenye vitabu vyao ambavyo ni miongoni mwa Sihah Sitta ambavyo Ahadithi zote zilizoandikwa humo zahesabiwa kuwa ni sahihi kabisa.

4. Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais

Huyu alikuwa ni mwana wa nduguye Khalifa Abu Bakr na mwana wa Munafiq (mnafiki) mkuu aliyeitwa Ash'ath bin Qais na ni umbu lake Ju'dah binti Ash'ath mwuuaji wa Imamu Hassan(a.s) . Ibn Ziad alimtuma mtu huyu kwenye kupigana na Hadhrat Muslim bin Aqil, na huko Karbala, aliongoza kikosi cha askari elfu nne. Yeye naye anahesabiwa kuwa yu mpokeaji wa Ahadith, mkweli wa Ahlul Sunnah. Kwenye Tahdhibut Tahdhib anaelezwa hivi: "Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais Kindi Abul Qasim alikuwa yu mkazi wa mjini Kufah. Mama yake alikuwa ni umbu lake Abu Bakr Siddiq. Ibn Ash'ath amepokea Ahadith kutoka kwa babayake na 'Umar na 'Uthman na Ibn Mas'ud na Ayisha; na kutoka kwake amezipokea Ahadith hizo mwanawe (aitwaye) Qais na Shu 'bi na Mujahid na Zuhri n.k. Ibn Habban amemwingiza miongoni mwa watu waaminifu. Mwenye Sunnan ya Ibn Dawuud liko moja miongoni mwa mapokezi yake juu ya Abdul Rahman ibn Qais na iko Hadith moja kwenye Sunnan ya Nasa'i izungumziayo juu ya Funga. Abu Zubair Razi ameeleza kwa Ibn Zubair alimpa mtu huyu ugavana wa Mosul". Kwenye kile kitabu kiitwacho Tahdhibut Tahdhib imeelezwa hivi:- "Muhammad ibn Ash'ath ibn Qais Kindi ambaye jina lake la utoto ni Abul Qasim, ni mpokeaji (wa Ahadith) anayekubalika - yeye yumo kwenye kundi la pili (yaani yu miongoni mwa Tabi'in)." Baadae Muhammad Ibn Ash'ath alidai Ukhalifa na Ulama wa Kiwahhabiya wanasema: "Yeye yu miongoni mwa wale ambao watu waliwapa Ukhalifa kwa makubaliano ya pamoja". Ukweli ni kuwa, hata sahaba maarufu wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) Anas ibn Malik alikula kiapo cha utii kwake na akamtii. (Soma kitabu kiitwacho Hayatul Hayawan, Juzuu 2. ukurasa wa 48.)

5. Shabth ibn Rab'i

Mlaaniwa huyu naye alikuwa miongoni mwa waliomua Imamu Husayn(a.s) . Yeye nae aliongoza kikosi cha askari kwenye masaibu ya Karbala. Kwenye kitabu kiitwacho Taqribu Tahdhib imeonyeshwa kuwa yeye nae yu mpokeaji wa Ahadith za Sihah na upokeaji wake umejipatia nafasi kwenye vitabu vya Abu Dawuud na Imamu Nasa'i.

6. Sumrah ibn Jundab

Alikuwa miongoni mwa maamiri jeshi wajeshi la Yazid. Yeye alikuwa ni sahaba wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) ambaye kuhusiana naye Mtukufu Mtume(s.a.w.w) alitabiri akisema kuwa atakuwa miongoni mwa watu wa Motoni. Hivyo basi, mwenye Sharh lbn Abil Hadid, mwenye Ma'arif cha Ibn Qatbiya na mwenye Isti'ab ameelezwa hivi: "Mtume(s.a.w.w) akiwa anazungumza na Sumrah, Abu Huraira na Hudhaifa bin Yaman alisema kwamba miongoni mwao vule atakayekuwa wa mwisho kufa atakwenda Motoni. Abu Huraira alikuwa kila mara akisema kwamba Hudhaifa alitutangulia kufa na ninategemea kuwa nitakufa kabla ya Sumrah. Hivyo, Sumrah ibn Jundab aliwaishilizia wengine katika kufariki dunia na alikiwepo kwenye mauaji ya Karbala. Imamu Husayn (a.s) alipoitangaza azma yake ya kwenda Iraq, Samrah alikuwa kwenye jeshi la polisi la Ibn Ziad na alikuwa na desturi ya kuwashawishi watu kwenda kupigana dhidi ya Imamu Husayn(a.s) ." Ingawa aliyatenda yote hayo, kwa sababu tu yu sahaba wa Mtukutu Mtume(s.a.w.w) amewekwa kwenye kundi la kwanza la wapokeaji wa Ahadithi na mapokezi yake huzipamba Sihah kwenye Isti'ab imeandikwa hivi: "Yeye alikuwa ni sahaba wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na wakazihadithia". Hawa watu sita walikuwa ni maamiri-jeshi kwenye majeshi ya Yazid huko Karbala. Sasa tutawataja wale ambao uadui wao kwa Ahlul Bayt (a.s) kwa ujumla na hasa kwa Imamu Husayn(a.s) unajidhihirisha wenyewe. Miongoni mwao, wa kwanza wao ni Marwan ibn al-Hakam.

7. Marwan Ibn al-Hakam

Baba yake aitwaye Hakam alifukuzwa mjini Madina na Mtukufu Mtume(s.a.w.w) ambaye alimwita "guruguru mwana wa guruguru". Mwenye Isti'ab imeelezwa hivi: "Ayisha alisemo. "Ewe Marwan! Ninashuhudia ya kwamba Mtume alimlaani baba yako ulipokuwo (bado u mbegu za uzazi) mwenye kiuno chake (hivyo basi wewe nawe umo kwenye laana hiyo)." Marwan alikuwa na kawaida ya kumlami Amiirul Mu'minnin Ali(a.s) mbele ya Imamu Hassan(a.s) na akamzuia Imamu Hassan(a.s) asizikwe karibu na kaburi la babu yake Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Walid (gavana wa Yazid mjini Madina wakati ule) alipomwita Imamu Husayn(a.s) kula kiapo cha utii kwa Yazid na Imamu(a.s) akaamua kuwa jambo hilo liahirishwe hadi siku ifuatayo, ni huyu Marwan ibn Hakam aliyemwambia Walid kuwa kama atamwachia Imamu(a.s) aende, katu hataweza tena kumkamata na akamhimiza amwue Imamu(a.s) pale pale. Huyu Marwan aliyefukuzwa mjini Madina na akafahamika kwa majina ya "Mfukuzwa wa Mtume(s.a.w.w) " na "guruguru mwana wa guruguru" na aliyemshawishi gavana wa mjini Madina kumwuua Imamu Husayn(a.s) , alipandishwa cheo hadi kukifikia cheo cha Ukhalifa na akawa anazungumziwa kuwa yu mpokeaji Ahadithi wa kuheshimika. Kitabu kiitwacho Taqribut Tahdhib kinaandika hivi: "Marwan aliushika Ukhalifa mnamo mwaka wa 64 Hijiriya." Kwenye kitabu kiitwacho Tahdhibut Tahdhib imeandikwa hivi:- "Marwan ibn Hakam amepokea Ahadith kutoka kwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) ingawa inadhihirika wazi wazi kuwa katu hakuzisikia hadithi hizo moja kwo moja kutoka kwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) mwenyewe. Vile vile amepokea Ahadithi kutoka kwa 'Uthman na Ali (a.s) na Zaidi bin Thabit, na Abu Huraira, na Bushra binti Safwan na Abdulrahman bin Aswad bin Abd Yaghuth. Na mwanawe 'Abdul Malik na Sahl bin Sa'd Sa'idy (ambaye yu mtu mzima kuliko Marwan), Sa'id ibn Musayyab, Urwah bin Zubair, Abu Bakr bin Abdulrahman bin Harith, Ubaidullah bin 'Abdullah, bin 'Utbah Mujahid na Abu Sufyan (Mawla wa Ibn Abi Ahmad) wamepokea Ahadith kutoka kwake. Marwan alikuwa ni Katibu wa Khalifa 'Uthman bin Affan na mwenye utawala wa Mu'awiya alifanywa gavana wa Madina. Baada ya kufariki dunia kwa Mu'awiya bin Yazid bin Mu'awiya watu walikula kiapo cha utii kwa Ukhalifa wake. 'Urwah bin Zubair alisema kuwa Marwan hatiliwi shaka kwenye mapokezi yake." Mtu ahitaji kusema mengi zaidi baada ya kuiona hiyo orodha ndefu ya watu waliopokea Ahadith kutoka kwa mtu huyu? Haishangazi kumwona mtu huyu akizipamba kurasa za Sahih Bukhari, Sahih Muslim, na Sunan Abi Dawuud

8. Abdullah bin Hani Azdi

Adui mwingine wa Bwana wa Mashahidi(a.s) alikuwa ni Abdullah bin Hani Azdi. Mtu huyu alikuwa ni askari wa jeshi la Hajjaj bin Yusuf. Alikuwa kila mara akisema: "Ninazo sifa nyingi ambazo hakuna yeyote yule aliye nazo. Kwanza, katu, hatujawahi kumsema kwa ubaya Khalifa Abdul Malk ibn Marwan; pili, wanawake wetu wameapa kwamba iwapo Husayn bin Ali atauawa, kila mmoja wao atatoa sadaka ngamia warefu kumi. Hivyo wote wakafanya hivyo (alipouawa Husayn), tatu, hakuna hata mtu mmoja miongoni mwetu ambaye, alipoambiwa kumtukana Abu Turab (Ali a.s.) hakufanya hivyo, na katika kufanya hivyo asiwajumlishe Fatima, Hassan, Husayn nao". (Taarifa hii inatoka kwenye: "Sharh Ibn Abil Hadid, Juzuu 1, ukurasa wa 195). Adui wa Ahlul Bayt(a.s) wa aina hii na mchochezi dhidi ya Imamu Husayn(a.s) anathi-bitishwa uaminifu. Tahdhib imeandikwa hivi: ("Abdullah bin Hani Azdi) yu mfuasi mwaminifu wa Hajjaj bin Yusuf Thaqafi; amethibitishwa na 'Ijli kuwa yu mtu mwaminifu na wa kutegemeka".

9. Dhahhaka bin Qais na Ziad bin Sumaiyya n.k.

Zaidi ya hapo Dhahhak bin Qais na Ziad bin Sumaiyya na wengineo waliokuwa na uhusiano maalum na Yazid ni miongoni mwa wale ambao mapokezi yao yanahesabiwa na Mawahhabiya kuwa ni yenye kutegemeka. Mpaka hapo tumetoa upande nimoja wa picha hii. Upande mwingine wa picha hii ni wa yule mtu ambaye kwa kusukumwa na nguvu ya huba yake kwa Ahlul Bayt(a.s) aliwakamata wale waliomchinja Imamu Husayn(a.s) na akawaua, anatukanwa na kulaumiwa. Hivyo basi, Mukhtar ibn Abu 'Ubaidah Thaqafi Rahmatullahi Alaih) anatukanwa kama ifuatavyo: "Mukhtar ibn Ubaidah alikuwa mwongo mkubwa. Haifai kuyakubali mapokezi yake yoyote ya Ahadith kwa kuwa sio tu kwomba alijipoteza, bali vile vile alijaribu kuwapoteza watu. Alidai kwamba Jibrili alimjia. Mukhtar yu mwovu kama Hajjal au yu sawa na yeye. Inasemekana kwamba yeye yu mwongo ambaye Hadith ya Mtume ilimzungumzia kwamba kutokana na kabila la Thaqaf atajitokeza mtu mwongo na mchochezi. Hadithi hii imo kwenye Sahih Muslim" (Taarifa hii imechukuliwa kutoka kitabu Lisanul Mizan). Maelezo haya yanaweza kumfanya mtu kufikiria kwamba pengine Bwana Mukhtar alikuwa na tabia za namna hiyo hasa na hivyo Ulama wa Rijal wakamfanyia upinzani. Lakini tunapoyatazama maelezo yaliyomo kwenye Isti'ab tunaona kwamba chuki yote hii inatokana na kwamba Bwana Mukhtar aliwaangamiza wauaji wa Husayn(a.s) . Hii ndio sababu iliyowafanya wale walioyachukia matendo yake walitwae rungu na kumsema kwa maneno ya uovu. Hicho kitabu kiitwacho Isti'ab kimeandika hivi: "Mukhtar alidai kwamba katika kuilipizia kisasi damu ya Husayn(a.s) alikuwa yu mjumbe wa Muhammad ibn Hanafiyyah. Hivyo akaomba msaada wa Ibrahim ibn Malik Ashtar na akawarukia wauaji wa Imamu Husayn(a.s) na akawaua. Allah aliwafanya wengi wa wauaji wa Husayn(a.s) kufa mikononi mwa Mukhtar; na ni kwa amri yake kuwa 'Ubaidullah ibn Ziad aliuawa na Ibrahim. Hii ndio sababu kwamba Waislamu wengi wanampenda na wale wasiozipenda itikadi zake humtukana na kumtusi." Kwa kauli nyingine ni kuwa kiini cha maelezo haya ni kwamba wafuasi na wapenzi wa wauaji wa Imamu Husayn(a.s) humtukana Bwana Mukhtar. Kutokana na maelezo hayo hapo juu ni rahisi kuamua kuwa, Mawahhabiya huwatukuza wauaji wa Imamu Husayn(a.s) . Kila kiongozi wajeshi hili la wauaji amezipamba kurasa za Sihah. Wengi wao wamepewa vyeo vya kuwa wakweli, ukweli na kukubalika. Kwa upande mwingine, licha ya kuwa wauaji, wachochezi wa mauaji ya Imamu Husayn(a.s) na kufukuzwa na Mtukufu Mtume wamefanywa kuwa Makhalifa. Kwa upande mwmgine, mwenye kuilipizia kisasi damu ya Imamu Husayn(a.s) kama vile Bwana Mukhtar Thaqafi anashu-tumiwa kwa kupotoka na kuwa-poteza watu na kuwa mwongo na kuwa mwovu zaidi ya Hajjaj - na Allah anajua ni yapi mengineyo wayasemayo juu yake.

MWISHILIZO

Kutokana na mazungumzo haya ni dhamiri kwamba, Mawahhabiya na Wanavyuoni wanaowaunga mkono sio tu kwamba hawauungi mkono msimamo wa Imamu Husayn(a.s) bali vile vile huyahesabu mauaji yake kuwa ni ya haki kwa sababu kamwasi Yazid na hawapingi kushiriki kwa watu hao kwenye mauaji hayo, na wanaendelea hadi wakathubutu kuyafanya mapokezi ya Ahadith ya watu hawa msingi wa itikadi zao. Wanawasifa wauaji hao. Ingawa watu hawa walihusika kwenye mauaji hayo, wanafanya kuwa Makhalifa kwa makubaliano ya watu. Wanasema kuwa, iwapo watu watayajali mambo madogo madogo kama hayo, basi itakuwa vigumu kuwapata wapokezi wa Ahadithi. Wale walioyaridhia mauaji ya Imamu Husayn(a.s) walifanywa kuwa watu wa kuaminika na wakweli. Lakini aliyelipizia kisasi damu hii isiyo na kosa, anachukiwa. Je, ipo haja ya kuendelea kuonyesha ni Madhehebu ipi iliyokuwa ikifuatwa na wauaji wa Imamu Husayn(a.s) ? Hadi hivi sasa Mawahhabiya wakiifuata Fatwa ya Imamu Ghazali wanajaribu kuizuia kumtaja Imamu Husayn(a.s) ili kwamba matendo yao maovu yaweze kusalia kwenye hali ya kufichikana. (Makala hii imetafsiriwa kutoka kitabu kiitwacho "Karbala Shanasi" cha Kiurdu, kilichoandikwa na Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, ukurasa wa 199-220.

HATI YA NYONGEZA

Makala hiyo hapo juu (iliyoandikwa kwa lugha ya Kiurdu) ilichapishwa kwanza kwenye gazeti la kila juma liitwalo Sarfaraz (Toleo la Muharram) la mwaka 1354 Masihiya). Makala hii ilichapishwa huko ikiwa imefanyiwa masahihisho fulani fulani na ikaungwa na ile makala yangu ya Kiurdu iitwayo "Karbala Shanasi" (toleo la pili la mwaka 1989, ukurasa wa 199-220). Kwenye mwaka wa 1954 watawala wa Rasiya Uarabuni (ambao kwa makosa huitwa Saudi Arabia) walikuwa bado hawajatiwa kiburi na dola ya petroli. Hivyo, hawakuhisi kuwa walikuwa mashujaa mno kiasi cha kuyatangaza mapatano na mapenzi yao kwa Yazid. Hii ndio maana ilinibidi nizipange thibitisho za kiuandishi hizo hapo juu, ili kuonyesha uhusiano wao na wauaji wa Imamu Husayn(a.s) . Kwenye miaka ya 1960 Mwarabu mmoja (ambaye nadhani ni Mwahhabiya), hapa mjmi Dar es Salaam aliniambia: "Nyie watu mlimwua Imamu Husayn". Nikamjibu: "Sawa! Lakini hebu, yasikilize haya ninayotaka kukueleza. Mimi nikasema: La'ana Allahu ummat qatalat al-Husayn Wa la'ana Allahu ummat dhalamat al-Husayn Wa la'ana Allahu ummat sami'at bi dhaalika faradhiyat bihi "(Laana ya Allah na iwe juu ya watu waliomwua Imamu Husayn; na laana ya Allah na iwe juu ya watu waliomdhulumu Husayn; na laana ya Allah na iwe juu ya watu walioyasikia hayo (maovu aliyotendewa Husayn) na wakayaridhia)." Kisha nikamwambia ayatamke maneno haya iwapo yu mkweli kwenye hilo dai lake. Yeye alikataa. Kwenye mwaka 1973 bei ya petroli ilipanda kwa kiwango ambacho hakikuweza kutegemewa kabla yake. Sasa Mawahhabiya wa Saudia wakawa na uwezo wa kukodi kalamu na vinywa, kila mahali ulimwenguni na sasa wakaanza kuionyesha rangi yao halisi, Wizara yao ya Elimu, kwa ujasiri mkubwa ikachapisha na kuwatawanyia bure Mahujaji, kitabu kiitwacho: Haqaiq 'an Amir al-Mu'minin, Yazid ibn Mu'awiyah (Ukweli juu ya Amirul Muminin, Yazid ibn Mu'awiyah). Mnamo tarehe 6 Aprili 1989, nilisimama kwenye soko kuu la mjini Karachi (Pakistan) nikiutazama msikiti mpya, mkubwa na wenye mnara mrefu sana. Kwenye kitako cha mnara huo ilikuwako sentensi ya Kiurdu iliyoandikwa kwa maandishi makubwa na yenye kuvutia machoni. Sentensi hiyo ilidai hivi: "Hadhrat Amiirul Muuminiin Yazid - Allah na Amwie Radhi - yu miongoni mwa watu wa Peponi." Hivyo, mwuaji wa Seyyid wa vijana wa Peponi ataingia Peponi! Inashangaza, au sivyo? Lakini linaloshangaza zaidi ya hayo ni ule ufedhuli wao wa kuendelea kuwashutumu Mashia kuhusiana na mauaji ya Imamu Husayn(a.s) kama ilivyofanywa na Mawahhabiya wa mjini Dar es Salaam mwaka uliopita na kumhimiza Al-Haj Muhsin Alidina kuitafsiri makala yangu ya Kiurdu. Mawahhabiya waelekea kuielewa vizuri sana methali ya Kiarabu isemayo: "Kama huna haya basi fanya lolote lile upendalo." Sayyid Saeed Akhtar Rizvi 5 Mei 1991.

Mawahhabiyah na Wauaji wa Imamu Husayn(a.s)

Kimeandikwa na

Sayyid Saeed Akhtar Rizvi

Kimetafsiriwa na

Maalim Dhikiri Omari Kiondo.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

MAWAHABI NA MAUWAJI YA IMAM HUSEN (A.S) 1

KIMEANDIKWA NA: SAYYID SAEED AKHTAR RIZVI 1

KIMETAFSIRIWA NA: MAALIM DHIKIRI OMARI KIONDO 1

SWALI LA KWANZA 1

SWALI LA PILI 4

SWALI LA TATU 4

MWISHILIZO 10

HATI YA NYONGEZA 10

SHARTI YA KUCHAPA 11

MWISHO WA KITABU 11

YALIYOMO 12