• Anza
  • Iliyopita
  • 5 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 6661 / Pakua: 2394
Kiwango Kiwango Kiwango
MEZA YA UCHUNGUZI

MEZA YA UCHUNGUZI

Mwandishi:
Swahili

1

MEZA YA UCHUNGUZI

QURAN NA AHLUL BAIT

Imepokewa kutoka kwa Sahaba Zaid bin Arqam: Amesema Mtume(s.a.w.w) : "Mimi ninakuachieni vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, Quran na AhIul Bait wangu, viwili hivi havitaachana mpaka vitakaponifikia katika Haudh. "

Taz: Tafsir Ibn Kathir J.4 Uk. 122 Tafsirul Khazin J.1 Uk. 4 Tarikh Bughdad J.8 Uk. 442 Sahihi Muslim J.4 Uk. 1873 Sahihi Tirmidh J.2 Uk. 308 Jamiul Usul J.1 Uk. 187 AIbidayatu Wannihaya J.7 Uk. 362 Majmauz Zawaid J.9 Uk. 163.

Hadithi hii inathibitisha kuwa baada ya kuondoka Mtume watakaoshika mahala pake ni Ahlul Bait(a.s) ambao tumekwisha waona katika tukio Ia "KISAA" na katika tukio la "Mubahala" Mwenyezi Mungu ameamrisha kufuata uongozi wao aliposema: "Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msitengane".(Qur’an 3:103).

Tamko la kamba hapa ni Ahlul Bait" na hapa tutaonyesha maneno ya Imam Shaafy "Na nilipowaona watu Madhehebu yao yamewapeleka katika bahari yao ya upotovu na ujinga, nikapanda kwa jina Ia Mwenyezi Mungu katika meli yenye kuokoa, nao ni watu wa nyumba ya Mtume mwisho wa Mitume. Na nikaishika kamba ya Mwenyezi Mungu nayo ni kuwatawalisha (Ahlul Bait) kama tulivyoamuriwa kushikamana na kamba, watakapo farakana katika dini makundi sabini na kidogo kama ilivyokuja katika Hadithi. Na asipatikane wa kuokoka miongoni mwao isipokuwa kundi moja, niambieni ni kundi gani hilo enyi wenye akili na maarifa je! Katika makundi yatakayoangamia mojawaponi ni lile kundi la watu wa Muhammad? Au wao ni katika kundi litakalo salimika, niambieni. Ikiwa utasema kundi la Muhammad ni katika kundi litakalookoka, basi huo ni msimamo wa kweli, na ukisema kundi hilo ni katika makundi yatayoangamia bila shaka umepotosha uadilifu, basi niachie Ali awe kiongozi wangu na kizazi chake, na wewe bakia katika mapambo ya ulimwengu." Imam Shaafy hapa anatukumbusha tamko muhimu Ia Mtukufu Mtume(s.a.w.w) aliposema: "Mfano wa Ahlul Bait wangu ni kama mfano wa Meli ya Nuhu, atakaepanda humo ataokoka, na atakaebaki nje atazama ".

Taz: Manaqib Ali Uk. 132 Mustadrakus Sahihain J.2 Uk. 343 Majmauz Zawaid J.9 Uk. 168 Kanzul Ummal J.6 Uk. 216 Hilyatul Awliyaa J.4 Uk. 306.

Mwenyezi Mungu anasema: "Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na Ulul'amri katika nyinyi ." 4:59.

Katika Aya hii kuna mambo matatu muhimu:

(a) Kumtii Mwenyezi Mungu

(b) Kumtii Mtume

(c) Kuwatii Ulul'amri.

Kumtii Mwenyezi Mungu, maana yake ni kushika amri zake na kuacha makatazo yake. Kama ambavyo; kumtii Mtume(s.a.w.w) maana yake ni kufuata uongozi wake. Katika Aya hii mwenyezi Mungu anaamrisha wa atiiwe Ulul'amri na yeyote ambaye Mwenyezi Mungu anaamrisha atiiwe lazima awe maasum (Mwenye kuhifadhiwa na makosa). Basi, lazima Ulul'amri waliotajwa katika Aya hii wawe Maasum. Naam; kidogo tujikumbushe lile tukio Ia "KISAA" Mwenyezi Mungu aliposema:

"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu watu wa nyumba (ya Mtume) na (anataka) kukutakaseni sana sana." (Qur’an 33:33).

Hapa tutaangalia Nukta mbili katika Aya hii:

(a) Ar'rijsu = Uchafu, matendo mabaya, Haramu Laana, Kufru, Adhabu. Taz: Al-Muujamal wasit (kamusi) Kwa mantik hii utaona kuwa: Ahlul Bait, Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na matendo mabaya. Amewaepusha haramu, hawana Iaana, wanarehema, amewaondolea kufru na adhabu.

(b) At'tuhru: Kutokuwa na uchafu wa aina yoyote.

Taz: Al-muujamal wasit (Kamusi) Kwa hiyo; Ahlul Bait(a.s) hawana uchafu wa aina yo yote. Natija inaonyesha kuwa: Ahlul Bait ni Watakatifu na ni Maasum.

JESHI LA USAMA

Katika mwaka wa kumi Hijjra, Mtukufu Mtume(s.a.w.w) alipeleka jeshi kwenda kupigana Roma. Katika jeshi hilo Mtume aliamuru liongozwe na Usama bin Zaid akasema: "Nenda ukapigane alikouliwa baba yako".

Uteuzi huu Masahaba haukuwapendeza, kwa hiyo walisikika wakipinga amri hiyo wakisema: "Itakuwaje mtoto mdogo huyu apewe madaraka makubwa juu yetu? Ilipomfikia habari hii Mtume(s.a.w.w) aliwaambia: "Nimesikia lawama zenu nilivyomtawalisha Usama katika jeshi hili, sioni ajabu, maana mlikwisha nilaumu zamani nilipomtawalisha baba yake kabla yake. Wallahi baba yake alikuwa ni mtu aliyefaa kushika uongozi wa jeshi hilo, kama ambavyo mtoto huyu anastahiki kabisa uongozi wa jeshi hili". Mtume(s.a.w.w) akasisitiza watu wote isipokuwa Ali, waende na jeshi Ia Usama akisema: "Andaeni jeshi la Usama, Mwenyezi Mungu amlaani atakaebaki asiende na jeshi hilo ".

Taz: AI-miIalu Wannihal J.1 Uk. 20.

Alipofika nje kidogo ya mji, Usama aliweka kambi ili watu wakusanyike pamoja tayari kwa msafara. Hapo Abubakar akaanza kumahawishi Usama kwamba asipeleke hilo jeshi kwa sababu haiwezekani kutoka na kumwacha Mtume(s.a.w.w) akiwa hali hii ya maradhi. Abubakar alikuwa ni mtu mzima kwa umri kuliko Usama, takriban umri wa Abubakar wakati huo si chini ya miaka hamsini, na umri wa Usama si zaidi ya miaka Kumi na Tisa.

Abubakar alitumia hila mbali mbali kwa kuendesha majadiliano kati yake na kijana mdogo Usama, baina ya jeshi liende kupigana Roma kama alivyoamuru Mtume, au lisiende kama anavyotaka Abubakar. Hali hii ilichelewesha na kuchukua muda mrefu bila ya kwenda alikoamrisha Mtume, mpaka mauti yakamfikia akafa Mtume(s.a.w.w) .

Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

"Haiwi kwa mwanamume aliyeamini wala kwa mwanamke aliyeamini, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapohukumu jambo lo lote wawe na khiari katika hukumu hiyo. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi". (Qur’an 33:36).

Amri aliyohukumu Mtume hapa ni Usama kuwa Mkuu wa jeshi litakalokwenda kupigana Roma, matoke ni kwamba; baadhi ya Waislamu hawakutii amri hiyo. Katika Aya, iliposema: "Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika amepotea upotevu ulio wazi." Hapa Abubakr na Umar wanapatikana na hatia ya kumuasi Mtume(s.a.w.w) , na mwenye kumuasi Mtume amemuasi Mwenyezi Mungu.

TUKIO LA KARATASI

Waandishi wa tarikh na Hadithi wamelieleza tukio la Karatasi kama hivi: "Mtume(s.a.w.w) alipokuwa mgonjwa mahtuti, watu wengi walikusanyika ndani ya nyumba ya Mtume akiwamo Umar Ibn Khattab. Mtume(s.a.w.w) aliwaambia kuwa: "Nileteeni Karatasi niwaandikieni maandiko hamtapotea baada yake." Umar akasema: Mtume anaweweseka! Mtume akawaambia: "Niondokeeni" wakaondoka. Katika kauli nyingine inasema: Umar alimwambia Mtume baada ya kuagiza karatasi: "Mtume yamemzidi maradhi inakutosheni Quran mliyo nayo". Kauli ya kwanza na ya pili utazipata katika: Sahih Bukhar Kitabul Ilmi Sahih Bukhar Kitabul Tibb Sahih Bukhar Kitabun Nabi ila Kisra Sahih Bukhar Babu Karahiyatul Khilaf Sahih Bukhar Babu Jawaizil wafdi Sahih Muslim Babu Tarikil Wasia Tarikhut Tabari J.2 Uk. 436 Sharhush Shifaa J.2 Uk. 353.

Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٣﴾ إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَىٰ ﴿٤﴾

"Wala hasemi kwa matamanio (ya nafsi yake) hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa." (Qur’an 53:3-4).

Amesema Abdallah bin Amri: "Nilikuwa nikiandika kila kitu ninachokisikia kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) ili nikihifadhi, Makuraishi wakanikataza wakanambia: Wewe unaandika kila kitu unachokisikia kwa Mtume!? Na Mtume ni binadamu, anazungumza (wakati mwingine) katika hali ya ghadhabu. Basi nikajizuia kuandika, nikamjulisha hayo Mtume(s.a.w.w) . Akasema Mtume, "Andika, na muape ambae nafsi yangu imo katika milki yake, mimi sisemi isipokuwa haki tupu".

Taz: Tafsir Ibni Kathir J.4 Uk. 264 Tafsir Maraghi J.27 Uk. 45.

Somo hili linatufundisha kuwa: Wakati wote Mtume(s.a.w.w) anaposema, huwa ni Wahyi. Sawa sawa awe katika furaha kubwa au katika ghadhabu, na awe katika maradhi au afya. Sasa: kwa nini Umar kuzuia usiandikwe Wahyi na nini hukumu ya mtu kama huyu? Sikiliza, Mwenyezi Mungu anasema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾

"Atakaempinga Mtume baada ya kudhihirikiwa muongozo, na kufuata njia isiyokuwa ya waumini, tutamgeuza alikogeukia mwenyewe, na tutamwingiza katika moto wa Jahannamu." (Qur’an 4:115).

RIWAYA KUHUSU SWALA

Imepokewa kwa Mwana Aisha kuwa, Mtume(s.a.w.w) alipougua maradhi aliyofia, aliamrisha kuwa: Abubakr aslishe watu, mimi (Aisha) nikasema, Abubakr ni mtu mpole sana, atakaposimama mahala pako atashindwa (kusalisha) Mtume akaamuru: Abubakr asalishe. Nikasema kama nilivyosema kwanza, Mtume akakasirika akasema: Nyinyi ni watu wa Yusuf. Mara Mtume akahisi woga moyoni mwake, akatoka akichechemea kwa kushikiliwa na watu wawili (Ali na Abbas) alipofika Msikitini, Abubakr akarudi nyuma ya safu ya kwanza. Mtume akakaa kuongoza swala, Abubakr akawa anafuata sala ya Mtume(s.a.w.w) na Waislamu wakawa wanapokea kwa Abubakr."

Taz: Tarikhut Tabari J.2 Uk. 439.

Afatu As'habil Hadithi Uk. 13-30 Hapa pana mambo matano yanahitaji kuangaliwa:

(a) Abubakr ni katika watu walioamriwa na Mtume kutoka pamoja na jeshi Ia Usama bin Zaid. Kwa hiyo basi, amma Abubakr aliwenda pamoja na jeshi hilo, na kwa hivyo hakusalisha maana hakuwepo. Amma alikuwapo mjini, kwa hivyo alipinga amri ya Mtume(s.a.w.w) na kwa hivyo Abubakr amelaaniwa.

(b) Mtume(s.a.w.w) alipougua maradhi aliyofia, alikuwa ndani ya nyumba ya Mwana Aisha, Mtume alisema: "Niitieni Ali" Aisha akajibu: "Laiti ungemwitisha Abubakr" Hafsa (mtoto wa Umar) akasema: "Laiti ungemwitisha Umar" (kila mmoja akamwita baba yake) wakakusanyika mbele ya Mtume. Alipowaona Mtume akawaambia "Ondokeni nikikuhitajini nitakuiteni". Taz: Tarikhut Tabari J.3 Uk. 439.

(c) Mtume(s.a.w.w) alipowaambia Aisha na Hafsa, "Nyinyi ni watu wa Yusufu" hapa inaonyesha kuwa amri ya kusalisha Abubakr si ya Mtume(s.a.w.w) , hali ya kisa cha wanawake waliomtaka Nabii Yusufu (a.s) na yeye akajizia, na kisa cha Aisha na Hafsa kuwatanguliza mbele baba zao ni jambo lililofanana.

(d) Mtume(s.a.w.w) alitoka akichechemea taabani na watu wawili wamemshikilia, Abubakr akapisha mahala hapo, na Mtume(s.a.w.w) akashika mwenyewe kusalisha. Ni jambo gani lililomlazimisha kutoka akiwa hali hii, ikiwa yeye ndiye aliye amuru Abubakr asalishe? Jambo gani lililomsonga asalishe watu hali amekea chini kwa taabu na dhiki kubwa?

(e) Kuonyesha dalili zote hizi, haina maana kuwa: kama itasihi kuwa Abubakr amesalisha, basi itapasisha Abubakr kushika uongozi baada ya kuondoka (kufa) Mtume(s.a.w.w) . Hii haina maana, kwa sababu nafsi ya kusimama mbele na kusalisha watu si jambo lenye kima na thamani tukufu ambalo litampasisha kupata kila apitae mbele na kusalisha watu!! Kwa mujibu wa Hadithi za ndugu zetu Masunni, inasema kuwa: Mtume(s.a.w.w) amesema, "Salini nyuma ya kila mwema na muovu ". Na kwa msingi huu Madhihabi ya Imam Shaafy na Imam Ahmad na wengine wamepasisha Mwislamu asali nyuma ya ye yote japokuwa Fasiq.

Taz: Assunanu Walmubtadiatu Uk. 182.

Lakini pia tukiliangalia kwa wema suala hili tunaona kuwa: Mtume(s.a.w.w) alipokuwa akitoka kwenda vitani, nyuma alikuwa akiweka mtu wakushika mahala pake katika masuala mbalimbali, ikiwa ni pamojana kusalisha.

SAQIFA

Kwanza; ni vizuri kujua maana ya neno: Saqifa: Ni Klabu au ukumbi. Amesema Mwana Aisha kuwa: "Zilipotangazwa habari za kifo cha Mtume(s.a.w.w) Umar bin Khattab na Mughira bin Shuubam waliingia ndani alikolazwa Mtume(s.a.w.w) . Umar akasema: Oh msiba mzito kwa kuondokewa na Mtume, kisha walitoka nje, walipokuwa mlangoni Mughira akasema: Ewe Umar! Kwa kweli Mtume amekufa, Umar akajibu: Wewe muongo, Mtume hajafa isipokuwa wewe ni mtu unayesumbuliwa na fitina. Mtume hatakufa mpaka wanafiki wamalizike wote.

Taz: Albidayatu Wannihaya J.5 Uk. 212.

Hatimae Umar alikamata upanga akaonya kuwa: Ye yote atakaesema kuwa Mtume amekufa atakata kichwa chake. Alipofika Abubakr, Umar akanyamaza na akaweka upanga wake chini. Kisha Abubakr akatangaza kuwa Mtume amekufa, na hapo ndipo alipoondoka yeye na Umar kwenda mwenye ukumbi wa Bani Saida. Huko walijumuika na Masahaba kutoka Ansar wa Madina tayari kwa uchaguzi. Abubakr alitoa hutuba ndefu katika mkutano huo akiwakumbusha kuwa wao (Muhajir) ndio wenye haki ya kushika uongozi mahala pa Mtume(s.a.w.w) . Hutuba ambayo ilijibiwa baadae na Hubab bin Mundhir katika Ansar, naye akionyesha kuwa ma-Ansar wanayo haki zaidi yao, kwa sababu kwao (Madina) ndiko kuliko shamiri na kukomaa nguvu za Uislam, na Waislamu kupata Uhuru wa kuabudu. na ikiwa hapana budi basi kwa Muhajir atoke mmoja na kwa Ansar atoke mmoja. Hapo ndipo Umar aliposimama akasema: "Hilo haliwezekani, panga mbili hazikai katika ala moja, Wallahi Waarabu hawakubali kuwatawalisheni na hali Mtume wao hatokani na nyinyi".

Baada ya mabishano makali na kushutumiana, karibu wauwane, hatimae Abubakr akachaguliwa. Kama asemavyo Umar: "Kuchaguliwa kwa Abubakr kulitokea ghafla, Mwenyezi Mungu alizuia shari zake, na atakaerejesha kitendo kama hiki auliwe".

Taz. Tarikhul Tabari J.2 Uk. 446/457 Tarikh Ibn Athir J.2 Uk. 223 Sahih Bukhar J.8 Uk. 210 Albidayatu Wannihaya J.5 Uk. 215.

Abubakr na Umar hawakuwahi kumzika Mtume(s.a.w.w) .

Taz: Kanzul Ummal J.5 Uk. 652.

Wakati wote huo Imam Ali yuko nyumbani kwa Mtume(s.a.w.w) akishughulikia maandalizi ya kumzika Mtume. Kisha baada ya kumzika Mtume(s.a.w.w) Imam Ali alibaki nyumbani kwake yeye na mkewe Mwana Fatima (a.s) wakawa wanakusanyika hapo Bani Hashim. Abubakr baada ya kutawalishwa alimpeleka Umar bnil Khattab nyumbani kwa Mwana Fatima(a.s) ili akawatoe wote waje kumbai Abubakr akamwagiza kuwa: Endapo watakataa kutoka kuja kumbai, awauwe. Umar akaenda na kijinga cha moto, Mwana Fatima alipomuona mlangoni na kijinga hicho akamuuliza: Ewe Umar! Umekuja iwasha nyumba yetu? Umar akajibu Ndiyo Wallahi nitakuunguzeni au mtoke kwenda kumbai Abubakr". Inasemekana kuwa: Umar alipoingia nyumbani kwa Mwana Fatima, alimpiga ngumi ya tumboni, ngumi ambayo iliumiza ujauzito na kuzaliwa mtoto aliyekufa! Na kwa sababu ya kipigo hicho, afya ya Mwana Fatima ilidhoofu sana na baadae kufariki. Umar alikuwa akiyakumbuka haya, mwenyewe husema "Laiti ningelikuwa kondoo niliyefugwa, nikanenepeshwa kiasi cha kupendeza. Akija mgeni nikatwekatwe sehemu nyama yangu ikaangwe na sehemu ibanikwe, kisha wanile na wanitoe nikiwa mavi nisiwe binadamu".

Taz: Kanzul Ummal J.12 Uk. 619.

ALI HAKUMBAI ABUBAKR

Mwana Aisha amesema kuwa:- "Ali (a.s) hakumbai Abubakr ila bada ya miezi sita kupita ". Abubakr alikwenda nyumbani kwa Imam Ali(a.s) akawakuta Bani Hashimu wamekusanyika, Imam Ali akamwambia "Sisi haikutuzuilia kukubali ewe Abubakr, kwa kupinga heshima yako wala ubora aliokupa Mwenyezi Mungu, lakini sisi tunaamini kuwa jambo hili (la uongozi) ni letu na nyinyi mmelipokonya kwetu ". Kisha akawa anamtajia nafasi aliyonayo kwa Mtume(s.a.w.w) na haki zake mpaka Abubakr akaangua kilio.

Taz: Tarikhut Tabari J. 2 Uk. 448

Abu Bakr Aliposhika utawala, alitoa hotuba kwa mara ya kwanza, na hii ni sehemu ya hotuba hiyo "Hakika mimi ninae shetani hunifikia mara kwa mara basi wakati wo wote atakaponifikia muniepuke ".

Taz: Tarikhut Tabari J.2 Uk. 460.

Mwenyezi Mungu anasema "Hakika sisi tumewajaalia mashetani kuwa marafiki wa wale wasioamini " 7:27.

Abubakr anae shetani, na kila mwenye kuambatana na shetani si muumin, Abubakr ni nani? Mwenyezi Mungu anasema: "Na yule ambaye amekuwa shetani ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya sana " 4:38

TUKIO LA HIJRA

Mwenyezi Mungu anasema:

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا ﴿٤٠﴾

"Kama hamtamsaidia basi Mwenyezi Mungu amekwisha msaidia walipomfukuza wale waliokufuru, alipokuwa wa pili katika wawili walipokuwa wote, wawili katika pango. Alipomwambia swahibu yake; usihuzunike hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Ndipo Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona" 9:40.

Uchunguzi wetu katika Aya hii utahusu silabi zilizotumika katika mfumo wa Aya hii, kwa hiyo tutajadili hapa nukta saba:

(a) Amekwisha msaidia

(b) Walipomfukuza

(c) Alipokuwa wapili katika wawili

(d) Alipomwambia swahibu yake

(e) Usihuzunike

(f ) Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi

(g) Akamteremshia utulivu wake.

(a) Amekwisha msaidia lliposemwa "Mwenyezi Mungu amekwishamsaidia". Hapa pana dhamiri ya mmoja aliyesaidiwa, naye ni Mtume Muhammad(s.a.w.w)

(b) Walipomfukuza lliposemwa:- "Walipomfukuza" ni mtu mmoja aliyefukuzwa, Mtume Mohammad(s.a.w.w) .

(c) Alipokuwa wa pili katika wawili lliposemwa "Alipokuwa wa pili katika wawili". Hii ni jumlatul haliyya, swahibul hali ni dhamiri katika: "Akhrajahu" inayomrejea Mtume Mohammad(s.a.w.w) . Natija inasema "Walimfukuza peke yake".

(d) Alipomwambia Swahibu yake lliposemwa "Alipomwambia Swahibu yake" watu wengi wanafikiri kuwa Mwenyezi Mungu kulitumia tamko la "Swahibu" katika Aya hii ni ibara inayompa sharaf kubwa Abubakr. Ni vizuri kuliangalia tamko Ia "Swahibu" linavyotumiwa katika Quran: "Akamwambia Swahibu yake hali akibishana naye, mimi nina mali nyingi kuliko wewe na nguvu zaidi kwa wafuasi. Na akaingia bustani yake hali ya kujidhulumu nafsi yake, Swahibu yake akamwambia hali ya kubishana naye. Je! Umemkufuru yule aliyekuumba kwa udongo tena kwa tone Ia manii kisha akakufanya mtu kamili? 18:34-37 Mazungumzo haya yalikuwa kati ya muumini na kafiri, wakiambizana "Swahibu yangu".

(e) Usihuzunike Iliposemwa "Usihuzunike", hapa pana Suratun Nahyi, ambayo Huzuni imepatikana kwa Abubakr ama kwa Sura ya Twaatullah au kwa Sura ya Maaswiyatullah!! Ikiwa ni twa'atullah, basi Mtukufu Mtume(s.a.w.w) hakatazi twa'a bali anaiamrisha na kuwataka Waislamu wawe watiifu. Na ikiwa ni maasi, basi Mtume(s.a.w.w) ameyakataza, Abubakr alihuzunika na Mtume(s.a.w.w) akamkataza.

(f) Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi Iliposemwa "Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi" Naam: "Hawashauriani kwa siri watatu ila Mwenyezi Mungu ni wa nne wao. Wala watano ila Mwenyezi Mungu ni wa sita wao, wala wachche kuliko hao wala zaidi ila Mwenyezi Mungu huwa pamoja nao popote walipo " 58:7.

(g) Akamteremshia utulivu wake Iliposemwa: "Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake " Assakiina (utulivu) ni jambo wanalolipata watu wema tu. Hapa tutataja taratibu za matumizi ya tamko hili lilivyokuja katika Quran:

a. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha Utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya waumini" 9:26.

b. "Yeye ndiye aliyeteremsha Utulivu katika nyoyo za waumini ili waongezeke imani juu ya imani yao" 48:4.

c. Basi akateremsha Utulivu juu yao (waumini) na akawapa ushindi wa karibu" 48:18.

d. Mwenyezi Mungu akateremsha Utulivu wake juu ya Mtume na juu ya waumini" 48:26

Lakini katika pango tunasoma hivi "Mwenyezi Mungu akamteremshia Utulivu wake na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona". Aliyeteremshiwa hapa ni Mtume Muhammad tu peke yake.

ABUBAKR AMTEUA UMAR

Abubakr alipokuwa mgonjwa taabani alimwitisha Uthmani bin Affan ili aandike wasia juu ya Umar binil Khattab, akamwambia: "Andika Bismillahir Rahmanir Rahimi, hili ni agizo la Abubakr bin abi Quhafa kwa Waislamu wote" mara Abubakr akazimia Uthman akaendelea kuandika: "Amma baada ya haya, nimekutawalisheni Umar bnil Khattab na sikuacha kukupendeleeni kheri". Kisha Abubakr akazimuka, akauliza: Umeandika nini? Uthmani akassomea yale aliyoyaandika, Abubakr akashangilia sana kisha akasema Uliogopa kuwa khitilafu ingetokea kama ningezimia moja kwa moja? Uthmani akajibu: "Ndiyo Abubakr akasema Mwenyezi Mungu akulipe wema". Umar akashika mahala pa Abubakr.

Taz: Tarikhut Tabari J.2 Uk. 618 Tarikh Ibn Athir J.2 Uk. 292.

Katika tukio la Ghadir Khum, vitabu vya tarikh vimeonyesha kuwa Umar alitoa Baia kwa Imam Ali bin Abi Talib(a.s) . Na katika kumbukumbu ya tarikh vile vile vitabu kama vile: Assunanu Walmubtadia'tu ukurasa wa pili, inasimuliwa kuwa: Katika zama za Mtume(s.a.w.w) Waislamu wawili waligombana wakaenda kwa Mtume kuamuliwa. Mtume(s.a.w.w) baada ya kusikiliza ugomvi baina yao, mmoja akamtia makosa na wa pili akampa haki. Yule aliyeonekana na makosa mbele ya Mtume (s.a.w.w) akakafaa kukubali makosa yake, kwa hiyo akashauri kesi yao ipelekwe kwa Abubakr. Wakaenda kwa Abubakr, wakamhadithia namna kesi yao ilivyosikilizwa na kuhukumiwa na Mtume(s.a.w.w) , Abubakr akasema: Sina zaidi ya alivyohukumu Mtume(s.a.w.w) . Hapo vile vile ikashindikana, wakaamua kwenda kwa Umar binil Khattab, wakamhadithia walivyoanzia kwa Mtume kisha kwa Abubakr. Umar akachomoa upanga akakata kichwa cha aliyekataa kutii hukumu ya Mtume(s.a.w.w) . Pale pale Mwenyezi Mungu akateremsha Aya ya 65 ya Sura ya 4 kuwa:

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

"Naapa kwa Mola wako, hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye hakimu wao katika yale waliyohitilafiana kati yao, kisha wasione dhiki katika nyoyo zao kwa hukumu uliyotoa na wanyenyekee sana sana".

Ikiwa Umar amekata kichwa cha mtu aliyekataa kutti hukumu ya Mtume, kisha Mwenyezi Mungu akambariki kwa kitendo hicho.

(a) Kwa nini Umar hakukata kichwa cha Abubakr aliyekwenda kinyume na Aya ya 67 ya Sura ya 5 ambayo imeshuka kwa ajili ya kumtawalisha Imam Ali bin Abi Talib(a.s) . Kitendo ambacho kilihudhuriwa na zaidi ya Waislamu laki moja, akiwamo Abubakr na yeye mwenyewe Umar?

(b) Na; kwa nini Umar hakukatwa kichwa kwa kuipinga Aya 67 ya Sura ya 5 ambaye alionekana hadharani akitoa BAIA kwa Imam Ali(a.s) kuwa ndiye Imam wake baada ya kuondoka Mtume?

MAMBO ALIYOYAONDOA KATIKA DINI

Umar binil Khattab ameondoa: "Ndoa ya Mut'a na Tamattuu ya hija." Taz: Tafsirut Tabari J.5 Uk. 9 Tafsirul Qurtubi J. 5 Uk. 130 Tafsirul Razi J. 3 Uk. 200 Umar ameondoa: "Hayya a'la khairil-amal" (katika adhana na Iqama). Taz: Lisanul Mizani J.1 Uk. 268 Mizanul Itidal J.1 Uk. 139 Sunanul Bayhaq J.1 Uk. 524 Da'aimul Islami J.1 Uk. 45.

MAMBO ALIYOYAWEKA KATIKA DINI

Umar binil Khattab aliweka: "Talaka tatu kuwa tatu" (zinazotolewa kwa mara moja)

Taz: Tafsirul Qurtubi J.3 Uk. 130 Sahihi Muslim J.4 Babut Talaka Fiq'hus Sunna J.2 Uk. 231 Musnadu Ahmad J.1 Uk. 314.

Umar ameweka: "Assalatu khairun minan-nawm" (katika adhana ya asubuhi). Taz: Al-Muwattau J.1 Uk. 25.

Umar aliweka: "Swala ya Tarawih" (kwa jamaa).

Taz: Tarikhu Ibn Athir J. 3 Uk. 31 Tabaqatul Kubra J. 3 Uk 281 Tarikhul Khulafai Uk. 136.

TUKIO LA SHURA

Imepokewa kwa Qatada kuwa: Umar alipozidiwa karibu atakufa, aliwaita Waislamu mbele yake akasema: "Laiti Abu Ubaida bin Jarrahi angelikuwa hai ningelimchagua kuwa khalifa wenu, na laiti Salim mtumwa wa Hudhaifa angekuwa hai ningemchagua kuwa Khalifa wenu". Siku ya pili Umar akamwita Ali bin Abi Talib, Uthman bin Affan, Saad bin Abi Waqas, Zuberi bin Awwam, Abdur Rahman bin Awf, akawaambia: "Nimefanya uchunguzi kutafuta atakaeshika mahala pangu, sikuona mwingine isipokuwa nyinyi. Shaurianeni kwa muda wa siku tatu mchague mmoja atakaekuwa Khalifa wenu, Katika siku tatu hizo za mashauriano atakusalisheni Suhaibu, na Talha bin Ubeidillahi. Mchague mmoja atakaekuwa Khalifa wenu. Katika siku tatu ni mwenzenu katika mashauri haya, akirudi katika siku tatu hizi mtieni katika wagombea. Na asipowahi basi chagueni na yeye yuko pamoja nanyi, mwanangu Abdillahi atahudhuria kikao chenu kama mashauri tu. Watano kati yenu wakimchagua mmoja, na mmoja akipinga, basi kateni kichwa chake. Wanne wakichagua mmoja, na wawili wakikataa, basi wauweni. Ikiwa watatu wakikubaliana mmoja wao, na watatu wakikataa, elekezeni shauri hili kwa mwanangu Abdillahi. Kama atakataa, basi angalieni upande aliosimama Abdur Rahmani bin Awf, ndio ulio na haki na watatu waliobaki wauliwe".

Waislamu wakamuomba ajaribu kumpendekeza anayemuona anafaa kushika mahala pake. Umar akawaambia: "Wallahi hainizi wilii kukupa Ukhalifa ewe Saadi isipokuwa ukatili ulio nao na kwamba ni mpiganaji.

Na haikuniziwia kukupa wewe Abdur Rahmani ila ni kwa sababu wewe ni firauni wa umma huu. Na haikuniziwia kukupa wewe Zuberi isipokuwa tabia uliyonayo, unapofurahi huwa muumini kweli kweli na uanapoghadhibika huwa kafiri hasa. Siku moja unakuwa shetani, siku nyingine unakuwa binadamu. Unaonaje siku unayokuwa shetani nani atashika Ukhalifa siku hiyo? Na sitaki kumpa Talha kwa sababu ya majivuno yake, na kama atashika Ukhalifa akili yake yote itafikiria wanawake. Na sitaki kumpa Uthmani kwa sababu uongozi atawaachia Bani Umayya. Na haikuniziwilia kukupa wewe Ali isipokuwa pupa uliyo nayo, na wewe ndiye bora ya watu wote, ikiwa utashika Ukhalifa bila shaka utasimamia sheria za Mwenyezi Mungu". Baada ya kufa Umar, ile kamati ikakutana, Talha akajitoa katika wagombea, na haki yake akamwachia Uthman bin Affan. Zubeir naye akajitoa na haki yake akaiacha kwa Ali.

Saad yeye naye akaacha haki yake kwa Abdur Rahman. Kwa hiyo wagombea wakabaki watatu: Ali, Uthman, na Abdur Rahman. Walipokaa kikao, Abdur Rahman aliuliza: "Nani kati yenu atajitoa katika kugombea ili awe na haki ya kuchagua mwingine"? Jamaa wakakaa kimya. Abdur Rahman akawaambia Nimefanya utafiti kujua nani mnampendelea kuwa Khalifa wenu, nimegundua ama Ali au Uthman. Kisha baada ya majadiliano marefu siku ya tatu, Abdur Rahman akamwita Ali akamshika mkono na kumwambia: "Toa ahadi kuwa utaongoza kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na sunna za Mtume wake na utafuata mwenendo wa Abubakr na Umar". Ali akajibu: "Hapana, isipokuwa nitafuata Quran na Sunna za Mtume"(s.a.w.w) Abdur Rahman akamwachia mkono kisha akamwita Uthman naye akamshika mkono na kumwambia: "Toa ahadi kuwa utaongoza kwa kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake na utafuata mwenendo wa Abubakr na wa Umar?" Uthman akakubali; "Ndio" Abdur Rahman akasema, "Ee Mola! Sikia na ushuhudie, mimi nampa dhamana hii Uthman". Ali bin Abi Talib akatoka nje huku akisema: "Ipo siku itafikia".

Taz: Tarikhut Tabari J.3 Uk. 301 Tarikh Ibn Athir J.3 Uk. 34 Kanzul Ummal J.5 Uk. 741.