HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s.

HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s.27%

HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s. Mwandishi:
Kundi: VITABU VYA HADITHI

HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s.
  • Anza
  • Iliyopita
  • 13 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 30816 / Pakua: 10370
Kiwango Kiwango Kiwango
HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s.

HADITH ZA MTUME s.a.w.w.NA MA-IMAMU a.s.

Mwandishi:
Swahili

HADITH ZA MTUME (s.a.w.w) NA MA-IMAMU (a.s)

ZIMEKUSANYWA NA KUTARJUMIWA NA AMIRALY M.H.DATOO

UTANGULIZI

Allah swt anatuambia katika Al-Qur'an tukufu: Sura al-Nahl, 16, Ayah 43 Nasi hatukuwatuma kabla yako ila watu wanaume tulio wapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui. Sura Al-Ambiya, 21, Ayah 7 Na kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa Wahyi (ufunuo). Bas waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui. Ayah hii Tukufu inawasihi Waumini kujielekeza kwa Ahl-Dhikr yaani watu wenye busara na Wanazuoni wa Ummah ili kuweza kubainisha baina ya haki na batili, wakati ambapo Waumini wanapokumbana na shida au ugumu katika masuala mbalimbali, kwa sababu Allah swt baada ya kuwafundisha ilimu, aliwachagua hao kwa hayo. Hivyo, wao wamebobea katika ilimu na ambao ndio watu halisi wanaoielewa, kuifundisha na kuitekeleza kwa usahihi mafunzo ya Qur'an.

Ayah hii iliteremshwa kwa ajili ya kuwatambulisha Ahlul-Bayt(a.s) nao ni Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) , Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) Fatimah(a.s) , Al-Imam Hassan ibn Abi Talib(a.s) . na Al-Imam Husayn ibn Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) , ambao kwa ujumla wanaitwa Watukufu watano au 'Al-i-'Aba ambapo pamoja na hao wameongezeka Ma-Imamu(a.s) . wengine tisa kutokea kizazi cha al-Imam Husayn ibn Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) mara nyingi katika nyakati mbalimbali aliwatambulisha hao kuwa ni Ma-Imam waongozi, nuru katika kiza, na ni wale ambao wamebobea katika ilimu na bila shaka Allah swt amewajaalia Ilimu ya Kitabu Kitukufu. Ukweli huu, kama ilivyorejewa mahala pengi katika Ahadith mbalimbali kuanzia zama za Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) kuanzia ufunuo hadi leo hii, na vile vile wanazuoni wengi na Wafasiri kutokea Ahl-Sunnah wamekiri waziwazi katika vitabu vyao kuwa Ayah hizi za Qur'an zilikuwa zimeteremshwa hususan kwa ajili ya kuelezea na kuwatambulisha Ahl-ul-Bayt (a.s) Baadhi ya mifano ya vitabu vyenyewe ni kama ifuatavyo:

1. Imam Tha'labi katika tafsiri ya kitabu chake juu ya Ayah hiyo ya 42 kutokea Sura An-Nahl, namba 16

2. Tafsir ibn Kathir, j.2, Uk.591

3. Tafsir at-Tabari, j.14, Uk.75

4. Tafsir-i-Alusi, ijukanavyo kama: Rahul-Bayan , j. 14, Uk. 134

5. Tafsir-i-Qartabi, j.11, Uk. 272

6. Tafsir-i-Hakim, au Shawahid-ut-Tanzil, j. 1, Uk. 334 7. Tafsir-i-Shabistrary, au: Ihqaq-ul-Haq, j.3, Uk.482 8. Yanabi'-ul-Muwaddah, cha Ghanduzi Hanafi, Uk. 119.

Kwa kutegemea ukweli huu, sisi lazima tujielekeze kwa Wananyumba ya Ahlul-Bayt(a.s) , na kutekeleza maneno yatuongozayo ili kuelekeza maisha yetu mema. Kwa sura hii, Imam-ul-Hadi(a.s) anasema katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na 'Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha: "Maneno yenu yenye busara yanatupa nuru, maamrisho yenu ni hidaya kwa watu na usia zenu ni Taqwa na usawa."

MUWE TAHADHARI ENYI WASOMAJI

Kwa kupitia Watukuu hawa ndipo sisi tunaweza kuokoka humu duniani na Aakhera na maisha yetu yakawa mema na salama. Twapata katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na 'Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha: "Ni kwa sababu yenu Allah swt ametutoa nje ya upotofu (wa ukafiri), ametufanya huru kutoka huzuni na masikitiko, na kutuchukua pa usalama dhidi ya maangamizo ya dunia na mioto ya Jahannam pia." Katika katika Man la Yahdhuruh-ul-Faqih, Tahdhib na 'Uyun-i-Akh-bar-ur-Ridha twasoma:

"Ni kwa sababu ya Ukuu na uongozi wenu kuwa Allah swt ametufundisha ilimu ya kanuni za Dini , na kuweka sawa na vyema yale yote yaliyovurugika na kufasidika katika dunia. (Naye ametuepusha na umasikini, udhalilifu na ujahili, na kututunukia ilimu, heshima na hadhi.) Kwa hakika, iwapo sisi tutawaacha hawa watukufu waliobarikiwa na kutukuzwa na Allah swt, basi hakuna shaka kuwa tutatumbukia katika upotoshi na maangamizi katika kila hali. Ndipo Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) amesema: "Mfano wa Ahlul-Bayt(a.s) yangu ni sawa na Safinah ya Mtume Nuhu(a.s) Yeyote yule atakaye ipanda basi kwa hakika ameokoka na yeyote yule atakayekhilafu kuipanda, basi kwa hakika amezama na kutokomea mbali." Amesema Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) :

"Inawezekana nikaitwa hivi karibuni nami nikaitikia. Hivyo, mimi ninawaachieni miongoni vitu viwili vilivyo vizito (vyenye thamani na maana kubwa mno): Kitabu cha Allah swt (yaani Qur'an) ni kamba iliyovutika kutoka mbinguni hadi ardhini, na Ahlul-Bayti(a.s) yangu; kwa hakika Allah swt, Mrehemevu, Mwenye kuwa Makini, amenijulisha kuwa kamwe, kamwe vitu hivi viwili havitatengana hadi kukutana na mimi hapo Hawdh-Kauthar (Chemchemi ya milele). Hivyo, muwe waangalifu mutakavyojishikiza navyo wakati ambapo mimi sitakuwapo." Na vile vile katika Hadith nyingineyo imeongezeka: "Kamwe, kamwe, hamtapotoka iwapo mutakuwa mumeshikamana navyo hivi vitu viwili." Hivyo, je ni heshima gani itakayopita kuliko Qur'an , Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) na Ahlul-Bayt(a.s) vikawa ni mifano yetu, waalimu na viongozi wetu? Na kwa sababu hizi ndipo sisi kwa moyo halisi na unyenyekevu tunasema:

Sisi tumefadhilika kwa sababu sisi ni wafuasi wa Madhehebu ambayo muasisi wake Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) na Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) (mja ambaye amekombolewa kutokana na minyororo ya udhalili na kuchaguliwa kuwa mkombozi wa binadamu wote kutoka utumwa mbali na ule wa Allah swt ) kwa kufuata mwongozo kutoka Allah swt. Sisi tumetukuzwa kwa kuwa na kitabu kitakatifu cha Nahjul-Balagha, ambacho ni kitukufu baada ya Qur'an Tukufu, chenye maandiko matukufu kwa ajili ya maisha yetu wanaadamu, ni kitabu kikubwa kwa ajili ya ukombozi wa mwandamu na maelekezo yake ya kiroho na kisiasa yanayo thamani kubwa kwa ukombozi na kimeandikwa na Ma'sum Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) Vile vile tumebarikiwa kwa Imam Al-Mahdi(a.s) atokanaye na Al Imam 'Ali ibn Abi Talib(a.s) .yu bado hai na kwamba anahabari na kujua habari zetu zote.

Sisi tumebarikiwa kuwa na Doa ambazo ndizo zilizofunzwa na Ma-Imam(a.s) kama Dua za Sha'baniyyah, Dua ya 'Arafah ya al-Imam Husayn ibn 'Ali ibn Abi Talib(a.s) , Sahifa-i-Sajjadiyah ya al-Imam Zayn-al-'Aabediin(a.s) , na Sahifa-i-Fatimah. Vile vile sisi tumebarikiwa kuwa na Mwanazuoni mkubwa katika zama zetu ambaye hawezi kueleweka kwa watu wengine isipokuwa Allah swt, Mtume Muhammad Mustafa(s.a.w.w) na Ma-Imamu(a.s) kwa sababu ya kipaji chake kikubwa cha ilimu na hekima. Vile vile sisi tumebarikiwa kwa kuitwa Madhehebu ya Ja'afariyyah na kwamba Fiqh ambayo ni bahari isiyo na mwisho ( ya ilimu ), ambayo ni mchango mmojawapo wa Al-Imam Ja'afar as-Sadiq(a.s) Vile vile sisi tunafakhari kubwa sana kwa kuwa na Ma-Imamu(a.s) wote, na tunawafuata kikamilifu. Sisi tumebarikiwa kwamba Maimam(a.s) wetu walikuwa wameteswa, kuwekwa mahabusu na vile vile kutolewa makwao kwa sababu wao walikuwa daima wamejitolea muhanga kuutetea ubinadamu na kuinua hali ya Dini ya Islam na kuyatekeleza maamrisho ya Qur'an yakiwemo maamrisho ya kutengeneza Serikali adilifu na hatimaye hao Ma-Imamu(a.s) waliuawa katika harakati zao za kutokomeza serikali dhalimu na Taghuti katika kila zama.

Sasa, ewe mpenzi kaka na dada Wewe ni shahidi wa macho, katika dunia hii ndogo, ndogo zaidi kuliko kijiji katika ulimwengu, unajionea kuwa hali ya binadamu inaendelea ipo inateketea katika jangwa la dhuluma na pasi na haki, wakati mwanadamu huyo yupo anatumbukia chini zaidi katika matingatinga ya kutokuhurumiwa na kukosekana kwa uadilifu. Wale wote wanaojidai kuhusu uhuru na raha ya mwanadamu wanashuhudia kwa makini kumomonyoka kwa maadili katika mazingira waliyoyaumba wao wenyewe. Wao hawana tena uwezo wa kudhibiti hali hiyo isipokuwa kuangamia kwa binadamu na ubinadamu. Lakini, je ni kweli kuwa huo ndio mwisho wa mstari huo? Jibu kwa kushangaa litakuwa ndiyo, hadi hapo mwanadamu atakaporejea katika uumbwaji kwake wa kiAllah swt, akimulika makosa na kasoro zake zilizopita kama ndiyo tochi kwa maisha yake ya mbeleni na akiitumia Islam kama ndiyo dawa ya matatizo yake yote.

Katika zama hizi, Islam ambayo ndiyo tukufu, na bora kabisa katika kutuongoza, bora katika katika historia, imetoa mikono yake kwa ajili ya kumnusuru mwananadamu ili asije akazama na kughalibiwa na maovu na kwa baraka za Allah swt, imesimama imara kumtibu mwanadamu dhidi ya magonjwa maovu kabisa ya maovu. Islam ipo kwa ajili ya kutuliza kiiu cha mwanadamu anayezurura katika majangwa ya chumvi kali zisizo na taqwa kwa kumnywisha maji matamu na baridi ya itikadi zilizonurishwa kwa ilimu na maarifa na utukufu wa Ahlul-Bayt(a.s) , ambayo ndiyo sura halisi ya tafsiri kamili ya ufunuo ambayo kamwe haikuwa na kosa au kasoro ya aina yoyote ile. Inatoa mwanga kwa hali zote na kimwili na kiroho ya maisha ya mwanandamu. Hivyo, imefungua milango kikamilifu kwa mwanadamu kukamilika kikamilifu. Lakini Ewe rafiki mpendwa NI jambo la muhimu na kwanza kabisa kwa kutaka kujua habari za shule yoyote ile pamoja na mafunzo yake, inatubidi sisi kutazama kwa undani maandiko na kuelewa mazungumzo na maneno ya viongozi wake. Na kwa njia hii ndipo sisi tutakapoweza kujua kuhusu itikadi na imani na malengo ya shule hiyo kuhusu dunia na matatizo yake na hivyo kuweza kufikia maamuzi na makisio ya upeo wake. Al-Imam 'Ali ar-Ridha(a.s) amesema: "Rehema za Allah swt zimfikie mja ambaye huisha maamrisho yetu " Nami nilimwuliza ni vipi mtu anaweza kuziweka hai maamrisho yenu? Imam(a.s) alijibu "Yeye anaweza kujifunza ilimu na maarifa yetu na kuwafundisha wengineo. Kwa hakika, iwapo watu watazijua faida na mema za miihadhara na misemo yetu, basi kwa hakika watazifuata kuzitekeleza. "[1]

Matumaini mema Twategemea kuwa msomaji kwa kuyasoma na kuyazingatia maneno yenye thamani isiyosemekana, kuwa kwa kupitia maneno na maongozao ya Ahlul-Bayt(a.s) vizazi vyetu hususan vijana wataongoka na kamwe hawatapotoka wala kuvutiwa na mavutio yanayotuongoza kuelekea maangamizo ya milele na kwamba utamaduni wetu hautamomonyoka siku baada ya siku na badala yake tutatengeneza utamaduni wetu uwe utamaduni wa Kiislamu kwa baraka na miongozo za Ahlul-Bayt(a.s) na kwamba tutakuwa washupavu na maaskari kulinda imani na Din ya Islamu dhidi ya maadui wake walio ndani na nje. Tutakuwa Waislamu bora na mfano kwa watu wote. Amani na Salaam ziwafikie wale wote waliongoka.

1. MAIMAMU WA SHIA KATIKA UANDIKAJI NA UENEZAJI WA HADITH

Katika sehemu hii, twategemea kuzungumzia kwa mukhtasari msimamo wa Shia kuhusu uandikaji wa Hadith kutokea mwanzoni. Itaonekana kuwa ni kinyume na msimamo wa wengine kuhusu swala hili. Msimamo wa Kishia ulisisitiza mno juu ya uandikaji wa Hadith zikisaidia uhifadhi wake wakati ambapo Maulamaa mashuhuri wa Kisunni, hata kufikia mwanzoni mwa karne ya 3A.H./9 A.D. walikuwa wakipinga uandikaji wa Hadith. Ni baada ya uandikaji wa Hadith ulipokuwa dhahiri hao wanaopinga walipoanza kwenda kinyume na Hadith walizokuwa wamezitoa wakipinga uandishi na uenezaji wake na hapo wakaanza kuziandika. Alba ibn al-Ahmad ananakili kuwa mara moja Ali ibn Abi Talib(a.s) wakati akitoa Hotuba juu ya mimbar, alibainisha: "Je, ni nani atakayeinunua elimu kwa Dirhamu moja?" Al-Harith ibn al-A' war alinunua karatasi yenye thamani ya Dirhamu moja na kumwijia Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) na kuandika kiasi cha kutosha cha elimu juu yake. Riwaya hii inatuonyesha vile Imam(a.s) alivyokuwa akisisitiza juu ya uandikaji. Imam Hassan ibn Ali ibn Abi Talib(a.s) ameripotiwa akiwashauri watoto wake kama ifuatavyo:

"Nyinyi sasa ni watoto wa Ummah ambao katika maisha ya mbeleni mtakuwa wakubwa wao. Jielimisheni Elimu; na yeyote yule miongoni mwenu atakayeweza kuhifadhi (kukariri) elimu (yaani Hadith), basi aiandike na kuiweka nyumbani mwake." Imeripotiwa kuwa Hujr ibn Adi, mmoja wa Sahaba wa Mtume(s.a.w.w) na Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) , aliziandika Hadith za Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) katika kitabu na kuzirejea pale alipohitaji msaada wa mwongozo katika masuala mbalimbali Mifano hii inadhihirisha umuhimu aliokuwa ameuambatanisha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) , watoto wake na Sahaba wake katika uandikaji wa Hadith. Mifano miwili ifuatayo itaonyesha dhahiri vile Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) alivyokuwa akisisitiza umuhimu wa Hadith na kuzihifadhi. Umar ibn Ali anaripoti kuwa mtu mmoja alimwuliza Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) ni vipi kuwa yeye (i.e. Ali) aliweza kunakili na kusimulia Hadith nyingi za Mtume(s.a.w.w) kuliko Sahaba wengineo. Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) alijibu: "Hii ni kwa sababu daima nilipokuwa nikimwuliza swali Mtume(s.a.w.w) , alikuwa akinijibu maswali yangu. Na pale nilipokuwa nikiwa kimya, basi Mtume(s.a.w.w) alianzisha mazungumzo mwenyewe." Ali ibn Hawshab anaripoti kutoka Makhul, mwanachuo kutokea Syria, kuwa Mtume(s.a.w.w) aliisoma Ayah (69:12).

Na hapo alimwambia Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) "Mimi nimemwomba Allah swt kuwa masikio hayo yawe ni yako." Baadaye Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) alisema: "Mimi kamwe sikusahau Hadith yoyote au chochote kile kilichosikilizwa na sikio langu kikisemwa na Mtume(s.a.w.w) Umar ibn al-Harith anasema: "Wakati mmoja Ali(a.s) aliuelekeza uso wake kuelekea mbinguni na kuurudisha chini akisema:"Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) wamesema kweli." "Je, kilikuwa nini?" Kikundi cha watu kiliuliza. Imam Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) . alisema: "Mimi ni mpiganaji wa vita na vita vinarithishia mtu ulaghai. Vivyo hivyo, ninaweza kukubali iwapo nitaporomoka kutokea mbinguni kwa ajili ya kunaswa na ndege kuliko kumsingizia uwongo Mtume wa Allah swt. Kwa hivyo fuateni chochote kile mukisikiacho kikitoka kwangu........" Kauli juu ya uandishi wa Hadith pia zimenakiliwa kutoka Maimamu wengine.

Al-Imam al-Sadiq(a.s) alisema: "Andikeni na kuieneza elimu yenu miongoni mwa ndugu zenu, na iwapo mtafariki basi watoto wenu watarithi vitabu vyenu. Itafika siku ambapo patatokea machafuko na hapatakuwapo na mtu wa kumfanya rafiki na wala hapatakuwa na chochote cha kuweza kutegemewa isipokuwa ni vitabu tu.... Al-Imam al-Sadiq(a.s) pia amenakiliwa kwa kusema: "Hifadheni vitabu vyenu kwani mutakuja kuvihitaji hivyo siku moja." Vile vile ameripotiwa akisema kuwa nguvu za moyo na kuhifadhi akilini inategemea mno juu ya maandishi. Abu Basir anaripoti kuwa aliambiwa na Imam al-Sadiq(a.s) : "Baadhi ya watu waliotoka Basrah walikuwa wakija na kuniuliza kuhusu Hadith na waliziandika. Je, kwa nini nawe hauziandiki?" Na aliongezea kusema, "Elewa wazi wazi kuwa wewe kamwe hautaweza kuhifadhi Hadith bila ya kuiandika." Idadi kubwa ya mapokezi yanaonyesha kuwa Maimamu(a.s) walikuwa navyo vitabu na maandishi ambavyo walirithi kutoka vizazi vilivyowatangulia.

Katika riwaya nyingine Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) ameripotiwa akiwa amesema: "Ikamateni elimu (kwa kuiandika)," ambavyo aliirejea mara mbili Imeripotiwa kutoka Ja'bir kuwa Abu Hanifa alikuwa akimwita al-Imam al-Sadiq(a.s) "Kutubi" (yaani mwenye vitabu) kwa sababu ya kutumia mno vitabu, na Imam(a.s) alifurahishwa kwa jina kama hilo. Vile vile imeripotiwa kuwa al-Imam Muhammad ibn Ali al-Baqir(a.s) ameziandika Hadith za Mtume(s.a.w.w) ambazo zilikuwa zikinakiliwa na Jaabir ibn Abdullah Ansaari. (Ingawaje taarifa hii inaonyesha kuwa siyo ya ukweli kwani Jaabir alikuwa ameshakwisha kufariki wakati Imam(a.s) alikuwa na umri wa miaka mitano tu, labda inawezekana kuwa Hadith ziliandikwa na mjumbe).

2. MASHIA NA UANDISHI WA HADITH

Kwa kuwa riwaya (desturi) ya uandishi wa Hadith ilikuwapo miongoni mwa Shia tangia mwanzoni, wao walikuwa wanaongoza katika uandishi wa Hadith na Fiqh. Dr. Shawqi Dayf anaandika: "Mwelekeo na umuhimu wa Mashia katika uandishi wa Fiqh umekuja daima ni madhubuti mno. Sababu nyuma yake ilikuwa ni imani yao katika Maimamu wao ambao walikuwa ni kiongozi wao (haad) na wakiwa wameo ngozwa na Allah swt (mahdi) na fatawa zao zimekuwa zimeshikamana. Kwa hivyo, wao walipatiwa uzito na umuhimu katika misemo ya Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) Na kwa sababu hiyo, mkusanyiko wa kwanza ulifanywa na Mashia, ulifanywa na Sulaym ibn Qays al-Hilali, katika zama za al-Hajjaj." Al-Allamah al-Sayyid Sharaf al-Din anaandika:

"Imam Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) na wafuasi wake walitilia mkazo na kufuatilia swala la uandishi kuanzia mwanzo kabisa. Jambo la kwanza kabisa lililotiliwa mkazo na kufuatiwa na Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) ilikuwa ni kuiandika Quran nzima, ambayo aliifanya baada ya kifo cha Mtume(s.a.w.w) kwa kuiandika kimpangilio wa ufunulio wa Aya za Qurani.Katika Qurani hiyo pia alikuwa ameonyesha ni aya zipi zilizokuwa 'amm au khass, mutlaq au muqayyad, muhkam au mutashabih. Baada ya kukamilisha hayo, aliendelea na kazi ya ukusanyaji wa kitabu kwa ajili ya Fatimah, ambacho kilikuwa kikijulikana kwa vizazi vyao kama Sahifat Fatimah. Baada ya hayo, aliandika kitabu juu ya diyat (fidia) ambacho kilijulikana kama Sahifah. Ibn Sa'id amenakili hivyo katika musnad kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) . mwishoni mwa kazi yake mashuhuri al-Jami.' Mtunzi mwingine wa Kishia ni Abu Rafi, ambaye alikusanya maandiko yakiitwa kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya. " Marehemu Sayyid Hassan al-Sadr anaandika kuwa Abu Rafi, aliyekuwa mawla wa Mtume(s.a.w.w) ndiye aliyekuwa wa kwanza miongoni mwa Mashia kwa kukikusanya kitabu. al-Najashi katika Fihrist ameelezea kuwa Abu Rafi alikuwa ni mtunzi katika kizazi cha kwanza cha Mashia. Mfuasi wa Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) Abu Rafi alishiriki katika vita vya Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) na alikuwa ni mwangalizi wa hazina ya Serikali huko Kufah. Kitabu chake kilichokuwa kikiitwa Kitab al-Sunan wa al-ahkam wa al-qadhaya, ambacho kilikuwa kimeanza kwa sura izungumziayo Salat, kufuatiwa na sura juu ya Saumu, Hajj, Zakat, kutolewa kutoka kwa Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) katika Kufah, Kitabu hiki kilinakiliwa na Zayb ibn Muhammad ibn Ja'afer ibn al-Mubarak katika nyakati za al-Najashi. Ali ibn Abi Rafi, mwana wa Abu Rafi, aliye tabi't na Mshia khalisi ameweza vile vile kukusanya kitabu kilichokuwa na sura mbali mbali juu ya mambo ya Sheria kama vile wudhuu, Salaat, n.k.

Kama ilivyoelezwa hapo awali, abu Hanifa alimwita al-Imam al-Sadiq(a.s) kutubi (akisema 'innahu kutubi' ) sifa ambayo ilimtambulisha na wengineo. Wakati Imam(a.s) aliposikia kuhusu hayo, alicheka na kusema, "...... lakini kila alichokisema kuwa kwangu suhufi ni kweli; mimi nimesoma suhuf (vitabu) vya mababu zangu." Riwaya hii inaonyesha kwa wazi wazi kuwa Imam(a.s) . alikuwanavyo vitabu fulani ambavyo alipewa na mababu zake, na hiki kilikuwa ni kipindi ambacho Ahl al-Sunnah walikuwa hawakutilia mkazo katika uandishi wa Hadith. Miongoni mwa mapokezi ambayo inatuonyesha kuwa ma-Imam(a.s) walikuwa navyo vitabu kama hivyo, ni mojawapo iliyoripotiwa na Muhammad ibn 'Udhafir al-Sayrafi anasema: "Mimi nilikuwa pamoja na al-Hakam ibn Utaybah na tulimtembelea al-Imam al-Baquir(a.s) Al-Hakam alimwuliza swali Imam(a.s) Abu Ja'afer(a.s) alikuwa akimstahi sana. Wao walitofautiana juu ya swala fulani na hapo Abu Ja'afer alisema: "Mwanangu (mtoto wake), inuka na ukilete kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) Huyo mtoto alimletea kitabu kikubwa, ambacho Imam(a.s) alikifungua, na kulipitishia macho hadi kulipata swala walilokuwa wakilizungumzia. Na hapo Abu Ja'afer(a.s) alisema: "Haya ni maandishi ya Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) na yaliyosemwa na Mtume(s.a.w.w) ..........." Katika riwaya nyingineyo ameripotiwa Imam al-Baquir(a.s) akisema: "Katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) nimepaona ambapo Mtume(s.a.w.w) akisema: 'Wakati zakat itakapokuwa hailipwi, basi baraka itapotea kutoka ardhi." Vile vile ipo imeripotiwa kuwa Imam al-Sadiq(a.s) amesema:

Baba yangu alisema: "Mimi nimesoma katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) kuwa Mtume(s.a.w.w) ameandika mkataba baina ya Muhajirun na Ansar na watu wengineo wa Yathrib ambao waliungana naye, ikisemwa humo hivi: "Jirani ni sawa na mtu mwenyewe; asitendewe visivyo haki au kutendewa madhambi. Utukufu wa jirani wa mtu ni sawa na ule utukufu wa mama yake." Katika riwaya nyingine al-Imam al-Sadiq(a.s) amesema: Imeelezwa katika kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) "Mfano wa dunia ni sawa na mfano wa nyoka: ngozi yake nyororo mno, lakini ndani yake ni sumu kali mno. Mtu aliye mwenye busara hujiweka naye mbali, lakini jahili anafanya kila aina ya jitihada ya kutaka kuikaribia." Kwa mujibu wa riwaya nyingineyo, habari ifuatayo imetoka katika kitab adab Amir al-Muminiin: Mtu yeyote asijaribu kurejea katika mithali katika masuala ya Din, kwani amri ya Allah swt haiwezi kutambuliwa kwa mithali. Watatokezea watu ambao watakuwa wakirejea katika mithali, na hao watakuwa na uadui pamoja na Din. Zurarah anaripoti:

Nilimwuliza al-Imam al-Baquir(a.s) kuhusu hisa ya babu katika urithi. Imam(a.s) alijibu: "Sijawahi kumwona mtu yeyote yule akilisemea swali hili bila ya kuongezea mawazo yake ya kibinafsi, isipokuwa Amir al-Muminiin Ali ibn Abi Talib(a.s) .." Mimi nilimwuliza: "Na jee alisema nini?" Imam(a.s) alinijibu: "Njoo kesho, mimi nitakusomea kutoka kitabuni." Mimi nilisema, "Mimi niwe fidia juu yako, naomba uiseme katika mtungo wa Hadith kwani Hadith zako ni afadhali kwangu kuliko kukisoma kitabu." Imam(a.s) alisema: "Tafadhali usikilize kile nilichokuambia. Njoo kesho na mimi nitakusomea kutoka kitabu hicho ." Siku ya pili mimi nilimwendea Imam(a.s) wakati wa adhuhuri. Jaafer ibn Muhammad mwanae Imam(a.s) alinikaribia na Imam(a.s) alimwambia kunisomea kitabu hicho........ Katika riwaya nyingine, Imam al-Sadiq(a.s) anasema: "Ipo imeelezwa katika Kitabu cha Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) kuwa mtu anywaye pombe na mwenye kumsaidia aliyelewa (muskir) basi wote wanastahili kuadhibiwa, ambavyo ni sawa katika sura zote mbili." Muhammad ibn Muslim, Sahaba wa Imam al-Baquir(a.s) asema: "Abu Jaafer alinisomea kitabu kitab al-faraidh, ambacho yalikuwemo yaliyosemwa na mtume(s.a.w.w) na kuandikwa na Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) "Habari zote zilizotajwa hapo juu, ambazo ni chache sana kutokea riwaya nyingi mno kama hizo, zinatudalilisha kuwa desturi ya Mashia ya kuandika Hadith imetangulia mawaidha ya ma-Imam(a.s) kwa sahaba wao kuhusu uandishi wa Hadith. Ilikuwa ni desturi ambayo ilianzia katika zama za Mtume Mtukufu(s.a.w.w) na ilikuwa imeanzishwa na Imam Ali ibn Abi Talib(a.s) Zipo Hadith, nyingi katika desturi ya Mashia ambazo zimetimiza kanuni za tawatur, na vile vile yapo marejeo katika Sunni ambazo zinathibitisha na kushuhudia Hadith kama hizo.

Mambo yote hayo yanakuelekeza katika uimara na uhakikisho wa usahihi wa Hadith zilizonakiliwa na Mashia. Hii ni kwa sababu pamoja na kuendelea na maongozo ya Maimamu(a.s) hadi kufikia katikati ya karne 3 A.H./9 A.D., Hadith za Mashia zilitoa watunzi wengi mno na ambao maandishi yao kuanzia kipindi cha al-Imam al-Sadiq(a.s) yamekuwa kwa hakika ni katika idadi kubwa sana. Iwapo mtu ataweza kutupia macho Rijal al-Najashi, basi huyo ataweza kuona kuwa wafuasi wa Imam(a.s) wametupatia kazi kubwa ambazo zimetumika kama misingi ya Fiqh katika Ushia. Ukweli ni kwamba, Mashia idadi yao ndogo kwa upande mmoja na maisha ya hatari waliyokuwa wakiishi kwa upande wa pili ambayo iliwazuia watu waovu na wenye kuvizia majukumu kuingia katika Ushia pamoja na umuhimu uliosisitizwa na Maimamu(a.s) na wafuasi wao katika uandishi, ndivyo vilivyoleta matokeo ya utajiri na usahihi wa Fiqh ya Kishia. Haya ndiyo faida ambazo hazikupatikana kwa Ahl al-Sunnah kwani, kwanza, wingi wa idadi yao, pili, kwa kuwa madhehebu ya Sunni ndiyo iliyokuwa Dini ya utawala wa Dola, na tatu, kwa sababu ya ukosefu wa Hadith zilizoandikwa kwa Waislam kwa ujumla kuyafuatilia yale yanayotokana na ukweli wa misingi ya kihistoria.

3

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

SURAT YUNUS 19-23

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an.

AYA YA 19

Hii ni darsa ya 310, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 ambayo inasema:

وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلَّا أُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُوا وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ فِيمَا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿١٩﴾

19. Wala watu hawakuwa ila umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka hukumu ingelikwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.

Mwenyezi Mungu sw amewaumba wanaadamu wote wakiwa na fitra yaani maumbile safi ya tauhidi ya kukubali kuwepo kwa Mungu mmoja.

Hivyo hapo awali wanaadamu wote walikuwa ni sawa na umma mmoja. Lakini kwa kupita muda, na kuzainiwa na shetani kundi miongoni mwa watu wakatumbukia kwenye upotofu wa shirki na hivyo watu wakagawika katika makundi mawili ya wampwekeshao Allah na Mushrikina. Ama Mwenyezi Mungu hakutaka kuwateza nguvu waja wake, bali alitaka kila mtu achague kwa hiyari yake njia anayoamua kufuata. Na ni kwa sababu hiyo ndipo akaamua kuwapa fursa na muhula wale waliokhitari upotofu kufanya lolote lile watakalo.

Na lau si utaratibu huo aliouweka Mwenyezi Mungu basi angewaadhibu papa hapa duniani na kumaliza hitilafu kati ya waumini na makafiri. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa thamani na utukufu wa mwanadamu unapatikana kwa kule kufanya ayatakayo ikiwa ya thawabu au ya madhambi kwa hiyari yake. Vinginevyo hakuna fakhari yoyote kwa mtu kuamini na kufuata njia ya haki kwa kulazimishwa.

AYA YA 20

Ifuatayo sasa ni aya ya 20 ambayo inasema:

وَيَقُولُونَ لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَقُلْ إِنَّمَا الْغَيْبُ لِلَّـهِ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa kutoka kwa Mola wake miujiza (tunayoitaka)? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu.Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja na nanyi katika wanaongoja.

Nabii Muhammad(s.a.w.w) alikuja na miujiza mbali mbali kama walivyokuwa Manabii waliomtangulia. Tabaan muujiza mkuu wa Mtume huyo wa mwisho ni quran tukufu ambao washirikina walishindwa kukabiliana nao hata kwa kuleta walau aya moja mfano wake.

Lakini katika kutafuta visingizio, washirikina hao kila siku walikuwa wakitaka waonyeshwe muujiza mpya ikiwa ni pamoja na kumtaka Bwana Mtume awaletee kila wanachotaka. Ndipo katika kuwajibu Bwana Mtume akawaambia muujiza ni suala lililoko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu na wala haliko mikononi mwangu mimi, na ni kila pale anapotaka yeye ndipo muujiza unapoletwa, ama mnachotaka nyinyi si kitu kingine ghairi ya kutafuta visingizio tu.

Ukweli wa haya wapenzi wasomaji unashuhudiwa pia kama tulivyoona katika aya zilizotangulia pale washirikina wa kikureishi walipomtaka Bwana Mtume azibadilishe aya za quran au hata ikiwezekana awaletee qurani nyingine mpya badala ya ile aliyoteremshiwa na Mola wake.

Pamoja na mambo mengine aya hii inatufunza kuwa chanzo na chimbuko la shirki na ukafiri si kutokuwepo muujiza na hoja za kuthibitisha ukweli wa risala ya haki, isipokuwa ni tabia ya ukaidi, inda na inadi mbele ya haki.

AYA YA 21

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 21 ambayo inasema:

وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً مِّن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُمْ إِذَا لَهُم مَّكْرٌ فِي آيَاتِنَا قُلِ اللَّـهُ أَسْرَعُ مَكْرًا إِنَّ رُسُلَنَا يَكْتُبُونَ مَا تَمْكُرُونَ ﴿٢١﴾

21. Na tunapowaonjesha watu rehma baada ya shida iliyowapata, mara huanza kutunga hila (za kutaka kupinga) Aya zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayoyapanga.

Historia inasimulia kuwa ilitokea wakati mmoja mji wa Makka ulikumbwa na ukame mkubwa lakini Mwenyezi Mungu kwa baraka ya kuwepo Nabii Muhammad(s.a.w.w) akateremsha mvua zake za rehma na kuuletea faraja mji huo.

Ama washirikina wao walidai kuwa kunyesha kwa mvua hizo kulitokana na baraka za masanamu yao.

Ndipo aya tuliyoisoma ikashuka na kuwatanabahisha kuwa kama nyinyi ni wenye kutaka hakika ya mambo, basi tambueni kuwa mvua hizo ilikuwa ni muujiza utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo inadi yenu imekufanyeni muzue hila hizi na zile za kuzinasibisha na masanamu yenu rehma hiyo iliyotoka kwa Mola wenu.

Pamoja na hayo tambueni kuwa malaika wa Mwenyezi Mungu ambao hutumwa kwa watu wanayanakili na kuyarekodi yote yanayotendwa na waja na hivyo mushirikina wajiandae na majibu ya kwenda kumpa Mola wao siku ya kiyama kwa yote wanayoyatenda.

Tabaan katika dunia hii pia Mwenyezi Mungu atawapa jaza ya vitimbi na hila zao, nao katu hawawezi kusimama dhidi ya irada ya Allah s.w.t.

AYA ZA 22 NA 23

Aya za 22 na 23 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

هُوَ الَّذِي يُسَيِّرُكُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ حَتَّىٰ إِذَا كُنتُمْ فِي الْفُلْكِ وَجَرَيْنَ بِهِم بِرِيحٍ طَيِّبَةٍ وَفَرِحُوا بِهَا جَاءَتْهَا رِيحٌ عَاصِفٌ وَجَاءَهُمُ الْمَوْجُ مِن كُلِّ مَكَانٍ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ أُحِيطَ بِهِمْ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ لَئِنْ أَنجَيْتَنَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ ﴿٢٢﴾

22. Yeye ndiye anayekuendsheni bara na baharini. Hata mnapokuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, mara upepo mkali ukawazukia na yakawajia mawimbi kutoka kila upande na wakaona wameshatingwa, hapo ndipo wanapomwomba Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia utii (wakisema): Ukituokoa na haya bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

فَلَمَّا أَنجَاهُمْ إِذَا هُمْ يَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا بَغْيُكُمْ عَلَىٰ أَنفُسِكُم مَّتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُكُمْ فَنُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٣﴾

23. Lakini akishawaokoa mara wanafanya jeuri tena katika ardhi bila ya haki.Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Ni starehe (chache tu) za maisha ya dunia. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.

Bila shaka mngali mnakumbuka wapenzi wasomaji kuwa tulisema mwanzoni mwa darsa yetu hii kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu wote katika fitra na maumbile safi ya tauhidi ya laa ilaha illa llah, yaani kukana waungu wengine wote bandia na kuthibitisha hakika ya kuwepo kwa Mola mmoja tu wa haki.

Baada ya kueleza hayo, aya hizi tulizosoma hivi punde zinabainisha kuwa mapumbao haya na yale ya kidunia huwa mithili ya utando unaogubika na kufililiza nuru hiyo ya tauhidi ndani ya nafsi ya mtu na kumfanya mja aghafilike na Mola wake.

Ama pale mtu anapotingwa na kupatwa masaibu yanayomfanya akate tamaa ya kupata nusra kupitia njia yoyote ile hapo ndipo utando ule unapotoweka mithili ya vumbi lililosukumwa na upepo na kuiamsha fitra na maumbile ya tauhidi, na kumshuhudia mja akimlingana na kumwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu Mola wake aliyemuumba msaada wa nusra na uokozi.

Lakini kama tulivyowahi kuashiria katika moja ya darsa zilizopita baada ya kupata nusra ya Allah mwanadamu husahau kila kitu mara moja, akighafilika kwamba maisha haya ya dunia ni mafupi na ya kupita tu, na kwamba sisi sote mwisho wetu na marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu, na huko kila mmoja atasimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ili kuwajibika kwa yote aliyoyafanya hapa duniani.

Aya hizi zinatuoenyesha kuwa majanga ya kimaumbile husaidia kuondoa ghururi na kiburi cha mwanadamu na kuamsha hisia za kumtambua na kumnyenyekea Mola wake.

Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa imani ya msimu na ya mazingira fulani haina faida; imani ya kweli ni ya kudumu na ya katika kila hali, awe mtu katika raha na neema au shida na nakama.

Darsa ya 310 inaishia hapa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaomwamini na kuikiri tauhidi katika hali zote. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 24-27

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 24

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 311 tunayoianza kwa aya ya 24 ambayo inasema:

إِنَّمَا مَثَلُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ مِمَّا يَأْكُلُ النَّاسُ وَالْأَنْعَامُ حَتَّىٰ إِذَا أَخَذَتِ الْأَرْضُ زُخْرُفَهَا وَازَّيَّنَتْ وَظَنَّ أَهْلُهَا أَنَّهُمْ قَادِرُونَ عَلَيْهَا أَتَاهَا أَمْرُنَا لَيْلًا أَوْ نَهَارًا فَجَعَلْنَاهَا حَصِيدًا كَأَن لَّمْ تَغْنَ بِالْأَمْسِ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mawinguni, kisha mimea ya ardhi wanayoila watu na wanyama ikachanganyika nayo (maji hayo, ikastawi). Hata ardhi ilipokamilika uzuri wake na ikapambika, na wenyewe wakadhani wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana na tukaifanya kama iliyofyekwa, kama kwamba haikuwako jana. Namna hivi tunazipambanua aya (zetu) kwa watu wanaofikiri.

Katika kubainisha baadhi ya masuala, Mwenyezi Mungu ametumia ndani ya quran lugha ya tamthili na tashbihi. Aya tuliyoisoma ni miongoni mwa aya hizo ambayo imelinganisha na kushabihisha hali ya kupita na kumalizika haraka dunia kuwa ni sawa na ardhi iliyonawiri kutokana na kunyeshewa na mvua lakini pale inapokuja kukumbwa na kimbunga au mafuriko tahamaki kila kitu kilichopandwa katika ardhi hiyo kinatoweka kana kwamba havukiwepo hapo kabla.

Aya hii wapenzi wasomaji inatuelimisha kuwa umri wa mwanadamu katika dunia hii ni mfupi mithili ya umri wa mimea na maua hivyo tusihadaike tukadhani kuwa tutabaki milele katika ulimwengu huu.

AYA YA 25

Ifuatayo sasa ni aya ya 25 ambayo inasema:

وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَىٰ دَارِ السَّلَامِ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٢٥﴾

25. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea nyumba ya amani, na humuongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka (maadamu anakubali uwongofu).

Mkabala wa maisha haya ya mafupi na ya kupita ya dunia kuna maisha mengine ya milele ya akhera ambayo Mwenyezi Mungu amewataka waja wake wayapiganie hayo na akawapelekea Mitume pia wa kuongoza watu kuelekea kwenye makazi ya utulivu wa kweli.

Ni wazi kuwa watu wanaoshikamana na kamba ya uongofu ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewahisi kuwa wana ustahili wa kufikia makazi hayo na ambao matendo na amali zao hapa duniani hazikuwa sababu ya kujiweka mbali na njia iliyonyooka.

Aya hii inatufunza kuwa raha na uzima wa dunia ni vitu vya kupita tu, kinyume chake raha na uzima wa akhera ni za kudumu na za milele. Funzo jengine tunalolipata katika aya hi ni kuwa njia pekee ya kufikia kwenye utulivu na raha za kweli ni kupiga hatua kuelekea kwenye njia ya iliyonyooka ya Allah, ambayo hapa duniani huupa moyo wa mja utulivu na huko akhera humuongoza kuelekea kwenye pepo ya saada.

AYA YA 26

Tuitegee sikio sasa aya ya 26 ambayo inasema:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ وَلَا يَرْهَقُ وُجُوهَهُمْ قَتَرٌ وَلَا ذِلَّةٌ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٦﴾

26. Wale waliofanya wema watapata (jaza ya) wema (wao) na ziada; Wala vumbi halitawafunika nyuso zao wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi; humo watakaa milele.

Baada ya aya iliyotangulia kuashiria juu ya pepo, aya hii inasema Mwenyezi Mungu ameiandaa pepo hiyo kwa wale waja wake waliofanya mema, na kwamba jaza na malipo watakayopata waja hao iwe ni kwa sura ya wingi au ubora, yatakuwa makubwa na bora zaidi kuliko amali walizotenda hapa duniani, .kama ambavyo katika aya nyinginezo Allah s.w.t anasema yeyote atendaye jema moja hupata thawabu na malipo mara kumi ya jema hilo, ambapo kwa upande wa utoaji, malipo ya mja hufikia hata mara mia saba ya kile alichotoa.

Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa ikiwa Mwenyezi Mungu ametuita tuifuate njia yake ya uongofu kisha akatuonyesha njia ya kuifikia, na kisha akatushajiisha na hata kuwalipa thawabu na malipo bora kabisa wale wanaoifikia njia hiyo, ni kitu gani basi cha kutufanya tuache kuitikia mwito wa Mola wetu na kuwafuata wengine wasiokuwa yeye?

AYA YA 27

Aya inayotuhitimishia darsa yetu ni aya ya 27 na ambayo inasema:

وَالَّذِينَ كَسَبُوا السَّيِّئَاتِ جَزَاءُ سَيِّئَةٍ بِمِثْلِهَا وَتَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ مَّا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِنْ عَاصِمٍ كَأَنَّمَا أُغْشِيَتْ وُجُوهُهُمْ قِطَعًا مِّنَ اللَّيْلِ مُظْلِمًا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٧﴾

27. Na wale waliochuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile; na yatawafika madhila. Hawatakuwa na awezaye kuwalinda na (adhabu ya) Mwenyezi Mungu. Zitakuwa nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni; humo watakaa daima.

Wakati ambapo wale waliotenda matendo mazuri watakuwa na mwisho mwema huko akhera, wale waliokhitari kufuata upotofu kwa kumkufuru na kumwasi Mola wao hawatapata jaza nyingine ghairi ya adhabu ya Allah, na wala hawatoweza, wala kupata pa kukimbilia, ambapo ukali wa adhabu watakayopata utazifanya nyuso zao zititie na kupiga weusi.

Tabaan adhabu hiyo italingana kabisa na uzito na kiwango cha madhambi waliyofanya, ama kwa upande wa watenda mema wao watapata fadhila zake Mola za kulipwa malipo ya kheri yaliyo makubwa zaidi ya mema waliyotenda.

Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu akiwa amewapa uhuru na hiyari ya kuchagua njia ya kufuata. Na ndiyo maana kundi moja linaamua kufuata mema na jengine linakhitari kufuata maovu.

Halikadhalika aya inatufunza kuwa katika mfumo wa malezi wa Uislamu siku zote ushajiishaji kwa kutoa hidaya na zawadi unapewa kipaumbele kuliko utiaji adabu na utoaji adhabu.

Darsa ya 311 inaishia hapa. Tunamwomba Allah ajaalie bora ya amali zetu ziwe ni zile za lahadha ya mwisho ya uhai wetu, na siku bora kwetu iwe ni ile ya kukutana na yeye. Amin

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 28-33

Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an.

AYA ZA 28 NA 29

Hii ni darsa ya 312, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya za 28 na 29 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ نَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ نَقُولُ لِلَّذِينَ أَشْرَكُوا مَكَانَكُمْ أَنتُمْ وَشُرَكَاؤُكُمْ فَزَيَّلْنَا بَيْنَهُمْ وَقَالَ شُرَكَاؤُهُم مَّا كُنتُمْ إِيَّانَا تَعْبُدُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na siku tutakapowakusanya wote, kisha tutawaambia wale walioshirikisha: 'Simameni mahali penu nyinyi na wale mliowafanya washirika wa Mungu.' Kisha tutawatenga baina yao. Na hao waliowashirikisha watasema: 'Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.

فَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ إِن كُنَّا عَنْ عِبَادَتِكُمْ لَغَافِلِينَ ﴿٢٩﴾

29. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yetu na baina yenu. Hakika sisi tulikuwa hatuna habari ya ibada yenu.

Aya hizi zinabainisha jinsi hali itakavyokuwa siku ya Kiyama, ambapo Mwenyezi Mungu atawasimamisha mushirikina na wale waliokuwa wakiwaabudu na kuliuliza kila kundi peke yake; kwa nini nyinyi mlikuwa mkiyaabudu masanamu na miungu wa kubuni? Na nyinyi pia ilikuwaje mkaridhia kuabudiwa na watu hawa? Hapo ile miungu ya masanamu isiyo na uhai itapewa uhai kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuwakana wale waliokuwa wakiwaabudu na kutamka kuwa, "sisi hatukuwa tukijihesabu kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu, bali nyinyi mlijitengenezea taswira akilini mwenu, na kuziabudu na sisi kutufanya kama kisingizio tu".

Aya ya 41 ya suratu Sabaa pia imeashiria maudhui hii na kueleza kuwa malaika nao ambao walikuwa wakiabudiwa wanadhihirisha, kuchukizwa kwao na kitendo hicho cha Mushrikina.

Nukta yenye mguso wa aina yake hapa ni kuwa katika aya hizi Allah s.w.t amewataja waabudiwa hao kuwa ni washirika wa Mushrikina kwa maana kwamba, hao hawakuwa waungu wanaoshirikishwa na Mwenyezi Mungu, bali ni washirika wenu nyinyi mushirikina mliojibunia na kujitengenezea wenyewe.

Miongoni mwa yale tunayojifunza katika aya hizi ni kuwa siku ya Kiyama, mbali ya wanaadamu, miungu na waabudiwa bandia yakiwemo masanamu yatapewa uhai ili kutoa ushahidi katika mahakama ya uadilifu dhidi ya mushirikina.

AYA YA 30

Ifuatayo sasa ni aya ya 30 ambayo inasema:

هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَّا أَسْلَفَتْ وَرُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٣٠﴾

30. Huko kila mtu atayajua aliyoyatanguliza. Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki. Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua.

Baada ya masanamu na waabudiwa wengine kuwakana mushirkina, hapo makundi mawili hayo yatatenganishwa na mushirikina hawatoweza kuwaomba msaada hao waliokuwa wakiwafanya washirika wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na badala yake watarejea kwa Mola wao wa haki yaani Allah sw na hapo ndipo watapata jaza na malipo ya amali zao.

AYA YA 31

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 ambayo inasema:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣١﴾

31. Sema: 'Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na katika ardhi. Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani amtoaye mzima katika mfu na kumtoa mfu katika mzima?Na nani anaye yadabiri mambo yote?' Watasema: 'Ni Mwenyezi Mungu.' Basi sema: 'Je Hamuogopi?

Baada ya aya zilizotangulia ambazo zimeonyesha unyonge na udhalili utakaowapata washirikina siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake awaulize watu hao kuwa nyinyi ambao mnamkubali Mwenyezi Mungu, na mnajua kuwa ni yeye ndiye anayekuruzukuni, na ni yeye ndiye anayesimamia mambo yenu yote, kwa nini basi badala ya kumwabudu yeye mnayaabudu masanamu na kuyafanya wasita na waunganishi wa mambo yenu kwa Mwenyezi Mungu?

Kama ambavyo katika aya nyingine za quran imeelezwa kuwa mushirikina wa enzi za ujahiliya walikuwa wakikubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wao na Muumba wa ulimwengu, ama katika suala la kuendesha mambo, mamlaka hayo yako mikonnoni mwa malaika na vitu vingine vya maumbile, kama kwamba Mwenyezi Mungu ameumba tu kisha akakaa kando na kulikabidhi kwa viumbe hao suala la uendeshaji wa ulimwengu.

Fikra ya aina hii imeelezwa na quran tukufu kuwa ni batili na aina mojawapo ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa uendeshaji wa ulimwengu unahitajia tadbiri isiyobadilika, na hili halingewezekana kama kungekuwepo na Muumba zaidi ya mmoja.

AYA ZA 32 NA 33

Aya za 32 na 33 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ ﴿٣٢﴾

32. Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki isipokuwa upotofu tu? Basi huwaje mkageuzwa?

كَذَٰلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ فَسَقُوا أَنَّهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٣﴾

33. Hivi ndivyo kauli ya Mola wako itakavyowathubutikia wale walioasi, ya kwamba hawataamini.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha mifano ya ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na kukiri kwa washirikina kuhusu uumbaji wa Mwenyezi Mungu.

aya hizi zinabainisha wazi kuwa Mungu huyu ndiye Mola wenu, na vile vile ndiye muendeshaji mambo yenu; na si kwamba yeye ni muumba wenu lakini masanamu yakawa ndio waendeshaji wa mambo yenu.

Kisha aya zinaendelea kwa kutoa kauli ya mkato kwamba, hakuna hali ya tatu baada ya haki na batili. Kwa maana kwamba kila kitu ima ni haki au ni batili, na kwa hivyo kwa kuwa Mwenyezi azza wa jal ndiye haki, basi bila shaka masanamu na miungu wenu wengine wa kubuni hawawezi kuwa haki, na hivyo wale watu wanaoamua kuipa mgongo haki kwa inadi, ubishi na ukaidi hawawezi kupata taufiki ya kuufikia uongofu.

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa hakuna njia ya tatu baada ya haki na batili. Na kwa hivyo yanapothibitika mawili hayo, hakuna nafasi ya mtu kudai kuwa yeye hayuko huku wala huku bali ni mtu wa kati na kati.

Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuepushe na shirki na kuijenga imani kamili na safi ya tauhidi ndani ya nyoyo zetu. Amin

SURAT YUNUS 34-38

AYA ZA 34 NA 35

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 313 tunayoianza kwa aya za 34 na 35 ambazo zinasema:

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ قُلِ اللَّـهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣٤﴾

34. Sema: Je Yupo katika miungu yenu ya ushirikina, aliyeanzisha kuumba viumbe kisha akavirejesha? Sema: Mwenyezi Mungu ameanzisha kuumba viumbe kisha ndiye atakayevirejesha. Huwaje basi mkadanganywa?.

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ قُلِ اللَّـهُ يَهْدِي لِلْحَقِّ أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لَّا يَهِدِّي إِلَّا أَن يُهْدَىٰ فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ ﴿٣٥﴾

35. Sema: Je Yupo katika miugu yenu ya ushirikina anayeongoa kuendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi je anayestahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiyeongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?.

Zikiendelea kuzungumzia yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu kutoa changamoto kwa mushrikina ya kuwaonyesha jinsi miungu yao bandia isivyo na uwezo wa kufanya lolote, aya tulizosoma zinasema, ikiwa mtatupia jicho na kuzingatia uumbaji ulivyo mtabaini kuwa hakuna yeyote ghairi ya Mungu Mmoja awezaye kuumba kila kilichopo na kukipa uhai mpya, na hayo masanamu yenu mnayoyaabudu na viumbe vingine vyote vilivyoko, vyote hivyo vimeumbwa na vinamhitajia Muumbaji, basi yawaje vitu hivyo viweze navyo kuwa waumbaji wa ulimwengu?

Kama nyinyi ni wenye kutafuta uongofu na kutaka kuifikia saada tambueni kuwa miungu wenu hao wenyewe hawana cha kumuongoza mtu hata muweze kupata muongozo wa kufuata kutoka kwao, na kama ni suala la kupata uongofu, inalazimu wao wenyewe kwanza wawe na sifa hiyo ya kuweza kuufikia huo uongofu kisha ndipo waweze kukuonyesheni nyinyi pia njia ya kuufikia. Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muongozaji wenu wa kukufikisheni kwenye njia iliyonyooka. Tabaan uongofu wa Mwenyezi Mungu unapatikana kupitia Mitume wake na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo ambavyo kila kilichomo ndani yake ni maneno yake Mola Muumba.

Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa kutumia mfumo wa masuali na majibu ni mojawapo ya mbinu bora kwa ajili ya kujadiliana na wapinzani wa kiitikadi na kifikra, mbinu ambayo Allah sw amewafunza Mitume wake. Aidha aya zinatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu si Muumbaji wa ulimwengu tu, bali baada ya kuwaumba viumbe wake hakuwaacha kama walivyo, ila amewaonyesha pia njia yao ya uongofu itakayowafikisha kwenye saada ya duniani na akhera.

AYA YA 36

Ifuatayo sasa ni aya ya 36 ambayo inasema:

وَمَا يَتَّبِعُ أَكْثَرُهُمْ إِلَّا ظَنًّا إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayoyatenda.

Aya hii wapenzi wasomaji inaashiria chanzo na chimbuko la upotofu wa kifikra la wale wanaomkanusha na kumkufuru Mwenyezi Mungu na kueleza kuwa kufuata dhana na mambo ya udhanifu yasiyo na msingi ambayo kwa hakika ni njozi za kifikra ndiyo yaliyowafanya watu hao waipe mgongo haki na kung'ang'ania fikra na itikadi batili.

Hali ya kuwa katika masuala ya kifkra na kiitikadi, dhana na mambo ya udhanifu hayana nafasi wala itibari yoyote, na ukweli ni kuwa hakika na yakini ndiyo mambo yanayoweza kumfikisha mtu kwenye haki.

Mbali na hayo chimbuko la itikadi nyingi za zama za ujahilia lilikuwa ni watu kufuata yale waliyowakuta nayo babu zao na kushikilia na kuyanng'ang'ania mambo kwa sababu ya taasubi tu za kikabila, mambo ambayo hayakuwa na thamani wala itibari yoyote ya kielimu na kifikra.

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa katika masuala ya kiitikadi na kimaadili wingi hauwi kipimo cha kuonyesha haki. Kwani si hasha walio wengi katika watu wakawa wamepotoka kifikra na kimatendo.

AYA ZA 37 NA 38

Tunaihitimisha darsa yetu ya juma hili kwa aya za 37 na 38 ambazo zinasema:

وَمَا كَانَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ أَن يُفْتَرَىٰ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٧﴾

37. Na haiwezekani Qurani hii kuwa imetungwa, na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Bali inayasidikisha yaliyotangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake kutoka kwa Mola wa walimwengu wote.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّثْلِهِ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٣٨﴾

38. Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema:" Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao isipokuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnasema kweli.

Quran tukufu imetoa changamoto mara kadhaa ya kuthibitisha kuwa ni maneno ya mbinguni na kuonyesha kwamba si majini wala binaadamu walio na uwezo wa kuleta kitu kilicho mfano wake.

Bali ikafika mbali zaidi na kueleza kwa kujiamini kwamba, si kuleta mfano wa Quran yote au moja ya sura zake tu, bali kama wana uwezo, wapinzani wa muujiza huo wa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na walete walau aya moja tu iliyo mfano wa Quran.

Hata hivyo licha ya maadui na wapinzani wengi ambao Uislamu na Quran imekabiliana nao katika kipindi cha karne 14 zilizopita, hadi leo hii hakuna aliyethubutu kujitokeza kukabiliana na changamoto hiyo iliyotolewa na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.

Magwiji wa kila zama wa nahau na balagha pamoja na fani nyinginezo za lugha ya kiarabu wasio waislamu, wote hao wameshindwa kubuni walau aya moja tu iliyo na sifa za aya ya Quran tukufu.

Wapenzi wasomaji quran tukufu ina miujiza na maajabu ya aina kwa aina, machache kati ya hayo ni haya yafuatayo:

Kwanza : ni utamu wa maneno yake na mvuto wa ajabu yalionao, kiasi kwamba hata kama mtu ataisoma mara elfu hahisi kuwa amesoma kitu cha kushosha na kilichopitwa na wakati. Si hayo tu, bali vibwagizo vya maneno yake, mianguko yake ya sauti na mahadhi yake yamejipambanua na maneno mengine yote ya lugha ya kiarabu.

Ujumuishaji wa quran wa kila kipengele cha maisha ya mwanadamu vikiwemo vya masuala ya mtu binafsi, familia, jamii, masuala ya kisheria, kiuchumi, kisiasa na kiakhalqi ni wa namna ambayo, ni muhali kwa mwanaadamu yeyote kuweza kuufikia upeo wake.

Wapenzi wasomaji darsa ya 313 imefikia tamati. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aturuzuku kuisoma quran usiku na mchana, kwa namna airidhiayo yeye, na kutuwafikisha kutekeleza kivitendo yaliyomo ndani yake ili tuweze kupata uombezi wa quran siku ya kiyama. Amin.

SURAT YUNUS 39-44

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Karibuni katika mfululizo huu wa 314 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus.

AYA ZA 39 NA 40

Tunaianza darsa yetu kwa aya za 39 na 40 ambazo zinasema:

بَلْ كَذَّبُوا بِمَا لَمْ يُحِيطُوا بِعِلْمِهِ وَلَمَّا يَأْتِهِمْ تَأْوِيلُهُ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ ﴿٣٩﴾

39. Bali wameyakanusha wasiyoyaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Namna hivi walikanusha waliokuwa kabla yao. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa madhalimu hao.

وَمِنْهُم مَّن يُؤْمِنُ بِهِ وَمِنْهُم مَّن لَّا يُؤْمِنُ بِهِ وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِالْمُفْسِدِينَ ﴿٤٠﴾

40. Na miongoni mwao wapo wanaoiamini. Na miongoni mwao wapo wasioiamini. Na Mola wako anawajua vyema waharibifu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kutokana na dhana tu na bila kuwa na ushahidi mushirikina na makafiri walikuwa walivurumiza tuhuma kuwa Quran ni maneno ya Bwana Mtume na kukanusha kwa kudai kuwa kitabu hicho kitukufu hakina uhusiano wowote na Mwenyezi Mungu.

Aya tulizosoma zinasema kuwa kinachofanywa na makafiri na mushirikina hao ni kukariri yale yaliyosemwa na wenzao waliotangulia, kwani mitume wa kabla ya Nabii Muhammad(s.a.w.w) walikabiliwa na tuhuma sawa na hizo.

Hii ni pamoja na kuwa ukadhibishaji wao hauna mashiko yoyote ya kielimu, hivyo kitendo chao hicho ni sawa na kujidhulumu nafsi zao na pia ni dhulma kwa dini ya haki ya mbinguni na mitume waliotumwa na Allah kuitangaza dini hiyo kwa watu.

Lakini katika upande mwingine, kuna watu wanaoitambua na kuiamini haki, na hivyo, kama tulivyowahi kuashiria mara kadhaa, ndivyo alivyokadiria Allah s.w.t, kwamba: kila mtu kwa hiyari mwenyewe aamue ima kuwa muumini au kafiri. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa chanzo cha ukafiri, ukanushaji na ukadhibishaji haki ni kukosa utambuzi wa kuielewa haki hiyo. Kwani wale wanaokusudia kwa dhati kuitafuta na kutaka kuijua haki hufika mahali wakaitambua risala ya tauhidi waliyokuja nayo Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakaiamni.

Aidha aya zinatuelimisha kuwa kuyakanusha na kuyapa mgongo mafundisho ya manabii wa Allah ndiyo chanzo cha dhulma na ufisadi tunaoushuhudia ulimwenguni.

AYA YA 41

Ifuatayo sasa ni aya ya 41 ambayo inasema:

وَإِن كَذَّبُوكَ فَقُل لِّي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ أَنتُم بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٤١﴾

41. Na wakiendelea kukukadhibisha sema: Mimi nina amali yangu na nyinyi mna amali yenu. Nyinyi hamna dhima kwa niyatendayo, wala mimi sina dhima kwa mnayotenda nyinyi.

Aya hii inabainisha jinsi ya kuamiliana na makafiri na wapinzani wa haki na kueleza kuwa jukumu lenu nyinyi kwa watu hao ni kuwaonyesha tu na kuwatambulisha uongofu; si kuwalazimisha wao waufuate kwa nguvu, wala nyinyi kutaka kuwakumbatia wao ili kiwe kishawishi cha kuwafanya wavutiwe na haki.

Ikiwa wao watakuwa wamekaidi na kukataa kata kata kuiamini haki, dhima yenu kwao imeshaondoka, kwani imani ni jambo la moyoni na la hiyari, na hivyo watu hao ni kwamba wameshaamua hawataki kuielewa haki, na kama wameielewa, basi hawataki kuiamini.

Katika suala hili hutokezea baadhi ya Waislamu wakahisi kuwa labda ikiwa wao wenyewe wataamua kuacha kushikamana na baadhi ya mambo ya msingi ya dini huenda hilo linaweza kuwavutia wale wanaowalingania waikubali haki. Hali ya kuwa mtu hana haki yoyote ya kufanya hivyo kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya watu walioukubali uongofu.

Na ndiyo maana tunaona katika aya hizi Bwana Mtume Muhammad saw anatakiwa awaambie makafiri kwamba, madamu nyinyi hamko tayari kuyaamini maneno yangu, tambueni kuwa mimi najiweka mbali kabisa na matendo yenu na wala sina dhima wala jukumu lolote kwenu.

Funzo mojawapo tunalolipata katika aya hii ni kuwa Uislamu ni dini ya hoja, maadili na msimamo. Inatangaza na kuweka wazi msimamo wake; na kama ambavyo haimlazimishi mtu kuifuata, ndivyo vivyo hivyo nayo haiko tayari kulegeza msimamo katika misingi ya mafundisho yake.

AYA ZA 42, 43 NA 44

Darsa ya 314 inahitimishwa na aya za 42, 43 na 44 ambazo zinasema:

وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ وَلَوْ كَانُوا لَا يَعْقِلُونَ ﴿٤٢﴾

42. Na wako miongoni mwao wanaokusikiliza. Je wewe unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapokuwa hawafahamu?.

وَمِنْهُم مَّن يَنظُرُ إِلَيْكَ أَفَأَنتَ تَهْدِي الْعُمْيَ وَلَوْ كَانُوا لَا يُبْصِرُونَ ﴿٤٣﴾

43. Na wapo miongoni mwao wanaokukodolea macho. Je wewe utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٤﴾

44. Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao.

Katika kuendeleza yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu jinsi wapinzani wa haki walivyokuwa wakiamiliana na Bwana Mtume, aya hizi zinasema, si hasha baadhi ya wapinzani hao wakawa ni watu wanaohudhuria vikao vya Bwana Mtume, wakimwona kwa macho yao mtukufu huyo na kuyasikia yale anayoyasema; lakini yote hayo hayazipi athari yoyote nafsi zao. Na sababu ni kuwa yote hayo waliyokuwa wakiyashuhudia na kuyasikia hayakuwa yakipenya kweli kwenye masikio yao na kukita kwenye fikra na nyoyo zao.

Kana kwamba watu hao walikuwa ni vipofu wasioona au viziwi wasioweza kusikia chochote. Kimsingi ni kwamba kitu kinachompambanua mwanadamu na mnyama ni uwezo wake wa kufikiri na kutafakari, vinginevyo mnyama naye anaona na anasikia, bali hata uwezo na nguvu zake zake za kuona na kusikia ni kubwa zaidi kuliko za binaadamu. Hivyo linalomstahikia mwanadamu ni kuyatia kwenye tafakuri yale ayaonayo na ayasikiayo, kwa kupambanua la haki na la batili, kisha kushikamana na lile la haki na kujiweka mbali na lile la batili. Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa kuona na kusikia, ni utangulizi wa kutafakari na kuifahamu haki.

Wapenzi wasomaji darsa yetu ya juma hili inaishia hapa. Tunamwomba Allah atuwafikishe kuitambua haki na kuifuata, na kuielewa batili na kuiepuka. Amin.

SURAT YUNUS 45-49

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 45

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 315 tunayoianza kwa aya ya 45 ambayo inasema:

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ كَأَن لَّمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّنَ النَّهَارِ يَتَعَارَفُونَ بَيْنَهُمْ قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّـهِ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿٤٥﴾

45. Na siku atakapowakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa (duniani) ila saa moja tu ya mchana. Watatambuana. Hakika wamekhasirika wale waliokanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.

Ijapokuwa makafiri wamekadhibisha na kukanusha kuwepo kwa siku ya kiyama, hata hivyo watake wasitake ni kwamba wao pia kama ilivyo kwa wanaadamu wote watafufuliwa tu na kuishuhudia siku hiyo.

Uzito wa siku hiyo utakuwa hauna mfano wake kiasi cha kuwafanya wale waliokufuru wahisi kwamba umri wao wote walioishi hapa duniani, pamoja na kipindi chote cha maisha ya barzakh huko makaburini, ulikuwa ni sawa na muda wa saa moja tu ya mchana mzima.

Pamoja na wanaadamu kupitiwa na miaka bali pengine karne nyingi za baada ya kufa kwao, lakini watahisi kana kwamba wameamka tu kutoka kwenye usingizi wa kawaida. Katika hali hiyo watu watatambuana vizuri na wala hawatokumbwa na usahaulifu.

Ni wazi kwamba katika lahadha hiyo wale ambao hapa duniani walikanusha kuwepo kwa kiyama, wakati kweli itakapodhihiri na kujiona wamesimamishwa katika uwanja wa siku ya kiyama, hapo ndipo watakapobaini kuwa wao ni watu waliokhasirika kwa kufika mahala hapo wakiwa mikono mitupu, huku kukiwa hakuna tena fursa ya kurudi walikotoka.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa umri tunaoishi hapa duniani ni mfupi, kiasi kwamba siku ya kiyama mtu atajuta na kujihisi amekhasirika na kupata hasara kubwa kwa kutoitumia fursa hiyo ya uhai wa kupita aliojaaliwa hapa duniani.

Halikadhalika inatubainikia kutokana na aya hii ni kuwa hasara ya kweli ni ile ya mtu kuhitari na kufadhilisha starehe za kupita za hapa duniani kwa raha na neema za milele za huko akhera.

AYA YA 46

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 46 ambayo inasema:

وَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ اللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ ﴿٤٦﴾

46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayowaahidi au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni shahidi wa wanayoyafanya.

Aya hii inamliwaza Bwana Mtume na waumini kwa kuwaambia kuwa ikiwa mnaona Mwenyezi Mungu hawashushii adhabu kamili makafiri hapa duniani ni kwa sababu malipo hasa ya waja iwe ni adhabu ya moto au neema ya pepo wataipata huko akhera pale wote watakaporejea kwa Mola wao.

Hata hivyo sio kwamba adhabu ya kila ovu itasubiri huko akhera tu bali baadhi ya adhabu zitawashukia wakanushaji hapo papa hapa duniani, nawe Mtume utashuhudia kwa macho yako; na baadhi ya adhabu zitawashukia hata baada ya wewe kuaga dunia.

Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa waislamu wasikate tamaa kuona muda unapita bila makafiri kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mtimizaji wa ahadi anayotoa, tabaan kulingana na hikima yake mutlaki.

AYA YA 47

Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ فَإِذَا جَاءَ رَسُولُهُمْ قُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na kila umma una Mtume. Alipowajia Mtume wao walihuhukumiwa baina yao kwa uadilifu; wala hawakudhulumiwa.

Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa katika makundi mawili. Wale waliopewa vitabu na sheria, na wale ambao walikuwa wafikishaji na walinganiaji tu wa risala za Mitume waliopewa vitabu na sheria. Kutokana na aya za quran inabainika kuwa katika kipindi cha historia, na katika umma na kaumu mbali mbali za wanaadamu wamekuwepo watu waliokuwa wakiwafikishia wanadamu wenzao mafundisho ya mitume na yale yaliyokuja katika vitabu vya mbinguni.

Na ujumbe mkuu katika risala za manabii ulikuwa ni kusimamisha haki na uadilifu na kupambana na dhulma na uonevu. Na hivyo siku ya kiyama Allah sw ataawafufua watu wa kila kaumu na umati pamoja na Mtume wao na kuwasimamisha na kuwahukumu kwa uadilifu katika mahakama ya siku hiyo ya malipo.

Funzo mojawapo tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa: hakuna uma au kaumu yoyote ambayo Mwenyezi Mungu ameiwacha vivi hivi bila ya kuhakikisha imefikiwa na ujumbe wa mafundisho ya Mitume wake.

AYA ZA 48 NA NA 49

Tunaihitimisha darsa yetu kwa aya za 48 na na 49 ambazo zinasema:

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾

48. Na wanasema: Ni lini ahadi hii ikiwa mnasema kweli?

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ إِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَلَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao waliowekewa. Ukifika muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii.

Makafiri ambao waliamua kukanusha hakika ya kuwepo kwa siku ya kiyama waliamua kuzusha visingizio vya kila aina alimradi kuutia shaka uhakika huo.

Hivyo wakaibuka na suali kwamba ikiwa ni kweli kiyama kitatokea na wewe Muhammad unayoyasema ni kweli kuhusu hilo, tuambie basi kujiri kwake kutakuwa lini hasa! Walizusha hoja hiyo ilhali uhakika wa kutokea jambo haushurutishi kujua wakati halisi wa kutokea kwake. Mfano wa hili ni sawa na mauti.

Kila mmoja wetu ana hakika kuwa iko siku ataiaga dunia tu, lakini hakuna yeyote kati yetu ajuaye ni lini hasa atafikwa na mauti. Kwa upande wa Bwana Mtume, naye pia kupitia wahyi alioushushiwa na Mola wake aliwapa khabari watu wa umati wake kwamba baada ya kumalizika dunia itawadia siku ya Kiyama, hata hivyo Allah s.w.t hakumbainishia Mtume wake ni wakati gani hasa litajiri tukio hilo kubwa kabisa la kutikisa nyoyo.

Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume walikuwa ni waja wateule wanaozungumza na watu kwa uwazi na ukweli mtupu; na hivyo wakiwaeleza bayana kuwa binafsi hawana nguvu na uwezo usio wa kawaida wala mamlaka ya kujiamulia kupata manufaa fulani au kujilinda na kujiepusha na shari yoyote ile ila kwa uwezo na idhini ya Allah s.w.t

Wapenzi wasomaji, kwa haya machache tunaifunga darsa hii ya 315. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoyakinisha kiimani juu ya kuwepo kwa siku ya kiyama kutokana na amali zao na matendo yao.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

4

5

6

7

8

9

10

11