WAULIZE WANAOFAHAMU

WAULIZE WANAOFAHAMU0%

WAULIZE WANAOFAHAMU Mwandishi:
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi: Misingi mikuu ya Dini

WAULIZE WANAOFAHAMU

Mwandishi: Muhammad Tijani As-samawi At-Tunisi
: SHEIKH MUSABBAH SHA'ABANI
Kundi:

Matembeleo: 49378
Pakua: 4114

Maelezo zaidi:

WAULIZE WANAOFAHAMU
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 26 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 49378 / Pakua: 4114
Kiwango Kiwango Kiwango
WAULIZE WANAOFAHAMU

WAULIZE WANAOFAHAMU

Mwandishi:
Swahili

WAULIZE WANAOFAHAMU

KIMEANDIKWA NA: MUHAMMAD TIJANI AS-SAMAWI AT-TUNISI

KIMETARJUMIWA NA: MUSABAH SHABAN MAPINDA

UTANGULIZI:

ALLAMAH SAYYID SAEED AKHTAR RIZVI

Kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Kitabu kilichopo mikononi mwako ni tafsiri ya kitabu cha Kiarabu kiitwacho Fas'alu Ahladh-Dhikr kilichoandikwa na Shaikh Muhammad Tijani Samawi wa Tunisia. Ndani ya Kitabu hiki ameelezea mkusanyiko wa itikadi za Kiislamu kwa namna zilivyo ndani ya Qur'an na Sunna Tukufu ya Mtume(s.a.w.w) . Kitabu hiki ni kama vile vya mwanzo, nacho kimepata umaarufu hasa kutokana na jinsi mwandishi alivyozichambua itikadi hizo kwa mujibu wa mtazamo wa Sunni na Shia, kisha akayabainisha maeneo wanayohitilafiana. Kwa mara nyingine tena mimi binafsi sikusita kumuomba Shaikh Musabah Shaban Mapinda kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya Kiswahili kutoka kwenye asili yake ya lugha ya Kiarabu. Sababu iliyoifanya Tasisi zetu isimamie kazi hii ni kama zile za mwanzo, ambayo inatokana na maombi ya Maulamaa wengi katika Afrika Mashariki kututaka tukifasiri kitabu hiki kiingie kwenye lugha ya Kiswahili. Namshukuru Shaikh Musabah kwa kuifanya kazi hii kwa moyo mmoja. Nimeiangalia pamoja naye tafsiri hii kwa makini kuhakikisha kuwa maudhui yake ya asili hayakupotoshwa katika lugha ya Kiswahili. Shaikh Tijani Samawi ameandika vitabu vifuatavyo, Thummah-Tadaytu, Li Akuna Ma'as-Sadiqin na Fa'salu Ahladh-Dhikr, na Sheikh Musabah Shaban Mapinda amezitafsiri vitabu zote tatu za mwandishi huyu chini ya Tasisi ya Ahlul-Bayt(a.s) Assembly of Tanzania (ABATA) kwa lugha ya kiswahili viitwavyo Hatimaye Nimeongoka, Hi Niwe Pamoja Na Wakweli na Waulizeni Wanaofahamu, vilivyo pangwa katika kompyuta na Ahlul-Bayt(a.s) Assembly of Tanzania na kuchpishwa na Bilal Muslim Mission of Tanzania.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu tena kwani vitabu zetu "Hatimaye Nimeongoka na Hi Niwe Pamoja Na Wakweli "kimependwa mno na wasomaji na hivyo kutupa ari ya kuchapisha hiki ulichonacho mkononi. Ushahidi wa kupendwa kwa kitabu hicho ni shukurani na pongezi tunazozipokea toka kwa wasomaji kwa namna mbalimbali ikiwemo kutuandikia barua n.k. BILAL na ABATA zinatoa shukurani kwa mfasiri na wale wote waliosaidia kwa njia moja au nyingine katika uchapishaji wa kitabu hiki. Wa Ma Tawfeeqi IlIa Billah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi Dar-es-salaam 29th Zilqaadah, 1422 13th Feb, 2001.

DIBAJI

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU, MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu, na Sala njema na salamu zimshukie Bwana wetu Muhammad aliyetumwa awe ni Rehema kwa walimwengu, ni Bwana wa waliotangulia hapo mwanzo na waliokuja baadaye. Naye ametakasika kutokana na kila kinachochukiza, na (Sala na Salamu) ziwashukie (watu wa) kizazi chake waliowema tena watakatifu, (ambao) ndiyo bendera ya uongofu na taa iondowayo kiza (tena wao) ndiyo viongozi wa Waislamu.

Ama Ba'd, Haya ni masuali niliyoyaandaa hasa kwa Waislamu wanaofanya utafiti, wakiwemo Waislamu wa Madhehebu ya Sunni ambao wanadhani kwamba wao peke yao ndiyo wanaoshikamana na Sunna sahihi ya Mtume, Sala njema na Salamu zimshukie (yeye Mtume) na watu wa kizazi chake waliotakasika, (na zaidi ya hapo) wao Sunni wanashikilia (msimamo) wa kuwapinga wasiokuwa wao miongoni mwa Waislamu wengine na huwataja kwa majina mabaya. Na kwa hakika kumetumwa vikundi vipya katika sehemu mbali mbali za nchi za Kiislamu kwa jina la kutetea Sunna ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) na kwa Jina la kunusuru sunna na kuwatetea Masahaba, na kumeandikwa vitabu vingi kuwashutumu na kuwakufurisha Mashia na Maimamu wao na kuwakejeli wanavyuoni wao, navyo vyombo vya habari vya Ulimwengu vimeeneza fikra hii kwenye nchi zote za Ulimwengu wa Kiislamu na zile zisizokuwa za Kiislamu (kiasi kwamba) leo mazungumzo ya watu yamekuwa ni juu ya "Usunni na Ushi'a." Mara nyingi nimekuwa nikikutana katika minasaba mbali mbali na baadhi ya vijana wenye taaluma miongoni mwa Waislamu wa kweli ambao wanajiuliza na kuuliza kuhusu uhakika wa Shi'a na upotovu wao, hali ya kuwa ni wenye kuchanganyikiwa kati ya mambo wayaonayo na kuishi nayo pamoja na rafiki zao miongoni mwa Mashi'a, na yale wanayoyasikia na kuyasoma kuhusu Mashi'a na wanashindwa kufahamu haki inapatikana wapi. Nilipata kuzungumza na baadhi yao na nikawazawadia kitabu changu (kiitwacho) "Thummah-Tadaitu", Nanamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba wengi miongoni mwao na (hasa) baada ya majadiliano na utafiti, wanaongoka kwa kuufahamu ukweli na wanaufuata. Lakini hali hii inabakia kwa kikundi kidogo miongoni mwa vijana ambao inatokezea kukutana nao, ama waliobakia huenda wasipate nafasi kama hii ya kukutana nao, basi watabakia ni wenye fikra iliyochanganyikiwa baina ya maoni yanayopingana.

Japokuwa kuna dalili zinazokinaisha na hoja madhubuti ndani ya kitabu (kiitwacho) Thummah-Tadaitu na kitabu (kiitwacho) Ma'as-Sadiqina, lakini vitabu hivyo havitoshelezi kukabili mashambulizi na madai mengi (ya uongo) ambayo yanadhaminiwa kipesa na baadhi ya nchi ovu kutokana na mafuta (waliyonayo) na dollar (walizonazo) kwa kupitia njia mbali mbali za upashaji habari. Pamoja na yote hayo, sauti ya haki itaendelea kuvuma katikati ya makelele yanayoudhi, na nuru itabakia inang'ara katikati ya kiza nene, kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli na hapana budi itimie. Mwenyezi Mungu anasema:

يُرِيدُونَ لِيُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَاللَّـهُ مُتِمُّ نُورِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٨﴾

"Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, naye Mwenyezi Mungu ataikamilisha nuru yake japokuwa makafiri watachukia." (Qur'an 61:8).

Na amesema Mwenyezi Mungu akibainisha kwamba matendo yao haya yatashindwa na kuwageukia wao wenyewe.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ ﴿٣٦﴾

"Bila shaka wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuwiya (watu wasiamini) njia ya Mwenyezi Mungu, basi watazitoa (mali hizo) kisha zitakuwa majuto juu yao, hatimaye watashindwa, na wale waliodumu katika ukafiri watakusanywa katika Jahanamu". (Qur'an, 8:36).

Kwa ajili hiyo basi, imekuwa ni wajibu kwa Wanachuoni waandishi na wanafikra kuwabainishia watu mambo yanayowatatiza na kuwaongoza kwenye njia ya sawa. Mwenyezi Mungu amesema:

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ ﴿١٥٩﴾ إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَبَيَّنُوا فَأُولَـٰئِكَ أَتُوبُ عَلَيْهِمْ وَأَنَا التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٠﴾

"Bila shaka wale wanaoficha tuliyoyateremsha miongoni mwa hoja zilizowazi na uongofu, baada ya sisi kuubanisha kwa watu ndani ya kitabu, hao anawalaani Mwenyezi Mungu na kinawalaani kila chenye kulaani. Isipokuwa wale waliotubu na wakarekebisha (mienendo yao) na kubainisha (waliyokuwa wakiyaficha) basi hao nitawapokea na mimi ni Mwenye kupokea Toba na ni Mwenye huruma." (Qur'an 2:159-160).

Basi ni kwa nini wanachuoni hawasemi na kufanya uchunguzi juu ya maudhui haya kwa bidii na utakaso wa moyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na iwapo Mwenyezi Mungu ameteremsha hoja zilizo wazi na uongofu, na ameikamilisha dini na kuitimiza neema (yake kwetu), na ikiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ameifikisha amana (aliyokabidhiwa) na ameufikisha ujumbe (aliotumwa) na akatoa nasaha (njema) kwa ajili ya umma, basi ni za nini tofauti hizi na uadui, bughudha na kuitana majina mabaya na baadhi yetu kuwakufurisha wengine? Mimi hapa kwa upande wangu ninasimama msimamo ulio wazi ili niwaambie Waislamu kwamba, "Hakuna uokovu wala umoja na wala mafanikio wala pepo isipokuwa kwa kurejea kwenye misingi miwili ya asili (ambayo ni) Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Watu wa kizazi cha Mtume(s.a.w.w) , na (pia tutafanikiwa) kwa kupanda ndani ya meli ya uokovu, nayo ni ile Meli ya watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) . Maneno haya (nisemayo) siyo maneno niliyoyazusha mimi, bali ni maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) yaliyomo ndani ya Qur'an na Sunna tukufu ya Mtume.

Kwa hakika leo hii Waislamu wanakabiliwa na mitazamo miwili kuifikia njia ya umoja unaotakiwa.

Kwanza : Ni kwa Ah-lus-Sunnati Wal-Jama'a kuyakubali Madh-hebu ya watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) ambayo yanafuatwa na Shia Imamiyyah Al-Ithna'Ashariyyah peke yao. Kwa maana hiyo yawe ni Madh-hebu ya tano kwao wao, na watumie mfumo wake wa Kifiq-hi kama wanavyotumia katika Madh-hebu manne ya Kiislamu. Wasiyatie dosari wala kuwatuhumu vibaya kwa chochote (watu) wanaoyakubali Madh-hebu hayo ya (Shia), na wawaachie wasomi na wanafikra uhuru wa kuchagua Madhehebu wanayoyaafiki. Katika kufuata mwenendo huu, ni wajibu kwa Waislamu Masunni na Mashia, kuyakubali Madh-hebu mengine ya Kiislamu ya Kiibadhi na Zaidiyyah.

Bila shaka mwelekeo huu utauepushia umma wetu mizozo mingi na mifarakano, ingawaje hautafikia kiwango cha ufumbuzi utakaoondosha matatizo ya kihistoria ambayo yamekuwepo tangu karne nyingi (zilizopita).Pili : Ni kwa Waislamu wote kushikamana kwenye itikadi moja iliyowekwa na kitabu cha Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) na hilo litawezekana kwa njia moja, njia iliyonyooka nayo ni kuwafuata Maimamu wa Nyumba ya Mtume(s.a.w.w) ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na akawatakasa mno, na ni kwa sababu hii Waislamu wote Masunni na Mashia wameafikiana juu ya kuwa Maimamu wa nyumba ya Mtume ni wajuzi mno (wa dini), ni wenye kutangulia kwa kila kitu ikiwa ni pamoja na ucha Mungu, utakatifu, kutosheka, tabia njema, elimu na matendo (mema). Kwa upande mwingine, Waislamu wametofautiana kuhusu Masahaba wa (Mtume).

Basi hebu Waislamu na wayaache yale waliyotofautiana ndani yake na wafuate kile walichoafikiana juu yake kwa mujibu wa kauli ya Mtume (isemayo), "Acha kinachokutia mashaka, ufanye kisichokutia mashaka ". Basi Umma wa (Kiislamu), na ushikamane kwenye jambo hilo na uwe kitu kimoja kwenye kanuni ya msingi ambayo ndiyo nguzo ya kila kitu alichokiasisi Mtume pale aliposema; "Nimeacha kati yenu vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo kamwe hamtapotea, kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu watu wa nyumba yangu " Sahih Muslim.

Kwa kuwa hadithi hii ni Sahihi kwa pande zote mbili (Sunni na Shia) bali kwa Waislamu wote pamoja na tofauti za Madhehebu zao, basi ni kwa nini sehemu fulani ya Waislamu hawaitekelezi? Na lau Waislamu wote wangeitekeleza hadithi hii basi ingeleta umoja miongoni mwao, tena umoja wa Kiislamu wenye nguvu ambao usingetikiswa na upepo wala kubomolewa na kimbunga na wala usingechafuliwa na vyombo vya habari wala maadui wa Uislamu wasingefanya umoja huo ushindwe. Kwa mujibu wa itikadi yangu huo ndiyo ufumbuzi pekee utakaowaokoa Waislamu na kuwakwamua, na ufumbuzi mwingine kinyume cha huu ni upotovu na ni kauli za uongo. Na kwa yeyote atakayeifuatilia Qur'an na Sunna ya Mtume na akaifuatilia historia ya (Uislamu) kisha akayazingatia (hayo) kwa akili yake, bila shaka atakubaliana nami juu ya (maoni yangu) haya. Ama mtazamo wa kwanza ukishindikana na ulishindikana kufaulu tangu siku aliyofariki Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) Masahaba walipohitilafiana na jambo hili ndilo lililosababisha Umma (wa Kiislamu) ugawanyike na kutawanyika.

Kwa kuwa katika karne nyingi zilizopita umma (wa Kiislamu) umeshindwa kurejea kwenye muelekeo wa pili ambao ni kushikamana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi cha Mtume(s.a.w.w) tangu zamani katika zama za Bani Ummaya na Bani Abbas na sasa hivi katika zama zetu (umma pia umeshindwa kufanya hivyo) kutokana na vyombo vya habari kupotosha ukweli na kuwahukumu upotovu na ukafiri wafuasi wa Watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) , basi hakuna njia iliyobakia mbele yetu isipokuwa kukabiliana wazi wazi na kuidhihirisha haki kwa kila aipendaye. Hali ya kuwa tukiulenga mfumo wa Qur'an Tukufu kwani inatoa sababu za kuthibitisha kwa kusema: " Waambie leteni hoja zenu ikiwa ninyi ni wa kweli " (Qur'an, 2:111).

Hoja na dalili hazifanywi kwa nguvu wala kwa kutumia mali, wala hazivunjwi kwa vivutio na vitisho kwa watu waliohuru ambao nafsi zao wamemkabidhi Mwenyezi Mungu peke yake, hawakuridhia na hawataridhia cho chote badala ya haki japokuwa kufanya hivyo kutawalazimu kupoteza nafsi. Basi laiti Wanachuoni wa umma (wa Kiislamu) leo hii wangekutana wakafanya mkutano ili wayatafiti mas-ala haya kwa mioyo mikunjufu na akili zenye mazingatio na nia njema, na hayo wakayafanya kwa ajili ya kuhudumia umma wa Kiislamu, na wakatenda haya ili kuondosha mifarakano na kutibu majeraha ya umma wa Kiislamu na kuimarisha umoja wake, basi hapana shaka umoja huu utakuja bila kizuwizi cho chote, wapende au wasipende kwani Mwenyezi Mungu amemuweka kwa ajili ya jambo hili Imamu kutoka katika kizazi cha Mtume(s.a.w.w) ambaye ataijaza (dunia) haki na uadilifu kama ambavyo (leo hii) imejazwa dhulma na ujeuri.

Imam huyu ni kutoka katika kizazi kitukufu, na imekuwa kama kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu ameupa mtihani umma huu kwa muda wote wa kuwepo kwake, mpaka pale muda wake utapokaribia ataudhihirishia umma kosa la uchaguzi wake, na ataupa fursa ya kurejea kwenye haki na kufuata njia ya asili ambayo Mtume Muhammad(s.a.w.w) aliilingania na alikuwa akisema: "Ewe Mwenyezi Mungu! waongowe watu wangu kwani wao hawafahamu ". Na mpaka utakapofika wakati huo mimi "ninatoa kitabu changu hiki "Fas-Alu Ahl-Ladhikri " ambacho kimekusanya maswali na majibu kwa mujibu wa msimamo na mafundisho ya Maimamu wa Nyumba ya Mtume(s.a.w.w) Huenda Waislamu wakafaidika kwayo katika kila nchi ya Kiislamu na kisha wafanye (juhudi) ya kuunganisha maoni kwa ajili ya kuandaa umoja unaotafutwa.

Hayatakuwa mafanikio yangu isipokuwa (nimetegemea) kwa Mwenyezi Mungu, kwake yeye ndiko ninakotegemea na kwake ndiko nitakakorejea. Ewe Mola wangu nikunjulie kifua changu na uniwepesishie jambo langu na ufungue fundo ulimini kwangu wapate kufahamu maneno yangu. Namuomba Mwenyezi Mungu mtukufu anikubalie kazi yangu hii, na ajaalie kheri na baraka ndani yake, kwani kazi hii ni kama tofali moja tu kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano na umoja. Nasema hivi kwa sababu leo hii Waislamu bado wako mbali mno na haki ndogo ya binadamu na kutendeana mema miongoni mwao. Nimeyashuhudia hayo mwenyewe wakati wa safari zangu nyingi za kutembelea nchi za Kiislamu au nchi ambazo wapo Waislamu, na safari ya mwisho ni ya hivi karibuni katika Bara Hindi ambalo wakazi wake ni zaidi ya Waislamu milioni mia mbili, robo yao ni Mashia na robo tatu yao ni Masunni. Kwa hakika nimeyasikia mengi kutoka kwao, lakini niliyoyashuhudia yanashangaza na yanatisha. Na kwa kweli nilisikitika na nikalia juu ya hatima ya umma huu (sijuwi itakuwaje). Ilikuwa karibu moyo wangu ukate tamaa lau siyo matumaini na imani (yangu).

Haraka baada ya kurudi kwangu kutoka India, nilituma barua ya wazi kwa Mwanachuoni wa India ambaye ndiye marejeo yaAh-Lis-Sunnah Wal-Jama'a , katika nchi hiyo:Sayyid Abul-Hasan An-Nadawi , na nilimuahidi kuichapisha pamoja na jawabu lake lakini sikupata jawabu mpaka sasa. Nami naichapisha (barua hiyo) katika utangulizi wa kitabu hiki ili iwe ni uthibitisho wa kihistoria utakaotushuhudia mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya watu kwamba sisi ni miongoni mwa wanaolingania umoja. Doctor Muhammad At-Tijani As-Samawi

KWA JINA LA MWENYE ENZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

KISHA SALA NA SALAMU ZIMSHUKIE MBORA WA MITUME NA AALI ZAKE WATUKUFU

BARUA YA WAZI KWA MWANACHUONI WA INDIA, SAYYID ABUL-HASAN AN-NADAWI

Amani ya Mwenyezi Mungu ikushukieni na Rehema na Baraka zake zikushukieni. Amma Ba'ad: Mimi Muhammad At-Tijani As-Samawi, Mtunisia, ambaye Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa uongofu na mafanikio, nayakubali Madh-hebu ya watu wa nyumba ya Mtume baada ya uchunguzi (uliochukua muda) mrefu na kabla ya hapo nilikwa (mfuasi wa Madh-hebu ya) Malik. Si hivyo tu, bali nilikuwa miongoni mwa wafuasi wa Tariqa mashuhuri ya Kisufi huko Afrika ya Kaskazini iitwayo "AT-TIJAN1YYAH". Hatimaye nikaufahamu ukweli wakati wa safari yangu iliyofana kwenda kwa Wanachuoni wa Kishia, na niliandika kuhusiana na safari hiyo kitabu nilichokiita, "THUMMAH-TADAITU", kilikamilika kuchapishwa huko kwenu India kwa lugha nyingi kutokana na ukarimu wa Majimau Al-ilmiyyi Al islamiyyi, na kwa ajili ya munasaba (huu) niliitwa kuitembelea India. Ewe Bwana wangu mpendwa, nilifika India kwa matembezi mafupi, na matarajio yangu yalikuwa ni kukutana nanyi kutokana na sifa zenu ninazozisikia na kutokana na kufahamu kwangu kwamba ninyi ndio mategemeo kwa AH-LIS-SUNNAT WAL-JAMA'A. Lakini nilishindwa kufanya hivyo kutokana na umbali na kukosa muda, na nikatosheka kwa kuzuru Bombay, Puna, Jabal Pur na miji mingine iliyoko Gujarat. Nilihuzunika sana kutokana na mambo niliyoyaona huko India (hasa) kutokana na uadui na bughudha iliyoko baina ya Ahli-Sunnah Wal-Jama'a, na ndugu zao Waislamu wa Kishia. Kwa hakika nilikuwa nikisikia kwamba wao hupigana na hupata wakati mwingine wakauana na kumwaga damu za watu wasio na kosa lolote kutoka pande mbili hizi eti kwa niaba ya (kutetea) Uislamu. Mimi nilikuwa siamini (haya) huku nikiitakidi kuwa habari hizo zimepewa mno sura isiyo yake, lakini niliyoyaona na kuyasikia wakati wa ziyara yangu kwa kweli yanashangaza na nimeyakinisha kwamba huko kuna makusudio mabaya na ushauri wa hatari unaoundwa dhidi ya Uislamu na Waislamu ili kuwamaliza wote Masunni na Mashia. Miongoni mwa mambo yaliyozidisha uwazi wa yakini yangu na kuimarisha ufahamu wangu (juu ya hayo) ni ule mkabala uliopita baina yangu na kundi la wanachuoni wa Kisunni wakiongozwa na Sheikh Azizur -Rahman Mufti wa Al-Jamaatul-Islamiyyah, na mkutano wetu ulikuwa ndani ya Msikiti wao huko Bombay na wao ndiyo walioniita.

Baada tu ya kufika, dharau, tuhuma na matusi na kuwalaani Mashia (Wafuasi) wa kizazi cha nyumba ya Mtume vilianza, na walikuwa wamekusudia kunitisha na kuniudhi kwa kuwa walikuwa wanajua kwamba mimi nimeandika kitabu kinachotoa wito wa kushikamana na Madh-hebu ya Ahlul-Bait(a.s) . Lakini mimi nilifahamu makusudio yao na nikaimiliki nafsi yangu na nilitabasamu hali ya kuwa nikisema: "Mimi ni mgeni kwenu ninyi, nanyi ndiyo mlioniita na nimekuja kwa haraka kuitika wito, basi je mumeniita ili mnitukane na kunishutumu, na Je, hii ndiyo tabia ambayo Uislamu umekufundisheni. Basi walinijibu kwa kujiamini kabisa kwamba, mimi hata siku moja sijapata kuwa Muislamu kwa sababu mimi ni Shia na Mashia hawana Uislamu wowote, na waliapa kuthibitisha jambo hilo. Mimi nilisema, "Mcheni Mwenyezi Mungu enyi ndugu zangu, Mola wetu ni mmoja na Mtume wetu ni mmoja na Kitabu chetu ni kimoja na Qibla chetu ni kimoja, na Mashia wanampwekesha Mwenyezi Mungu na wanautumikia Uislamu kwa kumfuata Mtume na Watu wa nyumba yake, wanasali Sala (Tano) wanatoa zaka na wanahiji kwenye nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu, basi vipi inajuzu kwenu ninyi kuwakufurisha wao? Walinijibu, "Ninyi Hamuamini Qur'ani, ninyi ni WANAFIKI mnatumia TAQIYYAH, na Imam wenu amesema: "Taqiyyah ni Dini yangu na ni Dini ya wazazi wangu" Nanyi ni kikundi cha Kiyahudi alichokianzisha Abdallah ibn Saba'a Myahudi."

Niliwaambia hali ya kuwa nikitabasamu, "Hebu tuwaache Mashia na zungumzeni nami binafsi, kwani mimi nilikuwa (wa Madhehebu ya) Malik kama ninyi, na baada ya uchunguzi wa muda mrefu niliyakinisha kwamba Watu wa nyumba ya Mtume ndiyo wenye haki na ndiyo bora kuwafuata. Basi Je, mnayo hoja ya kunijadili au kuniuliza ni ipi dalili yangu na hoja yangu ili pengine tuweze kuelewana miongoni mwetu?" Walisema: "Ahlul-Bait (Watu wa Nyumba ya Mtume) ni wakeze Mtume na wewe huna ukijuacho ndani ya Qur'ani." Nikasema: "Bila shaka Sahih Bukhar na Sahih Muslim zinafundisha kinyume cha mlivyotaja! Wakasema: "Yote yaliyomo ndani ya Bukhari na Muslim na vitabu vingine vya Kisunni miongoni mwa hoja mnazozitoa ni katika uzushi wa Mashia waliouweka vitabuni kwetu."

Niliwajibu hali ya kuwa nacheka; "Ikiwa Mashia wamefikia kiasi cha kuingiza uzushi ndani ya vitabu vyenu, basi vitabu hivyo havina maana tena na pia Madhehebu yenu ambayo yamesimama juu ya vitabu hivyo!!" Walinyamaza wakakosa hoja, lakini mmoja wao alikusudia kuleta fujo na chuki kwa mara nyingine akasema: "Ye yote asiyeamini Ukhalifa wa Makhalifa waongofu (ambao ni) Sayyidina Abu Bakri, Sayyidna Umar na Sayyidna Uthman, Sayyidna Ali, Sayyidina Muawiyyah na Sayyidna Yazid (r.a) basi huyo siyo Muislamu. Nilishangaa kwa maneno haya ambayo sijasikia mfano wake maishani mwangu nayo ni kumkufurisha asiyeamini Ukhalifa wa Muawiyyah na Yazid, na nilisema kimoyo moyo: "Ni jambo linaloingia akilini Waislamu kumuombea radhi Abubakar, Omar na Uthman jambo hili limezoeleka, ama kumuombea radhi Yazid kabisa sijasikia (popote) isipokuwa India na niliwageukia nikawauliza: "Je mnakubaliana na huyu juu ya maoni yake? Wote kwa pamoja wakajibu "Ndiyo". Hapo ndipo nilipofahamu ya kuwa hakuna faida ya kuendeleza mazungumzo, na nikafahamu pia kwamba hakuna kingine isipokuwa wanataka kuniudhi (nikasirike) ili wapate kunishambuha na pengine waniuwe kwa madai ya kuwatukana Masahaba, nani ajuaye (nia zao)? Niliona machoni mwao (ishara ya) shari, nikamuomba rafiki yangu aliyenileta kwao anitoe haraka, akanitoa huku akisikitika na kunitaka radhi kwa yaliyotokea. Mtu huyu hakuwa na kosa alikuwa akifuatilia mkutano huo kwa kutaka kufahamu ukweli, ni kijana mwenye heshima (akiitwa) Sharafud-Din ambaye anamiliki Maktaba na Kiwanda cha uchapishaji cha Kiislamu mjini Bombay. Basi yeye ni shahidi wa yote yaliyopita baina yetu katika majadiliano yaliyotajwa, na hakuficha kutoridhika kwake na watu hawa ambao yeye alikuwa akiamini kwamba wao ni miongoni mwa Wanachuoni wakubwa.

Niliwaacha hali ya kuwa nimechukia na kusikitika juu ya hali ambayo imewafikia Waislamu na hasa wale wanaosimamia vituo vya uongozi na kujiita kuwa ni Wanachuoni, na nilisema moyoni kuwa, ikiwa hali ya Wanachuoni iko kwenye kiwango hiki cha ung'ang'anizi wa kipofu, basi hali itakuwaje kwa watu wa kawaida na wale wasiojua kitu? Hapo ndipo nilipofahamu ni vipi yamekuwa yakizuka mapambano na vita ambavyo ndani yake damu iliyoharamishwa humwagwa na kuvunja heshima na utukufu (wa watu) kwa jina la kuutetea Uislamu, na nililia juu ya hatima ya umma huu uliogawanyika na kuangamia, umma ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu ameubebesha jukumu la uongofu na Mtume wa Mwenyezi Mungu vile vile ameubebesha jukumu la kuifikisha nuru kwenye nyoyo zenye kiza zinazohitaji kupata nuru inayong'ara na kwa wakati huo huo katika India peke yake kuna watu wapatao milioni mia saba wanaabudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanamtukuza Ng'ombe na Masanamu. Badala ya juhudi za Waislamu kuunganika ili wawaongowe na kuwaongoza na kuwatoa kwenye kiza watu hao na kuwapeleka kwenye nuru ili wasilimu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mola wa Walimwengu, tunawaona Waislamu leo hii hasa India wao ndiyo wenye haja ya uongofu na kujisahihisha.

Kwa sababu hii wewe Bwana wangu (Sayyid Abul-Hasan An-Nadawi) ninaleta kwenu barua yangu nikikulinganieni kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma Mwenye kurehemu na kwa jina la Mtume wake Mtukufu na kwa jina la Uislamu Mtukufu na kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu (Aliposema) "Shikamaneni katika Dini ya Mwenyezi Mungu na wala msifarakane. " (Qur'an 3:103)

Nakulinganieni msimame msimamo wa Muislamu shujaa ambaye haogopi kutekeleza la Mwenyezi Mungu na (haogopi) lawama ya mwenye kulaumu na wala ubinafsi haumchukui wala vikundi (havimchukui) kumpeleka namna apendavyo shetani na wafuasi wake. Nakulinganieni msimame msimamo safi ulio wazi, kwani ninyi ni miongoni mwa wale ambao Mwenyezi Mungu amewabebesha jukumu (la uongozi) muda wote mtakaokuwa mkizungumza kwa niyaba ya Uislamu katika nchi hiyo. Mwenyezi Mungu hatakuridhieni iwapo mtasimama msimamo wa mtazamaji mwenye kuridhika na yale yanayotokea huku na huko miongoni mwa misiba inayosababisha kupoteza (maisha ya watu) wasio na makosa miongoni mwa Waislamu wa Kisunni na Kishia. Mwenyezi Mungu atakuulizeni siku ya Qiyama kwa kila dogo na kubwa, na atakuhesabuni kutokana na kila linalopita na linalokuja kwa kuwa Hawawi sawa wale wanaojua na wale wasiojua, kwani kwa kiwango cha bidii mtu afanyacho ndivyo yatavyokuwa mafanikio, na kwa kadiri ya kiwango cha utukufu ndivyo yajavyo mambo matukufu. Na maadam ninyi ndiyo mnaowaongoza wanachuoni wa India, basi jukumu lenu ni kubwa na bila shaka neno litokalo kwenu huenda ndani yake kukawa na mafanikio kwa umma (wa Kiislamu) nchini India kama ambavyo huenda kukawa na maangamivu ya mali na watu (likitumika vibaya), basi mcheni Mwenyezi Mungu enyi watu wenye akili! Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewapa Wanachuoni daraja ya kwanza baada ya Malaika akasema:

شَهِدَ اللَّـهُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَالْمَلَائِكَةُ وَأُولُو الْعِلْمِ قَائِمًا بِالْقِسْطِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿١٨﴾

"Mwenyezi Mungu ameshuhudia ya kwamba, hapana aabudiwaye kwa haki ila yeye tu na Malaika na wenye elimu (wameshuhudia hivyo), (Yeye) ni Mwenye kusimamia uadilifu." (Qur'an, 3:18).

Na ikiwa Mwenyezi Mungu anatuamuru sote kwa kusema: "Na pimeni kipimo kwa haki na wala msipunguze kipimo ". (Qur'an, 55:9).

Iwapo wafasiri wanaona umuhimu wa kufanya uadilifu katika vipimo vya kimaadda ambavyo vina viwango maalum, basi mwaonaje hali ya kufanya uadilifu katika mambo ya kiitikadi, ambayo yanamvutano baina ya haki na batili na kwa mambo hayo ya kiitikadi ndipo mahala unapotegemea uongofu wa watu na uokovu wa watu wote? Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema; "Na mtakapohukumu basi hukumuni kwa uadilifu". Na amesema tena; "Ewe Daud bila shaka sisi tumekufanya uwe Khalifa (msimamizi) katika nchi, basi hukumu baina ya watu kwa haki na wala usifuate matamanio yatakupotosha kutoka njia ya Mwenyezi Mungu." Hapana shaka Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Sema kweli japokuwa ni dhidi ya nafsi yako, sema kweli japokuwa ni chungu." Ewe Bwana wangu Mtukufu, nakuiteni kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na sunna ya Mtume wake, semeni kweli wazi wazi kwa sauti kubwa japokuwa ni chungu itakushuhudieni mbele ya Mwenyezi Mungu. Naapa kwa Mola wako hivi kwenu ninyi Mashia siyo Waislamu? Hivi kweli mnaitakidi kwamba wao ni makafiri? Je wafuasi wa Watu wa nyumba ya Mtume ambao wanampwekesha Mwenyezi Mungu na kumtukuza zaidi kuliko vikundi vyote kwa usemi wao wa kuwa hafanani na chochote kwa kumtakasa kutokana na kufanana, na kutokana na kuwa hana umbo na mwili. Si hivyo tu bali wanamuamini Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) na wanamuheshimu mno kuliko vikundi vyote wasemapo kuwa, "Yeye Mtume ni Maasum moja kwa moja hata kabla ya kupewa utume". Je, hawa ndiyo munaowahukumu kuwa ni makafiri? Je, wale wanaomtawalisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini na wanawapenda kizazi cha Mtume na kuwatawalisha kama alivyowatambulisha Ibn Mandhur ndani ya "Lisanul-A'rab" katika mada ya Shia, basi je ninyi mwasema kwamba wao siyo Waislamu? Je, Mashia hawa ambao wanatekeleza wajibu wa Sala kwa namna iliyo bora, na wanatoa Zaka na kuzidisha juu yake Khumsi ya mali zao kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wanafunga (saumu ya) mwezi wa Ramadhani na nyingine na wanahiji nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu na kuyatukuza mambo matukufu ya Mwenyezi Mungu, kadhalika wanawaheshimu Mawalii wa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na maadui wa Uislamu, hivyo kwenu ninyi watu hawa ni washirikina?

Je, hivi watu wasemao kuwa Uimamu hasa ni (haki) wa Maimamu kumi na wawili kutoka katika watu wa nyumba ya Mtume ambao Mwenyezi Mungu amewaondolea uchafu na amewatakasa sana sana, na Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataja kama alivyotoa Bukhari na Muslim na wengineo katika Sahihi za Ahlu-Sunnah, hivi watu hawa kwenu ninyi ni watu waliotoka nje ya Uislamu? Je hivi kuna siku ambayo Waislamu wamekuwa hawautambui Uimamu na wala hawakubali sawa sawa liwe hilo katika uhai wa Mtume au baada ya kufa kwake mpaka kufikie kuihusisha nadharia ya Uimamu kwa Waajemi na Majusi? Na je hivi mnasema kwa kujiamini kuwa, "Ni Kafiri asiyekubali Uimamu wa Yazidi ibn Muawiyyah ambaye uovu wake unaeleweka kwa Waislamu wote? Na itoshe uovu na udhalimu wa Yazidi kwa maelezo walioafikiana Waislamu wote kutokana na yeye kuruhusu kufanyika maasi kwenye mji Mtakatifu wa Madina kwa kutumia jeshi lake na askari wake kufanya wayatakayo mjini humo ili wachukuwe viapo vya utii (kutoka kwa watu) kwa nguvu kama kwamba (watu hao) ni watumwa wake. Si hivyo tu, bali wa Yazid waliwaua maelfu ya Masahaba watukufu na Tabiina, wakavunja heshima za wanawake na wasichana wa Kiislamu waliojihifadhi kiasi walizaliwa kutokana na uchafu huo idadi ya watoto ambao hakuna awezaye kuidhibiti isipokuwa Mwenyezi Mungu.

Na yamtosha Yazidi aibu mbaya mno na udhalim wa kudumu kule kumuuwa Bwana wa vijana wa peponi na kuwateka Mabinti wa Mtume na kuyachokora meno ya Husein(a.s) kwa kijiti kisha kuimba kwake beti za ushauri ambazo ni maarufu akasema, "Laiti wazee wangu (waliouawa) katika Badri wangeshuhudia... " Mpaka akafikia kusema: "Banu Hashim walichezea Ufalme, hakuna habari yeyote iliyokuja wala Ufunuo ulioshuka. " Ni wazi kabisa kwamba hakuamini utume wa Muhammad(s.a.w.w) wala Qur'an Tukufu, basi je, ni kweli mnaafiki kumkufurisha anayejitenga na Yazid? Na baba yake Muawiyyah ambaye alikuwa akimlaani Ali (a.s) na huamuru alaaniwe, bali na (alikuwa) akimuuwa kila anayekataa kufanya hivyo miongoni mwa Masahaba wema kama alivyomfanyia Hujr ibn Adiyy Al-Kindi na jamaa zake, na (tendo la kumlaani Alia.s ) aliliusia likawa ni sunna iliyofuatwa kwa miaka sabini hali ya kuwa (Muawiyyah) anaijua kauli ya Mtume(s.a.w.w) aliposema "Yeyote atakayemtukana Ali, basi kanitukana mimi, na atakayenitukana mimi amemtukana Mwenyezi Mungu". Kama ambavyo zilivyoandika Sahih za Ahli-Sunnah kwa ziyada ya matendo aliyoyatenda miongoni mwa mambo yanayopingana na Uislamu kwa kuwauwa watu wema wasio na kosa ili achukue kwao kiapo cha utii kwa ajili ya mwanawe Yazid. Vilevile kumuua kwake, Hassani ibn Ali(a.s) kwa kumtumia Ju'da binti Ash-ath, na maovu mengine mengi yanatajwa na historia kwa Masunni kama ambavyo pia yanashuhudiwa na wafuasi wa Imam Ali(a.s) .

Mimi, ewe Bwana wangu, sikudhani kwamba ninyi mnaafikiana na hayo, vinginevyo basi na tuyaache kama yalivyo, na ikifika hapo basi hapatabakia baada ya hayo kipimo wala akili, wala sheria na wala hekima pia dalili. Na Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli. " (Qur'an, 9:119).

Namuapa Mwenyezi Mungu, bila shaka mwanachuoni wa Kipakistan Abul-A'ala Al-Maududi, Mwenyezi Mungu amrehemu amesema kweli alipotaja katika kitabu chake kiitwacho, "Ukhalifa na lifetime" katika ukurasa wa 106 akimnukuu Al-Hasan Al-Basri aliposema, "Mambo manne alikuwa nayo Muawiyyah, lau angekuwa na jambo moja miongoni mwa hayo lingetosha kumuangamiza.

1) Kuchukua ukhalifa bila ya mashauriano ya Waislamu na hali wamo miongoni mwao waliobakia Masahaba na wenye nuru ya ubora.

2) Kumpa Ukhalifa baada yake mwanawe mlevi ambaye alikuwa akivaa hariri na kupiga magitaa.

3) Kumfanya Ibn Ziyad kuwa ni mwana wa baba yake na hali Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mtoto ni wa kitanda na mzinifu mwanaume atapata jiwe. "

4) Kumuua kwake Hujr na Jamaa za Hujr, basi ole wake kwa kumuua Hujr na jamaa zake Hujr (akakariri mara tatu).

Basi Mwenyezi Mungu amrehemu Abu A'ala Al-Maududi, aliyepasua ukweli, na lau angetaka angeongeza zaidi ya mambo haya manne yakawa mambo arobaini lakini aliona kwamba hayo yanatosheleza kumuangamiza Muawiyyah. Huenda Maududi alikuwa akichelea hisia za watu ambao wamejifunza kwa watangulizi wao kumtukuza Muawiyya, kumuheshimu na kumuombea radhi, bali hata mwanawe Yazid vile vile (kutukuzwa n.k.) kama nilivyosikia mimi mwenyewe binafsi toka kwa Wanachuoni wenu huko India. Lahaula wala Quwwata Illa Billahil-'Aliyyil-Adhim.

Kutokana na yote hayo mimi pia nilichelea hisia za wale watu walioniita wasije wakanivamia, basi sikuwatajia chochote katika matukio hayo. Kwa hiyo ewe bwana wangu, ninakulinganieni muwe na msimamo ulio wazi mkitafuta radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa msimamo huo, kwani Mwenyezi Mungu haichelei haki, na wala sikutakeni mkiri makosa ya watu hawa wala kuisambaza aibu yao kwa kuwa historia inatutosheleza sisi na ninyi kutuhadharisha juu ya hayo. Lakini kinachotakiwa kutoka kwenu ni kukiri na muwafahamishe wafuasi wenu kwamba, "Watu ambao hawaukubali Uimamu wa watu hawa (Muawiyya Yazid, Abubakr, Omar na Uthman) na wala hawawatawalishi, wao ni Waislamu wanaostahiki heshima na jambo hilo halina shaka, museme ya kwamba Mashia ni wenye kudhulumiwa siku zote kwani wao hawakuufuata na kuukubali Uimamu wa mti uliolaaniwa ambao Mwenyezi Mungu ameupigia mfano ndani ya Qur'ani. Basi ni lipi kosa la Mashia kwa Mola wenu, ikiwa Mtume(s.a.w.w) anawaamuru Waislamu kuwafuata Watu wa nyumba yake baada yake, mpaka akawafanya wao kuwa ni kama Safina ya Nuh, anaokoka mwenye kupanda ndani yake na anaangamia anayeikwepa. Na ni lipi kosa la Mashia ikiwa walitekeleza amri ya Mtume aliposema: "Nimekuachieni vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu, vitu ambavyo mkishikamana navyo kamwe hamtapotea baada yangu. " Kama ambavyo zinashuhudia Sihah za Sunni ukiachilia mbali vitabu vya Kishia. Badala ya kuwashukuru (Mashia) na kuwatanguliza na kuwaboresha juu ya wengine kwa kufuata kwao maamrisho ya Mtume(s.a.w.w) , tunawashutumu na kuwakufurisha na kujitenga nao, jambo hili siyo uadilifu wala haliingii akilini.

Ewe Bwana wangu, hebu tuachane na kauli za kijinga na za uongo ambazo haziwezi kusimamisha dalili wala hoja na hazina uzito kwa wanataaluma miongoni mwa watoto wa umma wetu kwamba, "Eti Mashia wanayo Qur'ani yao, au eti wao wanasema kwamba aliyepewa Utume ni Ali, au kwamba Abdallah ibn Sabaa' Myahudi ndiye muanzilishi wa Ushia."Na mengineyo miongoni mwa kauli dhaifu ambazo Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hayo ni miongoni mwa uzushi wa maadui wa Uislamu na maadui wa Ahlul-Bait na wafuasi wao. Na hayo ni mambo hayakuzushwa isipokuwa ni kutokana na ubinafsi mpotovu na ujinga wenye kero iliyopita kipimo. Ewe Bwana wangu mpendwa mimi nauliza, "Wana daraja iliyoje wanachuoni wa India kuliko ile ya wanachuoni wa Az-Har Tukufu waliotoa Fat-wa inayoruhusu kufanya Ibada kwa mujibu wa Madhehebu ya Shia Imamiyyah tangu miaka thelathini iliyopita? Na miongoni mwa Wanachuoni wa Az-Har kuna aonaye kuwa fiqihi ya Mashia ya Jaa'fari ambayo wanaitumia Mashia ni pana yenye manufaa na iko karibu mno na Roho ya Uislamu kuliko Madhehebu nyinginezo ambazo zinaitegemea. Na anayewaongoza Wanachuoni hawa (kwa fikra hii) ni Mtukufu Marehemu Sheikh Mahmud Shal-Tut Mwenyezi Mungu amrehemu, ambaye aliiongoza Az-har katika uhai wake.

Je hivi wanachuoni kama hawa hawaujui Uislamu na Waislamu? Au wanachuoni wa India ni wajuzi mno kuliko wanachuoni hao? Mimi siwadhanieni kabisa kwamba ninyi mnasema namna hiyo...!! Ewe Bwana wangu Mtukufu, mategemeo yangu kwenu ni thabiti na moyo wangu kwenu uko wazi kwa mapenzi na huruma, na hapo zamani nilikuwa kama ninyi nimefunikwa sioni haki wala Ahlul-Bait(a.s) na wafuasi wao. Mwenyezi Mungu akaniongoza kuelekea kwenye haki ambayo hapana baada yake ila upotovu, na nikawa huru kutokana na minyororo ya ung'ang'anizi na kufuata kama kipofu, na nilifahamu kwamba wengi wa Waislamu bado wamefunikwa na habari zisizo na ukweli na za uzushi. Kampeni zilizoandaliwa kuwapa baadhi ya watu utukufu wasiostahili zinawazuwia (Waislamu) kuufikia ukweli ili wote wapate kupanda meli ya uokovu na washikamane na kamba imara ya Mwenyezi Mungu, na hakuna tofauti kama mjuavyo baina ya Sunni na Shia isipokuwa ni katika yale waliyotofautiana kwa ajili ya Ukhalifa baada ya Mtume, na msingi wa tofauti ni itikadi yao kuhusu Masahaba, nao Masahaba (r.a) walitofautiana kati yao mpaka wakalaaniana, kupigana na kuuana wao kwa wao. Ikiwa kutofautiana kati yao ni kutoka katika Uislamu basi Masahaba ndiyo wa mwanzo kutuhumiwa kwa tuhuma hii na Mwenyezi Mungu apishe mbali. Mimi siitakidi kwamba ninyi mnayaridhia hayo, na uadilifu unakulinganieni msiridhiye Mashia kutolewa nje ya Uislamu, kama ambavyo Mashia wana desturi ya kuwatukuza Ahlul-Bait(a.s) na kuwaheshimu vile vile Masunni wanayo desturi ya kuwatukuza Masahaba wote, na misimamo hii miwili iko mbali mbali.

Basi ikiwa Mashia kwa desturi yao hiyo wanakosea, basi Masunni ndiyo watakaokuwa wanakosea zaidi (katika desturi yao) kwani Masahaba wote wanawatanguliza Ahlul-Bait(a.s) kuliko nafsi zao, na huwatakia rehma kama wamtakiavyo rehma Mtume(s.a.w.w) . Na hatumfahamu yeyote miongoni mwa Masahaba (r.a) aliyeitanguliza nafsi yake au aliyejitukuza juu ya watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) katika elimu au matendo mema. Basi wakati umefika kuliondosha giza la kihistoria kwa wafuasi wa Ahlul-Bait (a.s) , kushirikiana nao, kuunga udugu, kusaidiana kwa mema na kumcha Mwenyezi Mungu na imetosha kwa umma huu kumwaga damu na kusambaza fitna. Huenda Mwenyezi Mungu Mtukufu akaunganisha kupitia kwenu kauli (ya umoja) na kuuondoa utengano, akalitibu jeraha hili na akauzima moto wa fitina na kumdhalilisha shetani na kundi lake na mtakuwa ninyi mbele ya Mwenyezi Mungu ni wenye kufaulu hasa kwa kuwa ninyi mnatokana na kizazi kitukufu kama ninavyosikia.

Basi fanyeni hayo ili mpate kufufuliwa pamoja nao. "Na hakika umma wenu ni mmoja nami ndiye Mola wenu." "Na waambie, fanyeni Mwenyezi Mungu ataona matendo yenu na Mtume wake na waumini". Mwenyezi Mungu akuwafikisheni ninyi na sisi kwa mambo ambayo ndani yake kuna kheri ya nchi na waja, Mwenyezi Mungu akujaalieni ninyi na sisi kuwa miongoni mwa wenye kutenda (mema) wenye utakaso kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Nakutumieni kwa heshima yenu pamoja na barua hii nakala ya kitabu changu "Thummah-Tadaitu" ambacho nilikitunga maalumu kuhusiana na maudhui haya, hiyo ni zawadi yangu kwenu huenda kikapata kukubalika mbele yenu. Was-salaam Alaikum Warahmatullahi Taala wa Barakatuh. Muhammad Tijani As-Samawi At-Tunisi