• Anza
  • Iliyopita
  • 5 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Matembeleo: 3413 / Pakua: 1765
Kiwango Kiwango Kiwango
YAZID HAKUWA AMIRUL MUMININ

YAZID HAKUWA AMIRUL MUMININ

Mwandishi:
Swahili

YAZID HAKUWA AMIIRUL-MUMININ

UTANGULIZI

Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu; na swala na salamu zimshukie Mtume Wake pamoja na aali zake waliotwahirishwa, amin.

Mwanzo mwanzo wa mwezi wa Muharram wa mwaka (1424 BH), palitolewa karatasi katika mji wa Mombasa zenye kichwa cha habari "Barua ya wazi kwa wahubiri na maimamu wa sunna" (uk. 30 humu). Lengo la karatasi hizo lilikuwa ni kuwaonyesha hao wahubiri na maimamu wa kisunni makosa wanayoyafanya ya kuweka "vikao vya mawaidha, khususan katika siku kumi za mwanzo wa mwezi wa Muharram". Kwa maoni ya waandishi wa karatasi hizo, "hakuna hadith (dalili) ambayo inatuambia tufanye hivyo" isipokuwa huo ni "uzushi" ambao, kwa kuufanya, "mwawapoteza wafuasi wa Sunna kwa kuwaiga hao hao Mashia".

Waliozitoa karatasi hizo walijiita "Ahlul-Tawheed" ambao, kama wasomi wote wanavyojua, ni mawahabi. Wao hutumia jina hilo kwa sababu mbili: Sababu ya kwanza ni kuficha uwahabi wao wanaojua kwamba unapingwa na Waislamu wote. Kwa hivyo wanaogopa kukosa kuungwa mkono. Sababu ya pili ni kutokana na ile imani yao kwamba wao peke yao ndio wanaompwekesha Mwenyezi Mungu; Waislamu wengine wote wasiokubaliana nao, kwao wao, ni mushrikina.

Lakini kwa kuwa Waislamu wote wanaamini kwamba wao ni ahlul-tawheed, kwa vile wote wanaikiri Laa ilaaha illallaah, waandishi wa karatasi hizo, kwa kutumia jina hilo, walitaka kuwavungavunga Waislamu wawafikirie kuwa ni wenzao.

Ili kuzijibu tuhuma walizozifanya dhidi ya mashia kuhusu mauaji ya Imam Hussein(a.s) , na ili kuyasahihisha madai waliyoyafanya katika karatasi zao, kuwa Yazid alikuwa Amiirul-mu’minin, nilitoa mfululizo wa karatasi kumi, kuanzia tarehe 8 Muharram, 1424/12 Machi, 2003 hadi 14 Rabiul Awwal, 1424/16 Mei, 2003, nilizozipa kichwa cha habari "Barua ya wazi kwa mawahabi". Karatasi hizo ndizo hizi tulizozikusanya katika kitabu hiki. Na kuwafikiwa ni kwa Mwenyezi Mungu.

Abdilahi Nassir

Mombasa, Kenya

10 Rabiiuth Thaani, 1424

11 Juni, 2003

YAZID HAKUWA AMIRUL MUMININ

MTUME (s.a.w.w) AMESEMA

1.Kwa hakika kifo (shahada) cha Husayn kitaamsha mori, katika nyoyo za waumini, ambao hautapoa milele .

2.Amrisheni mema na kukataza maovu. La sivyo, waovu watatawala na mwito wenu, kuwa yule aliye bora (anapasa kutawala), hautatiwa maanani .

3.Yeyote anayekwenda kwa tajiri na kujifanya mnyonge mbele yake, kwa sababu ya mali aliyonayo, huwa ameshapoteza thuluthi mbili za dini yake.

4.Mfano wa watu wa nyumba yangu ni kama vile safina ya Nuhu. Yeyote aliyeipanda, aliokoka. Na aliyebaki nyuma (asiipande), alighariki .

5.Yeyote anayependa kumfurahisha mtawala wake, japo kwa kitu kidogo kitakachokuwa ni sababu ya kumuudhi Mola wake, huwa ameshaitoka dini ya Mwenyezi Mungu .

IMAM HUSAYN (a.s) AMESEMA

1.Kufa katika utukufu ni bora kuliko kuwa na maisha ya uadilifu.

2.Taifa linalonunua starehe za maisha kwa kubadilishana na hasira za Muumba, halipati kuongoka .

3.Iwapo hamna dini (mnayoiamini), basi kueni (angalau) watu walio huru .

4.Tahadhari na uepukane na ushirika wa mtu dhalimu, maana yeye hukuuza kwa kupata tonge moja (ya chakula) ama kiasi kidogo zaidi ya hicho .

5.Uhusiano, ushirikiano na tangamano na watu wanaotenda dhulma na ukatili, husababisha lawama na kutoaminiwa .

SI UZUSHI WA MASHIA

Katika karatasi zao, mawahabi wamesema: "Waandishi wa kiSabai wa Iraq walizua hadithi za urongo, za kikatili na za kutisha, kama vile kunyimwa maji ya kunywa (Hussein na watu wake) na kulazimishwa kupigana, kukatwa vichwa. Ambazo haziaminiki wala haziwezi kutegemewa na pia ziko mbali na ukweli."

Majibu yetu : Penye vitabu vya Kiswahili, viwezavyo kupatikana madukani humu humu mwetu, hapana haja ya kutaja vitabu vya lugha nyengine ambavyo wengi wa watu hawana au hawawezi kuvipata au hawaijui lugha iliyoandikiwa vitabu hivyo. Kwa hivyo tuangalie kitabu kiitwacho Maisha ya Sayyidna Huseyn (chapa ya 1999) kilichoandikwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy na kuchapishwa na Adam Traders wa Mombasa.

Katika uk. 37 wa kitabu hicho, Sheikh Abdalla ameandika hivi: "Alipowajibu kwa yakini (yaani Imam Husein) kuwa hakubali kwenda kuuawa na Ubeydillah na kudhalilishwa, wala kuuawa watu wake na kudhalilishwa, wanaume na wanawake na watoto, waliwazunguka darmadar wasiwe na njia ya kupenya na kukimbia. Wakakosa maji na chakula tangu hapo mwezi nane Mfunguo Nne 61 mpaka mwezi kumi 61; hapo wakaingia kuwapiga baada ya kuwa hawajifai kwa njaa na kiu". Baada ya hayo, akataja orodha ya watu kumi na moja ambao ndio "wa mwanzo kuuawa"; wote wakiwa ni jamaa zake Mtume(s.a.w.w) ! Na katika uk. 39 wa kitabu hicho hicho, akasema kwamba baada ya kuuliwa hivyo, walipelekwa "kwa shangwe kubwa na ngoma mpaka Al Kufa kwa Liwali. Kila mtu akajitapa mbele ya huyo Liwali 'Mimi nimemuua fulani. Mimi nimemuua fulani' na huku wanapewa tuzwa (tunza)". Wakifika huko, Sheikh Abdalla anasema, ikawa "vichwa vimetawanywa chini".

Jee, vichwa hivyo vilitoka vyenyewe miilini mwao au vilikatwa? Wakasema tena katika hiyo karatasi yao: "Na madai ya Mashia kwamba Hussein alikatwa kichwa chake ni urongo mtupu."

Majibu yetu : ni tumsome tena Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Katika uk. 38 wa hicho kitabu chake, shekhe wetu huyo anaeleza kwamba, baada ya kumzingira "kila upande kwa kumpiga kwa mishare, mikuki na panga mpaka akaanguka chini wakamkata kichwa. Na qawli mashuhuri (ni) kuwa aliyemkata kichwa ni Shimr bin Dhiljawshan " Kisha akaongeza: "Pesa na kutaka ukubwa kunafanya kazi."

Wala madhalimu hao hawakutosheka tu na kukikata kichwa cha Imam Hussein(a.s) . Anavyoeleza Sheikh Abdalla Saleh Farsy (uk. 39) ni kwamba, kilipofika kwa Liwali Ubeydillah, ikawa "anakigonga kichwa cha Al Huseyn kwa kifimbo mkononi kama kwamba anapiga upatu au chapuo." Na kilipofika kwa Mfalme mwenyewe (Yazid bin Muawiya), Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 40), alifanya "kama yale aliyoyafanya Liwali wake wa Al Kufa. Akakamata kifimbo akawa anayagonga meno ya Huseyn " Basi hayo ndiyo aliyoyaandika Sheikh Abdalla Saleh Farsy aliyekuwa Kadhi Mkuu wa Kenya na, kabla ya hapo, Zanzi bar. Jee, yeye alikuwa "mwandishi wa ki-Sabai wa Iraq?" Alikuwa Shia? Ni "mrongo"? Hakuwa shekhe mkubwa waliyekuwa wakijifakhiri naye hao "Ahlul Tawheed", na mpaka leo hujifakhiri naye? Sasa wanasemaje?

JINSI YAZID ALIVYOTAWALISHWA

Kabla ya Yazid kutawala katika mwaka wa 60 BH, Waislamu walitawaliwa na babake aliyekuwa akiitwa Muawiya bin Abii Sufyan. Wote wawili hao -- babake na babu yake -- walisilimu kwa kukosa budi baada ya Makka kutekwa na (kabla ya hapo) baada ya kuongoza upinzani mkali dhidi ya Mtume Muhammad(s.a.w.w) , na kushindwa. Huyo Muawiya ndiye yule aliyesimama kumpinga na kumpiga vita "Khalifa wa Nne" (Imam Alii bin Abii Twaalib(a.s) alipochaguliwa na Waislamu kuwa Khalifa wao; na baada ya Imam Alii(a.s) kuuliwa, akaingia kumpinga na kumpiga vita Imam Hassan(a.s) (ndugu yake Imam Husseina.s ) ambaye, anavyotwambia Sheikh Abdalla S. Farsy, aliuliwa "kwa sumu" na yeye huyo Yazid tunayeambiwa kuwa ati ni "Amirul-muuminin"! (Tizama uk. 24 wa kitabu chengine cha Sheikh Abdalla S. Farsy kiitwacho Maisha ya Sayyidna Hassan (chapa ya 1999) kilichochapishwa na Adam Traders wa Mombasa vile vile). Lakini kwa kiasi cha miaka kumi kabla ya kupawa hiyo sumu, Imam Hassan(a.s) na Muawiya, babake Yazid, baada ya vita vikali, walifanyiana suluhu na kuandikiana mkataba. Kati ya waliyokubaliana katika mkataba huo, anavyotueleza tena Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 16 wa kitabu chake hicho, ni kwamba Imam Hassan(a.s) amwachie Muawiya Ukhalifa. Lakini Muawiya akifa, basi Imam Hassan(a.s) ataukamata yeye. Na lau Imam Hassan(a.s) atakufa, basi ushikwe na Imam Hussein(a.s) .

Kuona hivyo, Sheikh Abdalla S. Farsy anaendelea kutueleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho hicho cha Maisha ya Sayyidna Hassan, "akili ilimjia (Yazid) akaona kuwa huu ufalme wa baba yangu utanipotea kwani akifa baba yangu atatawala Hasan, wala haikuandikwa kuwa akifa nitatawala mimi. Akaona amuue kwa sumu. Akapeleka watu madhubuti kwa siri kwa mke wa mwisho wa Sayyidnal Hasan, wala hakuzaa naye, akiitwa Jaada bint Ash-ath. Wamtumainishe kuwa akimuua huyu mumewe atamuoa Yazid na tangu sasa atampa dirham laki moja,, na mengineyo makubwa kabisa anayoyataka. Bibi akavutika akampa sumu kali kabisa huyo mumewe. Akasononeka muda wa siku arbaini; kisha akakata roho hali ya kuwa shahidi "

Na katika uk. 18 wa Maisha ya Sayyidna Huseyn, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema: "Kabla ya kufa Sayyidna Hasan Muawiya aliona ajifungue na ahadi ya kumtawalisha Al Hasan wala hana ahadi ya kumtawalisha mwengine. Basi aliona amfanye mwanawe anayempenda zaidi - naye ni Yazid - awe waliyyul ahdi (heir-apparent). Itangazwe kwa raia wote kuwa akifa yeye hakuna uchaguzi wowote ila kuwa mwanawe - Yazid - ndiye Khalifa tu. Akiridhia Hasan asidhie na mwengine yeyote yule akiridhia asiridhie." Akamalizia kwa: "Maliwali wake wengine -- kwa ajili ya kutaka kujipendekeza ili waendelee na Uliwali wao -- walimtia nguvu katika fikira hii ijapokuwa siyo ya Uislamu " Baada ya Imam Hassan a.s. kufa kwa ile sumu, Muawiya alipanga mikakati yake ya kumtawalisha mwanawe (Yazid). La kini, hata hivyo, haikuwa rahisi. Anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 18 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Huseyn, ni kwamba "aliona ni uzito kabisa kutaka kulivunja jambo hili, sharti alichukulie mbinu kwa taratibu, akaona awafundishe Maliwali wake watoe fikira hii, isiwe imetokana na yeye. Akawaambia walisemeseme wenyewe tu huko katika nchi wanazoziendesha kama mchezo tu hivi kwanza."

Baada ya hapo, aliwakusanya wote mahali pamoja na, kama alivyowafundisha, ikawa mmoja baada ya mmoja husimama na kupendekeza utawala aachiwe Yazid. Lakini hata hivyo, si wote walimkubalia Muawiya; wengine walipinga: mmoja wao akiwa Al Ahnaf bin Qays. Huyu, Sheikh Abdalla S. Farsy anatwambia (uk. 20 wa hicho kitabu chake), alisema hivi: "La! Sisi watu wa Iraq sote si radhi kwa haya, na watu wa Hijaz wote pia hawawafiki. Hatumridhii kattu Yazid kuwa Khalifa wa Waislamu. Na wewe unamjua zaidi mwanao, kuliko watu wengine, kuwa hafai. Usijitwike mzigo wa kukutia Motoni kwa khiyari yako. Sisi haturidhii ila kizazi cha Ali."

Mambo yakakorogeka. Sheikh A. S. Farsy anasema (uk. 20): "Akainuka Abu Khunayf akatoa upanga wake akamwonyesha Muawiya akamwambiya 'Asiyekubali mlishe huu atashika adabu yake'. Akainuka Muawiya akasema, 'Huyu ndiye khatibu barabara. Khatibu vite ndo si maneno tu. Na huyu ndiye bora wa wote waliohudhuria hapa na wengineo'. Baraza ikavunjika." Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume(s.a.w.w) , aliposikia habari hiyo, Sheikh A. S. Farsy anaendelea (uk. 21), "alikasirika sana sana kuona vile Muawiya anazivunj a zile ahadi alizompa Sayyidnal Hasan " Mambo yakamalizikia hapo, yasende mbele zaidi. Lakini baada ya muda (mwaka wa 50 BH), Muawiya alikwenda Madina, asemavyo Sheikh A. S. Farsy (uk. 21), "kugonga gogo asikie vipi mlio wake". Huko alikutana na "watoto wa kisahaba wenye jina kubwa kabisa"; nao ni mabwana "Abdulla bin Abbas bin Abdul Muttalib (hakuweta ndugu zake), Abdulla bin Jaafar bin Abii Talib bin Abdil Muttalib (hakuweta ndugu zake), na Abdulla bin Zubeir bin Awam (hakuweta ndugu zake) wala hakumwita Sayyidnal Huseyn." Akasema nao kwa ulatifu ili wamkubali Yazid, lakini wote wakapinga; na baada ya siku mbili tatu, akenda zake mtungi mtupu!

"Alipokufa Sayyidnal Hasan", Sheikh A. S. Farsy anazidi kutueleza (uk. 22), " Muawiya aliwaamrisha watu wa Sham wote wamkubali Yazid kuwa ndiye Khalifa baada yake. Wakakubali wote kwa umoja wao." Akamwamrisha Liwali wa Madina awalazimishe watu wake nao wamkubali Yazid. Yeye, anavyosema Sheikh A. S. Farsy (uk. 23), "yakamuudhi haya akaona kwa nini tumkubali kijana asiyekuwa na mwendo mzuri atutawale sisi watu wazima na Masahaba". Kwa hivyo akamjulisha Muawiya msimamo wake, na Muawiya papo hapo "akamwandikia barua ya kumtoa katika Uliwali". Alipopata barua hiyo, Liwali huyo (Marwan bin Hakam) alihamaki "sana sana na akachukua wakubwa wa jamaa zake wa kukeni -- Bani Kinana -- mpaka Sham kwa Muawiya kumtishia kuwa atafanya thora (mapinduzi). Muawiya akamwogopa akampa -- na akawapa na hao jamaa zake -- maneno mazuri na fedha nyingi na mshahara wa maisha. Yeye pouni mia tatu kila mwezi, na kila mmoja katika hao jamaa zake pouni khamsini kila mwezi."

Huko Madina, Liwali mpya aliifuata baraabara ile amri ya Muawiya ya kuwalazimisha watu wake wamkubali Yazid. Lakini hawakukubali; walipinga. Liwali akamjulisha Muawiya hilo pamoja na kumtajia waliokuwa mstari wa mbele katika upinzani huo. Naye akampelekea "barua za watu hao, akamwamrisha awapelekee na amletee jawabu ya kila mmoja katika wao. Nao ni mabwana hawa: Abdulla bin Abbas bin Abdil Muttalib, Huseyn bin Ali bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, Abdalla bin Jaafar bin Aby Talib bin Abdil Muttalib, na Abdalla bin Zubeir bin Safiyya bint Abdil Muttalib." Aliwaandikia "maneno makali kabisa", Sheikh A. S. Farsy anaeleza katika uk. 24 wa kitabu chake hicho, "na kuwahadidi kuwa atawaua wakikataa kumkubali Yazid awe Khalifa baada yake." Walipozipata barua hizo, mabwana hao (anavyosema Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 24) walimjibu "kwa maneno makali kabisa na tahadidi kubwa kabisa. Na aliyemwandikia maneno mengi kabisa ni Sayyidnal Huseyn."

Alipozipata jawabu zao hizo, Muawiya alimwambia tena huyo Liwali wake "azidi kuwalazimisha kwa tashdidi kubwa zaidi kabisa. Akafanya", Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk. 24), "zisifae kitu." Kwa hivyo akamwandikia Muawiya ende tena huko Madina akaonane nao yeye mwenyewe. Alipofika Madina, na "baada ya kupumzika", Sheikh Abdalla anasema (uk. 25), Muawiya "aliwaita kila mmoja akamsemeza siri peke yake ili wasimjibu wote kwa jawabu moja." Wa kwanza alikuwa ni Imam Husseina.s "Akamwambia, 'Mwanangu! Usiutilie fujo uma wa babu yako. Watu wote wamekwisha kuridhia kuwa Yazid awe Khalifa baada yangu. Hakuna wanaopinga ila nyinyi tu, na wewe ndiye unayewaongoza. Ukikubali wewe na wao wataridhia, kama walivyonambia.' (Imam Husseina.s ) akamwambia, 'Wete mbele yangu hapa waseme hayo. Mimi sisadiki kuwa wamesema hivyo. Wakikiri mbele yetu hapa na mimi nitakuwa pamoja nao. Lakini nina yakini kuwa hawatakiri.' Akamwambia, "Basi nenda zako. Lakini usimhadithie yo yote lo lote katika tuliyoyasema." Hivyo ndivyo alivyoandika Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 25 wa kitabu chake hicho.

Baada ya Imam Hussein(a.s) , alimwita Bwana Abdalla bin Zubeir, kisha Bwana Abdulla bin Umar bin Al Khattab. Nao wakamjibu kama alivyojibu Imam Husseina.s "neno kwa neno". Hapo tena, Sheikh Abdalla anasema (uk. 25 -- 26), "akapeleka mtu kumwita Bwana Abdur Rahman bin Aby Bakrinis Sidiqq. Akamsemesha maneno makali kabisa na yeye akamjibu makali kabisa. Wakaghadhibishana kweli kweli kwani yeye alikuwa mtu mzima kama yeye." Baada ya hapo ilimbidi Muawiya abadilishe mbinu. Kwa hivyo "siku ya pili", Sheikh Abdalla anasema (uk. 26), " akapeleka mtu kumwita Sayyidnal Huseyn bin Ali na Bwana Abdalla bin Abbas." Baada ya kuzungumza nao "mambo ya hali zao na hali za majumbani mwao", aliingia "kumsifu mwanawe Yazidi kwa aliyonayo na asiyokuwa nayo. Kisha akawaambia, 'Basi kwa hivi anastahiki kuwa Khalifa wa Waislamu ' " Imam Hussein a.s. akamjibu, Sheikh Abdalla anaendelea (uk. 26), kwa kumtajia "sifa mbovu za Yazid na akamwambia, 'Usizidishe madhambi kuliko uliyoyachuma. Yamekutosha hayo.' Na akamwambia, 'Unaudhulumu Uislamu na Waislamu kwa hayo uliyoazimia kufanya."

Baada ya kutofaulu mbinu zake hizo, aliamrisha waitwe mabwana wote watatu: Abdur Rahman bin Aby Bakr, Abdulla bin Umar, na Abdalla bin Zubeir. Sheikh Abdalla anasema (uk. 27), "Akawakaribisha wote pamoja kwa wakati mmoja. Akawaambia, 'Hili jambo la kufanywa Yazid kuwa Khalifa kishalichagua Mwenyezi Mungu na watu wote wameliridhia isipokuwa nyinyi. Basi tahadharini na kuleta balaa. Itakufikeni wenyewe kwa adhabu ya Mwenyezi Mungu na yangu 'Wakampinga wote Akataka aseme faragha na Bwana Abdur Rahman bin Abi Bakr. Alipomwambia maneno hayo ya kutawalishwa Yazid, alimwambia, 'Hatutaki. Na ukiyapitisha kwa nguvu tutavirejesha upya vita vya m wanzo wa Uislamu; uwe na wenye shauri moja na wewe upande wa ukafiri kama alivyokuwa baba yako.' " Hapo Bwana Abdur Rahman akaondoka. Baada ya siku tatu ikatoka amri ya kukusanyika watu wote wa Madina. Hapo Muawiya akawaweka wale wapinzani karibu yake, na akawaeleza waliohudhuria kuwa mikoa yote imemkubali Yazid kuwa Khalifa isipokuwa wao watu wa Madina, na kuwa lau yeye (Muawiya) angelikuwa anamjua aliye bora kuliko Yazid, angelimtawalisha; lakini hakuna bora kuliko yeye! Kisha akawaonya asisikie "kupinga kokote kule". Na akatangaza mkutano mwengine jioni.

Kabla ya huo mkutano, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 28 -- 29), aliweta wale wapinzani "wote pamoja ili atoke nao wende mkutanoni. Walipofika akawaambia: 'Nimekwisha weka machakari (wauaji) huko mkutanoni. Na mimi nitawaambia watu wote huko kuwa nyinyi nyote sasa mmekubali kutawalishwa Yazid. Asiyetaka roho yake ainuke hapo anipinge. Papo hapo kitaonekana kichwa chake kinagaragara chini.' "Na huko mkutanoni alikuwa ameshawaambia "mbele hao maaskari kuwa ye yote atakaesema kitu muuweni. Na akafanya ijulikane habari hii kwa watu wote ili wote wawemo katika khofu." Haya! Huyo ndiye Muawiya! Na hivyo ndivyo alivyopanga kumtawalisha mwanawe (Yazid) ambaye leo mawahabi wetu wasema kuwa mtu kama huyo ni Amiirul-mu'minin! Astaghfirullaah!

Kwenye mkutano huo, kama alivyowaonya kina Imam Hussein(a.s) , alipanda juu ya mimbari akasema, "Shuhudieni kuwa hawa waliokuwa wakipinga, sasa wameridhia. Na wenyewe hawa wote wako hapa. Na hawa ndio wazalendo wa Madina na wa Kisahaba. Hakuna lililosalia tena." Hivyo ndivyo anavyoeleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29 wa kitabu chake; na akaendelea kuandika, "Akatoa hapo mafedha kwa mafedha kuwapa kila wakubwa wa kila qabila za Kimuhajiri na Ansari na nyinginezo " Na hivyo ndi vyo Yazid alivyopatiwa utawala katika mwezi wa Rajab, mwaka wa 60 BH, baada ya babake kufa.

Ewe ndugu Mwislamu! Ikiwa mambo yalikwenda hivyo, kama yalivyoelezwa na Sheikh Abdalla Saleh Farsy, kweli Mwislamu yoyote anayeujua Uislamu wake, na anayetaka kubakisha jina jema la Uislamu, anaweza kujifakhiri kuwa mtu kama Yazid alikuwa ni kati ya viongozi wake wa Kiislamu, sambe (seuze) kumkubali kuwa ni Amiirul mu'minin?! Lakini hayo si aliyoyafanya Yazid, yeye mwenyewe; ni aliyofanyiwa na babake, Muawiya. Aliyoyafanya yeye mwenyewe, baada ya kutawala, ni makubwa zaidi! Ni yapi?

1

YAZID HAKUWA AMIRUL MUMININ

ALIYOYAFANYA YAZID ALIPOTAWALA

Kwa ufupi, anavyotueleza Sheikh Abdalla S. Farsy katika uk. 29-41 wa kitabu chake hicho, alifanya yafuatayo:

1. Alimpelekea habari Liwali wake wa Madina wa wakati huo, naye ni Khalid bin Hakam, awaapishe mabwana hawa: Huseyn bin Ali bin Abi Talib, Abdalla bin Umar bin Al Khattab, Abdalla bin Al Abbas na Abdalla bin Zubeir. (Abdur Rahman bin Abi Bakr hakuwamo; alikuwa ashakufa). Alimwamrisha "awaapishe yamini kali kabisa kuwa wamekwisha mkubali Yazidi kuwa ndiye Khalifa wa Waislamu wote. Na kuwa wakenda kinyume naye mali yao yawe halali yake, wake zao waachike. Na watumwa wao wawe mahuru,"

2. Liwali huyo alipoweta Imam Hussein(a.s) na Abdalla bin Zubeir, waliomba waachwe mpaka siku ya pili. "Kufika majumbani mwao tu", Sheikh Abdalla anaeleza (uk.30),"waliwaaga watu wao wakatoka kwa siri kwenda Makka kukaa huko kwani mwenye kuweko huko huwa katika amani " Yazidi, kupata habari hiyo tu, alihamaki "akamtoa( Liwali huyo) katika Uliwali wake."

3. Alipotawala Yazid, kimabavu kama tulivyokwisha kuona, watu wa Al Kufa (Iraq) walimpelekea Imam Hussein a.s. "mabarua ya kumhimiza ende huko Iraq azatiti vita huko kumuondoa huyo asiyestahiki kuwa Khalifa wa Waislamu". Hata hivyo, Imam Hussein a.s. hakwenda papo hapo, bali alimtuma binami yake (Muslim bin Aqyl) ende huko ili amjulishe ukweli wa mambo ulivyo. Alipopata habari hiyo, Sheikh Abdalla anatueleza (uk 34-35), Yazid "alimchagua Liwali qatili, dhalimu, jabbar, shujaa anayemchukia Sayyidna Ali na kizazi chake, aliyekuwa akiitwa Ubeidillah bin Ziyad ambaye baba yake alithibitishwa na Muawiya -- kwa siyasa tu -- kuwa ndugu yake. Akatiwa katika kabila yake ya Bani Umayya hali ya kuwa hakhusiani naye hata chembe, wala hakhusu Uqureshi hata kidogo, bali wala Uwarabu. Ni mtu mwanaharamu tu aliy ekuwa hodari sana hata akampinga Muawiya kweli kweli. Akaona amthibitishe kuwa ndugu yake na amwachie amri ya Iraqi yote". Hivyo akawa mwana haramu wa kwanza, katika historia ya Uislamu, kufanywa mwana halali!

4. Baada ya kumchagua Liwali huyo, Sheikh Abdalla anaeleza (uk. 35), Yazid alimpa amri hii: "Muuwe huyu Muslim bin Aqyl, na kila waliokuja pamoja naye, na kila waliompokea, na kila walio pamoja naye; na mfunge umuadhibu jamaa na jirani wa kila mmoja katika hawa, usiwe na huruma na yeyote." Na hivyo khaswa ndivyo ilivyokuwa. "Alifanya kama alivyoamrishwa na Yazid, akawamaliza hao wote alioamrishwa awaue, na akawafunga hao alioamrishwa awafunge " Katika kitabu chake, Sheikh Abdalla S. Farsy hakueleza jinsi alivyouliwa Muslim bin Aqyl. Lakini vitabu vye ngine vya historia vinaeleza kwamba alichukuliwa mpaka juu ya kasri moja, akakatwa kichwa ambacho kilitupwa chini kikifuatishwa na pingiti lake. Baadaye kichwa hicho kikapelekwa kwa Yazid!

5. Kama tulivyokwisha kuona humu uk. 1 - 3, baada ya Imam Hussein(a.s) na aliokuwa nao kuuwawa kikatili na kukatwa vichwa vyao, Yazid (alipopelekewa vichwa hivyo) alikamata kifimbo, Sheikh Abdalla S. Farsy anatueleza (uk 40), "akawa anayagonga meno ya Huseyn na kuimba kusema, 'Nimemlipa leo Muhammad! Kama alivyoniuliya wazee wangu siku ya Vita vya Badr, leo nimemuulia wajukuu wake. Na huu ndio mwendo wetu utakaokuwa. Kila anayetupinga tutamwua japokuwa anatukhusu " Ewe ndugu Mwislamu! Hebu jiulize: Mtu anayejasiri kusema kuwa anamlipa kisasi Mtume Muhammad(s.a.w.w) kwa kuw auwa makafiri (waliokuwa babu zake yeye Yazid) hufaa au huweza kuitwa Amiirul-mu'minin? Acha hilo! Huweza hata kuitwa Mwislamu? Hivi hao mawahabi wetu hawakulijua hilo? Au watatwambia kuwa Sheikh Abdalla Saleh Farsy alikuwa Shia? Kuna yaliyobaki, na si madogo!

6. Baada ya kumuuwa Imam Husein(a.s) na aliokuwa nao katika mwaka wa 61 BH, Yazid aliiingilia Madina. Sheikh Abdalla Saleh Farsy anatwambia (uk. 41): "Wakauawa Masahaba wengi hapo Madina na wasiokuwa Masahaba. Na wakafanya fisadi kubwa sana hapo Madina muda wa siku tatu mfululizo. Ikawa hakuna kisichoharibiwa; si roho wala mali wala hishima. Aliwaamrisha Yazid wafanye hivyo. Na masahaba wasiokufa aliwaamrisha wapigwe chapa za mgongo za kuonyesha kuwa wao ni watumwa wa Yazid." Subhaanallah! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi wetu! Katika dondoo hilo hapo juu, hata hivyo, Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; hakulifunua. Lakini wanazuoni wenziwe wamelifunua. Kati ya hao ni Ibn Kathir ambaye, kwa mawahabi wa ulimwengu, ni kama Sheikh Abdalla Saleh Farsy kwa mawahabi wa Afrika ya Mashariki; wanamuenzi sana. Yeye, katika uk 220 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, amesema kuwa idadi ya hao "masahaba wengi" waliouwawa ilikuwa " mia sabaa: vigogo vya muhaajiriin na answaar"; na "wasiokuwa masahaba" walikuwa " elfu kumi". Kuhusu "fisadi kubwa sana", alizosema Sheikh Abdalla S. Farsy, Ibn Kathir anasema (uk. 222) kuwa "hazisemeki hazielezeki; hakuna anayezijua ila Mwenyezi Mungu" japokuwa, kabla ya hapo katika uk. 220, alikuwa ameshatasua kuwa " wanawake walihashiriwa mpaka ikasemwa kuwa 1000 (elfu moja) walishika mimba na kuzaa bila kuwa na waume"! Baada ya Ibn Kathir kuyaeleza hayo, na kama kwamba anataka kuzindua tumfahamu Yazid ni nani, anatutajia (uk 223) Hadith tatu za Bwana Mtume(s.a.w.w) Ya kwanza, iliyopokewa na Bukhari, inasema: "Hakuna yoyote atakayewafanyia vitimbi watu wa Madina ila atayayuka kama inavyoyayuka chumvi katika maji." Ya pili, iliyopokewa na Muslim, inasema: " Haikusudii Madina yoyote kwa uovu ila Mwenyezi Mungu atamyayusha katika moto myayusho wa risasi, au myayusho wa chumvi katika maji." Ya tatu, iliyopokewa na Imam Ahmad bin Hambal, inasema: "Anayewatakia khofu watu wa Madina kwa dhulma, Mwenyezi Mungu naye atamtia khofu na ashukiwe na laana ya Mwenyezi Mungu na malaika na watu wote. Wala Mwenyezi Mungu, Siku ya Kiyama, hatamkubalia toba wala fidia."

Haya! Kama hayo yaliyofanywa Madina yalifanywa kwa amri ya Yazid, kama asemavyo Ibn Kathir (uk. 220 ) na Sheikh Abdalla S. Farsy (uk. 41), mtu huyo -- kwa Hadith zilizotajwa hapo juu -- bado yu salama? Ni Amiirul-mu'minin gani huyo anayeshukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu, malaika Wake na watu wote?

7. Mwaka mmoja baada ya kuiingilia Madina, aliiingilia Makka (katika mwaka wa 64 BH)! Huko, Sheikh Abdalla S. Farsy anasema (uk.41): "Majeshi ya Yazid yaliuwa watu wengi na kuivunja Al Kaaba." Hapo pia Sheikh Abdalla "amefinika kombe" ; lakini wenziwe wamelifunua. Kwa mfano, huyo huyo Ibn Kathir ameandika (uk. 225) kuwa majeshi hayo "yaliipiga mawe Al Kaaba kwa teo (manjaniiq) na kuishambulia hata kwa moto mpaka ukuta wake ukaungua"! Na katika uk. 72 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab, Ibnul Imaad al Hambalii anasema: "mpaka likaanguka jengo lake"! Haya! Hiyo ni "Nyumba ya Mwenyezi Mungu" ambayo Qur'ani Tukufu inatwambia (Sura 3:97) kwamba aliyeko nje akakimbilia huko, huwa katika amani; leo Yazid anaiondolea amani hivyo! Na huyo ndiye Amiirul-mu'minin wa mawahabi ambaye wanataka Waislamu wamtambue hivyo! Subhaanallah! Hayo basi, kwa mukhtasari, ndiyo yaliyofanywa na Yazid. Jee, acha ya Amiirul-mu'minin, Mwislamu wa kawaida tu anaweza kuyafanya kama hayo? Bila shaka hawezi. Ikiwa ni hivyo basi, vipi Yazid aliweza? Kuijibu suali hiyo, itabidi tujue Yazid alikuwa ni mtu wa aina gani. Hilo inshallah tutalitizama katika sura ijayo kwa kunukuu maneno yaliyomo katika vitabu vilivyotungwa na wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kisunni (si wa Kishia).

YALIYOSEMWA NA WANAZUONI WA KISUNNI

Tuanze na Sheikh Abdalla Saleh Farsy. Yeye amesema hivi katika uk.40 wa kitabu chake, Maisha ya Sayyidna Huseyn: "Utawala wa Yazid -- kama tulivyoona -- ulikuwa wa nguvu tu bila ya ridhaa ya watu". Suali ya kuuliza hapa ni: jee, inawezekana utawala wake ukawa ni "wa nguvu", lakini yeye mwenyewe akawa si wa aina hiyo? Jee, kwa mafunzo ya Kiislamu, Amiirul-mu'minin huruhusiwa kutawala watu kwa "nguvu tu bila ya ridhaa" yao? Maneno kama hayo takriiban yamesemwa na Sheikh Muhammad Abduh. Chini ya maelezo ya Sura 5:36-37, katika uk 367 wa Juzuu ya Sita ya tafsiri yake ya Qur'ani Tukufu ijulikanayo kwa jina la Tafsiirul Manaar, shekhe huyo amemwita Yazid "kiongozi wa dhulma na ukandamizaji ambaye alitawala mambo ya Waislamu kwa nguvu na makri"! Jee, aliye hivyo huitwa Amiirul-mu'minin ? Wa tatu ni Allaamah Shawkaani katika kitabu chake cha Hadith za Mtume(s.a.w.w) kiitwacho Naylul Awtwaar. Katika uk. 362 wa Juzuu ya Sabaa ya kitabu hicho, amemweleza Yazid kuwa: "mlevi, katembo, mvunjaji utukufu wa sharia takatifu"! Huyo ndiye Amiirul-mu'minin kwa mawahabi wetu? Wa nne ni Abul Hassan Alii bin Muhammad bin Alii at Twabarii, mwanachuoni mashuhuri wa Kishaafi'i. Alipoulizwa kuhusu Yazid, kati ya ila alizomtia ni: "alikuwa mlevi wa kutopea (kubobea) ambaye mashairi yake ya (kusifu) ulevi yanajulikana". Hayo yamenukuliwa katika uk. 287 wa Juzuu ya Tatu ya Wafayaatul A'yaan ya Ibn Khalikaan.

Wa tano ni Imam Ibn Hazm, katika uk. 98 wa Juzuu ya Kumi na Moja ya kitabu chake kiitwacho Al Muhallaa, amemtia Yazid bin Muawiya katika kundi la wale "waliosimama kwa lengo la kutaka dunia tu", na akasema kuwa msimamo wake huo ulikuwa "ni ukandamizaji mtupu usiokuwa na udhuru (wa kisharia)". Haya! Mtu wa aina hiyo huwa Amiirul-mu'minin? Wa sita ni Abul Falaah Abdul Hayy Ibnul Imaad, mwanachuoni mkubwa wa Kihambali, katika uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya kitabu chake mashuhuri kiitwacho Shadharaatudh Dhahab. Katika ukurasa huo amemnukuu Imam Dhahabi, mwanachuoni mwengine mkubwa, kuwa amesema kwamba. Yazid "alikuwa naasiby (mtu anayemchukia Imam Aliia.s ), fidhuli, jeuri, anakunywa pombe na kufanya munkar. Aliianzisha dola yake kwa kumuuwa Hussein, na akaimaliza kwa tukio la Harra. Watu wakamchukia, wala hakubarikiwa katika umri wake". Tukio la Harra ni lile shambulizi la Madina tulilolitaja uk. 15 - 16. Jee, mtu ambaye ameianza dola yake kwa kumuuwa mjukuu wa Bwana Mtume(s.a.w.w) , na kuimaliza kwa kuushambulia "mji wa Mtume(s.a.w.w) " (Madina) na kuwaachia mimba za haramu wanawake wasiopungua elfu moja, hufaa kuitwa Amiirul-mu'uminin? Tunawauliza mawahabi wetu: Kwa hujja gani ya Kiislamu? Wa sabaa ni Ibn Kathir ambaye, kwa kawaida, mawahabi humtegemea mno. Yeye, katika uk. 235 - 236 wa Juzuu ya Nane ya kitabu chake kiitwacho Al Bidaaya Wan Nihaaya, ameyataja "yaliyopokewa" kuhusu Yazid. Kati ya hayo ni "kwamba Yazid alikuwa mashuhuri kwa kupenda muziki na kunywa pombe kufanya urafiki na watoto wa kiume na wanawake waimbaji Na hakuna siku ambayo aliamka hakulewa "!

Na kabla ya hapo, katika uk. 216 wa kitabu hicho hicho na juzuu hiyo tuliyoitaja hapo juu, Ibn Kathir anaeleza ya ujumbe wa "watukufu wa watu wa Madina" uliokwenda kwa Yazid. Anasema: "Waliporejea Madina, walitangaza shutuma zao dhidi ya Yazid na aibu zake. Wakasema, 'Tunatoka kwa mtu asiyekuwa na dini, anayekunywa pombe, ambaye wanawake waimbaji humuimbia na kumpigia muziki " Pia ametaja yaliyosemwa na kiongozi wa ujumbe huo, Mundhir bin Zubeir, aliporejea Madina baada ya kupitia Basra kwa swahibu yake, Liwali wa huko (Ubaidillaah bin Ziyaad), kuwa Yazid "anakunywa pombe na kulewa mpaka akaacha swala"! Haya! Mambo yakifikia hapo, ni Mwislamu wa aina gani atakayejifakhiri kuwa na Amiirul-mu'minin sampuli ya Yazid? Mawahabi waliotoa karatasi zao na kumwita Yazid Amiirul-mu'minin bakhti yao hawakuwako zama za Ukhalifa wa Umar bin Abdulaziz. Wangekiona cha mtema kuni! Khalifa huyo, aliyekuwa kabila moja na Yazid, alimpiga mtu aliyemwita Yazid hivyo, viboko ishirini! Kama wataka kuyaona hayo, nawatizame uk. 69 wa Juzuu ya Tatu ya Shadharaatudh Dhahab.

YALIYOSEMWA NA MTUME KUHUSU YAZID

Hadith ambazo nitazitaja humu ni zile zilizomo katika Sahih Bukhari peke yake. Kama wengi wetu tunavyojua, kitabu hicho -- kwa masunni na kwa mawahabi pia -- ndicho kitabu kilicho sahihi (kweli) mno baada ya Qur'ani Tukufu. Kwao wao, Hadith iliyotolewa humo huwa haina shaka! Katika Kitaabul Fitan, mlango wa Qawlin Nabiyyi(s.a.w.w) Hilaaku Ummatii Alaa Yaday Ughaylimatin Sufahaa, muna Hadith (kwa Kiingereza, ni Hadith Na. 180 iliyomo uk 147 wa Juzuu ya Tisia) isemayo: "Amr bin Yahya bin Said bin Amr bin Said amesema: 'Babu yangu amenipa habari kwa kusema: Nilikuwa nimekaa na Abuu Hurayra msikitini kwa Mtume(s.a.w.w) Madina, tukiwa na Marwaan. Abuu Hurayra akasema, 'Nimemsikia mkweli na mwenye kuswadikiwa na Mwenyezi Mungu (yaani Bwana Mtume(s.a.w.w) akisema: Uangamifu wa umma wangu utakuwa mikononi mwa vijana wa Kikureshi. Marwaan akasema: 'Laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie vijana (hao).' Abuu Hurayra akasema: 'Lau ningelitaka kusema ni Banii fulani na Banii fulani ningelisema.' Nikawa ninatoka na babu yangu kwenda kwa Banii Marwaan pale walipoitawala Sham. Walipokuwa wakiwaona ni vijana wadogo, akitwambia: Huenda wale wakawa ni miongoni mwao. (Nasi) tukimwambia: Wewe unajua zaidi."

Kabla hatujanukuu ilivyoelezwa Hadith hiyo, ningependa wale wajuwao Kiingereza (wasiojua Kiarabu) wajue kwamba Hadith hiyo haikufasiriwa yote kwa ukamilifu katika hiyo nuskha ya Kiingereza. Kipande kikubwa, ambacho tumekichapisha kwa italiki katika tafsiri yetu ya Kiswahili hapo juu, hakikufasiriwa kwa Kiingereza -- sijui ni kwa mfasiri wake kughafilika au ni kwa kujighafilisha! Hata hivyo, katika kuisherehe (kuifafanua) Hadith hiyo, Imam Ibn Hajar Al Asqalaani, katika uk. 10 wa Juzuu ya Kumi na Tatu ya kitabu chake kiitwacho Fat'hul Baari, ameitaja riwaya ya Ibn Abii Shayba isemayo "kwamba Abuu Hurayra alikuwa akenda sokoni na akisema: 'Ewe Mola! Usinidirikishe na mwaka wa sitini wala utawala wa vijana.' "Halafu (yeye Ibn Hajar) akasema: "Na katika maneno haya muna ishara kuwa wa kwanza wa vijana hao alikuwa katika mwaka wa 60; na hivyo ndivyo ilivyokuwa. Maana Yazid bin Muawiya alitawalishwa katika mwaka huo, na akabakia mpaka mwaka wa 64; akafa. Kisha akatawala mtoto wake, Muawiya, aliyekufa baada ya miezi (michache)."

Kwa hivyo, kwa mujibu wa Imam Ibn Hajar, miongoni mwa "vijana wa Kikureshi" ambao Bwana Mtume(s.a.w.w) alitabiri kuwa umma wake utaangamia mikononi mwao, na ambao Abuu Hurayra alikiomba Mwenyezi Mungu asimkutanishe nao katika huo mwaka wa 60, ni Yazid. Jee, maneno ya Mtume(s.a.w.w) yalianguka? Jee, baada ya mauaji aliyoyaamrisha Karbalaa na Madina na Makka, kama tulivyoona humu mpaka sasa, umma wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) haukuangamia? Au hao waliouliwa walikuwa ni makafiri, si Waislamu? Hivyo basi, bado Yazid ni Amiirul-mu'minin? Wala si kwamba Abuu Hurayra, pale alipotaja "Banii fulani na Banii fulani" katika Hadith tuliyoitaja hapo juu, alikuwa hawajui ni kina nani; la! Alikuwa akijua, lakini akiogopa kuwataja kwa majina. Na hilo li wazi tunapoiangalia tena Sahih Bukhari. Katika Kitaabul Ilm, Mlango wa Hifdhil Ilm muna Hadith (kwa Kiingereza ni Hadith Na. 121 iliyomo uk. 89 wa Juzuu ya Kwanza) isemayo: "Imepokewa kwa Abuu Hurayra akisema, 'Nimehifadhi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aina mbili za ilimu. Moja ya ilimu hiyo nimeitangaza. Lakini nyengine, lau ningeliitangaza ingelikatwa koo (yangu) hii.' "

Katika kuifafanua Hadith hiyo, katika uk. 216 wa Juzuu ya Kwanza ya Fat'hul Baari, Imam Ibn Hajar amesema: "Wanazuoni wamechukulia kuwa ilimu ambayo (Abuu Hurayra) hakuieneza ni ya zile Hadith ambazo ndani yake mumetajwa majina ya watawala waovu, na hali zao na zama zao. Abuu Hurayra alikuwa akiwataja kikuu tu baadhi yao, wala hakuwa akiwatasua kwa kuiogopea nafsi yake kwao; kama alipokuwa akisema, 'Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na mwaka wa 60 na utawala wa vijana'; alikuwa akiashiria Ukhalifa wa Yazid bin Muawiya kwa sababu ulikuwa katika mwaka wa 60 BH." Wala ufafanuzi huo haukutolewa na Imam Ibn Hajar peke yake. Hata Imam Shihaabuddin Ahmad Al Qastwalaani, katika sherehe yake ya Hadith hizo hizo, ametoa karibu ufafanuzi kama huo. Wale wajuwao Kiarabu, wakitaka kuyaona hayo, nawatizame uk. 374 wa Juzuu ya Kwanza na uk. 11 - 12 wa Juzuu ya Kumi na Tano ya Irshaadus Saari.

Kwa hivyo Abuu Hurayra hakumtaja Yazid kwa jina kwa kujiogopea nafsi yake, asije akakatwa koo; si kwamba alikuwa hajui. Kwa lugha nyengine, alifanya taqiyya! Lakini kama Abuu Hurayra alifanya taqiyya, jee wenziwe pia walifanya hivyo? Hilo inshallah tutaliona katika sura ijayo.

2

MUANDAMO WA MWEZI

SURA YA PILI

JAWABU KWA WANAFUNZI WA BACHOO JAWABU YA UTANGULIZI

Wahusika ndugu zetu wa Masjid Al-Sunna Zanzibar, wameanza kitabu chao hicho kwa utangulizi wenye kumshukuru na kumuhimidi Allah na kumtakia rehema na amani Bwana wetu Muhammad (s.a.w.) kama zilivyo khutuba na vitabu vya kiislamu. Na hayo yote yamefanyika chini ya utangulizi wenye anwani:

UKWELI JUU YA KUANDAMA KWA MWEZI

Na hii ndio sehemu ya kwanza ya kitabu chao. Wakasema katika utangulizi huo: Msisitizo wetu mkubwa katika kitabu hiki ni ile nukta muhimu ya kwamba suala la kufunga na kufungua kwa muandamo mmoja kwa dunia nzima si jambo jipya kama wanavyodhani baadhi ya watu, ni jambo la kale mno ambalo linaweza kutekelezeka na kwamba huo ndio uliokuwa msimamo wa 'Jamhur' ya wanavyuoni.

Jawabu Nakubali kuwa hili ni jambo la zamani, lakini kudai kuwa hii ni kauli ya Jumhuri ni madai hewa: hayana ushahidi. Leo hii duniani hakuna madhehebu yoyote ambayo inaitendea kazi kauli hio kama ni madhehebu nzima, bali kuna baadhi ya watu tu katika kila madhehebu ambao wanafata kauli hio. Hata zile madhehebu ziliotajwa kuwa ni zenye kufata kauli hio kama vile Malik, Hanbal na Hanafi, basi hawaitendei kazi kauli hio ila baadhi yao tu. Libya, Algeria na nchi nyengine za Afrika Kaskazini na Magharibi - kwa mfano - ni nchi za wafuasi wa madhehebu ya Malik, nao wanafata miandamo yao wenyewe. Kwa hivyo, dai kuwa hii ni kauli ya Jumhur ya wanavyuoni, si dai sahihi.

SEHEMU YA PILI

Katika sehemu ya pili, ndugu waandishi wanasema:

2. Si Fikra Za Shaykh Naaswir Bachuu "Ndugu yetu Juma Muhammad Rashid Al-Mazrui amejitahidi kuandika kitabu alichokiita: "Ushahidi Uliowekwa Wazi Katika Suala La Miandamo Ya Mwezi. Makusudio yake yalikuwa ni kutaka kukijibu kitabu kilichoandikwa na Shaykh Naaswir Abdullah Bachuu kinachojulikana kwa jina la "Ufafanuzi Wa Mgogoro Wa Kuandama Kwa Mwezi."

Jawabu Kidogo na mimi naomba niweke wazi kwamba kitabu changu hakikuwa kabisa na lengo la kujibu kitabu cha Sheikh Nassor Bachoo. Hili la kunukuu maneno yake na kuyajadili lilikuwa ni jambo la kutokea tu baada ya mtu Fulani kuniletea kitabu chake. Kwa havyo, kama mulivyosema nyinyi katika kitabu chenu kwamba: Kitabu hiki ni kama nasaha kwa Waislamu wote ili kuweza kudumisha umoja wetu hususan pale ambapo pamejitokeza misimamo tofauti katika mambo ya ibada. Wala lengo la kitabu hiki sio kuendeleza malumbano baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe hata kwa wale wenye misimamo tofauti. Kutajwa ndugu yetu Juma Muhammad Rashid lilikuwa ni jambo lisilobudi wala hapakuwa na lengo la kumkashifu au kumuumbua bali ni kutokana na kuwa hapakuweza kupatikana njia mbadala kwa vile ameshaandika kitabu ambacho ameshakichapisha chapa ya kwanza na ya pili.

Basi na mimi nakuombeni munielewe hivyo hivyo, kwamba wakati mimi naikubali fikra Fulani na kuikataa fikra Fulani, hakuna budi ninukuu fikra pinzani na kuonesha kwanini siikubali; na kwa upande wa pili ni lazima nioneshe kwanini naikubali fikra ninayoikubali. Na nitaposema kuwa kuna watu wana fikra hii, basi nadhani haitokuwa jambo la busara kama watu hao sikuwataja na nikiwataja ni lazima nitaje marejeo. Kwa sababu hii ndio maana nimekuwa nikinukuu maelezo ya Sheikh wetu Nassor Bachoo na kumjadili mule nisimokubaliana naye. Naomba musihuzunike kwani kujibizana katika kutafuta ukweli ni suala mashuhuri katika uwanja wa elimu. Wanavyuoni wakubwa wa kale na wa sasa wamekuwa wakijibizana ili kutafuta ukweli na hatimae huwabainikia woa pamoja na wasomaji. Kwa hivyo, hamukuwa na haja ya kutumia lugha: "Wala hapakuwa na lengo la kumkashifu": hii si kashfa hata kidogo: hii ni elimu.

Lakini, hakuna haja ya kufichana; kitabu chenu mumeandika kwa kujibu kitabu changu. Hamuna haja ya kusema: "Wala lengo la kitabu hiki sio kuendeleza malumbano baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe hata kwa wale wenye misimamo tofauti. Kutajwa ndugu yetu Juma Muhammad Rashid lilikuwa ni jambo lisilobudi wala hapakuwa na lengo la kumkashifu au kumuumbua bali ni kutokana na kuwa hapakuweza kupatikana njia mbadala kwa vile ameshaandika kitabu ambacho ameshakichapisha chapa ya kwanza na ya pili", kwani kitabuchenu kimeanza kwa kunitaja mimi mwanzo hadi mwisho na kuniaga kwa kunipa nasaha mimi. Ama mimi naandika jawabu hii kukujibuni nyinyi: sikufichini wala sisemi uwongo.

Munasema Kutokana na jambo hilo , sisi kwa upande mmoja tunashukuru kwa juhudi yake hiyo na kwa upande wa pili tunatuma masikitiko yetu kwake kwa kutokuwa makini na muadilifu katika kulifafanua jambo hilo muhimu. Kwani kitabu chake hicho kimeandikwa katika mfumo wa chuki, kibri, kejeli na malumbano huku akisisitiza kwa mara nyingi kauli chafu ambazo muandishi hapaswi kuzitumia katika kitabu au katika mijadala ya Dini. Jawabu Hizi chuki, kibri na kejeli, mimi nimezisoma kwenu, kwa hivyo na iwe kama msemo wa Waswahili: "Papa akipea mafuta huwapa wanawe". Je nyinyi munayakumbuka haya:

1) Munaukumbuka muhadhara wa Sheikh Bachoo ambao alisema kuwa wasionyanyua mikono katika sala wanasali kama mipopoo? Jamani! Hii si kejeli? Je katika nyinyi yuko aliyetoa muhadhara au kuandika kitabu ili kumjibu Sheikh wetu. Sasa uadilifu uko wapi?

2) Je munaukumbuka muhadhara wa Sheikh Bachoo aliozungumzia mas-ala ya udhu kasha akasema: "Wengine wakitia udhu kiungo hiki huomba dua hii na kiungo hiki huoma dua hii; upumbavu mtupu". Je haya si matusi? Je hii si kejeli?

3) Siku moja palikuwa na maziko. Maiti alisaliwa msikiti wa wajiitao "Watu wa Sunna". Kijana mmoja akasimama akasema: "Leo tunataka kukuonesheni vipi Mtume (s.a.w.) kamsalia maiti: si kama wanavyofanya Ibadhi na Shia.

4) La nne ni kuwa ikiwa nyinyi mumethubutu kunita mjeuri, mwenye kibri na kejeli; maneno ambayo mimi sikukwambieni wala kumwambia Sheikh Nassor; mimi nimemtoa makosa tu Sheikh wetu: na hii ni kawaida katika uwanja wa elimu; sasa je na nyinyi pia ni majeuri, wenye kibri na kejeli? Katika uwandishi wenu, pia mumesema: "Hatujui dhana hii potofu ameitoa wapi." Mwenye dhana potufu naye ni mpotufu, kwa hivyo na nyinyi hamukutoa nasaha bali mumetukana. Nakupeni mifano hii mitatu ya Sheikh wetu na mmoja wenu nyinyi wenyewe enyi wenye kuandika Radan mardudan na mifano iko mingi. Inatosha kuwaita kwenu watu wengine kuwa ni watu wa bidaa na nyinyi ndio watu wa Sunna. Kwa hivyo, hii hali mumeiuda nyinyi wenyewe: Zanzibar bali Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla haikuwa hivi. Chuki mumeziunda nyinyi; mukijirekebisha kwa kutumia lugha nzuri nadhani hakuna atayekwambieni jambo kwa lugha nzito.

Mnasema Mfano wa kauli zake mbaya ni kama zifuatazo:

(vuta-nikuvute) [uk. 6]

(hii ni ajabu katika ajabu za dunia!) [uk. 124]

(Kwa hivyo, uwezekano huo alioutoa Sheikh hauwashi wala hauzimi [uk. 124]

(Ninasema: Enyi walimwengu wenzangu tazameni hoja za kielimu hizo!!!!!!! Kwani nyinyi Wazanzibari kabla ya kuja fikra hio ya Sheikh Nassor Bachoo ya kufunga kwa muandamo mmoja,)

(Utaona kwamba masuala yote haya si yenye kima katika soko la elimu, bali ni masuala ya kuwababaisha watu wasiojua nini cha kujadiliwa katika mas-ala haya ya funga) [uk. 167]

(Hoja nyengine - nayo pia ni hoja ya mitaani - ni kuwa watu wengi wa kawaida wanapouona mwezi mkubwa husema: "E basi ule ndio mwezi wa leo ule?!!!")

(Jawabu hii ya mwisho, inaufanya upinzani mzima wa Sheikh Bachoo kuwa hauna maana yoyote.) [uk. 132]

(Kwa ufupi ni kuwa hicho walichokidai watetezi wa rai pinzan) [uk. 32]

(utaona jinsi gani mwanamume alivyokuwa bingwa wa kubadilika! Na hili si jengine bali ni lile Waswahili wanalolisema: "Mfa maji hukamata maji.") [uk. 128]

(Hakuna hapa kinachoonesha mas-ala ya kufunga kwa muandamo mmoja wala kumi na moja.)) [uk. 125] (haina maana kwamba usiku ukiingia sehemu moja ndio umeingia dunia nzima. Kwa ufupi ni kuwa hii ni hoja ambayo haina faida yoyote ya kielimu, lakini tunaijadili kwa ajili ya watu wa mitaani tu.)

Jawabu Sikubaliani na nyinyi kwamba humu muna maneno mabaya. Lakini hata nikikubali basi nasema kwamba lugha ya namna hii sababu ni nyinyi, na kwa hivyo, utaona kwamba ninapojadiliana na watu wengine basi lugha yangu hubadilika. Kwa hivyo, tujirekebisheni sote na tujadili tafauti zetu kwa lugha ya kiungwana. Ama ukinita mpopoo, basi usinilaumu na wewe nikikwita mnazi: unanilaumu nini na wewe unakifanya kile kile nikifanyacho?! Bali hata katika kitabu hiki munachonijibu, basi nanyi mumetumia lugha hizo hizo. Katika baadhi ya sehemu umesema: "Kwa hakika katika kitabu chake hicho kwenye uk 6, anajionyesha alivyo na kauli mbili tofauti..". Na mwishoni mwa kitabu mumesema: "Dhana ya pili ya ndugu Juma imejengeka katika msingi dhaifu wala haina nafasi katika uwanja wa fani (kitaalamu) nao ni kule kusukuma kwake juu ya elimu ya Jiografia". Na yamo mengi katika kitabu chenu. Sasa nyinyi mwasema nini na mwatenda nini?

Munasema "Kwa hakika katika kitabu chake hicho kwenye uk 6, anajionyesha alivyo na kauli mbili tofauti: Kwanza anakubali kwamba suala la muandamo wa mwezi lina ikhtilafu katika kufunga kwa kumuelezea Shaykh Naaswir Bachuu kwamba: (Tunampongeza kwa juhudi) Kisha pale pale anageuka kwa kusema: (madamu hili ni suala la khilafu - basi i likuwa ni kutolizungumza kabisa,) Sasa hebu tumuulize ndio anapongeza nini? Na ni nani aliyemwambia kwamba jambo lenye khitilafu halizungumzwi? Yeye angezungumza nini katika kitabu chake kama si masuala ya ikhtilafu? Pia anatwambia haya ni katika mambo ya furui (matawi) za Kidini, kwa hivyo zisizungumzwe. Kwani ni nani aliyemwambia kuwa furui za Kidini hazizungumzwi?"

Jawabu Ikiwa lugha hii ndogo hamukuweza kuifahamu, vipi mutaweza kufahamu kitu chenye kuhitaji fani za lugha na usuli na mengineo. Ikiwa mimi niliingia msikitini kwenu Raha Leo nikakuta juu ya ubao wenu munawasomesha vijana na katika darsa hio Mubtadaa mumemwita Fa'il (vipi mutaweza kujadili masuala haya?!!! Mimi nimempongeza Sheikh Bachoo kwa juhudi au moyo wake; na sikumpong eza kwa kulikuza suala ambalo:

1) Ni la furuu'i

2) Lina khilafu. Na hii haina maana kuwa Furu'i zisizungumzwe; suala la Furu'i huwa halishadidiwi; bali unawaacha watu kama walivyo tu. Lakini yeye anapenda kushadidia katika mas-ala kama haya; ndio maana akashadidi hata katika suala la kufunga mikono hata kuwaita watu mipopoo bali na kuwambia kuwa hawana Sala. Kwa hivyo, nieleweni kwamba ninachokipinga ni kushadidia au kuwakoroga watu katika kitu ambacho ni furu'i za dini ilhali yeye kawakuta na msimamo tafauti tangu zamani. Katika mas-ala ya furu'i, wanavyuoni huwa hawashadidi juu ya Mas-ala kama haya. Mimi leo nikisimama nikaanza kufanya kampeni kwamba watu wasiitikie amina wa kisali, nalo ni jambo la furu'i, si nitakuwa natia fitna tu? Jambo kama hili huwachwa wasomi wakalitafiti kaiha kila mmoja akafanya vile ilivyombainikia. Lakini kufanya kampeni maalumu na da'awa kana kwamba waliotangulia wote ni wapotovu, hili ndilo jambo la kulaumiwa.

Ama kauli yenu: "Kwanza anakubali kwamba suala la muandamo wa mwezi lina ikhtilafu katika kufunga kwa kumuelezea Shaykh Naaswir Bachuu kwamba: (Tunampongeza kwa juhudi) Kisha pale pale anageuka kwa kusema: (madamu hili ni suala la khilafu - basi ilikuwa ni kutolizungumza kabisa,) Sasa hebu tumuulize ndio anapongeza nini?" Mwisho wa kunukuu. Na mimi nikuulizeni nyinyi mumenishukuru kwa juhudi yangu kisha mwisho wa kitabu mukaniambia: "Mwisho tunachukua fursa hii kumuonya ndugu Juma kuwa amuogope Mwenyezi Mungu hususan katika mas-ala ya kielimu. Akumbuke kuwa Mwenyezi Mungu Ameonya juu ya mtu kusema jambo au kufanya asilolijua. Aelewe kwamba ataulizwa juu ya hilo. Lingekuwa jambo la busara kama ndugu Juma angalikubali kuuliza na kufanya utafiti zaidi juu ya mas-ala haya kama agizo la Mwenyezi Mungu linavyotutaka". Sasa na nyinyi munanishukuru nini?

Munasema "Sisi tunapenda kumfahamisha kuwa suala hili la kwamba mwezi ukiandama sehemu moja unatosheleza kufuatwa kwa kufunga au kufungua ulimwengu mzima, si suala jipya bali ni jambo la kale. Tunasikitika kwamba hakuangalia vizuri maoni ya Wanavyuoni wakubwa walivyoelezea msimamo huo. Angalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 51-58. Hapa tunanukuu baadhi ya kauli hizo:

Imamun-Nawawy aliyekisherehesha Kitabu cha Sahihi Muslim anasema:

"Na jambo lililo sahihi kwa wenzetu (Mashaffi) ni kuwa muandamo mmoja hauwahusu watu wote bali unawahusu wale walio karibu kwa kiasi ambacho hawaruhusiki kupunguza Sala (Sala ya safari). Pia imesemwa kuwa iwapo matlai ni mamoja watalazimika (watu) kufunga pamoja. Pia imesemwa kuwa ikiwa (wanaishi) katika eneo la Iklimu moja (maili 72 au km 89) (watalazimika kufunga pamoja) vyenginevyo kila mmoja atafunga kwa muandamo wake. Na wakasema wenzetu wengine (Mashaffi) kuwa muandamo katika sehemu moja utawahusu wote wa dunia nzima".

Shaykh Jaadul Haq wa chuo kikuu cha Al-Azhar katika kitabu chake "Bayaanullinnas" J. 2 uk 203 - 204 ameandika yafuatayo juu ya kauli hiyo ya Imamun-Nawawy:

"Hapa Imamu An-Nawawy ametaja kwa mukhtasari kauli zilizomo katika madhehebu ya Kishaffi (juu ya kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu mengine ya Kiislamu. Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika maf ungu matatu makuu: "...Hapo Imamu An-Nawawy ametaja kwa mukhtasar kauli zilizomo katika madhehebu ya Shaffi (juu ya kuandama kwa mwezi) na ambazo pia zimo katika madhehebu nyengine za Kiislam. Kauli hizo tunaweza kuzigawa katika mafungu matatu makuu: Kauli ya kwanza: "Kila nchi iwe na matlai yake, wala muandamo wa nchi moja hautalazimu nchi nyengine ya mbali wala karibu". Kauli ya pili: "Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi zote za dunia hata kama ziko mbali".

Kauli ya tatu: "Muandamo wa nchi moja unalazimu nchi iliyo karibu nayo au inayowafikiana kimatlai". Kisha, Shaykh Jaadul-Haq akaendelea kusema kwamba:

"Na (kauli) zote hizo ni maoni yatokanayo na Ijtihaadi ambazo hazikusimama juu ya hoja kat-ii, si sanad wala matni. Kwa hivyo ingefaa ichaguliwe kauli ambayo inakubaliana na maslahi ya (Waislam wote wa) dunia nzima kwa jumla"."

Jawabu Sikubaliani na mtazamo wa Sheikh Shaykh Jaadul Haq wa chuo kikuu cha Al-Azhar, kwamba zote hizi ni rai na itihad kwani kanuni ni kuwa "Hakuna ijtihadi mbele ya andiko" Ijtihad mwahala mwake ni musimo andiko. Wakatika katika suala hili, utaona kwamba asemaye kuwa tufunge kwa muandamo mmoja, hoja yake ni Hadithi "Fungeni kwa kuuona"; na anayesema kuwa kila mahala na muandamo wake, anatoa ushahidi wake ni Hadithi ya Ibn Abbaas na Kuraib. Kwa hivyo, ijtihad ni katika kuyafahamu maandiko: si ijtihad kwa maana ya rai tupu pasi na andiko kama alivyosema Sheikh. Kilichobaki ni kuzijadili riwaya mbili hizi zina maana gani?

Munasema Tungependa kumueleza ndugu yetu kwamba hata hapa Afrika ya Mashariki jambo hili hakulianzisha Shaykh Naaswir Bachuu kama alivyodai mwenyewe (Nd. Juma) kwamba: (Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro)) Inasikitisha hakuweza kuangalia katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu uk 161-163 wametajwa walioonyesha kwa vizuri kabisa misimamo hiyo tofauti. Mashaykh wenyewe ni hawa wafuatao: Al-marhuum Shaykh Juma Abdul Waduud (wa Zanzibar), Shaykh Abdillahi Naaswir ( Nairobi Kenya ), na Shaykh Naaswir Khamis Abdul Rahman ( Mombasa Kenya ).

Jawabu Kwani wapi katika kitabu changu nilisema kuwa Sheikh Nassor Bchoo ndiye aliyeanzisha fikra hii hapo Afrika ya Mashariki hata mukaleta dai hili? Mimi nimeeleza kuwa zamani Afrika Mashariki watu wote wakifata muandamo mmoja. Nilisema: Karne zimepita bila ya sikio la Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro juu ya suala la muandamo wa mwezi. Harakati za elimu zilipobadilika na kuelekea zaidi - kwa kujua au bila kujua - katika mrengu wa Kihanbali na Kiwahabi, pakajitokeza mapinduzi ya ghafla ya fikra na matendo. Dr. Ramadhan Al-butti - miongoni mwa wanavyuoni wakubwa wa ulimwengu wa sasa - anaona kwamba harakati hizi hazisifiki kama ni madhehebu: bali ni hatua (phase) katika mapito ya Historia.

Na katika uk. 97, nimesema:

Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya. Kwa hivyo, ni wazi kwamba mimi nazungumzia Afrika Mashariki. Na mfano wa hilo pia kalisema Sheikh Nassor Bachoo, lakini yeye hamukumjibu. Anasema: "Pamoja na kuwa mgogoro wa kuandama kwa mwezi umeanza kuonekana hadharani katika jamii za Waislam wa hapa Afrika ya Mashariki katika miaka ya hivi karibuni". Inasikitisha kwamba hata maneno yangu mumeyakata na kuchukua yale ambayo hayakamilishi maana nilioilenga. Maneno "Karne zimepita" hamukuyataka kwani hayakufikisheni kule mutakako!

Pili narejea tena kusema kwamba hao wanavyuoni aliowataja Sheikh Nassor, hawajathibitisha habari za kuwa watu wafunge au wakifunga kwa muandamo mmoja Africa Masharik, ukimtoa Sheikh Nassir Khamis wa Mombasa ambaye naye pia ni mtu wa sasa. Ama sheikh Juma Abdu-Wadood yeye, kwa mujibu wa nakala hio ya Sheikh Nassor Bachoo, kasema hivi: Kuona huku kwa mwezi kumekusudiwa kuonekana na Waislam, na kuonekana na Waislamu huko, sio lazima kuonekana na Waislamu wote. Bali inatosha shahada ya mtu mmoja muadilifu".

Pia inampasa mtu mmoja pekee kama ameuona mwezi yeye afunge na kila aliyemuamini; hata akiwa haijakubaliwa shahada yake. Haya ndio maneno ya Sheikh Juma Abdu-Wadood kwa mujibu wa alivyomnukuu Sheikh Bachoo. Sasa ikiwa ndugu zetu mumeshindwa kuyafahamu maneno haya ya Sheikh Juma Abdu-Wadood, bado mutaendelea kupoteza watu bila ya elimu?! Sheikh Juma Abdul-Wadood hapa anazungumzia mas-ala ya ushahidi kwamba si lazima - katika suala la kuonekana kwa mwezi - kwamba kila mmoja auone: bali akiona mtu mmoja basi inatosha kwa wengine kufunga. Hii ndio kauli ya Sheikh Juma Abdul-Wadood na hili nimelieleza kwa urefu katika kitabu changu.

Kisha Sheikh Juma Abdul-Wadood akazungumzia suala la kufunga kwa muandamo mmoja akasema: "Rai za Maimamu wengine wameifasiri hadithi isemayo: (Fungeni kwa kuuona Mwezi) kwamba ukionekana popote mashariki au magharibi (watu) wafunge; hapana kutazama masafa fulani au nini. Hii ni rai nayo na wengi wamesema (hivyo) kama Imamu Malik , Ahmad na kundi kubwa la Hanafi. Inakurubia kuwa n dio rai ya Jamhuri - kufata rai hii ni kuhakikisha umoja wa dunia nzima. Wala hatuwezi kusema kwamba rai ya Shaffiy ndio ya Jamhur". Hapa Sheikh Juma anasimulia rai za Maimamu wengine: si rai za Maulamaa wa Afrika Mashariki. Mimi dai langu nililodai ni kuwa jambo hili la kufunga kwa muandamo mmoja, napenda munifahamu: ni jipya kwa Africa Mashariki. Mimi sikusudii jambo la wanazuoni kuzungumzia rai mbali mbali: bali nazungumzia jambo la watu kufata muandamo mmoja kwamba karne zimepita ya sikio la Muafrika Mashariki wa Kawaida halijiapata kusikia. Na nimetumia maneno "Muafrika wa Mashariki wa kawaida" ili kuwatoa wanavyuoni wao hata kama walikuwa hawafati kauli hio, lakini wanaijua. Kwa hali yoyote ile:

1) Sheikh Juma Abdul-Wadoo hajazungumzia kwamba Afrika Mashariki watu walikuwa wakifunga au wafunge kwa muandamo mmoja, bali kazungumzia rai za wanavyuoni wasio wa Afrika Mashariki - Al-Imamu Shafi, Hanbal n.k. Na mimi sijakanusha tafauti hizi.

2) Kauli yake ilikuwa ni kuhusu suala la mashahidi.

Ama Sheikh Abdillahi Nassir, yeye ni mwanachuoni wa sasa. Na mimi sijasema kuwa sasa hakuna rai hizo. Pili ni kuwa nakala alizotupa Sheikh Bachoo za kitabu cha Sheikh Abdillahi utaona kwamba Sheikh Abdillahi hazungumzii kuwa kauli ya kufatwa ni ile ya muandamo mmoja; bali yeye kasema kuwa hili ni suala la khilafu kwa hivyo tusigombane kila mtu afate rai anayoiona kuwa ni sawa. Sheikh Abdillah kayasema haya baada ya kutokea mizozo hii ya sasa. Kwa hivyo tunarudi pale pale kwamba "Karne zimepita bila ya sikio la Muafrika wa Mashariki wa kawaida kusikia sauti ya mgogoro juu ya suala la muandamo wa mwezi. Harakati za elimu zilipobadilika na kuelekea zaidi - kwa kujua au bila kujua - katika mrengu wa Kihanbali na Kiwahabi, pakajitokeza mapinduzi ya ghafla ya fikra na matendo". Kwa hivyo, nukta hii hamukuuijibu: na wala sioni kuwa kuna haja ya kuijibu kwani haina umuhimu katika maudhui yetu. Bali kitabu chenu chote, munachagua mambo yasio na umuhimu "Juma kantutukana; Juma kanfanya hivi" nyinyi ndio munajibu baada ya kuzungumzia dalili za kielimu.

Ama Sheikh Nassor: yeye pia ni mtu wa sasa na ni mfuasi wa skuli hio hio munayoifuata nyinyi, kwa hivyo kusema kwake alivyosema hakujapindua nilioyasema kuwa - kimatendo - hili ni suala jipya kwa kwetu Afrika ya Mashariki. Wala mimi sikusema kuwa Sheikh Nassor Bachoo ndiye muasisi wa fikra hio huko kwetu. Naomba munifahamu ninachokisema kwanza kisha ndio munijibu. Na sijui munapinga nini kitu ambacho watu wote wanakijua. Bila ya kusahau kwamba mimi sikusudii kusema kuwa kitu sahihi ni kilichofanywa zamani au kilichofanywa leo: laa! Bali kitu sahihi ni chenye ushahidi sahihi uliojengeka juu ya misingi sahihi ya kielimu. Na kielimu, suala la kuzingatia muandamo mmoja - hamutoweza kulithibitisha.

MNASEMA

Pia Shaykh Ahmad Al Khalil, Mufti wa Omani amethibitisha kwamba Ikhtilaf hii ya muandamo wa mwezi katika hukmu ya kufunga au kufungua ipo na kwamba ni jambo la kale. Kama alivyosema maneno yake yaliyotafsiriwa na Shaykh Muniir Sulayman 'Aziz kwamba: "Hakuna madhehebu iliyokuwa imesalimika na kuwa na Khitilafu baina ya Wanavyuoni wake juu ya suala la kutafautiana miandamo ya mwezi." Jee ndugu Juma anataka kusema kwamba Shaykh Naaswir Bachuu ndiye mwalimu aliyeanzisha madhehebu zote? Au ndiye aliyeanzisha mtafaruku huu kama alivyouita mwenyewe ndugu Juma?

JAWABU

Suala hilo jiulizeni wenyewe; mujijibu wenyewe; kwani nyinyi ndio mulioliunda: mimi sikusema hivyo kamwe bali nilichokisema ni hiki: "Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya". Nami sikusudii kusema kwamba upya huo ni katika kuzungunzwa au kusomwa suala hilo katika vitabu; nakusudia kimatendo sula hili lilikuwa halipo Afrika Mashariki. Sasa ili muwe mumenijibu, twambieni nani alikuwa akifata muandamo mmoja hapa Afrika Mashariki. Jamani! Tafuteni hoja mujadili: musijadili kitu kisichokuwa na umuhimu. Kama hamuna hoja nyamzeni musijitie aibu!

MNASEMA

Katika kudhihirisha udhaifu wake wa kumuandama mtu fulani; Ndugu Juma anasema: (Kama tunavyojua kwamba Sheikh Nassor Bachoo, ni mmoja wa wenye kusisitiza ulazima wa kuwa na muandamo mmoja.) Sisi kwa upande wetu tunasema: Katika kitabu cha Shaykh Naaswir Bachuu hakuna pahala alipolazimisha watu wafuate huo aliouita ndugu Juma (msimamo wa Shaykh Naaswir). Bali yeye ameonesha mitizamo ya Wanavyuoni kwa kutumia Aya za Qur-aan, Hadiythi na vitabu vinavyokubalika. Lugha aliyotumia Shaykh Naaswir katika huo unaonekana ni msimamo wake ni maneno yaliyozimuliwa kilugha (polite language) kama vile: (inawezekana) ((inaonyesha) .

JAWABU

Na mimi hapa sijasema kuwa Sheikh Nassir Bachoo kalazimisha watu wafunge kwa muandamo mmoja. Nimesema "Anasisitiza ulazima" yaani yeye analingania msimamo huo kwani kwake ndio msimamo sahihi na ndio wajibu kuufata. Naomba tena tuelewane musiseme kitu kinyume na nilivyosema. Wala musitafute kitu kisicho na maana mukajadili eti ndio jawabu! Pili maneno yenu: "Katika kudhihirisha udhaifu wake wa kumuandama mtu fulani". Sasa je na nyinyi pia munaonesha udhaifu huo huo kwa kumuandama mtu fulani katika kitabu chenu?

MNASEMA

Aliyelazimisha rai ni ndugu Juma mwenyewe kama anavyosema: (Lakini kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali) [uk. 112]

JAWABU

Bali hata Sheikh Bachoo pia kalazimisha kwani ukidai kuwa huu ndio msimamo wa haki au ndio msimamo sahihi au ndio wajibu kufatwa, bila kusema kuwa rai zote zinafaa basi na wewe huwa umelazimisha rai yako. Sasa je Sheikh Bachoo anakubali hivyo kuwa rai zote ni sawa? Mimi kweli sisemi kuwa rai zote ni sawa: nasema kuwa nyinyi mumekosea na sahihi ni kinyume na munavyofanya, na kwa hivyo bado nipo katika msimamo wangu huo huo kwamba: "Kilicho lazima na ambacho tunatakiwa tukubaliane ni kuwa muandamo wa mbali hautendewi kazi mbali".

MUNASEMA

"Kisha katika uk 85 ndugu Juma anataja kwamba msimamo huu wa muandamo mmoja kwa dunia nzima ni ((kitu kipya)) na kwamba jambo hilo halitekelezeki na ni kauli iliyobaki vitabuni tu baada ya kutaja baadhi ya nchi zinazofuata miandamo yao - yaani kila nchi na muandamo wake kama Al-yaman , Oman , Misri na Saudia. Kisha hapo hapo akataja: ((isipokuwa Imarati katika miaka ya mwisho wamekuwa wakifata Saudia.)) Inafaa ndugu Juma aulizwe masuala yafuatayo:

i) Kama ni jambo lisilotekelezeka vipi tena Imarat wanalitekeleza?

ii) Je hawa wa Imarat nao ni wanafunzi wa Shaykh Naaswir Bachuu?

iii) Kwani hiyo sio kauli ya Jamhuur ambayo ndio msimamo wa maimamu wakubwa wakiwemo Ahmad bin Hanbal, Malik na Abu Hanifa? (Angalia pia sehemu ya 11 na 13 za kitabu hiki)

JAWABU

Kwanza mumemefanya ghushi: maneno yangu hamukuyanukuu yote. Mimi nimesema: "Kwa kwetu - Afrika Mashariki - kusema kwamba mwezi muandamo wa nchi moja ni muandamo kwa nchi nyengine zote za dunia ni kitu kipya". Nyinyi maneno "Kwa kwetu Afrika Mashariki" mumeyatoa ili ionekane kuwa mimi nasema kuwa hili ni suala jipya kila pahala. Watu kama nyinyi vipi tutakuamini katika dini yenu na uadilifu wenu, ikiwa munaghushi maandiko hivi? Hii ndio kamati ya Msikiti Sunna na hii ndio suna yenyewe?! Halafu mukaendelea na tadlis (ghushi) yenu mukasema: "Na kwamba jambo hilo halitekelezeki na ni kauli iliyobaki vitabuni tu". Mimi sikusema hapa kuwa "Halitekelezeki", bali nimesema:

Lakini ukweli ni kuwa hata katika nchi nyengine zote za dunia taqriban kauli kwamba tufunge kwa muandamo mmoja, ni kauli ilioishia katika vitabu tu, kimatendo (practically) kauli hio haitumiwi isipokuwa na mtu mmoja mmoja. Hadi leo hii: watu Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao, Misr wanafata muandamo wao na nchi zote taqriban ni hivyo, isipokuwa Imarati katika miaka ya mwisho wamekuwa wakifata Saudia.

Haya nionesheni hapa maneno "Halitekelezeki". Mimi nimesema kuwa kimatendo kauli hii, hadi leo haitendewi kazi isipokuwa na baadhi ya watu. Nyinyi mumebadilisha na kuweka ghushi yenu mukasema nimesema halitekelezeki. Kwa hivyo, hilo Sula (a na b) jibuni wenyewe kwani mumesema kinyume na nilivyosema. Suala (d), najibu kuwa sio: hio si kauli ya jumhur bali jumhur kauli yao ni kinyume na hivyo na hili nimelithibitisha katika uk. 189-193 wa chapa ya pili ya kitabu changu au uk. 171 wa kitabu hicho chapa ya kwanza. Na Al-Imamu Malik riwaya zake zimegongana na riwaya kwamba kila watu na muandamo wao ndio ilio bora kwani ni riwaya ya Madina aliko kuweko Al-Imamu Malik, wakati riwaya nyengine ni ya watu wa Irak kulikokuwa na viwanda vya kutunga riwaya!

MNASEMA

Na sisi tunamuongezea habari moja ambayo ni vyema kuielewa, kwamba nchi ya Uganda iliyo katika Afrika ya Mashariki pia inafuata rasmi muandamo mmoja wa duniani. Pia aelewe kwamba huo msimamo wa kila nchi na mwezi wake huku Afrika ya Mashariki haukuwepo tokea zamani. Mashaykh wote wa huku wanakubaliana mwezi ukionekana popote katika nchi hizi tatu ( Kenya , Uganda na Tanzania ) wanafunga pamoja. Yeye anaendelea kushika msimamo wake: (Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao). Lile analoliona yeye halitekelezeki, basi ndio linatekelezeka.

JAWABU

1) Kitu rasmi Uganda hakizingatiwi kwani Uganda kimsingi sin chi ya Kiislamu wala ya Waislamu: Waislamu ni wachache ukilinganisha na Wasio Waislamu. Kwa hivyo, hakuna kitu rasmi. Na jambo hilo ni jambo la sasa. Na mimi sijapinga kwamba sasa fikra hio ipo Afrika Mashariki.

2) Ama kauli yenu: "Mashaykh wote wa huku wanakubaliana mwezi ukionekana popote katika nchi hizi tatu ( Kenya , Uganda na Tanzania ) wanafunga pamoja". Ndio maana nikatumia lafdhi "Kwa kwetu Afrika Mashariki" nikijua kuwa wanavyuoni wote wa kwetu Afrika Mashariki wana msimamo huo. Ama kauli yenu: "Yeye anaendelea kushika msimamo wake: ((Al-yaman wanafata muandamo wao, Oman wanafata muandamo wao, Saudia wanafata muandamo wao,)). Lile analoliona yeye halitekelezeki, basi ndio linatekelezeka". Mwisho wa kunukuu. Inaonesha kuwa kitabu changu mumekijibu bila ya kukifahamu. Nilichosema ni kuwa, ijtihadi ifanywe katika kubainisha wapi hadi wapi watu wafunge pamoja. Kwa vile, hakuna andiko lililobainisha hivyo. Ama muandamo mmoja kwa dunia nzima hili ni kinyume na andiko. Kwa hivyo, wakiwa wanavyuoni wa zamani wamefanya ijtihad hio, sisi tunafata ijtihad yao kwa vile hapa ni mahala pa ijtihad na haikugongana na andiko. Ama madai yenu nyinyi ni kinyume na andiko lilivyoonesha.

MNASEMA

"Kuna suala moja la nyongeza tunapenda tumuulize ndugu yetu Juma: Hata kama hizo nchi alizozitaja ( Al-Yaman , Oman , Misri na Saudia) hazijakubaliana kufuata muandamo mmoja, je hakuna uwezekano (japo wa sadfa) unaoweza kutokea kufunga siku moja ijapokuwa kila mmoja ameona mwezi katika nchi yake? Sasa tuseme kila nchi katika hizo imeona mwezi usiku wa Alkhamisi kuamkia Ijumaa - Wote si watafunga siku moja ya Ijumaa? Basi huo ndio utekelezaji aliosema hautekelezeki. Ni wazi kuwa unatekelezeka.

JAWABU

Munaendelea kuuliza masula haya kwa sababu masuala yenu mumeyajenga katika kitu nisichokisema kamwe. Wapi nimesema kuwa "Hilo halitekezeki" hata mukauliza masuala haya?