• Anza
  • Iliyopita
  • 5 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 4995 / Pakua: 2059
Kiwango Kiwango Kiwango
WAJIBU WA VIJANA

WAJIBU WA VIJANA

Mwandishi:
Swahili

2

WAJIBU WA VIJANA

MAPAMBANO DHIDI YA UJINGA NA UPOTEVU

Ili kupambana na hali hii mbaya yenye kusikitisha unaoishi umma wetu wa Kiislamu, panahitajika sana kuwepo moyo wa kimapinduzi na moyo wa kutaka kuleta mabadiliko na kuwa na msimamo wa kukataa na kupinga utaghuti (udhalimu). Serikali za kidikteta na za kidhalimu zinaendelea kuzitwisha tawala zao kwa mataifa yetu manyonge na zinayatawala kwa siasa yao ya kikoloni na kwa kutumia njama za mataifa makubwa. Vilevile fikra za zamani zilizoyaweka nyuma mataifa bado zingalimo ndani mwa akili za viongozi wetu na wakuu wetu wa kidini na kijamii, na wakiwa katika wao wako katika hali kama hi wanauongoza umma wetu.

Nazo ada mbaya pamoja na mienendo iliyo chakaa ingali inazidi kuleta matatizo na vikwazo katika umma wetu. Kubakia nyuma katika maendeleo kunazidi, na udikteta unaotawala umetia fora. Haya ndiyo maisha tunayoishi kila siku na ndiyo hali iliyoenea katika umma wetu. Sasa imebakia tujiulize: Ni nini msimamo wa umma wetu juu ya kuishi katika hali kama hii na maisha kama haya? Hali ambayo inachoma mioyo yetu na kutuudhi? Hakika ile roho ya kimapinduzi ya kutaka mabadiliko na kukataa kudhalilishwa iliyokuwemo ndani mwa nafsi za umma wetu imeyeyuka kabisa. Msimamo wa kupinga ufisadi pia umetoweka. Nafsi zilizothubutu kupinga zimekosekana. Mioyo yenye ghera na kaa lenye kuwasha utambi wa upinzani limezimika. Kila mmoja wetu amekuwa akipuuza kila jambo isipokuwa yale mambo yanayohusiana na maisha yake tu. Hafikiri kitu isipokuwa mambo yanayohusiana na maslahi yake ya kibinafsi. Ama kufikiria hali ya umma au hali ya muundo wake wa kisiasa na kiuchumi, hayo yote ni mambo ambayo fikra yake haimpi nafasi kuya fikiria, wala hamu yake haiyapi umuhimu wowote.

Hadi hivi sasa tungali tumebakia twaishi katika hali hi ya kupooza na kukosa thamani. Yawezekana watu wabadilike na mambo pia kubadilika na yakawa mengine, lakini hali yetu itabakia kuwa ni ileile ya ujinga, upotevu, kubakia nyuma katika elimu na uchumi na kutengwa kwenye uongozi wa nchi yetu. Tutabakia katika hali ileile ya kupomoka na kuwa katika dhiki na mateso. Tutabakia katika maisha haya na hali hii hadi pale roho ya kutaka mapinduzi na mabadiliko itakapozaliwa upya ndani mwa nafsi zetu na mioyo yetu, na pale hisia za upinzani zitakapojumuika kwa wingi na tushughulike na misimamo ya kupinga na kukataa hii hali yetu ya kubakia nyuma katika maendeleo yanayoenea. Mwenyezi Mungu Mtukufu asema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ﴿١١﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu h a yabadili yale yalioko kwo kaumu (watu) hadi (wao) wabadili yale yaliyomo nafsini mwao." (13:11).

Ikiwa tunaitamani roho hii ya kimapinduzi na tunataka kumiliki mioyo yenye kukataa na kupinga, basi katika kipindi cha ubarobaro ziko mbegu zilizo hai kabisa, na iko hali ya kimaumbile kabisa inayokubaliana kutekeleza matakwa haya. Na huu ndio wakati unaotakikana kwenda mbio kuitafuta roho kama hii.

Na hii ni kutokana na sababu zifuatazo:

Kwanza : Kijana huhisi kuwa na nguvu nafsini na viungoni mwake baada ya kuwa alikuwa akiishi katika hali ya udhaifu alipokuwa mdogo. Kutokana na sababu hii hujiona ana jukumu Ia kupinga na kukataa.

Pili : Tukimzingatia kwa makini tutamkuta kwamba kijana huanza maisha yake yungali hajavaana nayo bado wala hana pupa nayo kama wanavyoyapupia watu wakubwa, bali inakuwa kinyume chake, yeye hupendelea kujitosa kwenye ukinzani na kukabiliana na hatari. Haya ndiyo yanayostahiki kuigwa na nafsi inayotaka kumiliki roho ya kutaka mapinduzi na kukataa.

Tatu : Kijana hana fungamano na maisha haya ya dunia wala hajaonja ladha zake zenye kumfanya aipondokee. Na hii ni kutokana na muda mfupi aliyoishi hapa duniani na kwa sababu ya kutokuwepo maslahi mengi yenye kumvuta zaidi kuyapenda maisha haya. Ni tabia ya binadamu kwamba anapoishi katika hali maalum kwa muda mrefu na maslahi yake yakawa mengi katika hali kama hiyo, huwa inakuwa vigumu kwake kufikiria kuibadili hali kama hiyo au maisha kama hayo, bali mara nyingine hupatwa na babaiko pakiwepo matara jio ya kupatikana mabadiliko. (Kwa mfano, Jean Jacques Rousseau alikuwa akiona hali kama hiyo kwa ufalme wa Kifaransa. Yasemekana alikuwa akisema kwamba alikuwa akipatwa na babaiko kutokana na kuisawiri Ufaransa ikijiendeleza bila ya kuwa na mfalme, juu ya kuwa alikuwa ni miongoni mwa wanafikra na wanafalsafa wakubwa waliowaita watu katika kuendeleza hali ya kisiasa wakati ule. Hii ni kwa sababu Rousseau alikulia katika chombo cha utawala wa kifalme na kuvuta hewa yake kwa muda wote wa maisha yake).

Vivi hivi utaona kwamba kundi Ia vijana ndilo kundi ambalo linaelekea zaidi kuwa na roho ya kutaka mapinduzi na kuleta mabadiliko, na wao ndio watu ambao wako tayari kabisa kuleta upinzani na kukataa ufisadi na dhuluma. Ushahidi mkubwa ni hizi hoja zifuatazo: Tume zote zilizotoka mbinguni, mapinduzi yote ya kijamii yaliyofanyika yamefaidika na vijana. Vijana walitegemewa kama viongozi wa kuleta mabadiliko na kuwa kama nguzo ya kuyaendeleza mapinduzi. Ama katika jamii zetu za Kiislamu kuna kosa kubwa linalotendeka katika kuamiliana na vijana wetu wanaokulia. Badala ya wao kuzikuza na kuziogoza roho zao ya kutaka mapinduzi na mabadiliko waliyonayo, vilevile badala ya kuiongoza roho ya kupondokea kwao katika upinzani, kuupinga ujinga ulioenea na upotevu uliotawala, sisi hufanya kila juhudi kuiua roho hii ya kimapinduzi iliyomo ndani mwa nafsi za vijana wetu. Pia huziua hamasa zao zilizowaka moyoni mwao ambazo ziko tayari kupambana na hali kama hizi. Mara nyingine utaona tunashughulika zaidi katika kutafuta njia za kuwakinaisha na kuwafanya wasalimu amri na kutii hii miweko ya ufisadi na kukubali kufuata hii miongozo michafu kwa njia za kuwavunja mioyo na kuzirudisha nyuma azima walizonazo na kuwakatisha tamaa nafsini mwao. Wakati huu tunapotumia hila za kuwakinaisha mabarobaro, huwa tunatumia kila mbinu na kila njia hata ikiwa ni kwa kuyapotoa baadhi ya mafunzo ya Kiislamu ili tu tuwakinaishe vijana wetu wasiweze kupinga au kukataa lolote analoambiwa.

Miongoni mwa tashwishi za kuvunja moyo ni ile itikadi ya taqiya (ufichaji wa imani), eti taqiya ni wajibu wa kisheria inayomruhusu mtu amnyamazie au amnyenyekee dhalimu yeyote anayetawala umma kwa dhuluma na maonevu!! Eti kupambana ni kuiingiza nafsi kwenye maangamivu, na kufanya huko ni haramu katika sheria yetu ya Kiislamu!! Eti kufanya mapinduzi au kuleta aina yoyote ya mabadiliko kunahitaji fatwa ya mujtahidi (mufti) ambaye haoni kuwepo maslahi kwa dini kwa hivi sasa kutoa fatwa!! Eti fursa ya kufanya mapinduzi imepita kitambo, na ni wajibu kwa waumini kwa hivi sasa kungojea kudhihiri kwa Imam Mahdi!! Hebu tafakari kidogo. Je, haya mafundisho na fikra hizi zisizo nyofu na zenye kupinga mapinduzi zinakubaliwa na vijana wetu wote? Vijana wanaotaka kuleta mabadiliko, waliojaa hamasa, walio na matumaini ya kuasi udhalimu na walio na lengo Ia kuhakikisha kupatikana mapinduzi watakubali fikra hizo?

La hasha!! Umma wetu na watu wetu wana akili imara zilizo madhubuti ambazo hufikiria na kuyapima mambo yanayotolewa na fikra hizi na mafunzo haya. Ndiyo, yawezekana wapatikane baadhi ya vijana ambao watahadaika na kukubaliana na hali hii ya ufisadi. Kisha wajiondoe kwenye mkondo wa kutaka mapinduzi ambapo utawakuta wengine wanaitafuta njia ya mapinduzi popote ilipo ili waiandame hadi wahakikishe kwamba lengo lao Ia kuleta mabadiliko limepatikana. Hii ndiyo fursa wanayoipatiliza makundi ya upinzani na ndiyo nafasi inayopatilizwa na watu wenye hila za kikoloni ili wawawinde vijana wetu kwa jina Ia kuleta mabadiliko na maendeleo chini ya wito wa kupinga na kukataa. Wakati ambapo kijana anapoona njia mbili mbele yake: njia inayomwamuru kutii na kunyenyekea upotevu na utaghuti (udhalimu) (kama wanavyoiona baadhi ya wapingamaendeleo), na njia inayomshajiisha kufanya mapinduzi na kumtia moyo wa kuleta maendeleo na mabadiliko - ni dhahiri na ni kawaida kwamba vijana wengi watafuata njia ya pili, kwa sababu njia hiyo inakubaliana zaidi na tabia yao na maumbile yao ya kutaka mabadiliko. Vilevile njia hi inachukuana na maumbile yao ya kutaka mabadiliko na inaafikiana na maumbile ya mwanadamu ya kutokata tamaa na kuwa na moyo wa matumaini usiokuwa na kifani.

Kwa hakika, tukizingatia, tutaona kwamba dhati au umbile Ia Uislamu ni mapinduzi, linapinga kubakia nyuma na linakataa dhuluma na upotevu. Tamko Ia KiisIamu Ia Laa ilaaha illa-Ilah (Hapana mungu mwingine anayeabudiwa ila Allah tu) linamaanisha kuwakufuru na kuwakataa waungu wote wa udikteta na upotevu. Mafunzo ya Kiislamu yamemfaradhia kila binadamu aliyeukubali Uislamu kupambana na dhuluma, kukomesha ufisadi na ubatilifu, kukataa ujeuri na upotovu, na kuukomesha kabisa. Lau sisi twasimama kwa nia safi na kufundisha Uislamu halisi kwa vijana wetu pamoja na kuyaejezea mafunzo yake ya kimapinduzi na misingi yake ya kuleta mabadiliko, basi vijana wetu wangekuwa walinganifu, wenye nia safi ya kuuhudumia Uislamu, na wangekuwa wanamapinduzi wenye kupambana kwa ajili ya kuuhuisha Uislamu na kuujenga umma wenye imani na wenye kuiongoza dunia.

Barobaro na Kujitolea katika Njia ya Mwenyezi Mungu Njia ya Mwenyezi Mungu ni njia ya haki, uadilifu na uhuru. Kuitumikia njia ya Mwenyezi Mungu ni kushughulika katika kuitekeleza haki, kuiandama na kuhakikisha kwamba uadilifu uko juu na uhuru uko kwa wote. Matukio ya tarekhe (historia) na mazingira ya maisha yametufundisha na kututhibitishia kwamba haki, uadilifu na uhuru haviwezi kupatikana ila kwa njia ya kupambana na kujitoa mhanga. Umma ule unaomiliki roho yakujitolea, kujitoa mhanga na njia ya mapambano na mapigano unastahiki kupata uadilifu na uhuru ili ufikie anga Ia kuvuta hewa iliyojaa haki na usawa. Ama umma ulio bahili na mwoga, jazaa yake ni kutawaliwa na tawala za kibatili, kidikteta, na kidhalimu ambazo zakandamiza umma na kuutia utumwani. Na wale wanaongojea uadilifu na uhuru usimame na kuenea kila pahali kwa kuomba dua misikitini, kumnyenyekea Mwenyezi Mungu, kutamani au kutumaini tu bila ya kusimama na kuyahakikisha hayo kwa vitendo, hao ni juu yao kuzidi kungojea dhuluma, maonevu, madharau, vitisho, n.k.

Uadilifu ni njia ambayo haimkiniki kuifikia ila kwa kulendea; uhuru wenye thamani haumkiniki kupata ila kwa kuilipia. Njia ya kupata haki na uadilifu ni mapambano tu. Thamani ya kupata uhuru ni kujitoa mhanga, kujitetea na kuinyakua haki hiyo kwa nguvu. Mtume Mtukufu amesema: "Kheri yote iko upangani. Hakuna kinachowanyorosha watu isipokuwa upanga, na upanga ndio vishikilio vya Pepo." Naye Amirul Mu'miniyn Ali bin Abu Talib akiwatahadharisha wale wanaopenda kujiweka nyuma kuuacha mkondo wa kujitoa mhanga na kujitolea kusaidia na wanaojitenga na kuiacha njia ya mapambano na kujikomboa, alisema: "Jihadi ni mlango miongoni mwa milango ya Peponi. Mwenyezi Mungu ameifungua kwa wale mawalli Wake mahususi. Ni nguo ya uchaji Mungu, deraya ya Mwenyezi Mungu iliyo na hifadhi, na ni Pepo Yake iliyoimarishwa na inayotegemewa. Mwenye kuiacha (jihadi) kwa ajili ya kuichukia, Mwenyezi Mungu atamvika nguo ya udhalilifu na balaa itamwenea, na atadhalilika kwa madogo na matwevu. "

Vijana wa umma ndlo walio na uwezo zaidi wa kupambana na kujitoa mhanga. Umbile lao na tabia yao wanayokuwa nayo katika kipindi hiki cha ujana huwavuta zaidi na kuwapambia kujiingiza kwenye mambo ya hatari bila ya kuyajali maisha, kwa sababu za kinafsi tulizotangulia kuzielezea katika faslu zilizotangulia. Kwa hivyo, ni juu yetu kuihifadhi hii tabia iliyoko kwa wingi nafsini mwa vijana wetu. Tujibidiishe kuwaongoza kwenye njia ya kujitolea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, yaani katika njia ya kuhakikisha kuisimamisha haki, kuusimamisha uadilifu na kuulinda uhuru. La sivyo, umbile hili laweza kuelekezwa katika upande uliopotoka, na wakati huo kutapatikana vikundi vya vitisho na mapote yenye kuleta uharibifu na upotevu. Vipote hivyo vitakuwa na tabia ya kuilingiza kwenye ufisadi bila ya kujali, au vijana wetu watalelewa na makundi mengine maovu yaliyo kinyume chetu na kuwafanya wawe ndizo kuni za kuidumisha mipango yao ya uadui, au madaraja yao ya kuwavusha na kuwafikisha kwenye matakwa yao ya kikoloni.

Mafunzo ya Kiislamu Yazinduayo Ndiyo Yanayotakikana Zaidi Fikra huzinduka na kuamka. Bongo hufunguka na alama za kuuliza huanza kuambata fikrani mwa vijana chipukizi. Maswali mengi humjia akilini mwake. Mimi ni nani? Kwa nini nimekuja ulimwenguni? Ni nani aliyeniumba na kunipa uhai? Ni mwisho gani unaonisubiri ambao utakomesha maisha yangu? Ni nini msimamo wangu katika jamii ninayoishi nayo? Maswali kama haya na makumi mfano wake huchoreka ndani mwa akili ya kijana chipukizi na hubakia katika hali hii yakitafuta majibu ya maswali hayo ambayo yatapoza na kukinaisha moyo wake. Hi ni kwa sababu kijana huishi katika hali ya upungufu wa fikra na ni punde tu ambapo bongo lake hufunguka na kuanza kuyafikiria mambo haya kwa makini. Hi ndiyo fursa inayopatilizwa na makundi yaliyopotoka, yanayoingilia wakati kama huu ili kusimamia uandalizi wa fikra ya kijana kwa miongozo iliyopotoka ambayo hutayarishwa kwa ustadi na kwa lengo Ia kutupiga sisi wenyewe. Makundi haya huijaza fikra ya kijana kwa kumpa jawabu zenye upotevu ambazo si za haki katika kuyajibu maswali yake yaliyomo akilini na mawazoni mwake. Kutokana na sababu kama hizi ndiyo utaona kwamba mafunzo ya viongozi wa kidini yanatilia mkazo na kututanabahisha juu ya hatari ya kipindi hiki cha ujana kwa upande huu. Mafunzo hayo na riwaya hizo zinawakumbusha wazazi, viongozi na wanavyuoni wa jamii yetu umuhimu wa kufanya haraka kupatiliza kuwaelimisha watoto na vijana na kuijaza faragha ya kifikra kwa itikadi sahihi za Kiislamu na kwa mafunzo yake yaliyo salama.

Uislamu unazingatia kwamba kumwelimisha mtoto ni haki mojawapo miongoni mwa haki za mzazi kwa mwanawe. Baba wa mtoto akiacha kutoa haki hiyo, basi Mwenyezi Mungu atamhoji na kumwuliza, na ikiwa atapatikana na makosa basi Mwenyezi Mungu hatasita kumtesa siku hiyo ya Kiyama. Imam Ali bin Husayn Zaynul Abidiyn AS amesema: "Ama haki ya mwanao, ujue kwamba yeye atokana nawe, na Akhera atawekwa nawe pamoja na kheri na shari zake. Nawe utaulizwa juu ya yote uliyomfunza katika adabu nzuri na katika kumthibitishia (Uungu wa) Mola wake Mwenyezi na Mtukufu na kumsaidia katika kumtii Mwenyezi Mungu. Basi mfanyie mwanao matendo mazuri na jueni kwamba mtalipwa thawabu kwa kumfanyia vizuri na mtateswa kwa kumfanyia maovu." Ali bin Abu Talib AS ameitaja hali ya faragha ambayo kijana anayekulia huishi nayo. Ameitaja kwa kuashiria kwamba ni miongoni mwa sababu zinazomwandaa kukubali fikra yoyote anayoelezwa. Akasema: "Hakika moyo wa kijana ni kama ardhi isiyokuwa na kitu (isiyolimwa), chochote kinachoingizwa (kinachopandwa) hukikubali."

Imam Ja'far Sadiq(a.s) anasisitiza kuharakisha kuelimishwa vijana wanaokulia ili kuwafutisha fursa mirengo iliyopotoka na kuwakinga kutokana na misingi inayobomoa. Alisema: "Wapatilizeni watoto wenu wadogo kwa kuwafunza Qur'ani na Hadithi kabla hamjatanguliwa na wapingamaendeleo. " Wapingamaendeleo (marjaiyyah) ni kundi lililokuwa na fikra zilizopotoka katika jamii ya Kiislamu katika zama hizo. Leo katika zama zetu hizi tunaposhuhudia jinsi mawimbi ya upotevu yanavyoleta uharibifu na yanavyouweka Uislamu mbali na wengi wa vijana na mabarobaro wetu, na jinsi yanavyowavuta na kuwakumba vijana wetu waliozama katika malezi ya Mashariki na Magharibi, huwa hatuna budi ili kufikiria kwa makini misingi ya matatizo hayo na chanzo chake ili tuweze kupambana na haya mawimbi ya upotofu ambayo yanahatarisha kwa kiwango kikubwa hali ya usoni ya umma wetu na ujumbe wa Kiislamu.

Si sahihi wala si kweli kwamba yote haya waliyonayo vijana wetu yanasababishwa na ubaya na uovu ambao uko ndani mwa nafsi zao. Vivyo hivyo, haifai kuzikubali fikra zilizochakaa za hao viongozi wapingamaendeleo ambao wanayafasiri haya yote yanayotokea na kutendeka kwamba hayana bud yatokee. Wana dalili kwamba ni lazima ufisadi udhihiri katika bara na bahari na ujeuri na dhuluma uenee ulimwenguni kote. Vivyo hivyo, wanasema kwamba haimkiniki kuyazuia yale yaliyokadiriwa na yaliyojaaliwa na historia. Kwa jumla, udhaifu wa vijana wetu wa kutopendelea dini na kutoshikamana na mafunzo yake na badala yake kushikamana na mafunzo maharibifu yaliyoingizwa kutoka nje, unatokana na sababu maalum zinazotokana na hali yetu ya kubakia nyuma katika maendeleo ya kila aina. Sisi tuna jukumu mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya historia katika suala Ia kupotea umma wetu ujao. Kwa sababu sisi ndio chanzo cha kupotea kwao na kwenda kombo. Kutokana na hali ya kujibakiza kwetu nyuma, kuacha kuwaongoza na kutojali kuwaelimisha hadi kufikia kiwango sahihi kinachostahili na kinachotakikana.

Uislamu Uliopotoshwa Miongoni mwa misingi muhimu na sababu zilizowasababisha vijana wetu kuyatoroka mafunzo ya dini yao ni hii hali ya Uislamu uliopotoshwa katika umma wetu wa kila mahali. Kijana anapofumbua macho yake na kuiona jamii yake jinsi iliyotanikatanika katika mila, desturi na tabia, ilivyorudi nyuma katika elimu na maendeleo kadha wa kadha, ilivyotawaliwa na ubinafsi na ukabaiIa na badala yake kuthamini utabaka na dhuluma, au atakapoiona jamii hiyo ikiwa na fikra finyu na huko hayo yote hutendwa kwa jina Ia Uislamu na katika vazi Ia kidini, basi huchukulia kwamba yule mtawala au kiongozi hutawala kwa jina Ia Uislamu. Vilevile hudhania kwamba kilichosababisha watu kubakia nyuma ni mfumo wa Kiislamu. Kwa kawaida, zile fikra za wale viongozi wapingamaendeleo zilizoganda hushikilia nafasi ya fikra za wanavyuoni halisi wa Kiislamu. Zile fikra ambazo hazikushikamana na mafunzo halisi ya KiisIamu na zilizojaa mafunzo ya woga na kupokonya moyo wa ushujaa, ndizo ambazo zinatangulizwa mbele ya watu ili zionyeshwe kama mafunzo sahihi ya Kiislamu.

Maadamu Uislamu unaonyeshwa na kufundishwa kwa mabarobaro wetu kwa sura kama hii iIiyochushwa ambayo inaonyesha kwamba ndilo chimbuko halisi lililosababisha umma kubakia nyuma, basi utakuwaje msimamo wa hao vijana wetu kuihusu dini hii? Hapana shaka kwamba watautoroka Uislamu huu na kuyakataa mafunzo yake, na badala yake watatafuta njia nyingine waifuate ili waweze kuleta mabadiliko ndani ya umma, mabadiliko ambayo watayatarajia kulendeleza jamii yao. Maisha haya ya kubaki nyuma, kuishi kwa jina na vazi Ia Kiislamu na kushikilia fikra hizo za kutotaka kuleta mabadiliko ambayo yanatoa picha iliyochafuliwa ya maendeleo ya Kiislamu, ndiyo sababu muhimu iliyowafanya vijana hao wanaokulia kuacha kushikamana na dini yao ya Kiislamu.

Wanajua Nini katika Dini ya Kiislamu? Kabla hatujatoa mawaidha ya kuwashambulia, kuwakufurisha na kuwafanya mafasiki vijana wetu, ni wajibu juu yetu kujiuliza wenyewe: Je, tumejaribu kuueleza Uislamu na kuwafunza kisha wao wakaukataa? Jawabu ni la. Aghlabu ya vijana hawajui chochote katika mafunzo ya mfumo na misingi ya Kiislamu.Taaluma zote zilizokuwa zikifunzwa katika jamii zetu za Kiislamu, hazikukeuka hukumu za shaka katika masiala ya hedhi, nifasi, n.k. ambayo ni miongoni mwa mafunzo ya kifiqihi na kiibada. Ama kwa upande wa fikra, uchumi, siasa au elimujamii ya Kiislamu, mafunzo haya muhimu hayakupatikana ila kwa uchache. Vijana wetu hawakuweza kuyapata mafunzo namna hii kwa urahisi. Je, haya yote si kweli? Katika hali kama hii ambapo kumeenezwa kasumba ya kila aina ya kupotosha na propaganda zinazotangazwa na mashirika pamoja na makundi mbalimbali potofu, tunataraji nini kwao? Wengi wa vijana walioyaepuka mafunzo ya dini na kuacha kushikamana na sheria zake walifanya hivyo kutokana na kutoujua kwao Uislamu, kutojua umbile lake tukufu na umuhimu wake. Nasi tujue kwamba Mwenyezi Mungu atatuuliza kuhusu huu upungufu tulioufanya wa kutowafunza vijana wetu Uislamu halisi na kuwapa misingi ya mafunzo yake bora.

Vipi Tuifundishe Dini? Mfalme aliota ndoto iliyomfadhaisha sana. Akaamka akiwa na fadhaa na hali ya kuingiwa na hofu. Akamwita mfasiri ndoto na kumwelezea yote aliyoyaona ndotoni. Akasema: "Nimeona meno yangu yakidondoka moja baada ya jingine. Hebu niambie maana yake ni nini?" Mfasiri ndoto akainamisha kichwa kwa muda mfupi huku akifikiria, kisha akainua kichwa chake na kusema kwamba aliyoyaona yatakuwa kweli, na maana yake ni kuwa watu wote wa familia yake (mfalme) watakufa katika wakati wa uhai wake.

Tafsiri hi kavu yenye kisirani na fali mbaya ilimkasirisha mfalme na kumtia hofu. Kwa hivyo, akaamuru mtaalamu huyo auawe mara moja. Kisha akaamuru aletwe mfasiri ndoto mwingine; na akaletwa haraka mbele yake. Mfalme akamwelezea ndoto ileile; naye mfasiri ndoto akamjibu jawabu kama ile iliyotolewa na mfasiri ndoto wa kwanza, kwamba watu wa nyumbani kwake watakufa katika wakati wa uhai wake. Jawabu hii pia haikumridhisha, na akaamrisha tena auawe. Wakamletea mfasiri ndoto wa tatu. Tena mfalme akamwelezea ile ndoto kwamba ameyaona meno yake yaking'oka moja likifuatiwa na jingine. Mfasiri ndoto huyo akamsikiliza kwa makini kisha akainamisha kichwa kufikiri; na baada ya muda kupita katika kuwaza na kuzingatia, akasema: "Ikiwa yale uliyoyaona ni kweli, basi wewe utakuwa mtu mwenye umri mrefu zaidi katika familia yako, inshaallah." Jawabu hii iliufanya moyo wa mfalme kukunjuka na uso wake ukaonyesha furaha na kuondokewa na dhiki kutokana na tafsiri hiyo nzuri. Hivyo, akaamuru mfasiri ndoto apewe zawadi yenye thamani.

Msomaji mtukufu hebu zingatia kisa hiki. Je, unaona tofauti yoyote katika maana baina ya tafsiri hizo mbili? Ukweli ni kwamba hapana hitilafu. Zote mbili zinathibitisha hakika moja tu, nayo ni kuwa mfalme atabakia baada ya kuwakosa (kufa) watu wake wote. Basi kwa nini msimamo wa mfalme ulitofautiana mbele ya wafasiri ndoto hadi akaamuru wale wawili wa awali wauawe, na wa mwisho apewe zawadi? Ukizingatia utaona kwamba siri kubwa mefichika katika nija iliyotumika kueleza, kwani hakika ni ileile moja haikubadilika, lakini mara ya kwanza ilielezwa kwa njia inayoleta kisirani na kutisha, na mara ya pili ilielezwa kwa njia iliyojaa bishara, fali njema na furaha. Mbinu ya Kuelezea ni Muhimu Sana Katika kisa hicho imetudhihirikia wazi umuhimu wa mbinu ya kulielezea jambo lolote lile na umuhimu wake katika kuhadidisha msimamo wa watu kutokana na jambo lililoelezwa. Hata ikiwa jambo moja ni la kweli lakini ikawa halikuelezwa kwa mbinu nzuri, basi hakuna dhamana kwamba watu watalikubali jambo hilo. Vivyo hivyo, ikiwa jambo jingine ni la batili lakini kukatumika mbinu nzuri katika kulielezea, basi huenda watu wengi wakahadaika na kulifuata. Hivi sasa tunashuhudia vile hali ya watu kuelekea katika dini na kule kupungua katika kushikamana nayo. Tutaweza vipi kuwavuta na kuwaelekeza kwenye dini yao na kuwaelimisha ujumbe wao mtakatifu?

Ninaitakidi kwamba ni dharura mno kufikiria njia na mbinu nzuri ya kulelezea dini kwa watu. Wabalighi (wanatablighi) wengi na wanavyuoni hawajafaulu katika kuchagua ile mbinu nzuri, na kutokana na sababu hi hawakuafikiwa kufaulu katika shughuli zao, bali mara nyingine matokeo yake huwa kinyume chake na mara nyingine hutokea kwa baadhi yao upinzani na chuki ambavyo husababisha kuitoroka dini. Qur'ani Tukufu inatuzindua juu ya umuhimu wa jambo hili katika kulingania Uislamu. Inasisitiza juu ya kutumia mbinu nzuri katika tablighi. Inasema:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ﴿١٢٥﴾

"Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa lile ambalo ni zuri." (16:125).

Pia Qur'ani yatuzungumzia kuhusu maadili (akhlaki) ya Mtume Mtukufu na taathira yake katika kuwavuta watu katika dini. Inasema:

وَلَوْ كُنتَ فَظًّا غَلِيظَ الْقَلْبِ لَانفَضُّوا مِنْ حَوْلِكَ ﴿١٥٩﴾

"Na lau ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu wangetawanyikatawanyika pembezoni mwako." (3:159).