• Anza
  • Iliyopita
  • 3 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 1577 / Pakua: 505
Kiwango Kiwango Kiwango
PAMOJA NA MITUME KATIKA NJIA YA MASHAKA

PAMOJA NA MITUME KATIKA NJIA YA MASHAKA

Mwandishi:
Swahili

PAMOJA NA MITUME KATIKA NJIA YA MASHAKA

MTUNGAJI: SAYYID MUHAMMAD TAQI MUDARRISI

MFASIRI: HASSAN A MWALUPA

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Mpenzi msomaji! Assalaamu alaykum wa rahmatullahi wa barakaatuh! Je, imetokea siku moja kuwa na shaka na ukahisi upweke katika njia ya haki kwa sababu ya uchache wa wafuasi wake? Je, umejikuta siku moja uko peke yako katika uwanja wa mapambano? Je, umewahi kuzunguka huku na huko ukimtafuta mtu atakayekusaidia kutatua matatizo ya maisha na njia yake ngumu? Je, umewahi siku moja kuhitajia akiba ya chakula kwa ajili ya safari ya maisha ya mashaka? Je, yamekutokea yote hayo?

Sitangoja jibu kutoka kwako! Kwan i jibu la watu wote litakuwa moja tu, nalo ni: "Ndiyo. Mambo hayo yote yametufika." Ndugu yangu Mwislamu! Hakika hukuwa peke yako katika njia iliyokupwekesha; wametangulia katika njia hiyo Mitume watukufu, wanaharakati na wanamapinduzi wa mwanzoni. Hakika hukuwa peke yako katika uwanja wa mapambano uliosimama kuutetea Uislamu na itikadi za Waislamu, bali walitangulia mawalii na watu wema katika uwanja huohuo na mahali hapohapo ambapo ulisimama kwa lengo hilohilo na matumaini hayohayo uliyokuwa nayo. Basi njia ni moja kufuatana na malengo na matumaini yake. Kwa hivyo, hukuwa peke yako. Pengine umekuwa peke yako katika wakati wako ambao ulifuata njia hiyo, lakini hukuwa peke yako katika nyakti zote ambazo amefaradhia Mwenyezi Mungu kukata mbuga ya maisha yenye miba. Mitume watukufu, maimamu wema, wanaitikadi (wenye kubeba ujumbe) wa mwanzoni na mashahidi watukufu, kila mmoja wao ameingia katika majaribio hayo magumu ya kiitikadi, akayakabili na kuyavumilia kwa msimamo thabiti. kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akamlipa malipo yake bila ya kupungua chochote. Basi makusudio yetu tunapokwenda katika njia yenye kudumu ya hao waliotutangulia ni kuwafuata na kuchukua mwanga wa taa yao na azma, subira na msimamo wao.

Ewe ndugu yangu Mwislamu! Hakika kitabu hiki kitakuonyesha visa vya Mitume na Manabii jinsi walivyopambana na mashaka na matatizo ya maisha na jinsi usafi wao ulivyozidi na ukatoa johari ambazo zinadhihirisha hakika yao safi isiyokuwa na vumbi. Vilevile kitabu hiki kinaonyesha kwamba kila mashaka ya njia ya Manabii yalivyozidi ndivyo azma na uthabiti wa njia yao ya haki ulivyozidi. Mafanikio hayo yanatokana na kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na kuhakikisha malengo yao ya kiitikadi. Visa vya Mitume vilivyotajwa katika kitabu hiki vimenukuliwa kutoka Qur'ani Tukufu na vitabu vya kihistoria na vya kiitikadi. Kwa hakika fikra za kitabu hiki na darasa zake zinawezekana kuzingatiwa kuwa ni mwanga utakaotuongoza kushika njia ya kujenga hadi ya mwislamu kufuatana na maoni ya Qur'ani. Hakika uzoefu wao ni mali waliyoturithisha ili tugharamie mahitaji yote katika njia ya kiitikadi. Kuirudisha hadhi ya Kiislamu katika tukio la maisha huhesabiwa na katika mambo muhimu zaidi ya wanaofanyia kazi Uislamu leo. Kwa hivyo, halipatikani hilo ila kwa kupatikana kiigizo chema, nacho ni Mitume. Kutikana na umuhimu na haja kubwa ya kitabu hiki, Jumuia ya Udugu wa Kiislamu imekichapisha tena kitabu hiki kama ni mojawapo ya kazi zake za kuitamaduni na kimaarifa.

Chapa ya kwanza ya kitabu hiki (kwa kugha ya Kiarabu) kilichapishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini pamoja na kupita muda huo mrefu bado kitabu hiki kinatoa pumzi ya uhai. Kwa nini kisiwe hivyo ilhali mishipa yake imeambatana na mishipa ya historia ya kiitikadi iliyo hai? Mtungaji wa kitabu hiki ni mwanachuoni mtukufu Sayyid Muhammad Taqi al-Mudarrisi ambaye ameingia katika nyanja mbalimbali za kazi za Kiislamu kama vile kujenga shule na vyuo vya kidini vya kisasa. Vilevile amejiendeleza katika kutunga vitabu vya darasa na utafiti wa Kiislamu pamoja na huduma nyinginezo za Kiislamu ambazo anaendelea kuzitoa katika Umma wa Kiislamu. Kitabu hiki chenye fasaha ni miongoni mwa natija zake za mwanzoni, na amekiandika akiwa na umri wa miaka ishirini.

Ifuatayo ni orodha ya vitabu vyake vya darasa vilivyokwishachapishwa ambavyo vinajadili kwa mapana katika fani mbalimbali za Kiislamu:

1) fikra za Kiislamu: Mwelekeo wa Kisasa

2) Mantiki ya Kiislamu: Misingi na Njia Zake

3) Amali za Kiislamu: Asili na Malengo Yake

4) Jamii ya Kiislamu: Asili na Malengo Yake

5) Historia ya Kiislamu

6) Ufufuo wa Kiislamu

7) Fiqihi ya Kiislamu

8) Mijadala katika Qur'ani Tukufu

9) Tafsiri ya Qur'ani. Mwongozo katika Qur'ani.

Kuna vitabu kadhaa vya Kiislamu na mamia ya kaseti za Mihadhara yake ambayo anaendelea kutoa. Vyote ni katika lugha ya asili ya Kiarabu. Mchapishaji wa kitabu hiki ni Maktab As-Sayyid al-Mudarrisi ambayo ni taasisi ya utamaduni wa Kiislamu yenye lengo la kueneza fikra za Kiislamu yenye lengo la kueneza fikra za Kiislamu miongoni mwa wana wa Umma wa kiislamu na kuingiza roho ya udugu wa Kiislamu. Jumuia hii inafanya kazi nyingi za Kiislamu. Mwishowe, tunapenda kuwakumbusha ndugu zetu mambo mawili:

1) Kitabu hiki kinatoa zingatio, faida na kielelezo, kwa kuwa Mitume ni kiigizo chetu.

2) Saidia kueneza kitabu hiki wa upana zaidi, kisome, kisha mpe rafiki yako afaidike. Tunakuombea mafanikio mema na kabuli njema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maktab as-Sayyid al-Mudarrisi

UTANGULIZI WA MTUNGAJI

Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu Mtukufu, na rehema na amani zimshukie Mtume Wake Muhammad(s.a.w.w) , Nabii wa Mwisho, na juu ya kizazi chake kitakatifu. Hakika Umma wa Kiislamu umeshindwa kabisa, na kushindwa huko kunafuatia machungu na mateso; kisha ukosefu mkubwa katika pande mbili: upande wa kimaada (kidunia) na upande wa kimaanawi (kiroho). Kukosekana upande wa kimaanawi ni sababu ya kukosekana upande wa kimaada, kwani umaada sio nguvu inayojileta yenyewe kwa mtu na kuweza kubaki au kuondoka wakati wowote, bali ni natija ya kazi ya mtu na mapato ya juhudi yake. Mtu hafanyi bidii ila baada ya kujua maana ya juhudi yake. Kwa hivyo, kukosekana umaanawi katika Umma wa Kiislamu ndiko ambako kunapasa kuupiga vita na kuupigania ili urudi utukufu na ushindi na Umma uishi katika neema baada ya kuwa katika adhabu. Hatuwezi kuupiga vita ukosefu huu bila ya kueneza mwamko sahihi wa Kiislamu kwa kutafsiri Qur'ani, kueneza maarifa yake. kuelezea maisha ya mashujaa wa Kiislamu, n.k. Kitabu hiki kidogo ni jaribio dogo katika kutimiza lengo hili, kwani tumenakili mifano michache ya visa vya Mitume.

KILELE CHA UTUKUFU

Hakika Mitume (amani iwe juti yao) wamekumbana na matatizo mengi na wamepita katika njia ya miiba (mashaka) kuelekea kwenye utukufu wa kitu hadi wakafika kwenye kilele cha ukamilifu na utukufu. Wakawa ni watu wa ngazi za juu kwa kufikia kwenye kilele cha ubinadamu. Kwa hivyo, wao walijua njia, wakaongoka na wakajua malengo ya njia hizo na wakalingania watu na kuwaongoza wale waliopotea kwenye lile walilolijua. Waliwafungulia watu njia ambazo zilikuwa hazijulikani kwa kuwa walikuwa wenyeji katika mambo hayo na walikuwa na nguvu na uwezo kutokana na bahari yao ya elimu, upole na sifa zao za uvumilivu na uthabiti. Hatuwezi kuvipima vipawa vyao vinavyoshindania kheri, utiifu na utukufu. Hatuwezi kuvipima kwa vipawa vyetu. Nguvu yao ya uwezo, udhibiti wao wa nafsi, matamanio, dunia na udanganyifu wake, na kuvumilia kwao misiba, ni muujiza wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake.

Kwa hakika, Mitume wametuachia athari nyingi na mazingatio mengi ambazo ndizo zinazotusaidia. Wao ndio waliotufundisha namna ya kuvumbua vitu visivyojulikana na kutosalimu amri mbele va vitu hivyo. Wametufundisha namna ya kupambana na kuyashinda matamanio, kuwa na msimamo mzuri katika kuyakabili matamanio na kuwa na azma imara. Lau tusingefuata ushauri wao tusingekuwa watu kama tulivyo. Lau tungekubali ujinga tangu siku ya kwanza na kutawaliwa na matamanio, tungejikuta tumo katika pango la ushenzi na tungelikuwa kama wanyama tu! Ni lazima tulizingatie an tufaidike kutokana na ibra au mafunzo ya mambo yetu muhimi ya kidini na kidunia. Mazingatio hayo hayawezi kutekelezwa bila ya sisi wenyewe kutaka kuelekea na hayawezi kutuhimiza bila ya sisi wenyewe kujihimiza. Mfano wake ni kama umeme unaotoa mwangaza wakati ule tunapotaka utoe mwangaza.

Mazingatio haya huunda nguvu, uwezo na azma katika harakati, huimarisha kazi na hutakasa utiifu; na kila mmoja katika misimamo hiyo mitukufu ya kiutu hutukuza athari zake katika maisha na hutoa matumaini makubwa kwa maazimio yake. Haya ndiyo mapinduzi ya hakika ambayo kipimo cha utukufu wake yanaonekana katika malengo yake.

1. Vipi Tutazingatia? Vipi tutazingatia visa vya Mitume na Manabii? Vipi tutaweza kuilinganisha historia ya zamani na matatizo yetu ya sasa? Hakika swali hili linataka jibu pana. Hakika mtu ana tabia ya kuogopa vitu asivyovijua na hujihadhari na upotofu. Kwa hivyo, hujiepusha na mambo yasiyojulikana. Mitume wameondoa tatizo hili katika maisha ya kiutu kwa kujiingiza katika mambo yasiyojulikana, na huko ni kwa kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu. Wameweza kumthibitishia mtu kwamba utafiti wa mambo yasiyojulikana ndiyo njia ya pekee ya maendeleo katika maisha; kisha wakamfundisha mtu ushujaa katika kazi hii tukufu kukabiliana na kitu kisichojulikana.

Mitume wamewashajaisha watu kuvunja vikwazo vya matamanio ambavyo vimemzunguka mtu kila upande mpaka kumfanya mnyonge kabisa ilhali Mwenyezi Mungu amemuumba mtukufu. Unyonge ni udhalilifu mfano wa kuni zinazomchoma. Ikiwa ni hivyo, basi ni juu yetu kujifunza mwenendo wao uliojaa jihadi iliyoimarika na bidii ya amali (utendaji) katika njia ya kujikomboa kifikra na kumpeleka mtu kwenye kheri. Hebu tuangalie mambo haya mawili matukufu ambayo ni ushujaa na ujasiri katika kuyapetuka mambo yasiyojulikana, na ushujaa katika kuondoa vikwazo vya matamanio.

2. Kiigizo Kizuri Tumesema kuwa maisha ya Mitume ni kiigizo cha mambo ya kheri walivoyafanya, kuyafundisha, kuyawekea mpaka mambo ya shari na kuthibitisha bidii ya jihadi na harakati za kudumu. Kwa hivyo, tunajifunza kutoka kwao mambo haya:

1. Namna ya kujikomboa kutokana na shari na washari. Vilevile namna ya kujikomboa kutoka katika makucha ya mataghuti (madhalimu) na wanyonyaji wa nchi.

2. Namna ya kuvumilia udhalilifu, unyonge, uduni, mateso, adhabu na machukivu ili tusikwame katika shabaha yetu wala zisidhoofike nishati zetu.

3. Namna ya kuendelea daima katika jihadi na mapambano dhidi ya adui wetu. Ijapokuwa natija yake itachelewa, lakini ni lazima tuendeleze mapambano hata kama mauti yatatufikia njiani na kuwaigiza walioendeleza harakati zao kwa bidii mpaka wakapata yale waliyoyatamani kabla ya kufikia mwisho.

4. Namna ya kumnyenyekea Mwenyezi Mungu kwa moyo safi bila ya kutegemea malipo au shukrani kutoka kwa viumbe.

5. Namna ya kutatua maelfu ya matatizo yaliyozidi ambayo yanatuongoja katika harakati zifanywazo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na ambayo Mitume wameyapatia ufumbuzi wake kamili.

3. Sababu za Kijinga Kuna baadhi ya watu wanaopendelea uvivu, wanaostahabu udhaifu na kupendelea kungojangoja bila ya kufanya bidii yoyote. Husema: "Hakika harakati huleta matatizo", au husema: "Hatuna uwezo wa kufanya kazi fulani za kiharakati." Wakijibiwa: "Mbona Mitume waliweza kuwa na harakati licha ya matatizo waliyokuwa nayo?" Husema "Mitume walikuwa wakipata msaada wa wahyi (ufunuo) na wakilindwa kwa nguvu za Kiungu. Isitoshe, wameumbwa wakiwa na ujuzi, hekima, usafi, uwerevu na mengineyo ambayo yaliwaandalia njia na kuwawekea msingi mzuri; kisha wao walikuwa na miujiza iliyowaandaa kwa tablighi na kuhami nafsi zao na za wasaidizi wao." Ninawaambia watu hawa: "Ukweli ni kuwa sababu hizi haziwezi kukuteteeni, enyi wavivu! Wenyewe mnasema kinagaubaga kuwa hamwezi kuwa na harakati, hivi ni kwa sababu mnadharau na ni wazembe."

Bila shaka sababu hizi zinaweza kuwapa faida wale walio tayari kupiga mbizi katika mawimbi makubwa ya bahari. Kwa hivyo, si Mitume peke yao ndio wenye kulindwa na kusaidiwa, bali yeyote yule mwenye kufanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hupata taufiki na msaada Wake. Qur'ani inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّـهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ ﴿٧﴾

''Mkimsaidia Mwenyezi Mungu atakusaidieni na ataithibitisha miguu (hatua) yenu." (47:7).

Uzoefu umeonyesha kwamba mwenye kuwa na harakati kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hana budi kupata nusura kutoka Kwake. Vivyo hivyo, vipawa vyao (Mitume) wameviweka wazi katika vitendo vyao, maneno yao, visa vyao na utukufu wao wamevibakisha kwetu kama ni hazina safi ambayo tunaweza kutoa kiasi tunachotaka na tunachohitajia. Qur'ani inasema: "Hakika katika visa vyao kuna mazingatio kwa wenye akili ." (12:111).

Kuna mifano mingi katika Qur'ani ya uzoefu katika maisha ya Mitume na maadili yao. Vivyo hivyo, katika vitabu vya sira kuna hekima nyingi zilizotolewa na Mitume katika karne nyingi zilizopita. Madai ya baadhi ya watu kwamba Mitume walikuwa na miujiza ni sawa, lakini ukweli ni kuwa Mitume hawakuutumia uwezo huu ila kwa nadra sana. Mara nyingi walijadiliana na watu kwa dalili za kiakili, na walipoanza kuwalingania watu walikuwa wakifukuzwa na kuadhibiwa wao pamoja na masahaba zao. Lau wangelikuwa wakitegemea miujiza ya kujikinga, basi kazi yao ingekuwa nyepesi sana na wala wasingeadhibiwa. Kwa hivyo, miujiza ilikuwa ni kwa ajili ya kubainisha Utume wao na hoja ya Mwenyezi Mungu kwa watu ili katika siku ya Kiyama watu wasidai na kusema: "Ewe Mola wetu! Sisi tumemkanusha mtu aliyetaka kututawala na kuchukua milki zetu." Mitume hawakuzitatua kazi nyinginezo kwa kutumia miujiza, bali kwa kufuata maumbile ya Mwenyezi Mungu anayowaumbia viumbe Vyake na neon Lake wakati alipokadiria kila kitu kwa mujibu wa sababu zake. Wao ni kama watu wengine - hula. huenda sokoni, hufanya tablighi, na hujitahidi kufuata mwendo wa watu wa kawaida. Tukiangalia mfano mmoja tu utatosha kutupa dalili dhahiri ya hoja hiyo.

4. Njia ya Mashaka Mitume (amani iwe juu yao) wamekumbana na mashaka (miiba) katika mwendo wao wa kuwaongoza watu kwenye njia ya uongofu. Ni watu wachache sana miongoni mwa wanaofanya kazi za daawa (tablighi) wanaopata mashaka kama hayo. Hakika Mitume wamepata shida na misukosuko mingi sana, matusi na tuhuma. lakini wao walitegemea nguzo ya haki mbele ya batili, mwanga mbele ya giza na ukweli mbele ya hadaa na vitimbi. Wakathibiti katika hali hiyo kama jabali mbele ya kimbunga, na walikwenda katika njia hiyo ngumu ya mashaka kwa mwendo wa kasi bila ya kuogopa wala kujali masumbuko yaliyokuwa yakiwangoja njiani. Tunathibitisha hapa visa vichache vya Mitume hao ambavyo vinaonyesha msimamo wao thabiti katika njia ya daawa (tablighi), visa ambavyo vina mazingatio na ukumbusho kwa waumini.

Tutadondoa hapa visa vya maisha yao yaliyojaa jiihadi na mapambano, na tunataraji kwamba wasomaji watagundua njia yao pana ya kufuata jihadi yao tukufu ili iwe ni somo kwao. Jambo hili ni wajibu kwa kila binadamu mwema kulifanya mbele ya ubatilifu na watu wake. Wasomaji wazingatie kwamba lau wangechukua nafasi ya Mitume na wangeitakidi itikadi yao, je. wangefanya nini mbele ya ubatilifu unaotawala? Hebu tuchukulie kwamba hii ni zama za Mitume na watu ndio haohao na matatizo ndiyo hayohayo, nasi tunataka kutenda kama walivyotenda wao ili kuiga mifano yao.

VISA VYA JIHADI NDEFU

1. NABII IDRIS(a.s)

Kuna watu wengine ambao wanapotiwa hima na tamaa, na wanapodanganywa na makosudio yao, mara huanza kufanya bidii na kutafuta kila njia ili wapate matamanio na makusudio haya. Kuna wengine ambao kazi yao ni vitimbi, hila na wizi, na wengine kazi yao ni kutafuta utawala na uongozi wa kuhukumu watu na miji. Watu hao hujitahidi kwa kila njia ili kufikia malengo yao. Hakika watu wa aina hii ni waovu sana, kwa sababu wameharibika na wanawaharibu wengine, wamepotea na wanawapoteza wengine. Hao ndio viongozi waovu wanaowaongoza watu kwenye Moto.

Mfano mmojawapo wa aina ya watu tuliyowataja alikuwa dhalimu mmoja aliyeishi katika zama za Nabii Idris(a.s) ambaye aliwamiliki watu na kuwafanya watumishi wanyonge wanaomtumikia kwa kila analolitaka na kulitamani. Ikiwa mmoja wao alionyesha upinzani wowote basi alikuwa akimtesa kwa adhabu mbaya sana. Siku moja alipokua akitembea njiani aliona shamba zuri lenye rutuba lililokuwa ni mali ya mja mwema wa Mwenyezi Mungu ambaye alikuwa akijipatia maisha ya ukoo wake kwa kulimia ardhi hiyo. Mfalme dhalimu alivutiwa sana na shamba hilo, na alipouliza ni la nani, akaambiwa kuwa ni la mpinzani mmoja fulani. Akataka kulinunua, lakini yule mtu akakataa kwa kumjibu "Ardhi hii wanahitaji zaidi ukoo wangu kuliko wewe." Mfalme akarudi nyumbani kwake akiwa amekasirika. Akamhadithia mkewe habari hiyo. Mkewe akamwambia: "Usikasirike, ikiwa unashindwa kumwua kwa kukosa sababu, mimi nitafanya mpango."

Mwanamke yule akawaita watu na kuwaamrisha washuhudie kwamba mtu fulani ni mpinzani wa dini ya mfalme. Kwa hivyo, mfalme akapata sababu. Akamwua yule mja mwema na akachukua ardhi na kuwafukuza wajane na mayatima wake. Mwenyezi Mungu akakasirika kwa kitendo hicho. Akampa wahyi (ufunuo) Nabii Idris(a.s) kuwa aende kwa mfalme. Akamwendea mfalme na ujumbe wa Mwenyezi Mungu unaosema: "Hivi umeridhia kumwua mja Wangu muumini na kuitia ufakiri familia yake ili uchukue ardhi yake? Naapa kwa Utukufu Wangu, nitakutesa nitaondoa ufalme wako, nitauharibu mji wako na nitawalisha mbwa nyama ya mke wako."

Mfalme aliposikia maneno hayo kutoka kwa Nabii Idris(a.s) , akamwambia: "Toka, ewe Idris nisije nikakuua." Mkewe akamwambia: "Usikofazaishe ujumbe wa Mungu wa Idris. Mimi nitatuma watu wakamwue, hivyo, utabatilika ujumbe wa Mungu wake" Mfalme akamwamrisha mkewe atekeleze njama hiyo. Akatuma watu arobaini wakamwue Nabii mwaminifu. Nabii Idris(a.s) akakimbia mwituni na akawa akiishi humo na kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa tahadhari. Baada ya muda, mfalme taghuti akafa. Mke wake akafa pia, na mwili wake ukawa chakula cha mbwa. Mji wake ukaharibika kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu kupitia ulimi wa Nabii Idris(a.s) .

Akatawala dhalimu mwingine na akawa kama yule wa kwanza kwa ushenzi na kiburi. Ikapita miaka ishirini baada ya kuondoka Nabii ldris(a.s) na mvua haikunyesha. Hali ya watu ikawa mbaya sana na wakawa wanatafuta chakula kutoka katika miji jirani. Kisha watu wa mji ule wakakusanyika kumwomba Mwenyezi Mungu awaepushe na balaa iliyowasibu. Wakajua kuwa hakuna wa kutegemewa isipokuwa Mwenyezi Mungu. Wakanaza kutubia na wakafikiri namna ya kumwabudu Mungu. Je, wangeweza kumtii Mwenyezi Mungu bila ya kuongozwa? Mwenyezi Mungu akamleta Nabii ldris(a.s) kutoka mahali pake alipokuwa akimwabudu. Nabii Idris(a.s) akawaombea mvua, ikanyesha sana mpaka ikakaribia kuwagharikisha. Pamoja na mwujiza huo, Nabii Idris(a.s) alikuwa ni mtu wa pekee aliyeweza kuandika na kushona nguo, na vilevile alikuwa ni mwenye maarifa ya ujuzi wn hesabu na nyota.