MAISHA YA BIBI KHADIJA

MAISHA YA BIBI KHADIJA0%

MAISHA YA BIBI KHADIJA Mwandishi:
Kundi: Waheshimiwa wa Kidini

MAISHA YA BIBI KHADIJA

Mwandishi: Syed A .A .Razwy
Kundi:

Matembeleo: 23515
Pakua: 3038

Maelezo zaidi:

MAISHA YA BIBI KHADIJA
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 23515 / Pakua: 3038
Kiwango Kiwango Kiwango
MAISHA YA BIBI KHADIJA

MAISHA YA BIBI KHADIJA

Mwandishi:
Swahili

1

MAISHA YA BIBI KHADIJA

SURA YA TATU

MUHAMMED MUSTAFA (S.A.W.W) ALIYETEGEMEWA KUWA MTUME WA UISLAMU

Ingawaje nchi ya Arabu haikuwa na serikali yoyote- ya kitaifa, kijimbo au kienyeji - jiji la Makka lilikuwa linatawaliwa na kabila la Qurayishi, kama ilivyotajwa kabla. Kabila la Qurayish lilikuwa na koo kumi na mbili. Koo hizi zilishirikiana majukumu ya kudumisha kiasi kidogo cha sheria na utulivu katika mji wa Makka. Moja ya koo za kabila la Qurayshi ilikuwa Bani Hashim. Kila ukoo ulikuwa na kiongozi wake. Kiongozi wa Bani Hashim alikuwa Abu Talib bin Abdul Muttalib bin Hashim bin Abd Manaf bin Qusayy. Kama walivyokuwa babu zake, Abu Talib pia alikuwa mfanyabiashara. Zaidi ya kuwa mkuu wa ukoo, alikuwa pia mlezi wa Al-Kaaba - Nyumba ya Mwenyezi Mungu - iliyojengwa Makka, karne nyingi zilizopita, na Mtume Ibrahim na Ismaili na wakaitoa wakfu imtumikie Mwenyezi Mungu.

Abu Talib alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Abdullah. Mwaka wa 570 A.D., Abdullah alikwenda Syria na msafara wa biashara. Miezi michache kabla hajasafiri kwenda Syria alimuoa Amina binti Wahab, mwanamke kutoka Yathrib (Madina). Wakati Abdullah alipokuwa anarudi kutoka Syria, aliugua na kufa. Alikuwa na umri wa miaka 17 tu alipokufa. Alipoondoka Makka, mke wake alikuwa mja mzito na alikuwa anaishi nyumbani kwa shemeji yake, Abu Talib. Miezi miwili baada ya kifo cha Abdullah, alijifungua mtoto wa kiume. Babu wa mtoto huyu, Abdul Muttalib, alimpa jina la Muhammad. Muhammad alizaliwa tarehe 8, Juni, 570, nyumbani kwa baba yake mdogo, Abu Talib mjini Makka.

Siku za usoni, mtoto mchanga Muhammed alikuwa ateuliwe na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa Mjumbe Wake wa dunia yote, na alikuwa abadilishe majaliwa na historia ya binadamu daima milele. Muhammad alikuwa na umri wa miaka sita wakati mama yake, Amina binti ya Wahab, alipokufa baada ya kuugua kwa muda mfupi. Kutokana na kifo chake hicho, babu yake Muhammad, Abdul Muttalib, alimchukua ili amlee nyumbani kwake. Lakini ilikuwa baada ya miaka miwili tu Abdul Muttalib naye alifariki. Abdul Muttalib alikuwa na watoto wa kiume kumi. Alipokaribia kufa, aliwaita watoto wake wote, na alimteuwa mwanae Abu Talib kama mkuu mpya wa ukoo wa Bani Hashim. Pia alimfanya mlezi wa Muhammad. Wote wawili Abu Talib na Abdullah, baba wa Muhammad, walikuwa watoto wa mama mmoja, ambapo watoto wengine wa Abdul Muttalib walizaliwa na wakeze wengine.

Abu Talib alimpeleka Muhammad nyumbani kwake. Muhammad ali-washinda wote (kwa tabia). Abu Talib na mkewe walimpa Muhammad mapenzi makubwa sana. Walimpenda zaidi kuliko walivyowapenda watoto wao. Muhammad alizaliwa ndani ya nyumba yao. Kuzaliwa kwa Muhammad ndani ya nyumba hiyo ilisababisha nyumba hiyo iwe na neema nyingi; na sasa baada ya kifo cha Abdul Muttalib, alirudi tena ndani ya nyumba hiyo. Muhammad alipokuwa mtoto, hakuonyesha kuvutiwa na mwanasesere na michezo ya watoto. Katika ujana wake, hakuonyesha kupenda michezo na burudani, au kuwa katika makundi ya vijana wa rika lake. Pamoja na kwamba alikuwa kijana, alipendelea zaidi upweke kuliko kuchanganyika kwenye makundi ya vijana wenzake. Kama walivyokuwa watu wengine wa kabila la Qurayish, Abu Talib pia alikuwa akipeleka bidhaa zake Syria na Yemen kila mwaka. Wakati mwingine alikwenda yeye mwenyewe na misafara, na kipindi kingine aliajiri Wakala ambaye aliuza bidhaa zake kwenye masoko ya nchi hizo. Mnamo mwaka wa 582 A.D. Abu Talib aliamua kutembelea Syria akiwa na msafara. Mpwa wake, Muhammad, alikuwa na umri wa miaka 12 wakati huo. Abu Talib alimpenda sana hivyo kwamba alikuwa hawezi kuachana naye hata kwa muda wa miezi michache. Kwa hiyo, alimchukua na kwenda naye Syria.

Akili ya Muhammad ilikomaa upesi, na pamoja na kwamba umri wake ulikuwa bado mdogo sana, alikuwa mchunguzi na mdadisi aliyebariki-wa. Wakati wa safari yake nje na ndani ya Syria, kwa uangalifu sana ali-wachunguza watu na mila zao, desturi zao, namna wanavyo abudu, mavazi yao, hotuba na upembuzi wao wa mambo. Na kila alichokiona, alikumbuka. Aliporudi Makka, aliyakumbuka yote yale aliyoyaona toka mwanzo hadi mwisho na aliweza kukumbuka uchunguzi wake wote bila kubakisha kitu. Hakusahau kitu; kwa hakika, alikumbuka kila kitu. Ingawaje alikuwa mdogo kwa umri, alikomaa kihekima na matumizi ya akili ya kawaida. Abu Talib alitambua kwamba Muhammad alikuwa na hekima na akili iliyopevuka kuliko umri na uzoefu wake. kwa hiyo, hakumchukulia kama mtoto mdogo kwani ilibidi aonyeshe heshima kwake kama ile anayostahili kupewa mtu mzima wa jamii ya Kiarabu.

Haikupita muda mrefu Muhammad alipata umri unaozidi miaka kumi. Ingawa katika rika la kijana aliye balehe, alikuwa bado hakuvutiwa na starehe ambazo vijana wengine huzitafuta. Alijiepusha na purukushani za aina zote na kama ilivyoelezwa huko nyuma, alipendelea kuwa peke yake na tafakuri yake. Alikuwa na fursa ya kutosheleza upendeleo huu alipokwenda kuchunga kondoo wa ami yake. Alikuwa peke yake chini ya anga. Jangwa lililo kimya na kujitandaza hadi upeo wa macho, na ambalo lilimpa matumaini ya kutafakari kuhusu maajabu ya Uumbaji, siri za mbingu na ardhi, na maana na madhumuni ya maisha. Alitazama mandhari ya ardhi kutoka upeo wa macho huu hadi mwingine, na ilionekana kama vile ukubwa wa ulimwengu ulikuwa ndio swahiba pekee "aliyekuwepo" pamoja naye. Upweke kwake ulionekana kuwa "kipimo" kipya cha ulimwengu wake.

Wakati Muhammad alipokuwa amevuka ujana wake, watu wa Makka walikwishaanza kumtambua. Walijua kwamba kamwe hakupotoka kuto-ka kwenye maadili mema na utu mwema na hakufanya kosa kamwe. Aidha walitambua kwamba hakupenda kusema sana na alipofanya hivyo, aliongea kweli tupu, na alitamka maneno ya hekima tu. Kwa kuwa watu wa Makka walikuwa hawajamsikia akisema uongo, walimwita "As-Sadiq" (Mkweli). Katika kipindi cha miaka michache iliyofuata, raia wa Makka walimpa Muhammad cheo kingine. Kwa kutambua kwamba alikuwa makini sana, wengi wao walianza kumpa mali zao ili awatunzie kama vile: fedha taslimu, vito, mapambo, na vitu vingine vya thamani. Wakati mtu yoyote alipotaka mali yake, Muhammad alimrudishia yote. Kamwe hapakutokea kasoro yoyote katika kurudisha mali za watu. Baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa na tabia ya namna hiyo, kwa kipindi cha miaka kadhaa watu walianza kumwita Muhammad "Al-Amin". (Mwaminifu) Ni yeye, na yeye peke yake aliyeitwa As-Sadiq na Al-Amin na watu wa Makka. A. Yusuf Ali mtarjumi na mfasiri wa Qur'anTukufu, amelielezea neno "A-Amin" kama ifuatavyo: "Al-Amin Mtu ambaye amana imewekwa kwake, pamoja na maana mbali mbali kidogo zimedokezwa:

1. Aanyestahiki kuaminiwa;

2. Anayewajibika kuitoa amana yake, kama Mtume yeye huwajibika kutoa Ujumbe wake;

3. Anawajibika kabisa kutenda kama ambavyo amana inaelekeza, kama mtume anawajibika kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu tu, na asiongeze chochote cha kwake, na

4. hatafuti masilahi yake mwenyewe."

Waarabu walioishi kabla ya Uislamu kila mwaka walifanya "Msimu wa maonyesho" sehemu mbalimbali za nchi. Baadhi ya maonyesho haya yalionyeshwa Makka na sehemu nyengine za karibu yake. Maonyesho yaliyojulikana sana ni: Ukkaz, Majanna na Dhul-Majaz. Muhammad aliyatembelea maonyesho hayo pale muda ulipomruhusu kufanya hivyo. Maonyesho yote haya yalionyeshwa wakati wa miezi minne mitakatifu ya Rajab, Dhil-Qaada, Dhil-Hajj na Muharram, kufuatana na mila za Waarabu wa kale. Ndani ya miezi hii minne, mambo yafuatayo yalip-igwa marufuku: vurugu, vita, kuteka nyara na unyang'anyi. Mnamo mwanzo wa "Msimu wa amani" tangazo la kusimamisha vita lilitolewa. Tangazo la kusitisha vita lilitambuliwa na kuheshimiwa na makabila yote ya Waarabu. Wafanya biashara, wakulima na wastadi (wachonga sanamu) waliku-sanyika kwenye maonyesho haya kutoka sehemu za mbali na za karibu (kwa ajili ya) kuuza, kununua na kubadilishana. Walileta pamoja nao mazao yao yaliyo bora kabisa, na kwa fahari waliyafanyia maonyesho. Sanaa nyingine za amani, mashairi yakiwa miongoni mwao, yalikuzwa (na kutukuzwa katika wakati zilipositishwa vurugu (na vita)

Mashairi yalikuwa penzi la kwanza la Waarabu. Kama kipaji cha mashairi kiligunduliwa kwenye kabila lolote, lilikuwa jambo la kush-erehekewa na kila mmoja. Makabila mengine yenye uhusiano mzuri na kabila husika, yalilipongeza kabila hilo kwa kuzalisha kipaji cha namna hiyo. Waarabu walikuwa washabiki wakubwa wa maneno ya Kiarabu na maana yake nyingi. Wao walijiita "watoto wa Kiarabu." Kwenye maonyesho haya washairi walisoma tunzi zao mpya, sifa ambayo Waarabu waliithamini kuwa ya muhimu na maana sana. Mojawapo ya misemo yao ni kwamba uzuri wa mwanamke upo kwenye uso wake; lakini uzuri wa mwanamume upo katika uhodari wake wa kujieleza. Walipenda ustadi wa utunzi na ufasaha wa yale yanayosemwa kwenye mashairi.

Mafumbo yasiyo ya kawaida ya jangwani na watabiri wanaofanana na wanyama pori na waaguzi wa makabila, huwafurahisha asikilizaji kwa hotuba zao za mafumbo hadithi zao za mafumbo na siri za ubashiri, hata hivyo, wachache waliweza kuelewa ishara hizo. Waarabu wengi waliamini kwamba utabiri wa nyota uliamua mwisho mzuri au mbaya wa maisha ya mtu. Kwa hiyo, watu wa nchi nzima waliwaogopa watabiri, iliaminika kwamba walikuwa na uwezo wa kuzungumza na nyota. Waimbaji, wacheza dansi, wachekeshaji, wana sarakasi na wana mazingaombwe wote walishindana ili wapate kusifiwa na watazamaji.

Maonyesho haya yalihudhuriwa na watawa, makuhani na watu watakat-ifu ambao walihubiri imani ya ibada zao. Wote walikuwa huru kueneza itikadi zao na fikira zao bila woga wa kuonewa na mtu yeyote katika kipindi chote cha miezi minne. Amani na sanaa za amani vilishamiri dhidi ya mfululizo wa mambo ya uchangamfu wa binadamu usio na mipaka. Kwenye maonyesho haya, Muhammad alipata fursa ya kuchunguza wakazi wa rasi ya Bara Arabu. Pia alijifunza, kwa mara ya kwanza, mila na imani za watu wa jamii tofauti, na utamaduni na usuli za kijogorafia.

Mnamo majira ya kuchipua ya mwaka wa 595 A.D., wafanyabiashara wa Makka walikusanya msafara wao wa majira ya kiangazi ili wapeleke bidhaa zao Syria. Pia Khadija alitayarisha bidhaa zake lakini alikuwa hajapata mtu mwanamume atakayesimamia msafara wake na kuwa wakala wake. Majina machache yalipelekwa kwake lakini hakupata lililompendeza. Kupitia kwa baadhi ya weza wake wa chama katika wachuuzi wa Makka, Abu Twalib alipata habari kwamba Khadija alikuwa anatafuta wakala ambaye atachukua mizigo yake pamoja na msafara kwenda Syria na kuiuza kule. Ilipita akilini mwa Abu Twalibu kwamba mpwa wake Muhammad ambaye sasa alikuwa na miaka ishirini na tano angelifaa kwa kazi hiyo Alikuwa na hamu kubwa ya kumtafutia kazi mpwa wake. Alijua kwam-ba yeye (Muhammad) hana uzoefu wa kazi ya uwakala lakini pia alijua kwamba yeye (Muhammad) angeweza kazi hiyo kwa sababu ya kipaji chake. Alikuwa na imani na uwezo na akili za mpwa wake na alikuwa na uelewa wa kutosha kufanya kazi yake ya uwakala kwa tajiri yake. Kwa hiyo, pamoja na makubaliano yake ya kimya (na Muhammad), alikwenda kwa Khadija, na alianzisha mazungumzo kuhusu suala la uteuzi wake (Muhammad), kama wakala wake mpya.

Kama ilivyo kwa raia wengine wengi wa Makka, Khadija pia alikwisha sikia kuhusu Muhammad. Khadija alijua kwamba hangehoji kuhusu heshima ya Muhammad. Aliona kwamba angeweza kumwamini Muhammad kwa wazi na kwa siri. Kwa hiyo alikubali kumteua Muhammad kuwa wakala wake. Hakufikiria kutokuwa na uzoefu ingekuwa tatizo kwa Muhammad, na akasema kwamba, kwa jinsi yoyote ile, angempeleka mtumwa wake Maysara, ambaye alikuwa na uzoefu wa kusafiri, awe pamoja naye (Muhammad) amsaidie katika kazi zake.

Khadija alikuwa mwendeshaji mzuri sana na mpangaji aliyekamilika. Lakini pia alikuwa na bahati njema. Kila mara alikuwa na bahati ya kupata mawakala wazuri kwa biashara yake. Hata kama alikuwa na hali ya kufuzu, alistaajabu baada ya kipindi kifupi kugundua kwamba akiwa na Muhammad kama wakala wake, bahati yake iliongezeka kwa kiwango ambacho ilikuwa haijapata kutokea. Kwa Khadija, kamwe palikuwa hapajatokea siku za nyuma, na kamwe haingetokea kwa siku za baadaye kuwa na wakala kama Muhammad. Kama Khadija alikuwa na kile kitu kinachoitwa "mguso wa dhahabu" (golden touch) mkononi mwake, Muhammad alikuwa na "mguso wa baraka" mkononi mwake.

Khadija na Abu Talib walitayarisha vipengele vyote vya mpango mpya. Na Muhammad alipokwenda kumuona tajiri wake mpya kwa madhu-muni ya kukamilisha mkataba, alimwambia mambo yote kuhusu biashara hiyo. Muhammad alielewa haraka sana katika yote Khadija aliyomwambia na hakuuliza swali lolote lile lililohitaji ufafanuzi. Khadija alimwambia Abu Talib kwamba ujira ambao atampa Muhammad kwa kazi yake utakuwa mara mbili zaidi ya ule aliokuwa anawapa mawakala wengine huko nyuma. Jambo ambalo Khadija hakulijua wakati huu ni kwamba ulikuwa ni ule mkono wa majaliwa ndiyo uliokuwa unafanya kazi katika kuusukuma mpango huu. majaliwa yalikuwa na mipango mingine kwake yeye na Muhammad. Mipango hiyo ilivuka mipaka ya ulimwengu huu na masu-ala ya thamani ndogo ya pesa, kama kupata faida kwenye biashara, kama ambavyo hivi punde matukio yatakavyoonyesha.

Kwa wakati huo, "msafara wa kiangazi" wa wafanya biashara wa Makka ulikwisha kamilika, na ulikuwa tayari kuondoka kuelekea kwenye safari yake ndefu. Wafanyabiashara walileta mizigo yao kuto-ka kwenye maghala ili ipakiwe kwenye ngamia. Mikataba ilitayarishwa na kusainiwa. Mahitaji ya njiani yalichukuliwa, na viongozi na wasindikizaji waliajiriwa. Kwa muda uliopangwa, Muhammad na Abu Talib na ami zake wengine walifika. Walisalimiwa na ami yake Khadija ambaye alikuwa anawangojea akiwa na Cheti cha orodha ya Shehena na hati nyingine.. Muhammad aliamua kuhesabu mali ya kuuza huko Syria. Akisaidiana na Maysara, alikagua mali yote na aliona kila kitu kiko sawa sawa. Maysra alifanya kazi ya makaratasi yahusuyo mauzo na manunuzi. Alikuwa mtunza taarifa ya mali.

Abu Talib alitoa maelekezo maalumu kwa Maysara na kwa kiongozi wa msafara kuhusu usafiri wa raha na salama kwa Muhammed. Waliahidi kuhakikisha kwamba Muhammed angesafiri kwa raha na salama. Abu Talib na ndugu zake waliwashukukuru kwa kuonyesha ushirikiano kuhusu safari ya Muhammad. Walimwombea dua apate mafanikio kati- ka kazi yake mpya na kurudi salama. Halafu wakamkabidhi Mwenyezi Mungu amlinde arudi salama, na wakaagana. Wakati wa kiangazi misafara mingi ilisafiri usiku kukwepa joto kali la mchana, na kupumzika mchana. Safari ya mchana ingechosha sana wafanya biashara, ngamia na farasi. Kwa hiyo, misafara mingi iliondo-ka Makka saa za alasiri, kama walivyosema Waarabu, au jua linapokuwa limepita katikati, na joto huwa limepungua.

Msindikizaji mmoja aligonga kengele. Wasafiri wote walijitayarisha na msafara ulikuwa tayari kuondoka. Ngamia waliokuwa wamepumzika walisimama, bila kupenda, walionyesha kutokutaka kuondoka kwa kukataa na kukoroma lakini waliingia kwenye msafara. Takribani saa tatu kabla ya jua kuchwa kiongozi wa msafara alitoa ishara, na msafara ukawekwa tayari kwa kuondoka. Msafara ulielekea Kaskazini. Ndugu na marafiki wa wasafiri walikaw-ia kwa muda fulani huku wakiwa wanapunga mikono na kutazama msafara unavyosonga mbele. Ngamia wa mwisho alipokingizwa na vilima, wasindikizaji nao walisambaa.

Wasafiri wapya walikaa pamoja na wasafiri wazoefu ambao walikuwa wanawaonyesha sehemu za kuvutia walizokuwa wanazijua na walielezea upekee wa sehemu hizo. Maysara alimwonyesha Muhammad sehemu nyingi za kupendeza. Muhammad pia alizitambua sehemu nyingi alizoziona barabarani alipopita humo miaka kumi na tatu iliyopita akiwa na ami yake. Hakuna kilicho badilika wakati wa miaka hiyo 13. Maysara alithibitisha kuwa msafiri mwenza mchangamfu ambaye aliweza kusimulia hadithi nyingi na aliweza kukumbuka matukio mengi sana aliyoyaona wakati wa safari zake za siku za nyuma. Muhammad aligundua kwamba wasafiri wengine pia walikuwa wachangamfu na wenye kufanya urafiki.

Baada ya takribani mwezi mmoja, msafara ulifikia mwisho wa safari yake ulipofika Syria. Mipango ya nyumba ya kupanga ilikwisha tayarishwa kwa ajili ya wasafiri waliochoka kwa msafara, na wote wal-itaka kupumzika baada ya safari ndefu iliyowapitisha kwenye mandhari zilizosababisha safari kuwa ngumu na joto kali. Waliweza kupumzika kiasi cha wiki moja ili kuponyesha sehemu muhimu za mwili zilizo athirika. Wafanyabiashara walipokwisha pumzisha viungo vyao vilivyokuwa vinauma na kupata nguvu upya tena, walikwenda sokoni kuuza mali zao walizoleta kutoka Makka. Kiasi fulani cha mali waliuza kwa fedha taslimu, na iliyobaki walibadilisha mali kwa mali kwa bidhaa za Syria. Iliwabidi pia wanunue bidhaa kwa ajili ya soko la nyumbani, na wal-itafuta na kupata mali nyingi yenye faida. Shughuli za msafara ziliweza kudumu kuanzia miezi miwili hadi minne.

Muhammad pia aliuza na kununua mzigo mpya. Ingawa kwake yeye ilikuwa msafara wa kwanza wa kibiashara, hakusita kwa sababu ya kutokuwa na uzoefu, katika shughuli za biashara. Hakika alimshangaza Maysara kwa werevu wake katika biashara. Aidha Maysara aligundua kwamba Muhammad alikuwa mwepesi kuelewa na kuamua katika mazungumzo ya biashara na upevu wake wa akili na uaminifu wake kama muuzaji. Muhammad alilinda maslahi ya tajiri yake na wateja wake, na bado alipata faida kubwa zaidi katika shughuli hiyo ya Khadija kuzidi mara zote alizokuwa amefanya biashara tangu bibi huyo kurithi biashara ya baba yake. Na bidhaa alizonunua Syria kwa ajili ya biashara ya Khadija zilikuwa safi sana kwa ubora wake na hakika zingepata bei nzuri Makka, na ilitokea hivyo. Huko Syria yeyote aliyemuona Muhammad, alivutiwa naye. Alikuwa na umbo la kuvutia ambalo liliwafanya watu wasimsahau hata kwa kumuona mara moja tu.

Ingawa Muhammad alijishugulisha na kuuza mali, mapatano ya biashara, kuchunguza soko, na kununua, Maysara aling'amua kwamba hata hivyo alipata muda wa kukaa peke yake. Kwa maoni ya Maysara, hivi vipindi vya ukimya wa Muhammed, vilikuwa chanzo cha jambo lililojificha, lakini hakuviingilia kati. Maysara hakuwa anajua kwamba bosi wake mwenye umri mdogo alikuwa na desturi ya kutafakari kuhusu hali na majaliwa ya mwanadamu. Wakati akiwa Syria Muhammad alikutana na Wakristo na Wayahudi wengi. Alidhani kwamba kila kundi kati ya hayo mawili yangekuwa na "imani ya Mungu Mmoja." Lakini alistaajabu alipofahamu kwamba haikuwa hivyo. Makundi yote mawili yaligawanyika katika makundi mengine madogo mengi, na aina ya ibada ya kila kundi ilikuwa tofauti na ile ya makundi mengine. Miongoni mwao kundi lipi lilikuwa sahihi na lipi halikuwa sahihi? Hili lilikuwa swali ambalo lilimsumbua Muhammad. Utafiti wa udadisi wa jibu la swali hili, na maswali mengine madogo madogo yenye kufanana na hili yalimfanya Muhammad asilale usingizi wakati kila mmoja amekwenda kulala.

Hatimaye, shughuli za biashara zilipokwisha, na zawadi za ndugu na marafiki kununuliwa, msafara ulirudi Makka. Kwa wasafiri wakum-bukao sana nyumbani, kurudi nyumbani mara zote ni tukio la kufu-rahisha. Ni tukio lililojaa matumaini kwani mtu atakutana na awapendao ambao mtu hakuwa nao kwa miezi mingi. Wasafiri wachovu hawawezi kungoja kwa muda mrefu kusikia vicheko vya furaha vya watoto wao na wanatambua kwamba wakati mzuri kama huo ukiwadia hawawezi kuzuia na kuficha machozi. Wanajua kutokana na uzoefu wa muda mrefu kwamba pangekuwapo na kulia machozi - machozi ya furaha. Kicheko na Machozi vyenye mchanganyiko ulio huru kabisa katika vipindi vya heri na furaha isiyo na upeo.

Kuwasili kwa msafara mara kwa mara kulisisimua mji. Kwa hakika ulikuwa wakati wa kusherehekea kwa kila mkazi wa Makka na vitongoji vilivyomo pembezoni mwake. Sehemu zilizotengwa maalum kwa ngamia kushushia abiria na mizigo, zilikuwa changamfu mno. Raia walio wengi na hata yale makabila yanayohamahama waliona pilika pilika za kuwasili kwa msafara kwamba yalikuwa mabadiliko ya kutia moyo katika mwenendo wa maisha. R.V.C. Bodley, ameandika katika kitabu chake: "Kuwasili na kuondoka kwa misafara yalikuwa matukio muhimu kwa maisha ya watu wa Makka. Karibu kila mkazi wa Makka alikuwa na aina fulani ya uwekezaji kwenye mali iliyobebwa na maelfu ya ngamia, mamia ya watu, farasi na punda:- bidhaa hizo zilikuwa ngozi, zabibu kavu, vinoo vya fedha, na walirudi na mafuta, manukato na bidhaa zili-zozalishwa viwandani kutoka Syria, Misri na Uajemi, na viungo na dhahabu kutoka Kusini. (The Messenger- the life of Muhammed,1946)

Watu walikuja kuwasalimia wapenzi wao ambao walikuwa wanarudi nyumbani baada ya kutokuwepo kwa kipindi cha miezi sita. Wengi wao walikuja wakiwa na fikira mchanganyiko wa matumaini na woga. Ilipotokea mtu anaondoka mjini kwenda na msafara, hapakuwepo na njia yoyote kwa ndugu zake kujua kama wangemuona akiwa mzima tena. Wasafiri wengine walikufa wakiwa safarini na walizikwa kwenye sehemu ambazo ni njia za ndani ndani sana, na hazipitiki. Ndugu zao kamwe hawakuweza kuyatembelea makaburi yao. Na ilikuwa hapo tu ambapo msafara ulifika ndipo wakazi wa Makka waliweza kusikia habari za dunia nje ya bara Arabu. Waarabu wa siku hizo waliishi katika hali ya upweke sana katika dunia yote. Katika dunia hiyo Waarabu walikuwa na njia moja tu ya kupata habari nayo ni msafara.

Takriban kila raia wa Makka aliwekeza fedha kwenye msafara wa biashara. Watu matajiri miongoni mwao waliweza kutembelea nchi za nje kwa muda mrefu zaidi wa miezi mingi. Lakini watu ambao hawakuwa na uwezo wa kifedha walibaki nyumbani. Hivyo, waliwapa bidhaa zao watu walio waaminifu kuwa mawakala wao wauze kwa niaba yao, na waliwapa wao fedha ya kwenda kununua bidhaa ambazo zilikuwa zinatakiwa Arabuni na ziliweza tu kupatikana kwenye masoko ya Syria, Yemen, Habeshi na Misri. Baada ya mawakala wao kuleta mali za nje Makka, waliuza bidhaa hizo na kupata faida. Ulikuwa ni utaratibu ambao baada ya uzoefu wa muda wa miaka mingi, mpango huu ulionekena unafaa na unatekelezeka.

Wafanyabiashara na mawakala waliokuwa kwenye msafara pia walileta zawadi kutoka nchi za nje na tuzo kwa ndugu na marafiki zao, kufuatana na mila za zamani. Kila mtu alitaka kuona zawadi hizo ambazo ziliwakumbusha utajiri uliopo Syria na anasa za Falme za Ajemi na Roma. Muhammad alipofika Makka, kitu cha kwanza kufanya ni kuzunguka Al-Kaaba mara saba kama ilivyokuwa desturi, na halafu alikwenda kumuona muajiri wake. Alimwelezea tajiri wake kwa kina kuhusu safari na shughuli za biashara alizozifanya kwa niaba yake. Baadae, alimwelezea ami yake Abu Talib, kuhusu matukio ya kuvutia kwenye uzoefu wake kama mfanyabiashara.

Maysara, mtumwa wa Khadija, naye alikuwa na taarifa yake mwenyewe ya kumpa mmilki wake. Alimwambia Khadija kuhusu safari ya kwenda na kurudi kutoka Syria, na faida ambayo Muhammad aliingiza kwenye biashara yake. Lakini kwake yeye (Maysara), kilichompendeza zaidi kuliko kufuzu katika biashara, ni tabia na utu wa Muhammad. Maysara alimwambia Khadija kwamba alipendezwa na kipaji cha Muhammad katika biashara. Aliendelea kumtaarifu Khadija kwamba uwezo wa Muhammad kuona mbali kibiashara ilikuwa kinga; uamuzi wake ulikuwa wa uhakika na uelewa wake haukuyumba. Maysara pia alimwambia Khadija kuhusu bashasha, uungwana na kukubali madaraka yaliyo chini ya uwezo wake, Muhammad.

Khadija alivutiwa na taarifa hiyo, na alimuuliza Maysara maswali kuhusu msimamizi wake mpya, Muhammad. Pengine Khadija hange-shangaa hata kidogo kama Maysara angemwambia kwamba Muhammad alikuwa mtu asiye wa kawaida kulinganisha na watu ambao amewaona katika maisha yake, na alikuwa mtu anayeweza kufanya mambo yasiyo ya kawaida. Siku iliyofuata, Waraqa bin Naufal alikwenda kumuona Khadija. Yeye pia alitaka kusikia habari zilizoletwa na wasafiri kutoka ng'ambo. Habari zilizomvutia yeye sana ni zile za ugomvi wa siku nyingi baina ya Falme za Ajemi na Roma. Kila moja ya hizo Falme ilitaka kuwa na mamlaka kwenye kanda yote iliyojulikana kama "Bara lenye Neema." Pengine pia kama walivyokuwa raia wengine Waraqa aliwekeza fedha kwenye biashara ya Makka ya kusafirisha nje na kuingiza ndani ya nchi bidhaa na alitaka kujua jinsi ambavyo msafara ulifanikiwa kibiashara.

Khadija alimwambia binamu yake habari zote kama alivyozipata kutoka kwa Muhammad mwenyewe na Maysara. Aidha alisema kwamba msimamizi wake mpya alipata faida kubwa ambayo hakuitegemea. Waraqa pia alizungumza na Maysara kuhusu safari na kuhusu Muhammad. Maysara, hata hivyo, alitaka kuzungumzia tu kuhusu Muhammad. Hakuna kitu kingine chochote kilichomvutia, hata hizo shughuli za biashara za kuuza na kuuziwa hakuzitia maanani kabisa.. Waraqa aliposikia taarifa hiyo ndefu inasemekana alipatwa na mawazo mengi sana. Baada ya kipindi kirefu cha kimya, alimwambia Khadija: "Baada ya kusikia yale ambayo wewe na Maysara mmesema kuhusu Muhammad, na pia kufuatana na vile ninavyomjua, mimi ninaona kama kwamba anazo sifa zote, tabia, ishara na uwezekano wa kuwa Mjumbe wa Mungu. Hakika, inawezekana Muhammad atakuja kuwa mmoja wao katika siku zijazo."

Kwa mtazamo wa makini ndani ya giza la upagani wa Arabuni, Waraqa aliwezeshwa labda na ubashiri wake, kuona dalili ndogo za Mwanga wa Uislamu ambazo si muda mrefu zingejitokeza kwenye upeo wa macho na Muhammad ndiye ambaye angeleta Mwanga huo.

Vitabu vingi vinavyoeleza maisha ya Muhammad Mustafa, Mtume wa Uislamu(s.a.w.w) vimetaja miujiza kadhaa inayodaiwa kufanywa naye wakati wa safari yake ya kwenda na kurudi kutoka Syria. A. Yusuf Ali, mtrjumi na mfasiri wa Qur'an Tukufu, ameandika ifuatavyo: "Hakuna Mtume yeyote aliyeweza kufanya mujiza wowote au kuonye-sha "Alama", bila ridhaa ya Mungu. Ridhaa ya Mungu (Mashiyat) ni Mpango wenye hekima unaohusu dunia yote, mpango huu upo si kwa faida ya kabila, mila, kipindi au nchi moja. Mujiza mkubwa kuliko yote katika historia ni Qur'an. Tunaweza kutambua uzuri wake na utukufu wake leo kama ambavyo walitambua watu wa zama za uhai wa Mustafa, hata zaidi, kwani jumuisho la uelewa wetu kuhusu asili na Uumbaji wa Mungu umeongezeka."

Mahali pengine A. Yusuf Ali anasema: "Dalili zilizopelekwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad, zilikuwa:

(1) Aya za Qur'an na

(2) Maisha na kazi yake,

Ambamo humo mpango na makusudio ya Mungu yalifunuliwa." Inaonyesha kwamba uchangamfu na kipaji cha Muhammad pia vil-imuathiri Khadija. Kama ilivyotokea kwa Maysara, Khadija naye aliin-gia kwenye kundi la watu wanaompenda Muhammad, na ni nani awaye yeyote miongoni mwa watu ambaye angekataa kumpenda. Khadija alimfahamu Muhammad kuwa mtu mpole mwenye staha, mkimya na asiye mpinzani. Aidha Khadija alitambua kwamba watu wa Makka walimpa jina la Sadiq na Amin. Na sasa alionyesha uwezo wake wa kuwa mfanyabiashara. Ustadi na werevu wake vilikuwa sababu ya mtu huyo kuwa na kipaji. Tathmini mpya ya Khadija kuhusu Muhammad, ni kwamba mtu huyu hakuwa mwenye masihara bali alikuwa na uwezo wa kufanya mambo. Tathmini hii ilimshawishi Khadija kufanya uamuzi wa kumwajiri Muhammad kuwa Meneja wa biashara yake kwenye misafara yote ya baadaye.

2

MAISHA YA BIBI KHADIJA

SURA YA NNE

NDOA YA MUHAMMAD MUSTAFA (S.A.W.W) NA KHADIJA

Msafara wa kibiashara wa Muhammad kwenda Syria ulikuwa ndio chanzo cha ndoa yake na Khadija. Mtarjumi na mfasir wa Qur'an Majid, A. Yusuf Ali, anauliza swali: "Tunaweza kushangaa jinsi Yakuub alivyokutana tena na mwanawe Yusuf, au jinsi Musa alivyokutana na Harun, au jinsi Muhammad Mustafa alivyokutana na Bibi Khadija?"

La, Hatuwezi kushangaa. Ilikuwa ni amri ya Mwenyezi Mungu kwamba watumishi wake wawili- Muhammad na Khadija wangekutana kati-ka ndoa, na walioana. Kuna taarifa isemayo kwamba mmoja wa marafiki wa Khadija alikuwa anatoka kwenye ukoo bora wa Makka jina lake Nafisa (au Nufaysa) binti Mumyah. Mwanamke huyu alikuwa na habari kwamba Khadija alikwisha kataa posa nyingi za ndoa. Alikuwa anashangaa kama pange-tokeza mtu katika Bara Arabu ambaye angekuwa wa kiwango alichoafi-ki Khadija. Marafiki hawa wawili walilizungumzia jambo hili mara nyingi. Hatimaye, Nafisa alifanya mazungumzo ya mara ya mwisho kuhusu jambo la ndoa yake Khadija na akapata kutambua kwamba rafiki yake (Khadija) hakujali utajiri, cheo au uwezo wa mume mtarajiwa. Nafisa alijua kwa hakika kwamba rafiki yake Khadija alitaka kuolewa na mtu mwenye tabia nzuri, tabia inayokubalika. Khadija alitaka kuolewa na mwanamume mwenye maadili mema na msimamo wa uadilifu.

Pia Nafisa (au Nufaysa) alijua kwamba alikuwepo mtu wa aina hiyo Makka na jina lake alikuwa Muhammad. Kuna taarifa isemayo kwamba siku moja Muhammad alikuwa anarudi nyumbani kutoka Al-Kaaba, Nafisa alimsimamisha na mazungumzo yalifanyika kama ifuatavyo: Nafisa: Ewe Muhammad, wewe ni kijana wa kiume na bado hujaoa. Wanaume ambao unawazidi umri, wamekwisha oa na wengine wamezaa watoto. Kwa nini hujaoa? Muhammad: Bado sina uwezo wa mali; mimi ni fukara. Nafisa: Bila kujali ufakiri wako, ungejihisi vipi endapo ungemwoa mwanamke mwenye sura nzuri, tajiri, mashuhuri na mwenye kuheshimika?

Muhammad: Mwanamke huyu anaweza kuwa nani? Nafisa: Mwanamke huyu ni Khadija, binti Khuwaylid. Muhammad: Khadija? Inawezekanaje Khadija kukubali kuolewa na mimi? Unajua kwamba wanaume wengi matajiri na uwezo na wakuu wa makabila wamemposa na amewakataa wote. Nafisa: Kama wewe upo tayari kumuoa Khadija, sema hivyo, na niachie mambo mengine mimi. Nitapanga kila kitu. Muhammad alitaka kumwambia ami wake na mlezi wake, Abu Talib, kuhusu azima ya Nafisa, na kupata ushauri wake kabla hajatoa jibu. Abu Talib alimfahamu Khadija kama alivyokuwa anamfahamu mpwa wake. Alikubali ushawishi wa Nafisa. Hakuwa na shaka kwamba Muhammad na Khadija wangekuwa wanandoa makini. Kwa hivyo, alilibariki pendekezo la ndoa yao. Hapo hapo Muhammad alimtaarifu Nafisa kwamba pendekezo lake limekubaliwa na hivyo amepata mamlaka ya kuendeleza mazungumzo kuhusu ndoa yake na Khadija. Mara tu baada ya Abu Talib kuthibitisha ndoa hiyo, alimtuma dada yake.

Safiya, kumuona Khadija, na kuzungumza naye kuhusu jambo hilo. Wakati huohuo, Nafisa alikwisha fanya mazungumzo ya awali, na Khadija alikuwa anategemea kupata mgeni kutoka nyumbani kwa wakwe wategemewa. Khadija alimpokea Safiya kwa uchangamfu, alimkirimu, na kumwambia kwamba yeye Khadija alimteua mpwa wake Safiya kuwa mwenzi wake wa maisha bila masharti yoyote. Safiya ali-furahishwa sana na mafanikio ya ujumbe wake. Kabla hajaondoka kurudi kwao, Khadija alimpa Safiya kanzu nzuri sana na ambayo ali-ikubali kwa furaha na shukrani nyingi. Abu Talib aliamua kutekeleza kanuni za desturi za ndoa. Alimpa Khadija zawadi, na aliwachukuwa kaka zake, Abbas na Hamza, wote watatu wakaenda nyumbani kwa Khadija na kulifikisha pendekezo la ndoa ya mpwa wake na Khadija rasmi. Khadija alikubali zawadi ali-zopewa na Abu Talib na kama ilivyotarajiwa alikubali pendekezo la ndoa. Pande zote mbili zilikubaliana na kuweka tarehe ya harusi.

Abu Talib mwenyewe alichukuwa madaraka ya matayarisho ya ndoa ya mpwa wake mpendwa. Kwa ajili ya tukio hilo lenye baraka, Abu Talib alileta kumbukumbu zote zenye kuheshimika sana za urithi wa familia. Vitu hivi vilikuwa pamoja na joho na fimbo ya Abdul Muttalib, mare-hemu, mkuu wa kabila la Bani Hashim. Bwana harusi alivaa joho na kuishika mkononi mwake ile fimbo. Abu Talib alimvisha kichwani Bwana harusi kilemba cheusi cha ukoo wake, na alivaa pete yenye kito cha kijani kwenye kidole chake. Pete hii, ilikuwa raslimali ya Hashimu bin Abd Manaf bin Qusayy - mnamo siku za nyuma.

Harusi ilihudhuriwa na wakuu wote wa Quraysh na mamwinyi wa Makka. Bwana harusi alipanda farasi mwenye kutembea kwa majivuno, na vijana mashujaa wa Bani Hashim walitikisa Majambia yao yaliyokuwa yanameremeta juu ya vichwa vyao wakati walipokuwa wana msindikiza kutoka nyumbani kwa Abu Talib kwenda nyumbani kwa Khadija. Wanawake wa ukoo wa Quraysh walikwisha mtangulia bwana harusi, na tayari walikuwa wanakirimiwa nyumbani kwa bibi harusi.

Nyumba ya Khadija ilipambwa kwa taa nyingi sana. Ndani ya nyumba, mashada ya taa zenye mapambo yalining'inizwa kwa minyiroro ya dha-habu kwenye dari, kila shada lilikuwa na taa saba. Wageni walifika wakati giza lilianza kuingia. Msimamizi mkuu wa eneo la makazi ya Khadija aliunda kamati ya kumkaribisha Bwana harusi na wageni mashuhuri. Kamati ya makaribisho iliwaongoza wageni ndani ya nyumba kupitia kwenye lango la juu na kuingia kwenye ukumbi wenye umbo la mstatili ambao kuta zake zilibandikwa vigae na dari yake ilipakwa dhahabu. Wageni waliketi kwenye mazulia na mito.

Kwa madhumuni ya shughuli hii maalum, Khadija aliagiza washonewe sare watu wote wa nyumbani mwake - wanaume na wanawake. Wanaume walivaa vilemba vyenye kumetameta, mashati mekundu, na walivaa mikanda (mishipi) kwenye viuno vyao yenye rangi nyeusi. Mashada ya hariri yenye rangi ya pembe za ndovu yalishikizwa kwenye vilemba. Wasichana walivalia mavazi yaliyonakishiwa kwa kutonewa dhahabu na kumetameta. Walivalia taji dogo kichwani na lulu nyingi na vito vyenye kumetameta. Nywele zao ziliporomoka hadi kwenye mabega na kutoka kwenye mabega hadi kiunoni zilisokotwa kwa lulu. Mapambo ya chumba cha Bibi harusi yalikuwa mazuri sana, na hakika hayakuzidiwa kwa ustadi. Hariri iliyoning'inizwa na nguo iliyotariziwa kwa rangi nyingi nyororo, ilipamba ukuta; na busati, jeupe laini lili-tandikwa sakafuni. Moshi wa ubani ulichomoza kutoka kwenye chatezo cha rangi ya fedha na almasi inayometameta, johari ya rangi ya bluu na rubi.

Khadija, bibi harusi, aliketi kwenye jukwaa lililofunikwa kwa nguo iliy-onakishiwa kwa urembo mwingi wa kufuma. Alionekana mchangamfu na kung'aa kama jua linalochomoza. Kichwani kwake alivaa taji la dhahabu na lulu yenye thamani na uzuri wa kushangaza. Gauni lake, lenye mchanganyiko wa rangi nyekundu iliyoiva na kijani, ilirashiwa dhahabu na kuwekwa mapambo ya lulu na Zamaradi. Walikuwepo wanawake wawili wa kumsaidia yeye binafsi, kila mmoja wao alikuwa amevalia taji la dhahabu, gauni la hariri lenye rangi ya zambarau, na makubazi yaliyotapakaa vito. Baada ya wageni wote kuketi kwenye nafasi zao, Abu Talib, mlezi wa Bwana harusi, alisimama na kusoma hotuba ya harusi.

"Utukufu na sifa zote ni zake mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na dunia, na shukrani zote ni Zake kwa neema Zake zote, riziki na huru-ma. Ametuleta sisi hapa duniani kutokana na vizazi vya Ibrahim na Ismael. Alitufanya sisi waangalizi wa Msikiti na kuwa viongozi wa Nyumba yake, Al- Kaaba, ambayo ni kimbilio la viumbe wake wote. Baada ya utangulizi huu Abu Talib aliendelea: "Mpwa wangu, Muhammad bin Abdullah bin Muttalib, ni mtu mzuri kuliko wote katika jamii ya binadamu kiakili, hekima, uzao ulio safi, utakatifu wa maisha yake mwenyewe, na kwa heshima ya familia. Anazo dalili zote za mtu ambaye hatimaye atakuwa mtu mkubwa. Anamuoa Khadija binti Khuwayled kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Natangaza kwamba Muhammad na Khadija sasa ni mume na mke. Mwenyezi Mungu na awabariki wote, na Awe Mlinzi wao." Kwenye hotuba yake, Abu Talib alitangaza kwamba ukoo wa Bani Hashim walikuwa warithi wa Ibrahim na Ismail, na walikuwa wabebaji au wachukuaji wa urithi huo. Kwa hiyo, hawakuchafuliwa na ibada ya masanamu.

Abu Talib alipomaliza hotuba yake, Waraqa bin Naufal alisimama kusoma hotuba ya harusi kwa niaba ya bibi harusi. Alisema: "Sifa zote na utukufu wote anastahili kupewa Mwenyezi Mungu. Tunashuhudia na kukiri kwamba yale ambayo umeyatamka kuhusu Bani Hashim ni kweli. Hapana mtu anayeweza kukanusha ubora wao. Kwa sababau ya uzuri wao, tunakubali ndoa ya Khadija na Muhammad. Ndoa yao inaziunganisha familia zetu mbili na kuoana kwao imekuwa chanzo cha furaha kubwa kwetu. Enyi Walezi wa Quraysh, nawatakeni kuwa mashahidi kwamba ninaridhia Khadija kuolewa na Muhammad bin Abdullah kwa mahari ya vipande 400 vya dhahabu. Mwenyezi Mungu na ajaalie ndoa yao iwe ya furaha."

(M. Shibli, mtaalam wa historia kutoka India, anasema kwamba mahari ya Hadhrat Khadija ilikuwa vipande 500 vya dhahabu - Siira). Amr bin Asad, ami yake Khadija mwenye umri mkubwa, naye pia alise-ma kwenye sherehe hiyo na aliyaunga mkono, kwa maneno yake mwenyewe, yale aliyoyasema Waraqa bin Naufal. Na alikuwa yeye ambaye kama mlezi, wa bibi arusi, aliridhika na kumtoa Khadija aolewe na Muhammad bin Abdullah. (Abu Talib alilipa mahari ya mpwa wake.) Edward Gibbon.

"Nyumbani na ng'ambo, wakati wa amani na vita, Abu Talib, ami wa Muhammad aliyekuwa anaheshimiwa sana, alikuwa kiongozi na mlezi wa kijana wake; wakati alipotimu miaka 25 alimuoa mwanamke tajiri mwenye daraja kubwa na mkazi wa Makka, ambaye aliuzawadia uaminifu wake kwa kukubali kuolewa naye pamoja na mali yake. Mkataba wa ndoa, katika jinsi rahisi ya kizamani, unasema kuhusu maelewano ya kimapenzi kati ya Muhammad na Khadija, unamwelezea yeye kama ni mtu hodari sana miongoni mwa kabila la Quraysh na unataja mahari ya wakia kumi na mbili za dhahabu na ngamia ishirini, ambayo ilitolewa kwa ukarimu wa ami wake." (Rejea: The Decline and Fall of Roman Empire) Washington Irving. "Khadija alijaa imani ya kusisimua aliyokuwa nayo kwa msimamizi wake bora sana, Muhammed. Kwenye sherehe ya harusi yake, Halima ambaye alikuwa yaya wa Muhammed wakati alipokuwa mtoto mchanga, aliitwa na kupewa zawadi ya kondoo arobaini." (Rejea: The Life of Muhammed). Wageni wote walimpa hongera Muhammad Mustafa siku ya harusi yake na walimtakia maisha ya furaha. Pia walimpongeza ami wake Abu Talib, kuhusu hafla yenye heri. Pande zote mbili Bwana na Bibi harusi, wali-washukuru wageni wao kwa uchangamfu.

Baada ya kwisha sherehe hizo, Mkuu wa Itifaki aliwaagiza watumwa kugawa chakula. Chakula kilikuwa kingi kupita kiasi kwani ilikuwa haijapata kutokea hapo Makka. Wageni walikula chakula kizuri sana na kila mlo ulikuwa wa mapishi ya aina yake. Wageni walituliza kiu kwa kinywaji kilichochanganywa na maji matamu yatokanayo na maua.

Baada ya chakula kila mgeni alipewa zawadi ya kanzu ya heshima, ili kuafikiana na mila za kale na uungwana wa Arabuni. Wakati huo huo mkuu wa Itifaki alitangaza kwamba Bibi harusi alikuwa tayari kuondoka. Ngamia jike aliyetandikwa mapambo ya kitajiri, alibeba kibanda mgongoni kwake, alikuwa anangoja kwenye lango la nyum-ba. Wageni wote walikusanyika sebuleni kumwona Bibi harusi akisindikizwa kwenye lango. Watumishi wake walimsaidia Bibi harusi kupanda kwenye kibanda cha harusi.

وَقَالَ ارْكَبُوا فِيهَا بِسْمِ اللَّـهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٤١﴾

"Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillah, kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu." (Qur'an 11:41)

Mmojawapo wa watumishi wa kike aliketi kwenye kibanda na Bibi harusi. Kwenye kichwa chake, alivalia tiara la maua na nywele zake zil- isokotwa kwa utepe wa buluu na ncha zenye lulu za kifahari. Alivalia bangili zenye nakshi ya vito vigumu na zenye kung'aa, na alishika kipepeo kilichopambwa na vito. Kikundi cha watumwa wa Kinubi walibeba mienge, walitembea mbele ya ngamia jike kulia na kushoto.

Bwana harusi naye pia alipanda farasi wake, na yeye, na ami zake, vijana wa Bani Hashim na wageni wao, walirudi nyumbani kwa Abu Talib katika hali na mavazi yale yale waliyoenda nayo mapema siku ile nyumbani kwa bibi arusi. Wakati msafara huu ulioongozwa kwa mienge ya moto ulipofika nyumbani kwa Abu Talib, mke wake na dada zake Abu Talib walimsaidia Bibi harusi kuteremka kutoka kwenye kipando chake, ngamia jike. Msimamizi mkuu alimkinga kwa mwavuli wa hariri nyeupe juu ya kich-wa chake na akamwongoza kwenye vyumba vya ndani zaidi kwenye nyumba hiyo.

وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾

"Na sema; Mola wangu Mlezi! Niteremshe mteremsho wenye bara-ka, na Wewe ni Mbora wa wateremshaji."(Qur'ani 23:29).

Kila kitu kilifanyika kwa usahihi wa kiwango cha juu sana. Mawasiliano yalikuwa mazuri sana toka mwanzo hadi mwisho. Kuoana kwa Muhammad na Khadija ni tukio lililomfurahisha kila mtu lakini furaha ya Abu Talib ilivuka mipaka ya kawaida. Alikuwa na dukuduku la kumuoza mpwa mke mzuri. Dukuduku hili liligeuka kuwa furaha kubwa isiyo na kifani baada ya mpwa wake na Khadija kuoana. Haingekuwa rahisi kupata malingano kama hayo. Abu Talib alimshuku-ru Mwenyezi Mungu kwa furaha mpya aliyoipata, na furaha yake iliwapata pia ndugu zake, Abbas na Hamza na watu wengine wote wa ukoo wa Hashim.

Siku tatu baada ya harusi, Abu Talib alifanya karamu ya chakula kush-erehekea tukio ambalo tangu hapo mpaka sasa linaitwa "karamu ya walima." Jiji lote lilinga'a kwa ukarimu wake. Kila mkazi wa Makka alikuwa mgeni mwalikwa wa karamu hiyo. Muhammad, ambaye alikuwa Bwana harusi, alikuwa anawakaribisha wageni. Yeye mwenyewe (Muhammad), ami zake, Binamu zake na vijana wote wa ukoo wa Bani Hashim, walijivunia kuwa wenyeji wa sherehe hiyo. Karamu hiyo ilidumu kwa muda wa siku tatu. Miaka mingi baadaye, Uislamu uliifanya karamu ya walima kuwa kumbukumbu ya karamu ya Abu Talib aliyoifanya kwenye harusi ya Muhammad na Khadija, na kuiweka kama desturi ya ndoa zote za Waislamu. Abu Talib alikuwa mtu wa kwanza kuitekeleza. Karamu ya walima haikujulikana katika bara lote la Arabu kabla ya harusi ya Muhammed na Khadija.

Abu Talib alilazimika kufikiri kama ingewezekana ndugu yake mpend-wa Abdullah na mkewe Amina, Mwenyezi Mungu awateremshie rehe-ma zake, wao pia kama wangekuwepo kushuhudia na kuibariki ndoa ya mtoto wao, na kushiriki pamoja katika ile furaha yake (Abu Talib). Lakini hata kama Abbullah na Amina wangekuwepo, harusi ya mtoto wao hainge sherehekewa kwa fahari na tamasha kuzidi alivyofanya Abu Talib kama mlezi wa Muhammad. Ilifuata zamu ya Khadija kuonyesha ukarimu na wema wake. Ukarimu na wema yalikuwa mazoea yake makubwa. Na hafla gani ambayo ingemfaa zaidi au kupendelea kama si kwenye sherehe ya harusi yake kutosheleza hulka yake? Kwa hiyo, Khadija, alimwagiza mkuu wake wa Itifaki kutayarisha mipango kwa kuandaa karamu na tafrija kubwa kabisa ya chakula na kuweka historia katika Makka.

Hiyo ilikuwa karamu ya kukumbukwa kweli. Hata ombaomba wa Makka na makabila ya watu wanaohama hapa na pale na wanawake, walikuwa kwenye kundi la waalikwa. Watu walikula vyakula ambavyo kamwe hawajapata kuviona. Wale Waarabu wa jangwani ambao kamwe walikuwa hawajawahi kuonja kitu chochote isipokuwa maji ya chumvichumvi au yanayonuka katika maisha yao siku hiyo walikunywa maji ya waridi wakiwa wageni wa Khadija. Kwa muda wa siku nyingi wageni waalikwa matajiri na fukara, mashuhuri na wenye daraja la chini, mamwinyi na wanyonge, vijana na wazee walikula nyumbani kwa Khadija. Khadija aliwapa wageni waalikwa walio maskini, vipande vya dhahabu na fedha na nguo, na alijaza nyumba za wajane wengi na watoto yatima mahitaji mengi ya muhimu ambayo hawakuwa nayo.

Khadija alikaa miaka mingi ya maisha yake akingojea mwanamume anayefaa kumuoa. Alipata mafanikio baada ya kungoja kwa muda mrefu alipojitokeza Muhammad, na wakaunganishwa katika ndoa takat-ifu. Ndoa ya Muhammad na Khadija ilikuwa ya kwanza na ya mwisho kwa aina yake hapa duniani. Ilikuwa ni ndoa hiyo tu duniani pote ambayo ilipata neema za akhera na mali za hapa duniani. Ilikuwa ndoa ambayo ilipata rehema nyingi zisizo na kipimo na hesabu za peponi na hapa duniani.

Inawezekana kabisa kwamba katika Bara Arabu lote, hakuna mwanamke yeyote ambaye alipata kwenda nyumbani kwa mumewe na mahari nyingi kiasi hicho kama alivyofanya Khadija. Ilijumuisha watumwa, wasichana, mbuzi na kondoo, na nguo zake binafsi za bei ghali, vitu vya ziada, vitu vya urithi visivyoweza kukadiriwa bei, mapambo, vitu vya thamani vya chuma, vito vya thamani na dhahabu nyingi na vipande vya fedha.

Mahari hii, ambayo haikutazamiwa kuwa hivyo kwa ubora na wingi wake, haikuwa zawadi aliyopewa Khadija, Bibi harusi na ami zake au kutoka kwa kaka zake. Haya yalikuwa ni matokeo ya jitihada zake mwenyewe. Alizalisha mali hiyo kwa uangalifu wake, bidii yake, busara zake na uwezo wa kuona mbali kifikira. Lakini huu haukuwa ndio tu utajiri aliokuja nao Khadija. Khadija pia alikuja na utajiri wa moyo na akili, na hivi vilikuwa havina kipimo na visivyokwisha. Katika miaka iliyofuata, Khadija aliyatajirisha pasipo kipimo maisha ya mumewe kwa kutumia vipaji hivyo. Mara tu Khadija alipoolewa, alionekana kupoteza upendeleo wake kwenye biashara na milki yake ya biashara. Maisha ya ndoa yalibadil-isha tabia yake, kujitolea kwake, na wajibu wake. Alimpata Muhammad Mustafa, hazina kubwa kuliko zote hapa duniani. Mara Khadija alipompata Muhammad, dhahabu, fedha na almasi zilipoteza thamani; kwake Muhammad Mustafa Mjumbe mtarajiwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume mtarajiwa wa Uislamu, akawa ndio tu, kitu cha kuelekeza mapenzi yake, uangalifu wake na bidii yake.

Mambo kama yalivyokuwa, hakupoteza uwezo wake mkubwa wa kupanga mambo, lakini badala ya kutumia uwezo huo katika biashara zake, aliutumia kwa kumtumikia mumewe. Aliyapanga maisha yake yote upya na kumfanya Muhammad Mustafa kuwa ndio mhimili wake wa maisha. Khadija hakusitisha biashara zake nyingi mara moja. Alizisimamisha kwa awamu. Kwa hiyo, kwa viwango alisimamisha biashara ya kuingiza mali ndani ya nchi na kutoa nje ya nchi ambayo baba yake aliianzisha.

Miaka iliyofuata baada ya ndoa yake, Muhammad alianza kusafiri tena na misafara ya Khadija kwenda Syria. M. Shibli, mtaalam wa historia kutoka India, anasema kwamba pia alikwenda Yemen. Popote alipok-wenda, alipata faida kubwa. Khadija pia aliajiri Mameneja wengine ambao waliuza bidhaa zake, au walinunua bidhaa kwa ajili ya mauzo yake, na wao pia walipata faida. Lakini, msisitizo ulibadilishwa, badala ya kupanua biashara yake kama alivyokuwa anafanya kabla ya kuolewa, Khadija alianza kupunguza bidhaa polepole hadi hapo ambapo bidhaa zote ziliuzwa, na alikusanya fedha zote kutoka kwenye miradi.

Wakati Malikia wa Makka alipoingia nyumbani kwa mumewe, Muhammad Mustafa, awamu ya maisha yake ya furaha kubwa ilianza. Awamu hii ilidumu miaka ishirini na tano - hadi kifo chake. Mara moja Khadija alibadili maisha yake na kuafikiana na mazingira mapya. Tangu siku ya kwanza alianza usimamizi wa kazi yake ambayo ilikuwa kuyafanya maisha ya mume wake kuwa ya furaha na mazuri. Katika kufanya kazi hii alifuzu vizuri sana kama historia ya siku zilizofuata ilivyosadikisha kwa ufasaha kabisa.

Maisha ya ndoa yalifungua ukurasa mpya ya maisha ya Muhammad na Khadija. Jambo la msingi la "ukurasa" huu mpya ilikuwa furaha - furaha isiyo na dosari. Pamoja na kwamba ndoa yao ilipewa baraka za furaha, pia ilipata neema ya watoto. Mtoto wao wa kwanza, alikuwa wa kiume aliyeitwa Qasim. Ilikuwa baada ya kuzaliwa Qasim, baba yake Muhammad Mustafa alipewa jina la Abul-Qasim - (Baba wa Qasim) - kufuatana na mila za kiarabu. Pia mtoto wa pili alikuwa wa kiume, Jina lake lilikuwa Abdullah. Alipewa majina ya lakabu ya Twahir na Twayyib. Watoto wote wawili walikufa wakiwa bado wachanga.

Mtoto wa tatu na wa mwisho na ndio huyo tu aliyeishi muda mrefu miongoni mwa watoto wa Muhammad na Khadija alikuwa binti yao, Fatuma Zahra, mtoto wa kike. Ingawa Mwenyezi Mungu aliwatunuku zawadi nyingi, hakukuwepo na chochote kile kingine walicho kithami-ni zaidi ya binti yao. Fatuma alikuwa "mwanga wa macho" ya baba yake, na alikuwa "starehe ya moyo wa baba yake." Alikuwa pia "Kiongozi wa Wanawake wa Peponi." Baba na mama walimpenda sana, na alileta pamoja naye matumaini na furaha na baraka na huruma Zake Mwenyezi Mungu ndani ya nyumba yao.