TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39054
Pakua: 2745

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39054 / Pakua: 2745
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

26

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA MAUN ( MANUFAA) (NA. 107)

INA AYA 7

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

أَرَأَيْتَ الَّذِي يُكَذِّبُ بِالدِّينِ ﴿١﴾

1. Je, umemwona (unamjua) yule ambaye anakadhibisha dini.

فَذَٰلِكَ الَّذِي يَدُعُّ الْيَتِيمَ ﴿٢﴾

2. Huyo ni ambaye humsukuma yatima.

وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ الْمِسْكِينِ ﴿٣﴾

3. Wala hahimizi kulisha maskini.

فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾

4. Basi ole wao wenye kuswali.

الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾

5. Ambao wanapuuza swala zao.

الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾

6. Ambao wao hujionyesha.

وَيَمْنَعُونَ الْمَاعُونَ ﴿٧﴾

7. Na wakazuilia (watu) manufaa.

UBAINIFU

Sura hii inaelezea kiaga anachopewa yule mwenye kusifika na sifa za kiunafiki kama vile kuipuuza swala kufanya ria na kuzuwiya misaada. Sura hii inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina. Na inasemekana nusu yake imeshuka Makka na nusu yake imeshuka Madina.

Aya Na 1

Neno Araayta lina maana ya kuona kwa macho au kwa kiakili. Makusudio ya dini hapa ni malipo siku ya malipo na kukadhibisha malipo maana yake ni kukadhibisha kufufuliwa. Imesemwa kuwa makusudio ya dini ni kwa maana ya mila.

Aya Na 2

Neno yaduu lina maana ya kusukuma na kufukuza kwa nguvu na jeuri. Hapa ina maana ya yule anayemsukuma na kumfukuza yatima kwa nguvu na jeuri bila ya kujali matokeo ya mabaya hayo ayafanyao. Lau hakukataa siku ya malipo angeliogopa siku hiyo. Na lau aliigopa siku hiyo angelimhurumia yatima.

Aya Na 3

Yaani ni yule ambaye hapendelei watu wawalishe maskini. Imekuja ibara ya kuhimiza, kwa vile kuhimiza kunaenea zaidi kuliko kufanya tu! Inasemekana kuna neno Twaam lina maana ya chakula kama lilivyo, kwa kufahamisha kwamba yule mwenye kupewa ni kama vile anamiliki kile anachopewa, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na katika mali zao ilikuwako haki ya kupewa maskini aombae na ajizuiae kuomba ." (51:19).

Na inasemwa Twaam katika aya ina maana ya kulisha.

Aya Na 4-5

Wanaopuuza swala ni wale wasiopatiliza swala wala hawajali kukosa swala zote au baadhi, au kuchelewa na wakati wake bora (wa mwanzo). Aya hii inawaunganisha wale wanaopuuza swala na wale wanaokadhibisha malipo, kufahamisha kuwa wao hawaachani na unafiki wao kwa vitendo huku wakijidhihirisha kwa imani.

Aya Na 6

Wanaojionyesha ni wale wanaofanya ibada kwa kujionyesha kwa watu, kwa hiyo wanafanya ibada kwa ajili ya watu na sio kwa ajili ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Aya Na 7

Neno Maun lina maana ya msaada wa aina yoyote inayoondoa dhiki au tatizo la aina yoyote kama vile kumkopesha mtu pesa, au kumfanyis wema au kumuazima chombo cha nyumbani.

Utafiti Wa Hadithi. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu Aya Na 1 anasema ilishuka kwa Abu Jahl na makafiri wa Kiquraish, na kuhusu Aya Na 5 wanakusudiwa wale wanaocha swala na wala sio kusahau, kwa sababu kila mtu anaweza kusahau katika swala. Amesema Abu Abdiallah(a.s) : "Ni kuichelewesha swala na wakati wake bila ya udhuru ". Katika Khiswal katika hadith ya mia nne imepokewa kutoka kwa Ali(a.s) amesema: "Hakuna amali inayopendeza zaidi kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuliko swala, kwa hivyo kisiwashughulishe chochote na swala kwani Mwenyezi Mungu amewashutumu watu kwa kusema: "Wale ambao swala zao wanazipuuza" yaani wanaopuuza wakati wake.

Katika Kafi kwa isnadi ya Muhammad bin Alfadhil, anasema: "Nilimuuliza mja mwema(a.s) kuhusu Aya Na 5 akasema ni kupuuza, na ziko riwaya nyingi katika madhumuni haya haya. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jariyr, Ibn Hatim na Bayhaqai kutoka ka Ali bin Abu Twalib kuhusu neno, wale amabo wanafanya ria ni kufanya ria katika swala. Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Abu Naim, Dilami na Ibn Asakir kutoka kwa Abu Hurayra naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kuhusu Aya Na 7 ni vitu wanavyosaidiana watu kama shoka, ndoo, sufuria nk.

Katika Kafi kwa Abu Baswir naye kutoka kwa Abu Abdiallah(a.s) amesema: "Na neno lake Mwenyezi Mungu (s.w.t): Na wakazuilia (watu) na manufaa" ni kuzuilia kukopeshana na kufanyiana mema na kuazimana vyombo vya nyumbani na pia kuzuilia zaka. Kilifasiri neno Maun kwa maana ya zaka pia imepokewa kwa njia ya Ahli Sunnah, kutoka kwa Ali(a.s) kama ilivyo katika Durril Manthur kuwa tamko Maun ni zaka ya wajibu. Yaani wanajionyesha katika swala zao na huku wanazuia zaka zao.

Katika hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Qani kutoka kwa Ali Ibn Abu Twalib(a.s) amesema: "Nimemsikia Mtume(s.a.w.w) akisema: "Muislamu ni ndugu ya muislamu mwengine anapokutana naye humuamkia kwa salam na humpatia kila chenye heri na hamzuilii Maun nikasema, "Ewe Mtume wa Mungu nini maun" akasema Mtume "ni jiwe, chuma, maji nk." Amefafanua Mtume(s.a.w.w) katika hadith nyengine kuwa chuma ni sufuria za shaba na shoka ya chuma. Na mawe ni nyungu za mawe.

SURA KAWTHAR (HERI NYINGI) (NA. 108)

INA AYA 3

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾

1. Hakika sisi tumekupa kheri nyingi.

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ﴿٢﴾

2. Basi mswalie Mola wako na uchinje mnyama.

إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الْأَبْتَرُ ﴿٣﴾

3. Hakika mwenye kukubughudhi wewe yeye ndiye mwenye kuishiwa.

UBAINIFU

Sura hii inaeleza kuneemeshwa kwa Mtume kwa kupewa neema nyingi. Na Sura hii ndiyo Sura fupi katika Qur'an. Mapokezi yamekithalifiana kuwa Sura imeshuka Makka au Madina, lakini inaonyesha kwamba imeshuka Makka. Wengine wamesema imeshuka mara mbili.

Aya Na 1

Imesemwa katika Majmau kwamba neno Kawthar liko katika kipimo cha Faw-al yenye maana ya wingi, kwa hiyo Kawthar ni heri nyingi. Wamehitilafiana kiajabu sana katika tafsiri ya neno Kawthar. Imesemwa kuwa ni heri nyingi, wengine wamesema ni mto peponi, wengine wamesema ni birika ya Mtume katika pepo au katika siku ya kukusanywa watu. Pia imesemwa ni watoto wake, masahaba wake, wafuasi wake mpaka siku ya Kiyama, au wanavyuoni wa umma wake.

Na imesemwa ni Uislamu, Tawhid, elimu na hekima, ubora wake, maqamu yenye kusifiwa, nuru ya moyo wake na zaidi ya hayo yamesemwa mpaka kufikia kauli ishirini na saita (26). Baadhi ya riwaya zimetegemea kwenye kauli mbili za mwanzo (heri nyingi na to katika pepo). Lakini kauli nyingine pia haziwezi kuachwa. Kwa hali yoyote iwayo. Neno abtar kwa dhahiri lina maana ya mwenye kukatikiwa na kizazi. Kwa hiyo makusudio hapa ya kawthar ni kizazi kingi, au heri nyingi kwa maana ya kuwa hicho kizazi ni heri nyingi lau kama si hivyo, basi ingelikuwa jumla ya aya ya haina faida yoyote.

Hadith zimeeleza kwamba Sura hii ilishuka, kutokana na mtu mmoja aliyemtusi Mtume(s.a.w.w) , kwa kuwa eti amekatikiwa na kizazi chake kutokana na kufa kwa watoto wake wa kiume (Kassim na Abdulla). Kwa hivyo Mwenyezi Mungu akamrudishia majibu kwa kusema huyo mwenye kukubughudhi wewe ndiye abtar aliyekatikiwa na heri zote: Neno "hakika sisi tumekupa wewe", limekuja kwa wingi kwa kuadhimisha tu. Jumla yote hiyo ya maneno inafahamisha kuwa kizazi cha Fatima(a.s) ni kizazi cha Mtume(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu amekifanya kingi sana kizazi hicho kuliko kizazi kingine chochote pamoja na misiba iliyowashukia na kuuliwa kwa makundi katika mauaji ya kuchukiza na ya kinyama.

Aya Na 2

Kushukuru neema ni jambo linalotakikana. Hapa Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume wake kuwa tumekupa heri nyingi, basi wewe shukuru neema hiyo kwa kusali na kuchinja mnyama. Imesemekana maana ya ayah ii ni kuswali swala ya Idd na kuchinja mnyama. Pia imesemwa maana ya neno wanhar ni kunyanyua mikono miwili katika swala wakati wa kusoma takbira.

Aya Na 3

Imesemwa maana ya neno abtar hapo ni kuepukana na heri au kuepukana na watu wake. Yatakuja maelezo katika utafiti wa hadith. Neon shani ni yule mwenye kubughudhi naye ni Asi bin Wail.

Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Bukhari, Ibn Jariyr na Hakim kwa njia ya Abu Bashar kutoka kwa Said bin Jubayr naye amepokea kutoka kwa Ibn Abbas kwamba yeye amesema: "Kawthar ni heri alizopewa Mtume". Abu Bashar akasema kumwambia Said bin Jubayr: "Hakika watu wanadai kuwa kawthar ni mto katika pepo". Akajibu "mto katika pepo ni katika heri ya Mwenyezi Mungu aliyompa Mtume wake." Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim, Hakim, Ibn Murdawayh na Bayhaqi katika hadith zake kutoka kwa Ali bin Abu Twalib(a.s) amesema:

"Iliposhuka Sura ya Kawthar, Mtume(s.a.w.w) alisema kumwambia Jibril: Ni uchinjo gani huu alioniamrisha Mungu? Jibril akasema: "Sio uchinjo isipokuwa anakuamrisha kunyanyua mikono yako katika swala wakati wa kuhirimia, kurukui na wakati wa kunyanyua kichwa baada ya rukui, kwani hiyo ndiyo swala yetu na swala ya Malaika walioko katika mbigu saba, na kwamba kila kitu kina kipambo chake na kipambo cha swala ni kunyanyua mikono miwili kila unaposoma takbira. Katika Majmau imepokewa kutoka kwa Muqatil naye kutoka kwa Asbagh bin Nabata, kisha akasema wamepokea Thaalabi na Wahidi katika tafsiri zao, kwamba imepokewa kutoka kwa kizazi chote kitakatifu cha Mtume kitabu hicho hicho ametoa Ibn Jariyr kutoka kwa Abu Jaffar kwamba maana ya msalie Mola wako, ni swala na maana ya wanhar ni unyanyue mikono miwili unapotoa takbira mwanzo wa swala.

Tena katika hiyo hiyo Majmau ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas kuhusu Aya Na 2 amesema: Hakika Mwenyezi Mungu alimpelekea Wahyi Mtume wake kwa kusema : "Nyanyua mikono yako muelekeo wa sehemu ya juu ya kifua hiyo ndiyo nahr". Katika hiyo hiyo Majmau imepokewa kutoka kwa Umar bin Yazid amesema: "Nimesikia Abu Abdillahi akisema? Maana ya wanhar ni kunyanyua mikono yako pambizoni mwa uso wako. Na pia imepokewa kutoka kwa Abdulla bin Sinan mfano wa hadith iliyo karibu na maana hayo kutoka kwa Jamil. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Saad na Ibn Asakir katika njia ya Kalabi kutoka kwa Abu Saleh naye kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Alikuwa mtoto mkubwa wa Mtume(s.a.w.w) ni Kassim kisha Zaynab, Abdulla, Ummu Kulthum, Fatima na Ruqayya. Akafa Kassim, naye ndiye maiti wa kwanza katika kizazi chake, kisha akafa Abdullah. Ndipo akasema Asi bin Wail Assahmi :"Kizazi chake kimekwisha katika, kwa hiyo yeye ni abtar. Basi akateremsha Mwenyezi Mungu; Hakika mwenye kukubughudhi wewe yeye ndiye abtar (mwenye kuepukana na heri zote)".

Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim kutoka kwa Assadi amesema. "Walikuwa Maquraish wakisema: mtu anapofiwa na mtoto wa kiume, ni abtar basi alipokufa mtoto wa Mtume(s.a.w.w) , Asi bin Wail akasema Mtume ni abtar. Tena katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Zubeir bin Bakar na Ibn Muhhamd kutoka kwa baba yake amesema: "Alikufa Kassim mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu huko Makka, Mtume alipokuwa akitoka kuzika akapita kwa Asi Bin Wail akiwa na mtoto wake Amru, akasema alipomwona Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . "Mimi ninamchukia sana." Akasema Asi: "Achana naye kwani yeye ameshakua Abtar". Mwenyezi Mungu ndio akateremsha Sura hiyo.

Ibn Abi Hatim amepokea kutoka kwa Assadi amesema: "Mtu anapofiliwa na mtoto wa kiume, Quraish walikuwa wakisema: "Fulani ameshakuwa abtar." Basi alipokufa mtoto wa Mtume(s.a.w.w) Asi bin Wail alisema : "Amekuwa abtar". Wamehitalifiana juu ya aliyembughudhi Mtume(s.a.w.w) ; wengine wanasema ni Walid bin Al-Mughira, wengine wanasema ni Abu Jahl, wengine ni Uqbah bin Abu Muiit na wengine wanasema ni Ka'ab bin Ahsraf. Lakini kauli yenye tutegemewa ni ile inayomtaja Asi nin Wail.

Hayo yanatiliwa nguvu na yale yaliyo katika Ihtijaj ya Tabrasiy kutoka kwa Hasan bin ali(a.s) katika hadith anayomwambia Amru bin Al-Asi: "Hakika wewe umezaliwa kutokana na kitanda kilichoshirikianwa, wakabishana juu yako wanaume wa Kiquraish ambao ni Abu Sufyan bin Harb, Walid bin Al-Mughira, Uthman bin Al-Harith, Annadhri bin Al-Harith bin Kaldah na Asi bin Wail. Kila mmoja anadai kuwa wewe ni mtoto wake, ndipo akashinda yule mchafu wao zaidi.

Katik Tafsiri ya Qummi amesema Kawthar ni mto katika pepo aliopewa Mtume badala ya mtoto wake Ibrahim (aliyekufa). Kwa vyovyote iwavyo kutafsiri Kawthar kuwa ni mto katika pepo hakupingani na tafsiri ya heri nyingi, kama yalivyokwisha tangulia maelezo ya Ibnu Jubeir.

SURA KAFIRUN (MAKAFIRI)(NA. 109)

INA AYA 6

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ﴿١﴾

1. Sema: Enyi makafiri

لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٢﴾

2. Mimi siabudu mnachokiabudu.

وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٣﴾

3. Wala nyinyi hamkiabudu ninachokiabudu mimi.

وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ﴿٤﴾

4. Wala mimi sitaabudu mnachokiabudu nyinyi.

وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٥﴾

5. Wala nyinyi hamtakiabudu ninachokiabudu mimi.

لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾

6. Nyinyi mna dini yenu, na mimi nina dini yangu.

UBAINIFU

Katika Sura hii Mwenyezi Mungu anamwamrisha Mtume kudhihirisha kujitenga kwake na dini yao. Dini yake haingilii dini yao wala dini yao haingilii dini yake. Yeye katu haabudu lile wanaloliabudu wala wao katu hawaabudu anachokiabudu. Kwa hivyo wakate tamaa na namna yoyote ile ya kudanganya. Wamekhitalifiana wafasiri kuwa Sura imeshuka Makka au Madina, lakini mpangilio wa maneno unaonyesha kuwa imeshuka Makka.

Aya Na 1

Kwa dhahiri ni watu maalum sio makafiri wote. Hilo linafahamisha kuamrishwa kwake Mtume(s.a.w.w) kuwambia makafiri kutakasika kwake na dini yao na kujizuilia kwao na dini yake.

Aya Na 2

Makusudio ya kile mnachokiabudu, ni masanamu waliyokuwa wakiyaabudu. Herufi laa hapa ni ya kukanusha kwa muda ujao (mustaqbal) na herufi maa ni ya muda wa sasa hivi. Yaani siabudu milele kile mnacho kiabudu hivi sasa katika msanamu.

Aya Na 3

Pia ni ya kukanusha kwa muda ujao yaani kumpa habari Mtume(s.a.w.w) kwamba makafiri hawataabudu kile anachokiabudu Mtume(s.a.w.w) kama walivyokuwa wakidai. Kwa kuunganisha amri iliyo katika mwanzo wa maneno, aya hizi mbili zinaonyesha ya kwamba Mwenyezi Mungu ameniamrisha kudumu kumuabudu Yeye. Halikadhalika ameniamrisha kuwaeleza kama nyingi hamtamuabudu katu. Kwa hivyo hapana ushirikiano wa dini kati yangu na nyinyi. Ayah ii ina maana sawa na ile aya isemayo: "Bila shaka kauli (ya adhabu) imehakikika juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini ." 36:7.

Halikadhalika inakubaliana na aya isemayo: "Hakika wale waliokufuru (Kwa ukaidi na inadi) ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini ". (2:6). Ilikuwa sawa ni kusema: "Wala nyinyi siwenye kuabudu ninayemuabudu". Lakini imesemwa "Ninachokiabudu". Kwa jili ya kufuata mpangilio ulioanzia: "Siabudu mnachokiabudu".

Aya Na 4-5

Ni kutilia mkazo yale yaliyotangulia, kama ilivyo katika Sura ya (102: 3-4); aliposema: "Komeni punde kidogo tu! Mtajua kisha komeni punde kidogo tu! Mtajua ". Na katika Sura (74: 19-29):

"Amelaaniwa, namna gani alivyokadiria (kutia ila Qur'an) kasha amelaaniwa, namna gani aliyokadiria (kutia ila Qur'an) ."

Imesemekana kuwa ma katika neno Abadtum sio mausul yenye maana kurejea kwenye jina, bali ni ya masdariya ya kufanya jina la kitendo yenye maana wa Wala mimi siabudu ibada yenu wala nyinyi siwenye kuabudu ibada yangu. Kwa maana kuwa siwashirikishi wala hamnishirikishi si katika mwenye kuabudiwa wala ibada. Ninayemuabudu mimi ni Mungu na mnayeabudu nyinyi ni sanamu. Na ibada yangu ni ile aliyoiweka Mwenyezi Mungu, lakini ibada yenu ni ile mliyoizusha wenyewe kwa ujinga na uzushi. Yatakuja maelezo katika utafiti wa hadith (Inshallah).

Aya Na 6

Nikuzidi kutilia mkazo kukanusha kushirikiana. Na herufi lam ni ya kuhusisha, yaani dini yenu ya kuabudu masanamu inahusika na nyinyi na hii dini yangu inahusikana na mimi tu! Inasemekana kwamba dini hapa ina maana ya malipo yaani; Mna malipo yenu na nina malipo yangu. Na inasemekana pia kuna kitu kilichoondoshwa yaani, mna malipo ya dini yenu nami nina malipo ya dini yangu. Lakini njia mbili zote hizo, ziko mbali na ufahamu.

Utafiti Wa Hadithi Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jariyr, na Ibn Abu Hatim na Ibn Anbari, kutoka kwa Said Ibn maynai Huru (aliyekuwa mtumwa) wa Abul Bakhtari amesema: "Walid bin El-Mughira, Asi bin Wail, sa-wad bin El-Mutwalib na Umayya bin Khalaf, walikutana na Mtume wakamwambia "Ewe Muhammad ! njoo tuabudu kile unachokiabudu na wewe uabudu kile tunachokiabudu na tushirikiane sisi na wewe katika mambo yetu yote, ikiwa haya yetu ni sahihi zaidi kuliko yako, basi utakuwa umepata cha kupata, na kama ikiwa yale unayoyaabudu wewe ni sahihi zaidi kuliko yetu, basi tutakuwa tumechukua la kuchukua". Mwenyezi Mungu ndio akateremsha Sura hiyo yote.

Katika Tafsiri ya Qummi amepokea kutoka kwa baba yake naye amepokea kutoka kwa Ibn Abu Umeir amesema: "Abu Shakir alimuuliza Abu Jaffar El-Ahwal kuhusu Sura ya Kafirun "Jee Mwenye hekima anasema maneno kama haya na kuyarudia mumo kwa mumo? "Abu Jaffar El-Ahwal hakuwa na jibu. Basi akaenda Madina kumuuliza Abu Abdillahi(a.s) akasema: :Sababu ya kushuka Sura hiyo na kukariri maneno hayo, ni kwamba Maquraish walimwambia Mtume(s.a.w.w) : 'abudu miungu wetu mwaka mmoja na tuabudu Mungu wako mwaka mmoja na tena abudu miungu wetu mwaka moja na tuabudu Mungu wako mwaka mmoja".

Mwenyezi Mungu akawajibu kama vile walivyo sema. Akasema juu ya yale waliyoyasema kuwa aabudu miungu yao mwaka alisema: Sema enyi makafiri. Mimi siabudu mwachokiabudu. Na katika yale waliyoyasema kuwa watamwabudu Mungu wake mwaka alisema: Wala nyinyi hamkiabudu ninachokiabudu mimi. Na juu ya yale waliyosema aabudu miungu yao mwaka mmoja alisema: Wala mimi siabudu mnachokiabudu nyinyi.

Na katika yale waliyoyasema wataabudu Mungu wake mwaka mmoja alisema: Wala nyinyi hamtakiabudu ninachokiabudu mimi. Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu. Akarudi Abu Jaffar El-Ahwal kwa Abu Shakir akampa habari juu ya hayo!

27

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA NASR (MSAADA)NA 110

INA AYA 3

Kwa jina la allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

إِذَا جَاءَ نَصْرُ اللَّـهِ وَالْفَتْحُ ﴿١﴾

1. Utakapokuja msaada wa Allah na ushindi.

وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّـهِ أَفْوَاجًا ﴿٢﴾

2. Ukawaona watu wanaingia katika dini ya Allah makundi makundi.

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا ﴿٣﴾

3. Basi hapo mtakase Mola wako pamoja na kumsifu na umwombe maghufira. Hakika yeye ni mwingi kukubali toba.

UBAINIFU

Mwenyezi Mungu alimwahidi Mtume(s.a.w.w) ushindi na kwamba yeye atawaona watu wakiinga katika Uislamu makundi kwa makundi, akamwamrisha kufanya tasbih, tahlil na istighfar. Sura hii imeshuka Madina baada ya Sul-hul Hudaibiya (mapatano ya Hudaibiya) na kabla ya ushindi wa Makka, kama vile itakavyobainika.

Aya Na 1

Idha ni neno linaloonyesha muda ujao, kwa hiyo madhumuni ya aya hii ni kulitolea habari jambo litakalo hakikika baadaye. Ikiwa jambo linalotolewa habari ni msaada na ushindi na hilo ni katika mambo yanayomtuliza moyo Mtume, basi ni ahadi nzuri na biashara kwake. Msaada na ushindi uliokusudiwa hapa sio ule ambao amempatia Mwenyezi Mungu katika msimamo wake wote kama vile ushindi juu ya maadui zake katika vita na iman ya Ansar na watu wa Yemen, wala pia sio makusudio ya Sulhul Hudaibiya (mapatano ya amani ya Hudaibiya) ambayo Mwenyezi Mungu ameyaita ushindi wakati aliposema: "Hakika sisi tumekupa ushindi ulio wazi ". (48: 1).

Kwa vile Aya Na pili haioani na madhumuni yake. Kwa hiyo makusudio hapa ni ushindi wa kuiteka Makka ushindi ambao ulikuwa ndio mama wa ushindi wake Mtume(s.a.w.w) katika zama za ushindi wake na ulikuwa msaada wa ushindi ambao ulivunja vizingiti vya ushirikina katika Bara-arabu.

Hayo yanatiliwa nguvu na kiaga cha msaada uliotajwa katika aya zilizoshuka katika Sul-hul Hudaybiya: "Hakika sisi tumekupa ushindi ulio wazi, ili Allah akusamehe makosa yako yaliyotangulia na yanayokuja, na kukutimizia neema zake na kukuongoa katika njia iliyonyooka. Na akunusuru Allah nusura (msaada) yenye nguvu habisa " (48:1-3).

Lililo karibu zaidi kufahamika kutokana na yaliyomo katika aya hizo ni msaada wa Mwenyezi Mungu kwa Mtume(s.a.w.w) wake juu ya Maquraish kwa kuichukua Makka ijapokuwa ni baada ya kupita miaka miwili baada ya ushindi wa Alhudaibiya. Pia hayo ni jawabu la madai kuwa ni kuitikia watu wa Yemen kuiingia kwao katika Usilamu, bila ya vita. Yenye kukubalika ni kuwa kusudio la ushindi hapa ni ushindi wa Mtume(s.a.w.w) juu ya Maquraish na kuiteka Makka. HAya Na nadhihirisha kuwa Sura hii iliteremka baada ya Sulhul Hudaibiya kuteremka Suratul Fath (ushindi) na kabla ya kutekwa Makka.

Aya Na 2

Raghib amesema: Fawj ina maana ya makundi yanayopita kwa haraka. Wingi wa Fawj ni Afwaja. Maana ya kuingia watu makundi ni kuingia kundi baada ya kundi jengine. Makusudio ya dini, ni dini ya Kiislamu, kama alivtyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika dini mbele ya Allah ni Uislamu ." (3:19)

Aya Na 3

Msaada huu na ushindi huu, ni namna mojawapo ya kuidhalilisha shirki na kuipa nguvu Tawhid. Au kwa maneno mengine, kuibatilisha batili na kuihakikisha haki. Basi hayo yananasabiana na kumtakasa Mwenyezi Mungu, na kumsabihi kwa upande wa kwanza na kumsifu (Sifa) Menyezi Mungu na kumshukuru kwa upande wa pili. Ndio akaamrishwa Mtume(s.a.w.w) ikasemwa (Mtakase mola wako pamoja na kumsifu na umtake msamaha.) Mwelekeo mwengine wa amri ya kumtakasa Mungu, kumsifu na kumtaka msamaha, ni kwamba ni juu ya mja kumkumbuka mola wake kwa sifa za ukamilifu wake, na kujikumbusha (mja) upungufu wake na haja yake. Ilivyokuwa kwamba ushindi huu umemaliza lile alilokuwa akilihangaikia Mtume(s.a.w.w) katika kuondoa batili na kukata shina la ufisadi, basi ameamrishwa Mtume(s.a.w.w) kumkumbuka Mola wake kwa utukufu na mwisho kujikumbusha upungufu wake wa kumhitajia kwake Mwenyezi Mungu ambako nikutaka maghufira. Maana ya kutaka maghufira, (msamaha) hapa ni kudumu hayo maghufira, kwani Mtume(s.a.w.w) amekwisha ghufiriwa.

Utafiti Wa Hadithi Katika Majmau imepokewa kutoka kwa Muqatil. Iliposhuka Sura hii, Mtume(s.a.w.w) aliwasomea Masahaba zake, wakafurahi. Alipoisikia Abbas alilia. Mtume(s.a.w.w) akamwambia: "Ni lipi linalokuliza ewe ami?" Akasema Abbas: "Ninadhani umejitolea habari za kifo chako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu." Akasema Mtume(s.a.w.w) : "Ndio kama unvyosema". Basi akaishi baadae miaka miwili, hakuonekana akicheka kwa furaha. Simepokewa hadith nyingi kwa maana haya. Katika hiyo Majmau, imepokewa kutoka kwa Ummu Salama, amesema: "Alikuwa Mtume(s.a.w.w) siku za mwisho hasimami wala hakai, wala hendi au kuja mahali illa husema: "Subhanallahi wabihamdihi, astaghfirullah waatubu ilaihi." Kutakakata na maovu ni kwa Mwenyezi Mungu na pamoja na kumsifu. Namtaka maghufira Mwenyezi Mungu na ninarejea (tubia) kwake." Tukamuuliza juu ya hilo, akasema: "Hakika mimi nimeamrishwa hilo" kisha akasoma "Sura ya Idhaa- jaa (Nasr).

Pia ziko hadith zaidi zilizokuja kwa maana haya, lakini kwa kuhitalifiana yale aliyoyasema Mtume(s.a.w.w) . Katika kitabu cha Uyun kwa isnadi yake kwa Hussein bin Khalid, amesema: "Amesema Ridha(a.s) : "Nimemsikia baba yangu anazungumza kutokana na baba yake(a.s) kwamba Sura ya kwanza ni Iqraa (Alaq) na Sura ya mwisho kushuka ni Idha-jaa (Nasr)". Huenda ikawa makusudio ni Sura ya mwisho kushuka ikiwa kamilifu.

Katika Majmau, katika kisa cha ushindi wa Makka imesemwa: Alipotiliana mkataba wa amani Mtume(s.a.w.w) pamoja na Maquraish, katika mapatano ya Hudaibiya (Sulhul-Hudaibiya), ilikuwa moja ya masharti ni kwamba atakayetaka kujiunga na Mtume(s.a.w.w) aruhusiwe. Basi kabila la Khuzaa likajiunga na Mtume(s.a.w.w) , na Bani Bakr wakajiunga na Maquraish, makabila haya mawili yalikuwa na ugomvi mkubwa sana tangu zamani. Baadaye vikazuka vita kati ya Bani Bakr na Khuzaa. Maquraish wakawa wanawapa silaha Bani Bakr, na pia wakawa wanawasidia kupigana wakati wa usiku hali ya kujificha. Miongoni mwa waliokuwa wakiwasaidia ni Akrama bin Abu Jahal na Suhail bin Amru.

Mtu mmoja katika Khuzaa anayeitwa Amru bin Salim, akasafiri hadi Madina kwa Mtume(s.a.w.w) . Na hilo lilikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyoleta harakati za ushindi wa kuiteka Makka. Basi Salim akasimama mbele ya Mtume alipokuwa msikitini katikati ya watu na akasema: "Leo mimi meazimu mumwona Muhammadi Rafiki mwema rahimu Ja mzaziwe wa jadi Quraishi madhalimu wamepangua ahadi Miadi yako muhimu wameivunja kusudi wakatuua kaumu Rukuuni na Sujudi". Mtume akasema kumwambia Amru: :Inatosha ewe Amr". Kisha akasimama akaingia nyumba ya mkewe Maymuna Akamwambia: "Nimiminie maji" Akawa anajiosha huku akisema "Kama sikulisaidia kundi la Amr basi itakuwa sikusaidia kitu." Baadaye akaja tena kwa Mtume(s.a.w.w) Badil bin War'qai na kikundi cha Bani Khuzaa wakampasha habari Mtume(s.a.w.w) yale wanayofanyiwa na Maquraish na jinsi walivyojitokeza kuwasaidia bani Bakr.

Kisha wakaenda zao kurejea Makka. Mtume(s.a.w.w) alikuwa ameshawaambia watu: Naona kana kwamba Abu Sufiani atakuja kuitilia nguvu mkataba na kuongeza muda wake. Walipofika sehemu inayoitwa Asfa na wakakutana na Abu Sufiani akiwa ametumwa na Maquraish ili aongeze muda wa Mkataba. Basi Abu Sufiani alipokutana na hao jamaa alimuuliza Badil, "umetoka wapi?" Badil akamwambia "nimekwenda katika mwambao huu ndani ya wangwa huu". Akauliza tena Abu Sufiani, "hukumwendea Muhammad ?" Akajibu, "La!" Basi alipoondoka Badil kuelekea Makka Abu Sufiani akajisemea, "Ikiwa ametoka Madina atakuwa amemlisha ngamia wake kokwa za tende," kwa hivyo akaenda pale alipokuwa ametulia ngamia wa Badil akachukua kinyesi chake na kukichangua, akaona kokwa za tende, akasema,: "Ninaapa kuwa Badil ametoka Madina kwa Muhammad".

Kisha katoka Abu Sufiani mpaka kwa Mtume(s.a.w.w) akamwambia "Ewe Muhammad ilinde damu ya watu, upatane na Maquraish na uongeze muda wa Mkataba wetu." Mtume(s.a.w.w) akasema: "Ewe Abu Sufiani mnajifanya wajanja !" Akasema "La! Sisi bado tunashikilia mkataba wetu na amani" Akatoka Abu Sufiani akakutana na Abu Bakr akasema "Fanya mapatano na Maquraish." Aby Bakr akajibu "Ole wako! Kuna mtu anayeweza kufanya mapatano zaidi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ". Kisha akakutana na Umar akamwambia hivyo hivyo. Kisha akatoka akaingia nyumbani kwa Ummu Habiba, (mke wa Mtume) akawa anataka kukaa kwenye tandiko. Ummu Habiba akanyanyua tandiko na kulikunja, akasema: "Ewe binti yangu kwa nini unanikataza kukalia hili tandiko?" Akasema: "Ndio hili ni tandiko la Mtume wa Mwenyezi Mungu haiwezekani ulikalie wewe najisi unayemshirikisha Mwenyezi Mungu."

Basi akatoka akaingia nyumba ya Fatima(a.s) akamwambia: "Ewe binti wa bwana wa waarabu, hufanyi mapatano na Maquraishi na kuongeza muda wa mkataba ili uwe bibi mkarimu zaidi katika watu?" Akasema" "Mapatano yangu ni mapatano ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Kisha akasema: "Basi waamrishe watoto wako (Hassan na Hussein) wafanye mapatano" Akasema: "Hawajafikia watoto wangu kufanya mapatano, na hakuna yeyote anayeweza kufanya mapatano zaidi ya Mtume(s.a.w.w) .

Akasema: Abu Sufiani "Ewe Abul-Hassan(a.s) naona mambo yamekuwa magumu, nishauri". Akasema Ali(a.s) "Wewe ndiwe mzee wa Maquraish, basi simama msikitini uwapatanishe Maquraish. Halafu wende zako kwenu". Abu Sufiani akasema: "Unaona kua hilo litatosha?" Akasema: "Hapana wallah sioni hivyo, lakini sina jengine zaidi ya hilo". Basi akasimamam Abu Sufiani msikitini akasema: "Enyi watu! Hakika mimi ninataka mapatano kati ya Maquraish". Akapanda ngamia wake akaenda zake, alipofika kwa Maquraish akaulizwa, akawapa kisa, wakasema: "Wallah Ali Bin Abu Twalib hakukufanyia lolote ila kukuchezea tu". Tumefaidika nini kwa hayo uliyasema? Akasema : "Lakini sikupata jengine zaidi ya hilo.

Mtume(s.a.w.w) akaamrisha maandalizi ya vita vya kuipiga Makka. Akawaamrisha watu wajitayarishe. Akaomba dua kwa kusema: "Ewe Mwenyezi Mungu yapoteze macho na ziepushe habari zetu hizi na Maquraish mpaka tuwaiingilie mjini mwao ghafla". Hatib bin Abu Bal-Taah akawaandikia Maquraish kuwafahamisha habari hizi za vita, lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu akapata habari kutoka mbinguni, akamtuma Ali(a.s) na Zubeir kuchukua barua ka mwanamke aliyetumwa na Hatib. Kisa cha barua hii kimeelezwa zaidi katika Sura ya 60.

Kisha mtume(s.a.w.w) akatoka na jeshi la Waislamu elfu kumi wakiwemo wapanda farasi mia nne. Hakubakia yeyote katika Muhajirina na Ansar. Akamwacha Abudharr El- Ghifari kuwa khalifa wake hapo Madina. Ikatokea Abu Sufiani bin Harith bin Abdul Muttwalib na Abdalla bin Ummay kukutana na Mtume(s.a.w.w) kati ya Makka na Madina wakaomba kukutana na Mtume lakini hakuwapa idhini. Ummu Salama akamwambia Mtume: "Ewe Mtume na Mwenyezi Mungu binamu yako ni mkoi wako aliye mkweo (hao hapo)." Mtume akasema: "Sina haja nao; huyo binamu yangu ndiye aliyevunja heshima yangu na huyo mkoi aliye mkwe wangu ndie aliyesema aliyoyasema juu yangu huko Makka." Basi walipopopata habari hiyo, Abu Sufiani ambaye alikua pamoja na mtoto wake akasema: "Wallah! kama hataniruhusu kusema naye nitakwenda mbali pamoja na mtoto wangu huyu mpaka tufe kwa kiu na njaa." Mtume alipopata habari hiyo akawaonea huruma, hivi akawaruhusu kuzungumza naye na wakasilimu."

Mtume(s.a.w.w) alipopita Dhahran, huku Maquraish wakiwa hawana habari yoyote, alitoka usiku huo Abu Sufiani bin Harb, Hakim bin Huzam na Badil bin Warqai wakipeleleza Abbas alikuwa amekwishasema usiku huo: "Ee kupambaukiwa kubaya kwa Maquraish; kama Mtume akifanikiwa kuwavamia kuingia Makka, basi ndio itakuwa kuangamia kwa Maquraish milele." Akaendelea kusema: " Wacha nitoke huenda nitakamwona, kidomo domo au muuza maziwa au yeyote yule anayeingia Makka ambaye anaweza kwenda kuwapa habari Maquraish wakaweza kumjia Mtume(s.a.w.w) .

Abbas anaendelea kusema: "Wallah nilipokua nazunguuka kwenye miti ya miswaki, mara nikasikia sauti ya Abu Sufiani, Hakim bin Hizam na Badil bin Warqai, nikamsikia Abu Sufiani akisema: "Wallahi sijaona moto kama huu wa leo", akasema Badil: "hii ni mioto ya Bani Khuzaa." Akasema Abu Sufiani "Khuzaa niwachache kuliko hao". Basi nikajua sauti yake nikamwambia: "Ewe Abu Handalah (Abu Sufiani)!" Akasema "Ewe Abul Fadhli" nikasema "Naam!" Akasema" "Labeka! Baba yangu na mama yangu wawe wakombozi wako! Niambie kuna nini nyuma yako? Nikamwambia " Huyo hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu amekuja na kundi la Waislamu wasiopungua Elfu Kumi (10,000).

Akasema : "Sasa unasemaje?" Nikamwambia "Panda juu ya mgongo wa ngamia huyu na nitakutakie amani kwa Mtume: "Kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu wakikupata wataikatilia mbali shingo yako." Basi nitatoka naye, kila nilipokuwa nikipita kwenye kikundi fulani walikuwa wakisema huyo ni Ami wa Mtume na yuko juu ya ngamia wa Mtume mpaka tulipofika katika kundi la Umar bin Al-Khattab akasema Umar: "Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kukupata wewe bila ya taabu wala mapatano yoyote."

Kisha tukafanya haraka tukaelekea kwa Mtume(s.a.w.w) , akatangulia Umar kwa Mtume, akasema : "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu huyu Abu Sufiani adui wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu amekuletea bila matatizo yoyote, kwa hiyo wacha nimkate shingo yake!" Nikasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mwacheni kwanza." Lakini Umar alikuwa bado anashikilia tu! Basi nikwambia" "Ngoja ewe Umar". Huyu mtu ni katika watu wa Bani Abdu Manaf, lau angelikuwa ni katika Bani Adi nisingesema, hivyo Akasema Mtume(s.a.w.w) : "Nenda naye mpaka kesho."

Basi kulipopambazuka, nikaenda naye kwa Mtume(s.a.w.w) , alipomwona akasema: "Ole wako ewe Abu Sufiani! Bado hujafikiwa kujua kuwa hapana Mola illa Mwenyezi Mungu? Akasema: "Mkombozi wako ni baba yangu na mama yangu ni huruma zako zilioje na upole wako!, Wallah nimedhani kwamba, lau angelikuwako Mungu mwingine, basi angelitosheleza siku ya vita vya Badr na Uhud". Akasema tena Mtume(s.a.w.w) : "Je, bado hujafikiwa kujua kwamba mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: "Ama hili moyoni mwangu mna kitu". Basi nikamwambia: "Ole wako! Toa shahada ya kweli kabla hawajakiondoa kichwa chako", basi akashahadia."

Mtume(s.a.w.w) akamwambia Abbas: "Nenda naye na umfunge kwenye njia ya jangwani mpaka jeshi la Mwenyezi Mungu lipite." Anaendelea kusema Abbas: "Nikamfunga kwenye jabali, yakawa yanapita makabila mbali mbali na yeye anasema : "Ni nani hawa" nikamjibu: "Aslam, Juhayna na Fulani na ?.." mpaka akapita Mtume(s.a.w.w) katika kikosi cha kijani wakiwemo Muhajirina na Ansar akiwa amezungukwa huko na huko. Akasema Abu Suffiani "Ni kina nani hawa? Nikamwambia: "Huyu ni Mtume, wa Mwenyezi Mungu akiwa pamoja na ndugu yako amekuwa mfalme mkubwa" Nikamwambia: "Ole wako! Huo si ufalme, bali ni utume" akasema "Ndio hivyo, sasa!"

Akaja Hakim bin Hizam na Badil bin Warqai kwa Mtume(s.a.w.w) , wakasilimu na wakambai. Basi Mtume(s.a.w.w) akawatuma kwa Maquraish kuwalingania katika uislamu. Akasema Mtume(s.a.w.w) "Mwenye kuiingia nyumba ya Abu Sufiani iliyoko sehemu ya juu ya Makka, amesalimika na mwenye kuinigia nyumba ya Hakim iliyoko chini ya Makka, amesalimika, na mwenye kufunga mikono yake amesalimika. Alipotoka Abu Sufiani na Hakim kuelekea Makka, Mtume alimpeleka Zubeir bin Awam, akamwamrisha kukita bendera yake sehemu ya juu ya Makka na akamwambia " Usiondoke mpaka nije huko." Kisha Mtume(s.a.w.w) akaingia Makka na akapiga kambi. Akaanza kumpeleka Saad bin Ubadah na kikosi cha Ansar na akampeleka Khalid bin El-Walid pamoja na wale waliosilimu katika Kudhaa na Bani Salim, akamwamrisha kuingia sehemu ya chini ya Makka na kukita bendera yake kando ya majumba.

Mtume(s.a.w.w) akaamrisha wote kuizuwiya mikono yao, wasipigane na mtu yoyote isipokuwa yule anayetaka kupigana nao Na akamrisha kuuliwa watu wane, (1) Abdalla bin Saad bin Abu Sarh (2) Huwayrith bin Nufayl (3) Ibn Khatal (4) Muqbis bin Dhubaba. Pia akamrisha kuuwawa wajakaza wawili waliokuwa wakiimba nyimbo za kumkebehi Mtume. Akasema Mtume(s.a.w.w) : "Wauweni hao hata kama mkiwakuta wamejifunika pazia ya Al-Kaaba." Ali(a.s) akamuuwa Huwayrith bin Nufayl, na mmoja wa wajakazi wawili na mjakazi mwingine akatoroka, akamuuwa Muqbis katika soko na akamkuta Ibn Khatwal amejifunika na pazia ya Al-kaaba, wakatangulia Said bin Hureith na Ammar bin Yassir , Said akatangulia yeye akamuuwa. Abu Sufiani akamuendea Mtume akachukua kikuku chake cha kupandia farasi akakibusu, kisha akasema: "Makombozi wako ni baba yangu na mama yangu hivi hukusikia yale anayosema Saad: "Leo ni siku ya vitakuu, leo wanawake watatekwa."

Mtume(s.a.w.w) akamwambia Ali mfuate, uchukue bendera kwake, na uwe wewe ndiye utakayeingia nayo na uingie nayo kwa upole. Basi ali akaichukua akaingia nayo kama alivyoamrishwa. Mtume(s.a.w.w) alipoingia Makka, alikwenda kusimama kwenye mlango wa Al-Kaaba akasema: "Hapana Mola isipokua Allah hali ya kuwa yupekee yake, ametekeleza ahadi yake. Na amemnusuru mja wake, amevishinda vikundi vya madui hali yakuwa yupeke yake. Jueni kwamba mambo yote na damu inayodaiwa, vyote hivo viko chini ya miguu yangu hii, isipokuwa utumishi wa Al-Kaaba na kunywesha mahujaji. Hivyo viwili vitarudishiwa wenyewe. Jueni kwamba Makka ni yenye kuharamishwa kwa uharamisho wa Mwenyezi Mungu, haikua halali kwa yeyote aliyekuwa kabla yangu na haikua halali kwangu isipokuwa saa moja katika mchana, nayo ni yenye kuharimishwa mpaka Kiyama; Haukatwi mti wake wala hawindwi mnyama wake, wala sihalali kuokota kitu ila kwa atakayekitangaza kisha akasema: "Eee! Majirani wabaya wa Mtume(s.a.w.w) mlikuwa mkifanya mrongo, mkamfukuza na mkamuudhi; kisha hamkutosheka na hayo mpaka mkanifuata katika mji wangu kunipiga vita, basi nendeni nimewasamehe. Wakatoka watu kama walifufuliwa kutoka makaburini na wakaingia katika Uislamu. Mwenyezi Mungu alikuwa amemwezesha Mtume kuwachukua mateka, lakini akaacha, kwa hiyo wakaitwa watu wa Makka 'walioachiwa'. Kisha akaja Ibn Zabary akasilimu.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Masud amesema: aliingia Mtume(s.a.w.w) siku ya kuichukua Makaa akakuta katika Al-Kaaba sanamu mia tatu na sitini, akawa anazichoma kwa mti aliokuwa mkononi mwake huku akisema: "Imekuja haki na batil haina msingi wala haitarudi tena, imekuja haki na imeondoka batil, hakika batil ni yenye kuondoka."

Imepokewa kwa Ibn Abbas, amesema: "alipofika Mtume Makka alikataa kuingia Al- Kaaba ikiwa na masanamu akamrisha yatolewe miongoni mwayo yalikuwepo masanamu ya Ibrahim na Ismail(a.s) yakiwa na miti ya kupigia mburuga mikononi mwake. Mtume(s.a.w.w) akasema: " Mungu awatokemeze. Kwa hakika walijua kuwa hawakuwa wakipiga mburuga kabisa." Hadith katika kisa hiki cha ushindi wa Makka ni nyingi na yaliyotangulia ni kama muhtasar tu!