TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39036
Pakua: 2743

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39036 / Pakua: 2743
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

28

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA LAHAB (MIALI) (NA. 111)

INA AYA 5

Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

تَبَّتْ يَدَا أَبِي لَهَبٍ وَتَبَّ ﴿١﴾

1. Imehasirika mikono miwili ya Abu Lahab, naye amekwisha hasirika.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُ مَالُهُ وَمَا كَسَبَ ﴿٢﴾

2. Haitamfaa mali yake wala alichokichuma.

سَيَصْلَىٰ نَارًا ذَاتَ لَهَبٍ ﴿٣﴾

3. Atauingia moto wenye miali.

وَامْرَأَتُهُ حَمَّالَةَ الْحَطَبِ ﴿٤﴾

4. Yeye na mkewe hali ya kuchua kuni.

فِي جِيدِهَا حَبْلٌ مِّن مَّسَدٍ ﴿٥﴾

5. Ambaye ana katika shingo yake kamba ya ndifu.

Ubainifu Kiaga kikali kwa Abu Lahab, kwa kuangamia nafsi yake na matendo yake katika moto wa Jahannam, na mkewe hali kadhalika. Sura hii imeshuka Makka.

Aya Na 1

Neno Tab lina maana ya kuhasirika na kuangamia kama alivyosema Jawhari. Na kudumu kuhasirika kama alivyosema Raghib. Imesemwa kuwa maana yake ni kutokuwa na lolote, pia imesemwa kuwa maana yake ni kuepukana na kila la heri. Maana yote hayo yanakurubiana. Mkono wa mtu ndio kiungo ambacho anakitumia kupata makusudio yake, na kazi nyingi za mtu zinanasibishwa kwenye mikono yake. Kwa hivyo kuhasirika mikono yake ni kupata hasara katika chumo lake. Ukitaka unaweza kusema kubatilika kwa amali yake anayoifanya kwa mikono yake miwili, bila ya kufikilia kwenye lengo analolitaka na kukosa kunufaika na kitu chochote katika hiyo amali yake, na kuhasirika nafsi yake kwa kuzuiliwa na wema wa milele.

Kwa hivyo kusema kwake Mwenyezi Mungu : "Imehasirika mikono miwili ya Abu Lahab ni dua ya kumtakia kuangamia na kubatilika ile kazi aliyokuwa akiifanya kwa kujaribu kuizima nuru ya Utume au lile alilokuwa akilipitisha Mwenyezi Mungu. Abu Lahab huyu, ni Abu lahab ami yake Mtume (Abu Lahab bin Abdul Muttwalib). Alikuwa ni adui mkubwa ma Mtume, akimpinga na kumuudhi sana Mtume kwa kiasi anachoweza kwa maneno na vitendo. Ndiye ambaye alimwambia Mtume "Umehasirika wewe!" Aliyasema haya wakati Mtume alipowalingania kwenye Uislamu kwa mara ya kwanza. Ndipo ikashuka Sura na akamrudishia Mwenyezi Mungu maangamizi juu yake. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Abu Lahab ni jina lake halisi ijapokuwa hapa limekuja kama kinaya. Inasemekana kama jina lake halisi ni Abdul Uzza, wengine wengine wamesema jina lake halisi ni Abdu Manaf. Sawa zaidi ni yale yaliyosemwa kwamba hiyo ni Kun-ya yake, kwani hilo ni kwa istihzai (kudharau) kwa sababu Abu Lahab inamaanisha kunasibika na miali ya moto, kama vile inavyosemwa, Abul Khayri, Abul Fadhli au Abu Shari, kwa kunasibishwa kwenye Heri, Fadhli na Shari Mwenyezi Mungu aliposema: "Atauingia moto wenye miali" imefahamisha kuwa kuitwa kwake Abu Lahab kumenasibishwa kwenye miali ya moto.

Imesemwa kuwa hakutajwa kwa jina lake ( Abdul-Uzza) kwenye aya, kwa sababu linamaanisha mtumwa wa Uzza, Uzza ni jina la sanamu mojawapo kati ya miungu ya Maquraish. Kwa hiyo ikawa makruh kutaja neno la asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kiasi cha kumnasibisha mtu na asiyekuwa Mungu na hali ya kuwa kila mtu ni 'Abdullah' mtumwa au mja wa Mungu.

Aya Na 2

Mali yake ambayo ameichuma kwa mikono yake miwili ni amali yake.

Aya Na 3

Moto yenye miali ni moto wa Jahannam.

Aya Na 4-5

Inaonekana kuwa makusudio ya aya mbili hizi, ni kwamba huyo mkewe Abu Lahab atauingia moto siku ya Kiyama katika kipambo alichokua akijipamba nacho duniani, nacho kuwa ni yeye alikuwa akichukua matawi ya miba na mengineyo akitupa usiku katika njia ya Mtume kwa ajili ya kumuudhi. Kwa hiyo naye ataadhibiwa kwa moto hali ya kuchukua kuni na katika shingo yake kuna kamba ya ndifu. Katika Majmau amesema: "Kama ikisemwa kwamba je, Abu Lahab alikuwa akilazimiwa kuamini baada ya Sura hii? Na kama angeamini, basi habari za Mwenyezi Mungu kuwa Abu Lahab atauingia moto wenye miali, zingekua za uwongo?"

Jibu: Imani inamlazimu yeye, kwa sababu takilifu ya imani ni yenye kuthibiti juu yake, na kwamba kiaga cha Mwenyezi Mungu ni kwa sharti ya kutoamini. Mushkili huu unatokana na kughafilika kuwa hukumu inayotokana na Mwenyezi Mungu haiwajibishi kutokuwepo kwa hiari ya mtu, wala haiwajibishi kulazimika mtu na kitendo, kwani matakwa ya Mwenyezi Mungu, hayafungamani na hiyari ya mtu, yaani afanya vile anavyotaka. Kwa hiyo ikiwa jambo lenye kufungamana na hukumu ya Mungu, linawajibisha hiyari, basi kuliwacha pia ni hiyari, hata kama halitokei. Imebainika kwamba Abu Lahab alikuwa katika hiyari ya kuamini na kuiokoa nafsi yake na moto ambao alikuwa amehukumiwa kuuingia kutokana na kufuru yake."

Katika Majmau kuhusu aya inayosema: "Na waonye jamaa zako walio karibu" (26:214), Ibn Abbas amesema: "Iliposhuka aya hii Mtume alipanda Jabal Safa akasema: "Enyi wenzangu!" wakasema Maquraish: 'una nini?' Akasema Mtume: "Je, mtaniamini kama nikiwaambia kuwa adui atawavamia asubuhi au jioni?" wakasema Maquraish: "Kwa nini tusikuamini", akasema: "basi mimi ni muonyaji wenu kabla ya kufika adhabu kali." Akasema Abu Lahab: "Kuhasirika kwako ewe Muhammad, hivi umetuitia jambo hili!". Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Sura ya Tabbat.

Katika hiyo Majmau, kutoka kwa Tariq El Muharibi amesema: "Wakati mmoja nilipokuwa katika soko linaloitwa Dhul Mezaj mara nikamwona kijana mmoja akisema: 'enyi watu semeni hapana apasaye kuabudiwa ila Mwenyezi Mungu' mtafaulu. Huko nyuma kuna mwanaume mmoja akimtupia mawe mpaka miundi yake ikaiva damu na huku anasema: "enyi watu huyo ni muongo msimuamini." Nikauliza, ninani huyu? Nikaambiwa "Huyo ni Muhammad anadai kuwa yeye ni Mtume na huyu ni ami yake Abu Lahab anadai kuwa ni mwongo."

Katika isnadi ya Musa bin Jaffar(a.s) katika hadith ndefu anayotaja alama za Mtume(s.a.w.w) , amesema: "katika alama hizi ni kwamba, wakati iliposhuka Sura ya Tabbat Yada, Ummu Jamil, mke wa Abu Lahab, alimjia Mtume akiwa pamoja na Abu bakr bin Abu Quhafa, Abu Bakr akamwambia Mtume: huyu hapa Ummu Jamil amekasirika anataka kukupiga mawe. Mtume akamwambia Abu Bakr: 'hataniona'.

Yule mwanamke akamwambia Abu Bakr: "yuko wapi sahibu yako?" Abu bakr akamjibu: "yuko pale anapotaka Mwenyezi Mungu"; kisha akasema: "Nimemfuata yeye na lau ningemwona ningempiga mawe, kwani yeye amenitukana. Naapa kwa Lata na Uzza kuwa mimi ni malenga." Kisha Abu Bakr akamuuliza Mtume, kwa nini hakukuona? Akajibu Mtume(s.a.w.w) : "Mwenyezi Mungu ameweka pazia kati yangu na yeye." Imepokuwa hadith iliyokaribu na maana haya katika upande wa Ahli Sunnah.

Katika Tafsiri ya Qummi katika neno lake Mwenyezi Mungu: "Yeye na mkewe hali ya kuchukua kuni.", mke mwenyewe ni Ummu Jamil bint Sakhar, na alikua akimkejeli Mtume kisha ananakili habari kuwapelekea makafiri.

SURA IKHLAS (IKHLASI) (NA. 112)

INA AYA 4

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

قُلْ هُوَ اللَّـهُ أَحَدٌ ﴿١﴾

1. Sema huyo Allah ni mmoja tu!

اللَّـهُ الصَّمَدُ ﴿٢﴾

2. Allah ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote.

لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ ﴿٣﴾

3. Hakuzaa wala hakuzaliwa.

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ ﴿٤﴾

4. Wala hakuwa yeyote mfano wake.

UBAINIFU

Sura hii inamsifu Mwenyezi Mungu kwa umoja wa dhati, na kumrejea Yeye Mwenyezi Mungu katika haja zote, bila ya kumshirikisha Yeye Mwenyezi Mungu na kitu chochote, si katika dhati yake wala katika sifa zake na wala katika vitendo vyake. Hiyo ndiyo Tawhid ya Kiqur'an ambayo inahusika na Qur'an tukufu ambayo maarifa yote ya Kiislamu yanatokana nayo. Zimukuja hadith nyingi sana juu ya ubora wa Sura hii, kiasi ambacho imepokewa kutoka kwa Shia na Sunni, kwamba Sura hiyo inalingana sawa na theluthi ya Qur'an, kama yatakavyokuja maelezo yake (Inshallah). Sura hii inawezekana kuwa imeshuka Makka au Madina lakini kutokana na baadhi ya yaliyopokewa katika sababu za kushuka kwake, ni kwamba imeshuka Makka.

Aya Na 1

Neno Ahad lenye maana ya mmoja tu; ni sifa yenye kuchukuliwa katika neno Wahid lenye maana ya moja lakini neno Ahad linatumiwa juu ya kitu ambacho hakihisabiki yaani hakikubali wingi si kwa dhahiri wala kwa kiakili. Kwa hiyo neno Ahad haliingii katika idadi kinyume cha neno Wahid, kwani kila moja ina ya pili na ya tatu na kadhalika. Ama katika neno Ahad kila unapokadiria kitu cha pili, kinakuwa ni hicho hicho hakizidi kitu. Kwa mfano mtu akisema: "Ma Jaani Minal Qaumi Ahad" yenye maana hakunijia mimi yeyote katika watu, atakuwa anakanusha kuja kwa yeyote katika wao; wawili, watatu, au zaidi, lakini kama akisema :Ma Jaani Wahidu Minhum," yenye maana hakunijia mmoja wao, hapo atakuwa anakanusha kuja kwa yeyote mmoja tu!, lakini si wawili au zaidi. Kwa maana hayo neno hili ni lazima litumike pamoja na kutegemezwa kwenye kitu kingine isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu linatumika bila ya kutegemezwa kwenye kitu kingine chochote.

Aya Na 2

Asili ya neno Swamad, ni kukusudia pamoja na kutegemea. Wameifasiri Swamad ambao ni sifa kwa maana nyingi. Zaidi wameeleza kuwa ni Bwana mwenye kukusudiwa kwa haja zote. Kwa kuwa katika aya hili neno hili limetajwa bila ya kutegemezwa katika neno jengine, basi moja kwa moja maana yake ni mwenye kukusudiwa kwa haja zote. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyepatisha kila chenye kupatikana (kisichokuwa Yeye), basi kila kisichokuwa Yeye kitakua kinakusudia kwake. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Fahamuni kuwa kuumba (ni kwake tu!) na amri zote ni zake ."(7:54).

Na amesema tena "Na kwamba mwisho (wa kila jambo) unarejea kwa Mola wako. "(53:42).

Ama kulileta tena neno Allah katika aya hii kwa kusema: "Allah ndiye Mwenye kukusudiwa katika haja zote." Na wala asiseme ' Yeye ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote', hiyo ni kuonyesha kwa kila moja kati ya jumla hizi mbili inaweza kutosheleza katika kumweleza Mwenyezi Mungu. Aya hizi mbili zinamsifu Mwenyezi Mungu kwa sifa ya dhati ya kitendo. Kwa hiyo neno Allahu Ahad lenye maana ya Mwenyezi Mungu ni mmoja, ni sifa ya dhati yake na Mwenyezi Mungu na Allahu Swamad lenye maana ya Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote, ni sifa ya kitendo ambayo inamsifu Mwenyezi Mungu kwa kuishia kwake kila kitu. Pia imesemwa kuwa maana ya neno Swamad ni ambaye hali, wala hanywi, halali, hazai wala hazaliwi. Kwa hiyo aya inayofuata (hakuzaa wala hakuzaliwa), ni tafsiri ya Swamad.

Aya Na 3-4

Aya hizi mbili zinakanusha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezaa kitu kwa kugawa kitu au kutoa kitu kutokana na Yeye, kama wanavyodai wakristo kuhusu Masih(a.s) kuwa eti yeye ni mtoto wa Mungu au kama wanavyodai waabudu masanamu kuhusu baadhi ya waungu wao kuwa ni watoto wa Mungu. Vile vile aya hizi mbile zinakanusha kuwa Yeye amezaliwa au ametokana na kitu kingine, kama wanavyodai waabudu masanamu. Katika miungu yao, kuna Mungu baba, Mungu mama na Mungu mwana. Pia aya hizi zinakanusha kuwa kuna anayefanana na Mungu katika vitendo vyake, kama walivyodai akina Firaun na Namrud kuwa eti ni miungu. Kuzaa ni namna moja ya kugawanyika kwa maana yoyote ile utakavyofasiri, itakuwa yule mwenye kuzaliwa ni lazima aambatane na yule aliyemzaa, kwani itakuwa yule mwenye kuzaliwa ni fungu la yule mwenye kuzaa na bila shaka itakuwepo haja ya kuhitajiana kati yo mafungu hayo, na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hahitaji chochote isipokuwa vitu vyote vinamhitajia. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu hakuzaa.

Ama kuwa hakuzaliwa, ni kwamba kinachozaliwa, ni lazima kitakuwa kinamuhitajia yule aliyekizaa, na Mwenyezi Mungu siyo muhitaji, hivyo hakuzaliwa. Ama kuwa hana kifano, ni kwamba hakuwezi kuhakikika kupwekeka kwake ni kujitosheleza kwake ikiwa yuko mwenye kufanana na Yeye. Mwenyezi Mungu pekee ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote, hivyo hana kifano. Kwa hiyo imebainika kuwa aya hizi mbili zinaeleza maana ya Swamad na kuthibitisha umoja wake Mwenyezi Mungu katika dhati Yake na sifa zake na vitendo vyake na kuongeza yale yanayoambatana na ukubwa wake na utukufu wake. Kwa hiyo Sura nzima hii, inaeleza sifa yake Mwenyezi Mungu kwamba Yeye ni mmoja tu. Pia imesemekana kwamba maana ya neno Kuf-wan ni mke, kwa sababu mke ni kifano cha mume, kwa hiyo aya inakuwa katika maana ya aya inayosema: "Utukufu wa Mola wetu umetukuka kabisa, hakujifanyia mke wala mtoto ."(72:3).

Utafiti Wa Hadithi Katika Kafi kutoka kwa Muhammad bin Muslim kutoka kwa Abu Abdillah(a.s) amesema: "Hakika Mayahudi walimuuliza Mtume wakasema. 'Tusifie Mola wako! Akaongojea M tume(s.a.w.w) siku tatu bila kuwajibu, kisha ikashuka ' Qulhuwallah' mpaka mwisho." Katika Ihtiyaj imepokewa kutoka kwa Askary(a.s) , kwamba aliyemuuliza Mtume ni Abdallah bin Suriyyah (Myahudi). Katika baadhi ya riwaya za ahli Sunnah ni kuwa muulizaji alikuwa Abdallah bin Salam, alimuuliza Mtume alipokuwa Makka kisha akasilimu, lakini akaficha imani yake. Riwaya nyingine katika Sunni zinasema kuwa ni watu katika Mayahudi na nyengine zinasema waabudu masanamu waliouliza ni watu wa Makka wanaowamshirikisha Mungu.

Katika Ma'an kwa isnadi kutoka kwa Asbagh bin Nabata kutoka kwa Imam Ali(a.s) amesema: " Sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni Qulhuwallah". Na katika Ilal kwa isnadi kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) katika hadithi; kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume soma Qulhuwallah kwani hiyo Qulhuwallah ni sifa yangu. Imepokewa kutoka kwa Musa bin Jaffer(a.s) kwa maana hayohayo, na zimepokewa riwaya nyingi sana kwa maana hayo katika njia za Ahli Sunnah kutoka kwa Masahaba wengi, kama vile Ibn Abbas, Abu Dardai, Jabir bin Masud, Abu Sais El- Khudr, Muadh bin Anas, Abu Ayyub, Abu Amama na wengineo. Vile vile zimepokewa hadithi nyingi kwa upande wa Shia. Wameieleza Sura hii kuwa inakuwa sana na theluthi ya Qur'an kwa njia tofauti, moja wapo ni kwamba, maelezo yaliyomo katika Qur'an yanaeleza misingi mitatu: Tawhid, Utume na Marejeo ya Akhera, na Sura hii (Ikhlas) inaeleza moja ya msingi hiyo, Tawhid.

Katika Tawhid imepokewa kutoka Amirul Muminin Ali(a.s) amesema: "Nilimwona Khidhr(a.s) katika usingizi siku moja kabla ya vita vya Badri, nikamwambia: Nifundishe kitu kitakachonilinda na maadui, akasema: " Sema; Yaa huwa man la huwa illa huu ewe ambaye hapana mwengine ila Yeye." Basi nilipoamka nikamuhadithia Mtume(s.a.w.w) , akaniambia ewe Ali umefundishwa jina tukufu. Kwa hiyo likawa katika ulimi wangu siku ya vita vya Badri. Hakika Amirul Muminin alisoma Qulhuwallah, alipomaliza akasoma "(Ya! Huwa man la huwa illa huu! Ighfirliy wansurni alal qawmil kafirin)." Ewe ambaye hapana mwengine ila yeye nisamehe na uninusuru na makafiri. Katika Usulul Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Daud bin El-Qassim Jaffari, amesema: "Nilimuuliza Abu Jaffar(a.s) : nini maana ya Swamad, akasema: "ni Bwana Mwenye kukusudiwa kwa kichache na kingi ."

Katika tafsiri ya Swamad maana nyengine zilizopokewa kutoka kwa Maimamu(a.s) . Kutoka kwa Baqir(a.s) : amesema Swamad ni Bwana Mwenye kutiiwa ambaye hakuna zaidi yake. Na kutoka kwa Husayn(a.s) Swamad ni ambaye hana mfano, ambaye halali na ambaye hakuwacha kuwa ni Mwenye kupatikana na wala hatawacha kuwa ni Mwenye kupatikana. Kutoka kwa Assajjad(a.s) : Swamad ni yule ambae kitu hukiambia kuwa kikawa na Swamad ni yule ambaye amezusha vitu na akaviumba namna moja na vinahitalifiana kwa namna mbali mbali na kwa kiume na kike. Asili ya maana ya neno Swamad ni ile tuliyoipokea kutoka kwa Abu Jaffer wa pili, kutokana na maana hasa yaliyomo katika mada yake nayo ni kukusudiwa. Kwa hivyo maana mbalimbali yaliyopokewa na kunakiliwa kutoka kwa Maimamu(a.s) katika tafsiri ya Maimamu(a.s) yanalazimisha kuwa maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusudiwa katika kila haja. Kwa hiyo vitu vyote vinakomea kwake, bila ya yeye kuhitaji chochote.

Katika Tawhid imepokewa kutoka kwa Wahab bin Wahab El- Qurashi naye amepokea kutoka kwa Assadiq(a.s) naye kutoka kwa wazazi wake(a.s) kwamba watu wa Kuffa walimwandikia Husayn(a.s) wakimuuliza maana ya Swamad, kisha akawarudishia majibu hivi: "Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, amma baadu; msingilie Qur'an wala msiifanyie mjadala bila ya kuwa na elimu yoyote, kwani nimemsikia babu yangu (Mtume) akisema: Mwenye kusema juu ya Qur'an bila ya elimu yoyote, basi na ajichagulie mahali pake katika moto. Na Mwenyezi Mungu ametafsiri Swamad aliposema: "Allah ni mmoja tu! Allah ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote, kisha akaifasiri kwa kusema: Hakuzaa wala hakuzaliwa wala hakuwa kifano cha mtu yoyote". Katika hiyo Tawhid kwa isnadi yake kwa Ibn Abu Umair kutoka kwa Musa bin Jaffar(a.s) kwamba yeye amesema "Jua kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mmoja tu! Mwenye kukusudiwa haja zote, hakuzaa akarithiwa wala hakuzaliwa akashirikishwa."

Katika hotuba nyingine ya Ali(a.s) anasema: "Hakuzaliwa asijekuwa na mshirika katika utukufu wake, wala hakuzaa ili asiwe mwenye kurithiwa .." katika maana hayo yaliyotangulia kuna riwaya nyingi.

SURA FALAQ (ASUBUHI) (NA. 113)

INA AYA 5

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ الْفَلَقِ ﴿١﴾

1. Sema ninajilinda kwa Mola wa asubuhi.

مِن شَرِّ مَا خَلَقَ ﴿٢﴾

2. Na shari ya alichokiumba.

وَمِن شَرِّ غَاسِقٍ إِذَا وَقَبَ ﴿٣﴾

3. Na shari ya usiku wa giza unapoingia.

وَمِن شَرِّ النَّفَّاثَاتِ فِي الْعُقَدِ ﴿٤﴾

4. Na shari ya wenye kupuliza katika mafundo.

وَمِن شَرِّ حَاسِدٍ إِذَا حَسَدَ ﴿٥﴾

5. Na shari ya hasidi anapohusudu.

UBAINIFU

Aliamrishwa Mtume kujikinga na shari zote na baadhi ya shari nyengine maalum. Sura hii imehuka Madina, kutokana na ilivyopokewa katika sababu za kushuka kwake.

Aya Na 1

Mwenyezi Mungu ametumia neno Falaq lenye maana ya kupasua kwa maana ya asubuhi, kwa sababu asubuhi inapasuliwa kutoka katika giza. Kwa hivyo maana yake ninajilinda kwa bwana wa asubuhi ambaye anaipasua. Na ibara hii inaamanisha kutaka hifadhi na shari ambayo inafunika heri. Imesemwa kuwa maana ya Falaq ni kila kinachoumbwa na kupatikana. Kupatikana kitu kunakuwa baada ya kukosekana, yaani kupatikana kumepasua kukosekana, na kutoa kile kinachopatikana. Pia imesemwa kuwa maana ya Falaq ni shimo katika Jahannam na baadhi ya riwaya zimetilia nguvu hilo.

Aya Na 2

Maana ya shari ya alichokiumba, anakusudia yoyote mwenye kuchukua shari katika watu, majini, wanyama na viumbe vinginevyo vyenye shari.

Aya Na 3

Shari imenasibishwa na usiku kwa sababu giza linmsaidia mshari katika shari yake, kwa vile linamsitiri, kwa hiyo usiku unakuwa na shari zaidi kuliko mchana, na mtu anakuwa mnyonge kuweza kuikabili shari wakati wa usiku kuliko mchana. Mwenyezi Mungu ametanguliza kutaja shari ya usiku baada ya kutaja shari ya kiumbe kwa kuzidisha uzito wa shari ya usiku. Mwenyezi Mungu ametilia umuhimu katika Sura hii namna tatu za shari (shari ya usiku, shari ya wachawi na shari ya hasidi), kwa vile watu wanaghafilika sana katika vitu hivi.

Aya Na 4

Yaani wanawake wachawi ambao wanafanya uchawi wao kwa namna hiyo ya kupuliza katika mafundo. Wamehusishwa wanawake na uchawi kwa sababu wanawake walikuwa wanapendelea uchawi zaidi kuliko wanaume. Hii inathibitisha kuweko athari za uchawi, kwa jumla; kama vile alivyosema Mwenyezi Mungu katika kisa cha Haruta na Maruta: "Na wakajifunza kwao mambo ambayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawakua ni wenye kumdhuru yeyote kwa hayo ila kwa idhini ya Allah ". (2 : 102).

Na vile vile athari hii inadhihirika katika kisa cha uchawi wa Fir'aun. Pia imesemwa kuwa maana ya wanawake wenye kupuzia katika mafundo ni wanawake ambao wanabadilisha maoni ya waume zao katika yale wanayoyataka wao tu! Kwa hiyo maoni ni mafundo na kupuzia katika mafundo ni kuyatatua maoni hayo. Lakini kauli hii iko mbali na maana.

Aya Na 5

Inasemekana kuwa aya hii inakusanya msaidizi wa hasidi na husuda, kwa hiyo msaada wa hasidi ni namna mojawapo ya husuda.

Utafiti Wa Hadithi Katika Durril Manthur, ametoa Abdi bin Hamid kutoka kwa Zaid bin Aslam, Amesema: "Mtu mmoja katika Mayahudi alimroga Mtume(s.a.w.w) akawa hajisikii vizuri, akajiwa na Jibril, akamteremshia Sura mbili (Nas na Falaq), akasema Jibril, hakika mtu katika Mayahudi amekufanyia uchawi na uko katika kisima Fulani." Basi Mtume akamtuma Ali akaulete ule uchawi. Jibril akamuamrisha Mtume kuufungua huku akisoma aya mpaka Mtume akasimama akiwa amechangamka. Mfano wa hadith hii unapatikana katika Twibbul Aimma kwa isnadi hya Muhammad bin Sinan kutoka kwa Mufadhal naye amepokea kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) , na riwaya nyingi kutoka katika njia za Ahli Sunnah kwa tofauti ndogo tu! Baadhi ya riwaya za pande zote mbili zinasema kuwa Mtume alimpeleka pamoja na Ali, Ammar bin Yaasir na Zubeir.

Watu wengine wameiitilia mashaka hadith hii, wakisema kwamba Mtume ni mwenye kuhifadhiwa na kuathiriwa na uchawi. Lakini vipi wanatia mashaka na hali Mungu aliposema: "Na madhalimu wakasema nyinyi hamumfuati ila mtu aliyerogwa. Tazama jinsi wanavyokupigia mifano (isiyoelekea), basi wamepotea wala hawataweza (kushika) njia iliyonyooka : (25:8-9).

Hapa Mungu anamkinga Mtume kwamba makusudio kwa aliyerogwa ni kuharibikiwa na akili kwa uchawi. Ama kuathirika na uchawi kwa maradhi yanayompata katika mwili wake, na mfano wa hayo, hakuna dalili ya kuhifadhiwa kwake.

Katika Majmau imepokewa kwamba Mtume mara nyingi akiwatakia hifadha Hassan na Hussein kwa kuwasomea Sura mbili hizi. Na katika hiyo Majmau kutoka kwa Uqba bin Amir amesema; 'Amesema Mtume(s.a.w.w) ': "Nimeteremshiwa aya ambazo hazijatereremshwa mifano yake, nazo ni Almuawwidhatyn (Qul audhu bi Rabbi nnasi na Qul audhu bi Rabbil Falaq)."

Hadith hii inapatikana katika Sahih na imetegemezwa kwa Tirmidhi, Nasai na wengineo katika Durril Manthur. Na vile vile imepokewa hadith kwa maana haya kutoka kwa Tabrani kwa wasta wa Ibn Masud. Na huenda maana ya kuwa hazijateremshwa mifano yake, ni katika aya za hifadhi tu; lakini si katika Qur'an yote.

Katika Durril Manthur ametoa Ahmad, Bazzar, Tabrani na Ibn Murdawayh katika njia sahih imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas na Ibn Masud, kwamba huyo Ibn Masud alikuwa akizifuta Muawwidhatayn (Nas and Falaq) katika msahafu na alikuwa hazisomi; kisha akasema Suyuti amesema Bazzar; "Hakuna sahaba yeyote aliyemfuata Ibn Masud. Na imethibitishwa kutoka kwa Mtume, kwamba yeye alikuwa akizisoma Sura hizo mbili katika swala na zimethibiti katika msahafu. Katika Tafsiri ya Qummi kwa isnadi yake kutoka kwa Abu Bakr El-Hadhrami amesema: "Nilimwambia Abu Jaffar(a.s) ; Hakika Ibn Masud alikuwa akifuta Muawwidhatayn katika msahafu. Akasema hakika baba yangu alikuwa akisema; "Hakika Ibn Masud ameyafanya hayo kwa maoni yake tu!"

Ziko riwaya nyingi katika njia ya Kisunni na Kishia zilizopokewa na vikundi vyote vya Kiislamu Mutawatir Qat'iyy kwamba Muawwidhatayn ni katika Qur'an. Wametia mashaka baadhi ya wakanushaji juu ya muujiza wa Qur'an kwamba, kama Qur'an ingekuwa ni muujiza kwa ufasaha wake, basi kusingekuweko na hitilafu kuwa Sura mbili hizi ni katika Qur'an. Wamejibiwa kwamba kukubaliana watu wengi kuwa ni katika Qur'an (Tawatur Qat'iyy) imetosha katika hilo na kwamba haikunukuliwa kutoka kwa yeyote kuwa Sura hizo hazikumshukia Mtume au kwamba Sura hizo si muujiza kutokana na ufasaha wake, bali wmaesema tu; kuwa ni fungu katika Qur'an na hilo limeshindwa nguvu na hadith Mutawatir.

Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jaffar kutoka kwa Abu Huraira kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba yeye amesema Falaq ni kisima katika Jahannam kilichofunikwa. Na maana yake siyo moja katika hadith; kuna riwaya nyenginezo zinasema kuwa Mtume amesema: Falaq ni mlamgo katika moto, unapofunguliwa huwaka na hadith nyengine inasema kuwa ni kisima katika Jahannam, inapowaka Jahannam nacho huwa na moto. Katika Majmau imesema kuwa Falaq ni kisima katika Jahannam watataka hifadhi watu wa Jahannam kutokana na joto lake kali. Imepokewa kutoka kwa Abu Hamza na Ali bin Ibrahim katika Tafsiri zao na katika Tafsiri ya Qummi kutokana na baba yake kutoka kwa Naufal naye kutoka kwa Sukuni naye kutoka kwa Abu Abdillahi(a.s) amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) :'Unakurubia ufakiri kuwa ni ukafiri na husuda inakurubia kushinda Qadar ."

Hadith hii pia imepokewa kutoka kwa Anas kwa lafdh hiyo na katika Uyun kwa isnadi yake kutoka kwa Sultiy kutoka kwa Ridha(a.s) kutoka kwa baba yake naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) Amesema: "Hasadi inakurubia kushinda Qadar". Na katika Durril Manthur ametoa Ibn Shayba kutoka kwa Anas, amesema: 'Amesema Mtume(s.a.w.w) ': "Hakika Husuda Inakula Mambo Mema Kama Vile Moto Unavyokula Kuni ."

SURA NAS ( WATU) (NA: 114)

INA AYA 6

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

قُلْ أَعُوذُ بِرَبِّ النَّاسِ ﴿١﴾

1. Sema ninajilinda kwa Bwana, Mlezi wa watu.

مَلِكِ النَّاسِ ﴿٢﴾

2. Mfalme wa watu.

إِلَـٰهِ النَّاسِ ﴿٣﴾

3. Mungu wa watu.

مِن شَرِّ الْوَسْوَاسِ الْخَنَّاسِ ﴿٤﴾

4. Na shari ya mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma.

الَّذِي يُوَسْوِسُ فِي صُدُورِ النَّاسِ ﴿٥﴾

5. Ambaye hutia wasiwasi katika nyoyo za watu.

مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ ﴿٦﴾

6. (Ambaye ni) katika majini na watu.

UBAINIFU

Ni amri kwa Mtume(s.a.w.w) ya kujilinda na hari ya mwenye kutia wasiwasi. Sura hii imeshuka Madina kama Sura iliyotangulia. Haya ni kwa mujibu wa ufahamisho wa sababu za kuteremshwa kwa Sura hii. Bali pia imefahamika kutokana na riwaya kwamba Sura hii na Falaq zimeshuka pamoja.

Aya Na 1 – 3

Ni tabia ya mwanadamu, anapokabiliwa na shari ( hatari) anayoiogopea nafsi yake, na anapojiona kuwa yeye ni mnyonge, huwa anataka msaada kwa yule ambaye anamwona kuwa ana nguvu zaidi za kuweza kumlinda na kumkinga na shari hiyo isimfike. Kwa hiyo anaeyefaa kumtegemea na kumshikilia katika jambo hilo ni mmoja kati ya watatu. Ama mlezi ambaye anamlea na kumtekelezea haja zake zote; na miongoni mwa yale anayohitajia katika maisha yake ni kumkinga na mambo yanayomwogopesha; na hii ni sababu inayobaki milele katika nafsi yake ( kutaka awe na mwenye kumtegemea). Au mwenye nguvu ya utawala - nguvu za kupinduukia na utawala unaokubalika - amkinge anapotaka kinga, na amwepushie shari kwa kufuatana na uwezo wake, kama mfalme yeyote anavyofanya. Na hii vile vile ni sababu inayobaki milele katika nafsi yake (kutaka awe na mwenye kumtegemea). Ama, wa tatu, ni Mungu mwenye kuabudiwa, kwani lazima ya kuabudiwa Mungu hasa akiwa ni mmoja asiyekuwa na mshirika, ni kumpwekesha, kutomwomba asiyekuwa Yeye, asitake isipokuwa alitakalo Yeye, wala asifanye isipokuwa alipendalo Yeye.

Na mwenyezi Mungu (s.w.t) ni Mlezi wa watu, Mfalme wa watu na Mungu wa watu, kama alivyoikusanya sifa tatu katka neno lake; "Huyu ndiye Allah, Mlezi wenu. Uflame ni wake, hakuna Allah ila Yeye. Basi nyinyi mnageuzwa wapi? " (39:6).

Halikadhalika ameishiria sababu za ulezi wake na uungu wake kwa kusema:"(Yeye ndiye) mola wa Mashariki na Magharibi hakuna Allah ila Yeye, basi mfanye kuwa mlinzi(wako) " (73:9).

Na ameishiria sababu ya Ufalme wake kwa kusema: "Ni wake Ufalme wa mbingu na ardhi, na mambo yote yanarudishwa kwa Allah " (57:5).

Kwa mwanadamu akitaka kujilinda kwa mlezi na shari inayomwogopesha, basi mwenyezi Mungu (s.w.t), ndiye Mlezi. Hakuna Mlezi isipokuwa Yeye. Na akitake kujilinda kwa mfalme, basi Mwenyezi Mungu ndiye Mfalme wa haki. Ufalme ni wake na Utawala ni wake. Na pindi mwanadamu atakapotaka Mungu amlinde, basi yeye ndiye Mungu; hapana mwengine. Kyw hiyo kusema kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Sema ninajilinda kwa Bwana Mwenye kuwalea watu?" mpaka mwisho. Ni amri kwa Mtume(s.a.w.w) kutake hifadhi Kwake, kwani huyo Mtume ni katika watu na Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mlezi wa watu, Mfalme wa watu na Mola wa watu. Na kutokana na hayo yaliyotangulia, imetudhhirikia sifa zote tatu za Mwenyezi Mungu; na zimetajwa sifa hizo tatu kwa mpangilio:

Kwanza : Mlezi - kwa vile mtu anakuwa karibu na mlezi na anakuwa ndiye anayemuhusu zaidi kwa utawala.

Pili : Mfalme- kwa vile ingawaje hayuko karibu zaidi na mtu, lakini anakuwa ni mtawala, hivyo anakuwa ni mtawala wa kila mtu ambaye hana mtu wa karibu wa kumkinga. Na mwisho, ni Mungu- kwa vile Yeye ni walii anayekusudiwa na watu kwa amali bila ya kuwa na mshirika katika ibada.

Kutokana na kutajwa sifa zote moja kwa moja bila ya kuweka kiunganishi atfu inaonyesha kuwa sifa zote hizo tatu pamoja na ni sababu ya kujikinga na shari. Yaani ulinzi na hifadhi unatokana na sifa hizo tatu, na Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye kuzikusanya: ni Mlezi, ni Mfalme , na ni Mungu, kama ilivyoelezwa katika Sura ya (112:2): "Allah ndiye Mwenye kukusudiwa kwa haja zote"

Aya Na 4

Imesemwa katika Majmau kuwa wasiwasi ni mazungumzo ya nafsi kama sauti yenye kujificha. Mwenye kurejea nyuma (shetani), ni yule mwenye kujificha baada ya kudhihiri. Imesemwa kuwa shetani ameitwa "mwenye kurejea nyuma" kwa sababu anapomtia mtu wasiwasi, mtu yule akimtaja Mwenyezi Mungu, basi hurudi nyuma; na kama akighafilika, basi shetani hurudi tena kumtia wasiwasi.

Aya Na 5

Wasiwasi unafungamana na msingi wa utambuzi wa mtu, na in nasi yake (moyo). Mwenyezi Mungu ametumia neno Suddor yaani vifua, kama alivyosema katika Sura ya (22:46): "lakini zimepofuka nyoyo zao ambazo zimo vifuani ??"

Aya Na 6

Kila mwovu anafaa kuitwa shetani hata kama ni binadamu , kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Sura ya (112:6) "Mashetani katika watu na katika majini"

Utafiti Wa Hadithi Katika Majmau Abu Khadija amepokea kutoka kwa Abu Abdillah(a.s) kwamba amesema: "Alikuja Jibril kwa Mtume na hali ya kuwa Mtume hajisikii vizuri; akamwagua kwa Almuawwidhatayn (Sura Nas (114) na Falaq (113) na Qul huwa Allah (112) Akasema Jibril: "kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Mwenyezi Mungu akupoze kila ugonjwa unaokuudhi. Akasoma Qul audhubi Rabbi n-nasi mpaka mwisho."

Na imepokuwa kutoka kwa Anas bin Malik, amesema: "Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Hakika shetani hukweka pua yake juu ya moyo wa binadamu. Kama binadamu akimtaja Mwenyezi Mungu, shetani hurudi nyuma; na kama akimsahau, basi hummeza. Basi huyo ndiye mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma." Na katika hiyo Majmau, imepokewa kya Iyash, kwa isnadi yake kutoka kwa Aban bin Taghlab kutoka kwa Jaffar bin Muhammad(a.s) amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) : "Hapana Mumin yeyote ila pana katika moyo wake, ulioka kifuani mwake, tundu mbili: tundu moja inapulizwa na Malaika na tundu nyingine unapulizwa na mwenye kutia wasiwasi, mwenye kurejea nyuma." Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa nguvu Mumin kwa Malaika kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Na akawatia nguvu kwa roho atokaye kwake " (58:22).

Katika Amali ya Saduq kwa isnadi yake kwa Imam Sadiq(a.s) , amesema: "Iliposhuka aya hii: "Na ambao wanapofanya uchafu au kudhulumu nafsi zao humkumbuka Allah " (3:135), Iblis alipanda jabali linaloitwa Thuwayr lililoko Makka, akapiga kelele kuwaita maafriti wake, wakakusanyika na kumuuliza: "Umetuitia nini ewe bwana wetu?"

Akasema: "Imsehuka aya hii, basi nani awezaye kupambana nayo?" Akasimama Afriti akasema: "Mimi naiweza. Nitapambana nayo kwa namna kadhaa." Akasema Iblis: "Sio yako" Akasimama mwengine akasema hivyo hivyo, Iblis akamwambia: "Hapana! hutoiweza." Akasimama Wasiwasil Khannas (mwenye kutia wasiwasi mwenye kurejea nyuma) akasema:

"Mimi naiweza." Akaulizwa: "Vipi utaiweza?" Akasema: "Nitawapa ahadi na kuwatamanisha kufanya hayo madhambi mpaka wafanye. Pindi watakapofanya madhambi hayo, nitawasahaulisha kuomba msamaha." Hapo basi Iblis akamwambia: "Wewe kweli utaiweza Aya hiyo." Akamstakabadisha mpaka siku ya Kiyama.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU