TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39336
Pakua: 2867

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39336 / Pakua: 2867
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURAT NABA' (HABARI)

SURAT NABA' (HABARI)(NA. 78)

Aya 17 - 40

17. Hakika siku ya upambanuzi imewekewa wakati maalum.

إِنَّ يَوْمَ الْفَصْلِ كَانَ مِيقَاتًا ﴿١٧﴾

18. Siku itakayopulizwa parapanda, mje makundi makundi.

يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ فَتَأْتُونَ أَفْوَاجًا ﴿١٨﴾

19. Na mbingu zifunguliwe, ziwe milango.

وَفُتِحَتِ السَّمَاءُ فَكَانَتْ أَبْوَابًا ﴿١٩﴾

20. Yaondolewe majabali yawe mlenge.

وَسُيِّرَتِ الْجِبَالُ فَكَانَتْ سَرَابًا ﴿٢٠﴾

21. Hakika Jahannam ni malindilizo.

إِنَّ جَهَنَّمَ كَانَتْ مِرْصَادًا ﴿٢١﴾

22. Ni marejeo kwa wenye kupetuka mipaka.

لِّلطَّاغِينَ مَآبًا ﴿٢٢﴾

23. Watakaa humo karne nyingi.

لَّابِثِينَ فِيهَا أَحْقَابًا ﴿٢٣﴾

24. Hawataonja humo raha wala kinywaji.

لَّا يَذُوقُونَ فِيهَا بَرْدًا وَلَا شَرَابًا ﴿٢٤﴾

25. Isipokuwa maji ya moto na usaha.

إِلَّا حَمِيمًا وَغَسَّاقًا ﴿٢٥﴾

26. Malipo yalitosawa (na makosa yao).

جَزَاءً وِفَاقًا ﴿٢٦﴾

27. Kwa sababu wao walikuwa hawaogopi kuhesabiwa.

إِنَّهُمْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ حِسَابًا ﴿٢٧﴾

28. Wakazikadhibisha sana aya zetu.

وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا كِذَّابًا ﴿٢٨﴾

29. Na kila kitu tumekidhibiti kwa kukiandika.

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ كِتَابًا ﴿٢٩﴾

30. Basi onjeni, hatutawazidishia ila adhabu.

فَذُوقُوا فَلَن نَّزِيدَكُمْ إِلَّا عَذَابًا ﴿٣٠﴾

31. Hakika wanaomcha Allah wana mahali pa kufuzu.

إِنَّ لِلْمُتَّقِينَ مَفَازًا ﴿٣١﴾

32. (Wana) mabustani na mizabibu.

حَدَائِقَ وَأَعْنَابًا ﴿٣٢﴾

33. Na wasichana walio marika.

وَكَوَاعِبَ أَتْرَابًا ﴿٣٣﴾ وَكَأْسًا دِهَاقًا ﴿٣٤﴾

34. Na vikombe vilivyojaa.

لَّا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا وَلَا كِذَّابًا ﴿٣٥﴾

35. Hawatasikia humo upuuzi wala kukadhibishana.

جَزَاءً مِّن رَّبِّكَ عَطَاءً حِسَابًا ﴿٣٦﴾

36. Wamelipwa na Mola wako kipawa chenye kutosha.

رَّبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا الرَّحْمَـٰنِ لَا يَمْلِكُونَ مِنْهُ خِطَابًا ﴿٣٧﴾

37. Bwana wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yake, Mwingi wa Rehema Ambaye hawataweza (siku hiyo) kusema naye.

يَوْمَ يَقُومُ الرُّوحُ وَالْمَلَائِكَةُ صَفًّا لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابًا ﴿٣٨﴾

38. Siku ambayo atasimama roho na Malaika, wamepiga safu hawatazungumza ila aliyepewa ruhusa na (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa Rehema na akasema yaliyosawa.

ذَٰلِكَ الْيَوْمُ الْحَقُّ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ مَآبًا ﴿٣٩ ﴾

39. Hiyo ndiyo siku ya haki. Basi anayetaka naashike njia ya kurejelea kwa Mola wake.

إِنَّا أَنذَرْنَاكُمْ عَذَابًا قَرِيبًا يَوْمَ يَنظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا ﴿٤٠﴾

40. Hakika sisi tunawaonya nyinyi adhabu iliyo karibu. Siku ambayo mtu ataona kilichotangulizwa na mikono yake, na kafiri atasema: laiti ningelikuwa mchanga.

UBAINIFU

Aya zinasifu siku ya upambanuzi ambayo imetolewa habari kwa ujumla na aya ya 4. Kisha inasifu yale yatakayowapitia wanaopetuka mipaka na wanaomcha Mwenyezi Mungu. Mwisho Sura inamalizia kwa tamko la kuonya, na hilo ndilo kama natija.

Aya Ya 17

Ni kuingilia kusifu yale yanayokusanywa na habari kubwa ambayo imetolewa utisho katika aya ya 4; Kisha Mwenyezi Mungu akasimamisha hoja juu ya hayo kuanzia aya ya 6 na kuendelea. Mwenyezi Mungu ameiita siku hiyo siku ya upambanuzi na akaielezea kuwa ni siku ya kupambanuliwa hukumu. Kuleta ibara ya tamko "kanat" ni dalili ya kuthibiti kwake na kubainishwa kwake katika ujuzi wa Mungu kutokana na hoja iliyotangulia kutajwa. Maana yake hakika siku ya upambanuzi wa hukumu ambayo habari yake ni kubwa, imekua katika ujuzi wa Mwenyezi Mungu tangu siku aliyoumba mbingu na ardhi na akapitisha katika siku hiyo nidhamu. Yeye Mwenyezi Mungu alikuwa anajua kwamba umbile hili aliloliumba haliwezi kutimia bila ya kukomea kwenye siku ya kupambanuliwa hukumu.

Aya Ya 18

Yamekwisha tangulia maelezo kuhusu maana ya kupuziwa parapanda. Maneno yamekuja kwa njia ya kuambiwa watu kwa kuelezea haki ya kiaga. Kama kwamba aya iko katika mwelekeo wa aya inayosema: "Siku tutakapowaita kila watu pamoja na kiongozi wao ." (17:71)

Aya Ya 19

Utaungana ulimwengu wa watu na ulimwengu wa Malaika. Imesemwa kuwa kukadiria kwake ni: 'zikawa zenye milango.' Na imesemwa ni njia katika hizo mbingu. Lakini njia zote hizo mbili haziepukani na kuangaliwa vizuri.

Aya Ya 20

Kuondolewa majabali na kugongwa kunaishia kwenye kutawanyika vipande na kuondoka umbo lake kama ilivyotokea katika maneno yake Mwenyezi Mungu wakati wa kusifu tetemeko la Kiyama na athari yale alopisema: "Na majabali (yang'oke) yawe yanakwenda mwendo (mkubwa) " (52:10).

Na amesema: "Na ikaondolewa ardhi na majabali ikavunjwa mvunjo mmoja ." (69:14).

Amesema tena "Na majabali ya kawa kama sufi iliyopurwa ." (101:5).

Na amesema: "Na majabali yakasagwasagwa " (56:5).

Amesema: "Na pindi majabali yatakaposagwasagwa ." (77:10).

Ndio kunaishilia kusagwasagwa kwake kwenye kukosekana na kupotea kabisa umbo lake. Majabali yaliyokuwa yamekita kabisa yaliyokuwa yakionekana na nguvu yasiyoweza kutingishwa na kimbunga, leo yana pondwapondwa na kupotea. Aya hii iko katika mwelekeo wa aya inayosema: "Na unayaona majabali unayadhania yametulia, nayo yanakwenda kama mawingu ." (27:88). Yaani hiyo siku ya mtetemeko wa Kiyama.

Aya Ya 21

Mwenyezi Mungu ameita Jahannam ni malindilizo kwa kuwa watu wataipitia. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala hakuna yoyote katika nyinyi ila ni mwenye kuifikia (hiyo Jahannam) " (19:71).

Aya Ya 22

Kuihisabu Jahannam ni marejeo, ni kwamba wao walijiandalia wenyewe marejeo walipokuwa duniani. Kisha waliachana na dunia na kurejea.

Aya Ya 23

Maana ya neno Ahqab ni muda mrefu usio na kikomo. Wamehitalifiana kuhusu neno hilo. Baadhi yao wamesema ni miaka 80 au miaka 80 na kitu. Wengine wakaongezea kusema kwamba mwaka katika hiyo Ahqab una siku 360 na kila siku inalingana na miaka elfu. Wengine wamesema ni miaka 40 na wengine wamesema ni miaka 70,000. Wala hakuna dalili yoyote kutoka katika Qur'an inayofahamisha juu ya viwango hivi, wala haikuthibiti katika lugha. Ukweliulivyo ni kuwa neno "Ahqab" ni muda wa wakati usiojulikana.

Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ya waliopetuka mipaka ni wale waliofanya inadi katika makafiri.

Hayo yanatiliwa nguvu na aya ya (27) ya Sura hii inayosema; "Kwa sababu wao walikuwa hawachi kuhesabiwa ."

Imesemwa kuwa aya zinazofuatia ni sifa ya hilo neno (Ahqab) maana yake ni kuwa watakaa humo karne nyingi katika sifa hizi nazo nikuwa wao hawataonja raha wala kinywaji isipokuwa maji ya moto na usaha, kisha watakuwa kwenye sifa nyengine kwa muda usiokuwa na kikomo. Kauli hii ni nzuri kama ingelisaidiwa na mpangilio wa maneno.

Aya Ya 24-25

Zinaelezea hali watakayokuwa nayo ndani ya Jahannam.

Aya Ya 26

Ni dalili ya kuwafikiana kwenye kutimia kati ya malipo na amali. Mtu kwa amali yake anataka malipo yaliyo sawa na kazi yake. Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mliokufuru msitowe udhuru leo; Hakika mnapewa malipo ya yale mliyokuwa mkiyatenda ." (66:7).

Aya Ya 27 – 28

Ni sababu ya kufafanua muwafaka wa malipo yao kwa amali yao. Kwamba wao hawakutarajia kuhisabu siku ya upambanuzi wakaona kuwa hakuna maisha ya akhera, wakazikadhibisha aya zinazofahamisha hayo wakakanusha Tawhid na Utume na wakaakiuka kuwa wenyewenyekevu katika amali zao, hivyo wakamsahau Mwenyezi Mungu naye amewasahau na kuwanyima wema wa nyumba ya akhera. Kwa hiyo hawakubakiwa na chochote isipokuwa machukivu na ndio kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Basi onjeni! Hatutawazidishia ila adhabu ".

Aya hii ya (27) ni dalili ya kuafikiana kwenye kutimia kati ya malipo na amali. Mtu hutaka malipo kwa amali yake aliyoifanya. Anasema Mwenyezi Mungu katika aya ya 30 ya Sura hii: "Enyi mliokufuru! Msilete udhuru leo; Hakika mnapewa malipo ya yale mliyokuwa mkiyatenda ." (66:7).

Aya Ya 29

Yaani kila kitu tumekidhibiti na tukakibainisha katika kitabu. Aya hii iko katika mwelekeko wa aya inayosema: "Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari linalobainisha ." (36:12)

Au makusudio yake ni kuwa na kila kitu tumekihifadhi hali ya kuwa ni chenye kuandikwa katika "Lawh Mahfudh" (ubao wenye kuhifadhiwa) au katika karatasi za amali. Na wamejuzisha kuwa maana ya neno "Ihsau" ni kuandika, maana yake itakuwa na kila kitu tumekiandika kitabuni. Kwa vyovyote vile makusudio ya aya ni kutoa sababu ya yaliyotangulia; maana yake; malipo ni yenye kuwafikiana na amali zao, kwa sababu wao walikuwa kwenye hali kadha wa kadha na tumezihifadhi, kwa hiyo tumewalipa malipo yenye kiafiki.

Aya Ya 30

Ni mtiririko wa yaliyotangulia unaoelezea kuwakatisha tamaa ya kutarajia kuokoka. Kuwasemesha kwa kutumia neno "Basi onjeni" ni kwa kutahayariza; Makusudio ya kuwaambia "Basi onjeni hatutawazidishia ila adhabu" ni kuwa mnayoyaonja baada ya adhabu ni adhabu nyengine, hiyo ni adhabu baada ya adhabu na adhabu juu ya adhabu, hamtaepukana na kuongozewa adhabu mpya kwenye ile adhabu ya zamani, basi kateni tamaa katika mnayoyataka na mnayoyapenda. Aya hii haiepukani na kudhihiri kuwa makusudio ya aya 30 ni kukaa milele bila kikomo.

Aya Ya 31-35

Zinaelezea kufuzu kwa wale wamchao Mwenyezi Mungu kwa kupata heri na salama.

Aya Ya 36

Yaani wamefanyiwa wale wanaomcha Mwenyezi Mungu yake waliyofanyiwa hali ya kuwa ni malipo kutoka kwa Mola wako na kipawa chenye kuhisabiwa. Imesemwa kuwa kutegemezwa neno malipo kwa Mola kisha kwa Mtume ni kwa ajili ya kuyatukuza na halikutegemezwa kwa Mwenyezi Mungu neno malipo ya wenye kupetuka mipaka, kwa ajili ya kumtakaza nayo Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwani shari yao iliyowapata imetokana na wao wenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyofanywa na mikono yenu. Na hakika Allah si mwenye kuwadhulumu waja ". (8:51)

Kutokea tamko la hisabu katika mwisho wa malipo ya wenye kupetuka mipaka na wenye kumcha pamoja ni kuthibitisha yale yanayoishiriwa na siku ya upambanuzi yaliyotokea mwanzo wa maneno.

Aya Ya 37

Ni ubainifu wa neno "Mola wako" inakusudiwa kuwa ubwana wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni wenye kuenea kwa kila kitu na kwamba Mola ambaye Mtume anamfanya kuwa Bwana na kulingania watu kwake, ni Mola wa kila kitu sio kama walivyokuwa wakisema washirikina kwamba kila taifa lina Mola na Mwenyezi Mungu ndiye Bwana wa mabwana, au kama walivyokuwa wakisema wengine kwamba Yeye ni Mola wa mbingu. Kumsifu Mola kwa kuwa "Mwingi wa Rehema" ni kuonyesha kuenea rehema yake na kwamba hiyo ni alama ya uungu wake hakizuilii chochote na kupata rehema hiyo isipokuwa mtu kujizuilia mwenyewe kwa kuzembea kwake na ubaya wa uchaguzi wake. Na katika uovu wa hao waliopetuka mipaka ni kwamba wao wamejinyima hiyo rehema kwa kutoka katika hali ya unyenyekevu.

Kuhusu "ambaye hawataweza (siku hiyo) kusema naye" kutokana na kuanza aya na "Bwana wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yake Mwingi wa Rehema" ni dalili kwamba makusudio ya hawataweza kusema naye ni kumsemesha katika baadhi ya aliyo yafanya kwa njia ya swali kama kusema: kwa nini umefanya hayo? Na kwa nini hukufanya. Kwa hiyo jumla "hawataweza kusema naye" inakuwa katika maana ya neno lake Mwenyezi Mungu: "Haulizwi (Mwenyezi Mungu) anayoyafanya, lakini wao (viumbe) wataulizwa .." (21:23)

Lakini aya inayofuatia baada ya jumla hii inaonyesha kuhusika na Malaika yaani hao Malaika hawatasema na Mwenyezi Mungu katika atakavyopitisha kwa kumwingilia au kuwaombea kama alvyosema Mwenyezi Mungu: "kabla ya haijafika siku ambayo hapatakuwa kujikomboa wala urafiki (wa kusaidiana) wala uombezi ." (2:254)

Aya Ya 38

Makusudio ya roho ni kiumbe kinachohusikana na Mwenyezi Mungu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "sema roho ni jambo linalohusika na Mola wangu ". (17:85)

Imesemwa kuwa ni mtukufu wa Malaika. Imesemwa ni Malaika mwenye kuchukua roho, lakini hakuna dalili juu ya kauli hizi. Imesemwa makusudio ni Jibril, imesemwa ni roho za wanaadamu na kusimama kwao pamoja na Malaika. Katika wakati ulio kati ya mipuzio miwili ya parapanda kabla ya kuingia roho katika viwiliwili hali ya kupiga safu. Na imesemwa ni Qur'an na makusudio ya kusimama kwake ni kudhihiri athari yake siku hiyo katika wema wa waumini na uovu wa makafiri.

Lakini hizi kauli tatu zinapingwa, kwamba ingawaje ametumia Mwenyezi Mungu neno roho katika kila moja yao lakini ni pamoja na kuifunga (kuihusisha) na kitu chengine. Kama katika kauli yake: "Na kumpulizia roho inayotokana na mimi ." (15:29).

Na kauli yake: "Ameyateremsha hayo roho (Jibril) mwaminifu"

(26:193). Na kusema kwake: "....Na tukampelekea roho wetu ." (19:17).

Na kauli yake: "Sema ameiteremsha roho mtakatifu ." (Jibril) (16:102).

Na kauli yake:

"Namna hivi tumekufunulia (Qur'an) kwa roho atokaye kwetu ". (42:52) Kusema kwake "Hawatasema" ni ubainifu wa neno "ambaye hawataweza kusema haya". Dhamiri ni ya kundi lote la roho, Malaika, Watu na Majini kutokana na unavyofahamisha mpangilio wa maneno. Imesemwa dhamiri ni ya roho na Malaika. Na imesemwa ni ya watu lakini kutokea neno hawataweza na hawatasema katika muundo mmoja hakuafikiani na kauli hizo mbili.

Kusema kwake "Ila aliyepewa ruhusa na Allah, Mwingi wa Rehema" ni yule atakayeweza kusema. Jumla hiyo iko katika maana ya kauli yake: "wakati itakapokuja (siku hiyo) kiumbe chochote hakitasema ila kwa ruhusa yake (Mwenyezi Mungu)". (11:105).

Kusema kwake "Na akasema yaliyo sawa " yaani ni neno lililosawa lisiloingiliwa na kosa, ni haki isiyoingiliwa na batili. Kwa hakika jumla ni kuifunga idhini na haki, ni kama vile imesemwa 'wala hatapewa idhini isipokuwa yule atakayesema yaliyosawa." Kwa hiyo aya iko katika maana ya aya inayosema: "Wala hawana uwezo wa uombezi wale wanaowaomba badala yake ila wale wanaokiri (hii) haki, wakaijuwa ." (43:86).

Kuhusu Roho Katika Qur'an Limekaririka tamko la roho katika maneno ya Mwenyezi Mungu, na maana inayofahamika haraka ni kitu ambacho no msingi wa uhai. Na Mwenyezi Mungu hakulitumia neno hili kwa mtu au kwa mtu na mnyama pekee, bali amelithibitisha sehemu nyengine; kama katika kauli yake "na tukampelekea Mariam roho wetu.. " (19:17).

Na kusema kwake: Namna hivi tumekufunulia (Qur'an) kwa roho atokaye kwetu." (42:52) Kwa hiyo roho ina uthibitisho kwa mtu na penginepo, kauli inayoweza kuielezea roho zaidi ni ile ya Mwenyezi Mungu isemayo "Na wanakuuliza habari ya roho. Sema roho ni amri ya Mola wangu". Na ameielezea amri kwa kusema kwake: "Hakika amri yake anapotaka chochote ni kukiambia kuwa kikawa. Ametutuka yule ambaye mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu, na kwake mtarejezwa nyote ." (36:82-83)

Kwa hiyo amebainisha kwamba hiyo roho ni tamko linalofanya kitu kipatikane; hii ikimaanisha kwamba hilo tamko ndiyo kupatikana (kwa kitu) kwa vile kunavyonasibiana na Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu anavyosifika na kupatikana huko, na siyo huko kupatikana kunavyonasibiana na ila au sababu za nje. Kwa makusudio haya amemuhisabu Masihi (AS) kuwa ni tamko na roho kutoka kwake aliposema: "Na tamko lake alilompelekea Mariam. Na ni roho iliyotoka kwake ." (4:171).

Hapo ni wakati alipompa Mariam, Isa (AS) kwa njia isiyokuwa ya kawaida. Inakurubia katika makusudio hayo kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika mfano wa Isa kwa Allah ni kama mfano wa Adam alimuumba kwa udongo, kisha akamwambia kuwa, basi akawa ". (3:59).

Na Yeye Mwenyezi Mungu ingawaje aghlabu ameitaja hiyo roho kwa kutegemeza au kwa kuifunga na kitu; kama kauli yake "na kumpulizia roho inayotoka na mimi " (15:29).

Na kauli yake: "na akampulizia roho yake " ( 32:9). Na kauli yake:

"na tukamplelekea roho wetu ." (19:17).

"Na ni roho kutoka kwake.. " (4:17)

"Na tukamtia nguvu kwa roho mtakatifu . " (2:87).

Na mengineyo, lakini pia yamekuja baadhi ya maneno yake kwa kutaja roho bila ya kuitegemeza au kuifunga na chochote. Kama kauli yake; "Hushuka Malaika na roho katika Lailatul-Qadri kwa amri ya Mola wao kwa ajili ya kila jambo ". (97:4).

Dhahiri ya aya hiyo ni kwamba roho hapo ni kiumbe kingine cha mbinguni ambacho ni Malaika. Aya hiyo iko katika mwelekeo wa kauli yake: "Malaika na roho hupanda kwake katika siku ambayo muda wake ni miaka elfu hamsini " (70:4). Ama roho yenye kufungamana na binadamu ameitolea taabiri Mwenyezi Mungu kwa mfano wa kauli yake: "Na kumpulizia roho inayotokana na mimi ." (15:29).

Na "na akampulizia roho inayotoka kwake ." (32:9) Na ameleta neno "Min" lenye kufahamisha umwanzo. Na kitendo cha kuleta "umwanzo" akakiita kuwa ni "kupulizia'. Ametaja roho aliyowahusisha waumini kwa mfano wa kauli yake " na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake." (58:22).

Ameleta herufi "Ba" katika aya hiyo yenye kufahamisha sababu na akakiita kitendo hicho 'kutia nguvu'. Ametaja roho aliyowahusisha mitume katika mfano wa kauli yake "na tukamtia nguvu kwa roho mtakatifu" (2:87).

Kwa hiyo akaongezea utakatifu, pia ametaja kuwa ni kutia nguvu.

Kwa kuzikusanya aya hizi pamoja na mfano wa aya, iliyoko katika Sura ya Qadr inadhihiri kwamba mnasaba kati ya roho yenye kutegemezwa kitu ambayo iko katika aya hizi, na roho ambayo haikusasibishiwa chochote ni kama kunavyonasibishwa kumimina na mmiminaji au kivuli na chenye kuleta kivuli. Vinaponasibishiwa na idhini ya Mwenyezi Mungu.

Vile vile roho yenye kufungamana na Malaika, isipokuwa ni kwamba hakusema katika roho ya Malaika kwa kupuzia na kutia nguvu, kama alivyosema kwa binadamu bali ameita roho tu kama katika kauli yake: "Na tukampelekea roho wetu." (19:17). Na kusema kwake: "Sema ameiteremsha roho mtakatifu " (16:102). Kwa sababu Malaika ni roho pekee, kulingana na kuhitalifiana daraja zao katika ukaribu na umbali na Mola wao. Wanavyoonekana na viwiliwili ni kwa kujifananisha tu; kama linavyoonyesha neno lake: "Na tukampelekea roho wetu akajifananisha kwake na (sura ya) binadamu aliye kamili ". (19:17). Kwa sababu hiyo hawakuambiwa roho zao 'zimepuliziwa' tofauti na binadamu ambaye ana sehemu ya kiwiliwili ambacho ni maiti na roho ambayo iko hai, huyu inanasibu kusema amepuliziwa; kama anavyosema Mwenyezi Mungu: "Nikishamkamilisha na kumpulizia roho yangu, angukeni mumsujudie." (15:29).

Kama ambavyo umbile la roho ya mwanadamu ni tofauti na ile ya Malaika, kwa vile katika mwanadamu kuna'kupulizia' na katika Malaika hakuna, hivyo ndivyo tofauti kati ya roho inavyopatikana. Tofauti ya maisha ya roho kuwa mazuri au mabaya, imeleta tofauti katika kuielezea roho inayohusika. Hivyo ndivyo 'kutiwa nguvu' kwa Malaika, na waumini. Miongoni mwa roho, ni roho zenye kupuliziwa kwa mtu anasema "nikapuzia roho itokayo kwangu ". (15:29).

Na roho zenye 'kutiliwa nguvu' ni roho za waumin. Mwenyezi Mungu anasema: "Hao ndio ambao (Mwenyezi Mungu) ameandika nyoyoni mwao imani na akawatia nguvu kwa roho itokayo kwake " (58:22).

Hiyo ni daraja ya juu zaidi katika roho za kibinadamu kama inavyoelezea kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ambayo iko katika maana ya aya hii tuliyoitaja sasa hivi: "Je aliyekuwa maiti kisha tukamfufua na tukamjaalia nuru, kwa nuru hiyo hutembea mbele za watu, atakuwa sawa na yule ambaye hali yake yuko gizani asiweze kutoka humo ". (6:122).

Kwa hiyo amemuhisabu muumin ni hai mwenye nuru anayotembea kwa nuru hiyo, ni athari ya roho. Na kafiri amemuhisabu kuwa maiti naye ni mwenye roho ya kupuliziwa.

Kwa hiyo inadhihiri kwamba daraja za roho kuna zile zilizo katika mimea kutokana na athari ya uhai. Zinazofahamisha hilo ni aya zenye madhumuni ya kuihuyisha ardhi baada ya kufa. Miongoni mwa aina za roho ni zile wanazotiliwa nguvu mitume nazo. Ama kauli yake: "Hupeleka roho kwa amri yake kwa amtakaye miongoni mwa waja wake, ili kuwaonya siku ya kukutana (naye)" (40:15) Na kauli yake: "Namna hii tumekufunulia roho kwa amri yetu ". (42:52).

Inawezekana kuwa roho zinazozungumziwa katika aya mbili hizo, ni roho ya Imani au roho mtakatifu (Jibril).

Aya Ya 39

Ni ishara ya hiyo siku ya upambanuzi. Kuishiria kwa ishara ya mbali ni kuonyesha uzito wake. Kauli yake "Basi anayetaka naashike njia ya kurejelea kwa Mola wake." ni mtiririko wa habari za siku ya upambanuzi maana yake mwenye kutaka kurudi kwa Mola wake na arudi.

Aya Ya 40

Makusudio ya adhabu hapa ni adhabu ya akhera na kusema iliyokaribu ni kwa kuwa ni kweli hapana shaka kuileta, na kila linalokuja liko karibu. Kuhusu ambacho kimetangulizwa na mikono yake ni amali yake aliyoifanya mwenyewe. Mwenyezi Mungu anasema: "Siku ambayo itakuta kila nafsi mema iliyoyafanya yamehudhurishwa na pia ubaya ulioufanya ". (3:30). Kusema kafiri laiti ningelikuwa mchanga yaani atatamani hivyo kutokana na shida ya siku hiyo kwamba yeye lau angelikuwa kitu kisichokuwa na hisiya yoyote.

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (19) amesema: "Itafunguliwa milango ya peponi " na kuhusu aya ya (20) anasema: yatakwenda majabali mfano wa mlenge ambao unametameta katika jangwa. Katika hiyo hiyo Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (23) amesema neno "Ahqab" ni miaka na mwaka una siku 360 na siku moja huko ni kama miaka elfu mnayoihisabu. Katika Majmau amepokea Nafi'i kutoka kwa Ibn Umar amesema: amesema Mtume(s.a.w.w) 'Hatatoka motoni mpaka akae humo kitambo cha Huqb nyingi na Huqb moja ni miaka 60 na kitu na mwaka mmoja ni siku 360, kila siku ni kama miaka elfu mnavyohisabu kwa hiyo asitegemee yoyote kutoka katika moto. Riwaya kama hiyo imekuja katika Durril Manthur na imepokewa vile vile riwaya nyengine kutoka kwake(s.a.w.w) kwamba "Huqb" ni miaka 40. Katika hiyo hiyo amepokea Iyashi kwa isnadi yake kutoka kwa Hamran amesema: 'Nilimwuliza Abu Jaffar(a.s) kuhusu aya hii akasema: "Aya hii inawahusu ambao watatoka motoni ."

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya (31) amesema: "Watafuzu ". Na aya (33) ni wake wa watu wa peponi. Katika riwaya ya Abul Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) kuhusu aya (31) amesema ni utukufu. Na aya (33) amesema ni wasichana wenye matiti yaliyosimama. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Abu Hatim, Abush Shaykh katika Adhama na Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema: "Roho ni askari katika askari wa Mungu sio Malaika wana vichwa, mikono na miguu, kisha akasema "Siku atakayosimama Roho na Malaika wamepiga safu akasema: Hao ni askari na hao ni askari ." Imekwisha tangulia riwaya katika aya zinazoelezea roho kutoka kwa Maimamu(a.s) .

Ndio katika riwaya ya Qummi aliyoipokea kutoka kwa Himran ni kwamba Roho ni malaika mkubwa kuliko Jibril na Mikail na alikuwa pamoja na Mtume(s.a.w.w) na yuko pamoja na Maimamu(a.s) . Huenda makusudio ya Malaika ni kwa vile yuko mbinguni au hizo ni dhawa za wapokezi wa hadith katika kunakili maana wala hakuna hali ya kufahamisha kuwa kila kinachopatikana mbinguni ni malaika bali iko dalili ya kinyume cha hilo kama inavyofahamisha kauli yale Mwenyezi Mungu: "Ewe Ibilisi! Kipi kilichokuzuia kumsujudia yule niliyemuumba kwa mikono yangu? Je, umetakabari au umo miongoni mwa wakubwa ". (38:75).

Katika Usul-Kafi kwa isnadi yake kutoka kwa Muhammad bin Al-Fadhil naye kutoka kwa Abul Hassan(a.s) amesema: Nilisoma aya; "Siku ambayo atasimama Roho na Malaika, wamepiga safuu hawatazungumza ila aliyepewa ruhusa na (Allah) Mwingi wa Rehema na akasema yaliyosawa ." Niliposoma aya hiyo akasema: "Wallah sisi ndio tutakaopewa idhini siku ya Kiyama na ndio wenye kusema yaliyosawa ." Nikasema : "Mtasema nini? " Akasema: "Tutamsifu Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume wetu na kuwaombea wafuasi wetu wala hataturudisha Mola wetu ".

Katika Majmau imepokewa hadith hiyo Iyash ikiwa Marfua kutoka kwa Muawiya bin Ammar naye kutoka kwa Abu Abdillah(a.s) . Riwaya hii ni kwa upande wa kuelezea baadhi ya mambo yanayosadikiwa, kwani wako waombezi wengine, katika malaika, mitume na waumini watapewa idhini katika kuzungumza. Na wako mashaidi wa uma watakaopewa idhini ya kuzungumza; kama inavyoeleza Qur'an na hadith.