TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39318
Pakua: 2864

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39318 / Pakua: 2864
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURAT NAAZIA'AT (KUTOA KWA NGUVU)

SURA NAAZIA'AT (KUTOA KWA NGUVU) (NA. 79 )

INA AYA 46

Aya 1 - 41

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

وَالنَّازِعَاتِ غَرْقًا ﴿١﴾

1. Naapa kwa (Malaika) wanaotoa roho (Kwa nguvu).

وَالنَّاشِطَاتِ نَشْطًا ﴿٢﴾

2. Na wanaotoa roho (kwa upole).

وَالسَّابِحَاتِ سَبْحًا ﴿٣﴾

3. Na wanokwenda (nazo hizo roho) kwa haraka.

فَالسَّابِقَاتِ سَبْقًا ﴿٤﴾

4. Na wenye kutangulia mbio mbio.

فَالْمُدَبِّرَاتِ أَمْرًا ﴿٥﴾

5. Na wenye kupanga mambo.

يَوْمَ تَرْجُفُ الرَّاجِفَةُ ﴿٦﴾

6. Siku itapolia parapanda (ya kwanza)

تَتْبَعُهَا الرَّادِفَةُ ﴿٧﴾

7. Ifuatiwe na yenye kufuatia (ya pili).

قُلُوبٌ يَوْمَئِذٍ وَاجِفَةٌ ﴿٨﴾

8. Nyoyo siku hiyo zitatemeka.

أَبْصَارُهَا خَاشِعَةٌ ﴿٩﴾

9. Macho yake yatatazama chini.

يَقُولُونَ أَإِنَّا لَمَرْدُودُونَ فِي الْحَافِرَةِ ﴿١٠﴾

10. Wanasema: Je, ni kweli sisi tutarejezwa katika hali ya kwanza?

أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا نَّخِرَةً ﴿١١﴾

11. Pindi tutakapokuwa mifupa iliyooza?

قَالُوا تِلْكَ إِذًا كَرَّةٌ خَاسِرَةٌ ﴿١٢﴾

12.Watasema: Hayo, hapo, yatakuwa marejeo ya hasara.

فَإِنَّمَا هِيَ زَجْرَةٌ وَاحِدَةٌ ﴿١٣﴾

13. Hakika hayo yatakuwa ni ukelele mmoja tu.

فَإِذَا هُم بِالسَّاهِرَةِ ﴿١٤﴾

14. Mara wao watakuwa juu ya Ardhi.

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ مُوسَىٰ ﴿١٥﴾

15. Je, imekujia habari ya Musa?

إِذْ نَادَاهُ رَبُّهُ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى ﴿١٦﴾

16.Wakati Mola wake alipomlingania katika wangwa mtakatifu wa Tuwa.

اذْهَبْ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿١٧﴾

17. (Akamwambia) nenda kwa Firaun, hakika yeye amepetuka mipaka.

فَقُلْ هَل لَّكَ إِلَىٰ أَن تَزَكَّىٰ ﴿١٨﴾

18. Umwambie: Je, unataka kujitakasa?

وَأَهْدِيَكَ إِلَىٰ رَبِّكَ فَتَخْشَىٰ ﴿١٩﴾

19. Ni kuongoze kwa Mola wako ili umche?

فَأَرَاهُ الْآيَةَ الْكُبْرَىٰ ﴿٢٠﴾

20. Akamwonyesha miujiza mikubwa.

فَكَذَّبَ وَعَصَىٰ ﴿٢١﴾

21. Akakadhibisha na akaasi.

ثُمَّ أَدْبَرَ يَسْعَىٰ ﴿٢٢﴾

22. Kisha akapa mgongo akaanza kufanya jitihadi.

فَحَشَرَ فَنَادَىٰ ﴿٢٣﴾

23. Akakusanya (watu) akatangaza.

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾

24. Akasema: Mimi ndiye Mola wenu mkubwa.

فَأَخَذَهُ اللَّـهُ نَكَالَ الْآخِرَةِ وَالْأُولَىٰ ﴿٢٥﴾

25. Allah akampatiliza kwa adhabu ya Akhera na ya ulimwengu.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّمَن يَخْشَىٰ ﴿٢٦﴾

26. Hakika katika hayo mna mazingatio kwa anayemcha (Mwenyezi Mungu).

أَأَنتُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَمِ السَّمَاءُ بَنَاهَا ﴿٢٧ ﴾

27. Je, nyinyi ni wenye umbo gumu zaidi, au mbingu alizozijenga?

رَفَعَ سَمْكَهَا فَسَوَّاهَا ﴿٢٨﴾

28. Akainua kimo chake akazipanga vizuri.

وَأَغْطَشَ لَيْلَهَا وَأَخْرَجَ ضُحَاهَا ﴿٢٩﴾

29. Akautia giza usiku wake, akaudhihirisha mchana wake.

وَالْأَرْضَ بَعْدَ ذَٰلِكَ دَحَاهَا ﴿٣٠﴾

30. Na ardhi baada ya hapo, akaitandika.

أَخْرَجَ مِنْهَا مَاءَهَا وَمَرْعَاهَا ﴿٣١﴾

31. Akatoa ndani yake maji yake na malisho yake.

وَالْجِبَالَ أَرْسَاهَا ﴿٣٢﴾

32. Na majabali akayathibitisha.

مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ ﴿٣٣﴾

33. Kwa manufaa yenu na wanyama wenu.

فَإِذَا جَاءَتِ الطَّامَّةُ الْكُبْرَىٰ ﴿٣٤﴾

34. Basi pindi itakapokuja balaa kubwa.

يَوْمَ يَتَذَكَّرُ الْإِنسَانُ مَا سَعَىٰ ﴿٣٥﴾

35. Siku ambayo mtu atakumbuka alichokitenda kwa bidii.

وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِمَن يَرَىٰ ﴿٣٦﴾

36. Na moto udhihirishiwe wenye kuona.

فَأَمَّا مَن طَغَىٰ ﴿٣٧﴾

37. Ama aliyepetuka mipaka.

وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٣٨﴾

38. Akapendelea zaidi maisha ya dunia.

فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٣٩﴾

39. BAsi moto ndio makazi yake.

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٤٠﴾

40. Na ama yule aliyegopa cheo cha Mola wake, akaizuilia nafsi (yake) na matamanio.

فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٤١﴾

41. Basi pepo ndiyo mashukio yake.

UBAINIFU

Katika Sura hii kuna habari za kutilia mkazo tukio la ufufuo na Kiyama. Na kutoa hoja kutokana na njia ya mpangilio wa Mwenyezi Mungu yenye kutoa natija kuwa watu siko hiyo watagawanyika makundi mawili, watu wa peponi na watu wa motoni. Inamalizia Sura kuonyesha kumwuliza kwao Mtumwe(s.a.w.w) kuhusu wakati wa Kiyama pamoja na jawabu lake. Sura hii imeshuka Makka kwa ushahidi wa mpangilio wa aya zake.

Aya Ya 1-5

Wafasiri wamehitalifiana kiajabu tafsiri ya aya hizi, ingawaje wameafikiana kuwa ni kiapo. Kauli ya wengi wao nikuwa jawabu la kiapo limeondolewa, kukadiria kwake ni Ninaapa kwa. mtafufuliwa.

Aya ya 1

Imesemwa makusudio yake ni Malaika wanaotoa roho kutoka katika viwiliwili neno "Gharqa" nikutilia nguvu kutoa. Imesemekana kuwa makusudio yake ni Malaika wanaotoa roho za makafiri kutoka katika viwiliwili vyao kwa nguvu. Pia imesemwa ni mauti yanatoa roho kutoka katika viwiliwili kwa nguvu sana. Imesemwa ni nyota zinatoka na kutua. Imesemwa ni upinde unatoa mshale yaani kuvutwa kwa nguvu. Kwa hiyo kuapa kwa upinde ni wale wanaopigana Jihadi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Vile vile imesemwa makusudio ni mnyama mwitu anayeendea malisho.

Aya ya 2

Makusudio yake ni kutoa kwa upole yaani Malaika ambao wanatoa roho katika viwiliwili. Imesemekana kuwa makusudio yake ni Malaika ambao anatoa roho za waumini kwa upole, kama vilke ambavyo makusudio ya aya 1:ni Malaika waotoa roho za makafiri .

Imesemwa ni Malaika wanaotoa roho za makafiri kutoka katila viwiliwili vyao. Imesemwa ni roho za waumini. Imesemwa ni nyota zinatoka katika pembe moja mpaka nuengine. Imesemwa ni mshali unaotoka katika upinde siku ya vita. Imsesemwa ni mauti yanayotoa roho kutoka katika viwiliwili. Na imesemwa ni mnyama mwitu anayetoka upande mmoja kwenda upande mwengine.

Aya ya 3

Imesemwa kuwa makusudio yake ni kwenda haraka na roho za waumini peponi na roha za makafiri motoni. Imesemwa na Malaika wanazichukua roho za waumini. Imesemwa ni Malaika wanaozitoa kwa upole roho za waumini, kisha wanaziacha zistarehe kama anavyoogelea mtu na kitu katika maji na kukiacha.

Imesemwa ni Malaika wanaoshuka kwa haraka kutoka mbinguni. Na imesemwa ni nyoota zinazoogelea; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na vyote vinaogelea katika njia zao ."(36:40).

Vile vile imesemwa ni farasi wa vita wanaokimbia kwa kasi. Imesemwa ni mauti yanaogelea katika nafsi za wanyama. Imesemwa ni majahazi yanayoelea majini. Imesemwa ni mawingu: Na imesemwa ni wanyama wa baharini.

Aya ya 4

Imesemwa kuwa ni Malaika, kwani wao wametangulia binadamu kwa heri, imani na amali njema. Imesemwa ni Malaika wa mauti wanatangulia kuipeleka roho ya muumini peponi na ya kafiri motoni. Imesemwa ni Malaika wa wahyi (ufunuo) wanawatangulia mashetani kwa Mitume kwa kuwapa wahyi. Imesemwa ni roho za wauminii zinawatangulia Malaika wazozichukua, kwa shauku ya kuonana na Mola wao. Imesemwa ni nyota zinazotanguliana katika kwenda. Imesemwa ni farasi wa vita wanatanguliana katika vita. Na imesemwa ni mauti yanatangulia tamaa.

Aya ya 5

Imesemwa ni Malaika woote wanaopanga mambo. Wafasiri wengi wamesema hivyo mpaka ikadaiwa kuwa wameafikiana wafasiri. Hata hivyo pia imesemekana kuwa makusudio ni Malaika wanne wenye kupanga mambo ya Dunia:

1. Jibril: anayepanga mambo ya upepo, askari na wahyi.

2. Mikail: anayepanga mambo ya mvua na mimea.

3. Izrail: Mwenye kuwakilishwa kuchukua roho.

4. Israfil: Mwenye suri (parapanda).

Imesemekana kuwa ni falaki zinatokewa na jambo la Mwenyezi Mungu, halafu (athari) ya hukumu ya Mwenyezi ikaonekana duniani. Kuna kauli kwamba kiapo katika aya zote tano kiko katika tamko lililoondolewa, kukadiria kwake ni "naapa kwa Mola wa Malaika wanaotowa roho." Kwa kuangalia kwako mwenyewe utaona kwamba mpangilio wa aya tano ni mpangilio mmoja wenye kuambatana na kufanana mafungu yake, hauafikiani na nyingi ya kauli hizi kwa kuhitalifiana maana ya chenye kuapiwa; kama vile kuwa makusudio ya aya ya kwanza yawe Malaika wenye kuchukua roho za makafiri na aya ya pili iwe ni wanyama mwitu, ya tatu majahazi ya nne mauti kutangulia tamaa na ya tano iwe ni falaki. Zaidi ya hayo nyingi katika kauli hizo hazina dalili kwa upande wa mpangilio isipokuwa kuangalia kilugha tu. Tena nyingi katika kauli hizo hazinasibiana na mpangilio wa aya za Sura ambayo inataja ufufuo na kutoa hoja juu ya kutukia kwake, kama ilivyo katika Sura ya Al-Mursalaat (77) ambayo ina mazungumzo yenye kunasibiana katika kiapo na jawabu yake.

Tunayoweza kusema:

Na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi - ni kwamba yale yaliyomo katika aya hizi katika sifa za chenye kuapiwa yanakubali kufungamana na sifa za Malaika katika kufuata amri wanazopewa kutoka katika upande wenye nguvu amri zinazofungamana na kupanga mambo ya ulimwengu huu wenye kushuhudiwa; kisha wasimamie (malaika) mipango yenyewe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Aya hizo zinafanana na aya za mwanzo wa Sura ya Assaffat zinazosema:

"Naapa kwa Malaika wajipangao safu tena kwa wale wanaokataza mabaya. Kisha kwa wale wasomao mawaidha (ya Mwenyezi Mungu)." (37: 1-3).

Pia zinafanana na aya za mwanzo za Sura Wal-Mursalaat. "Naapa kwa (kundi la Malaika) linalopelekwa kwa kufuatana. Wakafuatana kama pepo zinazovuma kwa kasi. Na kwa (Malaika) wanaotawanya (kurasa zenye kuandikwa wahyi). Wakapambanua (haki na batili na halali na haramu). Wakapeleka wahyi (kwa Mitume). Kwa ajili ya kuondosha udhuru au kuhadharisha". (77:1 - 6).

Zote hizo zinasifu Malaika kufuata kwao amri ya Mwenyezi Mungu, hizo zinasifu Malaika wa wahyi, lakini Sura hii inasifu Malaika wote katika kupanga mambo ya ulimwengu, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kisha linalodhihirisha zaidi sifa zilizotajwa katika aya hizi tano katika kufungamana na Malaika, ni neno lake "na wenye kupanga mambo". Ikiwa aya ya 3, imeanza na herufi "Fa" inayofahamisha kuwa sifa ya kupanga imetokana na sifa ya kutangulia. Vile vile aya ya 4 imekutanishwa na herufi "Fa" kufahamisha kuwa sifa ya kutangulia imetokana na kufanya haraka, hayo yanafahamisha kuwa maana ya aya tatu (3, 4 na 5) ni ya jinsi moja. Ufahamisho wake ni kuwa wao wanapanga mambo baada ya kutanguliana na kwenda haraka. Kwa hiyo makusudio ya wenye kwenda haraka na wenye kutangulia, ndio wale wenye kupanga mambo. Kwa kuzingatia kushuka kwao kwenye lile waliloamrishwa kulipanga. Aya hizo tatu ziko katika maana ya aya hii: "Ana (kila mtu) kundi (la Malaika) mbele yake, nyuma yake wanamuhifadhi (na kuyadhibiti anayoyafanya) kwa amri ya Allah." (13:11)

Ikiwa makusudio ya aya tatu ni kuonyesha kuharakisha Malaika kushuka kwenye lile waliloamrishwa na kutangulia na kulipanga, inaonyesha aya ya (1-2) ni kutoka kwao pale wanapoambiwa kuliendea lile waliloamrishwa na kutoka kwao sehemu zao. Kama vile, ambavyo aya ya (3) ni kuharakisha kwao baada ya kutoka. Na hilo linafuatiwa na kutangulia kwao na kupanga mambo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo aya tano ni kiapo kwa sifa wanazokuwa nazo wakati wanapoamrishwa kupanga mambo ya ulimwengu, kuanzia wanapoanza kushuka mpaka kutimia kupanga.

Pia zinaonyesha nidhamu ya mpangilio wa Mwenyezi Mungu, wakati wa kuzuka tukio; kama vile ambavyo aya zinazofuatia (yaani aya ya 15..) zinaonyesha mipango ya Mungu iliyowazi katika ulimwengu huu. Katika mipangilio ya Malaika ni hoja juu ya ufufuo na malipo; kama vile ambavyo mipangilio ya kidunia yenye kushuhudiwa ni hoja juu ufufuo; kama yatakavyokuja maelezo (Inshallah) katika utafiti wa hadith.

Malaika Ni Mawakala Katika Kupanga Mambo Malaika ni mawakala kati yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na vitu, tangu mwanzo hadi marejeo, kutokana na maana yanayotolewa na Qur'an, kwamba wao ni sababu ya matukio zaidi ya sababu zinazoonekana katika ulimwengu huu tunaouona, kabla ya kufa watu na kugura kwenye ufufuo wa akhera na baada yake. Uwakala wa Malaika uko wazi katika marejeo ambayo ni hali ya kudhihiri mauti, kuchukuliwa roho, kuulizwa kaburini ikiwa ni pamoja na thawabu zake na adhabu yake na kuuliwa wote kwa mpuzio wa suri.

Vile vile kufufuliwa, kupewa kitabu, kuwekwa mizani (hisabu) na kupelekwa peponi au motoni, katika yote hayo uwakala wa Malaika uko wazi. Na aya zinazofahamisha hilo ni nyingi hazina haja ya kuzirudia. Vile vile hadith za Mtume(s.a.w.w) na Maimamu hazina hesabu. Ama uwakala wao katika kupanga mambo unafahamishwa na yaliyoko mwanzo wa Sura hii. Aya ya (1-5) kama yalivyotangulia maelezo. Vile vile kauli yake Mwenyezi Mungu: "Aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa, mbili mbili, tatu tatu na nne nne.. " (35:1).

Yaani Malaika wote wameumbwa kuwa mawakala kati yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na viumbe vyake. Wanapelekwa kutekeleza amri yake, kama linavyofahamisha neno lake Mwenyezi Mungu: "..bali hao (Malaika) ni waja waliotukuzwa. Hawamtangulii (Mwenyezi Mungu) kwa neno na wao wanafanya kwa amri yake ." (21:25-26).

Na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Wanamwogopa Allah aliye juu yao na wanatenda wanayoamrishwa ." (16:50) Kwa hiyo Malaika hawana shughuli yoyote isipokuwa uwakala kati ya kiumbe na Mwenyezi Mungu S.W.T kwa kutekeleza amri yake, bila ya tofauti yoyote. Mwenyezi Mungu anasema : "Hakika Mola wangu yuko juu ya njia ilinyooka ." (11:56) Anasema tena: "Wala hutapata mabadiliko katika kawaida (desturi) ya Allah wala hutakuta mageuzo katika kawaida (desturi) ya Allah ." (35:43)

Katika uwakala baadhi yao wana vyeo vya juu kuliko wengine na mwenye cheo cha juu humwamrisha wa chini katika kupanga mambo. Kwa mfano Malaika wa mauti anamwakilisha Mwenyezi Mungu kwa kutoa amri kwa wasaidizi wake wachukue roho. Mwenyezi Mungu anasema kuzungumzia Malaika: "Na hakuna yoyote miongoni mwetu ila anapo mahali pake maalum ." (37:164) Na anasema tena: "Mwenye kutiiwa huko mwaminifu ." (81:21)

Aya Ya 6-7

Imefasiriwa ya kwanza kwa maana ya ukelele mkubwa wa kwanza ambao una migongano. Na ya pili imefasiri kuwa ni ukelele wa pili. Kwa hiyo zinafungamana aya mbili na kelele mbili za parapanda ambayo inafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na itapigwa parapanda watoke roho, watu waliomo mbinguni na waliomo ardhini ila yule amtakaye Mwenyezi Mungu. Tena itapigwa mara nyengine hapa watafufuka wawe wanatazama (nini kitatokea) ." (39:67)

Imesemekana kuwa maana yake ni mtetemeko na makusudio yake vile vile ni mpuzio wa kwanza utakaotetemesha ardhi na majabali. Imesemwa makusudio yake ni mbingu na nyota ambazo zitatetemeka na kugongana na kupasuka. Njia zote hizo mbili haziepuki kuwa mbali na maana hasa ya mwisho. Kwa hali yoyote lenye kunasibiana zaidi ni kuwa aya hizo ni jawabu la kiapo kilichoondolewa kwa kufahamisha juu ya uzito wake nacho ni: naapa mtafufuliwa.

Aya Ya 8-9

Kunasibisha macho na nyoyo mahali pamoja ni kwamba makusudio ya nyoyo katika mfano wa sehemu hizo ambazo zinaegemezwa sifa za utambuzi kama elimu, hofu, matarajio na n.k., ni nafsi. Na kunasibisha kunyenyekea kwa macho ambako ni katika hali za moyo, ni kwa kudhihiri athari ya moyo yenye kufahamika katika macho yenye nguvu zaidi kuliko viungo vyengine.

Aya Ya 10

Ni kueleza kusema kwao kuwa ufufuo uko mbali; na kuonyesha kuwa hawa ambao nyoyo zao zitatetemeka na macho yao kuinama chini siku ya Kiyama ni wale wanaokanusha ufufuo katika dunia. Neno Hafira - kama ilivyosemwa- lina maana ya mwanzo wa kitu, Na swali limekuja kwa maana ya kukanusha maana yake ni: Je, hivi sisi tutarudisha hali yetu ya mwanzo baada ya kufa?

Imesemekana kuwa maana ya neno "Hafira" ni ardhi ya kaburi, maana yake ni: Je, tutarudi kuwa hai na kutoka katika makaburi yetu baada ya kufa? Pia imesemwa aya inatolea habari kukiri kwao ufufuo siku ya Kiyama. Na maneno hayo watayasema baada ya kufufuliwa. Swali ni la kushangaa; kana kwamba wao watapofufuliwa wakashuhudia waliyoyashuhudia watashangaa, na watataka kujua walivyorudi hai baada ya mauti. Haya ni maana mazuri, kama sikuhitalifiana na mpangilio wa maneno.

Aya Ya 11

Kukaririka kuuliza ni kwa ajili ya kukokoteza kuliweka mbali suala la ufufuo.

Aya Ya 12

Ishara ya kusema "hayo" ni hayo ya kurudi kunakofahamishwa na aya ya 10. Kauli yao hiyo ni kwa njia ya kucheza shere. Au ni kwa kukadiria kuwa watasema hivyo wakati wa kufufuliwa kwa njia ya kuona wameharibikiwa.

Aya Ya 13-14

Dhamiri ni ya marejeo. Imesemwa kuwa ni ua ukelele wa pili. Aya hizi mbili ziko katika mahali pa jawabu la swali lililoulizwa katika aya ya 10-11.

Maana yake: Sio uzito kwetu kuwafufua baada ya kuwafisha. Kwani huko kuwarudisha au huo ukelele wa pili utakuwa ni ukelele mmoja tu! Mara wao watakuwa juu ya ardhi baada ya kuwa ni wafu ndani yake.

Aya hizo ziko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Wala halikuwa hilo jambo la Kiyama ila ni kama kupepesa jicho au ni karibu zaidi.. " (16:77)

Aya Ya 15

Kuanzia aya hii mpaka ya 26 ni kuonyesha kwa ujumla kisa cha Nabii Musa na ujumbe wake kwa Firaun aliyepinga mlingano wake na kupatwa na adhabu ya akhera na ulimwengu. Katika kisa hicho mawaidha na maonyo kwa wanaomshirikisha Mungu, wenye kukanusha ufufuo. Hawa wamefanya kukanusha kufufuliwa kuwa ni kisingizio cha kukanusha mlingano wa kidini kwa sababu hakuna maana ya sheria ya dini la hakuna krejeshwa tena kuwa hai. Na katika kisa hicho pamoja na hayo ni kutuza moyo wa Mtume(s.a.w.w) kutokana na kukadhibishwa na watu wake.

Pamoja na yote hayo kisa kizima ni hoja ya kutokea ufufuo na malipo. Kwani kuangamia kwa Firaun na jeshi lake- kisa ambacho ni cha kufazaisha ni dalili juu ya ukweli wa Mtume Musa kutoka upande wa Mwenyezi Mungu kwenda kwa watu. Wala hautimii ujumbe wake kutoka upande wake Mwenyezi Mungu Mtukufu isipokuwa kwa uungu wake kwa watu, kinyume na wanavyodai wanashirikisha Mungu kwamba hakuna uungu kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa watu na kwamba kuna waungu wengine, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa miungu hiyo tu. Kwa hiyo aya hii ya (15) ni swali la kumkaribisha msikilizaji katika kusikia mazungumzo ili atuze moyo wake na iwe ni onyo na kutimiza hoja kwa wale wanaokanusha.

Aina hii ya swali haikanushi kwa msikilizaji anayajua hayo yenye kuzungumza, kwa sababu makusudio ni kuuelekeza mtazamo wa msikilizaji kwenye mazungumzo na wala sio swali la kihakika au kutaka kufahamisha. Kwa hiyo inawezekana kuwa aya hizi ndiyo mwanzo wa Mwenyezi Mungu kusimulia kisha cha Musa au kuwa zilikwishatanguliwa na masimulizi mengine ya Musa. Kama katika Sura ya Al-Muzzammil (73) kilivyosimuliwa kisa kwa ujumla. Sura hiyo imetangulia sura hii An-Nazia'at kwa kuteremshwa. Vile vile katika Sura ya A'araf (7), Twaha (20) n.k.

Aya Ya 16

Hapo ilikuwa ndiyo mwanzo wa kupewa wahyi Mtume Musa(a.s) .

Aya Ya 17

Ni tafsiri ya mlingano.

Aya Ya 18

Makusudio ya kujitakasa hapa, ni kujitakasa na uchafu wa kupetuka mipaka.

Aya Ya 19

Inaungana na aya iliyotangulia. Makusudio ya kumca Mwenyezi Mungu ni kumcha kwenye kulazimiana na imani inayompelekea kufanya twaa, kujikinga na maasia baada ya kujitakasa kwa toba.

Aya Ya 20

Makusudio ya muujiza mkubwa ni muujiza wa fimbo. Imesemwa makusudio yake ni mkusanyiko wa miujiza ya Nabii Musa aliyomwonyesha Firaun.

Aya Ya 21

Yaani alimkadhibisha Musa na akamwita mchawi. Na akamwasi kwa aliyomwamrisha au alimwasi Mungu.

Aya Ya 22

Yaani alifanya jitihadi kubatilisha jambo la Musa na kumpinga.

Aya Ya 23

Maskusudio ya watu aliowakusanya ni watu wa mamlaka yake. Imesemwa kwa makusudio yake ni kuwakusanya wachawi kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Basi Firaun akawatumwa wakusanyo watu katika miji ." (26:53)

"Basi Firaun akapa mgongo na akatengeneza hila yake kisha akaja. " (20:60) Lakini hakuna dalili ya kuwa makusudio ya kukusanya katika aya hii ndiyo hayo hayo yaliyoko katika aya mbili hizo.

Aya Ya 24

Kwa dhahiri ni kuwa yeye alidai kuwa juu zaidi ya waungu wengine waliokuwa wakiabudiwa na watu wake wanaoabudu masanamu. Huenda makusudio ya kujifanya Mungu bora, pamoja na kuwa Yeye naye anaabudu miungu, ni kwa kujiona kwamba yeye ni Mungu aliyekaribu, riziki zao zinapitia mikononi mwake na yeye ndiye anayewatengenezea maisha yao na ndiye anayechunga utukufu wao; na miungu wengine hawana sifa hizi. Imesemwa makusudio ya aliyoyasema, ni kujifanya bora kwa kila kiongozi wa mamlaka yake; yaani kujifanya mfalme na kwamba yeye ndiye aliye juu ya wanaoshikilia mamlaka mbali mbali kama vile mahakimu n.k. Kwa hiyo aya inakuwa katika maana ya aya inayosema: "Na Firaun alitangaza kwa watu wake, akanena: Enyi watu wangu! Utawala wa Misri si wangu, na pia mito hii ipitayo mbele yangu? Je, hamuoni? " (43:51).

Lakini hayo ni kinyume na dhahiri ya maneno yaliyo katika aya hii: "Enyi watu wakuu simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi ." (28:37)

Aya Ya 25

Maana yake Mwenyezi Mungu akamwadhibu Firaun adhabu ya dunia na akhera; ama adhabu ya dunia ni kumgharikisha yeye na jeshi lake, na adhabu ya akhera nu kumwadhibu baada ya mauti. Kwa hivyo makusudio ya "Akhirata wal-ula"ni akhera na ulimwengu.

Imesemwa makusudio yake ni tamko lake (Firaun) la kwanza alilosema kabla hii ambalo ni "Simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi ." (28:38).

Na la pili ni pale aliposema "Mimi ndiye Mola wenu mkubwa." Lakini maana haya yamejificha sana, Imesemwa kuwa "ula" ni kukadhibisha kwake na kuasi kwake kulikotajwa katika mwanzo wa kisa na "Akhirata" ni kusema kwake "Mimi ni Mola wenu mkubwa." Lakini maana haya pia yamejificha sana." Pia imesemwa "ula" ni mwanzo wa maasi yake na "Akhirata" ni mwisho wake. Lakini kauli zote hizo haziko wazi.

Ay Ya 26

Inaishiria kwenye mazungumzo ya Musa. Maana yake mazungumzo haya ya Musa mna mazingatio kwa mwenye kucha na akawa na maumbile ya kuucha uovu na adhabu, ambayo ni ya mtu mwenye umbile la sawasawa. Imesemekana kuwa kuna maneno yalioondolewa; kukadiria kwake ni 'kwa anayemcha Mwenyezi Mungu.' Lakini njia tuliyoelezea kwanza ndiyo inayowakilisha maana zaidi.

Aya Ya 27

Ni matahayarizo kwa njia ya lawama kwa wanaomshirikisha, wenye kukanusha ufufuo na wenye kucheza shere. Pia inakusanya jawabu la kuweka mbali kwao ufufuo, kwa neno lao lililo katika aya ya (10-11) katika Sura hii. Kwamba Mwenyezi Mungu ameweza kuumba vitu vilivyo na umbo gumu zaidi yenu basi kuwaumba na kuwafufua tena anaweza tu. Pia inakusanya hoja ya kutokea ufufuo kutokana na kutaja mpangilio wa kijumla wa kilimwengu, kufungamana kwake na ulimwengu wa kibinadama ambako kumelazimisha kuweko Mwenyezi Mungu na kuweko Utume na sharia na hayo yamelazimu na malipo ambayo sehemu yake ni ufufuo. Ndio maana Mwenyezi Mungu akafuatisha aya hizi na aya inaoelezea Kiyama (aya ya 34). Kwa hiyo aya ya 27 ni swali la kutahayariza kwa kuondoa madai yao ya kuuweka mbali ufufuo baada ya kufa. Kufafanua mbingu kwa ksemwa "alizozijenga" ni dalili ya kuthibitisha kuwa mbingu ina umbo gumu zaidi.

Aya Ya 28

Yaani kuinua sakafu yake na kuifanya sawa kulingana na mafungu yake kwa kuliweka kila moja mahali pake panapopitishwa na hekima.

Aya Ya 29

Mchana na usiku umenasibishwa na mbingu kwa sababu ya asili ya vitu hivyo ni ya mbiguni, nayo ni kwamba maumbo ya vitu vyenye giza yanasababishwa kwa kujificha nuru hasa ya jua na inapodhihiri ndipo maumbo ya vitu hivyo pia yanang'aa. Wala hauhusiki usiku na mchana na ardhi tunayoishi tu, bali na maumbile ya vitu vingine kadhaa.

Aya Ya 30

Yaani akaitandika ardhi baada ya kuijenga mbingu. Imesemwa kuwa maana ya neno "Baada" ni pamoja na wala sio baada. Kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu aliyotumia tamko "Baada" kwa maana ya pamoja. "Mwovu sana pamoja na hayo ni mtu asiyekuwa na asili ." (69:13).

Aya Ya 31

Makusudio ya kutoa maji ni kufungua chemchemi na kupitisha mito juu ya ardhi inayootesha mimea ambayo ni chakula cha binadamu na wanyama. Kwa hiyo makusudio ya neno "Mar-a" ni mmea wote wa chakula cha watu na wanyama kama inavyo tambulisha aya inayofuatia. Wala sio malisho ya wanyama tu; Kama ilivyozoeleka kutumika tamko hilo.

Aya Ya 32

Yaani ameyathibitisha katika ardhi ili zisiwayumbishe. Na akaweka hazina ya maji na madini kama zinavyofahamisha aya nyengine.

Aya Ya 33

Yaani yote yaliyoumbwa yaliyotajwa mbingu, ardhi n.k. ni kwa ajili ya manufaa yenu na ya wanyama wenu ambao amewalishieni ili mustarehe nao katika maisha yenu. Kwa hiyo maumbile haya na mipangilio hii ni migumu kimaumbile kuliko kuumbwa kwenu; basi si sawa kuona ajabu kuumbwa kwenu mara ya pili.

Aya Ya 34

Makusudio ya balaa kubwa ni Kiyama kwani ni balaa ya mabalaa. Kuanza aya hii kwa herufi "Fa" ya kuunganisha na kuonyesha kuwa Kiyama ni katika mambo yanayolazimiana na kuumbwa mbingu na ardhi na mipangilio yake.

Aya Ya 35

Ni siku hiyo ya balaa kubwa.

Aya Ya 36

Yaani utadhihirishwa moto kwa kuondolewa pazia, aushuhudie kila mwenye kuona kwa macho yake. Aya iko katika maana ya aya inayosema: "Kwa hakika ulikuwa umo katika kughafilika na jambo hili; basi tumekuondolea pazia yako; kuona kwako leo kumekuwa kukali ." (50:22).

Isipokuwa ay hii ina upana zaidi wa maana. Vile vile ayah ii ya 36 inadhihirisha kuwa moto ni wenye kuumbwa kabla ya siku ya Kiyama, na kwamba utadhihiri siku hiyo kwa kuondolewa pazia.

Aya Ya 37 - 41

Ni ufafanuzi wa hali za watu siku hiyo katika kugawanyika kwao. Mwenyezi Mungu S.W.T. amewagawanya watu wa motoni na wa peponi. Ametanguliza sifa za watu wa motoni kwa sababu maneno zaidi yameelekezwa kwa wanaomshirikisha Mungu. Amewasifu watu wa motoni kwa kupituka mipaka na kupendelea maisha ya dunia. Kinyume chake ni vile alivyowasifu watu wa peponi kwa kuogopa kusimama mbele za Mola na kuizuilia nafsi na matamanio. Ikiwa makundi mawili yanakabiliana hali zao, itakuwa kila sifa ya kundi moja ni mkabala wa sifa ya kundi jengine. Kwa hiyo hofu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu na kuizuilia nafsi na matamanio mkabala wake ni kupetuka mipaka ambako ni kukosa kuathirika kwao na kusimama mbele ya Mola wao kwa kiburi na kutoka kwao na kipambo cha utumwa hawanyenyekei, hawapiti katika sehemu wanazotakiwa kupita wala hawachagui waliyochaguliwa miongoni mwa wema wa milele, bali wanafuata mapenzi ya nafsi zao katika anasa za maisha ya ulimwengu.

Kwa hiyo kupetuka kwao mipaka ni kuchagua kwao maisha ya dunia kama alivyowasifia Mwenyezi Mungu kwa kusema "Akapendelea zaidi maisha ya dunia". Ikiwa kupetuka mipaka ni kuikataa akhera na kuathirika na maisha ya dunia ambako ni kufuata nafsi vile inavyotaka na kuitii na kumkhalifu Mwenyezi Mungu Mtukufu itakuwa mkabala wake ni kuogopa kufuata matamanio ya nafsi, ambako ni chimbuko la kujizuilia na kushikamana na maisha ya dunia. Ndivyo alivyowasifu Mwenyezi Mungu watu wa peponi kwa kusema:"Akaizuilia nafsi na matamanio" baada ya kuwasifu kuwa wanaogopa.

Hakjika Mwenyezi Mungu amesifu "kuzuilia nafsi na matamanio" bila ya kusema kuacha kuifuata kimatendo. Kwa sababu binadamu ni mdhaifu, huenda akasukumwa na ujinga kwenye maasia bila ya kiburi. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe kama alivyosema: "Ni vya Allah vilivyomo mbinguni na ardhini ili awalipe wabaya kwa hayo wanayoyatenda, na kuwalipa mema wale wanaofanya mema. Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu isipokuwa makosa hafifu, hakika Mola wako ndiye mwenye maghufira mengi ." (53:31-32).

Amesema tena:

"Kama mkijiepusha na maovu makubwa mnayokatazwa, tutawafutia makosa yenu madogo na tutawaingiza mahali patukufu ." (4:31)

Maana inayopatikana katika aya tatu ni kuwa watu wa motoni ni watu wa kufuru na ufasiki na watu wa peponi ni watu wa imani na takuwa. Kuna makundi mengine katika wanyonge na ambao wamekiri dhambi zao wamechanganya amali njema na mbovu na wengineo jambo lao liko kwa Mwenyezi Mungu, huenda Mwenyezi Mungu atawakusanya kwenye maghufira kwa kuombewa n.k.

Neno "Maqam" kwa asili ni mahali kinaposimama kitu au kusimama, lakini mara nyengine huja kwa ibara ya sifa na hali kwa mahali kama Cheo; Mwenyezi Mungu amelitumia neno hilo kwa maana hayo aliposema: ",,,,Basi wawili wengine watasimama mahali pao ." (5:107).

Kwa hiyo cheo chake Mwenyezi Mungu penye kunasibishiwa naye, ni sifa ya Ubwana wake inayolazimiana na sifa zake tukufu; kama ujuzi, uwezo, nguvu, ushindi, rehema na ghadhabu na yanayonasibiana na sifa hizo. Mwenyezi Mungu anasema: "Wala msipetuke mipaka katika hayo, isije ikawashukia ghadhabu yangu. Na ambaye imemshukia ghadhabu yangu, huyo ameangamia " (20:81 - 82).

Amesema tena: "Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ni Mwingi wa Kusamehe, Mwingi wa Kurehemu. Na hakika adhabu yangu ni adhabu inayoumiza kweli kweli ." (15:49-50).

Basi daraja ya Ungu wake ndiyo inayoogopesha waja wake, nayo ni msingi wa Rehema Yake, na msamaha wake kwa mwenye kuamini na Kumcha Mwenyezi Mungu na ni uchungu wa adhabu yake kwa mwenye kukadhibisha na kuasi. Imesemwa kuwa makusudio ni kusimama mbele ya Mola wake siku ya Kiyama wakati atakapoulizwa amali zake. Pia imesemwa maana yake ni kumwogopa Mola wake.

Utafiti Wa Hadith Katika Faqih amepokea Ali bin Mahziyar amesema: Nilimuuliza Abu Jaffar(a.s) kuhusu viapo anavyoapia Mwenyezi Mungu kama kuapia kwa usiku wa manane n.k. Akasema: "Hakika Mwenyezi Mungu anaweza kuapa kwa viumbe vyake vile anavyotaka lakini viumbe hawawezi kuapia kitu chengine isipokuwa Yeye Mwenyezi Mungu." Katika Durril Manthur ametoa Said bin Al-Mansur Ibn Al-Mundhir kutoka kwa Ali kuhusu aya ya 1 akasema: "Ni Malaika wanaotoa roho za makafiri na aya ya (2) ni Malaika wanaing'oa roho kati ya kucha na ngozi mpaka waitoe. Aya ya (3) ni wanaogelea na roho za waumini kati ya mbingu na ardhi. Aya ya (4) ni Malaika wanaotanguliwa na roho za waumini kwa Mwenyezi Mungu. Aya ya (5) ni Malaika wanaopanga mambo ya waja."

Katika hiyo Durril Manthur, ametoa Ibn Abu Hatim kutoka kwa Ali bin Abu Twalib, kwamba Ibnul Kawwa alimuuliza kuhusu aya ya (5) akasema ni Malaika wanaozingatia utajo wa Mwenyezi Mungu na amri yake. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (6) amesema itapasuka ardhi na neno "Radifa" ni ukelele. Katika hiyo tafsiri kuhusu aya ya (10) amesema: Walisema Maquraish hivi tutarudi baada ya kufa?

Tena katika hiyo hiyo Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya (12) anasema walisema hivi kwa njia ya kucheza shere. Katika hiyo hiyo tafsiri katika riwaya ya Abul Jarud kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) amesema kuhusu aya ya (10) wanasema kuhusu umbo jipya ama aya ya (14) walikuwa katika makaburi waliposikia ukelele walitoka katika makaburi yao wakawa juu ya ardhi.

Katika Usulul-Kafi kwa kutegemezwa kwake kwa Daud Arraqi kutoka kwa Abu Abdillahi kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na mwenye kuogopa cheo cha Mola wake atapewa mabustani (pepo) mawili ." (55:46). Amesema: Mwenye kujuwa kwamba Mwenyezi Mungu anamuona, na kusikia anayoyasema na kujuwa anayoyajua katika heri au shari hilo litamzuwiya na kufanya matendo mabaya huyo ndiye yule anayeogopa cheo cha Mola na akaizuilia nafsi na matamanio.

Hadith hiyo inatilia nguvu maana yaliyotangulia kuelezwa kuhusu kuogopa cheo chake Mwenyezi Mungu (s.w.t) Katika hiyo Usulil-Kafi kwa kutegemezewa Yahya bin Akil amesema: Amesema Amirul Mominin(a.s) : Hakika mimi ninaogopa kwenu mambo mawili; kufuata matamanio na tamaa ndefu. Ama kufuata matamanio hakika kunazuia haki. Ama tamaa ndefu inasahauliza akhera.

Aya Ya 42 - 46 42.

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ﴿٤٢﴾

42. Wanakuuliza habari ya Kiyama kutokea kwake kutakuwa lini?

فِيمَ أَنتَ مِن ذِكْرَاهَا ﴿٤٣﴾

43. Ujo wapi wewe na kuwatajia (habari ya Kiyama).

إِلَىٰ رَبِّكَ مُنتَهَاهَا ﴿٤٤﴾

44. Ukomo (wa ujuzi) wake ni kwa Mola wako peke yake.

إِنَّمَا أَنتَ مُنذِرُ مَن يَخْشَاهَا ﴿٤٥﴾

45. Wewe ni mwonyaji tu. Kwa anayekiogopa.

كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا ﴿٤٦﴾

46. Siku watakayoiona, watakuwa kana kwamba hawakukaa ila kitambo cha jioni moja na asubuhi yake.

UBAINIFU

Ni kuonyesha kuuliza kwao Kiyama na majibu yake, kwamba ujuzi wa Kiyama uko kwa Mwenyezi Mungu tu.

Aya Ya 42

Kwa dhahiri ibara ya wanakuuliza inafahamisha kuendelea; walikuwa wanaomshirikisha Mungu baada ya kusikia mazungumzo ya Kiyama wakimrudia Mtume(s.a.w.w) na kumtaka awaelezee hasa wakati wa Kiyama. Walikuwa wakiendela hivyo. Qur'an imelikariri hilo mara nyingi. Kusema: Kutokea kwake kutakuwa lini na kubainisha swali na maana yake: wanakuuliza hawa wanakanushaji kuhusu Kiyama kwa kucheza shere.

Aya Ya 43

Ni swali la kukanusha; yaani hataweza kukijua kwa kukitaja sana. Au ikiwa "Dhikra" ni kwa maana ya kuhudhuria hakika ya kitu katika moyo wa mtu, maana yake ni: huna ujuzi nacho hata uweze kujua hakika yake. Maana haya ndiyo yanayosibiana zaidi kuliko yaliyotangulia. Imesemwa maana yake ni: kukitaja hicho Kiyama sio mambo yanayofungamana na ujumbe wako, wewe umepelekwa kumwonya anayekiogopa. Imesemwa maana yake ni kukanusha kuuliza kwao, kwa maana ya kuwa; swali hili ni lanini, na hali wewe utakitaja tu, kwa sababu hilo linafungamana na utume wako kwa kuwa wewe ni Mtume wa mwisho. Imesemwa aya ni swali kamili walilouliza wanaomshirikisha Mungu kwa Mtume(s.a.w.w) . Maana yake: Unajua nini kuhusu Kiyama na wakati wake? Au umepata kujua nini na kukitaja kwako sana? Wewe mwenyewe msomaji unajua zaidi kwamba mpangilio wa aya hauoani kabisa na chochote katika maana haya.

Aya Ya 44

Ni sababu ya maneno yaliyotangulia maana yake: wewe hujui wakati wake kwa sababu ukomo (wa ujuzi wake) ni kwa Mola wako. Haijulikani hakika yake na sifa zake. Sio mbali - Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi - kuwa aya iko mahali pa sababu ya maana nyengine nayo ni kuwa Kiyama kitasimama kwa kuishi vitu na kuondoka sababu zote, na kudhihiri kuwa hakuna ufalme isipokuwa wa Mwenyezi Mungu pekee mwenye kushinda, hainasibishwi siku isipokuwa kwake Yeye Mwenyezi Mungu bila ya kuingiliwa kati na sababu yoyote. Kwa hivyo siku hiyo haikubali kuwekewa wakati kwa hakika.

Kwa hiyo ndio maana hayakuja katika maneno ya Mwenyezi Mungu maelezo ya kuelezea siku halisi isipokuwa tu, kuelezea siku kwa kwisha dunia, kama vile kusema kwake:

"Na itapigwa parapanda watoke roho watu waliomo mbinguni na waliomo ardhini (39:68). Miongoni mwa maana ya aya hiyo ni kufahamisha juu ya kuharibika dunia kwa kubadilika ardhi, mbingu na kupukutika nyota n.k. Sehemu nyengine ameielezea siku kwa kufananisha tu, kama vile aya ya mwisho wa Sura hii, na pia kauli yake Mwenyezi Mungu: "Siku watakayoyaona waliyoahidiwa itakuwa kama kwamba hawakukaa ulimwenguni ila saa mmoja ya mchana " (46:35).

Kisha anataja uhakika wa kauli katika hilo kwa kusema: "Na waliopewa ilimu na imani watasema: Hakika nyinyi mmekaa kwa hukumu ya Allah mpaka siku ya kufufuliwa, basi hii ni siku ya kufufuliwa ." (30:56) Yanafahamisha maneno ya Mwenyezi Mungu kwamba Kiyama kitafika kwa ghafla tu. Mwenyezi Mungu anasema: "Hakitawafikia ila kwa ghafla (tu!) ." (7:187).

Hii ni njia iliyondani sana inayohitaji ukamilifu wa kufikiria vizuri, ili kuondoa shaka ya yanayodhihiri katika aya nyingi za kiyama. Hebu angalia vizuri aya hii: "Kwa hakika ulikuwa umo katika kughafilika na jambo hili, basi tumekuondolea pazia yako; kuona kwako leo kumekuwa kukali ." (50:22).

Pamoja na aya nyengine zenye maana haya. Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kutakwa msaada.

Aya Ya 45

Yaani tumekukalifisha kumwonya anayekiogopa Kiyama, sio kutolea habari wakati wake. Kwa hiyo hakuna haja ya kuwajibu kuhusu wakati wake. Makusudio ya kuogopa kutokana na kunavyonasibiana na mahali hapa, ni kuogopa kinapotajwa.

Aya Ya 46

Ni ubainifu wa kukaribia Kiyama kwa njia ya kufananisha. Imedhihiri kwamba makusudio ya kukaa ni kukaa kati ya uhai wa dunia na kufufuliwa yaani kukaa makaburini. Imesemwa kuwa makusudio ya kukaa ni baina ya wakati wa hayo hayaafikiani na dhahiri ya aya nyengine zinazoonyesha kukaa kwao dhahiri ya aya nyengine hayo hayaafikiani na dhahiri ya aya nyengine zinazoonyesha kukaa kwao kabla ya kufufuliwa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka? Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku ." (23: 112-113)

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri Al-Qummi kuhusu aya ya (40-41) amesema ni mja akiwa kwenye maasi na akawa anaweza kuyafanya; kisha akayawacha kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu na makatazo yake, akaizuilia nafsi, basi malipo yake ni pepo. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Hatim na Ibn Murdawayh kwa Isnad dhaifu kutoka kwa Ibn Abbas amesema: Hakika washirikishaji Mwenyezi Mungu wa Makka walimuuliza Mtume(s.a.w.w) kwa kumchezashere: Ni lini kitakuwa Kiyama? Ndio ikashuka aya hiyo ya (42).

Katika hiyo hiyo Durril Manthur ametoa Al-Bazzar, Ibn Jariyr, Ibn Al-Mundhir na Ibn Murdawayh kutoka kwa Aisha amesema: "Hakuwacha kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu anauliza kuhusu Kiyama mpaka ziliposhuka aya hizo (44-45) ndipo hakuuliza tena. Amepokea vile Urwa kutoka kwa masahabu wengi, vile Shihab bin Twariq kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) lakini mpangilio hauafikiani kuwa ni jawabu la swali la Mtume(s.a.w.w) na hali Mtume alikwisha pewa wahyi katika Sura nyingi za Qur'an hasa zile zilizoshuka Makka kwamba ujuzi wa Kiyama unahusika na Mwenyezi Mungu (s.w.t) haijuwi isipokuwa yeye tu, na akaamrishwa kumjibu anayemuliza wakati wake, kuwa hajuwi.