TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39316
Pakua: 2864

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39316 / Pakua: 2864
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA ABASA (ALIFINYA USO (NA. 80)

INA AYA 42)

AYA 1-16

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

عَبَسَ وَتَوَلَّىٰ ﴿١﴾

1. Alikunja uso akapa mgongo.

أَن جَاءَهُ الْأَعْمَىٰ ﴿٢﴾

2. Kwa sababu alijiwa na kipofu.

وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّهُ يَزَّكَّىٰ ﴿٣﴾

3. Ni lipi la kukujulisha huenda akajitakasa.

أَوْ يَذَّكَّرُ فَتَنفَعَهُ الذِّكْرَىٰ ﴿٤﴾

4. Au akawaidhika ukamfaa waadhi?

أَمَّا مَنِ اسْتَغْنَىٰ ﴿٥﴾

5. Ama ajionaye amejitosha.

فَأَنتَ لَهُ تَصَدَّىٰ ﴿٦﴾

6. Wewe ndiye unayemshughulikia.

وَمَا عَلَيْكَ أَلَّا يَزَّكَّىٰ ﴿٧﴾

7. Wala si juu yako asipojitakasa.

وَأَمَّا مَن جَاءَكَ يَسْعَىٰ ﴿٨﴾

8. Ama yule anayekujia mbio mbio.

وَهُوَ يَخْشَىٰ ﴿٩﴾

9. Na hali yeye anamcha (Mungu)

فَأَنتَ عَنْهُ تَلَهَّىٰ ﴿١٠﴾

10. Wewe unajipurukusha naye!

كَلَّا إِنَّهَا تَذْكِرَةٌ ﴿١١﴾

11. La usifanye! Hakika hizo (aya za Qur'an) ni waadhi.

فَمَن شَاءَ ذَكَرَهُ ﴿١٢﴾

12. Anayependa ataukumbuka.

فِي صُحُفٍ مُّكَرَّمَةٍ ﴿١٣﴾

13. Umo katika vitabu vitakatifu.

مَّرْفُوعَةٍ مُّطَهَّرَةٍ ﴿١٤﴾

14. Vyenye kutukuzwa, vyenye kutwahirishwa.

بِأَيْدِي سَفَرَةٍ ﴿١٥﴾

15. Vimo katika mikono ya wajumbe.

كِرَامٍ بَرَرَةٍ ﴿١٦﴾

16. Watukufu watenda njema.

UBAINIFU

Zimekuja riwaya katika njia ya Ahli Sunnah kuwa aya ziliteremshwa katika kisa cha Ibn Umma Maktuum kipofu aliyeingia kwa Mtume akamkuta yuko na mabwana wa Kiquraysh anawaelezea jambo la Uislamu, Mtume akafinya uso wake. Ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamlaumu kwa aya hizi. Ziko baadhi ya riwaya za Shia zinazosema hivyo. Baadhi ya riwaya za Shia zinasema kuwa mwenye kukunja uso ni mtu moja katika Bani Umayya, alikuwa kwa Mtume akaingia Ibn Ummi Maktuum, akafinya uso yule mtu ndio zikashuka hizo aya, Utakujia ufafanuzi wa utafiti wa hilo katika utafiti wa hadithi (Inshallah). Vyovyote iwavyo kusudio la aya ni lawama kwa yule anayewatanguliza matajiri kuliko wanyonge na maskini walio waumini. Anawatukuza watu wa dunia na kuwaangusha watu wa akhera. Kisha zinakusudia kuonyesha vile anavyopuuza mtu kuumbwa kwake na kujizulia kwake kuzingatia vizuri jambo lake. Pia Sura inataja kwa Muhtasari kufufuliwa kwa mtu na kulipwa kwake, kama onyo. Sura hii imeshuka Makka bila ya ubishi.

Aya Ya 1-2

Ni maelezo ya kukunja uso na sababu yake.

Aya Ya 3-4

Makusudio ya kujitakasa hapa ni kujitakasa kwa amali njema baada ya kuwaidhika na kuzinduka kuitakidi haki. Kufaa waadhi ni kule kulingana kwake kujitakasa na imani na amali njema. Katika aya hizo nne mna lawama kubwa. Kunazidisha lawama kuzileta aya mbili za mwanzo kwa mfumo wa kumweleza mtu asiyekuwepo, kisha kuzileta aya mbili nyengine kwa mfumo wa kumwelekeza mtu kwa kutahayarisha na kuzidisha lawama.

Ibara ya kuja kipofo nayo inazidisha lawama, kwa vile haja ya kumshughulikia kipofu ambaye haja ya dini yake imemwacha ahangaike kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu, ilikuwa ni zaidi kumhurumia na kumpokea wala sio kumkunjia uso. Imesemwa kwamba ikiwa aya zinamhusu Mtume, kuleta ibara ya dhamiri ya mbali kwa aya mbili za mwanzo ni kumtukuza Mtume kwa kuchukulia, kuwa aliyefinya uso ni mtu mwengine sio Mtume(s.a.w.w) . Na kuleta aya mbili nyengine kwa dhamiri ya kumsemesha ni utukuzo pia kwa kuwa inaonyesha kumliwaza (Mtume) baada ya kumkaripia.

Lakini hayo hayaafikiani na dhamiri ya kusemesha iliyo katika aya zinazofuatia. (Ama ajionaye amejitosha. Wewe diye unayemshughulikia) ambazo zinalawama zaidi ya zilizo tangulia.

Aya Ya 5 -7

Makusudio ya kujitosha ni kujitosha na kuonekana mkubwa katika macho ya watu na kutakabali katika kuifuata haki. Mwenyezi Mungu anasema: "Hakika mwanadamu hupetuka mpaka kwa kujiona amejitosha " (96:67).

Kwa hivyo sio juu yako kumshughulikia huyo na kumwacha anayetaka kujitakasa na huku anamwogopa Mwenyezi Mungu. Ni kitu gani kinachokulazimu, ikiwa hakujitakasa na kufuru na uovu? Kwani hakika wewe ni mjumbe, ni juu yako kufikisha tu! Imesemwa kuwa maana ya aya "7" ni usijali kwa kukosa kujitakasa kwake na uchafu wa kufuru na uovu. Maana haya yanasibiana zaidi na mpangilio wa lawama.

Aya Ya 8-9

Kumcha Mwenyezi Mungu ni alama ya kuwaidhika. Mwenyezi Mungu anasema: "Hatukukuteremshia Qur'an ili upate mashaka. Bali ni mawaidha kwa wanaomcha (Mwenyezi Mungu) ." (20:2-3).

Amesema tena: "Atawaidhika nao mcha (Mungu) ". (19:10). Kutanguliza dhamiri "wewe" ni kuthibitisha lawama.

Aya Ya 11 - 12

Ni makatizo ya yale aliyolaumiwa kwayo ambayo ni kufinya uso kupa mgongo, kumshughulikia anayejiona amaejitosha na kujipurukusha na anayemcha Mwenyezi Mungu. Kusema kwake "Mwenye kutaka ataukumbuka" ni jumla yenye kuingia kati. Dhamiri ni ya Qur'an au yanayowaidhiwa na Qur'an. Ibara hii inaonyesha kuwa hakuna kulazimisha kuwaidhika, kwani hakuna manufaa yanayomrudia mwenye kutoa mawaidha isipokuwa anayenufaika ni yule mwenye kuwaidhiwa, kwa hiyo na chague anayoyachagua.

Aya Ya 13-14

Neno Suhuf lina maana ya chenye kuandikiwa; ni habari ya aya ya 11. Hiyo inadhoofisha kauli inayosema kuwa makusudio ya "Suhuf" ni ubao wenye kuhifadhiwa Lawhin Mahfuudh. Wala hakuna katika maneno ya Mwenyezi Mungu kukusudia ubao wenye kuhifadhiwa kwa tamko la wingi. Pia kuna udhaifu wa kauli ya kuwa makusudio ya Suhuf ni vitabu vya Mitume kwa sababu ya kutoafikiana na aya ya 15. Kusema kwake kutakaswa, ni kutakaswa na uchafu wa batili, maneno ya upuuzi, shaka na kupingana. Mwenyezi Mungu anasema: "Haiifikii batili mbele yake wala nyuma yake ." (41:42). Na amesema tena: "Hakika (hii Qur'an) ni kauli ya haki wala si upuuzi " (86:14).

Amesema tena:

"Hiki ni kitabu kisicho na shaka ndani yake ." (2:3).

Amesema: "Na kama ingelitoka kwa asiyekuwa Allah bila shaka wanagalikuta ndani hitilafu nyingi ". (4:82).

Aya Ya 15

Neno Safarah ni wingi wa Safiyr kwa maana ya mjumbe. Ni sifa baada ya sifa. Watukufu ni sifa ya hao wajumbe kwa kuzingatia dhati zao na watenda njema ni sifa kwa kuzingatia kazi yao. Maana ya aya hizi ni kwamba Qur'an ni waadhi uliyoandikwa katika vitabu vitukufu vilivyo toharishwa na kila aina ya uchafu, vilivyomo mikononi mwa Malaika, Watumishi ambao ni watukufu mbele za Mwenyezi Mungu kwa vile wao wenyewe ni tohara, na ni wema mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu ya matendo yao yaliyo mema matupu.

Inadhihiri katika aya kwamba wahyi unashughulikiwa na Malaika kwa kuchukua vitabu na kutoa wahyi. Wao ni wasaidizi wa Jibril wako chini ya amri yake. Kunasibisha wahyi kwa Malaika wengine, hakukanushi kunasibika nao Jibril katika mfano wa kauli yake. "Ameyateremsha Ruuh mwaminifu juu ya moyo wako " (26:193-194).

Na amemsifu Mwenyezi Mungu katika kauli yake: "Hakika hii (Qur'an) ni kauli ya mjumbe mtukufu mwenye nguvu, mwenye daraja mbele za mwenye ufalme. Mwenye kutiiwa huko mwaminifu "; (81:19-21).

Kwa hiyo yeye ni mwenye kutiiwa na Malaika, mwenye kutoa amri yake. Na kitendo chake na chao, vyote ni vya Malaika. Inasemekana kuwa makusudi ya "Safarah" ni waandishi katika Malaika lakini maana iliyotangulia ndiyo iliyowazi zaidi. Pia inasemekana kuwa makusudio ni wasomaji, wanayaandika kisha wanayasoma.

Utafiti Wa Hadithi Katika Majmau imesemwa aya ziliteremshwa kwa sababu ya Abdallah bin Ummi Maktuum, naye ni Abdallah bin Sharih bin Malik bin rabia Al-Fahri katika ukoo wa Amir bin Luayyi. Ni kwamba yeye alimjia Mtume(s.a.w.w) akiwa anawasemesha Utba bin Rabia, Abu Jahl bin Hisham, Abbas bin Abdul-Muttwalib, Ubayya na Ummayya Khalaf akiwalingania kwa Mwenyezi Mungu na hali anawatarajia wasilimu. Akasema Ibn Ummi Maktuum: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nifundishe aliyokufundisha Mwenyezi Mungu." Akawa anasema kwa nguvu na kulikariri hilo wala hajui kwamba yeye ni mwenye kushughulika na wengine. Mpaka kukadhihiri kuchukia katika uso wa Mtume(s.a.w.w) kwa kukatishwa maneno yake akawa Mtume anasema kimoyo: 'hawa wakuu watasema wafuasi wake ni vipofu na watumwa'. Kwa hivyo akampa mgongo na akawaelekea watu aliokuwa akiwazungumza nao; ndio zikashuka aya hizo.

Baada ya hapo Mtume akawa anamtukuza. Kila amwonapo husema: "Karibu ewe ambaye amenilaumu Mola wangu kwaye". Kisha humwambia, Je, unayo haja. Aliwahi kumfanya kaimu wake Madina mara mbili katika vita. Amepokea Suyut katika Durril Manthur kisa hicho kutoka kwa Aisha, Anas na Ibn Abbas kwa hitilafu ndogo.

Lakini aya haziko dhahiri kufahamisha kuwa makusudio ni Mtume(s.a.w.w) bali katika hadithi; hakufafanuliwa aliyehusika. Na tukichunguza vizuri katika aya hiyo tutafahamu anayekusudiwa si yeye; kwani kukunja uso si katika sifa ya Mtume(s.a.w.w) hata kwa adui aliyewaziwazi, sembuse kwa waumini wenye kutaka uongofu. Kisha kumsifu kwamba yeye anawashughulikia matajiri na kujipurukusha na makafiri hakufanani kabisa na tabia zake. Mwenyezi Mungu amezitukuza tabia zake aliposema katika Sura ya Al-Qalam (68) iliyoshuka kabla ya hii ambayo wapokezi wenye kubainisha utaratibu wa kushuka Sura wameafikiana kuwa imeshuka baada ya Sura ya Iqraa' (96). (Sura ya kwanza kushuka).

Aya inasema: "Hakika wewe unatabia njema " (68:4).

Itaingiaje akilini kuwa Mwenyezi Mungu amtukuze mwanzo wa Biitha yake kisha arudie kumlaumu juu ya tabia yake na amshutumu kwa mifano hiyo ya kuwashughulikia matajiri hata wakikufuru na kujipurukusha na makafiri hata wakiamini na kutaka kuongoka. Vile vile Mwenyezi Mungu amesema: "Na uwaonye jamaa zako waliokaribu. Na uinamishe bawa lako kwa yule anayekufuata katika wale waliomini ." (26:214-219).

Hapo ameamrishwa kuwachukulia upole waumini. Surah hiyo imeshuka Makka. Na mpangilio wa kusema kwake "Waonye jamaa zako walio karibu", ni wa kushuka mwanzo mwanzo wa mlinganio. Pia kauli yake Mwenyezi Mungu: "Usinyooshe (usidokowe) macho yako (kutazama) yale tuliyowastareheshea makundi mbali mbali ya hao (wabaya) wala usiwahuzunikie (huzuni kubwa ya kujiumiza nafsi yako) na inamisha bawa lako kwa waumini " (15:88).

Na katika kauli yake: "Basi yatangaze uliyoamrishwa na ujitenge mbali na hao washirikina " (15:94).

Sasa vipi itawezekana kwa Mtume kukunja uso na kuwapa mgongo waumini huku akiwa ameamrishwa kuheshimu imani zao na kuwainamishia bawa na kutoikodolea macho dunia. Hayo tuliyoyaelezea, pia ni jibu la yale yaliyosemwa kuwa Mwenyezi Mungu hakumkataza kitendo hicho ila wakati huo tu!, kwa hivyo hakikuwa haramu kwake kabla ya kukatazwa, bali ni haramu baada ya kukatazwa.

Katika Majmau imepokewa hadith kutoka kwa As Sadiq(a.s) kuwa aya hizo zilishuka kwa mtu mmoja katika Bani Umayya, alikuwa mbele za Mtume(s.a.w.w) akaja Ibn Ummi Maktuum, alipomwona akamkunjia pua kwa kumwona mchafu na akamkunjia uso na kumpa mgongo, ndio akalielezea Mwenyezi Mungu hilo. Katika hiyo hiyo Majmau imepokewa kutoka kwa Asswadiq(a.s) kwamba yeye amesema: Alikuwa Mtume(s.a.w.w) anapomwona Abdallah Ibn Ummi Maktuum husema. Marhaba! Marhaba! Waallahi hatanilaumu Mwenyezi Mungu kwa sababu yako milele. Na alikuwa akimfanyia upole mpaka akawa anajizuia na Mtume, yaani alikuwa anajizuia kuwa na Mtume kwa jinsi anavyomshughulikia sana.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA ABASA (ALIFINYA USO)

Aya Ya 17-42

قُتِلَ الْإِنسَانُ مَا أَكْفَرَهُ ﴿١٧﴾

17. Amelaniwa mwanadamu si ukafiri wake huo!

مِنْ أَيِّ شَيْءٍ خَلَقَهُ ﴿١٨﴾

18. ( Jee anajua) kwa kitu gani amemuumba ?

مِن نُّطْفَةٍ خَلَقَهُ فَقَدَّرَهُ ﴿١٩﴾

19. Kwa tone la manii amemuumba akamwezesha.

ثُمَّ السَّبِيلَ يَسَّرَهُ ﴿٢٠﴾

20. Kisha akamfanyia nyepesi njia.

ثُمَّ أَمَاتَهُ فَأَقْبَرَهُ ﴿٢١﴾

21. Kisha akamuua, akamfanyia kaburi.

ثُمَّ إِذَا شَاءَ أَنشَرَهُ ﴿٢٢﴾

22. Kisha anapotaka atamfufua.

كَلَّا لَمَّا يَقْضِ مَا أَمَرَهُ ﴿٢٣﴾

23. Hakika hajatekeleza aliloamrishwa

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ﴿٢٤﴾

24. Basi mtu naatazame chakula chake.

أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ﴿٢٥﴾

25. Sisi tumemebubujiza maji.

ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ﴿٢٦﴾

26. Kisha tukaipasua Ardhi.

فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ﴿٢٧﴾

27. Tukaotesha humo nafaka.

وَعِنَبًا وَقَضْبًا ﴿٢٨﴾

28. Na zabibu na mboga.

وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا ﴿٢٩﴾

29. Na zaituni na mitende.

وَحَدَائِقَ غُلْبًا ﴿٣٠﴾

30. Na mabustani yenye miti mingi.

وَفَاكِهَةً وَأَبًّا ﴿٣١﴾

31. Na matunda na malisho.

مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ ﴿٣٢﴾

32. Kwa manufaa yenu na wanyama wenu.

فَإِذَا جَاءَتِ الصَّاخَّةُ ﴿٣٣﴾

33. Basi itakapokuja sauti ya nguvu.

يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾

34. Siku ambayo mtu atamkimbia ndugu yake.

وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾

35. Na mama yake na baba yake.

وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾

36. Na mke wake na watoto wake

لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾

37. Kila mtu katika wao siku hiyo atakuwa na jambo limshughulishalo.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُّسْفِرَةٌ ﴿٣٨﴾

38. Nyuso siku hiyo zitanawiri.

ضَاحِكَةٌ مُّسْتَبْشِرَةٌ ﴿٣٩﴾

39. Zitacheka na kufurahika.

وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ ﴿٤٠﴾

40. Na nyuso nyingine siku hiyo zitakuwa na mavumbi.

تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ ﴿٤١﴾

41. ( Zitakuwa) zimefunikwa na weusi weusi.

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَفَرَةُ الْفَجَرَةُ ﴿٤٢﴾

42. Hao ndio makafiri, watendao maovu.

UBAINIFU

Aya Ya 17- 42

Ni kumwombea laana mtu na kumstaajabia kwa kuendelea kwake kuukanusha ubwana wa Mola wake. Kwani yeye mtu hawezi hata chembe kujiumba na kujiangalia. Bali Mwenyezi Mungu ndiye aliyeuumba katika tone la manii lililo duni. Akamkadiria akamzua kisha akamfanyia nyepesi njia kisha akamuua. Akamfanyia kaburi kisha atakapotaka atamtafufua. Basi yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye Mola wake aliyemuumba, mwenye kuangalia vizuri mambo yake katika hali zote. Na yeye mtu hatekelezi aliyoamrishwa na Mola wake, wala haongoki kwa ungozi wake. Lau angelitazama mtu chakula chake tu! ambacho ni onyesho moja katika maonyesho ya mazingatio yake na ukufi mmoja tu! Katika bahari ya rehema yake, angeliona wasaa wa mapitilizo na upole wa utengenezaji ambao utaishangaza akili yake. Ni neema zisizohisabika. "Kama mkitaka kuzihesabu neema zote za Mwenyezi Mungu hatamweza ." (14:34). Kwa hiyo kuficha mtu kumzingatia Mola wake na kuacha kushukuru neema zake ni jambo la ajabu. Hakika mwanadamu ni dhalimu mkubwa nwa mwenye kukufuru sana.

Aya hizi kama unavyoona hazikatai kuambatana na aya zilizotangulia katika mfumo mmoja ingawaje baadhi wanasema zimeshuka kwa sababu nyengine kama ukavyoona. (Inshallah).

Aya Ya 17

Ni kumwombea laana mtu kutokana na tabia yake ya kujiingiza kufuata matamanio na kuusahau ubwana wa Mola wake, na kuwa na kiburi katika kufuata amri zake. Makusudio ya ukafiri ni hali yoyote ya kuficha haki iliyowazi na unafungamana na kukanusha uungu na kuacha ibada. Yanatilia nguvu hayo yale yanayoonyesha mazingatio ya Mungu. Baadhi yao wamefasiri ukafiri kwa kuacha kushukuru na kuzikanusha neema. Ingawa hivyo ni sawa, lakini yanayonasibiana zaidi kwa kuangalia mpangilio, ni yale yaliyotangulia. Amesema katika Kash-shaf: "Amelaaniwa mtu" ni dua ya kumwombea laana na kauli na "namna gani alivyoendelea na ukafiri wake" ni kustajaabu kutokana na kupetuka mpaka katika kuzikufuru neema za Mwenyezi Mungu. Huwezi kuona mfumo mkali wa kulaani zaidi ya huo. Imesemekana kuwa jumla na "Namna gani alivyoendelea na ukafiri" ni swali na maana yake ni jambo gani lilimfanya kuwa kafiri? Lakini maana yaliyotangulia ndiyo yaliyokaribu zaidi.

Aya Ya 18

Maana yake ni kuwa ni kitu gani alichoumbiwa mtu hata ikawa anapetuka mpaka na kiburi katika imani na twaa? Swali hili ni la mkazo yale yaliyotangulia (ya kustaajabu). Mastaajabu yanakuwa katika matukio yasiyokuwa na sababu kwa hivyo. Kwanza: Inafahamisha kuwa ni katika maajabu kwa mtu kupetuka mpaka katika kufuru. Pili: Panaulizwa je, katika umbile lake aliloumbwa na Mwenyezi Mungu kuna linalowajibisha kukufuru? Jibu ni hakuna? Wala hapana hoja atakayoitoa wala udhuru kwani yeye ni kiumbe aliyeumbwa na maji duni. Hamiliki chochote katika umbile lake wala katika kuangalia mambo ya uhai wake, kifo chake na kufufuliwa kwake. Jibu la swali hili liko katika aya zinazofuatia.

Aya Ya 19

Kuleta neno Nutfa (tone la manii) kwa njia ya (Nakra) kutojulikana kwa kudharau yaani ametokana na tone la manii lililoduni, dhalili katika umbile lake, kwa hivyo hana haki ikiwa asili yake ni hii, kupetuka mpaka kwa kufuru yake na kuwa na kiburi na twaa. Kusema kwake Akamwezesha yaani akampa uwezo katika dhati yake, na sifa zake na vitendo vyake; kwa hivyo hafai kupetuka kiasi alichowezeshwa na kupetuka mipaka aliyowekewa. Yamemzunguka yeye maangalizi ya Mungu katika kila upande. Haifai kwake kujihukumia kupata yale asiyowezeshwa.

Aya Ya 20

Kwa dhihiri ya mpangilio ulivyo, makusudio yake ni kukanusha udhuru wa mtu wa kufuru yake na kiburi chake, kwamba makusudio ya njia ni njia ya twaa ya Mwenyezi Mungu na kufuata amri, ukipenda unaweza kusema njia ya kheri kwa hivyo aya itakuwa inaondoa mushkili, kwa sababu ikisemwa "kwa tone la manii alimuumba kisha akamuwezesha" inawezekana kumfahamikia msikilizaji kwamba ikiwa kuumba na kuwezesha kumemzunguka mtu kwa kila upande, itakuwa vitendo vya mtu kwa dhati yake na sifa zake ni vyenye kuwezeshwa na kufungamana na matakwa ya Mungu ambayo hayahalifu. Kwa hivyo mtu atakuwa ni mwenye kutenzwa nguvu, asiyekuwa na hiyari. Hivyo ukafiri siyo matakwa ya mtu wala ufasiki. Kwa sababu hayo yanakuwa kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) Kwa hiyo hakuna shutuma wala lawama kwa mtu.

Kwa sababu hiyo, Mwenyezi Mungu ameondoa mushkeli huo kwa kusema "Kisha akamfanyia nyepesi njia" inafahamisha kuwa kuumba na kukadiria hakukanushi hiyari ya mtu katika lile aliloamrishwa miongoni mwa imani na twaa. Anayo njia ya kuendea wema alioumbiwa. Hivyo ni kwamba kuwezesha ni kwenye kuwa juu ya vitendo vya mtu kwa njia ya hiyari yake na matakwa ya Mungu ni yenye kufungamana na vitendo vya mtu kwa matakwa yake na hiyari yake. Kitendo ni chenye kutokana na mtu kwa hiyari yake ambayo kwa kuwa ni hiyari basi ni yenye kufungamana na uweza. Kwa hivyo mtu ana hiyari katika kitendo chake lakini ni mwenye kuulizwa juu ya hivyo vitendo. Utafiti juu ya suala hili utaelezewa mara nyingi katika aya zinazofanana na hii.

Imesemekana makusudio ya kufanya nyepesi njia ni kutoka katika tumbo la mama yake kwa maana ya: Kisha akafanyiwa nyepesi mtu njia ya kutoka hali yakuwa ni mtoto mchanga aliyeumbwa kutokana na tone la manii. Imesemekana kuwa makusudio yake ni kuongoza kwenye dini na kubainisha njia ya heri na shari kama alivyosema: "Na tukambainishia njia mbili" (90:10) lakini yaliyotangulia ni bora.

Aya Ya 21

Makusudio ya "Akamfanyia kaburi" ni kumzika na kumficha ndani ya ardhi. Hii ni kuchukulia vile walivyozowea watu. Kwa mnasaba huo ndio akaunasibisha kwake Mwenyezi Mungu; kwa sababu Yeye ndiye aliyewaongoza kwenye hilo la kufanya kaburi na akawafahamisha. Imesemekana kuwa makusudio ya kumfanyia kaburi, ni amri yake Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kumtukuza ili kuuficha mzoga usiwaudhi watu. Nja iliyoelezwa kwanza ndiyo yenye kunasibu zaidi.

Aya Ya 22

Mpangilio ni kumfufua anapotaka yaani kuwa huo ufufuo utakuwa ni wa ghafla hajui isipokuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Aya Ya 23

Kutokana na mpangilio wa manno ulivyo neni " Kalla" ni la kukataa. Ni kama kuna swali; yaani baada ya kuonyeshwa kuwa binadamu ni kiumbe mwenye kuangaliwa vizuri na Mwenyezi Mungu, tangu kupatikana kwake mpaka mwisho wake; kuumbwa, kukadiriwa, kufanyiwa nyepesi njia, kuuliwa, kutiwa kaburini na kufufuliwa. Yote hayo ni neema kutoka kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa hivyo likaja swali amefanya nini mtu? Je, amemnyenyekea Mola wake? Au je, ameshukuru neema? Pakajibiwa" hapana sivyo hivyo; kisha pakafafanuliwa zaidi kwa kusemwa: "hajatekeleza alioamrishwa." Kwa hiyo imedhihiri kuwa dhamiri ya neno hajatekeleza inamrudia mtu. Vile vile imedhiri kuwa shutuma na lawama zilizomo katika aya hiyo ni za mtu kutokana na tabia yake na kupetuka mipaka katika kufuru na inadi. Imedhihiri kutokuwa sawa yale waliyoyasema baaadhi, kuwa aya inaenea kwa kafiri na muislam. Kwa sababu dhamiri ya mtu aliyetajwa ni kwa kutokana na tabia yake inayompelekea kukufuru basi inafungamana na mwenye vitendo hivyo.

Aya Ya 24

Ni mtiririko wa yaliyotangulia kwa ajili ya kufafanua. Ndani yake mna maelekezo ya kuangalia mtu chakula chake tu, ambacho anakila na kukitegemea ili aishi. Hilo ni jambo moja tu, kati ya yasiyohisabika liloandaliwa na maangalizi mazuri ya Mungu, ili aweze mtu kuchunguza na kushudia upana wa maangalizi mazuri ya Mungu ambayo yataweza kuishangaza akili yake. Makusudio ya mtu kama ilivyosemwa sio yule mtu aliyetajwa katika aya ya 17. Kwani makusudio ni kumhusu mtu mwenye kukufuru sana, kinyume cha mtu yule aliyetajwa katika aya ile aliyeamrishwa kuangalia vizuri, hii ni yenye kuenea kwa kila mtu. Ndio maana ikaletwa kwa dhahiri bila ya dhamira.

Aya Ya 25-32

Ni ubainifu wa ufafanuzi wa maangalizi mazuri ya Mwenyezi Mungu. Makusudio ya kububujiza maji nikuteremsha mvua ya Ardhi, wala sio mbali kuwa ni pamoja na mito na chemchemi kwa sababu hazina ya maji iliyo ndani ya ardhi inatokana na mvua. Kuipasua ardhi ni kwa mmea unaotoka. Neno Qadhba lina maana ya kukatakata; yaani mboga anyoikatakata mtu na kuila. Imesemekana kuwa makusudio ni chakula cha wanyama. Imesemekana kuwa yametajwa yale matunda mengine kwanza kwa majina yao kwa ajili ya kuyapa kipaumbele (umuhimu). Kuacha dhamiri ya asiyekuwepo na kuleta dhamira ya wenye kusemeshwa na kwa ajili ya kutilia mkazo neema alizowaneemesha.

Aya Ya 33

Makusudio ya sauti ya nguvu ni kupuziwa Suur. Yaani siku ya Kiyama. Hiyo ni kuishiria ule mwishilio wa yaliyotajwa katika mipangilio ya Mungu kwa ajili ya mtu, kwamba kuna jambo la Mungu kwa mja nalo ni siku ya Kiyama ambayo atalipwa mtu malipo ya matendo yake.

Aya Ya 34-37

Ni kuonyesha ugumu wa siku hiyo ya Kiyama. Wale ambao mtu aliwahesabu kuwa ni jamaa zake wa karibu na wanaomuhusu ambao alikuwa nao na kuwafanya ni nguzo na wasaidizi wa kuwategemea katika dunia, lakini leo anawakimbia kutokana na matatizo yaliyomzunguuka, kiasi ambacho hayamruhusu kumshughulikia mwengine vyovyoye atakavyokuwa. Balaa likiwa kubwa na likizidi, mtu kujivutia mwenyewe na kuwaacha wengine. Dalili ya maana hii ni aya inayosema: "Kila mmoja katika wao siku hiyo atakuwa na jambo la kumshughulisha". Zimesemwa sababu nyengine za mtu kuwakimbia jamaa zake wanaomuhusu, ambazo hazina dalili yoyote kwa hivyo tumezifumbia macho.

Aya Ya 38-39

Ni ubainifu wa kugawanyika watu siku hiyo mafungu mawili; watu wema na waovu, na kuonyesha kuwa watajulikana kwa alama zao za nyusoni mwao. Kunawirika uso ni kuangaza kunawirika uso kwa furaha na kushangilia kwake kushuhudia yale yenye kufurahisha.

Aya Ya 40

Vumbi ni alama ya hamu na ghamu.

Aya Ya 41

Yaani zitakuwa na giza na weusi. Imebainishwa hali ya makundi mawili katika aya nne kwa ubainifu wa nyuso, kwa vile uso ndio kioo cha moyo katika furaha yake na kuchukiwa kwake.

Aya Ya 42

Yaani wenye kukusanya ukafiri kiitikadi na kiuovu. Hayo ni maasi mabaya sana.

Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Ibn Al-Munathir kutoka kwa Akram kuhusu aya ya 17: amesema. "Imeshuka kwa Utbah bin Abilahab wakati aliposema: "Nimemkufuru Mola wa nyota zinapoanguka". Mtume akamwapiza, akauawa na simba katika njia ya Sham. Katika Ihtijaj imepokewa kutoka kwa Amirul Muminin(a.s) hadith ndefu kuhusu aya hiyo yaani amelaaniwa mtu. Katika Tafsiri al Qummi kuhusu aya ya 20 amesema amemfanyia nyepesi njia ya heri. Makusudio yake ni kumfanya ni mwenye kuchagua katika kitendo chake kinachomsahilishia kufuata kwake njia ya wema na kufika kwenye ukamilifu ambao amemuumbia. Haya yanafungamana na yale tuliyotangulia kuyaeleza katika tafsiri ya aya.

Katika Durril Manthur ametoa Abu Ubayd katika Fadhail kutoka kwa Ibrahim Attaymi amesema: aliulizwa Abu Bakr As-Swiddiq kuhusu neno "Abba" akasema: "Ni mbingu gani itakayonifunika na ni ardhi gani itakayoniua kama nikisema katika kitabu cha Mwenyezi Mungu jambo nisilolijua". Katika hiyohiyo Durril Manthur ametoa, Sadi Bin Mansuur, Ibn Jariyr, Ibn Saas, Abd bin Hamid, Ibn Al-Mundir, Ibn Murdawayh na Bayhaqi katika Shiilbul-Iman, na Khatib, na Al-Hakim. Ikasahihishwa kutoka kwa Anas kwamba Umar alisoma juu ya mimbar aya ya 28 - 31 akasema 'yote haya tumeyajua' basi ni nini "Abba"?' Kisha akainyanyua fimbo yake iliyokuwa mkononi mwake akasema; "Hii naapa kwa umri wa Mwenyezi Mungu ndio taklifa, lakini si lawama kwako kutojua nini "Abba" fuateni yale aliyowabainishia uongozi wake katika kitabu muyafanye na msiyoyajua yategemezeni kwa Mungu."

Katika Irshadul-Mufid imepokewa kwamba Abu Bakr aliulizwa kuhusu neno lake Mwenyezi Mungu (s.w.t) Abba hakujua maana yake akasema; Ni mbingu gani itakayonifunika au ni ardhi gani itakayoniua au nitafanya nini nikisema katika kitabu cha Mwenyezi Mungu sijui? Ama Fakiha tunajua, lakini Abba Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi."

Yakamfikia hayo Amirul Muuminin Ali(a.s) akasema: Subhannallah hajui kuwa "Abba" ni malisho na kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu "Na matunda na malisho" ni kuhesabu Mwenyezi Mungu neema zake juu ya viumbe vyake katika alivyowalisha na kuwaumbia kwa ajili yao na kwa ajili ya wanyama wao ambavyo vinawapa uzima na kuimarisha miili yao. Katika Majmau imepokewa kutoka kwa Ataa' bin Yasar naye kutoka kwa Sawdah mke wa Mtume(s.a.w.w) amesema: Amesema Mtume: "Watafufuliwa watu uchi, bila viatu, wenye mizunga, wakitokwa na majasho yanayofikia ndewe za masikio ". Anasema Sawdah, nikamuuliza: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu tutaangaliana uchi". Akasema: "Watu hawatakuwa na habari na hilo". Akasoma Mtume wa Mwenyezi Mungu: "Kila mtu katika wao siku hiyo atakuwa na jambo limshughulishalo".