TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39413
Pakua: 2921

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39413 / Pakua: 2921
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA TAKWIR (KUKUNJA) (NA. 81)

INA AYA 29.

Aya 1 - 14

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾

1. Jua litakapokunjwakunjwa.

وَإِذَا النُّجُومُ انكَدَرَتْ ﴿٢﴾

2. Na nyota zitakapoanguka.

وَإِذَا الْجِبَالُ سُيِّرَتْ ﴿٣﴾

3. Na majabali yatakapoendeshwa.

وَإِذَا الْعِشَارُ عُطِّلَتْ ﴿٤﴾

4. Na ngamia wenye mimba watakapotupiliwa mbali.

وَإِذَا الْوُحُوشُ حُشِرَتْ ﴿٥﴾

5. Na wanyama wa mwitu watakapokusanywa.

وَإِذَا الْبِحَارُ سُجِّرَتْ ﴿٦﴾

6. Na bahari zitapowashwa moto.

وَإِذَا النُّفُوسُ زُوِّجَتْ ﴿٧﴾

7. Na nafsi zitakapokutanishwa.

وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ ﴿٨﴾

8. Na kijana mwanamke aliyezikwa angali hai atakapoulizwa.

بِأَيِّ ذَنبٍ قُتِلَتْ ﴿٩﴾

9. Kwa makosa gani aliuawa?

وَإِذَا الصُّحُفُ نُشِرَتْ ﴿١٠﴾

10. Na madaftari yatakapofuniliwa.

وَإِذَا السَّمَاءُ كُشِطَتْ ﴿١١﴾

11. Na mbingu zitakapoondolewa mahali pake.

وَإِذَا الْجَحِيمُ سُعِّرَتْ ﴿١٢﴾

12. Na moto utapokokwa.

وَإِذَا الْجَنَّةُ أُزْلِفَتْ ﴿١٣﴾

13. Na pepo itakaposogezwa.

عَلِمَتْ نَفْسٌ مَّا أَحْضَرَتْ ﴿١٤﴾

14. Itajua nafsi ilichokihudhurisha.

UBAINIFU

Sura inataja siku ya Kiyama, kwa kutaja baadhi alama zake na matukio yake. Inaisifu siku hiyo kwamba yatafunuka ndani ya siku hiyo yale aliyoyafanya mwanadamu. Kisha inaisifu Qur'an kwamba aliyeileta kwa Mtume ni mjumbe wa mbingu ambaye ni Malaika wa wahyi na sio shetani, wala Mtume sio mwenda wazimu aliyepagawa na mashetani. Sura hii inakubaliana kwa mpangilio wake kuwa ni katika Sura za mwanzo. Hili linaungwa mkono na maelezo yaliyomo ndani yake yanayohusu kumtakasa Mtume(s.a.w.w) na visingizio vya kuwa ni mkichaa; ambavyo makafiri walimsingizia mwanzo wa utume wake. Vile vile Sura Al Qalam ambayo ni katika Sura za mwanzo nayo ina maelezo ya kumtakasa Mtume(s.a.w.w) . Sura imeshuka Makka bila ya ubishi.

Aya Ya 1

Maana ya neno Takwir ni kukunja kwa kuzungusha; kama kukunja kilemba juu ya kichwa. Huenda makusudio ya kukunjwa jua ni kuwa giza umbo lake kwa mzunguko.

Aya Ya 2

Neno Inkadarat lina maana ya kuanguka kutoka hewani mpaka kwenye ardhi. Huenda ikawa ni kwa maana ya kugeuka, ikawa makusudio ni kuondoka mwanga wake.

Aya Ya 3

Yaani yataendeshwa kutokana na mtingishiko wa Kiyama yawe kama vumbi lenye kupeperushwa.

Aya Ya 4

Imesemwa kuwa neno Ishar wingi wake ni ushara naye ni ngamia mwenye mimba ya miezi kumi, huitwa hivyo mpaka azae, huenda akaitwa hivyo hata baada ya kuzaa. Na ngamia ndiyo mali yenye thamani zaidi kwa waarabu. Kana kwamba ni ishara ya fumbo kwamba mali yenye thamani ambayo wanaishindania watu itabakia bila ya mtu wa kuimiliki na kuitumia, kwa sababu watu watakuwa wanajishughulisha na kuokoa nafsi zao tu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Kila mtu katika wao siku hiyo atakuwa na jambo la kumshughulisha ". (8:37).

Aya Ya 5

Dhahir ya aya kulingana na mpangilio wa aya za kukisifu Kiyama ni kwamba hata wanyama mwitu pia watakusanywa kama watu. Hayo yanatiliwa nguvu na kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake mbili ila ni umati kama nyinyi. Hatukupuuza kitabuni (mwetu) kitu chochote kisha watakusanywa kwa Mola wao ". (6:38).

Ama hali yao baada ya kukusanywa haikuelezwa katika maneno yake Mwenyezi Mungu wala yale yanayotegemewa katika hadith. Ndiyo kusema kwake Mwenyezi Mungu katika Sura (6:38). ni umati kama nyinyi na kusema kwake "Hatukupuuza kitabuni kitu chochote" huenda hayo yakafafanua hali yao kwa mwenye huzingatia na kuangalia kwa makini. Pengine husemwa, kukusanywa wanyama ni katika alama za Kiyama na si katika matukio ya Kiyama. Hivyo itakuwa maana ya kukusanywa wanyama; ni kule kutolewa kutoka mwituni na mapangoni mwao.

Aya Ya 6

Imefasiriwa Sujjirat kwa kuwako moto na imefasiriwa kwa kujaa.

Aya Ya 7

Nafsi njema zitakutanishwa na wanawake wa peponi Mwenyezi Mungu anasema: "Humo watakuwa na wake waliotakaswa ". (4:57).

Amesema tena: "Na tutawaoza Mahurilaini " (44:54).

Ama nafsi za waovu zitakutanishwa na mashetani, Mwenyezi Mungu anasema: "Wakusanyeni wale waliodhulumu (nafsi zao) pamoja na wenziwao na wale waliokuwa wakiwaabudu ." (37:22).

Na amesema: "Na mwenye kuyafanyia upofu maneno ya mwingi wa rehema tunamwekea shetani kuwa rafiki yake " (43:36).

Aya Ya 8

Waarabu walikuwa wakiwazika wazima watoto wa kike kwa kuogopa aibu; kama kunavyoonyesha kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Anapopewa habari mmoja wao ya (kuzaliwa) mtoto wa kike husawijika uso wake akajaa sikitiko". Anajificha na watu kwa sababu ya habari mbaya ile aliyoambiwa! (Anafanya shauri) Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? " (16:58 - 59).

Mwenye kuulizwa kwa hakika ni baba yake aliyemzika nzima ili asiaibishwe, lakini amehisabiwa kuwa mwenye kuulizwa ni kijana mwanamke kwa namna ya kuaibishwa na kufedheheshwa huyo muuaji na kumsahilishia huyo kijana wa kike kumuomba Mwenyezi Mungu amwadhibu muuaji wake. Maneno yako katika mfano wa kusema kwake Mwenyezi Mungu kuhusu Isa(a.s) :

"Na (kumbuka) Allah atakapo sema: "Ewe Isa bin Maryam! Je, wewe uliwaambia watu 'Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa waungu badala ya Allah ? " (4:116).

Imesemwa kuwa kutegemeza kuuliza kwa kijana wa kike ni kwa njia ya fumbo. Makusudio yake ni kuuliziwa, mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Kwa hakika ahadi itaulizwa ". (17:34)

Aya Ya 10

Yaani yatafunuliwa kwa ajili ya hisabu. Ama watu wa peponi watakutanishwa na wanawake wema. Ama watu wa motoni kila mtu atakuwa na shetani; yaani nafsi za makafiri na wanafiki zitakutanishwa na mashetani ndio marafiki zao". Katika Durril Manthur ametoa Ibn Abu Maryam, Addiylamiy kutoka kwa Abu Maryam kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema kuhusu kauli yake "Jua litakapokunjwa kunjwa ", amesema: "Litakunjwa katika Jahanam ".

Aya Ya 11

Maana ya neno Kushitwat ni kubanduliwa. Kisha Mwenyezi Mungu ataikunja; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na mbingu zitakunjwa kwa uweza wake" (39:67) Na siku itakapopasuka mbingu zilete chungu ya mawingu " (25:25).

Aya Ya 12

Yaani utakokwa mpaka uzidi kuwa mkali.

Aya Ya 13

Makusudio ya kusogezwa ni kwa ajili ya kuingia watu wake.

Aya Ya 14

Makusudio ya nafsi ni jinsi ya nafsi yoyote. Na makusudio ya ilichokihudhirisha ni amali yake iliyoifanya. Aya iko katika maana ya aya inayosema: "Siku ambayo kila nafsi itakuta mema iliyoyafanya yamehudhurishwa na pia ubaya ilioufanya ." (3:30).

Aya Ya 15-29

فَلَا أُقْسِمُ بِالْخُنَّسِ ﴿١٥﴾

15. Naapa kwa nyota zirudizo nyuma.

الْجَوَارِ الْكُنَّسِ ﴿١٦﴾

16. Ziendazo na kujificha.

وَاللَّيْلِ إِذَا عَسْعَسَ ﴿١٧﴾

17. Na kwa usiku unapotoka.

وَالصُّبْحِ إِذَا تَنَفَّسَ ﴿١٨﴾

18. Na asubuhi inapotoa mwanga.

إِنَّهُ لَقَوْلُ رَسُولٍ كَرِيمٍ ﴿١٩﴾

19. Hakika hiyo (Qur'an) ni kauli ya Mjumbe Mtukufu.

ذِي قُوَّةٍ عِندَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ ﴿٢٠﴾

20.Mwenye nguvu, Mwenye daraja mbele za Mwenye ufalme.

مُّطَاعٍ ثَمَّ أَمِينٍ ﴿٢١﴾

21 Mwenye kutiiwa huko, Mwaminifu.

وَمَا صَاحِبُكُم بِمَجْنُونٍ ﴿٢٢﴾

22. Wala mwenzenu si mwendawazimu.

وَلَقَدْ رَآهُ بِالْأُفُقِ الْمُبِينِ ﴿٢٣﴾

23. Na hakika alimwona pambizoni mwa mbingu mlimo wazi.

وَمَا هُوَ عَلَى الْغَيْبِ بِضَنِينٍ ﴿٢٤﴾

24. Wala yeye kwa jambo la ghaibu si mwenye kutuhumiwa,

وَمَا هُوَ بِقَوْلِ شَيْطَانٍ رَّجِيمٍ ﴿٢٥﴾

25. Wala (Qur'an) si kauli ya shetani aliyefukuzwa.

فَأَيْنَ تَذْهَبُونَ ﴿٢٦﴾

26. Basi mnakwenda wapi?

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ ﴿٢٧﴾

27. Hi (Qur'an) siyo ila ni waadhi kwa walimwengu.

لِمَن شَاءَ مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ ﴿٢٨﴾

28. Kwa anayetaka kunyooka katika nyingi.

وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٢٩﴾

29. Wala hamtataka ila kwa matakwa ya Allah Mola wa viumbe.

UBAINIFU

Niutakaso kwa Mtume(s.a.w.w) kwa wazimu na kwamba Qur'an inayomjia Mtume haina mwingiliano wowote na shetani. Na hiyo Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) tu anayoletewa Mtume na Malaika wa wahyi ambaye hafanyi hiyana katika ujumbe wake. Na kwamba hiyo Qur'an ni waadhi kwa walimwengu, yenye kuongoza kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kwa anayetaka kuongoka katika nyinyi.

Maana yake ninaapa hakika Mtume alimwona Jibril akiwa pambizoni mlimo wazi, ambayo ni sehemu ya juu kabisa kuliko sehemu zote zinazonasibiana na ulimwengu wa Malaika. Imesemwa kuwa maana yake ni hakika Mtume alimwona Jibril na sura yake ya asili wakati wa kuchimbuka jua akiwa yuko sehemu ya juu kabisa upande wa Mashariki. Hakuna dalili inayofahamisha hayo hasa kufungamana kuona kwa sura yake ya asili au kumwona kwa mfano wowote. Ni kama vile zimechukuliwa baadhi ya riwaya kwamba alimuona mwanzo wa Biitha na yeye yuko kati ya mbingu na ardhi amekaa juu ya kiti. Hayo yamechukuliwa kwa kufananisha.

Aya Ya 15 - 16

Aya mbili zinazofuatia hizi zinatilia nguvu kuwa makusudio ya nyota zirudizo nyuma, ziendazo na kujificha, ni nyota zote au baadhi yake. Lakini sifa za baadhi ya nyota zinanasibiana zaidi na sifa zilizoapiwa ambazo ni kurudi nyuma na kwenda kwa kujificha. Nazo ni sayari tano Zohal (Saturn), Mushtara (Jupitar), Mirikh (Mars), Zuhura (Venus) na Zebaki (Mercury). Kwani hizo zina sifa ya kwenda na kurudi na kujificha katika maficho yake kama wanyama wa porini. Imesemwa kuwa makusudio yake ni nyota yoyote. Ama kurudi nyuma ni kule kujificha mchana chini ya mwanga wa jua. Kwenda kwake ni kwenda kunakoonekana usiku na kujificha kwake ni kutua upande wa magharibi yake. Imesemwa kuwa makusudio yake ni Nyati na Paa. Sio mbali kuwa kutaja nyati au paa ni kwa upande wa mithali tu. Na kwamba makusudio ni mnyama wowote wa mwituni. Kwa vyovyote ilivyo, kauli ya kwanza iko karibu zaidi, ya pili iko mbali na ya tatu iko mbali zaidi.

Aya Ya 17

Inaungana na aya mbili zilizotangulia. Neno As'as huja kwa maana ya kuingia usiku na kutoka usiku. Raghib anasema; Ni mwanzo wa usiku na mwisho. Kwa hiyo As'as ni giza jembamba. Yanayosibiana zaidi na jumla na aya inayofuatia ni kuwa makusudio yake ni kutoka kwa usiku. Imesemwa makusudio yake ni kuingia, lalini kauli hii iko mbali.

Aya Ya 18

Inaungana na aya iliyotangulia limetumiwa neno kupumua kwa maana ya kutoa mwanga, kwa sababu asubuhi unakunjuka mwanga wake kwenye anga na giza lililoufunukia linaondoka. Ametaja Zamakhshari njia nyengine katika Kash-Shaf: ukisema nini maana ya kupumua asubuhi? Nitasema: "Ikija asubuhi huja upepo wa asubuhi kwa hiyo umejaaliwa juo upepo ndio pumzi zake". Kauli ya kwanza ndiyo iliyokaribu zaidi.

Aya Ya 19 -21

Ni jawabu la kiapo dhamiri ni ya Qur'an au ni ya yaliyotangulia katika Sura hii kwa maana ya kuwa ni Qur'an. Makusudio ya mjumbe hapa ni Jibril, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Sema: Anayemfanyia ushinde Jibril hakika yeye ameiteremsha Qur'an moyoni mwako kwa idhini ya Allah (2:97). Kulitegemeza neno kwake kama mjumbe ni dalili kwamba neno ni la Mwenyezi Mungu. Amemsifu Mwenyezi Mungu Jibril kwa sifa sita: Mjumbe: Inafahamisha ujumbe wake na kuleta kwake wahyi wa Qur'an kwa Mtume(s.a.w.w) . Mtukufu: Yaani mwenye utukufu na cheo. Mwenye Nguvu: Yaani mwenye uwezo wa kutekeleza.

Mwenye Daraja mbele ya Mwenyezi Mungu : Yaani mwenye nafasi ya ukaribu mbele za Mwenyezi Mungu. Mwenye kutiiwa huko: Yaani mbele ya

Aya Ya 22

Inaungana na aya ya 19, kupinga kumsingizia kwao wazimu. Kuleta ibara ya "mwenzenu" ni kukadhibisha masingizio yao. Kwa kuonyesha kuwa huyo ni mwenzenu amekaa nanyi akatangamana nanyi kwa muda mrefu, nanyi mnajua zaidi mlivyomkuta na ukamilifu wa akili, rai ya sawa na ukweli wa maneno. Mwenye sifa hizi haambiwi kuwa ni mwenda wazimu. Kumsifu Jibril kwa sifa zilizopita bila ya kumsifu Mtume(s.a.w.w) sio dalili ya ubora wa Jibril kuliko Mtume. Kwa sababu maneno yanakusudia kubainisha kuwa Qur'an ni maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyoteremshwa kwa Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wahyi sio kwa njia ya fikra za kiwenda wazimu kutoka kwa shetani. Yaani makusudio yake ni kubainisha kusalimika njia ya kushuka na kumtukuza yule anayeiteremsha kwa kutaja sifa zake tukufu na kuzidi kumtakasa na makosa na hiyana. Ama yule mwenye kuteremshiwa hakuna haja ya kutaja sifa nyingi zaidi ya zile wanazomtilia shaka.

Ni miongoni mwa maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumsifu Mtume(s.a.w.w) hata kwa yale asiyotiliwa shaka katika ubora wake kuliko Malaika wote. Na Mwenyezi Mungu aliwafanya Malaika wote wamsujudie Mtume ambaye ndile Khalifa wake katika ardhi.

Mwenyezi Mungu kuna Malaika anawaamrisha na wanamtii, hapa inaonyesha kuwa ana msaada wa Malaika anaowaamrisha. Muaminifu: Yaani hafanyi hiyana kwa yale anayoamrishwa. Imesemwa Rasul ni kwa maana ya Mtume(s.a.w.w) , lakini kama unavyoona hayo hayaafikiani na aya inayofuatia.

Aya Ya 23

Dhamira ya mwenye kuona inamrudia "mwenzenu" yaani Mtume na mwenye kuonwa ni Jibril. Kwa dhahir pambizoni mlimo wazi ni kama vile ilivyoonyesha aya inayosema: "Na yeye yuko pambizoni juu kabisa " (53:7).

Aya Ya 24

Dhamiri inamrudia Mtume. Jambo la ghaibu ni Wahyi kutofanya ubakhili yaani haufichi huo wahyi wala haubadilishi baadhi yake au wote. Anawafundisha watu kama alivyofundishwa na Mwenyezi Mungu na anawafikishia yale aliyoamrishwa kuyafikisha.

Aya Ya 25

Ni kanusha la kuitegemeza Qur'an na shetani. Shetani ni kwa maana ya yule aliye mwovu aliyefukuzwa, kama vile anavyoitwa na Mwenyezi Mungu Iblis na kizazi chake. Vile vile anaitwa hivyo majini wengine waovu. Mwenyezi Mungu anasema: "Allah akasema: "Basi toka humo kwani umebaidishwa na rehema ." (38:77).

Anasema tena: "Na tumezilinda na kila shetani aliyefukuzwa ." (15:17). Maana yake nikuwa Qur'an siyo ushawishi wa shetani na askari wake wala sio kupagawa na majini waovu kama wanavyopagawa wenda wazimu.

Aya Ya 26

Ameweka wazi Mwenyezi Mungu katika aya ya saba zilizotangulia uhaki wa Qur'an hali ya kuikinga na mashaka wanavyomsingizia aliyekuja nayo kuwa ni mwenda wazimu.

Pili : Kwamba imeteremshwa na malaika wa mbinguni, mwenye cheo kikubwa ambaye ni mwaminifu wa wahyi naye ni Jibril asiyekuwa na kizuwizi chochote kati yake na Mwenyezi Mungu wala kati yake na Mtume.Tatu : kwamba aliyeteremshiwa ni mwenzenu ambaye hali yake haikujificha kwenu, sio mwenda wazimu kama wanavyomzulia. Hakika alimwona malaika mwenye kuchukua huyo wahyi na akauchukua kwake wala si mwenye kuficha aliyopewa wahyi wala kugeuza.

Nne : Kwamba sio ushawishi na kiibilisi na askari zake wala sio kupatwa na shari za majini. Natija ya ubainifu huu ni kwamba Qur'an ni kitabu cha uongofu, anaweza kuongoka nacho mwenye kutaka kwa kuongoka kwenye haki. Ndio kusema kwake Mwenyezi Mungu "Hii (Qur'an) siyo ila waadhi kwa walimwengu." Kusema kwake "Basi mnakwenda wapi?" ni kianzio cha kutaja natija ya ubainifu huo, swali katika aya hii ni la kutahayariza; maana yake ikiwa ni hivi basi mnakwenda wapi, mnaiacha haki yenu nyuma yenu?

Aya Ya 27

Yaani ni waadhi kwa watu, katika wale wanaoweza kuiona haki.

Aya Ya 28

Ni ubainifu kuwa sharti ya kunufaika na waadhi huo ni kutaka kunyooka juu ya haki nako ni kuwa na uthabiti wa utii.

Aya Ya 29

Yameelezwa zaidi maana yake katika aya zilizotangulia zenye kufanana na hii. Aya hii kwa unavyofahamisha mpangilio wa Sura hii ni kuwa iko katika maana ya kukinga uwezekano wa tuhuma kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu "kwa anayetaka katika nyingi kunyooka" kwamba wana uhuru wa kutaka kunyooka. Wakitaka watanyooka, wasipotaka hawatanyooka; kwa hiyo Mwenyezi Mungu, kwa kutaka hao wanyooke, ana haja fulani kwao. Ndipo fikira hiyo ikaondolewa na aya hii, kwamba huko kutaka kwao kunyooka hakuwezekani ila tu anapopitisha Mwenyezi Mungu hilo. Hivyo ni kusema vitendo vya mwanadamu vile anavyoitaka, Mwenyezi Mungu pia amevitaka (vitokeo) kupitia kwa matakwa ya binadamu. Yaani ni Mwenyezi Mungu kumtakia mwanadamu afanye kadha wa kadha kwa mapenzi yake (mwanadamu) mwenyewe.

Utafiti Wa Hadith Katika Durril Manthur ametoa Said bin Mansur, Al-Fariyabi, Abdu bin Hamid, Ibn Jariyr, Ibn Hatim na Hakim na amesahihisha kutoka katika njia ya Ali, kuhusu kauli yake "Naapa kwa nyota zirudizo nyuma" amesema ni nyota zinazorudi usiku na kujificha mchana zikiwa hazionekani. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya hiyo hiyo anasema: maana yake ni: Ni naapa kwa Al-Khunnas (jina la nyota) ziendazo kwa kujificha amesema: zinajificha mchana hazibainiki. Katika Majmau kuhusu "zirudizo nyuma"-amesema zinarudi nyuma mchana na zinadhihiri usiku. "Ziendazo" ni sifa yake kwa sababu zinatembea katika Falaki (njia yake). "Ziendazo kwa kujificha" ni katika sifa yake vile vile kwa sababu zinajificha katika ngome zake kama anavyojificha paa kwenye nyumba yake; nazo ni nyota tano Zohal, Mushtara, Mirikh, Zuhura na Zebaki. Hadith hiyo imepokewa kutoka kwa Ali. Kuhusu aya ya 17 inapoingia yaani linapoondoka giza lake. Kutoka kwa Ali.

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu aya ya 17 amesema ni kuingia giza na kuhusu aya ya 18 ni kuondoka giza. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Asakir ktuoka kwa Muawiya bin Qurrat amesema: Anasema Mtume(s.a.w.w) kumwambia Jibril ni uzuri ulioje wa alivyokusifu Mola wako. Mwenye nguvu, mwenye daraja, mbele za mwenye ufalme. Mwenye kutiiwa huko, na muaminifu. Ni zipi hizo nguvu zako? Na ni upi huo uaminifu wako? Akasema Jibril: "Ama nguvu zangu ni wakati nilipopelekwa katika miji ya lut nayo ni minne. Katika kila mji kuna wapiganaji laki nne nikawanyanyua kutoka katika ardhi ya chini mpaka wakasikia watu wa mbingu sauti za kuku na kelele za mbwa, kisha nikawaporomosha, wakafa. Ama umanifu wangu sikuamrisha kitu chochote nikakipeleka kwa mwengine.

Riwaya hii haiwezi kupita hivihivi. Ameidhoofisha Ibn Askari. Katika Khiswal kutoka kwa Abu Abdillahi amesema: mwenye kusema katika kila siku ya Shabaan " Astaghfirullaha lladhiy laa ilaha huwa rrahmanurrahim. Al-hayyul qayyuum wa atubu ilayh" mara sabaini huandikwa katika pambizoni mwa mbingu mlimwowazi. Akasema nikauliza nini pambizoni mwa mbingu? Akasema ni sehemu katika Arsh yenye mito yenye kupita. Katika Tafsiri ya Qummi katika hadith aliyoitegemeza kwa Abu Abdillah kuhusu aya ya 25 amesema shetani mwenye kufukuzwa ni makuhani wa Maquraish yananasibishwa maneno yao na maneno ya mashetani.