TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN0%

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi: Muhammad Hussein Tabaatabaai
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 39410
Pakua: 2919

Maelezo zaidi:

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 29 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39410 / Pakua: 2919
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

Mwandishi:
Swahili

11

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA TARIQ (CHENYE KUJA USIKU) (NA. 86)

INA AYA 17

Kwa Jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.

وَالسَّمَاءِ وَالطَّارِقِ ﴿١﴾

1. Naapa kwa mbingu na chenye kuja usiku.

وَمَا أَدْرَاكَ مَا الطَّارِقُ ﴿٢﴾

2. Na lipi la kukujulisha ni nini chenye kuja siku.

النَّجْمُ الثَّاقِبُ ﴿٣﴾

3. Ni nyota inayong'ara usiku.

إِن كُلُّ نَفْسٍ لَّمَّا عَلَيْهَا حَافِظٌ ﴿٤﴾

4. Hakuna nafsi isipokuwa kuna mwenye kuitunza.

فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ مِمَّ خُلِقَ ﴿٥﴾

5. Basi mtu na ajitazame ameumbwa kwa kitu gani..

خُلِقَ مِن مَّاءٍ دَافِقٍ ﴿٦﴾

6. Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa nguvu.

يَخْرُجُ مِن بَيْنِ الصُّلْبِ وَالتَّرَائِبِ ﴿٧﴾

7. Yanayotoka baina ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua.

إِنَّهُ عَلَىٰ رَجْعِهِ لَقَادِرٌ ﴿٨﴾

8. Hakika yeye ni mweza wa kumrejeza.

يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾

9. Siku zaitakapofunuliwa siri.

فَمَا لَهُ مِن قُوَّةٍ وَلَا نَاصِرٍ ﴿١٠﴾

10. Basi hatakuwa na nguvu wala wa kumnusuru.

وَالسَّمَاءِ ذَاتِ الرَّجْعِ ﴿١١﴾

11. Naapa kwa mbingu yenye kurudi.

وَالْأَرْضِ ذَاتِ الصَّدْعِ ﴿١٢﴾

12. Na ardhi yenye mipasuko.

إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ ﴿١٣﴾

13. Hakika hii (Qur'an) ni kauli yenye kupambanua.

وَمَا هُوَ بِالْهَزْلِ ﴿١٤﴾

14. Wala si upuuzi.

إِنَّهُمْ يَكِيدُونَ كَيْدًا ﴿١٥﴾

15. Hakika wao wanakuchimbia vitimbi.

وَأَكِيدُ كَيْدًا ﴿١٦﴾

16. Nami (pia) ninawachimbia vitimbi.

فَمَهِّلِ الْكَافِرِينَ أَمْهِلْهُمْ رُوَيْدًا ﴿١٧﴾

17. Basi wape muhula makafiri wape muhula kidogo.

UBAINIFU

Katika Sura hii kuna maonyo kwa marejeo ya akhera na kufufuliwa. Na hayo yanafamisha uwezo wake Mwenyezi Mungu. Na inamalizia Sura kwa kueleza kiaga cha makafiri. Sura hii imeshuka Makka bila ya ubishi.

Aya 1-3

Neno Twariq asili yake- kama ilivyosemwa- ni kugonga kiasi cha kutoa sauti, miongoni mwao, ni nyundo na lina maana njia. Njia imeitwa hivyo kwa vile mpita njia anaigonga kwa nyayo zake. Kywa hivyo likaenea neno hilo kutumiwa kwa njia, kisha likahusishwa na kuja usiku, kwa sababu mwenye kuja usiku aghlabu hukuta milango imefungwa, kwa hiyo hugonga, kisha likaenea hilo neno kwa kila chenye kuhidhiri usiku. Makusudio ya neno hilo katika aya ni nyota yenye kutokeza usiku. Neno Thaqb asili yake ni kupasua; kisha likawa ni nuru yenye kuangaza, kwa sababu inapasua giza, na linakuja kwa maana ya kuwa juu kama kusema: imepaa juu ndege, nikama vile inapasua anga kwa kuruka kwake. Kwa hivyo makusudio ya Aya Na kwanza ni kuapa kwa mbingu na nyota inayotokeza usiku. Na Aya Na pili ni kwa ajili ya kulikuza jambo la chenye kuapiwa ambacho ni hicho chenye kutokeza usiku. Aya Na tatu ni ubainifu wa hicho chenye kutokeza usiku. Jumla hiyo ni jawabu ya swali.

Aya Na 4

Ni jawabu la kiapo. Herufi Lamma ni kwa maana ya illa (isipokuwa). Makusidio ya kutunza hapa ni kuandika matendo yake mema na maovu, ili yaweze kuhisabiwa siku ya Kiyama na kulipwa. Kwa hivyo mtunzaji ni malaika na chenye kutunzwa ni matendo, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na hakika mna wenye kuwatunza watukufu wenye kuandika ." (82:10-11).

Sio mbali kuwa makusudio ni kutunza nafsi dhati yake na vitendo vyake, kwa hiyo inafahamisha kuwa nafsi ni zenye kutunzwa hazimaliziki kwa mauti wala haziharibiki mpaka Mwenyezi Mungu atakapovifufua viwiliviwili, atavirudisha nafsi na atakuwa mtu kama alivyokuwa mtu wa duniani kwa dhati yake; kisha alipwe kwa mujibu wa vitendo vyake vyenye kuchungwa, vikiwa ni kheri au shari. Hilo linatiliwa nguvu na aya nyingi zinazofahamisha juu ya kutunzwa vitu, kama vile kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Sema atawaua Malaika wa mauti aliye wakilishwa kwenu kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu. " (32:11).

"Allah huzichukua roha wakati wa mauti yake na zile zisizokufa katika usingizi wao. Basi huzizuwiya zile alizozihukumia mauti. ." (39:42).

Hayo hayakanushi dhahiri ya Aya Na Sura ya (82:10).

kuwa kutunza kwa Malaika ni kuandika, kwa sababu kuitunza nafsi pia kutokana na kuandika kama anavyofahamisha Mwenyezi Mungu kwa kusema: "Hakika sisi tulikuwa tukiandika yale aliyokuwa mkiyatenda ." (45:29).

Kwa njia hii kunabatilika kutia makosa juu ya yale yanayofahamisha juu ya marejeo ya Kiyama katika kuenea Kudura, kwamba kumrusisha mtu kwa dhati yake ni muhali kwa sababu mtu ataumbwa tena mara ya pili mfano wa yule mtu wa duniani aliyeumbwa kwanza, lakini si yule yule na mfano wa kitu sio kitu chenyewe. Njia ya kubatilisha hoja hiyo ni kwamba: utu wa mtu unatokana na mtu kwa nafsi yake sio kwa kiwilikiwili chake na nafsi ni yenye kihifadhiwa kwa hivyo akiumba kiwilikiwili na kukifungamanisha na nafsi atakuwa ndiya yule yule mtu wa duniani kwa utu wake, ijapokuwa sio dhati yake.

Aya Na 5

Yaani aangalie nini mwanzo wa umbile lake? Na ni kitu gani ambacho Mwenyezi Mungu amekifanya kuwa mtu? Jumla hii ni mtiririko wa aya iliyotangulia. Maana yanavyofahamisha kutokana na mpangilio wake, ni kwamba, ikiwa kila nafsi ni yenye kuhifadhiwa kwa dhati yake na vitendo vyake, bila ya kwisha hiyo nafsi na kusahauliwa vitendo vyake basi akubali mtu ukweli kwamba yeye atarudi kwa Mola wake na kulipwa aliyoyatenda, wala hilo asilihisabu kuwa ni mbali. Naangalie ukweli huu kwenye asili ya umbile lake na akumbuke kwamba yeye ameumbwa kwa maji yanayoka kwa nguvu yanayotoka baina ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua. Basi yule aliyeanza kumuumba kutokana na maji haya anaweza kumrudisha na kumuhuisha baada ya mauti.

Aya Na 6

Maji yenye kutoka kwa kuruka ni manii. Jumla hiyo iko katika jawabu la swali.

Aya Na 7

Neno Sulb lina maana ya mgongo na Taraib ni mifupa wa kifua. Wamehitalifiana kiajabu kwenye matamko yao katika aya hii na iliyo kabla yake. Kwa dhahiri makusudio yake ni sehemu iliyokatikati ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua.

Aya Na 8

Yaani ambaye amemuumba mtu kutokana na maji, sifa yake ni hiyo hiyo, ni mwenye kuweza kumrudisha na kumuhuisha baada ya mauti.

Aya Na 9: Ni siku yatakayofichuka yale alioyoyaficha mtu na kuyafanya siri katika itikadi na matendo ya kheri au ya shari. Aya hii iko katika maana ya aya inayosema "Na mkidhihirisha yaliyomo katika nyoyo zenu au mkiyafichua, Allah atawataka hisabu ya (yote) hayo ." (2:284)

Aya Na 10

Hana uwezo katika nafsi yake utakaomzuia na adhabu ya Mwenyezi Mungu wala hana wa kumnusuru atakayemkinga na adhabu yaani hakutakuwa na uwezo wowote utakaomkinga na shari kutoka kwake au kwa mtu mwengine.

Aya Na 11

Kiapo baadha ya kiapo, ni kwa ajili ya kutilia mkazo jambo la Kiyama na kurejea kwa Mungu. Makusudio ya kurudi ni kuhisi kwenda kwake kwa kuchimbuka nyota na kutua. Imesemwa kuwa makusudio yake ni mvua. Makusudio ya kupasuka ni kupasuka kwa ajili ya mimea.

Aya Na 12-13

Maana ya neno Fasl ni kupambanua kati ya vitu viwili. Aya hizi mbili ni jawabu la kiapo kwa maana; ninaapa kwa hivyo nilivyoviapia hakika Qur'an ni neno lenye kupambanua kati ya haki na batili na sio maneno yasiyokuwa na maana. Yale inayoyahakikisha ni haki isiyokuwa na shaka na yale inayoya batilisha ni batili isiyokuwa na shaka. Kwa hiyo yale iliyoyatolea habari katika ufufuo na marejeo ni haki isiyokuwa na shaka ndani yake. Imesemekana kuwa dhamiri katika neno Innahu ni ya hayo yaliyotangulia kuelezwa katika habari ya marejeo lakini tuliyoyaeleza mwanzo ndiyo yanayoelekea zaidi.

Aya Na 15

Yaani makafiri wanaichimba vitimbi wakikusudia kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu na kubatilisha mlingano wako.

Aya Na 16

Ikiwa wao wanavyo vitimbi na mimi ninavyo vitimbi. Na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kushinda juu ya jambo lake, kwa hivyo wangojee tu; wala usifanye haraka, ngoja kidogo tu! Yatawajia yale waliyoahidiwa, na kila linalokuja liko karibu.

Utafiti Wa Hadithi Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu "Hakika kila nafsi ina mwenye kuichunga" amesema ni Malaika. Na kuhusu "Ameumbwa kwa maji yanayotoka kwa nguvu" amesema ni manii ambayo hutoka kwa nguvu". Kuhusu "yanayotoka kati ya uti wa mgongo na mifupa ya kifua" amesema uti wa mgongo ni mwanaume na mifupa ya kifua ni mwanamke. Katika Majmau imepokewa hadith marfuu kutoka kwa Abu Dardai amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) :Amedhamini Mwenyezi Mungu kuumba kwake vitu vine: Swala, Zaka, Kufunga Ramdhan na kuoga janaba na hizo ndizo siri alizozisema Mwenyezi Mungu "Siku itakayofunuliwa siri ."

Huenda ikawa maana ya hadithi hiyo ni kutaja baadhi ya mambo ya ukweli, kama inavyotilia nguvu hilo hadithi inayofuata. Katika hiyo hiyo Majmau kutoka kwa Muadh bin Jabal amesema: "Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu: ni siri zipi ambazo Mwenyezi Mungu atawafunuliwa waja katika akhera? Akasema siri zenu ni matendo yeno ya swala, kufunga, zaka, udhu, kuoga janaba na kila lenye kufaradhiwa, kwa sababu matendo yote ni siri yenye kufichamana, mtu akitaka anaweza kusema ameswali na asiwe ameswali au aseme ametawadha kumbe hakutawadha. Basi ndiyo kusema kwake Mwenyezi Mungu "siku itakayofunuliwa siri."

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu: "Basi hatakuwa na nguvu wala wa kumnusuru." Amesema: hatakuwa na nguvu yoyote kwa muumba wake wala wa kumnusuru kama Mwenyezi Mungu akimtakia uovu. Katika hiyo Tafsiri ya Qummi amesema kuhusu neno Raj'n amesema ni mvua na ardhi yenye mipasuko ni ardhi yenye mimea. Katika Majmau kuhusu : "hakika hii Qur'an ni kauli ya haki" amesema "Hakika Qur'an inapambanua kati ya haki na batili kwa kuibainisha kila moja. Hayo yamepokewa kutoka kwa Imam Assadiq(a.s) .

Katika Durril Manthur ametoa Ibn Abi Shayba, Addarami, Tirmdhi, Muhammad bin nasr na Ibn el- Ambari katika Masahif kutoka kwa Harith el-Aa'war amesema: Niliingia msikitini mara watu wakaingia katika mazungumzo. Nikamwendea Ali nikampa habari; akasema: "Je wamekwishafanya? Mimemsikia Mtume(s.a.w.w) akisema: "Kutatokea fitna. Nikasema: Ni kitu gani cha kutokea katika fitna hiyo Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Je ni sawa hapa? Akasema:kitabu cha Mwenyezi Mungu kina habari za kabla yenu baada yenu na kimekwisha wahukumia, ni upambanuzi na sio upuuzi, mwenye kukiacha Mwenyezi Mungu kumuangamiza, mwenye kukusudia pengine Mwenyezi Mungu humpoteza .

Ni kamba madhubuti, mauidha yenye hekima na njia yenye kunyooka. Ni ambachi hakipotezi wala hawashibi nacho wanavyuoni, hazitatiziki nacho ndimi wala haiishi ajabu yake. Ndicha ambacho majini waliposikia walisema: " Hakika tumesikia Qur'an ya ajabu inaongoza kwenye uongofu." Mwenye kusema kwacho huwa mkweli, mwenye kuhukumu kwacho amefanya uadilifu na mwenye kuganya amali kwacho amepata thawabu, na mwenye kulingania kwenye kitabu hicho ameongoka katika njia iliyonyooka. Amepokea karibu na maana hayo Muadh bin Jabal kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) .

12

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA A'ALAA (MTUKUFU) (NA. 87)

INA AYA 19

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.

سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى ﴿١﴾

1. Litakase jina la Mola wako aliye Mtukufu.

الَّذِي خَلَقَ فَسَوَّىٰ ﴿٢﴾

2. Ambaye ameumba (kila kitu) akakiweka sawa.

وَالَّذِي قَدَّرَ فَهَدَىٰ ﴿٣﴾

3. Na ambaye amekadiria (kila kitu) na akakiongoza.

وَالَّذِي أَخْرَجَ الْمَرْعَىٰ ﴿٤﴾

4. Na ambaye ameotesha malisho.

فَجَعَلَهُ غُثَاءً أَحْوَىٰ ﴿٥﴾

5. Kisha akayafanya makavu yenye kupiga weusi.

سَنُقْرِئُكَ فَلَا تَنسَىٰ ﴿٦﴾

6. Tutakusomesha wala hutasahau.

إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ إِنَّهُ يَعْلَمُ الْجَهْرَ وَمَا يَخْفَىٰ ﴿٧﴾

7. Ila anachopenda Allah. Hakika yeye anayajua yaliyowazi na yaliyofichika.

وَنُيَسِّرُكَ لِلْيُسْرَىٰ ﴿٨﴾

8. Tutakusahilishia njia nyepesi.

فَذَكِّرْ إِن نَّفَعَتِ الذِّكْرَىٰ ﴿٩﴾

9. Basi waidhisha ikiwa utafaa waadhi.

سَيَذَّكَّرُ مَن يَخْشَىٰ ﴿١٠﴾

10. Atawaidhika nao mcha (Mungu).

وَيَتَجَنَّبُهَا الْأَشْقَى ﴿١١﴾

11. Na atajiepusha nao asiyemcha.

الَّذِي يَصْلَى النَّارَ الْكُبْرَىٰ ﴿١٢﴾

12. Ambaye atauingia moto mkubwa..

ثُمَّ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿١٣﴾

13. Kisha humo hatakufa wala hatokuwa hai.

قَدْ أَفْلَحَ مَن تَزَكَّىٰ ﴿١٤﴾

14. Hakika amekwishafaulu mwenye kujitakasa.

وَذَكَرَ اسْمَ رَبِّهِ فَصَلَّىٰ ﴿١٥﴾

15. Akakumbuka jina la Mola wake na akaswali.

بَلْ تُؤْثِرُونَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿١٦﴾

16. Lakini nyinyi mnapenda zaidi maisha ya ulimwengu.

وَالْآخِرَةُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٧﴾

17. Hali akhera ni bora na yenye kubaki.

إِنَّ هَـٰذَا لَفِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ ﴿١٨﴾

18. Hakika hAya Na mo katika vitabu vya kwanza.

صُحُفِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ ﴿١٩﴾

19. Vitabu vya Ibrahim na Musa.

UBAINIFU

Ni amri ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu juu ya yale yanayoelekeana na upande wake Mtukufu na kuitakasa dhati yake tukufu na kutaja pamoja na jina lake Mtu mwengine au kutegemeza kwa mwengine yale yanayopasa kutegemezwa kwake, kama kuumba kuangalia vizuri mambo na kuruzuku. Na nikiaga chake kwa Mtume kwa kumpa nguvu kwa elmu, hifadhi na kummakinisha katika njia ambayo ni nyepesi kwa tabligh na inayonasibiana zaidi na mlingano. Mpangilio wa aya katika mwanzo wa Sura ni mpangilio wa ki Makka. Ama mwisho wake yaani kuanzia Aya Na 14 mpaka mwisho wa Sura, imepokewa katika njia ya Maimamu wa Ahlul Bait vile vile katika njia ya Ahli Sunnah kwamba, makusudio yake ni zaka ya fitr, na swala ya Idd, na ni maalum kuwa saumu na yanayofuatia saumu miongoni mwa zaka ya fitr na swala ya Idd ilianzishwa Madina baada ya Hijra. Hivyo zitakuwa aya za mwisho zimeshuka Madina. Katika hiyo Sura mwanzo wake ni Makka na mwisho wake ni Madina, wala hayo hayakanushi yale yaliyokuja kuwa Sura imeshuka Makka, kwani ilivyo nikuwa haikataliki kuchukulia hivyo mwanzo wa Sura.

Aya Na 1

Ni amri ya kulitakasa jina lake Mwenyezi Mungu S.W.T. na kulitukuza. Na kwa vile hapa kutakaswa Mwenyezi Mungu kumefungamanishwa na jina yake, basi huko kumtakasha kunamaanisha asitajwe yeyote ambaye yeye Mwenyezi Mungu ametakata naye. Kwa sababu jina linatokea katika kusema. Hivyo isitajwe pamoja na jina lake miungu wengine washirikina, waombozi na kuwanasibishia uungu. Na vile vile kama kutaja baadhi ya yanayohusika naye Mwenyezi Mungu (s.w.t) kama kuumba kupatisha, kuruzuku, kuhuisha na kufisha na mfano wake kwa kuyanasibisha kwa asiyekuwa yeye Mwenyezi Mungu Au kama kutaja baadhi ya yasiyofanana na upande wa utakatifu wake, katika vitendo kama kushindwa, ujinga, dhuluma, mghafala na mfano wake katika sifa za upungufu na aibu kwa kuyanasibisha kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Kwa ujumla kulitakasa jina lake ni kuepuka kauli na kutaja yasiyonasibiana kuyataja kwake na jina lake Mwenyezi Mungu (s.w.t), na huko ni kumtakasa katika kiwango cha kauli kwenye kuafikiana na kumtakasa kwake katika kiwango cha kitendo. Hiyo inalazimisha Tawhid (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) iliyo kamili kwa kukanusha kumshirikisha Mwenyezi Mungu kuliko waziwazi; kama ilivyo katika kusema kwake Mwenyezi Mungu:

"Na anapotajwa Allah peke yake nyoyo za wale wasioamini akhera, huchukiwa na wanapotajwa wale walio kinyume naye, mara wanafurahi ". (39:45).

Na pia kusema kwake: "Na unapomtaja Mola wako katika Qu'ran peke yake, basi wao hugeuza migongo yao kwa kuchukia ." (17:46).

Kutegemeza jina Mola kwa dhamiri ya mwenye kusemeshwa (jina la Mola wako) ni kutilia nguvu yale tuliyotangulia kuyataja, kwani maana ni litakase jina la Mola wako ambaye umemfanya ni Mola na wewe unalingania kuwa yeye ni Mola wa waungu, basi isitokee katika maneno yako pamoja na kutaja jina lake kwa uungu wake na kutaja mwengine, kwa kiasi ambacho kitakanusha kumwita Mungu kama alivyojijulisha kwako.

Kusemwa kwake: Mtukufu ni ambaye yuko juu ya aliye juu na kushinda kila kitu, hiyo ni sifa ya Mola wako yaani litakase jina lake kwa sababu yeye ni Mtukufu zaidi. Imesemwa kuwa maana ya aya hii ni kusema "Subhana rabial aala" hayo ni kutoka kwa Ibn Abbas, pia amesema, ni kuswali. Imesemwa makusudio ni jina vile, anavyoitwa yaani mtakase Mwenyezi Mungu S.W.T. na kila sifa na vitendo visivyofanana naye. Imesemwa kuwa makusudio ni kuyatakasa majina yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na yale yasiyofanana naye wala haitwi asiyekuwa yeye na jina linalomhusu yeye Mwenyezi Mungu, wala halitamkwi katika mahali pasipo nasibiana naye kama chooni n.k. Yale tuliyotanguliza kuyataja katika maana ndiyo mapana zaidi na yenye kukusanya zaidi maana na ndiyo yanayonasibiana zaidi na aya inayosema "tutakusomesha wala hutasahau" na "tutakusahilishia njia nyepesi". Kwa sababu mpangilio ni wa kupewa utume mpaka kwenye ukumbusho na tabligh. Hivyo ikaanzwa kwa maneno yake Mtume(s.a.w.w) ya kumtakasa na kila linalo tambulisha shirika kwa uwazi au kwa undani. Akamwahidi mara ya pili kumsomesha kiasi ambacho hataweza kusahau chochote katika yale aliyopewa Wahyi na kusahilishiwa njia ya Tabligh.

Aya Na 2

Kuumba kitu ni kukusanya mafungu yake na kuyapanga sawasawa kiasi ambacho huwekwa kila kitu mahali pake panapo nasibiana napo na kukipa haki yake, kama kuweka kila kiungo katika viungo vya binadamu mahali panapo nasibu. Ayah ii mpaka mwisho wa Aya Na nne zinasifu mipangilio mizuri, ya Mungu na hayo ni dalili ya uungu wake Mwenyezi Mungu (s.w.t)

Aya Na 3

Yaani ni kuvifanya vitu alivyoviuumba juu ya kiasi mahususi na mipaka yenye kuonyesha dhati zake na sifa zake na vitendo vyake visivyozidi kipimo chake na akaviandaa na yale yanayonasibiana na yaliyokadiriwa. Kwa hiyo kila mmoja anafuata upande wa yale yaliyokadiriwa kwake, kwa uongozi wa Mungu, kama mtoto kuendea titi la mama yake, kifaranga kutegemea riziki ya mama yake, mwanamume kwa mwanamke na mifano ya hayo. Mwenyezi Mungu anasema:"Na hakuna kitu chcochote ila hazina yake iko kwetu wala hatukukiteremsha ila kwa kipimo maalum ." (15:21).

Amesema tena: "Kisha akamfanyis nyepesi njia " (80:20). Amesema tena: "Kila mmoja ana mwelekeo wake wa kuelekea ." (2:148).

Aya Na 4 -5

Kutoa malisho kwa ajili ya chakula kisha kuyafanya makavu meusi ni katika usadikisho wa mipangilio ya Mungu na dalili zake; kama ilivyo katika kuumba, kulinganisha sawa, kukadiri na uongozi.

Aya Na 6-7

Amesema katika Mufradati: "Kusoma ni kukusanya herufi na matamko pamoja katika kusoma, lakini sio mkusanyiko wowote ni kusoma, huwezi kusema umewasoma watu, kama ukiwakusanya." Hiyo inafahamisha kuwa hakuwezi kuitwa kusoma kwa herufi moja. Katika Majmau anasema kusomesha ni kuchukua kisomo kwa msomaji kwa kumsikiliza ili usahihishe makosa.

Kumsomesha kwake Mtume, sio kama vile tunavyosemeshana sisi kwa kumsikiliza msomaji kisha kumsahihisha anayoyakosa. Haikuwa kwa Mtume kusoma chochote katika Qur'an akakikosea au asahau wahyi kisha asome ndipo arekebishwe la, bali makusudio yake ni kumwezesha Mtume (SAWW) kuisoma Qur'an kama ilivyoteremsha bila ya kuibadilisha, kwa kuzidisha kitu au kupunguza au kuifanya kombo kwa sababu ya kusahau. Kwa hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu tutakusomesha hutasahau ni kiaga kitokacho kwake Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kumuwezesha kuijua Qur'an na kuifikisha kama ilivyoteremshwa, kiasi ambacho hataisahau. Huo ni msingi wa kufikisha wahyi (ufunuo) kama iluvyofunuliwa. Kusema kwake "Ila anachopenda Allah, ni kuvua kunakofahamisha uwezo wa Mungu ulio huru na kwamba kipawa hiki cha kutosahau sio kuwa Mungu amelazimika macho. Yeye anao uwezo wa kukusahaulisha kama akitaka.

Ayah ii kwa mpangilio wake, haiepukani kuwa inatilia nguvu yale yaliosemwa kwamba Mitume(s.a.w.w) alipokuwa akiletewa wahyi (ufunuo) na Jibril humsomea kwa kuogopa kusahau, ikawa Jibril akimaliza tu naye huanza. Basi iliposhuka ayah ii hakusahau kitu baadaye. Inakurubia kuzingatia kuwa ayah ii tutakusomesha hutosahau ilishuka kwanza ndipo ikashuka aya inayosema: "Usiutikise ulimi wako kwa (kuufanyia haraka) wahyi kwa hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. Wakati tunapokusomea, basi fuata kusomwa kwake, kisha ni juu yetu kuubainisha ". (75:17-19).

Kisha aya inayosema: Usiifanyie haraka (hii) Qur'an kabla haujamalizika wahyi (ufunuo) wake, Na (uombe) useme. Mola wangu nizidishie elimu" (20:114).

Kusema kwake "Hakika anajua yaliyowazi na yaliofichika" kuwa wazi ni kwa kuona au kusikia kama Qur'an inavyosema: "Wakasema tuonyeshe Mungu waziwazi ". (4:153).

"Hakika yeye anajua kauli iliyo dhahiri ". (21:110) Jumla ya aya iko katika mahali pa sababu kwa maana tutakufanyia uzuri katika kupokea wahyi (ufunuo) na kuuhifadhi kwa sababu sisi tunajua dhahiri na ndani ya hali yako na vile unavyojihimu katika jambo la wahyi na unavyopupia twaa katika yale uliyoamrishwa.

Aya Na 8

Wepesi ni sifa yenye kusimama mahali pa msifiwa yaani njia nyepesi, kwa maana ya kuwa daima tutakufanyia njia ya tabligh ni nyepesi kwa maneno na vitendo utaongoza watu na itatimia hoja kwa wengine na utafanya subira juu ya maudhi yao.

Aya Na 9

Ni mtiririko wa amri iliyotangulia ya kulitakasa jina la Mola wake kuahidiwa kwake kusomeshwa wahyi kiasi ambacho hatasahau, na kusahilishiwa njia nyepesi, hizo ni sharti za kidharura ambazo zinaweza kuzuwia kufaulu mlinganio wa kidini. Maana ni kuwa ukitimiza amri ya kufuata yale tuliyokuamrisha, kukusomesha hutosahau na kukusahilishia njia ya wepesi, basi waidhisha ikiwa utafaa (huo) waadhi.

Imeshartiwa kuwa waadhi uwe wenye kunufaisha. Na hilo ni sharti juu ya uhakika wake. Kwani ikiwa waadhi hautanufaisha basi itakuwa ni upuuzi, naye Mwenyezi Mungu ametakata na kuamrisha upuuzi. Kwa hiyo kumwadhia mwenye kumcha Mwenyezi Mungu kwanza kunafahamisha kupondokea haki na hayo ndio manufaa yake (huo waadhi), vile vile kuwaidhika kama alivyosema: "Atawaidhika anayemcha (Mungu). Na kumwaidhia muovu ambaye haogopi katika moyo wake, kwanza kunafahamisha kutimia hoja juu yake na ndio manufaa yake (huo waadhi) na kunalazimisha kuejiepusha kwake, na kuikataa kwake haki kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na atajiepusha nayo muovu". Waadhi baada wa waadhi haunufaishi na chochote kwa hiyo kukaamriwa kuachana naye. Mwenyezi Mungu amesema: "Basi jiepushe na wale wanaoupa mgongo ukumbusho wetu huu na wala hawataki ila maisha ya dunia ." (53:29)

Imesemekana kuwa sharti ni sharti la kisura tu! Sio la kihakika, kwamba ni kutolea habari kuwa waadhi ni wenye kunufaisha katika kuzidisha twaa na kukoma na maasi, kama inavyosemwa: Muulize inafaa kumuuliza, kwa hiyo ndio baadhi yao wakasema: "Herufi In katika aya ni kwa maana ya (Qad) hakika". Na imesemwa kuwa maneno ni ya mkato kwa kuondoa maneno mengine, kukadiria kwake ni "Basi waidhisha ikiwa utafaa waadhi na hata ukitofaa". Hilo ni kwamba yeye Mtume(s.a.w.w) amepelekwa kwa waadhi na kuonya. Kwa hiyo ni juu yake kuonya na kutoa waadhi uwe una manufaa au usiwe na manufaa; Kwa hiyo aya inaelekeana na aya inayosema: "Na amewafanyia kanzu zinazowakinga na joto (na baridi) ". (16:81).

Imesemwa kuna ishara ya kuweka mbali manufaa ya hawa wenye kutajwa; Ni kama vile imesemwa: Fanya unayoamrishwa hata kama hayatanufaisha.

Aya Na 10

Yaani atawaidhika na Qur'an yule ambaye moyoni mwake mna kitu cha kumwogopa Mwenyezi Mungu na kuogopa mateso yake.

Aya Na 11

Dhamiri ni ya mawaidha. Makusudio ya neno Ashqa kwa kulinganisha na aya iliyotangulia, ni yule asiyemwogopa Mwenyezi Mungu.

Aya Na 12

Mto mkubwa ni moto wa Jahanam, ni mkubwa kulinganisha na wa dunia. Imesemwa makusudio yake ni daraja ya chini ya Jahanam ambayo ina adhabu kali zaidi.

Aya Na 13

Makusudio ya kutokufa wala kuwa hai, ni kutookoka kabisa kwa maana ya kuwa adhabu haitakwisha wala maisha hayatabadilika kuwa mazuri. Kwa hiyo makusudio ya uhai ni maisha mema; kama alivyosema katika Ardhi; "Si hai wakutarajiwa wala si maiti wakusahauliwa".

Aya Na 14 -15

Makusudio ya kujitakasa hapa, ni kujitakasa na uchafu wenye kufungamana na dunia kwa dalili ya kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Lakini nyinyi mnapendelea zaidi uhai wa kilimwengu." Kurejea kwa Mwenyezi Mungu kwa kumuelekea yeye Mwenyezi Mungu ni kujitakasa. Kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kujitakasa na uchafu unaofungamna na mali. Hata udhu wa swala ni mfano wa kujitakasa na yale yaliyochumwa na nyuso, mikono na miguu. Kusema kwake: Akalikumbuka jina la Mola wake akaswali, makusudio yake kwa dhahiri ni kumtaja Mwenyezi Mungu kwa kutamka, na kuswali ni swala ya kawaida ya Kiislamu. Aya mbili hizi kwa dhahiri ufahamisho wake ni kuenea a kila kitu, lakini imepokewa kutoka kwa Maimamu wa Ahlul Bait(a.s) kuwa aya hizo zinahusu zaka ya fitri na swala ya Idd. Vile vile hayo yamepokewa katika Ahli Sunnah.

Aya Na 16

Msemo huo unaelekezwa kwa watu juu ya tabia yao ya kiutu inayopelekea kufungamana kabisa na dunia na kujishughulisha na kuiamirisha. Imesemwa kuwa msemo unawaelekea makafiri tu. Kwa hali yoyote maneno ni yenye kuelekezwa kwenye lawama.

Aya Na 17

Imehisabiwa akhera ni yenye kubakia kulinganisha na dunia, pamoja na kuwa yenyewe akhera ni yenye kubaki milele, kwa sababu ya kupima kati ya dunia na akhera.

Aya Na 18-19

Neno haya "Linaonyesha yale yaliyobainishwa kuanzia aya 14 mpaka 17. Imesemwa kuwa ni hAya Na kuwa akhera ni bora na ni yenye kubaki. Imesemwa kuwa kusema vitabu vya kwanza tu. Kisha kuvibainisha kuwa ni vitabu vya Ibrahim na Musa ni kwa ajili ya kutukuza na kukuza jambo.

Utafiti Wa Hadith Katika Tafsiri ya Iyashi kutoka kwa Uqba bin Amir El-Jahaniy amesema iliposhuka aya inayosema: "Litakase jina la Mola wako aliye mkuu" Mtume(s.a.w.w) alisema ifanyeni katika kurukui kwenu. Na iliposhuka "Litakase jina la Mola wako aliye Mtukufu akasema": Ifanyeni katika kusujudi kwenu. Hadith hiyo pia imepokewa katika Durril Manthur kutoka kwa Ahmad, Abu Dawud, Ibn Maja Ibn El-Mundhir na Ibn Murdawayh nao wamepokea kutoka ka Uqba naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) .

Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu Aya Na kwanza amesema: "utakata ni kwa Mola wangu aliye Mtukufu". Kuhusu na ambaye ameumba akakamilisha na ambaye makadirio ya mwanzo kisha akaviongoza.

Katika Durril Manthur ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Mtume(s.a.w.w) alikuwa anajikumbusha Qur'an kwa kuhofia kusahau akaambiwa tumekutoshea na hilo", na ikashuka aya Tutakusomesha wala hutasahau. Katika Faqih aliulizwa Imam As Sadiq(a.s) kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Hakika amefaulu mwenye kuitakasa " Akasema: "Ni mwenye kutoa zaka ya fitr". Akaulizwa: na akamkumbuka Mola wake, akaswali? Akasema ni aliyetoa uwanjani akaswali. Amepokea hadith kwa maana hii Hammad, naye kutoka kwa Jarir naye kutoka kwa Abu Baswir na Zurarah kutoka kwake Imam Jaffar As Sadiq(a.s) . Katika Durril Manthur ametoa Ibn Murdawayh kutoka kwa Abu Said Al-Khudri amesema: Mtume(s.a.w.w) alikuwa akisema: "Hakika amefaulu mwenye kujitakasa na akamkumbuka Mola wake akaswali " Kisha hugawanya zaka ya fitr kabla ya kwenda kwenye mswala siku ya Idd-ul-fitr.

Vile vile kumepokewa kushuka aya mbili hizo katika zaka ya fitri na swala ya Idd kwa njia mbili kutoka kwa Abu Said, vile vile kwa njia mbili kutoka kwa Ibn Umar kwa njia moja kutoka kwa Naila bin Al-Asqa, kwa njia mbili kutoka kwa Abu Aliya na kwa njia moja kutoka kwa Atau. Vile vile kwa njia moja kutoka kwa Muhammad bin Sirin, kwa njia moja kutoka kwa Ibrahim Annakhyi na kutoka kwa Amru bin Awf naye kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) .

Katika Khiswali imepokewa kutoka kwa Utbah bin Amru Allaythi naye kutoka kwa Abu Dharr katika hadith inayosema: "Nilimuuliza Mtume(s.a.w.w) ni kitu gani katika dunia alichokuteremshia Mwenyezi Mungu kilichokuwa katika vitabu vya Ibrahim na Musa? Akasema, Ewe Abu Dharr, soma: hakika amefaulu mwenye kujitakasa akalikumbuka jina la Mola wake akaswali. Lakini nyinyi mnapendelea zaidi uhai wa kilimwengu. Hali akhera ni bora na yenye kubaki. Hakika hayo yamo katika vitabu vya kwanza vitabu vya Ibrahim na Musa. Hadithi inatilia nguvu kuwa ishara na neno "haya" ni mkusanyiko wa aya nne kama ilivyotangulia. Katika Baswir kwa isnadi yake kutoka kwa Abu Baswir amesema Abu Abdillah: Tunazo suhuf alizozitaja Mwenyezi Mungu katika Aya Na 19: Nikamwambia ni mbao? Akasema ndio. Amepokea vile vile kwa njia nyengine Abu Baswir kutoka kwake Abu Abdillah(a.s) . Kwa dhahiri ni kwamba makusudio ya kuwa Suhuf ni mbao nikuwa ni Taurat yenye kuelezewa katika Qur'an kama mbao; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Na ukamwandikia katika mbao kila kitu ." (7:145).

Na pia kusema kwake Mwenyezi Mungu:'na akazitupa mbao .." (7:150). Na kusema kwake "aliziokota zile mbao " (7:154).

Katika Majmau imepokewa kwa Abu Dharr, yeye amesema: "Nilimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu ni Mitume wangapi? Akasema: Ni laki moja na ishirini na nne elfu (124,000) nikamuuliza ni wangapi walio Mursaal katika wao? Akasema mia tatu na kumi na tatu (313). Nikasema Adam alikuwa Mtume. Akasema ndio Mwenyezi Mungu alimsemesha na amemuumba kwa mkono wake. Ewe Abu Dharr, Mitume waarabu ni Hud, Saleh, Shuayb na Mtume wako.

Nikasema tena: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ameteremsha vitabu vingapi? Akasema mia moja na nne (104). Kwa Adam mbao kumi, kwa Shiyth hamsini kwa Ukhnun ambaye ni Idris thelathini naye ndiye wa kwanza kuandika kwa kalamu, Ibrahim kumi na Taurat, Injil, Zabur na Qur'an. Yamepokewa hayo katika Durril Manthur kutoka kwa Abd bin Hamid, Ibn Murdawayh na Ibn Asakir nao kutoka kwa Abu Dharr isipokuwa hazikutajwa mbao za Adam na zimetajwa mbao kumi za Musa kabla ya Taurat.

13

TAFSIRI YA QURANI AL-MIIZAAN

SURA GHASHIYA (KIYAMA) (NA. 88)

INA AYA 26

Kwa jina la Allah, Mwingi wa Rehema, Mwnye kurehemu

هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ الْغَاشِيَةِ ﴿١﴾

1. Je, imekujia habari ya Kiyama?

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ خَاشِعَةٌ ﴿٢﴾

2. Nyuso siku hiyo zitadhalilika.

عَامِلَةٌ نَّاصِبَةٌ ﴿٣﴾

3. Zitatumika na kutaabika.

تَصْلَىٰ نَارًا حَامِيَةً ﴿٤﴾

4. Zitaingia katika moto mkali.

تُسْقَىٰ مِنْ عَيْنٍ آنِيَةٍ ﴿٥﴾

5. Zitanyweshwa maji ya chemshemi ichemkayo.

لَّيْسَ لَهُمْ طَعَامٌ إِلَّا مِن ضَرِيعٍ ﴿٦﴾

6. Hawatakuwa na chakula isipokuwa cha miba.

لَّا يُسْمِنُ وَلَا يُغْنِي مِن جُوعٍ ﴿٧﴾

7. Hakinenepeshi wala hakiondoi njaa.

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاعِمَةٌ ﴿٨﴾

8. Nyuso siku hiyo zitanawiri.

لِّسَعْيِهَا رَاضِيَةٌ ﴿٩﴾

9. Zitakuwa radhi kwa amali yake.

فِي جَنَّةٍ عَالِيَةٍ ﴿١٠﴾

10. (Zitakuwa) katika pepo iliyo tukufu.

لَّا تَسْمَعُ فِيهَا لَاغِيَةً ﴿١١﴾

11. Hazitasikia humo upuuzi.

فِيهَا عَيْنٌ جَارِيَةٌ ﴿١٢﴾

12. Humo mna chemichemi inayotiririka.

فِيهَا سُرُرٌ مَّرْفُوعَةٌ ﴿١٣﴾

13. Mna malili yaliyotukuzwa.

وَأَكْوَابٌ مَّوْضُوعَةٌ ﴿١٤﴾

14. Na vikombe vilivyowekwa.

وَنَمَارِقُ مَصْفُوفَةٌ ﴿١٥﴾

15. Na mito iliyopangwa.

وَزَرَابِيُّ مَبْثُوثَةٌ ﴿١٦﴾

16. Na mazulia yaliyotandikwa.

أَفَلَا يَنظُرُونَ إِلَى الْإِبِلِ كَيْفَ خُلِقَتْ ﴿١٧﴾

17. Je, hawamtazami ngamia namna gani alivyoumbwa.

وَإِلَى السَّمَاءِ كَيْفَ رُفِعَتْ ﴿١٨﴾

18. Na mbingu namna gani zilivyoinuliwa?

وَإِلَى الْجِبَالِ كَيْفَ نُصِبَتْ ﴿١٩﴾

19. Na majabali namna gani yalivyo simamishwa.

وَإِلَى الْأَرْضِ كَيْفَ سُطِحَتْ ﴿٢٠﴾

20. Na ardhi namna gani ilivyotandikwa.

فَذَكِّرْ إِنَّمَا أَنتَ مُذَكِّرٌ ﴿٢١﴾

21. Basi kumbusha, hakika wewe ni mkubushaji tu!

لَّسْتَ عَلَيْهِم بِمُصَيْطِرٍ ﴿٢٢﴾

22. Wewe si mtenza nguvu.

إِلَّا مَن تَوَلَّىٰ وَكَفَرَ ﴿٢٣﴾

23. Lakini mwenye kupa mgongo akakufuru.

فَيُعَذِّبُهُ اللَّـهُ الْعَذَابَ الْأَكْبَرَ ﴿٢٤﴾

24. Allah atamwadhibu adhabu kubwa mno!

إِنَّ إِلَيْنَا إِيَابَهُمْ ﴿٢٥﴾

25. Hakika ni kwetu sisi marejeo yao.

ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا حِسَابَهُم ﴿٢٦﴾

26. Kisha ni juu yetu sisi hesabu yao.

UBAINIFU

Ni Sura ya maonyo na biashara. Inasifu Kiyama kwa hali ambayo watu watakuwa nayo ya kugawanyika makundi mawili: Wema na waovu, na kutua kwao katika sehemu walizoandaliwa miongoni mwa pepo na moto. Inamalizia kwa kumwamrisha Mtume(s.a.w.w) kuwakumbusha watu fani za mazingatio ya Mungu katika ulimwengu zenye kufahamisha juu ya uungu wake, na kurudi kwao kwake kwa ajili ya kuhisabiwa. Sura imeshuka Makka kwa ushahidi wa mpangilio wa aya zake.

Aya Na 1

Ni swali linalopelekea kukuza mambo. Limetumiwa neno kufudikiza (Ghashiya) kwa maana ya Kiyama, kwa sababu kitawafudikiza watu na kitawazingira kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na tutawafufua wala hatutamwacha hata mmoja katika wao ." (18:47). Au kimeitwa hivyo kwa kuwa kitafudikiza nyuso za makafiri kwa adhabu.

Aya Na 2

Yaani nyuso ni zenye kudhalilika kwa ghamu na adhabu itayozifunika. Kudhalilika kutawapata wenye nyuso, lakini hapa kumenasabishwa kwenye nyuso, kwa sababu kunadhihiri katika uso.

Aya Na 3

Makusudio yake kwa kulinganisha na aya inayokabiliana nayo katika sifa ya watu wa peponi inayosema "Zitakuwa radhi kwa mali yake" ni kuwa kutumika kwake ni katika dunia na kutaabika kwake ni katika akhera. Hakika mtu anafanya anayoyafanya katika dunia ili atengenekewe, na apate matakwa, lakini amali zao ni bure tu; Hazitawafaa na chochote, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika amali tuyafanye kama mavumbi yaliyitawanywa ". (25:23).

Kwa hiyo hakirudi chochote katika waliyoyafanya isipokuwa taabu, kinyume cha watu wa peponi, kwani hakika wao mahangaiko yao waliyohangaika katika dunia ni kibali kitakachowapeleka katika pepo siku ya Kiyama. Imesemwa makusudio yake ni kutumika katika dunia kwa maasi na kutaabika katika moto siku ya Kiyama.

Aya Na 4

Yaani ni moto katika ukomo ya joto.

Aya Na 5

Yaani ni yenye joto kali.

Aya Na 6

Dhwarii ni aina ya miba ambayo watu wa Hijazi wanaita hivyo inapokauka. Na chakula kibaya sana, hawawalishi hata wanyama wao. Huenda hiyo ya motoni imeitwa hivyo, kwa kufanana.

Aya Na 7

Kunawiri ni fumbo la furaha inayodhihiri usoni kama ilivyosemwa: "utaona katika nyuso zao mng'ao wa kunawiri ." (83:24). Au itakuwa kwa maana ya kuneemeka. Imesemwa haikuwekwa herufi za kuunganisha kwa kuonyesha ubainifu kamili kati ya hali za makundi mawili.

Aya Na 8

Makusudio ya amali njema yaani imeridhia amali yake njema kwa kulipwa malipo mema.

Aya Na 9-16

Ni utukufu wa daraja yake, kwani katika hiyo pepo kuna maisha yasiyokuwa na kifo, ladha isiyokuwa na machungu yoyote, na furaha isiyokuwa na huzuni. Kusema kwake "Hazitasikia humo upuuzi" yaani hizo nyuso hazitasikia tamko lolote lisilokuwa na faida. Kuhusu chemchemi makusudio yake ni jinsi yake, na amezihesabu Mwenyezi Mungu chemchemi katika hiyo pepo katika maneno kama Salsabil Kinywaji kitakatifu nk.

Aya Na 17

Baada ya kumaliza kukisifu Kiyama na kubainisha hali za makundi mawili wa waumini na makafiri, amefuatishia kuishiria kijumla mipangilio mizuri ya Mungu ambayo inabainisha uungu wake, inayohukumilia kumwabudu kwake, na hilo likafuatiwa na hisabu ya matendo na malipo ya muumin kwa imani yake na kafiri kwa kufuru yake. Wakati wake hayo ni siku ya Kiyama. Kwanza amewaambia kuangalia ngamia vile alivyoumbwa. Vipi alivyoitia sura Mwenyezi Mungu ardhi isiyokuwa na uhai wala hisia, kwa Sura hii ya ajabu katika viungo vyake, nguvu zake na vitendo vyake. Akaitiisha kwao ili wanufaike nayo kwa kuipanda, uchukuzi, nyama yake, maziwa yake, ngozi yake na sufu yake. Na hata mkojo wake na kinyesi chake. Je, yote hAya Na mezuka tu kwa bahati bila ya kupangwa? Kuhusisha kutaja ngamia ni kwa njia kuwa Sura imeshuka Makka na ngamia alikuwa ndio nguzo ya maisha ya waarabu.

Aya Na 18

Imepambwa hiyo mbingu kwa jua, mwezi na sayari nyenginezo kwa manufaa ya watu wa dunia; na amejaalia hewa ambayo wanalazimika wanyama kuivuta.

Aya Na 19

Majabali ndio vigingi vya ardhi vinavyoizuia ardhi isitetemeke na hazina ya maji ambapo mito na chemchem hububujika kutoka huko na ni hifadhi za madini.

Aya Na 20

Yaani imatendikwa ili mwanadamu aweze kukaa na kumsahilikia kuguru hapa na pale na matumizi mengine ya kiufundi. Basi mipangilio yote hii imetegemezwa kwa Mwenyezi Mungu bila ya wasiwasi wowote. Yeye ni Mola wa mbingu ardhi na vilivyo ndani yake. Yeye ni Bwana wa ulimwengu wa kibinadamu, niwajibu kwao kumfanya ndiye Mola, kumpwekesha na kumwabudu na mbele yao kuna Kiyama ndiyo siku ya hesabu ya malipo.

Aya Na 21

Ni sehemu ya yaliotangulia maana yake ikiwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola na hakuna Mola asiyekuwa yeye na mbele yao kuna siku ya hesabu na malipo kwa aliyeamini katika wao au aliyekufuru, basi wakumbushe hilo. Kusema kwake "Hakika wewe ni mkumbushaji tu " ni ubainifu wa kuwa kazi ya Mtume ni kukumbusha tu kwa kutarajia kuitikiwa na kuaminiwa bila ya kulazimisha.

Aya Na 22

Ni ubainifu na tafsiri ya aya iliyotangulia.

Aya Na 23

Hapo anavuliwa na ukumbusho yule mwenye kupa mgongo na kukufuru. Ilivyo ni kuwa kukanusha kumekuja baada ya ukumbusho; kukanusha kwa kuvua, ni ukumbusho baada ya ukumbusho. Ni kama vile imesemwa wakumbushe na udumishe ukumbusho isipokuwa yule ambaye umemkumbusha akapa mgongo na kukufuru. Kwa hiyo huna haja ya kudumisha kumkumbusha bali achana naye. Mwenyezi Mungu atamwadhibu adhabu kubwa. Aya Na 21 - 24 katika Sura hii zinalingana na Aya Na 9 -12 ya Sura ya Al-A'laa (87). Imesemekana kuwa sio kuvuliwa na ukumbusho bali nikuvuliwa kutenza nguvu, na maana ni wewe simtenza nguvu isipokuwa juu ya yule mwenye kupa mgongo akakufuru ndio Mwenyezi Mungu anakusaliti naye na kukuamrisha kufanya jihadi; utapigana naye na kumuua. Na imesemwa kuvua hapa ni kwa kukataa tu, Kwa maana; wewe si mtenza nguvu, lakini mwenye kupa mgongo akakufuru katika wao hataachwa bure. Atamwadhibu Mwenyezi Mungu adhabu kubwa. Tuliyoyatanguliza kuyataja yako karibu na yenye nguvu zaidi.

Aya Na 24-25

Imetangulizwa "ni kwetu sisi" kwa sababu ya kutilia mkazo. Na aya hiyo iko katika mahali pa illa (sababu) ya kuadhibu kulikotajwa katika aya iliyotangulia.

Utafiti Wa Hadith Katika Majmau imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas amesema: "Amesema Mtume(s.a.w.w) Dhwarii ni kitu katika moto kinafanana na mwiba kichungu kuliko shubiri. Kinanuka uvundo kuliko mzoga na ni kikali kuliko moto. Katika Tafsiri ya Qummi kuhusu kwake Mwenyezi Mungu "Hawatasikia humo upuzi" ni upuuzi na uwongo." Kuhusu Aya Na 22 amesema yaani sio mwenye kuwachunga. Katika Durril Manthur ametoa Ibn Jariyr, Hakim, Ibn Murdawayh na Bayhaqi kutoka kwa Jabir amesema: 'Amesema Mtume(s.a.w.w) : "Nimeamrishwa kupigana na watu mpaka waseme: "La ilaha illa llahu" wakisema, damu yao na mali zao zitakuwa zimesalimika isipokuwa kwa haki yake, na hisabu yao iko juu ya Mwenyezi Mungu, kisha akasoma aya "Basi kumbusha hakika wewe ni mkumbushaji wewe si mtenza nguvu ". Hakuna dalili yoyote kwamba kuvua kunatokana na dhamiri ya wao na hilo ni dhahiri.

Katika hiyo Durril Manthur katika hadith iliyopokewa kutoka kwa Abu Jaffar(a.s) kuhusu kusema kwake Mwenyezi Mungu: "Lakini mwenye kupa mgongo na akakufuru" anakusudia yule asiyewaidhika, na asiyesadiki akakanusha uungu na akakufuru neema. "Atamwadhibu Allah adhabu kubwa mno!" anakusudia adhabu nzito ya milele. "Hakika ni kwetu sisi marejeo yao" anakusudia mwisho wao "kisha hakika ni juu yetu sisi hesabu yao" anakusudia malipo yao. Katika Nahj aliulizwa Ali(a.s) vipi atawahisabu Mwenyezi Mungu watu na wingi wao huo? Akasema: Kama vile anvyowaruzuku na wingi wao. Kukaulizwa vipi atawahisabu na hawamuoni? Akasema kama anavyowaruzuku na hawamwoni.

Katika hiyo hiyo Nahj amesema As Sadiq, kila Umma utahisabiwa na Imam wa zama zake. Na wanawajua maimam marafiki zao na maadui zao kwa alama zao na ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na juu ya mahali hapo palipoinuka watakuaweko watu hao watakaowafahamu wote kwa alama zao ". (7:46). Imepokewa hadith kwa maana haya katika Baswir kutoka kwa Sadiq, katika Kafi kutoka kwa Baqir na Kadhim(a.s) na katika Faqih kutoka kwa Hadi(a.s) .