• Anza
  • Iliyopita
  • 4 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 2309 / Pakua: 650
Kiwango Kiwango Kiwango
DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU

Mwandishi:
Swahili

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU

MWANDISHI: DKT. ABU AMINA BILAAL PHILIPS

MFASIRI: MUHAMMAD AL-MAAWY

NI IPI DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU?

Kila mtu anazaliwa katika hali isiyokuwa ya uchaguzi wake. Dini ya familia yake au ideolojia ya dola inalazimishwa kwake. Kuanzia mwanzo wa kuwepo kwake katika dunia hii. Wakati anapofika miaka ya ujana, anakuwa tayari ametiwa kasumba kuamini kuwa itikadi za jamii yake ndizo sahihi ambazo kila mtu anafaa kuzifuata. Hata hivyo, pindi baadhi ya watu wanapo baleghe na kuwa na akili timamu na kufunuliwa kwao mifumo ya Imani, wanaanza kuuliza usahihi wa Itikadi zao wenyewe. Mtafutaji ukweli mara nyingi anafikia mahali ambapo anatatizika pale anapotambua kuwa kila dini, dhehebu, ideolojia na falsafa yoyote inadai kuwa ndiyo njia ya pekee iliyo sahihi kwa mwanadamu. Kwa hakika, zote zinawahimiza watu kufanya mambo mema na mazuri. Hivyo, ipi ndiyo iliyo sahihi? Haiwezekani zote kuwa sahihi kwa vile kila moja inadai kwamba zile nyengine hazipo sawa. Kwa hivyo, vipi mtafutaji haki na ukweli ataweza kuchagua njia ya sawa.

Mwenyezi Mungu Ametupatia sote akili na bongo kutuwezesha kufanya uamuzi huu muhimu. Ni uamuzi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Kwayo kunategemea mustakbali wake. Kwa hiyo, kila mmoja wetu ni lazima achunguze dalili zilizotolewa bila ya jazba wala upendelea na achague ile inayoonekana kuwa sawa mpaka dalili nyengine zitakapopatikana au kujitokeza.

Kama Dini au falsafa nyengine yoyote, Uislamu pia unadai kuwa ndio njia moja na ya pekee katika kumfikia Mwenyezi Mungu. Kwa muono huu haina tofauti na mifumo mingine. Kijitabu hiki kina lengo ya kutoa baadhi ya dalili kwa usahihi wa dai hilo. Hata hivyo, ni lazima kwa wakati wote ifahamike kuwa mtu anaweza tu kuamua njia ya kweli kwa kueka kando mhemuko, jazba na upendeleo ambao mara nyingi zinatupofua katika kuona uhakika wa mambo. Baadaye tu, ndio tutaweza kutumia akili tuliyopewa na Mwenyezi Mungu katika kufanya uamuzi wa kimantiki na wa sawa.

Zipo hoja nyingi ambazo zinaweza kutolewa kuunga mkono dai la Uislamu kuwa ni Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu.

Zifuatazo ni hoja tatu tu za wazi.

Hoja ya kwanza inahusiana na asli yake ya kuwa inatoka kwa Mwenyezi Mungu kwa majina ya Dini na ukamilifu wake katika maana yake.

Ya pili inahusu mafunzo ya kipekee na yasiyokuwa na utata wala mafumbo kwa yale mahusiano baina ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu na uumbaji.

Hoja ya tatu inatokana na hakika kuwa Uislamu unaweza kufikiwa kilimwengu na watu wote kwa wakati wote.

Hizi ni sehemu tatu za msingi ambazo mantiki na akili zinaamuru ulazima kwa Dini kutambuliwa kuwa ni Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Kurasa zifuatazo zitajaribu kukuuza na kufafanua kwa kina fikra hizi.

JINA LA DINI

Kitu cha kwanza ambacho mtu ni lazima akijue na kukifahamu barabara kuhusu Uislamu ni maana ya neno hili, "Islaam - Uislamu".

Neno hili ni la Kiarabu "Islaam" ambalo linamaanisha kunyenyekea, kutii au kujisalimisha kwa hiari yake mtu kwa Mwenyezi Mungu wa kweli tu anayeitwa kwa Kiarabu "Allah". Yule anayetii na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu kwa kupenda kwake anaitwa kwa Kiarabu "Muslim - Muislamu".

Dini ya Kiislau haijaitwa kwa jina la mtu au kaumu wala halikuamuliwa na kizazi cha baadae, kama ilivyo kwa Ukristo ambao uliitwa kwa jina la Yesu Kristo, Ubudha baada ya mwanzilishi wake Gautama Buddha, Ukomfushiasi baada ya Confucius, Umaksi baada ya Karl Marx, Uyahudi kutokana na kabila la Yuda na Ubaniyani kutokana na Mabaniyani (Wahindi).

Uislamu (kunyenyekea kwa kufuata matakwa ya Allah) ni Dini aliyopewa Adam, mwanadamu wa kwanza na Nabii wa mwanzo wa Mwenyezi Mungu na ilikuwa ni Dini ya Manabii na Mitume wote waliotumwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa wanadamu. Mbali na hayo jina lake (Uislamu) lilichaguliwa na Mwenyezi Mungu Mwenyewe na kutajwa kwa uwazi katika Kitabu cha mwisho kilichoteremshwa kwa watu. katika Wahyi huo wa mwisho, unaoitwa kwa Kiarabu Qur'aan (Qur'ani), Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amesema yafuatayo:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ﴿٣﴾

"Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini" (5: 3).

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٨٥﴾

"Na anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa katika wenye kukhasiri" (3: 85).

Kwa hiyo, Uislamu haudai kuwa ni Dini mpya iliyoletwa na Nabii Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) huko Arabuni katika karne ya saba, bali kuwa ni udhihirisho mpya katika mfumo wa mwisho wa Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu Mweza na Mwenye nguvu, Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), kama ilivyoteremshwa mwanzo kwa Adam ('Alayhis Salaam) na baadae kwa Manabii waliomfuata. Kwa sehemu hii tunaweza kueleza kwa muhtasari kuhusu Dini nyengine mbili zinazodai kuwa ni njia za kweli. Hakuna kifungu chochote katika Biblia kinachoonyesha kuwa mwenyezi Mungu Aliwafunulia kaumu ya Nabii Musa ('Alayhis Salaam) au vizazi vyao kuwa Dini yao inaitwa Uyahudi, na pia kwa wafuasi wa Kristo kuwa Dini yao inaitwa Ukristo. Kwa maneno mengine, majina "Uyahudi" na "Ukristo" hayatoki kwa Mwenyezi Mungu au kukubaliwa naye. Haikuwa ila baada ya muda mrefu wa kuondoka kwake ndipo jina Ukristo likapatiwa Dini ya Yesu.

Je, Dini ya Yesu kwa uhakika ilikuwa tofauti kabisa na jina lake?[1]

Dini yale iliakisiwa na kuonekana kwa mafundisho yake, ambayo aliwahimiza kwayo wafuasi wake kuyakubali kama misingi ya uongofu katika mahusiano yao na Mwenyezi Mungu. Katika Uislamu, Yesu ni Mtume aliyetumwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), na jina lake kwa Kiarbu ni 'Isa ('Alayhis Salaam). Kama Mitume kabla yake, aliwalingania watu wake kwa ridhaa na hiari yao kujisalimisha kwa maelekezo ya Mwenyezi Mungu (Uislamu unasimamia hilo). Kwa mfano, katika Agano Jipya inaelezwa kuwa Yesu aliwafunza wafuasi wake kumuomba Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:

"Baba! Jina lako litukuzwe; ufalme wako ufike" (Luka 11: 2).

Na pia: "Baba yetu uliye mbinguni: Jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni" (Mathayo 6: 9 - 10)

Fikra hii ilihimizwa sana na Yesu kwa kauli zake nyingi zilizorikodiwa katika Anaajiil (Gospels). Kwa mfano: alifundisha kuwa wale wanaonyenyekea watarithi Pepo.

Yesu aliashiria kuwa yeye pia ananyenyekea na kutii maagizo ya Mwenyezi Mungu.

"Si kila aniambiaye , 'Bwana, Bwana', ataingia katika ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza matakwa ya Baba yangu aliye mbinguni" (Mathayo 7: 21).

"Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma" (Luka 5: 30).

Zipo ripoti nyingi katika Anaajiil (wingi wa Injili) zinazoonyesha kuwa Yesu aliwawekea wazi kabisa wafuasi wake kuwa yeye hakuwa Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli. Kwa mfano, alipokuwa akizungumza kuhusu Siku ya Mwisho (Kiyama), alisema:

"Lakini juu ya siku au saa hiyo hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala Malaika wa mbinguni, wala mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye" (Marko 13: 32).

Hivyo, Yesu kama Mitume wengine kabla yake na yule aliyekuja baada yake, walifundisha Dini ya Uislamu: Kunyenyekea na kutii kwa amri ya Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli.

MWENYEZI MUNGU NA UUMBAJI

Kwa vile ujumla wa unyenyekevu kwa hiari ya mtu kwa Mwenyezi Mungu unawakilisha kiini cha 'Ibadah, ujumbe wa msingi wa Dini ya Mwenyei Mungu, Uislamu, ni kumuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake. pia inahitajia kuepuka 'Ibadah iliyoelekezwa kwa mtu yeyote yule, pahala popote pale au kitu mbali na Mwenyezi Mungu. Kwa vile vitu vyote mbali na Mwenyezi Mungu, Muumbaji wa kila kitu (na vitu vyote), kuwa ndiyo kiini cha Uislamu, kumuepusha mwanadamu awe mbali na kuabudu viumbe kwa kumlingania na kumuita katika kumuabudu Muumbaji wake peke Yake. ni peke Yake ndiye Anayestahiki kuabudiwa na mwanadamu, kwa sababu ni kwa ridhaa Yake ndio maombi yanakubaliwa na kujibiwa. Kwa hiyo, ikiwa mtu atauomba mti na maombi yake yakajibiwa, si mti uliokubali na kujibu maombi yake, bali ni Mwenyezi Mungu ndiye aliyekubali kw ahali hiyo iliyoombwa kutukia.

Mmoja anaweza kusema: "Hiyo ni dhahiri". Hata hivyo, kwa wenye kuabudu mti, si hivyo kabisa. Hivyo hivyo, maombi kwa Yesu, Buddha, Krishna au mtakatifu Christopher, au mtakatifu Jude au hata Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam), hayajibiwi na wao, lakini na Mwenyezi Mungu.

Yesu hakuwambia wafuasi wake kumuabudu yeye, lakini aliwaamuru wamuabudu Mwenyezi Mungu, kama inavyosema Qur'ani:

وَإِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ أَأَنتَ قُلْتَ لِلنَّاسِ اتَّخِذُونِي وَأُمِّيَ إِلَـٰهَيْنِ مِن دُونِ اللَّـهِ قَالَ سُبْحَانَكَ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أَقُولَ مَا لَيْسَ لِي بِحَقٍّ إِن كُنتُ قُلْتُهُ فَقَدْ عَلِمْتَهُ تَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِي وَلَا أَعْلَمُ مَا فِي نَفْسِكَ إِنَّكَ أَنتَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿١١٦﴾

"Na pale Allah Atakaposema: Ewe 'Iisaa bin Maryam! Ati wewe uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu badala ya Allah? (Na 'Iisaa) atasema: Subhanaka, Wewe umetakasika! Hainifalii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi Yako. Hakika Wewe ndiye Mjuzi mkubwa wa yaliyofichikana" (5: 116).

Wala Yesu hakuiabudu nafsi yake pale alipoabudu, lakini alimuabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu. Yesu alinukuliwa katika Anaajiil kuwa alisema: "Imeandikwa:

'Utamwabudu Bwana Mungu wako, na kumtumikia yeye peke yake'" (Luka 4: 8).

Kanuni ya msingi inapatikana katika Surah ya ufunguzi ya Qur'ani, inayojulikana kama Suratul Faatihah Ayah ya 5:

"Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada".

Mahali pengine, katika Kitabu na Wahyi wa mwisho, Qur'ani, Mwenyezi Mungu Anasema:

"Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni Nitakuitikieni" (40: 60).

Ni vyema kutilia mkazo kuwa ujumbe wa msingi wa Uislamu (yaani, kumuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake) pia unatangaza kuwa Mwenyezi Mungu na uumbaji Wake (au viumbe Vyake) ni tofauti kabisa. Mwenyezi Mungu hako sawa na viumbe Vyake wala sehemu yao, wala viumbe Vyake haviko sawa na Yeye wala si sehemu Yake.

Hii inaweza kuonekana ni dhahiri kabisa, lakini mwanadamu kuabudu viumbe vyengine, badala ya Muumba ni kwa kiasi na kiwango kikubwa imeegemea ujinga, au kupuuza, kwa fikra na wazo hili. Ni itikadi na imani kuwa kiini cha Mwenyezi Mungu ni kuwa yupo kila mahala katika viumbe Vyake na uumbaji Wake au Uungu Wake kwa dhati Yake ipo au ilikuwepo katika baadhi ya sehemu ya viumbe na uumbaji Wake, ambayo imethibitisha na kutetea masala ya kuabudu viumbe vya Mwenyezi Mungu na kuita jambo hilo kuwa ni kumuabudu Mwenyezi Mungu. hata hivyo, ujumbe ya Uislamu, kama ilivyoletwa na Manabii wa Mwenyezi Mungu, ni kumuabudu Mwenyezi Mungu tu na kujiepusha kuabudu viumbe Vyake ama moja kwa moja au kwa njia nyengine yoyote. Katika Qur'ani Mwenyezi Mungu Anaeleza kwa uwazi kabisa:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ﴿٣٦﴾

"Na kwa hakika kwa kila ummah Tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Allah, na muepukeni Shetani (na miungu wasio wa kweli)" (16: 36).

Pale wenye kuabudu masanamu wanapoulizwa, ni kwa nini wanayasujudia hayo masanamu yaliyotengenezwa na wanadamu, sikuzote na kila wakati wanajibu kuwa kwa uhakika wao hawaabudu hiyo taswira ya mawe, lakini Mwenyezi Mungu ambaye yupo ndani yake. wanadai ya kwamba hilo sanamu la jiwe ni alama tu ya kutazamia kwa kiini cha Mwenyezi Mungu na sio Mwenyezi Mungu Mwenyewe. Yeyote aliyekubali dhana ya kuwa Mwenyezi Mungu yuko kwa njia yoyote ile ndani ya viumbe Vyake atalazimika kukubali hoja hii ya kuabudu masanamu. Kwa maana, mtu anayefahamu ujumbe wa msingi wa Uislamu na athari yake hatakubali kamwe kumshirikisha Mwenyezi Mungu kwa kuabudu masanamu kwa jinsi yoyote itakavyoelezwa kimantiki. Wale waliodai uungu kwao wao wenyewe katika historia waliegemeza itikadi yao potofu na ya kimakosa kuwa Mwenyezi Mungu yuko ndani ya mwanadamu. Kuchukua hatua moja mbele, walidai kuwa Mwenyezi Mungu yuko ndani yao sana kuliko kwa wengine wetu, hivyo wanaadamu wengine ni lazima wanyenyekee na kuwatii na kuwaabudu wao kama mungu mwenyewe kwa dhati Yake au kama Mwenyezi Mungu aliyejikoleza ndani yao. Hivyo hivyo, wale waliotetea uungu wa wengine baada ya kufa kwao walipata eneo lenye rutuba miongoni mwa wale wenye kukubali itikadi ya uwongo ya kuwepo Mwenyezi Mungu ndani ya binadamu.

Inatakiwa iwe wazi kabisa sasa kuwa yule mwenye kuelewa msingi wa ujumbu wa Uislamu na athari yake hawezi kukubali kuabudu kiumbe kingine kwa hali yoyote ile. Kiini cha Dini ya Mwenyezi Mungu ni mwito wa dhahiri wa kumuabudu Muumbaji na kukataa kuabudu viumbe kwa mfumo wowote ule. Hii ndio maana ya wito wa Uislamu: "Laa ilaaha Illaa Llah"

(Hapana Mola wa kuabudiwa ila Allah).

Tangazo hili la kweli katika ibara hii na kuukubali Unabii moja kwa moja unamleta mtu kuwa Muislamu, na Imani ya uhakika na kweli inamdhaminia mtu Pepo. Kwa hiyo, Mtume wa mwisho wa Uislamu (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amenukuliwa akisema:"Yeyote anayesema: 'Hapana Mola wa kuabudiwa ila Allah, na akafa akishikilia (Imani hiyo) ataingia peponi".

Itikadi kwa tangazo hili la Imani inahitaji kuwa mtu anyenyekee na kutii kwa hiari amri za Mwenyezi Mungu kwa njia iliyofunzwa na Manabii wa Mwenyezi Mungu. Pia inahitaji kwa mtu kuwa Muumini kuacha kabisa kuabudu miungu ya uwongo.

1

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU

RISALA YA DINI ZA UWONGO

Yapo madhehebu, vikundi, dini, falsafa, na harakati nyingi sana katika hii dunia, zote hizo zikidai kuwa ni njia sahihi na ya sawa au njia ya pekee ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Vipi mtu anaweza kutambua ile njia iliyo sawa au ama, kwa hakika, zito ziko sawa?

Njia moja ambayo jibu linaweza patikana ni kuondoa zile tofauti za juujuu katika mafunzo ya wenye kudai kadhaa kwa ukweli wa mwisho na wa msingi, na kutambua malengo ya msingi 'Ibadah wanayo walingania, moja kwa moja au kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja.

Dini zote za uwongo zina fikra moja ya msingi iliyo sawa kwa zote, kuhusiana na Mwenyezi Mungu: ama wanadai kuwa watu wote ni miungu (wenye kuabudiwa), au watu fulani mahsusi walikuwa mungu, au maumbile ni mungu, au kuwa Mwenyezi Mungu ni kitu kilichobuniwa na mwanadamu.

Hivyo, inaweza kusemwa kuwa risala (ujumbe) wa msingi kwa Dini za uwongo ni kuwa Mwenyezi Mungu Anaweza kuabudiwa katika mfumo wa viumbe Vyake. Dini za uwongo zinamuita mwanadamu kuabudu viumbe vya Allah wa kuita viumbe hivyo au sehemu yake kuwa ni mungu. kwa mfano, Nabii Yesu aliwaita wafuasi wake kumuabudu Mwenyezi Mungu, lakini wale wanaodai kuwa wao ni wafuasi wa Yesu leo wanawalingania watu wengine wamuabudu Yesu, wakidai kuwa Yesu alikuwa mungu.

Buddha alikuwa ni mwana-mageuzi aliyeanzisha idadi kubwa ya kanuni za kibinadamu na utu katika dini za India. Hakudai kuwa yeye ni Mwenyezi Mungu wala hakutoa rai kwa wafuasi wake kuwa yeye mwenyewe ni kitu au kiume cha kuabudiwa.

Ilhali kuwa leo Mabuddha wengi wanaoishi nje ya India wamemfanya yeye kuwa mungu na wanasujudia masanamu yaliyotengenezwa, kwa muono wao kwa sura yake. Kwa kutumia msingi na kanuni ya kutambua kitu cha kuabudiwa, tunaweza kwa urahisi na wepesi kuzijua dini za uwongo na kuvumbua maumbile ya asili yake, kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika Qur'ani:

مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٠﴾

"Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyoyapanga nyinyi na baba zenu. Allah Hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hapana hukumu ila ya Allah tu. Yeye Ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka. Lakini watu wengi hawajui" (12: 40).

Inaweza kutolewa hoja kuwa dini zote zinafunza mambo mazuri, hivyo kwa nini tujali ni dini gani tunayofuata?

Jibu ni kuwa dini zote za uwongo zinafunza uovu mkubwa sana: kuabudu uumbaji na viumbe.

'Ibadah ya kuhuluku na viumbe ni dhambi kubwa ambalo mwanadamu anaweza kufanya kwa sababu inakwenda kinyume na lengo la uumbaji. Mwanadamu aliumbwa kumuabudu Mwenyezi Mungu peke Yake kama alivyosema Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa uwazi kabisa katika Qur'ani:

"Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi" (51: 56).

Kwa hiyo, kuabudu uumbaji, ambayo ni kiini cha ushirikina ni dhambi la pekee ambalo halisamehewi. Yeyote mwenye kufariki katika hali hiyo ya ushirikina, ameiziba Qadari yake katika maisha ya baadaye (Akhera). Hii si rai, lakini ni Wahyi wa uhakika kama alivyosema Mwenyezi Mungu katika ufunuo Wake wa mwisho kwa mwanadamu:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ﴿٤٨﴾

"Hakika Allah Hasamehe kushirikishwa, na Husamehe yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye" (4: 48 na 116).

KILIMWENGU CHA DINI YA MWENYEZI MUNGU

Kwa vile matokeo ya kufuata dini ya uwongo ni makubwa, Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kueleweka kilimwengu na yenye kuweza kufikia kilimwengu hapo awali.

Na ni lazima iendelee daima dawamu kufahamika na kufikiwa katika ulimwengu mzima. Kwa ibara nyengine, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuzuiliwa kwa kaumu moja, pahala, au zama fulani. Wala haingii katika mantiki kuwa Dini kama hiyo itaweka masharti ambayo hayana mahusiano yoyote kabisa baina ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu, kama ubatizo, au itikadi ya kuwa mwanadamu ni mwokozi, au kipito na wasta ya kuwafikisha.

Ndani ya msingi wa kati wa Uislamu na maana yake (kujisalimisha kwa hiari katika kutekeleza amri za Mwenyezi Mungu) imelala mizizi ya kilimwengu cha Uislamu. Pindi mwanadamu anapofahamu kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na ni tofauti kabisa na uumbaji Wake, na akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, anakuwa Muislamu wa kweli katika mwili na roho na hivyo kustahiki kuingia Peponi.

Kwa hiyo, yeyote kwa wakati wowote anaweza kuwa Muislamu hata akiwa katika maeneo za ndani na mbali katika ulimwengu, mfuasi wa Dini ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, kwake yeye tu kukataa kuabudu uumbaji na viumbe na kurudi kwa Mwenyezi Mungu peke Yake. Hata hivyo, inatakiwa ifahamike kuwa ili kunyenyekea na kutii amri za Mwenyezi Mungu, mtu anatakiwa daima na milele awe ni mwenye kuchagua baina ya haki na batili, ukweli na uwongo. Hakika, mwanadamu amepatiwa kipawa, nguvu, uwezo na akili na Mwenyezi Mungu ya kuweza kutofautisha ukweli kutokana na uwongo, lakini pia kuchagua baina yao.

Uwezo huu uliopatiwa na Mwenyezi Mungu inabeba pamoja nayo jukumu muhimu sana, kwamba mwanadamu ataulizwa na Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa uchaguzi anaofanya. Kwa hivyo, inafuata kuwa mwanadamu anafaa kujaribu uwezo wa upeo wake kufanya mema na kuepukana na mabaya. Fikra hizi zimeelezwa katika Wahyi wa mwisho kama ifuatavyo:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالنَّصَارَىٰ وَالصَّابِئِينَ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴿٦٢﴾

"Hakika Walioamini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini Allah na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika" (2: 62).

Ikiwa, kwa sababu yoyote ile, wanshindwa kukubali ujumbe wa mwisho baada ya kuwa imeelezwa kwao kinaganaga, basi watakuwa katika hatari kubwa mno. Mtume wa mwisho (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amesema:

"Yeyote miongoni mwa Wakristo na Mayahudi atasikia kuhusu mimi, lakini bila ya kuyakinisha Imani yake kwa yale niliyoyaleta na akafa katika hali hiyo, atakuwa miongoni mwa wakaazi wa Moto" (Sahih Muslim [Tafsiri ya Kiingereza], Mj. 1, uk. 91, Nambari 284).

KUMTAMBUA MWENYEZI MUNGU

Swali linaloibuka hapa ni: Vipi watu wote watatizamiwa kuamini Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli, ukitazama usuli zao tofauti, jamii zao na tamaduni? Kwa watu kusualiwa na kubeba majukumu yao kwa kuabudu Mwenyezi Muja wa kweli, wanahitajiwa wawe na fursa na njia ya kuifikia elimu ya kumfahamu na kumjua Yeye.

Wahyi ya mwisho inafundisha kuwa wanaadamu wote wala utambuzi wa Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli iliyochapwa katika roho zao kama sehemu ya maumbile yao waliyoumbwa nayo.

Katika Surah ya saba ya Qur'ani, Mwenyezi Mungu Ameeleza kuwa pindi Alipomuumba Adam Alivifanya vizazi vyote vya Adam kuwepo (katika uhai) na Akachukua ahadi kutoka kwao kwa kusema:

أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ قَالُوا بَلَىٰ شَهِدْنَا ﴿١٧٢﴾

"Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia".(Al-A'raaf, Ayah 172).

Kisha Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaeleza ni kwa nini Aliwaleta wanaadamu wote washuhudie kuwa Yeye ndiye Muumba na Mwenyezi Mungu, mmoja wa kweli anayestahiki kuabudiwa. Anasema Aliyetukuka:

"Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo" (7: 172).

Hiyo ni kusema, hatuwezi kudai siku hiyo kuwa hatukuwa ni wenye kumjua Allah (Subhaanahu wa Ta'ala), kuwa ndiye Mwenyezi Mungu wetu na kuwa hakuna aliyetuambia kwamba tunafaa sisi kumuabudu Allah peke Yake. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anaendelea kutueleza kuwa:

أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ ﴿١٧٣﴾

"Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?" (7: 173).

Hivyo, kila mtoto anazaliwa katika maumbile ya kuwa na Imani ya Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa asili na silika kumuabudu Yeye peke Yake. itikadi ya kiasili na mwelekeo unaitwa katika lugha ya Kiarabu, "Fitrah". Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) amenukuliwa akisema kuwa Allah Aliyetukuka amesema:

"Nimewaumba waja Wangu katika Dini ya sawa (na sahihi), lakini Shetani ndiye aliyewafanya kupotea".

Pia amesema Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam):"Kila mtoto anazaliwa katika Fitrah. Baadaye ni wazazi wake ndio wanaomfanya ama awe Myahudi, au Mkristo au Mmajusi" (Al-Bukhaariy).

Ikiwa mtoto ataachwa peke yake, atamuabudu Mwenyezi Mungu kwa njia yake mwenyewe, lakini watoto wote wanaathiriwa na mazingira. Hivyo, kama vile mtoto ananyenyekea kwa kanuni za kimaumbile ambazo Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amezilazimsha kwa ulimwengu na viumbe vyote, kwa njia hiyo hiyo roho yake inanyenyekea kwa kawaida kwa ile hakika kuwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) ndiye Mola wake Mlezi na Muumba Wake. Lakini, ikiwa wazazi wake watajaribu kumfanya afuate njia nyengine tofauti, kijana huwa si mwenye nguvu za kutosha katika mwanzo wa maisha yake kupingana na kwenda kinyume na matakwa ya wazazi wake. Katika hali hiyo, dini anayofuata mtoto ni ile ya kiada na malezi, na Mwenyezi Mungu Hamuhesabu au kumuadhibu kwa dini hiyo anayofuata mpaka anapofika kipindi cha miaka fulani katika maisha yake.

ISHARA NA MIUJIZA YA MWENYEZI MUNGU

Katika maisha ya wanaadamu wote, kutoka wakati wa ujana na utoto hadi wakati wanapofariki, ishara za Mwenyezi Mungu mmoja peke Yake wa kweli zinaonyeshwa kwao katika maeneo yote ya ardhi, hata katika nafsi zao mpaka ibainike kwao kuwa yupo Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli (Allah). Mwenyezi Mungu Anasema katika Qur'ani:

سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٥٣﴾

"Tutawaonyesha Ishara Zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?" (41: 53).

Hapa tunatoa mfano jinsi Mwenyezi Mungu Anavyompatia ishara mtu mmoja kwa upotevu kwa kuabudu masanamu. Katika eneo la kusini mashariki mwa msitu wa Amazon huko Brazil, Amerika Kusini, kabila la asili lisiostaarabika lilijenga kibanda kipya ili kumpatia makazi sanamu-mtu, Skwatch, likiwakilisha mungu mkubwa kabisa wa uumbaji wote. Siku ya pili kijana mmoja aliingia katika kibanda hicho ili kutoa heshima zake kwa mungu. Alipokuwa katika hali ya kusujudu kwa jinsi alivyofundishwa kuwa hilo sanamu ni muumba na mlezi wake, na mwenye kuruzuku, mara aliingia mbwa mzee, hafifu na mwenye upele na aliyejawa na viroboto kwenye kibanda hicho. Kijana huyo alinyanyua uso wake kwa wakati muafaka, wakati tu wakumuona mbwa huyo akinyanyua mguu wake wa nyuma na kulikojolea sanamu hilo. Kijana alimfukuza mbwa huyo katika hekalu kwa ghadhabu kubwa mno; lakini hasira na ghadhabu ilipofifia alitambua kuwa sanamu hawezi kuwa mola wake mlezi wa ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu ni lazima awe kila pahala, alihitimisha. Ajabu kama inavyoonekana, mbwa kulikojolea sanamu ilikuwa ni ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kijana huyo. Ishara hii ilikuwa na risala ya Mwenyezi Mungu kuwa anachokiabudu ni cha uwongo. Tukio hili lilimuacha huru kijana huyo na utumwa wa kufuata ada alizofundishwa za kuabudu mungu wa uwongo.

Matokeo yake ni kuwa huyu kijana alichaguzishwa: ama kutafuta mungu wa kweli au kuendelea katika upotevu wa njia zake.

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anatutajia kiu aliyokuwa nayo Nabii Ibraahim ('Alayhis Salaam) katika juhudi ya kumtafuta Mwenyezi Mungu kama mfano wa wale wenye kufuata ishara Zake jinsi wanavyoongoka (na hivyo kufuata njia nyoofu na ya sawa).

Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾ فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ الْآفِلِينَ ﴿٧٦﴾ فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ ﴿٧٧﴾ فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٧٨﴾ إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

"Na kadhaalika Tulimwonyesha Ibraahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na ulipomuingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipotua akasema: Siwapendi wanaotua. Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu waliopotea. Na alipoliona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipotua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayofanyia ushirikina. Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliyeziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina" (6: 75 - 79).

Kama ilivyotajwa hapo awali, Manabii walitumwa kwa kila taifa na kabila kuunga mkono itikadi ya kimaumbile ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa silica aliozaliwa nao mwanadamu wa kumuabudu Yeye, vile vile kutilia nguvu ukweli wa kutoka kwa mungu. Kwa ishara za kila siku zilizodhihirishwa na Mwenyezi Mungu. Japokuwa mafunzo mengi ya Manabii hawa yaligeuzwa, sehemu zinazoonyesha vifungu zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu zimebaki bila ya waa na zimewatumikia wanaadamu kuwaongoza katika kuchagua baina ya ukweli na uwongo, na haki na batili. Ushawishi wa risala zilizofunuliwa na Mwenyezi Mungu kupitia kwa zama zote zinaweza kuonekana katika "Amri Kumi" za Uyahudi katika Taurati ambazo baadaye zilichukuliwa na kuingizwa katika mafunzo ya Ukristo. Vile vile kuwepo kwa kanuni dhidi ya mauaji, wizi na uzinzi katika jamii nyingi sana kote duniani, katika zama za kale na sasa. Matokeo kwa ishara za Mwenyezi Mungu kwa wanaadamu kupitia kwa zama zote zikichang'anywa na wahyi Wake kupitia kwa Manabii Wake, wanaadamu wote wamepatiwa fursa ya kumtambua Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli. Kwa hiyo, kila nafsi itahesabiwa kwa itikadi yake kwa Mwenyezi Mungu na kukubali kwake kwa Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, ambayo ina maana ya kunyenyekea na kutii amri za Allah (Subhaanahu wa Ta'ala).

HITIMISHO

Maudhui zilizotangulia zinatuonyesha kuwa jina la Dini ya Uislamu, inaeleza msingi wa kati mno wa Uislamu kumnyenyekea na kumtii Mwenyezi Mungu. Ieleweke kuwa jina "Islaam" halikuchaguliwa na mwanadamu lakini na Mwenyezi Mungu kwa mujibu wa Kitabu kitukufu cha Uislamu. Pia imeonyeshwa kuwa Uislamu peke yake ndio unaofundisha sifa za Mwenyezi Mungu zisio na kifani na unahimiza kuabudiwa kwa Mwenyezi Mungu peke Yake bila ya kuwa na wenye kuwajongeza na kuwaleta karibu Naye. Mwisho, kwa sababu ya mwelekeo wa mwanadamu aliyopatiwa na Mwenyezi Mungu kumuabudu Yeye na ishara zilizoteremshwa na Mwenyezi Mungu kupitia miaka na zama kwa kila mtu binafsi, Uislamu unaweza kufikiwa na watu wote katika zama zote. Kwa muhtasari, umuhimu wa jina Uislamu (kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu), msingi wa Uislamu kukiri kwa ule upweke wa Mwenyezi Mungu na kufikiwa kwake na wanaadamu wote kwa zama zote. Haya yanadhibitisha dai la Uislamu kuwa kuanzia mwanzo wake, kwa lugha yoyote iliyotumiwa kuueleza, Uislamu peke yake ndio uliokuwa, na umebaki kuwa Dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu.

Kuhitimisha, tunamuomba Allah, Aliyetukuka, kutueka na kutubakisha katika njia nyoofu na ya sawa ambayo Ametuongoa nayo, na Utukirimu, Uturidhie na kutupatia rehema, kwani Wewe ni Mwingi wa Kurehemu. Sifa njema zote ni za Allah, Mola Mlezi wa viumbe vyote, sala na salamu zimfikie Mtume Muhammad (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam) na kwa Manabii wote wa Allah ('Alayhimus Salaam) na watangu wema.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU 1

MWANDISHI: DKT. ABU AMINA BILAAL PHILIPS 1

MFASIRI: MUHAMMAD AL-MAAWY 1

NI IPI DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU? 1

JINA LA DINI 2

MWENYEZI MUNGU NA UUMBAJI 3

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU 6

RISALA YA DINI ZA UWONGO 6

KILIMWENGU CHA DINI YA MWENYEZI MUNGU 7

KUMTAMBUA MWENYEZI MUNGU 8

ISHARA NA MIUJIZA YA MWENYEZI MUNGU 9

HITIMISHO 11

SHARTI YA KUCHAPA 11

MWISHO WA KITABU 11

YALIYOMO 12


[1] . Majina yote mawili "Jesus - Yesu" na "Christ - Kristo" yametokana na maneno ya Kiebrania, kupitia kwa Kiyunani na Kilatini. Jesus ni Kiingereza na pia kwa Kilatini (Yesu kwa Kiswahili), mfumo wake wa Kiyunani "Iesous", amabyo kwa Kiebrania ni "Yeshua" au "Yehoshua" (Joshua - Yoshua). Neno la Kiyunani "Christos" ni tafsiri ya neno "messiah" kwa Kiebrania, ambacho ni cheo kinachomaanisha "mpakwa mafuta".