• Anza
  • Iliyopita
  • 9 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 5118 / Pakua: 1990
Kiwango Kiwango Kiwango
MASOMO YA KI-ISLAMU 4

MASOMO YA KI-ISLAMU 4

Mwandishi:
Swahili

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

DIBAJI

Ewe Ndugu Yangu!

Je, wajua nani Mwislamu? Mwislamu ni ambaye anaamini kuwa Mwenyezi Mungu ni Mmoja na Muhammad ni Mtume wake wa mwisho. Kama ukiamini haya, basi wewe ni Mwislamu.

Lakini haitoshi kusema tu kuwa mimi ni Mwislamu; bali ni wajibu juu yako kutenda kwa mujibu wa kanuni za Ki-islamu, ili uwe Mwislamu wa ukweli, na uishi duniani katika raha, na upate utukufu Akhera[1] kwa kuingia peponi na kupata ridhaa za Mwenyezi Mungu.

Basi ni lazima juu yako kujitahidi kufanya hayo.

Na Uislamu una sehemu tatu:

(1) Asili (Mizizi) ya Dini

(2) Matawi ya Dini

(3) Tabia (Mwenendo) ya Dini

Basi anayekubali kwa ukweli Asili ya Dini, na kutumia Matawi ya dini, na akiishajipamba na tabia ya dini, basi yeye ni mbora duniani na akhera (Kiyama[2] .

Kitabu hiki Kimefasiriwa na Sheikh Muhammed Ali Ngongabure, na kimesahihishwa na kimepangwa na Ayatullah Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Muasisi na Muhubiri wa Bilal Muslim Mission of Tanzania.

Wabillahi Tawfiq.

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

SOMO LA KWANZA

TABIA NZURI

Akataja Mtume Mtukufu(s.a.w.w) lengo muhimu la utume wake. Na akasema hivi:

"Kwahakika nimetumwa tu kwa ajili ya kutimiza mwenendo mzuri."

Na hakika dini yote ni tabia nzuri; na Uislamu na sehemu zake zote (yaani ibada na mwenendo na maamuzi na hukumu zake zote) hukusanyika kati ya tabia nzuri.

Kama tulivyo eleza katika kitabu cha kwanza, Tabia nzuri ni sehemu muhimu ya Ki-Islamu. Katika sehemu hii ni mambo na matendo yanayopendeza kuyatenda. Na mambo na matendo yanayo pendeza kuyaacha.

Katika masomo yanayo fuata tutataja mambo na matendo matukufu ambayo baadhi yao ni wajibu juu ya kila Muislamu, na baadhi yao ni sunna.

SOMO LA PILI

MATENDO YALIYO FARADHI

(1) Kufanya amali njema kwa moyo wa bidii na unyoofu:

Mtukufu Mtume amesema:'Kwa hakika amali zote zinategemea nia zake ."

(2) Kutegemea Mwenyezi Mungu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na anayemtegemea Mwenyezi Mungu yeye humtoshea "........... (Qur'an Sura ya 65 aya ya3).

"Na tegemeeni kwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini ", (Qur'an Sura ya 5, aya ya23).

(3) Kutendeana Haki: (Kuto kudhulumiana).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Haikamiliki imani ya kiumbe hadi awe na sifa tatu, kutoa msaada wakati wa dhiki, usawa na unyoofu kati yake na mwenziwe, mwingi wa kutoa salamu ."

(4) Kuwatendea mema wazee wawili:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na Mola wako amehukumu kuwa msimwabudu yoyote ila yeye tu, na kuwafanyia wema wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee mbele yako. au wote wawili, basi usiwaambie hata Ah; Wala usiwakemee. na useme nao kwa msemo wa heshima kabisa. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme 'Molawangu! Warehemu (Wazee wangu) kwani walinilea katika utoto".

(5} Kuwaangalia jamaa wa damu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Mcheni Mwenyezi mungu ambaye kwaye mnaomba na (kuangalia) jamaa wa damu, hakika Mwenyezi Mungu ni mlinzi juu yenu ". (Qur'an Sura ya 4, aya ya 2).

(6) Kusaidiana mambo mema:

Mwenyezi Mungu katika Qur'an amesema: "Saidianeni katika wema na kumcha Mwenyezi Mungu, wala msisaidiane katika dhambi na maasi ." (Sura ya 5, aya ya 2).

(7) Kupatanisha watu:

Mwenyezi Mimgu amesema: "Basi mwogopeni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni katika wanao amini (kweli) ".(Sura ya 8, aya ya 1).

"Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu. na mcheni Mwenyezi Mungu, (msipuuze jambo la kupatanisha) ili mrehemiwe ." (Quran Sura ya 49, aya ya 10).

(8) Ukweli:

Mwenyezi Mungu amesema: "Kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale walio wa kweli na walio waongo ." (Sura ya 29, aya ya 3). "Mwenyezi Mungu ametuamrisha tuwe wakweli ". (Qur'an Sura ya 9, aya ya 119).

SOMO LATATU

MATENDO MATUKUFU (I)

(1) Kuwa na tabia nzuri:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hakika alio kamilika imani miongoni mwa walioamini ni yule mwenye tabia nzuri ".

(2) Kuwa na elimu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Kwa hakika wanaomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale wataalamu (wanavyuoni) ". (Quran Sura ya 35 aya ya 28).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kutafuta elimu {mwanafunzi} hupendwa na Mwenyezi Mungu, hupendwa na Malaika, hupendwa na Mitume, na wala hatapenda elimu ya dini isipokuwa yule mtu ambae ni mwema ."

(3) Ushujaa:

MtukufuMtume(s.a.w.w) amesema: "Hamfalii mwenye imani awe bahili wala mwoga ".

Mwenyezi Mungu anawasifu wenye imani katika Qur' an hivi:

'Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na walio pamoja nae ni wenye nyoyo thabiti {mashujaa} mbele ya makafiri ". (Qur'an Sura ya 48, aya ya 29).

(4) Unyenyekevu:

Mtume Mtukufu(s.a.w.w) amesema: "Kwa hakika unyenye kevu humzidishia kiumbe daraja na cheo kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo nyenyekeeni, Mwenyezi Mimgu atawahurumien i."

(5) Huruma na upole:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye Imani imechanganyika elimu yake na upole, kwani elimu bila kuwa na upole haina faida yoyote ".

(6) Kukaa vyema na watu:

Amesema Imam Jaffer As -Sadiq(a.s) : "Muislamu ni ndugu wa Muislamu, asimdhulumu, asimdanganye, asimtupe na kumuacha, asimsengenye, asimfanyie hiyana wala asimnyime ".

(6) Ukarimu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Yule anayetoa zaka, (Sadaka na mengineyo) na kumcha Mwenyezi Mungu na kusadiki mambo mema akafanya, Tutamrahisishia njia ya kwenda peponi . (Qur'an Sura ya 92 aya ya 6-7). Mtume(s.a.w.w) amesema "Mkarimu ni mpenzi wa Mungu na bahili adui wa Mungu ".

(7) Utawa:

Uzuilifu wa tamaa hasa wa kike na kiume

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kuzuwia tumbo lake na haramu, na utupu wake kwa haramu na ulimi wake na kila kilicho katazwa kusema, basi mtu huyo amejilinda kikweli kweli na mahala pake peponi ."

(8) Kuwasaidia wanyonge:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wamchao Mwenyezi Mungu ni ambao katika mali zao ni haki ya masikini aombaye na ujizuiaye kuomba ." (Qur'an, Sura ya 51 aya ya 19).

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

SURAYANNE

MATENDO MATUKUFU (II)

(10) Kutoa Salamu kwa kutangaza:

Kwa kutangaza maana yake ukitoa salamu toa kwa sauti hata isikike. usitoe kimya kimya hata waseme hukutoa salaamu.

(11) Kusubiri:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na wapashe habari njema wanaosubiri. Ambao uwapatapo msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na kwake yeye tutarejea. Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao na rehema; nao ndio wenye kuongoka . (Qur'an Sura ya 2 aya ya 156-157).

Mwenyezi Mungu amesema: "Na bila shaka wafanyao subira watapewa ujira wao pasipo hesabu ." (Qur'an Sura ya 39, aya ya 10).

(12) Kukirimu:

Kukirimu watu huleta baraka na huondoa maafa na balaa. Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Akifika mgeni kwa watu huja na riziki yake kutoka mbinguni na akila chakula Mwenyezi Mungu huwaghofiria wale watu aliowashukia ."

(13) Kusameheana:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na mkiwasamehe na kupuuza yaliyopita na kuyafuta kabisa katika nyoyo zenu basi Mwenyezi Mungu atafurahi kwani Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwingi wa rehema ." (Qur'an, Sura ya 64, ayaya 14).

(14) Kukidhi haja za watu:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kukidhi haja ya ndugu ye mwenye kuamini Muislamu basi kama amefanya ibada ya Mwenyezi Mungu maisha yake ."

(15) Kufanya usawa kwa kila kitu:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Unachopendelea kwa ajili ya nafsi yako, wapendelee wenzio pia. Fanya usawa kati ya wake zako kama unao wengi na kati ya wanao, wala usipendelee kabisa ."

Mwenyezi Mungu amesema:Lawama iko juu ya wale wanao dhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki. hao ndio watakao pata adhabu . (Qur'an, Sura ya 42 aya ya 42).

(16) Kumcha Mwenyezi Mungu:

Kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu na kuepukana na kila maasi yake yote. Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Amali chache na uchaji wa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko amali nyingi bila uchaji ."

(17) Usafi (Unadhifu):

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Unadhifu na usafi ni katika imani." Amesema Imam Ali Ar-Ridha(a.s) : "Kuwa nadhifu ni katika tabia na mienendo ya Mitume ."

(18) Kuwa na Haya:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Kuwa na haya ni katika imani ." Asiyekuwa na haya, akafanya atakavyo si Muislamu.

(19) Kuoa:

Kuoa ni sunna ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) .

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kuoa ameilinda nusu ya imani yake basi amche Mwenyezi Mungu kwa nusu iliyobakia .'

(20) Kuwa na (ukunjufu) furaha:

Mwenyezi Mungu amesema: "Basi kwa sababu ya rehema ya Mwenyezi Mungu umekuwa laini kwao, na kama ungekuwa mkali na mwenye moyo mgumu, bila shaka wangalikukimbia . (Qur' an, Sura ya 3 aya ya l59).

(21) Kuwaheshimu watu:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Waliokuwa watu wazima uwaheshimu kwa uzee wao, na walio wadogo wako uwaonee huruma na kuwapenda, na waliokuwa makamo yao watende kama upendavyo kutendewa nao ."

(22) Kumshukuru Mungu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na anayeshukuru, ana shukuru kwa manufaa ya nafsi yake kwa ajili yake tu, na anayekufuru, kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi Mkarimu. " (Qur'an Sura ya 4, aya ya 147).

Tena Mwenyezi Mungu amesema: "Kama mkishukuru nitakuzidishieni, na kama mkikufuru,jueni kuwa adhabuYangu nikali sana ." (Quran, Sura ya 14, aya ya 7).

SOMO LA TANO

MATENDO YALIYO HARAMU (1)

(1) Kuwaasi na kuwahalifu wazazi:

Katika hadithi tukufu, Mwenyezi Mungu amesema: "Naapa kwa utukufu na nguvu zangu kwamba mtu yeyote asiyewatii wazazi wake, hata akija kwangu na amali njema za mitume wote sitazikubali kamwe ."

(2) Kuzini:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wala msikaribie zina. Hakika hiyo ni uchafu mkubwa nani njia mbaya kabisa. " (Qur'an Sura ya 17, aya ya 32).

(3) Kufira:

"Na anayemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuiruka mipaka yake, Mwenyezi Mungu atamwingiza Motoni, humo atakaa milele, na atapata adhabu zifedheheshazo ." (Qur"an Sura ya 4 aya ya 14).

(4) Kusagana wanawake:

Hukumu yake ni kama hukumu ya kufirana, ni katika maasi makubwa yaliyo katazwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

(5) Kunywa ulevi:

Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mlio amini, bila shaka ulevi na kamari na masanamu ya kuabudu na mishale ya ramli ni uchafa wa kazi ya Shetani. Basi jiepusheni nayo, ili mpate kufaulu . (Qur'an Sura ya 5. aya ya 91).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Naapa kwa yule alio niteua na kunipa Utume, kwamba mlevi atakufa hali ana kiu, na kaburini anakiu, na atafufuliwa hali yeye anakiu na atakuwa anapiga kelele 'kiu kiu' kwa miaka elfu; ataletewa (kwa kiu kubwa iliomshika) maji ya shaba iliyoyayushwa itayounguza nyuso zao. Kinywaji kibaya kilioje hicho. Basi utaiva uso wake na kutoka meno yake na kuchopoka macho yake mule katika lile kaburi, na atakuwa hana budi kunywa na huyeyuka yalio tumboni mwake ."

(6) Kucheza Kamari:

Hukumu ni kama ulevi, na Mwenyzi Mungu ameyataja maasi haya yote mawili katika aya kama tuliyo eleza katika ulevi . (Qur'an, Sura ya 5 aya ya 91).

(7) Kula mizoga na nguruwe na vingine vilivyoharamishwa:

Mwenyezi Mungu amesema: "Yeye amekuharamishieni mizoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kisichotajiwa katika kuchinjwa kwake jina la Mwenyezi Mungu ." (Qur'an, Sura ya 2, aya ya 173).

(8) Kula mali za watu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mlio amini. Msiliane mali zenu kwa batili ispokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu {hiyo inajuzu} ." (Qur'an Sura ya 4 aya ya29).

(9) Kula (rushwa) mlungula:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na utawaona wengi katika wao wanakimbilia kwenye dhambi na uadui na ulaji wao wa haramu mlungula. Bila shaka wayafanyayo hayo ni mabaya kabisa ." (Qur'an Sura ya 5, aya ya 62).

Amesema Imam Ali(a.s.) : "Mwenyezi Mungu amemlaani mla (rushwa) mlungula, mtoa mlungula na yule mwenye kusababisha hayo ."

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

SOMO LA SITA

MATENDO YALIYO HARAMU (II)

(10) Kupoteza haki:

Hapa kuna maana nyingi, kuna haki za Mwenyezi Mungu, haki za Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na haki za Waislamu kwa wenzao. Zote hizo ukipoteza moja wapo ni dhambi.

(11) Kuiba:

Ni dhambi ambayo inajulikana pote ulimwenguni. Mwenyezi Mungu amesema: 'Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, malipo ya yale waliyo yachuma. Ndio adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu." (Qur'an Sura ya 5 aya ya38).

(12) Ukuwadi na kusaidia katika mambo ya ndoa hata kwa mke wake:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hataingia peponi wala hapati harufu ya peponi." Akaulizwa, "Ni nani huyo ?

Akasema, "Yule mume ambaye anajua vema kwamba mke wake analala na mwanamume mwingine (na haoni aibu).

(13) Kusema uwongo:

Ni haramu, dhambi kubwa sana. Amesema Imam Al-Baqir(a.s) : "Hakika Mwenyezi Mungu ameweka kwa kila shari {uovu} kufuli na ufunguo wa makufuli hayo ni ulevi, na uwongo ni ubaya zaidi kuliko ulevi ."

(14) Kuteta na kufitinisha:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wala baadhi yenu wasiwaseme wengine. Je! Mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa ?" (Qur'an, Sura ya 49 aya ya 12).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hataingia peponi mfitini (mwenye kutangaza maneno ya huyu kwa yule ili atie fitina na kuwagombanisha) ."

(15) Kula riba:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wale wanao kula riba................ wakasema, 'Biashara na ni kama riba.' Hali Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na kaiharamisha riba. " (Qur'an, Sura ya 2, aya ya 275).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenyezi Mungu amemlaani mla riba, mtoa riba, na mwandikaji wa riba na mshuhudiliaji hayo .''

(16) Kuua:

Mwenyezi Mungu amesema:'Na mwenye kumuua Muislamu kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu, humo atakaa milele, na Mwenyezi Mungu amemghadhibikia na amemlaani na amemwandalia adhabu kubwa. " (Qur'an Sura ya 4a ya ya 93).

(17) Hiyana:

Mwenyezi Mungu amesema: "Hakika, Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao hiyana . (Qur'an, Sura ya 8, aya ya 58).

(18) Dhuluma:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafirika na haya wanayoyafanya madhalimu. Hakika yeye anawaakhirisha tu mpaka siku ambayo macho yao yatakodolea yatoke nje kwa khofu ." (Qur'an, Sura ya 14 aya ya 42).

SOMO LA SABA

MATENDO YALIYO HARAMU (III)

(19) Kutumia kwa fujo:

Mwenyezi Mungu amesema: "Kuleni na kunyweni. Lakini msipite kiasi tu. Hakika yeye (Mwenyezi Mungu) hawapendi wapitao kiasi (wapindukiao mipaka) ." (Qur'an,Sura ya7 aya ya 31).

(20) Kudharau watu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mlio amini, Wanaume wasidharau wanaume wenzao, huenda wakawa bora kuliko wao, wala Wanawake wasiwadharau wanawake wenzao, huenda wakawa bora kuliko wao." (Qur'ani, Sura ya 49, aya ya 11).

(21) Kuwaudhi watu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na wale wanao waudhi wanaume Waislamu na wanawake Waislamu pasipo wao kufanya kosa lolote, bila shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri." (Qur'an, Sura ya 33 aya ya 58).

Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwislamu ni yule ambaye wamesalimika watu na vitimbi vya mkono na ulimi wake ."

(22) Kutoa siri:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mazungumzo kati ya watu wawili yaliyo zungumzwa ni amana; basi ukiyasema kwa watu huwa si mwaminifu. " Kwa hiyo kutoa siri ya mwenziwe ni dhambi kubwa (siri ina weza kuwa ni aibu ya mtu au ni jambo lingine, mradi yote ni siri).

(23) Kuficha bidhaa (chakula) ya mahitajio kwa kutaka kuuza kwa thamani kubwa:

Imepokewa hadithi tukufu ya Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mficha vyakula kalaaniwa na Mwenyezi Mungu ."

(24) Kuwatazama wanawake wasio halali na wanawe:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Tazama mtupo wajicho ni mshale wenye sumu katika mishale ya Shetani. Mwenye kuacha kutazama kwa kumuogopa Mwenyezi Mungu, Atampa Mwenyezi Mungu imani na atapata utamu wake moyoni mwake ."

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur' an: "Waammbie Waislamu wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyo katazwa) ...................Na waambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao ." (Qur'ani, Sura ya 24, aya ya 30).

(25) Kuhudhuria magomani na sinema za haramu:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amekataza kuhudhuria mahala popote patendwapo maasi na mambo yaliyo haramishwa. Katika sinema inakuwepo miziki, maneno na matendo ya aibu na matusi; na vitu hivi vimekatazwa sana katika Uislamu, kama ilivyoelezwa humu humu kitabuni.

(26) Kuimba na kusikiliza muziki:

Mtukufu Mtume(s.aw.w) amesema: "Mpiga zeze atafufuliwa siku ya Qiyama na uso wake hauna nuru, na mikononi mwake zeze la moto, na juu ya kichwa watakuwepo Malaika sabini elfu wa adhabu na mikononi kwa kila Malaika patakuwepo mundu wanampiga kichwani na usoni mwake, na atafufuliwa mwimbaji chongo, bubu, kiziwi, na mzinifu vivyo hivyo, na pia mwenye filimbi za zumari na mpiga dafu ."

SOMO LA NANE

MATENDO YALIYO HARAMU

(27) Kujitoa shahawa kwa mkono:

Ni haramu na dhambi, na pia huleta madhara mengi mwilini.

(28) Kuvunja ahadi:

Katika alama za imani, Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema; "Akitoa ahadi hutimiza, basi asiyetimza ahadi yake anatoka katika imani ."

(29) Kuvaa pete ya dhahabu na kujipamba wanaume kwa dhahabu:

Ni haramu kwa mwanaume kuvaa dhabhabu kwa kiasi chochote.

(30) Kuhadaa:

Kuficha aibu au ubaya wa kitu unachomuuzia mtu ni haramu.

(31) Kughushi:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hayuko nasi mwenye kumghushi Muislamu mwenziwe ."

(32) Kupekua (kupeleleza) mambo ya watu:

Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'an: "Enyi mlio amini; Jiepusheni sana na kuwadhania watu dhana mbaya, kwani kuwadhania watu dhana mbaya ni dhambi. Wala msipeleleze habari za watu ." (Qur'an, Sura ya 49 aya yal 2).

(33) Kutukana na kushutumu:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Kumtukana au kumshutumu mwenye imani mwenzio ni ufasiki ."

(34) Kenda utupu wanawake kama hali ya sasa:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na kaeni (enyi wanawake) majumbani mwenu wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za ujahili (ujinga,ukafiri). (Qur'an, Sura ya 33 aya ya 33).

(35) Kumsaidia mdhalimu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na saidianeni katika wema na utawa, wala msisaidiane katikadhambi na uasi. " (Qur'an, Sura ya 5 aya ya 3).

(36) Kuhukumu kinyume cha sheria ya Kiislamu:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri ." (Qur' an, Sura ya 5 aya ya 44).

"Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu basi hao ndio waasi ." (Qur'an, Sura ya 5 aya ya 47).

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

SOMO LA TISA

TABIAMBAYA (I)

(1) Tabia mbaya:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Tabia mbaya huharibu amali ya mtu kama siki inavyo haribu asali ."

(2) Ubahili:

Mwenyezi Mungu amesema: "Wala wasione wale ambao wanafanya ubahili katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubahili huko); La, ni vibaya kwao, Watafungwa kongwa za yale waliyofanyia ubahili siku ya Qiyama . (Qur'ani, Sura ya 3 aya ya 180).

(3) Husda:

Mwenyezi Mungu anasema: "Wala msitamani vile ambavyo Mwenyezi Mungu amewafadhili baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wanayo sehemu ya vile walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake; hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu . (Qur'an, Sura ya 4 aya ya 320.

Mwenyezi Mungu anasema: "Au wanawafanyia watu husda kwa yale Aliyowapa Mwenyezi Mungu kwa ukarimu wake? " (Qur'an, Sura ya 4 aya ya 54).

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Husuda hula (huangamiza) mema kama kuni invyoangamizwa na moto na kugeuka jivu ."

(4) Uwoga:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Haimfalii mwenye imani kuwa bahili wala kuwa mwoga ." Lakini kumwogopa Mwenyezi Mungu na kuacha maasi ni sifa nzuri mno.

(5) Kukosa hima:

Mtu kutokuwa na bidii na juhudi ni miongoni mwa wabaya, au kuwa na bidii katika mambo maovu yote haya ni maovu, na lazima uepukane nayo.

(6) Ukaidi na inadi:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kuwa na inadi na ukaidi moyoni mwake hata kidogo sana, basi Mwenyezi Mungu atamfuata mtu huyo na wale watu wa zama za ujahili (ukafiri kabla ya kuja Uislamu) ."

(7) Lipiza kisasi:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Naapa kwa yule mwenye roho yangu mikononi mwake, mambo matatu haya ni katika matukufu; Haikupungua mali kwa kutoa Sadaka kwa hivyo toeni Sadaka, wala hakujuta mwenye kumsamehe Lil-LLaahi alio mdhulumu ila Mwenyezi Mungu kamzidishia heshima yake siku ya Qiyama, na mwenye kuanza kuomba omba basi Mwenyezi Mungu humfungulia umasikini ."

Mwenyezi Mungu amesema: "Mkidhihirisha wema au mkificha au mkiyasamehe maovu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu. mwenye uwezo ." (Qur'an, Sura ya 4 aya ya 149).

(8) Kulalamika unapopata msiba:

Hii ni sifa mbaya kabisa; na kinyume chake ni kusubiri na kuvumilia; Mwenyezi Mungu atakupa jaza ya subira yako.

SOMO LA KUMI

TABIA MBAYA (II)

(9) Kutafakhari (kujiboresha):

Siku ya kuteka Maka Mtukufu Mtume(s.a.w.w) akapanda mimbari akasema:

"Enyi watu, Mwenyezi Mungu ameondoa kwenu ufahari {majivuno} wa ujahili na kujivuniana na ukoo; kwa hakika nyinyi nyote mnatokana na ADAM na ADAM anatokana na Udongo; mbora wenu ni yule mwenye kumcha Mungu ."

(10) Pupa:

Kuwa na pupa katika mambo mazuri ni sifa nzuri, lakini kuwa na pupa katika kula ni tabia mbaya mno na pia pupa katika kukusanya mali.

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Wenye pupa wawili hawashibi, mwenye pupa ya kujifunza elimu, na mwenye pupa ya kukusanya mali ."

(11) Haraka:

Upo usemi usemao: "Haraka haraka haina baraka ."

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Haraka hutokana na shetani na subira kwa Mwenyezi Mungu ."

(12) Uvivu:

Ni tabia mbaya; mvivu siku zote kwa uvivu wake hukosa mema mengi na siku zote huwataabuni.

Mwenyezi Mungu amesema: "Na ya kwamba mtu hatapata ila aliyoyafanyia juhudi ." {Qur'an, Sura ya 53 aya ya 39}.

(13) Kusema ovyo ovyo:

Mwenyezi Mungu amesema: "Hatoi kauli yoyote isipokuwa karibu naye yuko mngojeaji tayari (kuiandika) ." {Qur'an, Sura ya 50 aya ya l8}.

(14) Kusema upuuzi (yasiyo na maana):

Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'an tukufu kuhusu mambo ya Qiyama, watapoulizwa wahalifu (wafanyao maasi): "Nikipi kilichowapelekeni Motoni?" Watasema: Hatukuwa miongoni mwa waliosali, wala hatukuwa tukilisha masikini. Na tulikuwa tukipiga porojo pamoja na wapigao porojo." (Qur'an, Sura ya 74 aya ya 42-47).

(15) Kudharau:

Mwenye kujidharau kuwa dhalili na hana hima. Imam Jaffer As-Sadiq(a.s) amesema: "Hakika Mwenyezi Mungu amemwachilia mwenye imani mambo yake yote, lakini hakumwachia ajidhalilishe, kwani hukusoma Qur'an inasema ,'Nautukufu hasani wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na walio amini. ' (Qur' an, Sura ya 63 aya ya 8).

SOMO LA KUMI NA MOJA

TABIA MBAYA (II)

(16) Kiburi:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hataingia Peponi mwenye kuwa nao moyoni kiburi hata kikiwa kiasi cha punje cha hardali ."

Na Nabii Musa(a.s) akasema: "Hakika najikinga kwa Mola wangu na Mola wenu Anilinde na kila mwenye kiburi asiyeamini siku ya Hesabu ." (Qur'an, Sura ya 40 aya ya 27).

(17) Mghafala (kusahau sahau)

Ni tabia mbaya na huleta hasara kwako na kwa watu. Mwenyezi Mungu amewaonya katika Qur'ani wale ambao wanao tabia ya mghafala: "Na bila shaka tumewaumbia moto wa Jahannam wengi katika wanadamu na katika majini kwa sababu hii: 'Nyoyo wa nazo, lakini hawafahamu kwazo (Hawataki kufahamu kwazo), Na macho wanayo lakini hawaoni kwayo, na maskio wanayo lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama; bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika. " (Qur'an, Sura ya 7 aya ya 179).

(18) Ufedhuli na ujuvi (kutokuwa na haya):

Mtu kama anayo tabia mbaya kama hii hupatikana na misukosuko mingi, kwani hajali analolisema, wala hajali anae mfanyia ufedhuli huo na matokeo yake ni mabaya sana.

(19) Kuwa na wasiwasi mwingi:

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) amesema: "Wasiwasi hutokana na Shetani ."

Mwenyezi Mungu amesema katika Qur'ani "Sema Najilinda na shari ya wasiwasi, shetani, aendaye kisirisiri kwa hila, atiaye wasiwasi katika mioyo ya watu ." (Qur'an Sura ya 114, aya ya 5 na 6).

( 20) Uchafu:

Mtukufu Mtume(s.aw.w) amesema: "Msikae wachafu bali muwe nadhifu, kwani unadhifu ni katika imani ."

(21) Kukosa huruma:

Mwenyezi Mungu katika mazungumzo na Mtume Musa(a.s) akamwambia, "Mwenye kuwa na moyo mgumu (kukosa huruma) ni yumbali nami ."

(22) Ulaghai:

Mwenyezi Mungu amesema: "Na maisha ya dunia hii si kitu ila ni starehe idanganyayo ." (Qur'an, Sura ya 3 aya yal 85).

''Bila shaka ahadi ya Mwenyezi Mungu ni haki, basi yasikulaghaini maisha ya dunia hii, wala asikudanganyeni mdanganyifu mkubwa {Ibilisi}, katika (mambo ya) Mwenyezi Mungu ." (Qur'an, Sura ya 31 aya ya 33).

(23) Kusimbulia:

Mwenyezi Mungu amesema: "Enyi mlio amini Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia ." (Qur' an, Sura ya 2 aya ya 264).

"Kauli njema na kumsamehe anayekukosea ni bora kuliko sadaka inayofuatishwa na udhia (masimbulizi) ." (Qur'an, Sura ya 2 aya ya 263).

MASOMO YA KI-ISLAMU

KITABU CHA NNE

SOMO LA KUMI NA MBILI

ADABU YA KUAMKIANA

Uislamu unawafundisha wafuasi wake kila njia ya kheri, udugu na kupendana kujuana kwa hali na kusaidiana na kuondoa kila ovu na kila baya baina yao.

Basi leo ndugu zanguni, nitakuleteeni adabu njema katika sheria ya kiislamu, nazo ni sheria za Waislamu, kuamkiana ili wapendane. Anaye amkia, huvunja majivuno (kiburi) ambayo ni tabia mbaya kabisa nayo humtia mtu motoni, (Jahannam) anayeitikia maamkio, anamtukuza mwenziwe, humfanya bora kuliko yeye, na wote wawili hupata kheri kubwa, (Thawabu) Mtume wetu Muhammad(s.a.w.w) amesema hivi:

Hapana zawadi bora kwa Mwislamu kumpelekea nduguye. ila kumpa neno la maarifa ambalo litamzidishia mafanikio mema na litalo mzuia kufanya maovu .

Kama nilivyoeleza, ikiwa hatuna tabia ya kuamkiana, na tuwe na hamu ya kuanza tabia hii bora na tupeane mikono na kuulizana hali, kama alivyosema Mtume wetu, Muhammad(s.a.w.w) hivi:

Bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume watu Muhammad(s.a.w.w) aliwataka Masahaba wake wawe na sifa saba kama hizi zifuatazo:

1. Kwenda kuwatazama wagonjwa.

2. Kushiriki kwa kufuata jeneza la maiti, (Tashyiy-il Janaaza).

3. Atayeapa, kuthibitisha maneno yake akubaliwe.

4. Anayekwenda chafya aombewe kheri kwa Mwenyezi Mungu.

5. Aliyedhulumiwa avushwe na asaidiwe.

6. Anayemkuta yeyote amwamkie.

7. Anapoalikwa akubali, (ila maaliko yasiyofuata sheri ya Ki-Islamu).

Hadithi ya pili kweli (Sahii) kuwa Mtume wetu Muhammad(s.a.w.w) kasema hivi:

Peponi kuna majumba yanayoweza kuonekana ndani na nje (Transparent) katika majumba haya watawekwa wale katika wafuasi wangu wenye tabia hizi:

1.Anapozungumza na watu, huzungumza kwa adabu na heshima.

2.Anatabia ya kulisha (ukarimu) watu.

3. Huamkia kwa sauti (hutoa salamu kwa sauti).

4.Humuabudu Mwenyezi Mungu (husali) wakati wa usiku ambao watu wamelala.

Baadae kasema; kuamkia kwa sauti ni makusudio ili Muislamu yoyote asiwe bakhili kuamkia Mwislamu mwenziwe.

Imamu wa sita Hazarat (Bwana) Ja'far bin Muhammad Sadiq(a.s) amesema hivi: Moja katika alama za unyenyekevu wa Muislamu ni yeyote anayekuja usoni mwake humwamkia (kwa sauti).

Amesema Mtume wetu, Muhammad(s.a.w.w) hivi: Mtu yoyote. kabla ya kuamkia (kukupa salaam) akizungumza nawe usimjibu.

Anayekuja kwako bila ya kukuamkia {kukupa Salaamu} usimkaribishe chakula. mpaka aamkie.

Asiyeweza kufanya lolote kabisa {mvivu} ni yule mtu asiyeweza kumwomba Mwenyezi Mungu (Kuomba Duaa).

Kuliko wote bakhili ni yule asieamkia (Kutoa Salaam)

Mtu yoyote anapoondoka katika baraza yoyote {Majlis} na akaaga kwa kutoa salaam, baadae walio bakia wakizungumza lolote la kheri, yeye hupata sehemu ya thawabu, na kama watazungumza la shari, yeye hato kuwamo katika dhambi zao.

Tumekwishaeleza na kutoa hadithi za Mtume wetu, Muhammad(s.aw.w) na ya ImamJa-afar Sadiq(a.s) namna za faida zitazopatikana kwa kuamkiana (kutoa Salaam) katika dini ya Ki-Islamu; sasa tutazame Qur an, Mwenyezi Mungu kasema hivi:

Mtapo amkiwa mjibu kwa ubora au mjibu kama mlivyo amkiwa.

Kwa mfano, mtapo amkiwa hivi:

Amesema Mtume wetu, Muhammad (s.a.w.w) hivi:

Atakaye kuamkia (Assalaamu Alaykum Warah Matullahi wa Barakaatuhu) ataandikiwa thawabu thalathini.

SOMO LA KUMINA TATU

ADABU YA KI-ISLAMU JUU YA KULA

Ukila, kula kwa unyenyekevu kama alivyo mtumwa. Chukua tonge dogodogo, utafune vizuri ndipo uimeze. Usile chakula cha moto, wala usipulize kwa mdomo, bali ukiwa una haraka upepee ndipo ule, au ukiweke mpaka kipoe.

Unapokula usimtazame usoni mwenzio unavyokula. Ukila usile kwa kasoro ya kutumia vidole vitatu. Chukua tonge kwenye chombo kilicho mbele yako wala usinyoshe mkono kuchukua kitu kilichopo mbele yamwenzio.

Ukila uanzie kwa kula chumvi kabla ya kitu chochote. na ukisha kula kabisa mwishoni, umalizie kwa chumvi. Kwa kufanya hivyo, utaepukana na namna sabini na mbili za maradhi, miongoni mwao, wazimu, ukoma, mabalanga na maumivu ya koo, meno na tumbo; kama ilivyosema hadithi ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Ukila, kula kwa mkono wa kulia, na unapoanza kula sema, Bismi llaahi, na kila ukimeza tonge sema Alhamdu - Li-Llaahi.

Imepokewa hadithi kutokana na Imam wa pili, Al -Hassan Bin Ali(a.s) kwamba amesema, "Zipo adabu ambazo ni wajibu kwa kila Muislamu kuzijua anapokaa kwenye meza ya chakula.Nne katika hizo ni faradhi. Nazo ni:

(a na b) Kumjua na kuridhia aliyekujaalia hiyo rizki naye ni Mwenyezi Mungu.

(c) Kusema Bismi Lahi, unapoanza kula.

(d) Kumshukuru Mola kukupa siha kuweza kula chakula hicho.

Nne nyingine ni Sunna, nazo ni:

(a) Kuosha mkono kabla ya kula na baada ya kula.

(b) Kaa na uegemee kushoto.

(c) Tafuna kwa uzuri na ilainike.

(d) Usimtazame mwenzio usoni.

Imepokewa hadithi iliyotokana na Imamu wetu wa kwanza Sayyidna Ali bin Abi Talib(a.s) kumwambia mwanawe Imam wetu wa pili Al -Hassan(a.s) hivi: Unataka nikufundishe tabia nzuri nne ambazo ukizifuata hutahitajia kwenda kwa tabibu? Akajibu ndio, ewe Ameerul -Mumineen. Akasema:

(l) Usikae kwenye meza ya chakula ikiwa huoni njaa

(2) Ondoka mezani kabla ya kushiba (iwe bado waweza kula)

(3) Tafuna sana mpaka kilainike

(4) Kabla ya kula kwanza nenda haja (chooni).

Ni sunna ukiosha mkono kabla ya kula, usifute mkono {kama wafanya vyo wengi) bali ule vivyo hivyo mkono umaji. Ukifanya hivyo huingia baraka katika chakula, na ukiosha baada ya kula ni sunna, kabla ya kufuta, upake usoni na machoni. na ukifanya hivyo utaepukana na ugonjwa wa macho na ukisoma dua hii pia ni vizuri sana:

Al - Hamdu Lil - Laahil - Ladhii Hadaanaa Wa At-Amanaawasaqaa-Naa, Wa Kul- Lu Balaa - In Saa - Lihin Aw - Laa - Naa.