MWENGE WA UKWELI

MWENGE WA UKWELI0%

MWENGE WA UKWELI Mwandishi:
: L.W Hamisi kitumboy
Kundi: Imam Saadiq (a.s(

  • Anza
  • Iliyopita
  • 3 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 1786 / Pakua: 1481
Kiwango Kiwango Kiwango
MWENGE WA UKWELI

MWENGE WA UKWELI

Mwandishi:
Swahili

MWENGE WA UKWELI

Mwenge wa Ukweli

Imamu Jaafar al-Sadiq a.s

Kimetungwa Na:

Maulana Sayyid 'Ali Naqi Saheb

Kimetafsiriwa Na:

Bwana L W Hamisi Kitumboy

Kimetolewa na kuchapishwa na:

Bilal Muslim Mission of Tanzania

PO Box 20033

Dar es Salaam

Tanzania

Mwenyezi Mungu Anasema:(Ewe mwanadamu! Ikumbuke) siku Tutakapowaita kila watu pamoja na Imamu wao; basi atakayepewa kitabu (chake cha Amali) kwa mkono wa kulia, hao watavisoma vitabu vyao (kwa furaha)

(Banii Israeil, 17:71)

Mtukufu Mtume(s.aw.w) Amesema:"Ye yote yule afaye pasi na kumjua Imamu wa zama zake, atakuwa kafa kifo cha ujinga."

Mtukufu Mtume (s.a.w.w) Amesema:"Hao (Ulul Amr watajwao mwenye Qur'ani 4:59) ni Mak-halifa wangu na Maimamu wa Waislamu baada yangu. Wa kwanza ni Ali, kisha ni Hassan, kisha ni Husayn, kisha ni Ali bin Husayn, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Jaafar bin Muhammad, kisha ni Musa bin Jaafar, kisha ni Ali bin Musa, kisha ni Muhammad bin Ali, kisha ni Ali bin Muhammad, kisha ni Hassan bin Ali, kisha ni Muhammad bin Hassan (Mahdi)" ("Kifayatul Athar" na "Rawdhatul Ahbab", vya Hafidh Jamaluddin Muha ddith).

SHUKRANI

Kitabu hiki kiliandikwa kwa lugha ya Urdu na Mtukufu Saiyadul Ulama Maulana Sayyid Ali Naqi Saheb, Mujtahidi wa Chuo Kikuu cha Lucknow, Uhindi. Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na Sayyid Hashim Raza Rizvi, B.A., B.T., Yadgr-e-Husaini H.S. School, Allahabad, Uhindi na kutolewa na Imamia Mission, Lucknow, U.P., Uhindi.

Kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili kutoka hiyo tafsiri ya Kiingereza na Marehemu l. W. Hamisi Kitumboy aliyekuwa (Mubalighi Mkaguzi, wetu) na kikachekiwa na kusahihishwa na Mwalimu Dhikiri (Zakir Ali) U.M. Kiondo, Edita wa "Sauti ya Bilal"

UTANGULIZI

Njia ya Ukweli ambayo Mtukufu Mtume wa Uislamu(s.a.w.w) amewaonyesha wanadamu kwa muda mrefu ilikuwa chini ya wingu kwa ajili ya udhalimu wa watawala wale waliojifanya kuwa warithi wake (Mtume s.a.w.w) na kwa sababu ya maisha ya kujitenga yaliokiishi wale warithi wake wa kweli. Ni katika wakati wa mrithi wa sita wa haki wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) ambapo mafundisho yake waliletwa tena katika asili yake sahihi.

JINA NA NASABA

Mrithi huyu wa Mtume(s.a.w.w) aliyekuwa wa sita katika mfululizo wa warithi wake wa haki aliitwa Jaafar, kunyat (jina la utoto) lilikuwa Abu Abdallah. Jina lake la heshima linalojulikana sana ni As-Sadiq. Alikuwa mtoto wa lmamu Muhammad Baqir(a.s.) , mjukuu wa Imamu Ali Zainul Abidiin na kitukuu cha Imamu Husayn(a.s.) . Mama yake alikuwa akiitwa Ummi Farwah, binti wa Bwana Qasim bin Muhammad bin Abu Bakr. Bwana Qasim alikuwa mmoja wa watu saba wenye elimu ya juu zaidi ya Fiqah (Sheria za Kiislamu) wa mjini Madina.

KUZALIWA KWAKE

Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) alizaliwa mnamo tarehe 17 Rabi-ul-Awwal (mfunguo Sita)katika mwaka wa 83 Hijiriya, wakati wa uhai wa babu yake Imamu Zainul Abidiin(a.s.) . Wakati huo baba yake alikuwa na umri wa miaka ishirini na sita. Kama kawaida kuzaliwa kwake kuliwafurahisha sana watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w).

KULELEWA KWAKE

Aliishi chini ya malezi ya babu yake Imamu Zainul Abidiin(a.s) kwa muda wa miaka kumi na miwili, ambaye kila mara alimwona akishughulika na sala au akimuombolezea lmamu Husayn(a.s.) . Ni miaka ishirini na miwili tu iliyopita tangu masaibu ya Karbala yatokee na bado muda huo hauonekani kwake kuwa ni zaidi ya siku moja ukilinganisha na upya wa fikara zilizomo akilini mwa Imamu as-Sadiq(a.s,) kuhusu tukio Ia Karbala. Imamu as-Sadiq(a.s.) alifungukwa na macho katika mazingara yaliyokuwa yakiungua kwa kuwaombolezea mashahidi wa Karbala na alipofahamu kuwa baba yake, Imamu Muhammad Baqir(a.s.) alikuwepo katika masaibu ya Karbala akiwa mtoto mdogo, bila shaka Imamu Jaafar as- Sadiq(a.s.) mwenyewe aliweza kuhisi kule kutokuwepo kwake huko Karbala. Hivyo maishani mwake mwote alifanya juhudi kuhifadhi kumbukumbu ya Imamu Husayn(a.s.) kubakia kuwa mpya miongoni mwa watu siku zote.

Baada ya kifo cha babu yake Imamu Zainul Abidiin(a.s.) , aliishi chini ya ulinzi wa baba yake kwa muda wa miaka kumi na tisa. Ulikuwa muda ambao ujanja wa Bani Umayyah ulikuwa ukishindwa kufaulu na watu walianza kumwelekea Imamu Muhammad Baqir(a.s.) ili kujifunza Uislamu wa kweli. Kila mara Imamu Jaafar as-Sadiq aliandamana na baba yake awapo nyumbani au safarini. Mfalme Hisham bin Abdul Malik, alipomwita Imamu Muhammad Baqir(a.s.) , Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) alikwenda pamoja naye.

UIMAMU WAKE

Imamu Jaafar As-Sadiq(a.s.) alikuwa Imamu katika mwaka 114 Hijiriya wakati baba yake, Imamu Muhammad Baqir(a.s.) alipofariki. Wakati huo mfalme alikuwa Hisham bin Abdul Malik aliyekuwa na makao yake makuu mjini Dameski (Shamu). Fujo za kisiasa zilikuwa zimejaa kila mahali katika milki yake. Dhuluma za watu wa ukoo wa Bani Umayyah zilikuwa zikijenga fikara mbaya miongoni mwa watu dhidi yao, na watu walikuwa wakingojea uwezekano wa kuwapindua. Wengi wa watu wa ukoo wa Bani Fatimah walipenda kushirikiana na watu. Mmoja wao ambaye alijitokeza sana katika jambo hilo alikuwa Bwana Zaid Shahid(a.s.) ambaye alikuwa mtoto wa Imamu Zainul Abidiin(a.s.) . Bwana huyu alijulikana sana kwa Uchamungu na huruma na alikuwa Hafidh (mtu aliyekariri) Qur'ani wa daraja la kwanza.

Wakati huu ulikuwa mbaya sana kwa Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) . Katika fikara za chuki juu ya dhuluma za watu wa ukoo wa Bani Umayya alikuwa pamoja na Bwana Zaid, ambaye alikuwa ami wake aliyemheshimu sana lakini alifahamu wazi kuwa majaribio ya Bwana Zaidi ya kutaka kuwapindua watu wa ukoo wa Bani Umayya yatashindwa, akijua wazi kuhusika kwake na maisha ya Zaid, hivyo Imamu Jaafar As-Sadiq(a.s.) alijaribu kumshauri Bwana huyu aachilie mbali jambo hilo. Lakini Bwana Zaid alipoona kuwa watu wa Iraq wengi walikuwa pamoja naye, alikuwa na mategemeo makubwa ya kushinda. Bwana Zaid alikufa kishahidi mnamo mwaka wa 120 Hijiriya baada ya kupigana kishujaa kwa muda wa siku tatu. Aliuawa na jeshi la watu wa ukoo wa Bani Umayyah, alikatwa kichwa na kikapelekwa kwa Hisham, mwili wake ukasulubiwa katika lango la inji wa Kufa na aliachwa hapo kwa siku kadhaa.

Mwaka mmoja baada ya kuuawa kwa Bwana Zaid, Bwana Yahya mwanawe Zaid alifanyiwa hayo hayo. Bila shaka matukio haya yalimuathiri sana Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.), lakini aliutangazia Ujumbe Mtakatifu kimya kimya.

KUANGUKA KWA SERIKALI YA BANI UMAYYAH

Miaka ya mwishoni ya utawala wa ukoo wa Bani Umayyah ulikuwa na mabadiliko mengi kwa ajili ya fitina zisizomalizika ambazo zilikuwa jambo la kawaida wakati huo. Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) aliona utawala wa Hisham bin Abdul Malik, Walid bin Yazid bin Abdul Malik, Yazid bin Walid bin Abdul Malik, Ibrahim bin Walid bin Abdul Malik na mwishoni Marwan al-Himar ambaye utawala wa ukoo wa Bani Umayyah uljishilizia kwake.

Wakati serikali yoyote ile inapoanguka, makundi yote yale yaliyokumbwa na udhalimu wake hujaribu kuamka mara moja na kuiangusha, mara moja wote kwa pamoja. Na viwango vya upole hupitwa. Ni wale tu waliozishinda fujo za hisia zao ambao huthubutu kuvijali viwango hivyo.

Watu wa ukoo wa Bani Hashim (ukoo wa Mtume(s.a.w.w) walikuwa wakipatwa na mishtuko mikubwa katika muda huu. Ukoo wa Bani Abbas waliodai kuwa walikuwa wakipigana kwa ajili ya Bani Fatimah ambao walikuwa wana wa ndugu yao walipata nafasi ya kuwatumia watu wasiotosheka ambao waliokuwa tayari kufanya jambo lolote lile waambiwalo.

Katika miaka ya mwisho mwisho ya utawa la wa Bani Umayyah, watu wa ukoo wa Bani Abbas waliendesha kikundi cha siri kilichoapa kuchukua utawala kutoka kwa ukoo wa Bani Umayyah na kuwapa watu wa Bani Hashim ambao walisema kuwa ulikuwa haki yao. Lakini hao Bani Hashim ambao serikali hii ilikuwa haki yao ni wale viongozi wa wanadamu walioteuliwa na Mwenyezi Mungu waliozishinda ghasia za hisia na ambao hawakufikiria kuzitumia nafasi hizo. Kunyamaza kwa viongozi hawa walioteuliwa na Mwenyezi Mungu pamoja na huruma walizokuwa nazo watu kwa watu wa ukoo wa Bani Hasham, viliwafanya watu kutumiwa na watu wa ukoo wa Bani Abbas kujinyakulia serikali. Na mara baada ya kuinyakuwa serikali hiyo, Bani Abbas walionekana mbele ya Bani Hashim (watu ambao jina yao walilitumia kwa faida yao wenyewe), kuwa ni wabaya kuliko watu wa ukoo wa Bani Umayyah.

Mtu wa kwanza wa ukoo wa Bani Abbas kuanzisha propaganda dhidi ya ukoo wa Bani Umayah alikuwa Muhammad bin Ali bin Abdallah bin Abbas. Alituma watu nchini Iran kwenda kupokea "Bai'at" (kiapo cha utii) kwa watu wa ukoo wa Bani Hashim kutoka kwa watu wa nchi hiyo. Mtu huyu alirithiwa katika kazi hii na mwanawe aitwaye Ibrahim. Mwishilizo wa kimasaibu wa Bwana Zaid na mwanawe Yahya uliongezea hisia za watu dhidi ya ukoo wa Bani Umayyah na hisia hizi pia zilitumiwa na watu wa ukoo wa Bani Abbas na walizidisha umaarufu wao nchini Iraq kupitia kwa mtu mmoja aliyeitwa Abu Salmah. Pole pole watu wa Iraq ya Mashariki waliingia mikononi mwao kwa kupitia mikono ya mtu mwingine aliyeitwa Abu Muslim Khurasani. Ilimbidi Gavana wa Serikali ya ukoo wa Bani Umayyah nchini Iran akimbie ili kusalimisha maisha yake, na tangu mwaka 129 Hijiriya majina ya watawala wa ukoo wa Bani Umayyah yaliondolewa katika hotuba za kawaida na jina la Ibrahim liliwekwa mahala pao.

Bani Umayyah walidhania kuwa ilikuwa ni serikali ya kienyeji iliyohusu Iran tu, lakini walipogundua kuwa ilishawishiwa na Ibrahim, aliyeishi mjini Jabalqa, Ibrahim alikamatwa na kukatwa kichwa alipokuwa gerezani. Jamii yake iliyobakia na watu wengine wa Bani Abbas walikwenda kuishi na Abu Salamah nchini Iraq. Abu Muslim Khurasani alipopata habari hizi alipeleka jeshi huko Iraq ambalo liliwaondoa Bani Umayyah wote, kutoka Iraq.

Abu Salamah aliyejulikana kwa jina la "Wazir-i-ali-Muhammad" (Waziri wa Dhuria wa Muhammad) aliandika barua chache kwa baadhi ya watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , akiwemo Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) lakini Imamu alizichoma barua hizo.

Wafuasi wa Abu Muslim Khurasani na wafuasi wa Ukoo wa Bani Abbas walikula kiapo cha utii kwa Abdallah al-Saffah mjini Kufa, mnamo tarehe 14 ya mwezi wa Rabi ul-Thani (Mfunguo Saba) mwaka 132 Hijiriya na walimkubali kuwa mtawala wa Dola ya Kiislamu. Baada ya Bani Abbas kuichukua kabisa lraq, waliishambulia Damaski. Mfalme Marwan (wa ukoo wa Bani Umayyah) aliwakabili akiwa na jeshi kubwa kabisa ambalo mara moja lilishindwa na ilimbidi Marwan kukimbia ili kusalimisha maisha yake, lakini alikamatwa na kuuawa Barani Afrika. Kisha Saffah aliamrisha kuuawa kwa watu wa ukoo wa Bani Umayyah po pote wakutwapo, akachimbua makaburi ya watawala wengi wa ukoo wa Bani Umayyah na akazitendea maiti zao kama ambavyo wangelitendewa walipokuwa hai.

Mnamo mwaka 136 Hijiriya Abdullah Al-Saffah alifariki na alifuatiwa na nduguye Abu Jaafar Mansur ajulikanaye sana kwa jina la Mansur Dawaniqi (Mansur Bahili).

DHULUMA JUU YA BANI FATIMAH

Mara tu baada ya ukoo wa Bani Abbas kujinyakulia utawala kwa kuwaghilibu watu kuwafanya waamini kuwa walikuwa wakiwasaidia watu wa ukoo wa Bani Fatimah (Dhuria wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) , walihofia watu wasigundue kuwa ni lazima Ukhalifa uende kwa Bani Fatimah. Kwanza kabisa walimgeukia Abu Salmah mtu aliyejulikana sana kwa kuwaheshimu kwake Bani Fatimah, na ambaye Bani Abbas walimfikiria kuwa ni lazima aondoshewe mbali kabla ya kuanzishwa kwa ghasia zozote zile za kuwasaidia Bani Fatimah ambazo angeliweza kuziunga mkono. Hivyo, licha ya yale yote aliyowatendea Bani Abbas, Abu Salmah alikumbwa na dhuluma zao na mwishowe alikatwa kichwa katika zama za utawala wa Saffah mwenyewe. Nchini Iran umaarufu wa Abu Muslim Khurasani ulikuwa chanzo cha hatari kwa utawala wa Bani Abbas, na Mansur alimuua mtu huyu kwa njia ya kijanja sana.

Sasa hali ikawa nzuri kwa Mansur na isiyokuwa na shaka yo yote kutoka kwa mwanasiasa maarufu ye yote aliye dhidi yake na hivyo wakazielekeza dhuluma zao kwa Bani Fatimah. Maulana Shibli ameandika katika kitabu chake kiitwacho "Sirat-Nu'man" kuwa, "Mansur alianza kuwatesa vikali Bani Fatimah bila ya sababu yo yote ile nyingine ila ubadhilifu wake na dhana mbaya juu yao. Wale waliokuwa mashuhuri zaidi miongoni mwao waliteswa zaidi. Muhammad bin Ibrahim aliyejulikana kwa jina Ia "Dibaj" kwa ajili ya sura yake nzuri sana aliwekwa juu ya ukuta na kisha ukuta huo ukajengwa juu yake. Moyo mgumu kama jiwe ndio unaohitajika kwa kuweza kuielezea hadithi hii ya ukatili."

Imamu aliathiriwa sana na matukio haya. Wakati Dhuria wa Imamu Hasan(a.s.) walipochukuliwa kutoka Madina huku wakiwa wamefungwa minyororo, Imamu(a.s.) alikuwa akilitazama tukio hili kutoka nyuma ya nyumba na akawalilia akisema, "Ole! Hata Makka na Madina haiwezi kuwa sehemu za kukimbilia". Kisha alizieleza huzuni zake juu ya kunyamaza kwa wana wa Maansari waliomkaribisha Mtume(s.a.w.w) kuja Madina kwa kumwahidi kuwa watamhifadhi yeye na jamii yake kama vile watakavyoweza kuzihifadhi jamii zao wenyewe, lakini hawa watu waliokumbwa na dhuluma za Bani Abbas hawakusaidiwa na mtu ye yote yule miongoni mwao. Baada ya hayo alirudi nyumbani kwake na aliugua sana kwa muda wa siku ishirini.

Mmoja wa wafungwa hao alikuwa Bwana Abdallah, Bwana Muhammad aliyejulikana sana kwa jina la "Nafs Zakiyyah" "(Roho safi) aliamka kuipinga serikali na alikufa kishahidi mnamo mwaka wa145 Hijiriya karibu na Madina. Kichwa chake kilikatwa na kupelekewa baba yake aliyekuwa mzee na aliyekuwa kifungoni. Baba yake alipokiona kichwa cha mwanawe hakuweza kuuvumilia mshtuko alioupata na akafariki. Baada ya hapo mwana mwingine wa Bwana Abdallah aliyeitwa Ibrahimu alikufa kishahidi alipokuwa akipigana na jeshi la Mansur mjini Kufa, Vivyo hivyo Mabwana Abbas bin Hassan, Umar bin Hasan, Musanna, Ali na Abdallah wana wa Bwana Nafs Zakiyyah, Musa na Yahya ndugu wa Bwana Nafs Zakiyyah, nao pia waliuawa kikatili sana na bila ya huruma. Wengi wa watu wa ukoo wa Bani Fatimah waliwekwa katika kuta na kisha kuta hizo zikajengwa juu yao.

IMAMU ADHULUMIWA

Licha ya hali hizi mbaya ambazo chache zao tu zimetajwa hapo juu, Imamu aliendelea kuutangazia Ujumbe wa Ulslamu wa kweli kwa amani. Kwa kawaida hata wale ambao hawakukitambua cheo cha Imamu(a.s.) au hawakupenda kukitambua walikuja kusoma kwake, kwa sababu walijua kuwa ndiye mtu pekee aliyeweza kuwatosheleza kielimu.

Kwanza kabisa, Mansur, ili kuizuia heshima aliyokuwa nayo lmamu machoni pa watu, alimuwekea wapinzani wa mafundisho yake kutoka watu ambao hawakuweza hata kushindana na wanafunzi wa Imamu(a.s.) na ambao walikuball kuwa walipata elimu yao hiyo kutoka kwake. Lakini serikali iliwatambua rasmi kuwa wao ndio watoaji wa sheria za kidini. Hata hivyo majaribio haya yalishindwa. Hapo Mansur alijaribu kumtia kizuizini na kumwua na au kuwatia msukosuko wafuasi wake. Alipeleka majasusi kila mahali ili kumkamata na kumtia kizuizini mtu ye yote yule aonekanaye akimpendelea Imamu.

Bwana Mu'alla bin Knunais alikuwa mmoja wa wale waliotiwa kizuizini na kuuawa kikatili sana. Imamu(a.s.) mwenyewe aliitwa kutoka Madina kwenda kortini huko lraq karibu mara tano jambo ambalo lilisababisha mateso makali ya kimwili na kiakili kwake. Lakini mdhalimu huyo hakupata sababu yoyote ya kumfunga au kumwulia Imamu(a.s.). Kwa upande mwingine alipoona kuwa kukaa kwa Imamu(a.s.) nchini Iraq kuliongezea umaarufu wake. Alimuamuru arudi Madina. Lakini hata hivyo hakumuacha aishi kwa amani. Nyumba yake ilitiwa moto, lakini mara moja moto huo ulizimishwa na hakukuwa na mtu ye yote aliyejeruhiwa.

TABIA ZAKE

Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) alikuwa na tabia kama zile walizokuwa nazo Maimamu wengine wa nyumba ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) . Jambo muhimu sana la wakati wa maisha yake na ambalo wanahistoria wamelitaja sana ni matukio mbalimbali ya huruma, ukarimu, misaada ya kisiri siri kwa wahitaji na maskini, alikuwa akitimiza wajibu wake kwa ndugu zake, uvumilivu, na ustahimilivu.

Safari moja hujali mmoja alikuja Madina na akalala katika Msikiti wa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) na alipoamka alidhania amepoteza kifuko chake cha fedha. Alipokuwa akizatazama huku na huku alimwona Imamu(a.s.) akisali katika pembe ya Msingiti huo. Kwa kuwa hakumfahamu Imamu(a.s.) , alimwendea na kumwambia, "umechukua kifuko changu cha fedha". Imamu(a.s.) akamwuliza, "Kifuko hicho kilikuwa na fedha kiasi gani? Yule hujaji akasema, Kina dinar (vipande vya dhahabu) elfu moja." lmamu alimchukua nyumbani kwake na akampa dinari elfu moja. Yule hujaji alirudi msikitini na huko alikiona kile kifuko chake miongoni mwa mizito yake. Alirudi upesi upesi kwa Imamu(a.s.) na kuomba radhi kwa lawama zake za haraka haraka na akataka kuzirudisha zile dinari elfu moja za Imamu(a.s.) . Lakini Imamu(a.s.) alimwambia kuwa haikuwa tabia ya watu wa Nyumba ya Mtukufu Mtume(s.a.w.w) kuchukua kitu walichokwisha kukitoa.

Inaonekana kila siku kuwa kila watu walipoogopa kutokea upungufu wa nafaka kila mtu hujaribu kuweka akiba kiasi cho chote kile awezacho kukiweka. Lakini Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) alimwambia mkurugenzi wake Bwana Mu'tab, akisema, "Kila siku Nafaka zinaendelea kuwa ghali". Tunacho kiasi gani cha nafaka? Bwana Mu'tab alijibu, "Hatuna hofu yo yote, tunayo nafaka ya kututosha kwa muda mrefu." Imamu(a.s.) aliamrisha akiba yote iuzwe. Kisha akasema, "Sasa hatutakula tena ngano tupu, bali tutakula mikate ya unga wa ngano uliochangaywa nusu kwa nusu na unga wa Shayiri". Imamu(a.s.) alifanya hivi kwa sababu alitaka kuwafundisha watu wale walio na kitu kuwa ni lazima washirikiane na wale wasio na kitu.

Kila mara aliwaheshimu sana maskini kuliko matajiri. Aliiheshimu sana kazi. Alijishughulisha sana na biashara. Kila mara alionekana akifanya kazi shambani mwake. Wakati fulani alipokuwa akilima na huku akitokwa na jasho mwili mzima, mtu mmoja alimwomba alime pamoja naye lakini Imamu(a.s.) alijibu, "Sio fedheha kwa mtu kulivumilia jua kali na joto ili kujipatia chakula chake."

Alikuwa kama wale Maimamu wengine, alikuwa mwenye huruma sana kwa watumishi na watumwa wake, Bwana mmoja aliyekuwa akiitwa Sufyan Suri amehadithia kuwa siku moja alikwenda nyumbani kwa Imamu(a.s.) na aliona kuwa uso wa Imamu (a.s.) ulionyesha dalili za huzuni na alipomwuliza sababu yake, Imamu(a.s.) alimjibu akisema, "Nimemkataza kila mtu kwenda kwenye orofa ya juu ya nyumba. Nilipoingia ndani nilimwona mjakazi yaya akipanda ngazi za orofani huku amenishika mtoto. Aliponiona aliogopa sana kiasi ambacho alimwangusha yule mtoto na mtoto akafa. Simsikitikii sana yule mtoto bali nahuzunikia kwa kule kuogopa kwake yule mjakazi. Kisha Imamu(a.s.) alimwita yule mjakazi na kumwambia, "Usiogope, ninakupa uhuru kwa jina la Mwenyezi Mungu" kisha Imamu(a.s.) alikwenda kwenye mazishi ya yule mtoto'.

KUIENEZA ELIMU

Imamu Jaafar As-Sadiq(a.s.) alijulikana sana kila mahali katika ulimwengu wa Kiislamu kwa elimu yake na watu wa kila mahali walimjia ili kujifunza. Wanafunzi wake walifikia elfu nne na miongoni mwao walikuwemo wanafunzi wa Sheria za Kiislamu (Fiqah), Elimu ya Tafsiri ya Qur'ani, Mantiki na Elimu ya Majadiliano. Kila mara wapinzani walimjia Imamu(a.s.) na kufanya majadiliano na wanafunzi wake. Mara nyingine bada ya majadiliano hayo Imamu(a.s.) aliyasahihisha yale majibu yaliyotolewa na wanafunzi wake. Wakati mwingine yeye mwenyewe aliingia katika kujadiliana na wapinzani wa kidini na makafiri. Vile vile aliwapa baadhi ya wanatunzi wake mafunzo ya Sayansi na Hesabu. Bwana Jabir bin Hayyan (anayejulikana katika nchi za Ulaya kwa jina la Geber) aliekuwa mmoja wa wanafunzi wake aliandika vitabu mia nne vya Sayansi na Hesabu. Wengi wa wanafunzi wake walikuwa wanavyuoni wakbuwa Elimu ya Sheria za Kiislamu (Fiqah) na idadi ya vitabu vyao ilifikia mamia.

KUFARIKI KWAKE

Vipi maisha ya namna hii yanaweza kuhusika na kutafuta mamlaka fulani au serikali? Lakini Uchamungu huo na elimu ya Imamu vilionekana machoni pa watawala kuwa hatari kwao. Wakati kila jaribio la kutafuta jambo lolote lile liwezalo kuchukuliwa dhidi yake liliposhindwa, silaha ile ile ya kisiri iliyotumiwa kwa Maimamu wengine ilitumiwa kwake pia. Alipelekewa zabibu zilizotiwa sumu kupitia kwa Gavana wa Madina na Imamu alipozila, sumu hiyo ilianza kufanya kazi yake na Imamu akafariki mnamo tarehe 15 Shawwal (Mfunguo Mosi), mnamo mwaka wa 148 Hijiriya akiwa na umri wa miaka 65. Mwanawe Imamu Musa bin Jaafar al-Kadhim aliongoza sala ya mazishi na akamzika katika makaburi ya Jannatul-Baqi (mjini Madina) kandoni mwa makaburi ya Maimamu Hasan(a.s. ), Ali Zainul Abidiin(a.s.) na Muhammad Baqir(a.s.).

NYONGEZA

Baadhi ya Hadithi za Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) : Ziko hadithi chache za Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) zilizoandikwa na Bwana Ya'qubi, mwanahistoria maarufu. Hapa tunazinakili hadithi hizo kutoka kitabu cha mwanahistoria huyo kiitwacho "Tarikh" kilichohaririwa na Houtsma, kama zilivyonakiliwa na Bwana D.M. (Mhubiri wa Kikristo) na kutoka vitabu vingine vilivyonakiliwa na Mhubiri huyo:

1. Wako watu wa daraja tatu ambao huhitaji kuhurumiwa, tajiri aliyefilisika, mtu mwenye cheo aliye tukanwa, na mwanachuoni anayefanywa baradhuli na mjinga.

2. Ye yote yule anayeondolewa na Mwenyezi Mungu kutoka katika aibu ya dhambi, na kuwekwa katika utukufu wa Uchamungu, ndiye yule ambaye Mwenyezi Mungu humfanya kuwa tajiri bila ya kuwa na mali yo yote ile, na mwenye kuheshimiwa bila ya msaada wa jamii yake."

3. "Ye yote yule amwogopaye Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu huvifanya vitu vyote vimuogope, na ye yote yule asiyemuogopa Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanya aviogope vitu vyote.

4. "Ye yote yule anayetosheka mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kidogo alichokipata kutokana na ukarimu (wa Mwenyezi Mungu), Mwenyezi Mungu atatosheka kwake na kila kidogo miongoni mwa kazi alizotakiwa kuzifanya".

5. Siku moja Imamu(a.s.) alisema, "Wako marafiki wawili, na ye yote yule atakayewafuata ataingia peponi. "Mtu mmoja alimwuliza, "Ni nani hao? Imamu(a.s.) alijibu, "kukubali kile unachokichukia Mwenyezi Mungu anapokipenda, na kukataa kile unachokipenda Mwenyezi Mungu anapokichukia". Yule mtu aliuliza tena, "Ni nani awezaye kufanya hivyo?" Imamu(a.s.) aIijibu, "Ye yote, yule anayekimbia kutoka motoni kwenda Peponi."

6. "Kama ukitumbukiza mkono wako kinywani mwa nyoka hadi kwenye kiwiko, ni bora kuliko kumwombea mtu fulani kitu ambacho hakiwezi kutoIewa."

7. "Jihadhari usijishirikishe na watu wa aina tano, kwanza, mjinga, kwa maana atapenda akusaidie lakini kwa hakika atakuumiza; pili mwongo kwa maana yu kama mazigazi (madanganyo ya macho) yanayofanya sehemu za mbali zionekane kuwa za karibu na za karibu kuwa za mbali, tatu, mtu mpotovu au mtenda mabaya kwa maana atakuuza kwa ajili ya kujipatia chakula chake au maji yake, nne, bahili kwa maana atakuacha na kujiokoa kwa kulipa fidia."

8. "Wenye kuamini wataonyesha mapenzi na mapenzi yataonyeshwa kwao, ili kuweza kufunika mashogi yao. (Katika misafara ni kawaida kufunika mashogi mabovu ya wanyama waliochukuzwa mizigo kwa zulia au tandiko lenye rangi zing'arazo ili kuficha vilivyomo ndani visionekane. Imamu alitoa mfano huu kutokana na desturi hii).

9. "Ye yote yule unayemchukiza mara tatu, lakini hakusemei maneno mabaya, mhesabu kuwa yu rafiki yako, lakini ye yote yule atakayekuomba umwonyeshe urafiki wa ndugu, ambapo yeye mwenyewe hajirafikishi na nduguye au hajishirikishi naye au hamkaribishi nyambani kwake fahamu kuwa mtu huyo atakuumiza."

10. "Kuhusu suala Ia uhuru wa mapenzi ya mwanadamu (Irada) lililokuwa likijadiliwa sana wakati huo, Imamu Jaafar as-Sadiq(a.s.) alifundisha watu kuwa "Mwenyezi Mungu aliyetukuka ameamuru mambo fulani kwetu na vivyo hivyo ameamuru mambo fulani kutendeka kupitia kwa mawakili wetu; yale aliyotuamria aliyoamua kwa ajili yetu ametufichia, lakini yale aliyoamrisha kutendeka kupitia kwa mawakili wetu ametudhihirisha. Hivyo hatuhusiki sana na yale aliyokwisha kutuamulia, kwa vile tunayo yale ambayo ameyaamua kupitia kwa wakili wetu".

11. lmamu(a.s.) alikuwa na kawaida ya kusema katika dua zake, "Ewe Mwenyezi Mungu, Sifa ninazokupa zakustahili Wewe, na msamaha uko kwako kama nikikukosea tena; hakuna kazi yo yote yenye kustahili sifa ile kwangu au kwa mtu ye yote yule mwingine na katika mabaya hakuna msamaha wo wote kwangu wala kwa mtu ye yote yule mwingine".

12. Imamu(a.s) alikuwa akivaa pete yenye mhuri uIioandikwa "Mwenyezi Mungu ni Bwana wangu na Ulinzi wangu kutoka kwa Viumbe vyake."

MWISHO

FAHARASA

MWENGE WA UKWELI1

SHUKRANI 2

UTANGULIZI 2

JINA NA NASABA 2

KUZALIWA KWAKE 3

KULELEWA KWAKE 3

UIMAMU WAKE 3

KUANGUKA KWA SERIKALI YA BANI UMAYYAH 4

DHULUMA JUU YA BANI FATIMAH 5

IMAMU ADHULUMIWA 6

TABIA ZAKE 7

KUIENEZA ELIMU 8

KUFARIKI KWAKE 8

NYONGEZA 9

MWISHO 10