TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA20%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Mwandishi:
Kundi: tafsiri ya Qurani

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Juzuu 9 Juzuu 10 Juzuu 11
  • Anza
  • Iliyopita
  • 20 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 39068 / Pakua: 4814
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu. Kitabu hiki kilicho mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London. Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana `kwenda na wakati. Sifa kubwa ya pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kungangania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo suala la madhehebu ni nyeti nchini humo,hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilmsaidia sana hata

kuweza kutoa kitabu kiitwacho Al-Fiqh alaa madhaahibil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah). Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri,na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa. Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Ruhusa imetolewa kwa yeyote anaetaka kukichapisha upya kitabu hiki kwa sharti tu kwamba asibadilishe chochote bila ya kutujulisha, na atutumie nakala moja baada ya kukichapisha. Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji. Mwisho, shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.Mchapishaji.

CHAPA YA PILI

Kutokana na maombi mengi ya wasomaji wetu wa Kiswahili, ambao ni wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu, walioko Afrika Mashariki na Kati, Uarabuni na hata nchi za Ulaya, tumeonelea kukichapisha tena Kitabu hiki ili kupunguza kiu yao kama si kuiondoa kabisa. Tafauti iliyojitokeza katika chapa hii ya pili ni utaratibu mpya uliotumika, ambapo baada ya Aya kufasiriwa, maelezo yake yanapatikana moja kwa moja chini yake bila ya kwenda kwenye ukurasa mwingine, na utaratibu huu ndio utakaotumika katika chapa zote zitakazofuata.

Vilevile tumejaribu sana kusahihisha baadhi ya makosa ambayo kibinadamu yalikuwa yamefanywa katika toleo la kwanza. Hatuna budi kuwashukuru wote waliotumia wakati na akili zao katika kufanikisha lengo hili adhimu, bila ya kuwasahau wafadhili na wasimamizi wetu.Mwenyezi Mungu awalipe kheri nyingi. Vilevile tunawashukuru sana wasomaji wetu amabao waliotukosoa, hivyo kuchangia, kwa kiasi kikubwa, kuisahisha chapa hii.Na tunawaomba waendelee kufanya hivyo. Mchapishaji

 DIBAJI

Sifa njema zote zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe. Baada ya hayo: Mimi nimetunga mfululizo wa vitabu vidogo vidogo katika itikadi na misingi yake. Nimevitunga kulingana na mfumo na mantiki ya kizazi cha kisasa, ambacho hakiamini kitu ila kile kinachokitaka na chenye kuafikiana na malezi yake na maendeleo yake.

Alhamdulillah Mwenyezi Mungu amejaalia tawfiki na kufaulu kwa mfululizo huo na umerudiwa kuchapishwa mara nyingi. Kimsingi ni kuwa kila kazi inayoafikiana na hekima na lengo inayolikusudia, Mwen-yezi Mungu huipa ufanisi na tawfiki. Hakika tawfiki inatokana na Mwenyezi Mungu, hakuna shaka, lakini Mwenyezi Mungu amekataa kupitisha mambo isipokuwa kwa njia yake na desturi yake.

Kuandika juu ya karatasi tu, sio sharti la kufaulu katika kitu chochote; isipokuwa kufaulu ni kumridhisha na kumpendeza msomaji kile atakachokisoma. Msomaji naye hawezi kuridhia kitabu chochote, isipokuwa kiwe kwa ajili yake na sio kwa ajili ya mwandishi.Na huko kuridhia kunampa nguvu mwandishi kuendelea. Hapo ndipo msomaji na mwandishi wanapoathiriana. Kwa vyovyote ilivyo, kuenea kwa mfululizo huo wa vitabu vidogo vidogo kumenipa nguvu ya kutunga vitabu vikubwa na vipana; kama vile: Maalimu Falsafatil Islamiya, Alfiqhu Ala Madhahibil Khamsa, Fadhail Imam Ali n.k.

Mwenyezi Mungu naye akavifanyia vitabu hivi kama alivyofanyia vile vingine. Nikapata msukumo wa kutunga Fiqhul Imam Jaffar Assadiq katika juzuu sita kubwa; nacho kikawa kama vingine vilivyotangulia. Kwa hiyo vikanipa msukumo wa kutunga kitabu kikubwa na kitukufu, Tafsir ya Qur`an ambayo nimeiita Tafsir Al -Kashif.

Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na nguvu Zake, vile vile kwa tawfiki Yake na fadhila Zake, imetimia juzuu hii ninayow-aletea. Ndani yake mna Sura mbili kamili za Al-Fatiha na Al-Baqara. Sijui kama uhai utaniruhusu nione natija ya lile nililojitolea mhanga, au kwamba kudra itafanya kinyume? Na kama ikitimia Tafsir Al-Kashif je, itakuwa na mafanikio, kama ilivyokuwa kwa tungo nilizozitunga, ya kutoa matunda? Je, itazaa kitabu kingine baada yake kama ilivyokuwa kwa Fiqh?

Hayo ni maswali ambayo hapana ajuaye jawabu lake isipokuwa Mwenye tamko la kwanza na Mwenye uwezo wa juu.

﴿وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ﴾

Na nafsi yoyote haijui itachuma nini kesho, wala nafsi yoyote haijui itafia ardhi gani" (31:34)

Hata hivyo kuamini kwangu ukweli huu hakunizuii kuendelea na juhudi zangu. Kwa sababu, vile vile ninaamini kwamba azma yangu ya kujitahidi ina athari kubwa katika kuhakikisha yale ninayoyataka. Imani hii inanipa msukumo wa kutoa juhudi zangu zaidi, kwa kuogopa kupoteza fursa.

Kwa hivyo basi, nitaendelea kuandika na kuwa na ndoto ya kutimia na kufaulu mpaka kufa.Yeye peke yake ndiye ambaye atasimamisha nishati yangu.Nami nitaendelea kutoa juhudi zangu muda wote ule ambao mauti yatakuwa yako mbali nami.

Natamani sana yanijie mauti huku nikiwa ninaandika kulingania kwenye haki na uadilifu. Bali mapendeleo yangu ni kuingia peponi ili niweze kusoma na kuandika, nikiwa sina mawazo mengine yoyote ya kunishughulishi, nitakuwa sina mawazo ya kushughulikia familia na kadhalika.

Mara nyingi sana hunijia swali hili: Kama nikiingia peponi nitakuwa mvivu? Je, itawezekana nisome na niandike? Halafu hujijibu: Ndio, huko kuna yanayofuvi rahiwa na macho na yanayopendwa na nyoyo; hata kama moyo unapenda kusoma na kuandika. Kisha linanijia swali jingine: Nimwandikie nani na watu wote wa peponi ni wakamilifu?

Samahani kwa kuiachia kalamu iandike hayo; au kwa usahihi zaidi, kuiacha dhati yangu kujieleza. Kwa kweli mimi ni mtu wa kawaida tu, ambaye ni vigumu kumtenganisha na dhati yake na ambaye inakuwa vigumu kujizuia kuyaelezea yaliyo katika pango la moyo wake, wakati inapopatikana fursa ya kujieleza.

Kizazi cha kisasa Kila kitu kina sababu ya kutokea kwake, ni sawa kiwe ni cha kimaumbile, kama vile tufani na tetemeko; au cha kijamii, kama vile ujinga na ufukara; au kiwe ni katika mambo ya moyoni, kama vile imani na kufuru. Hakuna kitu chochote kinachotokea kwa sadfa bila ya sababu yoyote, au bila ya mipangilio yoyote. Nitayafafanua maelezo haya kwa swali na jibu lifuatalo:

Kwa nini kizazi cha sasa hakijishughulishi na misimamo ya kidini kama kilivyokuwa kizazi kilichopita? Vijana wengi wa kileo wameachana na ibada na mazingira ya kidini; bali imekuwa uzito sana kwao kusikiliza mawaidha na nasaha za kidini; hata msimamo mzuri wa kiutu - kama udugu, usawa, amani, kusaidiana, ukweli na uadilifu - haumo katika nyoyo zao kabisa.

Inapotokea kuuzungumzia basi wanauzungumzia katika ndimi zao tu, sio katika nyoyo zao; ila ikiwa kuna manufaa ya kibinafsi.

Jibu ni kuwa, mataifa ya Kiislamu ya Kiarabu na yasiyokuwa ya Kiarabu yalikuwa hayategemei misingi yoyote wala misimamo yoyote ila ile iliyotokana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) na Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , sio iliyotokana na ujamaa au ubepari, wala demokrasia au ubaguzi. Hakuna kitu chochote walichotegemea isipokuwa wahyi wa Mwenyezi Mungu.

Humo ndimo mlimochukuliwa misingi ya itikadi, adabu, tabia na njia za taaluma. Vile vile kanuni na hukumu zinazotumiwa katika mahakama na mambo mengine ya kibinafsi na ya kijamii, yalitoka humo. Kwa hiyo, ndio maana yakawa mafundi-sho ya dini yako wazi katika bongo za watu wengi; wakawa wanayajua yanayotakiwa na sharia na yanayokatazwa. Yule aliyekuwa akiishi maisha ya dini alikuwa ndio tegemeo la wote na ndio mahali pa amana zao. Na,yule mbaye hana dini hakuaminiwa au kutegemewa katika jambo lolote.Yaani misimamo ya kijamii ilikuwa ni misimamo ya kidini.

Yeyote anayetoka katika msimamo huo,anakuwa ametoka katika usalama.Kisha siku zikapita, yakatokea mapinduzi kutoka nchi za Kimagharibi, wakavamia miji ya Kiislamu.Kwanza kabisa walielekea kwenye sharia ya Qur`an, wakaiondoa katika mahakama. Badala yake wakaleta kanuni za Kifaransa na za Kiingereza.Wakaondoa mafunzo ya kidini katika taaluma. Wakaanzisha majumba ya ufuska; kama vile mabaa, vilabu vya usiku pamoja na kila kitu ambacho waliona kingeweza kuondoa itikadi na maadili.

Kwa hiyo athari za Qur`an na Sunna za Mtume zikafichika katika maisha ya kijamii. Hata lugha ya Kiarabu pia ilipatwa na kile kilichopatwa na dini. Ndio kikawa kizazi hiki hakijishughulishi na dini wala maadili mema. Hiyo ni natija ya ufisadi waliokulia na kulelewa nao. Na kama kawaida, hali hiyo ilienea. Kwa hiyo ni makosa kukitenga kizazi na jamii yake na malezi yake. Hawakukosea wale waliosema: Panapofuka moshi hapakosi moto

Dawa Unaweza kuniuliza: Umeelezea ugonjwa, sasa dawa yake ni nini? Kwa kweli jibu la swali hili si la kujibiwa na msomi mmoja tu; hapana budi zikutane akili kubwa zenye ikhlas. Kwa sababu, tabia na ada zikiingia katika kizazi na zikabaki kwa muda mrefu, huwa zimemea. kazi rahisi kuzing`oa. Kwa vile zinafanya kazi katika nafsi, kama zinavyofanya kazi athari za kisayansi.

Kuzibadilisha kunahitaji juhudi na jihadi ndefu, zenye mashaka; kama juhudi aliyoifanya Mtume(s.a.w.w) katika kubadilisha ada za kijahiliya na itikadi zao. Kuna Hadith zinazoonyesha hayo; kama ile inayosema: "Uislamu ulianza katika hali ya ugeni na utarudi katika hali ya ugeni, kama ulivyoanza." Kwa hivyo, hauwezi kuepukana na ugeni wake na kutulia katika kurudi kwake, isipokuwa kwa kiongozi kama Mtume Muhammad(s.a.w.w) na Masahaba kama Wahajiri na Ansari Mwenyezi Mungu hashindwi kufanya Qur`an, sharia yake na maadili yake kuwa ndiyo inayotawala leo. Lakini ni juu yetu kufanya juhudi kadiri ya uwezo wetu, wala tusingoje muujiza wa mbinguni.

Na kazi ambayo tunaiweza kuifanya, nionavyo mimi,ni:

Kwanza : tuitilie mkazo dini katika mashule, hasa Qur`an, kuisoma, kuihifadhi na kuifasiri.Kwani hiyo ndiyo msingi. Kama wasimamizi wakikataa kufundisha dini katika mashule na watakataa tu,basi ni juu yetu kuanzisha Shule za kibinafsi kwa ajili ya lengo hilo tu. Tuanzishe Shule hizi kutokana na mamillioni yanayotolewa sabili kwa wanavyuoni wakubwa na wengine Wala sijui kama kuna kazi nyingine bora zaidi ya kutumia pesa hizo kuliko kufufua na kuyaeneza mafundisho ya dini.

Pili : kila mmoja katika watu wa dini atekeleza wajibu wake kwa ikhlasi, baada ya kujiandaa kuwa kiongozi mwenye mwamko, anayejua namna ya kuwakinaisha vijana, kuwa dini ndio chimbuko la msimamo ulio sawa, ambalo litawapa maisha mema zaidi.

Tatu : kuufafanua uhakika wa dini, kuufanya mwepesi kufahamika na kuutangaza kwa vitabu, hotuba, makala na matoleo kadhaa. Tumthibitishie mjinga na mwenye shaka kuwa Uislamu kwa sharia na maadili yake, unatosheleza kabisa mahitaji ya mwanadamu ya kiroho na ya kimaada; na unaweza kutatua matatizo yake; na kwamba una lengo la kumfanya afaulu katika dunia yake na akhera yake.

Msomaji atapata dalili ya hayo katika tafsiri hii ambayo inaunganisha dini na maisha, na ambayo imeshughulikia zaidi upande wa ubinadamu kuliko kushughulikia ufasaha wa maneno.

Mfasiri Tafsiri, kilugha, ina maana ya kubainisha. Na, katika istilahi ina maana ya elimu inayotafiti maana ya maneno ya Qur`an na yanavyohusika. Ili mfasiri awe na ubainifu katika ambayo yanamstahiki Mwenyezi Mungu, hana budi kuwa na maandalizi yafuatayo:-

Elimu za kiarabu kwa nyanja zake zote, elimu ya Fiqh na Misingi (usul) yake, Hadith na elimu ya Tawhid. Na miongoni mwa maandalizi hayo, kama wanavyoona wengine, ni elimu ya Tajwid na elimu ya kisomo cha Qur`an.

Kuna kitu kingine anachokihitajia mfasiri ambacho ni muhimu na kikubwa kuliko chochote katika walivyovitaja wafasiri katika utangulizi wa tafsiri zao. Kwa sababu, ndio msingi wa kwanza wa kufahamu maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.); Wala sijamwona yeyote aliiyekielezea.

Kitu chenyewe ni kuwa, maana ya Qur`an hawezi kuyafahamu na hatayafahamu kwa uhakika wake na kujua ukubwa wake, isipokuwa yule mwenye kuyahisi ndani ya moyo na akili yake. Pia imani yake ichanganyike na maana ya Quan pamoja na damu yake na nyama yake. Hiyo ndiyo siri iliyo katika kauli ya Amirul Muminin, Ali(a.s.) :"Hiyo ni Qur`an iliyonyamaza na mimi ni Qur`an inayotamka."

Vile vile imenijia yakini wakati nikiendelea na tafsiri kwamba mfasiri yeyote asiyeleta fikra mpya, ijapokuwa moja tu, katika tafsiri yake yote, basi atakuwa hana akili ya mwamko, isipokuwa ana akili ya kusoma tu. Anamchorea mwingine yale anayoyasoma, kama inavyoonekana picha ya kitu katika kioo vile ilivyo kwa rangi na umbo.

Hiyo ni kwa sababu maana ya Quran yako ndani sana kiasi ambacho yeyote hawezi kuyafikia kwa vyovyote vile atakavyokuwa na elimu na fahamu; isipokuwa atagundua yale ambayo maarifa yake yanayamudu. Atakaposimama mfasiri aliyetangulia pale alipofikia, kisha akaja mwingine akafuata nyayo zake bila ya kuzidisha chochote ijapokuwa hatua moja tu, basi atakuwa ni kama kipofu kamili anayetegemea fimbo tu; anapoikosa anabakia pale alipo.

Nimepata rai nyingi na itikadi za hapa na pale wakati nilipokuwa nafasiri.Kwa kweli tafsiri imesahihisha fikra zangu nyingi za zamani. Nimekuwa na yakini kwamba hapana imani bila ya takua pepo haipati isipokuwa mwenye kujitahidi na akajitoa mhanga katika njia ya haki na kwamba hakuna msingi wowote katika misingi ya Kiislamu au tawi lolote katika matawi ya Kiislamu - katika kumwamini Mwenyezi Mungu au hukumu ndogo katika sharia - isipokuwa inafungamana na maisha.

Vile vile nimeyakinisha kuwa wengi wa wale ambao hawaujui Uislamu na makusudio yake ni wale wanaojinaki na Uislamu; na mengi ambayo atayakuta msomaji wakati wa kupekuwa kurasa za Tafsir hii, nimeyahusisha hayo katika vifungu mbali kwa vielelezo vyake.

Kwa kweli sijui kama kuna kazi ngumu na nzito kama kufasiri maneno ya Mwenyezi Mungu.Sio kazi rahisi kueleza matakwa yake Mwenyezi Mungu. Lakini jambo la kutia moyo, nikuwa mfasiri hufasiri maana ya Qur`an na makusudio yake kulingana na alivyofahamu yeye, sio kulingana na ilivyo hasa; sawa na mujtahid wa Fiqh ambaye hulipwa thawabu akifutu sawa na husamehewa akikosea, bali hupata thawabu, hata akikosea, kwa sababu ya juhudi yake na kutokuwa mvivu.

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

MWITO WA QURRAN

Mwenye kufuatilia Aya za Quran tukufu, akazingatia maana yake, atazikuta zina mfungamano mmoja tu katika kanuni zake zote na misingi yake. Vile vile katika sura zake na Aya zake. Mfungamano huu ni ule mwito wa kuwapa watu maisha mema yenye uadilifu, ustawi na amani. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾

"Enyi mlioamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai." (8:24)

MWITO WA MWENYEZI MUNGU NA MTUME

Mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume kwenye maisha, una mfumo wake na nguzo zake maalum zinazousimamia Mwenyezi Mungu ameupanga mfumo wa kulingania kwa kumwambia Mtume wake mtukufu(s.a.w.w) :

﴿ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ﴾

"Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora." (16:125)

MAKUSUDIO YA HEKIMA NA MAWAIDHA MAZURI

Makusudio ya hekima na mawaidha mazuri ni kuuambia moyo na akili, na kuuonyesha viumbe vya aina yake na vya ajabu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُ الْحَقُّ أَوَلَمْ يَكْفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴾

"Tutawaonyesha ishara zetu zilizo katika upeo wa mbali na katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli" (41:53)

Vile vile kuwahadharisha wapinzani na mwisho mbaya, na huwaonyesha mfano wa umma uliotangulia; kama alivyofanya Nabii Shuaib aliposema:

﴿وَيَا قَوْمِ لَا يَجْرِمَنَّكُمْ شِقَاقِي أَن يُصِيبَكُم مِّثْلُ مَا أَصَابَ قَوْمَ نُوحٍ أَوْ قَوْمَ هُودٍ أَوْ قَوْمَ صَالِحٍ وَمَا قَوْمُ لُوطٍ مِّنكُم بِبَعِيدٍ﴾

"Na enyi watu wangu! Kukhalifiana nami kusiwapelekee kuwasibu kama yaliyowasibu watu wa Nuh au watu wa Hud au watu wa Swaleh. Na watu wa Lut si mbali nanyi." (11:89)

Wakiendelea na inadi yao, na ikiwa hakuna dalili zaidi za kutoa, basi achana nao. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّـهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ﴾

"Na kama wakikuhoji, basi sema nimeusalimisha uso wangu kumwelekea Mwenyezi Mungu na walionifuata (3:20)

﴿فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ﴾

"... Hakika ni juu yako kufikisha na ni juu yetu hisabu."(13:40)

Ama nguzo za mwito wa maisha mema, ni hizi zifuatazo:-

1. Hakika mtu hakupatikana kibahati tu, bila ya makusudio yoyote.

﴿وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ ثُمَّ يَتَوَفَّاكُمْ﴾

"Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha atawafisha" (16:70)

2. Mwenyezi Mungu hakumwacha mtu bure bure tu, ajihukumilie kimapenzi yake, bali amemuwekea njia ya sawasawa, ambayo haijuzu kuikengeuka: Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَيَحْسَبُ الْإِنسَانُ أَن يُتْرَكَ سُدًى﴾

"Hivi anadhani kuwa mtu ataachwa bure bure tu !" (75:36)

﴿فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴾

"Naapa kwa Mola wako tutawauliza wote yale waliyokuwa wakiyatenda." (15: 92-93)

3. Amani na kuchunga nidhamu. Mwenye kuiharibu na akafanya uharibifu katika nchi ataadhibiwa adhabu kali duniani, na katika akhera atakua na adhabu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿إِنَّمَا جَزَاءُ الَّذِينَ يُحَارِبُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الْأَرْضِ فَسَادًا أَن يُقَتَّلُوا أَوْ يُصَلَّبُوا أَوْ تُقَطَّعَ أَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم مِّنْ خِلَافٍ أَوْ يُنفَوْا مِنَ الْأَرْضِ ذَٰلِكَ لَهُمْ خِزْيٌ فِي الدُّنْيَا وَلَهُمْ فِي الْآخِرَةِ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴾

"Hakika malipo ya wale wanaopigana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya uovu katika nchi, ni kuua-wa au kusulubiwa au kukatwa mikono yao kwa mabadilisho au kuhamishwa katika nchi; hii ndio fedheha yao katika dunia na akhera watapata adhabu kubwa." (5:33)

4. Amani na nidhamu haiwezi kuwako na wala haitakuwako ikiwa kila mtu hatachunga heshima yake na uaminifu wake. Kwa sababu jamii njema, kwa mujibu wa Quran, ni ile isiyokuwa na mbegu ya ufisadi hata moja. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا﴾

"Mwenye kumuua mtu bila ya yeye kuua mtu au kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha hai basi ni kama amewaacha hai watu wote." (5:32)

Hiyo ni kwamba hakika ya utu inakuwa kwa kila mmoja. Mwenye kumfanyia ubaya mmoja, atakuwa amewafanyia ubaya wote na mwenye kumfanyia wema mmoja, atakuwa amewafanyia wema wote.

Kusema kwake Mwenyezi Mungu: Mwenye kuua mtu bila ya yeye kumuua mwingine au kufanya ufisadi katika nchi", ni kuonesha kuwa kila mtu ana heshima yake ya kiutu, mpaka aivunje mwenyewe kwa kufanya kosa litakalovunja heshima yake hiyo.

5. Utangamano kati ya watu unakuwa juu ya misingi ya kuchunga heshima kwa kila mtu bila ya kubagua kati ya mwanamume au mwanamke, mweusi au mweupe na tajiri au maskini, katika mila yoyote aliyo nayo. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameuthibitisha ubainifu huu kwa ibara fupi:

﴿وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ ﴾

"Hakika tumemtukuza mwanaadamu..." (17:70)

Mwenye kuidharau heshima aliyopewa na Mwenyezi Mungu, atakuwa amemdharau Mwenyezi Mungu na sharia yake.

6. Kuamini Mwenyezi Mungu, Utume wa Muhammad(s.a.w.w) , siku ya mwisho na mengineyo, ni katika misingi ya dini na matawi yake, wala sio kuwa ni bendera ya dini inayopeperushwa na Quran. Kila msingi katika misingi ya Uislamu na kila hukumu katika hukumu zake, zina matunda na amali yenye manufaa. Mwenyezi Mungu amekukutanisha kumwamini yeye na amali njema katika Aya kadhaa. Ama kuamini Utume wa Muhammad(s.a.w.w) ni kuamini utu na wema wake. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴾

"Na hatukukutuma isipokuwa uwe rehema kwa walimwengu" (21: 107)

Ama kuingia peponi, kunafungamana zaidi na jihadi na amali njema katika maisha haya. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴾

"Je mnadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliopigania jihadi dini ya Mwenyezi Mungu miongoni mwenu na kuwajua waliofanya subira?" (3:142)

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ﴾

"Enyi ambao mmeamini mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita katika yale yatakayowapa uhai..." (8:24)

Hii ni dalili wazi kwamba mwito wowote ambao hauna muungano wowote wa maisha, basi sio wa dini. Na mwenye kuunasibisha kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atakuwa ameizulia uwongo dini. Kwa misingi hii, ndipo nikajaribu kufasiri Aya za Quran tukufu na kuifafanua kwa ufafanuzi ufuatao:-

Njia Makusudio ya njia hapa ni udhibiti anaokwenda nao mtungaji, bila ya kukengeuka. Kwani kazi yoyote ambayo haina njia ni shaghalabaghala tu, itakayoongozwa na migongano.

Njia niliyofuata katika tafsiri hii, inafungamana na kudhibiti mambo yafuatayo:-

1. Nimeitazama Quran kwa mtazamo kuwa hakika yake na sera yake ni kitabu cha dini na uongozi, kutengeneza na kuweka sharia inayolenga kuwapa watu wote maisha yaliyo katika misingi iliyosalimika, inayoongozwa na amani na uadilifu na iliyojaa furaha na wema.Hayo nimetangulia kuyaeleza.

2. Baadhi ya wafasiri wa kwanza walijishughulisha zaidi na lugha, wakarefusha maneno katika kubainisha siri ya matamko na wakaweka maswali; mfano: Kwa nini imetajwa wau na wala isitajwe fa au kwa nini amesema mafasiki na wala asiseme madhalimu, n.k. Kisha wakajibu majibu yasiyo na umuhimu.Mimi sikuingilia jambo hili.

Ikiwa kila tafsiri imepondokea upande fulani, basi mimi nimepondokea kwenye namna ya kumkinaisha msomaji kwamba dini kwa misingi yake yote na matawi yake pamoja na mafunzo yake mengine, ina lengo la kumpatia mtu heri na heshima na kwamba mwenye kukengeuka lengo hili, atakuwa ameikengeuka hakika ya dini na njia ya maisha yaliyonyooka.

Ili kuweza kulifikia lengo langu hili, nimejaribu kwa juhudi zangu zote kuleta ufafanuzi mwepesi na ulio wazi, atakaoweza kuufahamu msomaji kwa kiwango chochote atakachokuwa. Kwa vile zama walizoishi wafasiri wa zamani hazikuwa zama za kudharauliwa dini, sharia yake na misimamo yake kama ilivyo sasa, ndio maana wafasiri hao walijishughulisha zaidi na fasihi kuliko kumkinaisha msomaji kuwa dini ni msimamo ulio sawa sawa. Kwa hiyo lugha ya tafsiri ya zama hizo sio ya zama hizi.

Hakika tafsiri ni fani kamili inayokwenda na wakati. Ndio maana mimi nimeielekeza tafsiri yangu katika kukinaisha kizazi cha kisasa kuwa dini inakwenda sambamba na maisha. Lakini hiyo haimaanishi kuwa mimi nimeghafilika na upande wenye kunufaisha, ambao umeonyeshwa na wafasiri wakubwa, la! Isipokuwa nimeufupisha upande huo na kuuonesha kwa uwazi zaidi, hata nimeonyesha rai yangu ndani yake hasa katika masuala nyeti ya kifalsafa; mfano: Kulazimishwa watu au kuwa na hiyari, uongofu na upotevu, Uimamu na Isma ya Mitume.

Pia shafaa, mwenye madhambi makubwa, hisabu ya kaburi na mengineyo. Vilevile mara nyingi nimehusisha kifungu maalum cha lugha, kwa ajili ya kutafsiri misamiati ambayo si maarufu. Mara nyingine nimeweka kifungu kingine cha irabu kwa ajili ya kubainisha hukumu za Kinahw (sarufi) kwa tamko lenye utatanishi, ijapokuwa wafasiri wa kisasa hawakujishughulisha nalo, lakini mimi nimeangalia matakwa ya baadhi ya wasomaji wa nahw, ingawaje ni wachache.

Ama usanii wa methali za maneno, elimu ya usemaji, ulinganishaji na uunganishaji, nimemwachia Zamakhshari katika Kash-Shaf, Al-Andalusi katika Bahrul-Muhit, na wengineo. Ili kuthibitisha kuwa lugha ya tafsiri inatofautiana kulingana na wakati, ninataja maneno ya Muhyiddin Ibn El-Arabi katika kitabu Futuhatil Makkiyya, Juzuu ya nne, mlango wa Hadhratul-hikma, kuhusu kuisoma Quran, ambayo yana maana ya undani kabisa na yanayoafikiana na nadharia za kisasa; hasa ile nadharia ya Uwiano (Relativity) ya Einstein, ambaye anazingatia kuwa wakati na mahali ndivyo vinavyosimamisha kitu. Anasema huyo Ibnul Arabi:

Msomaji anasoma alichokihifadhi katika Qur'an, anakuta katika kila kisomo maana ambayo hakuyakuta katika kisomo cha kwanza pamoja na kuwa herufi zinazosomwa ni zile zile, isipokuwa matukio na hali ndivyo vipya.Kwa hivyo hapana budi maana hayo yawe mapya. Kwa sababu, wakati wa kusoma kwa kwanza sio kwa pili.

Hapa aliposema,hapana budi kuwa maana hayo yawe mapya, maana yake ni kuwa, kitu kinakuwa kipya kwa kuwa kipya wakati ule. Amesema kweli mwanafalsafa Rasil, aliposema: Hakika watu wa zamani waligundua nadharia zilizothibitishwa na elimu kulingana na fikra na jitahadi zao; na zilikuwa ni rai za sawa; ambapo katika zama zao hizo hakukuwa na kitu zaidi ya jitihadi ya maoni."

3. Nimeangalia hadith zinazohusu Israil ambazo zimekuja katika baadhi ya tafsiri, nikazikuta ni vigano tu. Kitu kinachofahamisha zaidi uwongo wake, ni kuzinasibisha kwa Waisrail. Vilevile nimejipurukusha na riwaya zilizoelezea sababu za kushuka, isipokuwa chache tu. Kwa sababu, wanachuoni hawakudhibiti mategemezo yake na kupambanua kati ya dhaifu na sahihi; kama walivyofanya kwa riwaya za hukumu. Hata hizo nazo hawakuangalia sana zile za Sunna na kuchunguza kwa makini, isipokuwa katika wajib na haramu.Bali wameweka utafiti mbali katika vitabu vya Usuul.

Vilevile sikujishughulisha na pia kumshughulisha msomaji, kutaja kufungamana au kunasibiana kati ya Aya na Aya nyingine; kama walivyofanya wafasiri

Wengine, Kwa sababu, Quran haikufunuliwa kwa Mtume(s.a.w.w) kwa mpigo, bali iliteremshwa kwa nyakati maalum, mara nyingine kwa kufuatana na mara nyingine kwa kuchelewa; wala sura au Aya hazikupangwa kama tunavyozisoma hivi sasa.Quran, tuliyo nayo hivi sasa, ilipangwa tangu siku za Mtume(s.a.w.w) . Mpango huu haukufuata utaratibu wa kushuka sura, wala kuwa sura ni ya Makka au Madina; vile vile hakuna tarehe ya kushuka Aya. Hivyo tunakuta Sura ya Baqarah,Al-Imran na Maida ziko mwanzo wa msahafu baada ya Sura ya Fatiha, pamoja na kuwa zimeshuka Madina. Mara nyingine tunakuta sura iliyoshuka Madina ina Aya zilizoshuka Makka.

Mwenye tafsir ya Al-Manar, akimnukuu mwalimu wake, Sheikh Muhammad Abduh, katika Juzu ya pili, ukurasa 451, chapa ya

Pili: anasema: Quran sio kitabu cha fani cha kuwa na mlango mahsusi na makusudio fulani; isipokuwa ni kitabu cha uongozi na waadhi, inamgurisha mtu kutoka hili mpaka lile. Na mara kwa mara inarudia kwenye utafiti wa kusudio moja, kwa ibara nyingine na namna nyingine ya ubainifu, ili asichoke mwenye kupewa mawaidha na kuongozwa.

4. Kabla ya kitu chochote nimetegemea, katika kutafsiri Aya na kubainisha makusudio, Hadith zilizothibiti kwa Mtume(s.a.w.w) . Kwa sababu, ndizo zinazofasiri Quran na ni njia ya kujua maarifa yake. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ﴾

"Alichowapa Mtume kipokeeni na alichowakataza jiepusheni nacho" (59:7)

Ikiwa hakuna hadith, basi ninategemea dhahiri ya Aya na mpangilio wake. Kwa vile, msemaji mwenye hekima, ubainifu wake hutegemea yale anayoyafahamu yule anayemwambia kutokana na dalili zilizo wazi; kama ambavyo mwenye kuambiwa anachukua dhahiri hiyo tu, mpaka pale itakapothibitika kinyume. Kama ikija Aya nyingine katika maana ya Aya ya kwanza na ikawa ina ubainifu na kuwa wazi zaidi, basi ninazitaja pamoja ili zifafanuke zaidi. Kwa vile chimbuko la Quran ni moja, inajitamkia yenyewe na kujiletea ushahidi. Kama ikipingana dhahiri ya tamko pamoja na hukumu ya kiakili, basi ninaitafsiri kwa namna ambayo inaafikiana na akili, kwa kuizingatia hiyo akili kuwa ni dalili na hoja juu ya amali iliyo wajibu.

Ikiwa dhahiri ya tamko inapingana na Ijmai ya Waislamu katika nyakati zote kwenye masuala ya Kifiqh, basi huchukua Ijmai: kama kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿إِذَا تَدَايَنتُم بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَاكْتُبُوهُ ﴾

"Mnapowekeana deni kwa muda uliowekwa, basi iandikeni" (2:282)

Ambapo neno iandikeni limefahamisha wajibu, lakini Ijmai imesimamia juu ya kuwa kuandika deni ni sunna. Kwa hiyo hapo nimechukua kuwa ni suna na sio wajibu.

Ama kauli za wafasiri, sikuzifanya ni hoja mkataa na dalili peke yake; isipokuwa kutilia nguvu njia mojawapo, ikiwa tamko linachukua maana nyingi. Hata hivyo wafasiri wamefanya juhudi kubwa sana za kufafanua maana ya Quran na siri zake, na kuonyesha lugha inayofahamika na ngeni. Wamekitafsiri kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa juhudi ambayo haijapatikana mfano wake katika umma wa zamani au wa sasa.

Kwa hakika kuna wafasiri wakubwa na waliobobea katika fani mbali mbali za elimu ya Quran ambao walikuwa ni watu muhimu sana katika historia ya Kiislam. Kwa hiyo ingawaje kauli za mabingwa hao si hoja, kama kauli ya Masum, lakini zinaweza kuwa ni mwangaza juu ya maana yanayokusudiwa na kuuandaa njia ya kufahamu.

Makosa ya Chapa Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo.Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa Swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146) Imeandikwa La Yaalamuun, (hawajui) badala ya Yaalamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya pili, Sura (2:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawmal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile. Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil Makosa ya chapa.

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbaina sanah badala ya: Hatta idha balagha ashuddahu arbai- na sanah. Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana. Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu" . Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyoyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani.(Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

NAJILINDA KWA MWENYEZI MUNGU NA SHETANI ALIYEFUKUZWA

Kujilinda na Shetani Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

﴿فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴾

"Unaposoma Quran jilinde kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa" (16:98)

Amesema tena:

﴿وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴾

"Na kama wasiwasi wa shetani ukikusumbua basi jilinde kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mwenye kusikia mjuzi" (7:200)

Maana ya kujilinda Kujilinda huku kwa Mungu hakutoshi kwa kusema: Audhubillahi minashshaytwanir rajim tu, isipokuwa linalotakikana ni kumwamini Mwenyezi Mungu, kumtegemea na kumwogopa; hata kama mtu hakutamka hivyo. Mwenye kutenda umuhimu wowote kwa kuitakidi kuwa nyuma yake kuna nguvu inayomsaidia kutenda amali njema; mwenye kupondokea kufanya haramu, lakini twaa ya Mwenyezi Mungu ikamzuia na mwenye kuchanganyikiwa akaifanya sharia ndio kipimo, wote hao ni katika wale wanaojilinda kweli kwa Mwenyezi Mungu na shetani aliyefukuzwa.

Hakuna kitu kinachofafanua zaidi kujilinda kuliko mtu kumtegemea Muumba wake, kuwa na yakini kwamba mja mwingine hawezi kumdhuru wala kumnufaisha na kwamba kabisa hakuna kitu kitakachozidi hifadhi ya Mwenyezi Mungu.

Majaribio yametufundisha kwamba mwenye kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu, amedhalilika; na mwenye kutaka uokovu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ameruka utupu; na matarajio hayawezi kupatikana kwa kuwakimbilia viongozi, chama, wala kwenye hazina za matajiri, bali Mwenyezi Mungu tu peke yake ambaye hana mshirika.

Shetani ni nani? Sisi hatujamwona Shetani ana kwa ana lakini ametolewa habari zake na wahyi. Kwa hivyo ni wajibu kusadiki kuwa yupo, na si wajibu kujua alivyo. Mwenyezi Mungu amemtaja katika Quran kwa sifa ya kupoteza watu na kuwaepusha na twaa ya Mwenyezi Mungu na amali ya heri. Kwa hiyo kila wazo linalokupitia moyoni au mtu anayejaribu kukuhadaa kukuweka mbali na twaa na kheri ya Mwenyezi Mungu, kukuhadaa kuasi sharia na kuuvika uovu na ubatilifu nguo ya uongofu, basi huyo ni Shetani wa hisia au wa kimaana.

Jambo la kushangaza ni kuwa mashetani watu nao wanaomba walindwe na shetani, hali wao wenyewe ni mashetani lakini hawajijui. Ni sawa na mtu anayesoma Quran na huku inamlaani mwenyewe; kama ilivyoelezwa katika hadith.Quran inamlaani mwongo aliye haini.Kwa hivyo huyo mwongo anapoisoma huwa amejitamkia laana yeye mwenyewe.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴾

"Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote". (3:87)

Hukumu ya Kusoma Audhubillah... kabla ya kusoma Quran ni sunna, wala si wajib; ni kama vile kuosha mikono na kusoma Bismillah kabla ya kula. Lau hiyo Audhubillahi ingelikuwa ni wajibu ingeliwajibishwa katika swala, mahali pa fatiha na Sura.Wanavyuoni wote wamesema kuwa si wajib. Mwenye Miftaahul-Karaama amesema: Hawakuhitalifiana katika hilo isipokuwa Ibn al-Junaid ambaye mafakihi wamemwita: aliyejitenga.

Mantiki ya Iblis Kwa mnasaba wa Audhu (kujilinda na Shetani) tutadokeza vigano alivyonasibishwa navyo Ibilisi. Kwa sababu ingawaje ni vigano, lakini vina picha wazi kwa watu wengi wa zama hizi; hasa wale wanaotaka kujinufaisha bila ya kuangalia maslahi ya wengine, kwa kufanya mbinu za kujaribu kila njia ya kucheza na maneno na kuficha haki. Tutayaonyesha hayo kwa matamko tu; bila ya kudhihirisha madhumuni.

Inasemekana kuwa Ibilisi alimwambia Mwenyezi Mungu (s.w.t):

Haijuzu kuniadhibu kwa kuacha kumsujudia Adam. Mwenyezi Mungu akamuuliza,Kwa nini? Akajibu: Kama ungelitaka hasa nimsujudie ungenifanyisha kwa nguvu. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akamuuliza: Wakati gani ulijua kwamba sikukutaka umsujudie Adam? Je ulilijua hilo baada ya kukuamrisha na kuasi amri yangu?Au kabla ya kukuamrisha kusujudu? Akasema: Ni baada ya kuniamrisha.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.).akasema: Basi umejishinda. Kwa sababu ulihalifu kabla ya kujua kuwa Mimi niliyataka yale uliyoacha kuyafanya. Zaidi ya hayo kama ningekufanyisha kwa nguvu, basi isingelikuwa amri. Utaona katika mantiki ya Ibilisi sura iliyo wazi kwamba Mwenyezi Mungu hawafanyishi wenye kuwajibikiwa na sharia kama vile anavyofanya katika kuumba kwa njia ya kun fayakun (kuwa, ikawa). Isipokuwa anawafanyisha kwa njia ya kuongoza matakwa ya mtu kwa sharia inayoelezwa ya kuamrisha mema na kukataza mabaya.

Inasemekana kuwa siku moja Ibilisi alikutana na Mtume Muhammad(s.a.w.w) akamwambia: Hakika Mwenyezi Mungu amekusifu kwa jina la kiongozi, na mimi amenisifu kwa jina la mpotezaji. Lakini uongozi na upotezaji vyote vinatokana na Yeye, kwa hiyo wewe na mimi hatuna chochote.

Mtume akasema:Hapana! Mimi hubainisha batili na kuikataza na kuitolea kiaga kibaya;hali wewe una unafiki na hadaa ya ubatilifu; na mtu ana uwezo, upambanuzi na hiyari. Kwa hivyo mwenye kufanya hiyari nzuri (akaongoka) anajifanyia mwenyewe, na mwenye kuifanya mbaya (akapotea) pia anajifanyia mwenyewe.

Imesemekana kuwa Ibilisi alimwendea Nabii Isa(a.s.) akamuuliza: Si unadai kuwa wewe una daraja kubwa kwa Mungu? Basi hebu jitupe kutoka juu tuone,je atakuokoa? Masihi akasema: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayemjaribu mja wake na sio mja kumjaribu Mola wake.

Imesemekana kuwa baada ya gharika na kukauka maji, Ibilisi alimwendea Nuh(a.s.) akamwambia: Hakika wewe umenisaidia, kwa hiyo ninataka kukulipa. Nuh(a.s) : Akasema: Mungu apishe mbali! kumsaidia na kiumbe kama wewe. Akasema Ibilisi: Ndio hivyo. Nuh(a.s) : Akasema kwa nimekusaidia nini? Akasema Ibilisi: Umewaapiza watu wako ili waangamie wakaangamia, na nilikuwa nikijishughulisha usiku na mchana kuwapoteza kwa muda huo. Baada ya kuaangamizwa watu wako, sina kazi ya kufanya; sipati wa kumpoteza. Nuh(a.s) akasema: Utanilipa nini?

Akasema: Ninakunasihi usikasirike, kwa sababu hasira ya mtu inarahisisha kunifuata.Wala usihukumu kati ya watu wawili. Kama ukifanya hivyo, basi mimi nitakuwa wa tatu wenu. Wala usikae faragha na mwanamke kwani mimi hukuvutia kwake na yeye humvutia kwako. Kutokana na mantiki hii ya kishetani, inaonyesha kuwa Shetani ndiye mchochezi, na kwamba yeye huzipongeza silaha zenye kuangamiza.

HEKAYA

Inasemekana kwamba Mtume(s.a.w.w) na sahaba zake walimpitia mtu mmoja akirukuu na kusujudu kwa unyeyekevu. Wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni uzuri ulioje wa swala ya mja huyu! Mtume akasema:Huyu ndiye aliyemtoa baba yenu peponi .

LENGO LA HEKAYA

Lengo la hekaya hii ni kuwa haifai mtu kughurika na kuhadaika kwa zuhudi na ibada ya dhahiri.

Inasemekana kuwa Nabii Musa(a.s.) alikuwa akienda kuzungumza na Mola wake, ikatokea kukutana na Ibilisi, akamwambia Unakwenda wapi ewe uliyezungumza na Mwenyezi Mungu? Nabii Musa(a.s) akasema: Ninakwenda kwa Mola wangu kupokea maneno kutoka kwake na niko tayari kukuombea akusamehe kama utaniahidi kuungoa upotevu wako. Ibilisi akasema: Mimi sina haja ya kuombewa na wewe wala mwingine, bali ni juu Yake Yeye Mungu kutaka radhi yangu.(Mungu apishe mbali). Musa(a.s) akamwambia: Kafiri mkubwa we Mwenye laana! Ibilisi Akasema: Kwani nina dhambi gani mimi? Mungu alinitaka nimsujudie Adam, na mimi kwa iIkhlas yangu, siwezi kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Sasa tangu lini Ikhlas ikawa ni dhambi? Musa(a.s) akamjibu: Hii ni kuchezea maneno tu nako hakuwezi kukufaa wewe hata chembe, utaona yatakayokupata Kesho (Kiyama). Ibilisi akasema: Na wewe utaona nitakavyofanya kesho. Akasema: Utafanya nini?

Ibilisi akajibu: Nitamtaka Mwenyezi Mungu atimize ahadi Yake na nitamtolea hoja kwa kauli Yake:

﴿وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ ﴾

"Na rehema yangu hukienea kila kitu" (7:156)

"Nami ni kitu, kwa hiyo ni wajibu rehema Yake inipate (inienee).Kama mimi si chochote, basi sitahisabiwa wala kuadhibiwa.

Akasema Musa(a.s) : Hakika rehema ya Mwenyezi Mungu inamwenea yule mwenye mwelekeo nayo, na wewe uko mbali sana nayo. Ibilisi akasema: Basi nitafanya njia nyingine. Nitawaita wafuasi wangu waliopotea na nitamtaka Mwenyezi Mungu (s.w.t.) naye awaite wafuasi Wake waumini, halafu ipigwe kura.Hapo atajulikana nani mshindi mwenye sauti ya wengi. Kama Mwenyezi Mungu akikataa kura, nitafanya maandamano makubwa mpaka nipate ninayotaka.

Kigano hiki kina lengo la kwamba watu wa batili ni wengi zaidi kuliko watu wa haki, kwa sababu haki ni nzito na batili ni nyepesi; kama alivyosema Amirul Muminin, Ali(a.s.) :Yapasa mwenye akili kutoangalia wingi kuwa ni kipimo cha haki, wala uchache kuwa ni kipimo cha batili.

Katika Nahjul-Balagha, amesema:Hakika kundi kubwa ni watu wa batili hata wakiwa wengi; na kikundi kidogo ni watu wa haki hata wakiwa wachache.

Quran tukufu nayo inasema:

﴿وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴾

Na wengi wao ni wenye kuchukia haki. (23:70)

﴿وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴾

Lakini watu wengi hawajui.(12:21)

﴿وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ ﴾

Lakini watu wengi hawashukuru.(12:38)

﴿وَأَكْثَرُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ ﴾

Na wengi wao hawatumii akili (5:103)

﴿بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴾

Bali wengi wao hawaamini (2:100)

Kuna Hadith inayosema:Wakikutana wasaidizi wa Ibilisi wanaweza kujaza Mashariki na Magharibi . Na kwa madondoo haya, na mengineyo mengi, ndipo Shia wakasema: Khalifa wa Mtume ni kama Mtume; huchaguliwa na Mwenyezi Mungu; siye yule anayechaguliwa na watu. Huyo anayechaguliwa na watu ni Mfalme wa watu; si Khalifa wa dini. Ama mkuu wa dini, kwa Shia, ni yule mwenye sifa zilizoelezwa. Sio yule anayechaguliwa na watu wala si yule anayewekwa na kiongozi wa kidunia.

Na kwa nini isiwe hivyo? Je,watu wenye matamanio ya dunia wanaweza kuaminika kuongoza dini ya Mwenyezi Mungu? Basi kama ni hivyo na wawachague na kuwapigia kura Mitume, na walifaradhishe hilo kwa Mwenyezi Mungu. Ametakata kabisa Mwenyezi Mungu na yale wayasemayo madhalimu. Natija ya kimantiki ni kwamba Khalifa wa Mtume hawi, na hatakuwa, isipokuwa kwa usimulizi unaotokana na Mtume mwenyewe, na kwamba mkuu wa dini ni yule mwenye sifa zilizosimuliwa.

Mwenye kujipachika ukuu wa dini bila ya kuwa na sifa zilizotajwa, basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na ameruka patupu mwenye kuzua. Kwa hivyo basi, yote hayo yanafahamisha kuwa suala lolote haliwezi kuwa la kweli mpaka liwe limefuata haki; na kwamba mbinu za kucheza na maneno, haziwezi kuifanya batili iwe haki, au haki iwe batili, wala kisichoingia akilini kiingie akilini; hata kama hizo mbinu zitakuwa za hali ya juu kiasi gani.

Tutakalolifahamu ni kuwa mwenye mbinu hizo ni mwanafunzi hodari wa Ibilisi katika kuificha haki, na kuifunika na moshi wa hadaa.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَوَاعَدْنَا مُوسَىٰ ثَلَاثِينَ لَيْلَةً وَأَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤٢﴾

142. Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini. Na Nabii Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifu- ate njia ya waharibifu.

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٤٣﴾

143. Na alipofika Musa kwenye miadi yetu Na Mola wake akamsemeza, alisema: Mola wangu nionyeshe nikutazame. Akasema: Hutaniona, lakini tazama jabali, kama litakaa pahali pake ndipo utaniona. Basi Mola wake alipojionyesha kwa jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika, na Musa akaanguka hali amezimia. Alipozinduka alisema: kutakasika ni kwako! Natubu kwako na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي فَخُذْ مَا آتَيْتُكَ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

144. Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.

وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا سَأُرِيكُمْ دَارَ الْفَاسِقِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha na ufafanuzi wa kila jambo. Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi, Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Aya 142 – 145

MAANA

Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini.

Nabii Musa(a.s) alimtaka Mola wake amteremshie Kitab atakachowaongozea watu kwenye yale wanayoyahitajia katika mambo ya dini yao. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwahidi kuteremshia Kitab baada ya siku thalathini, na utaendelea ushukaji wake kwa siku kumi. Kwa ujumla itakuwa muda wa miadi na wa kushuka ni siku arubaini.

Hapa tumefafanua baada ya kueleza kwa ujumla kwenye Juz. 1 (2:51).

Na Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.

Nabii Musa alipoondoka alimwachia mahali pake ndugu yake Harun kwa Wana wa Israel; akampa nasaha kusimamia mambo yao na kuyatengeneza. Akamhadharisha na tabia zao zinazopondokea zaidi kwenye ufisadi. Ni jana tu walipokodolea macho ibada ya masanamu mpaka Nabii Musa akawaambia kuwa ni watu wajinga.

Harun akakubali nasaha kwa moyo mkunjufu, kama anavyokubali nasaha kaimu kiongozi mwenye ikhlasi kutoka kwa kiongozi wake mwaminifu.

Na alipofika Nabii Musa kwenye miadi yetu ambayo aliiweka Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumpa Tawrat,

Na Mola wake akamsemeza bila ya kumwona kwa sababu:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا ﴿٥١﴾

“Haikuwa kwa mtu aseme na Mwenyezi Mungu ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia au kumtuma mjumbe” (42:51)

Nabii Musa alisema:Mola wangu nionyeshe nikutazame.

Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nabii Musa hakumwomba Mola wake kumwona kwa ajili yake isipokuwa ni kwa ajili ya watu wake. Lakini hii inapingwa na kauli yake Nabii Musa pale aliposema:

Kutakasika ni kwako, na natubu kwako.

Vyovyote iwavyo ni kwamba Nabii Musa alitaka kuona, ni sawa iwe ni kwa ajili yake au kwa ajili ya wengine, sisi hatuoni ubaya wowote katika ombi hili, kwa sababu nafsi ya mtu ina hamu ya kutaka kujua yanayokuwa na yasiyokuwa hasa kuona kile ambacho kitazidisha utulivu wa nafsi.

Ibrahim(a.s) alitaka mfano wa hayo. Angalia Juz.3 (2:260).

Akasema: Hutaniona.

Kwa sababu kumwona Mwenyezi Mungu ni muhali. Tumeyazungumza hayo kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz. 1(2:51).

Lakini tazama jabali, kama litakaa mahali pake utaniona.

Nabii Musa aligeuka kwenye jabali ili amwone Mwenyezi Mungu, mara akaanguka chini na hakuona chochote. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifanya hivi ili kumfahamisha Nabii Musa(a.s) kwamba kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani kwake wala kwa mwingine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliuwekea sharti uwezekano wa kuonekana kwake kwa kutulia mahali jabali na jabali halikutulia, Kwa hiyo kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani.

Mfumo huu alioutumia Mwenyezi Mungu hapa ni kama ule wa kusema: Nitafanya hivi kunguru akiota mvi, Au akipita ngamia kwenye tundu ya sindano.

Basi Mola wake alipojionyesha kwenye jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika.

Yaani ilipodhihiri amri ya Mola wake; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾

“Akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu.” (89:22).

Yaani ikaja amri ya Mola wako.

Na Musa akaanguka chini amezimia.

Akawa hana fahamu kwa kishindo cha ghafla, Mwenyezi Mungu akamhurumia akazinduka.

Alipozinduka alisema: Kutakasika ni kwako! Natubu kwako. Kwa kukuomba kukuonana mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

Kwa sababu wewe ni mtukufu zaidi ya kuonekana kwa jicho.

Makusudio ya wa mwanzo sio kulingana na hisabu ya wakati; isipokuwa makusudio yake ni uthabiti na kutilia mkazo.

Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.”

Baada ya Nabii Musa kunyenyekea kwa muumba wake, Mwenyezi Mungu alimkumbusha neema yake, kubwa zaidi ni Utume na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Makusudio ya watu ni watu wa zama zake, kwa dalili ya kauli yake: Kwa ujumbe wangu. Kwani Mwenyezi Mungu aliwachagua Mitume wengi kabla ya Nabii Musa na baada yake.

Ama kuhusika kwake na kuzungumza naye hakuna dalili ya ubora zaidi. Ikiwa kunafahamisha ubora wowote basi kupelekewa roho mwaminifu kwa mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume ndio daraja ya juu na bora zaidi.

Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidaha na ufafanuzi wa kila jambo.

Makusudio ya mbao ni Tawrat kwa sababu ndiyo aliyoteremshiwa Nabii Musa, ndani yake mna mawaidha na upambanuzi wa hukumu.

“Kila jambo ni neno la kiujumla, lakini limekusudia mahsusi; yaani kila linalofungamana na maudhui ya risala miongoni mwa mawaidha, hukumu, misingi ya itikadi, kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu, Mitume yake na siku ya mwisho, na hukumu za sharia, kama halali na haramu. Kwa hiyo kauli yake: Mawaidha na maelezo ni ubainifu wa tafsiri ya kauli yake kila jambo. Kwa sababu makusudio ya maelezo ni kubainisha hukumu za kisharia.

Basi yashike kwa imara.

Yaani ichunge Tawrat na uitumie kwa ukweli wa nia.

Na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi.

Kila aliloliteremsha Mwenyezi Mungu ni zuri, lakini kuna yaliyo mazuri zaidi. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: “Na fanyeni wema, Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”

Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Yaani fasiki na dhalimu atafikwa na majanga. Haya ndiyo niliyoyafahamu kutokana na jumla hii kabla ya kupitia tafsir, Baada ya kuzipita nikakuta kauli kadhaa. Miongoni mwazo ni kwamba Mwenyezi Mungu atawaonyesha makao ya Firauni na watu wake baada ya kuangamizwa kwao. Nyingine inasema kuwa atawaonyesha ardhi ya Sham iliyokuwa mikononi mwa waabudu mizimu wakati huo.

سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki. Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاءِ الْآخِرَةِ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٧﴾

147. Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zime- poromoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ ﴿١٤٨﴾

148. Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti, Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

وَلَمَّا سُقِطَ فِي أَيْدِيهِمْ وَرَأَوْا أَنَّهُمْ قَدْ ضَلُّوا قَالُوا لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

NITAWAEPUSHIA AYA ZANGU

Aya 146 – 149

MAANA

Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki.

Wenye kufanya kiburi katika ardhi ni wale wanaopinga haki na wasiotaka kutawaliwa nayo. Kusema kwake bila ya haki ni kwa ufafanuzi, sio kwa kuvua; sawa na kusema: “Na wakiwaua mitume bila ya haki.”

Neno Aya katika Qur’an mara nyingine hutumia kuwa ni Aya zenye misingi ya itikadi na hukumu ya sharia na mfano wake. Mara nyingine hutumi- ka kuwa ishara yaani hoja na dalili zenye kuthibitisha uungu na utume.

Ikiwa makusudio ni maana ya kwanza katika Aya hii tunayoifasiri, basi maana yatakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazihifadhi Aya na kuzilinda zisipotolewe; sawa na kauli yake: “Hakika sisi ndio tuliouteremsha ukumbusho huu na hakika ndio tutakaoulinda”

Na ikiwa makusudio ni maana ya pili, yaani ishara kwa maana ya dalili na hoja, basi maana ni kwamba baada ya wapinzani kujiepusha nazo na kuacha kuzisikiliza, basi Mwenyezi Mungu ataachana nao, wala hatawategemeza kwenye imani. Tumekwisha elezea hilo mara kadhaa; kama vile katika kufasiri Juz.5 (4:88).

Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

Huu ni ubainifu wa hakika ya wenye kiburi na sababu inayowajibisha kiburi chao vilevile. Ama hakika yao ni kuwa wao hawajizuilii na uovu wala hawapondokei kwenye uongofu.

Sababu inayowajibisha hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea hoja na dalili; akawataka wazichunguze, wazizingatie na wazitumie vile inavyotakikana, wakakataa na wakaendelea kuzipinga tena bila ya kuzichunguza. Lau kwamba wao wangeliziitikia na kuzichunguza dalili hizo kungeliwapelekea kuamini na kuikubali haki; wala wasingelikua na kiburi na kufanya ufisadi katika nchi.

Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zimeporomoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na kukutana na Mola wake, basi yeye ni katika wale watakaoangamia kesho na yote yale aliyokuwa akijifaharisha nayo yatakuwa si lolote. Hayo ni malipo ya ukafiri wake na inadi yake.

Yamenipendeza yale aliyoyasema mfasiri mmoja Mwenyezi Mungu amughufirie na amrehemu, namnukuu: “Kuporomoka amali kunachukuliwa kama wanavyosema: ‘Ameporomokaa ngamia.’ ikiwa amekula mmea wenye sumu na tumbo lake likafura kisha akafa.

Hiyo ndiyo sifa ilivyo kwa batili inayowatokea wenye kukadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana na akhera, Mwongo hufura mpaka watu wanamdhania kuwa ni mkubwa mwenye nguvu, kisha huporomoka, kama alivyoporomoka yule ngamia, aliyekula mmea wa sumu.”

Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti.

Imetangulia kuelezwa katika Aya 142 kuwa Nabii Musa(a.s) alikwenda kwa miadi ya Mola wake, na kwamba yeye alimpa ukaimu nduguye Harun kwa watu wake. Vilevile imeelezwa katika Aya 138 kwamba Wana wa Israel baada ya kupita bahari walimtaka Nabii Musa awafanyie sanamu watakayoiabudu; si kwa lolote isipokuwa tu wameona ni vizuri waabudu masanamu.

Kwa hivyo mara tu Nabii Musa alipokuwa mbali nao waliitumia nafasi hiyo; Msamaria (Samiri): akakusanya mapambo ya wanawake akaten- geneza ndama; akatengeneza katika umbo ambalo liliweza kutoa sauti ya ndama.

Akawaambia huyu ni Mola wenu na Mola wa Musa; wakaingilia kumwabudu. Harun aliwakataza, lakini hakuweza kuwazuia, na hawakum- sikiliza isipokuwa wachache, Yametangulia kudokezwa hayo katika kufasiri Juz, 1 (2: 51), Pia yatakuja tena maelezo.

Aya hii tuliyo nayo, inatilia nguvu yale tuliyoyakariri katika Juzuu ya kwanza na ya pili, kuwa Israeli haithibiti ila kwenye misingi ya matamanio na hawaa; ikiwa ni kweli kuwa matamanio ni misingi.

Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

Haya ndiyo mantiki ya kimaumbile na akili ambayo inakataa mtu amwabudu Mungu aliyemtengeneza kwa mkono wake, lakini waisraili hawana akili wala maumbile au dini.

Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotoea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

Hii ndiyo sifa nzuri pekee na ndiyo ya kwanza na ya mwisho, iliyosajiliwa na Qur’an kwa waisrael kwa ujumla, bila ya kuangalia uchache wa wachache waliomwamini Nabii Musa hadi mwisho.

Baadhi ya Wafasiri wamechukulia dhahiri toba ya Bani Israel kwamba wakati huo ilikuwa ni masalia ya maandalizi ya wema, kisha masalia hayo yakaenda; wala haikubaki athari yoyote kwao ya kuonyesha kujiandaa kwa kheri. Kuchukulia huku hakuko mbali na ukweli na kunaashiriwa na Aya isemayo:

ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ﴿٧٤﴾

“Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi” Juz.1(2: 74)

Aya hii ni baada ya kisa cha ng’ombe ambacho kilitokea baada ya kuabudu ndama.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَلَمَّا رَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا قَالَ بِئْسَمَا خَلَفْتُمُونِي مِن بَعْدِي أَعَجِلْتُمْ أَمْرَ رَبِّكُمْ وَأَلْقَى الْأَلْوَاحَ وَأَخَذَ بِرَأْسِ أَخِيهِ يَجُرُّهُ إِلَيْهِ قَالَ ابْنَ أُمَّ إِنَّ الْقَوْمَ اسْتَضْعَفُونِي وَكَادُوا يَقْتُلُونَنِي فَلَا تُشْمِتْ بِيَ الْأَعْدَاءَ وَلَا تَجْعَلْنِي مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿١٥٠﴾

150. Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika. Akasema: Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu na akazitupa mbao na akamkata kichwa ndugu yake akimvuta kwake. Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِأَخِي وَأَدْخِلْنَا فِي رَحْمَتِكَ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿١٥١﴾

151. Akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

إِنَّ الَّذِينَ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ سَيَنَالُهُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَذِلَّةٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُفْتَرِينَ ﴿١٥٢﴾

152. Hakika wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia, Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi.

وَالَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِهَا وَآمَنُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٥٣﴾

153. Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaamini, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

وَلَمَّا سَكَتَ عَن مُّوسَى الْغَضَبُ أَخَذَ الْأَلْوَاحَ وَفِي نُسْخَتِهَا هُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ هُمْ لِرَبِّهِمْ يَرْهَبُونَ ﴿١٥٤﴾

154. Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

ALIPORUDI MUSA KWA WATU WAKE

Aya 150-154

MAANA

Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika.

Nabii Musa(a.s) alipokuwa mlimani akizungumza na Mola wake mtuku- fu, alipewa habari na Mola wake kuwa watu wake wameabudu ndama baada yako; kama inavyofahamisha Aya isemayo:

قَالَ فَإِنَّا قَدْ فَتَنَّا قَوْمَكَ مِن بَعْدِكَ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ ﴿٨٥﴾ فَرَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا ﴿٨٦﴾

“Akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako bada yako na Msamaria amewapoteza. Nabii Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika.” (20:85-86).

Ghadhabu ilidhihiri kwa kusema:Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu.

Aliwaacha kwenye Tawhid, lakini aliporudi aliwakuta kwenye shirk.

Ama amri ya Mola wao ambayo hawakuingoja ni kumngoja Nabii Musa siku arubaini.

Hii inafahamishwa na Aya isemayo:

أَفَطَالَ عَلَيْكُمُ ﴿٨٦﴾

“Je, umekuwa muda mrefu kwenu?” (20:86).

Kama ambavyo ghadhabu yake ilidhihiri kwa kauli, Vilevile ilidhihiri kwa vitendo:

Na akazitupa mbao na akamkamata kichwa ndugu yake akimvuta kwake.

Wamesema baadhi ya maulama kuwa Nabii Musa alitupa Tawrat nayo ina jina la Mwenyezi Mungu na akamvuta nduguye Harun naye ni mja mwema. Imekuwaje na Nabii Musa ni ma’sum? Baada ya kujiuliza huku wakaanza kuleta taawili na kutafuta sababu.

Ama sisi hatu hatuleti taawili wala kutafuta sababu, bali tunayaacha maneno na dhahiri yake. Kwa sababu isma haibadilishi tabia ya maumbile ya binadamu na kumfanya ni kitu kingine wala haimuondolei sifa ya kuridhia na kukasirika hasa ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; tena ikiwa ni ghafla kama ilivyomjia Nabii Musa(a.s) .

Amekaa na watu siku nyingi akiwafundisha tawhid na dini ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kutulia imani yao; halafu ghafla tu waache yote na waingie kwenye shirki bila ya sababu yoyote ya maana.

Wengine wamesema kuwa Nabii Musa alikuwa mkali na Haruna alikuwa mpole. Sisi tunasemaNabii Musa alikuwa mwenye azma kubwa, mwenye nguvu ya alitakalo na mwenye kujiamini; na Haruna naye alikuwa chini kidogo ya Nabii Musa kulingana na masilahi.

Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

Anakusudia madui ni wale walioabudu ndama; kama kwamba anamwambia nduguye: unachinganya mimi na maadui zangu na maadui zako, tena unanivuta mbele yao wanicheke. Vipi unanichanganya nao kwenye hasira zako na mimi niko mbali nao na vitendo vyao? Tena nimewapinga na wala sikuzembea kuwapa nasaha na tahadhari!

Hapo Nabii Musa akarudi chini na kumuonea huruma nduguye, akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

Alijiombea maghufira yeye mwenyewe kwa ukali wake kwa nduguye, kisha akamuombea maghufira nduguye kwa kuhofia kuwa hakufanya bidii ya kuwazuia na shirk. Bila shaka Mwenyezi Mungu, aliitikia maombi ya Nabii Musa kwa sababu yeye ni mwenye kurehemu kushinda wenye kurehemu; na pia kujua kwake ikhlasi ya Nabii Musa na nduguye Harun.

Hakiaka wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi

Unaweza kuuliza kuwa : dhahiri ya Aya hii nikuwa wale walioabudu ndama wamekasirikiwa na Mwenyezi Mungu na hali wao walitubia na kuomba maghufira; kama ilivyoeleza Aya ya 149 ya Sura hii na Aya nyingine inasema:

ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾

“Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga; kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila shaka Mola wako ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu” (16:119).

Kwa hiyo vipi walazimiane na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ya milele na laana ya daima?

Baadhi wamejibu kuwa : waabudu ndama waligawanyika mafungu mawili baada ya kurudi Nabii Musa, Kundi moja lilitubia toba sahihi. Hao ndio waliosamhewa na Mwenyezi Mungu. Na wengine waling’ang’ania ushirikina; kama vile Msamaria na wafuasi wake. Hawa ndio waliokasirikiwa na Mwenyezi Mungu na akawadhalilisha katika maisha ya duniani.

Ilivyo ni kwamba kwenye Aya hakuna ufahamisho wowote wa makundi haya. Jibu linalonasibu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu alijua kuwa Mayahudi milele hawatubii wala hawatatubia toba ya kiuhakika ambayo hawatarudia. Hakia hii inafahamishwa na tabia yao na sera yao. Kwani wao walikuwa na wanaendelea kuwa ni watu wasiokatazika wala kukanyika na ufisadi na upotevu ila kwa kutumia nguvu peke yake.

Swali la pili : Mayahudi leo wanayo dola inayoitwa Israil, kwa hiyo hawana udhalili; je hili si jambo linalopingana na dhahiri ya Aya?

Jibu : Hapana! Tena hapana! Hakuna dola wala haitakuwa dola ya Mayahudi milele; kama kilivyosajili kitabu cha Mwenyezi Mungu. Israil sio dola, kama dola nyingine; isipokuwa ni kambi ya jeshi; kama vile askari wa kukodiwa waliowekwa na wakoloni kulinda masilahi yao na kuvunja nguvu za wazalendo. Tumeyathibitisha hayo katika kufasiri Juz.4 (3:112) na Juzuu nyenginezo.

Vilevile katika kitabu Min huna wa hunaka (Huku na huko) mlango wa man baa’ dinahu li shaitan (Mwenye kumuuzia dini yake shetani)

Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaami- ni, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

Maana ya Aya yako wazi, na mfano wake umekwishapita mara nyingi. Lengo la kutajwa kwake baada ya Aya iliyotangulia ni kutilia mkazo kwamba mwenye kutubia na akarudi kwa Mola wake kwa ikhlasi na asirudie maasi, kama walivyofanya waisrail, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamrehemu, awe ni mwisraili au Mkuraysh n.k.

Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

Nabii Musa ni Mtume aliye ma’sum, hilo halina shaka, lakini yeye ni binadamu, anahuzunika na kufurahi, anridhia na kukasirika. Hasira zilimpanda alipoona watu wake wamertadi dini ya Mwenyezi Mungu. Hasira aliiacha alipombwa na ndugu yake, Harun; na Mungu akamwahidi kuwaadhibu walortadi.

Baada ya Nabii Musa kurudia hali yake ya kawaida, alizirudia zile mbao alizokuwa amezitupa alipokuwa amekasirika na akatulizana kutokana na yaliyomo ndani yake katika uongofu kwa yule ambaye moyo wake utaifungukia kheri na rehema zilizomo kwa yule anayeogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha kumpa radhi na rehema kila mwenye kumtii kwa kuogopa adhabu yake, na kumletea adhabu na mateso kila mwenye kuasi kwa kubweteka na rehema yake.

وَاخْتَارَ مُوسَىٰ قَوْمَهُ سَبْعِينَ رَجُلًا لِّمِيقَاتِنَا فَلَمَّا أَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّايَ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا إِنْ هِيَ إِلَّا فِتْنَتُكَ تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَاءُ وَتَهْدِي مَن تَشَاءُ أَنتَ وَلِيُّنَا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الْغَافِرِينَ ﴿١٥٥﴾

155. Na Musa akachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi? Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na kumwongoza umtakaye, Wewe ndiye mlinzi wetu. Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiye bora wa kughufiria.

وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾

156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera, Sisi tunarejea kwako. Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye; na rehema yangu imekienea kila kitu. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini ishara zetu.

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾

157. Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawaahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale walioamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, Hao ndio wenye kufaulu.

HAIKUWA ILA NI ADHABU YAKO

Aya 155 – 157

MAANA

Na Musa akawachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu.

Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu Aya hii na zikagongana kauli zao katika kuifasiri. Wakatofautiana katika kubainisha miadi, kuwa je, ni miadi ya kuteremshwa Tawrat au mingine?

Vilevile wametofautiana kuwa ni kwa nini Nabii Musa aliwachagua watu sabini katika watu wake, Je, ni kwa kuwa wao walimtuhumu Nabii Musa na kumwambia hatutakuamini mpaka tusikie maneno ya Mwenyezi Mungu kama unavyosikia wewe; ndipo akasuhubiana nao ili asikie, kama alivyosikia; au ni kwa sababu nyingine?

Vilevile wametofautiana wafasiri katika sababu ambayo aliwaadhibu Mwenyezi Mungu, Hatimae wakahitalifiana kuwa je, mtetemeko uliwaua au ulikurubia tu kuvunja migongo yao, lakini hawakufa?

Katika Aya hakuna kidokezo chochote cha yale waliyoyachagua kikundi katika wafasiri. Linalofahamika ni kuwa tu, Nabii Musa aliwachagua watu sabini ili aende nao kwa miadi ya Mola wake. Kwa hali ilivyo ni kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Nabii Musa hafanyi ila aliloamrishwa; na kwamba Mwenyezi Mungu ali- wateremshia hao sabini aina ya adhabu kulingana na hekima ilivyoka.

Basi hatuna cha kuthibitisha miadi ilivyo kuwa wala sababu ya kuchagua au ya adhabu.

Ni kweli kwamba kauli ya Nabii Musa kumwambia Mwenyezi Mungu:Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi? inafahamisha kwamba wao walifanya yaliyowajibisha maangamizi, lakini halikubainishwa walilolifanya; nasi hatuna haki ya kusema tusiyoyajua.

Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeli- waangamiza wao na mimi zamani!

Nabii Musa alichagua watu sabini walio bora katika watu wake akaenda nao kwenye miadi ya Mola wake, walipofika huko wakaangamia wote akabakia, peke yake. Hilo ni tatizo la kukatisha tamaa hakuna la kufanya tena. Je, arudi peke yake kwa wa Israel? Atawajibu nini wakimuuliza watu wao?

Hakuna kimbilio kabisa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Basi akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu amwondolee tatizo hilo na akatamani lau Mwenyezi Mungu angelimwangamiza pamoja nao kabla ya kuja nao hapa.

Kisha akasema kumwambia mtukufu aliye zaidi:

Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi?

Yaani wewe ni mtukufu na mkuu kuliko kufanya hivyo. Kwa sababu wewe ni Mpole na Mkarimu.

Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na humwongoza umtakaye.”

Neno Fitna lililofasiriwa adhabu hapa, lina maana nyingi; ikiwemo upote- vu na ufisadi; kama ilivyo katika Aya ya 26 ya Sura hii. Maana nyingine ni kupigana na majaribu, mara nyingi hutumiwa kwa maana ya adhabu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ﴿٢٥﴾

“Na jikingeni na adhabu ambayo haitawasibu waliodhulumu peke yao” (8:25).

Haya ndiyo makusudio yake katika Aya hii tuliyonayo, Dhamir ya hilo inarudia tetemeko ambalo limekwishatajwa. Maana ya kumpoteza amtakaye, ni kuwa Mwenyezi Mungu humpelekea tetemeko, ambalo ndio adhabu, yule amtakaye katika waja wake, na maana ya kumwongoza ni kumwepushia tetemeko amtakaye.

Maana ya kijumla ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) huteremsha adhabu kwa amtakaye anayestahiki na kumwondolea asiyestahiki. Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli yake halikuwa hilo ila ni adhabu yako, maana yake yanafungamana na yaliyotangulia na yaliyo baada yake; na kwamba haijuzu kuitolea dalili kuwa upotevu unatokana na Mwenyezi Mungu.

Vipi Mwenyezi Mungu ampoteze mtu kisha amwaadhibu kwa upotevu huo? Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kutaka kuwadhulumu waja. Hakika Shetani ni adui mwenye kupoteza na inatosha kuwa Mola wako ni mwongozi na mwenye kunusuru.

Kwa maelezo zaidi rudia Juz.1 (2:26).

Wewe ndiye mlinzi wetu, Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiwe bora wa kughufuria. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera. Sisi tunarejea kwako”

Hakuna tafsir bora ya Munajat huu, kama kauli ya bwana wa mashahidi, Imam Husein bin Ali(a.s) wakati alipozungukwa na maelfu kila upande akiwa peke yake. Akakimbilia kwa Mola wake na kumtaka hifadhi dhidi ya maadui zake akisema:

“Ewe Mola wangu wewe ndiye matarajio yangu katika kila shida, Kila jambo lililonishukia wewe ni tegemeo, Ni matatizo mangapi ya kukatisha tamaa, ya kuondokewa na marafiki na kufuatwa na maadui, uliyoniteremshia, kisha nikakushitakia wewe, kwa kuwa sina mwingine zaidi yako, nawe ukanitatulia na kunifariji! Basi wewe ndiye mtawalia kila neema,mwenye kila hisani na mwisho wa matakwa yote!”

Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye katika wananostahiki adhabu.

Kwa sababu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanapitia kwenye haki na uadilifu tu, hakuna mchezo wala dhulma mbele ya Mwenyezi Mungu.

Razi anasema: “Amesoma Hasan: Usibu bihi man Asaa kwa sin (nitam- sibu nayo mwenyewe kufanya uovu), na Shafii amechagua kisomo hiki.”

REHMA YA MWENYEZI MUNGU INAMFIKIA IBLISII

Qur’an hutumia neno Rehma ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya msaada wake na kwa thawabu zake. Maana ya usaidizi kutoka kwake Mwenyezi Mungu ni kwamba vitu vyote vilivyoko, hata Iblisi, vinamhitajia Mwenyezi Mungu katika kubakia kwake na kuendelea kwake; kama ambavyo vinamhitajia yeye katika asili ya kupatikana kwake, na kwamba yeye ndiye anayevisaidia kubaki wakati wote, kiasi ambacho lau msaada wake huo utakiepuka kitu kitambo kidogo cha mpepeso wa jicho, basi kitu hicho hakitakuwako tena.

Ufafanuzi zaidi wa rehma hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ﴿٤٥﴾

“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, asin- geliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja” (35:45).

Rehma hiyo ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:Na rehma yangu imekienea kila kitu hata Iblisi aliyelaaniwa. Ama rehma kwa maana ya thawabu, Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa anayemwamini na kumcha. Ndiyo aliyoiashiria kwa kusema kwake. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa maasi na wakafuata amri ya Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake.

Na wanaotoa Zaka.

Ametaja Zaka badala ya Swala. Kwa sababu mtu hupituka mpaka kwa kujiona amejitoshea.

Na wanaoziamini ishara zetu ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika.

Rehma ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kwa maana ya thawabu haipati isipokuwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu, akatoa mali kwa kupenda kwake na akauamini utume wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) kama utamfikia ujumbe wake.

Amehusisha kutaja mali kutokana na tulivyoyadokezea, na pia kuwa mazungumzo ni ya Mayahudi ambao mali ndio Mola wao hakuna mwingine isipokuwa yeye. Mwenyezi Mungu amemsifu Nabii Muhammad(s.a.w.w) , katika Aya hii kwa sifa hizi zifuatazo:-

1.Nabii Asiyesoma Wala Kuandika.

Hiyo ni sifa inayomhusu yeye tu, kinyume cha Mitume wengine, kutambulisha kuwa licha ya kuwa hivyo lakini amewatoa watu kutoka katika giza mpaka kwenye mwangaza, akaathiri maisha ya umma wote wakati wote na mahali kote.

2.Ambaye Wanamkuta Ameandikwa Kwao Katika Tawrat Na Injil.

Rudia Juz.1 (2:136) na Juz.6 (4:163).

3.Ambaye Anawaamrisha Mema Na Anawakataza Maovu.

Rudia Juz, 4 (3:104 - 110).

4.Na Anawahalalishia Vizuri Na Kuwaharamishia Vibaya.

5.Na Kuwaondolea Mizigo Na Minyororo Iliyokuwa Juu Yao.

Makusudio ya minyororo ni mashaka. Mwenyezi Mungu aliwaharamishia waisrail baadhi ya vitu vizuri, vilivyodokezwa kwenye Juz.8 (6:146); kama ambavyo sharia ya Nabii Musa ilikuwa ngumu na yenye mashaka; kiasi kwamba mwenye kutubia katika waisrael hakubaliwi toba yake ila kwa kujiua:

فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ﴿٥٤﴾

“Basi tubuni kwa Muumba wenu na jiueni” Juz.1 (2:54).

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaambia waisrael ambao wamemkuta Nabii Muhammad(s.a.w.w) kwamba wao wakisilimu watahalalishiwa vizuri vilivyokuwa haramu, na atawaondolea mashaka katika taklifa. Kwa sababu Nabii Muhammad ametumwa na sharia nyepesi isiyo na mikazo.

Basi wale waliomwamini.

Makusudio ni waliomwamini Nabii Muhammad(s.a.w.w) miongoni mwa Mayahudi na wengine.

Na wakamheshimu.

Yaani kumsaidia katika mwito wake na kumheshimu kwa cheo chake.

Na wakamsaidia juu ya maadui zake.

Na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye.

Yaani wakafanya matendo kwa mujibu wa Qur’an.Hao ndio wenye kufaulu duniani na akhera.

6

7

8

9

10

11

12

13

14

15