TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Mwandishi:
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
Kundi:

Matembeleo: 35751
Pakua: 3052


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Juzuu 9 Juzuu 10 Juzuu 11
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 20 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 35751 / Pakua: 3052
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU

BISMILLAH

Tamko hili tukufu ni nembo maalum ya Waislamu. Kwalo Wanaanzia maneno na vitendo vyao vyote; na iko kwenye daraja ya pili baada ya shahada mbili. Ama wasiokuwa Waislamu, huanza: Kwa jina Lako ewe Mwenyezi Mungu Kwa jina Lake Mtukufu, kwa jina la Mwenye kuanza, na Mwenye kuishiliza au Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu n.k.

Huondolewa hamza katika neno ism katika Bismillahi, linapotamkwa na kuandikwa kwa sababu ya kutumiwa sana. Na, huondolewa hamza kwa kutamkwa, na sio kwa kuandika mahali pengine; kama vile sabbihisma rabbikal -aala na Uqsimu billah.

MAANA YA TAMKO: ALLAH

Tamko: Allah (Mwenyezi Mungu) lina maana ya Mwenye kuabudiwa kwa haki, ambaye husifika na sifa zote za utukufu na ukamilifu, wala hakisifiwi kwa sifa hiyo kitu kingine chochote.

Inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu ana jina moja Tukufu, na kwamba atakayelijua, basi atamiminikiwa na heri na atakuwa na miujiza. Lakini sisi tunaamini na kuitakidi kwamba kila jina la Mwenyezi Mungu ni tukufu; yaani huyo Mwenyezi Mungu ni Mtukufu. Kwa sababu haiwezekani kabisa kuufanya upande mmoja ni bora kuliko upande mwingine, kuboresha kutaleta ushirika na kuzidi; na ambaye hana mfano wa kitu chochote, hawezi kushirikiana na yeyote katika kitu.

MAANA YA NENO: RAHMAN

Neno: Rahman (Mwingi wa Rehema) ni sifa.Limechukuliwa kutoka katika Rahma (Rehema). Maana yake kwa upande wa Mwenyezi Mungu ni kufanya hisani na kwa upande wa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, lina maana ya upole.

BISMILLAH

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu wa moyo. Limezoeleka kutumiwa kwa maana ya dhati yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), likawa ni katika majina mema ya Mwenyezi Mungu.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿قُلِ ادْعُوا اللَّـهَ أَوِ ادْعُوا الرَّحْمَـٰنَ أَيًّا مَّا تَدْعُوا فَلَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ﴾

Sema! Muombeni (kwa jina la) Mwenyezi Mungu, au muombeni (kwa jina la) Mwingi wa rehema; kwa jina lolote mnalomwita (itafaa), kwani ana majina mema. (17:110)

MAANA YA NENO: RAHIM

Neno: Rahim (Mwenye kurehemu) vile vile, ni sifa. Limechukuliwa kutoka katika neno Rahma. Wafasiri wengi wametofautisha kati ya matamko haya (Rahman na Rahim) kwamba Rahman ni rehema yenye kuenea kwa muumini na kafir; na Rahim ni rehema yenye kuwahusu waumini peke yao. Wakasema: Ewe Mwingi wa Rehema katika dunia na Akhera na ewe Mwenye Kurehemu akhera tu. Ama mimi nasema: Ewe Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu katika dunia na akhera.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَهُمْ يَقْسِمُونَ رَحْمَتَ رَبِّكَ﴾

Je,wao wanaigawa rehema ya Mola wako? (43:32).

MAANA YA BISMILLAAHI RAHMANI RAHIM

Kwa ujumla maana ya Bismillaahi rahmani rahim ni kwamba: wewe unaanza kitendo chako kwa kumtaka msaada ambaye rehema Yake imekienea kila kitu, na kusajili katika nafsi yako kwamba unayoyafanya ni kwa jina lake, sio kwa jina lako wala kwa jina la mwingine yeyote asiyekuwa Yeye. Si kama vile anavyosema mtumishi wa serikali kuwaambia raia: Kwa jina la taifa ninawaambia kadhaa. Bismillah inafahamisha kwamba kitendo unachofanya ni halali hakina shaka ya haramu. Kama kitendo ni haramu na ukakifanya kwa Bismillaah, basi utakuwa umeasi mara mbili kwa mpigo:

Kwanza : ni kuwa kitendo chenyewe ni haramu.

Pili : ni kuwa umesema uongo kwa kukinasibisha na Mwenyezi Mungu. Ametakasikia Mwenyezi Mungu na hayo kabisa.

HUKUMU YA BISMILLAH

Hukumu ya Bismillah Kwa upande wa Shia Imamiya, ni sehemu ya sura, na wamewajibisha kuisoma kwa sauti katika swala ambayo ni wajibu kusoma Alhamdu na sura kwa sauti; kama vile swala ya Asubuhi (Al-fajr) na rakaa mbili za mwanzo za swala ya Maghrib na Isha. Ni sunna kusoma kwa sauti katika swala ambayo haisomwi kwa sauti kama vile swala ya Adhuhuri na Alasiri.

Hanafi na Maliki wamesema kuwa inajuzu kuiacha Bismillaah katika swala, kwa sababu si sehemu ya sura. Shafi na Hambali wamesema ni sehemu ya sura; ispokuwa Hambal wamesema kuwa isisomwe kwa sauti wakati wowote wa swala. Shafi nao kwa upande wao, wakasema isomwe kwa sauti katika swala ya Asubuhi (Al-fajr) na rakaa mbili za Maghribi na Isha.

Hapa kauli ya Shafi na Hambal haziko mbali na kauli ya Imamiya.

Kwa ujumla ni kwamba herufi hizi za Bismillah zinatengeneza jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu na sifa Zake. Hutamkwa na kuandikwa kama maneno mengine, lakini lina heshima na hukmu mahsusi. Haijuzu kuliandika juu ya karatasi, au kwa wino, kalamu au kitu chochote kilicho najisi.Vile vile haijuzu kuligusa bila ya twahara.

Wataalamu wa Fiqhi wa Kiimamiya wamefutu kwamba mwenye kuutupa msahafu makusudi katika uchafu, kuupiga teke, kuupasua kwa dharau, au kuufanyia kitu chochote kinachoonyesha dharau, basi amekuwa kafiri aliyeritadi. Msemaji mmoja amesema kuwa Sura ya Fatiha imekusanya maana yote ya Qurran, na kwamba Bismillah imekusanya maana yote ya Fatiha, na herufi Ba katika Bismillah imekusanya maana yote ya Bismillah. Hatimaye herufi Ba inakuwa imekusanya maana yote ya Quran.Msemaji huyu ni kama yule anayejaribu kuuingiza ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake katika yai bila ya kulikuza yai hilo au kuufanya mdogo ulimwengu!

NEMBO YA UISLAMU

Nilisoma makala katika gazeti la Al-Jumhuriyya la Misri la tarehe 21 Aprili 1967 yaliyoandikwa na Dhiyau Rayis, kwamba yeye alisoma makala katika jarida la fasihi la mwandishi mashuhuri wa Kiarabu akisema (Huyo mwandishi) alipokuwa Uingereza, aliwahi kubishana vikali na msomi mmoja Mwingereza kuhusu Uislamu na Ukristo. Akasema yule Mwingereza kupingana na Waislamu wote: Mimi ninaifupisha misingi yote ya Kikristo kwa neno moja tu,Upendo, Je unaweza wewe Mwislamu kuleta tamko linalokusanya misingi ya Kiislamu? Yule mwandishi akajibu: Ndio neno hilo ni Tawhid.

Baada ya Rayis kunakili mazungumzo haya akasema: Jawabu halikuwa sawa. Akataja sababu kadhaa za kutomwafiki kwake, kisha akasema: Lau swali hili ningeulizwa mimi, ningelijibu kuwa ni Rehema. Akatoa dalili kwa Aya nyingi na Hadith nyingi, akianzia na Bismillahir rahmanir rahim mpaka Aya inayosema:

﴿ وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ﴾

Nasi hatukukutuma ila uwe rehema kwa walimwengu. (21:107)

Amesema kweli Rayis kwamba jawabu la yule mwandishi halikuwa sawa.Lakini hata yeye Rayis pia jawabu lake halikuafiki,kwa kuchagua neno rehema.Kwa sababu hakuzidisha kitu katika aliyoyasema Mwingereza. Amechukua neno upendo na kulifasiri rehema. Kwa hiyo Uislamu unakuwa hautofautiani na Ukristo.

Lau mimi ningelikuwa pamoja na yule mwandishi, ningelijibu kwa neno unyoofu.(msimamo) Kwa sababu ni neno lenye kukusanya unyoofu katika itikadi tawhidi, vitendo, maadili, hukumu, na mafundisho yote yaliyo na rehema mapenzi na kusaidiana. Rehema ni moja katika misingi ya Kiislamu na sio Uislamu kamili; kama vile ambavyo tawhidi ni msingi katika misingi ya Uislamu na sio misingi yake yote.

Unyoofu ndio kipimo sahihi cha ukamilifu ambao mtu aweza kuufikilia wema wa dunia na Akhera. Ndio maana tunakariri katika swala zetu usiku na mchana: Tuongoze njia iliyonyooka. Mwenyezi Mungu amesema kumwambia Mtume wake mtukufu(s.a.w.w) :

﴿فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴾

Endelea na unyoofu kama ulivyoamrishwa, (wewe) na wale wanaoelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe; wala msiruke mipaka.Hakika Yeye anayaona mnayoyatenda. (11:112)

Amesema tena:

﴿إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴾

Hakika wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakafuata unyoofu, hao Malaika huwateremkia (wakiwaambia): Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa Pepo mliyokuwa mkiahidiwa. (41:30)

Hakuna kitu kinachofahamisha zaidi kwamba unyoofu ni muhimu, kuliko neno la Ibilisi aliyelaaniwa:

﴿قَالَ فَبِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ﴾

Basi nitawakalia (waja wako) katika njia yako iliyonyooka... (7:16)

Kuna Hadith tukufu inayosema kuwa Sufyan Thaqafi alimwambia Mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie neno ambalo sitamuuliza mtu mwingine baada yako milele.Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia:Sema nimemwamini Mwenyezi Mungu, kisha ufuate unyoofu (msimamo).

Kwa ufupi maana ya unyoofu ni kuwa ndani ya mipaka ya Mwenyezi Mungu bila ya kukengeuka na haki kwa kuifuata batili na kuacha uongofu na kuwa katika upotevu. Vile vile kuwa kwenye njia iliyonyooka, njia ya (wale) ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, sio ya wale walioghadhibikiwa wala waliopotea.

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

AL - FATIHA

BISMILLAH (UFUNGUZI)

SURA YA KWANZA KUSHUKA

Wametofautiana kuhusu mahali iliposhuka, imesemwa kuwa ni Makkah wengine wakasema ni Madina bali kuna kundi jengine linasema kuwa imeshuka mara mbili Makkah na Madina.Hata hivyo wafasiri wengi wamesema imeshuka Makkah.

Tofauti hii, kwa hakika, haina faida kwani surah hii tukufu haina Aya zozote zinazotofautiana kimaana kwa kutofautiana kushuka. Majina yake Wametaja majina mengi; yaliyo maarufu ni haya yafuatayo:-

Faatiha (ufunguzi) : Kwa sababu ndiyo sura ya kwanza katika msahafu, na ni wajibu kuisoma mwanzo wa swala. Pia mafundisho, kwa ujumla, yalikuwa yakianzwa kwa sura hiyo.

Al-Hamdu : kwa sababu ndilo tamko la mwanzo katika sura hiyo.

Ummul-Kitab na Ummul-Quran (mama wa Quran) : kwa sababu imetangulia sura nyingine, ijapokuwa ni kwa kimandishi tu.Kwani mama huwatangulia wanawe. Na kwa vile imekusanya misingi miwili; kutaja utawala wa Mungu na utumwa wa mja, na mambo mawili hayo ndiyo nguzo ya mafundisho ya Quran.

Sabu’ul-Mathani (Saba mbili) : kwa sababu ina aya saba, au ina Aya saba zinazorudiwa mara mbili katika swala, au ni kwa sababu inataja maambo mawili: Mola na mja wake.

Vyovyote iwavyo majina haya yana mwelekeo kidogo.

Ayah 1-7

﴿بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴾

1.Kwa jina la Mwenyezi Mungu,Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

﴿الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴾

2.Sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe (vyote).

﴿لرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴾

3.Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu.

﴿ مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ﴾

4.Mwenye kumiliki Siku ya Malipo.

﴿يَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴾

5.Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada.

﴿اهْدِنَا الصِّرَاطَ الْمُسْتَقِيمَ﴾

6.Tuongoze njia iliyonyooka.

﴿صِرَاطَ الَّذِينَ أَنْعَمْتَ عَلَيْهِمْ غَيْرِ الْمَغْضُوبِ عَلَيْهِمْ وَلَا الضَّالِّينَ ﴾

7.Njia ya (wale) uliowaneemesha; Sio ya (wale) waliokasirikiwa wala ya (wale) waliopotea.

SIFA NJEMA (ZOTE) NI ZA MWENYEZI MUNGU

Sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe (vyote).

Jumla hii ni habari, kwa maana ya insha; Kwa sababu msomaji anakusudia kuleta sifa njema za Mwenyezi Mungu, wala sio kutoa habari za kuthibitisha sifa Zake njema.

Jumla hiyo ina maana ya mafunzo kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa waja wake, jinsi watakavyomsifu Mwenyezi Mungu. Yaani:Semeni enyi Waja wangu! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.

Maana ya sifa njema (zote) ni za Mwenyezi Mungu, ni kumsifu kwa kukusudia kumwadhimisha katika hali zote, hata katika madhara. Amirul Muminin(a.s) anasema katika moja ya khutba zake za Nahjul-Balagha:

Tunamsifu Mwenyezi Mungu kwa neema zake, kama tunavyomsifu kwa balaa.

Muhammad, Ahmad, Mahmuud na Hamdaan, ni majina yaliyochukuliwa kutoka katika neno Al-Hamdu. Neno Hamd linakuja kwa kukisifu kitu unachokiridhia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa anataja Mahmuud (chenye kusifika) akisema:

﴿عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا﴾

Huenda Mola wako akakuinua cheo chenye kusifika (17:79)

Neno: Rabb linaweza kutumiwa kwa maana ya Bwana na Mwenye kumiliki.Maana zote mbili zinasihi hapa, lakini maana ya Mola Muumbaji ndiyo inayoelekea zaidi katika aya hii tukufu.

MAKUSUDIO YA ALALAMIN (VIUMBE)

Makusudio ya Alalamin (viumbe) hapa ni; kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo linaenea kwa viumbe vyote.

MAANA YA RABBIL-AALAMIN (MOLA WA VIUMBE VYOTE)

Maana ya Rabbil-Aalamin (Mola wa viumbe vyote) ni Muumbaji wa kila kitu, na mwenye kupangilia vizuri.

NENO MOLA

Neon: Mola linafahamisha utukufu; yaani:Hakika mimi ninamsifu Mwenyezi Mungu kwa sababu Yeye ni Mola wa viumbe vyote.

MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

Mwingi wa rehema mwenye kurehemu: Maelezo yake yameshapita katika maelezo ya Bismillah Miongoni mwa maneno ya Amirul Muminin katika kumsifu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:Ghadhabu haimshughulishi (asiwe) na rehema wala rehema haimshughulishi (asiwe) na mateso.

Nilivyofahamu jumla mbili hizi ni kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa waasi, na adhabu yao kesho, haimzuii Yeye kuwarehemu katika maisha haya wanayostarehe kwa neema yake na kwamba rehema Yake kesho haiwaondolei waumini balaa na maovu katika maisha haya. Mwenye kumiliki siku ya malipo Neno Din lina maana nyingi; miongoni mwayo ni malipo. Na maana haya ndiyo yanayonasibiana na hapa, ambapo siku hiyo italipwa kila nafsi yale iliyoyachuma.

NENO MAALIKI

Neno: Maaliki husomwa kwa alifu, kwa maana ya kuhusisha (umilikaji); kama inavyosemwa: Fulani ndiye mwenye kumiliki bustani hii (mwenye kuhusika nayo). Pia husomwa Maliki bila ya Alifu (kwa kutovuta) kwa maana ya mfalme, kama inavyosemwa: Mfalme wa Ugiriki, kwa maana ya Mtawala.

Visomo vyote viwili vinatumika, ingawaje cha kwanza ndicho kinachotumika zaidi.Maana inayokuja haraka akilini, kwa kusoma namna zote mbili ni moja: Kuwa kila kitu kiko mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake, leo na kesho. Yeye ni Mola wa viumbe vyote, na Mola wa Siku ya malipo. Lengo ni kukemea watu na maasia na kuwavutia katika twaa. Katika Nahjul Balagha Imam Ali(a.s) amesema:

Hakika sisi hatumiliki chochote kwa Mwenyezi Mungu, wala hatumiliki isipokuwa kile alichotumilikisha. Alipotumilikisha kile ambacho Yeye amekimiliki huwa ametukalifisha nacho, na anapotuondolea huwa ametuondolea taklifa yake.

Wewe tu tunakuabudu, na Wewe tu tunakuomba msaada. Mja kumzungumzia Mola wake kwa dhamiri ya Mmoja (Wewe tu) ni kwa ajili ya kumtakasa katika Umoja wake, na pia kumtakasa na shirk. Kwa ajili hii, halinganiwi Mwenyezi Mungu kwa tamko la wingi. Ama dhamiri ya wingi (sisi) katika neno tunakuabudu na tunakuomba msaada ni ya mwenye kusema (mja) pamoja na mwingine, wala sio ya kutukuza.

Ibada inathibitika kwa Saumu, Swala, Hijja na Zaka kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Vile vile inathibitika kwa huduma yoyote ya kibinadamu ya kutekeleza haja za watu. Kuna Hadith inayosema:Watu wa mema duniani ni wa mema Akhera. Bora wa watu ni yule mwenye kuwafaa zaidi watu.

MAANA YA WEWE TU TUNAKUABUDU NA WEWE TU TUNAKUOMBA MSAADA

Sio kwamba Mungu ni wa kuabudiwa tu basi iwe imetosha. Bali vile vile Aya inafahamisha kuwa mtu ni kiumbe kitakatifu aliyekombolewa (aliyehuru) kutokana na utumwa na unyonge isipokuwa kwa haki tu, ambayo iko juu ya kila kitu na wala haikaliwi juu. Kimsingi ni kwamba uhuru usiowekewa mpaka na haki, hubadilika na kuwa machafuko. Katika maneno yenye faida niliyoyasoma, yanayohusiana na mlango huu, ni maneno ya Jean Paul Sartre, aliposema, Hakika uhuru hasa ni akujilaz- imisha mtu kujitolea nafsi yake na uhuru wake katika kuwatumikia wengine.

KISA

Kulikuwa na watu wawili wakitembea katika bustani. Mmoja alikuwa na fimbo akicheza nayo.Mara ikagusa ncha ya pua ya mwenzake. Alipomlaumu kwa kitendo hicho, yule mwenye fimbo akajigamba: Nina uhuru bwana! Mwenzake akamwambia, Uhuru wako una mpaka; mwisho wake ni pua yangu!

Mimi siupingi uhuru ikiwa mpaka wake ni kumwamini Mwenyezi Mungu na kumwabudu Yeye peke yake. Kwa sababu mwenye kuabudu haki tu atakuwa amejikomboa na batili; na mwenye kujikomboa na kuabudu haki, bila ya shaka atakuwa mtumwa wa batili. Haiwezekani kutofautisha katika mawili hayo isipokuwa kwa yule ambaye hana mpangilio; asiyeamini halali wala haramu, wala kuamini kitu chochote kingine isipokuwa nafsi yake peke yake.

*1 Sartre mwanzo alikuwa na nadharia ya Existentialism (kuwako) akidai kwamba kila mtu na lake, na hanasibiani na chochote isipokuwa kuwako kwake peke yake. Huko kuwako kwake hakuwezi kuthibiti isipokuwa kwa kuwa huru bila ya kuwa na kikwazo chochote au sharti lolote. Ama dini, misingi, na kuweka mambo katika vipimo, ni upuuzi. Hakuna heri isipokuwa heri ya mtu mwenyewe wala hakuna shari isipokuwa shari yake mwenyewe.

Kwa nadharia hii Satre anatoa dalili kuwa mtu amekuja kutoka katika ulimwengu usiojulikana,na anaelekea ulimwengu usiojulikana na kwamba yeye alikuwako kabla ya kanuni za kiakili na za kidini. Kwa hiyo, yeyote atakayejitia katika dini au katika msingi wowote, atakuwa amejifunga na kuuacha uhuru wake na kwa hivyo amejikanushia kuwako kwake.

Kisha akabadilisha falsafa yake hii akaingia katika falsafa ya Uhuru mkubwa, nao ni uhuru kwa ajili ya mamilioni; kwamba mtu anaichumia, nafsi yake, ikiwa atajiweka katika kuwahudumia wengine; kwambamtu hasa ni yule anayelazimiana na misingi hii. Badala ya kuwa anazungumzia juu ya hali ya mtu mmoja peke yake, akawa Satre anazungumzia juu ya haki za watu wengi na kulitetea hilo!

MAKUSUDIO YA NJIA ILIYONYOOKA

Tuongoze njia iliyonyooka : Makusudio ya njia iliyonyooka si elimu tu, bali ni elimu pamoja na tawfiki katika vitendo (amali). Mwenye kukutakia uongofu amekutakia heri yote, na mwenye kukutakia elimu amekutakia baadhi ya heri.

Maajabu ni kuwa watu wengi wanakuwa wazito kuomba uongofu, hasa wanavyuoni na watu wakubwa, pamoja na kujua kuwa Mtukufu Mtume(s.a.w.w) alikuwa akikariri kuomba uongofu usiku na mchana katika swala zake na sehemu nyinginezo.

Sijui kama kuna uongofu na tawfiki bora na kubwa zaidi kuliko ile ya mtu kugundua aibu zake mwenyewe na kujilaumu, na kumchoma sana.Kwa kutambua hayo inawezekana mtu kuokoka. Mwenyezi Mungu atukinge na ghururi na maovu yake!

MAKUSUDIO YA WALIOKASIRIKIWA NA WALIOPOTEA

Njia ya (wale) uliowaneemesha; sio ya (wale) waliokasirikiwa wala ya (wale) waliopotea . Imepokewa Hadith kwamba:makusudio ya waliokasirikiwa ni Wayahudi, na waliopotea ni Wakristo . Lakini tamko la Aya ni la jumla, wala sio mahsusi au kuvua wengine (kubagua).

Kila mtiifu anaingia katika neema na rehema ya Mwenyezi Mungu, na kila mwenye kuasi ni mwenye kupotea na kughadhibikiwa.

LENGO LA SURA NZIMA YA FATIHA

Vyovyote iwavyo, lengo la Aya hii na sura nzima ya Fatiha, ni kuwa mja asimame mbele za Bwana wake akiwa ni Muumini mwenye kumpwekesha Mwenyezi Mungu, mwenye kushukuru, mwenye kumsifu, mwenye ikhlasi, na mwenye kuomba tawfiki kwa elimu na kwa vitendo.

Na kila mtu ataikuta amali aliyoitanguliza kwa Muumba wake. Ama maneno tu, hayana athari isipokuwa kujikurubisha na twaa, au kujiweka mbali na maasia.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

AL - BAQARAH (NGO’MBE)

SURA YA PILI

Amesema mwenye Majmaul-Bayan kwamba: sura hii yote imeshuka Madina, isipokuwa Aya ya 281.

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

﴿ الم ﴾

1.Alif Laam Miim

﴿ ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ فِيهِ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴾

2.Hiki ni kitabu kisicho na shaka ndani yake; ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu.

﴿ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِالْغَيْبِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴾

3.Ambao wanaamini ghaibu na wanasimamisha Swala na wanatoa katika yale tuliyowapa.

﴿ وَالَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴾

4.Na ambao wanaamini yaliyoteremshwa kwako, na yaliyoteremshwa kabla yako na akhera wana yakini nayo.

Amesema mwenye Majmaul-Bayan kwamba: sura hii yote imeshuka Madina, isipokuwa Aya ya 281.

﴿ أُولَـٰئِكَ عَلَىٰ هُدًى مِّن رَّبِّهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴾

5.Hao wako juu ya uwongozi utokao kwa Mola wao, na hao ndio wenye kufaulu.

MIANZO YA BAADHI YA SURA

Aya 1- 5

﴿الم﴾

Alif Lam Mim :

Wamehitalifiana wanavyuoni kuhusu makusudio ya mwanzo huu na ya mianzo ya sura nyingine inayofanana na hii mfano:

Alif Laam Miim Raa, Kaaf Haa Yaa Ayn Swaad na Haa Miim. Imesemekana kuwa herufi hizo ni katika elimu ya ghaibu ambayo Mwenyezi Mungu hakuidhihirisha kwa yeyote.Lakini sidhani kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anaweza kuwaambia watu jambo asilotaka walijue. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu amewakemea wale ambao hawaifikiri vizuri Quran, aliposema:

﴿أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا ﴾

Je,hawaizingatii (hii) Quran au katika nyoyo zao kuna kufuli? ( 47:24).

Pia imesemekana mianzo hii ni majina ya sura; vilevile imesemwa ni majina ya Mwenyezi Mungu, aidha ikasemwa kuwa; ni ya Muhammad(s.a.w.w) nk.. Lakini linaloelekea zaidi ni kauli inayosema kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwaambia wapinzani walete mfano wa Quran, au sura kumi, au moja; na wakashindwa, ndipo akataja herufi hizi. Yaani, kitabu hiki ambacho ni muujiza, hutokana na herufi hizi ambazo hata watoto na wajinga pia wanazitumia, lakini nyinyi mmeshindwa.

Kwa hivyo kushindwa kwenu ni dalili wazi kwamba kuna siri, na siri yenyewe ni kuwa hii Quran ni wahyi wa kidini sio usanii wa kidunia.

QURAN NA SAYANSI

Kauli yake Mwenyezi Mungu:Ni uwongozi kwa wamchao Mwenyezi Mungu , ni dalili wazi kwamba Quran si kitabu cha elimu ya Historia, wala Falsafa, au elimu ya Fizikia au ya Hesabu; isipokuwa ni kitabu cha elimu ya uongofu wa mwana-adamu katika dunia na akhera, au sema: Quran ni kitabu cha dini, maadili, itikadi na sharia.

Kama utauliza : Ikiwa Quran ni kitabu cha dini, mbona basi kuna Aya zinazohusu mambo ya kilimwengu; kama vile:

﴿وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ﴿٣٨﴾ وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ﴾

Na jua linakwenda mpaka kituoni pake; na mwezi tumeupimia vituo (36:38- 39).

Jibu : Lengo la Aya hizi sio kutubainishia hali ya maumbile kwa undani wa kielimu - kwani hilo limeachiwa akili na majaribio yake - isipokuwa lengo la kwanza la kutajwa Aya hizo ni kwamba, kujua ulimwengu na nidhamu yake kutatuongoza kujua kuwa kuna Mungu, na kwamba huu ulimwengu haukupatikana kibahati tu bila ya kukusudiwa; kama wanavyodai watu wa kimaada. Bali ulipatikana kwa matakwa ya kihekima. Mwenyezi Mungu amelibainisha hilo katika Aya isemayo:

﴿سَنُرِيهِمْ آيَاتِنَا فِي الْآفَاقِ وَفِي أَنفُسِهِمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ﴾

Tutawaonyesha ishara zetu zilizo katika upeo wa mbali na zilizo katika nafsi zao mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. (41:53).

Yaani, tutawafafanulia makafiri - kwa vile watakavyoufahamu ulimwengu kutokana na mipangilio mizuri ya Mwenyezi Mungu - kuwa wao wako katika upotevu. Quran inapotoa mwito wa kuangalia ulimwengu, inasema kwa lugha iliyo wazi kuwa dalili za ulimwengu ni hoja ya kweli na ni dalili yenye nguvu zaidi juu ya kuwapo Mungu, kuliko kitu chochote. Baadhi ya wenye hekima wamesema: Mwenyezi Mungu ana vitabu viwili: Kitabu kinachosomwa na kitabu cha akili, ambacho ni ulimwengu.

Ni kweli kuwa Quran inahimiza kusoma sayansi na kila elimu itakayompa binadamu ufanisi. Lakini kuhimiza ni kitu kingine na kuwa ni kitabu cha elimu hiyo ni kitu kingine. Katika ambayo yanatia nguvu na kuunga mkono kwamba Quran ni kitabu cha uongofu, sharia, na maadili mema, na kwamba Quran imeteremshwa kwa lengo hili, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿هَـٰذَا بَصَائِرُ مِن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ﴾

Hizi (Aya za Quran) ni dalili zitokazo kwa Mola wenu na ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini. (7:203).

Amesema tena:

﴿كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ لِتُخْرِجَ النَّاسَ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ﴾

(Hiki) ni kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu katika giza uwapeleke kwenye nuru. (14:1).

Na Mtume mtukufu(s.a.w.w) anasema:Hakika hapana jingine, nimetumwa kutimiza tabia njema . Na amesema Amirul Muminin(a.s) katika hotuba ya 174, ya Nahjul-Balagha:

Hakika Quran ni dawa ya ugonjwa mkubwa sana wa kufuru, unafiki na upotevu.

Kwa maneno haya tunapata tafsiri ya Aya isemayo:

﴿وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ وَلَا يَزِيدُ الظَّالِمِينَ إِلَّا خَسَارًا ﴾

Na tunateremsha katika Quran yale ambayo ni ponyo na rehema kwa wanaoamini, wala hayawazidishi madhalimu ila hasara tu! (17:82).

Kama utauliza mara ya pili: Unasemaje kuhusu Aya hii.

﴿مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ﴾

Hatukupuuza kitabuni kitu chochote, (6:38)

si inafahamisha kuwa katika Quran kuna elimu zote?

Jawabu : Kutosha kila kitu huwa ni kulingana na mahitaji. Ukisema: Nyumba hii ina kila kitu; itafahamika kwamba ina mahitaji ya mwenye kukaa humo. Kama ukisema: Kitabu cha Fiqh kina kila kitu, itafahamika kuwa mna masuala yote ya kifiqh. Quran ni kitabu cha dini. Kwa hiyo pale Mungu aliposema. Hatukupuza kitabuni kitu chochote, maana yake ni kila kinachoambatana na heri ya mtu na uongofu wake. Swali la tatu: Unasemaje kuhusu vitabu hivi vyenye majina kama: Quran na Sayansi, Uislamu na tiba ya kisasa, na vingenevyo?

Jibu :Kwanza : kabisa, kila anayejaribu kulinganisha kati ya uvumbuzi wa kielimu wa kisasa au wa kizamani na Qurani, atakuwa anajaribu jambo lisilowezekana. Kwa sababu elimu ya binadamu ina mpaka kulingana na nguvu yake ya kiakili; na Quran ni elimu ya Mwenyezi Mungu ambayo haina mpaka. Itakuwaje kitu kilicho na mpaka kiafikiane na kisichokuwa na mpaka?

Pili : elimu ya binaadamu inaingiliwa na makosa. Kwa sababu inakuwa ni dhana na makisio; inakosea na kupata. Mara ngapi tumewaona wataalamu wakikongamana juu ya nadharia fulani na kudai kuwa ni kweli mia kwa mia; kisha wao wenyewe au wale watakaokuja baada yao wanagundua kuwa ni makosa mia kwa mia? Quran ni yenye kuhifadhiwa na makosa. Itakubalika vipi kuoanisha chenye makosa na kile kisicho na makosa? Kisha je tuendelee kugeuza Quran kila yanapogeuka makisio ya elimu na nadharia zake? Hapana. Ndio! hapana ubaya kujisaidia na ugunduzi wa kielimu katika kufahamu baadhi ya Aya, lakini kwa sharti ya kutoufanya huo ugunduzi kuwa ni kipimo cha ukweli na kusihi Quran, bali hata kutozifanya hizo elimu kuwa ndio nyezo za kufahamu siri ya Quran na kufahamu hekima ya baadhi ya hukumu zake.

Inawezekana kuwa hili ndilo lililowafanya watungaji kutunga vitabu kama: Quran na Sayansi n.k. Vyovyote iwavyo, sisi tuna yakini kwamba tuna hoja zenye nguvu katika dini yetu, na tuna dalili za kutosha juu ya ukweli wake; hatuna haja kabisa na vilivyo kwa wengine. Bali tunaamini kwamba wengine ndio walio na haja kwetu katika hilo. Kwa hakika historia ya binadamu haitapata dini yenye utengeneo zaidi ya dini ya Kiislamu, wala kitabu chenye kunufaisha zaidi ya kitabu chake, au Mtume mtukufu zaidi ya Mtume wake. Na yule ambaye hakuongoka kwa dalili za Quran na mwito wake wa maisha mema, basi hataweza kukinaishwa na ugunduzi wa kisayansi wa sasa au wa zamani.

Kuna kitu nilichokifikiria ambacho huenda kikapunguza machovu ya msomaji kuhusu majibu ya yule anayejaribu kuilinganisha Quran na ugunduzi wa sayansi; kama ifuatavyo:

Uzayr alipita katika mji uliokufa, akiwa na punda wake, chakula chake na kinywaji chake akastaajabu na kusema:

﴿ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا﴾

Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? (2:259).

Mwenyezi Mungu akataka kuuondoa mshangao wake. Akamfisha miaka mia. Chakula na kinywaji alichokuwa nacho, kilibakia katika hali yake bila ya kuharibika katika muda wote huo. Kisha Mwenyezi Mungu akamfufua na akataka kumwonyesha miujiza yake ya ajabu, akamwambia:

﴿ فَانظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ﴾

Tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika (2:259).

Hebu angalia msomaji! Je,chakula cha Uzayr kilikuwa katika jokofu (friji)? Swali hili linamhusu mwenye kuilinganisha Quran na elimu ya kisasa.

Hakuna anayetia shaka kwamba jokofu hili ambalo lilihifadhi chakula na kinywaji kwa muda wa miaka mia, pengine linaweza kuwa ni sampuli ya mwaka 2000, na wala siyo ya mwaka 1967. Ndio! Inawezekana kulinganisha sayansi na kufahamu maana ya Quran tukufu; hasa kwa upande wa nadharia ya relativity (uwiano). Kwa vile kufahamu kunahusika na upande fulani katika maana yake, na kunatofautiana na hali ya anayesoma au anayesikiliza.

Kama mtu akisema kuwa tofauti hii haihusiki na Quran peke yake, kwa sababu nadharia ya uwiano ni ya jumla, isiyokubali kuhusishwa, tutajibu: Hiyo ni sawa, lakini maana ya Quran yamejiandaa na hilo. Na hili linatilia nguvu maelezo yetu kwamba mtu mwenye kuganda na kauli za wafasiri bila ya kuongeza kitu, atakuwa na akili ya kusoma tu, lakini sio akili ya mwamko. Basi twamuomba Mwenyezi Mungu azijaalie fahamu zetu katika Aya zake kuwa ni za mwamko na sio fahamu za kunakili.

Wamchao Mwenyezi Mungu Maana ya neno kucha (takua) kilugha ni kujichunga na kitu chochote. Na maana yake kisheria ni kujikinga na hasira za Mwenyezi Mungu na adhabu Yake, kujikinga na kuuacha wajibu na kutenda haram. Amesema Amirul Mumini Ali(a.s) :Kumcha Mwenyezi Mungu ndio msingi wa tabia njema. Wengine wamesema:kumcha Mwenyezi Mungu ni kuwa Mwenyezi Mungu asikuone na lile alilokataza na kutoacha alilokuamrisha.

Kumcha Mungu ndiko kunakomfanya mtu kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu.Quran inasema:

﴿ نَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴾

Hakika Mtukufu wenu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule amchae Mungu zaidi. (49:13).

Unaweza kuuliza, ikiwa wenye kumcha Mungu ni wenye kuongoka, basi wana haja gani ya kuongozwa? Je mwanachuoni anahitaji wa kumfundisha? Jibu: Hakika mwalimu hufundisha wanafunzi wote wajinga na wenye akili, lakini wale wanaonufaika na mwalimu ni wale wenye akili wanaojitahidi

ambao mwisho wao utakuwa ni kufaulu. Kwa hivyo ni sawa tukisema kuwa mwalimu ni wa wenye kufaulu. Vile vile Quran tukufu imewaeleza watu wote, lakini wanaonufaika nayo ni wale waumini wenye kumcha Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ ﴾

Na wale wanaokubali kuongoka Mwenyezi Mungu anawazidishia uongofu. (47:17)

WANAOAMINI GHAIBU

MAARIFA

Inasemekana kuwa mwanachuoni mmoja mkubwa aliyekuwa na heshima na cheo kikubwa huku watu wakimzunguka kwa kumuuliza maswali na kumnyenyekea, alionewa kijicho na mpinzani wake mmoja. Akamuuliza swali la kutatiza kwa sauti kubwa, ili wote wasikie. Mwanachuoni akasema: Sijui. Muulizaji akasema: Mahali ulipo ni pa anayejua sio pa asiyejua. Akasema mwanachuoni: Ole wako! Hapa ni mahali pa anayejua kitu sio kila kitu; anayejua kila kitu hana mahali.

Ndio! ni muhali kwa mtu kujua kila kitu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَمَا أُوتِيتُم مِّنَ الْعِلْمِ إِلَّا قَلِيلًا﴾

Nanyi hamkupewa katika elimu ila kidogo tu. (17:85).

Hakuna mtu yeyote anayezaliwa na ujuzi, isipokuwa hupata maarifa muda baada ya muda, kutokana na sababu fulani; hata hilo jina lake pia halijui, isipokuwa baada ya kuitwa mara kwa mara. Wajuzi wa fani ya maarifa wametaja sababu nyingi za maarifa ambazo ni:

1. Kujua kutokana na hisia tano: Kujua rangi kwa kuona, sauti kwa kusikia,harufu kwa kunusa, ladha kwa kuonja na ugumu kwa kugusa. Vile vile kuna yale anayoyahisi mtu kwa hisia za kindani; kama njaa, shibe, mapenzi na chuki.

2. Kupata maarifa kutokana na uchunguzi na majaribio.

3. Kujua kwa misingi ya kikawaida; yaani kushirikiana na kukubaliana akili zote; mfano: Moja na moja ni mbili; na chenye kunufaisha ni bora kuliko chenye kudhuru. Au kujua kutokana na majaribio; kwa mfano kuamua kwamba kila kipande cha chuma ni kigumu, baada ya kujaribu kipande kimoja tu. Kwa hiyo hukumu inaenea kwa vyuma vyote lakini maarifa yametokana na majaribio ya kimoja.

4. Kujua bila ya kupata maalumati yoyote ya hisia, majaribio au nguvu ya akili; bali kupata moja kwa moja. Hilo ni baada ya jitihadi ya kuitakasa nafsi na uchafu; kama wasemavyo masufi. Kwa ufasaha zaidi ni kwamba moyo mbele za msufi ni kama akili kwa wengine. Kama ilivyo akili kutambua baadhi ya vitu vingine kwa kujitahidi na kuangalia vizuri, basi hivyo hivyo moyo nao hutambua baadhi ya vitu bila ya jitihadi ya nafsi; kama kuhisi mapenzi, na chuki. Na hutambua vitu vingine baada ya jitihadi ya nafsi; kama kujua kuweko Muumbaji.

Kwa hiyo jitihadi ya akili kwetu sisi inafanana na jitihadi ya nafsi kwa masufi. Wala hakuna yeyote anayeweza kubishana na sufi katika maoni yake na itikadi yake. Kwa sababu ukimuuliza dalili, atakujibu kwamba imani yangu na elimu yangu inatoka katika dhati yangu peke yake. Na kama ukimuuliza: Kwa nini imani na elimu hii haitokei katika dhati za watu wote? Atakujibu: Kwa sababu wao hawakupitia majaribio ya kiroho niliyoyapitia mimi.

Sisi tunajiweka kando na msimamo wa kisufi, bila ya kufungamana na upande wowote. Hatuwezi kuuthibitisha, kwa sababu tuko mbali na tunavyoelewa na tulivyozowea. Pia hatuwezi kuukanusha, kwa sababu mamia ya

wanavyuoni katika kila zama hata katika zama zetu wanaamini kuwako nguvu ya usufi; na kutofautiana kwao kihali, kidini , na hata kilugha.Hatuna hoja yoyote inayokanusha majaribio ya kiutu kabisa. Inawezekana kuwa majaribio ya kisufi yanafanana na vipindi ambavyo anapata ilham (anafunukiwa) mshairi na msanii, lakini jambo hili linamuhusu yeye peke yake; wala hana hoja kwa mwingine.

GHAIBU (YASIYOONEKANA)

Kuna vitu ambavyo hakuna njia ya kuvijua kwa hisia, majaribio au nguvu ya akili, kama vile Lawhin Mahfudh (ubao uliohifadhiwa), Malaika, Iblis, Hisabu ya kaburi, Pepo na Moto.Vile vile miujiza ya Mitume; kama fimbo kugeuka kuwa nyoka, kufufua watu, n.k. Akili haiwezi kugundua mambo hayo wala hatujayaona. Yote hayo ni makusudio ya ghaibu katika neno lake Mwenyezi Mungu: wanaamini ghaibu.

Kwa hiyo ghaibu ni ile ambayo haijulikani isipokuwa kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kupitia katika ulimi wa ambaye umethibitika Utume wake. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ﴾

Na kwa Mwenyezi Mungu ziko funguo za siri hapana azijuaye ila Yeye (6:59)

Kwa hali hii, inatubainikia kuwa kuamini ghaibu ni sehemu ya Uislamu, na kwamba asiyeiamini sio Mwislamu.

Vile vile inabainika kuwa jambo ambalo halijulikani kwa kuona, majaribio au akili; au lisilosimuliwa na Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala mapokezi ya Mtume, basi litakuwa ni katika vigano. Na vigano vingi vinatokana na mapokezi ya Mayahudi na mfano wao.