TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Mwandishi:
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
Kundi:

Matembeleo: 35752
Pakua: 3052


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Juzuu 9 Juzuu 10 Juzuu 11
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 20 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 35752 / Pakua: 3052
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KWANZA Juzuu 1

Mwandishi:
Swahili

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KWANZA

AL - BAQARAH (NG’OMBE)

﴿وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تَذْبَحُوا بَقَرَةً قَالُوا أَتَتَّخِذُنَا هُزُوًا قَالَ أَعُوذُ بِاللَّـهِ أَنْ أَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ ﴾

67.Na Musa alipowaambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha mchinje ng’ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Najikinga kwa Mwenyezi Mungu kuwa miongoni mwa wajinga.

﴿قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا هِيَ قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَّا فَارِضٌ وَلَا بِكْرٌ عَوَانٌ بَيْنَ ذَٰلِكَ فَافْعَلُوا مَا تُؤْمَرُونَ ﴾

68.Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ni ng’ombe gani? Akasema: Hakika yeye anasema kwamba ng’ombe huyo si mpevu wala si mchanga, ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyoamrishwa.

﴿قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا لَوْنُهَا قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ صَفْرَاءُ فَاقِعٌ لَّوْنُهَا تَسُرُّ النَّاظِرِينَ ﴾

69.Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie rangi yake ni ipi? Akasema: Yeye anasema ng’ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imeiva sana, huwapendeza wanaomtazama.

﴿قَالُوا ادْعُ لَنَا رَبَّكَ يُبَيِّن لَّنَا مَا هِيَ إِنَّ الْبَقَرَ تَشَابَهَ عَلَيْنَا وَإِنَّا إِن شَاءَ اللَّـهُ لَمُهْتَدُونَ ﴾

70.Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ni vipi hali yake; hakika ng’ombe wamefanana na hakika sisi kama Mwenyezi Mungu akipenda (tutakuwa) ni wenye kuongoka.

﴿قَالَ إِنَّهُ يَقُولُ إِنَّهَا بَقَرَةٌ لَّا ذَلُولٌ تُثِيرُ الْأَرْضَ وَلَا تَسْقِي الْحَرْثَ مُسَلَّمَةٌ لَّا شِيَةَ فِيهَا قَالُوا الْآنَ جِئْتَ بِالْحَقِّ فَذَبَحُوهَا وَمَا كَادُوا يَفْعَلُونَ ﴾

71.Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo si ng’ombe anayefanyishwa kazi ya kulima ardhi wala kutilia maji mimea, mzima, hana kipaku. Wakasema: Sasa umeleta haki. Basi wakamchinja, na walikaribia wasifanye.

﴿وَإِذْ قَتَلْتُمْ نَفْسًا فَادَّارَأْتُمْ فِيهَا وَاللَّـهُ مُخْرِجٌ مَّا كُنتُمْ تَكْتُمُونَ ﴾

72.Na mlipoiua nafsi, kisha mkahitilafiana kwa hayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyokuwa mkiyaficha.

﴿فَقُلْنَا اضْرِبُوهُ بِبَعْضِهَا كَذَٰلِكَ يُحْيِي اللَّـهُ الْمَوْتَىٰ وَيُرِيكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴾

73.Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng’ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anawaonyesha ishara zake ili mpate kufahamu.

MWENYEZI MUNGU ANAWAAMRISHA MCHINJE NG’OMBE

Aya 67 - 73

MUHTASARI WA KISA

Aya hizi tukufu haziwezi kufahamika maana yake bila ya kufahamu tukio lililoteremshiwa. Kwa ufupi tukio lenyewe ni hili: Mzee mmoja tajiri katika Waisrail aliuliwa na binamu yake kwa tamaa ya kurithi mali yake; kisha akadai kuwa ameuliwa na watu wengine, na wakatakiwa walipe fidia. Ukazuka ubishi mkubwa na wakamwendea Musa(a.s) . Kwa vile hakukuwa na ushahidi wowote wa kugundua mambo walimtaka Musakama kawaida yao - kumwomba Mwenyezi Mungu awabainishie muuaji. Ndipo Mwenyezi Mungu akampa wahyi kuwa wachinje ngombe na sehemu ya huyo ngombe wampige yule aliyeuliwa atafufuka na ataeleza yule aliyemuua. Baada ya udadisi mwingi walifanya vile walivyotakiwa kufanya na yule aliyeuliwa akafufuka na akamtaja aliyemuua.

MAANA

Wakasema: Je unatufanyia mzaha? Yaani tunakuuliza kuhusu kuuliwa mtu nawe unatuamrisha kuchinja ngombe hakika huu ni mzaha. Akasema: Najikinga kwa Mwenyezi Mungu kuwa miongoni mwa wajinga. Yaani mimi sifanyi mzaha, hata katika mambo yasiyokuwa ya kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu, sembuse hayo ya kufikisha neno la Mungu ambaye umetukuka msemo Wake? Ilikuwa inatosha tu wamchinje ngombe yoyote, kwa sababu waliamrishwa wachinje ngombe tu; lakini kwa udadisi wao.

Wakasema:Tuombee Mola wako atupambanulie ni ng’ombe gani? Wakajibiwa kuwa ni ambaye yuko katikati si mkubwa wala si mdogo, basi fuateni amri wala msingoje, lakini wakarudia tena kuuliza Wakasema:Tuombee Mola wako atupambanulie rangi yake ni ipi? Akasema: ni wa manjano, lakini tena wakazidi kudadisi na kuuliza swali mara ya tatu, kwa sababu ngombe walio katika rangi hii na umri huu ni wengi. Akawaambia kuwani yule asiyefanyishwa kazi na asiyekuwa na kasoro yoyote. Wakamtafuta mpaka wakampata, wakamchinja; kisha wakampiga maiti kwa kipande cha nyama akafufuka na siri ikafichuka baada ya kumtaja aliyemuua. Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuyisha wafu na anawaonyesha ishara zake ili mpate kufahamu.

Yaani huku kumfufua huyu aliyeuliwa ni ushaidi wazi na dalili wazi ya kufufuliwa watu baada ya kufa, kwa sababu mwenye kuweza kufufua nafsi moja hawezi kushindwa na nyingine. Je, baada ya ushahidi huu wa kuona kwa macho mnaweza mkakanusha na kutia shaka na kuasi? Lakini pamoja na hayo na yasiyokuwa hayo nyoyo zenu zimesusuwaa, bali zimesusuwaa zaidi na zimekuwa ngumu zaidi kuliko jiwe, kama itakavyoeleza Aya inayofuatia. Baada ya maelezo tuliyoyaeleza kuhusu Mayahudi haiwezekani tena kuuliza swali lolote kuwa,kwa nini Mwenyezi Mungu hakumfufua yule aliyeuliwa tangu mwanzo, na hali Mwenyezi Mungu alikuwa anaweza kufanya hivyo? Vipi anaweza kufufuka mtu kwa kupigwa na nyama ya ngombe? Kwa nini ilikuwa lazima ngombe huyo? Kisha kuna faida gani ya kumpiga na ngombe huyo aliyeuliwa?

Maswali yote haya hayana nafasi baada ya kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwafanyia Mayahudi mambo maalum wao tu; na kwamba Yeye kwa upande huu ndio amewafadhilisha juu ya watu wote.

﴿ ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً وَإِنَّ مِنَ الْحِجَارَةِ لَمَا يَتَفَجَّرُ مِنْهُ الْأَنْهَارُ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَشَّقَّقُ فَيَخْرُجُ مِنْهُ الْمَاءُ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَهْبِطُ مِنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴾

74. Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe mengine yanayobubujika mito ndani yake, na kuna mengine yanayopasuka yakatoka maji ndani yake; na kuna mengine huanguka kwa sababu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na mnayoyafanya.

KUWA NGUMU NYOYO

Aya 74

Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo. Yaani ilikuwa ni wajibu kwa wazee wenu - enyi Mayahudi wa Madina - wazingatie na zilainike nyoyo zao baada ya kushuhudia waliyoyashuhudia katika miujiza na maajabu; ambayo miongoni mwake ni kufufua aliyeuliwa, lakini, kwa ukhabithi wao, wakafanya kinyume na vile inavyotakiwa; wakafanya ufisadi na nyoyo zao zikasusuwaa kama kwamba zimetokana na mawe, bali baadhi yake ni ngumu zaidi kuliko mawe, kwani kuna mawe, mengine yanayobubujika mito ndani yake, na kuna mengine yanayopasuka yakatoa maji. Unaweza kuuliza: Mito ni maji, sasa mbona yametajwa maji na mito? Inawezekana kutofautisha jengo na nyumba? Jibu: Hakika Aya tukufu imegawanya maji kwenye mafungu mawili mengi ambayo ni mto, na machache ambayo ni chemchem. Ibara ya mgawanyiko imekuja kwa tamko la maji, kwa hivyo kumetajwa kububujika maji kwa maana ya wingi na kupasuka kwa maana ya uchache.

Vyovyote iwavyo, lengo la Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuwa amefadhilisha aina za majabali na mawe kuliko nyoyo za Mayahudi, ni kwa sababu jiwe linaweza kupasuka likatoa maji, na kwamba jiwe mara nyingine huwa linatikisika likaondoka pale lilipokuwa. Lakini nyoyo za Mayahudi hazina hata chembe ya kheri wala hazitikiswi na uzuri wowote na hazielekei kwenye uongofu. Unaweza kuuliza kuwa mawe hayana uhai wala utambuzi, kwa hiyo hayawezi kumwogopa Mwenyezi Mungu, sasa kuna wajihi gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Na kuna mengine huanguka kwa sababu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu.

Swali hilo limejibiwa kwa majibu mengi, yaliyo karibu zaidi ni mawili: Kwanza, hayo ni makisio kwamba lau kama mawe yangelikuwa na fahamu na akili kama Mayahudi, yangelianguka kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu. Mifano hii ni mingi sana katika maneno ya waarabu. Jibu jingine, ni kwamba ni kawaida ya mawe kumnyenyekea Mwenyezi Mungu ambaye ndiye aliyeumba maumbile yote. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿تُسَبِّحُ لَهُ السَّمَاوَاتُ السَّبْعُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ إِنَّهُ كَانَ حَلِيمًا غَفُورًا﴾

Zinamsabihi (zinamtakasa) mbingu zote saba na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, na hakuna chochote ila kinamsabihi kwa sifa Zake njema. (17:44)

Utakuja ufafuanuzi tutakapofika Aya hiyo inshallah.

TOFAUTI YA HULKA

Anaweza kuuliza muulizaji: Je ndani ya binadamu kuna nguvu inayompa msukumo wa harakati; au yanayompa harakati ni matukio ya nje, kiasi ambacho ndani ni tawi lakini nje ndio shina? Au kila moja ni shina hiyo yenyewe peke yake, kwamba mtu mara nyingine hupata msukumo kutoka ndani na mara nyingine nje au mara nyingine ndani na nje? Kama tutafaradhia kuwa ndani ya binadamu kuna msukumo wa aina ya peke yake usioshirikiana na kitu kingine, Je msukumo huo ni wa aina moja kwa watu wote au kila mtu ana wa aina yake? Jibu: Hakika mtu anakuwa mtu kwa silika yake na nguvu yake ya kiroho. Lau tunavitoa vitu hivyo au tanavizuia utendaji kazi wake, basi binadamu atakuwa ni kama ganda tupu au unyoya katika mavumo ya upepo. Ndio! Ni kweli kwamba nguvu za kindani zinafanya kazi pamoja na matukio ya nje na kuathirika nazo, lakini kufanya kazi ni kitu kingine na kuathirika ni kitu kingine. Kwa mfano, silika ya kuchunguza inakuwa pamoja na mtu na ndio maana mtoto anakuwa mdadisi kwa umbile lake; bali sili- ka hiyo ni katika mambo yanayomuhusu mtu. Kisha silika hii inakua na kukoma kwa kuona matukio ya nje vilevile kwa utafiti na uvumbuzi; na kwa kukua kwake binadamu anaweza kuathirika vitu vya nje kulingana na haja yake na matakwa yake. Kwa hivyo harakati za binadamu zinachimbuka kutoka ndani na nje, yaani kutoka katika nafsi yake na kutoka katika matukio.

Hapa kuna kifungu cha tatu ambacho nimekigundua kutokana na majaribio yangu maalum; Kifungu hicho nimekipa jina Tawfik katika heri na kufaulu. Kifungu hiki hakitokani na nafsi wala matukio, bali kinatokana na nguvu iliyojificha ambayo iko katika ulimwengu uliojificha (usiojulikana), inawaandalia baadhi ya watu njia ya heri na inaingia katika kuwaelekeza watu kwenye lile linalomridhshia Mwenyezi Mungu bila ya mtu kutambua. Ni kawaida kwamba hatanikubalia juu ya hili isipokuwa yule anayemwamini Mwenyezi Mungu na hekima yake na kumpa cheo kinachomstahiki. Ninakiri kwamba mimi sina ufahamu wa ujumla wa kifungu hiki, isipokuwa nimekifahamu kutokana na majaribio yangu; kama nilivyotangulia kueleza.23 Ama jawabu la kuwa je, watu wanakuwa na namna moja katika silika na sifa za kinafsi, linataka ufafanuzi. Katika sifa za kinafsi kuna zile ambazo watu wanashir-ikiana; kama vile utambuzi wa kupambanua kati ya haki na batili, heri na shari, na kati ya baya na zuri.

* 23 Jambo la kushangaza lilotokea kwa sadfa.Baada ya kuandika maneno haya nikasoma nakala fulani, kuwa kiongozi mmoja wa kijeshi wa Kiingereza maarufu sana anayeitwa Montgomery alijieleza kwa kusema: Hakika yeye ni askari mdogo chini ya uongozi wa nguvu kuu; na kwamba yeye hakushinda katika vita isipokuwa kwa matakwa ya kudra hiyo; na kwamba bila ya kuamini nguvu hii kubwa yenye akili, haiwezekani kushinda katika vita vya dunia vya pili. Yeye anaamini kwamba kuna nguvu iliyofichika ambayo iliwaandalia njia ya kumshinda Romel, ambaye alikuwa akiitwa mbweha wa jangwani, naye alikuwa amirijeshi mkubwa wakati huo. Lau si ushirikiano huu isingeliwezekana kwa vyovyote vile kuthibitisha uovu na wema na isingelifaa kwetu kumlaumu au kumsifu mtu kwa kufanya jambo fulani. Vile vile kuna ushirikiano katika kujipenda na upendo wa mzazi na mwana, na mengineyo ambayo wanayo watu wote, ijapokuwa kuna tofauti ya wingi na uchache.

Kuna sifa nyingine za kinafsi, ambazo watu wanatofuatiana kama vile; ushujaa, woga, ukarimu, ubahili, ugumu wa moyo, ulaini wa moyo, udhaifu wa matakwa na nguvu yake na kupondokea kwenye heri au shari. Watu katika sifa hizi wanatofuatiana, kila mtu sio karimu au bahili,wala mwoga au mshari. Unaweza kuuliza: Hakika kauli yako si inakhalifu kawaida maarufu iliyozoeleka, kuwa hakuna mtu yoyote isipokuwa ana pande mbili, mzuri na usiokuwa mzuri; na wewe umetilia mkazo upande mmoja tu, na ukaufinyia jicho upande mwingine?. Jibu: Hakika uvivio wa heri ambao mara nyengine tunauona kwa baadhi ya watu wa shari, unakuwa umeingia kighafla tu, bila ya kukusudiwa; na kwamba suala la kuwa kila mtu ana pande mbili linawezekana kwa wasiokuwa Mayahudi.Kwa sababu, Mayahudi hawana lolote wao isipokuwa uovu tu; hawana wema kabisa. Ushahidi wa hayo ni Tawrat yao, Quran tukufu na historia sahihi. Vile vile vitendo vyao katika Palestina na kwingineko, mambo ambayo ni dalili wazi kwamba dini, maadili na mfungamano wote wa kiutu, kwao ni biashara na manufaa tu.Maudhui haya tutayarudia kila itakapolazimika.

﴿أَفَتَطْمَعُونَ أَن يُؤْمِنُوا لَكُمْ وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِن بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴾

75.Je mna matumaini ya kwamba wataamini na hali baadhi yao walikuwa wanasikia maneno ya Mwenyezi Mungu kisha wanayabadili baada ya kuwa wameyafahamu na hali wanajua?

HAKUNA MATUMAINI

Aya 75

MAELEZO

Kila mwenye ujumbe fulani huwa anapupia watu wauamini ujumbe huo. Kwa hivyo anaueneza kwa matumaini ya kupata wafuasi wengi, na anahimili taabu na mashaka katika hilo, kama alivyofanya Mtume(s.a.w.w) na sahaba zake, waliueneza mwito wa Uislamu katika pembe zote kwa kutaraji kupata wafuasi. Kulikuwa na mfungamano wa kijirani, kibiashara na hata kunyonyeshana watoto kati ya Ansar na Mayahudi. Hivyo wakawalingania kwenye Uislamu kwa amri ya Mtume. Wakawatolea dalili kwa hoja zinazoingia akilini na kwa mantiki mazuri, wakatumai kwamba nyoyo zao zitashtuka, hasa kwa kuzingatia kwamba wao ni watu wa Kitabu na kwamba sifa za Muhammad(s.a.w.w) zimetajwa kwa uwazi katika Tawrat yao. Walipoendelea Wayahudi kukaidi mwito wa Uislamu na kuendelea kukufuru na kuipinga haki, ndipo Mwenyezi Mungu alipomwambia Mtume wake kwa kusema: Je mnatumaini nyinyi Waislamu ya kwamba watawaamini hao Mayahudi, na hali wazee wao hawa Mayahudi walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu kutoka kwa Nabii Musa(a.s) pamoja na miujiza, lakini wakiyabadilisha na kuyageuza vile matamanio yao yanavyotaka pamoja na kujua kuwa hayo maneno ni ya haki?

Kwa hivyo, hali ya Wayahudi wa Madina ni kama hali ya wazee wao waliopita, ambao walibadilisha halali ikawa haramu na haramu kuwa halali kwa kufuata matamanio yao na wakabadilisha sifa za Muhammad(s.a.w.w) zilizopokewa katika Tawrat, ili isiweko hoja juu yao. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Katika Aya hii kuna dalili juu ya ukubwa wa dhambi ya kuibadilisha sheria. Na dhambi hiyo inapatikana katika kuleta Bida katika fatwa au hukumu na mambo yote ya kidini. Kuongezea juu ya maneno hayo ya mwenye Majmau ni kuwa Aya hii ni dalili juu ya kuwa mwenye kufuata upotevu kwamba sio kuwa anajifanyia uovu yeye mwenyewe tu, bali athari yake inaenea kwa vizazi, kama ilivyoelezwa katika Hadith.

﴿وَإِذَا لَقُوا الَّذِينَ آمَنُوا قَالُوا آمَنَّا وَإِذَا خَلَا بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ قَالُوا أَتُحَدِّثُونَهُم بِمَا فَتَحَ اللَّـهُ عَلَيْكُمْ لِيُحَاجُّوكُم بِهِ عِندَ رَبِّكُمْ أَفَلَا تَعْقِلُونَ﴾

76. Na wanapokutana na wale walioamini husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao, wao kwa wao husema: Mnawaambia yale aliyowahukumia Mwenyezi Mungu ili wapate kuhojiana nanyi mbele ya Mola wenu? Je,hamna akili?

﴿أَوَلَا يَعْلَمُونَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ﴾

77.Hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyayafanya siri na wanayoyadhihirisha?

WANAPOKUTANA NAWALE WALIOAMINI

Aya 76 - 77

MAELEZO

Baadhi ya Mayahudi walikuwa wakifanya unafiki na uwongo kwa Waislamu na wakisema: Sisi tunaamini yale mnayoyaamini nyinyi na tunashuhudia kuwa Muhammad ni mkweli katika maneno yake, kwani tumekuta katika Tawrat sifa zake. Lakini wanafiki hao wanapochanganyikana na viongozi wao, basi viongozi wanawalaumu kwa kusema: Vipi mnawahadithia wafuasi wa Muhammad yale aliyowahukumia Mwenyezi Mungu? Hivi hamfahamu kwamba huko ni kukubali nyinyi wenyewe kwamba mko katika batili na wao wako katika haki? Hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya siri na wanayoyadhihirisha? Yaani kwa vyovyote watakavyojaribu wanafiki, kuficha unafiki wao na viongozi wapotevu wanavyowaelekeza wafuasi wao, lakini kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakifichiki chochote. Basi nyinyi Mayahudi mnaficha njama zenu, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anamfahamisha Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) na anavifagia vitimbi vyenu.

﴿وَمِنْهُمْ أُمِّيُّونَ لَا يَعْلَمُونَ الْكِتَابَ إِلَّا أَمَانِيَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ ﴾

78.Na wako miongoni mwao wasiojua kusoma; hawajui kitabu isipokuwa matamanio tu nao hawana isipokuwa kudhani tu!

﴿فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ يَكْتُبُونَ الْكِتَابَ بِأَيْدِيهِمْ ثُمَّ يَقُولُونَ هَـٰذَا مِنْ عِندِ اللَّـهِ لِيَشْتَرُوا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَوَيْلٌ لَّهُم مِّمَّا كَتَبَتْ أَيْدِيهِمْ وَوَيْلٌ لَّهُم مِّمَّا يَكْسِبُونَ﴾

79.Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao. Kisha wakasema hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu ili wachukue kwacho thamani ndogo. Basi ole wao kwa yale iliyoyaandika mikono yao. Na ole wao kwa yale wanayoyachuma.

WAKO MIONGONI MWAO WASIOJUA KUSOMA

Aya 78 79

MAELEZO

Na wako miongoni mwao wasiojua kusoma. Yaani katika Mayahudi kuna wale waliokuwa hawakusoma; hawajui chochote katika dini ya Mwenyezi Mungu na kwamba mambo yao zaidi ni ya kudhania dhania tu, bila ya kutegemea elimu. Kimsingi ni kwamba ingawa maelezo haya yamekuja kwa sababu ya Wayahudi, lakini shutumu inamwendea kila mjinga.

TAFSIRI INA MISINGI NA KANUNI

Katika Aya hii kuna dalili wazi kwamba haifai kufasiri Quran na Hadith kwa kudhania na kukisia, bali hapana budi lazima mfasiri awe na elimu ya kanuni za tafsiri na misingi yake, na kuchunga kanuni hizi katika kubainisha makusudio ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kujihadhari na kuwazulia. Sharti la kwanza la kufaa kufasiri ni kujua kusoma na kuandika; kisha hujua elimu za Kiarabu kwa aina zake zote, ambazo ni kujua msamiati, Sarfa, Nahw, Bayan, Fiqh na misingi yake. Vile vile kujua elimu ya Tawhid na kuongezea elimu nyingine ambazo zitamsaidia katika kufasiri baadhi ya Aya. Yote haya mfasiri anaweza kuyajua kwa kuwaendea wenye kuhusika nayo. Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao. Hapa Mwenyezi Mungu anamkemea kila anayemnasibishia yale asiyokuwa nayo kwa ajili ya kuchukua thamani kwa shetani. Si lazima thamani iwe ni mali (pesa) tu; inaweza kuwa ni kupata jaha au chochote katika anasa za kidunia.

Mwenyezi Mungu amekariri makemeo mara tatu katika Aya moja kwa kutilia mkazo kwamba kumzulia yeye Mwenyezi Mungu na Mtume ni katika maasi makubwa na yenye adhabu kali; kama alivyosema mahali pengine:

﴿قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ وَيْلَكُمْ لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُم بِعَذَابٍ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ﴾

Ole wenu msimzulie uwongo Mwenyezi Mungu asije akawafutilia mbali kwa adhabu, Na ameruka utupu anayezua uwongo. (20:61)

MWANACHUONI HAWEZI KUHUKUMU KWAMATUKIO

Tunadokeza kwa mnasaba huu kwamba mwanachuoni, kwa namna yoyote atakavyokuwa na elimu, ni juu yake kutomnasibishia chochote Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kwamba kitu hicho kinatoka katika Lawh Mahfudh. Akitoa fatwa kwa uhalali au uharamu; au kuhukumia kitu kuwa ni haki; au kufasiri Aya au Hadith, basi ni juu yake kuifanya hukumu yake hiyo, fatwa yake au tafsiri yake kuwa ni rai yake tu. Inaweza kuwa ni makosa au sawa. Hapo ndio atakuwa anakubaliwa msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu kama akijitahidi kadiri ya uwezo wake. Lakini kama hakujitahidi sana au amejitahidi sana, lakini akasema kuwa kauli yake hiyo ni kauli ya

* 24 W amethibitisha wenye kuhusika na historia ya lugha na ada zake kwamba Tawrat ya sasa, ambayo Wayahudi wanaitakidi kuwa iliteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Musa, imetungwa. W atafiti wametoa hakika hii kutokana na muundo wa lugha ulivyo na ustawi wa kijamii na wa kisiasa ambao uko kinyume na Tawrat. Tutarudia kueleza maudhui haya kwa upana zaidi Inshallah. Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi atakuwa ni sawa na wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uwongo, ajapokuwa ni mwanachuoni wa wanachuoni. Kwa sababu mwanachuoni hatoi fatwa ya kweli wala hukumu ya kweli,bali anaitikadi tu kuwa ni haki. Huu ndio msingi wa kwamba yeye sio maasum.

﴿وَقَالُوا لَن تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَّعْدُودَةً قُلْ أَتَّخَذْتُمْ عِندَ اللَّـهِ عَهْدًا فَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ عَهْدَهُ أَمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴾

80.Na walisema: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu. Sema: Je, mmepata ahadi kwa Mwenyezi Mungu Kwa hivyo hatakhalifu ahadi yake.Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua?

﴿بَلَىٰ مَن كَسَبَ سَيِّئَةً وَأَحَاطَتْ بِهِ خَطِيئَتُهُ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

81. Ndiyo, wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni; humo watadumu.

﴿وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

82.Na wale walioamini na kutenda mema, hao ndio watu wa peponi, watadumu humo.

WALISEMA HAUTATUGUSA MOTO WA JAHANNAM

Aya 80 - 82

Na walisema: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu Mayahudi wanadai kwamba wao ni watoto wa Mungu na taifa lake teule na kwamba watu wote ni watoto wa shetani, isipokuwa wao tu, na ni mataifa yaliyotupiliwa mbali. Kwa hivyo ati Mwenyezi Mungu hatawaweka milele motoni, isipokuwa atawaadhibu kwa adhabu hafifu tena kwa muda mfupi, kisha atawaridhia. Yaani kwamba Mwenyezi Mungu anawaendekeza na kuuendekeza ukoloni wa kizayuni ambao unaikalia ardhi ya Palestina. Sema: Je, mmepata ahadi kwa Mwenyezi Mungu. Yaani waambie ewe Muhammad, kwamba madai yao haya ni porojo tu, na kama si hivyo, basi ni ahadi gani mliyowekeana na Mwenyezi Mungu? Madai yao haya, hayafahamishi chochote zaidi ya kudharau kwao madhambi na kufanya uovu.

Mtume mtukufu(s.a.w.w) anasema:Hakika mumini anaona dhambi yake ni kama jiwe anaogopa lisimwangukie na kwamba kafiri anaona dhambi yake ni kama nzi tu aliyepitia kwenye pua yake....

Anasema Amirul Muminin(a.s) :Dhambi kubwa zaidi ni ile iliyodharauliwa na mwenye kuifanya.

Kauli yake Mtume mtukufu(s.a.w.w) : Kama kwamba dhambi ni nzi anayepita juu ya pua ya mwenye dhambi. Inafanana kabisa na ya Mayahudi ambao wanadai kwamba wao ni watoto wa Mwenyezi Mungu wenye kutendekezwa. Huenda haya yakamnufaisha na kumzindua yeyote ambaye anapuuza dhambi kwa kutegemea utukufu wa nasabu. Mwenye kujitegemea yeye mwenyewe tu wala asihisi makosa ya nafsi yake, na asikubali nasaha za mwingine, basi ni muhali kuweza kuongoka kwenye heri. Hakika mwenye akili hajiangalii mwenyewe tu kwa kujihadaa na ndoto zake, bali daima anakuwa na msimamo wa kujilaumu makosa yake na kupambanua yale aliyonayo na yale anayotakiwa awe nayo. Vile vile huitoa nafsi yake na fikra za kitoto na mawazo ya kishetani. Kwa hali hii pekee ndio atakuwa anafaa kuitwa mtu kwa maana sahihi. Kuna hadith tukufu inayosema: Mwenye kujiona kwamba yeye ni mwovu, basi ni mwema.

Ndiyo, wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni na humo watadumu. Ubaya ni shirk na madhambi mengineyo, lakini makusudio yake hapa yanahukumu shirk tu! Kwa kulinganisha na kauli yake Mwenyezi Mungu hao ndio watu wa motoni humo watadumu. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Makusudio ya ubaya kuwa ni shirk ndiyo yanayoafiki, kwa sababu dhambi nyingine yoyote haiwajibishi kudumu motoni. Na wale walioamini na kutenda mema hao ndio watu wa peponi watadumu humo. Aya hii tukufu inafahamisha kuwa kuokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kesho kutatokana na imani sahihi ikiambatana na matendo mema. Hadith tukufu inasema: Abu Sufyani Athaqafiy, alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Niambie neno katika Uislamu ambalo sitamuuliza yeyote baada yako.Akasema Mtume:Sema: Nimemwamini Mwenyezi Mungu, kisha ufuate unyoofu (msimamo).

Katika hadith yake hii Mtume(s.a.w.w) anaelezea Aya inayosema:

﴿إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴾

Wale waliosema: Mola wetu ni Mwenyezi Mungu kisha wakawa na unyoofu hao huwateremkia malaika (wakawambia): Msiogope wala msihuzunike, na furahini kwa pepo mliyokuwa mkiahidiwa. (41:30).

Makusudio ya kuwa na unyoofu katika Aya na Hadith, ni kuwa katika msimamo wa kufanya amali kwa mujibu wa Quran na hadith za Mtume(s.a.w.w) .

MWISLAMU NA MUUMINI

Mwislamu kwa kuangalia muamala wake na kuthibiti Uislamu wake, anagawanyika kwenye mafungu mawili:

Kwanza : kumkubali Mwenyezi Mungu kuwa ni mmoja na kukubali Utume wa Muhammad bila ya kuangalia itikadi yake na amali (matendo) yake. Lakini ni sharti asikanushe zile dharura za dini, kama ulazima wa swala na uharamu wa zinaa na pombe. Huyu ndiye anayejulikana kwa Waislamu kuwa yeye ni Mwislamu atafanya na kufanyiwa mambo ya Kiislamu; kama kurithi, kuoa, na kuzikwa kiislamu, ikiwa ni pamoja na kumwosha, kumtia sandani, kumswalia na kumzika katika makaburi ya Waislalmu, anafanyiwa hayo kwa vile amepiga shahada.

Pili : ni kuamini na kushikamana na Uislamu kwa misingi na matawi; hakanushi hukumu yoyote katika hukumu za Kiislamu, wala hafanyi uasi wa hukumu katika hukumu za sheria. Huyu ndiye Mwislamu wa kweli (muumin) mbele ya Mwenyezi Mungu na watu, bali ni Mwislamu mwadilifu ambaye zimethibiti kwake athari zote za uadilifu wa Kiislamu duniani na akhera. Athari za dunia ni kukubaliwa ushahidi wake, kufaa kuswalisha, kuchukua hukumu zake na fatwa zake akiwa ni mujtahidi. Ama athari za kiakhera ni kule kuwa juu hadhi yake na thawabu. Mumin ni yule mwenye kukiri kwa ulimi na kusadikisha kwa moyo wake shahada mbili, wala haitoshi kukiri kwa ulimi tu au kusaidikisha kwa moyo tu, bali hapana budi yote mawili yaende sambamba. Kwa hivyo kila mumin ni Mwislamu, lakini si kila Mwislamu ni mumin.

Hapa inatubainikia kwamba amali njema haiitwi imani, kwa dalili kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Ameleta kiunganishi baina ya imani na amali njema kwa maana ya kuwa ni vitu viwili tofauti. Hata hivyo amali njema inaingia katika ufahamu wa uadilifu kama tulivyoonyesha. Utakuja ufafanuzi wake mahali pake. Mafaqihi wa kishia wanahusisha tamko la mumin kwa yule anayeamini Maimamu kumi na wawili, wakisema zaka inapewa mumin, na mwenye kuswalisha awe mumin, basi wanakusudia yule mwenye kuamini maimamu kumi na wawili tu. Istilahi hii wanahusika nayo mafaqih tu. Lakini hata huyo fakihi wa Kishia kama akizugumzia mumin katika mswala yasiyokuwa ya kifikihi, basi huwa anakusudia kila mwenye kukiri shahada mbili na kuzisadikisha kwa moyo; hata kama siye mwenye kuamini Maimamu kumi na wawili.

Kwa vyovyote ilivyo Uislamu na imani kwa maana tuliyoyaelezea, hautamuokoa mtu na adhabu ya Mwenyezi Mungu kesho, isipokuwa uwe pamoja na unyoofu ambao ni kufanya amali kulingana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake(s.a.w.w) .

MWENYE MADHAMBI MAKUBWA

Mafakihi wameyagawanya madhambi katika mafungu mawili Makubwa; kama kunywa pombe. Na madogo kama kukaa kwenye meza ya pombe bila kunywa. Utakuja ufafanuzi wa madhambi makubwa na madogo Inshallah, katika Aya isemayo:Ambao wanajiepusha na madhambi makuu na vitendo vichafu; isipokuwa makosa hafifu...

Wamehitalifiana Waislamu katika yule mwenye kukiri shahada mbili na akafanya madhambi makubwa, Je, yeye ni kafiri atakayebakia milele motoni au yeye ni mwislamu fasiki ambaye ataadhibiwa kiasi anachostahili, kisha atiwe peponi? Khawarij wamesema kuwa atabakia milele motoni.Shia, Ashari, Masahaba wengi na Tabiin, wamesema atatolewa motoni. Mutazila wamezusha fikra ya tatu ya kuthibitisha mawili, yaani hatakuwa kafiri wala Mumin. Allama Hilli ametoa dalili katika sherehe ya Tajrid juu ya ushahidi wa kauli ya kuwa mwenye madhambi makubwa ni fasiki hatokaa milele motoni, kuwa: Lau atabakishwa milele motoni, ingelazimika mwenye kumwabudu Mwenyezi Mungu muda wa umri wake wote; kisha akamuasi mwisho wa umri wake mara moja tu, pamoja na kubakia na imani yake, aingie motoni milele, awe sawa na yule aliyemshirikisha Mwenyezi Mungu katika umri wake wote. Na hilo ni muhali na haliingii akilini.

Hapana mwenye shaka kwamba ovu moja haliwezi kuondoa mema yote, bali ni kinyume; kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t). Kwa ajili hiyo basi, inapasa kulichukulia neno ubaya katika Aya (Na wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo), kuwa na maana ya shirk. Kama ambavyo Aya inayofuatia hiyo (Na wale walioamini na kutenda mema hao ndio watu wa peponi, watakaa humo milele) inafahamisha kwamba mwenye kufanya madhambi makubwa ataingia peponi,

* 25 Aya hii tukufu inakuwa ni jibu la yule anayesema: Katika madhambi hakuna kubwa wala dogo, bali yote ni makubwa. Jibu lenyewe ni tamko,Lamam, lenye maana ya uhafifu. wala hatakaa milele motoni. Kwa sababu Aya ile inamhusu pia mwenye kuamini na akafanya amali njema kisha akafanya madhambi makubwa na wala asitubie.

MAYAHUDI TENA

Madai ya Mayahudi kwamba wao ni watoto wa Mungu na taifa teule, ni kwamba dini na maadili yake, katika itikadi yao, ni kazi ya kibiashara na manufaa ya kiutu. Vinginevyo itakuwa ni bure tu. Unaweza kusema, hayo hayahusiani na Mayahudi tu, bali wako watu wa namna hiyo. Jibu, ndio, lakini tofauti iliyopo ni kwamba Mayahudi wana hasadi kwa watu wote isipokuwa wao.