MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU0%

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU Mwandishi:
Kundi: Familia na watoto

  • Anza
  • Iliyopita
  • 9 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12767 / Pakua: 2361
Kiwango Kiwango Kiwango
MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

Mwandishi:
Swahili

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

KIMEANDIKWA NA: JOPO LA MAULAMAA (MISRI)

KIMETARJUMIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

KIMEHARIRIWA NA: HEMEDI LUBUMBA SELEMANI

KIMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHTI PILI RAJAB

NENO LA MCHAPISHAJI

Kitabu ulichonacho mikononi mwako asili yake kimeandikwa kwa Kiingereza na jopo la maulamaa wa Misri kwa jina la Child Care in Islam. Sisi tumekiita: Malezi ya Watoto katika Uislamu.

Kama inavyofahamika kwamba; Uislamu ni dini na ni mfumo wa maisha, basi mafundisho yake hayakuacha kitu kinachohusiana na maisha ya mwanadamu - kuanzia tumboni mwa mama yake, kuzaliwa kwake, kunyonya na kulikizwa kwake, kufunzwa mambo ya kimsingi na mama yake, mpaka kufikia kimo cha kwenda shuleni. Haya yameelezwa kwa utaratibu mzuri sana kutoka kwenye vyanzo viwili vikubwa vya sheria ya Kiislamu - Qur'ani na Sunna.

Kwa mujibu wa Uislamu kipindi cha mafunzo ya watoto huanza wakati mwanaume na mwanamke wanapoingia katika ushirika wa ndoa, kama wazazi wa baadaye, ni lazima wajihisi kwamba wana wajibu wa kuwalea watoto wao. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa kanuni za kurithi (tabia), mwenendo wote wa tabia nzuri na mbaya wa wazazi hurithiwa na watoto wa wazazi hao. Hivyo, mzazi akiwa na tabia nzuri atawarithisha watoto wake tabia hiyo, na ni kwa sababu hii mafunzo ya watoto huanzia punde tu wakati mume na mke wanapoingia katika ndoa. Ili kufanikisha somo la kitabu hiki, jopo hilo la maulamaa limerejea sana kwenye vyanzo hivyo viwili - Qur'ani na Sunna. Watoto ni taifa la kesho, na ili kuwa na taifa zuri lenye maadili mema, lazima kuwalea watoto katika mazingira mazuri ya kimaadili; na ni mafunzo ya Kiislamu tu, kama yatafundishwa vizuri na kuzingatiwa basi Umma utaondokana na matatizo mengi ya kijamii kama inavyoonekana hivi sasa.

Tumekiona kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan katika wakati huu ambapo jamii inazidi kudidimia katika maovu kutokana na kumomonyoka kwa maadili mema. Taasisi yetu ya Al-Itrah Foundation imeamua kukichapisha kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili kwa madhumuni yaleyale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili. Tunamshukuru ndugu yetu A. Mohamed kwa kukubali jukumu hili la kukitarjumi kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha uchapishaji kitabu hiki.

Mchapishaji: Al-Itrah Foundation

S. L. P. 19701

Dar-es-Salaam, Tanzania.

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

Mwanzo Qur ani tukufu na Hadith, ndivyo vitu viwili vya kimsingi ambavyo vinaunda Sheria za Kiislamu na kuzi hakikisha, na ni kutokana na vitu viwili hivyo ndipo misingi yote ya dini inaporejea. Hata hivyo, ni Qur ani tukufu tu ndiyo marejeo makubwa ambayo Hadith zinategemea. Kwa ajili hiyo, Hadith hazitofautiani au kupingana na Qurani ambayo inaaminiwa kuwa ndi yo asili ya ukweli wote.

Miongoni mwa maudhui yenye maana sana ya Qur ani tukufu, ni kuwa inaeleza kanuni na Sheria zote za mwanzo kusaidia watu ili waweze kupanga vizuri maisha yao, na hivyo kuweza kubadilisha desturi zilizokuwa zikifuatwa.

Kwa maana hiyo Qur ani imehifadhi haki za kila mmoja, na za jamii, imefanya kuenea kwa uadilifu, imewapa watu moyo wa kuishi pamoja kwa ushirikiano na ihsani, na imeweka kipimo cha kumcha Mwenyezi Mungu kuwa ndiyo tofauti pekee baina ya watu. Hadith ni chochote kile ambacho Mtume(s.a.w.w) amekitenda na ambacho si Qurani; au mambo ambayo yamemfikia kupitia kwa ufahamu wake au maono, na kuthibitishwa na Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo (Sunnah) inakusanya vitendo na maneno yanayohusika na ufafanuzi wa itikadi, Swala au ibada nyinginezo, pia kulingana na uhusiano mwema baina ya ndugu, kumfundisha mwenendo mzuri, na kuamrisha mambo mema na kukataza maovu.

Kwa hivyo chochote kilichotendwa na Mtume(s.a.w.w) katika hali kama hiyo, huchukuliwa kama sunnah, na watu wanatakiwa kukifuata. Chochote kile ambacho hakihusiani na hayo yaliyotajwa hapo awali, kama vile kula, kunywa, au kuvaa nguo, hakichukuliwi kuwa ni sunnah, na watu hawalazimiki kukifuata.

Mtume(s.a.w.w) amesema:Hakika mimi ni mwanaadamu, pindi nitakapowaamrisha jambo linalohusiana na dini yenu, lifuateni, na nitakapowaamrisha jambo kutokana na maoni yangu, basi kumbukeni kuwa mimi ni mwanaadamu.

Ushahidi wa jambo hili ni ushauri ambao Mtume(s.a.w.w) alizoea kuutoa kuhusiana na kutaf uta tiba ya baadhi ya maradhi. Ushauri ambao hakuletewa wahyi ila ni kutokana na uzoefu alioupata kutokana na kuishi katika mazingira ya kibinaadamu.

Ametaja Abu Daud katika Isnadi yake, kutoka kwa Usama kwamba: Nilikwenda kwa Mtume(s.a.w.w) naye alikuw a ameketi na maswahaba zake, nao walikuwa (wametulia) kama kwamba kuna ndege juu ya vichwa vyao, nikawatolea salaam, kisha nikaketi. Wakaja mabedui kutoka huku na huko wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, je tunaweza kujitibu? Mtume(s.a.w.w) akasema:Mnaweza kujitibu, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuumba ugonjwa pekee ila ameumba na dawa yake, isipokuwa ugonjwa wa aina moja tu, kifo.

Hadith nyingine iliyopokewa kutoka kwa Umar Bin Dinar imetaja jambo hilo (pia).

Siku moja Mtume(s.a.w.w) alimtembelea mgonjwa, akawaambia nduguze, Mwiteni daktari, mmoja wao akasema: hata nawe pia wasema hivyo ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?! Mtume akasema:Ndiyo, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuumba maradhi ila ameumba na dawa yake.

Kitendo cha Mtume(s.a.w.w) cha kuwataka ndugu za wagonjwa kumwita daktari kinaonyesha kwamba utabibu wa madawa si miongoni mwa mambo aliyofunuliwa (wahyi) kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na ni kwa sababu hii ndipo akawashauri watu kufuata ushauri wa daktari pale unapohitajika.

Pia hali hiyo inahusiana na jinsi alivyokuwa akivaa na kula, ilivyokuwa ikilingana na tabia za wakati wake na mahali alipoishi. Na lau kama angeishi katika mazingira na wakati tofauti, basi pengine angestawisha desturi zingine.

Kwa hivyo basi, Sunnah (Hadith) inafafanua Qur ani, inachambua hukmu zake, inaikamilisha, inaelezea na kuamua kuhusu mipaka ambayo inatawala kanuni zake kamili, na inafafanua sehemu zenye kutatanisha. Na endapo itaongezea chochote, ziada hiyo haiwezi kupingan a na misingi ya kanuni za Qur ani. Kwa hivyo uhusiano wa Sunnah na Qurani ulivyo ni kama hali ya kiongozi na mfuasi. Kwa ajili hiyo, Hadith inafuata kile kilichokuja katika Qurani na inaambatana nayo moja kwa moja. Inadhihirika wazi sasa, kwa nini Quran i inatangulia Sunnah, na kuchukuliwa kuwa ni msingi wa Uislamu, wakati ambapo Sunnah inaikamilisha Qur ani kwa kanuni.

Mkusanyiko huu (wa kitabu hiki kinachohusu malezi ya mtoto) umetokana na yale yaliyotajwa katika Qur ani yahusuyo malezi ya mtoto, na k atika Sunnah kuhusiana na mambo haya. Ili kutoa mwanga, habari zaidi na ufafanuzi uliyomo katika Qur ani, baadhi ya methali na dondoo maarufu zimeongezwa ili ziwe ni mifano mizuri na yenye nguvu zaidi.

1

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

SEHEMU YAKWANZA

1.HALI NA HAKI ZA MTOTO KATIKA UISLAMU

Hawa ni watoto wetu kwetu sisi wenye hadhi Ni kama maini yetu yaendayo kwenye ardhi Na tulivyo kati yetu hatuwezi kuwa radhi Tuwaonapo wanetu wanaugua maradhi (Tafsiri ya shairi la kale la kiarabu) Umoja wa mataifa umeanza kuonyesha kuvutiwa na suala la watoto kwa kufanya maadhimisho ya Siku ya Watoto katika mwezi wa Novemba kila mwaka, ambayo inalingana na maadhimisho ya kutangazwa kwa haki za mtoto.

Kwa hali yoyote ile, ipo haja ya kutaja hapa kwamba, mazingatio ya Uislamu kwa watoto yameanza zamani na yanarejea nyuma zaidi ya miaka elfu moja na mia nne.

Uislamu kwa mfululizo unaadhimisha na kuonyesha huruma yake kwa mtoto, si baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla ya kuzaliwa, na umeelezewa kwa makini haki zake. Wakati wa utoto katika Uislamu umepewa picha ya ulimwengu mzuri wa furaha, uzuri, ndoto, mapenzi na ruya njema.

Na aya za Qur ani zinaonyesha mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa watoto, na ndipo akaapa Mwenyezi Mungu:

لَا أُقْسِمُ بِهَـٰذَا الْبَلَدِ ﴿١﴾ وَأَنتَ حِلٌّ بِهَـٰذَا الْبَلَدِ ﴿٢﴾ وَوَالِدٍ وَمَا وَلَدَ ﴿٣﴾

Naapa kwa mji huu, (wa Makkah). Na wewe utahalalishwa katika mji huu. Na (kwa) mzaz i na alichokizaa. (90:1-3).

Watoto wameelezwa katika Qur ani kuwa ni bishara njema. Amesema Mwenyezi Mungu:

يَا زَكَرِيَّا إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ اسْمُهُ يَحْيَىٰ ﴿٧﴾

Ewe Zakaria tunakupa habari njema ya (kupata) mtoto jina lake ni Yahya (19:7).

Pia watoto ni kiburudisho cha macho yetu. Amesema Mwenyezi Mun gu:

رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

Ewe Mola wetu, tupe katika wake zetu na watoto wetu watakaoyaburudisha macho yetu (25:74).

Na watoto ni pambo la maisha katika ulimwengu huu.

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ﴿٤٦﴾

Mali na watoto ni pambo la maisha ya duniani (18:16).

Mtume(s.a.w.w) anatudhihirishia ya kuwa ulimwengu wa utoto ni kama pepo, pale aliposema: Watoto ni vipepeo vya Peponi.

Kuwatunza watoto ni jambo la lazima, na kuwapenda humleta mtu karibu na Mwenyezi Mungu. Mtume(s.a.w.w) amesema:Lau kama si watoto wanyonyeshwao, na wazee wanaorukuu (kwa kuswali) na wanyama walishwao mashambani, basi mngelipatwa na adhabu kali.

Inaonyesha wazi kwamba huruma na uangalifu wa Mwenyezi Mungu kwa watoto ndiyo uliofanya Mwenyezi Mungu kuzuia adhabu juu ya watu wake.

MAPENZI YA MTUME KWA WATOTO

Mapenzi ya Mtume(s.a.w.w) kwa watoto yalijaa ndani ya moyo wake mwema, imeelezwa katika Hadith: Siku moja Mtume(s.a.w.w) alipanda juu ya mimbari akiwahutubia watu, (mara) akawaona Hasan na Husein(a.s) wanakimbia na huku wakijikwaa, akakatiza hotuba yake, akashuka kutoka juu ya mimbari kwenda kuwapokea watoto hao wawili. Akawabeba mikononi mwake, kisha akapanda tena juu ya mimbari akasema:Enyi watu, hakika mali zenu na watoto wenu ni fitina, Wallahi nimewaona wajukuu zangu wawili wakikimbia na kujikwaa, basi sikuweza kujizuia mpaka nimeshuka nikawabeba.

Siku moja Mtume(s.a.w.w) alikuwa anaswali, mara Hasan na Husein(a.s) wakaingia ndani na kumpanda mgongoni kwake wakati alipokuwa amesujudu, Mtume(s.a.w.w) akaendelea kusujudu tu. Alichukia kuwaharakisha washuke, mpaka waliposh uka wao wenyewe. Kisha alipotoa salaam na kumaliza Swala, akaulizwa na maswahaba zake sababu zilizomfanya asujudu kwa kitambo kirefu hivyo; akawajibu:Wajukuu zangu wawili walikuwa wamepanda juu ya mgongo wangu nami nilichukia kuwahimiza washuke kwa haraka.

Mtume(s.a.w.w) alizoea kuharakisha Swala yake pindi asikiapo mtoto analia, na husema:Mimi huchukia kumchosha mama yake . Siku moja alikuwa anapita nyumbani kwa Fatima(a.s) (binti yake), akamsikia mjukuu wake Husein(a.s) akilia, aliingia ndani n a baada ya kumkemea Fatima akasema:Je hujui kwamba nimsikiapo Husein akilia huwa nakereka? Siku moja Mtume(s.a.w.w) alitembelewa na Al-Akraa Ibn Habis, ambaye alimwona Mtume(s.a.w.w) akiwabusu wajukuu zake, Al-Akraa akasema: Unawabusu watoto wa binti y ako? Naapa kwa Mungu nina watoto kumi,

na sijawahi kumbusu hata mmoja. Mtume(s.a.w.w) akamjibu:Je ni kosa langu kama Mwenyezi Mungu ameing’oa rehma kutoka moyoni mwako.

2. UMUHIMU WA MTOTO KATIKA UISLAMU KABLA YA KUZALIWA

Kutilia maanani kwa Uislamu kuhusu malezi ya mtoto hakuanzi baada ya kuzaliwa tu, bali hata kabla hajaanza kupata umbo (tumboni) kwani Uislamu unamuamuru mtu kuoa mke mcha Mungu na mtulivu.

Mtume(s.a.w.w) amesema:Jitahidi umpate mwenye kushikamana na dini, basi furaha zote ni zako.

Uzuri, na utajiri si sifa pekee za kutosha kuchagua mke, sambamba na sifa hizo, pia mke ni lazima awe na sifa zingine, kwa mfano kumpata aliye na dini, na awe ametoka kwenye nyumba yenye mema. Kwa sababu watoto wake atakaow azaa mke huyo watarithi tabia, adabu na mwenendo wake. Mwenyezi Mungu amekataza kuoa mwanamke mzuri tu asiye na tabia nzuri na nidhamu. Mtume(s.a.w.w) amekataza:Jihadharini na wanawake wazuri wenye sifa mbaya.

Mtume(s.a.w.w) ameweka mwongozo kwa mwanamke ambaye yu tayari kuolewa:atafute mume mcha Mungu, mwenye tabia za kidini, atakayeangalia jamii yake kwa ukamilifu, kutekeleza haki za mke, na kusimamia malezi ya watoto.

Mtume(s.a.w.w) amesema:Atakapowajia mtu mtakayeridhishwa na jinsi alivyoshika dini, na tabia yake, basi muozeni, ama msipofanya hivyo, mtaleta fitina na ufisadi mkubwa duniani.

Mtume(s.a.w.w) ameonya pia kuhusu kuoana na ndugu wa karibu, ili watoto wasizaliwe wadhaifu, akasema:Oeni walio nje ya jamii yenu, msiwadhoofishe watoto wenu.

Qur ani imetaja ya kwamba, mwanadamu ameumbwa kutokana na tone la manii lililochanganyika:

إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٢﴾

Hakika tumemuumba mwanadamu kutokana na tone la manii lililochanganyika...(76:2).

Hii inaonyesha kwamba, mtoto azali waye na wazazi ambao si ndugu wa karibu atakuwa na uwerevu, utambuzi na mwenye nguvu za kimwili kuliko mtoto aliyezaliwa na wazazi wenye uhusiano wa karibu. Hii inaweza kuonekana kwamba Uislamu umezitangulia (kwa uvumbuzi) kanuni za kisayansi na elimu ya tabia zinazorithishwa (Heredity) kwa kuonyesha umuhimu ulioko katika sehemu ya urithi wa tabia, na namna gani uteuzi mzuri wa watu wawili wanaooana utakavyopelekea kupata watoto ambao ni tuzo la Mwenyezi Mungu na furaha ya maisha.

Kwa kuwa mtoto atachukua mwenendo wa wajomba na shangazi zake, asili ya undani ya baba yake na mama yake, na akajifunza kupitia kwa urathi ambao umepitia kutokana kwa muungano wa baba yake na mama yake, na ndipo Uislamu ukazitengeneza asili hizi kwa njia hiyo ili kumhifadhi mtoto awe ni kiumbe mwenye heshima na nidhamu, na hivyo kuepukana na upungufu wowote. Mara tu mtu anapoanza kufikiria kuoa na kutunza familia, Uislamu unamuongoza kupitia katika njia hizo.

3. FAMILIA KATIKA UISLAMU

Familia katika Uislamu, ina utaratibu mzuri na wa hali ya juu sana, na ni utaratibu unaoheshimiwa sana hata ina mahali panapostahiwa. Ni kwa sababu hii na ndio maana Uislamu huipa nguvu (familia) kuanzia mwanzo wa nguvu yake. Ndoa ni sura mpya katika njia ya kuunda jamii, na uangalifu wa Uislamu katika nguzo hiyo muhimu, hatimaye unaongoza kuelekea katika maisha ya amani na furaha.

4. PENDO LA WAZAZI

Mtoto ni matokeo ya kimaumbile ya uhusiano imara wa wazazi, ubaba na umama ni matamko mawili ambayo Mwenyezi Mungu ameyazatiti kwa ihsani na mapenzi Yake, akayatajirisha na kuyapitia kwa maana ya kuungana watu wawili na kuendelea kuwa pamoja.

Uhusiano wa karibu zaidi baina ya wazazi na watoto wao, ni miongoni mwa uhusiano ulio imara na wenye daraja ya juu zaidi kuliko uhusiano wowote ule wa kibinaadamu. Uhusiano huo umehifadhiwa na Mwenyezi Mungu, naye amehakikisha kuwa unaendelea na kustawi; kwa sababu kufanya hivyo ni kuendelea kwa jamii ya binaadamu na uhai. Upendo wa wazazi kwa watoto wao hauna nafasi yoyote ya kutia shaka, kwani ni alama ya Mwenyezi Mungu na ni neema Yake kubwa kwa walimwengu. Mwenyezi Mungu amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ﴿٢١﴾

Na katika alama zake, ni huku kuwaumbia wake zenu, kutoka miongoni mwenu ili mpate utulivu kwao, na akajaalia mapenzi na huruma baina yenu (30:21).

Baadhi ya wafasiri wameeleza pen zi na huruma hapa, kwa maana ya mtoto ambaye ameupa nguvu uhusiano baina ya wazazi na ameupa amani na usalama.

Familia ndicho kitu cha kwanza ambacho Uislamu unakichukulia kuwa ni cha kwanza katika jamii ya watu. Familia huunda nyoyoni mwao penzi lisilo na kikomo kwa watoto wao, penzi hili ni nuru waliyopewa na Mwenyezi Mungu. Mtume(s.a.w.w) aliwaambia maswahaba zake na huku akiwaonyesha mwanamke akasema:Je Mnaweza kufikiria kwamba siku moja mwanamke huyu anaweza kumtupa mwanawe motoni? Wao wakasema: La, akasema: Basi Mwenyezi Mungu ni mwenye huruma zaidi kwa waja wake kuliko mama huyu alivyo na huruma kwa mtoto wake.

Basi haya ni maumbile, na ni aina ya pendo la kiasili ambalo hapana yeyote awezaye kulizuia au kushindana nalo, na kwa sababu hii ndipo Mwenyezi Mungu akawausia wazazi kuwaangalia watoto wao, Amesema:

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ ﴿١٤﴾

Na tumemuusia mwanaadamu (kuwafanyia wema) wazazi wake, mama ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumnyonyesha na kumwachisha kunyonya katika miaka miwili, nishukuru Mi mi na wazazi wako na kwangu ndio marejeo (31:14).

Amesema tena:

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُ وَبَلَغَ أَرْبَعِينَ سَنَةً قَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَصْلِحْ لِي فِي ذُرِّيَّتِي إِنِّي تُبْتُ إِلَيْكَ وَإِنِّي مِنَ الْمُسْلِمِينَ ﴿١٥﴾

Na tumemuuusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake. Mama yake ameichukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na kubeba mimba yake (mpaka) kumwachisha kunyonya ni miezi thelathini mpaka anapofikia kubaleghe kwake, na akafikia miaka arubaini. Akasema: Ewe Mola wangu niwezeshe nizishukuru neema zako ambazo umenineemesha mimi na wazazi wangu. Na uniwezeshe nifanye amali njema uzipendazo, na unitengenezee watoto wangu. Kwa hakika natu bu kwako, kwa hakika mimi ni miongoni mwa waislamu (46:15).

Mwenyezi Mungu amefanya kuwapenda watoto na kuwahurumia ni sehemu ya maumbile ya kiasili ya kibinaadamu yasioepukika. Pia ameziingiza hisia hizi thabiti ndani ya nyoyo za wazazi. Ni kwa ajili h ii basi ndipo maelezo haya yote pamoja na wasia yameelekezwa moja kwa moja kwa watoto, kwa ajili ya kuwatendea wema na kuwapa heshima wazazi wao. Maelekezo haya amepewa mtoto ili kuzivutia hisia zake.

Ni maelekezo ya hali ya juu ambayo yanategemeza uhusiano wa karibu na hisia ya kibinaadamu ambazo ndio sababu kubwa ya kuwepo kwetu duniani.

5. USAWA BAINA YA WATOTO KATIKA UISLAMU NA MAONI YAKE JUU YA WATOTO WA KIKE

Kadri Uislamu unavyochukulia watoto kuwa ni kiburudisho cha macho yetu, ni lazima hii idhihiri kwa vitendo na kwa njia zake. Usawa baina ya watoto hauna budi kutekelezwa hata katika kuwabusu. Uislamu unataka usawa ufanywe kulingana na maagizo yake matukufu.

Siku moja Mtume(s.a.w.w) alimwona baba ambaye alikuwa na watoto waw- ili, akambusu mmoja na kumwacha mwingine, kisha Mtume mtukufu akamuuliza: Je huwezi kuwafanyia usawa? Tukiangalia mvuto wa kumpendelea mtoto mmoja zaidi ya mwingine au jinsia moja (wa kike au wa kiume) zaidi ya nyingine, hii ni kinyume kabisa na maadili ya kiislamu, mila n a fikra za usawa ambazo Uislamu umejengewa. Uislamu hautofautishi baina ya mwanamume na mwanamke, wala hautofautishi baina ya mvulana na msichana. Wote sawa, hapana yeyote ampitaye mwenzake ila kutokana na baadhi ya sifa alizonazo kitabia alizojipatia yeye mwenyewe, Mwenyezi Mungu amesema:

فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ ﴿١٩٥﴾

Mola akawakubalia (maombi yao), ya kwamba mimi sipotezi amali ya mwenye kutenda, awe ni mwanamume au mwanamke, baadhi yenu kwa baadhi nyingine (3:195).

Kwenda kinyume na misingi hii kunafuatia kwenda kinyume na fikra za usawa, maarifa, na haki. Kwa ajili hii, Uislamu unawaamuru Waislamu kuwafanyia usawa watoto wao ili kwamba kusiwe na yeyote yule atakayekuwa na kinyongo au kusononeka. Kwa njia kama hiyo, Uislamu unazuia kuzagaa kwa chuki badala ya mapenzi, na kusema maudhi badala ya amani. Mambo haya iwapo yataendelea, hatimaye yataleta matatizo ya kinafsi, majonzi, na utengano, na haya yote huvunja hisia za moyo. Mtume(s.a.w.w) mara kwa mara alikataza kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya wa kike pasi na sababu yoyote, kwa maana hiyo, ndiyo akaipa daraja la juu heshima ya watoto wa kike na akaipa nguvu thamani na staha yao.

Amesema Mtume(s.a.w.w) : Bora ya watoto wenu ni mabinti. Mtume(s.a.w.w) alipopew a habari ya kuzaliwa bintiye Fatima(a.s) , nyuso za maswahaba zilionekana kuparama, Mtume(s.a.w.w) akawaambia: Mna jambo gani linalowahuzunisha? (kumzaa Fatima) ni kama kupata ua la mrehani niunusao, na riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Hapa Mtume(s.a.w.w) kwa ubaba wake mtukufu alijaribu kubadilisha mawazo ya watu ya kuwapendelea watoto wa kiume zaidi ya watoto wa kike, tena hata aliwatanguliza watoto wa kike zaidi kwa kusema: Mwenye kwenda sokoni, na kununua zawadi na kuwapelekea jamii yake, (famili a yake) ni kama mtu aliyewapelekea sadaka wahitaji, basi aanze kuwapatia watoto wa kike kabla ya kiume.

Mtume(s.a.w.w) amejaribu kwa kadri awezavyo kuvutia penzi la watoto wa kike kama vile lilivyo penzi la asili kwa watoto wa kiume. Amesema:Mwenye kuwalisha (kuwalea) watoto watatu wa kike ataingia Peponi. Akaulizwa: Je wakiwa ni wawili?, akajibu:Hata kama wawili, Akaulizwa: Je mmoja, akajibu:Hata kama ni moja.

2

MALEZI YA WATOTO KATIKA UISLAMU

SEHEMU YA PILI

MAISHA NA MAKAZI YA MTOTO

Mtume(s.a.w.w) amesema: Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutowaangalia wanaomtegemea. Kuna maagizo kadhaa na misingi ya kanuni iongozayo, ambapo Uislamu unaamuru kwa jinsi gani maisha na maendeleo ya mtoto yalivyo lazima, na kwamba uzembe wowote ama kufanya ajizi katika kutimiza misingi hii ya kanuni ni kosa kubwa. Misingi hii imetolewa mfano kama ifuatavyo:

Amesema Mwenyezi Mungu: Wala msijiue. Amesema tena:

وَلَا تَقْتُلُوا النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ ﴿١٥١﴾

..wala msiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharamisha kuuawa ila kwa njia ya haki (6:151).

Amesema tena:

مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا ﴿٣٢﴾

Mtu atakayemuua mtu bila ya yeye kuua, au bila ya kufanya ufisadi nchini, basi ni kama amewaua watu wote, na atakayeokoa maisha ya mtu, basi ni kama ameokoa maisha ya watu wote (5:32).

Amesema tena:

وَلَا تَقْتُلُوا أَوْلَادَكُم ﴿١٥١﴾

Wala ms iwaue watoto wenu (6:151). Amesema tena:

يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَخُلِقَ الْإِنسَانُ ضَعِيفًا ﴿٢٨﴾

Mwenyezi Mungu anataka kukurahisishieni (mambo mazito) kwani mwanaadamu ameumbwa dhaifu. (4:28).

Amesema tena:

وَلْيَخْشَ الَّذِينَ لَوْ تَرَكُوا مِنْ خَلْفِهِمْ ذُرِّيَّةً ضِعَافًا خَافُوا عَلَيْهِمْ ﴿٩﴾

Na waogope (mawasii kuwadhulumu yatima, na wakumbuke) kama wao wangeacha nyuma yao watoto dhaifu wangekuwa na khofu juu yao. (4:9).

Amesema tena:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا ﴿٦﴾

Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu kutokana na moto. (66:6)

Amesema tena Mwenyezi Mungu:

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ﴿١٩٥﴾

Wala msijitie wenyewe katika maangamivu. (2:195).

Amesema Mtume(s.a.w.w) :Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kumtupa yule anayemtegemea.

1. KUISHI KWA MTOTO

Uislamu unamchukulia mtu kuwa ni khalifa wa Mwenyezi Mungu duniani, imetajwa katika Qurani: Hakika nitaweka katika dunia hii khalifa (2:30).

Kwa hivyo, jambo lolote litakalomtia khalifa huyu kwenye aibu, fedheha, ama kudhoofisha uwezo wake, limekatazwa na sheria ya Kiislamu.

Na hii ni kwa sababu ya kuhifadhi heshima na daraja ya mwanaadamu aliyopati- wa akiwa kama khalifa wake duniani. Mwenyezi Mungu amempa uwezo binaadamu kuwa na fahamu za kujua mambo bila ya kufundishwa, nguvu za ulinzi za kuweza kujihami, na kumwezesha kupata kudumu kwa ulimwengu. Pia Mwenyezi Mungu amempa mwanaadamu undani wa maarifa, na amemtukuza zaidi ya viumbe vyote vilivyosalia. Miongoni mwa uwezo aliopewa mwanaadamu ili kukabiliana na vitisho ni uwezo wa kujihami.

Uangalifu wa Uislamu kuhusiana na maisha ya mtoto na ulinzi wake, tayari wenyewe una mamlaka kwenye jamii ya kiislamu kimwili au kiroho, kwa sababu uangalifu huu unazalisha miili imara yenye siha. Kuwa na miili yenye afya katika Uislamu hakuleti natija ya nguvu ya kiakili tu, bali pia uhakika, mafanikio na matumaini katika kushughulika na maisha na watu. Ni kwa sababu hizi ndipo Uislamu umekusanya taratibu zifaazo za kujikinga, ili kuyahifadhi maisha ya waislamu na kuwaongoza katika njia yenye utaratibu na iliyopangwa katika maisha yao yote. Afya ndiyo neema bora kuliko zote alizotunikiwa mwanaadamu baada ya kuwa muislamu, kwani bila ya kuwa na afya huwezi kufanya kazi na kuweza kumtii Mungu sawasawa, kwa hivyo, hakuna chochote kinachoweza kulinganishwa nayo.

Imetajwa na Tirmidhy, kutokana na Abu Huraira ya kwamba Mtume(s.a.w.w) amesema: Kitu cha kwanza atakachoulizwa mwanaadamu Siku ya Kiyama, kutokana na neema alizopewa ni: Je mwili wako, sikuupa afya? (uliifanyia nini?)

2. JUKUMU LA WAZAZI HUKO AKHERA, NA MATUNZO YA WATOTO

Inasadikiwa ya kwamba, kulingana na maumbile na hisia za binaadamu, anaweza kuepuka hali zinazotishia (maisha yake). Zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu amemuumbia mwanaadamu nguvu ya kiasili inayomlinda kutokana na hatari hizo. Licha ya hivyo, Uislamu umeipa uwezo nguvu hiyo, na umemkumbusha mwanaadamu aitumie kwa kujihami na kwa kuongozea mikakati ya ulinzi kwa ajili ya maisha yake. Kwa hivyo inaonyesha wazi namna gani Uislamu ulivyoupa daraja ulinzi na kuuimarisha. Ulinzi kwa maana hiyo (ilivyotajwa hapa) ungeweza kuwa na maana ya ulinzi wa mwanaadamu hapo Akhera, ambao utamwokoa kutokana na moto na vitisho vya Siku ya Kiyama. Au ungeweza kuwa ni kujilinda kwa mtu kutokana na moto ambako kunamaanisha wakati huo huo, kuilinda familia yake.

Imetajwa katika Qur ani:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٦﴾

Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) yenu kutokana na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe (66:6).

Aya hizo zilizotangulia zinawataka wacha Mungu waumini kujilinda na kujihami wao na jamii zao pia kutokana na Moto ambao kuni zake zitakuwa ni watu waovu. Kujilinda maana yake (hapa) inarejea kwenye kutenda amali njema, na kuwa na mwenendo mzuri, kumtii Mwenyezi Mungu na kujizuia na makatazo yake. Miongoni mwa matendo ya kujilinda kwa Akhera, ni kujizuia na maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu, kuhusiana na chakula, kinywaji, mavazi, n.k.

Imetajwa katika Qur ani:

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾

Enyi Mitume! Kuleni vyakula vilivyo vizuri (halali) na tendeni mambo mema, hakika Mimi najua yote myafanyayo. (23:51).

3. JUKUMU LA WAZAZI MAISHANI NA MATUNZO YA MTOTO

Matunzo ya mtoto wakati wa maisha yake yanahusiana na kumkinga kutokana na magonjwa na maradhi yaambukizayo na yote yale yawezayo kumpata mtu kutokana na uzembe, na kutojihusisha. Imesema Qur ani:

Wala msijitie wenyewe katika maangamivu (2:1 95).

Katika Aya iliyotangulia hapo juu, Mwenyezi Mungu amemkataza mwanaadamu kuchangia maangamivu yake mwenyewe kupitia kwenye vitendo ambavyo angevitenda kulingana na mwenyewe. Ijapokuwa mtu kujidhuru au kujiangamiza kunaonekana kwamba kunapingana na fikra zilizo timamu (yaani haiwezekani), lakini yaelekea kuwa kunaweza kutokea kutokana na uzembe ama kutojihusisha na kuchukua kinga zifaazo ili kuyachunga maisha yake mwenyewe.

Kujiangamiza hapa, haina maana tu ya maangamivu yanayosababishwa na kiu, nja a, au mtu mwenyewe kujitoa mhanga kwa njia moja au nyingine kutokana na madhambi ayatendayo. Kuangamia kwa maana hiyo, kunamaanisha kwamba kufanya ajizi kidogo tu, au kuzembea katika kujikinga, ndiko kujiangamiza. Kwa hivyo hii ni pamoja na mtu kujihatar isha na magonjwa, maradhi yaambukizayo, ukosefu wa chanjo kutokana na maradhi yauwayo, na ukosefu wa uangalifu wakati wa shida na hatari. Vitendo hivyo vyote vilivyotangulia kutajwa vinachukuliwa kuwa ni kumchangia mtu katika maangamivu yake mwenyewe.

Kwa sababu hiyo ndipo Uislamu ukaamuru kuchukua kinga zifaazo, na kutafuta matibabu kwa ajili ya magonjwa yote. Mtume(s.a.w.w) amesema: Mwenyezi Mungu hakuweka maradhi ila ameleta na dawa ya kuyatibu.

4. JUKUMU LA WAZAZI NA MAKUZI YA MTOTO

Sheria ya Kiislamu imewaamuru wazazi kuwa ni dhamana kwa maisha ya mtoto na makuzi yake. Kwa msingi wa kwamba, mtoto huchukuliwa kuwa ni dhamana waliyopewa, ambayo inapaswa kutunzwa nao kwani watakujaeleza mbele ya Mwenyezi Mungu (jinsi walivyoitunza amana waliyopewa). Mtoto mwanzoni mwa maisha yake huwa hajui hatari hasa ambazo zingehatarisha maisha yake. Kwa kuongezea ni kwamba yeye hawezi kujilisha na kuchunga maisha yake, kwa hivyo basi, ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya wazazi kuwa ni dhamana kwa ajili ya kuwalinda watoto wao kutokana na magonjwa mbalimbali na hatari ambazo zingetishia maisha na makuzi yao.

Imetajwa katika Hadith:Kila mmoja wenu ni mchungaji na kila mmoja ataulizwa juu ya kile akichungacho.

Baba ni mlezi wa jamii yake. Mke ni mchungaji wa mali ya mu mewe na watoto wake, na ndiye atakayeulizwa kuhusu akitunzacho. Mtumishi ni mtunzaji wa mali ya tajiri yake na ndiye atakayeulizwa kuhusu mali aitunzayo. Ndiyo, kila mmoja wenu ni mchungaji na ndiye atakayeulizwa juu ya anachokiangalia. Mbali na kuwa ni d hamana, ni wajibu wao pia kuwalisha watoto wao na kuwatosheleza mahitaji yao, hii inaweza kuwa kwa kuwachagulia kwa njia nzuri chakula chao, na kuwalinda kutokana na maradhi yote yatakayowadhuru.

Miongoni mwa hatari zinazoweza kutishia maisha ya mtoto katika miaka yake ya mwanzoni ni uwezekano wa kupatwa na mojawapo ya maradhi yauwayo watoto kama: Ugonjwa wa kupooza (Polio), Surua (Ukambi), dondakoo (DPT au Diphtheria) n.k. Au upungufu wa maji mwilini uletwao na magonjwa ya kuharisha n.k. Magonjwa hayo yote yanaweza kumshambulia mtoto, kumlemaza na kumhuzunisha maisha yake na ya wazazi wake. Uislamu unatuonya vikali sana tusipuuze matunzo na matibabu ya watoto wetu kutokana na maradhi yauwayo watoto au mengineo. Kwa ajili hiyo, Uislamu unaamrisha waumini wake kuwa wenye nguvu na afya. Mtume(s.a.w.w) amesema: Muislamu mwenye nguvu ni bora na ndiye apendezaye zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko Muislamu mnyonge.

Kwa kuwa upendo wa wazazi kwa watoto ni sehemu ya maumbile yao (wazazi) ya kiasili, ndipo ikawa hapana haja ya kuagizwa juu ya jambo hilo, kwa hivyo Uislamu umetilia mkazo zaidi umuhimu wa matunzo ya watoto na ukaonya vikali wazazi wasizembee katika jambo hilo, ili familia na jamii ziweze kuishi kwa raha na furaha. Na hii hatimaye huleta muundo wa kizazi ambacho kitategemewa kuweza kubeba mzigo wake barabara na katika hali ya kujitegemea. Imetajwa katika Qur ani:

Wala msijitie wenyewe katika maangamivu. (2:145).

Na je ni maangamivu gani maovu zaidi ambayo mtu anaweza akajifanyia mwenyewe kuliko kuingiza kiwiliwili chake na damu (watoto) wake kwenye hatari ya kifo na adhabu? Imetajwa tena katika Qur ani:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ﴿٦﴾

Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu (jamii) wenu kut okana na moto, ambao kuni zake ni watu na mawe (66:6).

Kujilinda na maangamivu (ya ugonjwa n.k.) kuna maana sawa na kuna daraja moja na kuilinda jamii kutokana na maangamivu ya motoni. Ikiwa kujilinda kunahitajika kwa ajili ya maisha ya akhera, basi kujilinda huko kunahitajika zaidi wakati wa maisha ya duniani kwani kile ukipendacho katika maisha yako duniani ndicho utakachokivuna akhera. Kujilinda kwa maana hiyo, hakumaanishi kujizuia kutokana na kutenda maovu, madhambi na mambo ya fedheha tu, bali ina maana ya ndani zaidi kuhusiana na usawa baina ya mahitaji ya nafsi, kiwiliwili, roho, na kujilinda na maneno ya Mtume(s.a.w.w) aliposema:Yatosha kwa mtu kupata dhambi kwa kutomjali yule anaemtegemea.

Pia:Nyote ni wachungaji na kila mmoja wenu ataulizwa kutokana na kile anachokichunga.

Tukizingatia, inatudhihirikia wazi kwamba kuwakinga watu wetu kutokana na maradhi ni amri ya kidini na ni wajibu wa jamii na pia ni wajibu wa taifa zima. Mtume(s.a.w.w) amesema: Mwenye kuitunza jamii na hakuipa nasaha (maonyo), basi mtu huyo atanyimwa pepo. Kuwapatia watoto huduma za chanjo dhidi ya maradhi yauwayo na yalemazayo, humwokoa mtunzaji wa jamii kutokana na kosa la kupuuza jamii yake. Na mwishowe ataokoka Siku ya Kiyama kutokana na vitisho ambavyo vingempat a wakati Mwenyezi Mungu atapomuuliza kuhusu hali ya wafuasi wake (wenye kumtegemea) na sababu ya kuwa mzembe katika jambo hilo. Kwa hivyo basi, iwapo wazazi hawatachukua hatua zifaazo ili kulinda maisha ya watoto wao kuwakinga kutokana na maradhi, kuna uwezekano mkubwa wa kunyimwa pepo akhera.

Chanjo na huduma za O.R.S. (Maji ya dawa ya kurudisha maji mwilini kutokana na maradhi ya kuharisha) hutolewa bure na serikali. Wazazi wanachotakiwa kufanya ni kuzitumia huduma hizi, ili kuwakinga watoto wao kutokana na madhara na hatari ziletwazo na magonjwa. Hata kama watalazimika kulipa ili watoto wao wachanjwe, Uislamu unawapa moyo kufanya hivyo, kwani Mtume(s.a.w.w) amesema: Bora ya matumizi, ni kutumia (japo) senti kwa ajili ya familia yako.

5. KUWALINDA WATOTO NI HURUMA, NA HURUMA NI KINGA

Mtume(s.a.w.w) ametueleza mpango maalum wa kutuwezesha tuwe na huruma na upendo kwa watoto wetu. Ametaja Bukhari katika kitabu chake cha Al-Adab, katika mlango maalum kwamba wahurumieni watoto na pale Mtume(s.a.w.w) ali posema: Si katika sisi yule mtu asiyemhurumia mdogo, na asiyejua haki ya mkubwa (asiye mheshimu). Akasema tena: Rehemuni (sikitikieni) wenzenu, nanyi mtarehemewa. Ni dhahiri kutokana na Hadith zilizotajwa hapo juu kwamba Mtume(s.a.w.w) ameeleza jinsi wa le watu ambao hawana huruma kwa wadogo zao wanavyochukuliwa kuwa si waislamu wa kweli na hawako pamoja na Mtume(s.a.w.w) na ujumbe wake Mtukufu. Inasemekana kuwa hapana yeyote awezaye kuwa na huruma kwa mtoto kama ilivyo wazazi wake (mtoto).

Ikiwa Mtume(s.a.w.w) amewataka watu wote kwa pamoja kuwa na huruma kwa watoto, basi ni jambo lililo muhimu zaidi kwanza kwa wazazi kuwaonea huruma watoto wao kuliko watu wengine. Sehemu ya huruma yao kwa watoto wao ni kuwapeleka wakapatiwe chanjo na kinga kutokana na magonjwa na maradhi yote yenye kuenea yawezayo kuwashambulia.

Wazazi watakapokuwa na huruma kwa watoto wao, basi huruma hiyo hiyo huwarudia (wazazi) wakati wa uzeeni kwa sababu upendo ni kitu cha kulipana. Mtume(s.a.w.w) ameeleza kwa ubainifu kuhusiana na suala hili la huruma na kinga, na akaeleza jinsi huruma ilivyokuwa sehemu ya kinga na kinga ni sehemu ya huruma. Amesema: Harehemiwi (haonewi huruma) yule mtu asiyemrehemu mwingine, na hasemehewi yule asiyemsamehe mwingine, wala hapewi toba (na Mwenyez i Mungu) mtu asiyetubu, na wala halindwi yule asiyejilinda.

Katika Hadith hii Mtume(s.a.w.w) ametilia mkazo ya kuwa huruma ndilo jambo la msingi na akaeleza ya kwamba, yeyote asiyejilinda, basi Mwenyezi Mungu hatamlinda kutokana na maradhi. Ijapokuwa jambo hilo limeelezwa, lakini Mtume(s.a.w.w) amelielezea kimantiki kwa njia ya maombi. Amesisitiza Mtume(s.a.w.w) kwamba, yeyote asiyejilinda ama kulinda wengine kutokana na kitakachowadhuru au kuwaingiza hatarini au kwenye ugonjwa, basi Mwenyezi Mungu naye hawezi kumlinda kutokana na mambo hayo. Kwa hivyo basi Mtume(s.a.w.w) katika maelezo yake hapa anakusudia kuifanya huruma isambae miongoni mwa watu, na anaazimia kuwapa moyo watu kujaribu kupata huduma za kinga zifaazo dhidi ya hii ikiwa ni kukamilisha sehemu ya huruma.

6. UISLAMU NA UZAZI WA MPANGO

Qur ani imefafanua waziwazi kuhusu muda maalum ufaao kwa kutenganisha baina ya kuzaliwa mtoto mmoja hadi kupata mwingine. Imetajwa ndani ya Qurani kuwa kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha kunyonya ni kipin di cha miezi thelathini; Amesema Mwenyezi Mungu:

Kubeba mimba ya mtoto hadi kumwachisha ni miezi thelathini (46:15) Pamoja na hayo, Uislamu unaunga mkono kunyonyesha kwa maziwa ya mama kunakodumu kwa miaka miwili kamili kwa wale wanaotaka kutimiza muda huo kamili. Kwa kufanya hivi, kunamwezesha mama (aliyezaa) kurekebisha afya yake, na kumrudisha nguvu zake za mwilini alizozipoteza katika kipindi cha uja uzito hadi kujifungua.

Muda huu maalum pia utamwezesha mtoto kupata muda wa kutosha wa kunyonya matiti ambapo utaalamu wa utabibu (wa kisasa) umekuja kuunga mkono baada ya kutofaulu kwa muda mrefu, kwa kutumia chupa ya kunyonyea.

Kwa hivyo hapa ni dhahiri namna gani Uislamu unavyopigania uzazi wa mpango ili kuwapatia afya bora mama na mtoto.

Imetajwa katika Qur ani:

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ إِحْسَانًا حَمَلَتْهُ أُمُّهُ كُرْهًا وَوَضَعَتْهُ كُرْهًا وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا ﴿١٥﴾

Na tumemwusia mwanaadamu kuwatendea wema wazazi wake, mama yake amechukua mimba yake kwa taabu, na akamzaa kwa taabu, kubeba mimba yake mpaka kumwachisha kunyonya ni (kipindi cha) miezi thelathini (46:15).

Imetajwa pia katika Qurani:

وَوَصَّيْنَا الْإِنسَانَ بِوَالِدَيْهِ حَمَلَتْهُ أُمُّهُ وَهْنًا عَلَىٰ وَهْنٍ وَفِصَالُهُ فِي عَامَيْنِ ﴿١٤﴾

Na tumemuusia mwanaadamu kuwafanyia mema wazazi wake, mama yake amebeba mimba yake kwa unyonge juu ya unyonge, na (kumnyonyesha na) kumwachisha kunyonya katika miaka miwili.

7. UISLAMU NA KARANTINI ZA AFYA

Uislamu unaonya sana tuwe macho kutokana na maradhi yaambukizayo na unatusihi tujikinge na maradhi hayo. Imepokewa Hadith ya kwamba Mtume(s.a.w.w) alibaiwa (kuungwa mkono wa uongozi) na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma pasi na kupeana naye mkono[1] , ama kumruhusu kutangamana na watu. Imepokewa kutoka kwa Umar bin Shareed, kutoka kwa baba yake amesema:

Katika ujumbe wa Thaqif uliokuja kum bai (kumtambua kama kiongozi) kulikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa ukoma, basi Mtume(s.a.w.w) alimrejesha (bila ya kumpa mkono) kwa kusema: Hakika tumekutambua. Na katika Sahih Bukhari, Mtume(s.a.w.w) amesema: Kaa mbali na mwenye ukoma kama unavyokaa mbali na simba. Mtume(s.a.w.w) ameeleza wazi wazi kwamba wakati yatapoingia maradhi ya tauni, watu ni lazima wawe macho sana, na wachukue hadhari zote za lazima ili kujikinga na kujiepusha na mtu aliyeambukizwa.

Imetajwa katika Hadith:Tauni (ugonjwa ueneao) ni alama ya adhabu ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu huwajaribu nayo watu miongoni mwa waja wake. Mtakaposikia kuwa umeingia nchini, basi msiingie nchini humo na iwapo utatokea nanyi mko ndani ya nchi hiyo basi msitoke.

Hapa Mtume(s.a.w.w) anaamuru Karantini na anatukataza kuingia katika nchi iliyokumbwa na ugonjwa wa tauni, ili tujilinde kutokana na kifo, vile vile tumeonywa tusitoke nje ya nchi ambayo tayari imekumbwa na ugonjwa huo, ili tusisambaze maradhi. Na hii pia ni aina nyingine ya kujilinda. Aina hizi mbili za maonyo (zilizotangulia hapo juu) zinachukuliwa kuwa ni aina za hasi (Negative) za kujikinga. Wakati ambapo kuchanja kwa ajili ya kinga za magonjwa na maradhi ya kuambukiza ni aina ya chanya (Positive). Kwa hivyo Uislamu unapigania sana aina hii ya chanjo kwani ndiyo iliyo bora na ni yenye gharama ndogo zaidi kuliko matibabu.