TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 18979
Pakua: 2846


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 18979 / Pakua: 2846
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London. Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati. Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kungangania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh alaa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine. Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa. Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure, lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

MWISHO

Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji. Mchapishaji

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa. Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya Msahafu Mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswatu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Yaalamuun,(hawajui) badala ya Yaalamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile. Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail Makosa ya chapa. Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idaha balagha arbai na sanah badala ya: Hattaidaha balagha ashuddahu arbai na sanah Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana. Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin)

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿سَيَقُولُ السُّفَهَاءُ مِنَ النَّاسِ مَا وَلَّاهُمْ عَن قِبْلَتِهِمُ الَّتِي كَانُوا عَلَيْهَا قُل لِّلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴾

142.Watasema wapumbavu miongoni mwa watu: Nini kilichowageuza kutoka Qibla chao walichokuwa wakikielelekea? Sema: Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu, Humwongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka.

﴿وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا لِّتَكُونُوا شُهَدَاءَ عَلَى النَّاسِ وَيَكُونَ الرَّسُولُ عَلَيْكُمْ شَهِيدًا وَمَا جَعَلْنَا الْقِبْلَةَ الَّتِي كُنتَ عَلَيْهَا إِلَّا لِنَعْلَمَ مَن يَتَّبِعُ الرَّسُولَ مِمَّن يَنقَلِبُ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَإِن كَانَتْ لَكَبِيرَةً إِلَّا عَلَى الَّذِينَ هَدَى اللَّـهُ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُضِيعَ إِيمَانَكُمْ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴾

143. Na kama hivyo hivyo tumewafanya kuwa umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu wote, na Mtume awe shahidi juu yenu. Na hatukukifanya Qibla ulichokuwa nacho ila tupate kumjua yule anayemfuata Mtume na yule atakayegeuka akarudi nyuma. Na kwa hakika lilikuwa ni jambo gumu isipokuwa kwa wale aliowaongoza Mwenyezi Mungu. Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwapotezea imani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole Mwenye kurehemu.

NINI KILICHOWAGEUZA KUTOKA QIBLA CHAO?

Aya 142

LUGHA

Amesema Ibnul Arabi katika tafsiri yake: Kila asiyejua hakika ya Dini ya Kiislamu huyo ni mpumbavu, kwa sababu yeye ana akili hafifu.

Neno: Qibla limechukuliwa kutoka katika neno Istqbal (kuelekea); yaani kila upande anaoulekea mtu.

MAANA

Watasema wapumbavu miongoni mwa watu: Nini kilichowageuza kutoka Qibla chao walichokuwa wakikielekea?

Mitume waliotangulia walikuwa wakiswali kuelekea Baitul Maqdis.Na Mtume Muhammad(s.a.w.w) alikuwa akitamani lau Qibla kinageuzwa kuwa Al-Kaaba. Mwenyezi Mungu aliyathibitisha matamanio yake, kama itakavyoelezwa.

MAKUSUDIO YA WAPUMBAVU

Makusudio ya wapumbavu hapa ni Mayahudi, ndio waliowalaumu Waislamu kwa kuacha kwao kuelekea BaitulMaqdis.

MAANA YA TAMKO SAYAQULU (WATASEMA)

Tamko Sayaqulu (Watasema) kwa dhahiri linafahamisha kuwa: Mwenyezi Mungu alimfahamisha Mtume wake Mtukufu kauli ya wajinga kabla ya kutokea. Ama yule anayesema kuwa neno Sayaqulu ingawaje kwa dhahiri linafahamisha muda wa mbele, lakini makusudio ni muda uliopita; na kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wake baada ya kusema wajinga, sio kabla ya kusema; na kwamba limekuja kwa muda ujao, kwa vile yaliyosemwa yalikuwa yamekwisha kadiriwa, ama kwa hakika kauli hii ni kujaribu kutoa tafsir nyingine (Taawil) bila ya dharura yoyote na bila ya dalili yoyote inayofahamisha hilo.

Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) alimwamrisha Mtume wake Mtukufu Muhammad(s.a.w.w) kuwajibu wajinga hawa kwamba:Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; humwongoza amtakaye katika njia iliyonyooka . Yaani pande zote ni za Mwenyezi Mungu: Al-Kaaba na Baitul Maqdis ni sawa tu, lakini kwa hekima na masilahi mara nyingine humwongoza anayemtaka kwenye Baitul-Maqdis na mara nyingine kwenye Al-Kaaba.

KWA NINI KUSWALI UPANDE MAALUM?

Hili ni swali wanaloliuliza watu wengi kwa nini swala ni wajibu kwenye upande malum na haiswihi isipokuwa upande huo? Na hali yeye amekwisha sema waziwazi:

﴿ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ﴾

Na popote mnakoelekea (mtazikuta) radhi za Mwenyezi Mungu (2:115)

Jibu :Kwanza : Mwenyezi Mungu s.w.t. amesema:

﴿ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ﴾

...Na elekeza uso wako upande wa msikiti Mtakatifu (Al-Kaaba); na popote mlipo zielekezeni nyuso zenu upande huo... (2:144).

Aya hii ni ubainifu na Tafsir ya Aya 115 na makusudio yake ni kuelekea kwenye upande wowote katika swala ya Sunna na katika swala ya asiyejua Qibla kiko wapi. Makusudio ya Aya 144 ni kuelekea (Al-Kaaba) katika swala ya wajibu. Umekwishatangulia ufafanuzi wa hilo katika Aya 115.

Pili : kuswali swala kunategemea amri ya Mwenyezi Mungu. Kutokana na asili hii hapana budi tuangalie: Je inawezekana tuswali upande wowote tunaoutaka sisi au kwenye upande maalum. Ikiwa kauli ya kwanza ni sawa, basi itakuwa haiswihi swala isipokuwa kwenye upande ulioamrishwa tu; ni sawa iwe ni Al-Kaaba au Baitul-Maqdis au mahali pengine. Pia ifahamike kwamba kufuata amri ni jambo jengine na kuweko radhi za Mwenyezi Mungu kila upande ni jambo jengine. Hakika ibada ni katika mambo yanayongoja ubainifu wa Mwenyezi Mungu kupitia kwa Mtume wake, wala hakuna nafasi ya dhana na uwezekano; isipokuwa kwa kauli sahihi iliyo wazi. Na Mwenyezi Mungu aliaamrisha Waislamu kuswali kuelekea Baitul-Maqdis kwanza; lau wangeliswali kuelekea Al-Kaaba isingekubaliwa swala yao. Kisha Mwenyezi Mungu akawaamrisha kugeuka Al-Kaaba lau wangeling’ang’ania Baitul-Maqdis basi isingekubaliwa swala yao; pamoja na kuwa pande zote mbili ni za Mwenyezi Mungu. Hilo ni kwa sababu kipimo cha kusihi swala ni kuafikiana na sharti zote; kama vile ambavyo kuharibika swala ni kuhalifu amri.

UMMA WA WASTANI

Aya ya 143

LUGHA

Neno: Wast lina maana ya kati kati, na neno Wasat lina maana ya ubora, Mtume anasema:Bora ya mambo ni wastani. Linakuja neno wasata, Kwa maana ya kulingana sawa (wastani). Neno wastani na ubora yanakurubiana. Makusudio ya Wasat hapa ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameijaalia dini ya Waislamu ni ya wastani; yaani ni ya kati na kati katika itikadi na maadili. Kwa upande wa itikadi hakuna ushirikina wala ulahidi, bali ni Tawhid tu, na kwa upande wa maadili sio ya kimaada wala kiroho, bali ni pande zote mbili kwa sharti ya kulingana sawa na kukamilika. Neno kurudi nyuma ni istiara yaani kueleza mtu anayemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake; Kwa sababu mwenye kuacha imani yake yuko katika daraja ya asiyeendelea mbele.

MAANA

Tumewafanya kuwa umma wa wastani . Jumla hii ni ubainifu wa kauli ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

Humwongoza amtakaye kwenye njia iliyonyooka . (2:213).

Njia ya kubainisha hayo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amewaneemesha wafuasi wa Muhammad(s.a.w.w) kwa uongofu. Linalodhihirisha zaidi uongofu huu ni kuwa Yeye amewajaalia wao kuwa katikati; yaani hawakuzidisha, kama vile kuwazidisha waungu, wala hawakupunguza; kama vile ulahidi (kumkana Mungu). Hayo ni upande wa kiitikadi. Ama upande wa kimadili wastani wake ni, kwa kuwa amewachanganyia mambo ya kiroho na ya kimwili katika mafunzo yake na maelekezo yake - sio ubahili wa kiroho wala ubadhirifu wa kimaada, bali kuna uwiano kati yao.

Baadhi wameifanya kauli hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: Tumewajaalia ni umma wa wastani, kuwa ni dalili ya hoja ya Ijmai. Lakini hiyo ni kutoa dalili mahali pasipokuwa pake. Kwa sababu haikuja kubainisha Ijmai, kwamba ni hoja au sio hoja. Wengine wamesema kwamba kauli hii ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) inafahamisha kuwa kila Mwislamu ni mwadilifu kwa tabia. Hii pia nayo ni batil kabisa. Kwa sababu uadilifu hauthibiti isipokuwa kwa kujua au kwa ushahidi.

UKAMILIFU NA UWIANO KATIKA UISLAMU

Binadamu ni mwili uliotokana na mchanga unaokwisha na ni roho inayodumu inayotokana na siri ya Mwenyezi Mungu, kama alivyosema:

﴿ وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي ﴾

Na wanakuuliza kuhusu roho, Sema: Roho ni katika mambo ya mola wangu. (17:85).

Kwa vile vitu viwili hivyo (mwili na roho) vina mahitaji na matakwa ndipo ikaletwa sharia ya Kiislamu kwa ajili ya kutoa maelekezo ya msingi na nidhamu ili visizidiane. Kwa maneno mengine binadamu ni sehemu mbili, kupuuza moja wapo ni kumpuuza binadamu mwenyewe. Uislamu umekataza utawa na kuiepusha nafsi na maumbile ya kawaida, kama ambavyo umehalalisha starehe za maisha, kama kula, kuvaa vizuri nk. Atakayeziangalia Aya za Quran atakuta kwamba dunia yote imeumbwa kwa ajili ya uhai wa mtu kwa namna inayokubalika kwa wote, lakini wakati huo huo kuipupia kuifanyia hiyana na kuwazuia watu wengine na hiyo dunia ni ufisadi na hatari kwa usalama wa jamii. Riziki bora kabisa katika Uislamu ni ile iliyotolewa jasho.

Anas anasema: Siku moja tulikuwa na Mtume(s.a.w.w) safarini wengine wakawa wamefunga na wengine hawakufunga. Tukashuka sehemu fulani ilikuwa ni wakati wa joto. Basi waliofunga wakaanguka wote,ikawa wasiofunga wanawahudumia waliofunga. Mtume(s.a.w.w) akasema:Wasiofunga leo wamechukua malipo yote . Huu ndio msingi wa uwiano katika Uislamu. Sio ibada itayozuia kuhangaika wala sio ulafi utakayozuia kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Ili muwe mashahidi juu ya watu na Mtume awe shahidi juu yenu.

Maana ya matamko haya yako wazi na maana ya kiujumla pia iko wazi. Lakini tatizo liko kwenye kuelezea sisi Waislamu ni mashahidi juu ya akina nani? Mtume(s.a.w.w) atakuwa shahidi kesho dhidi ya yule aliyehalifu miongoni mwetu, je sisi tutakuwa mashahidi dhidi ya wasiokuwa Waislamu ambao wamehalifu Kitabu na Sunna? Kauli zimekuwa nyingi na kugongana juu ya hilo; nami sikupata ya kunituliza. Nionavyo mimi ni kwamba Ulama wa Kislamu wanawajibu wa kuufikisha ujumbe wa Muhammad(s.a.w.w) kwa watu wawe ni Waislamu au si Waislamu wasiojua au wawe wanajua. Mwenye kutekeleza wajib huu Mtukufu, basi atakuwa shahidi dhidi ya yule aliyemfikishia kuwa hakuyatumia mafunzo. Na, atakayepuuza wajib huu na asiufikishe, basi

Muhammad(s.a.w.w) atakuwa shahidi dhidi yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu kwamba yeye amefanya hiyana. Kwa ufafanuzi zaidi tupige mfano huu: Mtu ana mali na mtoto mdogo, alipohisi kifo chake kiko karibu akamuusia mtu anaye mtegemea kwa dini yake amlee mtoto wake kutokana na mali atakayoiacha. Akitekeleza yule aliyeusiwa na mtoto akafaulu, basi nisawa, lakini mtoto akifanya uasi na akakataa mfunzo, basi aliyeusiwa atakuwa shahidi dhidi ya mtoto na kama aliyeusiwa ndiye aliyezembea, basi mzazi atakuwa shahidi dhidi ya aliyeusiwa. Vilevile sisi Ulama tuna majukumu makubwa mbele ya Mwenyezi Mungu ya kufikisha mwito wa Kiislamu kwa watu wenye dini mbali mbali kwa hekima na mawaidha mazuri. Na atakayezembea wajib huu kesho atashuhudiwa na bwana wa viumbe na atahukumiwa. Hii ni ikiwa amepuuza, sikwambii ikiwa yeye ndiye sababu ya kupatikana shaka katika watu wake?

Na hatukukifanya Qibla ulichokuwa nacho ila tupate kumjua yule anayemfuata Mtume na yule atakayegeuka akarudi nyuma.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwamrisha Mtume wake kugeuza Qibla baadhi ya watu walianza kutia shaka na kusema: mara huku na kesho kule. Na Mayahudi nao wakachukua fursa ya kuwatia shaka wajinga kuhusu Mtume. Hao Mayahudi walikuwa wamekuwa na wataendelea kuwa ni watu wa fitina na uvunjaji; wenye vitimbi na hadaha. Wanatengeneza matatizo na kumwekea vikwazo kila mwenye Ikhlas na wanajaribu kuzigeuza jamii kuzipeleka kwenye matatizo. Ndio tabia na maumbile yao. Ndivyo ilivyo, mara nyingi maadui wa haki wanawatumia wadhaifu wa akili na kuwafanya ni chombo cha kufanya vitimbi, uharibifu na vurugu. Imam Ali amewaelezea kwa ufasaha zaidi aliposema: Ni wanyama wasiokuwa na mchungaji wanamfuata kila atakayewapigia kelele ni (bendera) wanafuata upepo, hawakupata mwanga wa elimu wala hawana cha kutegemea. Mwenyezi Mungu alimpa habari Mtume wake Mtukufu kwamba wale wanaotia shaka si waumini halisi na tumewapatia mtihani huu ili ufichuke ukweli kwako na kwa wengine.

Na kwa hakika lilikuwa ni jambo gumu, ispokuwa kwa wale aliowaongoza Mwenyezi Mungu.

Ambao ni wenye imani halisi sio imani ya kuazima. Unaweza kuuliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anajua kila kitu kabla ya kutokea, sasa kuna wajihi gani kusema: ili tumjue anayemfuata Mtume?

Jibu : Lengo hapa ni kumdhihirisha mtiifu na asiyekua mtiifu na libainike hilo mbele za watu. Wafasiri wengi wamesema kwamba Mwenyezi Mungu ana elimu mbili ya kujua kitu kabla ya kuwa ambayo ni elimu ya ghaib na elimu baada ya kuwa, ambayo ni elimu ya ushahidi na ndiyo iliyokusudiwa katika Aya hii, yaani Mwenyezi Mungu ametaka kujua baada ya kuwa, kama alivyo jua kabla ya kuwa.

Huku ni kucheza na maneno tu. Elimu ya Mwenyezi Mungu ni moja, elimu ya ghaib ndiyo hiyo hiyo elimu ya ushahidi

Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kupoteza imani yenu. Hakika Mwenyezi Mungu kwa watu ni mpole mwenye kurehemu

Hii ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa wale wenye uthabiti katika imani yao kwa Mtume(s.a.w.w) kwa shida na raha. Wanafuata amri yake na wanaacha makatazo yake. Wafasiri wengi wamesema kuwa sababu ya kushuka Aya hii ni kwamba baadhi ya masahaba waliswali na Mtume kibla cha kwanza na wakafa kabla ya kugeuzwa kibla cha pili, akaulizwa Mtume kuhusu swala yao, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo. Sisi hatutegemei mapokezi ya sababu za kushuka Aya isipokuwa machache tuliyo na yakini nayo. Kwa sababu maulamaa hawakujishughulisha sana na usahihi wake, kama walivyofanya kwa mapokezi ya hukumu.

﴿ قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَحَيْثُ مَا كُنتُمْ فَوَلُّوا وُجُوهَكُمْ شَطْرَهُ وَإِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَيَعْلَمُونَ أَنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّهِمْ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا يَعْمَلُونَ ﴾

144.Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni; basi tutakuelekeza Qibla ukipendacho. Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu (Al-Kaaba). Na popote mlipo geuzeni nyuso zenu upande huo. Na hakika wale waliopewa Kitabu wanajua kwamba huo ni haki itokayo kwa Mola wao; na Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.

﴿ وَلَئِنْ أَتَيْتَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ بِكُلِّ آيَةٍ مَّا تَبِعُوا قِبْلَتَكَ وَمَا أَنتَ بِتَابِعٍ قِبْلَتَهُمْ وَمَا بَعْضُهُم بِتَابِعٍ قِبْلَةَ بَعْضٍ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ إِنَّكَ إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ ﴾

145.Na hao waliopewa Kitabu hata ukawaletea hoja za kila namna, hawatafuata Qibla chako; na wala wewe si mwenye kufuata Qibla chao, wala baadhi yao si wenye kufuata Qibla cha wengine. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya kukufikia elimu, utakuwa miongoni mwa madhalimu.

HAKIKA TUNAKUONA UNAVYOGEUZA USO WAKO

Aya 144-145

MAANA

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Imepokewa kutoka kwa Imam Jaffar Sadiq(a.s) kwamba:Kiligeuka Qibla baada ya kuswali Mtume (s.a.w.w), Makka kwa muda wa miaka 13 akielekea Baitul Maqdis. Na baada ya kuhamia Madina, aliswali miezi saba, kisha Mwenyezi Mungu akamwelekeza Al Kaaba .

SABABU YA KUTEREMSHWA AYA

Sababu hiyo ni kwamba Mayahudi walikuwa wakimkejeli Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumwambia: Wewe unatufuata sisi, unaswali kwenye Qibla chetu. Mtume akaingiwa na majonzi makubwa, akatoka usiku akawaana angalia pambizoni mwa mbingu, akingojea amri ya Mwenyezi Mungu kuhusu jambo hilo. Kulipokucha akaswali swala ya Adhuhuri katika msikiti wa Bani Salim, alipomaliza rakaa mbili alishukiwa na Jibril akamshika na kumgeuza upande wa Al-Kaaba, akamteremshia Aya hii:Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako mbinguni, Mtume akaswali rakaa mbili kuelekea Baitul Maqdis na rakaa mbili kuelekea Al- Kaaba.

Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti mtakatifu (Al Kaaba).

Ameusifu Msikiti kwa utakatifu, ambapo ni wajibu kuutakasa na ni haramu kuuvunjia heshima. Al-Kaaba ni sehemu ya Masjidul Haram (Msikiti Mtakatifu) nao ni sehemu ya Haram ambayo inakusanya Makka na mipaka yake, kama ilivyoelezwa katika vitabu vya Fiqh, katika mlango wa Hijja, katika masuala ya Ihram na kuwinda katika Haram. Yanayojulikana katika Quran ni kwamba amri ya wajib yoyote ya kisharia inayoelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu inawahusu watu wote, mfano:

﴿ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ﴾

Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na mwanzo wa usiku. (11:114).

Haiwezekani kuwa amri ya wajib inahusika na yeye Mtume tu, ila kama kuna kitu kinachofahamisha hilo; kama Aya hii:

﴿ وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ﴾

Na katika usiku swali Tahajjud ([1] ), Hiyo niSunna kwa ajili yako... (17:79).

Neno: kwa ajili yako linafahamisha kwamba taklifa hii haimuhusu mtu mwingine isipokuwa yeye. Vile vile njia ya Quran ni kwamba taklifa zenye kuelekezwa kwa watu na Muhammad(s.a.w.w) pia huwamo, bila ya kuwako na tofauti hata ndogo ya mwelekezo huo kati yake na mwingine. Kwa hivyo umma unaingia katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Basi elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtukufu (Al-Kaaba).

Na popote mlipo geuzeni nyuso zenu upande huo .

Yaani popote mnapokuwa baharini au bara, kwenye tambarare au majabalini, Mashariki au Magharibi, ni juu yenu kuelekea Msikiti Mtukufu kwa sehemu ya mbele ya mwili, wala haijuzu kuupa mgongo katika swala au kuuelekea kwa upande wa kuume au kushoto, nk. Kutokana na hali hiyo Qibla kinahitalifiana kwa kuhitalifiana miji. Kwa ajili hii Waislamu wamejishughulisha sana na suala la Qibla na wakaweka elimu mahsus kwa jina la elimu ya Qibla, Kinyume na Wakristo ambao wanalazimiana na upande wa Mashariki daima na Mayahudi nao ni upande wa Magharibi popote walipo, hata kama hilo litalazimisha kuipa mgongo Baitul Maqdis.

Unaweza kuuliza: Ikiwa Umma unaingia katika msemo unaoelekezwa kwa Mtume na msemo unaolekezwa kwa Umma unamhusu Mtume; sasa kwa nini kukusanyika misemo inayoelekea sehemu mbili katika Aya moja na maudhui moja tena bila ya kuwako kitenganisho. Yaani Mwenyezi Mungu anasema elekeza uso wako- ewe Muhammad - upande wa Msikiti Mtakatifu, na popote mtakapokuwa - enyi Waislamu - elekezeni nyuso zenu upande uliko Msikiti Mtakatifu.

Jibu : Kugeuka Qibla ni tukio kubwa katika Uislamu na kulikuja kutokana na raghba ya Mtume(s.a.w.w) . Kwa hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akataka kumbainishia hilo, na kulitilia mkazo kwa kulikariri. Zaidi ya hayo ni kuwa kwa asili taklifa hiyo ni ya Muhammad(s.a.w.w) , kwa sababu imekuja kwa raghba yake na kufuatilia umma wake.

NI WAJIB WAKATI GANI KUELEKEA QIBLA?

Al Kaaba ni Qibla kwa aliye ndani ya Msikiti Mtakatifu ambao Al Kaaba imo ndani yake, Msikiti ni Qibla kwa watu wa Haram; yaani watu wa Makka na pembeni mwake na Haram au upande wake ni Qibla kwa watu wa Mashariki na Magharibi. Ni wajibu kuelekea Qibla katika swala za kila siku, swala ya ihitiyat, mafungu yaliyosahauliwa katika swala na sijda mbili za kusahau. Vile vile ni wajibu kuelekea Qibla kwa ajili ya swala yoyote ya wajibu, ikiwemo Swala ya tawaf, na Swala ya kumswalia maiti. Pia ni wajibu kumwelekeza Qibla mtu aliye katika hali ya kukata roho na wakati wa kumzika, na wakati wa kumchinja mnyama. Ama katika swala za sunna ni wajibu kuelekea Qibla katika hali ya utulivu tu, na wala sio wajibu katika hali ya kutembea na kupanda chombo cha kusafiria.

WATU WA QIBLA

Watu wa Qibla, watu wa Quran, watu wa shahada mbili na Waislamu, yote hiyo ni misamiati iliyo katika maana moja. Ama lile jina la Wafuasi wa Muhammad (Mohammedan), ni jina tulilobandikwa na maadui wa Uislamu, wakiwa na maana kwamba sisi ni wafuasi wa mtu na wala sio wa dini ya Mwenyezi Mungu; kama Mabudha ambao ni wafuasi wa Budha na Wazaradashti ambao ni wafuasi wa Zaradasht. Kwa vyovyote vile lengo la kifungu hiki ni kuzindua kwamba umma wa Kiislamu, pamoja na kutofautiana miji yake, rangi na lugha, lakini unakusanywa na kuwa pamoja na misingi ya aina moja, ambayo ni ghali na yenye thamani zaidi kuliko uhai. Kwa sababu Waislamu wanadharau maisha kwa ajili ya misingi hiyo na wala hawawezi kuidharau misingi hiyo kwa ajili ya maisha. Misingi hiyo ni pamoja kumwamini Mwenyezi Mungu na kitabu chake, kumwamini Muhammad(s.a.w.w) na sera yake na kuswali kwa kuelekea Qibla. Basi mwenye kumkufurisha mwenye kuswali kwa kuelekea Qibla na akamtoa katika idadi ya Waislamu, atakuwa ameidhoofisha nguvu ya Uislamu na atakuwa amelichana jina la Waislamu, na kusaidia maadui wa dini, atake asitake.

Na hakika wale waliopewa kitabu wanajua kwamba huo ni haki itokayo kwa Mola wao.

Makusudio ya waliopewa kitabu ni Mayahudi na Wakristo, na wala sio Mayahudi peke yao, kama ilivyosemwa. Kwa sababu neno linaenea, na wala hakuna dalili ya kuhusisha. Wafasiri wametofautiana katika dhamiri ya neno Annahul-haqq kwamba je ni huo Msikiti au ni huyo Mtume? Sababu ya kutofautiana ni kwamba Mwenyezi Mungu nyuma amemtaja Mtume kwa kusema: Kwa hakika tunakuona unavyogeuza geuza uso wako na vile vile ametaja Msikiti Mtakatifu. Sisi tuko katika upande wa wanaosema kuwa dhamiri inarudia Msikiti kwa sababu ndilo tamko la karibu zaidi, na dhamiri inarudia tamko la karibu zaidi.

Kwa hiyo maana yanakuwa, watu waliopewa kitabu wanajua kabisa kwamba Ibrahim(a.s) ni baba wa Mitume na ni mkubwa wao ambaye alijenga Nyumba Tukufu (Al Kaaba), lakini wao wameikataa kwa vile tu, iko mikononi mwa Waarabu ambao wanaitumikia na kuihami. Lau isingelikuwa mikononi mwa Waarabu, Mayahudi wangelikuwa wa kwanza kuitukuza na wangeliiheshimu sana.

Na hao waliopewa kitabu hata ukiwaletea hoja za kila namna hawatafuata Qibla chako .

Yaani hawafuati mila yako, sembuse kufuata Qibla chao.Nao hawana hoja yoyote isipokuwa ujinga na ukaidi .Na wala wewe si mwenye kufuata Qibla chao .

Huenda baadhi ya watu wa Kitab walitaraji kuwa Mtume(s.a.w.w) atarudia Qibla alichokielekea kwanza, ndipo Mwenyezi Mungu akawakatisha tamaa kabisa kwa kauli yake hiyo; kama alivyomkatisha tamaa Muhammad(s.a.w.w) kuwa wao hawatafuata Qibla chake.

Wala baadhi yao si wenye kufuata Qibla cha wengine.

Mayahudi wanaswali kuelekea Magharibi na Wakristo wanaelekea Mashariki, wala kundi moja haliwezi kulifuata kundi jingine, vipi wataweza kufuata Qibla chako ewe Muhammad? Bali hata hao Mayahudi wanatofautiana; kama walivyo Wakristo. Mauaji yaliyotokea kati ya Wakatoliki na Waprotestant, hayana mfano wa fedheha yake katika zama zote.

Na kama ukifuata matamanio yao baada ya kukufikia elimu, utakuwa miongoni mwa madhalimu.

Ni muhali kuwa Mtume afuate matamanio yao, kwa sababu yeye ni masum (mwenye kuhifadhiwa na madhambi), lakini lengo la makatazo haya ni kumpa nguvu Mtume katika kuamiliana kwake na Mayahudi na kusimama nao imara, na kwamba hakuna heri yoyote ya kupatana nao wala hakuna,tumaini lolote kwao. Haliwezi kufaa jaribio lolote la kuwazuia na vitimbi na ufisadi wao. Kwa sababu wao wana maumbile ya shari. Kupinga haki na kumfanyia uovu anayewafanyia wema. Yamekwishaelezwa maelezo zaidi katika kufasiri Aya ya 120.

UISLAMU NAWATU WENYE UPENDELEO NA DINI ZAO

Ni jambo lenye kuingia akilini kwamba wataalamu wanaweza kuhitilafiana katika aina yoyote ya masuala yasiyokuwa ya kidini. Baada ya kukumbushana na kudurusi, huafikiana katika lile walilohitilafiana. Hilo limekwishatokea. Ama wakihitalifiana katika masuala ya dini mbali mbali, basi kuafikiana kwao ni muhali, hata kama zitakuwepo dalili elfu. Imethibiti kwa wataalamu wa elimu ya saikolojia, kwamba watu kubadili tabia yao ni rahisi zaidi tena sana kuliko kubadili dini yao.

Hilo ni kwamba watu wengi hutegemea dini za mababa na mababu. Hakuna dini iliyojulikana kukataza kufuata mababu isipokuwa Uislamu ambao umetegemea akili peke yake katika kuthibitisha misingi yake. Mwenye kuangalia Aya za Quran na Hadith za Mtume ataziona zimetilia umuhimu kufuatilia akili kwa kiasi kile kile zinavyoitilia umuhimu kumwamini Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Imani hiyo haiepukani kabisa na nuru ya akili timamu katika kuongoka kwake.