TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 19028
Pakua: 2866


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 19028 / Pakua: 2866
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿ وَالْوَالِدَاتُ يُرْضِعْنَ أَوْلَادَهُنَّ حَوْلَيْنِ كَامِلَيْنِ لِمَنْ أَرَادَ أَن يُتِمَّ الرَّضَاعَةَ وَعَلَى الْمَوْلُودِ لَهُ رِزْقُهُنَّ وَكِسْوَتُهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ لَا تُكَلَّفُ نَفْسٌ إِلَّا وُسْعَهَا لَا تُضَارَّ وَالِدَةٌ بِوَلَدِهَا وَلَا مَوْلُودٌ لَّهُ بِوَلَدِهِ وَعَلَى الْوَارِثِ مِثْلُ ذَٰلِكَ فَإِنْ أَرَادَا فِصَالًا عَن تَرَاضٍ مِّنْهُمَا وَتَشَاوُرٍ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا وَإِنْ أَرَدتُّمْ أَن تَسْتَرْضِعُوا أَوْلَادَكُمْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِذَا سَلَّمْتُم مَّا آتَيْتُم بِالْمَعْرُوفِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴾

233.Na wazazi wa kike wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha; na ni juu ya aliyezaliwa mtoto huyo (baba) chakula chao na nguo zao kulingana na desturi. Wala haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa uweza wake. Mzazi (Mama) asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala aliyezaliwa mtoto (baba) kwa ajili ya mwanawe. Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha (kunyonya) kwa kuridhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao. Na kama mkitaka kuwapatia watoto wenu Mama (wengine) wa kuwanyoyesha, basi haitakuwa vibaya juu yenu kama mkitoa mlichowaahidi, kwa desturi. Na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

MAMAWANYONYESHE

Aya 233

MAANA

Na wazazi wa kike wawanyonyeshe watoto wao.

Wafasiri wamehitilafiana katika makusudio ya tamko la wazazi wa kike. Je, ni waliopewa talaka tu, au ni walio kwa waume zao tu, au wote pamoja? Wengi wanasema kwamba tamko hilo linawakusanya wote kwa kuangalia kidhahiri; wala hakuna dalili ya kuhusisha upande mmoja tu. Na sisi tunaelekea upande huu. Kwa sababu kunyonyesha kunamtegemea mama kwa hali yoyote awayo, sio kwa kuwa na mume wala kwa kuwa ni mtalikiwa. Wawanyonyeshe watoto wao: ni amri ya mapendekezo tu, sio lazima; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ وَإِن تَعَاسَرْتُمْ فَسَتُرْضِعُ لَهُ أُخْرَىٰ﴾

"... Na kama mkiona uzito kati yenu, basi amnyonyeshee (mwanamke) mwingine." (65:6)

Maana yake ni kuwa akina mama wanayo haki ya kuwanyonyesha watoto wao kuliko watu wengine. Unaweza kuuliza kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na ni juu ya baba chakula chao na nguo zao" inatilia nguvu kuwa makusudio ya Wazazi watakao nyonyesha ni wanawake walioolewa au walio katika talaka rejea tu; na wala sio walioachwa ambao imekwisha eda yao. Kwa sababu mtalikiwa, chake ni malipo ya kunyonyesha tu sio chakula; kwa hiyo Aya haiwahusishi waliopewa talaka.

Jibu : Hapana kizuizi kwa tamko moja kuenea kihukumu kwa upande mmoja na kuhusika upande mwingine pamoja na kupatikana dalili. Iko hadithi na wamekongamana wanavyuoni kuwa mwenye kupewa talaka hana posho isipokuwa malipo ya kunyonyesha; kwa hiyo hakuna dalili iliyohusisha upande fulani, basi tunafuata kuenea kwa wote.(aliye katika ndoa na mtalikiwa)

MIAKA MIWILI KAMILI

Hapa kuna maswali mawili: Kwanza: Je, inafaa mama kunyonyesha mtoto zaidi ya miaka miwili? Jibu: Ndio, hasa ikiwa mtoto anahitajia ziada. Kuwekwa kiwango cha miaka miwili kuna faida tatu:

1. Mama asidai malipo zaidi ya miaka miwili.

2. Ukitokea mzozano kati ya baba na mama kuhusu muda wa kunyonyesha mtoto, basi hukumu itakuwa ya Mwenyezi Mungu: 'Miaka miwili kamili.'

3. Kunyonyeshwa mtoto baada ya miaka miwili na mtu kando hakuwezi kusababisha uharamu kati ya mnyonyeshaji na mtoto: Hivyo ndivyo walivyosema Shia na Shafii. Ama Abu Hanifa yeye amesema hiyo ni mpaka baada ya miezi thelathini. Swali la pili: Je, inafaa kupunguza muda wa miaka miwili? Jibu: Inafaa kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha. Na pia kauli yake: Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa kwa kur-idhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao Je, tutarudia sharia katika kiwango cha chini cha muda wa kunyonyesha, au tutaangalia hali ya afya ya mtoto? Mafaqihi wengi wamesema uchache wa muda wa kunyonyesha ni miezi

21 kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ وَحَمْلُهُ وَفِصَالُهُ ثَلَاثُونَ شَهْرًا﴾

"... Na kubeba mimba kwake na kumwachisha ziwa ni miezi thelathini..." (46:15)

Tukitoa miezi tisa ambayo aghlabu inakuwa ya mimba, inabakia miezi ishirini na moja. Kwa vyovyote ilivyo, umuhimu ni kuchunga afya ya mtoto na maslahi yake ambayo yanatofautiana kwa kutofautiana miili. Na utafiti huu ulikuwa na umuhimu hapo zamani ambapo hakukuwa na lishe ya kutosha. Ama hivi leo ambapo lishe zimejaa tele, suala hili halina maudhui tena.

Na ni juu ya aliyezaliwa mtoto huyo (baba) chakula chao na nguo zao kulingana na desturi.

Kwa dhahiri ulazima wa kulea uliotajwa hapa ni kwa mke na aliye katika eda ya talaka rejea. Kimetajwa chakula na mavazi kwa sababu ya umuhimu wake.

Makusudio ya desturi ni kuangalia hali ya matumizi ya mke katika jamii yake. Ama kuangalia hali ya mume kimali, Mwenyezi Mungu anasema:

Haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa uweza wake.

Tafsir wazi ya jumla hii tunaweza kuipata katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ لِيُنفِقْ ذُو سَعَةٍ مِّن سَعَتِهِ وَمَن قُدِرَ عَلَيْهِ رِزْقُهُ فَلْيُنفِقْ مِمَّا آتَاهُ اللَّـهُ لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا مَا آتَاهَا سَيَجْعَلُ اللَّـهُ بَعْدَ عُسْرٍ يُسْرًا ﴾

"Mwenye uwezo atoe kadiri ya uwezo wake; na yule ambaye amepungukiwa riziki yake, atoe katika kile alichopewa na Mwenyezi Mungu; Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu yoyote ila kwa kadiri ya alichompa..." ( 65:7)

Imam Jaffar Sadiq(a.s) alikuwa na marafiki wengi, mara nyingine walikuwa wakichelewa kuondoka nyumbani kwake mpaka unafika wakati wa chakula, basi huwaletea chakula; mara huwaletea mkate na siki na mara nyingine huwaletea chakula kizuri kabisa. Mmoja akamuuliza sababu ya kufanya hivyo. Imam akamjibu:"Tukiwa na nafasi tunawapa cha nafasi na tukiwa na dhiki tunawapa cha dhiki."

Mzazi (Mama) asitiwe taabuni kwa ajili ya mwanawe, wala mwenye kuzaliwa mtoto (baba) kwa ajili ya mwanawe.

Inapasa kuangalia vizuri Aya hii, kwa sababu makadhi hivi sasa wanatoa ushahidi sana kwa Aya hii katika hukumu zao na kuifasiri kuwa baba asimdhuru mama kwa sababu ya mtoto. Ama watu wa tafsiri wanakurubia kuafikiana kwa pamoja kwamba maana yake ni kinyume na hivyo; kwamba mama asikatae kumnyonyesha mtoto wake na kumdhuru kwa kutaka kumkasirisha baba yake kwa hilo. Mwenye Majmaul Bayan anasema: "Mama asiache kumnyonyesha mtoto wake kwa ajili ya kumuudhi baba yake." Sasa haya yako wapi na ushahidi wa makadhi kwamba baba asimdhuru mama kwa sababu ya mtoto? Na sisi tunasema, baada ya kuitia akilini Aya bila ya kutegemea zaidi maneno ya mafaqihi na wafasiri, kwamba mara nyingi kunapotokea kutengana kati ya mtu na mkewe, humfanya mtoto ndio chombo cha kukasirishana, na matokeo yake mtoto hudhurika kwa kumfanya mtoto ndio kafara la ugomvi wao.

Mfano mama anaweza kukataa kumnyonyesha mtoto, hata kama iko haja, ili amuudhi baba. Au baba anaweza kumnyang'anya mama mtoto na kumpatia mtu mwingine amnyonyeshe, hata kama mamake anataka kumnyonyesha. Mwenyezi Mungu amekataza kudhuriana kwa namna yoyote ile, iwe kwa mtoto, baba au mama kwa sababu ya mtoto. Haya ndiyo yanayokuja haraka kwenye fahamu katika kauli yake Mwenyezi Mungu. Wala hayapingani na kauli ya wafasiri, isipokuwa yanayopingana ni kutolea ushahidi makadhi; ingawaje kauli yao yenyewe ni sahihi, lakini makosa yako katika kutolea ushahidi.

Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo.

Wamehitalifiana kuhusu makusudio ya mrithi, je ni mrithi wa baba au mrithi wa mtoto? Mfumo wa maneno unatilia nguvu kwamba ni mrithi wa mwenye mtoto (baba), lakini maana hayasimami sawa. Kwa sababu mtoto na mama ni katika jumla ya warithi wa baba na kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu mfano wa hivyo inaonyesha ni wajibu kwa mrithi wa baba kutoa posho ile iliyo wajibu kwa baba.

Kwa hivyo inamaanisha posho ya mama ni wajibu kwa mama, kwa mtoto wake na kwa warithi wengine wakiwepo. Inavyo-julikana ni kuwa posho ya mama si wajibu kwa yeyote ikiwa huyo mama anauwezo; ni sawa uwezo huo uwe umetokana na kumrithi mume, au la. Kwa hivyo basi hakuna maana kusema kuwa ni wajibu kujilisha kutokana na mali yake. Kama tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa mtoto, basi itakuwa tunahitalifiana na dhahiri kwa upande mmoja; pia tutakuwa tunahitilifiana na hali ilivyo kwa upande mwingine. Kwa sababu posho ya mama si wajibu kwa anaye mrithi mtoto. Ni kweli kuwa Mama anaweza kuchukua ujira wa kunyonyesha kutoka katika mali ya mtoto wake (anaye mnyonyesha), ikiwa anayo mali, lakini ujira wa kunyonyesha ni kitu kingine na posho ni kitu kingine kwa maana yake sahihi.

Ilivyo hasa ni kwamba Aya hii ni miongoni mwa Aya za mifano zenye kutatiza ndio maana Malik akasema kuwa ni Mansukh (iliyoachwa hukumu yake) kama alivyonakili Abu bakr Al-maliki katika kitabu cha Ahakamul Qur'an. Baadhi ya wafasiri wameiruka na wengine wameinakilia kauli zisizo kuwa na nguvu. Kutatiza kwake kama tulivyobainisha ni ikiwa itabaki dhahiri ilivyo, maana hayatasimama sawa; yaani tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa baba na kufasiri mfano wa hivyo kwa maana ya posho ya mama. Na kama tukifasiri mrithi kwa maana ya mrithi wa mtoto na mfano wa hivyo kwa maana ya malipo ya kunyonyesha, maana yatakuwa sawa lakini tutakuwa tunahitalifiana na dhahiri ya matamko mawili (mrithi na mfano wa hivyo). lakini hakuna njia nyingine zaidi ya kuhitalifiana na dhahiri ya tamko na kulifasiri kimaana (taawili). Sio mbali kuwa Hadith zenye kupokewa katika kunyonyesha na malipo yake, ni mfano wa dalili ya kuswihi taawili hii.

Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha (kunyonya) kwa kuridhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao.

Yaani baba na mama kwa kushauriana wanaweza kumwachisha mtoto kabla ya miaka miwili au baada yake kwa maslahi ya mtoto; bali inajuzu kwa baba kumpa mnyonyeshaji mwingine; Mwenyezi Mungu amelionyesha hilo kwa kusema:

Na kama mkitaka kuwapatia watoto wenu Mama (wengine) wa kuwanyonyesha, basi haitakuwa vibaya juu yenu kama mkitoa mlichowaahidi kwa desturi.

Msemo 'mkitoa mlichowaahidi,' unaele-kezwa kwa akina baba. Maana yake ni enyi akina baba! Hakika mama ana haki zaidi ya kumyonyesha mwanawe kuliko mtu wa kando; naye mama anastahiki malipo ya kawaida. Ikiwa mumempa haki hii na mkamdhamiria kumpa malipo ya kunyonyesha ya kawaida, lakini akataka zaidi, basi si vibaya hapo kuwapatia watoto wenu wanyonyeshaji wengine. Imesemwa kuwa maana yake ni mkiwapatia wanyonyeshaji wa nje malipo ya kawaida si vibaya kwenu. Vyovyote iwavyo, ni juu ya baba kumpatia haki (malipo) yake kila mmoja, awe mama au mama wa kunyonyesha tu.

﴿ وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا فَإِذَا بَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا فَعَلْنَ فِي أَنفُسِهِنَّ بِالْمَعْرُوفِ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴾

234.Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake (hao wake) wangoje miezi minne na siku kumi. Na wanapofikilia muda wao, basi si vibaya kwenu kwa yale wanayojifanyia, yanayoafiki ada. Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

﴿ وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا عَرَّضْتُم بِهِ مِنْ خِطْبَةِ النِّسَاءِ أَوْ أَكْنَنتُمْ فِي أَنفُسِكُمْ عَلِمَ اللَّـهُ أَنَّكُمْ سَتَذْكُرُونَهُنَّ وَلَـٰكِن لَّا تُوَاعِدُوهُنَّ سِرًّا إِلَّا أَن تَقُولُوا قَوْلًا مَّعْرُوفًا وَلَا تَعْزِمُوا عُقْدَةَ النِّكَاحِ حَتَّىٰ يَبْلُغَ الْكِتَابُ أَجَلَهُ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي أَنفُسِكُمْ فَاحْذَرُوهُ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ حَلِيمٌ ﴾

235.Wala si vibaya kwenu kuonyesha ishara ya kuwaposa wanawake, au kutia azma katika nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msifanye nao ahadi kwa siri; isipokuwa mseme maneno yaliyoruhusiwa na sharia. Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda uliofaradhiwa ufike. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo katika nafsi zenu, basi tahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghufira, mpole.

EDA YA KUFIWA

Aya 234 - 235

MAANA

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake; wangoje miezi minne na siku kumi.

Mafaqihi wote wameafikiana kwamba eda ya mwenye kufiwa na mume ni miezi minne na siku kumi. Awe mkubwa au mdogo; mwenye kutoka hedhi au aliyekoma, mwenye kuingiliwa au la. wamelitolea dalili hilo kwa Aya hii. Ama akiwa na mimba, madhehebu manne ya kisunni yamesema: Eda yake itakwisha kwa kuzaa; hata kama ni muda mchache tu, baada ya kufa mumewe, kiasi ambacho anaweza kuolewa hata kabla ya kuzikwa mumewe, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ﴾

"... Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa..." (65:4)

Mafaqihi wa Kishia wamesema: Eda yake ni ule muda utakaorefuka zaidi; yaani ikipita miezi minne na siku kumi kabla ya kuzaa atangojea mpaka azae; au akizaa kabla ya kupita miezi minne na siku kumi, atakaa eda ya miezi minne na siku kumi. Wametoa dalili juu ya hilo kwa ulazima wa kukusanya Aya mbili; "Wangoje miezi minne na siku kumi" na"Eda yao ni mpaka watakapozaa."

Aya ya kwanza imejaalia eda kuwa ni miezi minne na siku kumi, nayo inakusanya mwenye mimba na asiye na mimba; na Aya ya pili imeifanya eda ya mwenye mimba ni kuzaa, nayo inakusanya mwenye kuachwa na mwenye kufiwa na mumewe. Kwa hivyo kutakuwa na mgongano kati ya dhahiri ya Aya mbili kwa mwanamke mwenye mimba ambaye atazaa kabla ya miezi minne na siku kumi: Kwa mujibu wa Aya ya pili itakuwa eda imekwisha na kwa mujibu wa Aya ya kwanza itakuwa bado haijaisha kwa sababu miezi minne na siku kumi haikutimia. Vile vile utapatikana mgongano ikipita miezi minne na siku kumi, akiwa bado hajazaa; kwa mujibu wa Aya ya kwanza eda itakuwa imekwisha kwa sababu muda wa miezi minne na siku kumi umekwisha; na kwa mujibu wa Aya ya pili itakuwa eda bado haijaisha kwa sababu hajazaa. Na maneno ya Qur'an ni mamoja ni lazima yaafikiane.

Kwa hivyo tukiziunganisha Aya mbili na kuzikusanya katika jumla moja, zikawa hivi;"Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake; wangoje miezi minne na siku kumi. Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa." Tukizikusanya hivi, maana yake yatakuwa ni: Eda ya mwenye kufiwa na mumewe ni miezi minne na siku kumi, kwa asiyekuwa na mimba; na mwenye mimba ambaye atazaa kabla ya kupita miezi minne na siku kumi. Na itakuwa eda ya mwenye kufiwa, mwenye mimba ambaye atazaa baada ya kupita miezi minne na siku kumi, ni kuzaa. Kama akiuliza mwulizaji: Vipi Shia wamefanya eda ya mwenye mimba, aliyefiwa na mume, ni muda utakaorefuka pamoja na kwamba Aya "Na wanawake wenye mimba eda yao ni mpaka watakapozaa", iko wazi kwamba eda inaisha kwa kuzaa?

Shia naye anaweza kujibu kwa kusema: "Vipi madhehebu manne ya Sunni yakasema kuwa eda ya mjane mwenye mimba inaweza kuwa hata miaka miwili kama ikiendelea mimba pamoja na kuwa Aya"Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuwaacha wake, (nao wake) wakae wangoje miezi minne na siku kumi" iko wazi kwamba eda ni miezi minne na siku kumi?" Kwa hiyo hakuna jengine lolote la kuchukulia Aya mbili isipokuwa kuchukulia kauli ya muda utakaorefuka zaidi.

Na wanapofikia muda wao, basi si vibaya kwenu kwa yale wanayojifanyia, yanayoafiki ada Mwenyezi Mungu anazo habari mnayoyatenda.

Yaani kama ukisha muda wa eda ya mjane, basi hapana dhambi kwenu enyi Waislamu kwa mwanamke kufanya yale aliyozuiliwa wakati wa eda; kama kujipamba na kuonekana, na wanaotaka kuwaoa kwa njia ile iliyo maarufu kisheria. Hapa Mwenyezi Mungu anawaambia Waislamu wanaume, kwa sababu ni juu yao kuwazuia wanawake wanapopetuka mipaka ya kisheria. Wameafikiana mafaqihi kwa kauli moja kuwa mjane aliyefiwa na mume wakati wa eda ni wajibu kwake kujiepusha na kila linalomfanya kuonekana mrembo wa kutamanika.

Wala si vibaya kwenu kuonyesha ishara ya kuwaposa wanawake.

Mwenyezi Mungu ameharamisha ndoa katikati ya eda ya namna yoyote, bali ni haramu pia kwa mwanamume kumposa mwanamke akiwa katika eda yake, iwe ni eda ya kufiwa na mume au ya talaka bain, lakini Mwenyezi Mungu anahalalisha kufanya ishara ya posa bila ya kudhihirisha, katika isiyokuwa eda ya talaka rejea. Kwani mtalaka katika eda hiyo bado yuko mikononi mwa mumewe.

Au kutia azma katika nyoyo zenu.

Kila linalopita akilini na kuazimiwa na moyo halina ubaya kwa Mungu, kwa sababu liko nje ya uwezo wa mtu; lililo kwenye uwezo wa mtu ni zile athari. Kwa hivyo mtu akiazimia kuoa mke aliye edani, sio dhambi. Lakini akiidhihirisha azma yake hii akamposa, basi atakuwa ni mwenye dhambi. Kwa sababu kuazimia kuko nje ya uwezo na kudhihirisha kuko ndani ya uwezo wa mtu. Iko Hadith inayosema:"Ukiwa na donge moyoni usilitekeleze." Hapo amekataza kufanya, ambako ni athari ya hilo donge, lakini hakukataza kuwa na donge kwa sababu hakuzuiliki.

Mwenyezi Mungu anajua kwamba nyinyi mtawakumbuka.

Kwa hivyo ndio akawahalalishia kuonyesha ishara, lau angeliwazuia basi mngeliona mashaka. Lakini msifanye nao ahadi kwa siri. Hiyo ishara ya kuoa pia haifai kuionyesha kwa siri wakati wa eda katika faragha. Kwa sababu faragha kati ya mwanamume na mwanamke inaleta mambo asiyoyaridhia Mwenyezi Mungu. Iko Hadith inayosema: "Hakai faragha mwanamume na mwanamke isipokuwa shetani huwa watatu wao." Hasa ikiwa mume anamtamani aliyekaa naye faragha, isipokuwa ikiwa mume ana yakini kwamba faragha haitaleta haramu katika maneno wala vitendo, hapo ndipo itajuzu kusema naye yale ambayo si mabaya, hata kusema kwa dhahiri. Ndio Mwenyezi Mungu akalegeza kidogo kwa kusema; "Isipokuwa mseme maneno yaliyoruhusiwa na sharia."

Wala msiazimie kufunga ndoa mpaka muda uliofaradhiwa ufike.

Yaani msifunge ndoa ndani ya eda mpaka ishe.

NDOA KATIKA EDA

Baada ya kuafikiana Waislamu wote kwamba kufunga ndoa na kuposa wazi wazi katikati ya eda, ni katika mambo ya haramu, na kwamba ndoa itakuwa batili baada ya kuafikiana hivi, wakahitalifiana juu ya uharamu wa waliofunga ndoa ndani ya eda. Je mwanamke atakuwa haramu milele au inawezekana kufunga ndoa tena baada ya kwisha eda? Hanafi na Shafi wamesema hakuna kizuizi cha kumwoa mara ya pili. Hayo yamo katika kitabu Bidayatul Mujtahid. Shia wamesema: Akifunga naye ndoa na hali anajua kuwa yuko katika eda, basi atakuwa haramu kwake daima, iwe amemwingilia au hakumwingila. Na akifunga naye ndoa bila ya kujua kuwa yuko kwenye eda, basi hatakuwa haramu, isipokuwa kama amemwingilia, na anaweza kumwoa tena baada ya eda kama hakumwingilia. Hii ndio hukumu ya kufunga ndoa katikati ya eda. Ama kuposa hakuna athari yoyote isipokuwa dhambi tu.

Maajabu niliyoyasoma katika suala hili ni yale yaliyo katika kitabu Ahkamul Qur'an cha Abu Bakr Al Andalusi wa madhehebu ya Malik, pale aliposema: Akimposa katikati ya eda, kisha akafunga naye ndoa baada ya eda, basi ni lazima amwache talaka moja, kisha aanze upya kumchumbia na kufunga ndoa.

﴿ لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ﴾

236.Si vibaya kwenu kama mkiwapa wake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari. Na wapeni cha kuwali-waza, mwenye wasaa kadiri awezavyo na mwenye dhiki kadiri awezavyo. Kiasi cha kuwaliwaza, cha kawaida. Ndio haki kwa wafanyao mema.

﴿ وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ وَلَا تَنسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴾

237.Na kama mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa na mmekwisha wakadiria mahari, basi ni nusu ya hayo mahari mliyokadiria. Isipokuwa (wanawake wenyewe) wasamehe au asamehe ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake, na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua. Wala msisahau fadhila baina yenu; hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyafanya.

TALAKA KABLA YA KUINGILIA

Aya 236 -237

MAANA

Si vibaya kwenu kama mkiwapa wake talaka ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari Yaani hamlazimiwi na mahari.

Kwa ujumla maana yake ni kwamba mwenye kufunga ndoa na mwanamke wala asimtajie mahari katika ndoa, kisha akamwacha kabla ya kumwingila, basi hana ulazima wa kutoa mahari; isipokuwa mwanamke anastahiki kupewa kiasi cha kumliwaza tu. Kiasi hicho ataangalia mume uwezo wake; kwa mfano tajiri anaweza kutoa mkufu wa thamani ya shs. 1000, mtu wa kawaida akitoa bangili ya Shs. 500 na masikini akatoa nguo ya Shs. 20. Katika haya Mwenyezi Mungu anasema: Na wapeni cha kuwaliwaza mwenye wasaa kadiri awezavyo, na mwenye dhiki kadiri awezavyo. Kiasi cha kuwaliwaza, cha kawaida. Ndio Haki kwa wafanyao mema.

Wale ambao wanazifanyia wema nafsi zao kwa kumtii Mwenyezi Mungu (s.w.t). Na kama mkiwapa talaka kabla ya kuwagusa na mmekwisha wakadiria mahari, basi ni nusu ya hayo mahari mliyokadiria.

Ikiwa amefunga ndoa akataja mahari kisha akamwacha kabla ya kumwingilia, basi anastahiki nusu ya mahari.

Isipokuwa (wanawake wenyewe) wasamehe.

Yaani haifai kumzuilia mwanamke nusu ya mahari au kitu chochote, isipokuwa kama akisamehe mwenyewe kwa radhi yake. Au asamehe ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake.

Mume ndiye ambaye kifungo cha ndoa kiko mikononi mwake. Makusudio ni kwamba mwenye kupewa talaka kabla ya kuingiliwa hastahiki zaidi ya nusu ya mahari yaliyotajwa isipokuwa kama mume atampa yote au kumpa zaidi ya nusu.

Na kusamehe ndiko kuliko karibu zaidi na takua.

Msemo unaelekezwa kwa wote, mume na mke, kuwahimiza kusameheana.

﴿ حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ ﴾

238.Angalieni sana swala, na ile swala ya katikati. Na simameni kwa unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

﴿ فَإِنْ خِفْتُمْ فَرِجَالًا أَوْ رُكْبَانًا فَإِذَا أَمِنتُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَمَا عَلَّمَكُم مَّا لَمْ تَكُونُوا تَعْلَمُونَ﴾

239.Na kama mkiwa na hofu, basi ni hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale mliyokuwa hamyajui.

SWALA YA KATIKATI

Aya 238 - 239

Angalieni sana Swala na ile Swala ya katikati.

Kuziangalia sana ni kuzitekeleza kwa nyakati zake na njia zake. Mwenyezi Mungu ameihusisha hii kwa kuipa uzito na umuhimu; kama umuhimu wa Jibril na Mikail katika Malaika alipowahusu wao, baada ya kuwakusanya na Malaika wen-gine katika kauli yake:

﴿ مَن كَانَ عَدُوًّا لِّلَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ﴾

Ambaye ni adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na Mikail..." (2:98)

Wamehitalifiana kuhusu swala ya katikati, mpaka kufikia kauli kumi na nane; kama ilivyonakiliwa katika kitabu Naylul Awtwar. Kauli iliyo mashuhuri zaidi ni ile inayosema kuwa ni swala ya Alasiri, na kuna riwaya katika hilo.

Imesemwa kwamba imeitwa swala ya katikati kwa sababu iko baina ya swala mbili za (Maghribi na Isha) na swala mbili (Asubuhi na Adhuhuri). Ama sababu ya kutajwa kwake ni kwamba inakuwa wakati ambao aghlab watu wanashughulika. Mwenye tafsir ya Al Manar amenakili kutoka kwa Ustadh wake, Sheikh Muhammad Abduh, kwamba yeye amesema: Lau si kuwako kongamano juu ya tafsiri ya Wusta kuwa ni moja ya swala tano na wala sio tano zote, basi yeye angeliifasiri kwa swala bora; na Mwenyezi Mungu amehimiza na kutilia mkazo swala bora nayo ni ile ambayo moyo unakuwapo ndani ya hiyo swala, nafsi kuwa na mwelekeo wa kuwa na ikhlas kwa Mwenyezi Mungu na kuzingatia maneno Yake. Sio swala ya kujionyesha au ya mwili tu, lakini moyo haupo.

Haya ndiyo maelezo mazuri zaidi niliyosoma katika tafsiri ya Aya hii, nayo yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿ قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ﴾

Wamefuzu waumini ambao katika swala zao huwa ni wanyenyekevu."( 23:1-2)

Na simameni kwa unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Yaani mumuombe Mwenyezi Mungu katika swala zenu kwa unyenyekevu wa kuhisi ukubwa na utukufu wake, hali ya kuachana na mambo yanayoushughulisha moyo.

Na kama mkiwa na hofu basi ni hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Swala haisamehewi kwa hali yoyote ile.

Mtu akiwa anashindwa kufanya baadhi ya vitendo vyake, basi atatekeleza vile atakavyoweza. Akishindwa kufanya vitendo vyote, basi ataswali kwa kutamka na kuashiria. Ikiwa hivyo pia atashindwa, basi ataleta picha ya swala moyoni. Hapa anaashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwamba mtu anaweza kufikiwa na wakati wa Swala naye yuko vitani akiwa amekabiliana na adui, n.k. basi ataswali kadiri atakavyoweza, kwa kwenda au akiwa amepanda kitu; kwa kuelekea Qibla au bila ya kuelekea.

Mwenye Majmaul Bayan anasema: Swala ya kuhofia adui ni rakaa mbili iwe ni safirini au nyumbani, isipokuwa Maghrib tu, hiyo ni rakaa tatu. Imepokewa Hadith kwamba Imam Ali(a.s) katika usiku wa vita vya Harir aliswali kwa kuashiria na ikasemwa ni kwa takbir, na kwamba Mtume(s.a.w.w) siku ya vita vya Ahzab aliswali kwa kuashiria.

Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale mliyokuwa hamyajui.

Yaani hofu ikiondoka basi swalini swala ya kawaida ile mliyofundishwa mwanzo.

KUACHA SWALA KUNAPELEKEA UKAFIRI

Tumezungumzia swala katika kufasiri Aya iliyotangulia, na sasa tunaunganisha kifungu hicho na haya yafuatayo:

Majaribio yamethibitisha kwamba; kuacha swala mara nyingi kunapeleka ukafiri na athari zake. Hiyo ni kwamba kafiri hajali kufanya haramu, basi hivyo hivyo mwenye kuacha swala anafanya mambo ya haramu bila ya kujali. Popote penye ukafiri pana uovu na uchafu. Hali hiyo inaletwa na kuacha swala. Dalili kubwa zaidi inayoonyesha hakika hii ni ufisadi katika zama zetu hizi. Haya mabaa, madanguro na ma casino katika miji yetu. Na pia huku kutembea nusu uchi kwa mabinti zenu na tabia mbaya za watoto wetu (kuiga wazungu), yote hayo ni natija ya kuacha swala; kwa dalili ya kuwa haya yote hayakuwako wakati wa swala ilipokuwa imezoeleka kwa watoto wetu wa kiume na wa kike. Hiyo ndiyo tafsir ya Hadith tukufu inayosema:"Tofauti kati yetu sisi na nyinyi (makafiri) ni swala; mwenye kuiacha amekufuru."

Haitamtosha mtu kusema: Mimi ni Mwislamu au kutamka shahada mbili (kushahadia) tu, maadamu amali zake ni za kikafiri na kilahidi. Hakika mlahidi haoni haya wala kigegezi chochote kuacha swala, na hafichi hilo, bali hutangaza hasa, kwa sababu hafuati dini. Basi hivyo hivyo vijana wetu wa kileo wanaona fahari kujulikana kuwa hawaswali, bali wanamdharau mwenye kuswali na swala yenyewe. Kwa hivyo hakuna tofauti kati yao na walahidi.

Si vibaya kama tukinukuu mawaidha mazuri kutoka katika kitabu Al-Islam Khawatir wa Sawanih cha Mfaransa, Comte Henry Descarte kilichofasiriwa kwa Kiarabu anasema: "Nilisafiri katika jangwa la jimbo la Hawaran nikiwa na wapanda farasi thelathini, wote wakinihudumia mimi. Wakati tukiendelea na msafara, mara sauti ikanadi kwamba wakati wa swala ya Alasiri umefika. Wapanda farasi wote wakashuka haraka; mara wakajipanga safu za swala ya jamaa, nikawa ninawasikia wakilikariri neno Allahu Akbar kwa sauti ya juu. Likawa jina hilo la Mungu linaniingia akilini zaidi kuliko nilivyoingiwa akilini na somo la elimu ya Mungu. Nikahisi kukosa raha kuliko sababishwa na haya na kuhisi kwamba hao wapanda farasi ambao walikuwa wakinitukuza muda mchache uliopita, hivi sasa wakiwa katika swala yao, wanahisi kwamba wako katika makao ya juu zaidi na wenye nafsi tukufu zaidi kuliko mimi. Lau ningeitii nafsi yangu ningeliwapigia kelele kwa kusema: Mimi pia ninamkubali Mungu na ninajua Swala.

Ni uzuri ulioje wa mandhari ya watu hao katika swala yao na huku farasi wao wako pembeni mwao wakiwa wametulia kimya kamba zao zikiwa chini, kama kwamba wao nao wanainyenyekea swala; farasi aliyekuwa akipendwa na Mtume kwa mapenzi ambayo yalimpelekea Mtume kuifuta pua yake kwa shuka yake.

Nilisimama pembeni nikiwaangalia wan-aoswali na kujikuta mimi niko pweke kabisa nikionyesha alama ya kukosa imani, kana kwamba mimi ni mbwa tu, aliye mbele ya wale wanaomkariria Swala Mola wao kwa unyenyekevu unaotoka katika nyoyo zilizojaa ukweli na imani.