TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 18777
Pakua: 2709


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 18777 / Pakua: 2709
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

13

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا وَصِيَّةً لِّأَزْوَاجِهِم مَّتَاعًا إِلَى الْحَوْلِ غَيْرَ إِخْرَاجٍ فَإِنْ خَرَجْنَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِي مَا فَعَلْنَ فِي أَنفُسِهِنَّ مِن مَّعْرُوفٍ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾

240.Na wale wanaokufa miongoni mwenu na wakaacha wake, wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi ya mwaka mmoja bila ya kutolewa. Wakiondoka, basi si vibaya kwenu kwa yale waliyojifanyia wenyewe, yanayofuata desturi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

﴿وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ ﴾

241.Na wanawake waliopewa talaka wapewe cha kuwaliwaza kulingana na desturi; hiyo ni haki kwa wenye takua.

﴿كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴾

242.Namna hiyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya Zake ili mpate kufahamu.

NAWALE WANAOKUFA

Aya 240 - 242

MAANA

Ilikuwa ni ada ya Waarabu kabla ya Uislamu kwamba mtu akifa, mkewe hapati urithi wowote isipokuwa posho yake ya mwaka mmoja tu; kwa sharti akae eda katika nyumba ya mumewe. Akitoka kabla ya mwaka, basi hana posho. Aya hii ni uthibitisho wa hayo, na yalikuwapo katika mwanzo wa Uislamu. Wafasiri na mafaqihi wote wameafikiana kwa kauli moja kwamba Aya hii ni Mansukh, hukumu yake (haitumiki tena) na imenasikhwa na Aya mbili:

﴿وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجًا يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا﴾

1."Na wale wanaokufa miongoni mwenu na kuacha wake, wangoje miezi minne na siku kumi..."( 2:234)

﴿وَلَهُنَّ الرُّبُعُ مِمَّا تَرَكْتُمْ إِن لَّمْ يَكُن لَّكُمْ وَلَدٌ فَإِن كَانَ لَكُمْ وَلَدٌ فَلَهُنَّ الثُّمُنُ مِمَّا تَرَكْتُم﴾

2."...Nao (wake zenu) watapata robo ya mlivyoacha, ikiwa hamna mtoto, lakini ikiwa mnaye mtoto basi wao (wanawake) watapata thumuni..." (4:12)

Kwa maana kuwa atajilisha mwenyewe kutokana na fungu lake. Pamoja na kwamba Aya hii haitumiki kabisa hukumu yake katika sharia, lakini tutaifasiri kama walivyofanya wafasiri.

Na wale wanaokufa miongoni mwenu na wakaacha wake, wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi ya mwaka mmoja.

Ilikuwa kabla ya kutotumika Aya hii ni wajibu kwa wale ambao wanadhihirikiwa na alama za mauti kuusia kwa ajili ya wake zao wazuiliwe majumbani kwa kupewa posho.

Bila ya kutolewa.

Yaani posho itakuwa wajibu kama wakitaka kukaa katika nyumba ya bwana aliyefariki. Ama wakitoka, basi si wajibu. Kwa hivyo ndio akaashiria Mwenyezi Mungu kwa kusema:

Wakiondoka basi si vibaya kwenu.

Yaani hamna jukumu kuwapa posho. Kwa maneno mengine posho ni wajibu kwa kubaki nyumbani, wakitoka hakuna posho.

Kwa yale waliyojifanyia wenyewe, yanayofuata desturi.

Mwanamke akitoka nyumbani kwa mumewe aliyefariki, anaweza kujipamba na kuposwa katika mipaka ya sharia; yaani mwanamke aliyefiwa na mumewe ana hiyari kubaki nyumbani kwa mume kwa muda wa mwaka mmoja na kupewa posho au kutoka asipewe posho.

Na wanawake waliopewa talaka wapewe cha kuwaliwaza kulingana na desturi; hiyo ni haki kwa wenye takua.

Kutoa ni lazima kuangalia hali ya mtoaji; kama ilivyokwishaelezwa katika Aya ya 236. Tamko la wenye kupewa talaka linawakusanya watalikiwa wote ambao wanagawanyika sehemu nne.

1. Mwenye kupewa talaka akiwa amekwishaingiliwa na amekwisha bainishiwa mahari, huyu atapata mahari yote, kama ilivyobainishwa katika Aya ya 229.

2. Mwenye kupewa talaka bila ya kuingiliwa na amekwisha bainishwa mahari; yeye atapata nusu ya mahari; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 237.

3. Mwenye kupewa talaka akiwa ameingiliwa, lakini hakubainishiwa mahari; yeye atapata mahari kiasi cha makisio ya desturi yao. Hilo wameafikiana Waislamu wote.

4. Mwenye kupewa talaka, bila ya kuingiliwa na bila ya kubainishiwa mahari. Huyu hana mahari, isipokuwa atapewa cha kumliwaza tu; kama ilivyoelezwa katika Aya ya 236.

Kwa ufupi ni kwamba cha kuliwaza hupewa yule mwenye kupewa talaka bila ya kuingiliwa na bila ya kubainishiwa mahari wakati wa ndoa. Ama wengine hakuna ulazima wa kuwapa bali ataachiwa mwenyewe aliyetoa talaka akitaka atampatia cha kuliwaza, asipotaka ni basi. imesemwa kuwa ni sunna kumpatia.

Namna hiyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kufahamu.

Yaani mpate kujua. Kwa sababu ambaye haonyeki na kuacha kutumia hukumu za Mwenyezi Mungu, basi yuko katika daraja ya wasiokuwa na akili.

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَهُمْ أُلُوفٌ حَذَرَ الْمَوْتِ فَقَالَ لَهُمُ اللَّـهُ مُوتُوا ثُمَّ أَحْيَاهُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَذُو فَضْلٍ عَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ ﴾

243.Je, hukuwaona wale waliotoka majumbani mwao nao walikuwa maelfu wakiogopa mauti? Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni; kisha akawafufua. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.

﴿وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴾

244.Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

KUOGOPA MAUTI

Aya 243 - 244

MAANA

Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu Aya hii, wengi wao wameonyesha kuwa ni kisa cha kihistoria na kuchafua kurasa katika kukielezea kisa hiki. Baadhi yao wamesema hivi: Watu katika Waisrail waliamrishwa kupigana jihadi dhidi ya adui zao. Wakaogopa kupigana ili wasife, wakayakimbia majumba yao kwa kuogopa kufa. Mwenyezi Mungu akawaua ili kuwafahamisha kwamba hakuna kitu chochote kinachoweza kukinga mauti; kisha akawafufua ili wazingatie na wamalize umri wao uliobakia. Ya kushangaza zaidi niliyoyasema katika tafsiri ya Aya hii ni kwamba mmoja wa wafasiri anasema: "Mauti ni namna mbili: Mauti ya mateso, nayo ni yale ya ambayo mtu huhuishwa baada ya kufa hapa hapa duniani. Na mauti ya ajali ambayo mtu atafufuliwa akhera." Wengine wamesema walikimbia maradhi ya Tauni, lakini sio kwa kupigana jihadi. Muhyiddin bin Arabi ameifasiri Aya hii kwa tafsiri yake ya Kisufi kwa kusema: "Mwenyezi Mungu aliwaua kwa ujinga akawafufua kwa elimu na akili."

Sheikh Muhammad Abduh ameichukulia Aya hii ni tamthiliya ya mazingatio na maonyo na wala sio tukio la kweli, na kwamba lengo la ishara hii ni kubainisha desturi ya Mwenyezi Mungu katika umma mbali mbali, na kwamba umma ambao unapigana jihadi na kulinda haki yake, utakuwa na maisha mema; na umma ambao una woga na kusalimu amri kwenye dhulma, utaishi maisha ya udhalili. Kwa hivyo kauli yake Mwenyezi Mungu kufeni ina maana ishini kwa kutawaliwa na kukandamizwa kwa ajili ya woga wenu, kwa sababu mfano wa maisha kama hayo ni mauti sio uhai. Na kauli yake akawahuyisha; ina maana aliwahuyisha kwa maisha ya uhuru na utukufu kwa sababu ya jihadi yao na kupigania haki yao.

Huu ni muhtasar mfupi sana wa rai ya Sheikh Muhammad Abduh ambayo ameifafanua kwa urefu sana. Na rai hiyo, kama unavyoiona, ni ya kimwamko lakini haitokani na dalili ya tamko la Aya. Rai yake yenyewe ni sahihi bila ya shaka lakini iko mbali na dalili ya tamko. Huenda ikadhaniwa kwamba ni ya karibu kuliko zile kauli nyingine za wafasiri kwa upande huu. Kwa sababu kauli zao zinategemea riwaya za Kiisrail na ngano tu. Na kauli ya Sheikh ina lengo la kuhamasisha, kupinga dhulma na kujitoa mhanga kwa ajili ya uhuru na heshima ya mtu, jambo ambalo lina mwelekeo. Vyovyote iwavyo Aya hii inawezekana kuwa na maana mbali mbali, ndio maana kauli zikawa nyingi; wala hakuna kitu katika tamko la Aya kinachofahamisha kuswihi kauli kwa dhati. Hata hivyo, kauli ya Sheikh Abduh ndio yenye nguvu zaidi ya kauli zote kwa kuangalia mwelekeo, kama tulivyokwisha eleza. Pia inasaidiwa na mpangilio wa maneno, pale alipofuatishia Mwenyezi Mungu moja kwa moja na Aya inayosema:"Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni msikizi, mjuzi."

﴿مَّن ذَا الَّذِي يُقْرِضُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا فَيُضَاعِفَهُ لَهُ أَضْعَافًا كَثِيرَةً وَاللَّـهُ يَقْبِضُ وَيَبْسُطُ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴾

245.Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, ili amzidishie ziada nyingi? Mwenyezi Mungu ndiye anayezuia na hukunja na hukunjua na kwake mtarejezwa.

NI NANI ATAKAYEMKOPESHA MWENYEZI MUNGU

Aya 245

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kupigania haki katika Aya iliyotangulia, katika Aya hii anahimiza kutoa mali ya kuwaandaa wapiganaji. Kwa sababu vita, kama vile vinavyohitajia watu, pia vinahitajia mali. Mwenye kusoma bajeti ya vita, ya madola makubwa hivi sasa, hana budi kupotewa na tarakimu. Baadhi ya Dola za kimagharibi zimefikia zaidi ya elfu mia nne milioni. Lakini bajeti yote hii inahusika na kufanya uadui, kutaka ukubwa kutawala kimabavu, kuwakandamiza watu na kuwatawala katika mambo yao yote. Ama jihadi aliyoihimiza Mwenyezi Mungu katika kitabu chake ni jihadi kwa ajili ya kupigania haki na kujikinga na maadui.

Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri.

Ilivyo hii ni amri ya kujitolea. Imekuja kwa njia ya swali ili kuilainisha mioyo ya waumini, waweze kuona wepesi kujitolea kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Na kauli yake Mwenyezi Mungu mkopo mzuri ni kuonyesha kuwa mali itakayotolewa ni lazima iwe ya halali sio ya haram na kujitolea kwa radhi na kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Atimize sharti hizo, ili Mwenyezi Mungu amzidishie ziada nyingi. Imam Jaffar Sadiq(a.s) anasema: Iliposhuka Aya hii:

﴿مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا﴾

Atakayefanya wema atapata jaza bora kuliko huo (28:84).

Mtume alisema:Ewe Mola wangu nizidishie, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii:

﴿مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ عَشْرُ أَمْثَالِهَا﴾

Atakayefanya wema, atalipwa mfano wake mara kumi (6:160)

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akasema:Ewe Mola wangu nizidishie, basi Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii IliMwenyezi Mungu amzidishie ziada nyingi. Na wingi mbele ya Mwenyezi Mungu hauna idadi.

Na Mwenyezi Mungu hukunja na kukunjua.

Yaani hudhikisha na kufanya wasaa, kwa maana kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuwahimiza waja wake kutoa kwa kuwa ana haja; hapana, Yeye ni mkwasi, na wao ni wahitaji. Lengo hasa ni kuwaongoza kwenye amali ya heri.

Na Kwake mtarejeshwa.

Ili mwema alipwe kwa wema wake na mwovu kwa wovu wake.

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الْمَلَإِ مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ مِن بَعْدِ مُوسَىٰ إِذْ قَالُوا لِنَبِيٍّ لَّهُمُ ابْعَثْ لَنَا مَلِكًا نُّقَاتِلْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ قَالَ هَلْ عَسَيْتُمْ إِن كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ أَلَّا تُقَاتِلُوا قَالُوا وَمَا لَنَا أَلَّا نُقَاتِلَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَقَدْ أُخْرِجْنَا مِن دِيَارِنَا وَأَبْنَائِنَا فَلَمَّا كُتِبَ عَلَيْهِمُ الْقِتَالُ تَوَلَّوْا إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ ﴾

246.Je, Hukuona wakubwa wa wana wa Israil baada ya Musa walipomwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu. (Mtume wao) akasema: Je, haielekei kuwa hamtapigana mtakapoandikiwa kupigana? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa nje ya majumba yetu na watoto wetu? Walipoandikiwa kupigana, wakageuka isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

﴿وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ اللَّـهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا قَالُوا أَنَّىٰ يَكُونُ لَهُ الْمُلْكُ عَلَيْنَا وَنَحْنُ أَحَقُّ بِالْمُلْكِ مِنْهُ وَلَمْ يُؤْتَ سَعَةً مِّنَ الْمَالِ قَالَ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَاهُ عَلَيْكُمْ وَزَادَهُ بَسْطَةً فِي الْعِلْمِ وَالْجِسْمِ وَاللَّـهُ يُؤْتِي مُلْكَهُ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴾

247.Na Nabii wao akawaambia: Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu amemteua juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme Wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

﴿وَقَالَ لَهُمْ نَبِيُّهُمْ إِنَّ آيَةَ مُلْكِهِ أَن يَأْتِيَكُمُ التَّابُوتُ فِيهِ سَكِينَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَبَقِيَّةٌ مِّمَّا تَرَكَ آلُ مُوسَىٰ وَآلُ هَارُونَ تَحْمِلُهُ الْمَلَائِكَةُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴾

248.Na Nabii wao akawaambia: Hakika alama ya ufalme wake ni kuwajia lile sanduku ambalo ndani mna kitulizo na mabaki ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na wa Harun, wakilibeba Malaika. Hakika katika hayo mna dalili kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini.

﴿فَلَمَّا فَصَلَ طَالُوتُ بِالْجُنُودِ قَالَ إِنَّ اللَّـهَ مُبْتَلِيكُم بِنَهَرٍ فَمَن شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّي وَمَن لَّمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُ مِنِّي إِلَّا مَنِ اغْتَرَفَ غُرْفَةً بِيَدِهِ فَشَرِبُوا مِنْهُ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ فَلَمَّا جَاوَزَهُ هُوَ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ قَالُوا لَا طَاقَةَ لَنَا الْيَوْمَ بِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالَ الَّذِينَ يَظُنُّونَ أَنَّهُم مُّلَاقُو اللَّـهِ كَم مِّن فِئَةٍ قَلِيلَةٍ غَلَبَتْ فِئَةً كَثِيرَةً بِإِذْنِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴾

249.Basi Talut alipoondoka na jeshi, alisema: Mwenyezi Mungu atawafanyia mtihani kwa mto. Basi atakayekunywa humo si pamoja nami na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka fumba kwa mkono wake. Wakanywa humo isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi walipovuka, yeye na wale walioamini pamoja naye walisema: Leo hatumwezi Jalut, na Jeshi lake. Na wenye yakini ya kukutana na Mola wao walisema: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira.

﴿وَلَمَّا بَرَزُوا لِجَالُوتَ وَجُنُودِهِ قَالُوا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَثَبِّتْ أَقْدَامَنَا وَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴾

250. Na walipotoka kupambana na Jalut na jeshi lake walisema: Mola wetu, tumiminie subira na uisimamishe imara miguu yetu na utasaidie tuwashinde watu makafiri.

﴿فَهَزَمُوهُم بِإِذْنِ اللَّـهِ وَقَتَلَ دَاوُودُ جَالُوتَ وَآتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَهُ مِمَّا يَشَاءُ وَلَوْلَا دَفْعُ اللَّـهِ النَّاسَ بَعْضَهُم بِبَعْضٍ لَّفَسَدَتِ الْأَرْضُ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ ذُو فَضْلٍ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴾

251.Basi wakawashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu; na Daud akamuua Jalut, na Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima na akamfundisha aliyoyataka. Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwazuia watu, baadhi yao kwa wengine, ingeliharibika ardhi; lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya viumbe vyote.

﴿تِلْكَ آيَاتُ اللَّـهِ نَتْلُوهَا عَلَيْكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴾

252.Hizo ni Aya za Mwenyezi Mungu, tunakusomea kwa haki; na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.`

KISA CHA TALUT

Aya 246 - 252

Tumekwishaeleza katika tafsiri ya Aya ya 2 kwamba Qur'an ni kitabu cha mwongozo na dini, na ni kitabu cha kueleza tabia njema na sharia; sio kitabu cha visa na Historia au Filosofia na Sayansi, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akielezea tukio la Kihistoria hulieleza kwa ajili ya mawaidha na kuwataka watu wazingatie; na wala haileti kisa chote kwa upambanuzi katika pande zake zote. Hilo limeelezewa katika Aya kadhaa; kama vile:

﴿لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ﴾

"Kwa hakika katika visa vyao, kuna fundisho kwa wenye akili ..." (12:111)

﴿قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِكُمْ سُنَنٌ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ﴾

"Zimepita desturi kabla yenu, basi tembeeni katika nchi na muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha." (3: 137)

Sheikh Muhammad Abduh anasema; "Kujaribu kuifanya Qur'an kuwa ni kitabu cha Historia ni kuhalifu desturi ya Qur'an na ni kuziepusha nyoyo na mawaidha yake, na pia ni kulipoteza lengo lake na hekima yake. Lililo wajibu kwetu ni kufahamu yaliyomo ndani yake na kuzitumia fikra zetu katika kutoa mafundisho, tujivue na yale yanayoitusi na kuikebehi Qur'an, na tujipambe na yale yanayoisifu Qur'an na kuiweka vizuri. Mwenyezi Mungu amekidokeza kisa cha Talut katika Aya hizi (246-252), Nasi tutakitaja kama vile yanavyofahamisha matamko ya Aya hizi; kisha tutaidokeza sehemu za mafundisho na mawaidha.

Baada ya kufa Musa(a.s) walikuwako makhalifa wake katika Manabii waliokuwa wakiendeleza amri za Mwenyezi Mungu katika Waisrail. Miongoni mwa makhalifa ni Mtume aliyeelezwa katika Qur'an bila ya kutajwa jina lake, isipokuwa alikuwa wakati wa Nabii Daud(a.s) , kama zinavyofahamisha Aya. Wafasiri wengi wanasema alikuwa akiitwa Samuel. Siku moja kikundi cha Waisrail kilimwendea na kumwambia" "Tuwekee mkuu wa jeshi ambaye tutafuata rai yake katika kupanga vita, na tupigane pamoja naye katika njia ya Mwenyezi Mungu,"

Mtume wao akawaambia - na alikuwa amekwisha watahini - "Mimi naona mtamwacha kama vita vikianza na mkiitwa kwenye jihad," Wakasema: "Tutamwachaje ikiwa adui ametutoa katika majumba yetu; na kutuweka mbali na watoto wetu?" Basi Nabii wao akamtaka shauri Mwenyezi Mungu kwa yule atakayefaa kuongoza vita, Mwenyezi Mungu akampelekea wahyi kwa kusema kuwa "Mimi nimewachagulia wao Talut kuwa mfalme," Inasemekana - aliitwa Talut kwa sababu ya urefu wake; kutokana na neno la Kiarabu Tul (urefu),. Mtume alipowapa habari hiyo kwamba Mwenyezi Mungu amemchagua Talut walisema: "Atakuwaje mfalme wetu na wala hatokani na ukoo wowote mtukufu tena ni maskini?" Mtume akasema: "Kiongozi hahitaji ukoo isipokuwa awe na ushujaa na maarifa ya kuendesha mambo. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa Talut uwezo wa kielimu na ki-umbo na nyenzo nyingine za kiongozi,"

Wakasema: "Basi tunataka alama itakayofahamisha uwezo wake huu." Akasema: "Alama ni kurudishiwa kasha; litaletwa na Malaika kwa amri ya Mwenyezi Mungu," Inasemekana kasha hilo lilikuwa na mabaki ya mbao za Musa, fimbo yake, nguo zake na baadhi ya sehemu ya Taurat. Na walikuwa wamenyang'anywa na Wapalestina katika vita fulani. Pia imesemwa kwamba Mwenyezi Mungu aliliinua kulipeleka mbinguni baada ya kufa Musa. Lilipowajia kasha kutoka kwa Mwenyezi Mungu waliamini uongozi wa Talut. Talut akawaongoza kwenda kupigana na adui yao; akawafahamisha kuwa watapitia kwenye mto ambako watatahiniwa kuangaliwa ikhlasi yao. Ambaye atakuwa na subira hatakunywa isipokuwa kiasi cha kitanga chake cha mkono. Atakayefuata ndiye msafi mwenye kutegemewa. Ama ambaye atakunywa mpaka amalize kiu, sio wa kutegemewa katika vita na jihadi. Walipopitia kwenye mto waliasi kama kawaida yao, wakanywa isipokuwa kikundi kidogo tu, kilithibiti kwenye ukweli na uaminifu.

Yalipokutana makundi mawili, Waisiralil wakiongozwa na Talut (Sauli) na Wapalestina wakiongozwa na Jalut (Goliat), Waisrail wengi waliogopa na kumwambia Talut;"Hatumuwezi Jalut na jesShi lake," Waumini wachache ambao hawakunywa maji wakasema : Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu," Wakamwomba Mwenyezi Mungu awape subira uthabiti na ushindi. Mwenyezi Mungu akawatakabalia dua yao baada ya kujua nia yao, azma yao na ukweli katika nia. Daud akamuua Jalut na maadui wakahsindwa vibaya sana. Daud akawa maarufu mwenye kusikika sana baada ya kumuua Jalut. Baada ya hapo Mwenyezi Mungu akampa Utume, akamtremshia Zabur na akamfundisha kutengeneza deraya na elimu ya dini na upambanuzi wa maneno; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima."

Huu ndio muhtasari wa zinavyofahamisha Aya tukufu. Ama Daud kumwoa binti ya Talut na kujaribu kufanya vitimbi vya kumuua kwa kumuoza binti yake, teo ya Daud na mawe yake, na kisa cha Daud na wanyama wakali mwituni, na mfano wa hayo yaliyomo katika vitabu vya Tafsir, vyote hivi ni visa ambavyo havina tegemeo lolote la mapokezi isipokuwa mapokezi ya Kiisrail.

Ama somo la kisa hiki ni anayefaa kuongoza ni yule mwenye uwezo wa kielimu na kiumbo na wala sio yule mwenye nasaba na fahari au mwenye jaha na mali; na kwamba ushindi utakuwa pamoja na subira na imani na wala sio kwa wingi wa watu; na njia ya kumjua mwema na mwovu ni kwa majaribio na mitihani. Baada ya kuelezea muhtasari wa kisa na somo lake, sasa tunaingilia kufasiri jumla za maneno.

MAANA

Je, hukuona wakubwa wa wana wa Israil baada ya Musa.

Kwa dhahiri msemo unaelekezwa kwa Mtume, na katika maana unaelekezwa kwa wasikilizaji wote; na tamko linaelekezwa kwa mwenye kukijua kisa na asiyekijua pia. Unaweza kumwambia mtu; "Je hujui fulani amefanya nini," wakati huo unataka kumfahamisha aliyoyafanya.

Walipomwambia Nabii wao; Tuwekee mfalme ili tupigane katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Inasemekana Nabii waliyemwambia hayo ni Samuel.

(Mtume wao) akasema; Je, haielekei kuwa hamtapigana mtakapo andikiwa kupigana!

Yaani; je mambo yako kama ninavyoona kuwa miongoni mwenu kuna watakaojitoa na kuacha kupigana kama mkifaradhiwa vita?

Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na hali tumetolewa nje ya majumba yetu na watoto wetu?

Walikanusha kuwa na chochote kitakacho wafanya waache jihadi; na wakabainisha sababu itakayowafanya wapigane ambayo ni kutolewa majumbani mwao na kutenganishwa na watoto wao.

Walipoandikiwa kupigana waligeuka, isipokuwa wachache miongoni mwao.

Watu wengi wana sifa hii; wanathibitisha na wanaazimia kufanya mambo, lakini wakati ukifika wanajificha mvunguni. Ufasaha zaidi wa yaliyosemwa kuhusu mambo hayo ni kauli ya Bwana wa mashahidi Hussein bin Ali(a.s) ;"Watu ni watumwa wa dunia na dini wameilamba kwa ndimi zao tu, inachukulika yanapokuwa mazuri maisha yao. Wapatwapo na misukosuko, wenye dini wanakuwa wachache.

Na Mtume wao akawaambia; Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, na hali sisi tunastahiki zaidi ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali?

Mantiki hii haiwahusu Waisrail tu, bali watu wengi walikuwa na wanaendelea kuwa na mawazo kwamba cheo ni cha mwenye mali na jaha. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَإِذَا رَأَوْكَ إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَـٰذَا الَّذِي بَعَثَ اللَّـهُ رَسُولًا﴾

"Na wanapokuona hawakufanyi ila ni mzaha tu (wanasema); 'Ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa Mtume?" (25:41)

Akasema: Hakika Mwenyezi Mungu amemteua juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili.

Yaani uongozi haui kwa sababu ya mali na nasaba, bali ni kwa elimu na ikhlasi. Makusudio ya ukunjufu wa kiwiliwili ni kutokuwa na maradhi, kwa sababu maradhi yanamzuwia kiongozi kutekeleza wajibu wake. Inasemekana kuwa Talut alikuwa mrefu zaidi kuliko mtu wa kawaida kwa kiasi cha dhiraa moja ya mkono.

MATAKWA YA MWENYEZI MUNGU NA KIONGOZI MWOVU

Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye.

Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni Mfalme wa wafalme, humpa ufalme amtakaye na humvua amtakaye; humtukuza amtakaye na humdhalilisha amtakaye; heri imo mikononi mwake na Yeye ni muweza juu ya kila kitu. Hapana shaka katika hilo; lakini, Yeye ambaye hekima yake imetukuka, ni Mwadilifu, hamdhulumu yeyote na hafanyi mambo kiholela. Vipi isiwe hivyo na hali Yeye amesema:

"Na kila kitu kwake ni kwa kipimo."( 13:8)

Yaani kwa nidhamu na sababu, sio kwa sadfa au kiholela; hata mali ya haramu na utawala wa dhulma una sababu zake za kijamii. Unaweza kuuliza: Je utawala mwovu na utajiri wa unyanga'nyi unategemea matakwa ya Mwenyezi Mungu?

Jibu : Hapana, Mwenyezi Mungu ameharamisha dhulma na unyanga'nyi. Na Yeye hajiingizi katika mambo ya kijamii kwa njia ya Kun fayakun (kuwa ikawa). Mwenyezi Mungu hamzuwii kwa nguvu dhalimu kutokana na dhulma yake isipokuwa anamkataza kwa kisheria na kimwongozo na anamuhadharisha na kumtolea viaga. Atakapohalifu atamwadhibu siku ya malipo iliyo kubwa. Kama angelitaka kumzuwia angelifanya, lakini anaacha mambo yapite kwa sababu zake na desturi zake. Huenda ikawa huu ndio mwelekeo wa kumnasibishia Mwenyezi Mungu ufalme kwa jumla. Kwa hivyo yanakuwa maana. "humpa ufalme wake amtakaye" ni kwamba Mwenyezi Mungu lau angelitaka kuuzuwia kwa nguvu ufalme kwa asiyeustahiki, angelizuwia na wala asingelifikia kwenye ufalme mtu dhalimu pamoja na kuwepo sababu zake za kikawaida. Vyovyote iwavyo utajiri wa mtu na ufalme wake unakuja kutokana na natija yakijamii anayoishi. Ama kuunasibisha na matakwa ya Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya sababu yoyote ni makosa kabisa.

Na Mtume wao akawaambia: Hakika alama ya ufalme wake ni kuwajia lile sanduku.

Sanduku hilo lilikuwa la Musa alilokuwa akiwekea Taurat. Mwenyezi Mungu alikuwa amelipaza mbinguni baada ya kufa Musa kwa kuwakasirikia Mayahudi kama ilivyosemwa.

Ambalo mna ndani kitulizo.

Yaani kitulizo cha nyoyo zenu ambapo sanduku lilikuwa na jambo tukufu la kidini kwa Wana wa Israil.

Na mabaki ya yale waliyoyaacha watu wa Musa na wa Harun.

Mwenyezi Mungu hakubainisha ni mabaki gani hayo. Watu wa Musa na wa Harun ni Mitume ambao walilirithi sanduku hilo.

Wakilibeba Malaika.

Yaani kwa miujiza. Basi Talut alipoondoka na jeshi, alisema: Mwenyezi Mungu atawafanyia mtihani kwa mto, basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka fumba kwa mkono wake.

Imepokewa kwamba Talut aliwaambia Waisrail: "Asitoke na mimi kwenye jihadi mzee, mgonjwa, aliyejenga jengo ambalo hajalimaliza, mwenye kushughulishwa na biashara, au mume aliyeoa mke ambaye hajamwingilia." wakakusanyika jamaa wenye sifa zinazotakiwa, na ulikuwa ni wakati wa kiangazi na joto kali, wakafuata njia isiyokuwa na maji. Walipolalamikia kiu, Talut aliwaambia: "Mwenyezi Mungu atawapa mtihani katika utii na uasi kwa mto mtakaoupitia. Atakaye kunywa katika mto huo si katika wafuasi wangu waumini, isipokuwa akinywa kidogo kiasi cha kiganja.

Wakanywa humo isipokuwa wachache miongoni mwao.

Inasemekana idadi ya waumini ilikuwa ni 313 kama idadi ya watu wa vita vya Badr. Hakika wema walikuwa na wanaendelea kuwa ni nadra sana kupatikana.

Basi alipovuka yeye na wale walioamini pamoja naye walisema: Leo hatumwezi Jalut na jeshi lake.

Aliendelea mbele Talut pamoja na wale waliomtii baada ya kuvuka mto mpaka wakakutana na Jalut na jeshi lake. Walipoona wingi wa adui yao, waligawanyika makundi mawili; kundi lilisema hatumwezi Jalut na kundi likasema:

Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wafanyao subira.

Ambao wamejizatiti kwa kupigana jihadi na kujitoa mhanga kwa ajili ya maisha mema yaliyo bora ambayo ni kuishi huru katika nchi iliyo huru na kujitosheleza kwa chakula na wataalamu katika nchi iliyoendelea. Ama kuvumilia udhalili na umasik-ini ni uchafu katika kazi ya shetani.

Na walipotoka kupambana na Jalut na jeshi lake walisema: Mola wetu, tumiminie subira na uithubutishe miguu yetu, na utusaidie juu ya watu makafiri.

Waumini walipojiona ni wachache na maadui zao ni wengi walikimbilia kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa kuomba na kunyenyekea kwa ikhlas; na Mola wao akawatakabalia dua. Na Daud akamuua Jalut. Na Mwenyezi Mungu akawapa ushindi waumini dhidi ya makafiri. Ikathibitika, kwa fadhila Zake na rehema Zake, dhana ya waliosema: "Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu akampa ufalme na hekima na akamfundisha aliyoyataka.

Yaani Mwenyezi Mungu alimtawalisha Daud mahali pa Talut baada ya kufa kwake. Hekima ni ishara ya Zabur. Mwenyezi Mungu anasema:

"...Na tukampa Daud Zabur." (4:163)

Na akamfundisha kutengeneza deraya (mavazi ya vita), Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَعَلَّمْنَاهُ صَنْعَةَ لَبُوسٍ لَّكُمْ لِتُحْصِنَكُم مِّن بَأْسِكُمْ ﴾

"Na tukamfundisha (Daud) kutengeneza mavazi kwa ajili yenu ili yawahifadhi katika mapigano yenu ..." (21:80)

Na kama Mwenyezi Mungu asingeliwazuia watu baadhi yao kwa wengine ingaliharibika ardhi. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya viumbe vyote.

Yaani jamii yoyote ambayo ndani yake hamna utawala (serikali) basi itakuwa na vurugu. Na kwamba akili na sharia bila ya nguvu ya utekelezaji haiwezi kuleta amani na nidhamu.

Imam Ali(a.s) anasema"Mfalme ni msaidizi wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake... " Lakini mara ngapi wafalme wameiharibu ardhi na watu wake. Pamoja na hivyo, lakini hawatengenei watu wasiokuwa na mwendeshaji.

Hizo ni Aya ya Mwenyezi Mungu, tunakusomea kwa haki; na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.

Mwenyezi Mungu alimsomea Mtume wake Aya zake na Mtume akatusomea ili tuzingatie hakika yake na tuzifanye ndizo desturi za vitendo vyetu vyote ili tuwe na maisha mema yenye utulivu.

﴿قُلْ إِنَّمَا أُنذِرُكُم بِالْوَحْيِ وَلَا يَسْمَعُ الصُّمُّ الدُّعَاءَ إِذَا مَا يُنذَرُونَ ﴾

"Sema mimi nawaonya kwa wahyi na viziwi hawasikii mwito wanapoonywa." (21:45)

MWISHO WA JUZUU YA PILI

14

SHARTI YA KUCHAPA

sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.