TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 18983
Pakua: 2849


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 18983 / Pakua: 2849
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ ﴾

159.Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha, katika ubainifu na uwongofu, baada ya Sisi kuyabainisha kwa watu Kitabuni, hao anawalaani Mwenyezi Mungu na wanawalaani wanaolaani.

﴿ إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَبَيَّنُوا فَأُولَـٰئِكَ أَتُوبُ عَلَيْهِمْ وَأَنَا التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴾

160.Ila wale waliotubu na kujirekebisha na wakabainisha, basi hao nitawatakabalia toba, na Mimi ni Mwingi wa kutakabali toba, Mwenye kurehemu.

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ لَعْنَةُ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ﴾

161.Hakika wale waliokufuru, na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.

﴿خَالِدِينَ فِيهَا لَا يُخَفَّفُ عَنْهُمُ الْعَذَابُ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴾

162.Humo watadumu, hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa muda.

WANAOFICHA YALIOTEREMSHWA

Aya 159-162

MAANA

Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha katika ubainifu na uwongozi, baada ya sisi kuyabainisha kwa watu kitabuni hao anawalaani Mwenyezi Mungu na wanawalaani (kila) wanaolaani.

Dhahiri ya Aya ni kwamba inaanzia habari nyingine isiyofungamana na yaliyo kabla yake. Makusudio ni kuwa: kila mwenye kujua hukumu katika hukumu za dini ambazo ubainifu wake umekuja katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu au katika Hadith za Mtume wa Mwenyezi Mungu au katika hukumu ya akili na akaificha, basi yeye amelaaniwa mbele ya Mwenyezi Mungu na watu wa mbinguni na ardhini. Mwenyezi Mungu ameashiria hukumu ya akili kwa kusema Uwongofu.

Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Ubainifu ni dalili za kisharia na uwongofu ni dalili za kiakili... Laana haiko kwa watu wa Kitabu tu, bali inamhusu kila mwenye kuficha haki kwa vile:

1. Tamko la Aya halikufungwa na jambo lolote.

2. Lau tunakadiria kuwa mashukio ya Aya ni kutokana na waliyoyafanya watu wa Kitab ya kupotoa Tawrat na Injil, basi tutasema: mashukio hayafanyi hukumu iliyo shuka kuwa mahsusi; kama wasemavyo Wanafiqh, ambao wanakusudia kusema kuwa tukio mahsusi haliwezi kufanya tamko la kiujumla kuwa mahasusi.

3. Imethibiti katika elimu ya Usul kwamba kufungamana hukumu juu ya sifa kunafahamisha kuwa sifa ni sababu. Na hapa laana inafungamana na kuficha kwenyewe. Kwa hiyo inakuwa laana inaenea kwa kila chenye kufichwa.

4. Imekuja Hadith inayosema:Mwenye kuulizwa elimu anayoijua, akaficha, atafungwa lijamu ya moto siku ya Kiyama. Wameafikiana mafakihi kwa tamko moja kwamba kumfundisha asiye jua hukumu za dini yake ni dharura ya wajibu kifaya (wajibu wa kutosheana) kwa kila mwenye kuijua; wakiitekeleza baadhi basi jukumu limewaondokea wote; na wakiiacha wote, basi watastahili adhabu wote. Maana ya laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni kumtoa, mwenye kulaaniwa kutoka katika rehema Yake, na maana ya laana kutoka kwa Malaika na watu ni dua ya kutaka mwenye kulaaniwa atolewe katika rehema ya Mwenyezi Mungu.

UBAYAWAADHABU BILA YA UBAINIFU

Jukumu la mwenye kukalifiwa na sharia aliye baleghe na mwenye akili timamu, mbele ya Mwenyezi Mungu hupimwa kwa kumfikia taklifa zenyewe na kuzijua, wala sio kupatikana taklifa. Kwa sababu kuacha kumfikia ni sawa na kutokuwepo. Hata hivyo ni wajibu kwa kila mwenye kukalifiwa na sharia (makallaf) atafute na kufanya utafiti wa ubainifu na dalili za hukumu katika sehemu zinakopatikana na kuwaulizia wanaohusika katika dini na sharia, wala haifai kwake kufanya uzembe na kupuuza, kisha aje atoe udhuru kuwa hajui. Kwa sababu mwenye kuzembea ni sawa na mwenye kufanya makusudi, bali huo uzembe hasa ni makusudi, kwa vile mzembe anakuwa amekusudia kuacha kutafuta na kusoma. Kama akifanya bidii na asipate lolote, basi atakuwa hana jukumu, hata kama ubainifu uko. Hakika huu ni msingi ulio wazi kiakili; ni akili gani inayoweza kumlaumu mwingine, ambaye hakufanya uzembe, kwa jambo asilolijua? Wanavyuoni wa Fiqh wamesema kwa pamoja kuhusu msingi huu na umethibitishwa na sharia katika Aya kadhaa; kama Aya hii tunayoizungumzia; Baada ya sisi kuzibainisha kwa watu. Pia Aya inayosema:

...Na sisi si wenye kuwadhibu mpaka tumpeleke Mtume. (17:15).

Katika Hadith za Mtume iko inayosema:Umeondolewa umma wangu yale wasioyoyajua. Tutayarudia maudhui haya kila tutakapofikilia kwenye Aya inayoyagusia Inshaallah.

Ila wale waliotubu na kujirekebisha na wakabainisha.

Yaani wale wanaoificha haki ni wenye kulaaniwa, isipokuwa wale waliotubu na kujuta kwa ikhlas katika toba kwa kuazimia kutorudia makosa; kisha wakayabainisha wazi wazi yale waliyokuwa wameyaficha mwanzo. Kwani kutubia kwa mwizi hakutoshi maadamu hajarudisha haki ya wenyewe.

Basi hao nitawatakabalia toba na Mimi ni Mwingi wa kutakabali toba Mwenye kurehemu.

Neno: tawwab (mwingi wa kukubali toba) ni katika sifa za Mwenyezi Mungu (s.w.t.). Ameikutanisha rehema na kukubali toba, kwa kukumbusha kuwa sababu ya kukubali kwake toba kwa aliyemfanyia uovu ni rehema Yake kwa waja wake.

Hakika wale waliokufuru na wakafa hali ni makafiri, hao wana laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.

Hata mwenye kumkufuru Mwenyezi Mungu na akamkanusha, hukubaliwa toba yake akitubia na husamehewa na kurehemewa, wala hataadhibiwa isipokuwa yule atakayekufa akiwa ameng’ang’ania ukafiri na maasi, kwa sababu yeye katika hali hiyo anastahili laana ya watu wa mbinguni na wa ardhini. Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu anasema: Na ya watu wote na inajulikana kuwa katika watu kuna wasio mlaani kafiri, hasa wale makafiri?

Jibu : Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu; Na ya Malaika wote na ya watu wote ni kwamba huyo kafiri yuko mahali pa laana ya watu wa mbinguni na wa ardhini, iwe wamemlaani au hawakumlaani; hata kama ni makafiri kama wao, yeye ni wa kulaaniwa tu. Katika Quran inaelezwa kwamba makafiri kesho watalaaniana wenyewe kwa wenyewe

﴿ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُ بَعْضُكُم بِبَعْضٍ وَيَلْعَنُ بَعْضُكُم بَعْضًا ﴾

....Kisha siku ya Kiyama baadhi yenu watawakufurisha wengine na baadhi yenu watawalaani wengine... (29:25).

Humo watadumu, hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa muda humu, ni humo mwenye laana.

Maana ya kudumu katika laana ni kukaa milele katika athari ya hiyo laana ambayo ni moto. Razi anasema: Maana ya hawatapewa muda ni kwamba wakiomba muda hawatapewa na wakilia kutaka kuokolewa hawataokolewa na wataambiwa: Nyamazeni wala msiseme, Mwenyezi Mungu apishie mbali.

HUKUMU YA LAANA KATIKA SHARIA

Kumlaani mtu ni haramu na ni katika madhambi makubwa kwa sababu ni uadui sawa na kuingilia mali; katika Hadith inaelezwa:Hakika laana ikitoka kwa mtu, huzunguka, ikimkosa humrudia mwenyewe. Ziko laana zilizoruhusiwa na sharia ambazo ni:-

1. Kafiri: Aya ni nyingi sana kuhusu kafiri, kama hii tunayoizungumzia. Ama Hadith zimepetuka kuwa Mutawatir. Miongoni mwazo ni ile iliyo katika kitabu Ahkamul-Quran cha kadhi Abu Bakr Al-Muafiri, aliyoitaja wakati wa kutafsiri (2:161), kwamba Mtume alisema:Ewe Mwenyezi Mungu hakika Amr bin Al-Aas amenikebehi na anajua kuwa mimi si mshairi, basi mlaani.

2. Dhalimu: Awe Mwislamu au si Mwislamu, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate madhalim (7 : 44)

3. Mwenye kufanya ufisadi.

4. Mwenye kufitini na kusababisha zogo. Ama laana ya wasiokuwa hao waliotajwa kuna mushkeli na kuangaliwa vizuri. Ndio, ni kweli kwamba mwenye kudhihirisha maasia bila ya kujali inajuzu kumsengenya, lakini kusengenya ni kitu kingine na laana ni kitu kingine. Ama wanavyotumia watu kuwalaani wanyama, n.k. ni upuuzi, unaofaa kutupiliwa mbali.

﴿وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ ﴾

163.Na Mungu wenu ni Mungu Mmoja, hakuna Mungu isipokuwa Yeye, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

﴿إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَالْفُلْكِ الَّتِي تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِمَا يَنفَعُ النَّاسَ وَمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِنَ السَّمَاءِ مِن مَّاءٍ فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا وَبَثَّ فِيهَا مِن كُلِّ دَابَّةٍ وَتَصْرِيفِ الرِّيَاحِ وَالسَّحَابِ الْمُسَخَّرِ بَيْنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴾

164. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kuhitalifiana usiku na mchana, na vyombo ambavyo hupita katika bahari pamoja na viwafaavyo watu, na maji aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mawinguni, na kwa maji hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama, na mabadiliko ya pepo na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, ni ishara kwa watu wenye akili.

NA MUNGU WENU NI MUNGU MMOJA

Aya 163-164

MAANA

Na Mungu wenu ni Mungu mmoja, hakuna Mungu isipokuwa Yeye. Amirul Mumini katika kumuusia Mwanawe Hassan(a.s) alisema:

Ewe mwanangu! Jua kwaamba lau Mola wako angelikuwa na mwenzake,basi huyo mwenzake angelileta Mitume yake na ungeliona athari za ufalme na usultani wake, na ungelijua vitendo vyake na sifa zake. Maelezo ya kukanusha ushirika yatakuja katika kufafanua Aya ya (17:42) (21:22) na (23:91).

MBINGU

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi.

Katika mbingu kuna nyota zinazozidi chembe za mchanga kwa idadi; nyota iliyo ndogo zaidi miongoni mwazo, ni ile ambayo ni kubwa zaidi ya ardhi mara milioni. Kila kundi la nyota linakuwa katika mkusanyiko mkubwa unaoitwa Galaxy unaokusanya zaidi ya nyota milioni mia moja. Idadi ya mikusanyiko hiyo ni zaidi ya milioni mbili. Kila mji uko mbali na mwingine kwa masafa ya simu ya upepo ambayo umbali wake kufikiwa ni miaka milioni tatu, yaani mikusanyiko hiyo yote katika anga iliyo wazi ni sawa na nzi anayepotea katika dunia. Nyota zote hizo na sehemu zake zinakwenda kwa kipimo na utaratibu mzuri. Huu ni mfano mmoja wa mamilioni ya mifano juu ya kudura ya Mwenyezi Mungu na ukubwa wake uliovumbuliwa na Sayansi. Na Quran tukufu bado inawaambia wavumbuzi hao:

...Nanyi hamkupewa elimu ila kidogo. (17:85).

ARDHI

Ardhi ni tufe lililo hewani; inazunguuka mara moja katika kila baada ya masaa ishirini na nne, ambayo usiku na mchana unafuatana. Inaelea kandoni mwa jua mara moja kwa mwaka ambapo vinafuatana vipindi vinne kwa mwaka. Ardhi inazunguukwa na mfuniko wa gesi yenye mchanganyiko wa gesi muhimu ya uhai; gesi hiyo inahifadhi kiwango cha nyuzi joto kinachowiana na uhai. Vile vile inachukua mvuke wa maji kutoka baharini na kuupeleka masafa ya mbali juu na hatimaye yanaanguka nakuwa mvua. Lau kama upana wa ardhi ungelikuwa mdogo kuliko ulivyo sasa, ingelishindwa kuhifadhi uzani; na joto lingepanda kufikia mauti; na kama ungelikuwa ni mkubwa zaidi ya ulivyo ingelizidi mvutano wake, na ziada hiyo ingeliathiri maisha. Vile vile, lau kama umbali wa ardhi na jua ungelipungua kuliko ulivyo hivi sasa, kiasi cha joto kingelipungua, na kama ardhi ingelikurubia zaidi jua kuliko ilivyo hivi sasa, basi joto lingezidi, Katika hali zote mbili maisha yangelikuwa magumu juu ya ardhi.

Kwa hivyo mduara wa ardhi, na kipimo cha sehemu wazi zinazoizunguuka, mzunguuko wake pembeni mwa jua, kuzunguukwa na mfuniko anga, kuwa mahali maalum na kuwa upana wake ni kiasi maalum, yote hayo yanaandaa sababu za kupata uhai wa mtu juu ya ardhi. Lau ingekosekana moja ya sifa hizi; kwa mfano upana wake kuwa mdogo au mkubwa, au kuwa mbali au karibu na jua au kukosa mfuniko anga, ingelikuwa vigumu mtu kuwa ni wa duniani, kwa ushahidi wa wataalamu. Ni jambo lisiloingia akilini kuwa utaratibu huu uwe umepatikana kibahati tu. Bali yote hayo ni kwa hekima ya Mwenye hekima na mazingatio ya Mwenye kuzingatia.

KUWAPO MUNGU

Katika kufasiri Aya ya 21 na 22 za Sura hii, tumetaja dalili za kuwapo Mpangaji mambo, Mwenye hekima. Miongoni mwa dalili hizo ni dalili ya kufikia kikomo, na kwamba mpangilio wa ndani uliofanywa kwa hekima kati ya mbingu na ardhi hauwezekani kuwa umepatikana kwa sadfa (kibahati) tu! Wala hakuna tafsiri yenye kukinaisha isipokuwa kuwapo Muweza,Mwenye hekima. Quran imetegemea dalili hii na ikaionyesha katika Aya nyingi, kama vile Aya hii tuliyonayo. Kwa kunasibiana kwake, tunarudia kutoa dalili ya kuwapo Mwenyezi Mungu, lakini kwa mfumo mwingine sio ule tuliofuata wakati wa kufasiri Aya ya 21. Kabla ya kitu chochote kwanza tunatanguliza haya yafuatayo: Wamaada wameamua sababu ya elimu na maarifa ni kuona na kujaribu tu. Kila linaloaminika ni lazima kupitia majaribio, kila linaloitakidiwa kwa njia nyingine isiyokuwa na majaribio basi hawaliiti kuwa ni elimu bali ni itikadi. Kwa hiyo elimu na itakidi - katika istihali yao -ni vitu viwili tofauti katika matokeo yake. Mtu akipata msaada wa majaribio kwa kusihi yale anayoyaitakidi, basi yanakuwa yale yanayoitakidiwa ni elimu. Kwa msingi wao huo, kunakuwa kuamini kuwapo Mwenyezi Mungu ni itikadi si elimu. Nasi tunawaambia: Lakini vile vile kuamini kutokuwapo Mungu pia ni itikadi si elimu, kwa sababu pia hakutegemei majaribio,Kwa hiyo itikadi zimekutana. Kwa maneno mengine, ni kwamba, kila yanayoambatana na Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ikiwa ni kukubali au kupinga, basi ni katika mambo ya ghaibu (yaliyojificha). Ikiwa mwenye kuamini kuwapo Mungu anaamini ghaibu bila ya majaribio, vile vile mwenye kukanusha hategemei majaribio, bali hutegemea ghaibu. Kwa hiyo wote ni sawa.

Baada ya utangulizi huu tutaonyesha kauli ya wakanushaji - Wamaada, na tutaonyesha kauli ya wenye kuamini Mungu kisha tumwachie msomaji ajichagulie. Wakanushaji wanasema: Kupatikana ulimwengu na yaliyomo ndani yake, miongoni mwa nidhamu, mtu, pamoja na hisia zake na akili, yote hayo hayategemei udhibiti wowote isipokuwa yamepatikana kibahati (sadfa). Kwa hiyo ulimwengu ulipatikana kibahati, kisha ukapatikana mpango kibahati na kila kitu kimechukua mahali pake panapostahili kwa kibahati tu; na maada ndiyo iliyopatisha uhai na akili. Kwa maneno mengine, ni kwamba maada pofu ndiyo Mungu inayoweza kila kitu, lakini imepata uwezo hekima na kupangilia mambo kwa njia ya kibahati. Ama wanaoamini kuwapo Mwenyezi Mungu wanasema: Ulimwengu na nidhamu yake, umepatikana kwa makusudio na kwa hekima, na mpangilio kutoka kwa Mola Muweza na Mwenye hekima. Sasa msomaji jiulize swali hili: Ni nini chanzo cha ulimwengu, utaratibu na mipangilio? Je chanzo chake ni sadfa kama wasemavyo Walahidi? Au ni kwa makusudio na mipangilio, kama wasemavyo Waumini? Jiulize swali hili kisha ujijibu kwa akili yako. Ama Voltaire amelijibu swali hili kwa kusema: Fikra ya kuwapo Mwenyezi Mungu ni dharura, kwa sababu fikra ya kupinga ni upumbavu.

UPI ULIOTANGULIA: USIKU AU MCHANA?

Wataalamu wamehitalifiana kuwa je mwangaza umetangulia giza au giza ndilo lililotangulia mwangaza katika kupatikana? Wengine wanasema mchana ndio uliotangulia usiku kwa hiyo usiku wa siku ni ule unaokuja baada ya mchana. Wengine wamesema usiku ndio uliotangulia mchana kwa hiyo usiku unakuwa ni usiku wa mchana utakaokuja. Watu wa kwanza walipendelea kauli hii; kwa hiyo usiku wa Ijumaa kwao ni ule usiku unaokuwa kabla ya alfajiri ya ijumaa na masiku mengine yote. Katika waliyoyatolea dalili ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na usiku ni ishara kwao; tunauvua humo mchana... (36:37).

﴿وَمِنَ النَّاسِ مَن يَتَّخِذُ مِن دُونِ اللَّـهِ أَندَادًا يُحِبُّونَهُمْ كَحُبِّ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَشَدُّ حُبًّا لِّلَّـهِ وَلَوْ يَرَى الَّذِينَ ظَلَمُوا إِذْ يَرَوْنَ الْعَذَابَ أَنَّ الْقُوَّةَ لِلَّـهِ جَمِيعًا وَأَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعَذَابِ﴾

165.Na katika watu kuna wanaofanya waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini wale walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu sana. Na lau waliodhulumu wangejua watakapoiona adhabu kwamba nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

﴿إِذْ تَبَرَّأَ الَّذِينَ اتُّبِعُوا مِنَ الَّذِينَ اتَّبَعُوا وَرَأَوُا الْعَذَابَ وَتَقَطَّعَتْ بِهِمُ الْأَسْبَابُ ﴾

166.Pindi waliofuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali yakuwa wamekwisha iona adhabu na yatawakatikia mafungamano.

﴿ وَقَالَ الَّذِينَ اتَّبَعُوا لَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَتَبَرَّأَ مِنْهُمْ كَمَا تَبَرَّءُوا مِنَّا كَذَٰلِكَ يُرِيهِمُ اللَّـهُ أَعْمَالَهُمْ حَسَرَاتٍ عَلَيْهِمْ وَمَا هُم بِخَارِجِينَ مِنَ النَّارِ﴾

167.Watasema wale waliofuata: Lau kama tungeweza kurudi nasi tukawakataa kama walivyotukataa. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto juu yao; wala hawatakuwa wenye kutoka motoni

WANAFANYAWAUNGU ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU

Aya 165-167

MAANA

Na katika watu kuna wanaofanya waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Yaani kuna baadhi ya watu wanamshirikisha Mwenyezi Mungu kwa sababu wao wamemfanya kuwa na mshirika katika baadhi ya mambo anayohusikana nayo; kama vile kunufaisha na kudhuru. Imam Baqir(a.s) amesema:Waungu ambao wamewafanya na kuwapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu ni maimamu wa dhuluma na wafuasi wao. Imesemwa kuwa maana ya kumpenda Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni kumpenda kwa ukamilifu, kwa sababu Yeye ni ukamilifu mtupu. Imesemwa pia: Ni kujua utukufu wake, uweza wake na hekima yake. Na imesemwa: Ni kumwamini Mwenyezi Mungu kuwa Yeye ndiye mwanzilishi na mwenye kurejesha, na kwamba kila kitu kiko chini ya mamlaka yake.

Sisi tuko kwenye njia ambayo tunakwenda nayo - kuchagua maana yenye kuafikiana ambayo yako wazi na yaliyo rahisi kufahamika. Kwa misingi hiyo tunasema: Anayempenda Mwenyezi Mungu ni yule asiyefuata matamanio yake na akamtii Mola wake; kama alivyosema Imam Sadiq(a.s) katika kumwelezea ambaye dini itachukuliwa kutoka kwake. Kwa maneno mengine, kumpenda kwako Mwenyezi Mungu ni kuacha unayoyataka wewe na kufanya anayoyataka Yeye; kama ambavyo maana ya kumpenda Mtume(s.a.w.w) ni kufanya kulingana na Sunna yake. Ama Mwenyezi Mungu kumpenda mja wake ni kumlipa thawabu. Imekuja Hadith inayosema:

Nitampa bendera kesho mtu anayempenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake na anayependwa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Yaani Ali anamtii Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu atamlipa thawabu na Mtume anamtukuza na kumtanguliza. Kwa hiyo basi,kila anayemtii kiumbe, huyo amefanya waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu, atake asitake.

Lakini wale walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu sana . Kwa sababu wao hawamshirikishi na yeyote katika twaa na humtegemea. Ama wale wasioamini wanawategema waungu wengi na wanamshirikisha pamoja na Mwenyezi Mungu katika twaa kutaka heri na kujikinga na shari. Na lau waliodhulumu (nafsi zao) wangejua watakapoiona adhabu kwamba nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu. Yaani lau washirikina ambao wamezidhulumu nafsi zao wanajua kwamba hakuna mwenye usultani katika siku ya haki na ya kupambanuliwa hukumu, isipokuwa Mwenyezi Mungu, na kwamba Yeye peke Yake ndiye Mwenye mamlaka ya kuwaadhibu waasi na kuwalipa mema watiifu, lau wangelijua hivyo, basi wangelikuwa na yakini kwamba atakayekuwa peke yake kesho katika kuendesha mambo ya akhera ndiye huyo huyo aliyepanga ulimwengu huu. Kwa hivyo jawabu la lau limeondolewa, linafahamika kutokana na mpangilio wa maneno. Pindi waliofuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali ya kuwa wamekwishaiona adhabu na kuwakatikia mafungamano. Maneno bado yanaendelea kwa wale wanaofanya waungu wasiokuwa Mwenyezi Mungu; wao ndio wanaoongozwa na ni wafuasi, na waungu ndio viongozi. Kesho pazia litakapofunguka, kiongozi atamkataa mfuasi wake kutokana na shida ya adhabu itakayotokea, na uhusiano kwao utakatika. Mwenye Majmaul-Bayan anasema: Zitaondoka zile sababu zote ambazo zinafungamanisha mapenzi, udugu, cheo mikataba ya umoja, n.k. na hilo ni mwisho wa kukata tamaa.

Aya hii inafanana na Aya inayosema:

﴿كُلَّمَا دَخَلَتْ أُمَّةٌ لَّعَنَتْ أُخْتَهَا حَتَّىٰ إِذَا ادَّارَكُوا فِيهَا جَمِيعًا قَالَتْ أُخْرَاهُمْ لِأُولَاهُمْ رَبَّنَا هَـٰؤُلَاءِ أَضَلُّونَا فَآتِهِمْ عَذَابًا ضِعْفًا مِّنَ النَّارِ قَالَ لِكُلٍّ ضِعْفٌ وَلَـٰكِن لَّا تَعْلَمُونَ﴾

...Kila umma utakapoingia utawalaani wenzake, mpaka watakapokusanyika wote humo, wa nyuma wao watawasema wa kwanza wao: Mola wetu! Hawa ndio waliotupoteza; basi wape adhabu ya moto maradufu! Atasema: Itakuwa kwenu nyote (adhabu) maradufu, lakini nyinyi hamjui tu. (7:38).

Na watasema wale waliofuata: Lau kama tungeweza kurudi nasi tukawakataa kama wanavyotukataa. Kesho atatamani kila muasi arudi duniani kutengeneza yale aliyokuwa ameyaharibu, hasa wafuasi wa watu wapotevu. Na hakuna kitu kilicho mbali zaidi ya matamanio haya, bali ni majuto yanayoichoma nafsi, sawa na moto unavyochoma mwili. Majuto hayo ni matunda ya kufuata matamanio na kupetuka mipaka. Dhahiri ya tamko la Aya inafahamisha kwamba inahusika na makafiri, lakini kwa mujibu wa sababu ya hukumu, inamhusu kila mwenye kufuata na kusaidia dhuluma na ufisadi, na kila mwenye kuitakidi kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kunufaisha na kudhuru. Vile vile mwenye kuchukua dini yake kutoka kwa wasio jua na wapotevu. Kwa hakika Aya hii inawahusu wote; hata mwenye kutamka shahada mbili, akaswali na kutoa zaka; isipokuwa asiyejua ambaye hakuzembea katika kujua uhakika wa mambo na kujua mambo yanayoweza kujulikana na akili yoyote iliyo timamu.

TAQLID NA MAIMAMU WANNE

Yamekuja maelezo katika tafsiri ya Al-Manar kwa kunakiliwa kutoka kwa Sheikh Muhammad Abduh kwamba, Maimamu wane: Abu Hanifa, Malik, Shafi na Bin Hambal wamekataza kufuatwa na kuchukuliwa kauli zao, na kwamba wao wanaamrisha ziachwe kauli zao na kifuatwe Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake. Baada ya kunakili kauli ya kila Imam katika hilo, akasema: Lakini Karkhi - mmoja wa mafakihi wa Kihanafi- anasema wazi kwamba asili ni kauli ya Abu Hanifa. Kama Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume wake zitaafikiana na kauli ya Hanafi ni sawa; na kama si hivyo, basi ni lazima kauli ya Mwenyezi Mungu au Hadith ifanyiwe taawili ili iweze kuafikiana na kauli ya Abu Hanifa. Maana yake ni kuwa kauli ya Abu Hanifa ndiyo inayohukumu na kuitangulia Quran na Hadith. Kauli hii kwa dhati yake ni kufru. Kuna kufru gani kubwa zaidi kuliko kuiacha kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa sababu ya kauli ya Abu Hanifa na wafuasi wake? Je, kuna tofauti gani kati ya mwenye kusema haya na wale waliotajwa na Mwenyezi Mungu aliposema:

﴿وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا أَلْفَيْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا﴾

Na wanapoambiwa; Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu husema; bali tunafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu... (2:170).

Tutafafanua kwa upana zaidi suala la taqlid katika kufasiri Aya ya 170 ya Sura hii Inshaallah. Kwa hiyo kufanya amali kwa kutegemea kauli za Maimamu wane ni kufanya amali bila ya ijitihadi wala taqlid, kwa sababu hao wane wamekataza kufuatwa.

﴿يَا أَيُّهَا النَّاسُ كُلُوا مِمَّا فِي الْأَرْضِ حَلَالًا طَيِّبًا وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴾

168.Enyi watu! Kuleni vilivyomo ardhini halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shetani. Hakika yeye kwenu ni adui aliye dhahiri.

﴿إِنَّمَا يَأْمُرُكُم بِالسُّوءِ وَالْفَحْشَاءِ وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴾

169. Hakika yeye anawaamrisha tu maovu na machafu, na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

﴿وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّبِعُوا مَا أَنزَلَ اللَّـهُ قَالُوا بَلْ نَتَّبِعُ مَا أَلْفَيْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ شَيْئًا وَلَا يَهْتَدُونَ ﴾

170.Na wanapoambiwa: Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu; husema: Bali tutafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?

KULENI VILIVYOMO KATIKAARDHI

Aya 168-170

LUGHA

Halali ni kila ambalo halikuthibiti kukatazwa katika sharia; na haramu ni lile lililothibiti kukatazwa. Makusudio ya uzuri hapa ni lile ambalo linapendelewa na nafsi na kuburudika nalo kwa sharti ya kutokuwa ni lenye kukatazwa. Na ovu ni lile ambalo mwisho wake ni uovu.

Enyi watu! Kuleni vilivyomo ardhini halali na vizuri .

Msemo huu unawahusu watu wote; ni sawa awe mtu amejiharamishia mwenyewe baadhi ya vyakula au asiyejiharamisha; ni sawa awe ni Mumin au kafiri. Kwa sababu kafiri atazuiliwa neema za akhera tu sio starehe za dunia. Kuna Hadith Qudsi isemayo:Mimi ninaumba na anaabudiwa mwingine na ninaruzuku na anashukuriwa mwingine . Katika vyakula kuna vya halali na haramu. Kula ambacho hakikukatazwa na sharia ni halali. Hadith inasema: Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia vitu sio kwa kusahau. Kwa hivyo msijikalifishe navyo; ni rehema kwenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mara nyingine uharamu unaotokana na sababu iliyozuka; kama vile mali iliyochukuliwa kwa riba, utapeli, rushwa au wizi.

Wala msifuate nyao za shetani. Hakika yeye kwenu ni adui aliye dhahiri.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuhalalishia watu halali anawahadharisha kuifanya haramu. Ibara ya tahadhari hii ameileta kwa kukataza kumfuata shetani na tashwishi zake ambazo zinampambia mtu yale yasiyokuwa halali kwake na kila ambalo linamhadaa, ili afanye mambo ya haramu; kama vile kunywa pombe, zinaa, uongo na ria. Au kumhadharisha kufanya wajibu; kama vile kutia hofu ya ufakiri ikiwa mtu atatekeleza haki aliyonayo kwa kutoa mali au madhara ikiwa atafanya jihadi au kusema haki. Yote hayo ni katika mawazo ya shetani. Mwenyezi Mungu ameuelezea usemi wa shetani aliposema:

Na kwa hakika nitawapoteza na nitawatia tamaa... (4:119).

﴿لَأَقْعُدَنَّ لَهُمْ صِرَاطَكَ الْمُسْتَقِيمَ ﴿١٦﴾ ثُمَّ لَآتِيَنَّهُم مِّن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ وَمِنْ خَلْفِهِمْ وَعَنْ أَيْمَانِهِمْ وَعَن شَمَائِلِهِمْ وَلَا تَجِدُ أَكْثَرَهُمْ شَاكِرِينَ ﴾

...Basi nitawavizia (waja wako) katika njia yako iliyonyooka kisha nitawafikia mbele yao na nyuma yao na kuumeni kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta wenye kushukuru. (7:16-17).

Hakika yeye anawaamrisha mambo mabaya na machafu, na kusema juu ya Mwenyezi Mungu msiyoyajua.

Huu ni ubainifu wa athari na natija zinazotokana na kufuata mwito na nyayo za shetani, nazo ni tatu:

Kwanza : ubaya ambao ni kila kitendo ambacho mwisho wake ni ubaya.

Pili : uchafu nao ni aina mbaya ya maasi.

Tatu : kumsingizia Mwenyezi Mungu msiyoyajua kwamba yeye ana washirika na watoto, kuhalalisha haramu, na kuharamisha halali. Vile vile kufanya amali kwa kukisia na kupendelea katika kutoa hukumu ya sharia.Na wanapoambiwa! Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu husema: Bali tutafuata yale tuliyowakuta nayo baba zetu .

Dhamiri ya wanapoambiwa inamrudia kila anayefuata mwingine bila ya hoja wala dalili, na kuacha kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume, kwa sababu ya kauli ya mababa. Makusudio ya aliyoteremsha Mwenyezi Mungu ni kila yale yaliyo na dalili na hoja na yakaingia katika akili zilizo timamu.Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala hawakuongoka?

Yaani wanafuata baba zao hata kama hawafahamu chochote katika mambo ya dini. Makusudio sio kukanusha kufahamu kila kitu, ijapokuwa kwa dhahiri Aya hii inaonyesha hivyo. Bali makusudio ni kukanusha kufahamu, kwa vile maneno yanahusikia na mambo ya kidini. Tutaonyesha katika kifungu kifuatacho kwamba Aya hii inafahamisha ubaya wa kufuata mambo ya upotevu. Ama kufuata ya uongofu, hilo ni katika kufuata mwendo mzuri.

KUFUATA NA MSINGI WA ITIKADI

Kufuata (Taqlid) kulivyo hasa si kuzuri wala si kubaya kwa ujumla, bali kunatofautiana kwa aina zake zifuatazo:

1. Kufuata mkumbo, ambako kwa binadamu na wanyama ni sawa sawa; kama vile kuwika kwa jogoo anapomsikia mwenzake amewika na kulia kwa punda anapomsikia mwenzake. Hali kadhalika kwa upande wa binadamu, mmoja anaweza kupiga kofi kwa ajili ya hotuba, basi wengine wote wanaigiza bila ya kutambua, hata kama hawakufahamu kitu katika yaliyos-emwa. Au mtu anaweza kuangalia upande fulani basi kila anayemuona naye huangalia huko bila ya kukusudia. Huku ndiko kufuata ambako si kuzuri wala kubaya. Kwa sababu kuko nje ya hisia na matakwa.

2. Kufuata mitindo na desturi fulani ya jamii; kama vile namna ya mavazi na mengineyo katika mambo ya jamii ambayo yamefanywa na wakubwa na wadogo, na wajuzi na wasiokuwa wajuzi. Hii ni katika aina ya kufuata ambako kunaweza kuwa kuzuri au kubaya kulingana na mtazamo wa watu.

3. Asiyejua kumfuata mtaalam katika mambo ya kidunia; kama vile utabibu, uhandisi, kilimo, ufundi, n.k. Huku ni kufuata kuzuri bali ni muhimu sana katika ustawi wa jamii. Lau kama si hivyo, basi utaratibu ungeharibika na kazi zingelisimama. Kwani mtu hawezi kujua kila kitu na kupata kila anayoyahitajia peke yake. Mtu alikuwa na ataendelea kuwa na haja ya kusaidiana na kubadilishana huduma.

4. Mujtahid kumfuata mujtahid mwenzake katika mambo ya kidini. Huku kunakataliwa na akili na ni haramu kisharia. Kwa sababu, aliyoyajua ni hukumu ya Mwenyezi Mungu katika haki yake, haijuzu kuyaacha kwa sababu ya kauli ya mtu mwingine. Na ni mjuzi gani anayeacha kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake aliye Masum na kutegemea kauli ya anayekosea?

5. Asiye na elimu kumfuata mujtahid mwadilifu katika masuala tanzu ya kidini, kama vile hukumu za ibada, halali na haramu, twahara, najisi na kusihi muamala, n.k. Kufuata huku ni wajibu kisheria, kwa sababu ni kumfuata aliyechukua ujuzi wake kutokana na hoja na dalili; sawa na mgonjwa kumfuata daktari. Asiyejua anakalifiwa na hukumu, na hakuna njia ya kuzifuata isipokuwa kumrudia mjuzi.

﴿فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴾

...Basi waulizeni wenye kumbukumbu (wajuzi) ikiwa nyinyi hamjui. (16:43).

Hata hivyo, asiyejua akiswali na kufunga kwa kufuata baba zake na mfano wao, sio kwa kufuata mujtahid mwadilifu, na ibada zake zikaafikiana na fat-wa za mujtahid, hizo zitakuwa sahihi na kukubaliwa. Kwa sababu kufuata (taqlid) si sehemu wala sharti la yanayoamrishwa, isipokuwa ni nyezo tu ya kufikilia kwenye amri. Hata inaweza kusihi maamiliano yake kama yakiwa ni sawa sawa. Kuhusu kauli ya anayesema kuwa ibada inahitajia nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kwamba nia hiyo haithibitiki ila kutokana na mujtahid au mwenye kumfuata, kauli hiyo ni madai tu. Kwa sababu, maana ya nia ya kujikurubisha ni kutekeleza yaliyoamriwa kwa nia safi yenye kutakata na kila uchafu wa kidunia. Hapana mwenye kutia shaka kwamba hayo yanaweza kupatikana bila ya mujtahid. Kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

...Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala kuongoka? Inafahamisha kuwa ikiwa baba alikuwa kwenye uongofu na akaTafsir fuatwa na mtoto, itasihi.

6. Kufuata katika misingi (itikadi) ya dini kama kumjua Mwenyezi Mungu na sifa Zake, Utume wa Muhammad isma yake na ufufuo. Wanavyuoni wengi wa Kisunni na Kishia wameikataza aina hii ya kufuata, wakasema kuwa haijuzu (haifai). Kwa sababu kufuata (taqlid) huko ni kufuata bila ya dalili. Na huo ndio ujinga hasa; yaani mwenye kusema juu ya kuweko Mwenyezi Mungu kwa kufuata tu, ni sawa na mwenye kusema Mungu hayuko. Wanavyuoni hawa wamesema: Tumejuzisha kufuata katika matawi ya dini na masuala ya kuamiliana, lakini sio katika misingi ya kiitikadi. Kwa sababu linalotakiwa katika matawi ni amali tu kwa kufuata kauli ya mujtahid, jambo ambalo linawezekana, lakini kwa misingi ya kiitikadi, linalotakikana ni elimu na itikadi. Wahakiki katika Sunni na Shia wamesema kuwa kufuata kukiafikiana na uhakika ulivyo ni sahihi, kwa sababu hilo ndilo linalotakikana; na ijtahidi sio sharti wala fungu la imani na kusadikisha, isipokuwa ni njia tu. Hii ni kweli kabisa, kwa sababu linalozingatiwa katika misingi ya itikadi ni imani sahihi yenye kuafiki. Kwa ajili hii ndio Mtume(s.a.w.w) akakubali Uislamu wa kila mwenye kuuamini na ikatulia nafsi yake kwa ukweli wake na Utume wake bila ya kufanya ijtahidi na kuangalia. Ama Aya zilizokuja kukemea wanaofuata mababa, mfumo wake unafahamisha kuwa makusudio ni kufuata batili na upotevu, sio haki na uongofu. Hakika hii inadhihiri kwa kila mwenye kufikiria kwa undani maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا إِلَىٰ مَا أَنزَلَ اللَّـهُ وَإِلَى الرَّسُولِ قَالُوا حَسْبُنَا مَا وَجَدْنَا عَلَيْهِ آبَاءَنَا﴾

Na wanapoambiwa: Njooni katika hukumu alizoteremsha Mwenyezi Mungu na (anazozisema) Mtume husema: Yanatutosha yale tuliyowakuta nayo baba zetu (5:104).

﴿قَالَ أَوَلَوْ جِئْتُكُم بِأَهْدَىٰ مِمَّا وَجَدتُّمْ عَلَيْهِ آبَاءَكُمْ﴾

Hata kama nawaletea yenye mwongozo bora kuliko mliyowakuta nayo baba zenu. (43:24).

﴿أَوَلَوْ كَانَ آبَاؤُهُمْ لَا يَعْقِلُونَ شَيْئًا وَلَا يَهْتَدُونَ﴾

Je, hata kama baba zao walikuwa hawafahamu chochote wala kuongoka? (2:170).

Ufahamisho wa Aya zote hizi ni kwamba, kama mababa zao wangelikuwa na desturi yenye uongofu ambao umeteremshwa na Mwenyezi Mungu kwa Mtume, basi ingelifaaa kuwafuata mababa hao. Kwa sababu linalotakiwa ni kufuata aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu! Wakiyafuata, basi wamefuata amri na wametii, na hawataulizwa kitu kingine baada ya twaa. Kwa ufupi ni kwamba kila anyefuata kauli ya Mwenyezi Mungu na Mtume, atakuwa amefuata haki yenye kuthibiti kwa dalili, ni sawa awe amejua dalili hiyo au la. Inatosha kujua kwa jumla kwamba kuna dalili sahihi waliyoifuata wahusika wanaofanya ijtihadi. Bali mwenye kufuata haki bila ya kuijua kwamba hiyo ni haki, hataadhibiwa kwa kuacha kujifundisha hata kama hastahiki thawabu na kusifiwa.

Hayo yanafahamika kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

﴿وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا﴾

Na (wazazi wako) wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna elimu nayo, usiwatii (31:15).

Hiyo vile vile inafahamisha kuwa wakikushurutisha kumwamini Mwenyezi Mungu na ukawatii bila ya kuwa na elimu nayo, basi hapana ubaya kwako. Tumefafanua kuhusu kuwafuata (taqlid) Maimamu wane katika kufasiri Aya ya 167 ya sura hii, mwenye kutaka na arudie.