TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 18982
Pakua: 2849


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 16 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 18982 / Pakua: 2849
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA PILI Juzuu 2

Mwandishi:
Swahili

11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA PILI

﴿الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَن يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّـهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

229.Talaka ni mara mbili; kisha ni kushika kwa wema au kuacha kwa ihsani. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlichowapa, isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, itakuwa hapana ubaya kwao kupokea ajikomboleacho mke. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu; basi msiipetuke. Na watakao-ipetuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, hao ndio madhalimu.

﴿فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا أَن يَتَرَاجَعَا إِن ظَنَّا أَن يُقِيمَا حُدُودَ اللَّـهِ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ يُبَيِّنُهَا لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ﴾

230.Na kama amempa talaka ( ya tatu) basi si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine. Na akimwacha, basi hapo si vibaya kwao kurejeana waki-ona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wajuao.

TALAKA NI MARA MBILI

Aya 229 - 230

MAANA

Talaka ni mara mbili.

Waarabu katika zama za Ujahiliya (kabla ya Uislamu) walikuwa na talaka, eda na kurejeana katikati ya eda. Lakini talaka haikuwa na idadi maalum. Mtu aliweza kumwacha mkewe mara mia na kumrudia. Kwa hivyo mwanamke anakuwa ni kitu cha kuchezewa mikononi mwa mwanamume. Kuna riwaya inayoeleza kuwa mtu mmoja alimwambia mkewe: "Sitakukur-ubia milele, na pamoja na hivyo utabaki kwangu tu, hutaweza kuolewa na mwingine." Mke akauliza: "Itakuwaje hivyo?" Mume akajibu: "Nitakuacha mpaka ukikaribia muda wa kwisha eda nikurudie, halafu nikuache tena, n.k." Mwanamke akamshtakia Mtume(s.a.w.w) . Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii:"Talaka ni mara mbili" yaani talaka ambayo mnaruhusiwa kurejea ni talaka ya kwanza na ya pili tu! Ama ya tatu si halali kurejea, mpaka mke aolewe na mume mwingine; kama alivyosema Mwenyezi Mungu;"Na kama amempa talaka si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine."

Kisha ni kushika kwa wema au kuacha kwa ihsani.

Mume akimwacha mkewe mara ya pili ana hiyari kati ya mambo mawili akiwa katika eda. Jambo la kwanza ni kumrejea kwa kukusudia kupatana na kutangamana. Huku ndiko kumweka kwa wema. Jambo la pili, ni kumwacha mpaka ishe eda yake, amtekelezee haki yake asimtaje kwa ubaya baada ya kutengana wala asimkatishe anayetaka kumwoa baada yake. Huko ndiko kumwacha kwa ihisani. Unaweza kuuliza, wafasiri wengi wamefasiri kumwacha kwa ihisani ni talaka ya tatu na wakatoa ushahidi wa Hadith ya Mtume(s.a.w.w) . Sasa imekuwaje wewe kuipinga kauli yao na kufasiri kuacha, kuwa ni kupuuza kumrejea katika muda wa eda?

Jibu : Neno kumwacha, kwa dhati yake linawezekana kuwa ni talaka ya tatu na linawezekana kuwa ni kumnyamazia mtalaka na kuwacha kumrejea. Lakini kwa kuchunga mfumo ulivyo, maana ya neno inarudia maana ya pili; yaani kuacha kurejea, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu "Kama amempa talaka basi mwanamke huyo si halali kwake baada ya hapo." Inatokana na kumweka; maana yake yanakuwa ni akimwacha baada ya kumweka na akamrejea katikati ya talaka ya pili itakuwa talaka ni ya tatu wala si halali kwa mwenye kuacha kumwoa mpaka aolewe na mume mwingine. Kwa hivyo haiwezekani kuwa imetokana na kumweka kwa maana ya talaka ya tatu, kwa sababu maana itakuwa alimwacha mara ya nne baada ya kumwacha mara ya tatu. Na ilivyo ni kwamba hakuna talaka ya nne katika Uislamu. Ama Hadith iliyofasiri kumweka kwa maana ya talaka ya tatu si thabiti.

TALAKA TATU

Madhehebu manne ya Kisunni yameafikiana kuwa atakaye mwambia mkewe: Nimekuacha talaka tatu au akisema: Nimekuacha, nimekuacha, nimekuacha, basi itakuwa ni talaka tatu na itakuwa haramu mpaka aolewe na mume mwingine. Shia wamesema itakuwa ni talaka moja tu, na ni halali kumrejea, maadamu yuko katika eda. Katika tafsiri ya Al Manar imepokewa kutoka kwa Ahmad bin Hambal katika Musnad yake, na Muslim katika Sahih yake kwamba talaka tatu zilikuwa moja katika zama za Mtume(s.a.w.w) , za Abu Bakr na baadhi ya miaka ya ukhalifa wa Umar, lakini Umar ikamdhihirikia fikra nyingine akasema; "Hakika watu wamefanya haraka katika jambo lililokuwa na upole kwao, lau tungelipitisha."Basi akapitisha (kuwa kusema talaka tatu ni tatu).

Kisha amenakili mwenye tafsiri Al Manar kutoka kwa Al Qayyim kwamba masahaba wote walikuwa wakikubali kwamba talaka tatu hazikutokea kwa pamoja tangu mwanzo wa Uislamu mpaka miaka mitatu ya ukhalifa wa Umar. Vile vile walifutu hivyo jamaa katika masahaba, Tabiina (waliokuwapo baada ya maswahaba) na waliokuja baada ya hao Tabiina (Tabii-Tabiina), na kwamba fatwa juu ya hilo inaendelea kila wakati hata baadhi ya wafuasi wa Maimamu wanne walifutu hivyo.

Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika mlichowapa.

Katika mlichowapa hapa ina maana kiwe kingi au kichache; yaani ikiwa mume ndiye asiyemtaka mke na akapendelea kumpa talaka, basi si haki kwake kuchukua vile alivyompa zawadi mke au mahari. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا﴾

"Na kama mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke na hali mmoja wao mmempa rundo mali, basi msichukue chochote katika hiyo. Je, mnachukua kwa dhuluma na kwa dhambi iliyo wazi" (4:20)

Hiyo ni ikiwa mume ndiye asiyemtaka mke. Ama ikiwa mke ndiye asiyemtaka mume, basi hapana kizuwizi cha mke kumpa mume kile kinachomridhia ili amwache, ni sawa chenye kutolewa kiwe ni kiasi cha mahari au kichache au zaidi ya mahari. Talaka hii inaitwa Khul'u (kujivua); na mume katika talaka hii hana haki ya kumrejea katika eda maadamu anaendelea kulipwa. Isipokuwa kama huyo mke atabadilisha katikati ya eda.

Kuhusu talaka hii ya khul'u Mwenyezi Mungu anasema:

Isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkiogopa kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu, itakuwa hapana ubaya kwao kupokea ajikomboleacho mke.

Hii ni kuelezea uwezekano wa kuchukua kitu kutoka kwa mke. Mipaka ya Mwenyezi Mungu ni haki na wajibu wa kila mmoja kwa mwenzake (mke na mume).

Maana yake: Enyi waume! Msichukue kitu kutoka kwa watalaka wenu kwa sababu yoyote ile, isipokuwa sababu moja tu, ambayo ni ikiwa mke ndiye anayemchukia mume, wala hawezi kuishi naye, kiasi ambacho hali itapelekea kumwasi Mwenyezi Mungu katika kutia dosari haki za unyumba, na huenda mume naye akaogopa kumkabili mke kwa uovu. Katika hali hii, itafaa kwa mke kudai talaka kutoka kwa mume na kumlipa ridhaa; kama vile ambavyo inajuzu kwa mume kuichukua ridhaa hiyo.

Imekuja Hadith kwamba Thabit bin Qays alikuwa amemuoa bint wa Abdulla bin Ubay. Naye alikuwa akimpenda, lakini mke hampendi mume. Na alikuwa amempatia shamba. Mke akaja kwa Mtume(s.a.w.w) akasema: "Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Mimi na Thabit kichwa changu hakipatani na chake." Thabit akasaili: "Na lile shamba?" Mtume akamwambia bint Abdulla: "Unasemaje?" Akasema: "Ndio, tena na ziada nitampa." Mtume akasema: "Hapana, shamba tu," Basi wakafanyiana khul'u. Linakuja swali katika aya hii: Kwa nini ikaja dhamiri ya wawili katika "Isipokuwa wakiogopa (wote wawili) ya kwamba hawataweza kusimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu." Kisha ikaja dhamiri ya wengi kwa kusema: "Na kama mkiogopa". Kwa nini dhamiri zisiafikiane katika jumla mbili?

Jibu : Dhamiri ya wote wawili ni ya mke na mume na dhamiri ya 'mkiogopa' ni ya mahakimu na wasuluhishi; yaani wakiogopa, mahakimu na wasuluhishi kuacha kusimamishwa mipaka ya Mwenyezi Mungu. Makusudio hasa ni kuondoa hofu ya kutoa na kuchukua kwa wote. Swali la pili: Kwa nini ikaja dhamiri ya wawili katika: Si dhambi juu yao (mume na mke), na tunajua kuwa anayepokea ni mume tu. Jibu: Hapa inaonyesha kuwa si vibaya kutoa na kuchukua; kwa kufahamu kuwa kujuzu kutoa kunalazimisha kujuzu kupokea. Swali la tatu: Ikiwa mke na mume wameridhiana kufanya khul'u, mke akatoa mali ili aachwe; lakini uhusiano wao ni mzuri, je, itaswihi khul'u na itafaa mume achukue fidia? Madhehebu zote nne zimesema khul'u itafaa na itafungamana na athari zote za khul'u.

Shia Imamia wamesema haiswihi hiyo khul'u wala mtaliki hawezi kumiliki fidia, lakini talaka itaswihi na itakuwa ni talaka rejea kwa sharti zake. Wametoa dalili ya kuharibika khul'u na kutojuzu kuchukua fidia kwamba Aya imeshartisha kujuzu hilo kwa kuogopa kuingia katika maasi, kama ndoa ikiendelea. Ama Aya inayosema:

﴿وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً فَإِن طِبْنَ لَكُمْ عَن شَيْءٍ مِّنْهُ نَفْسًا فَكُلُوهُ هَنِيئًا مَّرِيئًا﴾

"Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni zawadi, kama wakiwatunikia kwa ridhia ya nafsi zao, katika hayo (mahari) basi kuleni kwa raha." (4:4)

Makusudio ya Aya hiyo ni kwamba anachotoa mke hapo ni zawadi tu, sio badali ya talaka. Hivyo Aya iko mbali na khul'u.

Swali la nne: Kama mume akifanya makusudi ubaya ili apate mali kutoka kwa mke, na mke naye akatoa mali na ikatolewa talaka kwa misingi hii; je, khul'u itakuwa halali? Na je, ni halali kuchukua mali? Abu Hanifa anasema: "Khul'u ni sahihi, mali ni lazima itolewe na mume ana dhambi." Shafi na Malik wamesema: "Khul'u ni batili na mali irudishwe kwa mke, kwa sababu ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ﴾

"... Wala msiwataabishe ili mpate kuwanyang'anya baadhi ya vile mlivyowapa..." (4:19)

Hayo yamo katika kitabu Al- Mughni, cha Ibn Quddama Juz 7, Uk 55 chapa ya 7. Shia Imamia wamesema: "Haiswihi khul'u, ni haramu kuchukua mali, lakini itakuwa ni talaka rejea kwa kukamilika sharti zake." Ama sisi tuko katika fikra ya kuwa talaka hiyo ni upuzi tu, sio khul'u wala talaka rejea. Kwa sababu kinachojengeka kwa uharibifu ndio kimeharibika chote. Hayo tumeyafafanua zaidi katika kitabu Fiqhul Imam Jaffar Sadiq Juz 6 mlango wa khul'u kifungu cha Hukumu za khul'u. Na kama amempa talaka (ya tatu) basi si halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwingine. Na akimwacha (mume wa pili), basi hapo hapana ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watasimamisha mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Maana ni kuwa mwenye kumwacha mkewe mara tatu, basi si halali kwake kumwoa tena mpaka aolewe na mume mwingine kwa ndoa sahihi tena amwingilie. Imekuja Hadith inayosema: "Si halali kwa mume wa kwanza mpaka wa pili amwonje (amwingilie)." Huyu mume wa pili ndiye anayeitwa muhallil (mhalalishaji); Ni lazima awe ni baleghe, na ndoa iwe ya daima sio ya Mut'a. Zikitimia sharti; kisha mume wa pili akatalikiana naye kwa mauti au talaka na ikaisha eda, basi itafaa kwa mume wa kwanza kufunga ndoa naye tena.

﴿وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَلَا تُمْسِكُوهُنَّ ضِرَارًا لِّتَعْتَدُوا وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ وَلَا تَتَّخِذُوا آيَاتِ اللَّـهِ هُزُوًا وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَمَا أَنزَلَ عَلَيْكُم مِّنَ الْكِتَابِ وَالْحِكْمَةِ يَعِظُكُم بِهِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴾

231.Na mtakapowapa wanawake talaka, wakafikia muda wao, basi washikeni kwa wema au waacheni kwa wema. Wala msiwaweke kwa kudhuriana mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu mwenyewe. Wala msizifanyie mzaha Aya za Mwenyezi Mungu. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na Kitabu alichowateremshia na hekima, kwa kuwaonya. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

﴿وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ ذَٰلِكَ يُوعَظُ بِهِ مَن كَانَ مِنكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ذَٰلِكُمْ أَزْكَىٰ لَكُمْ وَأَطْهَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴾

232.Na mtakapowapa wanawake talaka na wakafikia muda wao, msiwazuie kuolewa na waume zao, ikiwa wamepatana kwa wema. Hayo anaonywa nayo yule, miongoni mwenu, anaye-mwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.

MNAPOWAPATALAKAWANAWAKE

Aya 231 - 232

MAANA

Na mtakapowapa wanawake talaka, wakafikia muda wao, basi washikeni kwa wema au waacheni kwa wema.

Msemo huu unaelekezwa kwa waumini wote au kwa watu wote; ni kama vile Mwenyezi Mungu ametaka kusema: Enyi waumini! Atakapompa talaka mmoja wenu mkewe. Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu kwamba mwenye kupewa talaka ni lazima akae eda, kwamba anaweza kurudiwa na mumewe zikikamilika sharti, kwamba ni haramu baada ya talaka ya tatu mpaka aolewe na mume mwingine, na kwamba si halali kuchukua kitu kwa mke kwa ajili ya talaka, isipokuwa ikiwa mke ndiye asiyemtaka mume, baada ya kuyabainisha yote hayo, anatubainishia vile tunavyotakiwa kuchunga haki ya anaekaa eda.

Kuchunga haki kutathibitika kwa kuazimia mwenye kuacha moja kati ya mawili: Kumrejea mtalaka wake wakati inapokaribia kumalizika eda, kwa kukusudia usuluhishi na utangamano mzuri. Na huku ndiko kurejea kwa wema. Au kumwacha bila ya kumtaaradhi kwa ubaya pamoja na kumtekelezea kila analostahiki. Na huku ndiko kumwacha kwa wema. Kwa hivyo inatubainikia kuwa makusudio ya Aya iliyotangulia siyo makusudio ya Aya hii tuliyonayo. Aya ile iliyotangulia inabainisha kuwa kurejeana ni talaka ya kwanza na ya pili na siyo ya tatu. Na hii inabainisha vile tunavyotakiwa kuwafanyia waliopewa talaka; kama ambavyo makusudio ya kufikilia muda wao ni kukurubia sio kufika hasa.

Wala msiwaweke kwa kudhuriana mkafanya uadui.

Yaani msiwarudie kwa kukusudia kuwaudhi au kuwafanyia ubaya; muwareTafsir jee tu kwa makusudio ya kutekeleza haki za unyumba na kusaidiana yale yaliyo na maslahi kwa wote.

Unaweza kuuliza kwa nini imesemwa kudhuriana, ambapo makusudio ni kuepusha madhara ya mume kwa mke?

Jibu : Kumdhuru mke kunasababisha kudhurika kwa mume pia, kwa sababu ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu juu yake, shutuma za watu kwake, na mke kulipiza kisasi. Hapo ndio unyumba unageuka kuwa Jahannam kwa mume na mke na huenda moto ukaenea kwa jamaa na ndugu. Ndio maana Mwenyezi Mungu anasema:

Na atakayefanya hivyo, amejidhulumu mwenyewe. Yaani si kumdhulumu mke peke yake.

Wala msizifanyie mzaha Aya za Mwenyezi Mungu.

Hiki ni kiaga na kemeo kwa yule mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu katika haki za unyumba. Njia ya kuzifanyia mzaha Aya za Mwenyezi Mungu, ambaye limetu-kuka neno lake, ni kwamba kila mwenye kudai kumwamini Mwenyezi Mungu na hakufuata dini kwa sharia zake, halafu akapuuza hukumu zake, halali yake na haramu yake, basi atakuwa amefanya mzaha, atake asitake. Sawa na anayem-uahidi mtu kitu hali akiwa na niya ya kutotekeleza. Baadhi ya wahenga wamesema: "Mwenye kutubu dhambi na huku anaendelea nayo ni kama mwenye kumcheza shere Muumba wake."(Mungu apishie mbali!)

Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu.

Miongoni mwa hizo ni kuwa Mwenyezi Mungu ametuumbia wanawake ili tupate utulivu kwao na tusaidiane nao katika yale yenye utengeneo wa familia. Ikiwa tunamwamini Mwenyezi Mungu na tunafuata amri zake kweli, basi ni juu yetu kufanya lile litakaloleta lengo hili na kujie-pusha na kila linaloleta uovu katika familia na kuchafua usafi wa maisha ya ndoa.

Na mtapowapa talaka wanawake na wakafikia muda wao, msiwazuie kuolewa na waume zao.

Makusudio ya kufikia muda katika Aya iliyotangulia ni kukaribia kwisha eda na makusudio yake hapa ni kwisha kabisa hiyo eda. Katika Aya hii kuna mielekezo miwili ya misemo (mnapowapa talaka, na msiwazuie) ambayo wafasiri wamehitilafiana; kwamba, je yote inaelekezwa upande mmoja au pande tofauti? Kuna wenye kusema kuwa unaelekezwa kwa upande mmoja tu wa waume; na maana yake ni: Enyi waume, mnapowapa talaka wanawake na eda yao ikaisha, basi msiwazuwie kuolewa na waume wengine wanaowaridhia. Kwa sababu mwanamume alikuwa akimhukumu mtalaka wake na kumzuia, kuolewa na mume mwingine baada yake. Wengine wanasema: Msemo wa kwanza Mtakapowapa talaka, unaelekezwa kwa waume, na wapili msiwazuie, unaelekezwa kwa mawalii; kwa maana ya: Enyi waume, mnapowapa talaka wanawake, basi nyinyi mawalii msiwazuwie watoto wenu kurudiana na waume zao wa kwanza, ikiwa eda imekwisha. Wanaosema hivi wametoa ushahidi wa Hadith ya Mu'ukil bin Yasir( [12] ).

Inaeleweka kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu: "Mtakapowapa talaka wanawake na wakafikia muda wao msiwazuwie" ni jumla ya pamoja iliyo na sharti, na jawabu lake ni msiwazuie. Ikiwa sharti ya mwenye kumwambia ni mwingine na jawabu liwe kwa mwingine na maana yawe ni: Enyi waume mtakapowapa talaka wanawake basi nyinyi mawalii msiwazuie, hapa kutakuwa na mkorogano ambao haupaswi kuwapo katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Usahihi hasa ni misemo miwili (sharti na jawabu lake) inaelekezwa kumoja tu kwa waumini wote;

sio waume peke yao wala mawalii tu, wala pia sio kwa wote, bali ni kwa waumini. Hali hii inakuja mara nyingi katika maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.), na maana yanakuwa: Enyi mlioamini mmoja wenu akimpa talaka mkewe, eda ikaisha na akataka kuolewa na mume mwingine au kurudiwa na mumewe wa kwanza, basi msimzuie kama wakipatana kwa wema; yaani wakiazimia kuoana. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: Ikiwa wamepatana kwa wema inafahamisha kuwa mke anaweza kujioza yule anayemridhia, bila ya kumngoja walii.

Unaweza kusema: hakika Aya imeuondoa uwalii (usimamizi) kwa wanawake walioachwa tu, na wala haikuutaaradhi usimamizi kwa wengineo. Kwa hivyo kuuondoa usimamizi kwa wanawali kunahitajia dalili. Jibu: Kuthibitisha usimamizi ndiko kunakohitajia dalili; ama kuondoa, dalili yake ni ya asili kwamba kila aliyebaleghe mwenye akili mume au mke ni huru katika mambo yake wala hatawaliwi na yeyote, kwa vyovyote atakavyokuwa isipokuwa tu kama atakiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

Hayo anawaonywa nayo yule, miongoni mwenu, anayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Hayo ni ishara ya hayo aliyoyataja Mwenyezi Mungu katika hukumu zake. Anaonywa nayo, yaani wanaonyeka nayo wenye imani sahihi. Ama wengineo katika wenye imani mbovu, masikioni mwao mna vizuwizi, hawasikii mawaidha ya Mwenyezi Mungu na hukumu Zake wala uongozi Wake. Aya hii ni dalili ya wazi kwamba hakuna imani bila ya ucha Mungu na imani sahihi haiepukani na mawaidha, na asiye waidhika wala kunufaika na amri za Mwenyezi Mungu hana hata chembe ya imani.

Hayo ni mazuri mno kwenu na safi kabisa.

Hayo ni ishara ya mawaidha na kutumia hukumu ya Mwenye-zi Mungu katika maisha ya ndoa kwa ujumla na hasa katika waliopewa talaka. Hakuna mwenye shaka kwamba ndoa yenye lengo la utu na kusaidiana katika heri, inaleta ongezeko na usafi katika riziki, usafi wa tabia, heshima na ufanisi kwa watoto. Ama makusudio yakiwa mabaya, basi mwisho wake ni ukafiri, uharibifu, balaa na mashaka katika maisha ya wazazi na watoto.

Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.

Makusudio sio kutupa habari kuwa Yeye ni mjuzi au mjuzi zaidi, hapana. Hilo liko wazi halihiitaji mafunzo wala ufafanuzi. Makusudio hasa ni kutilia mkazo na kuhimiza kutekeleza hukumu Zake Mwenyezi Mungu; hata kama haikutubainikia njia ya manufaa yapatikanayo katika hukumu hiyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ambaye imetukuka hekima yake, haamrishi isipokuwa lenye heri na maslahi na wala si lazima tuijue heri hiyo kwa ufafanuzi; bali inatosha tu kujua kuwa Mwenye kuamrisha na Mwenye kukataza, ni Mjuzi Mwenye hekima, halijifichi lolote Kwake liwe ardhini au mbinguni. Kwa ujumla ni kuwa kuna tofauti kati ya mumin na asiyekuwa mumin. Mumin anaabudu kulingana na kauli ya Mwenyezi Mungu na anafanya amali katika hali ya kuyakinisha kupatikana manufaa, hata kama atashindwa kuyafahamu kwa ufafanuzi.

Ama asiyekuwa mumin hafanyi kitu mpaka ajue au adhani kuwa kuna manufaa anayoyajua yeye mwenyewe kwa akili yake au aongozwe na kiumbe kama yeye, ambapo mara nyingi anaruka patupu na kubainikiwa na kinyume, lakini mumin anakuwa katika amani ya Mwenyezi Mungu na hifadhi Yake.