TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 20%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17913 / Pakua: 3852
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

1

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿تِلْكَ الرُّسُلُ فَضَّلْنَا بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ مِّنْهُم مَّن كَلَّمَ اللَّـهُ وَرَفَعَ بَعْضَهُمْ دَرَجَاتٍ وَآتَيْنَا عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ الْبَيِّنَاتِ وَأَيَّدْنَاهُ بِرُوحِ الْقُدُسِ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلَ الَّذِينَ مِن بَعْدِهِم مِّن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَلَـٰكِنِ اخْتَلَفُوا فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ وَمِنْهُم مَّن كَفَرَ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَفْعَلُ مَا يُرِيدُ ﴾

253. Mitume hao tumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine. Miongoni mwao yuko ambaye Mwenyezi Mungu alisema naye; na wengine akawapandisha vyeo, na tukampa Isa mwana wa Maryam dalili zilizo wazi na tukamtia nguvu kwa roho takatifu. Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana wale waliokuwa baada yao, baada ya kuwafikia dalili zilizo wazi; lakini walihitilafiana kuna katika wao walioamini na wengine katika wao waliokufuru, lakini Mwenyezi Mungu hufanya anayoyataka.

KUWAFADHILISHA MITUME

Aya ya 253

MAANA

Mitume hao tumewafadhilisha baadhi yao zaidi kuliko wengine.

Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume Wake Muhammad(s.a.w.w) katika mwisho wa Aya iliyotangulia;"Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume," Halafu akafuatisha moja kwa moja na kauli Yake hii: "Mitume hao ..." Kwa hivyo basi, makusudio yanakuwa ni mitume wote ambao miongoni mwao ni Muhammad, sio kundi maalum, kama walivyosema wafasiri wengi.

Mitume wote ni sawa katika asili ya utume kuchaguliwa kwao na katika kufikisha ujumbe, wa Mwenyezi Mungu na kuongoza viumbe Vyake, lakini wanatofautiana katika mambo fulani. Yaani baadhi ya mitume wamekuwa mashuhuri kwa baadhi ya mambo fulani waliyohusika nayo, ambayo wengine hawakuwa nayo, ambayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu nayo katika Kitabu chake. Kwa mfano Ibrahim alikuwa mashuhuri kwa kuitwa rafiki wa Mwenyezi Mungu (Khalilullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَاتَّخَذَ اللَّـهُ إِبْرَاهِيمَ خَلِيلًا﴾

"Na Mwenyezi Mungu amemfanya Ibrahim kuwa ni rafiki" (4:125)

Musa naye akawa mashuhuri kwa jina la aliyesema na Mwenyezi Mungu (Kalimullah) kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا﴾

"... Na Mwenyezi Mungu akasema na Musa maneno" (4:164)

Isa naye akawa mashuhuri kwa, roho wa Mwenyezi Mungu (Ruhullah); kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

﴿إِنَّمَا الْمَسِيحُ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ رَسُولُ اللَّـهِ وَكَلِمَتُهُ أَلْقَاهَا إِلَىٰ مَرْيَمَ وَرُوحٌ مِّنْهُ﴾

"Hakika Masihi Isa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake alilompelekea Maryam. Na ni roho iliyotoka kwake ..." (4:171)

Muhammad naye akawa mashuhuri kwa, mwisho wa Mitume (khatamun nabiyyina) kwa kauli Yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴾

"Na Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Mitume ..." (33: 40)

Mwenyezi Mungu ametaja baadhi ya Mitume waliofadhilishwa au baadhi ya yanayohusika nao, kwa kauli Yake:

Miongoni mwao yuko ambaye Mwenyezi Mungu alisema naye.

Huyu ni Musa bin Imran kama walivyoafikiana wafasiri.

Na wengine akawapandisha vyeo.

Mwenye Tafsiri ya Al Manar amesema: "Wafasiri wamesema huyo ni Mtume wetu ..."Na amesema Razi: "Umekubaliana umma wote kwamba Muhammad ni bora ya Mitume," Ametoa dalili 19 juu ya hilo kwa dalili, Miongoni mwa dalili hizo ni kwamba Ali bin Abu Twalib siku moja alitokeza kwa mbali, Mtume akasema: "Huyu ni bwana wa Waarabu."Aisha akasema: "Siye wewe bwana wa Waarabu? "Mtume akasema: "Mimi ni bwana wa walimwengu na yeye ni bwana wa Waarabu" Dalili bora zaidi juu ya ubora wa Mtume kwa Mitume wote na watu wema wote ni sharia yake ilivyo na ukunjufu katika utukufu wake na utu wake.( [1] )

Na tukampa Isa mwana wa Maryam dalili zilizo wazi na tukamtia nguvu kwa roho takatifu.

Dalili zilizowazi hapa ni dalili ambazo zinadhihirisha haki; kama kufufua wafu, kuponyesha wagonjwa, kuumba ndege, n.k. Makusudio ya roho takatifu ni roho njema yenye kutakaswa. Imekwishapita tafsiri ya roho katika Aya ya 87 ya Sura hii.

Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana wale waliokuwa baada yao .

Yaani baada ya Mitume kuwajia na hoja zilizowazi na kuzifafanua haki kwa dalili, basi watu wao walihitalifiana baada yao.

Kuna katika wao walioamini na wengine katika wao waliokufuru.

Unaweza kuuliza: Kauli Yake Mwenyezi Mungu:"Na kama Mwenyezi Mungu angelitaka wasingelipigana. Si inafahamisha kwamba binadamu ni mwenye kuendeshwa hana hiyari na kwamba kukaririka jumla hii ni kutilia mkazo kunasibika kupigana na matakwa ya Mwenyezi Mungu (s.w.t)?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t.) amempa uwezo mja na akambainishia heri na shari na kumkataza hili na kumwamrisha lile. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا﴾

"Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msiachane..." (3:103)

Mtu akifuata njia ya mshikamano na kupendana, atakuwa yeye mwenyewe ndiye anayenasibika na huko kufuata, kwa sababu kumetokana na yeye na kwa hiyari yake iliyomfanya aone bora njia hiyo kuliko njia ya kutoelewana; wakati huo huo huko kufuata njia hiyo ya mshikamano kunafaa kunasibishwe kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye aliyemwezesha kuifuata na ndiye aliyemwamrisha kuifuata.

Ama akifuata njia ya chuki na uhasama, basi njia hiyo itanasibika na mtu pekee wala hainasibiki na Mwenyezi Mungu, kwa sababu mtu ameifuata kwa radhi yake na akaiona ni bora kuliko njia ya maafikiano; wala haifai kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu amemkataza. Unaweza kuuliza tena: Kwa nini Mwenyezi Mungu amemwezesha mtu kuifanya shari ambapo ilikuwa inatakikana ampe hima ya kuaacha na kufanya heri tu? Jibu: Lau Mwenyezi Mungu angelifanya hivi, binadamu asingebakiwa na fadhila yoyote wala vitendo visingekuwa na sifa ya heri na shari au vizuri na vibaya. Kwa sababu sifa hizi zinafungamana na matakwa ya mtu na hiyari yake. Bali lau Mwenyezi Mungu angelimfanya mtu kufanya kitu fulani tu, kusingelikuwako na tofauti ya mtu na mawe au tofauti na unyoya ulio katika mavumo ya pepo. Kwa ajili hii na kwa ajili ya kudumu mtu na utu wake, hakutaka Mwenyezi Mungu kuwalazimisha watu kwenye kitu fulani

"Na kama angelitaka wasingelipigana"

Kwa ufupi kupigana ambako kumepatikana kati ya watu sio kama kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanayoitwa Kun fa yakun. Isipokuwa kumekhalifu matakwa ya Mwenyezi Mungu ya sharia yake, ambayo ni ubainifu na uongozi; na hekima yake imetaka kumpa mtu uwezo wa kutosha wa kufanya heri na shari, ili ajichagulie yeye mwenyewe uongozi na heri na awe ni mtu anayetofautiana na mawe na wanyama.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ يَوْمٌ لَّا بَيْعٌ فِيهِ وَلَا خُلَّةٌ وَلَا شَفَاعَةٌ وَالْكَافِرُونَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴾

254.Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa. Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi. Na makafiri ndio madhalimu.

KUTOA

Aya ya 254

MAANA

Mwenyezi Mungu amehimiza kutoa mali kwa mifumo mbali mbali. Yameshatangulia maelezo katika tafsiri ya Aya 245; na unakuja tena mfano wake katika Aya hii:

Enyi mlioamini! Toeni katika vile tulivyowapa.

Mwenyezi Mungu anahimiza kutoa pamoja na kuashiria kwamba mali iliyo na watu ni Tafsir Al-Kashif: Juzuu ya Tatu 2. Sura Al-Baqarah 255. Mwenyezi Mungu hakuna mola ila Yeye Aliye hai msimamizi wa kila kitu. Hakumshiki kusinzia wala kulala. Ni Vyake vilivyomo ardhini na vilivyomo mbinguni. Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo. Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi. Wala hakumshindi kuzilinda. Na Yeye ndiye Mtukufu aliye Mkuu.

mali Yake aliyoitoa Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t); na kwamba kesho fursa itakosekana, kwa hivyo ni juu ya mumin mwenye akili kuchukua fursa kabla ya kupitwa na wakati.

Kabla haijafika siku ambayo hapatakuwa na biashara wala urafiki wala uombezi.

Makusudio ya biashara hapa ni kulipa fidia ili kujikomboa na moto kwa mali; urafiki ni urafiki wa kusameheana na uombezi na kuombewa na mtu mwingine kuepukana na moto. Maana yake ni kwamba kesho mtu atakuja peke yake hana chochote isipokuwa amali njema Aya hii ina maana sawa na Aya ya 48 ya Sura hii. Tumeuzungumzia uombezi katika Aya hiyo.

Na makafiri ndio madhalimu.

Wamejidhulumu wenyewe kwa kuacha amali njema ambayo inawaokoa na adhabu. Kwa ujumla ni kuwa neno dhulma na ukafiri yanakuja katika matumizi ya maana mamoja. Mara nyingine hutumiwa ukafiri katika dhulma, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t):

﴿إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ﴾

"... Hakika ushirikina ni dhulma kubwa" (31:13)

Na mara nyingine hutumiwa dhulma katika ukafiri, kama alivyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

﴿وَلَـٰكِنَّ الظَّالِمِينَ بِآيَاتِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ﴾

"...Lakini madhalimu wanakanusha ishara za Mwenyezi Mungu..." (6:33)

﴿اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ ﴾

255.Mwenyezi Mungu hakuna mola ila Yeye Aliye hai msimamizi wa kila kitu, Hakumshiki kusinzia wala kulala. Ni Vyake vilivyomo ardhini na vilivyomo mbinguni. Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake. Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo. Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi, Wala hakumshindi kuzilinda. Na Yeye ndiye Mtukufu aliye Mkuu

AYA YA KURSIY

Aya ya 255

MAANA

Mwenyezi Mungu hakuna mola ila yeye aliye hai, Msimamizi wa kila kitu.

Mwanafalsafa mashuhuri wa elimu inayohusika na mambo ya Mungu, aitwaye Mulla Sadra anasema: Neno Allah (Mwenyezi Mungu) linafahamisha kupwekeka dhati Yake Mwenyezi Mungu na sifa Zake. Kufahamisha juu ya kupwekeka katika dhati, ni kwamba jina hili tukufu haliitiwi mtu mwingine kiuhakika wala majazi. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴾

"... Basi mwabudu Yeye tu na udumu katika ibada Yake. Je, unamjua (mwingine) mwenye jina lake?" (19:65)

Ama kufahamisha kupwekeka Kwake katika sifa, ni kwamba jina hili linafahamisha juu ya dhati yenye kukusanya kila sifa za ukamilifu na utukufu, kinyume cha majina mengine kama; Mjuzi, Mweza na Muumbaji, ambayo umoja wake haufahamishi isipokuwa umoja wa maana katika elimu, au uweza au utendaji. Unaweza kuuliza: Hakika sifa za ukamilifu na utukufu ni nyingi na zenye kubadilika kulingana na kueleweka kwake; vipi ifae kusema zimepwekeka na tunaziona zinahisabika na kubadilika?

Jibu : Ukisema huyu ni mtu mjuzi yataeleweka mambo mawili - Sifa na Mwenye kusifiwa; na vyote ni vitu tofauti. Mtu sio ujuzi na ujuzi sio mtu. Hayo ni kwa upande wa kiumbe. Ama kwa upande wa Muumbaji hakuna jingine isipokuwa kuweko kiutukufu; na huko kuweko ndiko ujuzi ndiko uwezo, na ndiko hekima, n.k. Hakuna sifa na mwenye kusifiwa vyote ni vimoja tu; na huku hakukufanana na kitu kingine.

Hakuna mola ila Yeye.

Inasemekana maana yake ni hakuna anayepasa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Yeye. Lakini kueleweka kwake ni hakuna yoyote mwenye kukusanya sifa za uungu isipokuwa Yeye. Vyovyote iwavyo, maana zote mbili ni zenye kulazimiana.

Aliye hai Msimamizi wa kila jambo.

Ukiunasibisha uhai kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, maana yake yanakuwa ni kukua, kuhisi na utambuzi. Lakini ukiunasibisha kwa Mwenyezi Mungu unakuwa ni elimu na uweza. Makusudio ya kusimamia kila kitu ni kukisimamia katika mambo yake na kukipangilia vizuri. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴾

"Akasema: Mola wetu ni Yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akaongoza." (20:50)

Na amesema tena:

﴿وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴾

"....Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)." (25:2)

Mulla Sadra anasema: Kauli ya Aliye Hai inafahamisha kwamba Yeye ni Mjuzi na Muweza. Na kauli ya Msimamizi wa kila kitu inafahamisha kuwa Yeye ni Mwenye kujisimamia Mwenyewe na kumsimamia mwingine. Kwa hiyo sifa mbili hizi ni zenye kuafikiana katika maana na ni zenye kuingiliana." Anakusudia kuwa usimamizi hauepukani na uhai; kama vile ambavyo uhai kwa maana ya uwezo na elimu hauepukani na usimamizi.

MWENYEZI MUNGU NA DESTURI YA MAUMBILE

Unaweza kuuliza: Je maana ya kusimamia Mungu juu ya mipango ya vitu vyote, ni kwamba mambo yote ya dhahiri ya kimaumbile mpaka mafungu yake yanasimamiwa na Mwenyezi Mungu moja kwa moja Yeye Mwenyewe bila ya kuweko kati sababu yoyote ya kimaada; kama inavyodhihiri katika Aya isemayo:

﴿ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾ ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ﴾

"Kisha tukamfanya tone la manii, katika makao madhubuti. Kisha tukaliumba tone hilo kuwa pande la damu, na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, kisha tukaliumba pande la nyama kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama, kisha tukalifanya umbo jengine. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji" (23:13-14)

Kwa sababu yenye kuja haraka fahamuni katika Aya hii, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameingilia Yeye Mwenyewe moja kwa moja kwenye makuzi mbali mbali ya tone la manii; na tunajua kuwa nadharia ya kielimu inasema kuwa tone la manii linakuwa na kuzidi kulingana na kanuni maalum?

Katika kujibu hayo, hapana budi kupambanua kati ya jambo lisilokuwa la kawaida, kama vile kufufua wafu na kupatisha kitu bila ya kitu kingine, na matukio yanayo kuwa kulingana na kanuni za kimaumbile, kama kupatwa jua mwezi, n.k. Hili la aina ya kwanza linategemezwa kwake Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Na hili la aina ya pili linategemea desturi ya maumbile na linategemezwa kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu Yeye ndiye aliyeweka desturi ya maumbile pamoja na vilivyomo ndani yake vikiwa ni pamoja na nguvu na viasili. Viasili hivi kwa kupitia njia zake vinafanya dhahiri za maumbile zikiwa ni pamoja na tone la manii.

﴿وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا﴾

"...Na ameumba kila kitu akakikadiria kipimo (chake)." (25:2)

Yaani anakipitisha katika desturi na kanuni za kitabia. Lau angelikuwa Yeye Mwenyezi Mungu ndiye anayesimamia umbile moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine, kusingelikuweko na sababu na msababishaji. Kwa hivyo basi, inatubainikia kuwa kila mwenye kuamini kwamba kila tukio la kimaumbile linategemea Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya kuweko kati sababu yoyote yenye kuhisiwa ambayo imegunduliwa na utaalamu au inaweza kugunduliwa, mtu huyo atakuwa mjinga mwenye kukosea katika imani yake. Na lau ingelikuwa sahihi imani yake hii, kusingelikuweko na wajibu wa kitendo chochote na elimu isingelikuwa na faida yoyote; wala uvumbuzi na maendeleo ya mtu yasingekuwa na athari yoyote. Vile vile amekosa yule mwenye kuitakidi kwamba maumbile ndio kila kitu, kuwa ndiyo sababu ya kwanza na ya mwisho, wala hakuna kitu nyuma yake. Hayo ni makosa. Kwani kama ni hivyo kusingelikuwa na nidhamu wala athari yake na kungelikuwa na migongano na natija ingelikuwa kutokuwepo elimu wala uhai, Haya tumeyafafanua zaidi katika Aya ya 21 ya Sura hii, kifungu cha Tawhid.

Hakumshiki kusinzia wala kulala

Mwenyezi Mungu alipobainisha kwamba Yeye ni Hai Msimamizi wa kila jambo, ameendelea kulitilia mkazo hilo kwamba Yeye ni Mwenye kutukuka, haumzuwii usingizi wala kusahau au kitu chochote, katika kupanga kuumba K

wake kwa njia ya ukamilifu. Kwa sababu hilo linapingana na ukubwa Wake na kujitosha Kwake na kila kitu. Imam Ali amesema akimwambia Mola wake: "Sisi hatujui kiasi cha ukubwa wako, isipokuwa tunajua kuwa Wewe ni Aliye Hai wa Milele, Msimamizi wa kila jambo, hakukushiki kusinzia wala kulala; hutazamwi; wala halikuoni jicho, lakini Wewe unaliona; umezithibiti amali na ukazishika barabara."

Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini Makusudio ya vilivyomo ni ulimwengu wote na kila kilichomo ndani yake hakitoki nje ya ufalme Wake na mipangilio Yake.

Imam Ali(a.s) aliulizwa kuhusu:"Hapana hila wala nguvu isipokuwa kwa msaada wa Mwenyezi Mungu." Akajibu: "Sisi hatumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu, wala hatumiliki isipokuwa kile tulichomilikishwa; na anapomilikisha kile ambacho amekimiliki zaidi kuliko sisi, basi ametukalifisha nacho; na anapokiondoa, huwa ametuondolea taklifa."

Na ni nani huyo awezaye kuombea mbele Yake bila ya idhini Yake.

Umekuja mfumo wa swali kwa maana ya kukanusha; yaani hataombea yeyeote mbele Yake isipokuwa kwa amri Yake na hayo ni jibu na kubatilisha kauli ya washirikina kwamba masanamu ndiyo yanayowakurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anawasimulia hao kwa kusema:

﴿وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ﴾

"... Na wanasema: hao ndio waombezi wetu mbele ya Mwenyezi Mungu! Sema: 'Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi? ..." (10: 18)

Tumekwisha zungumzia uombezi katika Aya ya 48, Baadhi ya ulama wamesema kwamba siku ya Kiyama kutakuwa na aina mbalimbali za watu. Kama ifuatavyo:- Waliotangulia ambao ni wenye kukurubishwa; watakaokuwa upande wa kuume ambao ni watu wema watakaookoka, watakaokuwa upande wa kushoto ambao ni waovu watakao adhibiwa, na watakaokuwa na msamaha ambao amali zao njema zimechanganyika na maovu. Na hawa watakubaliwa kuombewa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

﴿وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّـهُ أَن يَتُوبَ عَلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾

" Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu, huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe Mwenye kurehemu" (9:102)

Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao.

Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.), anajua yaliyokuwa na yatakayokuwa katika waja wake, iwe heri au shari; na anamjua mwombezi na anayeombewa na anayestahiki msamaha na thawabu au adhabu na mateso. Ikiwa mambo yako hivyo, basi uombezi (shafaa) hauna nafasi yoyote isipokuwa kwa amri Yake Mwenyezi Mungu kwenye mipaka Yake anayoridhia.

Wala hawalijui lolote lililo katika elimu Yake ila kwa alitakalo.

Dhamiri katika hawalijui inawarudia waja wote wakiwemo Malaika na Mitume. Makusudio ya elimu ni linalojulikana, Maana yako wazi. Ukipenda kujua zaidi unaweza kuangalia Aya hizi:

﴿عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾ إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ﴾

"Yeye ni mjuzi wa siri; wala hamdhihirishii yoyote siri Yake isipokuwa Mtume aliyemridhia ..." (72: 26-27)

﴿سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا﴾

"...Utakatifu niwako! Hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha..." (2:32)

Elimu Yake imeenea mbingu na ardhi.

Kauli zimekuwa nyingi na zimegongana kuhusu maana ya neno Kursiy. Baadhi ya kauli hizo ni za kumzungumzia Mwenyezi Mungu bila ya elimu, lakini bora ya kauli ni mbili: Ya kwanza, ni fumbo la utukufu Wake Mwenyezi Mungu na cheo chake yaani enzi. Ya pili, ni elimu; yaani elimu Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) imezunguka kila kitu. Mpangilio wa maneno unarudia maana haya.

Wala hakumshindi kuzilinda na Yeye Ndiye Mtukufu aliye Mkuu.

Yaani hakumtii mashaka wala uzito wowote kuilinda mbingu na ardhi na kupangilia vizuri yaliyomo ndani yake. Vipi isiwe hivyo! Na hali kuumba nzi na kuumba ulimwengu Kwake ni sawa tu; maadamu Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.)

﴿إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ﴾

"... Akitaka chochote ni kukiambia kuwa, kikawa" (36:82)

KITU BILA YA KITU

Kutengeneza vitu kuko aina mbili: kutegeneza kitu kutokana na maada na kutengeneza bila ya maada. Na kunatofautiana kwa njia nyingi. 1. Anayetengeneza kwa maada anahitaji harakati na zana, lakini asiyetengeneza kwa maada hahitaji.

2. Wa maada anachoka, lakini asiyetumia maada hachoki.

3. Mwenye kutumia maada hawezi kupata kitu bila ya kitu kingine, lakini kwa asiyetumia, hilo sio jambo zito. Kwa hivyo inabainika kwamba kumlinganisha Muumbaji na Mwenye kuumbwa ni kulinganisha na kisicholingana. Itawezekana vipi kumfananisha mwenye kujitosha na mwenye kuhitajia; atakuwaje sawa na mwenye kushindwa?

﴿لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ قَد تَّبَيَّنَ الرُّشْدُ مِنَ الْغَيِّ فَمَن يَكْفُرْ بِالطَّاغُوتِ وَيُؤْمِن بِاللَّـهِ فَقَدِ اسْتَمْسَكَ بِالْعُرْوَةِ الْوُثْقَىٰ لَا انفِصَامَ لَهَا وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴾

256. Hakuna kulazimisha katika dini; uongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mjuzi.

﴿اللَّـهُ وَلِيُّ الَّذِينَ آمَنُوا يُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَوْلِيَاؤُهُمُ الطَّاغُوتُ يُخْرِجُونَهُم مِّنَ النُّورِ إِلَى الظُّلُمَاتِ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

257. Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza, lakini walio kufuru watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza, na kuwaingiza katika giza, hao ndio watu wa motoni, watadumu humo.

HAKUNA KULAZIMISHA KATIKA DINI

Aya ya 256 - 257

MAANA

Hakuna kulazimishwa katika dini

Lau tungeiangalia jumla hii peke yake, tungelifahamu kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuweka hukumu yenye aina yoyote ya kulazimisha na kwamba anayolazimishwa mtu katika kauli au vitendo hayaambatani na kitu chochote katika mtazamo wa sharia, si katika dunia wala akhera. Lakini kauli Yake Mwenyezi Mungu "Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu", ambayo ndiyo sababu ya kuacha kulazimisha, inaonyesha kuwa neno katika, hapa lina maana ya juu ya; Yaani uislamu haumlazimishi yeyote kukubali isipokuwa unamlazimisha mpinzani kwa hoja na dalili tu; kama inavyosema Qur'an:

﴿وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ﴾

"Na sema: (Huu) ni ukweli uliotoka kwa Mola wenu, basi anayetaka na aamini na anayetaka na akufuru ..." (18:29)

﴿أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ﴾

"... Je, wewe utawashurutisha watu kwa nguvu wawe waumini? (10:99)

Unaweza kuuliza: Hakika dini haiwezekani kufungamana na kulazimishwa, kwa sababu dini ni katika mambo ya moyo yaliyo nje ya uwezo. Sawa na kuleta picha ya kitu akilini. Vinavyoweza kufungamana na kulazimishwa ni kauli na vitendo ambavyo inawezekana kutendeka bila ya matakwa ya msemaji na mtendaji, Kwa hivyo umepita njia gani mpaka ukasema habari ya kukataza kulazimishwa juu ya dini?

Jibu : Hakika kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):"Hakuna kulazimishwa katika dini" Imekuja kwa tamko la kuelezea habari. Kama hivyo ndivyo, basi swali litakuwa halina msingi, kwa sababu maana yatakuwa dini ni itikadi na hilo ni jambo linalorudia kwenye kukubali ambako mtu halazimishwi kukubali. Ikiwa tamko limekuja kwa kukusudiwa kukataza, basi maana yatakuwa ni: Enyi Waislamu msimlazimishe yeyote kusema "Lailaha illa Llahu Muhamadurasuli Llahi." baada ya kuwako hoja na dalili juu ya Tawhid na Utume.

Lakini jibu hili linaweza kuzalisha swali jipya kwamba hayo hayataafikiana na kauli ya Mtume(s.a.w.w) :"Nimeamrishwa nipigane na watu mpaka waseme: 'Laillahailla Ilah'; wakisema hivyo, basi damu zao na mali zao zimehifadhika na mimi."

Jibu : uislamu unaruhusu kupigana kwa sababu mbali mbali. Miongoni mwa sababu hizo ni: Kujikinga - Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَقَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ الَّذِينَ يُقَاتِلُونَكُمْ وَلَا تَعْتَدُوا﴾

"Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaowapiga, wala msipituke mipaka." (2: 190).

Kudhulumiwa - Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَقَاتِلُوا الَّتِي تَبْغِي حَتَّىٰ تَفِيءَ إِلَىٰ أَمْرِ اللَّـهِ﴾

"... Lipigeni (kundi) lile linaloonea (wenzao) mpaka lirudi katika amri ya Mwenyezi Mungu ..." (49:9)

Kupigana ili kuudhihirisha uislamu, ijapokuwa ni kwa ulimi. Hilo ni kwa ajili ya maslahi yanayowarudia wote, sio waislamu peke yao. Na maslahi haya anayakadiria aliye Masum au naibu wake; wala haifai kwa mwislamu yeyote, vyovyote alivyo, kupigana kwa ajili ya kutamkwa tamko la uislamu au kuueneza, isipokuwa kwa amri ya Masum au naibu wake, ambaye ni mujtahid ( [2] ) mwadilifu.

Ni kwa njia hii peke yake ndio inachukuliwa Hadith"Nimeamrishwa nipigane na watu..." ; Yaani mimi nitapigana nao nitakapoona mimi au kaimu wangu kwamba maslahi ya kiutu yanalazimisha kupigana kwa ajili ya 'Lailaha illa llah'. Hapo inaonyesha kuwa kupigana kwa kujikinga au kuikinga dini na haki, hakungojei idhini ya yeyote. Tumekwisha yaeleza hayo katika tafsiri ya Aya ya 193 kifungu cha 'Uislamu unapiga vita dhulma na ufisadi'

Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu.

Makusudio ya uongofu hapa ni imani na upotofu ni ukafiri. Mwenyezi Mungu amekwisha ibainisha haki kwa uwazi zaidi, na ubainifu na dalili zenye nguvu, mpaka kafiri akaishiwa na hoja au udhuru wowote. Mwenye kuijua njia ya haki na ya uongofu atakuwa amekwisha ijua njia ya upotofu na ya batili, Kwani hakuna kitu kingine baada ya haki isipokuwa upotofu.

Mulla Sadra anasema: Maana ya uongofu umekwisha pambanuka na upotofu ni kuitambua haki kutokana na batili na imani kutokana na ukafiri kwa dalili na hoja pamoja na kuzifahamu na kuziangalia vizuri. Yeyote mwenye kuikubali haki kwa kufuata tu, hana tofauti na mnyama. Hata hivyo mwenye kuwafuata watu wema kwa nia njema na kwa dhamiri nzuri atayapata yale watakayoyapata wao kesho.

Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika.

Kauli zimekuwa nyingi kuhusu tafsiri ya taghuti, baadhi ya wafasiri wamefikisha kauli tisa. Miongoni mwa hizo ni kuwa makusudio yake ni shetani. Nyingine ni dunia iliyo twevu. Iiliyo karibu na ufahamu na yenye kufahamisha kutokana na tamko lenyewe, ni kauli ya Sheikh Muhammad Abduh kwamba taghut ni yule ambaye kwa kumwabudu na kumwamini yeye, ndiyo sababu ya kupetuka mpaka na kutoka katika haki. Makusudio ya kishiko madhubuti, ni kwenda kwenye njia iliyonyooka ambayo hapotei mwenye kuifuata. Maana kwa ujumla ni kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu ni kishiko cha kutegemewa hakikatiki milele na kwamba mwenye kushikamana nacho hapotei. Katika Sahih Muslim anasema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema:Hakika mimi ninaacha kwenu vitu ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, kimojawapo ni kikubwa kuliko kingine, nacho ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kamba yenye kuvutwa kutoka mbinguni hadi ardhini na kizazi changu Ahlul Bait wangu, vitu viwili hivyo havitaachana mpaka vije kwangu kwenye birika." Hadith hiyo pia imepokewa na Tirmidhyi, Lakini hivi sasa vitu vyote hivyo viwili vimeachwa. Ndio Imam Ali(a.s) akasema:"Utakuja wakati Qur'an haitabaki isipokuwa maandishi yake na Uislamu utabaki jina lake tu."

Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mjuzi.

Anasikia tamko la Tawhid kutoka kwa waumini, na la kufuru kutoka kwa makafiri; na anajua yaliyo katika nyoyo za watu wawili na atamlipa kila mmoja kwa amali zake.

Mwenyezi Mungu ni mtawala wa wale walioamini; huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Wafasiri wametofautiana sana katika Aya hii. Baadhi yao wakazalisha mushkeli wa kiitikadi; mpaka Mulla Sadra akasema: "Kuna mushkeli mkubwa ambao ni vigumu kuutatua kwa wenye fahamu." Sheikh Muhammad Abduh amesema: "Hakika baadhi ya tafsiri ni tafsiri za wafasiri wasiokuwa wataalamu ambao hawafahamu mifumo ya lugha ya hali ya juu, au ni tafsiri za wasiokuwa Waarabu ambao zaidi huwa hawafahamu." Ama sababu ya kutofautiana wafasiri na kuzalisha matatizo ya kiitikadi ni kwamba wao wamefahamu Aya kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mtawala na mwangalizi wa mambo ya waumini tu; na wala sio kwamba waumini wanamfanya Yeye tu kuwa ni mtawala na mwangalizi wa mambo yao. Hapo kuna tofauti kubwa kati ya maana hizi mbili, Kuanzia hapa ndipo umekuja mushkeli katika wanavyofahamu wafasiri, kwamba utawala wa Mwenyezi Mungu na msaada Wake unakuwa kwa viumbe vyote katika nidhamu moja; na wala sio kwa waumini tu.

Vyovyote itakavyokuwa, kauli za wafasiri au wengi wao hazioani na mfumo, na kwamba maana yaliyo salama, ambayo hayana matatizo yoyote na yanayoafikiana na kauli Yake Mwenyezi Mungu, Basi anayemkataa taghuti na akamwamini Mwenyezi Mungu, hakika yeye ameshika kishiko madhubuti kisichovunjika ni kuwa waumini hawamfanyi mtawala asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hawamfanyi yeyote kuwa mlinzi wao isipokuwa Mungu pekee Yake; Kwake wanakimbilia, na kwa Kitabu Chake na sunna ya Mtume Wake wanaongoka katika itikadi zao, kauli zao na vitendo vyao. Wala hawategemei watu wapotevu na mataghuti, hata wawe vipi. Kinyume chake ni makafiri ambao wanawafanya mataghuti ndio watawala wao.

Hapana mwenye shaka kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na akaendelea kumtii na kuongoka kwa Aya Zake na ubainifu Wake kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na msaada Wake atasalimika kutokana na giza la bid'a na upotevu, vilevile matamanio na ujinga. Na atapata mwanga kwa nuru ya maarifa ya kweli na imani sahihi. Hayo ndiyo maana ya Huwatoa gizani na kuwaingiza katika mwangaza.

Lakini waliokufuru, watawala wao ni mataghuti. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwiangiza katika giza.

Maana kwa ujumla ni kuwa makafiri wanawafanya watu wapotevu na mataghuti kuwa watawala wao badala ya Mwenyezi Mungu; wanachukua amri zao na kuacha makatazo yao. Hawa wanakwenda katika njia ya kuhiliki na wanawatoa kwenye mwangaza wa akili na maumbile na kuwati katika giza ukafiri na uzushi.

KUDUMU MOTONI

Watadumu humo

Mara nyingi sana Qur'an imetaja kuwa kuna aina ya waasi watakaodumu motoni; na imebainisha kuwa miongoni mwa aina hii ni: Mwenye kumkufuru na akakadhibisha Aya zake. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

"Na wale ambao wamekufuru na kukadhibisha ishara zetu, hao ndio watakoakuwa watu wa motoni, humo watadumu." (2:39)

Mwenye kumua mumini kwa makusudi, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا ﴾

"Na mwenye kumuua Muumin kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannam, humo atadumu ..." (4:93)

Mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na kuruka mipaka. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا ﴾

"Na anayemuasi Mwenyezi Mungu na Mtume, na kuiruka mipaka ya Mwenyezi Mungu, atamwingiza motoni, humo atadumu." (4:14)

Mwenye kuzungukwa na makosa yake; Mwenyezi Mungu anasema:

﴿بَلَىٰ مَن كَسَبَ سَيِّئَةً وَأَحَاطَتْ بِهِ خَطِيئَتُهُ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾

"Ndio wanaochuma ubaya na makosa yao yakawazunguka, hao ndio watu wa motoni, humo watadumu" (2:81)

Hapana mwenye shaka kwamba kwa mujibu wa uadilifu Wake Mwenyezi Mungu, hamwadhibu isipokuwa mwenye kustahili adhabu na adhabu yake inatofautiana kwa ukali na udhaifu kulingana na makosa na maasi. Kosa la mwenye kuhangaika akieneza ufisadi duniani, akaangamiza mimea na viumbe, si sawa na kosa la mwenye kuiba shillingi moja au aliyemsengenya anayeshindana naye katika kazi. Pamoja na haya tunaweza kujiuliza. kudumu katika moto kusikokuwa na mwisho, kugongwa kichwa kwa macheche yaliyo kama majumba, kuvurumishiwa marungu ya chuma mgongoni na kujazwa tumbo kwa maji ya usaha; kisha mtu asife akapumzika wala asipunguziwe angalau akapumua; mtu huyu ambaye anaumizwa na chawa na kufa kwa kusongwa koo na jasho humfanya anuke; kama alivosema Amirul Muminin Ali(a.s) . Tujiulize je machungu yote haya makubwa kwa mnyonge huyu mwenye kushindwa na chawa, yanaafikiana na dhati ya Mwenyezi Mungu ambaye ni heri tupu na rehema, ukarimu, neema, upole na hisani?" Je inaingilika akilini mtu huyu kuadhibiwa milele au kunyimwa kabisa neema Au huko kuwa milele na kila ngozi inapoiva kubadilishwa ngozi nyingine bila ya kupumzika, yote hayo ni ya kujiuliza.

Akisema msemaji: Hakuna adhabu ambayo itazidi ya mwenye kumuua Hussein bin Ali(a.s) au aliyetupa bomu la Atomic au Haidrojeni kwa watu na akawamaliza wote, au mwenye kuanzisha mambo mabaya, yakadumu na uovu wake ukazidi?

Jibu : Ni kweli kuwa hazidi yeyote katika uliowataja, lakini sio kila asi ni Yazidi wala sio kila bomu ni Atomic na Hadrojeni; wala sio kila desturi inawatawanya watu. Lakini swali halikuwa juu ya hawa, bali swali ni juu ya kudumu walio na daraja nyingine. Unaweza kusema: Maelezo ya Qur'an na Hadith za Mtume juu ya kudumu milele utazifanyaje?

Jibu : Hakuna katika hizo inayokataa Taawil.

Ukisema tena kuwa, kila kilicho elezwa ikiwa kukielewa kunawezekana kwa dhahiri, basi ni wajibu kudumu juu ya dhahiri yake, kwa hiyo kudumu wakosaji katika moto si muhali.

Jibu : Ndio, lakini lichukuliwe la kudumu muda mrefu badala ya milele, kwa kukusanya kati ya Qur'an na dalili za rehema ambako, hakukataliki wala hakupingwi na sharia na akili. Utasema mara ya tatu: Hakika mafaqihi hawawezi kuridhika na jawabu hili, kwa sababu wao hawaruhusu kuchukulia kinyume cha dhahiri ya tamko isipokuwa kwa sababu tatu: Kuunganisha na kitu kingine kwa kidesturi, kama vile kuchukulia mahsus kutoka katika jumla; au kisheria, kama kauli wazi yenye kuthibiti kutoka kwa Masum; au kiakili kusikokubali uwezekano wa kinyume, Na sisi hatuna chochote katika hivyo vitatu.

Jibu :Kwanza : Ninadhani kuwa mafaqihi waliozitambua dalili za rehema ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) wataafikiana nami, kwamba inawezekana kuziacha dhahiri za dalili za kudumu milele katika moto kwa baadhi ya wakosaji. Miongoni mwa dalili hizo ni Hadith Qudsi: "Rehema yangu imeshinda ghadhabu yangu." Vilevile Hadith tukufu inayosema: Hakika waombezi siku ya Kiyama ni wengi na mwisho wa waombezi ni mwenye kurehemu wenye kurehemu. Na kwamba rehema yake Mwenyezi Mungu itaenea siku ya Kiyama mpaka ibilisi atakuwa na tamaa na kunyoosha shingo yake. Katika baadhi ya riwaya ni kwamba Hassan al Basri alisema: "Si ajabu kwa aliyeangamia, kuwa vipi ameangamia. Lakini ajabu ni ya mwenye kuokoka vipi ameokoka." Imam Zainul Abidin(a.s) akasema: "Ama mimi ninasema; sio ajabu kwa aliyeokoka kuwa ameokoka vipi; isipokuwa ajabu ni kwa aliyeangamia kuwa ameangamia vipi pamoja na ukubwa wa rehema ya Mwenyezi Mungu!"

Tukiiunganisha riwaya hii na Aya inayosema:

﴿قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا﴾

"Sema! Enyi waja wangu waliojidhulumu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote ..." (39:53).

Tunapata ulinganisho mkataa wa kuacha dhahiri ya dalili za kudumu milele motoni.

Pili : Sisi tunazungumza mambo ya kiitikadi mkataa, sio masuala ya matawi ya kudhania; na mafaqihi pamoja na kujichunga kwao na nguvu ya imani zao, wanakuwa ni wataalamu wa hukumu za Mwenyezi Mungu za kisharia sio mambo ya itikadi. Bali wengi katika wao wako katika daraja ya kufuata yale yanayorudia sifa za Mwenyezi Mungu na vitendo Vyake. Ama yale yanayorudia kwenye dalili za kuweko Muumbaji (s.w.t) ni dalili za mzunguuko na kuendelea. Hata hivyo ni lazima ieleweke kuwa sisi tunaamini kuswihi kufuata katika misingi ya itikadi ikiafikana na mambo yalivyo.

Tatu : Akili huona vibaya kukhalifu ahadi, lakini sio kiaga, Ukimwambia mtu mwingine nitakufanyia wema; kisha uvunje ahadi, basi utakuwa mwenye kulaumiwa mbele za wenye akili. Ama ukamwambia unayemdai haki: Nitachukua haki yangu tu kutoka kwako kisha umsamehe, basi wewe utakuwa mwenye kusifiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na watu; hasa akiwa yule unayemdai ni fukara na wewe ni tajiri.

Na Mwenyezi Mungu ni tajiri kwa viumbe na adhabu zao. Na wao wana haja sana ya rehema Yake na msamaha wake.

Swali la nne na la mwisho: Kwa nini unaleta taawil ya Aya za kudumu motoni na ni maana gani unayoyachukulia?

Jibu : Inawezekana kuchukulia maana ya kudumu muda mrefu, lakini sio milele; au kudumu motoni bila ya adhabu; kama hema la Hatimtai ( [3] ) au kuwepo Ibrahim katika moto.

Haya yanatiliwa nguvu na yaliyopokewa katika baadhi ya Hadith kwamba baadhi ya watu wa motoni watakuwa wanacheza na makaa ya moto kama mpira wakirushiana. Hapana mwenye shaka kwamba mchezo huu hauwezi kuwa pamoja na adhabu hata hafifu sikwambii kali yake. Na Mungu si Mwenye kushindwa kuufanya moto baridi na salama kwa asiyekuwa Ibrahim kama alivyoufanya kwa Ibrahim(a.s) .

Muhhiddin Ibn al Arabi anasema katika al Futuhul Makkiyya J2 uk. 127: "Hatobaki motoni mwenye kumwamini Mungu mmoja katika waliopelekewa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , kwa sababu moto utarudi kuwa baridi na salama kwa wanaompwekesha Mwenyezi Mungu kwa baraka za Ahlul Bait katika akhera. Ni utukufu ulioje wa baraka za Ahlul Bait!

6

ILI NIWE PAMOJA NA WAKWELI

UCHAMBUZI WA MADA

Madda muhimu katika uchambuzi: Imebakia madda moja muhimu ndani ya uchambuzi wote huu, madda ambayo inataka kuangaliwa kwa makini na kusomwa, na huenda hiyo pekee ndiyo kikwazo ambacho huwachemua wapinzani pale wanaposhinikizwa kwa hoja nzito. Utawaona wanashangaa na kutokuamini ya kuwa Masahaba wapatao laki moja walihudhuria kutawazwa kwa Imam Ali (kuwa Khalifa wa Mtume) na hatimaye hao hao Masahaba wakaafikiana wote kumkhalifu Imam Ali na kumpuuza na miongoni mwao wamo Masahaba wakubwa.

Hali hii (ya kushangazwa kwa wapinzani) imepata kunitokea mimi mwenyewe wakati nilipoingia kikamilifu ndani ya utafiti, sikuamini na haiwezekani kwa mtu yeyote kuamini pindi tukio hili linapoaridhiwa kama lilivyo, lakini wakati tunapolisoma tukio hili kwa pande zote basi kule kushangaa kunaondoka kwani hali halisi haiko kama tunavyoitazamia sisi au kama wanavyoiaridhi Masunni (ya kuwa) haiwezekani Masahaba laki moja wakaenda kinyume na amri ya Mtume, hivyo basi ilikuwaje mambo yakatokea kama yalivyotokea?

Kwanza Siyo kila aliyehuduria Baia ya Ghadir alikuwa akiishi Madina, bali ilikuwa kama ambavyo hali halisi ilivyokuwa kwamba kwa kiasi kikubwa itakuwa ni watu elfu tatu au Nne tu miongoni mwa Masahaba hao ndiyo waliokuwa wakiishi Madina.Na tutakapofahamu ya kwamba wengi wa hawa walikuwa ni watumwa na walioachwa huru na wanyonge ambao walimfikia Mtume (s.a.w.) kutoka sehemu mbali mbali na hapo Madina hawakuwa na uwenyeji wala jamaa (kwa mfano watu wa As-Safah) basi haitabakia isipokuwa nusu yao yaani watu elfu mbili tu, na hata hawa nao ni watiifu kwa viongozi wa makabila na muongozo wa kidugu ambao ndiyo wanaohusika nao na Mtume aliwakubalia (kuwa watiifu kwa viongozi wao) kwani ulipokuwa ukimfikia ujumbe wa kabila fulani, Mtume (s.a.w.) humtawalisha juu yao kiongozi wao, na kwa ajili hiyo ndiyo tumekuta katika Uislamu Istilahi ya kuitwa kwao kuwa ni Ahlul-Hilli wal-Iqdi, watu wanaotumainiwa kutowa maamuzi katika jamii au nchi.

Kadhalika tunapoutazama mkutano wa Saqifah ambao ulikutana mara tu baada ya kufariki Mtume (s.a.w.), tunawakuta waliohudhuria ambao waliuthibitisha uchaguzi wa Abubakar kuwa ni khalifa, idadi yao haizidi watu mia moja kwa makadirio ya juu, kwani katika Ansari ambao ndiyo wenyeji wa Madina hawakuhudhuria isipokuwa viongozi wao kama ambavyo Muhajirina ambao ni wenyeji wa Maka waliohama pamoja na Mtume (s.a.w.) hawakuhudhuria isipokuwa watu watatu au wanne wakiwakilisha Maquraishi. Hali hii itoshe basi kuwa ni dalili ya kupima ukubwa wa hiyo Saqifah ikoje, Saqifah ambayo ilikuwa haina nafasi ya kutosha, kwani haikuwa inakosa kuwa karibu katika kila nyurnba.

Kwa hiyo haikuwa uwanja wa maadhimisho wala siyo jumba la mikutano, na tunaposema kuwa watu mia moja walihudhuria hapo Saqifah bani Saida basi idadi hiyo sisi ndiyo tunaoizidisha ili tu, mwenye kutafiti aweze kufahamu kwamba wale Masahaba laki moja hawakuwepo wala hata hawakusikia mazungumzo yalivyofanyika ndani ya Saqifah isipokuwa baada ya muda mrefu kupita, .kwani hapo zamani hapakuwa na mawasiliano ya anga wala simu au Satellite.

Na baada ya mabwana wakubwa hawa kuafikiana juu ya Abubakar pamoja na upinzani wa bwana wa Kiansari Saad bin Ubbadah ambaye ni kiongozi wa kabila la Khazraj na mwanawe Qais, lakini wengi mno miongoni mwao (kama isemwavyo hii leo) walipitisha makubaliano hayo na kumpa Abubakar mkono wa Baia, wakati ambapo Waislamu wengi hawakuwepo hapo Saqifah, na baadhi yao walikuwa wameshughulika kumuandaa Mtume (s.a.w.) kwa mazishi au walihamanika kutokana na khabari za kifo chake, ambapo Umar bin Al-Khatab naye alikuwa amewatisha na kuwatia khofu iwapo watasema kuwa Mtume amefariki. Taz: Sahih BukhariJuz. 4 -195.

Zaidi ya hayo wengi wa Masahaba wa Mtume walikuwa amewateua wawemo ndani ya Jeshi la Usamaha na wengi wao walikuwa wameweka kambi mahala paitwapo Jorfi wakiwa tayari kwenda vitani na jeshi la Usamah hawakuwepo Mtume alipofariki wala hawakuhudhuria mkutano wa Saqifah. Basi je, inaingia akilini baada ya haya yaliyotokea kwamba mtu fulani katika kabila au ukoo kumpinga kiongozi wake kwa lile alilolipitisha na hasa inapokuwa hilo alilolipitisha lina ubora na utukufu mkubwa ambao kila kabila linaukimbilia? Ni nani ajuwaye ya kwamba huenda siku moja naye atawatawalia Waislamu wote, maadamu mwenye haki hiyo kisheria amekwisha tupwa mbali na mambo sasa yanakwenda kwa kushauriana wanabadilishana kwa kuachiana, basi ni kwa nini wasilifurahie hilo, na ni kwa nini wasiliunge mkono?

Pili Ikiwa wenye uwezo wa kuamua ni wakaazi wa Madina na wamepitisha jambo fulani, basi watu walio mbali katika sehemu mbali mbali za bara Arabu hawawezi kupinga na hali ya kuwa hawajui yanayopita wakati hawapo kwani vifaa vya mawasiliano kwa zama hizo vilikuwa ni vile vya kizamani kisha wao walikuwa wakifahamu kwamba wakazi wa Madina ndiyo waliokuwa wakiishi na Mtume wa Mwenyezi Mungu hivyo basi hao ndiyo wajuao mno mambo mapya miongoni mwa hukmu, kwani huenda ukashuka Wahyi wakati wowote au siku yoyote. Kisha kama kuna kiongozi wa kabila lolote lililo mbali na makao makuu basi jambo la Ukhalifa kwake si muhimu sana sana iwapo Abubakr atakuwa Khalifa au Ali au mtu mwingine yeyote, kwani watu wa Maka ndiyo wajuao zaidi utaifa wao, na cha muhimu kwao ni kubakia kwenye uongozi wa ukoo wake ambapo hakuna anayemkera katika uongozi huo.

Basi ni nani ajuwaye kwamba huenda baadhi ya watu waliulizia juu ya jambo hilo (la Ukhalifa) na walitaka kufahamu mambo yalivyokwenda lakini vyombo vya mtawala viliwanyamazisha sawa iwe kwa njia ya kuwapa tamaa ya mali au vyeo au vitisho, na huenda kisa cha Malik bin Nuwairah ambaye alikataa kutoa zaka kwa Abubakr ni utokea jambo hilo. Na yeyote mwenye kufuatilia matukio hayo yaliyotokea katika vita ya wanaokataa kutoa zaka katika zama za Abubakr atakuta kuna kupingana (kwa maelezo), wala hawezi kutosheka kwa maelezo yaliyoelezwa na baadhi .ya wanahistoria kwa lengo la kulinda heshima ya Masahaba na hasa wale watawala.

Tatu Kiini cha tatizo hili ni kule kushitukizwa ghafla kupatikana kwa Khalifa, hili ni jambo lililochangia mno kukubalika kwa kile ambacho leo kinaitwa kuwa "Hali halisi iliyopo". Kwani mkutano wa Saqifah ulifanyika ghafla kwa kuwashitukiza baadhi ya Mashaba ambao walikuwa wakimshughulikia Mtume (s.a.w.), na miongoni mwao alikuwa Imam Ali na Abbas na wengine miongoni mwa Bani Hashim, Miq-dad, Salman, Abu Dharri, Ammar, Zubair na wengineo wengi. Ama wale waliokuwa Saqifah walipotoka huko hali ya kuwa wakimshangilia Abubakr walielekea msikitini huku wakitoa mwito kwa watu wafanye baia ya jumla na watu wakaipokea baia hiyo kwa wingi watake wasitake kipindi hicho Imam Ali na wafuasi wake walikuwa hawajamaliza wajibu wao Mtukufu ambao tabia zao (mwenendo wao) mwema uliwalazimisha (wautimize) basi haikuwezekana kwao kumuacha Mtume (s.a.w.) bila ya kumkosha, kumvisha sanda, kumtayarisha na kumzika eti badala yake wakimbilie Saqifah kugombea Ukhalifa.

Walipomaliza wajibu wao huo, mambo yalikuwa yamekwisha kamilika kwa Abubakr na yeyote mwenye kwenda kinyume na baia hiyo akawa anahesabiwa kuwa ni miongoni mwa watu wenye fitna ambaye anabomoa umoja wa Waislamu, hivyo ni wajibu kwa Waislamu kumpinga au hata kumuuwa ikiwa itabidi, na ndiyo maana tunamuona Umar alimuonya Saad bin Ubbadah kuwa atauawa pale alipokataa kumbai Abubakr, Umar akasema, "Muuweni hakika yeye ni mtu wa fitna"[52] na baada ya hapo Umar aliwatishia wote waliobaki ndani ya nyumba ya Ali ya kuwa atachoma moto nyumba hiyo na wote waliomo humo. Tukishakufahamu vyema maoni ya Umar bin Al-Khatab kuhusu baia tutatambua mengi baada ya hapo miongoni mwa mambo yanayotatanisha.

Kwa hakika Umar anaona kuwa baia inatosha kusihi pale mmoja miongoni mwa Waislamu anapowahi, basi hapo inakuwa ni lazima kwa wengine kumfuata na yeyote atakayeasi miongoni mwao huyo atakuwa ametoka nje ya mshikamano ya Waislamu na ni wajibu kumuuwa. Basi hebu na tumsikilize yeye mwenyewe hasa kuhusu baia, kama alivyoeleza Bukhar ndani ya Sahih yake juzuu ya nane ukurasa wa ishirini na nane, Babu Rajmi Al-Hubla Minaz-Zinaa Idha-Ah-Sanat amesema: akisimulia yale yaliyotokea ndani ya Saqifah. "Basi fujo ikazidi na sauti zikapaa mpaka nikatishika kuwa kutatokea kuhitilafiana, nikasema, Ewe Abubakr kunjua mkono wako, Abubakar akakunjua mkono wake nikambai nao muhajirina wakambai[53] Ansari (nao wakambai) na tukamruka Saad bin Ubbadah, akasema msemaji miongoni mwao, "Mmemuuwa Saad bin Ubbadah" Mimi nikasema:

"Mwenyezi Mungu amuuwe Saad bin Ubbadah" Umar akasema: "Wallahi sisi hatujakutana na jambo gumu katika yote tuliyohudhuria kuliko kumbai Abubakar, tulichelea kuwa hawa jamaa tukiwaacha bila kupitisha baia, basi watambai mtu miongoni mwao baada yetu, hivyo imma tuwape madaraka, jambo ambalo hatulikubali, au tuwapinge itokee uharibifu, (naonya) yeyote atakayetoa baia bila ya kushauriana na Waislamu asifuatwe yeye wala yule aliyembai ili asiuawe. Basi jambo lililovyo kwa Umar siyo uchaguzi wala hiyari wala mashauriano, bali inatosha pale Mwislamu mmoja anapoiwahi baia hiyo iwe ni hoja kwa wengine na ndiyo maana alimwambia Abubakr, "Kunjua mkono wako Ewe Abubakar," na Abubakr naye akakunjua mkono wake akambai bila ya mashauriano tena haraka haraka kwa kuchelea kutanguliwa na mwingine na kwa hakika Umar amekwisha ieleza rai hii pale aliposema:

"Tulichelea lau tutawaacha watu hawa bila ya kuipitisha baia, watambai mtu miongoni mwao baia yetu (Umar aliwachelea Maansar wasimtangulie wakambai mtu miongoni mwao), na kinachomuongezea ufafanuzi zaidi ni pale anaposema: "Basi imma tuwape Baia jambo ambalo hatulikubali na au tuwapinge patokee uharibifu."[54]

Na ili tuwe waadilifu katika maamuzi na wenye kuchunguza kwa undani, inatupasa tukiri kwamba Umar bin Al-Khatab alibadilisha mtazamo wake kuhusu baia mwishoni mwa uhai wake na hilo ni pale mtu mmoja alipomjia Umar mbele ya Abdur-Rahman bin 'Auf katika Hijja yake ya mwisho aliyohiji, yule mtu akamwambia: "Ewe Amirul-Muuminina unayo habari kuwa fulani anasema, bila shaka Umar akifa hakika nitambai fulani kwani wallahi baia ya Abubakar haikuwa isipokuwa kwa kushitukiza tu na ilitimia". Umar alikasirika na kwa ajili hii alisimama akawahutubia watu alipokuwa akirudi Madina, miongoni mwa aliyoyasema katika khutba yake ni haya yafuatayo:

"Kwa hakika nimepata habari kwamba kuna asemaye miongoni mwenu kuwa, Wallahi lau Umar atakufa nitambai fulani, basi na asijidanganye mmoja wenu kusema kuwa baia ya Abubakar ilikuwa hivyo lakini Mwenyezi Mungu aliikinga shari yake.."[55] Kisha Anasema: "Yeyote mwenye kumbai mtu bila mashauriano kutoka kwa Waislamu, basi huyo asipewe baia yeye wala huyo aliyembai kuhofia asije uwawa.[56]

Basi laiti Umar angekuwa na mtazamo huu siku ya Saqifah na asiwalazimishe Waislamu kumbai Abubakr ambako kulikuwa kwa kushitukiza, na Mwenyezi Mungu aliikinga shari yake kama alivyoshuhudia yeye mwenyewe, lakini imekuwaje Umari awe na rai hii mpya katika mtazamo huu mpya, hakika atakuwa amejihukumia kifo yeye mwenyewe na rafiki yake (Abubakr) kwa kuwa kwenye mtazamo wake mpya anasema: "Yeyote mwenye kumbai mtu bila ya mashauriano toka kwa Waislamu basi asipewe Baia yeye wala huyo aliyembai ili asije uwawa."

Imebakia juu yetu kufahamu ni kwa nini Umar alibadilisha maoni yake mwishoni mwa uhai wake pamoja na kwamba yeye anafahamu mno kuliko mwingine ya kuwa mtazamo wake mpya unatengua baia ya Abubakar iliyotimia bila ya mashauriano toka kwa Waislamu na ilikuwa ni baia ya kushitukiza? Pia mtazamo wake huu mpya unatengua baia yake yeye aliyopewa, kwani aliupata ukhalifa kwa tamko la Abubakar wakati wa kufa bila ya makubaliano kutoka kwa Waislamu, kiasi baadhi ya masahaba walikwenda kwa Abubakar wakamkemea kwa kuwatawalishia mtu msusuavu tena mgumu wa tabia.[57] Na Umar alipotoka ili awasomee watu maandiko ya Abubakr kuna mtu alimuuliza: "Ewe Baba Hafs kuna nini ndani ya waraka huo?" Umar akasema, Sijuwi, lakini mimi nitakuwa wa kwanza kusikiliza na kutii." yule mtu akasema: "Lakini Wallahi mimi najua kilichomo, wewe ulimtawalisha (Abubakar) kipindi cha mwanzo naye amekutawalisha kipindi hiki".

Taz: Al-Imam Was-Siyasah cha Ibnu Qutaibah Juz. 1 uk. 25Mlango unaohusu maradhi ya Abubakri na kumtawalisha kwake Umar. Kauli hii inafanana na kauli ya Imam Ali kumwambia Umar pale alipomuona anawalazimisha watu kwa nguvu wambai Abubakr akasema "Nifanye jambo ambalo wewe utakuwa na hisa (wanitaka) leo nilikazanie jambo lake ili kesho akurudishie"? Taz: Al-Imamah Was-Siyasah cha ibnu Qutaiba Juz. 1 uk. 18. Cha muhimu ni kufahamu ni kwa nini Umar alibadilisha mtazamo wake kuhusu Baia?

Mimi ninakurubia kuamini kwamba, wakati alipowasikia baadhi ya Masahaba wanataka kumbai Ali bin Abi Talib baada ya kufa Umar jambo ambalo yeye Umar kamwe hakubaliani nalo, kwa kuwa yeye ndiye aliyezipinga maagizo ya Mtume yaliyobayana, na akapinga Mtume (s.a.w.) asiwaandikie yale maandiko[58] kwa kuwa yeye alilifahamu lengo lake kiasi kwamba akamtuhumu Mtume kuwa anaweweseka na akawatisha watu wasiseme kuwa Mtume amekufa[59] yote hayo ni kwa sababu wasije wakawahi kumbai Ali. Umar alitilia mkazo baia ya Abubakr na akawalazimisha watu kwa nguvu waikubali baia hiyo na kisha kumuonya kila atayepinga kuwa atamuua[60] ili tu kumtenga mbali Ali na ukhalifa.

Hivi itawezekana Umar aridhie aseme msemaji kwamba fulani atapewa baia lau Umar atakufa? Hasa pale msemaji huyu ambaye jina lake limebakia kuwa halijulikani na hapana shaka kuwa alikuwa miongoni mwa Masahaba wakubwa? Msemaji huyu alitumia hoja ya kitendo alichokitenda Umar mwenyewe alipombai Abubakar pale anaposema: "Wallahi Baia ya Abubakr haikuwa isipokuwa ya kushitukiza na ikatimia", yaani pamoja na kuwa ilitokea kwa kuwashitukiza Waislamu na bila kupata ushauri wao lakini ilitimia na likawa jambo lililothibitika, kwa hiyo ilifaa kwa Umar kulifanya kwa Abubakr kwa nini isifae kwake kulifanya yeye mwenyewe kwa njia ile ile kwa mwingine? Na hapa tunaona kwamba ibn Abbas na Abdur-Rahman bin Auf na Umar bin Khatab wanakwepa kulitaja jina la huyu msemaji kama ambavyo wanakwepa kulitaja jina la mtu anayetaka kupewa baia msemaji huyu. Na ilipokuwa wawili hawa wanao umuhimu mkubwa kwa Waislamu, tunamuona Umar alikasirika kwa usemi huu na haraka katika Ijumaa ya kwanza aliwahutubia watu na akaieleza maudhui ya Ukhalifa itakavyokuwa baada yake na akawaonesha maoni yake mapya kuhusiana na Ukhalifa, ili azuwie njia ya huyu anayetaka kurudisha ile ghafla iliyokwisha tokea kwani njia hiyo itamnufaisha mgomvi wake, kwani kwa kupitia uchunguzi tumefahamu kuwa usemi huo haukuwa ni maoni ya fulani tu peke yake, bali ulikuwa ndiyo mtazamo wa Masahaba wengi, na ndiyo maana Bukhari anasema: "Umar alichukia na kisha akasema bila shaka apendapo Mwenyezi Mungu mimi nitasimama usiku huu miongoni mwa watu niwaonye hawa ambao wanataka kuwapora mambo yao..." [61]

Basi kubadilisha kwa Umar mtazamo wake kuhusu Baia ilikuwa ni kuwapinga hawa ambao wanataka kuwapokonya watu mambo yao na wambai Ali, na hili ni jambo ambalo Umar hakubaliani nalo kwani yeye anaitakidi kuwa Ukhalifa ni miongoni mwa mambo ya watu na siyo haki ya Ali bin abi Talib, na itikadi hii itapokuwa ni sahihi, basi ni kwa nini yeye Umar aliruhusu kuwapokonya watu mambo yao baada ya kufariki Mtume (s.a.w.) na haraka haraka akambai Abubakar bila ya makubaliano na Waislamu. Na msimamo wa Abu Hafs (Umar) dhidi ya Abul-Hasan (Ali) unaeleweka na ni mashuhuri mno, nao ni kumtenga Ali kwenye utawala kwa kutumia njia yoyote inayowezekana.

Na matokeo haya hatukuyafahamu kutokana na hotuba yake (Umar) iliyotangulia hapo kabla peke yake, lakini yeyote mwenye kufuatilia historia atafahamu kuwa Umar bin Al-Khatab alikuwa ndiye mtawala mtendaji hata katika Ukhalifa wa Abubakr na ndiyo maana tunamuona Abubakr anamuomba Usamah bin Zaid amuachie Umar bin Al-Khatab ili amsaidie kuhusu suala la Ukhalifa kama alivyoeleza hilo Ibn Saad ndani ya Tabaqat yake na pia wanahistoria wengi walioelezea jeshi la Usamah - pamoja na hayo tunamuona Ali bin Abi Talib anabakia mbali na majukumu, hawakumpa cheo chochote wala utawala wowote wala kumpa uamiri wa jeshi lolote lile na wala hawakumuamini kuwa mweka hazina na yote haya ni kwa kipindi cha Ukhalifa wa Abubakr, Umar na Uthman, nasi sote twamjua Ali bin Abi Talib ni nani.

Cha kushangaza kuliko yote haya ni kuwa, sisi tunasoma ndani ya vitabu vya historia kwamba kifo kilipomfikia Umar alisikitika kwamba lau Abu Ubaidah bin Al-Jarrah au Salim Huru wa Abu Hudhaifah wangekuwa hai angewatawalisha baada yake. Lakini hapana shaka Umar alikumbuka kuwa hapo kabla alikwisha badilisha mtazamo wake juu ya baia kama hii na akaiona kuwa ni ya kushitukiza na ni kupokonya mambo ya Waislamu, basi hapana budi kwake aweke njia mpya kuhusu baia ili kati kwa kati asije yeyote akafaulu kumbai amuonaye kuwa anafaa na kuwalazimisha watu kumfuata kama alivyofanya yeye kwa Abubakr na kama alivyofanya Abubakar kwake Umar au kama atakavyofanya fulani ambaye anangoja kufa kwa Umar ili ambai jamaa yake.Basi hili haliwezekani baada ya Umar kuwa ameuhukumia Ukhalifa kuwa ni jambo lililofanyika ghafla na kuwa linataka kuwa ni jambo la kupora, na haiwezekani pia kwake kuliacha jambo hili liwe la makubaliano baina ya Waislamu. Na ule mkutano wa Saqifah uliofuatia kufariki kwa Mtume (s.a.w.) yeye Umar alihudhuria na akajionea mwenyewe hitilafu iliyotokea ambayo karibu zitoke roho za watu na damu imwagike.

Basi baadaye alitoa fikra ya watu wa mashauriano au (tuseme) watu sita ambao peke yao ndiyo wenye haki ya kumchagua Khalifa na Muislamu mwingine yeyote hana haki ya kushirikiana nao katika jambo hilo, na Umar alikuwa akitambua kwamba tofauti baina ya watu hawa sita haiwezi kuepukwa, ndiyo maana aliusia ikiwa watatofautiana basi wawe kwenye upande alioko Abdur-Rahman bin Auf hata kama itapelekea kuwauwa watu watatu ambao watamkhalifu Abdur-Rahman bin Auf wakati watakapogawika watu hawa sita makundi mawili, na hilo ni muhali kwani Umar anafahamu kwamba Saad bin Abi Waqas ambaye ni ibn Ammi ya Abdur-Rahman bin Auf na wawili hawa ni ukoo wa Bani Zuhrah, na alifahamu pia kwamba Saad hampendi Ali na moyoni mwake kulikuwa na chuki kwani Ali ndiye aliyewauwa wajomba zake wa ukoo wa Abdis-Shams, kama ambavyo Umar alikuwa akifahamu kwamba Abdur-Rahman bin Auf ni shemeji wa Uthman kwani mkewe aliyekuwa akiitwa Ummu Kul-thum ni dada wa Uthman. Si hivyo tu kadhalika alifahamu kuwa Tal-hah akimpenda Uthman kutokana na mahusiano yaliyokuwepo baina yao kufuatana na maelezo ya baadhi ya wapokezi wa khabari, na hakika ilitosha kwa Tal-hah kumpenda Uthman kutokana na kumpinga kwake Ali kwani yeye Tal-hah ni katika ukoo wa Bani Taym, na kulikuwa na chuki fulani baina ya Bani Hashim na Bani Taym kutokana na Ukhalifa wa Abubakar.

Taz: Shark Najul-Balaghah ya Muhammad Abdoh, Juz. 1 uk. 88.

Umar alikuwa akiyajuwa yote hayo na kwa ajili hii ndiyo maana akawachagua hawa peke yao. Umar aliwachagua hawa watu sita na wote wakiwa ni Maquraish na wote ni kutoka katika Muhajirina na hakuna yeyote kati yao ambaye ni kutoka miongoni mwa Ansar na wote hawa kila mmoja wao akiwakilisha na kuongoza kabila lenye umuhimu wake na athari yake.

1. Ali bin Abi Talib, kiongozi wa Bani Hashim.

2. Uthman bin Affan kiongozi wa Bani Umayyah

3. Abdur-Rahman bin Auf, kiongozi wa Bani Zuhrah

4. Saad bin Abi Waqqas, yeye ni kutoka katika Bani Zuhrah na wajomba zake ni Bani Umayyah.

5. Tal-ha bin Ubaidullah, Bwana wa Bani Taym.

6. Zubair bin Al-Awwan, yeye ni mtoto wa Safiyyah ambaye ni shangazi yake Mtume na ni mume wa As-maa binti Abubakr.

Basi hawa ndiyo wenye kutoa maamuzi, na hukmu yao ikubaliwe na Waislam wote, sawa sawa wakiwa ni wakaazi wa Madina (Makao Makuu ya Ukhalifa) au wengineo katika ulimwengu wote wa Kiislamu na ni wajibu wa Waislamu yeyote atakayetoka miongoni mwao akawa kinyume cha maamuzi yao basi damu yake imwagwe (auawe). Na hili ndilo jambo pekee tulilokuwa tunataka kulisogeza katika akili ya msomaji kuhusiana na kunyamaziwa kwa tamko la Ghadir katika maelezo yaliyotangulia.

Na ikiwa Umar anaufahamu undani, mapenzi na mtazamo wa watu hawa sita, basi bila shaka yeye alikuwa kisha mpendekeza Uthman bin Affan kuwa Khalifah au alikuwa anajua kuwa wengi miongoni mwa hawa sita hawamkubali Ali, vinginevyo ni kwa nini na ni kwa haki gani Umar anatilia nguvu upande wa Abdur-Rahman bin Auf dhidi ya Ali bin Abi Talib wakati ambapo Waislamu tangu hapo zamani na mpaka leo wamekuwa wakishindana juu ya ubora wa Ali na Abubakar na hatujamsikia yeyote akimlinganisha Ali na Abdur-Rahman bin Auf.

Na hapa hapana budi nisimame kidogo ili niwaulize Masunni ambao wanatetea msingi wa mashauriano na pia (niwaulize) watu wenye fikra iliyohuru wote kwa ujumla, nawauliza wote hawa, ni vipi mnaafiki baina ya mashauriano kwa maana yake ya Kiislamu na baina ya fikra hii ambayo kama itajulisha kitu fulani basi haitajulisha isipokuwa ni maoni ya ki-dikteta, kwani yeye Umar ndiye aliyewachagua watu hawa sita na siyo Waislamu, na iwapo kuufikia kwake Ukhalifa lilikuwa ni jambo la ghafla, basi ni kwa haki ipi anawalazimisha Waislamu wakubali mmoja wa hawa sita?

Kinachojitokeza kwetu ni kwamba Umar anauona Ukhalifa kuwa ni haki ya Muhajirina peke yao na mwingine yeyote hana haki ya kuwakorofisha kwenye jambo hili, bali zaidi ya hivi ni kuwa Umar anaitakidi kama anavyoitakidi Abubakar kwamba Ukhalifa ni milki ya Maquraish, bali wamo pia wasiokuwa Waarabu, hivyo basi haistahiki kwa Sal-man Al-Farisi wala Ammar bin Yasir wala Bilal wa Uhabeshi wala Suhayb Mrumi, wala Abu Dharri Al-Ghifari wala maelfu ya Masahaba ambao siyo Maquraish (haistahiki kwao) kujitokeza kwa ajili ya Ukhalifa. Na haya siyo madai ya hivi hivi tu sivyo kabisa, bali hiyo ndiyo itikadi yao ambayo historia na wataalamu wa hadithi wameisajili kutoka vinywani mwao (kina Abubakar na Umar) na hebu tuirudie khutba yenyewe ambayo Bukhari na Muslim wameieleza ndani ya Sahih zao:

Umar bin Al-Khatab anasema:

"Nilitaka kusema, na nilikuwa nimetunga vizuri usemi ambao ulinifurahisha nikitaka niutamke mbele ya Abubakr na nilikuwa nikimzunguka karibu. Basi nilipotaka kusema Abubakr akasema, tulia (ewe Umar), na sikupenda kumkasirisha. Abubakar akazungumza, na alikuwa mpole mno kuliko mimi na mtulivu mno, Wallahi hakuacha neno lolote katika maneno nilioyaandaa isipokuwa aliyasema vizuri zaidi mpaka aliponyamaza kisha akasema, nilichokieleza kwenu katika wema ninyi ndiyo mnaostahiki (akiwaambia Maansari) na wala jambo hili halitatambulika isipokuwa kwa upande huu wa Maquraish. Taz: Sahih Bukhar Babul-Wasiyyah.

Kwa hiyo inatubainikia wazi- kwamba Abubakr na Umar hawaamini mashauriano na hiyari, na baadhi ya wanahistoria wanasema kwamba Abubakar alitoa hoja dhidi ya Maansar kwa hadithi ya Mtume (s.a.w.) isemayo kuwa "Ukhalifa uko kwa Maquraish" Na hadithi hiyo hapana shaka ni sahihi (kama walivyoitaja Bukhar na Muslim na Sahih zote kwa Masunni na Mashia) Mtume (s.a.w.) amesema: "Makhalifa baada yangu ni kumi na wawili na wote ni kutoka kwa Maquraishi" na hadithi iliyo wazi zaidi kuliko hii ni ile kauli ya Mtume (s.a.w.) aliposema:

"Jambo hili (la Ukhalifa) halitakoma kwa Maquraish muda wote hata wakibakia watu wawili"[62] pia kauli yake isemayo "Watu ni wafuasi wa Maquraishi katika kheri na shari[63].

Basi ikiwa Waislamu wote wanaziamini hadithi hizi, ni vipi mtu aseme kuwa Mtume aliliwacha suala la Ukhalifa liwe la mashauriano baina ya Waislamu wamchague wamtakaye? Na haiwezekani kwetu sisi kukwepa kupingana huku, isipokuwa tutakapoyachukua maneno ya Maimamu wa nyumba ya Mtume na wafuasi wao na baadhi ya wanachuoni wa Kisunni ambao wanasisitiza kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu aliwataja Makhalifa na akawabainisha kwa idadi yao na majina yao, na hapo ndipo utakapoweza pia kuufahamu msimamo wa Umar na kuuthibiti Ukhalifa kwa Maquraish na huyu Umar ni mtu aliyefahamika kwa Ijtihadi yake dhidi ya maagizo ya Mtume hata katika uhai wake mwenyewe Mtume (s.a.w.), kwani matukio ya Sul-hu ya Hudaybiyah[64] kuwasalia wanafiki,[65] msiba wa siku ya Al-Khamis,[66] na kuzuwiya kwake kubashiria watu pepo[67] ni ushahidi mkubwa wa haya tuyasemayo.

Basi haishangazi kwa Umar kufanya Ij-tihad baada ya kufariki Mtume dhidi ya hadithi inayohusu Ukhalifa, haoni ulazima wa kukubali agizo linalomuhusu Ali bin Abi Talib ambaye ni Quraish, mdogo kwa umri. Ni yeye aliyeidhibiti haki ya kumchagua Khalifa kwa Maquraish peke yao, na ni yeye ambaye alilazimisha peke yake kuchagua watu sita miongoni mwa watukufu wa Kiquraishi kabla hajafa ili ikubaliane kati ya hadithi ya Mtume (s.a.w.) na vile aonavyo yeye juu ya haki ya Maquraishi peke yao kuhusika na Ukhalifa. Huenda kumuingiza Ali katika kundi hilo hali yakuwa akifahamu kwamba wao hawatamchagua, ni udhibiti wake kwa Umma ili amlazimishe Ali kuingia pamoja nao ndani ya mchezo wa Kisiasa kama wanavyouita leo hii na ili pasibakie kwa Ali na wafuasi wake na wapenzi wake ambao walikuwa wakidai kuwa yeye ndiye wa mwanzo (pasibakie kwao) hoja yeyote. Lakini Imam Ali aliyazungumza yote hayo katika hotuba yake mbele ya watu wote akasema kuhusu jambo hilo:

"Nilivumilia muda wote wa taabu na majaribu mpaka alivyoondoka akauweka (Ukhalifa) chini ya maamuzi ya kikundi cha watu sita akidhania kuwa mimi nafanana nao oh! hayawi sawa ya Mungu na mashauriano! Toka lini nikatiliwa mashaka na wa kwanza miongoni mwao mpaka imebidi nilinganishwe na watu kama hawa! lakini nilitua walipotua na niliruka waliporuka (yaani, niliishi nao kwa hekima).

Nne: Hakika Imam Ali (a.s.) alitoa hoja dhidi yao kwa kila namna lakini bila mafanikio, na je, Imam Ali aombe baia ya watu ambao walimgeuzia nyuso zao na nyoyo zao zikawaelekea wengine imma kwa husuda dhidi yake kutokana na yale aliyompa Mwenyezi Mungu miongoni mwa fadhila zake, na imma kwa chuki dhidi yake kwani yeye ndiye aliyewaua mabwana zao, akawabomoa mashujaa wao, akawakatisha tamaa, akawadhalilisha na kuvunja ujeuri wao kwa upanga wake na ushujaa wake mpaka wakasilimu na kujisalimisha hali ya kuwa Imam Ali akiwa ni Mtukufu akimtetea mwana wa ammi yake (Mtume s.a.w.) na alipokuwa akifanya hayo haikumzuwia kuyatenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lawama ya mwenye kulaumu na wala hakurudi nyuma kwenye azma yake kutokana na tamaa ya dunia. Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.) naye alikuwa akiyajua vema hayo na kila tukio alikuwa akitilia mkazo fadhaila za nduguye na mwana wa ammi yake ili kuwafanya wampende. Mtume alikuwa akisema "Kumpenda Ali ni (dalili ya) imani na kumchukia (ni dalili ya) unafiki"[68] Na pia husema "Ali anatokana nami, nami natokana na Ali."[69] Na alikuwa akisema: "Ali ni mtawala wa kila muumini baada yangu"[70] na husema kuwa, "Ali ni mlango wa mji wa elimu yangu na ni baba wa wanangu."[71] Pia Mtume alikuwa akisema, "Ali ni Bwana wa Waislamu na ni Imamu wa wachamungu na ni kiongozi wa waumini wenye kutowa mwanga na nuru."[72]

Lakini inasikitisha kwamba yote hayo hayakuwazidishia isipokuwa chuki na husuda na kwa ajili hiyo Mtume alimuita Ali kabla ya kufariki akamkumbatia kisha akalia na akamwambia: "Ewe Ali bila shaka mimi nafahamu kwamba ndani ya nyoyo za jamaa hawa kuna shinikizo la chuki dhidi yako, na hapo baadaye watakudhihirishia baada yangu mimi, iwapo watakupa baia kubali vinginevyo basi subiri mpaka hapo utapokutana nami hali ya kuwa mwenye kudhulumiwa". Taz: Ar-Riyadun-Naz-Rah Fi Manaqibil-Asharah cha Tabari Babu Fadail Ali ibn Abi Talib. Basi ikiwa Abul-Hasan (a.s.) ilimlazimu kuvumilia baada ya baia ya Abubakr, hilo ni kutokana na usia wa Mtume kwake yeye na ndani ya hilo muna hekima ambayo iko wazi.

Tano: Zaidi ya yote hayo yaliyotangulia ni kwamba, Muislamu ataposoma Qur'an Tukufu na kuzizingatia aya zake, atafahamu kwa kupitia masimulizi yake kuhusu mambo ambayo yaliwafika watu na mataifa yaliyopita kwamba, kwao yalitokea mengi kuliko yale yaliyotokea kwetu sisi. Basi mwangalie huyu Qabil anamuuwa nduguye Habil kwa dhulma na uadui tu, na huyu hapa Nuh ambaye ni babu wa Manabii, baada ya miaka elfu moja ya jihadi hakuna aliyemfuata katika watu wake isipokuwa wachache tu, isitoshe mkewe na mwanawe walikuwa miongoni mwa makafiri.

Mtazame Nabii Lut haikupatikana katika kitongoji chake isipokuwa nyumba moja tu ya Waumini. Nao Mafirauni ambao walikuwa wenye kiburi katika nchi wakawafanya watu kuwa watumwa, hapakuwepo miongoni mwao isipokuwa Muumini mmoja anayeficha imani yake. Hawa hapa nduguze Yusuf watoto wa Yaaqub nao ni kikundi, wanakula njama kumuuwa ndugu yao mdogo asiye na kosa lolote lakini (wanafanya hivyo) kwa kumhusudu kwa kuwa yeye ni kipenzi kwa baba yao. Watazame wana wa Israel ambao Mwenyezi Mungu aliwaokoa kupitia kwa Musa na akawapasulia bahari na kumuangamiza adui yao Firauni na askari wake bila ya kuwakalifisha taabu yoyote ya vita, basi mara walipotoka baharini na nyayo zao hata hazijakauka, wakawafikia watu wanaoabudia sanamu (wana wa Israel) wakasema:

"Ewe Musa tutengenezee Mungu kama wao walivyo na Miungu, Musa akawaambia hakika ninyi ni watu msiojua." Na alipokwenda kwenye ahadi ya Mola wake na kumuacha nduguye Harun, walifanya njama dhidi yake karibu wamuuwe, wakamkufuru Mwenyezi Mungu, na wakamuabudia ndama kisha baadaye waliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema: "Kila walipokufikieni Mitume kwa yale ambayo nafsi zenu haziyapendi mlijivuna, kundi moja mlilipinga na kundi jingine mkaliua".(Qur'an, 2:87)

Huyu hapa naye Bwana wetu Yahya bin Zakariya naye ni Nabii na Mtawa miongoni mwa watu wema anauwawa na kichwa chake anazawadiwa mtu muovu miongoni mwa waovu wa Kibani Israel. Mayahudi na Wakristo nao walikula njama kumuua na kumsulubu bwana wetu Isa. Nao ummati wa Muhammad wanaandaa jeshi la kiasi ya watu elfu thelathini ili kumuuwa kipenzi cha Mtume wa Mwenyezi Mungu na Bwana wa vijana wa peponi ambaye hawakuwa pamoja naye isipokuwa watu Sabini miongoni mwa wafuasi wake, wakawauwa wote ikiwa ni pamoja na mwanawe mchanga. La ajabu ni lipi baada ya yote haya? Lipi litashangaza baada ya kauli ya Mtume kuwaambia Masahaba wake yakuwa: "Mutafuata nyendo za wale waliokuwa kabla yenu shubiri baada ya shubiri na dhiraa baada ya dhiraa mpaka hata wakiingia kwenye shimo la kenge nanyi mutaingia". wakasema, "Wadhani kuwa hao ni Mayahudi na Wakristo"? Mtume akasema, "Ni kina nani basi (kama si hao)"?

Taz: Sahih BukharJuz. 4 uk. 144 na Juz. 8 uk. 151. Ni kipi cha ajabu basi, nasi twasoma ndani ya Bukhar na Muslim kauli ya Mtume (s.a.w.) isemayo: "Siku ya Kiyama Masahaba wangu watapelekwa upande wa kushoto nami nitasema wanapelekwa wapi? Patasemwa Wallahi Motoni, nitasema, Ewe Mola wangu Masahaba wangu hao, patasemwa, Hakika wewe hujuwi waliyoyazusha baada yako, nitasema atengwe mbali aliyebadilisha baada yangu, na sitamuona anaokoka miongoni mwao isipokuwa kikundi kidogo kama cha ngamia waliotelekezwa".

Tax: Sahih Bukhar Juz. 7 uk. 209 na Sahih Muslim Babul-Haudh. Basi lipi la ajabu baada ya kauli yake Mtume (s.a.w.) aliposema: "Umati wangu utagawanyika makundi sabini na tatu na yote yataingia motoni isipokuwa kundi moja". Taz: Sunan Ibn Majah Kitabul-Fitan Juz. 2 hadith Na. 3993, Ahmad Juz. 3 uk. 120, Sunan Tirmidhi Kitabul-Iman. Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu Mola mwenye nguvu na Utukufu, mjuzi wa undani wa nyoyo pale aliposema: "Na watu wengi hawataamini japo utapupia" (Qur'an, 12:103)

"Bali amewajia na ukweli na wengi wao wanaichukia kweli" (Qur'an,23:70)

"Bila shaka tumekujieni na ukweli lakini wengi wenu hawaupendi ukweli" (Qur'an 43:78)

"Fahamuni ya kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli lakini wengi wao hawafahamu" (Qur'an, 10:55)

"Wanakuridhisheni kwa vinywa vyao na nyoyo zao zinakataa, na wengi wao ni mafasiki (Qur'an, 9:8)

"Bila shaka Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru" (Qur'an, 10:60)

"Wanaitambua Neema ya Mwenyezi Mungu kisha wanaipinga na wengi wanakataa ila kukufuru tu" (Qur'an, 25:50)

"Na wengi wao hawawezi kumuamini Mwenyezi Mungu ila hali ya kuwa wanamshirikisha" (Qur'an, 12:106)

"Bali wengi wao hawaijuwi haki basi wao wanapinga" (Qur'an, 21:24)

"Hivi mwashangazwa na mazungumzo haya na mnacheka wala hamlii hali ya kuwa ninyi mmeghafilika (mmejisahau)" (Qur'an, 53:61


4

5

6

7

8

9

10