TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16007
Pakua: 2425


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16007 / Pakua: 2425
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAAS|HIF JUZUU YA TATU

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَاجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رَبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴾

258.Je, hukumjua aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia na huhuisha na kufisha. Ibrahim akasema: Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi. Akafedheheka yule aliyekufuru, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

ALIYEHOJIANA NA IBRAHIM

Aya 258

MAANA

Mwenyezi Mungu, katika Aya iliyotangulia, amebainisha kuwa mtawala wa waumini ni Mwenyezi Mungu, na kwamba wao wanatoka katika giza la shaka kuingia kwenye mwangaza wa uongofu na imani. Na makafiri watawala wao ni mataghuti wanaowatoa kwenye mwangaza wa kimaumbile na kuwaingiza katika giza la ukafiri na upotevu. Baada ya hapo anatoa kisa, kwa Mtume wake mtukufu juu, ya Mumin aliyetoka kwenye giza la shaka na kuingia katika nuru ya imani, katika Aya ijayo. Na kisa cha kafiri aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake baada ya kutoka kwenye nuru ya kimaumbile kwenda kwenye giza la ukafiri, katika Aya hii.

Je, hukumjua yule aliyehojiana na Ibrahim juu ya Mola wake, kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu ni yule ambaye huhuyisha na kufisha. Yeye akasema: 'Mimi pia na huhuyisha na kufisha.'

Hii ni hoja anayoitaja Mwenyezi Mungu kwa Mtume na kwa watu wote katika mfumo wa kustaajabu pamoja na kukanusha. Ibrahim(a.s) alitoa mwito wa kutupiliwa mbali masanamu na mataghuti na kuwa kwenye dini ya uadilifu na usawa, lakini akapingwa na watawala., sio kwa kuona mwito wake sio sawa, bali ni kwa kuhofia manufaa na chumo lao na kupupia wasishuke vyeo vyao. Kama kawaida walianza kujadiliana na Ibrahim kwa maneno; waliposhindwa wakawa hawana la kusema, ispokuwa walitangaza vita na wakajaribu kummaliza kwa kumchoma katika moto; sawa na wanavyofanya wakoloni hivi sasa - wanaeneza propaganda za upotevu kwa njia ya magazeti, radio na mashirika ya habari yaliyonunuliwa; wakishindwa wanaanza kampeni za mapinduzi, wakishindwa hutupa mabomu ya Napalm kwa watu wanyonge wasiokuwa na hatia yoyote.

Basi yule ambaye amepetuka mpaka kwa mali na jaha alimuuliza Ibrahim: "Ni nani Mola wako?" Ibrahim akajibu: "Mola wangu ni yule anayempa uhai anayemtaka kisha huuondoa na wala hana anayeshirikiana naye katika hilo." Yule Taghuti akasema: "Mimi pia ninaweza hivyo." Akawaleta watu wawili; akamwua mmoja wao na kumwacha mwingine. Ibrahim alipoona kujigamba kwa Taghuti kwa kutegemea, maneno na kujitia kutofahamu hoja na maana halisi yaliyokusudiwa, alileta mfano mwingine ambao hauwezi kuingizwa makosa wala madai yoyote, akasema:

Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua Mashariki, basi wewe lichomoze Magharibi, Akafedheheka yule aliyekufuru

Kwa sababu alishindwa kubabaisha na kupotosha. Hivi ndivyo anavyojaribu kufanya kila mbatilifu - kujisifu na kufanya hila; hila zinaposhindwa hudangana akawa hana la kufanya. Kundi la wafasiri wamesema kuwa ni jawabu la pili la Ibrahim; la kwanza ni 'Ambaye huhuisha na kufisha' na la pili ni 'Basi wewe lichomoze magharibi' ili akate mjadala upesi bila ya kurefusha.

Razi na Sheikh Muhmmad Abduh, wanasema kuwa hilo ni kuleta mfano mwingine ili kufafanua zaidi dalili; kwa maana yakuwa yule ambaye anatoa uhai ndiye ambaye analichomoza jua kutoka mashariki; na kama ukiweza kuwafunika watu wako kwa mfano wa kwanza basi utashindwa kuwafunika katika mfano huu. Vyovyote itakavyokuwa, iwe ni majibu mawili au mifano miwili, lakini ni kwamba kafiri alishindwa na kuzibwa mdomo; na alishindwa kwa vile hana haki, naye hana haki, kwa vile ni kafiri.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu

Ambao wamejidhulumu kwa kuinusuru batili na kuipinga haki. Aya haikutaja jina la Taghuti kwa sababu, muhimu ni kupata mazingatio ya kisa sio jina la mhusika. Imetangaa kwamba alikuwa ni Namrud bin Kan'an bin Sam bin Nuh. Inasemekana kwamba yeye ndiye wa mwanzo kuvaa taji kichwani; akatakabari na kudai uungu. Tutarudia kuelezea kisa cha Ibrahim na watu wake katika Sura ya Anbiya (Mitume) na sehemu nyinginezo.

﴿أَوْ كَالَّذِي مَرَّ عَلَىٰ قَرْيَةٍ وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا قَالَ أَنَّىٰ يُحْيِي هَـٰذِهِ اللَّـهُ بَعْدَ مَوْتِهَا فَأَمَاتَهُ اللَّـهُ مِائَةَ عَامٍ ثُمَّ بَعَثَهُ قَالَ كَمْ لَبِثْتَ قَالَ لَبِثْتُ يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ قَالَ بَل لَّبِثْتَ مِائَةَ عَامٍ فَانظُرْ إِلَىٰ طَعَامِكَ وَشَرَابِكَ لَمْ يَتَسَنَّهْ وَانظُرْ إِلَىٰ حِمَارِكَ وَلِنَجْعَلَكَ آيَةً لِّلنَّاسِ وَانظُرْ إِلَى الْعِظَامِ كَيْفَ نُنشِزُهَا ثُمَّ نَكْسُوهَا لَحْمًا فَلَمَّا تَبَيَّنَ لَهُ قَالَ أَعْلَمُ أَنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

259.Au kama yule aliyepita karibu na mji nao umeangukiana sakafu zake, akasema: Mwenyezi Mungu atauhuisha vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia, kisha akamfufua, akamuuliza: Umekaa muda gani? Akasema: Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika. Na mtazame punda wako na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua,kisha tunaivisha nyama. Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.

ALIYEPITA KARIBU NA MJI

Aya ya 259

MAANA

Aya iliyotangulia ilikuwa ni mfano kwa kafiri ambaye amemfanya Taghuti kuwa ni mlinzi na mtawala wake, na kutoka katika mwangaza na kuingia katika giza; na Aya hii ni mfano wa Mumin aliyemfanya Mwenyezi Mungu kuwa mtawala wake; akatoka gizani na kuingia katika mwangaza.

Au kama yule aliyepita karibu na mji nao umeangukiana sakafu zake akasema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakufafanua jina la mji wala jina la aliyepitia, Hapo ndipo wakahitalifiana wafasiri - kwamba je, mtu huyo alikuwa kafiri, je alikuwa Uzairi (Ezra), Armila (Nehemia) au Khidhr? Vile vile wametofautiana kuhusu mji,je ulikuwa Baitil Maqdis au mji mwingine? Hakuna dalili yoyote juu ya hayo isipokuwa Hadith za Kiisrail tu. Maana ya mji ulioangukiana sakafu zake ni kuwa hauna watu na majumba yamevunjika umebaki magofu; na swali lilikuwa la kuuliza kufufuliwa watu wa mji sio mji wenyewe.

Yule anayedai kuwa aliyepita katika mji alikuwa kafiri kwa vile alitia shaka katika kudura ya Mwenyezi Mungu, tunamwambia kuwa, sio kila anayepitiwa na shaka akilini mwake na akataka ufafanuzi, ni kafiri; bali ni kinyume cha hivyo. Ibrahim alimtaka Mola wake amuonyeshe anavyohuisha waliokufa na hali yeye alikuwa akilingania imani na yakini. Zaidi ya hayo ni kwamba kutaka kujua zaidi kudura ya Mwenyezi Mungu ndio imani yenyewe. Kwa hivyo basi linabainika kosa la anayedai kuwa aliyepita mjini alikuwa kafiri sio kwa jengine ispokuwa tu, ati amesema: Mwenyezi Mungu ataufufua vipi (mji) huu baada ya kufa kwake? Hapana! Huko sio kukanusha, isipokuwa kubomoka huko alikokuona kulimfanya apigwe na butwaa na kushindwa kujua njia ambayo itawarudishia uhai watu wa mji huo.

Mwenyezi Mungu akamfisha kwa miaka mia.

Hayo yalikuwa ni mauti ya hakika sio majazi, Hapo hapahitaji taawil.

Kisha akamfufua

Alimfufua kama alivyokuwa. Wala si zito hilo kwa ambaye anauambia ulimwengu na kilicho katika ulimwengu 'kuwa', kikawa. Hakuna kitu cha ajabu kabisa kama kumlinganisha Muumbaji na viumbe katika uwezo Wake.

HISABU YA KABURINI

Akamuuliza: Umekaa muda gani?

Hili ni swali la kuthibitisha, sio la kutaka kufahamu.

Akasema: Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku.

Lau si Ijmai (kongamano la wanavyuoni) na hadithi ingeliwezekana kusema kuwa hakuna hisabu kaburini wala kuulizwa, isipokuwa siku ya ufufuo kwa kutegemea Aya hii na Aya nyingine inayosema:

﴿وَيَوْمَ تَقُومُ السَّاعَةُ يُقْسِمُ الْمُجْرِمُونَ مَا لَبِثُوا غَيْرَ سَاعَةٍ﴾

"Na siku kitakaposimama kiyama wataapa wenye makosa kuwa hawakudumu isipokuwa saa moja tu ..." (30:55)

Wala hakuna sababu ya wakosaji kuapa na kughafilika na muda uliopita toka kufa kwao isipokuwa kwa kukosa uhai, kwa sababu kuhisi muda hakuwi isipokuwa mtu huyo awe na uhai. Sheikh Mufid katika kitabu Awailul Maqalat anasema kwamba, watu baada ya kufa wako tabaka nne: Tabaka ya kwanza ni yule aliyeijua haki na akaitumia, Huyu atapewa uhai mzuri baada ya mauti kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya pili ni yule aliyeijua haki na asiitumie kwa inadi. Huyu vile vile atakuwa hai lakini ataadhibiwa, Tabaka ya tatu ni yule aliyefanya madhambi na maasi kwa kupuuza, sio kwa inadi. Huyu uhai wake ni wenye kutiliwa shaka baada ya kufa na kabla ya kufufuliwa. Tabaka ya nne ni wenye kuzembea kufanya twaa bila ya inadi na walio wanyonge. Hawa hawatafufuliwa, bali watabaki katika ulimwengu wa mauti mpaka siku ya kufufuliwa.

Sheikh Mufid amechukua ugavi huu kutokana na riwaya za Ahlul bait(a.s) ; miongoni mwa hizo ni: "Hataadhibiwa kila maiti, isipokuwa ataadhibiwa kwa ukafiri hasa na atapata neema kwa imani hasa; na wasiokuwa hawa wawili watapuuzwa na wala hawataulizwa mpaka siku ya ufufuo. "Haya tumeyazungumza kwa ufafanuzi katika kitabu Falsafatul Mabdai Wal Ma'ad mlango wa "Baina ya dunia na akhera" na mlango "Hisabu ya kaburi"

Akasema: Bali umekaa miaka mia, tazama chakula chako na kinywaji chako hakikuharibika.

Amesema hakikuharibika na hakusema havikuharibika, kwa maana ya kuwa chakula na kinywaji ni aina moja tu katika kuharibika haraka. Maana ya hakikuharibika ni kwamba havikubadilika, pamoja na kupita miaka, bali vimebakia katika hali yake. Huu ni muujiza wa Mungu, kwa sababu chakula na kinywaji huharibika haraka. Hapa nahofia yule anayejaribu kuiambatanisha Qur'an na sayansi asije akasema kuwa vilikuwa katika jokofu (friji).

Na mtazame punda wako

Jinsi alivyogeuka na kuoza, lakini chakula na kinywaji vimebakia katika hali yake.

Huu ndio muujiza zaidi na kudhihirisha kudura inavyogeuza kawaida. Kwa sababu anga ndiyo inayoathiri, kinywaji kingeharibika kabla ya punda, kwa sababu ndiye mwenye nguvu kuliko chakula na kinywaji. Kwa hivyo kufa punda na kudumu chakula, ni dalili ya kuwa Mwenyezi Mungu hashindwi na kitu chochote.

Inasemekana kuwa punda alibakia hai miaka mia bila ya kinywaji wala chakula, Kwa hali zote mbili, ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliyafanya hayo ili aondoe kustaajabu kwa Uzayr na kuona kwake ajabu ya kufufuliwa kwa mji huo; na pia ili amfanye kuwa ni hoja ya kupatikana ufufuo kwa yule atakayejua hali yake katika watu wa wakati huo. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): "Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu"

Na itazame mifupa jinsi tunavyoinyanyua, kisha tunaivisha nyama

Wamehitalifiana kuhusu mifupa hii: Je ilikuwa ya Uzair au mifupa ya punda wake? Msemaji mmoja alisema kwamba hiyo ni mifupa ya mwenye punda, na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifufua jicho lake kwanza ili aone sehemu iliyobakia ya mwili jinsi inavyokusanyika na kupata uhai. lakini huku ni kujisemea tu juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu. Lenye nguvu zaidi ni kwamba hiyo ni mifupa ya punda kwa sababu mwenye punda alisema: "Nimekaa muda wa siku moja au sehemu ya siku." Kwani lau angeliiona mifupa yake ilivyoharibika, angelitambua urefu wa muda aliokaa Mwenyezi Mungu aliivika nyama; sawa na alivyoanza kumuumba. Imam Ali(a.s) anasema:"Kuisha dunia baada ya kuweko sio ajabu kuliko kuianzisha."

Basi yalipombainikia alisema: Najua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

Aliyasema haya baada ya kupitiwa na majaribio binafsi yasiyo na shaka. Vipi atie shaka na yeye ameshuhudia kwa macho miujiza mitatu: Kurudishwa hai baada ya kufa, kufufuliwa punda wake na kudumu chakula chake miaka mia bila kuharibika. Funzo tunalolipata kutokana na kisa hiki ni kwamba mwenye akili hatakikani kukanusha lile lisilotambuliwa na akili yake, au lisiloafikiana na aliyoyasoma katika kitabu au kusikia kutoka kwa mwalimu wake, bali inatakikana ajizuie hata lile analoona linatofautiana na kanuni za kimaumbile.Elimu imethibitisha kuwa hakuna kanuni ya maumbile kabisa.

﴿وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴾

260.Na Ibrahim aliposema: Mola wangu! Nionyeshe jinsi unavyofufua wafu, (Mwenyezi Mungu) akasema: Huamini? Akasema: Kwa nini! (naamini) Lakini upate kutulia moyo wangu. Akasema: Basi chukua ndege wanne na uwakusanye kisha (uwachinje) uweke juu ya kila jabali sehemu katika wao. Kisha waite, watakujia mbio. Na jua kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

ILI MOYO WANGU UTULIE

Aya 260

MAANA

Maana ya Aya iko wazi, lakini wafasiri wanataka kupata sababu ya kusema kwa hali yoyote itakayokuwa. Kwa hiyo wakaulizana sababu iliyomfanya Ibrahim kuuliza hivi, pamoja na kujua kwamba yeye anaamini ufufuo kwa imani isiyo na shaka yoyote. Kisha wakahitalifiana katika jawabu lake kwa kauli kumi na mbili alizozitaja Razi Utafiti wao hauna msingi wowote, kwa sababu kuamini ghaibu hakupingani na kutaka kushuhudia kwa macho. Kwani kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na yaliyokuja katika vitabu vyake katika habari za ghaibu, anatamani kushuhudia kwa macho yale aliyoyaamini kwa njia ya ghaibu na wahyi, isipokuwa Ali bin Abu Twalib aliyesema:"Lau nitaondolewa pazia siwezi kuzidisha yakini (yangu)" Vyovyote iwavyo Khalilurrahman (rafiki wa Mwenyezi Mungu)(a.s) aliamini ufufuo kwa imani ya ghaibu kwa njia ya wahyi, kama Mitume wengine; kisha akapenda kushuhudia tukio kwa macho yake baada ya kushuhudia kwa moyo wake na akili yake. Kwa hilo zitatimia kwake njia zote za maarifa - kwa moyo, akili na majaribio. Mwenyezi Mungu alilikubali ombi lake, akamwamrisha kuchukua ndege wane, awakusanye pamoja kisha awakatekate aweke fungu juu ya kila jabali; kisha awaite, watamjia haraka kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Tunalomalizia katika Aya hii ni kwamba: kutaka kufunuliwa siri ya uumbaji au ufufuo mara nyingine kunatokana na kutia shaka kwenye jambo hilo. Huko ndiko kunakopingana na kuamini kudura ya Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na wahyi Wake na Mitume Yake. Mara nyingine kunatokana na kupenda kujua mambo na kupata maarifa pamoja na kuamini kudura ya Muumbaji na kuwa na imani na Mitume; hata kama hakuona jinsi Mwenyezi Mungu anavyofufua watu; kama ilivyokuwa kwa Ibrahim. Ombi hili halidhuru imani, lakini ni vigumu kulipata, bali haiwezekani, isipokuwa kwa Mtume, kama Ibrahim ambaye imani yake haitingishiki kwa kitu chochote, hata kama Mwenyezi Mungu hangemwitikia maombi yake. Kwa hivyo basi atakayeshartisha majaribio na kuona kuwa ndio sharti la kuamini kwake ufufuo, basi yeye ni kafiri kabisa. Lau angelikuwa ni mwenye kuamini kudura ya Mwenyezi Mungu kweli, asingelikuwa na haja ya sharti hili, kwa sababu kudura yake Mwenyezi Mungu haishindwi na kitu chochote mbinguni wala ardhini.

﴿مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّائَةُ حَبَّةٍ وَاللَّـهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ﴾

261.Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba; katika kila shuke pana punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mjuzi.

﴿الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ثُمَّ لَا يُتْبِعُونَ مَا أَنفَقُوا مَنًّا وَلَا أَذًى لَّهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

262.Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu kisha wasifuatishie kile walichotoa na masimbulizi wala udhia, wao wana ujira wao kwa Mola wao, wala hawatakuwa na hofu, wala hawatahuzunika.

﴿قَوْلٌ مَّعْرُوفٌ وَمَغْفِرَةٌ خَيْرٌ مِّن صَدَقَةٍ يَتْبَعُهَا أَذًى وَاللَّـهُ غَنِيٌّ حَلِيمٌ ﴾

263.Kauli njema na kusamehe ni bora kuliko sadaka inayofuatishiwa na udhia na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Mpole.

PUNJE MOJA INAYOTOA MASHUKE SABA

Aya 261 263

MAANA

Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an na kuzingatia maana zake atazikuta kuwa zinatilia umuhimu misingi mitatu:

Kueneza mwito wa Kiislamu, Jihadi na kutoa mali katika njia ya Mwenyezi Mungu. hiyo ni kwamba misingi hii mitatu ina athari kubwa katika kuupa nguvu uislamu na kuenea kwake. Kwa hivyo Qur'an imehimiza misingi hiyo kwa mifano mbalimbali ya kupendekeza na kutisha. Zimeshatangulia Aya kadhaa za kuhimiza Jihadi na kutoa mali, na zitakuja nyingine. Hivi sasa mbele yetu kuna zaidi ya Aya kumi zinazozungumzia kutoa mali; katika hizo kuna zinazomwahidi mtoaji badali ya mia saba au zaidi; nyingine zinakataza kufuatishia sadaka kwa masimbulizi na udhia; pia kuna nyingine zinazoamrisha kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa nia safi, na zinazoelezea kuwa kutoa kuwe kumetokana na chumo halali na zuri, sio chumo la haramu na baya n.k.( [4] )

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba; katika kila shuke pana punje mia, Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa Mjuzi.

Wameulizana wafasiri, vipi Mwenyezi Mungu amepigia mfano punje inayotoa mazao haya na inajulikana kuwa haiko? Baadhi yao wakajibu kwamba hilo ni fumbo la wingi, sio kitu hasa. Wengine wamesema kuwa hayo ni makadirio; kwamba mwenye akili akijua kuwa punje yake itamletea mia saba, basi atatoa bila ya kusita. Hapana shaka kuwa wafasiri wameuweka mbali sana mfano huu, kwa vile wao wamelinganisha kilimo kilivyokuwa wakati wao; ambapo hakukuwa na zana zozote zaidi ya ng'ombe, punda na jembe la mkono. Lau wengelikuwa wakati huu wasingeona ajabu yoyote katika mifano ya Mwenyezi Mungu, baada ya elimu kuingia katika kila kitu na zana na pembejeo za kilimo zinazotumiwa.

Zaidi ya hayo kutoa kwa Mola hakupungui wala hakudhibitiki. Kwa hiyo ongezeko la mia saba sio kiwango cha mwisho cha fadhila zake na kutoa Kwake. Kwa ajili hiyo ndipo akasema:"Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye" Kama ambavyo ongezeko la mia saba linaweza kuzidi, basi vile vile linaweza kupungua, kulingana na hali ya kutoa kwenyewe. Huenda shillingi moja anayoitoa mtu na huku anaihitaji ikawa bora mbele za Mwenyezi Mungu kuliko shilingi elfu zinazotolewa na aliyetosheka nazo. Vile vile shilingi moja inayotolewa kwa ajili ya kuinua haki, dini na maadili, au inayotolewa katika manufaa ya watu na kuwatoa katika dhulma na ufukara, shilingi hiyo ambayo athari yake itabaki na manufaa yake kudumu muda mrefu, ni bora mara millioni kuliko maelfu yanayotumiwa katika anasa na maarusi ya watoto.

Wale wanaotoa mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wasifuatishie kile walichotoa na masimbulizi wala udhia, wana ujira wao kwa Mola wao.

Mwenye Majmaul Bayan amesema: "Kusimbulia ni kumwambia uliyempa: Je, sikukufanyia wema? Au je, sikukupa? Na adha ni kusema: "Mwenyezi Mungu anipumzishe kwa kuniepusha nawe na aniondolee balaa kwa ajili yako." Maana ni kuwa, kutoa kunakobadilishiwa ziada na Mwenyezi Mungu, ni kule ambako mwelekeo wake ni kwa Mwenyezi Mungu peke Yake, sio kwa kutaka umashuhuri na kujionyesha na kuaibisha, kwa sababu hilo linabatilisha thawabu.

Kauli njema na kusamehe ni bora kuliko sadaka inayofuatishiwa na udhia.

Kauli njema ni maneno yanayokubaliwa na nyoyo. Makusudio ya kusamehe hapa ni kumsamehe mwenye kuomba ikiwa anaomba kwa lazima, au kutoa ufedhuli ikiwa mtu hakupata alichoomba; kama ilivyo kwa baadhi ya waombaji. Yaani kumkabili muombaji kwa maneno mazuri na kuwa na subira naye, ni bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko kutoa kwenye kukabiliana na maudhi. Mtume(s.a.w.w) anasema:"Muombaji akiomba msimkate maneno mpaka amalize, kisha mjibuni kwa upole; ama iwe ni kumpa (japo) kichache au kumwambia vizuri"

Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi.

Wa sadaka zote na twaa, na sisi ni mafukara tunaohitaji msaada wake, upole wake na thawabu zake.

Mpole

Hafanyi haraka kutoa adhabu katika maisha haya, isipokuwa anamwacha muasi mpaka siku isiyokuwa na shaka.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُبْطِلُوا صَدَقَاتِكُم بِالْمَنِّ وَالْأَذَىٰ كَالَّذِي يُنفِقُ مَالَهُ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ صَفْوَانٍ عَلَيْهِ تُرَابٌ فَأَصَابَهُ وَابِلٌ فَتَرَكَهُ صَلْدًا لَّا يَقْدِرُونَ عَلَىٰ شَيْءٍ مِّمَّا كَسَبُوا وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴾

264.Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia; kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu; wala hamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likafikiwa na mvua kubwa na ikaliacha tupu. Hawana uwezo wa chochote katika walivyovichuma; na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

﴿وَمَثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمُ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ وَتَثْبِيتًا مِّنْ أَنفُسِهِمْ كَمَثَلِ جَنَّةٍ بِرَبْوَةٍ أَصَابَهَا وَابِلٌ فَآتَتْ أُكُلَهَا ضِعْفَيْنِ فَإِن لَّمْ يُصِبْهَا وَابِلٌ فَطَلٌّ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴾

265.Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikafikiwa na mvua kubwa ikatoa mazao yake maradufu; na isipofikiwa na mvua kubwa, basi manyunyu (huitoshea), Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayotenda.

MUSIHARIBU SADAKA ZENU

Aya 264 -265

MAANA

Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na udhia; kama yule anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha kwamba kuacha kusimbulia na kuudhi ni sharti la kupatikana malipo na thawabu katika kutoa; na kukosa kutoa sadaka na kauli njema ni bora kuliko kusimbulia na kuudhi, vilevile kwamba mwenye kutoa bila ya masimbulizi na udhia, atapewa malipo na thawabu bila ya hisabu; Akapigia mfano hilo kwa punje moja inayomrudishia mkulima punje mia saba. Baada ya kubainisha haya yote anampigia mfano, katika Aya hii mwenye masimbulizi na adha kuwa sawa na mnafiki anayejionyesha, ambaye anatoa mali yake kwa kutaka sifa kwa watu, sio kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake.

Wala hamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Yaani kitendo cha ria (kujionyesha) ni sawa na cha kafiri, kwa sababu wote hao hawataki radhi ya Mweneyzi Mungu. Kwa ajili hiyo ndipo zikaja Hadith Mutawatir kwamba: ria ni shirk iliyojificha.

Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likafikiwa na mvua kubwa na ikaliacha tupu. Hawana uwezo wa chochote katika walivyovichuma.

Mwenyezi Mungu kwanza amemfananisha mwenye kusimbulia anayeudhi na mnafiki anayejionyesha; kisha akamfananisha na jabali ambalo juu yake pana udongo. Kwa dhahiri ni kwamba shabihi wa shabihi ni shabihi, kama vile rafiiki wa rafiki. Kwa hiyo inakuwa, mwenye kusimbulia anayeudhi, mnafiki na mwenye kuudhi na mwenye kujionyesha ni sawa na udongo juu ya jabali, na adha na ria ni kama mvua ambayo inaondosha udongo huo.

Na kauli ya Mwenyezi Mungu:"Hawana uwezo wa chochote." Maana yake ni kuwa: kama ambavyo hakuna yeyote katika viumbe anayeweza kurudisha udongo huo, vile vile hawawezi wenye kujionyesha na wenye kuudhi kurudisha sadaka zao. Makusudio ni kwamba: wao hawatanufaika nayo katika dunia, kwa sababu imekwishawatoka mikononi mwao; wala hawatanufaika nayo katika akhera kwa kuharibiwa na adha na ria.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri

Makusudio ya kuongoza hapa, ni thawabu ya akhera, kwa sababu maneno yanahusu thawabu ya Mwenyezi Mungu, Na makusudio ya makafiri ni kila anayefanya amali kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuna Hadith tukufu inayosema;"Kitakapokuwa Kiyama, atanadi mnadi: 'wako wapi wale waliokuwa wakiwaabudu watu? Simameni mchukue malipo yenu kwa wale mliokuwa mkiwatumikia, kwa sababu mimi sikubali amali iliyochanganyika na kitu chochote katika dunia na watu wake.'"

Na mfano wa wale wanatoa mali zao kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao, ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu, ikafikiwa na mvua kubwa ikatoa mazao yake maradufu, na kama isiponyeshewa na mvua kubwa, basi manyunyu (huitoshea).

Baada ya Mwenyezi Mungu kupiga mfano wa sadaka ya wenye kujionyesha na wenye kuudhi, amepiga mfano, katika Aya hii, sadaka ya mwenye kujitakasa; kama iliyo kawaida ya Mwenyezi Mungu kuleta mkabali wa vitu viwili vilivyo kinyume.

Ikiwa sadaka ya hao ni kama jabali lililofunikwa na mchanga, basi sadaka ya hawa ni kama bustani iliyo katika sehemu za miinuko, iliyojaa udongo ambao hauhofiwi kumomonyoka na kuondoka; sio kama ilivyo hali ya mchanga kidogo kwenye jabali; bustani hii huzaa matunda katika mwaka mara mbili zaidi ya inavyozaa bustani ya kawaida, wala haikauki kamwe kutokana na udongo wake ulivyo mzuri; inatosheka na mvua ndogo tu, kwa sababu ya rutuba yake na mazingira yake mazuri. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu:"Kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu na uimara wa nafsi zao," ni kuonyesha mambo mawili:

Kwanza : waumini wanataka radhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na kutoa.

Pili : kutoa huku kunatokana na msukumo wa nafsi zao wenyewe na wala sio msukumo unaotoka nje.

Inasemekana kwamba uimara wa nafsi zao ni kwa maana ya kwamba wao wanajitahidi kutii kwa kutoa. Maana haya yanaweza kuwa sawa ikiwa herufi Min hapa iko katika maana ya Lam; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿مِّمَّا خَطِيئَاتِهِمْ أُغْرِقُوا ﴾

"Kwa ajili ya makosa yao waligharikishwa ..." (71:25)

Baada ya hayo yote, Aya mbili hizi ni katika muujiza wa fasihi ambao huwezi kuupata mahali pengine isipokuwa katika maneno yake Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Kwanza, sadaka ya adha na sadaka ya ria ameifananisha na udongo ulioko kwenye jabali ambao unaondolewa na upepo na mvua. Kisha katika mkabala wa sadaka ya hasara, amefananisha na sadaka ya faida - sadaka ya imani, nayo ni kama bustani yenye rutuba inayotoa mazao kila mwaka, iwe na mvua nyingi au kidogo.

﴿أَيَوَدُّ أَحَدُكُمْ أَن تَكُونَ لَهُ جَنَّةٌ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ لَهُ فِيهَا مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَأَصَابَهُ الْكِبَرُ وَلَهُ ذُرِّيَّةٌ ضُعَفَاءُ فَأَصَابَهَا إِعْصَارٌ فِيهِ نَارٌ فَاحْتَرَقَتْ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَتَفَكَّرُونَ ﴾

266.Je, mmoja wenu anapenda kuwa na kitalu cha mitende na mizabibu ipitayo mito kati yake, naye humo hupata mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia, kisha ana watoto walio dhaifu; mara kifikiwe na kimbunga chenye moto kiungue? Hivi ndivyo anavyowabainishia Mwenyezi Mungu ishara ili mpate kufikiri.

JE, MMOJA WENU ANAPENDA…?

Aya ya 266

MAANA

Aya hii inamwambia kila mwenye kufanya amali na akaifuatishia na jambo litakaloondoa malipo yake na thawabu zake; kama vile masimbulizi, udhia, kujionyesha, ukafiri na shirk. Hali ya kila mmoja katika hawa ni sawa na mwenye shamba analopatia manTafsir ufaa yeye na watoto wake, likapatwa na janga kubwa, likaangamia wakati ambapo analihitajia sana kutokana na uzee wake na udhaifu wa watoto wake ambao hawajaweza kujitegemea; na wala hana kitu kingine zaidi ya shamba hilo. Mfano huo ni kwamba mwenye kufanya heri, akaiharibu, siku ya Kiyama atakuwa na haja sana ya thawabu za amali alizozifanya, lakini atakuta amali zake zimekwenda bure, kwa vile alipokuwa akizifanya, hakukusudia radhi ya Mwenyezi Mungu; na wakati huo hataweza kufanya lolote; sawa na mzee aliyeunguliwa shamba lake baada ya kuwa mzee, naye ana watoto wanyonge wanaolihitajia. Kwa mfano huu ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):

Na uzee ukamfikia, kisha ana watoto walio dhaifu; mara kimbunga chenye moto kikifikie kiungue?

Wafasiri wanasema imehusisha kutajwa mitende na mizabibu, kwa sababu ndio matunda mazuri kwa manufaa ya kiafya, ladha na mandhari pia. Lakini jibu hilo lilikuja katika wakati walioishi ambapo hapakuwa na matofaha, Matunda damu wala Machungwa au miwa. Lau wangelikuwa wakati huu wangelisema kuwa zimetajwa kwa sababu ni matunda bora ya wakati huo. Kwa hali hiyo inatubainikia kwamba hukumu juu ya vitu vya mazingira inapasa iwe kwa kulingana na kufungamana na wakati na mahali. Unaweza kuuliza: Je, maneno hayapingani kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): "kitalu cha mitende na mizabibu." na kauli yake: "Naye humo hupata mazao ya kila namna?" (sasa je ni mitende na mizabibu iliyomo au mazao mengine?)

Jibu : Inawezekana kuwa mitende na mizabibu ndiyo mingi zaidi katika kitalu; au inawezekana vilevile kuwa makusudio ya mazao ni manufaa, kwa maana ya kuwa mwenye shamba anapata manufaa yake yote na faida.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَنفِقُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا كَسَبْتُمْ وَمِمَّا أَخْرَجْنَا لَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَلَا تَيَمَّمُوا الْخَبِيثَ مِنْهُ تُنفِقُونَ وَلَسْتُم بِآخِذِيهِ إِلَّا أَن تُغْمِضُوا فِيهِ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ حَمِيدٌ ﴾

267.Enyi mlioamini! Toeni katika vizuri mlivyovichuma na katika vile tulivyowatolea ardhini; wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, Mwenye kusifiwa.

﴿الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ وَاللَّـهُ يَعِدُكُم مَّغْفِرَةً مِّنْهُ وَفَضْلًا وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴾

268.Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili; na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha utokao kwake na fadhila na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu, Mjuzi.

KUTOA KATIKA VIZURI

Aya ya 267 - 268

MAANA

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuhimiza sadaka katika Aya iliyotangulia na kubainisha ambayo anapaswa kusifika nayo mwenye kutoa sadaka, ikiwa ni pamoja na kumtakasia Mwenyezi Mungu katika sadaka yake na kujiepusha na ria, masimbulizi na kuudhi, sasa anataja sifa za sadaka yenyewe - kwamba inatakiwa iwe inatokana na mali nzuri na sio chafu. Hapo ndipo itakuwa sadaka imekamilika kwa njia zake. Mwenyezi Mungu anasema:

Enyi mlioamini! Toeni katika vizuri mlivyovichuma na katika vile tulivyowatolea kutoka ardhini

Lau tukiangalia Aya hii kwa dhahiri bila ya kuangalia Hadith za Mtume zilizobainisha wajibu wa kimali na kuweka kiwango cha kiasi chake na matumizi yake na pia aina yake, tungelifahamu kwamba katika mali yote anayochuma mtu kuna haki ya Mwenyezi Mungu ambayo anapaswa kuitoa kwa ajili ya radhi yake Mwenyezi Mungu (s.w.t), kwa sharti ya kutoa kizuri katika anavyovimiliki sio vibaya. Aya iliyo wazi zaidi ya hii ni ile inayosema:

﴿لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ﴾

"Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda ..." (3: 92)

Kutoa huku ni wajibu katika mali yote; ni sawa iwe imetokana na ufundi, biashara au kilimo. Vilevile urithi, madini au kitu kingine chochote, Haya ndiyo yanayofahamishwa na matamko ya Aya. Kwa sababu kutoa kumekuja kwa tamko la amri ambayo inafahamisha wajibu. Kauli yake Mwenyezi Mungu: "Katika vizuri mlivyovichuma" inakusanya uchumi wote; na kauli yake; Na katika vile tulivyowatolea kutoka ardhini" inakusanya mimea, madini na siku hizi petroli.

Lakini Hadith za Mtume - ambazo ni tafsiri na ubainifu wa Qur'an hasa Aya za hukumu za sheria - zimeweka kiwango cha mali ya Zaka au Khums, vile vile nadhiri au kafara. Zikabainisha kiasi cha kutoa na wanaopewa. Wanavyuoni wa kifiqh wamelieleza hilo kwa ufafanuzi katika mlango wa Zaka, Khums, kafara na nadhiri. Kwa hiyo Aya itakuwa ni ya kuleta sharia hiyo ya kutoa na kutilia mkazo; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ﴾

"Na simamisheni Swala na toeni Zaka ..." (2:110)

Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya

SABABU YA KUSHUKA AYA

Inasemekana kuwa sababu ya kushuka Aya ni kwamba baadhi ya Waislamu walikuwa wakitoa sadaka zile tende mbovu. Na jumla hii ni kutilia mkazo jumla ya kwanza ambayo ni "toeni katika vizuri." Kwa ujumla ni kuwa toeni vizuri na wala msitoe vibaya. Mafaqihi wametoa fatwa kwamba mwenye kumiliki aina ya mali ambayo baadhi yake ni nzuri na baadhi ni mbaya, haijuzu kwake kutoa mbaya, bali atatoa ile yenye uzuri wa wastani. Kama akichagua ile ya hali ya juu, basi ni bora zaidi. Lakini kama mali yote ni mbaya inajuzu kutoa mali mbaya kwa sababu haki inafungamana na dhati ya kitu kinachotolewa.

Hali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho.

Hii ni hoja fasaha kwa yule anayetoa sadaka mbaya, Imam Ali(a.s) anasema:"Kama unavyofanya nawe utafanyiwa." Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili. Maana ya kuwatisha na ufukara ni kuwatia wasiwasi wa kuwa na pupa na kuhofia kutoa, kuwa kunaleta ufukura na hali mbaya. Maana ya kuamrisha ovu ni kuhadaa kwa kutia kwake wasiwasi kufanya maasi na kuacha utii; kama vile ubakhili.

Na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha utokao kwake na fadhila.

Mwenye kutoa vizuri katika mali yake kwa kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t), Mwenyezi Mungu amemuahidi mambo mawili:

Kwanza : kusamehe makosa yake mengi kama alivyosema:

﴿خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا ﴾

"Chukua sadaka katika mali zao, uwatakase na uwasafishe kwazo..." (9:103)

Pili : kumlipa kheri zaidi mwenye kutoa kuliko alichokitoa - Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴾

"... Na chochote mtakachokitoa, basi Yeye atakilipa naye ni mbora wa wanaoruzuku" (34:39)

Miongoni mwa maneno ya hekima ya Imam Ali(a.s) ni:"Sadaka ni dawa yenye kuokoa," "Takeni riziki kwa sadaka" na"Fanyeni biashara na Mwenyezi Mungu kwa sadaka." Ilipokuwa roho ya dini inatawala kwenye nafsi na kwenye mwelekeo wa malezi na tabia za watu, ilikuwa baba anampa mtoto wake pesa na kumwamrisha kutoa sadaka kwa fukara kwa kuitakidi kwamba sadaka itamwandalia njia ya tawfik na kufaulu.