TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 30%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17915 / Pakua: 3852
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

1

2

3

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿يُؤْتِي الْحِكْمَةَ مَن يَشَاءُ وَمَن يُؤْتَ الْحِكْمَةَ فَقَدْ أُوتِيَ خَيْرًا كَثِيرًا وَمَا يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ﴾

269.Humpa hekima amtakaye. Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili.

HEKIMA

Aya 269

MAANA

Neno Hekima hutumiwa kwa maana nyingi, kama vile maslahi; mfano: "Hekima ya kitu hiki ni jambo fulani." Maana nyingine ni mawaidha; mfano: Hekima ni kitu (anachotafuta) kilichompotea "mumin," Pia lina maana ya elimu na fahamu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu (s.w.t.):

﴿وَلَقَدْ آتَيْنَا لُقْمَانَ الْحِكْمَةَ﴾

"Na hakika tulimpa Lukmani hekima ..." (31:12)

Maana nyingine ya neno hekima ni Utume, Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ ﴾

"....Na tukampa hekima na kukata hukumu." (38:20)

Vilevile neno hili linatumiwa kwa maana ya elimu ya Falsafa. Msemaji mmoja amesema: "Hekima ni elimu ya Fiqh", mwengine amesema ni elimu zote za kidini, watatu akasema ni kumtii Mwenyezi Mungu tu.

Vyovyote ilivyosemwa au itakavyosemwa, ni kwamba neno hekima haliwezi kutoka kwenye maana ya usawa na kukiweka kitu mahali pake kwa kauli na vitendo. Kwa hivyo mwenye hekima ni yule anayekihukumu kitu na kukileta kwa mujibu wa akili na hali ilivyo, sio kwa mujibu wa mapendeleo na matakwa. Kitu hicho hawezi kukifanyia haraka kabla ya muda wake au kukizuilia na wakati wake au kukipeleka kombo na mipaka yake. Kwa hali hiyo basi, hekima haihusiki na mitume na mawalii tu au na wanafalsafa na wataalamu tu, bali kila mwenye kufanya vizuri amali yoyote na akaiweka sawa, basi huyo ni mwenye hekima katika amali hiyo; awe ni mkulima au mfanyakazi, mwajiri au mwajiriwa. Vilevile ni sawa awe ni muhuburi, malenga, hakimu au askari, n.k. Sharti la kwanza na la mwisho la hekima ni kuthibiti lengo la kitendo kiakili, kisharia, kidunia na kidini.

Hapana mwenye kutia shaka kwamba ambaye hekima ni mwongozi wake atakuwa mwema katika nyumba mbili (duniani na akhera). Imam Jaffar Sadiq(a.s) anasema:"Hakumneemesha Mwenyezi Mungu mja neema kubwa na tukufu zaidi kuliko hekima. Mwenyezi Mungu anasema:

"Na aliyepewa hekima hakika amepewa heri nyingi na hawakumbuki ila wenye akili"

Yaani hajui yeyote siri ya hekima aliyoitoa Mwenyezi Mungu, isipokuwa mwenye kumtakasia Mwenyezi Mungu nafsi yake.

Hekima ni uongofu, ni uthabiti wa vianzio vya mambo na ni kituo cha mwisho wa mambo."

Hapa inaonyesha kuwa kuna tofauti kati ya elimu na hekima. Elimu ni kujua mambo na mfungamano uliopo wa mambo hayo; vile vile kujua athari yake ya kheri au ya shari. Ama hekima inaamrisha akili kufuata usalama, kufuata dini iliyo sawa na kukitumia kitu mahala pake, palipoumbwa kwa ajili yake. Mfano elimu inatengeza chembechembe za bomu na kutengeneza maroketi, lakini haiangalii lengo lake, la kheri au la shari; wala haikatazi hili na kuamrisha lile. Lakini hekima haijishughulishi na utafiti wa mabomu na uvumbuzi wa maroketi hayo isipokuwa inaangalia matumizi ya maroketi hayo na kumwelekeza binadamu lile litakalo mfanya kupata kheri na ufanisi sio uovu.( [5] )

﴿وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴾

270. Chochote mtoacho, au nadhiri mnazoweka, basi Mwenyezi Mungu anakijua, Na madhalimu hawana wasaidizi.

﴿إِن تُبْدُوا الصَّدَقَاتِ فَنِعِمَّا هِيَ وَإِن تُخْفُوهَا وَتُؤْتُوهَا الْفُقَرَاءَ فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَيُكَفِّرُ عَنكُم مِّن سَيِّئَاتِكُمْ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴾

271.Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; Na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mnayoyatenda.

CHOCHOTE MTOACHO

Aya 270-271

MAANA

Tena amerudia Mwenyezi Mungu kutaja kutoa na kukutilia mkazo kwa kusema:

Chochote mtoacho au nadhiri mnazoweka basi Mwenyezi Mungu anakijua

Neno: kutoa linakusanya kila kinachotolewa; kiwe cha wajibu au suna, kingi au kichache cha utii au maasi na kisiri au kidhahiri. Maana ya nadhiri kilugha ni ahadi; na kisharia ni kujilazimisha mtu kutenda jambo fulani au kuliacha kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Tamko lake ni kusema yule mwenye kuweka nadhiri: "Ni juu yangu kufanya jambo fulani kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, "Haitoshi kukusudia tu, bila ya kusema, wala kusema bila ya kumtaja Mwenyezi Mungu au kutaja mojawapo ya majina yake matukufu. Lau anasema: "Nimeweka nadhiri kufanya kitu fulani likiwa jambo fulani", hiyo haiwezi kuwa nadhiri kwa kutokuwa na jina la Mwenyezi Mungu.

Vilevile nadhiri haiwezi kuwa kabisa, ikiwa imefungamana na jambo la haramu au makuruhu. Wakati wa Mtume(s.a.w.w) mtu mmoja aliweka nadhiri ya kusimama tu bila ya kukaa wala kuwa kivulini, akiwa amefunga na asizungumze na mtu; Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akasema: "Mwamuruni azungumze akae kivulini na aendelee na Saumu yake." Maana ya "Mwenyezi Mungu anakijua" ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua lengo lolote la kutoa litakalokuwa na kulipatia malipo; ikiwa ni heri basi ni heri na kama ni shari basi ni shari tu.

Na madhalimu hawana wasaidizi

Makusudio ya madhalimu ni wote bila ya kuvua, wakiwa ni pamoja na wale wasiotoa chochote au wanaotoa vibaya au kwa ria. Vilevile wale wanaotoa kwa masimbulizi na adha au kuweka pasipokuwa mahali pake. Wengine ni wale wanaovunja ahadi na wasiotekeleza nadhiri. Wote hawa na walio mfano wao hawatakuwa na wasaidizi wala waombezi watakaowazuiilia na mateso ya Mwenyezi Mungu.

Kama mkizidhihirisha sadaka ni vizuri.

Yaani hakuna umakuruhu katika kudhihirisha sadaka maadam makusudio yake ni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Imam Jaffar Sadiq aliulizwa kuhusu mtu anayefanya jambo la kheri,watu wakamwona akafurahi. Imam akasema:"Hapana ubaya; kila mtu anapenda kuonekana na watu kwa kheri, ikiwa hakufanya hilo kwa ajili ya huko kuonekana."

Na kama mkitoa kwa siri na kuwapa mafukara, basi hivyo ni bora zaidi kwenu.

Hapana shaka kwamba kuficha sadaka ni bora kuliko kuidhihirisha, kwa sababu kunakuwa mbali na shubuha ya ria na kudhihirisha haja ya mafukara mbele ya watu. Huwa mara nyingine kudhihirisha sadaka kuna maslahi; kwa mfano ikiwa ni kwa kutaka kutoa mfano kwa wengine, hapo kudhihirisha kutakuwa bora zaidi. Inasemekana kuwa kuificha sadaka ya sunna ni bora kuliko kuidhihirisha; na kinyume chake kwa sadaka ya wajibu. Hatujui hoja ya ufafanuzi huu na Hadith ya "Sadaka ya siri inazima ghadhabu ya mola" inakusanya ya wajibu na suna; kama ambavyo Aya inakusanya fukara mwislamu na asiyekuwa mwislamu. Mafaqihi wametoa fatwa ya kutoa sadaka ya sunna kwa asiyekuwa mwislamu akiwa ni muhitaji kutokana na kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu:"Kulinywesha kila ini la joto kuna malipo, Na yatawaondokea baadhi ya maovu yenu.

Neno: Min hapa ni baadhi, kwa sababu sadaka haifuti madhambi yote isipokuwa inafuta baadhi tu.

Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda

Maadam Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua siri, sawa na anavyojua dhahiri, basi siri ni bora, kwa sababu hilo liko mbali na ria, isipokuwa kama katika kudhihirisha kuna maslahi; kama kuwaonyesha mfano wengine ili watende. Na wenye ikhlasi wengi wanaficha sadaka zao; wanajitolea kwenye mambo ya kheri kwa majina ya watu wengine wema.

﴿لَّيْسَ عَلَيْكَ هُدَاهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَهْدِي مَن يَشَاءُ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَلِأَنفُسِكُمْ وَمَا تُنفِقُونَ إِلَّا ابْتِغَاءَ وَجْهِ اللَّـهِ وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ﴾

272.Si juu yako kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye. Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa kwa ajili ya nafsi zenu, wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

﴿لِلْفُقَرَاءِ الَّذِينَ أُحْصِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ ضَرْبًا فِي الْأَرْضِ يَحْسَبُهُمُ الْجَاهِلُ أَغْنِيَاءَ مِنَ التَّعَفُّفِ تَعْرِفُهُم بِسِيمَاهُمْ لَا يَسْأَلُونَ النَّاسَ إِلْحَافًا وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴾

273.Ni kwa ajili ya mafukara waliozuiliwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia. Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'anga' nia. Na mali yoyote mnayoitoa, kwa hakika Mwenyezi Mungu anaijua.

﴿الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُم بِاللَّيْلِ وَالنَّهَارِ سِرًّا وَعَلَانِيَةً فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴾

274.Wale watoao mali zao usiku na mchana kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala wao hawatahuzunika.

SI JUU YAKO KUWAONGOZA

Aya 272- 274

MAANA

Si juu yako kuwaongoza,lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye.

Yametangulia maelezo katika Aya ya 26 ya Sura hii kwamba neno Huda (uongofu) linatuTafsir miwa kwa maana nyingi; miongoni mwayo ni ubainifu na (uongofu), hiyo ni kazi ya Mtume. Maana nyengine ni tawfiki kutoka kwa Mwenyezi Mungu ya kuandalia njia ya kufanya kheri; nyingine ni kuongoka, yaani kukubali nasaha na kuzitumia, huku kunategemezwa kwa mja. Pia neno hilo lina maana ya thawabu na mengineyo. Maana ya uongofu katika "Si juu yako kuwaongoza" ni kuongoka na kukubali nasaha; yaani, kuitumia kwao haki si juu yako wewe, isipokuwa ni juu yako kufikisha haki tu.

﴿فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ﴾

"... Basi juu yako ni kufikisha na juu yetu ni hisabu" (13:40)

Maana ya uongofu katika;"Lakini Mwenyezi Mungu humwongoza amtakaye" ni tawfiki katika njia ya kheri.

Inasemekana kuwa sababu ya kushuka"Si juu yako kuwoangoza" ni kwamba waislamu walikuwa hawatoi sadaka isipokuwa kwa watu wa dini yao, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume Wake kwa Aya hii na akataka kuwabanishia waislamu wote kwamba kafiri haadhibiwi kwa sababu ya kufuru yake kwa kunyimwa riziki na kudhikishwa ili alazimike kuamini; na haifai kwa yeyote kufanya hivyo hata kama ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.

﴿أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ﴾

"...Basi je wewe utawalazimisha ili wawe waumini?" (10:99).

Aya inafahamisha kwamba sadaka ya sunna au ya wajibu inajuzu kuwapa wasiokuwa waislamu, lakini kauli ya Mtume(s.a.w.w) :"Nimeamrishwa kuchukua sadaka kutoka kwa matajiri wenu na kuitoa kwa mafukara wenu", inahusu sadaka ya sunna tu sio ya wajibu.

Na mali yoyote mnayoitoa ni kwa ajili ya nafsi zenu.

Huenda mtu akadhania kuwa kutoa ni hasara kwake na ni kuwanyima watoto wake na ndugu zake. Ndipo Mwenyezi Mungu akaondosha dhana hii, kwamba mwenye kutoa inamrudia yeye kheri na nafuu katika dunia na akhera. Katika akhera atapata malipo na thawabu. Ama katika dunia, Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Kutoa kunazuia mafukara kuwafanyia ubaya matajiri, kwa sababu mafukara wakiwa na dhiki, watakwenda kuwaibia matajiri, kuwaudhi na kuwanyang'anya. Kisha uovu wao huu unawaendea wengine; mara nyingine ufisadi huo huenea kwa ujumla na kuondoa raha na amani." Sijui kama Sheikh Muhammad Abduh ameitoa fikra yake hii kutoka vyama vya wafanyakazi ambavyo vimewaletea matatizo matajiri na kuwalazimisha kukubali haki nyingi za wafanyakazi.

Wala hamtoi ila kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Yaani: maadamu mnakusudia radhi ya Mwenyezi Mungu katika kutoa kwenu, basi Mwenyezi Mungu atakubali. Ni sawa muwe mumempa mwislamu au asiyekuwa mwislamu kwa sharti ya kuwa iwe ni mali nzuri sio mbaya. Pia kusiweko na masimbulizi na maudhi. Inasemekana kuwa Aya ina maana ya kukataza kwa njia ya kutolea habari; yaani msitoe isipokuwa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu.

Na mali yoyote mnayoitoa mtalipwa kwa ukamilifu wala hamtadhulumiwa.

Hata kutoa kukiwa kwa asiyekuwa mwislamu, lakini hamtapunguziwa chochote katika malipo, ikiwa mliyempa ni muhitaji.

WATU WA SUFA (UPENUNI)

Kuna jamaa waliohamia Madina, wakiacha miji yao mali zao na watu wao. Hapa Madina hawakuwa na maskani yoyote wala jamaa na hawakuwa na nyezo za kujichumia maisha, wala hawakuweza kusafiri kutafuta riziki. Idadi yao ilikuwa watu mia tatu, wengine wanasema ni mia nne. Wakawa wako msikitini tu, wakiabudu na kuzilinda nyumba za Mtume. Pia walikuwa wakijifundisha Qur'an na kuihifadhi, jambo ambalo lilikuwa ni katika twaa bora zaidi, kwa sababu huko ni kuihifadhi dini. Wakati huo huo walikuwa wakitoka pamoja na Mtume katika kila vita. Walikuwa wakikaa upenuni mwa msikiti ndio maana wakaitwa watu wa upenuni (Ahlu Sufa). Mtume(s.a.w.w) , alikuwa akiwahimiza na kuwaambia:"Furahini enyi watu wa Suffa; yeyote atakayekuwa na sifa mlizo nazo nyinyi katika umma wangu, basi yeye ni katika marafiki zangu."

Hao ndio wanaofaa zaidi kupewa sadaka; Kwa sababu wao ndio walioshukiwa na Aya hii:

Ni kwa ajili mafukara waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu, wasioweza kwenda huku na huko katika ardhi. Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia. Utawafahamu kwa alama zao; hawaombi watu wakang'ang'ania.

Mwenyezi Mungu katika Aya hii amewataja watu wa Sufa kwa sifa tano:-

1. Kujitolea kwa Jihadi na kutafuta elimu. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu "waliozuiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu", kwa sababu mvivu hawezi kuambiwa kuwa ameifunga nafsi yake katika njia ya Mwenyezi Mungu.

2. Kushindwa kuchuma: ndiyo makusudio ya kusema kwake: "Wasioweza kwenda huku na huko."

3. Kujizuia, Mwenyezi Mungu anasema: "Asiyewajua hali zao anawadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia."

4. Kuonekana kuwa ni mafukara kwa hali yao tu, sio kwa sababu ya kuombaomba: ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Utawafahamu kwa alama zao."

5. Kuacha kuomba vilivyo mikononi mwa watu kwa kunga'ang'ania: Kwenye hilo Mwenyezi Mungu ameashiria kwa kusema "Hawaombi watu wakang'ang'ania". Tumetaja katika tafsiri ya Aya ya 177 katika Sura hii, kwamba kuomba bila ya dharura ni haram.

Wale watowao mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Mwenyezi Mungu ametaja hukumu ya kutoa katika Aya kumi na nne mfululizo, ya mwisho ikiwa ni hii ambayo ni muhtasari wa yaliyotangulia na kutilia mkazo fadhila ya kutoa katika nyakati zote, iwe ni usiku au mchana, na kwa siri au kwa dhahiri. Razi ametaja kauli nyingi katika sababu za kushuka Aya hii, miongoni mwa hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba Ali bin Abu Twalib(a.s) alikuwa na dirham nne tu, akatoa kwa siri na nyingine kwa dhahiri, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii.

ZAKA

Zaka sio sadaka ya sunna, kwa sababu sadaka huitoa mwislamu kwa hiyari, wala haihitaji kufikia kiwango fulani na haina jengine zaidi ya kukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu peke Yake; na malipo yake yanaanzia maradufu ya kumi hadi maradufu ya mia saba na zaidi ya hapo, kiasi ambacho hakina mwisho kulingana na lengo la kutolewa kwake. Ama Zaka, ni faradhi, ni haki ya lazima katika mali ya kiwango fulani na hutolewa kwa anayestahiki. Ni ya tatu katika nguzo tano za uislamu ambazo ni: Shahada mbili, Swala, Zaka, Saumu na Hijja. Baadhi ya wenye ghera na uislamu wanaona kuwa Zaka ni mpango wa uchumi au ni utaratibu fulani wa kiuchumi wa kiislamu. Wengine wanaichukulia kuwa ni kodi ya mali za matajiri. Ukweli ni kwamba Zaka si kodi au mpango fulani wa kiuchumi. Kwa sababu sharti ya msingi ya kukubaliwa Zaka, ni nia ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, bila hivyo haikubaliwi kabisa. Na kodi au utaratibu wa kiuchumi hauzingati sharti hii.

Zaidi ya hayo, utaratibu wa kiuchumi, kwa maana ya kisasa, kwanza unaangalia nyezo za uzalishaji; kama vile ardhi, madini na viwanda. Mfumo wa kibepari unazingatia kuwa ni milki ya mtu binafsi anayeimiliki. Ama mfumo wa kijamaa unazingatia kuwa ni milki ya umma inayoongozwa na serikali. Na Zaka haiangalii haya kabisa, Ama kodi nayo inasimamiwa na kiongozi wa nchi katika kupatikana kwake na kuitoa; haiwezekani kwa mtoaji kwa hali yeyote kuacha kuitoa kwa kiongozi, ambaye ndiye mwenye uwezo wa kuitumia. Mafaqihi wote wanasema kuwa mwenye kumiliki mali anaweza kutoa Zaka bila ya idhini ya kiongozi, naye anaweza kuaminiwa, bila ya ushahidi wowote au kiapo, akisema kuwa amekwishatoa. Sasa Zaka na kodi ni wapi na wapi? Bali mafaqihi wamejuzisha kwa mkusanyaji Zaka kuitoa kwa mafukara yeye mwenyewe bila ya kuipeleka kwenye Baitul Mal (hazina ya Waislamu).

Imam Ali(a.s) alimwambia mmoja wa wanaokusanya Zaka:"Tumia mali uliyonayo kwa wenye watoto wanaohitaji na wenye njaa." Kwa dhahiri ni kwamba kodi haina matumizi haya kabisa. Mtu anaweza kusema: Faradhi ya zaka maana yake ni kukubali kwamba ufukara lazima uwepo, na kwamba uislamu unaukabili ufukara kwa sadaka, jambo ambalo natija yake ni kuweko tabaka ya utajiri na umasikini?

Jibu : Matumizi ya Zaka hayakufungika kwa fakiri na maskini tu, isipokuwa katika jumla ya matumizi yake ni maslahi ya umma, ambayo Mwenyezi Mungu ameyaeleza kwa ibara ya sabilillah (njia ya Mwenyezi Mungu) katika Aya nyingi. Kwa hiyo kama hakukupatikana fukara, basi Zaka hutumiwa katika njia hii. Kwa hali hiyo, Zaka hailazimishi kuweko fukara kwa namna yoyote, wala Zaka sio ikrari ya kusema ufukara ni chapa isiyoepukika.

Pili : wajibu wa jamii ni kuwatunza masikini ili wasiwe ombaomba na wazururaji. Jambo hili

linapatikana hata katika miji ya kijamaa ambayo haikubali utabaka. Tatu: Tutamfanyaje mgonjwa asiyeweza hata kununua dawa na mwenye njaa ambaye hana njia yoyote ya kupata chakula katika jamii inayoongozwa na ufisadi. Je tuache mpaka hali itakapokuwa nzuri na umasikini utakapoondoka? Au tuweke kanuni itakayodhamini maisha yao? Je, inawezekana kupatikana mabadiliko kwa msitari wa kalamu? bila ya kupitia vipindi vingi? Hakika Uislamu unapiga vita aina zote za unyonge,na Mtume(s.a.w.w) aliutolea mawaidha, Baadhi ya riwaya zinasema:"Ufukara unakurubia kuwa kufuru". "Mwislamu mwenye nguvu ni bora kuliko mnyonge" Ujumbe wa Mwenyezi Mungu una lengo la heshima ya mtu na utengeneo wake; na ufukara ni upungufu na madhila na ni mashaka na balaa, Kwa hivyo haiwezekani uislamu kuukubali. uislamu haukatai kuweko katika jamii tajiri na tajiri zaidi au mwenye nguvu na mwenye nguvu zaidi, isipokuwa unachokataa ni kuweko fukara na mnyonge. Uislamu haukuweka Zaka kwa ajili ya masikini tu kama inavyodhaniwa bali ni kwa kutatua matatizo mengi, ukiwemo umasikini kama upo. Vilevile utumwa, ambapo unapatiwa uhuru na mali ya Zaka. Matatizo mengine ni kuhudumia askari wanaopigana Jihadi, na mengineyo katika maslahi ya umma; kama vile kujenga shule, hospitali, barabara na miradi ya maji.

Tutaeleza ufafanuzi wa matumizi ya Zaka katika Sura ya (9:60) Inshallah. Lau tunakadiria kuwa mtu ataweza kupitiwa na wakati ambao hauna masikini na mahitaji yote ya umma yametoshelezwa, kiasi ambacho matumizi ya Zaka hayatapatikana kabisa, basi bila shaka itaachwa. Na wakati huo utafika tu; kama ilivyokuja Hadith katika Sahih Bukhari Juzuu ya 9 mlango wa Fitan; anasema Mtume(s.a.w.w) : "Toweni sadaka, utakuja wakati mtu atatemebea na sadaka yake asipate wa kuikubali." Zaidi ya hayo, uislamu umemwajibishia mtoaji Zaka wakati anapompatia muhitaji kutomuudhi na kutomvunjia heshima yake na asikwaruze hisia zake. Kwamba huko kutoa ni wajibu wake na ni deni ambalo hapana budi kulitekeleza. Kwa kutilia mkazo maana haya Qur'an inasema:

﴿وَالَّذِينَ فِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ مَّعْلُومٌ ﴿٢٤﴾ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ ﴾

"Na ambao katika mali yao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye na anayezuilika kuomba." (70: 24 - 25)

Yamekwishatangulia maelezo katika tafsiir ya Sura hii Aya (262-263) kuhusu kuudhi, Pamoja na kuwa Uislamu umezishinda sheria zote za dini zingine na za kufanywa na watu kwa kuweka sheria hii ya Zaka sheria hii ya kibinaadamu ambayo hawakuigundua waweka nidhamu ispokuwa baada ya Uislamu kwa mamia ya miaka na kuiita 'dhamana ya jamii', pamoja na yote hayo jambo bora zaidi kuwapa wahitaji katika mtazamo wa kiislamu, ni kuwaandalia kazi inayonasibiana na uwezo wao ili wahisi thamani ya uhai. Mwenyezi Mungu humpenda mja wake mumin anayejishughulisha na kazi. Mwisho tunamaliza maelezo haya kwa kauli ya Imam Ja'far Asswadiq(a.s) :"Kila kiungo katika viungo vyako kina Zaka ya Mwenyezi Mungu: Zaka ya jicho ni kuzingatia na kulifumba na mambo ya haramu, Zaka ya sikio ni kusikiliza elimu na hekima, Zaka ya ulimi ni kumshukuru Mwenyezi Mungu na kuwapa nasaha Waislamu, Zaka ya mkono ni kutoa na Zaka ya mguu ni kuhangaikia jihadi na kusuluhisha watu."

﴿الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا فَمَن جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَانتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّـهِ وَمَنْ عَادَ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾

275.Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu. Hayo ni kwa sababu wanasema kuwa biashara ni kama riba. Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba. Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, akakoma, basi yake ni yaliyokwishapita na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

﴿يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ ﴾

276.Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyae dhambi.

﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ لَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

277.Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَذَرُوا مَا بَقِيَ مِنَ الرِّبَا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾

278.Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

﴿فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا فَأْذَنُوا بِحَرْبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَإِن تُبْتُمْ فَلَكُمْ رُءُوسُ أَمْوَالِكُمْ لَا تَظْلِمُونَ وَلَا تُظْلَمُونَ ﴾

279.Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

﴿وَإِن كَانَ ذُو عُسْرَةٍ فَنَظِرَةٌ إِلَىٰ مَيْسَرَةٍ وَأَن تَصَدَّقُوا خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴾

280.Na kama ana dhiki, basi angoje mpaka awe na uwezo. Na kama deni mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

﴿وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ﴾

281.Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma; nao hawatadhulumiwa.

Aya 275 - 281

MNASABA

Maudhui ya sadaka na riba yote ni mali, ingawa kuna tofauti ambayo ni: Sadaka hutolewa bila ya kutaka kurudishiwa; ni tohara, safi na dhamana. Ama riba ni kutoa kwa kutaka kurudishiwa mali pamoja na ziada; ni tamaa, uchoyo, uchafu, unyang'anyi na maangamizo. Kwa hiyo maudhui ni sawa, lakini hukumu na lengo ni kinyume kabisa. Ikiwa vitu hutajwa kwa mifano yake basi pia hutajwa kwa vinyume vyake, Ndio maana ikaja hukumu ya riba mara tu baada ya hukumu ya sadaka (Zaka). Kabla ya kuingilia kufasiri Aya, tutaanza kuonyesha riba inavyoeleweka katika sharia, dalili ya uharamu wake na yanayo sababisha uharamu.

NENO RIBA

Neno: 'riba' katika lugha maana yake ni ziada; kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu katika Sura (22:5). Katika sharia, riba inagawanyika kwenye mafungu mawili: Riba ya kukopesha na riba ya kuzidishiana katika bei. Maana ya riba ya kukopesha, ni mtu kumkopesha mwingine kitu chochote na kumlazimisha yule aliyemkopesha manufaa yoyote kwa sababu ya kumkopesha; kama vile kukopesha shillingi kumi kwa sharti ya kurudishiwa kumi na moja. Au kwa yasiyokuwa manufaa ya mali; kwa mfano mkopeshaji kumshurutisha aliyemkopesha amfanyie kazi fulani au amwazime kitabu au kitu chochote. Mtume(s.a.w.w) anasema:"Kukopesha kokote kunakovutia manufa ni haramu." Hapo hakutofautisha aina ya manufaa. Hata hivyo kama mkopaji akilipa deni pamoja na ziada ya ahsante, itafaa kwa mkopeshaji kuichukua. Mtume(s.a.w.w) alikuwa akilipa deni pamoja na ziada, akisema:"Bora ya watu ni yule anayewakopesha watu vizuri."

Inatakikana tuzingatie kuwa riba inathibiti katika kukopesha kwa kushurutisha ziada na manufaa kwa namna yoyote ile ya ziada, ni sawa iwe ziada ya kipimo cha mizani ujazo, urefu au idadi. Vilevile ni sawa iwe ni katika namna ya mali iliyokopeshwa au namna nyingine. Kwa maneno mengine riba ya kukopesha haina tofauti katika dhati ya kitu kwa kitu au manufaa.

Ama riba ya bei ni kuzidishiana kitu kil kile, na masharti yake ni mawili:

Kwanza: ni kupeana kwa ziada aina hiyo hiyo kwa jina lake la uhakika, kama kuuza ngano kwa ngano, au kuuza ngano nzima kwa unga wa ngano, kwa sababu unga umetokana na ngano nzima. Vilevile Wanga (nishaa) na unga, kwani vyote viwili vimetokana na asili moja ambayo ni ngano.

Dalili ya pili ni kuwa wanavyouziana viwe vinaweza kupimwa kwa ujazo au mizani tu. Kwa hiyo hakuna riba kwa vinavyouzwa kwa idadi; kama mayai. Inawezekana kuuzwa yai moja kwa mawili. Pia hakuna riba kwa kinachouzwa kwa kuonyeshana; kama nguo na wanyama. Kwa ufupi ni kwamba riba ni haramu katika deni kwa namna yoyote ile, na katika bei ni haramu kwa vinavyopimwa kwa namna yoyote, kwa sharti ya kuwa vyote viwili viwe ni jinsi moja. Hayo tumeyafafanua zaidi katika kitabu chetu Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq(a.s) Mlango wa Riba.

UHARAMU

Riba ni haramu kwa nukuu ya Qur'an, Hadith mutawatir na kongamano la Waislamu wote, tangu siku za Mtume(s.a.w.w) mpaka leo. Bali uharamu wake hauhitaji dalili, kwa sababu ni katika mambo yaliyo wazi; kama vile wajibu wa Swala na uharamu wa zina. Kwa sababu hiyo ndipo mafaqihi wakahukumu kwamba mwenye kukanusha uharamu wa riba, basi ni kafiri, kwa vile amekanusha dharura ya dini iliyothibiti. Kama ilivyo haramu kuchukua riba, pia ni haramu kuitoa. Hadith ya Mtume inasema:"Ameilaani Mwenyezi Mungu riba, mwenye kuila, mwenye kuuza, mwenye kununua, mwandishi wake na shahidi wake."

SABABU YA HARAMU

Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu, kwamba Yeye ndiye mwenye kuweka sharia ya halali na haramu, basi hawezi kutaka mengi zaidi ya wahyi katika kuharamishwa riba. Na kama ikitokea kuuliza sababu, basi haulizi kwa sababu ya kujikinaisha, isipokuwa ni kwa kutaka kufahamu tu; au kwa ajili ya kuwakinaisha wale walioelezewa na Aya hii:

﴿وَإِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَحْدَهُ اشْمَأَزَّتْ قُلُوبُ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ وَإِذَا ذُكِرَ الَّذِينَ مِن دُونِهِ إِذَا هُمْ يَسْتَبْشِرُونَ ﴾

"Na anapotajwa Mwenyezi Mungu pekee yake, mioyo ya wale wasioamini akhera huchafuka, na wanapotajwa wale asiyekuwa yeye wanafurahi." (39:45).

Vyovyote iwavyo ni kwamba wametaja sababu kadha za kuharimishwa riba. Miongoni mwa sababu hizo ni kama ifuatavyo:- Kupingana na misingi ya kibinadamu; kama vile kufanyiana wema, kusaidiana na kuoneana huruma. Kuwa hiyo riba maana yake ni kula mali ya batili, Kwa sababu mwenye kula riba anaichukua bila ya kufanya lolote. Mtu anaweza kusema kuwa anayechukua riba hufanya kitu, kwa sababu mali yake anaitoa kwa aliyekopa ambaye anaitumia na kunufaika nayo. Kwa hivyo hali ya riba ni sawa na kukodisha ardhi, nyumba au mnyama.

Mtu akisema hivyo tutamjibu: Kuna tofauti kubwa kati ya kukodisha na riba, kwani mwenye kukodisha hana jukumu la kulipa kile alichokikodisha, kama kikifa au kikihariibika, isipokuwa kama yeye ndiye aliyesababisha. Lakini chenye kukopwa kikiharibika,basi mwenye kukopa atakilipa. Kwamba mwenye kuchukua riba hupata faida daima na mwenye kukopa hupata hasara; matokeo yake, matunda yote yanaishia kwa mchukuaji riba Baadhi ya maprofesa wa mambo ya uchumi wa Ulaya wameijua aibu hii. Miongoni mwa hao wataalamu ambao wameinukia katika nidhamu za riba, ni Dkt. Schacht, Mjerumani, Meneja wa zamani wa Benki alisema katika mhadahara alioutoa Damascus mnamo mwaka 1953:

"Tukifanya mahesabu tutajua kuwa mali yote katika dunia inaishia kwenye idadi ndogo sana ya wanaokula riba. Hiyo ni kwa sababu anayekopesha kwa riba, daima hupata faida katika kila kitu, wakati ambapo mwenye kudaiwa kwa riba anatazamia kupata faida na hasara; hatimaye ndipo mali yote inaishia kwa yule mwenye uhakika wa faida, Nadharia hii iko njiani kuthibitika. Kwani wenye mali humiliki maelfu ya pesa. Ama wenye milki wote, na wenye viwanda ambao wanakopa kutoka katika mabenki, n.k. hawana lolote isipokuwa ni waajiriwa tu, wakiwatumikia wenye mapesa ambao wanachukua matunda ya jasho lao." Kuna baadhi ya wataalamu wa kiuchumi waliothibitisha kwamba msingi na asili ya fikra ya riba unatokana na mayahudi, na watu wengine wamechukua fikra hiyo kutoka kwao, hayo hayako mbali, kwani historia ya mayahudi wa kale na wa sasa inathibitisha kuwa Mungu wao, dini yao heshima ya siasa yao ni mali tu peke yake haina mshirika; na njia yoyote ya kuleta mali ni tukufu, hata kama ni umalaya, ukuwadi, uasi, wizi, unafiki au ria na uovu wowote ule.

MAANA

Ambao wanakula riba, hawainuki, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu.

Shetani hamzugi yoyote, wala hana uwezo wowote wa kumfanya mtu kuwa mwenda wazimu. Isipokuwa hiyo ni tash'bihi na kuleta karibu ufahamu wa watu wanaosema kuhusu mtu aliiyepatwa na wazimu: "Amepagawa na Shetani." Maana ya Aya ni kwamba hali ya wanaofanya riba, ni sawa na hali ya mwenda wazimu ambaye amezugwa, katika matendo yake, na kuwa shaghalabalaghala. Imepokewa Hadith kutoka kwa Ibn Abbas kuwa watu wa riba watafufuka kutoka makaburini mwao kama wenda wazimu, hiyo itakuwa ndio alama yao kwamba wao ni wala riba.

Hayo ni kwa sababu wamesema kuwa biashara ni kama riba.

Wamehalalisha riba kwa kuleta falfasa ya kuwa biashara na riba zinafanana kwa njia zote; basi kwa nini riba nayo isiwe halali? Si mtu anaweza kuuza kitu cha thamani ya shilling tano kwa shilingi sita na kwamba mtu anaweza kuuza kwa bei ya taslim shilingi moja tu na kwa mkopo shiling mbili? Kwa hiyo, eti inatakikana kuweko na ruhusa ya mtu kutoa shilingi kumi mpaka mwezi ujao kwa shilingi kumi na moja. Mwenyezi Mungu anayajibu madai haya kwa kusema:

Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na ameharamisha riba.

Njia ya majibu hayo ni kuwa, kule kufanana kwa kidhahiri hakufanyi kuwa ndio kufanana kabisa. Kwani biashara ni kazi ya kibiashara yenye kutafuta manufaaa; mwuzaji anakuwa kati ya kupata faida na hasara, kwa hivyo faida yake ni mavuno ya taabu yake, na wala sio kula mali ya batil, ambapo riba ni faida tu na kuchukua ziada bila ya jasho, kwa hiyo inakuwa ni kula mali ya batili.

Kwa ajili hiyo ndio Mwenyezi Mungu akahalalisha biashara na akaharamisha riba.

Basi kutofautiana kihukumu ni dalili ya kutofautiana kihali na kinyume chake.

Na aliyefikiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake, kisha akakoma, basi yake ni yaliyokwisha pita.

Yaani aliyekuwa amechukua riba, kabla ya kuteremshwa Aya ya kuiharamisha kisha akaacha baada ya kuharamishwa,Pia yule mwenye kusilimu sasa ikiwa amechukua riba kabla ya kusilimu kwake, si wajibu kurudisha baada ya kusilimu. Aya hii ni sawa na ile inayosema:

﴿وَلَا تَنكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُم مِّنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ﴾

"Wala msiwaoe wake waliowaoa baba zenu, isipokuwa yale yaliyokwishapita ..." (4:22)

Kuacha kuchukulia mambo yaliyopita, kuko katika mambo mengi, hasa mambo ya mali. Wameeleza sababu kuwa ni kutoleta matatizo ya kiuchumi.

Na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu

Wametaja njia nyingi katika kufasiri ibara hii, kiasi ambacho akili haiwezi kutosheka, ambalo tumelifahamu sisi ni kuwa mwenye kuchukua riba bila ya kujua hukumu yake na akaacha baada ya kujua makatazo ya Mwenyezi Mungu kwa kumtii, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atamsaidia na kumtosheleza kwa halali yake. Kwa sababu ameacha haramu kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu; na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu atamtoshea.

Lakini wanaorejea, basi hao ndio watu wa motoni; wao ni wenye kukaa humo milele.

Maana yake ni kuwa wale ambao hawafuati amri ya Mwenyezi Mungu wala kuacha makatazo yake na kuendelea kula riba kwa inadi na kupuuza, basi watawekwa milele motoni. Kwa sababu mfano wa inadi hii hauwi isipokuwa kutokana na kafiri mkanushaji.

Mwenyezi Mungu huipunguza riba na huizidisha sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila kafiri afanyaye dhambi.

Yaani mwenye kula riba hutaka ziada katika mali yake, lakini riba kwa hakika ni kupungua mali na uchafu ulioharamishwa. Na haramu hutoa mali kutoka kwa aliye nayo na inafanya matumizi ya riba yawe kama matumizi ya mali ya kunyang'anya, zaidi ya hayo ni dhambi na adhabu. Kimsingi ni kuwa kila linalokuwa ni sababu ya kumkasirisha Mwenyezi Mungu na adhabu, basi ni uchafu na upungufu na ni amali ya shetani. Ama sadaka, inasafisha mali na kuitakasa na inaifanya thabiti miliki ya mwenye kutoa sadaka na Zaka. Vilevile inaleta radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu Yake. Huo ndio ukamilifu na ziada hasa. Kwa maneno mengine ni kwamba wingi, wa mali ya haramu ni uchache, na uchache wa mali ya halali ni wingi.Kafiri afanyae dhambi ni yule anayefanya inadi ya kula riba bila ya kushtuka na ni yule anayeendelea kufanya inadi ya kukataa kutoa Zaka, na kutoshtuka na vitendo vya Mwenyezi Mungu na kiaga chake.

Kwa kutegemea Aya hii, yafaa kusema kuwa waislamu wengi wakati huu ni makafiri wafanyao dhambi, kwa sababu ya kung'angania riba na kuacha kutoa Khums na Zaka.

Hakika wale walioamini wakafanya vitendo vizuri na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.

Aya hii iko dhahiri katika maana, haihitaji tafsiri, zaidi ya hayo tafsiri yake imekwishapita katika Aya ya 25 na 82 ya Sura hii. Isipokuwa ameirudisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ahadi hii kwa kufuatisha ahadi baada ya kiaga na kinyume. Kwa hiyo alipoelezea kiaga cha wanaofanya riba amefuatishia ahadi kwa watu wema.

Kwa ujumla Aya kwa dhahiri inafahamisha kuwa imani ya nadharia tu, bila ya vitendo si chochote.

Enyi mlioamini! Mcheni Mungu na acheni yaliyobaki katika riba, ikiwa mmeamini.

Kusema: Acheni yaliyobaki katika riba kunafahamisha kuwa uharamu sio katika yale yaliyopita nyuma, kama tulivyoeleza.

Na kama hamtafanya, basi jitangazieni vita na Mwenyezi Mungu Na Mtume Wake.

Na hakuna jambo linalowajibisha kutangaza vita na Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kwa anayeng'angania kula riba ila, ni kwa kuwa yeye ni kafiri au yuko katika hukumu ya kafiri; hata kama kula kwake riba ni kwa kupuuza tu, si inadi. Lakini riwaya zilizopokewa kutoka kwa Masum zimegawanya kula riba katika mafungu mawili.

Kwanza : ni yule anayekula kwa kuifanya halali. Huyo ni kafiri bila shaka yoyote, kwa sababu amekana dharura ya dini. Imam Jaffar Sadiq(a.s) aliambiwa fulani anakula riba na anaita 'lubba" (kiini), akasema:"Nikimpata nitaikata shingo yake."

Pili : ni kula kwa kupuuza hukmu ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuamini uharamu wake. Huyu atatakiwa kutubia mara ya kwanza na ya pili; kama akiendelea atauliwa. Imepokewa kutoka kwa Imam Sadiq(a.s) kuwa mwenye kula riba atatiwa adabu baada ya kubainika, akirudia atatiwa adabu, akirudia atauliwa. Imesemekana kuwa atauliwa mara ya nne.

Na mkiwa mmetubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu; msidhulumu wala msidhulumiwe.

Yaani msimdhulumu mdaiwa kwa kumtaka zaidi ya rasilmali; wala msidhulumiwe kwa kupunguziwa rasilimali.

Na kama ana dhiki basi angoje mpaka awe na uwezo.

Kila mwenye kudaiwa riba, au isiyokuwa riba haijuzu kumdhiki ikiwa ana uzito; kama ambavyo pia haifai kwa mdaiwa kuchelewesha deni akiwa na uwezo. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Kama ambavyo si halali kwa mdeni wako kukucheleweshea deni akiwa na uwezo, vilevile si halali kwako nawe kumdhikisha akiwa na uzito"

Kiwango cha mwenye dhiki ni ambaye hamiliki chochote zaidi ya nyumba yake ya kukaa na vitu vyake vya dharura; kama nguo, vitabu na vyombo vya nyumbani vya lazima. Vilevile zana zake za kufanyia kazi zinazompatia chakula chake na cha familia yake na gharama yake ya siku moja. Vyote hivi si wajibu kuviuza kwa kulipa deni. Hayo tumeyataja kwa ufafanuzi katika kitabu 'Fiqhul-Imam Jaffar Sadiq' mlango wa Muflis.

Na kama (deni) mkizifanya sadaka, basi ni bora kwenu ikiwa mnajua.

Hapana shaka kwamba kumsamehe deni mwenye dhiki ni fadhila katika dini, bali ni katika utii mkubwa. Kwani hilo ni kumfanya apumue na kuweza kutekeleza haja zake vizuri. Imekuja Hadithi: "Mwenye kumvumilia mwenye uzito au kumsamehe, Mwenyezi Mungu atampa kivuli siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli cha Mwenyezi Mungu."

Mafaqihi wameafikiana kwa kauli moja kuwa mwenye kukopa katika dharura ya halali, kisha akashindwa kulipa, atalipiwa deni lake kutoka katika hazina ya waislamu (Baitul Maal). Imam Jaffar Sadiq(a.s) anasema:"Mwenye kuchukua riziki hii kwa uhalali kwa ajili yake na ya watoto wake, ili airudishe baadae anakuwa kama mpigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Akishindwa kulipa na amkope Mwenyezi Mungu na Mtume wake"

Maana ya kumkopa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ni kwamba deni lake litalipwa kutoka katika hazina ya waislamu. Na hilo ni kuitumia katika njia ya Mwenyezi Mungu. Qur'an imelieleza hilo kwa kusema:

﴿إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴾

"Sadaka hupewa: mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao na katika kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na wasafiri. Ni faradhi inayotoka kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima." (9: 60)

Kauli yake Mwenyezi Mungu "Ikiwa mnajua" ni kutilia mkazo kufanya kitu kwa kujua; yaani maadamu mnajua kuwa kumsamehe deni mwenye dhiki ni heri, basi ni juu yenu kufanya kwa kujua kwenu hili.

Imesemekana kuwa makusudio ya kujua ni kufanya; yaani mkiwa ni wafanya heri, basi litoeni sadaka deni kwa mwenye dhiki.

Maelezo haya hayako mbali, na kauli ya Imam Ali(a.s) anasema:"Elimu iko na matendo, mwenye kujua hufanya, elimu hubaki kwa kuifanyia kazi, vinginevyo huondoka." Wataalamu wengi wa kisasa hawaiti nadharia yoyote kuwa ni elimu mpaka wauone ukweli wake kwa kufuatishia na majaribio.

Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi ilipwe iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kukataza riba kwa mkazo na kuamrisha kumfanyia subira mdaiwa mwenye dhiki, au kumsamehe, katika Aya saba, kisha anafuatisha Aya anayowahofisha waasi na siku ya hisabu na malipo na adhabu yake. Katika Majmaul Bayan imeelezwa kuwa Aya hii ni ya mwisho kumshukia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) na kwamba yeye aliishi siku 21 tu baadaye.

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَوَاعَدْنَا مُوسَىٰ ثَلَاثِينَ لَيْلَةً وَأَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤٢﴾

142. Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini. Na Nabii Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifu- ate njia ya waharibifu.

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٤٣﴾

143. Na alipofika Musa kwenye miadi yetu Na Mola wake akamsemeza, alisema: Mola wangu nionyeshe nikutazame. Akasema: Hutaniona, lakini tazama jabali, kama litakaa pahali pake ndipo utaniona. Basi Mola wake alipojionyesha kwa jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika, na Musa akaanguka hali amezimia. Alipozinduka alisema: kutakasika ni kwako! Natubu kwako na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي فَخُذْ مَا آتَيْتُكَ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

144. Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.

وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا سَأُرِيكُمْ دَارَ الْفَاسِقِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha na ufafanuzi wa kila jambo. Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi, Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Aya 142 – 145

MAANA

Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini.

Nabii Musa(a.s) alimtaka Mola wake amteremshie Kitab atakachowaongozea watu kwenye yale wanayoyahitajia katika mambo ya dini yao. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwahidi kuteremshia Kitab baada ya siku thalathini, na utaendelea ushukaji wake kwa siku kumi. Kwa ujumla itakuwa muda wa miadi na wa kushuka ni siku arubaini.

Hapa tumefafanua baada ya kueleza kwa ujumla kwenye Juz. 1 (2:51).

Na Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.

Nabii Musa alipoondoka alimwachia mahali pake ndugu yake Harun kwa Wana wa Israel; akampa nasaha kusimamia mambo yao na kuyatengeneza. Akamhadharisha na tabia zao zinazopondokea zaidi kwenye ufisadi. Ni jana tu walipokodolea macho ibada ya masanamu mpaka Nabii Musa akawaambia kuwa ni watu wajinga.

Harun akakubali nasaha kwa moyo mkunjufu, kama anavyokubali nasaha kaimu kiongozi mwenye ikhlasi kutoka kwa kiongozi wake mwaminifu.

Na alipofika Nabii Musa kwenye miadi yetu ambayo aliiweka Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumpa Tawrat,

Na Mola wake akamsemeza bila ya kumwona kwa sababu:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا ﴿٥١﴾

“Haikuwa kwa mtu aseme na Mwenyezi Mungu ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia au kumtuma mjumbe” (42:51)

Nabii Musa alisema:Mola wangu nionyeshe nikutazame.

Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nabii Musa hakumwomba Mola wake kumwona kwa ajili yake isipokuwa ni kwa ajili ya watu wake. Lakini hii inapingwa na kauli yake Nabii Musa pale aliposema:

Kutakasika ni kwako, na natubu kwako.

Vyovyote iwavyo ni kwamba Nabii Musa alitaka kuona, ni sawa iwe ni kwa ajili yake au kwa ajili ya wengine, sisi hatuoni ubaya wowote katika ombi hili, kwa sababu nafsi ya mtu ina hamu ya kutaka kujua yanayokuwa na yasiyokuwa hasa kuona kile ambacho kitazidisha utulivu wa nafsi.

Ibrahim(a.s) alitaka mfano wa hayo. Angalia Juz.3 (2:260).

Akasema: Hutaniona.

Kwa sababu kumwona Mwenyezi Mungu ni muhali. Tumeyazungumza hayo kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz. 1(2:51).

Lakini tazama jabali, kama litakaa mahali pake utaniona.

Nabii Musa aligeuka kwenye jabali ili amwone Mwenyezi Mungu, mara akaanguka chini na hakuona chochote. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifanya hivi ili kumfahamisha Nabii Musa(a.s) kwamba kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani kwake wala kwa mwingine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliuwekea sharti uwezekano wa kuonekana kwake kwa kutulia mahali jabali na jabali halikutulia, Kwa hiyo kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani.

Mfumo huu alioutumia Mwenyezi Mungu hapa ni kama ule wa kusema: Nitafanya hivi kunguru akiota mvi, Au akipita ngamia kwenye tundu ya sindano.

Basi Mola wake alipojionyesha kwenye jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika.

Yaani ilipodhihiri amri ya Mola wake; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾

“Akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu.” (89:22).

Yaani ikaja amri ya Mola wako.

Na Musa akaanguka chini amezimia.

Akawa hana fahamu kwa kishindo cha ghafla, Mwenyezi Mungu akamhurumia akazinduka.

Alipozinduka alisema: Kutakasika ni kwako! Natubu kwako. Kwa kukuomba kukuonana mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

Kwa sababu wewe ni mtukufu zaidi ya kuonekana kwa jicho.

Makusudio ya wa mwanzo sio kulingana na hisabu ya wakati; isipokuwa makusudio yake ni uthabiti na kutilia mkazo.

Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.”

Baada ya Nabii Musa kunyenyekea kwa muumba wake, Mwenyezi Mungu alimkumbusha neema yake, kubwa zaidi ni Utume na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Makusudio ya watu ni watu wa zama zake, kwa dalili ya kauli yake: Kwa ujumbe wangu. Kwani Mwenyezi Mungu aliwachagua Mitume wengi kabla ya Nabii Musa na baada yake.

Ama kuhusika kwake na kuzungumza naye hakuna dalili ya ubora zaidi. Ikiwa kunafahamisha ubora wowote basi kupelekewa roho mwaminifu kwa mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume ndio daraja ya juu na bora zaidi.

Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidaha na ufafanuzi wa kila jambo.

Makusudio ya mbao ni Tawrat kwa sababu ndiyo aliyoteremshiwa Nabii Musa, ndani yake mna mawaidha na upambanuzi wa hukumu.

“Kila jambo ni neno la kiujumla, lakini limekusudia mahsusi; yaani kila linalofungamana na maudhui ya risala miongoni mwa mawaidha, hukumu, misingi ya itikadi, kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu, Mitume yake na siku ya mwisho, na hukumu za sharia, kama halali na haramu. Kwa hiyo kauli yake: Mawaidha na maelezo ni ubainifu wa tafsiri ya kauli yake kila jambo. Kwa sababu makusudio ya maelezo ni kubainisha hukumu za kisharia.

Basi yashike kwa imara.

Yaani ichunge Tawrat na uitumie kwa ukweli wa nia.

Na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi.

Kila aliloliteremsha Mwenyezi Mungu ni zuri, lakini kuna yaliyo mazuri zaidi. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: “Na fanyeni wema, Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”

Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Yaani fasiki na dhalimu atafikwa na majanga. Haya ndiyo niliyoyafahamu kutokana na jumla hii kabla ya kupitia tafsir, Baada ya kuzipita nikakuta kauli kadhaa. Miongoni mwazo ni kwamba Mwenyezi Mungu atawaonyesha makao ya Firauni na watu wake baada ya kuangamizwa kwao. Nyingine inasema kuwa atawaonyesha ardhi ya Sham iliyokuwa mikononi mwa waabudu mizimu wakati huo.

سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki. Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاءِ الْآخِرَةِ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٧﴾

147. Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zime- poromoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ ﴿١٤٨﴾

148. Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti, Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

وَلَمَّا سُقِطَ فِي أَيْدِيهِمْ وَرَأَوْا أَنَّهُمْ قَدْ ضَلُّوا قَالُوا لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

NITAWAEPUSHIA AYA ZANGU

Aya 146 – 149

MAANA

Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki.

Wenye kufanya kiburi katika ardhi ni wale wanaopinga haki na wasiotaka kutawaliwa nayo. Kusema kwake bila ya haki ni kwa ufafanuzi, sio kwa kuvua; sawa na kusema: “Na wakiwaua mitume bila ya haki.”

Neno Aya katika Qur’an mara nyingine hutumia kuwa ni Aya zenye misingi ya itikadi na hukumu ya sharia na mfano wake. Mara nyingine hutumi- ka kuwa ishara yaani hoja na dalili zenye kuthibitisha uungu na utume.

Ikiwa makusudio ni maana ya kwanza katika Aya hii tunayoifasiri, basi maana yatakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazihifadhi Aya na kuzilinda zisipotolewe; sawa na kauli yake: “Hakika sisi ndio tuliouteremsha ukumbusho huu na hakika ndio tutakaoulinda”

Na ikiwa makusudio ni maana ya pili, yaani ishara kwa maana ya dalili na hoja, basi maana ni kwamba baada ya wapinzani kujiepusha nazo na kuacha kuzisikiliza, basi Mwenyezi Mungu ataachana nao, wala hatawategemeza kwenye imani. Tumekwisha elezea hilo mara kadhaa; kama vile katika kufasiri Juz.5 (4:88).

Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

Huu ni ubainifu wa hakika ya wenye kiburi na sababu inayowajibisha kiburi chao vilevile. Ama hakika yao ni kuwa wao hawajizuilii na uovu wala hawapondokei kwenye uongofu.

Sababu inayowajibisha hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea hoja na dalili; akawataka wazichunguze, wazizingatie na wazitumie vile inavyotakikana, wakakataa na wakaendelea kuzipinga tena bila ya kuzichunguza. Lau kwamba wao wangeliziitikia na kuzichunguza dalili hizo kungeliwapelekea kuamini na kuikubali haki; wala wasingelikua na kiburi na kufanya ufisadi katika nchi.

Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zimeporomoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na kukutana na Mola wake, basi yeye ni katika wale watakaoangamia kesho na yote yale aliyokuwa akijifaharisha nayo yatakuwa si lolote. Hayo ni malipo ya ukafiri wake na inadi yake.

Yamenipendeza yale aliyoyasema mfasiri mmoja Mwenyezi Mungu amughufirie na amrehemu, namnukuu: “Kuporomoka amali kunachukuliwa kama wanavyosema: ‘Ameporomokaa ngamia.’ ikiwa amekula mmea wenye sumu na tumbo lake likafura kisha akafa.

Hiyo ndiyo sifa ilivyo kwa batili inayowatokea wenye kukadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana na akhera, Mwongo hufura mpaka watu wanamdhania kuwa ni mkubwa mwenye nguvu, kisha huporomoka, kama alivyoporomoka yule ngamia, aliyekula mmea wa sumu.”

Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti.

Imetangulia kuelezwa katika Aya 142 kuwa Nabii Musa(a.s) alikwenda kwa miadi ya Mola wake, na kwamba yeye alimpa ukaimu nduguye Harun kwa watu wake. Vilevile imeelezwa katika Aya 138 kwamba Wana wa Israel baada ya kupita bahari walimtaka Nabii Musa awafanyie sanamu watakayoiabudu; si kwa lolote isipokuwa tu wameona ni vizuri waabudu masanamu.

Kwa hivyo mara tu Nabii Musa alipokuwa mbali nao waliitumia nafasi hiyo; Msamaria (Samiri): akakusanya mapambo ya wanawake akaten- geneza ndama; akatengeneza katika umbo ambalo liliweza kutoa sauti ya ndama.

Akawaambia huyu ni Mola wenu na Mola wa Musa; wakaingilia kumwabudu. Harun aliwakataza, lakini hakuweza kuwazuia, na hawakum- sikiliza isipokuwa wachache, Yametangulia kudokezwa hayo katika kufasiri Juz, 1 (2: 51), Pia yatakuja tena maelezo.

Aya hii tuliyo nayo, inatilia nguvu yale tuliyoyakariri katika Juzuu ya kwanza na ya pili, kuwa Israeli haithibiti ila kwenye misingi ya matamanio na hawaa; ikiwa ni kweli kuwa matamanio ni misingi.

Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

Haya ndiyo mantiki ya kimaumbile na akili ambayo inakataa mtu amwabudu Mungu aliyemtengeneza kwa mkono wake, lakini waisraili hawana akili wala maumbile au dini.

Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotoea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

Hii ndiyo sifa nzuri pekee na ndiyo ya kwanza na ya mwisho, iliyosajiliwa na Qur’an kwa waisrael kwa ujumla, bila ya kuangalia uchache wa wachache waliomwamini Nabii Musa hadi mwisho.

Baadhi ya Wafasiri wamechukulia dhahiri toba ya Bani Israel kwamba wakati huo ilikuwa ni masalia ya maandalizi ya wema, kisha masalia hayo yakaenda; wala haikubaki athari yoyote kwao ya kuonyesha kujiandaa kwa kheri. Kuchukulia huku hakuko mbali na ukweli na kunaashiriwa na Aya isemayo:

ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ﴿٧٤﴾

“Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi” Juz.1(2: 74)

Aya hii ni baada ya kisa cha ng’ombe ambacho kilitokea baada ya kuabudu ndama.

5

وَلَمَّا رَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا قَالَ بِئْسَمَا خَلَفْتُمُونِي مِن بَعْدِي أَعَجِلْتُمْ أَمْرَ رَبِّكُمْ وَأَلْقَى الْأَلْوَاحَ وَأَخَذَ بِرَأْسِ أَخِيهِ يَجُرُّهُ إِلَيْهِ قَالَ ابْنَ أُمَّ إِنَّ الْقَوْمَ اسْتَضْعَفُونِي وَكَادُوا يَقْتُلُونَنِي فَلَا تُشْمِتْ بِيَ الْأَعْدَاءَ وَلَا تَجْعَلْنِي مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿١٥٠﴾

150. Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika. Akasema: Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu na akazitupa mbao na akamkata kichwa ndugu yake akimvuta kwake. Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِأَخِي وَأَدْخِلْنَا فِي رَحْمَتِكَ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿١٥١﴾

151. Akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

إِنَّ الَّذِينَ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ سَيَنَالُهُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَذِلَّةٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُفْتَرِينَ ﴿١٥٢﴾

152. Hakika wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia, Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi.

وَالَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِهَا وَآمَنُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٥٣﴾

153. Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaamini, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

وَلَمَّا سَكَتَ عَن مُّوسَى الْغَضَبُ أَخَذَ الْأَلْوَاحَ وَفِي نُسْخَتِهَا هُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ هُمْ لِرَبِّهِمْ يَرْهَبُونَ ﴿١٥٤﴾

154. Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

ALIPORUDI MUSA KWA WATU WAKE

Aya 150-154

MAANA

Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika.

Nabii Musa(a.s) alipokuwa mlimani akizungumza na Mola wake mtuku- fu, alipewa habari na Mola wake kuwa watu wake wameabudu ndama baada yako; kama inavyofahamisha Aya isemayo:

قَالَ فَإِنَّا قَدْ فَتَنَّا قَوْمَكَ مِن بَعْدِكَ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ ﴿٨٥﴾ فَرَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا ﴿٨٦﴾

“Akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako bada yako na Msamaria amewapoteza. Nabii Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika.” (20:85-86).

Ghadhabu ilidhihiri kwa kusema:Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu.

Aliwaacha kwenye Tawhid, lakini aliporudi aliwakuta kwenye shirk.

Ama amri ya Mola wao ambayo hawakuingoja ni kumngoja Nabii Musa siku arubaini.

Hii inafahamishwa na Aya isemayo:

أَفَطَالَ عَلَيْكُمُ ﴿٨٦﴾

“Je, umekuwa muda mrefu kwenu?” (20:86).

Kama ambavyo ghadhabu yake ilidhihiri kwa kauli, Vilevile ilidhihiri kwa vitendo:

Na akazitupa mbao na akamkamata kichwa ndugu yake akimvuta kwake.

Wamesema baadhi ya maulama kuwa Nabii Musa alitupa Tawrat nayo ina jina la Mwenyezi Mungu na akamvuta nduguye Harun naye ni mja mwema. Imekuwaje na Nabii Musa ni ma’sum? Baada ya kujiuliza huku wakaanza kuleta taawili na kutafuta sababu.

Ama sisi hatu hatuleti taawili wala kutafuta sababu, bali tunayaacha maneno na dhahiri yake. Kwa sababu isma haibadilishi tabia ya maumbile ya binadamu na kumfanya ni kitu kingine wala haimuondolei sifa ya kuridhia na kukasirika hasa ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; tena ikiwa ni ghafla kama ilivyomjia Nabii Musa(a.s) .

Amekaa na watu siku nyingi akiwafundisha tawhid na dini ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kutulia imani yao; halafu ghafla tu waache yote na waingie kwenye shirki bila ya sababu yoyote ya maana.

Wengine wamesema kuwa Nabii Musa alikuwa mkali na Haruna alikuwa mpole. Sisi tunasemaNabii Musa alikuwa mwenye azma kubwa, mwenye nguvu ya alitakalo na mwenye kujiamini; na Haruna naye alikuwa chini kidogo ya Nabii Musa kulingana na masilahi.

Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

Anakusudia madui ni wale walioabudu ndama; kama kwamba anamwambia nduguye: unachinganya mimi na maadui zangu na maadui zako, tena unanivuta mbele yao wanicheke. Vipi unanichanganya nao kwenye hasira zako na mimi niko mbali nao na vitendo vyao? Tena nimewapinga na wala sikuzembea kuwapa nasaha na tahadhari!

Hapo Nabii Musa akarudi chini na kumuonea huruma nduguye, akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

Alijiombea maghufira yeye mwenyewe kwa ukali wake kwa nduguye, kisha akamuombea maghufira nduguye kwa kuhofia kuwa hakufanya bidii ya kuwazuia na shirk. Bila shaka Mwenyezi Mungu, aliitikia maombi ya Nabii Musa kwa sababu yeye ni mwenye kurehemu kushinda wenye kurehemu; na pia kujua kwake ikhlasi ya Nabii Musa na nduguye Harun.

Hakiaka wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi

Unaweza kuuliza kuwa : dhahiri ya Aya hii nikuwa wale walioabudu ndama wamekasirikiwa na Mwenyezi Mungu na hali wao walitubia na kuomba maghufira; kama ilivyoeleza Aya ya 149 ya Sura hii na Aya nyingine inasema:

ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾

“Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga; kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila shaka Mola wako ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu” (16:119).

Kwa hiyo vipi walazimiane na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ya milele na laana ya daima?

Baadhi wamejibu kuwa : waabudu ndama waligawanyika mafungu mawili baada ya kurudi Nabii Musa, Kundi moja lilitubia toba sahihi. Hao ndio waliosamhewa na Mwenyezi Mungu. Na wengine waling’ang’ania ushirikina; kama vile Msamaria na wafuasi wake. Hawa ndio waliokasirikiwa na Mwenyezi Mungu na akawadhalilisha katika maisha ya duniani.

Ilivyo ni kwamba kwenye Aya hakuna ufahamisho wowote wa makundi haya. Jibu linalonasibu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu alijua kuwa Mayahudi milele hawatubii wala hawatatubia toba ya kiuhakika ambayo hawatarudia. Hakia hii inafahamishwa na tabia yao na sera yao. Kwani wao walikuwa na wanaendelea kuwa ni watu wasiokatazika wala kukanyika na ufisadi na upotevu ila kwa kutumia nguvu peke yake.

Swali la pili : Mayahudi leo wanayo dola inayoitwa Israil, kwa hiyo hawana udhalili; je hili si jambo linalopingana na dhahiri ya Aya?

Jibu : Hapana! Tena hapana! Hakuna dola wala haitakuwa dola ya Mayahudi milele; kama kilivyosajili kitabu cha Mwenyezi Mungu. Israil sio dola, kama dola nyingine; isipokuwa ni kambi ya jeshi; kama vile askari wa kukodiwa waliowekwa na wakoloni kulinda masilahi yao na kuvunja nguvu za wazalendo. Tumeyathibitisha hayo katika kufasiri Juz.4 (3:112) na Juzuu nyenginezo.

Vilevile katika kitabu Min huna wa hunaka (Huku na huko) mlango wa man baa’ dinahu li shaitan (Mwenye kumuuzia dini yake shetani)

Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaami- ni, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

Maana ya Aya yako wazi, na mfano wake umekwishapita mara nyingi. Lengo la kutajwa kwake baada ya Aya iliyotangulia ni kutilia mkazo kwamba mwenye kutubia na akarudi kwa Mola wake kwa ikhlasi na asirudie maasi, kama walivyofanya waisrail, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamrehemu, awe ni mwisraili au Mkuraysh n.k.

Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

Nabii Musa ni Mtume aliye ma’sum, hilo halina shaka, lakini yeye ni binadamu, anahuzunika na kufurahi, anridhia na kukasirika. Hasira zilimpanda alipoona watu wake wamertadi dini ya Mwenyezi Mungu. Hasira aliiacha alipombwa na ndugu yake, Harun; na Mungu akamwahidi kuwaadhibu walortadi.

Baada ya Nabii Musa kurudia hali yake ya kawaida, alizirudia zile mbao alizokuwa amezitupa alipokuwa amekasirika na akatulizana kutokana na yaliyomo ndani yake katika uongofu kwa yule ambaye moyo wake utaifungukia kheri na rehema zilizomo kwa yule anayeogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha kumpa radhi na rehema kila mwenye kumtii kwa kuogopa adhabu yake, na kumletea adhabu na mateso kila mwenye kuasi kwa kubweteka na rehema yake.

وَاخْتَارَ مُوسَىٰ قَوْمَهُ سَبْعِينَ رَجُلًا لِّمِيقَاتِنَا فَلَمَّا أَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّايَ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا إِنْ هِيَ إِلَّا فِتْنَتُكَ تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَاءُ وَتَهْدِي مَن تَشَاءُ أَنتَ وَلِيُّنَا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الْغَافِرِينَ ﴿١٥٥﴾

155. Na Musa akachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi? Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na kumwongoza umtakaye, Wewe ndiye mlinzi wetu. Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiye bora wa kughufiria.

وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾

156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera, Sisi tunarejea kwako. Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye; na rehema yangu imekienea kila kitu. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini ishara zetu.

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾

157. Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawaahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale walioamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, Hao ndio wenye kufaulu.

HAIKUWA ILA NI ADHABU YAKO

Aya 155 – 157

MAANA

Na Musa akawachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu.

Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu Aya hii na zikagongana kauli zao katika kuifasiri. Wakatofautiana katika kubainisha miadi, kuwa je, ni miadi ya kuteremshwa Tawrat au mingine?

Vilevile wametofautiana kuwa ni kwa nini Nabii Musa aliwachagua watu sabini katika watu wake, Je, ni kwa kuwa wao walimtuhumu Nabii Musa na kumwambia hatutakuamini mpaka tusikie maneno ya Mwenyezi Mungu kama unavyosikia wewe; ndipo akasuhubiana nao ili asikie, kama alivyosikia; au ni kwa sababu nyingine?

Vilevile wametofautiana wafasiri katika sababu ambayo aliwaadhibu Mwenyezi Mungu, Hatimae wakahitalifiana kuwa je, mtetemeko uliwaua au ulikurubia tu kuvunja migongo yao, lakini hawakufa?

Katika Aya hakuna kidokezo chochote cha yale waliyoyachagua kikundi katika wafasiri. Linalofahamika ni kuwa tu, Nabii Musa aliwachagua watu sabini ili aende nao kwa miadi ya Mola wake. Kwa hali ilivyo ni kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Nabii Musa hafanyi ila aliloamrishwa; na kwamba Mwenyezi Mungu ali- wateremshia hao sabini aina ya adhabu kulingana na hekima ilivyoka.

Basi hatuna cha kuthibitisha miadi ilivyo kuwa wala sababu ya kuchagua au ya adhabu.

Ni kweli kwamba kauli ya Nabii Musa kumwambia Mwenyezi Mungu:Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi? inafahamisha kwamba wao walifanya yaliyowajibisha maangamizi, lakini halikubainishwa walilolifanya; nasi hatuna haki ya kusema tusiyoyajua.

Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeli- waangamiza wao na mimi zamani!

Nabii Musa alichagua watu sabini walio bora katika watu wake akaenda nao kwenye miadi ya Mola wake, walipofika huko wakaangamia wote akabakia, peke yake. Hilo ni tatizo la kukatisha tamaa hakuna la kufanya tena. Je, arudi peke yake kwa wa Israel? Atawajibu nini wakimuuliza watu wao?

Hakuna kimbilio kabisa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Basi akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu amwondolee tatizo hilo na akatamani lau Mwenyezi Mungu angelimwangamiza pamoja nao kabla ya kuja nao hapa.

Kisha akasema kumwambia mtukufu aliye zaidi:

Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi?

Yaani wewe ni mtukufu na mkuu kuliko kufanya hivyo. Kwa sababu wewe ni Mpole na Mkarimu.

Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na humwongoza umtakaye.”

Neno Fitna lililofasiriwa adhabu hapa, lina maana nyingi; ikiwemo upote- vu na ufisadi; kama ilivyo katika Aya ya 26 ya Sura hii. Maana nyingine ni kupigana na majaribu, mara nyingi hutumiwa kwa maana ya adhabu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ﴿٢٥﴾

“Na jikingeni na adhabu ambayo haitawasibu waliodhulumu peke yao” (8:25).

Haya ndiyo makusudio yake katika Aya hii tuliyonayo, Dhamir ya hilo inarudia tetemeko ambalo limekwishatajwa. Maana ya kumpoteza amtakaye, ni kuwa Mwenyezi Mungu humpelekea tetemeko, ambalo ndio adhabu, yule amtakaye katika waja wake, na maana ya kumwongoza ni kumwepushia tetemeko amtakaye.

Maana ya kijumla ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) huteremsha adhabu kwa amtakaye anayestahiki na kumwondolea asiyestahiki. Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli yake halikuwa hilo ila ni adhabu yako, maana yake yanafungamana na yaliyotangulia na yaliyo baada yake; na kwamba haijuzu kuitolea dalili kuwa upotevu unatokana na Mwenyezi Mungu.

Vipi Mwenyezi Mungu ampoteze mtu kisha amwaadhibu kwa upotevu huo? Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kutaka kuwadhulumu waja. Hakika Shetani ni adui mwenye kupoteza na inatosha kuwa Mola wako ni mwongozi na mwenye kunusuru.

Kwa maelezo zaidi rudia Juz.1 (2:26).

Wewe ndiye mlinzi wetu, Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiwe bora wa kughufuria. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera. Sisi tunarejea kwako”

Hakuna tafsir bora ya Munajat huu, kama kauli ya bwana wa mashahidi, Imam Husein bin Ali(a.s) wakati alipozungukwa na maelfu kila upande akiwa peke yake. Akakimbilia kwa Mola wake na kumtaka hifadhi dhidi ya maadui zake akisema:

“Ewe Mola wangu wewe ndiye matarajio yangu katika kila shida, Kila jambo lililonishukia wewe ni tegemeo, Ni matatizo mangapi ya kukatisha tamaa, ya kuondokewa na marafiki na kufuatwa na maadui, uliyoniteremshia, kisha nikakushitakia wewe, kwa kuwa sina mwingine zaidi yako, nawe ukanitatulia na kunifariji! Basi wewe ndiye mtawalia kila neema,mwenye kila hisani na mwisho wa matakwa yote!”

Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye katika wananostahiki adhabu.

Kwa sababu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanapitia kwenye haki na uadilifu tu, hakuna mchezo wala dhulma mbele ya Mwenyezi Mungu.

Razi anasema: “Amesoma Hasan: Usibu bihi man Asaa kwa sin (nitam- sibu nayo mwenyewe kufanya uovu), na Shafii amechagua kisomo hiki.”

REHMA YA MWENYEZI MUNGU INAMFIKIA IBLISII

Qur’an hutumia neno Rehma ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya msaada wake na kwa thawabu zake. Maana ya usaidizi kutoka kwake Mwenyezi Mungu ni kwamba vitu vyote vilivyoko, hata Iblisi, vinamhitajia Mwenyezi Mungu katika kubakia kwake na kuendelea kwake; kama ambavyo vinamhitajia yeye katika asili ya kupatikana kwake, na kwamba yeye ndiye anayevisaidia kubaki wakati wote, kiasi ambacho lau msaada wake huo utakiepuka kitu kitambo kidogo cha mpepeso wa jicho, basi kitu hicho hakitakuwako tena.

Ufafanuzi zaidi wa rehma hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ﴿٤٥﴾

“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, asin- geliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja” (35:45).

Rehma hiyo ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:Na rehma yangu imekienea kila kitu hata Iblisi aliyelaaniwa. Ama rehma kwa maana ya thawabu, Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa anayemwamini na kumcha. Ndiyo aliyoiashiria kwa kusema kwake. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa maasi na wakafuata amri ya Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake.

Na wanaotoa Zaka.

Ametaja Zaka badala ya Swala. Kwa sababu mtu hupituka mpaka kwa kujiona amejitoshea.

Na wanaoziamini ishara zetu ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika.

Rehma ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kwa maana ya thawabu haipati isipokuwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu, akatoa mali kwa kupenda kwake na akauamini utume wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) kama utamfikia ujumbe wake.

Amehusisha kutaja mali kutokana na tulivyoyadokezea, na pia kuwa mazungumzo ni ya Mayahudi ambao mali ndio Mola wao hakuna mwingine isipokuwa yeye. Mwenyezi Mungu amemsifu Nabii Muhammad(s.a.w.w) , katika Aya hii kwa sifa hizi zifuatazo:-

1.Nabii Asiyesoma Wala Kuandika.

Hiyo ni sifa inayomhusu yeye tu, kinyume cha Mitume wengine, kutambulisha kuwa licha ya kuwa hivyo lakini amewatoa watu kutoka katika giza mpaka kwenye mwangaza, akaathiri maisha ya umma wote wakati wote na mahali kote.

2.Ambaye Wanamkuta Ameandikwa Kwao Katika Tawrat Na Injil.

Rudia Juz.1 (2:136) na Juz.6 (4:163).

3.Ambaye Anawaamrisha Mema Na Anawakataza Maovu.

Rudia Juz, 4 (3:104 - 110).

4.Na Anawahalalishia Vizuri Na Kuwaharamishia Vibaya.

5.Na Kuwaondolea Mizigo Na Minyororo Iliyokuwa Juu Yao.

Makusudio ya minyororo ni mashaka. Mwenyezi Mungu aliwaharamishia waisrail baadhi ya vitu vizuri, vilivyodokezwa kwenye Juz.8 (6:146); kama ambavyo sharia ya Nabii Musa ilikuwa ngumu na yenye mashaka; kiasi kwamba mwenye kutubia katika waisrael hakubaliwi toba yake ila kwa kujiua:

فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ﴿٥٤﴾

“Basi tubuni kwa Muumba wenu na jiueni” Juz.1 (2:54).

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaambia waisrael ambao wamemkuta Nabii Muhammad(s.a.w.w) kwamba wao wakisilimu watahalalishiwa vizuri vilivyokuwa haramu, na atawaondolea mashaka katika taklifa. Kwa sababu Nabii Muhammad ametumwa na sharia nyepesi isiyo na mikazo.

Basi wale waliomwamini.

Makusudio ni waliomwamini Nabii Muhammad(s.a.w.w) miongoni mwa Mayahudi na wengine.

Na wakamheshimu.

Yaani kumsaidia katika mwito wake na kumheshimu kwa cheo chake.

Na wakamsaidia juu ya maadui zake.

Na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye.

Yaani wakafanya matendo kwa mujibu wa Qur’an.Hao ndio wenye kufaulu duniani na akhera.

7

8

9

10