TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16180
Pakua: 2474


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16180 / Pakua: 2474
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا تَدَايَنتُم بِدَيْنٍ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَاكْتُبُوهُ وَلْيَكْتُب بَّيْنَكُمْ كَاتِبٌ بِالْعَدْلِ وَلَا يَأْبَ كَاتِبٌ أَن يَكْتُبَ كَمَا عَلَّمَهُ اللَّـهُ فَلْيَكْتُبْ وَلْيُمْلِلِ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ وَلْيَتَّقِ اللَّـهَ رَبَّهُ وَلَا يَبْخَسْ مِنْهُ شَيْئًا فَإِن كَانَ الَّذِي عَلَيْهِ الْحَقُّ سَفِيهًا أَوْ ضَعِيفًا أَوْ لَا يَسْتَطِيعُ أَن يُمِلَّ هُوَ فَلْيُمْلِلْ وَلِيُّهُ بِالْعَدْلِ وَاسْتَشْهِدُوا شَهِيدَيْنِ مِن رِّجَالِكُمْ فَإِن لَّمْ يَكُونَا رَجُلَيْنِ فَرَجُلٌ وَامْرَأَتَانِ مِمَّن تَرْضَوْنَ مِنَ الشُّهَدَاءِ أَن تَضِلَّ إِحْدَاهُمَا فَتُذَكِّرَ إِحْدَاهُمَا الْأُخْرَىٰ وَلَا يَأْبَ الشُّهَدَاءُ إِذَا مَا دُعُوا وَلَا تَسْأَمُوا أَن تَكْتُبُوهُ صَغِيرًا أَوْ كَبِيرًا إِلَىٰ أَجَلِهِ ذَٰلِكُمْ أَقْسَطُ عِندَ اللَّـهِ وَأَقْوَمُ لِلشَّهَادَةِ وَأَدْنَىٰ أَلَّا تَرْتَابُوا إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً حَاضِرَةً تُدِيرُونَهَا بَيْنَكُمْ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَلَّا تَكْتُبُوهَا وَأَشْهِدُوا إِذَا تَبَايَعْتُمْ وَلَا يُضَارَّ كَاتِبٌ وَلَا شَهِيدٌ وَإِن تَفْعَلُوا فَإِنَّهُ فُسُوقٌ بِكُمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّـهُ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴾

282.Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi liandikeni; na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu. Wala mwandishi asikatae kuandika kama vile alivyomfunza Mwenyezi Mungu; basi na aandike. Na aandikishe yule ambaye iko juu yake haki; na amwogope Mwenyezi Mungu Mola wake; wala asipunguze chochote katika deni. Na kama yule ambayeuu yake iko haki ni mpumbavu au mnyonge au yeye hawezi kutaja mwenyewe, basi na ataje msimamizi wake kwa uadilifu. Na muwashuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu waume, kama hakuna wanaume wawili, basi ni mwanamume mmoja na wanawake wawili, katika wale mnaowaridhia kuwa mashahidi, ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine, Na mashahidi wasikatae waitwapo. Wala msichoke kuiandika ikiwa ndogo au kubwa, mpaka muda wake, Hayo ndiyo uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na imara sana kwa ushahidi na ni karibu zaidi kutofanya shaka. Ila ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayopeana baina yenu, basi si vibaya kwenu msipoandika, Na wekeni mashahidi mnapouziana, wala asitiwe tabu mwandishi wala shaidi.

﴿وَإِن كُنتُمْ عَلَىٰ سَفَرٍ وَلَمْ تَجِدُوا كَاتِبًا فَرِهَانٌ مَّقْبُوضَةٌ فَإِنْ أَمِنَ بَعْضُكُم بَعْضًا فَلْيُؤَدِّ الَّذِي اؤْتُمِنَ أَمَانَتَهُ وَلْيَتَّقِ اللَّـهَ رَبَّهُ وَلَا تَكْتُمُوا الشَّهَادَةَ وَمَن يَكْتُمْهَا فَإِنَّهُ آثِمٌ قَلْبُهُ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴾

283.Na kama mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, basi ni rahani itakayokabidhiwa. Na kama mmoja wenu akimwamini mwingine, basi aliyeaminiwa atekeleze uaminifu wake na amche Mungu, Mola wake. Wala msifiche ushahidi, Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi kwa mnayoyatenda.

DENI

Aya 282 – 283

MAANA

Mwisho mwisho wa Sura hii Mwenyezi Mungu ametaja hukumu za sharia zinazofungamana na Zaka, riba, deni, biashara na rahani. Masuala ya Zaka na riba yamekwisha tangulia. Hivi sasa tuko katika baadhi ya masuala ya deni, rahani na biashara. Aya imetilia umuhimu sana kuandika deni na kuweko ushahidi; ambapo Mwenyezi Mungu ameamrisha kuandika kwa kuanza kusema: "Iandikeni" Pili, akasema: "Wala msichoke kuiandika" Na mara ya tatu, amebainisha hekima ya kuandika na kuweko ushahidi kwa kusema "Hayo ndiyo uadilifu zaidi na imara zaidi na karibu zaidi kutofanya shaka." Pamoja na hayo mafaqihi wengi hawakuwajibisha kuandika deni na kuuza, wala kuweko ushahidi. Wameichukulia amri ya hilo kuwa ni sunna. Kauli yao hiyo ya suna inatiliwa mkifanya hivyo, basi hakika hilo ni ufasiki kwenu. Na mcheni Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu anawaelimisha; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. nguvu na kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kuandika na kuweko ushahidi, amesema: "Kama mmeaminiana, basi aliyeaminiwa atekeleze amana"; Yaani kama mdai akimwamini mdaiwa bila ya kuandika wala ushahidi, basi ni juu ya mwenye kudaiwa kutekeleza. Hii ni ruhusa dhahiri ya kuacha kuandika na ushahidi, Itakuja tafsiri ya Aya hii Inshaallah.

Enyi mlioamini! Mnapokopeshana deni kwa muda uliowekwa, basi liandikeni.

Neno: Tadayantum lina maana mbili: Kudaiana kwa mali na kulipiziana. Imam Ali(a.s) anasema: "Kama utakavyomfanya (mwenzako) nawe utalipwa." Ilipokuwa neno tadayantum linachukua maana hizi mbili, ndio maana Mwenyezi Mungu akasema:"Tadaayan tum bidaynin. Ili kuondoa dhana ya kukusudia maana ya kulipa" Makusudio ya "Muda uliowekwa" ni muda wa kwisha deni uliotajwa iwe mwaka au mwezi, n.k. Kusema Kwake Mwenyezi Mungu: "Basi liandikeni" ni amri ya kuandika deni, na amri inafahamisha wajibu, lakini imekuwa ni sera ya waislamu tangu zamani kutolazimika kuandika deni na kuweko ushahidi. Kwa hiyo amri ikachukuliwa kuwa ni suna na mwongozo.

MKOPO NA DENI

Mkopo unashirikiana na deni katika kuwa mtu ananufaika nao kwa kuutumia, na ni haki ya mtu katika dhima. Lakini mkopo unatofautiana na deni katika kuwa kitu chenye kukopwa kinalipwa cha aina hiyo hiyo katika jinsi yake na sifa; ukikopa pesa, basi dhima yako ni kulipa pesa, ni lazima urudishe mfano wake, sio kima. Ama deni,( [6] ) dhima inathibiti kutokana na sababu fulani; kama kukopa, bei ya mkopo, kuoa kwa mahari ya kulipa baadaye jinai na mengineyo. Kwa hiyo deni ni kiujumla na linalipwa mfano wake likiwa na mfano; au kima ikiwa halina mfano

Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu.

Ilivyokuwa lengo la kuandika deni ni kudhamini haki ya mdai na mdaiwa na kuondoa ubishi kati yao, basi ni wajibu mwandishi awe mwaminifu mwenye kujua hukumu ya dini. Kwani kama akiwa mbumbumbu au mwenye upendeleo, basi lengo litakuwa limebatilika. Unaweza kuuliza: kwa nini amesema aandike mwandishi kwa uadilifu na asiseme aandike mwandishi mwadilifu?

Jibu : Kwa sababu kuandika si sharti mwandishi awe mwadilifu; kama ilivyo kwa kadhi, mufti na imam wa jamaa katika Swala. Kwa sababu lengo la kuandika deni ni kudhamini na kuhifadhi haki; kama tulivyoeleza. Kwa hivyo inatosha mwandishi kuwa mwadilifu kwa upande huu tu; na wala sio katika kauli zake na vitendo vyake vyote. Kwa sababu hiyo inawezekana kusema kuwa Aya hii inafahamisha kuwa shahidi sio lazima awe na uadilifu wa kisheria, bali inatosha kutegemea kuwa ni mkweli na mwadilifu katika ushahidi wake, bila ya kumpendelea yeyote; na tutauchukulia uadilifu wa shahidi ulioelezwa katika hadithi kuwa ni uadilifu wa kiwango fulani na sio uadilifu kwa ujumla. Kama ukisema kuwa kumpa shahidi hukumu ya mwandishi ni kutumia Qiyas na wewe si unasema Qiyas ni batili?

Jibu : Mwandishi ni shahidi hata kama haitwi hivyo. Kwa maneno mengine, shahidi ni aina mbili - wa kutamka na kuandika; huyu anashuhudia kwa kuandika na yule anashuhudia kwa kutamka; na kuandika ni ndugu wa kutamka.

Wala mwandishi asikatae kuandika kama vile alivyomfunza Mwenyezi Mungu; basi na aandike.

Makusudio ya alivyomfunza ni alivyomwamrisha; na alivyoamrishwa, ni kuandika kwa uadilifu, bila ya kupendelea. Kusema kwake "basi na aandike" ni kutilia mkazo kauli Yake "asikatae." Siri ya mkazo huu, ni kwamba wale waliokuwa wanajua kuandika wakati ule walikuwa kidogo sana, endapo mwandishi atakataa huwa vigumu kumpata mwingine. Unaweza kuuliza kuwa kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "wala mwandishi asikatae" ni katazo, na katazo linafahamisha uharamu; kwa maana hiyo basi, ni wajibu kwa mwandishi kukubali kuandika deni; na tunajua kuwa kuandika huku ni suna sio faradhi, Sasa itakuwaje tanzu izidi asili?

Jibu : Kama ambavyo kauli Yake Mwenyezi Mungu "basi iandikeni" tumeichukulia kuwa sunna,basi kauli Yake "Wala mwandishi asikatae" tunaichukulia kuwa ni makuruhu tu, wala sio haramu; isipokuwa ikiwa kuacha kuandika kutasababisha ufisadi na kusababisha wote wawili kuingia katika haramu, hapo ndio itakuwa kukataa ni haramu. Lakini hilo ni kwa upande wa kukinga ufisadi sio upande wa kuandika deni.

Na aandikishe yule ambaye iko juu yake haki; na amwogope Mwenyezi Mungu Mola wake; wala asipunguze chochote katika deni.

Ambaye haki iko juu yake ni mdaiwa. Maana ni kuwa ni wajibu kwa mdaiwa kutamka waziwazi mbele ya mwandishi, bila ya kupunguza, ili iwe ni ikrari yake kwa haki ya mwenyewe inayomlazimu yeye au warithi wake kulipa; haki inaweza kupotea kama hakuna uthibitisho wa madai.

Haya kwa uchache ndiyo yaliyo wajibu kwa mdaiwa juu ya aliyemkopa, ambaye amemsaidia kumaliza matatizo yake wakati wa dhiki. Nimewaona watu wengi wakimnyeyekea mwenye mali kwa upole kabisa kwa kutaraji kukopeshwa ili kumaliza matatizo. Basi mara mtu anaposaidiwa, anageuka adui na kukataa deni, eti kwa vile tu mwenye mali anataka haki yake. Mbali ya kuwa wema kuulipia maovu ni haram kisheria, lakini hilo linaonyesha ukhabithi na ushenzi.

KUMSHUKURU MUUMBA NA MUUMBWA

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ﴾

"... kwamba unishukuru Mimi na wazazi wako..." (31: 14)

Katika Hadith imesemwa:"Hamshukuru Mwenyezi Mungu asiyewashukuru watu" . Hadith nyingine inasema:"Mwenye kutendewa wema na mtu, akamshukuru Muumba kwa kusema "Shukrani ni za Mwenyezi Mungu", na akamsahahu aliyemtendea wema, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) haikubali shukrani mpaka amshukuru aliyemfanyia wema." Kwa sababu hiyo ndio ukawa mashuhuri msemo:"Asiyeshukuru kiumbe, hamshukuru Muumba."

Ulazima huu una siri nyingi:

1. Akili na sharia zinahukumu wajibu wa kumshukuru yeyote mwenye kutenda vizuri; na mwenye kuacha shukrani hii, basi amemwasi Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni na uasi kukanusha neema za Mwenyezi Mungu (s.w.t).

2. Hadhi ya mtu ni hadhi ya Mwenyezi Mungu. Hadith imesema: "Mwenyezi Mungu atamwambia mja katika waja wake: Kwa nini hukunitembelea nilipokuwa mgonjwa?" Mja atasema: "Kutakata na maovu ni kwako, wewe ni mlezi wa waja, huugui wala huumwi." Mwenyezi Mungu atasema: "Alikuwa mgonjwa nduguyo mumin wala hukumtembelea. Naapa kwa utukufu wangu, lau ungalimtembelea ungelinikuta mbele yake na ningeliziangalia haja zako na kukutekelezea; na hayo ni kwa heshima ya mja wangu na Mimi ni Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu."

3. Kumshukuru mwenye kukufanyia jambo zuri ni kutekeleza amana. Na kutekeleza amana ni dalili ya ukweli na amani, bali ndio asili ya fadhila. Kwani unapopatikana utekelezaji, ndipo hupatikana ukweli, ikhlasi, uaminifu na kujitolea. Na utekeleza ji haugawanyiki - mwenye kumtekelezea amana aliyemtenda wema, basi pia huwatekelezea watu wake, marafiki zake, nchi yake na watu wote kwa ujumla. Na asiyetekeleza amana kwa aliyemfanyia wema au kujitia hamnazo, basi hufanya hivyo hivyo kwa watu wake, marafiki zake, na nchi yake. Ndio maana kukasemwa:"Asiyetekeleza amana hana dini"

4. Inavyopendeza zaidi ni kutekeleza amana wakati wa shida. Kwa sababu kutekeleza wakati wa neema ni kutekeleza kwa ajili ya mali sio kwa ajili ya mwenye mali na ni kwa ajili ya dunia sio kwa ajili ya mwenye dunia.

Na kama yule ambaye juu yake iko haki ni mpumbavu au mnyonge au yeye hawezi kutaja mwenyewe, basi ataje msimamizi wake kwa uadilifu.

Mpumbavu hapa ni yule mbadhirifu aisyeweza kutumia mali vizuri, mnyonge ni mtoto mdogo, na asiyeweza kutaja ni mwenda wazimu, wote hawa hawafai kuandikisha au kufanya ikrari yoyote; isipokuwa ni lazima wasimamiwe mambo yao na wasimamizi (mawalii) wao wanaowaangalia.

Wasimamizi ni aina mbili: Msimamizi mahsusi ambaye ni baba na babu wa upande wa kwa baba; na msimamizi wa kiujumla ambaye ni hakimu wa sharia aliye mwadilifu au Mujtahid. Huyu hana usimamizi mpaka akosekane babu na baba. Ufafanuzi wa Swala hili uko kwenye kitabu Fiqh Imam Jaffar Sadiq.

Na muwashuhudishe mashahidi wawili katika watu wenu wanaume

Hili ni jambo la pili katika mambo aliyoyazingatia Mwenyezi Mungu katika deni: La kwanza ni kuandika na pili ni ushahidi. Kanuni za kutungwa zimeweka sheria ya kupatikana mashahidi wawili katika mikataba rasmi; sawa na ilivyokuja katika Qur'an. Shia Imamiya na Hanafi, wanasema sharti hilo ni, itakapokuwa mwenye kutolewa ushahidi ni mwislamu. Ama akiwa si mwislamu, basi ushahidi wa watu wa mila unakubaliwa kwa mila zao. Malik na Shafi wamesema haukubaliwi ushahidi wa asiyekuwa Mwislamu hata kama anawashuhudia asiyekuwa mwislamu. Haya yanapatikana katika kitabu Mughni na Fathul Qadir mlango wa ushahidi.

Kama hakuna wanaume wawili, basi ni mwanamume mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowaridhia kuwa mashahidi.

Haki za kimali zinathibiti kwa ushahidi wa wanaume wawili, au mwanamume mmoja na wanawake wawili au mwanamume mmoja na yamini, kwa maafikiano ya madhehebu yote; isipokuwa Abu Hanifa. Yeye anasema hautoshi ushahidi wa mtu mmoja na yamini. Qur'an Tukufu imetaja ushahidi wa wanaume wawili na mwanamume mmoja na wanawake wawili tu. Ama kuthibiti haki ya kimali kwa shahidi mmoja na yamini kumefafanuliwa na Hadith. Unaweza kuuliza: Je, inathibiti haki ya mali kwa ushahidi wa wanawake tu? Kisha je, inaweza kuthibiti kwa ushahidi wa wanawake wawili na yamini, kama ilivyo kwa mwanamume mmoja na yamini?

Jibu : Madhehebu yote yameafikiana kuwa haki za mali hazithibiti kwa ushahidi wa wanawake bila ya mwanamume na bila ya yamini, wametofautiana katika kuthibiti kwa ushahidi wa wanawake wawili na yamini. Malik na Imamiya wamesema inathibiti, wengine wamesema haithibiti. Kauli Yake Mwenyezi Mungu "katika wale mnaowaridhia," inachukuliwa maana mbili:

Kwanza : ni kuwa makusudio ya kuridhia ni kuhusisha radhi kwa ushahidi wenyewe hasa, bila ya kuangalia hali ya shahidi. Kwa hiyo hakuna ulazima wa uadilifu wa shahidi, bali itatosha kwa Kadhi kutegemea kwamba ushahidi unaambatana na tukio; kama ulivyo ushahidi katika kanuni zilizotungwa, ambapo kadhi pekee ndiye anayekadiria ushahidi. Maana yapili : ni kuridhia hali ya shahidi mwenyewe, kwa hivyo lazima shahidi awe mwadilifu, tamko la Aya linachukua maana zote mbili, lakini hadith na fatwa za Mafaqihi zinatilia nguvu matakwa ya uadilifu kwa shahidi mwenyewe, Imam Ali(a.s) anasema:

"Mshuhudieni ambaye mnaridhia dini yake, uadilifu wake utengeneo wake na kujiepusha kwake na dhambi." Kwa hivyo wakitoa ushahidi waadilifu wawili, basi ni juu ya Kadhi kuhukumu kwa mujibu wa ushahidi wao; ni sawa awe ameelewa kutokana na kauli yao au hakuelewa kwa kuchukulia Hadith. Ama akishuhudia asiyekuwa mwadilifu, hawezi kuhukumu kwa ushahidi wao isipokuwa kama amepata kuelewa kutokana na kauli yao, kiasi ambacho kujua ndio kutakuwa ni matokeo ya hukumu, sio ushahidi wa asiyekuwa mwadilifu.

Ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine.

Hapa pana maswali mawili:

Kwanza : kwa nini amesema: "Ili kama mmoja wao akipotea, mmoja wao amkumbushe mwingine." Na wala asiseme: Amkumbushe mwingine tu. Kuna haja gani ya kurudia nomino iliyo wazi katika jumla mbili ambazo hazikutengana kwa mbali wala karibu?

Hilo limejibiwa kwa njia nyingi, bora yao ni kuwa, ulipokuwa ushahidi wa wanawake wawili ni sawa na ushahidi wa mwanamume mmoja, basi ni wajibu kuukusanya ushahidi wa hao wanawake wawili, ili kwamba akisahau kitu, mwingine amkumbushe. Akimaliza, anaanza wa pili naye akisikilizwa na mwenzake wa kwanza, kama alivyofanya yeye. Kwa hiyo utakuwa ushahidi wa kila mmoja wao unatimiza ushahidi wa mwengine. Maana hayo hayawezi kuja, isipokuwa kwa kurudi neno 'Mmoja wao' ili uweko mfungamano wa wawili, lau angelisema: amkumbushe mwengine tu, basi maana yangalikuwa: "Ili akisahau mmoja akumbushwe na wa pili, Kwa hiyo mmoja atakuwa anasema na mwingine ni mkumbushaji tu, na hayo siyo makusudio yake." Kwa ujumla ni kuwa, si wajibu kuwakusanya pamoja mashahidi wakiwa wanaume; bali kuwatenganisha ni bora. Lakini kwa wanawake ni kinyume na hivyo.

Swali la pili : Kuna siri gani ya kuwa ushahidi wa wanawake wawili unalingana na ushahidi wa mwanamume mmoja?

Swali hili limejibiwa kwa njia nyingi. Miongoni mwazo ni kuwa mwanamke ana akili dhaifu. Kauli ya kushangaza ni kuwa kuna baadhi ya wafasiri wanaosema kuwa: Mwanamke ni mpole. Kama kauli hii ingelikuwa sawa, basi ingelikuwa upole ni nusu ya ushahidi, hata kama ni mwanamume; na kila asiyekuwa mpole basi ni shahidi kamili, hata kama ni mwanamke! Kauli yenye nguvu ni kuwa aghlab mwanamume anaweza kuzuwia hisia zake zaidi kuliko mwanamke. Na jibu sahih zaidi ni kwamba ni juu yetu kuikubali amri hata kama hatujui hekima yake. Kwa ujumla ni kwamba Kadhi mara nyingine anaweza kutegemea ushahidi wa mwanamke mmoja na kupata kujua kutokana na kauli yake zaidi, kuliko kutegemea ushahidi wa wanaume kumi wasiokuwa waadilifu. Na, inajuzu Kadhi kutoa hukumu kwa kujua kulikotokana na mwanamke, maadamu ni nyenzo ya kujua au kupata uhakika.

Na mashahidi wasikatae waitwapo

Akikuita mdai, ili umtolee ushahidi juu ya haki au deni, basi ni wajib kifaya (wa kutosheana) juu yako kuitikia wito wake; yaani kama akitekeleza mwingine umuhimu huu, basi wajibu utakuwa umekuondokea; vinginevyo utakuwa na jukumu mbele ya Mwenyezi Mungu. Dalili ni Aya hii na Hadith Tukufu:"Atakapokuita mtu ili umshuhudilie juu ya haki au deni, basi usirudi nyuma."

Wala msichoke kuiandika ikiwa ni ndogo au kubwa, mpaka muda wake.

Makusudio ni kuhimiza kuandika deni bila ya kutofautisha uchache wake au wingi wake, maadamu lengo ni kuchunga kusitokee tofauti na mizozo.

Haya ndiyo uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu na imara sana kwa ushahidi na ni karibu zaidi kutofanya shaka.

Yaani kuandika deni na kulishuhudilia ndiyo bora na imara na ni karibu zaidi kuondoa shaka. Unaweza kuuliza: Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameamrisha kuandika.

Kwanza : katika kauli yake: "Basi iandikieni"

Pili :"Wala msichoke kuandika"

Tatu : ameishiria hekima ya hilo, kwamba kuandika ndio bora na imara. Lakini pamoja na yote hayo mafaqihi wamefutu kuwa ni suna kuandika, sio wajibu. Wameendelea nalo hilo tangu zamani mpaka sasa. Nasi tuko pamoja nao kwa hilo, lakini kuna jambo jengine lisilokuwa kuandika deni na kulishuhudia, nalo ni kuwa mafaqihi wamewajibisha kadhi kuhukumu kwa mujibu wa ubainifu wenye uadilifu, hata kama hakupata kujua kitu kutokana na ubainifu huo.

Na hilo si ni kufuata tamko tu? Jambo ambalo mafaqihi hawakulifuata, katika suala la kuandika, kuwa ni njia ya kuthibitisha, kama ubainifu, wakasema: "Haijuzu kuhukumu kwa maandishi mpaka akipata kujua kitu kutokana na maandishi na aridhike" Je, amri hii iliyokaririka haifahamishi kuwa kuandika ni njia ya kuthibisha haki?

Jibu : Amri ya kuandika deni ili kuilinda haki kwenye kuthibiti, ni jambo moja, na kuzingatia ubainifu wenye uadilifu kuwa ni njia ya kuthibitisha haki, ni jambo jengine. Kwa hiyo ni wajibu kuhukumu kwa mujibu wa ubainifu, sawa awe mwenye kuhukumiwa amekiri au amekanusha.

Ama kuandika hapana budi kuulizwa mshtakiwa, akikiri, basi litakuwa ni suala la kukiri, na kama akikanusha, basi utahitajika uthibitisho kujaribu kupata uhakika kwa uchunguzi kwa kutumia njia nyingine; kama vile ushahidi, yamini au na kulinganisha hati ya mwandishi. Kwa hivyo basi maandishi peke yake hayatoshi, kuwa ni njia inayojitegemea.

Ila ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayopeana baina yenu, basi si vibaya kwenu msipoiandika.

Hapa maneno yanahusu biashara ya mkono kwa mkono na ruhusa ya kuacha kuandika.

Biashara ya mkono kwa mkono ni ile biashara ya kupeana muda huo huo.

Maana ya mnayoopeana baina yenu, ni kutoka mkono moja hadi mwengine, muuzaji anachukua thamani kutoka kwa mnunuzi na mnunuzi naye anachukua kile kilichotolewa mali kutoka kwa muuzaji.

Maana ya Aya kwa ujumla, ni kwamba si vibaya kuacha kuandika katika biashara ambayo thamani yake inatolewa muda huo huo. Ama siri ya kuacha kuandika, ni kwamba biashara hii hufanyika mara kwa mara kati ya watu; lau wangelikalifishwa kuandika kwa kila biashara, basi kungalikuwa na mashaka kwao hasa katika vitu vidogo. Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba sheria tukufu imewaachia watu mambo ya biashara kwa kiasi cha maslahi yao. Ikiwa maslahi yako kwenye kuandika, basi na waandike; kama ilivyo katika biashara ya viwanja, magari, n.k. Na kama maslahi ni kuacha kuandika, kama biashara ya vyakula na mavazi, basi na waache. Mwenyezi Mungu alipoamrisha kuandika deni na biashara au kuruhusu kuacha ni amri ya kupendekeza na kuongoza kwenye mambo ambayo yatawaepushia tabu na matatizo. Hata hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakataza na kuharamisha hadaa, riba na kula mali kwa batili bila ya kutoa chochote.

Unaweza kuuliza; Kusema kuwa si vibaya kuacha kuandika biashara ya mkono kwa mkono inafahamisha kuwa ni vibaya kuacha kuandika deni. Kwa hivyo basi, kuandika deni ni wajibu kinyume na wanavyosema mafaqihi kuwa ni suna na wala si wajibu.

Jibu : Makusudio ya kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t)"Basi si vibaya kwenu msipoiandika" ni kukanusha ubaya na madhara ya kidunia, sio kukanusha dhambi na madhara ya kiakhera na kuwa kuandika ni wajibu.

Na wekeni mashahidi mnapouziana

Mafaqihi wote wameafikiana kuwa kushuhudia biashara ni sunna sio wajibu, isipokuwa watu wa madhehebu ya Dhahiri (Dhahiriya) wanasema ni faradhi sio sunna, kwa kuchukulia dhahiri ya tamko.

Wala asitiwe tabu mwandishi wala shahidi

Wanaouziana wakiafikiana kuandika na ushahidi basi ni juu ya mwandishi kuandika kwa uadilifu na shahidi kushuhudia kwa haki.Yamekwishatangulia maelezo kuhusu asitiwe tabu, katika kufasiri Aya ya 233.

Na kama mkifanya hivyo; basi hakika hilo ni ufasiki kwenu.

Ufasiki ni kutoka katika twaa ya Mwenyezi Mungu; na kila anayefanya kitu kilichokatazwa na Mwenyezi Mungu au kuacha kitu kilichoamrishwa na Mwenyezi Mungu, basi huyo ni fasiki aliyetoka katika twaa ya Mwenyezi Mungu mwenye kustahili ghadhabu na adhabu Yake.

Na Mcheni Mungu

Kwa kutii amri Zake zote na makatazo yake yote.

Na Mwenyezi Mungu anawaelimsha; na Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

Anawaelimisha yale yaliyo na heri kwenu katika dini na dunia. Kimsingi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatufundishi Yeye moja kwa moja; wala haitii elimu katika akili zetu na nyoyo zetu; isipokuwa anatuelimisha kupitia wahyi anaouteremsha kwa Mitume Wake. Wahyi huu unakusanya kila lile lililo na mwongozo na kutuongoza kwenye maslahi yanayodhamini kudumu kwetu na utangamano wetu.

USUFI

Masufi wote au baadhi wanasema hakuna njia ya maarifa na kumjua Mwenyezi Mungu na wahyi Wake na sharia na siri Zake isipokuwa kwa imani na takua (kumcha Mungu). Mwenye kumcha Mwenyezi Mungu, basi ndio amemjua na amejua sharia Yake na hukumu Zake; na ndio ameijua akhera na vituko vyake. Vilevile atakuwa ameifahamu Qur'an na Hadith bila ya darasa au taaluma yoyote. Hii wanaiita elimu ya ki-Mungu na wakatoa dalili kwa kauli Yake Mwenyezi Mungu:

Na mcheni Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu anawaelimisha.

Lakini tamko la Aya linakataa dalili hii; Kwa sababu lau ingelikuwa kama walivyosema basi, kinahw, tamko Yuallimukum lingejazimishwa kuwa ni jawabu la Ittaqu na lingeambatanishwa na herufi Fai na wala sio kwa herufi Wau. Zaidi ya hayo maana katika fikra ya kauli hii ya kisufi, inafanana na kauli ya mtu aliyepagawa akisema: "Hakika nyumba haitimii kujengwa ila baada ya kukaliwa, na kwamba nguo haikamiliki kushonwa ila baada ya kuvaliwa." Sijui Masufi wanadai vipi hali hii; na hali imekuja hadith mutawatir kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) inayosema: "Tafuteni elimu japokuwa China" na" Elimu ni kwa kujifundisha". Sisi hatuna shaka kabisa kwamba nadharia inadhihirika kwa kufuatilia na kutenda, na kwamba mtaalamu mwenye kufanya kazi, hufungukiwa na mambo mapya. Lakini hili ni jambo jengine na kuwa taqwa ni nyenzo ya maarifa ni jambo jengine.

Na kama mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, basi ni itakayo kabidhiwa rahani

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kuandika deni kwa ajili ya kulihifadhi, amejaalia rahani ndio tegemeo badala ya kuandika, kama kukiwa na udhuru.Mafaqihi wameafikiana kwamba rahani haitimii bila kukabidhiana. Wametoa dalili kwa kauli hii: "Basi ni rahani itakayokabidhiwa" Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh; kama vile Fiqhul Imam Jaffar Sadiq Juzuu ya 4.

Unaweza kuuliza: Rahani inajuzu katika safari na nyumbani, na pamoja na kupatikana mwandishi au kukosekana; sasa nini makusudio hapa ya kuleta sharti la safari na kukosekana mwandishi?

Baadhi ya wafasiri wamelipuuza swali hili, ingawaje linaweza kumjia kila mwenye kujua hukumu za sheria, Wengine wamejibu kuwa Mwenyezi Mungu amepitisha kwa aghlabu, kwa kuwa wakati huo ilikuwa ni nadra kupatikana mwandishi safarini. Lakini iinavyoonekana ni kwamba pia aghlabu ni kukosekana rahani katika safari. Kwani ni nani anayechukua vitu vinavyoweza kuwekwa rahani katika safari, isipokuwa kwa nadra tu? Jibu: sahihi ni kwamba Aya kwa dhahiri inafahamisha kutojuzu rahani nyumbani, kwa kuchukulia kuwa sharti limefahamika; yaani kama hamko safarini basi hakuna rahani. Lakini dhahri hii haijuzu kuitegemea baada ya kuthibiti kwamba Mtume(s.a.w.w) aliyeshukiwa na wahyi, hakuitumia dhahiri hiyo. Yeye aliwahi kuweka rahani deraya yake kwa myahudi alipokuwa nyumbani Madina. Wala hii sio Aya pekee ambayo tunaiacha dhahiri yake kwa Sunna ya Mtume. Na ni kwa sababu hii ndipo umma wa kiislam umesema, kwa kauli moja, kwamba haijuzu kuchukulia dhahiri ya Aya katika Aya za hukumu ya sharia, ila baada ya utafiti wa Hadith za Mtume zilizopokewa kutolea dalili Aya Tukufu.

Na kama mmoja wenu akimwamini mwengine, basi aliyeaminiwa atekeleze uaminifu wake, na amche Mungu, Mola wake

Yaani mdeni akiwa na dhana nzuri kwa mdaiwa, akampa bila ya cheti wala rahani au ushahidi wowote wa kutegemea, basi ni juu ya mdaiwa aiendeleze ile dhana nzuri na amrudishie mdai haki kamili. Zaidi ya hayo hukumu hii ni ya ujumla haihusiki na deni tu, bali inachanganya amana zote. Mwenyezi Mungu amesema:

﴿إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha kutekeleza (kuzirudisha) amana kwa wenyewe..." (4:58)

Mtume naye anasema: "Msiangalie Swala ya mtu na Saumu yake, na wingi wa Hijja zake na umaarufu wake; na kuvuma kwake usiku, lakini angalieni ukweli wa mazungumzo yake na utekelezaji wake wa amana." Imam Zainul Abidini(a.s) anasema:"Lau kwamba aliyemuua baba yangu ananiwekea amana upanga aliomuulia baba yangu, basi nitamrudishia."

Wala msifiche ushahidi, Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini

Kuna tofauti kati ya kuchukua ushahidi na kuutekeleza. Maana ya kuuchukua ushahidi ni kuitwa ushuhudie haki au deni. Hapa kukubali ni wajib kifaya (wa kutosheana) na wala sio wajib ayni; kama tulivyyoeleza huko nyuma. Ama kuutekeleza ni kukuita mwenye haki baada ya wewe kuuchukua ushahidi, ili utoe katika mahakama; hapa huwezi kukataaa ikiwa haki haitaweza kuthibiti bila ya ushahidi wako, na kukawa hakuna madhara.

Kama hutafanya basi utakuwa na dhambi kutokana na kauli Yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) "Wala msifiche ushahidi"

Na makusudio ya moyo wake kuingia dhambini, ni kwamba yeye ataadhibiwa adhabu ya kukusudia dhambi, kwa sababu kukusudia ni katika sifa za moyo.

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿ لِّلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَإِن تُبْدُوا مَا فِي أَنفُسِكُمْ أَوْ تُخْفُوهُ يُحَاسِبْكُم بِهِ اللَّـهُ فَيَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

284.Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na kama mkidhihirisha lililo katika nafsi zenu, au mkilificha, Mwenyezi Mungu atawataka hisabu ya hilo; kisha amghufirie amtakaye, na amwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.

KAMA MKIDHIHIRISHA YALIYOMO KATIKA NYOYO ZENU

Aya 284

MAANA

Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na kama mkidhihirisha lililo katika nafsi zenu, au mkilificha, Mwenyezi Mungu atawataka hisabu ya hilo.

Mara nyingine katika moyo wa mtu hupita mawazo mabaya asiyowezea kuyazuia; kama vile kutamani kubomoka nyumba ya fulani au akanyagwe na gari. Katika mawazo kama haya hakuna hisabu wala adhabu, maadamu ni mawazo tu yasiyoonekana athari ya vitendo au maneno yake. Kwa sababu haya yako nje ya uwezo, kukalifishwa nayo ni kukalifishwa yasiyowezekana.

Mara nyingine mtu huazimia maasi kabisa na kukusudia kuyafanya, mpaka anapokurubia kuyafanya, basi hurudi nyuma, ama kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu au kuogopa watu. Basi ikiwa ni kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu hupata thawabu, kwa sababu kunahisabiwa ni kutubia. Na kama ni kwa kuwaogopa watu, basi hakuna malipo yoyote, si thawabu wala adhabu, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.

Kuna Hadith inayosema:"Mtu akikusudia wema na kisha asiufanye huandikiwa wema mmoja; na kama akiutenda, huandikiwa kumi, Na kama akikusudia uovu akaufanya, hundikiwa ovu moja, na kama hakuufanya, basi haandikiwi chochote."

Mara nyingine mtu huazimia kufanya maasi, na kuyafanya kwa vitendo. Maasi haya yako aina mbili: Kwanza ni kumwasi Mwenyezi Mungu waziwazi, bila ya kujali maneno ya watu na lawama zao. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na kama mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu." Aina nyingine ni ya kuficha maasi kwa unafiki na ria kufanya ufisadi kwa kujificha na kutangaza wema.Aina zote hizo anazijua Mwenyezi Mungu.

Kisha amghufirie amtakaye na amwadhibu amtakaye

Maadamu Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ni mfalme wa mbingu na ardhi Muweza wa kila kitu, asi anao uweza wa kusamehe amtakaye katika uasi na kumwadhibu amtakaye kutokana na inavyohukimilia hekima Yake. Muhyiddin Ibn al Arabi anasema katika tafsiri yake kwamba Mwenyezi Mungu anamsamehe mwasi akiwa ana nguvu katika imani yake, lakini akawa amezukiwa tu kufanya maasi, sio kuwa yameota mizizi katika nafsi yake, na humwadhibu muasi aliye mdhaifu wa imani ambaye maasi yameota mizizi katika nafsi yake.

﴿آمَنَ الرَّسُولُ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مِن رَّبِّهِ وَالْمُؤْمِنُونَ كُلٌّ آمَنَ بِاللَّـهِ وَمَلَائِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّن رُّسُلِهِ وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا غُفْرَانَكَ رَبَّنَا وَإِلَيْكَ الْمَصِيرُ ﴾

285.Mtume na Waumini, wote wameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake, na wamemwamini Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na Vitabu Vyake na Mitume Wake: Hatutofautishi baina ya yoyote katika Mitume wake. Na husema: Tumesikia na tumetii. Twaomba maghufira yako Mola wetu! Marejeo ni Kwako.

﴿لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴾

286.Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila uweza wake. Faida ya yale iliyoyachuma ni yake na hasara iliyochuma ni yake. Mola wetu! Usituadhibu tukisahau au tukikosa, Na usitutwike mzigo kama uliyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza na utusamehe na utughufurie na uturehemu wewe ndio Mola wetu na utunusuru na watu makafiri.

MTUME AMEAMINI

Aya 285 – 286

LUGHA

Makosa hutumiwa kwa maana tatu: Dhambi, kutokusudia, na kutofanya sawa. Maana hii ya mwisho,ndiyo iliyokusudiwa katika Aya.

MAANA

Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake

Hapa kuna swali linalojitokeza, kwamba: kila Mtume anaamini wahyi ulioteremshwa kwake, vinginevyo hatakuwa Mtume. Kwa hiyo kulielezea hili kunafanana na kuliweka wazi ambalo tayari liko wazi, na kujaribu kulipata ambalo lipo, jambo ambalo haliwezekani katika maneno ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa hiyo hapana budi kuwe na lengo la kulielezea hilo, Ni lipi basi?

Jibu : Lengo sio tu kueleza kuwa Mtume(s.a.w.w) amemuwamini Mwenyezi Mungu hapana! Kwani kila Mtume anazaliwa akiwa amemwamini Mwenyezi Mungu na Umoja wake, lakini sio kila Mtume anazaliwa akiwa Mtume, au kujua kuwa yeye ni Mtume isipokuwa Nabii Isa(a.s) ambaye mara tu alipozaliwa alisema:

﴿قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا﴾

"Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na amenifanya Nabii" (19:30)

Muhammad(s.a.w.w) hakushukiwa na wahyi mpaka alipofika miaka arobaini katika umri wake mtukufu. Alipoambiwa na Jibril mara ya kwanza

﴿اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ﴾

"Soma kwa jina la Mola wako ambaye ameumba" (96: 1)

Alitia shaka na akahofia isije ikawa sauti ile ni wasiwasi na mawazo tu, mpaka akamwambia mkewe mpenzi, Khadija, aliyekwenda naye kwa Waraqa bin Naufal; kisha akampa maelezo ya kutosha kwamba aliyemjia ni Malaika wala sio shetani. Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa lengo katika kauli yake Mwenyezi Mungu; "Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake" ni kwamba yaliyokuja katika Sura hii na mengineyo katika misingi ya imani na itikadi, maonyo, hukumu na kila aliyoyatolea habari Mtume, ni katika wahyi wa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) Na wahyi huo hakuuamini Mtume ila baada ya kupitiwa na shaka, utafiti na kuchunguza vizuri; na baada ya kufunuliwa na uhakika kabisa. Kwa hiyo kila analolielezea Mtume, basi linatoka kwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka yoyote.

MAELEZO

Maulamaa wengi wa Kishia hawakubaliani na usahihi wa Kisa hiki, miongoni mwao ni Mwanachuoni Sayyid Muhammad Hussein Tabatabai katika Tafsir Al-Mizani anasema katika kufasiri sura ya Alaq (97:1), baada ya kutaja kisa cha Waraqa bin Naufal: Kisa hiki hakiwezi kuepukana na shaka. Kinachodhoofisha usahihi wake ni shaka ya Mtume(s.a.w.w) kwa Wahyi wa Mwenyezi Mungu na kusitasita kwake na kudhani eti amezugwa na shetani?! Linalotia shaka zaidi ni kwamba yeye alipata uhakika wa Utume wake kutoka kwa Mkristo na hali Mwenyezi Mungu anasema katika Qur'ani

﴿قُلْ إِنِّي عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي﴾

"Sema mimi nina dalili ya wazi itokayo kwa Mola wangu" (6:57)

sasa dalili ya wazi ni kauli ya Waraqa? Na Aya isemayo:

﴿قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي وَسُبْحَانَ اللَّـهِ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴾

"Sema hii ndiyo njia yangu, ninailingania kwa Mwenyezi Mungu kwa ujuzi, mimi na wanaonifuata" (12:108)

Je, ujuzi ndio huo alioupata kwa Waraqa? Na ujuzi wa wale wanaomfuata unatokana na kumfuata yeye asiyekuwa na uhakika? "Mwenyezi Mungu anasema tena

﴿إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ﴾

"Hakika sisi tumekuletea Wahyi kama tulivyompelekea Wahyi, Nuh na Manabii baada yake" (4:163)

Je, hao Mitume wengine kupata kwao wahyi kulitegemea watu kama kina Waraqa? Ilivyo ni kuwa wahyi wa utume nilazima uwe na uhakika kutoka kwa Mtume mwenye kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika kufasiri Aya hii (Ameamini Mtume) mwenye Tafsir Al-Mizan anasema: Ni kusadikisha imani ya Mtume na waumini. Amewekwa peke yake Mtume kisha akaunganishwa na waumini kwa kumtukuza. Hii ni desturi ya Qur'an katika maelezo yanayohusiana na kumtukuza Mtume kumtaja yeye kwanza kisha kufuatishia wengine; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

﴿فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ﴾

"Basi hapo Mwenyezi Mungu aliteremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na Waumini" (48:26)

﴿يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ﴾

"Siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamfedhehesha Mtume na wale walioamini pamoja naye" (66:8)

Kwa ujumla sura ya Baqara imeanzia kwa kueleza sifa wanazostahiki kuwa nazo wachamungu.

Kama vile kuamini ghaib, kuswali, kutoa, kuamini Mitume na akhera, kinyume na makafiri na wanafiki. Kisha ikaelezea hali ya watu wa kitabu; hasa Mayahudi ambao Mwenyezi Mungu aliwaneemesha kwa neema mbali mbali, lakini wakakufuru badala ya kushukuru. Hivyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa aina mbali mbali za adhabu; kama kujiua, kugeuzwa kuwa manyani, kushuka vimondo adhabu kutoka mbinguni n.k Mwisho sura inaelezea wasifu wa Mtume na wafuasi wake kwamba wao ni kinyume na watu wa Kitab walivyoikabili neema ya Mwenyezi Mungu. Wamesikia na kutii, hali ya kumwamini Mwenyezi Mungu, Malaika wake, Vitabu Vyake na Mitume Yake bila ya kumbagua yeyote katika Mitume.

Na waumini; wote wamemwamini Mwenyezi Mungu na Malaika wake na vitabu vyake na Mitume wake: Hatutofautishi baina ya yoyote katika Mitume wake.

Maana kamili ya kumwamini Mwenyezi Mungu sio kuitakidi kwamba Yeye ni Muumbaji wa ulimwengu tu, hapana, mumin wa kweli ni yule anayemwamini Mwenyezi Mungu na Mitume na vitabu vilivyoteremshiwa wao pamoja na yaliyomo ndani yake, ikiwa ni pamoja na misingi, hukumu, Malaika na mengineyo katika mambo ya ghaibu, bila ya kuacha mengine. Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu bila ya kuamini Vitabu Vyake na Mitume wake, au kuamini baadhi ya Vitabu Vyake na Mitume Wake, hukumu yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu ni hukumu ya asiyeamini kabisa.

Lau watu wa dini wangelichukua misingi ya kumwamini Mwenyezi Mungu na kila alilolileta, basi kusingekuwa na makundi na migogoro; lakini wao wameamini baadhi na wakakanusha baadhi, ndipo kukawa na uadui huu wa kuendelea.

Mwenyezi Mungu hakalifishi nafsi yoyote ila uweza wake.

Kwa sababu kukalifisha bila ya uwezo ni dhulma

﴿وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴾

"... Na kwamba Mwenyezi Mungu si dhalimu kwa waja" (3:182)

Lakini Ashaira wamejuzisha taklifa bila ya uwezo, Shia Imamiya na Muutazila wamekanusha.Faida ya yale iliyoyachuma ni yake ; miongoni mwa kheri.Na hasara ya iliyochuma ni yake .Miongoni mwa shari na maovu.

﴿فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ﴾

"Mwenye kufanya heri sawa na chembe ataiona.Na mwenye kufanya shari sawa na chembe ataiona" (99: 7 -8)

Miongoni mwa rehema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni kwamba mja akifanya wema humwandika hapo hapo, lakini akifanya uovu, humpa muda, akiomba msamaha na kujuta, hamwandikii kitu. Baadhi ya wataalamu wanasema: Mtu hufanya wema kwa msukumo wa nafsi yake, kwa sababu ndio umbile lake; na hafanyi shari isipokuwa kwa vichocheo vya nje kama vile mazingira na malezi mabaya.

Kwa hali hiyo ndio maana Mwenyezi Mungu akatumia neno Kasaba katika heri lenye maana ya kuchuma tu na akatumia neno Iktasaba katika shari lenye maana ya kuchuma zaidi.

Mola wetu! Usituadhibu tukisahau au tukikosa

Hapa kuna mushkeli mashuhuri ambao umezungumzwa sana na umejaribiwa kujibiwa katika elimu ya Usul na Tawhid. Mushkeli wenyewe kwa ufupi ni kwamba kukosea na kusahau hakuko chini ya matakwa ya mtu na uwezo wake. Kwa hiyo kuadhibiwa hakuko; kwa mfano mwenye kusahau kuswali au akakosea katika kufahamu hukumu ya sharia, anahukumiwa kuwa na udhuru.Kwa hivyo basi hakuna maana wala haja ya kuomba kuondolewa adhabu. La kustaajabisha ni jinsi alivyojibu Sheikh Muhammad Abduh - kama alivyonakili mwenye Tafsiri ya al Manar - kwamba mwenye kusahau na mwenye kukosea inafaa kuadhibiwa kwa dalili ya sharia ya kiislamu na sharia zilizowekwa na binadamu, ambazo zimewajibisha kulipa mtu aliyeharibu mali ya mwingine kwa makosa, kama aliyeuwa kimakosa. Kushangaza kwake ni kwamba, makusudio ya kuadhibiwa katika Aya ni adhabu na majukumu ya kitabia, sio gharama. Kwa hiyo anayemuua mtu kimakosa au kuharibu mali kwa makosa haadhibiwi wala haulizwi kitu upande wa kitabia; isipokuwa atahukumiwa kulipa gharama ya kimali tu, sawa na mtu anayedaiwa.

Jibu sahihi ni kwamba kukosea na kusahau mara nyingine humtokea mtu baada ya kujichunga.Aina hii ndiyo ambayo mtu husamehewa wala haifai kumwadhibu.

Hayo ndiyo makusudio ya Aya tukufu, Na pengine kosa na kusahau hutokea kwa sababu ya kuzembea na kuacha kujihifadhi, kwa namna lau angezindukana na kujilinda hayangemtokea. Aina hii huwa mtu hasamehewi na inafaa kumwadhibu. Hilo,katika dua, ndilo linaloombwa liondolewe. Kwa hiyo hapo hakuna mushkeli tena.

Mola wetu! Wala usitutwike mzigo kama uliyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza

Makusudio ya mzigo hapa ni taklifa na mashaka. Mwenyezi Mungu aliwatwika wana wa Israil, pale alipowaamrisha kuswali Swala hamsini mchana na usiku na katika taklifa za mashaka ambazo wamezitaja wafasiri walipofasiri: "Kama ulivyowatwika wale waliokuwa kabla yetu" Kwa hivyo maana yanakuwa usitukalifishe yaliyo mazito.

Unaweza kuuliza: Kauli ya Mwenyezi Mungu; "usitutwike tusiyoyaweza" ina maana sawa na "usitutwike mzigo" ambapo hapo ni kuunganisha jumla zenye maana sawa?

Jibu : Kama tukiangalia jumla ya"usitutwike tusiyoyaweza" kuwa ni jumla mbali iliyoepukana na mfumo wa maneno, basi itakuwa hivyo. Kwa sababu maana ya dhahiri ni usitutwike yaliyo na mashaka na sisi. Lakini tukiangalia kuwa iko pamoja na mfumo mzima wa maneno, itakuwa na maana ya: Usituadhibu adhabu tusiyoweza. Kwa hiyo ikafasiriwa adhabu kuwa ni lile linalopelekea adhabu tusiyoiweza na kuivumilia. Sheikh Murtadha al Ansari katika kitabu chake kinachoitwa al Rasail mlango wa Baraa anasema: "Sio mbali kuwa makusudio ya tusiyoyaweza katika Aya ni adhabu na mateso, kwa hiyo maana ya usitutwishe tusiyoyaweza ni usitupe adhabu tusiyoiweza."

Na utusamehe na utughufurie na uturehemu

Msamaha, maghufira na rehema ni matamko yenye kukurubiana, tofauti ni ndogo kwam- ba msamaha ni kutoadhibiwa tu; maghufira ni kutoadhibiwa na kusitiriwa dhambi, na rehema ni kutaka kufadhiliwa na kuneemeshwa kwa thawabu. Wewe ndiwe Mola wetu na utunusuru na makafiri. Ambao wanaidharau dini ya Mwenyezi Mungu,na kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Katika Majmau imeelezwa kuwa: imepokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba: Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika kila kifungu cha dua hii husema:"Nimefanya na nimeitikia (maombi)." Kwa hivyo basi ndipo ikawa sunna kusoma sana dua hii:

"Mola wetu! Usitutese kama tukisahau au tukikosea. Na usitutwike mzigo kama ulivyowatwika wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu! Usitutwike tusiyoyaweza na utusamehe na utughufirie na uturehemu wewe ndiwe Mola wetu na utunusuru na watu makafiri"

MWISHO WA SURAT AL - BAQARAH (NGO’MBE)