TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU 0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16148
Pakua: 2467


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 12 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16148 / Pakua: 2467
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TATU Juzuu 3

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TATU

﴿وَمِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ مَنْ إِن تَأْمَنْهُ بِقِنطَارٍ يُؤَدِّهِ إِلَيْكَ وَمِنْهُم مَّنْ إِن تَأْمَنْهُ بِدِينَارٍ لَّا يُؤَدِّهِ إِلَيْكَ إِلَّا مَا دُمْتَ عَلَيْهِ قَائِمًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَيْسَ عَلَيْنَا فِي الْأُمِّيِّينَ سَبِيلٌ وَيَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴾

75.Na katika watu wa Kitabu yuko ambaye ukimwamini na mrundo wa mali atakurudishia. Na katika wao yuko ambaye ukimpa amana ya dinari moja hakurudishii, isipokuwa ukimsimamia hayo ni kwa kuwa walisema: "Hatuna lawama kwa wasiojua kusoma" Na wanamzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na hali wanajua.

﴿بَلَىٰ مَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ وَاتَّقَىٰ فَإِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ ﴾

76.Sivyo hivyo, bali anayetimiza ahadi na akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu huwapenda wacha Mungu

KUNA WAAMINIFU NA WAHAIN I KATIKA WATU WA KITABU

Aya 75 - 76

MAANA

Na katika watu wa Kitabu yuko ambaye ukimwamini na mrundo wa mali atakurudishia katika wao, Na yuko ambaye ukimpa amana ya dinar moja hakurudishii.

Makusudio ni kwamba katika watu wa Kitabu kuna ambao wako katika upeo wa uaminifu, hata ukiwaamini na mali nyingi, basi watatekeleza amana. Na pia wako walio katika upeo wa hiyana hawaaminiki hata kwa dinar moja tu. Umetajwa uaminifu wa mali, kwa sababu ndiyo mtihani sahihi wa kujua ubovu na uzima wa moyo wa mtu.

HAKUNA MAISHA ILA KWA UKAKAMAVU WA KUTOJALI MAUTI

Isipokuwa ukimsimamia

Mwenye hiyana hutaka zaidi ya haki yake wala hatekelezi haki ya watu, kwa sababu ni maiti wa dhamiri. Wala hakuna njia ya kuipata haki kutoka kwake isipokuwa kwa kumsimamia, kama alivyosema mwenye hekima kubwa. Maana ya kumsimamia mwenye hiyana mnyang'anyi ni kumsonga na kugombana naye kwa silaha yoyote uliyo nayo. Walikwishasema wahenga: "Uhuru huchukuliwa, wala hautolewi." Kumsonga mhaini ni faradhi ya lazima; vinginevyo ufisadi ungelienea duniani. Kosa la kunyamaza mdhulumiwa, ni sawa na kosa la dhalimu. Kwa sababu wote wawili wanaandaa kueneza dhulma na ufisadi. Lau dhalimu angelijua kuwa mdhulumiwa ana hisia za kutojali kufa kugombea haki yake,basi asingelidhulumu.

Majaribio yametufahamisha kuwa hakuna haki katika Umoja wa mataifa wala Baraza la usalama isipokuwa kwa kutumia nguvu; na kwamba hakuna maisha katika karne ya ishirini hasa Mashariki ya kati na hasa hasa waarabu, isipokuwa kwa ukakamavu wa kutojali mauti.

Hayo ni kwa kuwa walisema: Hatuna lawama kwa wasiojua kusoma.

Maana yake ni kuwa watu wa Kitabu walijihalalisha mali za waarabu, kwa sababu wao walidai kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatawaadhibu kwa unyang'anyi huo.( [13] ) Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu uzushi wao, kwa kusema:

Na wanamzulia Mwenyezi Mungu uwongo na hali wanajua.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kumzulia Mwenyezi Mungu kwa kukusudia, hiyana yake ni kubwa na kosa lake ni ovu zaidi. Unaweza kuuliza: Mataifa yote na watu wa dini zote, bali hata walahidi pia, kuna waaminifu na wenye hiyana; wakweli na waongo. Kuna walahidi kadhaa walio wakweli na kutekeleza amana kuliko wanaofunga na kuswali. Sasa kuna wajihi gani wa kuwahusisha watu wa Kitabu na kifungu hiki?

Jibu :Kwanza : katika Aya Mwenyezi Mungu amesema kuwa baadhi ya watu wa Kitab wanataka kuwapoteza, akasema tena wanataka kuamini asubuhi na kukufuru jioni. Na katika aya hizi anabainisha kuwa kuna waaminifu na wahaini, Na hii haimaanishi hakuna wengine wasiokuwa hivyo.

Pili : Inawezekana tuadhanie watu wa Kitabu wote wana hiyana; ndipo Mwenyezi Mungu akaondoa tuhuma hii, kwamba wao ni kama vikundi vingine na watu wa dini nyingine.

Si hivyo, bali anayetimiza ahadi yake na akamcha Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu huwapenda wacha mungu.

Ni kuthibitisha yale waliyoyakana watu wa Kitabu waliposema: Hatuna lawama kwa wasiojua kusoma na kwamba wao ni waongo katika madai haya.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuthibitisha njia ya mwenye kujihalalishia mali za watu, anaeleza kuwa mwenye kutekeleza ahadi na akaogopa yaliyoharamishwa, basi yeye ni mwenye kupendeza mbele ya Mwenyezi Mungu. Imepokewa Hadith, Mtume amesema:"Hakuna kitu kilichokuwa wakati wa ujahiliya isipokuwa kiko chini ya wayo wangu, isipokuwa amana; kwani hiyo inatekelezewa mwema na muovu". Imam Zainul-abidin(a.s) anasema:"Lau aliyemuua baba yangu Hussein ataniwekea amana upanga aliomuulia baba yangu, basi nitamtekelezea amana yake." Imam Jaffer Assadiq(a.s) anasema:"Mambo matatu hayana udhuru kwa yeyote: Kutekeleza amana kwa mwema au muovu, kuwatendea wema wazazi wawili wema au waovu na kutekeleza ahadi na mwema au muovu." Kwa sababu hiyo ndipo mafakihi wa Shia Imamia wakaafikiana kuwa Kafiri akitangaza vita na waislam, ni halali damu yake lakini haijuzu kumfanyia hiyana. Kwa mfano lau alikuwa ametoa mali yake kwa mwislam, ni lazima arudishe amana pamoja na kujua kuwa inajuzu kumuua na kuchukua mali yake, lakini sio ile aliyoiweka amana.

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّـهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَا يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾

77.Hakika wale wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao kwa thamani ndogo. Hao hawatakuwa na sehemu yoyote akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao watapata adhabu iumizayo.

ASIYE NA AHADI HANA DINI

Aya 77

MAANA

Arrazi anasema katika kufasiri Aya hii: "Yanaingia katika Aya hii yote aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu, yale aliyoyatolea hoja, yaliyochukuliwa kutoka upande wa Mtume na Tafsir Al-Kashif: Juzuu ya Tatu 2. Sura Al-Imran yanaingia yale yanayomlazimu mtu mwenyewe. Kwa sababu yote hayo ni katika ahadi ya Mwenyezi Mungu ambayo ni lazima kuitekeleza." Katika Hadith imeelezwa kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) hakuhutubia hotuba yoyote isipokuwa alisema: "Asiye kuwa na uaminifu hana imani na asiyekuwa na ahadi hana dini." Aya hii na Hadith hii na nyinginezo zinatufahamishia kuwa Uislam unafungamana na tabia na maadili; ndipo ukawajibisha kutekeleza mambo yote ya lazima ya kuamiliana na wengine; na ukakuzingatia kuwa ni kuamiliana na Mwenyezi Mungu, hata kama ni kuamiliana na mlahidi kwa sharti ya kuwa muamala wenyewe usipingane na misingi ya kimaadili; vinginevyo kutakuwa ni batili hakufai.

Vilevile kwa upande wa hukumu, ambapo uislam umemwajibishia kadhi kusikiliza sauti ya dhamiri na hoja ya kitabia kabla ya kusikiliza kauli ya wanaogombana. Nadharia ya tabia; ndio mkazo wa kwanza wa sharia za kiislamu kwa kawaida zake zote na hukmu zake. Kwa ajili hii Mwenyezi Mungu amewatishia wale wanaovunja ahadi na wasiokuwa na uaminifu kwa kitisho ambacho hakumtisha yeyote katika wafanyao madhambi makubwa; pale aliposema:

Hao hawatakuwa na sehemu yoyote akhera, wala Mwenyezi Mungu hatasema nao wala hatawatazama siku ya kiyama wala hatawatakasa, nao watapata adhabu iumizayo.

Ama siri ya kuhimiza huku na kutoa tisho kwa wasiotekeleza ahadi ni kuchunga maslahi ya watu, kuweko kutegemeana kati ya watu na kuchunga haki, mambo ambayo ndio msingi wa amani na nidhamu.

﴿وَإِنَّ مِنْهُمْ لَفَرِيقًا يَلْوُونَ أَلْسِنَتَهُم بِالْكِتَابِ لِتَحْسَبُوهُ مِنَ الْكِتَابِ وَمَا هُوَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَقُولُونَ هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَمَا هُوَ مِنْ عِندِ اللَّـهِ وَيَقُولُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴾

78.Na hakika miongoni mwao kuna kundi linalopinda ndimi zao kwa Kitabu ili mpate kuyadhani hayo kuwa ni ya Kitabu wala si ya Kitabu. Na wanasema: Haya yametoka kwa Mwenyezi Mungu, na hali hayakutoka kwa Mwenyezi Mungu; na wanasema uwongo juu ya Mwenyezi Mungu na hali wanajua

WANAPINDA NDIMI ZAO KWA KITABU

Aya 78

Aya hii ni mwendelezo wa Aya 75. Makusudio ya kupinda ni kugeuza. Kuna Aya nyingi zinazoelezea kugeuza kwao maneno ya Mwenyezi Mungu,

﴿تَجْعَلُونَهُ قَرَاطِيسَ تُبْدُونَهَا وَتُخْفُونَ كَثِيرًا﴾

"Miongoni mwa hizo ni: Mmekifanya kurasa mlizoonyesha baadhi na kuficha nyingi."( 6:91)

﴿وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِن بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴾

"Baadhi yao walikuwa wakisikia maneno kisha wakiyabadili baada ya kuwa wameyafahamu." (2:75)

Mtu atakayeiona Tawrat yao, atakubali kuwa wamezua, ambapo Mwenyezi Mungu amena sibishiwa kula na kupigana hata miereka; kama ambavyo mitume wamenasibishiwa ulevi, na kuzini na mabinti zao.

Kugeuza kunathibiti kwa kuongeza au kupunguza; kama kuzidisha katika maandishi au kupunguza. Vilevile kunathibiti kwa kugeuza irabu, kama kumfanya mtendaji kuwa ndiye mtendwa. Pia kugeuza kunaweza kuthibiti kwa tafsir; kwa kufasiri kiuhakika badala ya kimajazi; mfano mkono wa Mwenyezi Mungu badala ya uwezo wa Mwenyezi Mungu. Wafasiri wametofautiana kuhusu aina ya mageuzi iliyokusudiwa katika Aya hii.Sheikh Muhammad Abduh amesema kuwa makusudio ya kugeuza hapa ni kugeuza tafsir na kulipa tamko maana yasiyokusudiwa; akatoa mfano wa hilo kwa neno liliosemwa na Masih (Baba yetu aliye mbinguni) akiwa na makusudio ya huruma na upole wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake, lakini baadhi ya wakubwa wa kikristo wamefasiri kuwa Mwenyezi Mungu ni baba wa Isa (Yesu) kiuhakika.

Tunavyoona sisi katika tafsir ya Aya hii ni kwamba kikundi hicho cha watu wa kitabu kilikuwa kikipindua tamko lenyewe na kuzusha fikra nyingine na kuwafanya watu wafikirie kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu ili wawe na itikadi ya batili. Kwa hiyo, tamko la kwanza la Kitabu katika Aya ni kinachodaiwa kuwa ni kitabu; na tamko la pili na la tatu ni sifa ambayo. Kukadiri kwake ni wanapinda ndimi zao kwa kinachodaiwa kuwa ni Kitabu ambacho kimegeuzwa, ili nyinyi watu, mkifikirie kuwa kinatokana na Kitabu cha hakika cha asili, na wala sio Kitabu kamwe.

Ama kauli Yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Na wanasema hayo yanatoka kwa Mwenyezi Mungu na wala hayatoki kwa Mwenyezi Mungu , ni kutilia mkazo kauli yake: na wala hayatokani na kitabu. Imesemekana kuwa hayo ni kutilia mkazo upande wa kuunganisha ujumla juu ya umahusus. Kwa sababu kitabu kinahusika na wahyi ulioteremshiwa Mtume. Ama yale yanayotoka kwa Mungu yanakuwa ni Hadith za Mtume na hukumu ya kiakili.

﴿مَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُؤْتِيَهُ اللَّـهُ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ ثُمَّ يَقُولَ لِلنَّاسِ كُونُوا عِبَادًا لِّي مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن كُونُوا رَبَّانِيِّينَ بِمَا كُنتُمْ تُعَلِّمُونَ الْكِتَابَ وَبِمَا كُنتُمْ تَدْرُسُونَ ﴾

79.Haiwezekani kwa mtu aliyepewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hekima na Unabii, kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu. "Kuweni watumishi wa Mwenyeezi Mungu. Kwa kuwa mnafundisha Kitabu na kwa sababu mnakisoma .

﴿وَلَا يَأْمُرَكُمْ أَن تَتَّخِذُوا الْمَلَائِكَةَ وَالنَّبِيِّينَ أَرْبَابًا أَيَأْمُرُكُم بِالْكُفْرِ بَعْدَ إِذْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ﴾

80. Wala hatawaamrisha kuwafanya Malaika na manabii kuwa waungu. Je,atawaamrisha ukafiri baada ya kuwa nyinyi waislamu?

KUWENI WATUMISHI WA MUNGU

Aya 79 - 80

MAANA

Haiwezekani kwa mtu aliyepewa na Mwenyezi Mungu Kitabu na hekima na Unabii kisha awaambie watu: Kuweni wa kuniabudu mimi badala ya Mwenyezi Mungu.

Hapana mwenye shaka kwamba haiwezekani kwa mtu kupewa kitabu, hukumu na utume kuwaambia watu wamwabudu, kwa sababu hiyo ni kufuru na Mwenyezi Mungu hawachagui makafiri. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

"Na hakika tumewachagua kwa ujuzi juu ya walimwengu wote" (44:32) Aya hii Tukufu ni jibu la wale wanaowawekea mitume na mawali baadhi ya sifa za Mungu. Vilevile ni ushahidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwatakasa Mitume. Kwamba Mtume ana yakini kuwa yeye ni mja miongoni mwa waja wa Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye kuabudiwa. Sasa itawezekanaje yeye awatake waja wamwabudu yeye au waaabudu Malaika. Yeye anawaamrisha wawe waalimu na watumishi wa Mwenyezi Mungu kwa vitendo.

Imeelezwa katika Hadith kwamba mtu mmoja alimwambia Mtume: "Tukusujudie?" Mtume akajibu: "La, haitakikani kusujudiwa yeyote zaidi ya Mwenyezi Mungu." Mwengine naye alisema: "Je unataka tukuabudu na tukufanye Mungu." Akasema Mtume: "Mwenyezi Mungu anihifadhi na hilo! Sikuamrishwa hivyo wala sisemi hivyo" Ama kisa cha Imam Ali kuwachoma moto wale waliomnasibisha uungu ni mashuhuri kiasi cha kutohitajiwa kutajwa. Kila mwenye kuwataka watu wamwabudu, basi ni kafiri; na kila mwenye kuwataka wamtukuze kwa makusudio ya kujitukuza na kujiweka juu, basi ni fasiki. Unaweza kuuliza: "Aya imekusanya matamko matatu: Kitabu, hekima na unabii: na kila tamko maana yake yako wazi hayahitaji tafsir kama yakiwa peke yake. Lakini yakiwa pamoja katika jumla moja na yakaunganishwa, basi yanahitaji tafsir. Kwa sababu, maana yake yanaingiliana; hasa kupewa kitab na unabii. Na tunajua kuwa kuungana maneno kunamaanisha tofauti na kubadilika. Sasa kuna njia gani ya kutofautisha matamko hayo matatu?

Jibu : Makusudio ya Kitabu ni Kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu kama Tawrat, Zabur, Injil na Qur'an. Makusudio ya hekima ni elimu na sunna za utume. Mwenyezi Mungu anasema Kuhusu Yahya:

"Na tulimpa hekima akiwa mtoto (19:12)

Ama unabii maana yake ni maarufu; nao ingawaje unalazimisha kujua Kitabu na Sunna, lakini kuyajua hayo mawili hakulazimishi unabii. Kila nabii anajua Kitabu na Sunna, lakini sio kila anayejua Kitabu na Sunna ni nabii. Aya hii iko katika mfano wa Aya isemayo:

"Hao ndio ambao tumewapa Kitabu na hekima na unabii" (6:89)

Lakini kuweni watumishi wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa mnafundisha kitabu na kwa kuwa mnakisoma.

Yaani Mtume anawaambia watu kuweni wajuzi wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu, wenye kukitumia na wenye kuwafundisha wengine, Sheikh Muhammad Abduh anasema: "Aya inafahamisha kuwa mtu atakuwa mtumishi wa Mwenyezi Mungu kwa kukijua Kitabu, kukifundisha kwa watu na kukitangaza. Na ni uthibitisho kuwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu hakuwi kwa elimu pekee, bali ni lazima kuwa pamoja na vitendo"

Wala hatawaamrisha kuwafanya Malaika na manabii kuwa waungu.

Yaani Mtume haamrishi wala hatamwamrisha yeyote kuwafanya wengine kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu.

Je,atawaamrisha ukafiri baada ya kuwa nyinyi Waislamu?

Wao ni Waislamu kwa sababu wao wamemwamini nabii na wakachukua kauli yake. Mwenye kumwamini nabii yeyote wakati wowote yeye ni mwislamu kwa mujibu wa istilahi ya Qur'an. Ufafanuzi wa hilo umetangulia katika kufasiri Aya ya 19 ya Surah hii. Mwenye kufuatilia Aya za Qur'an na Hadith za Mtume wa Mungu, ataona kuwa miongoni mwa mambo ya asili yanayojitokeza zaidi, ambayo uislam unatofautiana na dini nyengine, ni kusisitiza kuwa haifai kwa hali yoyote kuinasibisha sifa ya Mungu kwa kiumbe, awe mtume, mfalme au walii. Siri ya kulitilia mkazo hilo ni kwamba umbile la mtu linapondokea sana kwenye kutopea kama tunavyoshuhudia hilo kwa baadhi ya watu wa dini. Pamoja na sisitizo hilo, lakini utawakuta waislam waliotopea (Ghulat) na kwamba Waislam leo- tukiwa katika karne ya ishirini - wanawanasibishia wafu mambo ambayo hayafai kuyanasibisha isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake, asiyekuwa na mshirika.

﴿وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ النَّبِيِّينَ لَمَا آتَيْتُكُم مِّن كِتَابٍ وَحِكْمَةٍ ثُمَّ جَاءَكُمْ رَسُولٌ مُّصَدِّقٌ لِّمَا مَعَكُمْ لَتُؤْمِنُنَّ بِهِ وَلَتَنصُرُنَّهُ قَالَ أَأَقْرَرْتُمْ وَأَخَذْتُمْ عَلَىٰ ذَٰلِكُمْ إِصْرِي قَالُوا أَقْرَرْنَا قَالَ فَاشْهَدُوا وَأَنَا مَعَكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ﴾

81.Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii. Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia. Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: Tumekubali. Akasema: basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.

﴿فَمَن تَوَلَّىٰ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴾

82.Na atakayegeuka baada ya hayo, basi hao ndio mafasiki.

﴿أَفَغَيْرَ دِينِ اللَّـهِ يَبْغُونَ وَلَهُ أَسْلَمَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَإِلَيْهِ يُرْجَعُونَ ﴾

83.Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu na hali waliomo mbinguni na ardhini wanamtii yeye wapende wasipende, Na kwake yeye watarejeshwa.

MSHIKAMANO WA MITUME

Aya 81 - 83

MTUME NA MREKEBISHAJI

Hakuna tofauti kati ya mtume na mrekebishaji katika ukweli wa nia na ikhlasi katika amali. Lakini wanatofautiana kwa kuwa mtume hakosei. Kwa vile yeye anasema na kutenda kwa wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu. Ama mrekebishaji, hufanya kwa kutegemea mtazamo wake na jitihadi yake. Na mwenye kujitahidi hukosea na kusibu. Kwa hivyo upo uwezekano wa kutofautiana katika jitihadi na mtazamo, Na imesihi kumwondokea jukumu akikosea. Ama kutofautiana mitume kabisa, hilo haliwezekani, Kwa sababu wote wanategemea chimbuko moja - wahyi unaowaelekea wote. Kwa hivyo mitume ni sawa na wafanyikazi wa serikali katika kufikisha amri kwa wananchi.

Haya yanafungamana na kuwa Mwenyezi Mungu anapopeleka manabii wawili kwenye umma mmoja, wakati mmoja, basi watakuwa ni wenye kuafikiana katika kila kitu; kama ilivyotokea kwa Musa na Harun(a.s) . Na kama watakuwa katika nyakati mbalimbali, watakuwa wanaafikiana wote katika fikra na misingi; kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Ikiwa kutakuwa na tofauti, basi ni tofauti katika picha yake na katika hukumu za matendo ambazo zinakwenda na wakati. Hata hiyo nayo wanaikubali Manabii wote kuwa ni ukweli na haki na ni dharura. Kwa hivyo basi hakuna tofauti kabisa kati ya manabii wote na ni kwa ajili hiyo ndipo kila mtume alisadikisha nabii mwenzake aliyemtangulia, Unaweza kuuliza kuwa inawezekana nabii kumsadikisha nabii mwenzake aliyemtangulia. Bali ndivyo ilivyo hasa: sisi tunaamini utume wa Isa na Muhammad; Ibrahim naye akaamini aliyokuja nayo Nuh; Musa akaamini waliyo kuja nayo wote wawili; Isa akaamini waliyokuja nayo wote watatu na Muhammad(s.a.w.w) akaamini waliyokuja nayo wote. Hili linaingilika akilini sana. Lakini litaingilikaje akili kuwa nabii aliyetangulia amwamini atakayekuja baadae,ambaye bado hajapatikana?

Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaampa wahyi Mtume aliyetangulia kwamba Yeye atamtuma Mtume baada yake na kubainisha jina lake na sifa zake. Na ni juu ya yule aliyetangulia kuwatangazia watu wa kizazi alicho yeye katika uma wake ili nao wawatangazie watakaofuatia. Kwa hivyo akija anayefuatia anakuta njia ya kusadikisha imani yake na ujumbe wake imeandaliwa. Tumeyaeleza haya kuwa ni utangulizi na kurahisisha ufahamu Aya hizi zifuatazo.

IRABU

Inawezekana kusoma Lima kwa kuifanya herufi Lam ni ya Jarri. Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu alipochukuwa ahadi kwa manabii kwa kwa ajili kuwapa Kitabu na hikima. Na inawezekana kusoma Lama, kwa fat-ha kuifanya lamu ni ya kuanzia (Mubtada). kwa maana ya, Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii: Nikiwapa Kitabu na hekima.

MAANA

Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa Manabii: Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia.

Kutokana na mfumo wa maneno ulivyo inafahamika kuwa makusudio ya manabii hapa ni manabi na wafuasi wao na wala si manabii peke yao. Na makusudio ya mtume ni mtume Muhammad(s.a.w.w) ; kama ilivyo Aya nyengine isemayo:

﴿وَلَمَّا جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُصَدِّقٌ لِّمَا مَعَهُمْ نَبَذَ فَرِيقٌ مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ كِتَابَ اللَّـهِ وَرَاءَ ظُهُورِهِمْ كَأَنَّهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴾

"Na walipojiwa na mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwenye kusadikisha yale yaliyo pamoja nao kundi moja miongoni mwa wale waliopewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui." (2:101).

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) baada ya kuwabainishia mitume na umma unaowafuata, katika misingi na matawi, alichukua ahadi kwao wote kwamba wamwamini Muhammad(s.a.w.w) na wamsaidie; kama ambavyo naye Muhammad anawasadikisha waliomtangulia na vitabu walivyoviacha, kama vile Tawrat na Injil. Kuchukua ahadi kwake Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa mitume ni kwa njia ya wahyi. Ama kwa wafuasi wa mitume ni kwa kupitia mitume. Yaani kila mtume anachukua ahadi kwa ulama wa umma wake kumwamini Muhammad na kumsaidia. Kwa maelezo ya ndani zaidi ni kwamba kuchukua ahadi kwa anayefuatwa ni lazima kuwe kwa mfuasi. Ikiwa ni wajibu kwa nabii kumwamini Muhammad basi imekuwa wajibu kwa wanaomfuata nabii huyo. Maana ya umma kumwamini Muhammad na kumsaidia, ni kuitakidi kwamba yeye atakuja baada yao na walibashirie hilo. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَإِذْ قَالَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُم مُّصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيَّ مِنَ التَّوْرَاةِ وَمُبَشِّرًا بِرَسُولٍ يَأْتِي مِن بَعْدِي اسْمُهُ أَحْمَدُ﴾

"Na Isa aliposema: "Enyi wana wa Israil mimi ni mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu; nisadikishaye yaliyokuwa kabla yangu katika Tawrat na kutoa bishara ya mtume atakayekuja baada yangu jina lake ni Ahmad (61:6)"

Imam Ali(a.s) anasema:"Mwenyezi Mungu hakupeleka Mtume yeyote ila huchukua ahadi naye kuhusu Muhammad (s.a.w.w) na kumwamrisha kuchukua ahadi na watu kuwa watamwamini na kumsaidia, kama watazikuta zama zake"

Maana ya Umma kumwamini Muhammad(s.a.w.w) na kumsaidia ni kumsadikisha wanavyuoni wao na viongozi wa dini zao na kuwatangazia wale wanaowategemea kwamba Muhammad bin Abdullah ndiye Mtume aliyebashiriwa na mitume, na kwamba jina lake liko katika Vitabu vya dini zao kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu.

﴿الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ﴾

"Ambao humfuata mtume ummi ambaye humkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injil (7:157)

Na wala wasiyapindue maneno ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru na inadi, kama alivyowaelezea Mwenyezi Mungu (s.w.t):

﴿وَقَدْ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْهُمْ يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِن بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ﴾

Hali ya kuwa baadhi yao walikuwa wanasikia maneno ya Mwenyezi Mungu kisha wanayabadili baada ya kuwa wanayafahamu; na hali wanajua. (2:75)

Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: Tumekubali.

Swali hapa ni la kuthibitisha na kutilia mkazo. Maana yake ni Mwenyezi Mungu aliziambia Umma kwa ndimi za mitume yao: Je, mmemkubali Muhammad na mmekubali ahadi? Umma ukasema: Ndio tumekubali wajibu wa kumwamini kumsaidia. Tumelikubali hilo na tumelazimiana nalo. Makusudio ya umma ni viongozi wa dini na wanavyuoni wao wanaojua vitabu vya dini. Akasema: Shuhudieni; yaani akasema Mwenyezi Mungu kwa ndimi za mitume Yake kwa umma shuhudizaneni kwamba mmekubali utume wa Muhammad(s.a.w.w) na wajibu wa kumsaidia.

Mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.

Mwenyezi Mungu na Malaika wake na mitume Yake wanashuhudia kuchukuliwa kwa ahadi ya wanavyuoni wa kidini, na kumkubali kwao Muhammad(s.a.w.w) , lakini pamoja na hayo wanavyuoni wa kiyahudi na wa Kinaswara walikana ahadi hii; wakamkadhibisha Muhammad na kumfanyia vitimbi na kiburi kama zilivyofafanua Aya zilizotangulia,

Na atakayegeuka baada ya hayo.

Yaani atakayegeuza kumwamini Muhammad baada ya kuchukua ahadi ya kumkubali na kumsaidia,

Basi hao ndio mafasiki.

Makusudio ya mafasiki hapa ni makafiri. Kwa sababu kila mwenye kugeuza Aya kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na akakanusha utume miongoni mwa mitume ya Mwenyezi Mungu huku akijua utume wake basi yeye ni kafiri.

Je, wanataka dini isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu na hali waliomo mbinguni na ardhini wanamtii yeye wapende wasipende.

Watu wote wanamwamini Mwenyezi Mungu bila ya kutofautiana mwema na muovu, isipokuwa kwamba mwema humwamini Mwenyezi Mungu kwa hiyari katika maisha haya. Na muovu atamwamini kwa nguvu siku ya kiyama itakapoondoka pazia, na kila mkanushaji ataona adhabu kinaga ubaga. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَلَمَّا رَأَوْا بَأْسَنَا قَالُوا آمَنَّا بِاللَّـهِ وَحْدَهُ وَكَفَرْنَا بِمَا كُنَّا بِهِ مُشْرِكِينَ﴾

"Walipoiona adhabu yetu wakasema: Tunamwamini Mwenyezi Mungu pekee na tunawakataa tuliokuwa tukiwashirikisha naye." (40:84).

Haya ndiyo maana ya 'wapende wasipende' tulivyofasiri ambayo si mazito kufahamiwa na yeyote vyovyote alivyo. Lakini Razi amefasiri kwa tafsiri ya kifalsafa. Aliyoyasema yako karibu, lakini ni kwa watu maalum watakaoelewa sio wote. Na hapa tunayanakili kwa ajili yao sio kwa ajili ya hawa: "Kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kinawezekana kwa dhati yake; na kila chenye kuwezekana kwa dhati yake hakipatikani ila kwa kukipatisha yeye na hakikosekani ila kwa kukikosesha yeye. Kwa hiyo, kila kisichokuwa Mwenyezi Mungu ni chenye kumnyeyekea Mwenyezi Mungu Mtukufu katika njia zote mbili za kupatikana kwake na kukosekana kwake, Na, huo ndio ukomo wa kunyenyekea"

﴿قُلْ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَمَا أُنزِلَ عَلَيْنَا وَمَا أُنزِلَ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَمَا أُوتِيَ مُوسَىٰ وَعِيسَىٰ وَالنَّبِيُّونَ مِن رَّبِّهِمْ لَا نُفَرِّقُ بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ﴾

84.Sema tumemwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa na yale aliyoteremshiwa Ibrahim na Ismail na Is-haq na Yaqub na wajukuu zao na alichopewa Musa na Isa na manabii kutoka kwa Mola wao; hatutofautishi baina yao hata mmoja na sisi ni wenye kusilimu kwake.

﴿وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴾

85.Na mwenye kutaka dini isiyokuwa uislam haitakubaliwa kwake, naye katika akhera ni miongoni mwa wenye kupata hasara.

TUMEAMINI MITUME YOTE

Aya 84 - 85

MAANA

Aya hii ya 85 imekwishapita pamoja na tafsiri yake katika Sura ya Baqara Aya 136. Kwa ufupi ni kwamba mayahudi na manaswara wanaamini baadhi ya manabii na wanawakanusha baadhi yao, Ama waislam, wao wanaamini wote. Kwa sababu, mwito wa manabii ni mmoja na lengo lao pia ni moja. Kwa hiyo, kujaribu kuwatofautisha ni sawa na kusema ndiyo na hapana kwa jambo moja tofuati ya kuamini unabii wao ni sawa na kitu kimoja, kwamba sawa ni hapana kwa pamoja, Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake.

Makusudio ya Aya hii yatajulikana kwa kurudia tafsiri ya Aya ya 19 ya Sura hii. Nimewaona baadhi ya watu wakitoa dalili kuwa hakuna tofauti baina ya mwislam, myahudi na mkristo maadam wote wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, kwa Aya isemayo:

﴿إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَالَّذِينَ هَادُوا وَالنَّصَارَىٰ وَالصَّابِئِينَ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُمْ أَجْرُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ وَلَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾

"Hakika wale ambao wameamini na mayahudi na manaswara na wasabai, yeyote atayemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akatenda mema, basi watapata malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika." (2:62)

Hilo ni kosa kwa njia mbili:

Kwanza : kwamba makusudio ya waliotajwa katika Aya ni kila aliyekufa akiwa na imani na amali njema katika watu wa dini zilizomtangulia Muhammad(s.a.w.w) . Tumeyafafanua hayo wakati wa kufasiri Aya hiyo.

Pili : Hata kama dhahiri ya tamko la Aya inaonyesha kuwa inaenea wakati wote, lakini kauli yake Mwenyezi Mungu: Na mwenye kutaka dini isiyokuwa uislam hatakubaliwa," inaihusisha Aya hiyo na wale waliokuwa kabla ya wakati wa Muhammad tu. Ama mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na asimwamini Muhammad baada ya kupewa kwake utume na ukawa mwito wake umemfikia, basi imani yake si chochote na yeye huko akhera atakuwa katika wenye kupata hasara.

﴿كَيْفَ يَهْدِي اللَّـهُ قَوْمًا كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ وَشَهِدُوا أَنَّ الرَّسُولَ حَقٌّ وَجَاءَهُمُ الْبَيِّنَاتُ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴾

86.Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada kuamini kwao, na wakashuhudia kwamba mtume ni wa haki na zikawafikia hoja zilizo wazi, Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

﴿أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُمْ أَنَّ عَلَيْهِمْ لَعْنَةَ اللَّـهِ وَالْمَلَائِكَةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ﴾

87.Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika, na ya watu wote.

﴿خَالِدِينَ فِيهَا لَا يُخَفَّفُ عَنْهُمُ الْعَذَابُ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ﴾

88.Ni wenye kudumu humo, Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi.

﴿إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾

89.Isipokuwa wale ambao wametubia baada ya hayo, na wakasahihisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe mwenye kurehemu.

ATAWAONGOZAJE MAKAFIRI

Aya 86 - 89

MAANA

Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada ya kuamini kwao, na wakashuhudia kwamba mtume ni wa haki na zikawafikia hoja zilizo wazi wazi.

Makusudio ya Mtume ni Muhammad(s.a.w.w) ; na watu, ni wanavyuoni wa kiyahudi na wa kinaswara kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja kuwa ni watu walioamini na wakashuhudia utume wake, lakini baada ya kuletwa na kuwajia wao ubainifu na dalili wazi juu ya utume wake, walimkanusha na wakakataa kumfuata. Sifa hizi zinalingana kabisa na wanavyuoni wa kiyahudi na wa kinaswara, kwa sababu, wao walikuta jina la Muhammad limeandikwa katika Tawrat na Injil, kwa hivyo wakawa wamemwamini kabla ya kuja kwake isipokuwa tu alipoletwa na kuwajia wao dalili walikufuru kwa chuki na hasadi na wakaifuta kila Aya inayofahamisha kwa uwazi au kwa umbali.

Unaweza kuuliza kuwa dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu; Atawaongozaje Mwenyezi Mungu watu waliokufuru baada ya kuamin kwao, inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu hataki warudie tena kwenye uislamu hata kama watajaribu kutubia; jambo ambalo litawafanya wasistahili adhabu wala kuwa na lawama yoyote. Jibu: Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamsimamishia mja dalili za haki, akiamini, basi atakuwa katika wenye kuongoka; na uongofu wake utatokana na Mwenyezi Mungu, Kwa sababu, Mwenyezi Mungu ndiye aliyemsimamishia dalili za haki. Vile vile uongofu utakuwa umetokana na mja mwenyewe. Kwa sababu yeye ameongoka kwa hiyari yake. Akirtadi baada ya uongofu kwa kiburi na inadi, basi Mwenyezi Mungu atamwachilia mbali katika maisha haya, na wala hatamwekea dalili mpya. Vilevile hawezi kumlazimishia uongofu kwa sababu hakuna taklifu ikiwa kuna kulazimisha.

Hao malipo yao ni kushukiwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika, na ya watu wote.

Yaani wanastahili hilo. Laana ya Mwenyezi Mungu ni kuelezea ghadhabu yake na machukivu yake. Na laana ya watu wote na Malaika ni dua yao ya kumtaka Mwenyezi Mungu awaadhibu na kuwaweka mbali na rehema yake, Katika Nahjul-balagha imeelezwa kwamba Ali(a.s) alikuwa akihutubu katika mimbari Kufa. Ash'ath akamkatiza na kumwambia "Laana ikushukie" Amirul-Muminini akasema: "Wajuaje laana itanipata au la, Mungu akulaani wewe na wakulani wanaolaani." Sheikh Muhammad Abduh katika kulifafanua hilo anasema: "Ash'ath katika masahaba wa Ali alikuwa kama Abdullah bin Ubayy katika masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) wote walikua viongozi wa wanafiki,

Ni wenye kudumu humo, hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa nafasi.

Dhamiri ya humo ni ndani ya Jahannam. Hawatapewa nafasi, yaani hawatapewa muda, bali wataadhibiwa haraka sana.

Isipokuwa wale ambao wametubia baada ya hayo, na wakasahihisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu.

Imekuja Hadith isemayo: "Mwenye kutubia ni kama asiyekuwa na dhambi." Imam Ali anasema: Mungu hamfungulii mja mlango wa toba, akamfungia wa msamaha." Unaweza kuuliza: Mtu akisilimu, kisha akartadi, kisha akarudi kwenye Uislamu lakini akapuuza hukumu sio misingi; kama vile kuacha Swala na Saumu kwa uvivu na kupuuza, Je, toba yake itakubaliwa? Jibu: Ndio, atakubaliwa, Kwa sababu, toba ilikuwa ya kukufuru, sio ya Swala au Saumu. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wakasahihisha, ni kuzitengeneza dhamiri zao na kuthibiti kwenye uislam na kutortadi mara ya pili.

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَّن تُقْبَلَ تَوْبَتُهُمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الضَّالُّونَ ﴾

90.Hakika wale ambao wamekufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, haitatakabliwa toba yao; na hao ndio waliopotea.

﴿إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَمَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يُقْبَلَ مِنْ أَحَدِهِم مِّلْءُ الْأَرْضِ ذَهَبًا وَلَوِ افْتَدَىٰ بِهِ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴾

91.Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri, basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidia ya dhahabu kwa kujaza ardhi yote lau angeliitoa. Hao watapata adhabu iumizayo wala hawatakuwa na msaidizi.

KISHA WAKAZIDI KUKUFURU

Aya 90 – 91

MAANA

Hakika wale ambao wamekufuru baada ya kuamini kwao, kisha wakazidi kukufuru, haitatakabliwa toba yao.

Maana ya kukufuru baada ya kuamini yako wazi. Ama kuzidisha kukufuru, kunakuwa kwa dhambi anazozifanya mwenye dhambi hasa kueneza ukafiri na kuwapiga vita waumini kwa kuwa tu ni waumini. Unaweza kuuliza; Hakika Mwenyezi Mungu amehukumu - katika Aya iliyotangulia - kumtakabalia toba mwenye kukufuru baada ya imani; na katika Aya hii amehukumu kutomtakabalia. Kuna wajihi gani wa kuungana haya? Wafasiri wamejibu kwa majibu mengi. Yenye nguvu zaidi ni kwamba kukufuru baada ya kuamini kuko mafungu matatu.

Kwanza : Kutubia toba ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu ameitaja kwa kusema: Isipokuwa wale waliotubia.

Pili : Toba isiyo ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu ametaja kwa kusema: Haitotakabaliwa toba yao."

Tatu : Ni kufa juu ya ukafiri kulikotajwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri. Jibu tunaloliona sisi, ni kwamba mtu anaweza akahisi usahihi wa jambo au kutokuwa sahihi. Kisha akachangayikiwa na kuwaza kuwa hisia zake zimebadilika na kuwa si sahihi au kuwa ni sahihi baada ya kutokuwa sahihi; ingawaje hisia zake hasa hazijabadilika; ambapo kuitakidi kwake kuwa zimebadilika ni kwa mawazo tu. Vilevile mapenzi na chuki, mfano, mtoto wako anaweza kukufanyia ubaya na ukachukulia kuwa yeye ni mtu anayemchukia zaidi kuliko watu wote, na kwamba unataka aangamie, lakini huruma za ubaba bado ziko kwenye nafsi yako bila ya kutambua, mara ngapi tunashuhudia mtu akifanya jambo au kuliacha kwa kufuata desturi, kuiga au kwa kwa kuhurumia huku mwenyewe kiitakidi kuwa ni kwa njia ya dini.

Pia inaonyesha watubiaji wengi wa dhambi zao kuwa ni wa kweli, lakini kwa ndani bado wamebakia nayo waliyokuwa nayo. Watubiaji hawa ndio walielezwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu: Hawatatakabaliwa toba yao. Ama wale walioelezwa na Aya iliyotangulia (Isipokuwa wale waliotubia), ni wale watubiaji wa kweli na wa haki.

Hakika wale ambao wamekufuru na wakafa hali ya kuwa wao ni makafiri, basi haitakubaliwa kwa yeyote katika wao hata fidiya ya dhahabu kwa kujaza ardhi yote.

Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kuishiliza maisha yake kwa ukafiri atahisabiwa hisabu ya makafiri.

Unaweza kuuliza; kuwa hakuna dhahabu siku ya kiyama wala hakuna njia yoyote ya kuweza kuimiliki wala kuitoa. Sasa kuna faida gani ya kuitaja.

Jibu : Makusudio ni kwamba hakuna njia ya kujikomboa kwa namna yoyote ile. Kimsingi ni kuwa kukadiri muhali si muhali. Katika aliyoyasoma Imam Ali, kuisifu Jahannam ni: "Haondoki mkazi wake wala hakombolewi mateka wake."

MWISHO WA JUZUU YA TATU

10

SHARTI YA KUCHAPA

sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini