TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 15969
Pakua: 2533


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 15969 / Pakua: 2533
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London. Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana. Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah). Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa. Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji. Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

Masahihisho Katika Juzuu ya pili: Uk 23- Aya ya 177 badala ya kusoma Lissaailina soma Walissaailina Uk. 23-25 Aya ya 177 tarjuma ya Kiswahili, mwisho kabisa wa Aya, badala "Hao ndio waliothubutu (katika Imani) soma: "Hao ndio wasemao" Uk. 29- Aya 184, Msitari wa tano- tarjuma ya Kiswahili "Na wale wasioweza, "Soma: "Wanaoweza kwa shida" Uk. 35- Aya ya 192- badala ya kusoma Ghafu soma Ghafuur

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo, Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa. Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswatu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun,(hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki. Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama". Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.' Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: "Hatta idaha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidaha balagha ashuddahu arbai ' na sanah" Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko ya kuufungia macho uzuri wa maana. Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi. Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu" Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyoyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿ لَن تَنَالُوا الْبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُوا مِمَّا تُحِبُّونَ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴾

92.Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda; na chochote mnachokitoa, basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.

MALI NDIO SABABU YA UGOMVI

Aya 92

MAANA

Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda, na chochote mnachokitoa, basi Mwenyezi Mungu anakijua.

Makusudio ya wema hapa, ni utukuzo wa Mwenyezi Mungu na fadhila kwa mja wake, Zimetangulia tafsir za Aya kadha kuhusu kutoa. Lakini Aya hii imetofautiana kabisa na Aya zingine zinazoelezea maudhui haya. Kwa sababu, haitosheki na kuamrisha kutoa tu, kama Aya nyinginezo, bali imeunganisha baina ya kupata mtu daraja ya juu mbele za Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kujitolea anavyovipenda. Kwa hiyo ibada isiyokuwa ya kujitolea, haikurubishi kwa Mwenyezi Mungu - kwa mujibu wa Aya hii- isipokuwa ikiambatana na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Kwa hivyo basi, kauli yake Mwenyezi Mungu; "Hamtaufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda," ni tafsiri na ubainufu wa kila Aya na Riwaya inayohimiza kufanya amali kwa ajili ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na kujikurubisha kwake hali ya kuwa ni ufafanuzi kwamba, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu hakupatikani wala hakutapatikana ila kwa kujitolea mtu nafsi yake na mali yake anayoipenda. Ni kama kwamba Imam Ali(a.s) alichukua kutokana na Aya hii, kauli yake:"Hapana haja ya Mungu kwa ambaye katika nafsi yake na mali yake hakuna fungu la Mungu"

Kutoa ni kugumu na hasa mali ambayo ndiyo mgomvi anayeipambanua imani ya asili. Mali ilikuwa na inaendelea kuwa ni yenye kuabudiwa na mamilioni ya watu. Watu wengi wanawazishwa na shetani kwamba wao wanamwabudu Mwenyezi Mungu (s.w.t), kumbe kwa hakika wanaabudu pesa, lakini wenyewe hawatambui. Kuna kisa kimoja kwamba Iblis, kabla ya kuanzishwa mfumo wa pesa, alikuwa na shughuli kubwa sana ya kuwapoteza watu na kuwaepusha na ibada ya Mwenyezi Mungu wawe waabudu sanamu. Kwa hiyo ikawa hana raha usiku na mchana. Baada ya kupita masiku, ukaja mfumo wa pesa ndipo Ibilisi akapumua, akafurahi sana, akaandaa hafla ya taarabu, akawa anacheza huku ameweka Dirham kwenye jicho moja na Dinar kwenye jicho jengine. Akasema: (kuziambia pesa hizo) mmenipumzisha sasa, sitojali kama watu wanawaabudu nyinyi au wataabudu masanamu. Kisa hiki kiwe ni cha kweli au uongo au hata kama ni katika vigano, lakini ni picha ya kweli. Kwa sababu hakuna tofauti kati ya kuabudu mali na kuabudu masanamu, kila moja inamwepusha mtu na Mungu na haki. Bali kuabudu mali kuna athari mbaya zaidi, na kuna madhara zaidi. Kwa sababu, mara nyingi sana mali ndio kiini cha matamanio na ni chimbuko la ufisadi. Wale waliozihaini nchi zao wamefanya hivyo kwa sababu ya pesa. Na wale waliowapiga vita Mitume na watu wema na kuibadilisha dini na sharia ya Bwana wa Mitume, walifanya hivyo baada ya kupata chochote.

Kadiri nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka kuwa walahidi na waabudu masanamu ambao hawakuzifanyia hiyana nchi zao wala kuwafanyia njama watu wema, kuwa ni bora mara elfu, kuliko mwenye kufunga, kuswali, kuhiji na kutoa zaka lakini anapanga njama pamoja na maadui kuuza nchi na riziki za waja. Kwa hiyo hapana ajabu kwa mtu kupata daraja mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kujitolea kwa mali, ambapo kutokana na kutoa huku kunaonyesha haki kuwa juu ya batili na akhera juu ya ulimwengu,

Unaweza kuuliza kuwa : mbona kauli yake Mwenyezi Mungu"Hamtapata wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda." Kwa dhahiri inafahamisha kuwa pepo haipati ila yule aliye nazo atakayejitolea vizuri katika mali, ambapo watu wengi hawamiliki chochote.

Jibu : Msemo katika Aya tukufu unamhusu mwenye nacho. Ama asiyekuwa nacho, yeye ndio anapasa achukue sio kutoa, bali yeye ni sehemu mojawapo ya kutolea hiyo mali. Zaidi ya hayo ni kwamba, ambao wanapigana jihadi kwa nafsi zao, wana cheo zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wale ambao wanapigana jihadi kwa mali zao. Kwa sababu, kuitoa nafsi ni ukomo wa kutoa. Kama ambavyo Aya imefahamisha, kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu kumedhaminiwa na kutoa na kujitolea. Basi vile vile imefahamisha kwamba, mali ni chimbuko la kheri na ni njia ya kumtii Mwenyezi Mungu; kama ambavyo pia ni kiini cha matamanio na ni ya kumridhisha shetani. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Mwenye kuitafuta dunia kwa ajili ya kujilimbikizia na kujifaharisha atakutana na Mwenyezi Mungu akiwa amekasirika. Na mwenye kuitafuta kwa kujistahi na kuichunga nafsi yake, atakuja siku ya Kiyama uso wake ukiwa kama mbalamwezi." Imam Ali(a.s) anasema:"Hakupewa yeyote kitu katika dunia ila hupungua fungu lake katika akhera" Mmoja wa waliokuwepo akasema: 'Sasa sisi tunaitafuta dunia (Itakuaje?)' Imam akasaili:"Mnaifanyia nini?" Akajibu: 'Kujikimu mimi, wanangu na kutoa sadaka na kuhiji.' Imam akasema: "huku si kutafuta dunia, bali ni kutafuta Akhera"

﴿ كُلُّ الطَّعَامِ كَانَ حِلًّا لِّبَنِي إِسْرَائِيلَ إِلَّا مَا حَرَّمَ إِسْرَائِيلُ عَلَىٰ نَفْسِهِ مِن قَبْلِ أَن تُنَزَّلَ التَّوْرَاةُ قُلْ فَأْتُوا بِالتَّوْرَاةِ فَاتْلُوهَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ﴾

93.Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israil ila alichojiharamishia Israil mwenyewe kabla ya kuteremshwa Tawrat. Sema: Leteni Tawrat muisome mkiwa ni wakweli.

﴿ فَمَنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴾

94.Basi wenye kumzulia uongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo, basi hao ndio madhalimu.

﴿ قُلْ صَدَقَ اللَّـهُ فَاتَّبِعُوا مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ﴾

95.Sema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu. Basi fuateni mila ya Ibrahim aliyeshikamana na haki; wala hakuwa katika washirikina

WANA WA ISRAIL NA CHAKULA

Aya 93 - 95

MAANA

Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israel.

Aya hii kwa ufupi inasimulia kwamba, Aya nyingi zinaonyesha wazi kuwa Muhammad(s.a.w.w) na walio pamoja naye wako kwenye mila ya Ibrahim; wanamwamini Mwenyezi Mungu na aliyoteremshiwa Ibrahim, Ismail, Is-haq,Yakub na kizazi chake. Vile vile Musa, Isa na Mitume wengineo.

Maana yake kwa dhahiri ni kwamba, kila lililokuwa haramu katika dini ya Mitume hiyo basi ni haramu katika dini ya Kiislamu. Mayahudi walikuwa wakiitakidi kuwa nyama ya ngamia na maziwa yake ni haramu katika dini ya Mitume iliyotajwa. Wakamwona Muhammad anaihalalisha na kwamba, uhalalishaji huo unapingana na kauli yake kuwa yeye yuko kwenye mila ya Ibrahim, na kwamba yeye anaamini alichoteremshiwa Ibrahim na Mitume walio baada yake.

Kwa kutegemea madai haya, wakatangaza na kueneza habari kwa makusudio ya kutia ila na kuleta shaka katika Uislamu kwamba Muhammad anajipinga mwenyewe. Anahalalisha chakula kilichokuwa haramu katika mila ya Ibrahim, na wakati huo huo anadai kwamba yuko katika mila ya Ibrahim.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: "Kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israel." Yaani Ibrahim na waliomfuata, hawakuharamisha nyama ya ngamia na maziwa yake, bali kila chakula kilikuwa halali kwao. Na mayahudi ni wakadhibishaji na ni wazushi katika kuwanasibishia Mitume kuwa ndio wenye kuharamisha.

Ila alichojiharamishia Israil mwenyewe.

Israel ni Yakub bin Is-haq bin Ibrahim. Alikuwa hatumii baadhi ya vyakula kwa sababu zake zinazomhusu yeye tu, si kwa sababu ya kuharamishiwa na Mwenyezi Mungu.

Ni kama mtu akiamua kutovuta sigara kwa sababu za kiafya n.k. Lakini alipojizuia ikawa ni desturi ya Wana wa Israil kumfuata baba yao katika yale aliyojizuilia mwenyewe na hilo lilikuwa kabla ya kuteremshwa Tawrat.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja hivyo, kwa sababu aliwaharamishia vitu vingi baada ya Tawrat kutoka na dhambi walizozifanya; kama asemavyo Mwenyezi Mungu:

﴿ فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ لَهُمْ وَبِصَدِّهِمْ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ كَثِيرًا﴾

"Basi kwa dhuluma ya Mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa, na kwa sababu ya kuzuilia kwao njia ya Mwenyezi Mungu kwa wingi" (4:160).

Ama aina ya vitu walivyoharamishiwa baada ya kuteremshwa Tawrat vimetajwa na Aya hii:

﴿وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا كُلَّ ذِي ظُفُرٍ وَمِنَ الْبَقَرِ وَالْغَنَمِ حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ شُحُومَهُمَا إِلَّا مَا حَمَلَتْ ظُهُورُهُمَا أَوِ الْحَوَايَا أَوْ مَا اخْتَلَطَ بِعَظْمٍ ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُم بِبَغْيِهِمْ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ﴾

"Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila(mnyama) mwenye kucha, na katika ng’ombe na kondoo tukawaharamishia mafuta yao isipokuwa yale iliyobeba migongo yao au matumbo au ile iliyogandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa uasi wao, "Na hakika sisi ndio wa kweli." (6:146)

Ufafanuzi zaidi utakuja mahali pake

Kwa ujumla ni kuwa Waislamu wameafikiana kwa kauli moja kwamba asili ya kila kitu ni halali mpaka ithibiti kinyume chake.

Sema: Leteni Tawrat muisome mkiwa ni wenyewe kusema kweli.

Hii ni kujadiliana na mayahudi kwamba walete Tawrat ambayo ndiyo wanayoitegemea waisome kadamnasi, wakiwa wanasema kweli katika madai yao ya uharamu wa ngamia au wengineo. Lakini wao baada ya pambano hili waliingia gizani na hawakuwa na ushujaa wa kuileta Tawrat, kwa sababu wao walikuwa wana yakini kabisa na ukweli wa Mtume(s.a.w.w) na uongo wao.

Mwenye kumzulia uongo Mwenyezi Mungu baada ya hayo

Yaani baada ya kudhihiri hoja na kusimama dalili ya haki.

Basi hao ndio madhalimu

Kwa sababu wamepotea na kuwapoteza wengine kwa kuing'ang'ania na kuipinga haki.

Sema: amesema kweli Mwenyezi Mungu.

Kwamba kila chakula kilikuwa halali kwa wana wa Israil na kwamba Muhammad ni Mtume wa haki.

Basi fuateni mila ya Ibrahim aliyeshikamana na haki.

Hapana budi kuashiria kwamba Muhammad(s.a.w.w) alikuwa katika mila ya Ibrahim na mila ya Mitume yote katika itikadi na misingi. Ama katika sharia alikuwa ni tofauti, ingawaje sharia zote zinasimamia masilahi, lakini masilahi yanatofautiana kulingana na hali ya mazingira na mnasaba.

Kuafikiana sharia katika kuhalalisha chakula, hakuwezi kukulazimisha kuwa sharia moja katika pande zote

Vyovyote iwavyo, ni kwamba makusudio ya Aya tulizozifafanua ni kuwakadhibisha mayahudi yale waliyowasingizia Mitume katika kuharamisha baadhi ya vyakula.

﴿ إِنَّ أَوَّلَ بَيْتٍ وُضِعَ لِلنَّاسِ لَلَّذِي بِبَكَّةَ مُبَارَكًا وَهُدًى لِّلْعَالَمِينَ﴾

96.Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na mwongozo kwa viumbe.

﴿ فِيهِ آيَاتٌ بَيِّنَاتٌ مَّقَامُ إِبْرَاهِيمَ وَمَن دَخَلَهُ كَانَ آمِنًا وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴾

97.Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani; Na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Na atakayekufuru, basi Mwenyezi Mungu si muhitaji wa viumbe.

NYUMBA YA KWANZA

Aya 96 -97

LUGHA

Neno 'Awwal' (Mwanzo) ni jina la kitu ambacho kimepatikana kwanza, ni sawa kipatikane kingine baadaye au la. Husemwa 'Ni mara yangu ya kwanza kuja hapa, na hii ndiyo mali yangu ya kwanza kuipata'.

Neno: Bakka lina maana ya Makka mara nyingi herufi 'Ba, huja mahali pa Miim. Na Maana ya neno Bakka ni msongamano: watu huko Makka hupigana vikumbo kwa sababu ya wingi wao.

Arrazi katika Tafsir yake amenakili Riwaya kwamba Imam Baqir(a.s) alikuwa akiswali Al-Kaaba, Mwanamke mmoja alipita mbele yake, Mtu mmoja akataka kumzuwia, Imam akamwambia: Mwache, hapa Makka panaitwa Bakka (msongamano) kwa sababu watu wanasongamana. Mtu anapita mbele ya mwanamke akiwa anaswali na Mwanamke naye anapita mbele ya mwananamume. Hilo halina ubaya kwa hapa.

MAANA

Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka.

Yameshatangulia maelezo kwa ufafanuzi zaidi - katika kufasiri Aya ya 142 na zinazofuatilia katika Sura ya Pili (Baqara) - kuhusu waliyosema Mayahudi juu ya kugeuza Qibla kutoka Baytul-Muqaddas na kuwa Al-Kaaba.

Aya hii tuliyonayo inafugamana na Aya hizo za Sura ya (Baqara), hasa kauli ya wapumbavu:

"Nini kilichowageuza kutoka Qibla chao walichokuwa wakikielekea?." (2:142)

Kauli yake Mwenyezi Mungu "Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu" haina maana kwamba hiyo ndiyo nyumba ya kwanza duniani, Bali kwa dhahiri ni nyumba ya kwanza ya ibada, Kwa sababu watu wote wanashirikiana ndani yake. Kimsingi ni kwamba watu wote hawashirikiani katika nyumba moja, isipokuwa masuala ya kiujumla; kama vile ibada na twaa.

Baadhi ya wafasiri wamechafua kurasa katika kupekua na kunukuu kauli kuhusu Al-Kaaba, kwamba je, ndiyo nyumba ya kwanza kujengwa duniani au sio. Kwa hakika, hakuna faida yoyote ya utafiti huu, Kwa sababu hayaungani na msingi wa dini au matawi yake, Wala hakutakiwi kuitakidi ndio au hapana.

Yenye kubarikiwa,na mwongozo kwa viumbe.

Makusudio ya baraka hapa ni kuzidishiwa thawabu. Mtume(s.a.w.w) amesema: "Fadhila za Masjidul-haram, juu ya Msikiti wangu ni kama fadhila za msikiti wangu juu ya misikiti mingine." "Swala ya Msikiti wangu huu ni bora kuliko swala elfu za misikiti mwingine." "Mwenye kuhiji na asifanye uchafu au ufasiki, atatakasika kutokana na dhambi zake kama siku aliyozaliwa na mama yake" "Hijja safi haina malipo ila pepo" Na mengineyo mengi.

Ama kwamba ni uongofu kwa viumbe ni kwamba inakumbusha Mwenyezi Mungu na inaleta unyeyekevu.

Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim.

Ni kama vile muulizaji ameuliza ni ipi dalili ya kwamba Al-Kaaba ni ya zamani, na kwamba ndiyo nyumba ya kwanza ya ibada na wala sio Baitul-Muqadas?

Aya hii inafaa kuwa ni jibu la swali hili, kwa sababu Ibrahim ni wa zamani naye ndiye aliyejenga Al-Kaaba. Kwa hiyo itakuwa ndiyo ya kale iliyotangulia kutokana na ukale wa mjenzi wake. Ama Baitul-Muqadas, ilijengwa na Nabii Suleiman nayo inaitwa mahali pa kuabudia pa Suleiman' mpaka sasa. Na kati ya Suleiman na Ibrahim kulipita karne nyingi. Mwenye tafsir Al-Manar amenukuu kutoka vitabu vya Mayahudi kwamba Suleiman alijenga Baitul-Muqadas miaka 1005 B.C. (Kabla ya kuzaliwa Isa)

Dalili ya kwamba Ibrahim ndiye aliyeijenga Al-Kaaba, ni athari za waziwazi zilizoko mpaka sasa; kama vile Maqam Ibrahim (Mahali aliposimama Ibrahim). Waarabu bado wananukuu kwa njia Mutawatir kutoka vizazi na vizazi kwamba sehemu hii maalum ya Msikiti ni sehemu aliyokuwa akisimama Ibrahim kuswali na kufanya ibada.

Kwa hivyo, kama linavyofahamisha jina la Msikiti wa Suleiman kwamba aliyeijenga Baitul Muqadas ni Suleiman, vile vile jina la Maqam Ibrahim, linafahamisha kuwa yeye ndiye aliyeijenga Al-Kaaba; na kwamba hiyo Al-Kaaba ndiyo iliyotangulia, kwa kuwa Ibrahim ametangulia.

Na mwenye kuingia humo huwa katika amani

Imekwishapita tafsir yake katika (2:125) Na hayo ni fadhila ya dua ya Ibrahim.

Na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea.

Uwezo uko namna mbili: Kiakili, ambao ni uwezekano wa kufika Makka, Hilo sio sharti. Na wa Kisheria, ambao ni uwezo wa kiafya, usalama wa nafsi, mali na uwezekano. Hayo yakikamilika, Hijja inakuwa ni lazima, Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqhi.

Na atakayekufuru, basi Mwenyezi Mungu si muhitaji wa viumbe.

Makusudio ya neno 'Kufru' hapa ni kukanusha kama tukilirudisha kwenye Al- Kaaba kwamba ndiyo nyumba ya kwanza ya ibada, au kwenye kutoitakidi wajibu wa Hijja. Na yatakuwa makusudio yake ni ufasiki kama tukilirudisha kwenye kuacha Hijja kwa kupuuza.

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَكْفُرُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا تَعْمَلُونَ﴾

98.Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnazikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na hali Mwenyezi Mungu ni shahidi juu ya muyatendayo!

﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ تَبْغُونَهَا عِوَجًا وَأَنتُمْ شُهَدَاءُ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴾

99.Sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu walioamini ? Mkaitafutia kosa na nyinyi mnashuhudia. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na muyatendayo

KUKANUSHA DALILI NA ISHARA ZA MWENYEZI MUNGU

Aya 98 -99

MAANA

Qur'an imejishughulisha sana na watu wa Kitabu, ikawateremeshia Aya kadha wa kadha zinazowakumbusha Tawrat na Injil na kuwaaibisha, kwa sababu ya kuzigeuza; ikawajadili kwa namna nzuri na kuwaelezea makosa yao mengi na dhambi zao. Miongoni mwa Aya hizo, ni Aya hizi mbili:

Ya kwanza ni : "Sema:Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnazikanusha ishara za Mwenyezi Mungu ambazo zimefahamisha Utume wa Muhammad(s.a.w.w) ; na kwamba Al-Kaaba ndiyo nyumba ya kwanza kuwekewa watu kwa ibada, pamoja na kuwa ishara hizo na hoja hizo ziko wazi kama jua, na hawezi kuzikanusha isipokuwa mwenye kiburi"

Ya pili ni "sema: Enyi watu wa Kitabu! Kwa nini mnawazuilia njia ya Mwenyezi Mungu walioamini Mkaitafutia kosa?." Hawakutosheka na kufanya ufisadi hao wenyewe, mpaka wakajishughulisha kuwaharibu wengine na kuwapoteza. Kwa hiyo wamechanganya upotevu na kupoteza, na ufisadi na kuwafanya wengine wawe wafisadi. Kila mfisadi anatamani na kufanya kadiri ya uwezo wake ili kuwe na mafisadi wengi kwa kutumia misingi ya Iblis aliposema:

﴿قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴾

"Kwa kunihukumu kupotea, basi nitawapambia katika ardhi na nitawapoteza wote" (15:39)

Tusisahau ishara ya aina hii ya upole wa kuwaambia watu wa Kitabu, na kuwakumbusha vizuri kuwa wao ni watu wa dini na Kitabu, ili angalau waweze kusikia mawaidha na kuongoka.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تُطِيعُوا فَرِيقًا مِّنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ يَرُدُّوكُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ كَافِرِينَ﴾

100.Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.

﴿وَكَيْفَ تَكْفُرُونَ وَأَنتُمْ تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ آيَاتُ اللَّـهِ وَفِيكُمْ رَسُولُهُ وَمَن يَعْتَصِم بِاللَّـهِ فَقَدْ هُدِيَ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴾

101.Na vipi mnakufuru na nyinyi mnasomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume wake mnaye? Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴾

102.Enyi mlioamini mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu.

﴿وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّـهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا وَاذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ كُنتُمْ أَعْدَاءً فَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِكُمْ فَأَصْبَحْتُم بِنِعْمَتِهِ إِخْوَانًا وَكُنتُمْ عَلَىٰ شَفَا حُفْرَةٍ مِّنَ النَّارِ فَأَنقَذَكُم مِّنْهَا كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ﴾

103.Na Shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane; na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu; na mlikuwa ukingoni mwa shina la moto naye akawaokoa nalo. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyozibainisha Aya Zake ili mpate kuongoka.

KUWATII MAKAFIRI

Aya 100 - 103

MAANA

Enyi mlioamini! Mtakapotii kikundi katika watu wa Kitabu, watawarudisha kuwa makafiri baada ya kuamini kwenu.

Katika Aya mbili zilizotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahadharisha watu wa Kitabu kuipinga haki pamoja na kuwazuia waumini na njia Yake Mwenyezi Mungu. Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawahadharisha waumini wasiwasikilize makafiri katika watu wa Kitabu wanaojaribu kuwapoteza waumini na kuwafitini na dini yao. Imepokewa Riwaya kwamba, sababu za kushuka Aya hii ni kuwa baadhi ya mayahudi walikusudia kuirudisha tena fitna iliyokuwepo baina ya kabila la Ansar na Khazraj wasiwe na umoja baada ya Mwenyezi Mungu kuwaweka pamoja kwenye Uislamu. Kwa hiyo, makafiri wakawa wanawakumbusha uadui na mapigano waliyokuwa nayo wakati wa ujahiliya. Hasa siku ya vita ya Bughat ambayo Aus na Khazraj waliuana, na ushindi ukawa wa Aus. Mori ukawapanda wakawa karibu wapigane kama si kuwahi Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Aya inafungamana na tukio hili, kama ambavyo inafungamana na jaribio la wahubiri wa Kikristo wakati huu; na majaribio yote ambayo baadhi ya watu wa Kitabu na wengineo katika kutawanya umoja wa waislamu na kuwaepusha na dini yao, uzalendo wao, na uhuru wao na kuwa windo la kila mnyang'anyi.

Haya ndiyo wayafanyao wakoloni wa Kimagharibi kwa waarabu. Na kazi hiyo hawaifanyi peke yao, bali wanashirikiana na vibaraka duni ambao wanawatii na kuwafuata; na waliokufuru dini yao baada ya kuamini na kuiuza nchi yao. Kwa hivyo basi, Aya inafungamana na vibaraka hawa na pia inafungamana na wanaohubiri fitina na ufisadi na wakapendelea ukafiri na upotevu. Ni sawa wawe ni katika watu wa Kitabu au wengineo; wa Mashariki na Magharibi. Vile vile, Aya hii inafungamana na wanawake wetu wanavyoiga wanawake wa kimagharibi katika kujiremba na kujipodoa, na vijana wetu katika kudharau dini na mwendo wa dini. Vile vile desturi zote za madhara na haramu tulizoziiga kutoka kwa wageni. Aya kwa dhahiri inakataza kuwatii makafiri katika kufuru na kurtadi. Lakini, linalosababisha hilo linaenea katika kila uigaji unaomkasirisha Mwenyezi Mungu na Mtume.

Na vipi mnakufuru na nyinyi mnaosomewa Aya za Mwenyezi Mungu na Mtume Wake mnaye?

Yaani, haitakikani kwa Mwislamu kuathirika na kuwa katika upotevu wa wapotezaji, na kuwafuata makafiri katika desturi zao na hulka zao wakati ambapo yeye mwislamu anasoma Qur'an Tukufu na kumsikiliza Mtume Mtukufu, anayembainishia haki na kumuondolea kila shubha. Anasema Nidhamuddin Al-Hasan Muhammad Annaisaburi katika Tafsir, Gharaibul- Qur'an: "Ama Kitabu kitabaki milele. Na Mtume(s.a.w.w) ingawaje amekwenda kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu, lakini nuru yake imebaki, Kwa sababu, kizazi na warithi wake wanakaimu nafasi yake. Kwa sababu hii ndipo Mtume akasema:"Mimi ninawaachia vizito viwili ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu"

Na mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu, basi ameongozwa katika njia iliyonyooka.

Kushikamana na Mwenyezi Mungu ni kushikamana na dini; dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni uislamu, nayo ndiyo hasa njia iliyonyooka. Makusudio ni kuwa mwenye kushikamana na Mwenyezi Mungu kwa haki kabisa, hawezi wala hataweza kuuwacha uislamu kwa namna yoyote ya majaribio na hadaa zitakavyokuwa.

Unaweza kuuliza : Imekuja Aya isemayo:

"Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka" (11:56)

Na wewe unafasiri kuwa njia iliyonyooka ni uislamu, Kwa hiyo itakuwa Mwenyezi Mungu yuko kwenye dini ya kiislamu.

Jibu : Hakika njia iliyoonyooka ikinasibishwa kwa mja, inakusudiwa uislamu. Ama ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu inakusudiwa uadilifu na hekima; yaani yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu anapanga mambo kwa uadilifu na hekima Yake.

Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha; wala msife isipokuwa mmekuwa waislamu

Kila mwenye kufanya ya wajibu na kujiepusha na mambo ya haramu, basi ndio amemcha Mwenyezi Mungu ipasavyo kumcha. Haya ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

"Mcheni Mwenyezi Mungu muwezavyo" (64:16)

Kwa sababu, lisilowezekana halikalifiwi na sharia, Na kila lisilowezekana kukalifiwa, basi liko nje ya kumcha Mwenyezi Mungu. Ama kauli yake Mwenyezi Mungu "Msife isipokuwa mmekuwa waislamu;" ni kukataza kuacha uislamu na kuamrisha kuwa imara nao mpaka siku ya kifo.

Na shikamaneni na kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane.

Kamba ni maarufu; na makusudio yake hapa ni uislamu. Maana ya Aya nzima, ni kuwa maadam waislamu ni wafuasi wa dini moja, Mtume mmoja na Kitabu kimoja, basi ni juu yao wote kuuchunga mfungamano huu wa kidini ambao ndio wenye nguvu zaidi kuliko mfungamano wa nasaba, na kuwa na hima nao; wala wasigawanyike vikundi.

Unaweza kuuliza : Je, mwito huu wa muungano wa kidini si aina ya ubaguzi wa dini?

Jibu : Hapana, mwito huu wa mshikamano wa wafuasi wa dini moja ni sawa na mwito wa mshikamano wa wanachama wa chama kimoja, au wa wafamilia moja, Mshikamano huu haulazimishi kuwabagua wengine. Bali ni kinyume na hivyo katika uislamuu, ambapo unatoa mwito wa kuwapenda na kuwahurumia watu wengine bila ya kuangalia dini zao, fikra zao au kabila zao. Kwa hivyo basi undugu wa Kiislamu ni nguzo ya udugu wa kibinadamu.

Kwa ujumla ni kwamba kundi ambalo ni wajibu kusaidiana nalo, ni lile lililojikusanya na kusaidiana katika jambo lililo na radhi ya Mwenyezi Mungu na masilahi ya watu. Ama kukutana kusikokuwa na faida yoyote ya kuridhisha hakutakikani. Imam Ali(a.s) anasema:"Utengano ni kwa watu wa batili hata wakiwa wengi, Na kuungana ni kwa watu wa haki hata wakiwa wachahe." Na hiyo ndiyo tafsir ya Hadith mashuhuri:"Msaada wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na wengi." Yaani kuwahusu wanaojumuika na kusaidiana kwa jambo la haki. Ama ikiwa ni kwa jambo la batili; basi hawatakuwa na yeyote zaidi ya shetani.

Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; hivyo kwa neema yake mkawa ndugu.

Mwenyezi Mungu anawakumbusha waislamu wa kwanza vile walivyokuwa na misukusuko ya vita, bughudha na vita vya kuendelea, kama vile vita vya Aus na Khazraj vilivyodumu kwa muda wa miaka mia moja na ishirini, kama ilivyoelezwa kwenye Tafsir Tabari. Basi Mwenyezi Mungu akaziunganisha nyoyo zao kwa baraka ya uislamu mpaka wakawa ni ndugu wanaohurumiana na kunasihiana. Jafar bin Abu Talib katika mazungumzo yake na Najjash alimwambia: "Tulikuwa watu wa ujahilia (ujinga) tukiabudu masanamu, tukila mizoga, tukifanya maovu, kuvunja undugu, kumfanyia uovu jirani na mwenye nguvu akimuonea mnyonge. Tulikuwa hivyo mpaka Mwenyezi Mungu akatuletea Mtume atokanaye na sisi; tunayemjua nasaba yake, ukweli wake, uaminifu na usafi wake.

Akatulingania kwa Mwenyezi Mungu ili tumwabudu yeye peke yake na tuachane na kuabudu wasiokuwa Yeye - mawe na masanamu. Akatuamrisha kusema kweli, kutekeleza amana, kuunga undugu, kumfanyia wema jirani na kujizuia na haki za watu na damu (zao). Akatukataza kufanya maovu, kusema uongo, uzushi, kula mali ya yatima na kuwavunjia heshima wanawake wanaojistahi. Akatuamrisha tumwabudu Mwenyezi Mungu na kutomshirikisha na chochote. Pia akatuamrisha kuswali, kutoa Zaka na kufunga"

Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto naye akawaokoa nalo

Yaani mlikuwa karibu na moto wa Jahannam, kwa ukafiri wenu, Mwenyezi Mungu akawaokoa nao kwa baraka ya Muhammad(s.a.w.w) .

﴿وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ﴾

104.Na liwepo miongoni mwenu kundi lenye kulingania kwenye heri, na kuamrisha mema na kukataza maovu. Na hao ndio wenye kufaulu

KUAMRISHA MEMA

Aya 104

Makusuido ya heri hapa ni uislamu, na mema ni kumtii Mwenyezi Mungu, na maovu ni kumwasi. Maana yanayopatikana ni kwamba hapana budi kupatikane kundi la watu litakalowalingania wasiokuwa waislamu kwenye uislamu; kwenye lile linalomridhisha Mwenyezi Mungu, analolilipa thawabu na kuacha lile linalomkasirisha analoliletea adhabu. Tamko kutokana na nyinyi katika Aya hii inafahamisha wajibu wa kuamrisha mema kwa njia ya kutosheana (kifaya). Yaani, wakilisimamia hilo baadhi, utakuwa wajibu umewaondokea wengine, Wala si lazima kuwa mwenye kutekeleza umuhimu huu, awe mwadilifu. Hapana, si hivyo, kwa sababu mbili:

Kwanza : kwamba sharti ya hukumu ni sawa na hukumu yenyewe, haithibiti ila kwa dalili wala hakuna dalili ya sharti ya uadilifu hapa; si kutoka katika Qur'an, Hadith au kutoka katika akili.

Pili : hukumu ya kuamrisha mema haitegemei maasi au utiifu wa mwengine katika hukumu. Mafakihi wengi wameshartisha wajibu wa kuamrisha mema kuwa mwenye kuamrisha awe atakuwa salama, kiasi ambacho hatapata madhara yoyote kwa kuamrisha mema na kukataza maovu. Lakini sharti hili haliingi sehemu zote, kwani, kupigana na anayetupiga kwa ajili ya dini yetu na nchi yetu ni wajibu, ingawaje tunafahamu kwamba, kwa kawaida kupigana huleta madhara.

Inafaa kwa kila mtu kuyatoa mhanga maisha yake, akiwa na yakini kwamba kujitoa mhanga huku kuna maslahi ya umma. Faida ya watu na nchi ni muhimu na adhimu zaidi kuliko maisha yake, bali hilo linashukuriwa mbele ya Mwenyezi Mungu na kwa watu. Kuna Hadith isemayo:"Jihadi bora zaidi ni tamko la haki mbele za Sultan dhalimu."

Kwa ufupi ni wajibu kukinga madhara yakiwa hayatakuwa na faida yoyote. Vyenginevyo, itajuzu kuyavumilia; kama inavyojuzu kwa mtu kukata kiungo kibovu katika viungo vyake kwa kupigania uhai wake na kuhofia kumalizika. Zaidi ya hayo, mifumo inaathari zake, Baadhi ya mifumo inaifukuza haki na kumsababishia mtu matatizo. Na mingine inalazimisha fikra kwa msikilizaji bila ya kujitambua. Mwenye akili na hekima anafanya kulingana na hali ilivyo ya taratibu au ya nguvu.

Firaun alikuwa na ukomo wa Usultani na kupetuka mipaka; Musa na Harun hawakuwa hata na msaidizi, lakini pamoja na hayo waliamrishwa kumlingania kwenye haki. Lakini kwa njia ya upole. Hata Muumba wa ulimwengu, (ambaye limetukuka neno lake) mara nyingine amewaambia waja wake kwa vitisho na kusema:

"Hakika nyinyi hamtanusuriwa nasi" (23:65) Mara nyingine hutumia upole na kusema:

﴿أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾

"Je, hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe Mwenye kurehemu." (24:22)

Kwa ujumla kutangaza mwito wa uislamu kwa watu, na waislamu kuamrishana mema na kukatazana mabaya, ni katika nguzo za uislamu. Kwa hiyo kunawajibisha kuwapo kwa kikundi kitakachosimamia umuhimu huu, sawa na kulazimika kuwapo uongozi utakaosimamia amani na nidhamu, wafanya kazi wa viwandani, wakulima na wengineo ambao wanachangia maisha.

Huu ni msingi wa kila dini, kila dhehebu na kila fikra. Kwa sababu, hiyo ndiyo njia nzuri ya kueneza mwito, kupata ushindi na kuwazuia maadui. Angalia jinsi watu wa siasa na uchumi wanavyotilia umuhimu vyombo vya habari, kuvikuza na kuvitolea mamilioni ya mapesa na kufanya mizinga na habari kuwa bega kwa bega. Hawakufanya hivyo ila ni kwamba wametambua, kutokana na uzowefu wao, kwamba habari ni silaha yenye nguvu kuliko mizinga na mabomu. Mmoja wa wakuu wa mapatano alisema baada ya kufaulu kwao katika vita vya ulimwengu: "Tumeshinda katika vita kwa mabomu ya karatasi." Yaani magazeti.

Unaweza kuuliza : kwamba unawezaje kuziunganisha Aya hizi mbili: "Na wawepo katika nyinyi watu wanaolingania kwenye heri na wanaoamrisha mema na kukataza maovu." Na Aya isemayo:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ﴾

"Enyi mlioamini! Jiangalieni nafsi zenu hatawadhuru aliyepotea ikiwa mmeongoka" (5:105)

Ambapo ya kwanza imefahamisha wajibu wa kuamrisha mema na ya pili imefahamisha kutokuwepo wajibu huo kutokana na neno "Jiangalieni nafsi zenu."

Jibu : Makusudio ya Aya ya pili, ni kwamba mwenye kutekeleza wajibu wa kuamrisha mema na kukataza mabaya, hatadhuriwa na upotevu wa aliyepotea wala upinzani wa mpinzani, maadamu yeye anaetekeleza wajibu wake tu,

"Hakika ni juu yako kufikisha tu, na juu yetu ni kuhisabu" (13:40)

Swali la pili : kuna Hadith mashuhuri ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) isemayo: "Mwenye kuona katika nyinyi uovu, na auondoe kwa mkono wake, akishindwa, basi (auondoa) kwa ulimi wake, akishindwa basi ni kwa moyo wake na hilo ni katika udhaifu zaidi wa imani." Mpangilio huu unapingana na ilivyo desturi ya sharia, kiakili na kimazoweya; kwamba kuondoa uovu kunaanzia kwa ulimi halafu ndio vita. Sasa kuna wajihi gani wa kauli hii ya Mtume?

Jibu : Kuna tofauti kubwa sana baina ya kuondoa uovu na kukataza uovu, kwani kukataza uovu aghlabu ni kabla ya kutokea uovu wenyewe; ni kama vile kukinga, kama kuona kuwa mtu fulani anafikiria kuiba, ukamkataza kufanya wizi huo, Ama kuondoa uovu, kunakuwa baada ya kutokea uovu wenyewe. Kwa mfano umejua kuwa mtu fulani ameiba mfuko wa mtu mwengine, hapo ukiwa unaweza kumnyang'anya na kumrudushia mwenyewe, basi ni wajibu kwako kulifanya hilo wewe mwenyewe, ikiwa kuna uwezekano wa kumyang'anya mwizi; na wewe usiweze kupata madhara. Kama hukuweza ni wajibu kwako kumwamrisha mwizi aurudishe kwa mwenyewe na kumkataza kuuzuwia. Kama utashindwa na vishindo vya mwizi, basi usikiridhie kitendo chake - baina yako na Mola wako. Kwa hivyo maudhui ya Hadith ni kugeuza uovu, si kukataza uovu([1] ) .