TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16196
Pakua: 2697


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16196 / Pakua: 2697
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿تِلْكَ حُدُودُ اللَّـهِ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴾

13.Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, atamtia katika pepo ipitayo mito chini yake ni wenye kudumu humo, na huko ndiko kufuzu kukubwa.

﴿وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَتَعَدَّ حُدُودَهُ يُدْخِلْهُ نَارًا خَالِدًا فِيهَا وَلَهُ عَذَابٌ مُّهِينٌ﴾

14.Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake na akapetuka mipaka yake, atamtia katika moto; ni mwenye kudumu humo, na atapata adhabu idhalilishayo.

MIPAKA YA MWENYEZI MUNGU

Aya 13 - 14

MAANA

Maana yako wazi, kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kubainisha viwango vya urithi kulingana na ujuzi wake na hekima yake, akamwahidi thawabu yule mtiifu na mateso yule mwasi; kwa kuhimiza utiifu na tishio la maasi. Ametumia tamko la wengi (ni wenye kudumu) kwa watu wa peponi kwa vile watu wa peponi watastarehe kwa pamoja. Na kwa watu wa motoni ametumia tamko la mmoja (ni mwenye kudumu) kwa vile kila mmoja atakuwa akiteseka kivyake. Kuna Hadith kadhaa zimepokewa kuhusu ubora wa ilimu ya mirathi (Faraidh), kwa vile inaangalia masilahi ya jamii na kumweka kila mtu na daraja yake kwa marehemu, bila ya kumnyima mwanamke wala mtoto mdogo; inaigawa mirathi yote bila kutoa nafasi ya kuilimbikiza mikononi mwa wachache; kama zilivyo baadhi ya taratibu za Kimagharibi ambazo zinamkusanyia urithi mtoto mkubwa.

Mtume(s.a.w.w) amesema: "Jifundisheni ilimu ya mirathi na wafundisheni wengine, kwani mimi ni mtu nitakayekufa na kwamba ilimu - yaani sharia ya Kiislam - itazuiwa, na idhihiri fitina, mpaka itokee wawili watofautiane katika fungu wasipate atakayewaamua. Jifundisheni mirathi kwani hiyo ni katika dini yenu na kwamba kuijua ni nusu ya ilimu na ndio kitu cha kwanza kitakachowatoka umati wangu." Kauli yake hii Mtume ya mwisho (kitu cha kwanza kitakacho watoka umati wangu), ni ishara ya hizi sheria za kutungwa ambazo zimechukua mahali pa sharia ya Kiislam.

﴿وَاللَّاتِي يَأْتِينَ الْفَاحِشَةَ مِن نِّسَائِكُمْ فَاسْتَشْهِدُوا عَلَيْهِنَّ أَرْبَعَةً مِّنكُمْ فَإِن شَهِدُوا فَأَمْسِكُوهُنَّ فِي الْبُيُوتِ حَتَّىٰ يَتَوَفَّاهُنَّ الْمَوْتُ أَوْ يَجْعَلَ اللَّـهُ لَهُنَّ سَبِيلًا﴾

15.Na ambao hufanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizieni watu wane katika nyinyi. Watakaposhuhudia, basi wazuilieni majumbani mpaka wafikwe na mauti au Mwenyezi Mungu awafanyie njia nyingine.

﴿وَاللَّذَانِ يَأْتِيَانِهَا مِنكُمْ فَآذُوهُمَا فَإِن تَابَا وَأَصْلَحَا فَأَعْرِضُوا عَنْهُمَا إِنَّ اللَّـهَ كَانَ تَوَّابًا رَّحِيمًا﴾

16.Na wawili ambao hufanya uchafu katika nyinyi waudhini. Na wakitubia na wakatengenea, basi waacheni. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kukubali toba mwenye kurehemu.

WAFANYAO UCHAFU

Aya 15 - 16

LUGHA

Neno Fahisha (uchafu) linatumiwa kwa maana ya zina au ulawiti.

MAANA

Na ambao hufanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudizeni watu wane katika nyinyi

Zina haithibiti isipokuwa akiri mwenye kuifanya (mke au mume) mara nne; au kwa kushuhudiwa na watu wane waadilifu walio waislam; kama linavyofahamisha tamko la Aya 'Katika nyinyi.' Hapana budi kila mmoja katika mashahidi wane awe ameshuhudia waziwazi kuingia uume kwenye uke; kama kinavyoingia kijiti kwenye kichupa cha wanja, Kama mashahidi wakipungua au ushahidi wao ukotafautiana basi kila mmoja wao (hao mashahidi) atapigwa viboko themanini. Na atakayemsingizia zinaa mume au mke na asilete mashahidi wane waadilifu basi atapigwa viboko thamanini, kwa hivyo ni bora mtu asitafute aibu za watu, kwani hilo huharibu jamii na kuzisambaratisha familia.

Watakaposhuhudia, basi wazuilieni majumbani mpaka wafikwe na mauti.

Yaani ikithibitika kuwa mwanamke amezini, basi atafungiwa nyumbani kwake mpaka afe, kama adhabu yake,

Au Mwenyezi Mungu awafanyie njia nyengine

Inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakuifanya adhabu hii kuwa ni ya daima, bali aliifanya kwa muda maalum, kisha alete sheria nyengine ya mwisho. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa, ambapo hukumu ya Aya hii iliondolewa na kufanywa adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa, akiwa mzinifu ameoa ua kuolewa; na kupigwa viboko mia akiwa mzinifu ni mseja. Ufafunuzi zaidi utakuja katka Sura ya Nur, Inshallah,

Na wawili ambao hufanya uchafu katika nyinyi waudhini

Wametofautiana wafasiri katika neno Alladhani (wawili ambao), Wengi wamesema ni wazinifu mke na mume. Lakini ilivyo ni kwamba kauli hiyo iko kinyume na dhahiri. Kwa sababu neno Alladhani ni la waume wawili na kwamba hukumu ya mzinifu mwanamke imekwishatangulia wala hakuna wajibu wowote wa kukaririka bila ya kuweko utenganishao. Ilivyo hasa makusudio ni wanaume wawili mfanyaji na mfanywa, Kwa sababu ya dhahiri ya neno Minkum yaani katika nyinyi wanaume.

Adhabu ya kulawiti ni kufanyiwa maudhi; kama vile kutahayariza, lakini adhabu hii iliondolewa - kama ile ya mzinifu wa kike ya kifungo cha maisha - na ikawa adhabu ya waume hao wawili ni kupigwa upanga mpaka kufa au kuchomwa moto, au kutupwa kutoka mlimani baada ya kufungwa mikono na miguu, au kuangushiwa ukuta. Kwa sababu hilo ni kosa baya lenye athari ya uovu ambao unamuondolea mtu ubinadamu wake na hugeuza hakika ya utu kichwa chini miguu juu. Wakale walisema: "Lau simba angeliingiliwa kinyume na maumbile, angelidhalilika."

Na wakitubia na wakatengenea, basi waacheni

Yaani msiache kumuudhi mkosaji huyu kwa kusema tu, nimetubu na Mungu anisamehe, madam haikuthibiti kwake toba ya kweli ya vitendo na kuwa na mwenendo mzuri.

﴿إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴾

17.Hakika toba ikubaliwayo kwa Mwenyezi Mungu ni ya wale tu wafanyao uovu kwa ujinga kisha wakatubia haraka. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu huwatakabalia toba zao na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hekima.

﴿وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا﴾

18.Na si toba ya wale ambao hufanya maovu mpaka mmoja wao akafikiwa na mauti akasema: Sasa mimi nimetubia, wala ambao hufa wakiwa Makafiri, Hao tumewaandalia adhabu iumizayo.

WAFANYAO UOVU KWA UJINGA

Aya 17 - 18

MAANA

Hakika toba ikubaliwayo kwa Mwenyezi Mungu ni ya wale tu wafanyao uovu kwa ujinga kisha wakatubia haraka.

Ujinga hapa ni kwa maana ya upumbavu wa kuacha uongofu na kufuata upotevu. Makusudio ya kutubia haraka ni kutubia mkosaji kabla ya kukaribiwa na mauti, kwani mauti yatakuja tu bila ya shaka yoyote, na kila kijacho ki karibu. Maana kwa ujumla ni kuwa mwenye kufanya uovu, kisha akajuta na kutubia, basi Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake na kumsamehe akawa kama hakufanya dhambi yoyote, Bali Mwenyezi Mungu atampa thawabu.

Unaweza kuuliza : Mbona dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa ni wajibu kwa Mwenyezi Mungu kukubali toba ya wanaojuta na hali twajua kuwa Mwenyezi Mungu ndiye awajibishaye kwa mwengine lile alitakalo, lakini hakuna anayeweza kumwajibishia yeye kitu chochote. Kwa sababu hana wa kufanana naye?

Jibu : Makusudio sio kuwa mwenginewe anamwajibisha Mwenyezi Mungu kukubali toba; isipokuwa makusudio ni kwamba fadhila zake na utukufu wake vinawajibisha kukubali huku; kama vile unavyomwambia mtu mkarimu "Ukarimu wako unakulazimisha kutoa," Mwenyezi Mungu anasema:"Mola wenu amejilazimishia rehema" (6:54)

Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu huwatakabalia toba zao

Maadamu wanataka kweli kurudi kwenye safu za waumini bora,Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa toba ya kweli na ya uongo,mwenye hekima , ya kukubali toba.

Na si toba ya wale ambao hufanya maovu mpaka mmoja wao akafikiwa na mauti akasema sasa mimi nimetubia.

Hakika Mwenyezi Mungu hukubali toba ya anayetubia kwa sharti ya kutubia kabla ya kudhihirikiwa na alama za mauti, Ama mwenye kutubia huku akiwa anachungulia kaburi, basi toba yake haitakubaliwa. Kwa sababu hiyo ni toba ya kuishiwa na kukata tamaa.

Unaweza kuuliza : Utasemaje kuhusu Hadith ya Mtume(s.a.w.w) isemayo: 'Mwenye kutubia saa moja tu, kabla ya mauti yake, basi Mwenyezi Mungu humtakabalia na kwamba hata saa ni nyingi; mwenye kutubia na roho yake imefika hapa - akionyesha koo lake - basi Mwenyezi Mungu humtakabalia toba."

Jibu : Inabidi kuangalia vizuri riwaya hii kwa mambo haya yafuatayo:Kwanza : Hadith hii inakhalifu Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Na imethibiti kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kuwa amesema: "Kumekuwa kwingi kuzuliwa mambo katika uhai wangu na kutazidi baada ya kufa kwangu. Na atakayenizulia, basi na ajichagulie makazi yake motoni. Ikiwajia Hadith kutoka kwangu, basi ilinganisheni na Kitabu cha Mwenyezi Mungu; yanayoafikiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu yachukueni na yanachohalifiana na Kitabu cha Mwenyezi Mungu basi msiyachukue"

Kwa ajili hiyo basi hatuikubali Hadith ya kukubaliwa toba wakati roho ikitolewa, Si ajabu kuwa baadhi ya viongozi wa Kibani Umayya na Bani Abbas waliwaambia wafuasi wao wakuu wawawekee Hadith hii, ili iwe ni hoja kwa wanaotawaliwa kwamba wao wanayo nafasi kwa Mwenyezi Mungu hata wakifanya dhuluma na ufisadi kiasi gani. Wao walikuwa na jopo la mafakihi waovu wa kuboresha vitendo vyao na kuifanya dini kulingana na matakwa ya ushetani.

Pili : Fikra ya kukubaliwa toba wakati wa kufa ni hadaa ya kufanya madhambi na hii ni kazi ya shetani sio ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema. Tatu: Mwenyezi Mungu (s.w.t) anakubali amali ya aliyeifanya kutokana na matakwa yake na uhuru wake kamili tu. Kwa dhahiri ni kwamba mtu anakuwa huru tu, ikiwa atafanya amali akiwa na uwezo wa kufanya na kuacha. Ama ikiwa anaweza kufanya tu, lakini hana uwezo wa kuacha; au anaweza kuacha tu bila ya kuwa na uwezo wa kufanya, basi atakuwa ni mwenye kuendeshwa bila ya hiyari. Hivi ndivyo ilivyo kwa kutubia wakati wa mauti kwani ilivyo ni kwamba mtubiaji katika hali hii ya mauti, huwa hawezi kufanya dhambi na maasi, sawa na atakavyoshindwa kesho yule atakayesema:Mola wetu! Tuondolee adhabu hii hakika sisi ni wenye kuamini" (44:12)

Ikiwa Mwenyezi Mungu atamkubalia toba anayechungulia kaburi,basi itatakikana pia amkubalie anayeadhibiwa motoni.

Kwa hivyo ndipo Mwenyezi Mungu akawafanya sawa na kuwaunganisha pamoja pale aliposema: "Wala wale ambao hufa wakiwa makafiri." Yaani pia Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubali toba ya wale wanaokufa wakiwa makafiri, na wala hawajuti mpaka waone adhabu Siku ya Kiyama, bali pia hawakubaliwi wakiwa njiani kuendea Siku hii ya Kiyama; kama isemavyo Qur'an:

﴿حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾ لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴾

"Hata yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu! Unirudishe ili nifanye mema katika yale niliyoyaacha. Hapana! Hakika hilo ni neno tu analolisema; na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa." (23: 99-100)

Ni kweli kuwa kimtazamo wa kiakili inawezekana kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu awasamehe wenye dhambi hata kama hawakutubia kwa ukarimu wake tu. Lakini hilo ni jambo jengine na kukubaliwa toba wakati wa kufa ni jambo jengine.

TOBA NA MAUMBILE

Toba ni tawi litokanalo na kuwepo dhambi. Kwa sababu ni kutaka kusamehewa hizo dhambi. Na mtu haepukani na dhambi iwe ndogo au kubwa, isipokuwa aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu (Maasum). Imenasibishwa kwa Mtume(s.a.w.w) kauli hii: "Ukighufiri unaghufiri dhambi zote, kwa mja wako mja yeyote." Mwenyezi Mungu amewajibisha toba kwa mwenye dhambi, kama vile alivyowajibisha Saumu na Swala. Miongoni mwa Aya zinazofahamisha wajibu ni Aya hii tunayoifasiri. Na pia Aya hizi zifuatazo: "Enyi mlioamini tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli." (66:8)

"Na kwamba mwombeni msamaha Mola wenu na mtubie kwake" (11:3)"Na wasiotubia, basi hao ndio madhalimu" (49:11) Kwa hakika hasa wajibu wa kutubia hauhitaji dalili; kwa sababu ni katika maswala ambayo yanakuwa na dalili pamoja. Kila mtu kwa maumbile yake anatambua kuwa mkosaji lazima aombe msamaha kwa kosa lake na pia kumtaka msamaha yule aliyemkosea. Na hilo limekuwa ni jambo la kawaida la kimataifa hata kama kitendo kimefanyika kimakosa na bila ya kukusudia. Ndege ikiingia anga ya nchi nyingine au mashua ikiingia bahari ya nchi nyingine bila ya ruhusa, basi ni lazima itangaze kuomba msamaha wake vingenevyo italaumiwa na kanuni.

Kwa hivyo basi, kila Aya au mapokezi yanayofahamisha wajibu wa toba, ni uthibitisho wa hukumu ya kimaumbile na wala sio sharia mpya. Basi mwenye kufanya dhambi na asitubie atakuwa amefanya uovu mara mbili. Kwanza amefanya dhambi, Pili, kuacha kutubia. Hali mbaya zaidi ni kuacha toba na kuiharibu kwa kurudia dhambi baada ya kumwahidi Mwenyezi Mungu kutekeleza twaa na kufuata amri. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿عَفَا اللَّـهُ عَمَّا سَلَفَ وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ ٍ ﴾

"Mwenyezi Mungu amekwishayafuta yaliyopita; lakini atakayefanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu," (5:95)

Hadith inasema:"Mwenye kuendelea na dhambi na huku anataka msamaha basi ni kama mwenye kucheza shere"

﴿اللَّـهُ يَسْتَهْزِئُ بِهِمْ وَيَمُدُّهُمْ فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴾

"Mwenyezi Mungu atawalipa shere zao na kuwaacha katika upotofu wao wakitangatanga ovyo" (2:15)

Dhambi inathibiti kwa kuacha aliyoyaamrisha Mwenyezi Mungu au kutenda aliyoyakataza kwa makusudi na kung'ang'ania.' Kwa dhahiri ni kwamba hukumu za kiakili ndizo hukumu za Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwa sababu anafikisha hukumu zake kwa njia mbili: Akili na kwa ulimi wa Mtume wake. Natija ya mwisho ni kwamba hakuna dhambi wala adhabu bila ya ubainifu kama wasemavyo mafakihi waislamu; au bila ya maandishi kama wasemavyo wanasheria. Kutokana na maelezo hayo yaliyotangulia, inatubainikia kuwa mtu anakuwa ni mwenye dhambi na mwasi ikiwa ameyafanya aliyokatazwa na Mwenyezi Mungu au kuacha aliyoamrishwa na Mwenyezi Mungu kwa makusudi na kujua. Lakini kama atafanya au kuacha kwa kusahau, au kulazimishwa au kwa kutojua kusikokuwa kwa uzembe na kupuuza, basi hatahisabiwa kuwa ni mwenye dhambi; na hakutakuwa na sababu za kuwajibisha toba. Mwenyezi Mungu anasema:"Mwenye kutubia baada ya dhulma yake." (5:39)

Kwa sababu kila mwenye kufanya dhambi basi amejidhulumu mwenyewe kwa kujiingiza kwenye hisabu na adhabu.

Toba ni kujuta mwenye dhambi aliyoyafanya na kutaka msamaha na maghufira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kutorudia dhambi mara ya pili. Akirudia basi toba imebatilika na atahitajia kuweka upya ahadi madhubuti zaidi na moyo mnyenyekevu. Imam Zainul-abiddin(a.s) anasema: "Ikiwa kujuta ni toba basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kutubia. Na ikiwa kuacha kukuasi ni kurejea kwako, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kurejea kwako. Na ikiwa kutaka maghufira ni kuondolewa dhambi, basi mimi ni wa mwanzo wa wenye kutaka maghufira"

Makusudio ya kutaka maghufira ni kufanya kwa vitendo sio kwa maneno, Kabla ya chochote kwanza aanze kurudisha haki za watu alizozidhulumu. Ikiwa amemnyang'anya mtu shilingi basi airudishe; na ikiwa amewambia maneno mabaya au kumfanyia vitendo vibaya, basi amwombe msamaha. Kisha alipe faradhi zilizompita; kama vile Hija, Saumu na Swala. Siku moja Amirul-muminin Ali(a.s) alimsikia mtu mmoja akisema: "Namtaka maghufira Mwenyezi Mungu." Imam Akasema:"Unajua kutaka maghufira? Hiyo ni daraja ya juu, na inakuwa katika maana sita." Basi Imam akayataja ikiwa ni pamoja na kuazimia kutorudia dhambi, kurudisha haki za viumbe na kulipa faradhi nk. Yakitekelezeka hayo kwa anayetubia basi atakuwa miongoni mwa aliowahusu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

﴿وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ﴾

"Na hakika mimi ni mwingi wa kumsamehe anayetubia na akaamini na akatenda mema, tena akaongoka ". (20:82)

Yaani kuendelea na uongofu ambao ni imani na amali njema. Hadith inasema:"Mwenye kutubia ni kama asiyekuwa na dhambi," Bali anakuwa katika watu wema: Mwenyezi Mungu anasema:

"Tubieni kwake atawastarehesha starehe njema" (11:3) Na akasema tena:"Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubia" (2:222)

Mtume(s.a.w.w) amesema: "Mwenye kujiona kuwa ni muovu basi yeye ni mwema." Ama siri ya kuwa mwema mtubiaji na ukubwa wa utukufu wa daraja yake mbele ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kule kujitambua mwenyewe na kuihisabu nafsi yake na kila aibu na upungufu na kuipigania hiyo nafsi jihadi kwa ukamilifu na utiifu. Hii ndiyo jihadi kubwa aliyoieleza Mtume(s.a.w.w), Walikwisha sema Mitume na wenye hekima: "Jitambue," Makusudio yao ni kuwa mtu azitambue aibu zake na ajisafishe.

Pengine mtu anaweza kusema kuwa mtu hupitia mikondo mingi; kama vile wazazi wake, shule, jamii yake mazingira na mengineyo yanayoathiri utu wake bila ya kuweza kuyaepuka. Kwa hiyo basi mtu hawezi kuambiwa kuwa ana dhambi au ni mwovu. Kwa sababu dhambi ni ya jamii na ya mazingira, Ikiwa hakuna dhambi basi maudhui ya kutubia yanafutika kabisa. Jibu: Ni kweli kuwa mazingira ya mtu yanamwathiri, lakini vile vile ni kweli kuwa matakwa ya mtu yanaathiri mazingira. Kwa sababu mtu na mazingira ni uhakika unaonekana, na kila kitu chenye uhakika unaonekana hakina budi kuwa na athari, vyinginevyo kitakuwa si chochote. Kwa hivyo basi mtu anaweza kuyaathiri mazingira yake, bali anaweza kuyageuza akiwa ni jasiri. Mazingira anayoishi binadamu huwa yanamsababishia mtu kupendelea kuona natija yake na matunda yake. Kwa hivyo basi ni juu ya mtu kuangalia na kuyachunguza matunda haya na hayo mapendeleo. Ikiwa yana mwelekeo mzuri, basi apate msukumo, vinginenvyo itambidi aachane nayo, Na hili sio jambo gumu.

Lau binadamu angekuwa hana uwezo wa kuyakabili mazingira, asingeliambiwa kwamba ni mwema au ni mbaya; na pia kusingekuwapo na adhabu au thawabu,. Vile vile kusingekuwako na njia ya kuelezea kuweko dini, hulka njema, sharia au kanuni. Swali la pili: Umesema kwamba toba ni tawi la dhambi, ambapo tunajua kuwa Mitume na Maimam walikuwa wakitubia kwa Mwenyezi Mungu wakati wao wako mbali na dhambi. Jibu: Mitume na Maimam wametwahirishwa na uchafu na maasi, hilo halina shaka. Lakini wao kutokana na walivyomjua Mwenyezi Mungu na kumwogopa sana, walijiona kama wana dhambi, Kwa hivyo walitubia dhambi ya kuwazia tu, wala haiko.

Na hiyo ni athari katika athari za kuhifadhiwa kwao na utukufu wao. Kwa sababu, mtukufu hajioni kuwa ni mtukufu, bali hajioni ni chochote kwa Mwenyezi Mungu, daima anajituhumu kuwa si mkamilifu katika kumtii Mwenyezi Mungu na kumwabudu. Kwa ajili hiyo ndipo humuomba msamaha na kumtaka msaada kwa mwisho mzuri kinyume na

﴿الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا﴾

"Wale ambao bidii yao imepotea bure katika maisha ya dunia na wao wanafikiri kwamba wanafanya vizuri." (18:104)

Bora zaidi ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kipande cha dua ya uokofu (munajat) ya Imam Zainul-abidin(a.s) akiwa anamtaka Mwenyezi Mungu ampelekee mja mwema anayetakabaliwa dua ili mja huyu amwone Imam akiwa na hali mbaya ya kumwogopa Mwenyezi Mungu; aweze kuathirika na kumhurumia Imam amwombee kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu aitakabalie dua ya mja huyu mwema. Hapo Imam aweze kuokoka na hasira ya Mwenyezi Mungu na machukivu yake. Na afuzu kwa kupata radhi Yake na maghufira Yake.

Haya ndiyo aliyoyasema Imam, namnukuu: "Huenda mmoja wao kwa rehema yako akanihurumia kwa msimamo wangu mbaya, akanionea huruma kwa hali yangu mbaya akaniombea dua inayosikilizwa zaidi kwako kuliko dua yangu; au uombezi (shafaa) unaotegemewa zaidi kwako kuliko uombezi wangu ambao utakua ni sababu ya kuokoka kwangu na ghadhabu yako na kufuzu kwangu kwa radhi yako" Imam Zainul-abidin aliyasema haya siku ambayo hakuweko yeyote duniani anayekurubia sifa moja katika sifa zake adhimu, Hapo ndipo inapokuwa siri ya utukufu. Baada ya maelezo yote haya ni kwamba toba ina maelezo mengi ambayo yanaweza kupanuliwa katika kitabu mbali kinachohusu toba tu, Huenda tukayarudia tena katika mahali patakapo nasibu.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَحِلُّ لَكُمْ أَن تَرِثُوا النِّسَاءَ كَرْهًا وَلَا تَعْضُلُوهُنَّ لِتَذْهَبُوا بِبَعْضِ مَا آتَيْتُمُوهُنَّ إِلَّا أَن يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ فَإِن كَرِهْتُمُوهُنَّ فَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَيَجْعَلَ اللَّـهُ فِيهِ خَيْرًا كَثِيرًا﴾

19.Enyi ambao mmeamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu; wala msiwataabishe kwa kutaka kuwanyang'anya baadhi ya mlivyowapa, ila watakapofanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema; na kama mkiwachukia basi huenda mkachukia kitu na Mwenyezi Mungu amejaalia heri nyingi ndani yake

﴿وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا﴾

20.Na mtakapotaka kubadilisha mke mahali pa mke na mkawa mumempa mmoja wao rundo la mali, basi msichukue katika mlichowapa. Je, mnakichukua kwa dhulma na kwa makosa yaliyo wazi?

﴿وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴾

21.Mtachukuaje na hali mmeingiliana na hali wao wamechukua kwenu agano madhubuti?

TANGAMANENI NAO KWA WEMA

Aya 19 - 21

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu.

Dhahiri ya Aya inaonyesha kukataza kuwachukulia wanawake kama wanyama na kuwarithi, kama walivyokuwa wakifanya wakati wa ujahiliya. Walikuwa wakimuhisabu mwanamke kuwa ni katika jumla ya mali ya mirathi aliyoacha marehemu. Mtu akifa msimamzi wa mali zake huja kumtupia nguo mjane, na kumchukua kwa hiyo nguo kama anavyochukua mateka au nyara. Akipenda anamuoa au amwoze mume mwengine na yeye (msimamizi) achukue mahari; kama anayeuza bidhaa na kuchukua pesa. Au akipenda anaweze kumfunga nyumbani mpaka ajikomboe kwa kitu atakacho kikubali.

Imesemekana kuwa makusudio sio kama ilivyo dhahiri ya Aya na kwamba kuna maneno yaliyokadiriwa kuwa ni msirithi mali za wanawake kwa nguvu. Na mfano wa kurithi kwa nguvu ni kuwa mwanamke na msimamizi wake wa karibu kama kaka; mwanamke akawa na mali na kaka yake akamzuwia kuolewa kwa kuwa na tamaa ya kumrithi. Kwa sababu akiolewa atarithiwa na mumewe na wanawe. Ndipo uislam ukaamrisha kumpa mwanamke uhuru wa kuolewa na kukataza kumzuia kwa tamko la kumrithi kwa nguvu. Kwa sababu kurithi ndio makusuido na lengo; na kuzuwia kuolewa ni sababu tu.

Sisi hatuoni tatizo kwa atakayechagua tafisiri ya kwanza au ya pili, au zote pamoja, maadamu uislam unakataza kumchukulia mwanamke kama bidhaa, na unampa uhuru katika kuolewa na kuchagua mume.

Wala msiwataabishe kwa kutaka kuwanyang'anya baadhi ya mlivyowapa.

Kama ambavyo si halali kwa mwanamume kummiliki mwanamke kama mnyama au kumzuilia kuolewa, vile vile si halali kwa mume kumfanyia uovu mkewe kwa kukusudia kuwa atoe mali ili ajikomboe. Ikiwa mke atatoa katika hali hii na mume akachukua mali, basi atakuwa ni mwenye dhambi. Kwa sababu mali ya mtu haiwezi kuwa halali (kwa mwengine) isipokuwa kwa kuridhika mwenyewe. Hata hivyo ikibainika kuwa amefanya zina itajuzu katika hali hii kumpa dhiki mpaka atoe kitakachomridhisha, kutokana na kauli yake:"Ila watakapofanya uchafu ulio wazi." Makusudio ya uchafu hapa ni zina. Kundi dogo la wanavyuoni limesema kuwa uchafu unakusanya pia unashiza([14] ) Mwenye Bahrul-muhita amenakili kutoka kwa Malik kwamba inafaa kwa mume kumdhikisha mkewe aliye nashiza na kumchukulia kila anachomiliki, Sheikh Muhammad Abduh anasema:

Uchafu ni pamoja na zina, unashiza, wizi na mengineyo katika mambo yaliyoharamishwa. Tuonavyo sisi ni kuwa si halali kumdhikisha mke kwa ajili ya mali ila akiwa amezini. Na ni haramu kumfanyia hivyo katika isiyokuwa zina, vyovyote itakavyokuwa dhambi; kwa kuangalia maana ya yakini yaliyokusudiwa na Aya. Zaidi ya hayo kufanyika dhambi hakuhalalishi kula mali za wanayofanya dhambi. Kama si hivyo utaratibu ungeharibika na mambo yangekuwa sambe jambe. Ni nani atakayekuwa na uhalali wa kula mali ya mwenye dhambi? Je, ni mwenye dhambi kama yeye au asiyefanya (mwenye kuhifadhiwa na) dhambi? Ikiwa ni mwenye dhambi kama yeye basi vipi atahalalisha mali ya mwengine; na kama atakayechukua ni maasum basi yuko wapi? Kwa hakika ni kwamba haijuzu kwa Kadhi kuhukumu kufuta mahari ya mke aliyethibitikiwa na zina kwa sababu ruhusa ya kumdhikisha na kuchukua kitu inamuhusu mume tu., ni kati yake yeye na Mola wake. Na kwa ibara ya mafakihi, Inajuzu kuchukua mahari katika mfano wa hali kwa ridhaa hii sio kwa kulipa.

MTAKA YOTE, HUKOSA YOTE

Na kama mkiwachukia, basi huenda mkachukia kitu na Mwenyezi Mungu amejaalia heri nyingi ndani yake.

Huenda mtu akachukia baadhi ya mambo ya mkewe, asivumilie, akamwacha na kuoa mke mwengine. Mara huyu mke mwengine anakuwa mbaya zaidi na mwenye vitendo viovu kuliko yule wa kwanza, Hapo hujuta tena, ambapo hakufai chochote. Kwenye kitabu Aghani anasema: Farazdaq alimwacha Nawal, kisha akaoa mwanamke mwengine aliyeachwa, akajuta. Ikawa anamsikia akipiga kite na kumlilia mumewe wa kwanza. Basi akatunga shairi hili; Mumewe wa kwanza amlilia, nami wangu wa kwanza namlilia. Nimewaona wengi ambao huwa hawana chochote, mtu hamiliki hata chakula chake anaishi kwa kuombaomba tu, Mara anapata kazi inayomsaidia maisha yake na kutekeleza haja zake kiasi cha kutomtegemea mwengine, kisha huikataa kazi hiyo kwa kutaka zaidi. Basi Mwenyezi Mungu humtia adabu kwa kupata hali mbaya zaidi, Hapo hujuta tena ambako hakumfai chochote. Kuna methali maarufu isemayo; 'Mtaka yote hukosa yote'

Vile vile tumeona wengi wenye shahada za juu lakini wakakubali kazi ile wanayopata wakawa makarani tu au chini ya karani; wakangoja fursa wakimtegemea Mwenyezi Mungu (s.w.t) Si baadae sana mara hupanda kidogo kidogo mpaka kufikia cheo cha juu. Kuna Hadith isemayo: 'Kukinai ni miliki isiyotoweka na ni hazina isiyokwisha' Maana yake ni kuwa mwenye kutosheka na apatacho na wala asidharau aliTafsir chonacho au kutaka asicho nacho, basi yeye daima ni sawa na aliyenacho (mwenye hazina isiyoisha daima).

Na mtakapotaka kubadilisha mke mahali pa mke, na mkawa mumempa mmoja wao rundo la mali, basi msichukue katika mlichowapa.

Maana yako wazi na yanafupilizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:"Muwaache muacho mzuri" (33:49)

Kuachana kuzuri ni kutoa talaka pamoja na kutekeleza haki zake zote. Baadhi ya wafasiri wanasema, kuwa wanavyuoni wametofautiana kufikia kauli kumi katika kuweka kiwango maalum cha mrundo wa mali kwa usahihi ni kuwa hilo ni fumbo la wingi. Na kisa cha mwanamke aliyempinga Umar bin Al-khattab - wakati alipotaka kumwekea kiwango cha mahari - kwa Aya hii, ni mashuhuri hakina haja ya kukitaja.

Je, mnakichukua kwa dhulma na kwa makosa yaliyo wazi?

Yaani mnanyang'anya kwa batili na dhuluma.

Unaweza kuuliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu amehusisha kukataza kunyang'anya mali ya mke katika hali ya kutaka kubadilisha ambapo tunajua kuwa kunyang'anya ni haram, ni sawa kuwe ni kwa kutaka kubadilisha au la.

Jibu : Hakuna mwenye shaka kuwa kunyang'anya kokote ni haramu huenda ikawa hekima ya kuhusisha kutaja kubadilisha ni kuwa mume anaweza akadhani kuwa anaruhusiwa kuchukua mahari ya mke ikiwa anataka kubadilisha mke mwengine, kwa vile mke mwengine anachukua nafasi ya yule wa kwanza na kuwa itakuwa uzito kwake kutoa mahari mara mbili,. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaondoa dhana hii, kwa kutaja kutaka kubadilisha.

Mtakichukuaje na hali mmeingiliana.

Baadhi ya wafasiri wamesema makusudio ya kuingiliana hapa ni kujamiiana tu. Wengine wamesema pia na faragha. Kundi jingine la tatu limesema kwa kuyapamba meneno: "Makusudio ya kuingiliana ni mapenzi, hisia, mawazo, siri, huzuni, majibizano, makumbusho na simanzi.." Na sifa nyinginezo zilizopangwa, Mungu awarehemu! Tafsiri nzuri ya maana ya kuingiliana ni ile aliyoisema Sheikh Muhammad Abduh aliposema: "Ni ishara ya kwamba kila mmoja kati ya mume na mke ni sehemu inayotimiza sehemu nyengine; ni kama kwamba ilikuwa sehemu moja imetenganishwa na sehemu nyingine halafu ikaunganishwa kwa mwingiliano huu na kuwa moja"

Lakini ni bora zaidi tufasiri maingiliano kwa maana ya kufanyiana hisani, kwa kufuata kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

"Wala msisahau hisani baina yenu" (2:237)

Yaani hisani ya kila mmoja kwa mwengine, mke na mume. Mwenyezi Mungu anamkubusha mume yale yaliyokuwepo kati yake na mkewe.

NDOA NI KUBADILISHANA ROHO KWA ROHO

Na hali wao wamechukua kwenu agano madhubuti.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekupangia kufunga ndoa kwa matamko aliyoyataja katika kitabu chake kitukufu na kuwajibisha kuyatumia hayo tu; sawa na matamko ya ibada, na akakuongezea huko kufunga ndoa, utukufu ambao hauko katika mapatano mengine; kama vile bei, ajira n.k. Kwa sababu bei ni kubadilishana mali kwa mali. Ama ndoa ni kubadilishana roho kwa roho na akayafanya ni mapatano ya rehema na mapenzi sio mapatano ya kumiliki mwili badala ya mali. Mafakihi wamesema: "Kufunga ndoa ni karibu zaidi na ibada kuliko mapatano mengine; na ni kwa sababu hii, ndipo wakaitegemeza kwenye jina la Mwenyezi Mungu Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kwa sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu"

Sheikh Muhammad Shaltut anasema: "Kama tukijua kuwa neno Mithaq' (agano) limekuja katika Qur'an kwenye ibara za mambo yaliyo baina ya Mwenyezi Mungu na waja wake katika wajibu wa Tawhid, na kulazimiana na hukumu, vile vile katika mambo hatari ya dola moja na nyengine tu, basi hapa tutajua cheo cha kutaja hilo neno katika kufunga ndoa. Vile vile kama tukijua kuwa kulisifu neno Mithaq kwa neno Ghalidh (madhubuti) hakuna katika Qur'an isipokuwa katika maudhui ya ndoa tu, basi utazidi utukufu wa jambo hili ambao umeletwa na Qur'an"

﴿وَلَا تَنكِحُوا مَا نَكَحَ آبَاؤُكُم مِّنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَمَقْتًا وَسَاءَ سَبِيلًا﴾

22.Wala msiwaoe walioolewa na baba zenu, ila waliokwisha pita. Hakika hilo ni ovu na chukizo na njia mbaya.

﴿حُرِّمَتْ عَلَيْكُمْ أُمَّهَاتُكُمْ وَبَنَاتُكُمْ وَأَخَوَاتُكُمْ وَعَمَّاتُكُمْ وَخَالَاتُكُمْ وَبَنَاتُ الْأَخِ وَبَنَاتُ الْأُخْتِ وَأُمَّهَاتُكُمُ اللَّاتِي أَرْضَعْنَكُمْ وَأَخَوَاتُكُم مِّنَ الرَّضَاعَةِ وَأُمَّهَاتُ نِسَائِكُمْ وَرَبَائِبُكُمُ اللَّاتِي فِي حُجُورِكُم مِّن نِّسَائِكُمُ اللَّاتِي دَخَلْتُم بِهِنَّ فَإِن لَّمْ تَكُونُوا دَخَلْتُم بِهِنَّ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ وَحَلَائِلُ أَبْنَائِكُمُ الَّذِينَ مِنْ أَصْلَابِكُمْ وَأَن تَجْمَعُوا بَيْنَ الْأُخْتَيْنِ إِلَّا مَا قَدْ سَلَفَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴾

23.Mmeharamishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu na shangazi zenu na khalat zenu, na binti wa kaka na binti wa dada, na mama zenu waliowanyonyesha na dada zenu wa kunyoyonya, na mama wa wake zenu na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu, waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia-hapana vibaya juu yenu ikiwa hamkuwaingilia-na wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu, na kukusanya kati ya dada wawili, ila waliokwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusameh Mwenye kurehemu.

WALIO HARAMU KUWAOA

Aya 22 - 23

IRABU

Yametangulia maelezo katika kufasiri Aya ya 3 ya sura hii kuwa herufi Ma pia hutumiwa kwa mwenye akili kama katika Aya hii: (Waliowaoa, baba zenu) kama ambavyo pia Man hutumiwa kwa asiyekuwa na akili; kama katika kauli yake Mwenyezi Mungu: Na wengine hutembea kwa matumbo yao (24:45) hapo ametumia neno Man kwa wanaotembea kwa matumbo ambao ni wanyama, hawana akili. Watu wa 'Nahau' ni lazima wafuate Qur'an na wala sio kinyume. Ajabu ni kuwa wafasiri wengi wanafanya taawil katika Qur'an kwa sababu ya kauli ya watu wa Nahau, lakini hawabatilishi kauli ya watu wa Nahau kwa Qur'an.

MAANA

Mwenyezi Mungu(s.w.t) ameharamisha kuoa aina kadhaa za wanawake. Na uharamu wao uko mafungu mawili: Fungu la kwanza ni la uharamu wa milele, kwa maana ya kuwa hakuna mabadiliko; kama vile mtoto, dada, shangazi n.k. Fungu la pili ni lile la uharamu wa muda; kama vile mke wa mtu mwengine au dada wa mke n.k. Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:

1.Wala msiwaoe waliowaoa baba zenu ila waliokwishapita.

Ilikuwa mtu anamuoa mke wa baba yake aliyekufa, ikiwa mke huyo si mama yake. Bali hata Umayya, babu wa Abu Sufiyan alimwacha mkewe, akamwoza mwanawe akiwa hai. Uislam umelikataza hilo kwa kulitilia mkazo na kulizingatia kuwa ni Uovu na chukizo na njia mbaya. Mafakihi na wafasiri wameafikiana kuwa uharamu unaenea kwa wake wa mababu wa upande wa baba au mama; na kwamba uharamu huu unapatikana kwa kufungika ndoa tu, iwe kumepatikana kuingilia au la. Lakini wametofautiana kwa baba aliyezini na mwanamke, je utapatikana uharamu kwa mtoto wake? Shia Imamia, Hanafi na Hambal, wamesema ni haramu. Shafi akasema hakuna uharamu. Na Malik ana riwaya mbili.

2.Mmeharamishiwa mama zenu.

Yaani mumeharamishiwa kuwaoa mama zenu, wakiwemo nyanya zenu wa upande wa baba na mama

3.Na binti zenu.

na kuja chini; wajukuu na vitukuu, vilembwe na vinying'inya na kuendelea

4.Na dada zenu.

Dada na kaka hapa ni ndugu mdogo au mkubwa; ni sawa wawe ni baba mmoja au mama mmoja, atakuwa haramu.

Lakini ni halali kuoa dada wa dada na dada wa kaka, akiwa siye dada. Mfano wa hayo ni kuwa wewe una mtoto aitwaye Rauf, uliyezaa na mke mwingine ukamuoa mwanamke ambaye tayari amezaa na mume mwingine mtoto anayeitwa Hind, na Rauf naye akamuoa Hind. Sasa wewe na mamake Hind mkizaa mtoto atakuwa ni kaka wa sehemu mbili, ni kaka wa Rauf kwa upande wa baba yake na kaka wa Hind kwa upande wa mama yake kwa hiyo Rauf atakaua ameoa dada wa dada yake na Hind ameolewa na kaka wa kaka yake.

5.Na shangazi zenu.

Shangazi ni kila mwanamke ambaye ni dada wa mtu ambaye nasaba yako inarejea kwake moja kwa moja au kupitia ngazi. Kwa hiyo shangazi yako ni dada wa baba yako ambaye amekuzaa wewe moja kwa moja. Shangazi wa baba yako ni dada wa babu yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (baba yako) na shangazi wa babu yako ni dada wa baba wa babu yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi mbili (babu na baba) na kuendelea wote hao ni haramu. Vilevile ni haramu shangazi wa mama yako. Kwa sababu yeye ni dada wa baba wa mama yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (mama) na kuendelea. Ni halali kumuoa binti wa shangazi na wa ammi Kwa sababu yeye siye dada wa aliyekuzaa wewe. Bali ni binti wa kaka yake au dada yake.

6.Na khalati zenu

Yaani dada za mama zenu, Ni kila mwanamke ambaye ni dada wa mtu ambaye nasaba yake inarejea kwako moja kwa moja au kupitia ngazi. Kwa hiyo khalat wako ni dada wa mama yako ambaye amekuzaa wewe moja kwa moja.Vilevile khalat wa mama yako ni dada wa nyanya yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi moja (mama yako) vile vile khalat wa baba yako hakuna tofauti isipokuwa huyu ni dada wa babu na yule ni dada wa nyanya. Pia khalat wa nyanya yako ni dada wa mama wa nyanya yako ambaye amekuzaa wewe kupitia ngazi mbili (mama na nyanya) na kuendelea. Wote hao ni haramu Hata hivyo ni halali binti wa Khalat na wa mjomba, kwa sababu yeye si dada wa aliyekuzaa bali ni binti wa kaka au dada yake.

7.Na binti wa kaka na binti wa dada

Na kuendelea chini

8.Na mama zenu waliowanyonyesha na dada zenu wa kunyonya.

Wameafikiana kwa kauli moja kuitumia Hadith hii: "Ni haramu kwa kunyonyesha yale yaliyo haramu kwa nasaba." Kwa hivyo kila mwanamke aliye haramu kumuoa kwa nasabu atakuwa haramu pia kwa kunyonya, awe ni mama, dada au binti. Vile vile shangazi, khalat, binti wa kaka au binti wa dada, Wametofautiana katika idadi ya kunyonyesha inayowajibisha uharamu. Shia Imamia wamesema ni manyonyesho kumi na tano kamili, ambayo hayakuingiliwa kati na nyonyesho la mwanamke mwengine. Au kunyonya mtoto mchana mmoja na usiku wake kwa sharti ya kuwa lishe yake katika muda huu iwe ni maziwa ya huyo mwanamke tu.

Shafii na Hambal wamesema, hapana, yawe ni manyonyesho matano kwa uchache. Hanafi na Malik wamesema kuwa uharamu unapatikana kwa kunyonyesha tu, kuwe kwingi au kuchache. Kuna masharti mengine ya kunyonyesha tumeyataja kwa ufafanuzi katika kitabu Ahwalush-Shakhsiyya Alal-madhahibil Khamsa.

9.Na mama wa wake zenu.

Wameafikiana kuwa mama wa mke (mama mkwe) na kuendelea juu, ni haram mara tu ukifunga ndoa na binti yake hata kama hukumwingilia. Amekua pekee yule aliyesema kuwa kufunga ndoa tu, hakuharamishi mama mkwe mpaka aingiliwe binti na akatoa dalili kwa Aya hii pale alipolifanya neno ambao mmewaingilia kuwa ni sifa ya mama za wake na wana wa kambo. Lakini mafakihi wamempinga kwa kauli hii kuwa sifa inamrudia aliye karibu zaidi na kwa Hadith sahihi kutoka kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) . Aina zote hizo zilizotajwa ni haramu milele.

10.Na binti zenu wa kambo walio katika ulinzi wenu, waliozaliwa na wake zenu mliowangilia, iwapo hamkuwaingilia hapana vibaya juu yenu.

Wameafikiana kuwa binti wa mke hawi haramu kwa kufunga ndoa tu na mama yake bila ya kumwingilia, Kwa hivyo inajuzu kwake kumtaliki mama kabla ya kumwingilia kisha kumuoa binti yake.

Walio katika ulinzi wenu, haina maana kuwa wasio katika ulinzi wenu ni halali. Kwani binti wa kambo ni haramu tu hata kama hayuko chini ya ulinzi wa baba wa kambo. Imetajwa ulinzi kwa kubainisha kuwa aghlabu inakuwa hivyo. Hanafi na Malik wamesema kugusa na kutazama kwa matamanio kunawajibisha uharamu, sawa na kuingilia. Shia Imamiya, Shafi na Hambal wamesema hakuna uharamu ila kwa kuingilia wala kugusa na kutazama hakuna athari ya kusababisha uharamu hata ikiwa ni pamoja na matamanio. Wameafikiana kuwa hukumu ya kumwingilia mwanamke kwa kutatizika ni kama hukumu ya kuingilia kwa ndoa sahih katika yaliyotajwa. Maana ya kuingilia kwa kutatizika ni kuingiliana mwanamke na mwanamume kwa kufikiria kuwa ni mke na mume washaria, halafu ikabainika kuwa ni watu kando.

11.Na wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu.

Wameafikiana kuwa mke wa mtoto na wa mjukuu, na kuendelea chini, ni haramu kwa baba, babu na kuendelea juu, hata kwa kufunga ndoa tu bila ya kumwingilia. Neno "kutoka katika migongo yenu," ni mtoto wa kumzaa mwenyewe, si mtoto wa kupanga yaani asiwe wa kulea. Ama mtoto wa kunyonya hukumu yake ni kama hukumu ya mtoto wa kumzaa, kutokana na Hadith: Ni haram kwa kunyonya yaliyo haramu kwa nasaba.

12.Na kukusanya kati ya dada wawili isipokuwa wale waliokwishapita.

Wameafikiana katika uharamu wa kukusanya dada wawili. Lakini kama mume akifarikiana na mkewe kwa kifo au talaka, basi inajuzu kumwoa dada yake. Imamia na Shafii wanasema kuwa mtu akimwacha mkewe talaka rejea, basi haijuzu kufunga ndoa na dada yake mpaka eda ishe. Ama ikiwa ni talaka isiyokuwa rejea, basi inajuzu kumwoa dada yake katikati ya eda. Kwa sababu ni talaka isiyo na uwezekano wa kurejeana. Madhehebu mengine yamesema kuwa haijuzu kufunga naye ndoa ila baada ya kwisha eda, bila ya kutofautisha talaka rejea na nyengineyo.

MWIAHO WA JUZUU YA NNE

10

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.