TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16190
Pakua: 2694


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16190 / Pakua: 2694
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA NNE Juzuu 4

Mwandishi:
Swahili

6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA NNE

﴿أَوَلَمَّا أَصَابَتْكُم مُّصِيبَةٌ قَدْ أَصَبْتُم مِّثْلَيْهَا قُلْتُمْ أَنَّىٰ هَـٰذَا قُلْ هُوَ مِنْ عِندِ أَنفُسِكُمْ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

165.Hivi mlipopata msiba - na nyinyi mmekwisha watia mara mbili yake - mnasema: imekuaje? Waambie hayo yanatokana na nyinyi wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

﴿وَمَا أَصَابَكُمْ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ فَبِإِذْنِ اللَّـهِ وَلِيَعْلَمَ الْمُؤْمِنِينَ ﴾

166.Na yaliyowasibu siku ya kukutana makundi mawili ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na ili wajue waumini.

﴿وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ نَافَقُوا وَقِيلَ لَهُمْ تَعَالَوْا قَاتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَوِ ادْفَعُوا قَالُوا لَوْ نَعْلَمُ قِتَالًا لَّاتَّبَعْنَاكُمْ هُمْ لِلْكُفْرِ يَوْمَئِذٍ أَقْرَبُ مِنْهُمْ لِلْإِيمَانِ يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يَكْتُمُونَ﴾

167.Na ili awajue wale ambao walifanya unafiki, na wakaambiwa njooni mpigane katika njia ya Mwenyezi Mungu au mjikinge. Wakasema: Lau tungelijuwa ni vita tungeliwafuata, wao siku ile walikuwa karibu na ukafiri kuliko imani. Wanasema kwa midomo yao yale yasiyokuwa nyoyoni mwao, Na Mwenyezi Mungu anayajua vizuri wanayoyaficha.

﴿الَّذِينَ قَالُوا لِإِخْوَانِهِمْ وَقَعَدُوا لَوْ أَطَاعُونَا مَا قُتِلُوا قُلْ فَادْرَءُوا عَنْ أَنفُسِكُمُ الْمَوْتَ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴾

168.Wale waliosema kuhusu ndugu zao na wao wakiwa wamebaki nyuma: Lau wangelitutii wasingeuawa. Sema jizuilie na mauti (msife) ikiwa mnasema kweli.

ULIPOWAFIKA MSIBA

Aya 165-168

MAANA

Hivi mlipopata msiba - na nyinyi mmekwisha watia mara mbili yake - mnasema: imekuaje?

aani, ulipowapata msiba siku ya vita vya Uhud na nyinyi mlikwisha watia msiba zaidi ya huo siku ya Badr, mnasema imekuaje, na sisi tunapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu? Kwa ufafanuzi zaidi, ni kwamba vita vya Badr vilikuwa mwaka wa tatu. Katika Badr, waislamu walipata ushindi kwa kuwaua washirikina sabini na kuwateka sabini. Vilevile waislamu walipata ushindi katika sehemu ya kwanza ya vita vya Uhud, na wakapata hasara sehemu ya pili, kwa sababu wapiga mishale walikhalifu amri ya Mtume(s.a.w.w) , hapo waislamu sabini wakauawa. Tukilinganisha ushindi wa Waislamu siku ya Badr na ushindi wa washirikina siku ya Uhud, tunapata kuwa Waislamu ni mara mbili zaidi, kwa sababu maiti sabini kwa sabini. Waislamu wanabaki na mateka sabini Sasa kwa nini wanafiki na baadhi ya waislamu washikwe na mshangao kiasi hiki? Tena pamoja na kuuliza wameshindwaje na washirikina, na wao ni maadui wa Mwenyezi Mungu. Kwa nini basi wanafiki wanasahau ushindi wa Badr ambao ulikuwa zaidi?

Waambie: hayo yanatokana na nyinyi wenyewe.

Hili ni jawabu la kauli yao: 'Imekuaje'? maana yake nyinyi ndio sababu ya yaliyowapata, Mtume alionelea kuwa watu wabaki Madina wasitoke, lakini mkakataa. Na mlipotoka, akawalazimisha mbakie sehemu alizowapangia, mkaondoka kwa sababu ya tamaa. Kwa ufupi ni kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hayo yanatokana na nyinyi wenyewe". Ni sawa na kauli yake:

﴿ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ﴾

"Hayo ni kwa sababu ya yaliyotangulizwa na mikono yenu na kwamba Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja." (3:182)

Na yaliyowasibu siku ya kukutana makundi mawili, ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya 'siku' ni 'siku ya Uhud,' 'makundi mawili', ni waislamu na washirikina, na makusudio ya neno 'idhini' ya Mwenyezi Mungu, ni kujua kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama alivyolitumia Mwenyezi Mungu neno hilo kwa maana ya kujua katika (2:179)

wala haijuzu kuwa makusudio ya idhini iwe kuhalalisha kwa sababu Mwenyezi Mungu hawahalalishii makafiri kuwaua waislamu.

Na ili Mwenyezi Mungu awajue waumini na ili awajue wanafiki.

Yaani, masaibu ya Uhud yalikuwa na faida, kama vile kudhihirisha elimu yake Mwenyezi Mungu, kuwa watu watambue imani ya waumini na unafiki wa wanafiki. Wanafiki kabla ya tukio la Uhud hawakuwa wakijulikana wala kutofautiana na waumini. Kwenye tukio hilo walijulikana, kwa hiyo makusudio ya elimu ya Mwenyezi Mungu hapa ni kudhihirisha elimu yake ijulikane kwa wengine, Sio kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu alipata kujua baada ya tukio la Uhud; Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua mambo kabla ya kutukia kwake, Maelezo ya Aya yameshatangulia katika kufasiri Aya ya 141 ya Sura hii.

Wakaambiwa njooni mpigane katika njia ya Mwenyezi Mungu au mjitetee.

Mwenyezi Mungu hubainisha nani aliyeyasema hayo kwa wanafiki. Kwa sababu yeye ameleta kauli kwa tamko la mbali na si kwa majina. Lakini wafasiri wengi wamesema kuwa Abdullah bin Ubayya alitoka pamoja na Mtume(s.a.w.w) siku ya Uhud akiwa na wapiganaji 300. Walipofika katikati ya njia Abdallah alirudi na genge lake akakataa kupigana. Alifanya hivyo kwa ajili ya kuwavunja nguvu wengine wasipigane vita. Abdullah (babake Jabir Ansari) akawauliza: "Kwa nini mnarudi nyuma? Mkiwa na dini basi piganieni dini yenu.

Haya ndiyo maana ya; 'mpigane katika njia ya Mwenyezi Mungu' Na kama hamna dini, basi mzitetee nafsi zenu, watu wenu na mali zenu. Haya ndiyo maana ya 'au mjitee' Watu wa historia pia wametaja kujitoa huku kwa bin Ubayya na watu wake na kauli ya Abdullah. Na tamko la Aya linafungumana na kitendo chao, Lakini haikutaja majina ya waliofanya wala jina la msemaji. Kwa vyovyote itakavyokuwa lakini wanafiki walijibu kauli ya mumini na wakasema:"Lau tungelijua ni vita bila shaka tungeliwafuata" Yaani, kwamba Waislamu na washirikina hawatapigana, lau tungelihakikisha kuwa watapigana, basi tungelipigana pamoja na nyinyi. Wengine wanasema kwamba makusudio ya jibu hilo la wanafiki ni kwamba kukabiliana na washirikina sio kupigana, bali ni kujipeleka machinjioni kwa sababu ya idadi kubwa ya maadui. Tamko la Aya linakubali maana zote mbili, lakini maana ya kwanza iko karibu zaidi na tamko la Aya.

Wao siku ile walikuwa karibu zaidi na kufuru kuliko imani.

Yaani, wanafiki waliposema lau tungelijua ni vita tungeliwafuata, walikusudia kuficha unafiki wao na kujiepusha na tuhuma. Lakini kauli yao ndiyo inayofahamisha zaidi unafiki wao, na ni kauli ya kuwasaidia washirikina; kwa sababu inafuata maslahi yao kutokana na inavyowavunja nguvu waliokuwa pamoja na Mtume(s.a.w.w) .Wanasema kwa midomo yao lau tungelijua ni vita tungeliwafuata yale yasiyokuwa nyoyoni mwao bali ni uongo na unafiki.Na Mwenyezi Mungu anajua vizuri wanayoyaficha ambayo ni kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumkanusha Mtume wake. Imam Ali(a.s) anasema "Ulimi wa Mu'min uko nyuma ya moyo wake na moyo wa mnafiki uko nyuma ya ulimi wake," Yaani, kauli ya Mu'min ni kioo cha yaliyo moyoni mwake, kwa sababu yeye husema kile anachokiamini. Ama mnafiki ulimi wake uko mbali na moyo wake na ulimi wake unafuata maslahi yake tu, na kutengeneza maneno vile yanavyotaka maslahi yake.

Wale waliosema kuhusu ndugu zao na wao wakiwa wamebaki nyuma, "Lau: wangelitutii wasingeuawa."

Yaani, wanafiki walisema lau wale waliouawa siku ya Uhud wangelitufuata sisi wakabaki, asingeliuawa yeyote, kama vile ambavyo sisi tumebaki. Yameshatangulia maelezo yake katika tafsir ya Aya ya 156 ya Sura hii.

Sema: Jizuilieni na mauti (msife) ikiwa mnasema kweli.

Hapana! Hakuna anayeweza kuyakimbia mauti wala hayamwachi yanayemtaka.

Imam Ali(a.s) amesema:"Mauti yanafuata, hayamkosi aliyekaa wala hayamshindi mwenye kuyakimbia, mauti ya utukufu ni kuuliwa, Naapa kwa ambaye nafsi ya mwana wa Abu Talib iko mikononi mwake, mapigo elfu kwangu si chochote kuliko kufa kitandani"

﴿وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ﴾

169.Na usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa wamekufa, bali wako hai mbele ya Mola wao wanaruzukiwa.

﴿فَرِحِينَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَيَسْتَبْشِرُونَ بِالَّذِينَ لَمْ يَلْحَقُوا بِهِم مِّنْ خَلْفِهِمْ أَلَّا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ ﴾

170.Wanafurahia aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake, na wanawashangilia wale ambao hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

﴿يَسْتَبْشِرُونَ بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُؤْمِنِينَ ﴾

171.Wanashangilia neema na fadhila za Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa waumini.

WAKO HAI MBELE YA MOLA WAO WAKIRUZUKIWA

Aya 169-171

MAANA

Na usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Mwenyezi Mungu kuwa wamekufa, bali wako hai mbele ya Mola wao wanaruzukiwa.

Anayeambiwa 'usiwadhanie' ni kila mwenye akili. Makusudio ya waliouwawa wako katika njia ya Mwenyezi Mungu, ni kila aliyeuawa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; ni sawa awe amekuwa shahidi mbele za Mtume, kabla yake, au baada yake. Dhahiri ya Aya ni kwamba mashahidi wako hai hivi sasa, na wala sio kuwa watakuwa hai pamoja na wengine siku ya ufufuo. Na wao wako hai kihakika, sio kimajazi, kama kutajwa vizuri n.k. Hii ndio dhahiri ya Aya, na yapasa kuitegemea, Kwa sababu hakuna la kuwajibisha kutafuta maana nyingine, maadam uhai uko mikononi Mwenyezi Mungu Mtukufu anampa amtakaye wakati wowote autakao. Wala hatujui dini au Umma uliotukuza mashahidi katika njia ya haki na uadilifu kama uislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Kuchwewa na jua na kupambaukiwa ukiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu ni bora kuliko dunia na vilivyo ndani yake." Na akasema:"Pepo iko kwenye ncha za mikuki." Ambayo itamaliza dhulma, shari na batili.

Ama wale wanaokufa shahidi katika njia ya haki, wao na haki ni sawa katika mtazamo wa kiislamu, kwa sababu mwenye kuutoa uhai wake kwa ajili ya haki, utakatifu wake ni utakatifu wa haki yenyewe.

Wanafurahia aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake

Furaha yao ya fadhila hizi iko mara mbili.

Kwanza : Kwa kuwa wao wanastarehe kwa fadhila hiyo.

Pili : Kwamba hili linafahamisha radhi ya Mwenyezi Mungu kwa wale waliojitolea uhai wao kwa ajili yake, sawa na zawadi ya mpenzi inayofahamisha upendo wake.

Na wanawashangilia wale ambao hawajajiunga nao, walio nyuma yao, ya kwamba haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.

Kila Mumin anampendelea ndugu yake katika imani lile analolipendelea nafsi yake, lakini kwa sababu ya matatizo na kwa sababu fulani huenda mtu asifikie makusudio. Lakini wale waliokufa shahid katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanao ndugu katika imani wanaowajua kwa majina wakiwa na iman na ikhlas kama wao, nao wamewaacha bado wako hai. Basi mashahidi watakapoona fadhila za Mwenyezi Mungu kwao, watafurahi na watashangilia kutokana na waliyoyapata, vilevile kwa ajili ndugu zao wanafuata njia yao katika iman, ikhlas na jihadi. Mashahidi Watashangilia kwa sababu, ndugu zao walio hai watapata kama waliyoyapata wao miongoni mwa fadhila na karama. Aya hii ni dalili ya wazi kwamba mashahidi wako hai kabla ya siku ya kiama kwa sababu kushangilia kwao ndugu zao walio hai kumekwishapatikana, na wala sio kuwa kutapatikana kesho.

Wanashangilia fadhila na neema za Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa waumini.

Unaweza kuuliza : kwa nini limerudiwa neno kushangilia na fadhila?

Jibu : Mashahidi wana furaha tatu:

Furaha ya kwanza : ni kwa yale waliyoyapata wao, kulikoelezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. Wanafurahia aliyowapa Mwenyezi Mungu kutokana na fadhila zake. Furaha ya

Furaha ya pili : ni kwa ajili ya ndugu zao wanaowajua ambao watajiunga nao, kama linavyoonyeshwa hilo na kauli yake Mwenyezi Mungu. "Na wanawashangilia wale ambao hawajajiunga nao."

Furaha ya tatu : ni kwa ajili ya kila Mumini wanayemjua na wasiyemjua shahidi na asiye shahidi. Hilo linaelezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: "Wanashangilia neema za fadhila za Mwenyezi Mungu." Linalotilia nguvu kuwa furaha hii ni kwa ajili ya waumini wote, ni kauli yake Mwenyezi Mungu:"Na Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa waumini."

Swali la pili : Mwenyezi Mungu ameunganisha fadhila na neema: na kuunganisha kunamaanisha tofauti. Tunavyoona sisi ni kwamba hakuna tofauti, sasa tofauti ni ipi hiyo?

Razi amejibu kuwa, neema ni thawabu na ujira anaostahiki mtenda amali kuwa ni malipo ya amali yake. Na fadhila ni ziada (Bahashishi) anayoitoa Mwenyezi Mungu kwa ukarimu sio kwa kustahiki. Jibu hili la Razi halifungamani na chochote, isipokuwa kupendelea tu kuwepo tofauti. Tunavyoona sisi ni kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya kusema: "Amenineemesha" na kusema: "Amenifadhili." Ilivyo hasa ni kwamba misamiati inaungana na kutofautiana tamko tu, kunatosha. Kuungana huku kunaitwa 'muungano wa tafsir' (Atfu Tafsir)

﴿الَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ مِن بَعْدِ مَا أَصَابَهُمُ الْقَرْحُ لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا مِنْهُمْ وَاتَّقَوْا أَجْرٌ عَظِيمٌ﴾

172.Wale waliomwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya majeraha yaliyowapata; kwa waliofanya wema na kumcha Mwenyezi Mungu wana ujira mkubwa.

﴿الَّذِينَ قَالَ لَهُمُ النَّاسُ إِنَّ النَّاسَ قَدْ جَمَعُوا لَكُمْ فَاخْشَوْهُمْ فَزَادَهُمْ إِيمَانًا وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ وَنِعْمَ الْوَكِيلُ﴾

173.Wale ambao waliambiwa na watu: Hakika watu wamewakusanyikia kwa hivyo waogopeni. Lakini yakawazidishia imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha na bora ya mwenye kutegemewa ni Yeye.

﴿فَانقَلَبُوا بِنِعْمَةٍ مِّنَ اللَّـهِ وَفَضْلٍ لَّمْ يَمْسَسْهُمْ سُوءٌ وَاتَّبَعُوا رِضْوَانَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ ذُو فَضْلٍ عَظِيمٍ ﴾

174.Basi wakarudi na neema za Mwenyezi Mungu na fadhila haukuwagusa ubaya na wakafuata radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.

﴿إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾

175.Hakika huyo ni shetani, anawatia hofu marafiki zake, basi msiwaogope na niogopeni Mimi, ikiwa nyinyi ni waumini.

WALIOMWITIKIA MWENYEZI MUNGU

Aya 172-175

MAANA

Wale waliomwitikia Mwenyezi Mungu na Mtume baada ya majeraha yaliyowapata, kwa waliofanya wema na kumcha Mwenyezi Mungu wana ujira mkubwa.

Inaelezwa katika vitabu vya Sera na Tafsir kuwa washirikina walipomaliza vita vya Uhud, walipokuwa wakirudi Makka, njiani walirudia kufikiria, wakajuta na kulaumiana. Wakaambiana: "Hatukuwamaliza Waislamu, kwa hiyo wataungana tena na watarudia mara nyingine tena." Hapo wakaazimia kumrudia Muhammad(s.a.w.w) , ili kumpiga vita, Mtume aliposikia hilo, alirudia kuwapanga watu wake haraka. Mpigaji mbiu akanadi, "Asitoke na sisi yeyote isipokuwa yule tuliyokuwa naye jana!" Hapo wakakusanyika waislamu wakiwamo waliojeruhiwa, wakaenda kupiga kambi sehemu ya Hamraul Asad, kiasi cha maili nane kutoka Madina, wakimngoja Abu Sufian na wenzake. Mkusanyiko huo ulifaulu, kwa sababu washirikina walipojua kuwa waislamu wamejikusanya upya, waliogopa na wakarudi Makka haraka sana. waislamu wakarudi Madina wakiwa na nguvu kwa upande fulani.

Wale ambao waliambiwa na watu: Hakika watu wamewakusanyikia, kwa hivyo waogopeni. Lakini yakawazidishia imani, wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosha na bora ya mwenye kutegemewa ni yeye.

Makusudio ya neno 'watu' la kwanza ni wale waliorudi wasiende vitani pamoja na Mtume(s.a.w.w) hao ndio waliowambia waumini waliotakiwa na Mtume(s.a.w.w) kupambana na washirikina kwa mara ya pili "Watu wamekusanyika, kwa hivyo waogopeni." Na makusudio ya neno 'watu' la pili ni washirikina waliojaribu kuwarudia waislamu. Maana ni kuwa waumini pamoja na majeraha yao mabichi, lakini waliitika wito wa Mtume(s.a.w.w) wa kukabiliana na Abu Sufian na jeshi lake bila ya kuwasikiliza wale waliowatia woga, Waliowaambia kuwa msitoke na Muhammad kwa sababu adui ana nguvu zaidi yenu. Badala yake kauli hii iliwazidishia imani kwa Mwenyezi Mungu na kuwa na imani na miadi yake, wakaendelea kumtii Mtume(s.a.w.w) na kutaka kupigana na adui potelea mbali itakavyokuwa, kwa kusema: "Mwenyezi Mungu anatutosha na bora ya mwenye kutegemewa ni yeye." Hivi ndivyo unavyokuwa msimamo na mshikamano wa mumini pamoja na imani yake, Haogopi kifo, kutekwa nyara au kuadhibiwa. Mtu mmoja wa ukoo wa Abdulash- hal anasema: "Mimi na ndugu yangu tulikuwa katika vita vya Uhud na kujeruhiwa. Mwito wa Mtume(s.a.w.w) wa kutoka ulipotolewa, tulitoka pamoja na Mtume. Jeraha langu lilikuwa nafuu kuliko la ndugu yangu kwa hiyo akibaki nyuma nilikuwa nikimbeba"

Basi wakarudi na neema za Mwenyezi Mungu na fadhila, haukuwagusa ubaya na wakafuata radhi ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.

Waumini walitoka pamoja na Mtume hadi Hamral-Asad, kama walivyoamriwa lakini hawakupata lolote kutoka kwa adui. Hiyo ndiyo maana ya kusema: Haukuwagusa na ubaya" Kwa sababu adui alipojua kuwa wamejikusanya tena, aliogopa na kurudi.

Baada ya adui kurudi, Waislamu wakarudi kwao na neema nyingi za Mwenyezi Mungu zikiwa ni salama, twa'a ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kumtisha adui. Kuna neema gani inayolingana na kutukuzwa na Mwenyezi Mungu na kusajiliwa fahari hii katika Lawh Mahfudh na katika Kitabu chake ambacho wanakisoma watu duniani hadi siku ya ufufuo?

Hakika huyo ni shetani anawatia hofu marafiki zake, basi msiwaogope na niogopeni Mimi, ikiwa nyinyi ni waumini.

Kila anayemtii Mwenyezi Mungu, basi ni katika vipenzi vya Mwenyezi Mungu, na kila anayemwitikia shetani, basi ni katika marafiki zake. Mwenyezi Mungu anawaamrisha na anawakataza shari na kuwahadharisha nayo. Ama shetani yeye ni kinyume. Anawaamrisha nayo na anawakataza mema na kuwahofisha nayo, mfasiri Muhammad bin Ahmad Al-Kalabiy anasema katika Tafsir Tashil, makusudio ya shetani hapa ni Abu Sufian au aliyetumwa na Abu Sufian au Iblis. Kauli ya aliyewaambia waumini "Hakika watu wamekusanyikia" Inatokana na mawazo ya shetani na kuhofisha kwake, Hakuna anayemsikiza isipokuwa rafiki zake wanaomtii. Ama wapenzi wa Mwingi wa rehema, kauli hii huwazidishia imani kwa kupigana jihadi na kujitolea mhanga kwa ajili ya uislamu na Mtume wa Uislamu.

Hayo ndiyo maana ya 'shetani anawatia hofu marafiki zake' Ama marafiki wa Mwenyezi Mungu hawamwogopi shetani akiwahofisha. Na maana ya msiwaogope, ni msiwaogope washirikina kwa sababu wao ni marafiki wa shetani wenye kuogopewa kwa kuwapa sifa ya nguvu, ili wapate nafasi ya kueneza ufisadi duniani, Na Mu'min hamuogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu.

SHETANI NI OMBAOMBA NA NI HODARI

Shetani ana majina mengi, kama: mlaaniwa, mwenye kuwekwa mbali na rehma, mpotevu na mpotezaji. Unaweza kumwita ombaomba, kwa sababu yeye husimama kwenye mlango wa moyo kwa kutia huruma na kubisha pole pole akitaka idhini ya kuingia, ukichelewa kumfungulia, hukuomba kwa unyenyekevu na maneno matamu ya kukufanya umfungulie japo kidogo. Ukifanya hivyo tu huingia na kuanza kukutolea hadaa na upotevu kutoka mfukoni mwake. Hapo ataanza kuufinika uhakika na kukubabaisha, na kuupamba uovu na kuufanya uonekane mzuri. Vilevile ataleta sura ya kazi njema kuwa mbaya, kupigania kuondoa batili kuwa kufuru, maovu kuyafanya mema na mema kuyafanya maovu. Pia atamvisha mhaini nguo ya mwema na mwenye ikhlas atamvisha nguo ya mfisadi, na mengineyo yenye hila na upotevu. Njia kubwa anayoitumia kufikia malengo yake ni kutengeneza hofu kwa kuleta nguvu za marafiki zake ambao ndio watekelezaji wa miradi yake. Shetani ni fundi aliye hodari. Ama nguvu zake za utekelezaji ni wafuasi wake ambao wanaeneza ufisadi duniani. Kwa ajili hii anawakuza na kuwatengenezea njia ya utekelezaji na kuwavisha kivazi cha utukufu na cheo, ili wasiwe na sauti au fikra yoyote ya kujitoa, usije ukadhoofika utawala wake na kukatika matarajio yake, shari na ufisadi wake kwa kuondoka athari yao.

Kwa ufupi ni kwamba kila anayewaogopa watu wa ufisadi na wapotevu lakini akapatana na mmoja wao, basi atakuwa amepatana na upotevu wenyewe na atakuwa amesaini mkatataba wa mapenzi na udugu kati yake na shetani. Hiki ni kipimo kisichokosea kabisa katika kumpambanua mwenye kulingania kumwamini Mwenyezi Mungu na kumwogopa Yeye tu, na yule mwenye kumtawalisha shetani na kuathirika na twa'a yake, wala hakuna kitu kinachofahamisha uhakika huu kuliko kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t), 'msiwaogope na niogopeni Mimi,' ikiwa nyinyi ni waumini. Kwani maana yake ni kwamba mwenye kuacha kuwapiga jihadi wafisadi na wapotevu kwa kuwaogopa, basi yeye ni katika marafiki wa shetani na wala hana chochote kwao. Aya hii iko karibu na kauli ya Mtume Mtukufu(s.a.w.w) "Mwenye kuinyamazia haki ni shetani bubu."

﴿وَلَا يَحْزُنكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْكُفْرِ إِنَّهُمْ لَن يَضُرُّوا اللَّـهَ شَيْئًا يُرِيدُ اللَّـهُ أَلَّا يَجْعَلَ لَهُمْ حَظًّا فِي الْآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴾

176.Wala wasikuhuzunishe wale wanaokimbilia ukafiri, Hakika wao hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee fungu lolote huko akhera, Nao wana adhabu kubwa.

﴿إِنَّ الَّذِينَ اشْتَرَوُا الْكُفْرَ بِالْإِيمَانِ لَن يَضُرُّوا اللَّـهَ شَيْئًا وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴾

177.Hakika wale walionunua ukafiri kwa imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu na wana adhabu iumizayo.

﴿وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ خَيْرٌ لِّأَنفُسِهِمْ إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴾

178.Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa ni heri kwa nafsi zao. Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika dhambi na wana adhabu idhalilishayo.

WANAOKIMBILIA UKAFIRI

Aya 176-178

MAANA

Wala wasikuhuzunishe wale wanaokimbilia ukafiri, hakika hao hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu.

Yametangulia maelezo kuwa washirikina walikusanya makundi, wakaandaa jeshi la kumpiga vita Mtume(s.a.w.w) na wanafiki walikuwa wakiwasaidia na wakiwapangia njama waislamu. Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wanafiki na washirikina kuwa ni waasi na wanafanya bidii kuipinga haki na kuipiga vita. Na Mtume(s.aw.w) alikuwa akihuzunika na kuona uchungu kutokana na vitendo vyao hivi. Ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamwambia: Usihuzunike, wao hawatakudhuru na chochote wewe, wala Waislamu na dini ya Mwenyezi Mungu, na kwamba njama zao hizo zitapotea tu. Ama dini itakuwa na utukufu. Na kweli hazikupita siku nyingi Mwenyezi Mungu akaumakinisha uislamu Mashariki na Magharibi kwa watu ambao jana walikuwa wakikimbilia kuupiga vita.

Mwenyezi Mungu anataka asiwawekee fungu lolote huko akhera. Nao wana adhabu kubwa.

Huu ndio ukweli wa kila mwenye kuendelea na upotevu mpaka akafa.Unaweza kuuliza : kuwa dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa shari inatokana na Mwenyezi Mungu, kwa sababu, adhabu ya Jahannam ni shari, na Mwenyezi Mungu amewatakia hiyo adhabu, itakuwaje?

Jibu : ni kweli kuwa Mwenyezi Mungu amewatakia adhabu, lakini ni baada ya kustahili, kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha kuamini na akawakataza kukufuru na akawaachia hiyari. Hivyo wakachagua ukafiri badala ya imani. Maana yake ni kwamba washirikina na wanafiki ndio waliosababisha adhabu. Baada ya wao kusababisha kwa hiyari yao, ndipo Mwenyezi Mungu akawatakia adhabu sawa na hakimu anayemtakia kifungo mwenye hatia baada ya kufanya makosa.

Hakika wale walionunua ukafiri kwa imani, hawatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu.

Neno:'walionunua' linafahamisha hiyari. Kwa sababu mnunuzi anachagua bidhaa na kuridhia anachokichukua badala ya thamani. Na kafiri ameridhia ukafiri badala ya imani, ndipo akastahili adhabu kali.

Unaweza kuuliza : kwa nini Mwenyezi Mungu amelikariri neno'hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kitu' katika Aya mbili, kuna siri gani?

Jibu : makusudio ya Aya ya kwanza ni makafiri wa kiquraishi walioandaa jeshi la kumpiga Mtume(s.a.w.w) na wale wanafiki waliokuwa wakiwasaidia. Aya ya pili, makusudio yake ni kila kafiri kuanzia wa mwanzo hadi wa mwisho, awe mpiga vita au la. Kwa hiyo Aya ya kwanza inakuwa ni mahsusi, na ya pili ni kutaja kiujumla. Mara nyingi inakuwa hivi katika maneno ya watu ambao husema "Fulani amecheza kamari akajimaliza na kila mwenye kufanya hivyo ataangamia"

Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa, ni heri kwa nafsi zao. Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika (kufanya) dhambi na wana wao adhabu idhalilishayo.

Umri wa mtu ni kama mali yake, akiitumia vizuri yeye, kwa watu wake na pia kwa watu wengine au jamaa zake wanaohitaji, basi atarudiwa na heri na wema. Kila mali yake inapozidi ndiyo kunavyozidi kutoa kwake na ndipo wema wake unavyozidi. Na kama akiitumia vibaya na kuitoa katika maasi, basi humrudia mabaya, na kila inavyozidi na kukuwa ndivyo anavyozidi uasi na ufisadi. Umri nao ni hivyo hivyo. Mtu hufikilia wema kama akifanya amali nzuri na unakuwa ni sababu ya uovu wake, kama akifanya uovu. Hiyo ndiyo desturi ya Mungu kwa kijamii. Kila desturi iliyozoeleka inayojulikana kimaumbile au kijamii, basi ni desturi ya Mwenyezi Mungu katika viumbe vyake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amepitisha desturi yake kwa makafiri na watu wote. Amewapa muda kwa kurefusha umri ili mtu ajichagulie mwenyewe, kheri au shari. Lakini kafiri akaghurika kwa kupewa muda na akajiachia katika upotevu. Kwa hiyo ikawa natija ya kupewa kwake muda, ni uovu wake na adhabu yake. Kinyume na Mumini, Mwenyezi Mungu akichelewesha ajali yake kheri yake huzidi na wema huwa mwingi. Bali mwenye kufanya wema katika sehemu iliyobakia katika umri wake, hataadhibiwa kwa dhambi zake zilizopita, kama ilivyoelezwa katika Hadith tukufu. Kwa hali hiyo basi, inatubainikia kuwa herufi Lam katika neno liyazdaadu ni ya mwishilio, sio ya sababu, yaani wanazidi tu na sio 'ili' wazidi.

KAFIRI NA AMALI NJEMA

Unaweza kuuliza : baadhi ya makafiri hufanya kheri kwa ajili ya kheri, na kila umri wao unavyozidi ndivyo wanavyozidi kuwanufaisha watu kwa elimu zao na juhudi zao zilizo nzuri kabisa. Je, hii haipingani na kauli yake Mwenyezi Mungu, na wanazidi tu, katika dhambi?

Jibu : mfumo wa Aya unakusudia dhambi tu, na kuwa wao kwa upande huu wanazidi ukafiri, na wala sio katika hali zote, kwani huenda wakawa ni wema katika baadhi ya matendo yao.

Swali la pili : Je kafiri akifanya wema na kuwanufaisha watu, atapata thawabu, au wema wake huo ni sawa na kutofanya chochote?

Jibu : mtu kwa mtazamo wa imani na matendo (amali), atakuwa katika mojawapo ya hali nne zifuatazo: -

1. Kuamini na kutenda amali njema, hali hii inafuatana na kauli ya Mwenyezi Mungu:

﴿إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ﴾

"Hakika wale wanaosema mola wetu ni Mwenyezi Mungu, kisha wakawa na msimamo, wao huteremkiwa na Malaika (na kuwaambia): msiogope wala msihuzunike na furahieni pepo mliyokuwa mkiahidiwa" (41:30)

2. Kutomuamini Mwenyezi Mungu na kutofanya amali njema, hawa ni katika wale ambao:

﴿اسْتَحْوَذَ عَلَيْهِمُ الشَّيْطَانُ فَأَنسَاهُمْ ذِكْرَ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ حِزْبُ الشَّيْطَانِ أَلَا إِنَّ حِزْبَ الشَّيْطَانِ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴾

"Shetani amewatawala, kwa hivyo akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu, Hao ndio kundi la shetani ni lenye kupata hasara" (58:19)

3. Kuamini bila ya kufanya amali njema, hawa ni katika wanachama wa shetani kama wale waliotangulia. Lau angelikuwa ni mumin wa kweli, basi zingeonekana alama za imani. Mtume(s.a.w.w) anasema: "Hakuna inayookoa isipokuwa amali. Lau ningeasi ningeliangamia" Ama ikiwa amali yake njema imechanganyika na mbaya na akatubia, basi atakuwa katika Aya isemayo:

﴿وَآخَرُونَ اعْتَرَفُوا بِذُنُوبِهِمْ خَلَطُوا عَمَلًا صَالِحًا وَآخَرَ سَيِّئًا عَسَى اللَّـهُ أَن يَتُوبَ عَلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾

"Na wako wengine waliokiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vizuri na vingine vibaya, Huenda Mwenyezi Mungu akapokea toba zao, Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu" (9:102)

4. Kufanya amali njema bila ya kuamini, kama kafiri amlishaye mwenye njaa au amvishaye aliye uchi, atengenezaye barabara, kujenga nyumba za mayatima, au hospitali, kwa njia ya kheri ya kibinadamu.

Imesemekana amali yake hii, kuwepo kwake na kutokuwepo ni sawa tu. Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu anawakubali wamchaye tu." (5:27)

Hapa Tunajibu hivi:

Kwanza : Makusudio ya kauli ya Mwenyezi Mungu: "Hakika Mwenyezi Mungu huwakubalia wamchaye tu," sio kuwa mtu akimwasi Mwenyezi Mungu katika jambo fulani, basi hamkubalii akimtii katika jambo jingine. Kama ni hivyo basi wasingekubaliwa isipokuwa waliohifadhiwa kutotenda dhambi (Maasum) tu, jambo ambalo linapingana na uadilifu wake na hekima yake. Isipokuwa makusudio ya Aya kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubali isipokuwa amali safi isiyokuwa na uchafu wowote wa kidunia na kwamba mwenye kufanya tendo lolote kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu na kwa kheri basi atatosheka na aliyemfanyia. Hakuna mwenye shaka kwamba mwenye kufanya kheri kwa ajili ya kheri na ubinadamu, basi amefanya kheri hiyo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni sawa awe amekusudia hivyo au la. Na mwenye kufanya amali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, basi malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu.

Ama makusudio ya 'hapana dhambi zaidi ya ukafiri' ni kuwa ukafiri ni dhambi kubwa na kwamba dhambi yoyote kadiri itakavyokuwa kubwa haishindi ukafiri. Lakini hili - la kuwa ukafiri ni dhambi kubwa - ni jambo jingine, na malipo ya wema ni jambo jingine. Pili: Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwadilifu, katika jumla ya uadilifu wake ni kwamba mwema na muovu hawako sawa bali mwema ana malipo yake na mwovu ana malipo yake.

Wala sio lazima malipo ya mtenda mema asiyekuwa mu'min yawe akhera

Inawezekana yakawa duniani kwa kuondolewa madhara na balaa, kama asemavyo Mtume(s.a.w.w) : "Kufanya wema ni kinga ya mambo maovu" Na pia sio kuwa malipo ya akhera ni pepo tu, inawezekana kuwa ni kwa kupunguziwa adhabu, au kutokuwa na adhabu wala malipo kama ilivyo hali ya A'raf. Kwa ufupi ni kuwa mtu atalipwa kwa vitendo vyake, vikiwa ni kheri basi atalipwa kheri na vikiwa ni shari atalipwa shari. Kafiri anastahili adhabu kutokana na ukafiri wake, na huenda akafanya kheri kwa ajili ya kheri akastahiki malipo mema, Kila tendo lina hisabu.

Ndio, ni kweli sisi hatujui aina ya malipo atakayolipwa mtenda wema asiyekuwa mu'min. Pia hatujui ni lini na wapi, duniani au akhera. Haya yanategemezewa kwenye ujuzi wa Mwenyezi Mungu na hekima Yake. Na kuyapanga hayo ni kama kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika elimu yake. Basi na amwogope Mwenyezi Mungu mwenye kumwamini. Kwa mnasaba huu tutataja maneno ya Sayyid Kadhim mwenye kitab U'rwathul- Wuthqa mlango wa waqf, maswala ya sharti ya niya ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Ninamnuku: "Inawezekana kusema kwamba, thawabu zinathibiti kwa matendo mema, hata kama hayakusudiwa kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu anayeyatenda anastahiki kusifiwa kwa wenye akili, hata kama hakukusudia kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Basi ikiwa hivyo, sio mbali kustahiki fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu"

Kwa hiyo mwanachuoni huyu mkubwa anasema wazi kwamba inawezekana mtu kulipwa malipo mema kwa vitendo vizuri hata kama hakukusudia radhi ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo kutakuwa na uwezekano mkubwa zaidi kupewa malipo mema anayekusudia njia ya kheri na ubinadamu. Imekwishaelezwa mara nyingi kwamba akili haikatai kuwa yawezekana mwenye dhambi aneemeshwe kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, isipokuwa linalokataliwa na akili ni kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu yule asiyestahili adhabu.

﴿مَّا كَانَ اللَّـهُ لِيَذَرَ الْمُؤْمِنِينَ عَلَىٰ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ حَتَّىٰ يَمِيزَ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَجْتَبِي مِن رُّسُلِهِ مَن يَشَاءُ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا فَلَكُمْ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴾

179.Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kutaka kuwaacha waumini juu ya hali mliyo nayo mpaka awapambanue wabaya na wazuri. Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu, lakini Mwenyezi Mungu humchagua amtakaye katika Mitume yake. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume Yake. Na kama mtaamini na kuogopa basi mtakuwa na ujira mkubwa.

KUPAMBANUA WEMA NA UOVU

Aya 179

MAANA

Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwaacha waumini juu ya hali mliyonayo mpaka awapambanue wabaya na wazuri.

Maadui wa Mtume(s.a.w.w) walikuwa aina mbili: Kwanza ni washirikina, nao ni wale walioukataa uislamu kwa ndani na nje, wakatangaza vita tangu mwanzo wakaishia kuunda vikundi,wakajiandaa kwa nguvu wanazoziweza. Wakawa ni maadui wanaojulikana wazi wakitofautika na waislamu. Aina ya pili ni wanafiki, nao ni wale walioficha ukafiri na uadui kwa Mtume na sahaba zake, wakadhihirisha mapenzi. Kazi yao ilikuwa ni njama dhidi ya Mtume(s.a.w.w) ndani ya safu za waislamu mara wanawababaisha watu kwa uongo, mara nyingine wanawavuta waislamu kwenye maasi, au kuwavunja nguvu za kupambana na adui na kuwatia hofu. Na katika baadhi ya vita walikuwa pamoja na jeshi la waislamu, kisha wakajitoa njiani.

Wanafiki walimsumbua sana Mtume kuliko alivyosumbuliwa na washirikina. Kwa sababu, washirikina walikuwa maadui wanaoonekana wazi, lakini wanafiki walikuwa wakifanya vitimbi kwa kujificha na kuleta madhara kichinichini. Na hivyo ndivyo walivyo kwa yeyote anayelingania kheri, wakati wowote na mahali popote. Wanajaribu kuchafua katika safu za watu wazuri, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja katika Aya nyingi, kama vile Aya ya 173 ya Sura hii, na katika Aya hii tuliyTafsir onayo na pia katika Aya isemayo:

﴿وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا شَيَاطِينَ الْإِنسِ وَالْجِنِّ يُوحِي بَعْضُهُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ زُخْرُفَ الْقَوْلِ غُرُورًا﴾

"Na namna hii tumefanyia kila Nabii adui, mashetani katika watu wa majini, Baadhi yao wanawafunulia wengine maneno ya kuwapamba pamba kwa kuwahadaa" (6:112)

Mtume aliamrishwa kuwafanyia hao wanafiki na kila aliyetamka shahada muamala wa kiislamu. Kuhifadhia damu zao na mali zao, kushirikiana nao katika vita na hata katika ngawira. Kwa sababu uislamu ulikuwa bado ni mchanga, lau atawaua au kuwafukuza wangelisema wakuzaji mambo kwamba Muhammad hampendi anayemwamini na asiyemwamini. Na washirikina wangelifanya hilo ni njia ya kuutangazia vibaya uislamu na Mtume wake.

Kwa sababu hiyo Mtume akawa hana la kufanya, Akiwakubali wataharibu na kuwaweka mbali waislamu na jihad, na akiwakataa alihofia mlinganio wake usipungukiwe na wasaidizi na wafuasi. Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii: "Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwaacha waumini" Yaani sio hekima ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwaacha katika hali hiyo, wanafiki wajifiche kwenye pazia la kudai Uislamu. La sivyo hivyo, bali anawafichua ili wajulikane na wafedheheshwe mbele ya watu na wasibakiwe na pa kutolea vitimbi na ufisadi. Na jambo la kuwafedhehesha sio kutamka shahada, kurukuu na kusujudu, na mambo mengine ambayo ni mepesi kuyafanya. La! Bali ni jambo zito ambalo litawafichua wanafiki na wasibakie na nafasi yoyote ya ria na hadaa au vitimbi na kutia sumu. Kwa mtihani huu mzito na amri ya kuwa na subira na kuwa na uthabiti katika vita vya Uhud, mtajua enyi waumini neema ya Mwenyezi Mungu kwenu na kwamba Yeye hakuwaacha katika hali mliyokua nayo, ya kuchanganyikana na maadui ambao mlitosheka nao hapo mwanzo kwa jina la uislamu. Makusudio ya wazuri ni waumini na wabaya ni wanafiki.

Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu.

Yaani si katika hekima yake Mwenyezi Mungu Mtukufu wala si katika desturi Yake kuwafahamisha watu elimu Yake na awaambie hili ni zuri na hili ni baya; bali ni juu yenu kuyafahamu hayo kupitia majaribio ya shida na misukosuko, kama ilivyotokea Uhud wakati Mtume(s.a.w.w) alipowaita maswahaba warudi kwa adui mara ya pili katika Hamraul Asad. Yaani Mwenyezi Mungu hamfahamishi yeyote yaliyo katika nyoyo za watu kuwa ni imani au unafiki, isipokuwa kuwaamrisha kujitoa mhanga kwa hali na mali, na kwenye utekelezaji ndipo anajulikana mwenye kujitiatia na mwenyewe hasa.

Ndio, Mwenyezi Mungu anawafichulia baadhi ya Mitume yake juu ya unafiki wa huyu na imani ya yule, kwa hekima ambayo yeye mwenyewe Mungu anaijua zaidi, Haya ndiyo maana ya kauli yake,

Lakini Mwenyezi Mungu huchagua katika Mitume yake amtakaye.

Kauli hiyo inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu isemayo:

﴿عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾ إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ﴾

"Mjuzi wa ghaibu, wala hamdhihirishi ghaibu Yake yeyote isipokuwa Mtume aliyemridhia" (72: 26- 27)

﴿وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴾

180.Na wasidhanie kabisa wale ambao wanafanyia ubakhili vile alivyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni bora kwao, bali ni shari kwao. Watatiwa mandakozi ya hivyo walivyofanyia ubakhili siku ya kiyama; na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ana habari ya mnayoyatenda.

﴿لَّقَدْ سَمِعَ اللَّـهُ قَوْلَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ فَقِيرٌ وَنَحْنُ أَغْنِيَاءُ سَنَكْتُبُ مَا قَالُوا وَقَتْلَهُمُ الْأَنبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَنَقُولُ ذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴾

181.Hakika Mwenyezi Mungu amekwishasikia kauli ya wale waliosema: Hakika Mwenyezi Mungu ni fukara na sisi ni matajiri. Tutaandika yale waliyoyasema; na kuua kwao Mitume; na tutawaambia: onjeni adhabu ya kuungua.

﴿ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴾

182.Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyotangulizwa na mikono yenu na kwamba Mwenyezi Mungu si dhalimu kwa waja.

URITHI WA MBINGU NA ARDHI NI WA MWENYEZI MUNGU

Aya 180-182

MAANA

Na wasidhanie kabisa wale ambao wanafanyia ubakhili vile alivyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake kuwa ni bora kwao, bali ni shari kwao.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuhimiza kujitolea mhanga kwa nafsi, amefuatishia kuhimiza kujitolea kwa mali. Makusudio ya Aya hii ni wale wanaojizuia kutoa Zaka na Khumsi ambazo ni wajibu, na wala sio kutoa sadaka ya sunna. Kwa sababu kiaga kikali ambacho kinaelezwa na Aya kinaonyesha kuacha wajibu, sio kuacha sunna. Imesemekana pia kuwa makusudio ni mwenye kuficha jina la Muhammad(s.aw.w) na sifa zake zilizokuja katika Taurat na Injil. Vilevile imesemekana ni kufanya ubakhili wa elimu kwa anayeihitajia. Lakini linalokuja haraka kwenye fahamu, ni kufanya ubakhili kwenye mali. Hilo linaonyeshwa na kauli yake Mwenyezi Mungu.Watatiwa mandakozi ya hivyo walivyovifanya ubakhili siku ya kiyama, Hii ni tafsiri ya;'na ni shari kwao.' Kutiwa mandakozi, hapa ni fumbo la adhabu kali, kama vile Mwenyezi Mungu alivyosema. Siku (mali) itakapotiwa moto katika moto wa Jahannam na vichomwe vipaji vyao vya nyuso na mbavu zao na migongo.yao kwa mali hiyo. (9:35)

MATAJIRI NI MAWAKALA SIO WENYEWE

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehimiza kutoa mali katika Aya kadhaa, nyingi katika hizo ameonyesha kuwa mali zote sio miliki ya aliyenazo, isipokuwa ni miliki ya Mwenyezi Mungu peke Yake na kwamba mtu amewekewa amana tu kuruhusiwa kuitumia kwa mipaka maalum bila ya kuikiuka kama alivyo wakala, hufuata matakwa ya mwenye mali katika matumizi yote. Miongoni mwa Aya nyingine zilizotaja hayo ni:

﴿وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّـهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ﴾

"Na tafuta - kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu - makazi mazuri ya akhera" (28:77).

"Toeni katika yale aliyowapa Mwenyezi Mungu" (36:47)

Aya iliyo wazi zaidi ni ile isemayo.

﴿وَأَنفِقُوا مِمَّا جَعَلَكُم مُّسْتَخْلَفِينَ فِيهِ﴾

"Na toeni katika yale ambayo (Mwenyezi Mungu) amewafanya kuwa makhalifa kwenye hayo" (57:7)

maana ya kuwa khalifa ni kuwa kaimu. Katika Hadith Qudsi anasema:"Mali (zote) ni zangu, na matajiri ni mawakala wangu, mafukara ni watu wangu (wanaonitegemea) basi mwenye kuwafanyia ubakhili watu wangu, nitamwingiza motoni bila ya kujali"

Kwa hivyo, Aya na Hadith zinafahamisha kuwa Uislamu haukubali miliki ya mtu kwa aina yoyote ile, ni sawa iwe ni miliki ya mtu binafsi kabisa, kama ulivyo mfumo wa kibepari, au milki ya kiwango maalum, kama ulivyo mfumo wa kijamaa, au hata miliki ya umma, kama ulivyo mfumo wa kikomunist. Aina zote hizi zinakanushwa na uislamu na kubakia milki ya kihakika ya Mwenyezi Mungu peke Yake, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehalalishia mtu kutumia mali kwa ajii yake na watu wake kwa uzuri, na pia kuitumia katika njia ya kheri kwa sharti ya kuipata kwa njia ya halili siyo ya haramu; kama vile kughushi, kuhadaa, kunyang'anya, rushwa, riba, ulanguzi na kufanya biashara ya ulevi. Kwa hivyo ruhusa ya kuitawala mali na kutumia ni kwa kiwango maalum.

Unaweza kuuliza , baadhi ya Aya zinafahamisha kuwa mali ni milki ya mtu,kama "Piganeni jihadi kwa mali yenu" "Wapeni mayatima mali zao" Katika Hadith imeelezwa: "Damu zenu na mali zenu ni haramu (kwa mwengine)." Na "watu ni wenye mamlaka juu ya mali zao." Na bei na urithi ni katika mambo ya lazima ya dini na sheria ya kiislamu. Kwa hivyo basi, si haifai kusema kuwa uislamu hautambui milki ya mtu kwa aina zote?

Jibu : kutegemeza mtu kitu kunafaa kwa mnasaba ulio karibu. Kwa mfano kumwambia mgeni sahani yako au kumwambia mpotea njia, "hii ndiyo njia yako" Hapa inajulikana wazi kwamba mgeni hana sahani, isipokuwa makusudio ni mgeni ale kwa kutumia sahani hiyo `na mpotea njia, hana njia isipokuwa ni kufuata hiyo njia. Kwa hiyo mali inaegemezwa kwa mtu kwa kutumia kwa njia ya halali na kwa ruhusa sio kwa njia ya milki; kama kauli yake Mwenyezi Mungu.

"Na Mwenyezi Mungu amewafanyia wake katika jinsi yenu." (16:72)

Na kauli ya Mtume(s.a.w.w) "Wewe na mali yako ni ya babako." Kwa dhahiri ni kwamba mke siye milki ya mume kabisa wala mtoto si milki ya kihakika ya mzazi. Ama mauzo na mirathi ni utambulisho wa haki; yaani uislamu umemjaalia mwenye mali kuitambulisha itumiwe na mwengine, wakati huo huo umehalalisha haki maalumu kwenda kwa mrithi na mnunuzi. Na tofauti kati ya milki ya utambulisho na milki ya hakika ni kubwa.

Kwa ufupi ni kwamba uislamu umehalalishia mtu kuhodhi mali kwa sharti maalumu na kuitoa kwa sharti mahsusi, ukasisitiza sana juu ya masharti haya na kuharamisha kuyakiuka. Hii peke yake inatosha na ni dalili wazi kwamba mwanadamu ni wakala wa mali na si mwenye mali, kama si hivyo, basi ingelijuzu kwake kutumia bila ya masharti yoyote. Ni vizuri tumalizie mlango huu kwa kauli ya Imam Jafar as-Sadiq(a.s) :"Mali ni ya Mwenyezi Mungu, nayo ni amana kwa waja wake. Amewaruhusu kula bila ya kuifuja, kuvaa bila ya kuifuja, kuoa bila ya kuifuja na kupanda (k.v. farasi) bila ya kuifuja. Itakayozidi hapo itarudi kwa mafukara waumini kurekebisha hali yao. Atakayefanya hivyo, basi anachokila ni halali, anachokinywa ni halali, anachokipanda ni halali na aliyemuoa ni halali, zaidi ya hivyo ni haram"

Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha sikia kauli ya wale waliosema: Hakika Mwenyezi Mungu ni fukara na sisi ni matajiri.

Aya haikutaja majina ya waliotamka kufuru hii, lakini wafasiri wamenakili kuwa Mtume alipoteremshiwa Aya hii:

"Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri" (2:245)

Wayahudi wa Madina waliwokuwako wakati wa Mtume, walisema "Fukara tu, ndiye anayetaka mkopo kwa tajiri. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu ni fukara na sisi ni matajiri" Hili sio la kushangaza kwa Mayahudi hasa wale matajiri. Kwa sababu misingi yao na kazi zao zinafahamisha wazi uovu huu na kutojali misimamo ya kibinadamu. Na mwenye kufuatilia historia ataona kuwa hakuna sehemu yoyote duniani isipokuwa imeathiriwa na ufisadi wao na malengo yao maovu.

Hakuna ufasaha unaofahamisha taswira ya hakika ya ukweli wa Uyahudi kuliko kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿وَتَرَىٰ كَثِيرًا مِّنْهُمْ يُسَارِعُونَ فِي الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَأَكْلِهِمُ السُّحْتَ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٦٢﴾ لَوْلَا يَنْهَاهُمُ الرَّبَّانِيُّونَ وَالْأَحْبَارُ عَن قَوْلِهِمُ الْإِثْمَ وَأَكْلِهِمُ السُّحْتَ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَصْنَعُونَ ﴿٦٣﴾ وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا﴾

"Na utawaona wengi wao wanakimbilia kwenye dhambi na uadui na ulaji wao haramu, Hakika ni mabaya kabisa wayafanyayo, Mbona watawa wao na wanavyuoni wao hawakatazi maneno yao ya dhambi na ulaji wao haramu. Hakika ni mabaya kabisa wayafanyao. Na Mayahudi walisema: mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa yale waliyoyasema" (5: 62-64)

Sina shaka kabisa kwamba kila mwenye kuingilia hekima ya Mwenyezi Mungu na akasema kwa ulimi wake maneno, kwa mfano, 'Ilikuwa haifai kwa Mwenyezi Mungu kufanya hivi, isipokuwa angefanya hivi' sina shaka kuwa anayesema hivyo atakuwa pamoja na waliosema. Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba; atake asitake.

Tutaandika yale waliyoyasema.

Hili ni kemeo la kiaga cha wale waliosema: "Hakika Mwenyezi Mungu ni fukara na sisi ni matajiri" Kwa sababu kuandika dhambi kunapelekea adhabu, Na kuuwa kwao Mitume. Pia tutaandika wa kale wao walivyowaua Mitume. Kumenasibishwa kuua kwao, ingawaje walioua ni wa kale wao, Hayo yamekwishaelezwa katika tafsir ya Aya 21 ya Sura hii.

Hayo ni kwa sababu ya yaliyotangulizwa na mikono yenu; na kwamba Mwenyezi Mungu si dhalimu sana kwa waja.

Vipi atadhulumu na Yeye amekataza dhulma na kuifanya kuwa ni kubwa ya madhambi makubwa na katika Aya nyingi akiita kuwa ni kufuru?

Zaidi ya hayo dhalimu anadhulumu kwa sababu tu anahitajia hicho anachokifanyia dhulma. Na Mwenyezi Mungu amejitosheleza na kila kitu. Kwa msingi huu wa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kujitosha na hahitajii kitu, kunathibitisha uadilifu wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) vilevile kunathibitisha kwamba yeye hana mwili, kwa sababu mwili unahitaji vitu.

Kwa hivyo, inatubainika kubatilikia kwa madhehebu ya wanaosema kuwa shari inatokana na Mwenyezi Mungu, na kwamba yeye anamtengenezea maasi mja, kisha amwadhibu, Pengine watafute njia ya kuhepa kauli hii ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Hakika Mwenyezi Mungu si dhalimu wa waja. Kwa vile ametumia neno Dhallam lenye maana kudhulumu sana iwe anaweza kudhulumu kidogo, lakini sio sana! Mwenyezi Mungu ametakasika kabisa na wayasemayo madhalimu.