TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17258
Pakua: 2340


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17258 / Pakua: 2340
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

Mwandishi:
Swahili

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO

﴿وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ كِتَابَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا تَرَاضَيْتُم بِهِ مِن بَعْدِ الْفَرِيضَةِ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا﴾

24.Na wanawake wenye kuolewa isipokuwa wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume, Ni Sharia ya Mwenyezi Mungu kwenu. Na mmehalalishiwa wasiokuwa hao, kwamba Muwatafute kwa mali zenu kwa kuoa bila ya kufanya zina. Ambao mmestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari yao yaliyo lazimu. Wala si vibaya kwenu katika yale mliyoridhiana baada ya (kutoa) kile kilichowalazimu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hekima.

﴿وَمَن لَّمْ يَسْتَطِعْ مِنكُمْ طَوْلًا أَن يَنكِحَ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ فَمِن مَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُم مِّن فَتَيَاتِكُمُ الْمُؤْمِنَاتِ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِكُم بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ فَانكِحُوهُنَّ بِإِذْنِ أَهْلِهِنَّ وَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ مُحْصَنَاتٍ غَيْرَ مُسَافِحَاتٍ وَلَا مُتَّخِذَاتِ أَخْدَانٍ فَإِذَا أُحْصِنَّ فَإِنْ أَتَيْنَ بِفَاحِشَةٍ فَعَلَيْهِنَّ نِصْفُ مَا عَلَى الْمُحْصَنَاتِ مِنَ الْعَذَابِ ذَٰلِكَ لِمَنْ خَشِيَ الْعَنَتَ مِنكُمْ وَأَن تَصْبِرُوا خَيْرٌ لَّكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴾

25.Na asiyeweza miongoni mwenu kupata mali ya kuoa wanawake waungwana waumini, basi (na aoe) katika wajakazi wenu waumini iliyowamiliki mikono yenu ya kuume; na Mwenyezi Mungu anajua sana imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na baadhi; Basi waoeni kwa idhini ya watu wao na muwape mahari yao kama ada - wawe ni wenye kujistahi si waasherati wala wenye kujifanyia mahawara. Watakapoolewa kisha wakafanya uchafu, basi itakuwa adhabu juu yao ni nusu ya adhabu iliyowekwa kwa waungwana. Hayo ni kwa mwenye kuchelea mashaka katika nyinyi. Na mkisubiri ni bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.

WALIOOLEWA

Aya ya 24-25

LUGHA

Neno Muhsanat limetoka katika neno Hisni (ngome) likiwa na maana ya Uislam, uhuru, ndoa, na kujistahi. Aya mbili tulizo nazo zinakusanya maana zote hizi nne, ufafanuzi unafuatia.

MAANA

Na wanawake wenye kuolewa isipokuwa wale iliyowamiliki mikono yenu ya kuume

Haya yanaungana na yale ya wanawake walio haramu katika Aya iliyotangulia. Yaani pia mmeharamishiwa wake wenye waume zao. Yametangulia maelezo katika kifungu cha lugha kwamba neno Muhsanat katika Aya mbili hizi linachukua maana nne: Ndoa, kujistahi, uhuru na Uislam, Makusudio ya Muhsanat hapa ni wanawake walioolewa. Kwa sababu ndoa ni ngome ya mke inayomzuia kufanya yasiyotakikana na ni ngome ya mume, kwa sababu hiyo hiyo. Hadith inasema:"Mwenye kuoa amehifadhi theluthi mbili za dini yake."

Makusudio yawale iliyowamiliki mikono yenu ni kutokea mwanamke kuwa ni miliki ya mwanamume mwingine. Kwa maana ya kuwa mwanamke akiolewa ni haramu kwa mtu mwengine, ila kama atamilikiwa na Mwislam. Hapo atakuwa halali yake yule (Mwislamu) aliyemmiliki hata kama ni mke wa mtu mwengine.

Mwislam anaweza kummiliki mwanamke kwa sababu zifuatazo:

Kwanza : Kuwa mateka wake. Hilo linakuwa kutokana na vita vya kidini baina ya Waislam na washirikina na Waislam wawashinde washirikina. Hapo wake wa washirikina, watoto wao na mali zao, zinakuwa ngawira ya vita. Mwislam akipata mateka wa kike bila ya mumewe, basi mwanamke huyu atatenganishwa naye na awe si mumewe tena, kwa kongamano la madhehebu yote. Wakitekwa wote pamoja (mume na mke) hawatatenganishwa kwa mujibu wa madhehebu ya Hanafi na Hambal ama kwa Shia Imamiya, Shafi na Malik, (wamesema mume na mke hao makafiri) watatenganishwa.

Mwislam akitaka kumwoa mwanamke wa kishirikina aliyemteka, anaweza kufanya hivyo baada ya kuzaa, ikiwa alikuwa na mimba, Au atangoja aingie hedhi moja ikiwa hana mimba, Ikiwa hana mimba wala hatoki hedhi atangoja siku 45 ndipo amwingilie.

Hukumu hizi zilifuatiliwa katika ushindi wa waislam wa kwanza. Wengine wamezitafutia sababu kuwa ati zilikuwa ni kwa sababu ya kuuzuwiya na kuukataza ukafiri, na kuhimiza kukubali uislam. Ama sisi tunasema kuwa hizo ni hukumu za ki-ibada, hatujui hekima yake. Tunachojua ni kuwa zina mifano katika sheria, kuna baadhi ya dini nyengine zimehalalisha kuwaua wanawake na watoto. Lakini Uislam umeamrisha kuwafanyia upole mateka na watumwa wakiwa wa dini yoyote au madhehebu yoyote.

Pili : Mwislam kummiliki mwanamke ni kumnunua akiwa mjakazi. Hilo ni kuwa mtu awe ana mjakazi aliyemwoza mtumwa wake au mtu mwengine. Kisha akamuuzia mwengine; uuzaji huu utabatilisha ndoa ya mjakazi kwa mujibu wa madhehebu ya Shia Imamiya. Itamhalalishia mnunuzi kulala naye baada ya kusafika kwa kuzaa, hedhi au siku 45. Sayyid Rashid Ridha mwenye Tafsir Al-manar anasema: "Baadhi ya masahaba kama Ibn Mas'ud wako kwenye rai hii wanayoitumia Mashia, lau si kwamba ustadh Imam[1] hakuichagua ingelikuwa kauli ya Shia Imamiya ni yenye nguvu zaidi kuliko madhehebu yote ya Sunni."

Sayyid Rashid anakiri kwamba kauli ya Shia ina nguvu zaidi kuliko madhehebu ya Sunni lakini pamoja na hivo anaikataa, si kwa lolote ila tu kwamba ustadh wake hakulisema. Ajabu ya watu wa mfano wa Sayyid Rashid ambaye ameilaumu Taqlid (kufuata) na wanaofuata, mpaka akawatoa katika dini sio katika elimu tu. Angalia tafsir yake ya Aya 165-167 ya Sura ya pili (Al-Baqara)

Kwa ujumla ni kwamba Uislam umehalalisha kwa Mwislamu kumwoa aliye na mume (aachike) akiwa ni mjakazi aliyemmiliki kwa kumnunua, au mshirikina aliyemteka katika vita vya kuupigania Uislam na kuulingania.

Unaweza kuuliza : Neno Muhsanat (wanawake walioolewa) ni wingi wa wanawake na maana yake yako wazi, sasa kuna faida gani ya Mwenyezi Mungu kusema katika wanawake

Jibu :Kwanza : mara nyingi huwa ni kwa kufafanua na kuyatlia mkazo zaidi mfano"Na kuwaua kwao Mitume pasi na haki" (3:181) pamoja na kuwa kuwaua Mitume daima huwa ni pasi na haki.

Pili : Huenda mtu akadhania kuwa makusudio ya Muhsanat ni wanawake waisl am tu. Ndipo likaja neno katika wanawake ili kubainisha ujumla; na kwamba ndoa ni ya kuheshimiwa tu, iwe kwa mwanamke wa Kiislam au mwengine.

Ni Sharia ya Mwenyezi Mungu kwenu

Ni kutilia mkazo yaliyotangulia kuhusu walioharamishwa, Kwa maana ya kuwa uharamu wa aina zilizotajwa ni sharia inayotoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwenye kuikhalifu, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye atakayemhukumu na kumwadhibu.

Na mmehalalishiwa wasiokuwa hao

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alipomaliza kubainisha walio haramu, anataja desturi ya kijumla, ambayo ni kwamba wasiokuwa wa aina zilizotajwa ni halali kuwaoa kwa sharti ya kuwa ndoa ifuate misingi iliyowekwa na sharia; kama kutoa mahari ya kisharia sio ujira wa ukahaba.

Hiyo ndiyo maana ya kusema:Muwatafute kwa mali zenu kwa kuoa bila ya kufanya zina.

Neno kuoa linatosha bila ya kutaja zina, lakini limekuja kwa kutilia mkazo na kuonyesha kuwa mwenye mali anaweza kutoa mali yake katika starehe zisizokuwa za haram. Kwa sababu Uislam kama ulivyoharamisha njia za chumo zisizokuwa za kisheria - kama riba, kughushi na kunyang'anya - pia umeharamisha kutoa mali katika mambo ya haram; kama vile zina au kuingilia uhuru wa wengine.

Sunni na Shia wameafikiana kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu:Na mmehalalishwa wasiokuwa hao , inafahamisha kujuzu kuchanganya mtu na shangazi yake au mamake mdogo. Kwa sababu inavyojulikana katika njia ya watu wa sharia ni kutaja ya haram tu, kwa vile inawezekana kuyadhibiti.

Ama yenye kuhalalishwa hayadhibitiki, Hivyo wanayaashiria kwa kusema: "Yasiyokuwa hayo." Lakini Sunni wamesema kuwa imethibiti kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba yeye amesema: "Haolewi mwanamke pamoja na shangazi yake wala khala (mama mdogo)."

Khawarij wamesema kuwa inajuzu kuwachanganya kwa hali yoyote, akikataa shangazi, mama mdogo au akikubali.

Shia Imamiya wametofautiana, kuna baadhi wanasema kama walivyosema Sunni. Wengi wao wanasema kuwa ikiwa mke wa pili anayetaka kumwoa ni shangazi au khala wa mke wa kwanza, anaweza kumwoa kwa hali yoyote. Lakini akimwoa shangazi au khala kwanza, haijuzu kuoa mpaka kwa idhini ya shangazi au khala. Wamelitolea dalili hilo kwa riwaya za Ahlul-bait(a.s)

NDOA YA MUT'A

Ambao mmestarehe nao katika wao, basi wapeni mahari yao yaliyo lazimu.

Dhamiri ya 'nao' na 'wao' inawarudia wale ambao ni halali kuwaoa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:"na mmehalalishiwa wasiokuwa hao."

Maana - kwa maafikiano ya wafasiri - ni kwamba mwenye kutaka kumwoa mwanake katika wale walio halali kwake, basi ni lazima atoe mahari ambayo ni lazma, sio sadaka wala hisani.

Mjadala umekuwa mkubwa kuhusu Aya hii; Je, makusudio ni ndoa ya daima tu, au ndoa ya muda, au zote pamoja? Na kama makusudio ni Mut'a je Aya imekua mansukh (hukmu imefutwa) pamoja na ndoa yenyewe ya Mut'a? Katika vitabu vya Hadith, Fiqh na Tafsir ya Sunni na Shia waislam wote wameafikiana kwa kauli moja kwamba Uislam ulileta sharia ya Mut'a ya wanawake, na kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwaaamrisha sahaba zake hilo; kama inavyoeleza Sahih Bukhar Juz, 7 mlango wa Targhib fin nikah, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alikuwa katika jeshi la waislam akawaambia:"Mwenyezi Mungu amewapa idhini ya kufanya Mut'a, basi fanyeni"

Riwaya ya pili ya Bukhari inasema: "Mwanamume yeyote aliyeafikiana na mwanamke wanaweza kuishi pamoja siku tatu, wakipen da wanaweza kuzidisha au wakiamua kuachana wataachana."

Katika Sahih Muslim Juz; 2 mlango wa 'Nikahul-mut'a' Uk. 623 chapa ya 1347 A.H. Kuna Hadith iliyopokewa kutoka kwa Jabir bin Abdillahi Al-ansary amesema: "Tulifanya M ut'a wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu; na wakati wa Abu Bakr na Umar." Katika ukurasa huo huo kuna Hadith nyengine kutoka kwa Jabir, amesema: "Kisha akatukataza Umar." Kuna Hadith kama hiyo katika Musnad Imam Ahmad bin Hambal. Juz. 3

Arrazi katika kufasiri,ambao mmestarehe nao an asema: "Amesema Imran bin Al-hasin, ambaye ni katika mafakihi wa kisahaba na mbora wao: "Hakika Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya ya Mut'a na wala Aya hiyo haikufutwa hukmu yake na Aya nyingine; na Mtume akatuamrisha kufanya Mut'a wala hakutukataza. Kisha mtu mwengine akasema kwa maoni yake atakavyo; Hapo anakusudia kuwa Umar alikataza.

Riwaya hizi na mfano wake zinapatikana zaidi katika Sahih za Sunni na Tafsir zao na katika vitabu vyao vya Fikihi. Kwa hiyo basi mzozo wa kuwa je, makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Ambao mmestarehe nao"

Ni ndoa ya daima tu, au ndoa ya Mut'a tu, au zote pamoja unakuwa ni mzozo tasa usiokuwa na faida yoyote. Kwa sababu, natija inakuwa ni hiyo hiyo haitofautiani na chochote. Ni sawa tuseme kuwa Aya inaenea katika n doa ya muda, au inahusika na ndoa ya daima tu. Kwa sababu linaloangaliwa ni kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ameamrisha ndoa ya Mut'a kwa kuafikiana Waislam wote. Na kwamba kila aliloliamrisha Mtume na Mwenyezi Mungu Mtukufu pia ameliamuru kama alivyosema: "Alichowapa Mtume, kipokeeni na alichowakataza jiepusheni nacho." (59:7)

Baada ya kuafikiana Sunni na Shia kwamba Uislam umeweka sharia ya Mut'a, wamehitalifiana katika kufutwa sharia hiyo na kuwa haramu baada ya kuwa halali.Sunni wamesema imeharamishwa baada ya kuhalalishwa, Shia wanasema ilikuwa na itaendelea kuwa halali mpaka siku ya mwisho.

Kimsingi ni kwamba ni juu ya Sunni kuthibitisha kufutwa hukumu hiyo na uharamu wake kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) . Kwa sababu wao wanadai kuondoka kitu kilichothibiti kwa njia ya mkato na yakini, Ama Shia hawalazimiki kuthibitisha kuwa haikufutwa. Kwa sababu wao wanasema linalothibiti kwa yakini haliondoki ila kwa yakini. Mfano watu wawili wameafikiana kuwa fulani alikuwa hai mwaka uliopita, kisha wakatofautiana kuhusu kufa kwake. Hapo atakayetakiwa kuthibitisha ni yule anayedai kuwa amekufa. Ama yule anayesema bado ni mzima, hatakiwi kufanya chochote. Kwa kuwajibisha hukumu ya kubakisha lilokuwa kama ilivyo mpaka ithibiti kinyume.

Sunni wamekiri kwamba ni juu yao kuthibitisha, na wala sio Shia ndipo wakatoa dalili za kuthibiti kufutwa hukumu hiyo, kwa Hadith za Mtume(s.a.w.w) , ambazo Shia wamezijadili kwa matini na isnadi na wakathibtisha kwa mantiki sahihi kwamba Hadith hizo zimesingiziwa Mtume(s.a.w.w) kwa dalili zifuatazo:

(i) Kwamba Sunni wenyewe wanakubali kuwa zinagongana na kupingana.

Ibn Rushdi katika kitabu Al-bidaya Juz, 2 Masuala ya ndoa ya Mut'a anasema: "Baadhi ya mapokezi ni kwamba Mtume(s.a.w.w) aliharamisha Mut'a siku ya vita vya Khaybar; nyingine zinasema ni siku ya ushindi wa Makka; na nyingine zikadai ni siku ya vita vya tabuk; nyingine zikasema kuwa iliharamishwa siku ya Hija ya mwisho (Hijjatul-wadaa); nyingine siku ya kulipa Umra, nyingine katika mwaka wa Autas - jina la mahali katika sehemu ya Hijaz palipiganwa vita katika vita vya Mtume(s.a.w.w) - kisha anaendelea kusema Ibn Rushdi - imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas kwamba yeye amesema: "Mut'a haikuwa ila ni rehema ya Mwenyezi Mungu aliyowarehemu umma wa Muhammad(s.a.w.w) lau si kuikataza Umar asingelazimika kuzini ila mwovu."

(ii) Riwaya hizo za kufutwa hukumu si hoja, hata kama zitakuwa hazina migongano. Kwa sababu ni Khabarul-wahid. Na 'kufutwa hukmu' kunathibiti kwa Aya au Khabar Mutawatir tu, na wala sio Khabarulwahid[2] .

(iii) Yaliyokuja kwenye Sahih Muslim kwamba waislam walifanya Mut'a wakati wa Mtume na wa Abu Bakr. Kwa hivyo haya yanapingana na kuwa ilifutwa wakati wa Mtume. Vyenginevyo basi khalifa wa kwanza atakuwa ni muhalalishaji wa aliloliharamisha (alilolifuta) Mwenyezi Mungu na Mtume.

Ukweli zaidi unaofahamisha kuwa haikufutwa ni kauli ya Umar mwenyewe: "Mut'a mbili zilikuwako wakati wa Mtume na mimi ninazikataza na nitaadhibu kwazo" Kila nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka wala sitatia shaka kwamba Umar, lau angelinyamazia basi wasingelitofautiana hata Waislam wawili katika kujuzu Mut'a na uhalali wake mpaka siku ya kufufuliwa.

Unaweza kusema : Ni ajabu sana kuwa Umar amesema haya. Kwa sababu ni kuharamisha alilolihalalisha Mwenyezi Mungu; na ni kumpinga Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye 'hatamki kwa matamanio.'

Jibu : Ni kweli, ni ajabu ya maajabu kama ulivyosema: "kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake", lakini waislam wameafikiana kwamba Umar ameyasema hayo, Sijaona hata mmoja aliyekanusha, Bali kuna riwaya nyingine zinazosema kuwa Umar alikataza mambo matatu aliyoyaamrisha Mtume sio mawili. Anasema Al-qawshaji - mwanachuoni wa Kisunni - katika sherehe ya Tajrid mwisho wa utafiti wa Uimam: "Umar alipanda mimbar akasema: 'Enyi watu! Mambo matatu yalikuwako katika wakati wa Mtume na mimi ninayakataza na kuyaharamisha na kumwadhibu atakayeyafanya: Mut'a ya wanawake, Mut'a ya Hija na neno Hayya ala khairil amal."

Amepokea Tabari na Razi kwamba Ali amesema: "Lau si Umar kukataza Mut'a asingelizini ila mwovu." Yako mfano wa hayo soma Tafsir ya Thalabi na ya Suyuti.

Swali la pili : Je, haifai - kwa nafasi ya Umar - kuchukua kauli hii, kwamba ni riwaya ya Mtume(s.a.w.w) na wala si rai ya Umar dhidi ya Mtume(s.a.w.w) ?

Jibu : Ni kweli kabisa kuchukulia hivyo kunafaa sana, lakini kauli ya Umar: "zilikuwako wakati wa Mtume na mimi ninazikataza" inakataa kuchukulia huku, Kwani yeye mwenyewe amenasibisha kuhalalisha kwa Mtume na kuharamisha kwake yeye. Lau kauli yake ingelikuwa ni riwaya na siyo rai, basi angelinasibisha kukataza kwa Mtume, Kwa sababu Mtume ndiye an ayefaa zaidi kukataza. Kwa ufupi haiwezekani kwa hali yoyote kuchanganya kauli mbili: "Kwamba Mtume alikataza Mut'a baada ya kuiamrisha na kauli ya Umar kuwa Mut'a ilikuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na mimi ninaikataza" Na imethibiti kwamba Umar ameyasema haya, Kwa hiyo ni wazi kwamba Mtume hakukataza Mut'a.

Haya ndiyo baadhi ya majibu ya riwaya za 'Naskh'(kufutwa hukumu) zilizolazimishwa kwa Mtume. Mwenye kutaka ufafanuzi na arudie Tafsir Alau-Rrahman ya Sheikh Muhammad jawad Al-balaghi; na Al-bayan Fi Tafsir Al-Qur'an ya Sayyid Khui, Naqdhul washi'a ya Sayyid Muhsin Al-amin na Juzuu ya tatu ya kitab Dalail s-swadiq cha Sheikh Muhammad Hassan Al-mudhaffar.

Kwa hakika ni kwamba hakuna tofauti kati ya ndoa ya daima na ndoa ya muda (Mut'a), kuwa haitimii bila ya mahari na Aqdi (kufunga ndoa); na katika uharamu unaoingia kwa ukwe; na katika wajibu wa urithi, kuwaangalia na kuwapa haki nyingine watoto; na katika wajibu wa eda ya mwenye kuolewa.

Katika kitabu chetu Fiqhul Imam Jaafar as-Sadiq(a.s) tumetaja mambo kumi na tano yaliyo sawa katika ndoa ya daima na ya muda, Na mambo kumi yanayotofautiana.

Wala si vibaya kwenu katika yale mliyoridhiana baada ya (kutoa) kile kilichowalazimu.

Ikipita ndoa kwa mahari maalum yaliyobainishwa wakati wa kufunga ndoa, basi yanakuwa ni haki ya mke; atayatumia kadiri atakavyo. Lakini hiyo haizuwii kuelewana mke na mume kusamehe mahari yote au baadhi hata kuzidisha.

Vilevile halizuwii kuelewana juu ya aina ya matumizi ya mke na kiasi chake, au kuacha kabisa. Vile vile kuelewana kuhusu talaka, kurejeana baada ya talaka au baada ya kwisha muda wa Mut'a na mengineyo ambayo hayatoki katika mipaka ya sharia.

Na asiyeweza miongoni mwenu kupata mali ya kuoa wanawake waungwana waumini; basi (na aoe) katika wajakazi wenu waumini iliyowamiliki mikono yenu ya kuume.

Maana ni kuwa asiyepata mali ya kumwezesha kumwoa mungwana, basi aoe mjakazi mumini.

Na Mwenyezi Mungu anajua sana imani yenu. Baadhi yenu mnatokana na baadhi.

Makusudio ya imani hapa ni dini. Maana ni kuwa haitakikani kwa mumin kuona unyonge kumwoa mjakazi kwa sababu ya rangi yake na kabila yake. Kwa sababu watu wote wanatokana na Adam; na Adam ametokana na mchanga.

Kuzidiana mbele ya Mwenyezi Mungu ni kwa takua tu, si kwa fahari na nasaba. Mjakazi anaweza akawa mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko muungwana kwa sababu ya wema wake na takua yake.

Basi waoeni kwa idhini ya watu wao na muwape mahari yao kama ada

Watu wao wajakazi, ni wale watu wanaowamiliki

Wawe ni wenye kujistahi si waasherati.

Yaani sio wazinifu kwa sura ya wazi, kama kahaba mzururaji.

Wala wenye kujifanyia mahawara

Yaani anayeizini kisiri siri.

Watakapoolewa kisha wakafanya uchafu basi itakuwa adhabu yao ni nusu ya adhabu iliyowekwa kwa waungwana.

Yaani mjakazi akizini, adhabu yake ni nusu ya adhabu ya muungwana. Adhabu hiyo ni ile iliyotajwa na Aya hii:

﴿لزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ﴾

"Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mpigeni kila mmoja wao mijeledi mia" (24:2)

Hayo ni kwa mwenye kuchelea mashaka katika nyinyi.

Mwenyezi Mungu hataki kuwapa mashaka waja wake wala kuingia katika fitna. Mwenye kuona kuwa ana haja na mke, basi aoe mungwana kama ana uwezo; na kama hana basi aoe mjakazi. Kama ataweza kuvumilia bila ya kuwa na mke na akawa salama na dini yake na afya yake, basi ni bora kuvumilia.

Na mkisubiri ni bora kwenu

Aya yote hii ndefu imeelezea hukumu ya mungwana kumwoa mtumwa, na adhabu ya mtumwa kama akizini. Sisi tumefupisha katika kuifasiri, kwa sababu maelezo ya utumwa na hukumu zao yamekuwa hayana umuhimu baada yakufutwa utumwa.

Ajabu ya maajabu ni kwamba dola ya kwanza kutangulia kuleta mwito wa kufutwa utumwa inawafanyia watu wa rangi nyengine kama wanyama nchini kwake na inazisaidia serikali za kibaguzi kila mahali na kufanya mambo ya kuutisha ulimwengu mzima, na mustakbali wa binadamu.

Dalili wazi ya ukweli huu, ni kushiriki kwake kuliunda taifa la Kiisrail na kuisadia kuzifanyia uadui nchi za Kiarabu na kuwafukuza wazalendo katika nchi zao ili kuzichukua. Ama kukusanya kwake mamia ya majeshi huko Vietnam na aina ya ukatili wa mauaji na uharibifu uliyoufanya, haina mfano katika historia. Naona kwamba njia pekee ya kuepuka uovu wa dola hii ni kila mtu wa Mashariki na Magharibi akatae lolote lile linalonasibiana au kuwa na athari na dola hiyo.

﴿يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُبَيِّنَ لَكُمْ وَيَهْدِيَكُمْ سُنَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ وَيَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴾

26.Mwenyezi Mungu anataka kuwabainishia na kuwaongoza Mwendo wa waliokuwa kabla yenu na awatakabalie toba. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

﴿وَاللَّـهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيْكُمْ وَيُرِيدُ الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الشَّهَوَاتِ أَن تَمِيلُوا مَيْلًا عَظِيمًا﴾

27.Na Mwenyezi Mungu anataka kuwatakabalia toba na wale ambao hufuata matamanio wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa.

﴿يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَخُلِقَ الْإِنسَانُ ضَعِيفًا ﴾

28.Mwenyezi Mungu anataka kuwahafifishia, Na mtu ameumbwa hali yakuwa ni dhaifu.

MWENYEZI MUNGU ANATAKA KUWABAINISHIA

Aya 26 - 28

MAANA

Mwenyezi Mungu anataka kuwabainishia na kuwaongoza mwenendo wa waliokuwa kabla yenu na awatakabalie toba.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha katika Aya zilizotangulia aina ya wanawake walio haramu kuwaoa kwa nasaba, ukwe na kunyonya na vile vile kubainisha walio halali, aliendelea kusema kuwa tumewawekea hukumu hizo na kuwabainishia ili mpate faida ya halali yake kutokana na haramu yake, na kwa twaa yake na maasi na mfuate nyayo za waliowatangulia katika kujiepusha na yaliyoharamishwa na kufuata uongofu na imani. Vile vile aweze kujua mtubiaji hukumu alizoziweka Mwenyezi Mungu, aweze kujikurubisha kwake Mwenyezi Mungu na kuacha aliyoyakataza.

Imesemekana kwamba makusudio yaawatakabalie toba ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameweka sharia hizo ili awajue wanaotubia yale yaliyopita katika zama za ujahiliya na mwanzo wa Uislam - kuoa wake wa mababa, kuoa pamoja dada wawili na mengineyo ya haramu.

Vyovyote iwavyo ni kwamba mwenye kutubia na asiyetubia hawezi kumtii Mwenyezi Mungu na kufuata hukumu zake ila baada ya kuzijua na kumbainikia. Kwa hiyo ubainifu wa hukumu zake Mungu, ni hisani na neema kutoka kwake. Kwa sababu haamrishi isipokuwa lile lenye heri na masilahi; wala hakatazi ila lililo na shari na ufisadi.

Na wala si lazima Mwenyezi Mungu atubainishie hekima ya kuamrisha Kwake na kukataza Kwake. Sisi hatukalifiwi kujua au kufanya utafiti, letu sisi ni kufuata na kutii, tukiwa ni wenye kuamini kuwa hukumu zake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni kwa ajili ya heri yetu ya dunia na akhera.

Na Mwenyezi Mungu anataka kuwatakabalia toba, Na wale ambao hufuata matamanio wanataka mkengeuko mkengeuko mkubwa.

Wanaofuata matamanio ni wale wanaotoa mwito wa kujivua na mikazo ya dini na tabia njema, na hufuatana na matamanio ya mwili vyovyote yanavyoelekea. Hawa siku zote wapo; hata wakitofautiana wanatofautiana katika mfumo tu, kulingana na hali zao. Katika karne ya ishirini wamejibandika jina la uhuru na maendeleo. Wamepetuka mipaka katika kuamsha tamaa ya maingiliano ya wanawake na wanaume kwa njia ya filamu, vitabu na picha za uchi. Huu ndio mgeuko na kwenda kombo ambako ameashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kauli yake: "mkengeuke mkengeuko mkubwa"

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekariri toba katika Aya mbili bila ya kuweko kitu kingine, pale aliposema:"Na awatakabalie toba na Mwenyezi Mungu anataka kuwatakabalia toba" Je, kuna makusudio gani katika hilo?

Jibu : Toba ya kwanza imekuja kuwa ni sababu ya kubainisha halali na hara- mu kwa wanawake bila ya kuangalia amri ya toba. Ama ya pili ni kuelezea amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuwataka watu watubie kwa kuacha mambo ya haramu; mkabala wake ni matakwa ya mfuasi wa matamanio. Kwa mfano unaweza kumwambia mwanao: "Nimekununulia kitabu hiki ili ukisome basi kisome." Umetaja kusoma kwanza kwa kubainisha sababu zinazowajibisha kusoma, na ukarudia mara ya pili kwa sababu wewe unamtaka asome na huku ukimwamuru.

Mwenyezi Mungu anataka kuwahafifishia katika kuhalalisha walio halali katika wanawake; bali hata katika mambo mengine vile vile. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

"Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi hawatakii yaliyo mazito" (2.185)

Wala hakuwawekea uzito katika dini (22:78)

Na kuna Hadith tukufu isemayo:"Nimewajia na dini nyepesi na ya kweli"

Na mtu ameumbwa hali ya kuwa dhaifu katika kukabiliana na mambo yanayosababisha ladha na starehe; hasa starehe ya mwili. Kwa ajili hiyo, ndipo Mwenyezi Mungu akahalalisha kustarehe na wanawake katika mipaka yake tuliyoielezea. Katika ngano la kale inaelezwa kuwa Iblis alimwambia Musa(a.s) :"Mwanamume hakai faragha na mwanamke ila mimi huwa sahibu yake."

Sijamuona yeyote aliyeleta picha ya udhaifu wa binadamu, katika nafsi yake na mwili wake, kuliko Imam Ali(a.s) aliposema:"Akijiwa na matarajio, tamaa humdhalilisha; Akiingiwa na tamaa, pupa humwangamiza. Akimilikiwa na kukata tamaa, simanzi humuua. Akipatwa na hofu, hadhari humshughulisha. Akipatwa na masaibu, fazaa humfedhehesha na akipatwa na ufukara, mtihani humshughulisha"

Akaendelea kusema tena:"Masikini binadamu! Ajali (yake) imefichwa, ugonjwa (wake) umefunikwa, na amali (yake) imehifadhiwa. Anaumizwa na kunguni, au anauliwa na kikohozi na ananukishwa na jasho"

Kama ambavyo Imam ameleta picha ya udhaifu wa mtu; vile vile ameleta picha ya nguvu na ukuu wa mtu; kwa kusema: "Mtu anashiriki kufika mbingu saba zenye nguvu." Yaani kipawa chake hakisimami katika mazingira yanayomzunguka tu, bali huvuka hadi mwezini, kwenye Zuhura na kwenye Merikh na sehemu nyenginezo zilizomo ulimwenguni anazitumia kwa haja yake.

Imam ameonyesha udhaifu wa binadamu ili asitegemee nguvu zake na kumhadaa akapetuka mpaka. Na akonyesha nguvu zake ili asisalimu amri kwa unyonge, akaacha kujitahidi na kufanya kazi. Mwenye akili ni yule mwenye kupigania huku akiwa na hadhari ya mambo yaliyofichika na yanayokuja ghafla.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ إِلَّا أَن تَكُونَ تِجَارَةً عَن تَرَاضٍ مِّنكُمْ وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا﴾

29.Enyi ambao mmeamini! Msiliane mali zenu baina yenu kwa batili. Ila itakapokuwa ni biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye rehema kwenu.

﴿ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ عُدْوَانًا وَظُلْمًا فَسَوْفَ نُصْلِيهِ نَارًا وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴾

30.Na atakayefanya hilo kwa uadui na dhulma, tutamtia motoni. Na hilo kwa Mwenyezu Mungu ni jepesi

MSILIANE MALI ZENU KWA BATILI

Aya 29-30

MAANA

Enyi ambao mmeamini! Msiliane mali zenu baina yenu kwa batili.

Jumla kama hii imekwishapita pamoja na tafsiri yake katika Aya ya 188 ya Sura ya Baqara. Tunaunganisha yaliyotangulia na Hadith iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar as-Sadiq(a.s) , kwamba Mwenye deni akiwa anayo mali, akaitumia katika haja yake bila ya kulipa deni, basi amekula mali ya batili bali ni juu yake kulipa deni; hata kama atahitajia sadaka." Inajuzu kwake kutumia mahitaji ya siku moja tu na usiku wake.

Ila itakapokuwa ni biashara kwa kuridhiana baina yenu.

Neno baina yenu ni ishara ya kwamba hapana budi kuridhiana pande mbili, Kusamehewa huku kunafahamisha kuwa biashara haishurutiwi kuwa bidhaa mbili za kubadilishana ziwe sawa sawa bila ya kupungua. Kwa sababu hilo linakurubia kuwa ni muhali. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemruhusu mnunuzi au muuzaji kula kinachozidi maadamu pande zote mbili zimekubaliana, lakini kwa sharti ya kutokuwapo kughushiana na kudanganyana.

Unaweza kuuliza : Kama mfanya biashara akiitangaza bidhaa yake na akaipamba; je itakuwa ni kughushi na kula mali ya batili?

Jibu : Hapana, lakini bei ikiwa ni kwa masharti ya sifa maalum; kisha ikawa kinyume, basi mnunuzi anayo hiyari ya kuvunja bei na kurudisha bidhaa kwa muuzaji, naye apewe pesa zake.Wala msijiue yaani baadhi yenu wasiwaue wengine, Hapo pana ufahamisho wa umoja wa ubinadamu. Kuna Hadith tukufu isemayo:"Waumini ni kama nafsi moja"

Imesemekana kuwa maana ya msijiue, ni kuwa msijiingize katika majanga kwa kufanya mliyokatazwa na Mwenyezi Mungu. Maana hayo yako sahihi, lakini yanatofautiana na dhahiri ya Aya.

Na atakayefanya hilo kwa uadui na dhulma, tutamtia motoni.

Hilo ni ishara ya kujiua, kula mali kwa batili, uadui na kuipetuka haki. Inawezekana kutofautisha baina ya uadui na dhulma; kwamba dhuluma inakuwa kwa mtu mwenyewe kujidhulumu na kumdhulumu mwingine. Ama uadui ni kwa kumfanyia mwingine tu.

Kwa vyovyote ni kwamba, mwenye kusahau, kukosea au kulazimishwa, hasifiki na dhuluma wala uadui, isipokuwa mwenye kulazimishwa kuua. Kwa mfano: Dhalimu mwenye uwezo akimwambia mtu: 'Muue huyu au nitakuua wewe.'

Hapo haijuzu kwa mtu huyo kuua hata kama ana hakika kuwa huyo aliyemwamrisha anaweza kumuua. Kwa sababu haifai mtu kujikinga kwa kumwingiza mwengine kwenye madhara. Kwa hiyo kama mtu huyo akitekeleza agizo la dhalimu na akaua, basi naye atauliwa na kulipiziwa kisasi, na yule dhalimu aliyeamuru mauaji atafungwa maisha.

﴿إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴾

31.Mkijiepusha na (madhambi) makubwa mnayokatazwa, basi tutawafutia makosa yenu (madogo) na tutawatia mahali patukufu.

MADHAMBI MAKUBWA

Aya 31

MAANA

Qur'an Tukufu imegawanya madhambi kwenye mafungu mawili: Makubwa na madogo, Mgawanyo huu umekuja katika Aya kadhaa, Kama vile Aya hii tuliyo nayo. Kwa sababu makusudio ya; basi tutawafutia makosa yenu ni yale makosa madogo; kama walivyoafikiana wafasiri. Na maana yake ni mwenye kujiepusha na madhambi makubwa hufutiwa madogo.

Aya nyengine zinazoyagawanya madhambi kwenye sehemu mbili ni kama hizi zifuatazo:

﴿الَّذِينَ يَجْتَنِبُونَ كَبَائِرَ الْإِثْمِ وَالْفَوَاحِشَ إِلَّا اللَّمَمَ﴾

"Wale ambao wanajiepusha na madhambi makubwa na maovu isipokuwa makosa madogo." (53:32)

"Haiachi dogo wala kubwa ila hulihisabu" (18:49)

"Na amewafanya muuchukie ukafiri na ufasiki na uasi" (49:7)

Hapa inabainika kwa yaliyokatazwa ni mambo matatu: Ukafiri ambao ni ukanushaji na upingaji, ufasiki ambao ni kufanya madhambi makubwa na uasi ambao ni kufanya madhambi madogo.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema: Dhambi zote ni kubwa wala hakuna ndogo, kwa vile kumwasi Mwenyezi Mungu katika jambo ni kukubwa, hata kama jambo lenyewe ni dogo, ni wazi kuwa kauli hii inakhalifu dhahiri ya Qur'an. Zaidi ya hayo, hata sharia za kutungwa pia zinagawanya makosa kwenye mafungu mawili: Kosa kubwa na dogo. Hata hivyo inawezekana kukanusha madhambi madogo kwa njia fulani tutakayoionyesha.

Kwa namna yoyote iwayo, ni kwamba Kitabu Kitukufu (Qur'an) hakikuweka mpaka wa kupambanua dhambi ndogo na kubwa, Kwa hiyo wametofautiana Mafaqihi katika maana ya dhambi kubwa. Kundi moja limesema kuwa kila lililokuja katika Qur'an kwa kukutanishwa na kiaga cha akhera hilo ni kubwa na lisilokuwa hilo ni dogo; kauli bora ni ile ya aliyesema: Hakika dhambi zote ni kubwa hizo zenyewe - kama alivyosema mwenye kukanusha dhambi ndogo - isipokuwa zinagawanyika ndogo na kubwa kwa kulinganishwa na nyengine.

Kwa mfano kumwangalia mwanamke wa kando kwa matamanio ni dhambi kubwa hilo lenyewe lakini ni dogo kulinganishwa na kumpiga busu, nako pia ni kudogo kulinganisha na kumwingilia. Au kula kwenye meza iliyo na pombe ni dhambi kubwa, lakini kwa kulinganisha na kunywa pombe yenyewe itakuwa ni dhambi ndogo.

Kwa hakika mtendaji dhambi na vivutio vyake vina athari kubwa katika kuifanya dhambi iwe kubwa au dogo; kama walivyosema Mafaqihi; na uhalifu au kosa la jinai; kama walivyosema wanasheria wapya. Kwa hiyo basi kabla ya kuichukulia dhambi kuwa ni ndogo au kubwa, ni lazima tumwangalie mtendaji kwanza, je amefanya aliyoyafanya kwa kutojua na udhaifu wa matakwa yake; kama vile kughilibiwa na mpotezaji mwenye dhambi; au alifanya kwa haja ya dharura; au ni kwamba yeye ana shauku ya kuwafanyia maovu watu; kama walivyo watu wengi. Zimekuja Hadith mutawatir kutoka kwa Mtume kwamba yeye amesema: "Hakika amali zote huzingatiwa kwa nia tu"

Hadith nyengine inasema:"Hakuna dhambi ndogo pamoja na kung'ang'ania, wala hakuna dhambi kubwa pamoja na kutubia."

Kutoka kwa Imam as-Sadiq anasema: "Hakika watu wa motoni watawekwa milele motoni, kwa vile nia zao ni kumwasi Mwenyezi Mungu katika dunia milele, kama wangebaki. Na hakika watu wa peponi watawekwa milele peponi kwa vile nia zao zilikuwa ni kumtii Mwenyezi Mungu milele, Kwa hiyo ni kutokana na nia ndio wamewekwa milele hawa na wale"

Tumefafanua athari ya nia katika kutafsiri Aya ya 144 Al-Imran, Litakuwa ni jambo zuri tutaje Hadith iliyopokewa kutoka kwa Imam Jafar as- Sadiq(a.s) akielezea aina za madhambi makubwa. Imepokewa kwamba Amru bin Ubaid, alikwenda kwa Imam na kumwuliza kuhusu madhambi makubwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, naye akasema: : "Kubwa ya madhambi makubwa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

"Hakika Mwenyazi Mungu hasamehi kwa kushirikishwa" (4:48)

Na akasema:

﴿إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ﴾

"Kwa hakika anayemshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu amemharamishia pepo na makazi yake ni motoni" (5:72)

Dhambi kubwa jengine ni kukata tamaa ya rehema ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

﴿إِنَّهُ لَا يَيْأَسُ مِن رَّوْحِ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْكَافِرُونَ﴾

"Wala hawakati tamaa ya rehema ya Mwenyezi Mungu ila watu Makafiri" (12:87)

Jingine ni kujiaminisha na hila (adhabu) za Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴾

"Hawajiaminishi na hila (adhabu) za Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara" (7:99)

Vilevile kuwaudhi wazazi wawili, kwa sababu Mwenyezi Mungu amekufanya kuwaudhi wazazi ni ujeuri na uovu katika kauli yake:

﴿وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا﴾

"Na kuwatendea wema wazazi wangu wala hakunifanya niwe jeuri muovu" (19:32)

Pia kuua nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu ila kwa haki, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا﴾

"Na mwenye kumuua muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahanam atadumu humo" (4:93).

Miongoni mwa madhambi makubwa ni kuwasingizia wanawake watakatifu kwani Mwenyezi Mungu anasema:

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ الْغَافِلَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ لُعِنُوا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴾

"Hakika wale ambao wanawasingizia wanawake wanaojiheshimu, walioghafilika (na zina), wamelaaniwa katika dunia na akhera; nao watapata adhabu kubwa" (24:23)

Jingine ni kula mali ya yatima; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا ﴾

"Hakika wale wanaokula mali ya yatima kwa dhulma, bila shaka wanakula moto matumboni mwao na wataingia motoni" (4:10)

Pia kukimbia vita, kwani Mwenyezi Mungu anasema:

﴿الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ﴾

"Ambao wanakula riba; hawatainuka, ila kama ainukavyo ambaye amezugwa na shetani kwa wazimu." (2:275)

Na uchawi, kwani Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَيَتَعَلَّمُونَ مِنْهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِ بَيْنَ الْمَرْءِ وَزَوْجِهِ وَلَقَدْ عَلِمُوا لَمَنِ اشْتَرَاهُ مَا لَهُ فِي الْآخِرَةِ مِنْ خَلَاقٍ﴾

"Wakajifunza kwao mambo ambayo kwayo waliweza kumfarikisha mtu na mkewe,Na hakika wanajua kwamba aliyenunua haya hatakuwa na sehemu yoyote katika akhera." (2:102) Pia zina, kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

﴿وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾ يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا﴾

"Wala hawazini; na atakayeyafanya hayo atapata adhabu. Na ataongezewa adhabu siku ya Kiyama atadumu humo kwa kufedheheka." (25: 68-69)

Vilevile dhambi kubwa ni kiapo cha kuzamisha[3] kwani Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَـٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ ﴾

Hakika wale wanaouza ahadi ya Mwenyezi Mungu na viapo vyao kwa thamani ndogo, hao hawatakuwa na thamni yoyote akhera (3:77)

Pia kufanya hiana, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَمَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ﴾

Na Mwenye kufanya hiyana, atayaleta yale aliyoyafanyia hiyana siku ya Kiyama (3:161)

Na kuzuia kutoa Zaka pia ni dhambi kubwa kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ ﴾

"Siku ( mali yao) itakapotiwa joto katika moto wa Jahannamu na kwayo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao (waambiwe) haya ndiyo mliyolimbikizia nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkiyalimbikiza." (9:35)

Pia kutoa ushahidi wa uongo na kuuficha ushahidi. Kwani Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَلَا تَكْتُمُوا الشَّهَادَةَ وَمَن يَكْتُمْهَا فَإِنَّهُ آثِمٌ قَلْبُهُ﴾

".. Wala msiufiche ushahidi, Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kuingia dhambini " (2:283)

Jingine ni kunywa pombe. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amelinganisha na kuabudu masanamu, Kuacha Swala makusudi au chochote alichofaradhisha Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Mwenye kuacha Swala makusudi atakuwa ameepukana na dhima ya Mwenyezi Mungu na dhima ya Mtume wake na atakuwa amevunja ahadi."

Na kuvunja udugu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ﴾

"Na wanakata aliyoamuru Mwenyezi Mungu yaungwe na wanafanya uharibifu katika nchi; hao ndio watakaopata laana na watapata nyumba mbaya" (13: 25)

Hapo Amr bin Ubaid akatoka na kilio huku akisema: "Ameangamia anayesema kwa maoni yake na kubishana nanyi katika fadhila na elimu enyi watu wa nyumba ya Mtume!"