TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17291
Pakua: 2359


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17291 / Pakua: 2359
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

Mwandishi:
Swahili

2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO

﴿وَلَا تَتَمَنَّوْا مَا فَضَّلَ اللَّـهُ بِهِ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ لِّلرِّجَالِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبُوا وَلِلنِّسَاءِ نَصِيبٌ مِّمَّا اكْتَسَبْنَ وَاسْأَلُوا اللَّـهَ مِن فَضْلِهِ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا﴾

32.Wala msitamani aliyowafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko baadhi nyingine. Wanaume wana fungu katika walichokichuma na wanawake wana fungu katika walichokichuma, Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

﴿وَلِكُلٍّ جَعَلْنَا مَوَالِيَ مِمَّا تَرَكَ الْوَالِدَانِ وَالْأَقْرَبُونَ وَالَّذِينَ عَقَدَتْ أَيْمَانُكُمْ فَآتُوهُمْ نَصِيبَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدًا﴾

33.Na kila watu tumewawekea wa kuwarithi yale waliyoacha wazazi wawili na jamaa na wale mliofungamana nao ahadi wapeni sehemu yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni shahidi wa kila kitu.

NA MUOMBENI MWENYEZI MUNGU FADHILA ZAKE

Aya 32 - 33

LUGHA

Neno Mawali ni wingi wa Maula. Neno hili lina maana nyingi; kama vile bwana aliyemwacha huru mtumwa wake; mtumwa aliyeachwa huru; na maana nyingine ni mwenye kurithi, Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa katika Aya hii. Na neno Aymanikum ni wingi wa Yamini kwa maana ya kiapo au kwa maana ya mkono kwa sababu watu hupeana mkono wanapofungiana ahadi.

MAANA

Wala msitamani aliyowafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko baadhi nyingine

Dhahiri ya katazo hili inaonyesha kuwa haijuzu kwa mtu kutamani kile anachokiona ni kizuri kilicho kwa mwenzake; ni sawa iwe ni kwa husuda,yaani kutaka mwenzake aondokewe na neema hiyo; au hata kwa wivu mzuri, yaani kutaka asiondokewe na neema hiyo na yeye apate kama hivyo.

Lakini dhahiri ya Aya siyo makusudio, kwa sababu wivu mzuri hauna ubaya wala madhara. Ama hasadi ni haramu ikiwa kuna kuhusudiana au kuingilia hekima ya Mwenyezi Mungu. Amesema Mtume Mtukufu(s.a.w.w) :"Ukifanya hasadi usiitokeze!" Yaani ukihisi katika nafsi yako kutaka mwenzako aondokewe na neema usiyokuwa nayo basi jizuiwe na usiitoe uipige vita isije ikadhihirika nje kwa kauli au kitendo. Ukiweza kufanya hivyo, basi wewe huna jukumu lolote mbele za Mwenyezi Mungu, lakini ukishindwa kufanya hivyo basi wewe ni mwenye dhambi.

Hali hii pekee ndiyo inayokatazwa katika Aya, Kwa sababu kauli ya Mtume(s.a.w.w) ni ubainifu na tafsiri yake. Ikiwa inajuzu kwa mtu kutamani mfano wa yaliyo kwa mwengine bila ya husuda, basi kutamani kheri kutakuwa kunafaa zaidi bila ya kuangalia aliyomfadhili Mwenyezi Mungu mtu mwengine. Mwenyezi Mungu anasema katika kusifu hayo:

﴿وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ﴾

"Na miongoni mwao wako wasemao: Mola wetu tupe mema duniani na (tupe) mema akhera na utulinde na adhabu ya moto." (2:201)

Wanaume wana fungu katika walichokichuma na wanawake wana fungu katika walichokichuma.

Katika tafsir Majmaul-bayan, imeeleza hivi: Ulikwenda ujumbe wa wanawake kwa Mtume(s.a.w.w) ukasema:

"Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwani Mwenyezi Mungu siye wa wanaume na wanawake? Na wewe si ni Mtume wa wote? Basi kwa nini Mwenyezi Mungu anawataja wao tu, na wala hatutaji sisi? Tunahofia kuwa sisi hatuna maana yoyote na kwamba Mwenyezi Mungu hana haja nasi! Hapo ikashuka Aya hii.

Maana ya dhahiri ni kuwa kila mtu atapata natija ya amali yake. Kwa hiyo haitakikani mtu kuishughulisha nafsi yake na husuda. Kwa sababu madhara yake yatamrudia mwenyewe duniani na akhera. Imam Ali(a.s) anasema: "Msihusudiane, kwani husuda inakula imani, kama moto ulavyo kuni." Amesema tena:"Siha ya mwili ni hasadi kuwa chache" Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wanawake kwa kukumbusha kuwa mke na mume ni sawa kila mmoja wao katika kupata alichokichuma. Mwenyezi Mungu amesema:

﴿فَاسْتَجَابَ لَهُمْ رَبُّهُمْ أَنِّي لَا أُضِيعُ عَمَلَ عَامِلٍ مِّنكُم مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ بَعْضُكُم مِّن بَعْضٍ﴾

"Mimi sitapoteza amali ya mfanya amali miongoni mwenu akiwa mwanamme au mwanamke ni nyinyi kwa nyinyi" (3:195)

KUMWOMBA MWENYEZI MUNGU BILA YA KUFUATA NJIA YAKE

Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake

Kwa sababu hazina yake haishi, na neema zake hazihisabiki. Imam Zainul-Abidin katika baadhi ya dua zake anasema:"Ninajua- Ewe Mola wangu - kwamba mengi ninayokuomba ni mepesi kwako; na kwamba chungu ya mambo ninayokutaka unipe si lolote katika ukunjufu wako; na kwamba ukarimu haumdhikishi yeyote kukuomba; na kwamba utoaji wako ni zaidi ya wa yeyote." Kuna Hadith isemayo:"Mwombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake na Mwenyezi Mungu hupenda kuombwa."

Unaweza kuuliza kuwa : amri ya kuomba inasababisha ulazima wa kujibiwa na inajulikana wazi kuwa watu wote au wengi wao wanaomba na kuomba, lakini hawajibiwi maombi yao?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t) kama alivyoamrisha kuomba dua, pia ameamrisha kujishughulisha na kujitahidi; na akasema:"Na kwamba mtu hatapata ila aliyoyachuma." (53:39)

Maana ya haya ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amedhamini kuitikia dua kwa njia ya kujishughulisha na amali, na wala hakudhamini kila ayawazayo mtu kwa kutaka tu na kuomba, Vipi isiwe hivyo? Lau angelifanya hivyo, ungeliharibika ulimwengu, Kisha je, Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mwenye kuamuru au kuamriwa? Na atafanya nini kama atapokea maombi mawili yanayopingana wakati mmoja? Na mwisho utasemaje kwa yule anayeomba na hafuati njia yake?

Kwa hivyo basi amri yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ya kuomba fadhila zake, ni ibara ya pili baada ya amri ya kujitahidi na kufanya amali; na kwamba ni juu ya mtu kuelekea kwenye shughuli zake akimtegemea Mwenyezi Mungu peke yake na kutomwingilia mwengine katika shughuli zake, kutokana na fadhila alizopewa na Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu yeyote aliye shughulishwa na mambo ya mwengine ila husongwa katika maisha yake, hudangana na kukosa namna katika mambo yake yote.

Kuna wanafunzi wenzangu fulani niliosoma nao huko Najaf, wakiwa werevu na wenye akili sana. Wakamaliza miaka mingi hapo Najaf, lakini pamoja na hayo hawakufaulu, si kwa lolote isipokuwa walishughulishwa na kuangalia mambo ya watu kuliko nafsi zao na masomo yao. Hakukosea aliyesema: "Mwenye kuchunguza mambo ya watu atakufa na kibuhuti." Tumezungumza kwa ufafanuzi kuhusu dua na kuitikiwa kwake katika kufasiri Aya 186 ya sura ya Baqara.

Na kila watu tumewawekea wa kuwarithi yale waliyoacha wazazi wawili na jamaa na wale mliofungamana nao ahadi wapeni sehemu yao.

Mwenyezi Mungu amewataja warithi wa aina tatu:

(i) Wazazi wawili wakiwemo mababu na mabibi.

(ii) Jamaa wa karibu wakiwemo watoto, akina kaka na akina dada, ami, shangazi na wajomba na khala.

(iii) Mfungamano maalum; kama vile ndoa, umiliki au mfungamano wakudhaminiana. Vile vile mfungamano wa kijumla ambao ni Uislam.

Wote hawa wanaingia katika kauli ya Mwenyezi Mungu:"Na mliofungamana nao ahadi." Mfungamano wa ndoa ni maarufu. Ama mfungamano wa miliki ni mtu kummiliki mtumwa, kisha akamwacha huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu bila ya kutoa chochote au kuwa ni kafara. Mtumwa huyu huria akifa na akawa hana mrithi basi mrithi wake atakuwa yule aliyemwacha huru. Mfungamano wa kudhaminiana, ni kuafikiana wawili kila mmoja amdhamini mwenzake, au mmoja tu adhamini.

Yakikamilika maafikiano haya kwa masharti yaliyotajwa katika vitabu vya Fiqhi, basi ni juu ya mdhamini kumdhamini mwenzake na pia atamrithi mdhaminiwa ikiwa hana mrithi.

Ama mfungamano wa kiislam makusudio yake ni mafugamano ya kijumla baina ya Mtume na aliyemwamini. Mwislamu akifa na hana mrithi kabisa, basi atarithiwa na Mtume au atakayekuwa katika nafasi yake.

Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amesema: "Mimi ni mrithi wa asiye na mrithi" katika riwaya ya pili anasema:"Mimi ni msimamizi wa asiye na msimamizi." Na katika riwaya ya tatu:"Mimi ni bwana wa huria asiye na mrithi, ninamrithi mali yake na kumwacha huru."

Inatosha kuwa ni dalili ya hayo kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Nabii ni bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao" (33:6)

Katika kitab Wasailu-Shia kuna Hadith kadhaa zisemazo kuwa Ali(a.s) alikuwa akisema:"Mtu akifa na akaacha mali bila ya mrithi, wapeni mali (hiyo) watu wa mjini kwake." Hii haipingani na kauli ya Mtume; Kwa sababu Mtume aliwahi kuwapa haki yake hii mafukara wa mji wa marehemu.

Yamekwishatangulia maelezo kuhusu mafungu ya baba, mama ndugu mume na mke, katika Aya ya 12 ya sura hii.

﴿الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ وَاللَّاتِي تَخَافُونَ نُشُوزَهُنَّ فَعِظُوهُنَّ وَاهْجُرُوهُنَّ فِي الْمَضَاجِعِ وَاضْرِبُوهُنَّ فَإِنْ أَطَعْنَكُمْ فَلَا تَبْغُوا عَلَيْهِنَّ سَبِيلًا إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيًّا كَبِيرًا ﴾

34.Wanaume ni wasimamizi wa wanawake, kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhili baadhi yao kuliko wengine na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa; basi wanawake wema ni wale wenye kutii na kujilinda hata katika siri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde Na ambao mnaogopa unashiza wao, basi wanasihini na muwahame katika vitanda na wapigeni, Watakapowatii msiwatafutie njia. Hakika Mwenyezi Mungu ni mtukufu mkubwa.

﴿وَإِنْ خِفْتُمْ شِقَاقَ بَيْنِهِمَا فَابْعَثُوا حَكَمًا مِّنْ أَهْلِهِ وَحَكَمًا مِّنْ أَهْلِهَا إِن يُرِيدَا إِصْلَاحًا يُوَفِّقِ اللَّـهُ بَيْنَهُمَا إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا خَبِيرًا﴾

35.Na kama mkihofia ugomvi ulio baina yao, basi wekeni mwamuzi mmoja katika watu wa mume na mwamuzi mmoja katika watu wa mke. Wakitaka suluhu basi Mwenyezi Mungu atawawezesha, Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye habari.

WANAUME NI WASIMAMIZI WA WANAWAKE

Aya 34 - 35

MAANA

Wanaume ni wasimamizi wa wanawake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine.

Mwanamume na mwanamke ni nguzo mbili za maisha, Ni muhali mmoja wao kuwa bila ya mwingine. Maana ya haya ni kuwa kati ya mume na mwanamke kuna aina ya kutofautiana. Lau wangelikuwa sawa katika pande zote, basi wasingelihitajiana na ingelikuwa kuwako na kutakuwako ni sawa. Kwa hivyo basi mwito wa kuwa sawa katika kila kitu unahalifu mantiki ya maisha.

Huenda mtu akasema kuwa : mwanamke na watetezi wake wanataka usawa katika haki na majukumu na wala hawataki usawa na mwanamume katika kila kitu; mfano kutunga mimba na kunyonyesha.

Jibu : Tofauti ya viungo inasababisha ulazima wa kutofautiana katika baadhi ya haki na mambo yaliyo wajibu, na hata katika baadhi ya matamanio ya kinafsi. Kwa hiyo basi anayetaka usawa katika haki zote na majukumu yote, atakuwa ameenda mbali sana, sawa na yule anayetaka utofauti katika yote.

Ilivyo hasa ni kwamba mwanamume na mwanamke wanalingana sawa katika haki nyingi; za muhimu zaidi ni usawa mbele ya Mwenyezi Mungu, kanuni, uhuru wa matumizi ya mali, hiyari ya kuchagua mshirika wa maisha n.k. Na wanatofautiana katika baadhi ya haki.

Katika kufasiri Aya 228 Sura Baqara, tumetaja tofauti 14 baina ya mwanamume na mwanamke katika sharia ya kiislam. Ama Aya hii tuliyonayo inafahamisha mambo haya yafuatayo:

1. Wanaume ni wasimamizi wa wanawake. Makusudio ya wanaume hapa ni kuwahusu waume wa ndoa; na wanawake, ni wake wa ndoa. Makusudio ya usimamizi sio mamlaka yote, kiasi cha kumfanya mume kuwa ni kiongozi dikteta na mke kuwa ni mwenye kuongozwa asiyekuwa na matakwa au hiyari yoyote, la! Si hivyo, bali makusudio ni kuwa mume ana aina ya usimamizi. Mafakihi wameueleza usimamizi huo, ikiwa ni pamoja na kuifanya talaka iwe mikononi mwa mume, kumtii kitandani na kutotoka nyumbani mke ila kwa idhini ya mumewe, Zaidi ya hayo wako sawa.

2. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja sababu mbili za aina hii ya utawala wa mume kwa mke. Ameashiria sababu ya kwanza kwa kusema: Kwa sababu Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao kuliko wengine. Na sababu ya pili kwa kusema: Na kwa sababu ya mali zao wanazozitoa.

Tuanze na sababu ya kwanza: Dhamiri katika baadhi yao inawarudia wanawake na wanaume pamoja; na makusudio ya baadhi ya kwanza ni wanaume na baadhi ya pili ni wanawake.

Unaweza kuuliza : kwanini Mwenyezi Mungu hakusema Alayhinna (juu yao wanawake) ambapo ingekuwa wazi zaidi?

Jibu : Lau angelisema hivyo ingelikuwa makusudio ni kufadhilisha wanaume wote juu ya wanawake wote; na hayo siyo makusudio yake. Kwa sababu hili liko mbali na hali ilivyo.

Kuna wanawake kadhaa ambao ni bora kuliko wanaume elfu. Kwa hiyo ndio limekuja neno 'baadhi' peke yake kuashiria kwamba ubora ni wa jinsi fulani kwa jinsi nyingine bila ya kuangalia watu wote.

Mwenyezi Mungu ameficha aina ya ubora kwa kusema:Kwa sababu Mwenyezi Mungu amefadhilisha baadhi yao.

Wafasiri na wengineo wamesema kuwa mwanamume ana nguvu zaidi kuliko mwanamke katika mweko wake wa viungo na kiakili; na wakarefusha maneno na dalili katika hilo, Kuna miongoni mwao waliotunga vitabu mahsusi katika maudhui haya.

Tunayoyashuhudia ni kwamba kazi muhimu katika nyanja za elimu, dini, fani falsafa na siasa zote zinashikiliwa na wanaume na wala sio wanawake. Kama itatokea mwanamke, basi itakuwa ni nadra sana; na unadra unatilia mkazo desturi na sio kama unaikanusha.

Zaidi ya hayo tumeshuhudia mwanamke kabla ya chochote, akijishughulisha zaidi na vipodozi na mavazi ambayo yanaunda uke wake na kudhihirisha uchi wake na kujibadilisha kwa namna ambayo anaweza kumvutia mwanamume na kumwamsha hisia zake. Kwa hali hiyo ndio ukaona kuwa majumba ya mitindo ya mavazi ni kwa ajili ya wanawake tu.

Wala hakuna tafsir ya kujishghulisha na uke wake; na mwanamume kujishughulisha na kazi muhimu katika nyanja za maisha ila ni kubainisha umbile na nafsi baina ya mwanamke na mwanamume.

Ama sababu ya pili ya ubora wa mwanamume ambao ameubainisha Mwenyezi Mungu kwa kusema:Na kwa mali zao walizozitoa , iko wazi kam a tulivyoieleza katika sababu ya kwanza. Kwa sababu ambaye anachukua juku- mu la kuwakimu wengine, hapana budi kuwa ni bora kuliko yule asiyetakiwa lolote; hata kujikimu yeye mwenyewe tu.

Kwa hakika kauli yake hiyo Mwenyezi Mungu:Na kwa mali zao walizozitoa , imetosha kuwa mume asipomkimu mkewe, hawezi kuwa msimamizi wake; au mke anaweza kutaka talaka kupitia kwa kadhi; na ni juu ya kadhi kumwonya mume.

Ikiwa mume ataendelea kumnyima matumizi, kwa kushindwa au kwa inadi, basi Kadhi atamwamrisha atoe talaka. Kama akikataa kutoa talaka, Kadhi atatoa talaka, kwa sababu Kadhi ni msimamizi wa anayekataa.

Hivi ndivyo asemavyo Maliki, Shafii na kundi la wanavyuoni wa Kishia akiwemo mwenye Urwatul-wathqa na Sayyid Muhsin Hakim. Nasi pia twaunga mkono rai hii, Suala hili tumeliwekea mlango maalum katika kitab Fiqhul-Imam Jafar as-Sadiq kwa kichwa cha habari 'Talaka ya kukosa kukimu.' Humo tumeonyesha dalili na kauli kwa ufafanuzi.

Wanawake wema ni wenye kutii na kujilinda hata katika siri, kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde.

Mke mwema ni yule mwenye kuafikiana kinyumba na mumewe, mwenye kujichunga, kulingana na alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu. Hamwasi mumewe katika mambo aliyohalalishiwa na Mwenyezi Mungu, wala hamtii katika mambo aliyoharamishiwa na Mwenyezi Mungu.

Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) :"Mwanamke ni yule anayekufurahisha ukimwangalia; anayekutii ukimwamrisha; na ukiwa mbali naye, hujichunga yeye mwenyewe na mali yako."

Maelezo ya unyumba hayaishi; wala hakuna yeyote anayejua siri iliyoko katika kauli ya asemaye: "Sioi tena hata mkinichinja;" isipokuwa yule aliyeoa tu. Baadhi ya wanawake ni saratani inayoua pole pole, Ikiwa kuna mtu aliye huru mwenye hiyari, basi mtu huyo ni kapera.

Ama mwenye mke hana uhuru wala hiyari isipokuwa wachache sana. Baadhi ya dini zinasema kuwa kesho Mwenyezi Mungu hatawaadhibu kwa moto wala hatawapa thawabu kwa pepo, bali yule mwasi atamwoza kikongwe kilichojishia kinachomchukiza umbo na tabia, na ataozwa mtiifu msichana mzuri anayemfurahisha kiumbo na tabia!

Na ambao mnaogopa unashiza wao, basi wanasihini, muwahame katika malazi na wapigeni.

Makusudio ya unashiza ni kuacha kutekeleza haki za unyumba. Unashiza unaweza kuwa kwa mke tu, au mume tu, au wote pamoja.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja mwanamke mwema, sasa anamtaja mwanamke mwasi (nashiza); na akamuhalalishia mume kumwonya mkewe nashiza, Akiendelea amuhame kitandani. Akiwa bado anaendelea ampige kipigo hafifu cha kumtia adabu sio cha kumtesa-kipigo kisichoumiza wala kugeuza rangi ya ngozi; kama ilivyoelezwa katika vitabu vya fiqh.

Ieleweke kwamba; kutoa onyo, kususia kulala naye na kupiga ni ruhusa tu, sio wajibu. Mafakihi wote wameafikiana kuwa kuacha kupiga ni bora; na kwamba anayevumilia maudhi ya mke, wala asimpige ni bora kwa Mungu, kuliko anayempiga; kama walivyoafikiana kuwa kila itakapopatikana njia nyepesi zaidi, basi itumike na kuwa haramu kutumia njia ngumu.

Mtume(s.a.w.w) amesema:"Asimpige mmoja wenu mkewe kama anavyompiga ngamia; anampiga mchana kisha analala naye usiku. Mbora wenu ni mbora wenu kwa familia yake, na mimi ni mbora wenu kwa familia."

Jambo la kushangaza ni kwamba Tabari ambaye anasifika kuwa ni Sheikh wa wafasiri, amesema katika kufasiri Aya hii kwamba ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa mume, ikiwa mkewe atamuasi amfunge kwa kamba - kama amfungavyo ngamia - katika nyumba anayolala naye. lililomfanya kufasiri hivi ni kwamba Waarabu wanaiita kamba wanyomfungia ngamia 'Hijaria', kwa hivyo maana ya 'Uhjuruhunna' ni wafungeni kwa hiyo 'Hijara' ni kufunga na sio kuwahama.

Jibu zuri sana la tafsir hii, ni kauli ya Zamakhshari; "Na hii ni katika tafsiri nzito kufahamika"

Watakapowatii msiwatafutie njia katika zile njia tatu; Kwa sababu kuonya, kumwacha kitandani, na kipigo ni njia ya kutafuta utiifu, Kwa hiyo lengo likitimia hakuna haja ya njia.

Kauli yake hii Mwenyezi Mungu inaonyesha kuwa haifai kwa mume kutafuta sababu za uongo za kumuudhi mke; hata kama mke anamchukia mumewe. Maadam anamtekelezea haki zake za kisharia; Kwa sababu pendo na chuki viko nje ya uwezo wa mtu, Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hahisabu wala kuadhibu isipokuwa kauli inayodhihiri au kitendo kinachodhihiri.

Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu mkubwa

Arrazi anasema kwamba: makusudio ya kauli hii ya Mwenyezi Mungu, kwa ufupi ni:

Kwanza : Kuwatisha wanaume wasiwadhulumu wanawake.

Pili : Mwenyezi Mungu hakalifishi isipokuwa haki.

Tatu : Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakalifishi lisilowezekana. Kwa hiyo ni juu ya mume kutowakalifisha wanawake wasioyaweza.

Nne : Mwasi hakalifishwi akitubia kutokana na uasi wake, basi nashiza akitubia, msimwadhibu.

Tano : Mwenyezi Mungu hafichui siri, kwa hiyo nyinyi ndio mnatakikana zaidi msifichue dhahiri ya hali ya mke; wala msitafute yaliyo moyoni mwake.

Arrazi ni katika Ashaira, wasemao kwamba Mwenyezi Mungu anamkalifisha mwanadamu asiloliweza. Naye ni mtetezi wa madhahebu haya kwa nguvu zake zote, ametetea katika sehemu nyingi kwenye tafsiri Al-kabir, hasa pale alipofasiri Aya isemayo:

"Haikalifishi Mwenyezi Mungu nafsi yoyote ila uweza wake." (2:286)

Lakini hapa ameyasahau madhehebu yake na kurudia kwenye umbile safi ambalo Mwenyezi Mungu amewaumbia watu, Akasema: (Ninamnukuu) "Hakika Mwenyezi Mungu hawakalifishi msioyaweza. Kwa hiyo msiwakalifishe wanawake wawapende kwa sababu wao hawawezi hilo"

Na kama mkihofia ugomvi ulio baina yao, basi wekeni mwamuzi mmoja katika watu wa mume na mwamuzi mmoja katika watu wa mke.

Aya iliyotangulia imeonyesha uasi wa mke; na Aya hii inaonyesha uasi wa mke na mume kwa kutokutekeleza kila mmoja wao haki ya mwingine.

Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:Mkihofia ugomvi ulio baina yao anakusudia kuhofia kuendelea ugomvi; na dhamiri katika 'mkihofia' na 'wekeni' inaelekezwa kwa makadhi. Amri ya kuwaweka waamuzi wawili ni ya sunna, siyo ya wajibu, lengo lake ni kupatikana suluhu, na kuhifadhi familia kwa kuhofia watoto wasipotee.

Ni sharti kwa mwamuzi awe na uwezo wa kusuluhisha; Kwa sababu (kuna msemo) 'asiye nacho hatoi.' Pia inafaa kuwa si katika jamaa; kwa sababu udugu si sharti katika uamuzi wala katika uwakili. Umetajwa udugu katika Aya kwa kuwa ni bora tu, sio kwa ulazima. Kwa sababu wao wanajua hali kwa undani zaidi, wenye huruma na wanaoweza kuficha siri.

Kazi ya waamuzi wawili ni kutafuta suluhu. Wakishindwa wampelekee Kadhi wamueleze hali ilivyo na maoni yao kwa masilahi ya pande zote mbili, wala hawana haki ya kuwatenganisha ila kwa idhini ya mume, wala mke kuachishwa ila kwa matakwa yake.

Wakitaka suluhu basi Mwenyezi Mungu atawawezesha

Wametofautiana wafasiri katika dhamiri ya 'wakitaka' kuwa inawarudia kina nani? Imesemekana kuwa dhamiri ya kutaka inawarudia waamuzi wawili, na dhamiri 'kuwawezesha' inawarudia mke na mume; na maana iwe: Waamuzi wakitaka suluhu, basi Mwenyezi Mungu atawawezesha mke na mume.

Lakini hayo yako mbali kabisa; Kwa sababu ilivyo ni kuwa wanalotaka waamuzi ni suluhu, vinginevyo wasingekuwa waamuzi.

Pili : Ni kuwa waamuzi wanaweza kutaka suluhu na tawfiki isipatikane ambapo Mwenyezi Mungu anasema:Wakitaka suluhu atawawezesha , kuonyesha ni wajibu kupatikana Tawfiq (kuwezeshwa) mara tu baada ya kutaka suluhu kutoka kwa waamuzi.

Ilivyo hasa ni kwamba dhamiri zote mbili zinawarudia mke na mume. Maana yake ni ikiwa mke na mume wakiwa na nia safi, kwa kukusudia ndoa yao iendelee na kuilinda familia, basi kazi za waamuzi zitaleta natija; na Mwenyezi Mungu bila shaka atawawezesha mume na mke; Kwani nia ikitengemaa mambo nayo hutengemaa. Na kama nia ya mume na mke ikiwa mbaya basi kazi ya waamuzi nayo haitafaulu, hata kama watakusudia usuluhishi kwa juhudi zao zote.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja uasi wa mke; kisha uasi wa mume na mke na wala hakutaja wa mume tu. Lakini mafakihi wameliingilia hilo na wakasema: "Mume akimwasi mke na akaacha kumtekelezea haki zake atamuonya; akikubali sawa, la si hivyo hawezi kumwacha peke yake kitandani wala kumpiga, kama anavyofanyiwa yeye akiasi; hata kama ataona kufanya hivyo kutaleta manufaa; Kwa sababu kufanya hivyo kunahitaji idhini ya sharia ambayo haiko kwa mke, isipokuwa lake la kufanya ni kwenda kumshtaki kwa Kadhi.

Na ni wajibu wa Kadhi kuthibitisha na kubainisha. Ikimthibitikia uasi wa mume, basi atamkataza, akirudia atamwaziri vile atakavyoona yeye; ikiwa ni kumshutumu au kumpiga au kumfunga gerezani.

Ikiwa ataacha kumtunza mkewe na ana uwezo, inajuzu kwa kadhi kuchukua mali ya mume na amlishe mke; hata ikiwa ni kwa kuuza kitu katika milki yake.

﴿وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا﴾

36.Na mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote, na watendeeni wema wazazi wawili na jamaa wa ukoo na mayatima na maskini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na msafiri na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia; Hakika Mwenyezi Mungu hapendi mwenye kiburi ajivunaye, Ikiwa hana kitu basi - kuna rai ya kuwa - kadhi anaweza kumlazimisha kutoa talaka, ikiwa mke atataka talaka, Hayo yametangulia kuelezwa nyuma.

KUWATENDEA WEMA WAZAZI WAWILI

Aya 36

MAANA

Na mwabuduni Mwenyezi Mungu

Hakuna kitu cha kumwabudu Mwenyezi Mungu kilicho bora zaidi kuliko kupigania na kufa shahid kwa ajili ya haki; uhuru na ubinadamu. Ama kutafuta elimu na kufanya kazi kwa ajili ya maisha, kusaidia mambo ya kheri na kupatanisha watu waliokosana ni bora kuliko Swala zote na Saumu zote; kama iliivyoelezwa katika Hadith.

Wala msimshirikishe na chochote.

Kuukana uungu ni ukafiri; na kumshirikisha Mungu kuko aina mbili; Kumshirikisha katika Uungu; kama vile kuamini kuwa mwenye kuumba na kuruzuku ni zaidi ya mmoja. Miongoni mwa ushirikina huu ni kuitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ana mawaziri, wasaidizi na washauri.

Aina nyingine ya ushirkina ni katika utiifu; huko ni kuamini kuwa muumba, mwenye kuruzuku ni mmoja hana mshirika wala msaidizi, lakini ukawa unamwasi kwa kumtii kiumbe kwenye jambo ambalo halitamridhisha Mwenyezi Mungu, Vilevile miongoni mwa ushirikina ni kumridhia mtawala dhalimu, waziri au naibu wake mwenye hiyana, na kadhi mjinga aliye mwovu, na yeyote anayesimamia mambo ya umma ambayo hana ujuzi nayo. Kuna Hadith isemayo 'Mwenye kuwaridhia watu kwa mambo wayafanyayo basi yu pamoja nao.'

Na watendeeni wema wazazi wawili

Mara nyingi Mwenyezi Mungu hukutanisha wajibu wa kuabudiwa kwake na wa kutendewa wema wazazi wawili, katika Aya kadha; kama vile:

﴿وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا﴾

"Na Mola wako amehukumu kuwa msimwabudu yeyote isipokuwa yeye tu, na kuwafanyia wema wazazi wawili; kama mmoja wao akifikiliwa na uzee, naye yuko kwako, au wote,basi usiwaambie hata Ah! Wala usiwakemee na useme nao kwa msemo wa heshima" (17:23)

Aya nyingine ni ile isemayo:

﴿أَنِ اشْكُرْ لِي وَلِوَالِدَيْكَ إِلَيَّ الْمَصِيرُ﴾

"kwamba unishukuru mimi na wazazi wako wawili; ni kwangu mimi marejeo" (31:14)

Miongoni mwa dua za Imam Zainul-abidin kwa wazazi wake ni: "Ewe Mola wangu! Ni urefu ul ioje wa kunishughulikia (wazazi) wangu kunilea! Ni tabu ilioje waliopata kunilinda! Na ni kujinyima kulikoje kwao kwa ajili ya kunitosheleza! Haiwezekani kwangu mimi kuwatekelezea haki zao, wala siwezi kutekeleza wajibu wangu kwao au kuwalipa huduma zao.

"Na jamaa wa ukoo

Hao ni kama ndugu wa kuzaliwa nao, ami n.k. Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha kuwafanyia wema wazazi wawili, hapa ameamrisha kuwafanyia wema ndugu kisha nimayatima na maskini . Hata kama si jirani kwa sababu yatima hana wa kumsaidia, yaani baba. Na kwamba maskini hawi sawa kijamii ila kwa kusaidiwa. Masikini anayehitajia kusaidiwa, ni yule dhaifu asiyeweza kuchuma.

Ama kumsaidia mwenye kuweza kufanya kazi lakini akawa ni mvivu, ni kuchochea uduni uzembe. Kuna Hadith isemayo: "Hakika Mwenyezi Mungu humpenda mja anayefanya kazi na humchukia mvivu." Wanafunzi walimwuliza Nabii Isa: "Ni nani mbora zaidi katika sisi" Akasema: "Mbora wenu zaidi ni yule anayefanya kazi kwa mkono wake na kula kwa chumo lake.

"Na jirani wa karibu na jirani wa mbali na rafiki wa ubavuni na msafiri na waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia.

Rafiki wa ubavuni ni yule mwenzako safarini, unayekaa naye mjini, unayesoma naye darasani au unayefanya kazi naye n.k. Msafiri hapa ni yule aliyeharibikiwa safarini.Waliomilikwa na mikono ni watu ambao hawako hivi sasa (watumwa).

Kufanya wema sio lazima kutoa mali tu, bali ni pamoja na kufanyiana upole, unyenyekevu, kujishughulisha kutimiza mahitaji yao kushauriana na kuficha siri. Pia ni pamoja na kuzifumbia jicho aibu za watu, kutotangaza ubaya wa watu, kuazimana vifaa na mengineyo mfano wa hayo. Kwa vyovyote ni kuwa amri ya kuwafanyia wema wote hawa ni Sunna si wajibu.

Hakika Mwenyezi Mungu hapendi mwenye kiburi ajivunaye

Hili ni kemeo kwa mwenye kujitenga na jamaa zake walio mafukara na jirani zake.

﴿الَّذِينَ يَبْخَلُونَ وَيَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبُخْلِ وَيَكْتُمُونَ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا﴾

37.Ambao hufanya ubakhili na huwaamuru watu kufanya ubakhili, na wakayaficha aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake, Na tumewaandalia Makafiri adhabu yenye kudhalilisha.

﴿وَالَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ رِئَاءَ النَّاسِ وَلَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَمَن يَكُنِ الشَّيْطَانُ لَهُ قَرِينًا فَسَاءَ قَرِينًا ﴾

38.Na wale ambao wanatoa mali zao kwa kuonyesha watu wala hawamwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho, Na ambaye shetani amekuwa ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya.

﴿وَمَاذَا عَلَيْهِمْ لَوْ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقَهُمُ اللَّـهُ وَكَانَ اللَّـهُ بِهِمْ عَلِيمًا﴾

39.Na ingeliwadhuru nini lau wao wangelimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakatoa katika aliyowaruzuku, na Mwenyezi Mungu anawajua.

HUFANYA UBAKHILI NA KUAMRISHA WATU KUUFANYA

Aya 37 -39

MAANA

Ambao hufanya ubakhili na huwaamuru watu kufanya ubakhili. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kutoa na kufanya hisani katika Aya iliyotangulia, katika Aya hii anamkemea yule anayefanya ubakhili na akaamrisha wengine wafanye ubakhili. Kila bakhili huwaamrisha watu kufanya ubakhili; bali kila mwovu hupendelea kupata wafuasi, ili asiwe peke yake katika uovu na asisemwe vibaya. Kimsingi ni kwamba mwizi hukiboresha kitendo cha wizi na kukifanya halali, bali hata huongeza kukifanya.

Sijaona kitu kinachokubaliwa haraka na nafsi kama amri ya ubakhili na kuzuia kutoa. Kwa sababu mali ni tamu sana rohoni, wala si rahisi - mara nyingi - kutoa hata kidogo, isipokuwa kwa juhudi kubwa. Kwa hiyo amri ya kuzuwia inaungana na matamanio ya nafsi na kuitikiwa kwa haraka na ni nyepesi.

Sheikh Muhammad Abduh katika kufasiri Aya hii anasema: "Wenye kuamrisha ubakhili wana nguvu ya kutia shaka, hata waliwahi kuniathiri; nikawa ninarudisha pesa mfukoni baada ya kuzitoa. Kwa sababu wasiopenda kutoa walikuwa wakiniambia: Huyu hastahili kupewa na kumpa kitu ni kupoteza; kama utatoa mali mahali pengine itakuwa bora zaidi."

Ukweli ni tulioueleza kwamba amri ya ubakhili inamwathiri mtu anapoitikia matamanio ya nafsi yake, si kwa kauli ya wabakhili na shaka shaka zao. Kwani mtukufu ni yule anayeyashinda matamanio na nafsi yake na kuyalazimisha kukubali mambo mazito yakiwa na kheri na utengeneo. Imam Ali(a.s) anasema:"Amali bora ni ile unayoilazimisha nafsi yako juu yake." Hadith inasema:"Amali bora ni ile iliyo nzito zaidi."

Na wakaficha aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila Yake

Fadhila za Mwenyezi Mungu zinakusanya kila neema, ikiwemo mali na ilimu. Kuficha ilimu ni haramu na kuieneza ni wajibu, lakini kwa mfumo wa kuvutia sio wa kuchukiza na unaokurubisha sio kuweka mbali. Kwa sababu ilimu ni nyenzo na kuitumia ni lengo.

Baadhi ya maulama wamesema: "Tajiri akificha utajiri wake na akajifanya ni fukara mbele za watu basi atakuwa amefanya haramu." Wametoa dalili kwa Aya isemayo:

"Na neema ya Mola wako izungumze" (93:11)

Kuna Hadith isemayo:"Mwenyezi Mungu akimneemesha mja neema yoyote hupendelea ionekane athari ya neema yake."

Na tumewaandalia makafiri adhabu yenye kudhalilisha

Mfumo wa Aya unafahamisha kuwa makusudio ya Makafiri hapa ni wale ambao wameficha fadhila za Mwenyezi Mungu na neema yake.

Imepokewa kutoka kwa Imam Jafar as-Sadiq(a.s) Kwamba yeye amesema:"kuzizungumza neema za Mwenyezi Mungu ni kushukuru na kuacha kuzizungumza ni kufuru." Mwenyezi Mungu anasema:

﴿وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴾

"Na alipo tangaza Mola wenu Mlezi: Kama mkishukuru nitawazidishia, na kama mkikufuru basi adhabu yangu ni kali sana." (14:7)

Kwa hivyo basi kufuru katika Aya hii inachukuliwa kuwa ni kukufuru neema, sio kumkufuru Mwenyezi Mungu.

Na wale ambao hutoa mali yao kwa kuonyesha watu wala hawaamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho.

Imetangulia Aya kama hii na tafsiri yake katika Sura ya Baqara (2:264). Kwa ufupi ni kuwa ambaye anatoa mali yake kwa ria (kujionyesha) na yule anayefanya ubakhili ni sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Na huenda mwenye kujionyesha akawa na hali mbaya zaidi. Kwa sababu yeye ni kama kafiri ambaye hafanyi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

RAFIKI WA SHETANI

Kila kinachoshawishi kitendo cha uovu, kuhadaa kufanya ufisadi na upotevu, unaweza kukiita shetani; iwe ni mawazo, mtu au kitu chochote. Neno shetani ni nembo ya kila mpotevu aliye mpotezaji, Anaficha hakika yake chini ya nguo za watu wema. Kwa ajili hii ndipo tukawaona watu wengi wanasema na kutenda kutokana na mwongozo wa kishetani na upotevu na wao wenyewe wanahisabu kuwa ni mwongozo kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aliye karibu zaidi na shetani ni yule ambaye watu humwamini kwa utakatifu wake, na hawajui hakika yake. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

Na ambaye shetani amekuwa ndiye rafiki yake, basi ana rafiki mbaya, na kauli yake:

﴿وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا﴾

"Na mwenye kufanya shetani ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi amepata hasara iliyo wazi." (4:119).

Kama ilivyokuwa shetani ni rafiki yake duniani, basi akhera pia ni rafiki yake vile vile. Kuna Hadith isemayo: 'Mtu yuko pamoja na anayempenda,' Shetani anawagawanya wafuasi wake kwenye mafungu na kuwapa majukumu yao; kama afanyavyo kamanda wa jeshi.

Wengine wanapoteza watu kwa kumwaga damu na kuyaingilia mataifa yenye amani; kama vile mataifa yaliyotengeneza Israel na kuipa mali na silaha kwa ajili ya kuwachokoza Waarabu na miji ya Kiarabu, si kwa lolote ila wawatawale kisiasa na kiuchumi.

Wengine kazi yao ni kuhadaa kwa ufasiki na uovu na kuvunja heshima. Wengine wanawaamrisha kuswali, kujivika nguo ya watu wema na wasiotaka mambo ya dunia, ili waweze kuwapata watu wema.

Ikiwa wameshindwa na wanaomcha Mungu na wakachoka na hila zao, basi huwa radhi kuwahadaa japokuwa kwa tamko la haki atakalolisema mtu kwa matakwa ya Iblis. Kuna riwaya kwamba Iblis alimwambia Isa bin Maryam(a.s) : "Sema: Lailaha illa Ilah," Isa akamwambia nitasema lakini si kwa matakwa yako, bali kwa kuwa ni neno la haki, Basi mlaanifu (Iblis) akawa dhalili. Hekaya hii inaonyesha kuwa imani haiwi kwa tahalili na takbira, wala kwa kufunga na Swala. Kwani yote hayo yanaweza kuwa ni mitego ya shetani na vitimbi vyake. Isipokuwa imani ya kweli hupimwa kwa namna ya kumjua Mwenyezi Mungu na hekima zake; na kujua milango ya shetani ambayo inaharibu ikhlasi ya muumin na amali yake.

Na ingeliwadhuru nini lau kama wao wangelimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakatoa katika aliyowaruzuku Mungu.

Mwenyezi Mungu ameunganisha baina ya kumwaini Yeye, kuamini Siku ya Mwisho na kutoa, kwa sababu bakhili anayeng'ang'nia amemtoa katika imani. Maana yake nikuwa kutoa ni dalili ya imani na ubakhili ni dalili ya ukafiri.

Hilo ni kwa sababu muumini anayemtegemea Mungu kikweli kweli hutoa akiwa anaamini badali atakayopata. Na mwenye kuyakinisha badali hutoa bila ya pingamizi; kama alivyosema Imam Ali(a.s) . Ama mwenye imani dhaifu humsikiliza shetani wake anayemwamrisha kuzuia na kumhofisha na ufukara kama akitoa.

Hata hivyo makusudio ya imani hapa ni imani ya utiifu na matendo sio imani ya itikadi; na ukafiri ni ukafiri wa utiifu na matendo sio wa kumkanusha Mwenyezi Mungu.

Miongoni mwa kauli za Imam Ali kuhusu ubakhili ni: "Namsatajabia bakhili anayeharakia ufukara alioukimbia na kuacha umpite utajiri alioutaka Anaishi duniani maisha ya kifukara na akhera anahisabiwa ni tajiri." Maana ya kuwa tajiri anakimbilia ufukara ni kuwa yeye ana hali mbaya kuliko fukara. Kwa sababu tajiri huwa anahofia utajiri wake utamwondokea, lakini fukara huwa na matarajio ya kuondoka ufukara wake.