TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO15%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 19935 / Pakua: 4434
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

Mwandishi:
Swahili

1

2

3

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO

﴿إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ وَإِن تَكُ حَسَنَةً يُضَاعِفْهَا وَيُؤْتِ مِن لَّدُنْهُ أَجْرًا عَظِيمًا﴾

40.Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu (hata) uzani wa chembe. Na liwapo (jambo) ni jema huzidisha na hutoa kutoka kwake malipo makubwa.

﴿ فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا ﴾

41.Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi na tukakuleta kuwa shahidi juu ya hawa.

﴿يَوْمَئِذٍ يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَعَصَوُا الرَّسُولَ لَوْ تُسَوَّىٰ بِهِمُ الْأَرْضُ وَلَا يَكْتُمُونَ اللَّـهَ حَدِيثًا ﴾

42.Siku hiyo watatamani waliokufuru na kumwasi Mtume ya kuwa ardhi isawazishwe juu yao, wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na mazungumzo (yao).

MWENYEZI MUNGU HADHULUMU HATA UZANI WA CHEMBE

Aya 40 - 42

LUGHA

Uzani ni uzito hata ukiwa mchache, na chembe ni zile zinazopatikana kwenye miili; na hapa zimekuja kufananisha uchache. Kwenye Aya nyingine uchache umefananishwa na hardali.

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu (hata) uzani wa chembe.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuamrisha aabudiwe, kuwafanyia wema wazazi wawili na jamaa, kushutumu ubakhili na kutoa kwa ria na mwenye kuficha fadhila za Mwenyezi Mungu na kuwapa kiaga marafiki wa shetani, baada ya hayo anabainisha tena kwa kutilia mkazo kwamba yeye hampunguzii yeyote katika malipo yake hata chembe, hata kama ni uzani wa chembe ya vumbi; bali huzidisha thawabu za wenye kufanya wema, akasema:

Na liwapo ni jema hulizidisha na hutoa kutoka kwake malipo makubwa.

Kusema 'kutoka kwake' ni ishara kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu, humpa mwenye kufanya wema kwa wema wake kisha humzidishia bahashishi.

Wanafalsafa wana kauli katika hili kuwa, je, Mwenyezi Mungu humpa thawabu mtiifu kwa kuwa ni lazima anastahiki, kiasi ambacho kama hatampa, basi Mwenyezi Mungu atakuwa dhalimu - Mungu ametaka na hilo- au ni kwa njia ya fadhila na hisani tu?

Tuonavyo lililo karibu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu hutoa thawabu kwenye wajibu kwa njia ya fadhila tu, Kwa sababu hakuna malipo wala shukrani kwenye tendo la wajibu. Ama mambo ya Sunna hutoa thawabu kwa kustahiki. Lakini kwa vyovyote ilivyo ni kuwa thawabu ziko hakuna shaka. Kwa hiyo mzozo wa kuwa sababu yake ni hisani au kustahiki ni mzozo tasa, maadamu sababu iko nje ya uwezo.

Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi na tukakuleta kuwa shahidi juu ya hawa?

Kesho Mwenyezi Mungu atawakusanya watu kwa ajili ya hisabu na adhabu. Kabla ya chochote ataushuhudiza kila umma na Mtume wao, kwamba amewafikishia ujumbe wa Mola wake na akawafundisha halali na haramu moja kwa moja; au kupitia sahaba zake, au wafuasi wao au wanavyuoni na mafakihi.

Kwa hiyo makusudio ya shahidi wa kwanza ni kila Mtume aliyemtangulia Muhammad na shahidi wa pili ni Muhammad(s.a.w.w) : Na neno 'hawa' ni umma wa Muhammad.

Umbali zaidi ni ule wa mwenye kusema kwamba neno 'hawa' ni Mitume wote waliotangulia na kwamba Muhammad atatoa ushahidi juu yao na wao watatoa ushahidi juu ya umma wao. Ameweka mbali msemaji huyu, kwa sababu ushahidi unajuzu kutolewa na kusikizwa juu ya ambaye anaweza kupuuza wajibu wake.

Tulipofasiri sura ya Baqara (2:143) tumetaja kwamba Muhammad(s.a.w.w) anatoa ushuhuda kwa maulama wa umma wake kwamba yeye amewafikishia Uislam na hukumu zake na ulama wa umma washuhudie kwamba wao wamefikisha risala ya Uislam kwa njia yake.

Sheikh Muhammad Abduh, katika kufasiri Aya hii, amesema kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) kesho atalinganisha baina ya itikadi ya kila umma, amali yake na hulka zake, na itikadi ya Mtume wake, Ikiwa ndiyo hiyo hiyo, basi umma utakuwa umeokoka, vinginevyo utakuwu umeangamia.

Tafsiri hii ni miongoni mwa mapinduzi yake juu ya uzushi na kufuata. Nayo haiko mbali sana na hali halisi. Kwani ulinganisho huu kama hautatokea mbele ya Muumba Mtukufu, lakini natija yake itapatikana tu.

Siku hiyo watatamani waliokufuru na kumwasi Mtume ya kuwa ardhi isawazishwe juu yao.

Yaani Makafiri watapofunuliwa pazia siku ya Kiyama, watatamani lau kwamba wao wasingeliumbwa, bora wangekuwa sawa na mchanga; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

﴿ يَوْمَ يَنظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا ﴾

"Siku ambayo mtu ataona kilichotangulizwa na mikono yake, na Kafiri atasema: Laiti ningelikuwa mchanga." (78:40)

Wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na mazungumzo (yao).

Haya ni maneno yanayoanza upya, na maana yake ni kuwa wao hawataweza kuficha dhambi yoyote miongoni mwa dhambi zao walizozifanya na kufichika katika macho ya watu hapa duniani. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewazunguuka na amali zao.

Na kwamba Malaika, masikio yao, macho yao, ndimi zao, ngozi zao, mikono yao na miguu yao, vyote vitashuhudia yale waliyoyafanya:

﴿حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴾

"Hata watakapoufikia (moto) yatashuhudia masikio yao na macho yao na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda." (41:20).

﴿يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴾

"Siku ambayo zitashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda." (24:24).

Ewe Mwenyezi Mungu mhurumie kwa uadilifu wako ambaye hana uwezo, Na mwokoe ambaye hana uokovu zaidi ya msamaha wako.

Unaweza kuuliza : Utaunganishaje baina ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wala hawatamficha Mwenyezi Mungu na neno lolote" na kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿وَيَوْمَ نَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ نَقُولُ لِلَّذِينَ أَشْرَكُوا أَيْنَ شُرَكَاؤُكُمُ الَّذِينَ كُنتُمْ تَزْعُمُونَ ﴿٢٢﴾ ثُمَّ لَمْ تَكُن فِتْنَتُهُمْ إِلَّا أَن قَالُوا وَاللَّـهِ رَبِّنَا مَا كُنَّا مُشْرِكِينَ﴾

"Na siku ambayo tutawakusanya wote pamoja kisha tuwaambie wale walioshirikisha: Wako wapi washirikishwa wenu mliokuwa mnadai. Kisha hautakuwa udhuru wao isipokuwa kusema: Wallahi Mola wetu hatukuwa washirikina." (6: 22-23)

Jibu : Inawezekana kuwa makusudio yao ni kwamba wao katika itikadi yao hawakuwa washirikina. Tukutane wakati wa kufasiri Sura hiyo ya sita (An'am) inshaallah.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَقْرَبُوا الصَّلَاةَ وَأَنتُمْ سُكَارَىٰ حَتَّىٰ تَعْلَمُوا مَا تَقُولُونَ وَلَا جُنُبًا إِلَّا عَابِرِي سَبِيلٍ حَتَّىٰ تَغْتَسِلُوا وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُمْ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا غَفُورًا ﴾

43.Enyi mlioamini, msikaribie Swala na hali mmelewa mpaka myajue mnayoyasema; wala mkiwa na janaba - ispokuwa wapita njia - mpaka muoge. Na muwapo wagonjwa au mko safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara; mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe mwenye kughufiria.

MSIKARIBIE SWALA MKIWA WALEVI

Aya ya 43

MAANA

Enyi mlioamini, msikaribie Swala na hali mmelewa mpaka myajue mnayoyasema; wala mkiwa na janaba - ispkuwa wapita njia - mpaka muoge.

Hapa kuna masuala kadhaa

1. Msemo huu unaelekezwa kwa Waislamu kabla ya kubainishwa hukumu ya kuharimishwa pombe kulikoelezwa katika Sura ya Maida (5: 90 - 91) na katika A'raf (7:32). Zikiungana na Baqara (2:219) ambayo tumeyaelezea hayo kwa ufafanuzi kabisa. Pia tumeeleza hayo katika kitab Fiqhul-Imam Jafar as-Sadiq(a.s) mlango wa vyakula na vinywaji.

Ilivyo hasa ni kwamba kukatazwa mtu kuswali hali ya kuwa amelewa hakufahamishi kwamba ni halali katika isiyokuwa Swala; kwa mfano ukisema: Usiwaangalie wanawake ukiwa unakwenda njiani hakufahamishi kuwa inafaa kuwaangalia ukiwa ukumbini. Kwa maneno mengine ni kuwa Aya imefahamisha uharamu wa Swala katika hali ya kulewa, na kunyamzia hukumu ya kulewa mahali pengine.

2. Wametofautiana (wafasiri) kuhusu makusudio ya Swala, je ni Swala yenyewe au msikiti ambao Swala iko ndani yake, kwa kuangalia desturi ya kutumia hali kwa mahali; kama kutumia jina la kahawani kwa maana ya mahali panaponywewa kahawa, Lakini wafasiri wengi wameelemea kwenye maana ya kwanza. Na hilo ni wazi zaidi kuliko kuwa ni msikiti.

3. Wametofautiana vilevile kuwa je, makusudio ya kulewa ni kulewa pombe au usingizi? Kwa dhahiri ni kulewa kileo sio usingizi.

4. Baadhi ya wapokezi wamesema kwmba kundi la Maswahaba walikusanyika kwa mmoja wao akawatengenezea chakula na pombe- Kabla ya kubainishwa hukumu ya pombe - Wakala na wakanywa. Walipolewa ukaingia wakati wa Swala; mmoja wao akawaswalisha; akakoroga Swala na akageuza Aya za Qur'an.

Sheikh Muhammad Jawad Balaghi[4] katika tafsir yake Alaurrahman amefuatilia na kuthibitisha uongo wa riwaya hizi moja baada ya nyingine. Kwa ufupi natija ya utafiti wake mkali ni kwamba Tirmidhi amepokea kuwa aliyewaita wenzake ni Abdul-rahman bin Auf na Ali ndiye aliyekuwa Imam. Abu Daud akapokea kuwa aliyealika ni mtu mmoja katika Ansari na Abdul-rahman alikuwa miongoni mwa waalikwa. Ibn Jarir Tabari amesema katika tafsir yake na Suyuti katika Durril-manthur wamesema kuwa Imam wa jamaa alikuwa ni Abdul-rahman bin Auf.

Miongoni mwa mambo yake ya kutokuwa na ubinafsi na kumwelekea kwake Mungu peke yake, alikuwa haweki jina lake katika vitabu vyake alivyovitunga katika maisha yake. Alipoulizwa sababu yake akasema: "Huenda nikakosea katika baadhi ya niliyoyasema, akatusi - yule mwenye maradhi moyoni mwake - taifa langu kwa sababu yangu, "Alikufa ulama huyu mwaka 1352 A.H.

Vile vile katika Durril-manthur… imesemwa kuwa Aya imeshuka kwa Abu Bakr, Umar, Ali, Abdul-rahman na Saad, na kwamba aliyewaalika wenzake ni Ali. Katika Musnad ya Ahmad na Nassai kwamba Umar alisema: "Ewe Mola tubainishie kuhusu pombe;" ndipo ikashuka Aya hii.

Mbali ya kugongana riwaya katika mwalishi, Imam na Maamum, vile vile riwaya zimegongana na kupingana kuhusu Aya iliyovurugwa. Kuna riwaya inayosema kwamba Imam Alisema: "Ninaabudu mnachokiabudu." Riwaya nyingine ikasema kuwa alisoma: "Sina dini."

Vile vile riwaya zimetofautiana kuhusu wakati wa kushuka Aya hiyo na sababu yake. Zaidi ya hayo yote mwenye Alaurrahman amethibtishia kuwa mwenye riwaya ya kwanza, ambaye amesema kuwa Imam wa jamaa alikuwa ni Ali, alikuwa ni Kharij na ni katika madui wakubwa wa Ali.

Kwa vyovyote iwavyo ikiswihi kuwa kikundi cha maswahaba walikunywa pombe na kwamba Imam wao alikoroga Swala yake; basi watakuwa ni wale ambao waliwahi kumshirikisha Mwenyezi Mungu, wakaabudu masanamu, wakanywa pombe na kula nyama za haramu katika ujahiliya waliokulia ndani yake na kulelewa,. Na Ali bin Abu Twalib hakuwa katika wao. Yeye alikulia katika malezi ya Mtume(s.a.w.w) , tangu utoto wake na akamrekebisha vile atakavyo.

Huenda mtu akasema : Kauli yako hii inatokana na mwongozo wa kiitikadi sio mwongozo wa matukio yalivyo.

Jibu : Hukumu ambayo inategemea makuzi ya mtu na malezi yake inatokana na mwongozo wa haki na matukio yalivyo. Sio mwongozo wa mawazo na itikadi.

Wala mkiwa na janaba - ispokuwa wapita njia - mpaka mwoge.

Imesemekana kuwa makusudio ya'mpita njia' ni msafiri; na kwamba maana yake, msikurubie Swala mkiwa mmelewa wala mkiwa na janaba ila katika hali ya safari. Ikumbukwe kwamba Aya imeeleza hukumu ya wasafiri pale iliposemwa:"Na muwapo wagonjwa au mko safarini."

Basi tukifasiri mpita njia kwa maana ya msafiri, italazimika kukaririka katika jumla moja bila ya dharura yoyote.

Pili : Kuna Hadith zilizofasiri 'mpita njia' kwa maana ya kupita msikitini; kwamba ni haramu kwa mwenye janaba kuingia msikitini, ila anayepita tu, isipokuwa Masjidul-haram (wa Makka) na Masjidun nabawi (wa Madina), haijuzu kabisa kuingia katika misikiti hiyo hata kwa kupitia.

Madhehebu mane yamesema kuwa mwili wote utakapoenea maji,basi litakuwa sahihi josho la janaba (janaba limeondoka), bila ya kuangalia kuanzia juu au chini.

Shia Imamia wameligawanya josho la janaba kwenye aina mbili; La mpango (tartib) na la kujivika (irtimasi), mpango kwao ni kujimiminia maji; wakawajibisha katika hali hii kuanza kichwa, kisha upande wa kuume na hatimaye kushoto, Lau atafanya kinyume, basi josho limebatilika.

Ama la kujivika ni kuuvika mwili wote ndani ya maji kwa mpigo mmoja; kama vile kuoga baharini, mtoni n.k.

MGONJWA NA MSAFIRI KATIKA TAYAMMAM

Na muwapo wagonjwa au mko safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni, au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara, mpake nyuso zenu na mikono yenu.

Zimegongana kauli za wafasiri katika Aya hii, mpaka Sheikh Muhammad Abduh akasema: "Nimeangalia tafsiri ishirini na tano, sikupata cha kutesheleza wala kauli ya kuondoa taklifa." Alusy naye katika Rawhul-bayan akasema: "Aya hii ni katika Aya zinazotatanisha."

Na sisi tumerejea kiasi tafsiri ishirini za Sunni na Shia. Wengi wa wafasiri wake wamenakili tafsiri kadhaa, tukaona kama alivyosema Sheikh Muhammad Abduh, lakini hatukuona utatanishi wowote au mushkeli wowote, kama alivyoona Alusy. Baada ya kutegemea maana yake na makusudio, tumejaribu kuifafanua kwa mfumo huu ufuatao:

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya watu aina nne:

Wagonjwa, wasafiri, waliotoka chooni na waliowagusa wanawake (makusudio ya kuwagusa wanawake ni kuwaingilia). Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa wote hawa kuelekea kwenye tayammam wakati wa kuyakosa maji.

Katika mambo waliyoafikiana madhehebu yote ni kuwa dhahiri ya Qur'an haijuzu kuitegemea - hasa katika kutoa hukumu za sheria - ila baada ya kurudia kwenye Hadith za Mtume. Kwa sababu Hadith ni moja ya chimbuko la sharia; kama ambavyo ni maelezo na ubainifu wa Qur'an, kama ilivyosema Qur'an yenyewe: "Analowapa Mtume lipokeeni na analowakataza, basi jiepusheni.

﴿وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴾

Na mcheni Mwenyezi Mungu kwa hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu" (59:7)

Ikiwa haikupatikana Hadith inayoichambua dhahiri ya tamko la Aya basi ni wajibu kuitumia dhahiri. Vinginevyo itawajibika kufanya amali kwa tutakavyofahamu kutoka katika Kitabu na Hadith kwa pamoja. Kwa sababu zinatoka katika chemchemi moja, ambayo ni Wahyi.

Tutazungumzia kila moja ya aina nne zilizotajwa na Aya. Hapo tutapata ufafanuzi wa jibu la swali hili: Kuwa je kuna Hadith inayopingana na dhahiri ya Aya katika moja ya aina hizi nne?

1. Mgonjwa: Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa yeye atatayamum akikosa maji, Wamekongamana kutumia dhahiri hii. Kwa sababu hata ambaye si mgonjwa atatayammum kwa kukosa maji.

Na mgonjwa akipata maji lakini akahofia kuyatumia je,atatayammum? Au atatumia maji hata akiwa anahofia madhara?.

Wameafikiana mafakihi kwamba mgonjwa atatayammum hata ikiwa maji yapo akihofia kuyatumia, Wametoa dalili ya Hadith hii:"Hapana madhara wala kudhuriana." Na kwa isemayo kuwa sahaba mmoja alipatwa na janaba naye alikuwa na jeraha kubwa, Akawauliza wenzake wakamwamrisha kuoga alipooga akafa. Mtume aliposikia hilo akasema:"Wamemuua, Mungu awaue (nao)."

Kwa hiyo basi kauli yake Mwenyezi Mungu, kisha msipate maji; ni ya aina zote zilizotajwa katika Aya. Haya ndiyo maana yanayopatikana kwa uasili wa Aya, sio kwa kufuatiza.

Ama maana yanayopatikana kwa kufuatiza kwa kupatikana ambako mafaqihi na maulama wa Usul wanakuita 'ufahamu wa sharti'. Mafhumushart, ni kwamba unawajibisha kila mmoja katika aina nne kutumia maji akiyapata wala haijuzu kwake kutayamammu kwa hali yoyote ikiwa maji yapo; hata akidhurika kwa kuyatumia.

Lakini umekwisha fahamu kutokana na yaliyotangulia kwamba mafakihi wamekongamana na kwamba Hadith za Mtume, zimefahamisha kuwa: mgonjwa atatayammam hata kama maji yapo ikiwa anahofia madhara kwa kutumia maji. Kwa hivyo basi hapana budi kumtoa mgonjwa na maana haya ya kufuatiza: na kubakisha aina tatu ambao ni wajibu kwao kutumia maji, yakiwapo, kwa mujibu wa ufahamu huu wa kufuatiza.

Kwa ufupi ni kwamba wote wane watatayammam ikiwa wamekosa maji, hili halina shaka, Ama maji, yakiwapo basi atayatumia yule asiyehofia madhara ya kuyatumia. Ama yule anayehofia kuyatumia ataacha na atatayammam.

2. Msafiri: Aya inafamisha kuwa yeye atatayammam akikosa maji, iwe safari yake ni ndefu au fupi, Hivyo ndivyo waliyoafikiana wote.

Lakini wametofautiana katika asiyekuwa msafiri ambaye si mgonjwa, Je atayammam na kuswali au atasamehewa kuswali?.

Abu Hanifa amesema: Swala itamwondokea. Kwa sababu dhahiri ya Aya ni kwamba tayammam inajuzu katika safari sio mjini.

Madhehebu mengine yote yaliyobakia wameafikiana kuwa mwenye kukosa maji ni wajibu atayammam na kuswali, ni sawa awe msafiri au nyumbani, Kwa sababu kujuzu kutayammam katika safari hakuzuwii kujuzu nyumbani. Zimekuja Hadith mutawatir, kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: "Hakika mchanga ulio twahara, humtwahirisha Mwislam hata akikosa maji miaka kumi."

Abu Bakr aliye maarufu kwa jina la Ibn A-arabi katika kitabu Ahkamul-Qur'an Juz, 1 Uk. 176 chapa ya mwaka 1331 A.H alisema: "Hakika Abu Hanifa mara nyingi huacha dhahiri na nukuu (nassi) kwa kukisia." Unaweza kuuliza: Ikiwa msafiri na aliye mjini wana hukumu moja katika wajibu wa kuyatumia maji yaliyopatikana na kutayammam yakikosekana maji, kwa nini basi Qur'an imetaja safari hasa. Wamejibu kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameitaja safari kwa sababu ndio aghlabu katika safari kukosa maji. Ama mtu akiwa mjini ni nadra. Hili ndilo jibu la kudhania na kuonelea ni vizuri katika kauli ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu halitegemei Aya au riwaya mutawatir au hukumu inayotokana na akili, Kwa hivyo sisi tunalinyamazia.

3.Au akiwa mmoja wenu ametoka chooni . Ni kinaya cha kutokwa na mkojo, kinyesi au upepo. Basi mtu akitokwa na kimojawapo katika hivyo na akataka kuswali, ni juu yake kutawadha akipata maji na atatayammam akiyakosa. Hilo ni kwa kongamano la wanachuoni na Hadith (Ijmai na Sunna).

4.Au mkagusana na wanawake, ni kinaya cha kujamii (kumwingilia kimwili) Qur'an, imetumia kwa kinaya katika hilo bila ya kueleza wazi; kama vile:"Basi sasa changanyikeni nao" (2:187)"Wala msiwakurubie." (2:222)"Kabla hamjawagusa" (2:237)

Na Shafi amesema: "Makusudio ya kugusa katika Aya ni kule kugusana mwili." Kwa v yovyote iwavyo ni kwamba mwenye kuwa na janaba na akapata maji ni juu yake kuoga akitaka kuswali, Akikosa maji atatayammam badala ya kuoga. Kila linalowajibisha kutawadha, mafakihi wanaliita hadath ndogo na kila linalowajibisha kuoga wanaliita hadath kubwa.

Basi tayammamuni na mchanga ulio twahara.

Mchanga ni ardhi. Aya hii iko katika maana ya Hadith tukufu isemayo:"Nimeumbiwa ardhi kuwa ni msikiti na yenye kutwaharisha."

Mpake nyuso zenu na mikono yenu.

Madhehebu yote yameafikiana kuwa kutayammam hakuwi ila katika viungo viwili hivi; na wakatofautiana mpaka wa sehemu zinazopakwa mchanga katika uso na mikono miwili. Madhehebu mane yakasema: "Ni wajibu kupaka uso wote zikiwemo ndevu; sawa na ilivyo katika udhu. Katika mikono, Hanafi na Shafi wamesema ni wajibu kupaka mchanga mpaka kwenye vifundo vya mikono kama udhu."

Shia Imamia wamesema ni wajibu kupaka baadhi ya sehemu ya uso, sio uso wote. Kwa sababu herufi 'Ba' ni ya tabiidh (kufanya baadhi); sawa na ile iliyo katika udhu kuhusu vichwa. Kwa sababu kama isingekuwa ya tabiidh basi ingekuwa ya ziada; na asili ni kutokuwa ziada. Wakasema inafaa kupangusa viganja viwili tu. Ufafanuzi uko katika vitabu vya fiqh.

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يَشْتَرُونَ الضَّلَالَةَ وَيُرِيدُونَ أَن تَضِلُّوا السَّبِيلَ﴾

44.Je, huwaoni ambao wamepewa fungu katika Kitabu hununua upotevu na kuwataka mpotee njia?

﴿وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِأَعْدَائِكُمْ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ وَلِيًّا وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ نَصِيرًا ﴾

45.Na Mwenyezi Mungu anawajua sana maadui zenu; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa msaidizi.

﴿مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ وَيَقُولُونَ سَمِعْنَا وَعَصَيْنَا وَاسْمَعْ غَيْرَ مُسْمَعٍ وَرَاعِنَا لَيًّا بِأَلْسِنَتِهِمْ وَطَعْنًا فِي الدِّينِ وَلَوْ أَنَّهُمْ قَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَاسْمَعْ وَانظُرْنَا لَكَانَ خَيْرًا لَّهُمْ وَأَقْوَمَ وَلَـٰكِن لَّعَنَهُمُ اللَّـهُ بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا﴾

46.Miongoni mwa mayahudi wako ambao hugeuza maneno kutoka mahali mwake, na husema: tumesikia na tumeasi; na sikia bila kusikilizwa; na (husema) raina kwa kupondoa ndimi zao na kuitukana dini. Na lau kama wao wangesema: Tumesikia na tumetii na usikie na utuangalie, ingelikuwa heri kwao na sawa zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu amewaalani kwa kufuru zao, basi hawaamini ila wachache tu.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ آمِنُوا بِمَا نَزَّلْنَا مُصَدِّقًا لِّمَا مَعَكُم مِّن قَبْلِ أَن نَّطْمِسَ وُجُوهًا فَنَرُدَّهَا عَلَىٰ أَدْبَارِهَا أَوْ نَلْعَنَهُمْ كَمَا لَعَنَّا أَصْحَابَ السَّبْتِ وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ مَفْعُولًا﴾

47.Enyi mliopewa Kitab! Aminini tuliyoyateremsha yenye kusadikisha mliyo nayo nyinyi, kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni, au tukawalaani kama tuliivyowalaani watu wa Sabato (Jumamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kufanywa.

HUNUNUA UPOTEVU NA KUWATAKA MPOTEE

Aya 44 - 47

ISRAIL NA NGUVU YA SHARI

Je huwaoni ambao wamepewa fungu katika Kitabu hununua upotevu na kuwataka mpotee njia.

Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa makusudio ya waliopewa fungu katika Kitabu ni Mayahudi ambapo amewasifu Mwenyezi Mungu kwanza kwa upotevu; pale aliposema hununua upotevu, na pili kwa upotezaji pale aliposema: na kuwataka mpotee. Kisha akawasifu kwa ugeuzaji maneno, pale aliposema:hugeuza maneno kutoka mahali pake.

Historia haikujua watu walio wapinzani zaidi wa haki na maadui wa kheri kuliko Mayahudi. Wamekuwa wapotevu, wapotezaji na wageuzaji maneno, pale walipokuwa madhalili waliotawaliwa. Ama leo baada ya dola dhalimu kuwatengenezea wao koloni, hawakuacha upotevu, upotezaji na kugeuza maneno.

Bali wamekuwa ni nembo ya shari ya kimataifa na silaha na maangamizi aliyonayo kila mkoloni mkandamizaji, na ni kipimo cha kupambanua nguvu ya shari na uhaini na ile ya heri na ukombozi.

Hakuna dola yoyote ya kikoloni, wakati huu inayotaka kutawala watu, lazima itakimbilia Israel ndipo itaweza kutekeleza lengo lake, Taifa lolote dhalimu Mashariki na Magharibi lazima liombe msaada wa kuhami masilahi yake kwenye watu hawa dhalimu wenye dhambi.

Al-hamdulillah, dalili zimejionyesha waziwazi katika Vietnam za kumwandalia binadamu mpya atakayejua njia ya kummaliza adui wa haki na wa ubinadamu.

Binadamu wa leo[5] katika Vietnam na binadamu wa kesho mahali popote, atatofautiana na binadamu wa jana.

Yeye anaweza kumtofautisha mwenye haki na uhaini bila ya utatanishi, hata kama atakinaishwa mara elfu na ataweza kumweka kila mmoja mahali pake. Hapo binadamu ataweza kuishi bila ya matatizo na mabomu.

Matukio yamethibitisha - hasa lile balaa la tarehe 5 June 1967- kwamba matatizo ya waarabu na waislam chimbuko lake ni kuweko watu wasiostahiki kuwa viongozi, Hili litakwisha kadiri siku ziendavyo.

Na Mwenyezi Mungu anawajua sana maadui zenu; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa mlinzi na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa msaidizi.

Mungu anajua na sisi tunajua vile vile kuwa Mayahudi na wanaowategemea ni maadui wa haki na ubinadamu, wala sio jambo lililojificha kwa yeyote kuwa dola ya Israel ni nembo ya uovu ya kimataifa, lakini wengi wetu hawawajui vibaraka wanafiki.

Kwa sababu wao wanajificha kwenye nguo ya watu wema na kuwakanganya watu duni. Na iko siku watafichuka na Mwenyezi Mungu atawafedhehesha na kuing'oa mizizi yao kwa mikono ya waumini na wakombozi.

Miongoni mwa Mayahudi wako ambao hugeuza maneno kutoka mahali mwake

Aya zilizo katika mwelekeo huo ni kama hizi zifuatazo:

﴿وَمِنَ الَّذِينَ هَادُوا سَمَّاعُونَ لِلْكَذِبِ سَمَّاعُونَ لِقَوْمٍ آخَرِينَ لَمْ يَأْتُوكَ يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ مِن بَعْدِ مَوَاضِعِهِ﴾

"Na miongoni mwa Mayahudi wako wanaosikiliza kwa ajili ya uongo wanasikiliza kwa ajili ya watu wengine wasiokufikia; hugeuza maneno kutoka mahali mwake." (5:41)

﴿يَسْمَعُونَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ يُحَرِّفُونَهُ مِن بَعْدِ مَا عَقَلُوهُ وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴾

"Wanasikia meneno ya Mwenyezi Mungu kisha wanayageuza baada ya kuwa wameyafahamu" (2:75)

Ni sawasawa na walivyolifanyia azimio la Umoja wa Mataifa la ulazima wa Israel ku ondoka sehemu za Waarabu wanazozikalia kwa mabavu walizozivamia tarehe 5 June 1967 na wakaliita wajibu wa ushirikiano pamoja na Waarabu[6] .

Maneno yoyote yasiyoafikiana na makusudio maovu wanayabadilisha na mahali mwake hata kama wakijua na kufahamu kuwa yanatoka kwa Mwenyezi Mungu. Mwanzo waliibadilisha Taurati; mahali pa Aya ya uadilifu na rehema wakabadilisha na kuwa unyang'anyi na dhuluma na kuwaua wanawake na watoto.

Mwenye Tafsiri Al-manar, katika kufasiri Aya hii, amesema: "Wamethibitisha wanavyuoni kugeuzwa kwa vitabu vya agano la kale na jipya kwa ushahidi mwingi"

Katika kitab Idh'harul-haq cha Sheikh Rahmatullah (wa India) kuna ushahidi mia moja wa kugeuzwa kimaandishi na kimaana.

Kisha akataja mwenye Al-manar baadhi ya ushahidi huo katika Juz,5 Uk. 141 chapa 1328 A.H. Sheikh Jawad Al-balaghi naye akatung a kitabu madhubuti kilichokusanya maudhui haya, alichokiita Rihlatul-madrasiyya; na kimechapishwa mara kadhaa. Mtume(s.a.w.w) aliwapa Mayahudi wa Hijaz (Madina) mwito wa kuifuata haki na kuacha kuyabadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu, lakini wakaendelea kuwa na inadi; na husema tumesikia; na tumeasi; na sikiza bila kusikilizwa;

Yaani hutasikilizwa wala kuitikiwa mwito wako unaotulingania, Hilo si ajabu kwa watu wenye asili ya shari na chimbuko la ufisadi.

Na (husema) Raina kwa kupondoa ndimi zao na kuitukana dini.

Wafasiri wamesema kuwa Mayahudi walisema Raina wakiwa hawakusudii maana ya dhahiri ya tamko hili ya kuwachunga, Isipokuwa walikusudia ru'una yaani upumbavu, Na jambo hili ni kupotosha na kuitusi dini, Yamekiwshatangulia maelezo zaidi ya tamko Raina katika kufasiri Aya 104 ya Sura ya Al-Baqara.

Lau kama wao wangesema: Tumesikia na tumetii, na usikie na utuangalie, ingelikuwa ni heri kwao na sawa zaidi.

Kwa kuwa kauli hiyo ni ya sawa zaidi na bora na salama zaidi ndipo wakaiacha na wala wasiiseme.

Katika kufasiri Aya hii, Arrazi anasema: Maana ya kwamba wao ni sawa lau wangelisema: Tumesikia na tumetii, badala ya kusema: Tumesikia na tumeasi, Kwa sababu wao wanajua ukweli wako. Na badala ya kusema: Na sikiza bila kuzikizwa, wangesema na sikia tu. Vile vile badala ya kusema kwao Raina waseme Undhurna; yaani tupe muda kidogo ili tukufahamu; lau wangeliyasema yote haya ingelikuwa bora na sawa.

Lakini Mwenyezi Mungu amewalani kwa kufuru zao.

Na kuifanyia inadi haki na kung'angania batili, na laana ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake na machukivu yake.

Basi hawaamini ila wachache tu.

Tangu enzi na enzi watu kutoka mataifa mbali mbali na dini mbalimbali wameingia katika Uislamu kwa makundi, isipokuwa mayahudi tu. Walisilimu wachache sana; kama vile Abdillah bin salam na baadhi ya wafuasi wake. Bali wao mayahudi waliupiga vita uislam na waislam na bado wanaendelea kuu- fanyia vitimbi kwa nyenzo zote. Hii ni dalili kubwa kuwa uislamu ni haki na kweli. Jambo la kushangaza ni kwamba viongozi wa uislam na wanaoutolea mwito, hawakuutolea dalili utukufu wa Uislam na utu wake kwa uadui wa Mayahudi waliosema;"Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba." (5:64) Uadui wao ni kwa uilsam na kila mwenye kusema: "Lailahailla Ilah."

Enyi mliopewa Kitab! Aminini tuliyoyateremsha yenye kusadikisha mliyonayo nyinyi

Kwa dhahiri msemo unawakusanya mayahudi na manaswara, kwa vile wote ni watu wa Kitab. Imesemekana kuwa msemo unawahusu mayahudi kwa kuangalia mfumo wa maneno. Makusudio ya tuliyoyateremsha ni Qur'an tukufu, kwa sababu ndiyo inayosadikisha Taurat, kama ilivyoteremshiwa Musa(a.s) na Injil, kama ilivyoteremshiwa Isa(a.s) Mtume(s.a.w.w) aliwapa mwito, mayahudi, wa kuingia kwenye uislam kwa kuuzingatia kuwa ni haki kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akawapa dalili na hoja kila mara. Lakini wapi! Haki na hoja zake si chochote kwa mayahudi. Dini yao ni faida na mali tu; na hawatapata faida ya haraka haraka katika uislam wala katika Taurat, isipokuwa faida na utajiri wa haraka haraka wataupata katika ulanguzi, riba, kunyang'anya, kughushi, utapeli, umalaya, kamari, kuleta fitina, vita na mengineyo.

Kwa ajili hiyo ndio wao wamekua msitari wa mbele katika uwanja huu; na Mtume anajua fika hali hii, lakini aliwalingania ili kutimiza hoja tu:

"Na sisi si wenye kuwaadhibisha mpaka tuwapelekee Mtume" (17:15)

Kabla hatujazigeuza nyuso tukazipeleka kisogoni

Katika tafsir ya Aya hii, tumeona tafsir nne zenye kupingana. Yenye nguvu tuonavyo ni ile ya Sheikh Muhammad Abduh ambayo kwa ufupi ni kwamba kugeuza ni kinaya cha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawapofusha njia wasijue pa kuelekea kwenye makusudio yao; sawa na wale wanaorudi nyuma kila wanapotaka kwenda mbele.

Au tukawalaani kama tulivyowalaani watu wa Sabato (Jumamosi).

Watu wa Sabato ni watu miongoni mwa Mayahudi waliobadilisha dini na wakapetuka mipaka ya Mwenyezi Mungu,. Kwa hiyo akawafedhehesha na kuwaadhibu duniani kabla ya akhera, Tumeyafafanua hayo katika sura Baqara. (2:65)

Katika Aya hii Mwenyezi Mungu anawakemea kuwa kama hawatajiepusha na upotevu, kupoteza na kubadilisha basi Mwenyezi Mungu Mtukufu atawafedhehesha kama alivyowafedhehesha mababu zao.

Kwenye tafsiri nyingi ikiwemo Tafsiri ya Arrazi, Majmaul-bayan na Bahlul-muhit nimesoma jumla ninayoinukuu hapa: "Hapana budi wafutwe Mayahudi kabla ya Kiyama," Amin!

Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima iwe ni yenye kufanywa. Hakuna wa kupinga hukumu yake wala kuvunja amri yake ambaye hukiambia kitu 'kuwa' kikawa. Ewe Mwenyezi Mungu! Liharakishe jambo litakaloifanya dini yako iwe juu na watu wako wawe na nguvu.

﴿إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴾

48.Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika, lakini husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye, Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu hakika amezusha dhambi kubwa.

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يُزَكُّونَ أَنفُسَهُم بَلِ اللَّـهُ يُزَكِّي مَن يَشَاءُ وَلَا يُظْلَمُونَ فَتِيلًا ﴾

49.Je, huwaoni wale ambao hujitakasa nafsi zao? Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye, nao hawatadhulumiwa hata kilicho kwenye uwazi wa kokwa ya tende.

﴿ انظُرْ كَيْفَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ وَكَفَىٰ بِهِ إِثْمًا مُّبِينًا ﴾

50.Tizama jinsi wamzuiliavyo Mwenyezi Mungu uongo. Na latosha hilo kuwa ni dhambi iliyo wazi.

MWENYEZI MUNGU HASAMEHI KUFANYIWA MSHIRIKA

Aya 48 - 50

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika lakini husamehe yasiokuwa hayo kwa amtakaye.

Kabla ya kufasiri Aya hii tuanze na mambo mawili yanayoambatana nayo sana:

1. Kushirikisha kunagawanyika kwenye aina mbili: Kushirikisha katika Uungu; kama kuitakidi kuwa kuna waumbaji wangi na wenye kutoa riziki. Na kushirikisha katika twaa; kama kuamini kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja kinadharia tu, lakini anamtii kiumbe katika kumwasi Muumba.

Ukafiri nao pia uko aina mbili: Kumkufuru Mwenyezi Mungu na kumkanusha na kukufuru katika twaa; kama kuamini Mungu mmoja kisha kumwasi kwa kupuuza. Vilevile kukufuru neema na kuacha kumshukuru mwenye kuneemesha.

Makusudio ya kushirikisha katika Aya hii ni aina mbili za kwanza za kushirikisha na kukufuru; yaani kuamini waungu wengi na kutoamini kabisa.

2. Yakija maneno ya ujumla, yanahukumu kiujumla kwa watu na yakija tena maneno mahsusi, yanawatoa baadhi ya watu waliokuwa katika ujumla. Ikiwa meneno yote mawili yametokea katika chimbuko moja, basi tutauchukulia ule umahsusi kwenye ujumla; yaani tutawatoa wale waliofahamishwa na kauli mahsusi. Kwa ufafanuzi hebu tupige mfano: Mwenyezi Mungu anasema:

"Mwizi mwanamume na mwizi mwanamke ikateni mikono yao" (5:38)

Hapa Aya imefahamsiha kwamba kila mwizi atakatwa mkono, hata kama ni siku za njaa. Kisha ikaja Hadith isemayo:"Mwizi hakatwi katika siku za njaa." Kwa hiyo kutokana na hali hiyo imepasa tuifunge Aya ya wizi na Hadith ya njaa na hukumu iwe kila mwizi atakatwa mkono isipokuwa siku za njaa.

Baada ya utangulizi huu sasa tuzikutanishe Aya tatu ambazo zitatupa ufafanuzi wa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kufanyiwa mshirika." Mwenyezi Mungu anasema: Sema:

﴿ قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴾

"Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu husamehi dhambi zote, Hakika Yeye ni mwingi wa kusamehe, mwenye kurehemu." (39: 53)

Tamko la Aya hii linaonyesha ujumla, na maana yake yako wazi nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu husamehe kila dhambi hata ya kushirikishwa Yeye.

Lakini Aya tuliyonayo 'Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kufanyiwa mshirika,' tamko lake ni mahsusi, na maana yake yako wazi vile vile, kwamba Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa, kwa hiyo imepasa kutoa kushirikisha katika Aya ya (39:53)

Tena ikaja Aya ya tatu isemayo;

﴿ وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ﴾

"Hakika mimi ni mwenye kusamehe sana kwa anayetubia na akaamini na akashika uwongofu." (20:82)

Aya hii nayo, imemtoa mwenye kutubia kutoka Aya ya kutosamehewa mwenye kushirikisha; kama ambavyo nayo ilimtoa mwenye kushirikisha kutoka Aya ya kusamehewa dhambi zote.

Kwa hivyo basi, maana yanayopatikana kwa kuzikutanisha Aya tatu na kuziunganisha, ni kwamba mwenye kutubia ushirikina, Mungu humsamehe. Kwa sababu yeye amezikana dhambi zake; na mwenye kufa akiwa msirikina hana uokofu. Kwa sababu ameacha kuitumia nafasi yake na kwamba kusamehewa yeye ni kuchochea ushirikina na kuinyenyekea dhuluma.

Zaidi ya hayo kumsamehe mshirikina sio kuwa Mwenyezi Mungu atamwambia aliyefanya uovu: 'Ahsante sana Mwenyezi Mungu ametakata na hayo kabisa.

Unaweza kuuliza kuwa ; kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Lakini husamehe yasiyokuwa hayo kwa amtakaye, inafahamisha kuwa dhambi hiyo - isiyokuwa kushirikisha - mtu akiifanya, inawezekana Mwenyezi Mungu akams amehe kabla ya kutubia. Kwa sababu kufutiwa dhambi pamoja na kutubia kumethibiti kwa Qur'an na Hadith. Kwa hiyo kauli ya Mwenyezi Mungu husamehe itahusika na muumin mwenye dhambi asiyetubia. Au kwa maneno mengine ni kwamba Aya inafahamisha kuwa kusamehewa dhambi muumin hakufungiki na toba tu, bali huenda Mwenyezi Mungu akasamehe dhambi za waumini bila ya kutubia?

Jibu : Wameafikiana waislamu kwamba mwenye kufa akiwa ametubia Mwenyezi Mungu humtakabalia toba yake, kulingana na Aya za Qur'an na Hadith za Mtume, Lakini wametofautiana kuhusu mwislamu mwenye dhambi akifa kabla ya kutubia.

Khawarij wamesema: "Atabakishwa milele motoni sawa na Kafiri, ni sawa dhambi yake iwe kubwa au ndogo.

Kikundi kimoja cha Marjaa kinasema kuwa ataingia peponi bila ya kuadhibiwa, kwa sababu maasi hayadhuru imani wala twaa hainufaishi chochote ukafiri; kama wanavyodai.

Shia na Sunni wamesema hatabakishwa milele motoni, na dhambi zake zitaachwa na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Akitaka atamsamehe na kumwingiza peponi moja kwa moja; na akitaka atamwadhibu kiasi anachostahili, kisha amtie peponi.

Maoni yetu hayatofautiani sana na kauli ya Sunni na Shia, na tutaeleza kwa mfumo huu: Mwenyezi Mungu (s.w.t) hataki kusamehe kwa michezo bila ya hekima inayosababishia hilo. Na hekima inayowajibisha kusamehewa, haifungiki na toba tu; inaweza kuwa ni shafaa au jambo jinginelo. Wala si dharura kufahamu kwa ufafanuzi, bali inatosha kujua kwamba Mwenyezi Mungu ni mwenye hekima, basi. Kwa hivyo, katika mtazamo wa kiakili, hakuna kizuizi cha kusamehewa dhambi kwa Muumin bila ya kutubia.

Yametangulia maelezo yanayofugamana na utafiti huu katika kufasiri Aya (2: 81) kifungu cha Madhambi makubwa.

DALILI YA UMOJA NA UTATU

Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika amezusha dhambi kubwa

Kwa sababu atakuwa ameamini lisilowezekana, Miongoni mwa dalili za kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na lau kungalikuwa na waungu wawili, basi ama atakuwa mmoja wao ni mweza zaidi wa kupangilia mambo ya ulimwengu, au asiweko.

Kwa hiyo akiwa mmoja ni muweza zaidi, basi wa pili atakuwa hana maana tena; na kama akitokuwapo muweza zaidi, basi hawezi kuwa Mungu, kwa kushindwa kwake kwa upande fulani na kutokuwa na faida ya kuweko kwake.

Dalili bora zaidi ya umoja wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni ile aliyoieleza yeye mwenyewe juu ya umoja wa dhati yake, pale aliposema:

﴿ لَوْ كَانَ فِيهِمَا آلِهَةٌ إِلَّا اللَّـهُ لَفَسَدَتَا فَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَرْشِ عَمَّا يَصِفُونَ﴾

"Lau wangelikuwako humo (mbinguni na ardhini) waungu wengine, isipokuwa Mwenyezi Mungu bila shaka zingeharibika, Ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa Arshi na yale wanayomsifu. (21:22)

Yaani lau kungelikuwako na Mungu mwengine katika mbingu na ardhi asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi zisingelikuwa sawa na wangeliharibika waliomo na vilivyomo na kusingekuwako na nidhamu. Kwa vile kama kungelikuwa na Miungu wawili angelikuwa kila mmoja ni muweza, na kawaida ya mwenye uwezo ni dhidi ya anavyotaka mwingine.

Kwa hiyo basi mmoja wao akitaka kuumba kitu na mwingine akitaka kinyume chake, hapo ama yatapatikana matakwa yao wote wawili kwa pamoja, jambo ambalo litalazimisha kupatikana na kukosekena kwa wakati mmoja na hilo ni muhali.

Au yatapatikana matakwa ya mmoja wao kinyume cha mwingine, atakuwa huyu mmoja ameshindwa na mwingine. Kimsingi ni kwamba anayeshindwa hawezi kuwa Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴾

"Mwenyezi Mungu hakujifanyia mtoto wala hakuwa pamoja naye mungu (mwingine), Ingekuwa hivyo basi kila mungu angeliwachukua aliowaumba, na baadhi yao wangeliwashinda wengine, Mwenyezi Mungu ameepukana na sifa wanazomsifu" (23:91)

Kuna mfano mashuhuri unaosema: "Fahali wawii hawakai zizi moja." Amirul-mumin, Ali alimwambia mtoto wake Hassan(a.s) :"Jua ewe mwanangu, lau Mola wako angelikuwa na mshirika wangelikujia Mitume wake na ungaliona athari ya milki yake na ufalme wake na ungelijua vitendo vyake na sifa zake."

Unaweza kuuliza : Je kusema kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja katika asili tatu: Baba, mwana na roho mtakatifu ni katika umoja au ni katika kuwafanya miungu wengi.

Jibu : Ikiwa makusudio ni sifa kama vile mwenye kurehemu, mwingi wa rehema hizo ni katika kumpwekesha, lakini ikikusudiwa mtu basi huo ni Utatu.

Amesema Said Al-Khauri Ashartuni katika kitab Aqrabul-mawarid: "Neno Aqnnim (lililotumiwa katika kueleza utatu) maana yake ni asili na mtu" Kwa hivyo basi litakuwa katika kuwa waungu wengi sio mmoja.

Hayo yanatiwa nguvu na neno baba na mwana ambayo yanahitajia kuweko na idadi na mabadiliko kwa mtu na dhati. Isitoshe, picha na sanamu zilizoko katika makanisa hasa ya bibi Maryam bikira(a.s) zinaonyesha idadi ya waungu waziwazi, kwa sabaau anaonyesha amempakata mtoto ambaye ni Bwana Masih(a.s)

Je, huwaoni wale ambao hujitakasa nafsi zao

Wafasiri wamesema kuwa Aya hii imeshuka kwa mayahudi. Ni sawa iwe ghururi ya mayahudi ndio sababu ya kushuka Aya hii au la, lakini ni picha inayosadikisha madai yao ambayo hayana mfano katika uzushi na uongo.

Mfano kama wasemavyo: 'Sisi ni watoto wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake.' Au kusema: 'Hataingizwa peponi ila aliye myahudi.' Vile vile 'Sisi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu'

Yaani kuwa Mwenyezi Mungu ni wao tu, peke yao, na kwamba Yeye amewaumba watu wengine wawe ni watwana wao. Hawakutosheka na haya, bali ujinga wao na ghururi yao iliwapelekea kusema: 'Mungu ni fukara na sisi ni matajiri.'

Kweli hakuna mtu anayewashinda kwa utajiri wa kuzusha na kutengeneza mambo yasiyokuwapo. Ni hivi majuzi tu walitangaza na kueneza uvumi, wakapiga kelele Mashariki na Magharibi kwamba waarabu wanajianda kuwashambulia, wakati ambapo wao na mabwana zao wakoloni wanapanga njama za kuvamia na kuwahujumu waarabu.

Baada ya kumaliza kupanga, wakatekeleza bila ya kutazamiwa, wakafanya dhulma na unyama uliowafanya watu wasahau aliyoyafanya Hitler na Jankis khan.

Haya ni madogo sana katika mifano ya madai ya mayahudi. Tumeyaleta kama mfano tu, lakini sio hali yao hasa, Je, inawezekana kuyamaliza yote ya mayahudi?

Unaweza kuuliiza : Ikiwa hali ya Israil ni hivi imekuwaje wakaweza kusimamisha dola zaidi ya miaka ishirini sasa?

Jibu : Mataifa ya kikoloni ndiyo yaliyoitengeneza Israel kwa kuhami masilahi yao katika Mashariki ya kati. mayahudi hawana dola isipokuwa jina tu. Ama kubakia kwake mpaka leo, kunatokana na kubakia ukoloni ambao umeipigia hema la Oksijeni.

Hivi sasa dola hiyo iko njiani kuisha; hata kama itachukua muda mrefu. Kimsingi ni kwamba mwenye kusimamia kitu huisha, mara tu kiishapo.Ukiuliza vipi Mwenyezi Mungu amewashakiza mataghuti Makafiri kwa waja wake wanaompwekesha, jibu utalipata kwenye tafsiri ya 3; 138. Kwenye kifungu cha Ushenzi wa 5 Juni

Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye

Sio yule anayejishuhudia yeye mwenyewe, Kimsingi, Mwenyezi Mungu hamtakasi ila ambaye vitendo vyake vinashuhudia utakaso. Ingawaje Aya imeshuka kwa mayahudi, lakini inamkusanya kila mwenye kujitakasa kwa sababu tamko ni la kiujumla; na linalozingatiwa ni ujumla sio sababu ya kushuka.

Majaribio yamethibtisha kuwa hakuna yeyote anayejitukuza ila ni kwa sababu ya ujinga wake na ghururi yake. Au kwa kasoro fulani anayojaribu kuificha, kwa ushahidi usiokubalika hata kwake yeye mwenyewe; kwa sababu anajua uongo wake.

Tizama jinsi wamzuliavyo Mwenyezi Mungu uwongo kwa kusema 'Sisi ni taifa teule la Mwenyezi Mungu', ni watoto wa Mungu na vipenzi vyake' na mengineyo mengi:"Na hatengenekewi mwenye kuzua uongo" (20:61)

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO

﴿ أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا هَـٰؤُلَاءِ أَهْدَىٰ مِنَ الَّذِينَ آمَنُوا سَبِيلًا﴾

51.Je, huwajui ambao wamepewa fungu katika Kitabu wanaamini sanamu na taghuti na wakisema kwa ajili ya wale waliokufuru kuwa hao wameongoka zaidi katika njia ya haki kuliko walioamini.

﴿ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ وَمَن يَلْعَنِ اللَّـهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ نَصِيرًا ﴾

52.Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu, na ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani, hatampatia wa kumsaidia.

WANAAMINI SANAMU NA TAGHUT

Aya 51 -52

LUGHA

Neno Jibt linatumika kwa maana nyingi. Makusudio yake hapa ni anayeabudiwa ambaye si Mungu (sanamu) Na Taghut ni aliyepetuka mipaka.

MAANA

Je, hawajui ambao wamepewa fungu katika Kitabu wanamini sanamu na taghuti.

Katika Aya zilizotangulia, Mwenyezi Mungu amewataja mayahudi kwa upotevu, upotezaji, kuyaweka maneno pasipo mahali pake na kupindua maneno. Kisha katika Aya hii amewataja kuwa wao wanaamini sanamu na taghuti; yaani masanamu wanayoyaabudu Maquraish.

Unaweza kuuliza : Imekuwaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuhusu mayahudi kwamba wao wanaamini sanamu na inajulikana wazi kuwa wao hawaamini masanamu ya Maquraish.

Jibu : mayahudi hawaamini masanamu ya Kiquraish katika nafsi zao, bali waliyakubali kiunafiki kwa kudanganya na kwa ajili ya kubagua na kumfanyia inadi Muhammad(s.a.w.w) na aliyemwamini. Wakawaambia waabudu masanamu: "Nyinyi mna njia ya uongofu zaidi kuliko waislamu."

Iliyo sawa ilikuwa ni kwa mayahudi wawasaidie waislamu dhidi ya waabudu masanamu kwa sababu waislam ni watu wa Kitabu na wanaikubali Taurat kinyume na waabudu masanamu.

Kwa hiyo mayahudi walikhalifu haki na wakasimama pamoja na washirikina, ndipo Mwenyezi Mungu akawataja kama waabudu masanamu. Kwa hali hiyo ndipo tunapoipata tafsiri ya:Hao wameongoka zaidi katika njia kuliko walioamini .

Yaani mayahudi walisema: Washirikina ni waongofu zaidi wa njia kuliko waumini, Kwa hiyo jibu la swali liko ndani ya Aya yenyewe. Kwa hali hii inatubainikia kuwa ishara ya hao ni ya waabudu masanamu na kwamba herufi lam katika neon: Lilladhina ni ya kwa ajili; yaani waliyoyasema ni kwa ajili ya kuwaridhisha wale waliokufuru, ambao ni washirikina wa kiquraish na hawakusema kwa kuamini wayasemayo.

Hao ndio waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu

Nao ni mayahudi waliofanya unafiki wakasadiki masanamu kwa ukaidi na inadi kwa waislam wanaowasadi ki Mitume yao; kama vile Musa, Daud, Suleiman, Yahya na Zakariya.

Na ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani, hatampatia wa kumsaidia.

Isipokuwa Amerika ambayo ilisheheneza Israil kwa silaha na kuisaidia tarehe 5 June; na Umoja wa Mataifa ukawatetea kwa namna ambayo mwarabu yeyote mwenye ikhlasi au mwislamu yeyote aliye muumin hatasahau hata ukipita muda gani.

Na sisi pamoja na majeraha tuliyo nayo, tunaamini kwa imani isiyo na shaka kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye msaidizi mwenye nguvu; na kwamba mwisho wa mambo utakuwa ni wa haki na uadilifu. Kwa hiyo ni juu ya wanaoitafuta haki kuvumilia, kutokuwa na pupa ya kuifikia, na kutotishwa na silaha ya adui kwa vyovyote atakavyokuwa na hatimaye kufaidika na majaribio.

﴿ أَمْ لَهُمْ نَصِيبٌ مِّنَ الْمُلْكِ فَإِذًا لَّا يُؤْتُونَ النَّاسَ نَقِيرًا ﴾

53.Au wao wana fungu katika ufalme? Basi hapo wasingewapa watu hata kitobwe cha kokwa ya tende

﴿ أَمْ يَحْسُدُونَ النَّاسَ عَلَىٰ مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ فَقَدْ آتَيْنَا آلَ إِبْرَاهِيمَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَآتَيْنَاهُم مُّلْكًا عَظِيمًا﴾

54.Au wanawahusudu watu kwa alichowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake? Basi tuliwapa watoto wa Ibrahim Kitab na h ekima na tukawapa ufalme mkubwa.

﴿ فَمِنْهُم مَّنْ آمَنَ بِهِ وَمِنْهُم مَّن صَدَّ عَنْهُ وَكَفَىٰ بِجَهَنَّمَ سَعِيرًا ﴾

55.Katika wao kuna walio mwamini na katika wao kuna waliojiepusha naye; na Jahanam yatosha kuwaunguza.

HAWAWAPI WATU HATA CHEMBE

Aya 53-55

MAANA

Bado maneno yako kwa mayahudi. Mwenyezi Mungu katika Aya ya 44 amewataja kwa upotevu na upotezaji; katika Aya 45 uadui wao kwa waislamu katika Aya ya 46 kwa kugeuza maneno; katika Aya 49 kwa kujitukuza; katika Aya 50 kwa uzushi na katika Aya ya 51 kwa inadi, ukaidi na kuboresha ibada ya sanamu kwa unafiki. Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawataja kwa ubakhili:

Au wao wana fungu katika Ufalme? Basi hapo wasingewapa watu hata kitobwe cha kokwa ya tende.

Maana ni kuwa mayahudi hawana dola wala ufalme. Lau wangelikuwa na sehemu ya ufalme, wangeliwazuilia watu wote heri na wasingelimwachia yeyote kitu; hata kiasi cha kitobwe cha kokwa ya tende kilicho kidogo sana kisichotumika.

Amesema kweli Mwenyezi Mungu Mtukufu, Walikuwa na wanaendelea kuwa hawawezi kuona neema ya Mwenyezi Mungu kwa mja yeyote miongoni mwa waja wake ila hujaribu kuiondoa kwa njama au kwa riba au kwa kudanganya kwa binti zao na wake zao. Na wakipata nguvu kidogo hunyang'anya na kumwaga damu.

Kuanzia siku walipovamia ardhi ya Palestina mwaka 1948, waliwatoa wazalendo nchini mwao baada ya kuwachinja wanawake na watoto kila mahali.

Na mnamo mwaka 1967 waisrail, kwa kusaidiwa na wakoloni, walivamia sehemu nyingine ya ardhi ya waarabu. Kikakaririka kitendo chao cha kwanza, cha kuua na kufukuza. Hili sio geni katika historia yao na tabia zao. Waarabu wametawala na ukaendelea utawala wao miaka kadhaa; ukaenea mashariki na magharibi; na mayahudi walikuwa ni miongoni mwa raia zao; wakafanya uadilifu kwa wote na kuwafanyia wema mayahudi na watu wa dini nyinginezo; mpaka wakasema watunzi wa kimagharibi; kama vile Gustav Lebon: "Haikujua historia utawala wenye huruma zaidi ya Waarabu." Wameshuhudia kama hivyo wengineo "chombo humimina kilicho nacho" anasema Ibin Swafiy.

Itakuwa ni vizuri kunakili aliyoyataja mwenye Al-amanar wakati wa kufasiri Aya hii, katika mwaka wa 60 wakati Palestina ilipokuwa katika utawala wa dola ya Uthmaniya, Ninamnukuu: "Maana yanayopatikana katika Aya hii, ni kwamba hawa mayahudi ni watu wachoyo na wabakhili sana, wanaona tabu kunufaika mwengine yeyote kutokana nao. Wakiwa na utawala wanawazuilia watu wasinufaike hata kidogo, japokuwa ni kitu kipuuzi tu. Basi kwa nini isiwe uzito kwao kutokea Mtume wa kiarabu (Muhammad) ambaye ana milki wakiwemo mayahudi?

Sifa hii bado wanayo hadi leo. Ikiwa juhudi zao za kuunda serikali katika Palestina zitafanikiwa, basi watawafukuza wa islamu na wakristo na hawatawapa hata kitobwe cha kokwa ya tende. Dalili ziko kwamba wanajaribu kumiliki ardhi takatifu na kuwazuia wengine na sababu zote za kupata riziki. Wameweka akiba ya mali nyingi sana kwa ajili ya hilo. Kwa hiyo ni wajibu kwa serikali ya Uthmaniya kutowapa nafasi mayahudi katika Palestina wala wasiwaache wakamiliki ardhi na kuhamia kwa wingi. Kwani hilo lina hatari kubwa.

Mwenye Tafsir Al-manar anasema Aya haithibitishi wala kukanusha kutawala mayahudi Palestina; isipokuwa inabainis ha tabia watakayokuwa nayo lau watatawala Palestina.

Haya ndiyo aliyoyasema ulama katika maulama wa Kiislam kuhusu tafsiri ya Aya hii, Ameisema miaka arobaini kabla ya kupatikana serikali ya Israel katika Palestina. Hii haifahamishi kitu zaidi ya kufahamisha ukweli wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) katika Utume wake na ujumbe wake, pale alipotoa habari kwa Wahyi wa Mwenyezi Mungu kabla ya zaidi ya miaka 1300, kwamba mayahudi lau watamiliki na kutawala wangelikuwa na yale yaliyotokea mwaka 1948 na 1967.

﴿ أَفَمَن شَرَحَ اللَّـهُ صَدْرَهُ لِلْإِسْلَامِ فَهُوَ عَلَىٰ نُورٍ مِّن رَّبِّهِ فَوَيْلٌ لِّلْقَاسِيَةِ قُلُوبُهُم مِّن ذِكْرِ اللَّـهِ أُولَـٰئِكَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ﴾

Je, ambaye Mwenyezi Mungu ameufungua moyo wake kwa uislam akawa yuko katika nuru itokayo kwa Mola wake (ni sawa na mwenye moyo mgumu)? Basi adhabu kali itawathubutukia wale wenye moyo mgumu wasimkumbuke Mwenyezi Mungu. Hao wamo katika upotevu ulio wazi (39:22)

Au wanawahusudu watu kwa alichowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake?

Hii nayo ni sifa nyingine katika sifa za mayahudi, hasadi. Makusudio ya watu hapa ni Mtume Muhammad(s.a.w.w) na waumini walio pamoja naye. Na hasadi yao mayahudi ni kutokana na dini ya haki aliyopewa Muhammad na waumi- ni na kumakinishwa katika ardhi.

Mayahudi waliposhindwa kuizuwia neema hii kwa waislamu, waliungana na washirikina dhidi ya waislam, wakaenezea propaganda dhidi ya uislamu na Mtume wake. Hatimaye uovu ukawazungukia wao na wakafukuzwa Hijaz kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

Basi tuliwapa watoto wa Ibrahim Kitabu na hekima na tukawapa Ufalme mkubwa.

Makusudio ya Kitabu ni Zabur ya Daud, Taurat ya Musa na Injil ya Isa. Hekima ni Utume na elimu: maana yake kwa nini mnamhusudu Muhammad(s.a.w.w) na waarabu kwa sababu ya Utume na kumakinika katika nchi? Mwenyezi Mungu amekwishawapa nyinyi mfano wa hayo katika waliopita; kama vile Yusuf, Daud na Suleiman.

Katika wao kuna waliomwamini na katika wao kuna waliojiepusha naye. Wafasiri wametofautina katika dhamiri ya 'waliomwamini;' kuwa je ni kumwamini Muhammad(s.a.w.w) , au Ibrahim au Kitabu? Lenye nguvu zaidi ambalo linaafikiana na maana na kusaidiwa na kuzingatia ni kuwa dhamiri inamrudia kila Mtume aliyepewa Kitabu na hekima.

Neno 'kila Mtume' hata kama halikutajwa katika Aya waziwazi, lakini linafahamika kutokana na mfumo wa maneno.

Kwa vyovyote iwavyo, hakuna tofauti kuwa maana ya Aya ni kwamba si jambo geni kwa hao na mfano wao kutomwamini Muhammad(s.a.w.w) . Kwani Mitume waliotangulia waliaminiwa na kikundi na wakakanushwa na kundi jingine. Na kundi la ukanushaji lilikuwa kubwa; kama asemavyo (s.w.t):

﴿ فَمِنْهُم مُّهْتَدٍ وَكَثِيرٌ مِّنْهُمْ فَاسِقُونَ﴾

"Wengine katika wao walikuwa waongofu na wengi katika wao walikuwa mafasiki" (57:26)

Jahannam yatosha kuwaunguza wale wapingao haki

﴿ إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِنَا سَوْفَ نُصْلِيهِمْ نَارًا كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴾

56.Hakika ambao wamezikufurisha Aya zetu tutawatia motoni; kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilishia ngozi nyingine ili waonje adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na Mwenye hekima.

﴿ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَنُدْخِلُهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا لَّهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ وَنُدْخِلُهُمْ ظِلًّا ظَلِيلًا﴾

57.Na ambao wameamini na wakatenda amali njema, tutawaingiza katika pepo zenye kupita mito chini yake, ni wenye kudumu milele humo; wana humo wake waliotakaswa na tutawatia katika vivuli vya daima.

KUBADILISHA NGOZI NYINGINE

Aya 56 - 57

MAANA

Hakika ambao wamezikufuru Aya zetu tutawatia motoni; kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilisha ngozi nyingine

Aya hii ni ubainifu wa mwisho wa Aya iliyotangulia, Na Jahannam yatosha kuwaunguza. Makusudio ya Aya hapa ni kila lililothibiti katika dini kwa dharura; mfano ujuzi wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, Malaika, pepo moto na mengineyo yanayorudia kwenye misingi ya dini. Vilevile mfano wa wajibu wa kufunga, Swala, uharamu wa zina, pombe na mengineyo katika masuala ya kifiqhi na ya matawi ya dini. Hakuna mwenye shaka kwamba kukanusha ni kukufuru; na je kutia shaka ni kukufuru pia.? Hilo tumelifanyia utafiti kwa ufafanuzi, wakati wa kufasiri Aya 115 ya sura Al-imran kifungu 'mwenye kuacha uislam.'

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwadilifu, hilo halina shaka. Anapoiunguza ngozi ya mwasi inaondoka na kuisha; kisha huumba ngozi nyingine mpya na kuiadhibu, je, huko si kuadhibui ngozi ambayo haikumuasi? Jambo ambalo halijuzu kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu?Jibu : Imepokewa Hadith kutoka kwa Imam Jaffar as-Sadiq(a.s) inayojibu swali hili:"Hakika ngozi ni hiyo hiyo, si nyingine . Akapiga mfano wa tofali unapolivunjavunja mpaka likawa mchanga, kisha ukalichanganya tena na maji na kutengeza tofali jipya. Hapo litakuwa ndio hilo hilo katika mada yake, lakini ni jengine katika sura yake. Si mbali kuwa 'kubadilisha ngozi' ni fumbo la adhabu na uchungu wake. Katika hali zote ni kwamba linalopatikana kwetu ni kuamini uadilifu wa Mwenyezi Mungu na uweza wake, Ama ufafanuzi hatuna jukumu nao.

Ili waonje adhabu

Yaani lililosababisha kubadilishwa ngozi ni kuhisi kwao adhabu ya kudumu. Aina hii ya adhabu inahusika na mkanushaji, na msihrikina na ambaye watu humwogopa kwa shari yake. Nasi daima, kufa na kupona, tuna imani ya Lailaaha illa illah, Muhammad rasuulu llah, na tunamfanyia uadui kila mwovu. Wanavyuoni wanasema: Watakaoingizwa motoni na wasitoke ni watano: Mwenye kudai uungu, kama vile Namrud na Fir'aun, mwenye kukanusha uungu moja kwa moja, mwenye kumfanyia Mungu washirika, mnafiki na muuaji wa nafsi isiyo na hatia.

Kwa dhahiri ni kuwa mnafiki zaidi ni yule anayeleta vita kwa jina la mwenye kulinda amani; mwenye kuwafanya watumwa watu kwa jina la kuchunga uhuru; mwenye kunyang'anya chakula cha watu kwa jina la kunyanyua maisha yao na mwenye kueneza uovu kwa jina la maendeleo.

Na ambao wameamini na wakatenda amali njema…

Umetangulia mfano wa tafsir yake katika Sura Al-imran Aya 15. Kwa hiyo haihitaji tafsir.

﴿ إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴾

58.Hakika Mwenyezi Mungu anawaamuru kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu muhukumu kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapa mawaidha mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia ni mwenye kuona.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا﴾

59.Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na kama mkipingana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake mkiwa mwamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri.

UAMINIFU NA UADILIFU

Aya 58 - 59

MAANA

Hakika Mwenyezi Mungu anawaamuru kurudishia amana kwa wenyewe.

Aya mbili zimekusanya wajibu wa kutekeleza amana na uadilifu katika hukumu na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume na mwenye madaraka katika nyinyi. Zimekuja Hadith kadha na Aya kadhaa katika kuhimiza kuchunga amana na kuitekeleza kwa mwenyewe awe mwema au mwovu. Kwa sababu ni haki yake kama binadamu, sio kwa kuwa ni mwema au mwovu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ﴾

"Enyi mlioamini msimkhini Mwenyezi Mungu na Mtume wala msikhini amana zenu" (8:27)

Mtume anasema: "Hana imani asiyekuwa na uaminifu, wala hana dini asiyekuwa na ahadi" Lakini hakuna katika Qur'an wal a Hadith - kwa tunavyojua - maelezo kamili ya amana. Tunavyofahamu ni kuwa amana ni dhamana iliyoko kwako kwa ajili ya mtu mwingine. Ni juu yako kuichunga na kuilinda na kuirudisha kwa mwenyewe anapoitaka kama ilivyo. Ukiizuia au kuirudisha pungufu, basi wewe ni mhaini wa hukumu ya Qur'an na Hadith.

Si lazima amana iwe ni kitu kinachoonekana, kama vile mali na kitabu, la inaweza kuwa ni siri, nasaha au kazi. Vilevile si lazima mwenyewe hiyo amana awe mtu hasa; inaweza kuwa ni dini au elimu, bali hata nafsi yako yenyewe ikawa ndiyo yenye amana.

Amana ya dini na elimu ni yale unayoyajua katika halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake na katika heri na shari. Amana hii itathibiti kwa kufanya unayoyajua. Ama amana ya nafsi yako iliyoko kwako, ni lile lililo la masilahi zaidi kwa dunia ya hiyo nafsi na akhera yake.

Kwa maneno mengine, mwaminifu ni yule anayetekeleza kwa ukamilifu bila ya upungufu, ni sawa aliyewajibisha wajibu huu ni dini, elimu, nchi, jamii au kitu chochote kingine.

Kwa hiyo basi amana sio muonjo ulio katika chakula au kinywaji hiki sio kile, au kuwa ni mwanamke huyu si yule wala sio wasifu unaowapendeza watu; kama upole, bali amana ni mshikamano wa maisha na msimamo wake ambao bila huo maisha hayaendi sawa.

Kwenye maana hayo Imam Ali(a.s) ameishiria kwa kusema:"Amana ni nidhamu ya umma"; yaani umma hautengenei mambo yake ila ikiwa kila mtu atatekeleza yanayotakikana kwake. Na amesema tena:"Ambaye siri yake haitofautiani na dhahiri yake na vitendo vyake havitofautiani na maneno yake, basi atakuwa ametekeleza amana na amewafanyia ikhlasi waja. Na mwenye kuipuuza amana akawa anafanya hiyana na wala asiepushe nafsi yake na dini yake kwa uhaini basi atakuwa amejiingiza katika fedheha duniani, na akhera atapata udhalili na fedheha. Na hakika hiyana kubwa ni kuuhaini umma, na fedheha kubwa ya utapeli ni kuutapeli umma."

Miongoni mwa dalili za kuutukuza uaminifu ni kauli ya mafakihi: "Mwenye kuutangazia vita uislamu na waislamu na akahalalisha damu zao na mali zao si kwa chochote ila kwa kuchukia Tawhid, basi ni halali mali yake na damu yake wala haiwi halali amana yake."

Imam Zainul-abidin(a.s) anasema:"Lau aliyemuua baba yangu angaliniwekea amana upanga aliomuulia, nisingelimuhini."

Mtu mmoja alimuuliza Imam Arridha(a.s) : "Yahudi amenihini Dirham elfu; kisha faida yake ikaingia mikononi mwangu, Je, nimlipizie?" Imam akamjibu:"Ikiwa amekudhulumu usimdhulumu."

Katika riwaya nyingine amesema:"Ikiwa amekuhini usimuhini wala usijiingize katika aliyokufanyia." Siri katika hilo ni kwamba amana ni haki ya mwenyewe kwa sifa ya kuwa ni mtu sio kuwa ni mwislamu wala mshirikina au si mwema wala mwovu, Tutarudia kuelezea uaminifu tutakapofasiri Aya 72 ya Sura ya Ahzab.

Na mutapohukumu baina ya watu muhukumu kwa uadilifu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwajibisha kurudisha amana kwa wenyewe, amefuatisha wajibu wa uadilifu katika kuhukumu baina ya watu, Kwa sababu asiyechunga haki za watu, hana haki ya kuwa hakimu. Wajibu wa uadilifu siyo kwa hakimu tu, bali mtawala vile vile, na mtawala mwadilifu ni yule anayejishughulisha na nyanja zote za maisha; kama vile afya maendeleo, chakula na uhuru kwa wote.

Kabla ya kila kitu ni wajibu kutomwacha mtawala mwenye tamaa - mzalendo au asiyekuwa mzalendo - kutawala mambo ya watu. Matukio tuliyoyapitia yamethibitisha kwamba chimbuko la kwanza na la mwisho la matatizo yaliyotufika ni kutokana na kuwarudisha wezi na wasiokuwa na ujuzi kwenye madaraka na vyeo vya juu.

Ama uadilifu wa hakimu unakuwa katika kuwafanyia kwake usawa watesi wawili katika kila kitu na kila mwenye haki kumpa haki yake, bila ya kuangalia dini yake na itikadi yake; urafiki wake na uadui wake au utukufu wake na uduni wake.

Katika Historia ya sheria hakuna sharia iliyojihimu na kulitilia mkazo hilo kuliko sheria ya Kiislam. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Mwenye kufanywa hakimu amechinjwa bila ya kisu." Anaonyesha kuwa wajibu wa hakimu ni mzito sana; Kwa sababu inabidi kupigana jihadi kwa nafsi yake na kufanya bidii ikiwa haki haiko. Na akasema tena:"Mahakimu ni watatu: wawili watakuwa motoni na mmoja peponi."

Ama yule atakayekuwa peponi, ni yule aliyejua haki akaihukmu, na wale wawili wataokuwa motoni ni aliyewahukumu watu bila ya ujuzi, na aliyekuwa anaijua haki, lakini akahukmu kinyume chake."

Hakika mwenyezi Mungu anawapa mawaidha mazuri sana.

Makusudio ya mawaidha hapa ni amri ya kurudisha amana. Neno mazuri linatambulisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) haamrishi ila ambalo ndani yake mna kheri na masilahi.

WENYE MAMLAKA NI NANI

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi.

Maneno na mabishano yamekuwa mengi kuhusu makusudio ya 'wenye mamlaka' na sifa zao; kama ambavyo watawala wamejibandika nayo kuwa ni wajibu kuwatii au angalau kuwanyamazia.

Vile vile kundi la mafakihi limetoa dalili kwa Aya hiyo kuwa chimbuko la sharia na misingi yake linathibiti kwa mambo manne:

1. Kitabu cha Mwenyezi Mungu; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:"Mtiini Mwenyezi Mungu."

2. Hadith za Mtume; kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:"Na mtiini Mtume."

3. Ijmai; kutokana na kauli yake:"Na wenye mamlaka"

4. Kiyasi; kutokana na kauli yake:"kama mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume." Wakadai kwamba maana yake ni kuwa: likisieni lile lisilo na nukuu (nassi) kutoka katika Qur'an na Hadith. Utakuja ufafanuzi wa hilo.

Hakuna tofauti kuwa Qur'an na Hadith ni machimbuko ya msingi ya sharia. Ama Ijmai na Kiyasi wametofautiana katika hoja yake na katika ufahamisho wa Aya juu yake. Yafuatayo ni madhumuni ya Aya na rai zilizosemewa juu ya Aya hiyo:

1. Hakuna waliotafoutiana katika waislam kwamba kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume kunakuwa ni kufanya amali kwa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake na kwamba hiyo ni misingi miwili katika ibara moja:Mwenye kumtii Mtume basi amemtii Mwenyezi Mungu. (4:80),

Alichowaletea Mtume kichukueni na alichowakataza kiacheni. (59:7),Wala hasemi kwa matamanio; hayakuwa haya ila ni Wahyi uliofunuliwa. (53: 3- 4)

Kuanzia hapo ndio wameafikiana waislam kwa kauli moja kukataa kila linalonasibishwa kwa Mtume(s.a.w.w) kama linapingana na msingi katika misingi ya Qur'an na hukumu zake.

Unaweza kuuliza : Kwa nini kukaririka neno utiifu katika kumtaja Mtume na wala halikukaririka wakati wa kutaja wenye mamlaka?

Jibu : Ni kwa ajili ya kutanabahisha kwamba kumtii Mtume ndio asili kwa dhati yake; sawa na kumtii Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo ndiyo ikawa kauli ya kila mmoja wao ni chimbuko katika machimbuko ya sharia, lakini si hivyo katika kuwatii wenye mamlaka. Bali ni tawi la kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume. Hakika wenye mamlaka ni wapokezi wa Mtume.

2. Neno miongoni mwenu, linafahamisha kwa uwazi wazi kwamba hakimu wa waislam anapasa awe ni miongoni mwao, wala haifai kabisa kuwa si miongoni mwao. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu:Na Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumini. (4:141)

3. Wametofautiana katika makusudio ya wenye mamlaka baada ya kuafikiana kwao juu ya sharti la uislam; kuna waliosema: Ni makhalifa (Khulafau rrashidun). Na waliosema kuwa ni makamanda wa jeshi. Na wengine wakasema ni maulama wa kidini. Sheikh Muhammad Abduh amesema: Wao ni machifu watawala, maulama, viongozi wa jeshi na viongozi wengineo ambao watu wanawarudia katika haja na masilahi. Wakiafikiana hawa juu ya jambo, ni wajibu kuwatii kwa sharti ya kuwa wawe waaminifu na wasihalifu amri ya Mwenyezi Mungu wala Sunna ya Mtume wake. Na wawe na hiyari katika utafiti wao wa amri na kuafikiana kwao.

Shia wamesema kuwa Mwenyezi Mungu ameunganisha kwa herufi (Wau) baina ya kuwatii wenye mamlaka na kumtii Mt ume bila ya sharti lolote; na kuunganishwa kwa herufi (Wau) kunahukumia kuchanganya na kushirikiana katika hukumu. Maana ya haya ni kuwa kuwatii wenye mamlaka ni kumtii Mtume na kwamba amri yao ni amri yake.

Hakuna mwenye shaka kwamba daraja hii tukufu haiwi ila kwa anayesifika na kustahiki twaa hii na hakuna kitu kitakachomfanya astahiki hayo isipokuwa kuhifadhika na makosa na maasi (isma). Ndiko pekee kunakokufanya kumtii yeye na kumtii Mtume kuwe sawa.

Arrazi amekiri waziwazi fikra ya Isma kwa kusema kuwa wenye mamlaka ambao ni wajibu kuwatii hapana budi wawe ni maasumin (waliohifadhiwa na dhambi). Na Arrazi - kama anavyojulikana - ni miongoni mwa maulama wakubwa wa kisunni; mwanafalsafa na mfasiri wao, Haya ndiyo aliyoyasema ninamnukuu; "Jua kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu, wenye mamlaka inafahamisha kwetu kwamba Ijmai ni hoja.

Dalili ya hilo ni kwamba: Mwenyezi Mungu ameamrisha kutiiwa wenye mamlaka moja kwa moja kat ika Aya hii. Na ambaye Mwenyezi Mungu anaamrisha atiiwe hapana budi awe amehifadhiwa na makosa; Kwa sababu lau asingelikuwa amehifadhiwa na makosa basi itakuwa anakadiriwa kufanya makosa, ambapo Mwenyezi Mungu ameamrisha afuatwe.

Kwa hiyo hilo litakuwa ni kuamrisha kufanywa makosa; na inajulikana kwamba kumfuata mwenye makosa kumekatazwa. Kwa hiyo imethibiti kwamba makusudio ya wenye mamlaka waliotajwa katika Aya hapana budi wawe wamehifadhiwa na makosa."

Hivi ndivyo walivyosema Shia katika kufasiri Aya hii, Tofauti iliyoko kati yao na Sunni ni katika kufuatilia na kumwainisha huyo mwenye kuhifadhiwa na makosa (maasum). Sunni wanasema kuhifadhiwa ni kwa umma. Wamefasiri umma kuwa ni watatuzi. Wengi wao wakasema ni baadhi ya watatuzi. Shia wamesema kuwa makusudio ya wenye mamlaka ni Ahlul-bayt ambao wametakaswa na makosa na kutwahirishwa na uchafu.

Kwa hiyo fikra ya Isma haihusiki na Shia tu, na wala sio waliosema peke yao, bali iko kwa Sunni; kama ambavyo iko kwa Shia. Hivyo kuchukulia kuwa shia tu ndio waliosema kauli hiyo ni kwa ajili ya ukaidi tu, na kueneza utengano.

Shia wametoa dalili juu ya Isma kwa Ahlul-baiti, kwamba: ni kipawa cha Mwenyezi Mungu, Anawahusu watu anaowaridhia miongoni mwa waja wake. Haiwezekani mtu kuitafuta mwenyewe Isma kwa namna yoyote atakavyojitahidi; kinyume na sifa nyingine. Kwa hiyo njia ya kujua Isma inajulikana kwa wahyi tu.

Na imethibiti kauli wazi katika Qur'an na Hadith juu ya Isma ya Ahlul- bait. Miongoni kwa hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

﴿إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا﴾

"Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondolea uchafu (Enyi) Ahlul-baiti na kuwatakasa kabisa kabisa" (33:33)

Pia kauli yake Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mwenye kunitii mimi ndio amemtii Mwenyezi Mungu; na mwenye kuniasi amemuasi Mwenyezi Mungu; na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu, ndio amenitii mimi na mwenye kumwasi ameniasi mimi." Ameipokea Hakim katika Mustadrak na akasema: "Hii ni Hadith sahihi."

Vilevile ameisahihisha Dhahabiy katika Tal-khisu al-mustadrka, Katika kitabu hicho kuna hadith ya Mtume(s.a.w.w) amesema:"Ali yuko pamoja na Qur'an na Qur'an iko pamoja na Ali, viwili hivyo havitatengana mpaka vinijie katika Birika."

Vile vile amepokea Tirmidhi katika Musnad yake, Hakim katika Mustadrak yake na Ibn Hajar katika Sawaiq yake kutoka kwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) kwamba yeye amesema:"Ewe Mola wangu izungushe haki pamoja na Ali popote aendapo." Pia Imam Ibn Hambal, Tirmidhi, Hakima na Ibn Hajar, wamepokea kauli yake Mtume(s.a.w.w) :" Mimi nawaachia vitu ambavyo kama mkishikamana navyo hamtapotea baada yangu, navyo ni vizito viwili: Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-bait wangu."

Imekuwa mashuhuri Hadith kutoka kwa Mtume isemayo: "Hakika mfano wa Ahlul-bait wangu kwenu ni kama mfano wa safina ya Nuh, mwenye kuipanda ataokoka." Na Hadithi nyinginezo nyingi, zote hizo zimeandikwa katika vitabu vya Hadith vya Sunni na sahih zao, na zimepokewa na wategemewa wao.

Shia wamezikusanya na kuziwekea vitabu maalum vya zamani na vya kisasa. Vya zamani ni kama Kitab shafi cha Shariff Murtadha, Tal-khisu shafi cha Sheikh Tusi, Nahjul-haq cha Allama Hilli na katika Hadith za Mujallad wa tatu katika A'yanusha Shia cha Sayyid Muhsin Amin. Vile vile Dalailus-swidq cha Sheikh Mudhaffir na Muraja't cha Sharafuddin.

Kwa ujumla ni kwamba Shia na Sunni wanaamini Isma kwa pamoja kama msingi[7] Vile vile wameafikiana Shia na Sunni wengi kwamba wenye mamlaka waliotajwa katika Aya wamehifadhiwa na dhambi.

Pia wanaafikiana kwamba dalili ya kuhifadhiwa kwao ni kwamba Mwenyezi Mungu amewajibisha watiiwe kama alivyowajibisha kutiiwa yeye Mwenyezi Mungu na Mtume. Lakini Sunni wakatofautiana na Shia kuwa makusudio ya wenye mamlaka waliohifadhiwa na makosa, ni watatutuzi wa mambo au ni Ahlul-bait?

Sunni wakasema ni watatuzi wa mambo. Shia wakasema ni Ahlul-bait. Kwa sababu Isma ni kipawa cha Mwenyezi Mungu, hakijulikani ila kwa kauli wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume. Na imethibiti kauli kutokana nao juu ya Isma ya Ahlul-bait, Kwa hiyo makusudio ya wenye mamlaka ni Ahlul-bait si wengineyo.

Kwa maneno mengine ni kuwa wenye mamlaka katika Aya ni wenye kuhifadhiwa na makosa kwa sababu ya wajibu wa kuwatii wao. Kwa sababu ambaye ni wajibu kumtii ni maasum. Vile vile kunathibiti kuhifadhiwa kwa Ahlul-baiti kwa kauli wazi na hakukukuthibiti kwa wengineo. Na ambaye kumethibiti kuhifadhiwa kwake, basi ni wajibu kumtii. Kwa hiyo natija ni kuwa Ahlul-baiti ndio wenye mamlaka si wengineo. Kama kusema: Msikilize mwenye kunasihi aliye mwaminifu, wala hakuna mwaminifu ila Zaid. Kwa hiyo natija ni msikilize Zaid. Katika ambayo wameyatolea dalili Shia juu ya kutojuzu kuwafuata watatuzi katika mambo ya kidini ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Lakini watu wengi hawajui." Na kauli yake:"Na wengi wao hawaelewi." (5:103)

Maana ya haya ni kuwa haki haijulikani kwa kuangalia idadi ya watu, wawe wengi au wachache isipokuwa hujulikana kwa kuchukuliwa kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake na hukumu ya kiakili ya msingi ambayo hakuna wanaotofautiana, - Kwa kuongeza - ninaandika maneno haya katika mwezi Machi 1968 na uchaguzi wa wabunge wa Lebanon umeuma mchanga; watu wanasongamana kwenye masanduku ya kura ili wamchague aliyenunua sauti za watu baada ya mnada, au yule aliyewaahidi watu wake kutekeleza matakwa yao.

Salaam zimfikie yule aliyesifu baadhi ya uchaguzi kwa kusema: "Mtu anaitikiwa pamoja na ukorofi wake. Mwengine anafuatwa kwa sababu ya udugu pamoja na maovu chungu nzima aliyonayo." Mwengine akasema: "Ni wachungwa mazuzu wanaufata kila sauti ya mchungaji, Ni bendera wanafuata upepo. Hawakupata mwanga wa elimu wala hawakuegemea nguzo thabiti.

Na kama mkipingana katika jambo, basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Tumetangulia kusema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu mtiini Mwenyezi Mungu na mtiini Mtume - kwa maafikiano ya wote inafahamisha kushikamana na Qur'an na Hadithi; na kwamba kauli yake Mwenyezi Mungu. Na wenye mamlaka katika nyinyi, inafahamisha - kwa shia - wajibu wa kuwatii Ahlul-bait; na kwa sunni wengi inafahamisha kuwatii watatuzi wa mambo. Sasa tuzungumzie kauli hii, Na kama mkipingana. Je inafahamisha wajibu wa kutumia kiasi au iko mbali na hayo?

Kabla ya jawabu tutupe swali hili: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibisha kurudishwa mapingano Kwake na kwa Mtume tu, bila ya wenye mamlaka, ambapo Yeye amewajibisha kuwatii wote watatu?

Jibu : Kwa sababu mzozo huenda ukatokea katika kuwajua hao wenye mamlaka; kama ambavyo limetokea hilo.

Sunni wakasema: Ni watatuzi wa mambo na Shia wakasema ni Ahlul-bait. Kwa hiyo katika mzozo huu inabidi kurudia Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume wake. Kwa ajili hiyo ndio Shia wakatoa dalili Aya ya tat-hir[8] na Hadith. Sasa turudie kwenye wajibu wa kutumia kiasi au kutotumia.

(Qiyas), ni kutoa hukumu ya tukio iliyoelezwa wazi na sharia kwa tukio jengine ambalo hukumu yake haikuelezwa wazi; kwa kushirikiana matukio mawili katika sababu zilizotolewa na fakihi.

Mfano sheria, imeeleza kuwa nyanya wa upande wa mama anarithi na wala isielezwe wa upande wa baba. Tukamrithisha nyanya wa upande wa baba kwa kuchukulia kiasi cha wa upande wa mama. Kwa sababu wote ni nyanya.

Sunni wamesema kuwa kauli yake Mwenyezi Mungu; Mkipingana katika jambo lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume inafahamisha kusihi qiyasi; kuwa maana yake ni lirudisheni kwenye tukio alilolibainisha Mwenyezi Mungu hukumu yake; yaani linalofanana nalo.

Shia wamesema kuwa Aya iko mbali kabisa na qiasi wala haifahamishi zaidi ya kurudia Qur'an na Hadith katika masuala ya kidini inapotokea tofauti baina ya mafakihi, Na kauli za maimamu walio maasum zinaingia katika hadith. Kwa sababu ni riwaya kutoka kwa babu yao Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Ama njia yao katika ambalo halikuelezwa wazi katika Kitab wala Hadith ni kurudia kwenye hukumu ya akili ya mkato iliyo dhahiri ambayo haiwezi kutofautiana. Mfano ubaya wa mateso bila ya ubainifu; na ambayo wajibu hautimii ila kwalo, basi ni wajib, Kwa hiyo qiasi sio katika kauli hii. Kwa sababu natija zake zote ni za kudhania; na dhana haitoshelezi kitu [9] .

Katika waliyoyatolea dalili Shia kuhusu kubatilika kwa qiyas ni kwamba mambo ya kawaida, inasihi kuyafanyia qiyas, Kwa vile sababu zake ziko kwenye ukawaida, Ama hukumu za kidini haisihi kufanya qiyas. Kwa sababu sharia imekusanya pamoja vitu vinavyotofautiana; kama katika mambo yanayovunja udhu ambapo imeweka sawa kulala na kukojoa.

Mkiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Mwenye Majmau anasema: "Ni ubainifu wa uwazi ulioje wa kauli hii!" Nasi twasema: Ni uzuri ulioje wa tafsir wa hiyo!

Hilo ni bora zaidi na mwisho mzuri

Yaani kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, na kuirudisha hukumu ya kutofautiana kwa Qur'an na Hadith ni mwisho mzuri. Hii ni ikiwa tutalifasiri neno Taawil katika Aya hii kwa maana ya mwishilio.

Imesemekana kuwa makusudio ya neno Taawil hapa ni tafsiri ambapo maana yatakuwa ni tafsir ya Mwenyezi Mungu na Mtume katika mnayopingana ni bora na nzuri kuliko tafsiri yenu.

Vyovyote iwavyo neno Taawil linachukua maana zote mbili


6

7

8

9

10

11

12

13