TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 17237
Pakua: 2334


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 14 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 17237 / Pakua: 2334
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA TANO Juzuu 5

Mwandishi:
Swahili

8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TANO

﴿ إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴾

97.Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao, wataambiwa: Mlikuwa katika hali gani? Watasema: Tulikuwa wanyonge katika ardhi, wataambiwa: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkahamia humo? Basi hao makazi yao ni Jahannam; nayo ni marejeo mabaya.

﴿إِلَّا الْمُسْتَضْعَفِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالنِّسَاءِ وَالْوِلْدَانِ لَا يَسْتَطِيعُونَ حِيلَةً وَلَا يَهْتَدُونَ سَبِيلًا﴾

98.Isipokuwa wale wanyonge katika wanaume na wanawake na watoto (ambao) hawawezi kufanya hila yoyote wala kufuata njia.

﴿فَأُولَـٰئِكَ عَسَى اللَّـهُ أَن يَعْفُوَ عَنْهُمْ وَكَانَ اللَّـهُ عَفُوًّا غَفُورًا ﴾

99.Basi hao huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe; na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa maghufira.

﴿وَمَن يُهَاجِرْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يَجِدْ فِي الْأَرْضِ مُرَاغَمًا كَثِيرًا وَسَعَةً وَمَن يَخْرُجْ مِن بَيْتِهِ مُهَاجِرًا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ ثُمَّ يُدْرِكْهُ الْمَوْتُ فَقَدْ وَقَعَ أَجْرُهُ عَلَى اللَّـهِ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴾

100.Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata katika ardhi mahali pengi pa kukikimbilia na wasaa. Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti, basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

ARDHI YA MWENYEZI MUNGU NI PANA

Aya 97 - 100

MAANA

Waislamu zama za Mtume(s.a.w.w) walikuwa na Hijra mbili kutoka Makka. Ya kwanza ilikuwa ni ile ya kuelekea Uhabeshi (Ethopia), na ilikuwa miaka mitano tangu Mtume kuutangaza utume wake, Ya pili ilikuwa ile ya kuelekea Madina iliyokuwa miaka minane baadaye.

Wako Masahaba ambao walifanya Hijra mbili kama Jafar bin Abu Twalib ambaye maisha yake yaliishia kwa kufa shahid baada ya kukatwa mikono yake. Mwenyezi Mungu akamkirimu kutokana na mikono hiyo mbawa mbili atakazoruka nazo katika pepo; na ndio akatiwa 'Attwayyar' (Mrukaji).

Ama sababu ya Hijra (kuhama) ni kujiepusha na kuingia katika maangamivu, kukimbilia mahali pa amani kupanga mipango ya Jihadi na kuipinga batili. Kwa kutokana na Hijra (kuhama) na fadhila zake, uislamu umeshinda maadui zake. Lau si hiyo ungelizimika mwenge wake na kugeuka jivu linalopeperuka. Kwa ajili hii Hijra ikawa wakati huo ni fadhila kubwa na ni kitendo cha fahari cha kwanza ambacho hakikurubiwi na kitu chochote.

Mtume(s.a.w.w) alihama kutoka Makka kwenda Madina na akawaamrisha waislamu wahamie huko. Wengi wakamwitikia na wengine wakabaki kwa kung'ang'ania mali zao na masilahi yao. Kwa sababu washirikina walikuwa hawamwachi mwenye kuhama kuchukua chochote katika mali yake.

Washirikina walikuwa wakimwudhi sana anayebaki hapo na kumzuilia na dini yake, akiwa hawezi kujitetea. Lakini alikuwa anaweza kujiepusha na vikwazo hivyo na kuisimamisha dini kwa njia za ukamilifu, kwa kuhama kutoka katika mji ulio na vita na waislam kwenda mji wa uislamu na amani (Madina) aliko Mtume na Sahaba. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu aliwatahayariza wale walioona kuwa ni heri kubaki katika nyumba ya ukafiri na kuipiga vita dini na watu wake. Aliwatahayariza na akawazindua kupitia Malaika kwa kusema:

Hakika wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao.

Kwa kuacha Jihadi na kuhama kwenda kwenye mji wa kiislamu, wakaridhia kubaki katika nyumba ya ukafiri, udhalili na kuharibu wajibu wa dini,Wataambiwa; mlikuwa katka hali gani? Yaani Malaika wa mauti watawaam- bia wale walioacha kuhama; mlikuwa vipi? Hili hasa si swali, isipokuwa ni lawama na kusutwa. Ilivyo hasa ni kuwa lawama zinakuwa kwenye tukio maalum, ambalo hapa ni kule kukaa kwao nyuma ya ndugu zao wahamiaji ambao wamemtii Mtume katika kutekeleza mipango ya kuumaliza ushirikina na kuliinua neno la Mungu.

Akiuliza muulizaji; Je, makaripio haya na masuto kutoka kwa Malaika kwa wale waliorudi nyuma yalikuwa wakati wa kukata roho au ni baada yake?

Tutajibu kuwa ujuzi wa haya uko kwa Mola; yeye amelinyamazia hilo. Kwa hiyo na sisi tunalinyamazia vilevile. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:"Hakika Mwenyezi Mungu amenyamazia mambo si kwa kusahau, basi msijikalifishe nayo"

Watasema: Tulikuwa ni wanyonge katika ardhi.

Huu ni udhuru na kutafuta sababu kwa waliorudi nyuma. Maana yake ni kuwa waliorudi nyuma wanawajibu Malaika wanaowalaumu kwa uzembe wao katika mambo ya dini. Wanawajibu kwa kusema: Tulikuwa tumeshindwa, tunaonewa katika mji wa makafiri, kusimamia wajibu wa kidini.

Kwa sababu washirikina walitukandamiza na kutuzuia kufanya tuliyokuwa tukiitakidi, Malaika wakajibu udhuru huu. Watasema: - Kwa kuwasuta –

Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa pana mkahamia humo? Yaani mlikuwa mnaweza kuhamia mji wa kiislamu ambako mtaepukana na udhalili na kuweza kuitekeleza dini kwa uhuru; kama walivyofanya waislamu wengine.

Kama kuna kitu kinachofahamisha zaidi kuhusu malumbano haya, basi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hamwadhibu yeyote ila baada ya kukamilisha hoja, bali ila baada ya kurundikana hoja kwake; kiasi ambacho kinamwacha mwenye dhambi asiwe na kimbilio ila msamaha wake Mwenyezi Mungu (s.w.t) na rehema yake ambayo imeenea katika kila kitu, "Ewe Mola wangu na mimi ni kitu zinienee rehema zako."

Basi hao - yaani waliorudi nyuma -makazi yao ni Jahannam, na ni marejeo mabaya. Isipokuwa wale wanyonge katika wanaume na wanawake na watoto (ambao) hawawezi kufanya hila yoyote wala hawawezi kufuata njia.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakemea waliorudi nyuma, aliwavua walio na udhuru kwa ugonjwa au kukosa posho na akawaondolea takilifa ya Hijra. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hakalifishi ila uweza wake.

Unaweza kuuliza : kuwa kutolewa wanaume na wanawake wenye udhuru kuna mwelekeo maalum. Sasa kuna mwelekeo gani wa kutolewa watoto na inajulikana kuwa watoto hawakalifiwi na kitu?

Swali hili limejibiwa kuwa : maana ya neno Wildan ni watumwa na wajakazi. Ama sisi tunajibu kuwa watoto wengine wanaweza kuhama hasa vijana wadogo, bali baadhi yao wana uwezo zaidi ya watu wakubwa. Kwa ajili hii mtu anaweza akadhania kuwa kuhama ni wajibu kwa kila anayeweza. Hivyo Mwenyezi Mungu ameiondoa dhana hiyo na kubainisha kuwa Hijra ni wajibu kwa kila mwenye uweza ila akiwa ni katika watoto.

MAFAKIHI NA WAJIBU WA HIJRA

Mafakihi wameitolea dalili Aya hii kwamba mwislamu haijuzu kwake kukaa kwenye mji wa ukafiri ikiwa hawezi kuitekeleza dini, hata kama ni mji wake akiwa na milki na masilahi, Lakini hukumu hii siku hizi haina maudhui. Kwa sababu kila mtu katika kila mji anaweza kumwabudu Mwenyezi Mungu kwa namna yoyote atakayo, Akiacha, basi yeye peke yake ndiye mwenye jukumu.

Unaweza kuuliza : Mtu akijua kuwa kukaa kwake katika mji usiokuwa wa kiislamu kunasababisha kuacha faradhi, si kwa kuwa mtu anamzuia, bali kwa udhaifu wa kukabiliana na msukumo; kama vile mchezo n.k. Je, inafaa kukaa katika mji huu?

Jibu : Akijua kwa yakini kwamba kwenda mahali popote, pawe ni mjini, kikao au sokoni ambako lazima kutamfanya aache wajibu au kufanya haram basi ni wajibu kwake kuepukana nako. Kwani sababu inayolazimu uharamu basi ni haramu. Mwenyezi Mungu anasema:"Basi baada ya kukumbuka usikae pamoja na watu madhalimu." (6: 68)

Amirul Mumin(a.s) anasema: "Hijra (kuhama) bado iko kwenye mipaka yake ya kwanza." Yaani, bado ipo hukumu yake ya wajibu kwa yule ambaye imekuwa uzito kutekeleza hukumu za dini yake ila katika mji wa waislamu.

Ama kauli ya Mtume(s.a.w.w) :Hapana Hijra (kuhama) baada ya kutekwa Makka," makusudio yake ni kuhama kutoka Makka. Hilo linafahamishwa na neno kutekwa Makka.

Na mwenye kuhama katika njia ya Mwenyezi Mungu atapata katika ardhi mahali pengi pa kukimbilia na wasaa.

Riziki haziko nyumbani tu na kuhama hakuwajibishi kukosa. Miji ya Mwenyezi Mungu ni mingi, riziki yake ni pana na neema katika kila mji hazihisabiki, na kwamba mafukara wengi wamejikusanyia mali kule walikohamia kiasi ambacho walikuwa hawaoti kupata hata sehemu ndogo tu walipokuwa nyumbani kwao.

Lau wale waliorudi nyuma wangelihama, wangelipata riziki na utukufu kiasi cha kuwadhalilisha washirikina waliowapa aina kwa aina za udhalili na vikwazo. Lakini waliorudi nyuma walilikataa hilo, wakachukua udhalili na utwevu kutoka kwa maadui wa dini yao, si kwa lolote ila ni kuwa shetani aliwatisha na ufukara iwapo watahama wakategemea vitisho vyake na wakaathirika kuacha maghufira ya Mwenyezi Mungu:

﴿الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ وَاللَّـهُ يَعِدُكُم مَّغْفِرَةً مِّنْهُ وَفَضْلًا وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴾

"Shetani anawatisha na ufukara na anawaamrisha ubakhili; na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha utokao kwake na fadhila na Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu, Mjuzi" (2: 268).

Na mwenye kutoka nyumbani kwake ili kuhamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfikia mauti, basi yamethibiti malipo yake kwa Mwenyezi Mungu.

Kila mwenye kukusudia kwa kujitahidi na kufanya ikhlasi kwa amali yoyote katika amali za twaa kisha akashindwa, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) humwandikia thawabu kamili kwa fadhila na ukarimu kutoka kwake Mwenyezi Mungu. Tumelifafanua hilo katika kufasiri Aya (3: 144) kifungu, kila mtu ana alilonuia.

Imepokewa kuwa Jundub bin Dhumra, aliposikia Aya ya Hijra aliwaambia wanawe; "Wallahi silali Makka mpaka nitoke, kwa sababu ninahofia kufa Makka;" naye alikuwa mgonjwa sana, wakatoka nae wakimchukua kitandani, Alipofika mahali panapoitwa Tan'im akafariki, Ndipo ikashuka Aya hii.

BAINA YA KUHAMA MTUME KUTOKA MJI MTUKUFU WA MAKKA NA KUHAMA WAPALESTINA KUTOKA ARDHI TAKATIFU

Katika maajabu ya sadfa ni kuafikiana - bila ya kukusudia - kufikia kwangu kufasiri Qur'an kwenye Aya ya Hijra mwanzo wa mwaka 1388 A.H. na Israel inakalia ardhi yetu takatifu, watu wetu wanahama wakikimbia mateso na mauaji waliyoyafanya waisrael na wanayoendelea kuyafanya.

Sadfa hii imenifanya nilinganishe tukio la uchokozi wa washirikina katika Makka kwa waislamu na kutolewa kwao mijini mwao, na tukio la uchokozi wa waisrael; au kwa usahihi zaidi uchokozi wa kikoloni kwenye ardhi takatifu na kuwatoa wenyeji mijini mwao.

Kisha nikatoka kwenye mlinganisho huu kufikia Ibra na mazingatio kutokana na jihadi ya Mtume(s.a.w.w) na waislamu katika kuhama kwao na kupanga mipango iliyowapeleka waislamu kwenye kilele cha ushindi kwa maadui zao, kuuvunja utaghuti na uchokozi wake na kuwasimamisha mamwinyi wa kiquraish, waliowatoa Makka mbele ya Mtume wakiwa madhalili, wenye kusalimu amri wakimsikiliiza akiwaambia "Mnadhani nitawafanya nini?"

Baadhi ya watu wanaweza kudhani kuwa lengo la kwanza la Mtume na waislamu ni kuikimbiza tu dini yao kutoka kwa washirikina ambao waliwaingilia kwa kuwaudhi na kuwazuia kutekeleza nembo za dini yao na amali za kidini; sawa na anavyokimbilia Daruweshi msikitini ili aswali vizuri kwa kuepuka fujo na kelele. Hapana! Hijra ya waislamu ilikuwa mbali na kuwa na undani zaidi ya hilo.

Dalili ya hilo ni natija na malengo yaliyotekelezwa na Hijra hiyo. Hijra hiyo zaidi ya kuikimbiza dini, ilikuwa na mipango iliyopangwa vizuri ya uandalizi wa vita; sawa na jeshi linapojitenga kutoka uwanja wa vita kwenda mahali pengine ili kujiandaa kwa shambulio kubwa la kummaliza adui. Mtume(s.a.w.w) baada ya kufika Madina aliwafanya ndugu Masahaba na akazichanganya pamoja nyoyo za mahasimu na akayeyusha vinyongo na vidonge walivyokuwa navyo.

Baada ya kukamilisha kazi hiyo aliwahimiza waislamu jihadi na kuwahimiza kulinda heshima yao na itikadi yao, na kumdhaminia pepo atakayepigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kupata utukufu na cheo duniani na akhera kwa atakayepona kifo.

Baada ya mafunzo haya kuwaingia, Mtume akaanza kuwaunganisha kijeshi na kuwazoesha vita vidogo vidogo akiwapeleka huku na huko; mara nyingi akiviongoza mwenyewe. Waislamu wakawa na amani na raha; na amani ya Maquraish ikaingia kwenye wasiwasi. Hatimaye vita vidogo vikageuka na kuwa vita vikubwa, huku waislamu wakijitolea roho zao na mali zao, mpaka ukaja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi.

﴿وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا ﴾

"Na akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu" (9: 40)

Nadhani ishara hii inatosha kuchukua ibra ambayo ni wajibu kunufaika nayo katika balaa letu na israel na wanaoisaidia

Mtume(s.a.w.w) alihama kutoka Makka kwa sababu ya uchokozi wa washirikina waliokuwa wakimfanyia yeye na masahaba wake. Na wapalestina nao walihama kutoka ardhi takatifu kwa uchokozi wa kizayuni na kutaka kuwatawala wao wanawake wao na watoto wao. Hijra ya waislamu wakati huo ilikuwa ni kujiepusha na maangamizo na kujitenga kutoka uwanja wa vita ili kukusanya nguvu na kujiandaa kwa shambulio la kummaliza adui.

Kwa hiyo basi ni wajibu kuwa kutoka kwa wapalestina mijini kwao kuwe ni kwa makusudio haya na kwa lengo hili; sio kwa kuwaachia wanyang'anyi Baitul- Maqdis waichezee.

Mtume alianza Hijra yake kwa kufanya udugu baina ya masahaba zake. Kwa hiyo ni juu ya viongozi wa kiarabu na waislamu, kuanza kufanyiana udugu na kusafiana nyoyo; wawe wamoja ili waweze kumkabili adui; sawa na alivyofanya Mtume kabla ya kukabiliana na washirikina. Mwenye kuepuka njia hii basi amekutana na waisrael na ametekeleza malengo yao, atake asitake.

Mtume alituma vikosi vidogo kubabaisha washirikina, alivipa vikosi hivyo mahitaji yao. Ni wajibu kwa waarabu na waislamu kuwashujaisha wanaojitolea mhanga na wengineo na kusaidiana nao hadi mwisho, ili kuwatia wasiwasi waisrael.

Mtume aliwaandaa waislamu wote kwa vita vikubwa na kuung'oa ushirikina na mizizi yake baada ya kuota mizizi, karibu karne nzima, katika kila sehemu ya ardhi ya Bara Arabu. Na hivyo ndivyo inavyopasa kwa kila kiongozi wa waarabu na waislam.

Ikiwa hatutalizingatia somo hili kutokana na turathi zetu na Historia yetu na kuwa sote ni askari katika askari wa Mwenyezi Mungu na wa nchi, basi hatutastahiki jina la uarabu na warabu, wala la uislamu na waislam; hata kwa jina za binadamu na ubinadamu; baada ya kuwa hizi ni zama za kujitolea na kutekeleza; na kujikomboa na kila aina ya dhulma na unyonyaji.

Tumalizie kwa kuwapa salaam watoto wetu wapiganaji waliojitolea mhanga ambao wameonyesha mfano mzuri wa kishujaa katika nchi yetu iliyovamiwa, wakauthibitishia ulimwengu wote kwamba sisi tuko katika zama za kujitolea na kupigania uhuru na heshima.

﴿وَإِذَا ضَرَبْتُمْ فِي الْأَرْضِ فَلَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَقْصُرُوا مِنَ الصَّلَاةِ إِنْ خِفْتُمْ أَن يَفْتِنَكُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنَّ الْكَافِرِينَ كَانُوا لَكُمْ عَدُوًّا مُّبِينًا ﴾

101.Na mnaposafiri katika ardhi, si vibaya kwenu kama mkifupisha Swala, ikiwa mnaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa. Hakika makafiri ni maadui wenu walio wazi.

﴿وَإِذَا كُنتَ فِيهِمْ فَأَقَمْتَ لَهُمُ الصَّلَاةَ فَلْتَقُمْ طَائِفَةٌ مِّنْهُم مَّعَكَ وَلْيَأْخُذُوا أَسْلِحَتَهُمْ فَإِذَا سَجَدُوا فَلْيَكُونُوا مِن وَرَائِكُمْ وَلْتَأْتِ طَائِفَةٌ أُخْرَىٰ لَمْ يُصَلُّوا فَلْيُصَلُّوا مَعَكَ وَلْيَأْخُذُوا حِذْرَهُمْ وَأَسْلِحَتَهُمْ وَدَّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ تَغْفُلُونَ عَنْ أَسْلِحَتِكُمْ وَأَمْتِعَتِكُمْ فَيَمِيلُونَ عَلَيْكُم مَّيْلَةً وَاحِدَةً وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن كَانَ بِكُمْ أَذًى مِّن مَّطَرٍ أَوْ كُنتُم مَّرْضَىٰ أَن تَضَعُوا أَسْلِحَتَكُمْ وَخُذُوا حِذْرَكُمْ إِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا﴾

102.Na utakapokuwa kati yao, ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na washike silaha zao. Watakaposujudu na wawe nyuma yenu; Na lije kundi jingine ambalo halijaswali, waswali pamoja na wewe na washike hadhari yao na silaha zao. Wanataka wale waliokufuru lau kama nyinyi mwasahau silaha zenu na vifaa vyenu ili wawavamie mvamio wa ghafla. Wala hapana vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkiwa wagonjwa kuweka silaha zenu, Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.

﴿فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا﴾

103.Mtakapomaliza Swala, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kusimama na kwa kukaa na kwa (kulala) ubavu. Mtakapopata amani, basi simamisheni Swala, Hakika Swala kwa waumin ni faradhi iliyoekewa wakati maalum.

SWALA YA HOFU

Aya 101- 103

MAANA

Swala haiachwi kwa hali yoyote; hata kwa maradhi, vita, au safarini. Anaitekeleza kila mwenye kukalifiwa na sharia kiasi cha uwezo wake; iwe ni kusimama au kukaa; akishindwa ataitekeleza hali ya kulala ubavu. Hata bubu pia ni wajibu kwake kutingisha ulimi wake na kuishiria kwa mkono wake badala ya kutamka, Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh.

Na mnaposafiri katika ardhi, si vibaya kwenu kama mkifupisha swala ikiwa mnaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa.

Aya hii imeshuka katika hukumu ya jihadi na hofu; sawa na Aya zilizotangulia, kwani mfumo wa zote ni mmoja. Uwazi zaidi wa kuwa mfumo mmoja ni kauli yake Mwenyezi Mungu: Ikiwa mtaogopa kuwa wale waliokufuru watawaletea balaa. Kwa sababu makusudio ya balaa hapa ni kuua. Ama safari imekuja mahali pa aghalabu, sio kuwa ni sharti.

Ama kauli yake 'si vibaya kwenu' makusudio yake ni wajibu na lazima sio ruhusa na kuhalalisha. Kwa sababu Hadith zimefasiri ulazima; kama vile Aya ya Tawaf:

﴿فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا﴾

"Basi anayehiji katika nyumba hiyo, au kufanya umra, si vibaya kwake kuvizunguka (vilima) hivyo viwili" (2:158)

Kwa kuwa Aya imekuja katika Swala ya hofu si Swala ya kupunguza ya msafiri, basi makusudio ya kauli yake Mwen yezi Mungu kufupisha Swala ni kupunguza idadi ya rakaa na kugeuza umbo la Swala, kulingana na dharura iliyopo.

Swala ya hofu ina sharti. Sharti lake muhimu ni kuwa upande wa maadui kuna nguvu zinazowawezesha kuhujumu na kuvamia. Ama aina yake, Shahid wa pili amesema katika Lum'a: ni nyingi zinazofikia kumi inasihi kwa jamaa na kwa mmoja mmoja.

Ifuatayo ni namna y a Swala ya hofu kwa mtu pekee aliyoielezea mwenye Kitab Ash-sharai: "Ama Swala ya hofu ni mfano wa hali ya kufikia kuuana. Ataswali kiasi atakachoweza, iwe ni kwa kusimama, kwenda au kupanda.

Ataelekea Qibla kwa Takbira ya kuhirimia; kisha ataendelea ikiwezekana kuendelea, vinginevyo, ataelekea Qibla kwa itakavyowezekana kwake, na ataswali kwa udhuru wa kuelekea popote patakapomwezekania. Ikiwa hakuweza kushuka, ataswali akiwa amepanda na atasujudu juu ya kiti cha saruji yake; kama hakuweza basi ataashiria, kama atakuwa (anazidi) kuhofia basi ataswali kwa tasbih, bila ya kurukuu na kusujudu. Atasema badala ya kila rakaa "Subhanullah Wal-hamdulillaah wa Lailaha illa Ilah Wallahu Akbar."

Sura hii inatosha kuwa ni dalili kwamba Swala ni laizma, hasamehewi hata katikati ya mapigano na wala wakati wa kukata roho. Na kwamba mtu ataitekeleza kwa namna na hali yoyote atakavyoweza.

Na utakapokuwa kati yao, ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na washike silaha zao.

Huu ni ubainifu wa Swala ya hofu ya jamaa. Maana yake, ukitaka Ewe Muhammad kuswali jamaa na wapiganaji, basi gawa makundi mawili: Moja liswali na wewe wakiwa na silaha zao; na la pili lisimame kulinda; kama ambavyo inaswihi jamaa pamoja na Mtume(s.a.w.w) ; vile vile inaswihi pamoja na mtu mwingine.

Watakaposujudu na wawe nyuma yenu.

Yaani watakaposujudu wale wanaoswali na Mtume(s.a.w.w) , lisimame kundi linalolinda nyuma ya wenye kuswali.

Na lije kundi jingine ambalo halijaswali, waswali pamoja na wewe na washike hadhari yao na silaha zao. Yaani baada ya kumaliza kundi la kwanza kuswali, kundi la pili lichukue mahali pa kundi la kwanza katika Swala na kundi la kwanza lichukue mahali pa ulinzi.

Wanataka wale waliokufuru lau kama nyinyi mwasahau silaha zenu na vifaa vyenu ili wawavamie mvamio wa ghafla.

Huu ni ubainifu wa hekima iliyofanya kuwekwa Swala ya aina hii. Hekima yenyewe ni kutopata fursa adui ya kuwavamia wakati wanaswali.

Wala hapana vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkiwa wagonjwa kuweka silaha zenu.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaamrisha walioswali kuchukua silaha, akawapa ruhusa ya kuziacha ikiwa wanaona uzito wa kuzichukua kwa sababu ya mvua au ugonjwa, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu amewalazimisha wajilinde na wawe macho na adui asijewaingilia ghafla.

Mtakapomaliza Swala, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kwa kusimama na kwa kukaa na kwa (kulala) ubavu.

Makusudio ya Swala hapa ni Swala ya hofu. Maana ni kuwa kumtaja Mwenyezi Mungu ni vizuri katika hali yoyote si katika Swala tu. Imam Ali(a.s) amesema:"Amefaradhisha Mwenyezi Mungu katika ndimi zenu dhikri na akawausia takwa na akaijaalia ndio mwishilio wa haja yake kwa viumbe vyake."

Anasema Ibn Al-arabi katika Futuhatil-Makkiyya J.5: "Mwenye kumtaja Mwenyezi Mungu katika kisimamo chake kukaa kwake na kulala kwake, basi amekusanya yote."

Mtakapopata amani, basi simamisheni Swala; Hakika Swala kwa Waislamu ni faradhi iliyowekewa wakati maalum.

Yaani wakati wowote vita itakapotulia na hofu ikiwaondokea basi ni juu yenu kutekeleza Swala kwa wakati wake wala msipuuze.

Tumezungumzia kuhusu Swala na jinsi uislamu ulivyoipa kipaumbele, katika Aya zilizotangulia; kama vile (2: 238- 239).

Unaweza kuuliza : Aya imewajibisha Swala ya hofu, ambapo vita vilikuwa vya panga na mikuki. Lakini hivi sasa kuna maendeleo ya silaha za vita kiasi ambacho hatufahamu katika silaha za kuangamiza, Kwa hiyo si inapasa Swala ya hofu iondolewe kwa vile maudhui yake hayapo?

Jibu : Lililosababisha Swala hii ni hofu, bila ya kuangalia vita na ala zake, ziwe za zamani au za kisasa. Kwa hiyo ikipatikana kwa sababu zisizokuwa za vita, basi imejuzu kuifupiliza Swala kwa idadi ya rakaa na kwa aina.

Mwenye Al-jawahiri anasema: "Kukiwa na hofu ya mafuriko, wanyama, nyoka, moto au mengineyo, basi inajuzu kuswali Swala ya shida ya hofu. Kwa hiyo atapunguza idadi na namna, Kwa kukosekana tofauti katika sababu ya hofu iliyoruhusiwa, Kwani aliulizwa Imam Jafar as-Sadiq(a.s) kuhusu anayehofia wanyama au wezi ataswali vipi? Akasema: "Atapiga Takbira na kuashiria."

Tunasisitiza tena kuwa Swala haiwezi kumwondokea mtu kwa hali yoyote. Na kwamba kila mtu anaitekeleza kwa namna anavyoweza katika maneno na vitendo, Akishindwa ataashiria, akishindwa kuashiria ataleta picha ya Swala moyoni mwake.

﴿وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ إِن تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا يَرْجُونَ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا﴾

104.Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu. Ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi mwenye hekima.

MSILEGEE KATIKA KUWAFUATA

Aya 104

MAANA

Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu, Ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji.

Lau kama Wahyi ungelishuka hivi sasa katika hali yetu na waisrael, basi usingezidi hata herufi moja ya Aya hii. Haja kubwa iliyopo sasa ya kupambana na adui huyu mwovu na fedhuli na kukomesha dhulma yake, ni kujifunga kib webwe na kumtegemea Mwenyezi Mungu na sisi wenyewe na kutowasikiliza wakoloni wanaotaka kutunyonya; wanaofanya propaganda ili watudanganye tuache nguvu zetu.

Kumtetemekea adui tu kunampa faida na kunamsaidia, sikwambii kumwogopa. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akatukataza kumwogopa adui wa Mwenyezi Mungu na wa ubinadamu kwa hali yoyote ilivyo na itakavyokuwa; na kutuamrisha udhabiti katika kupambana naye.

Vilevile ametuzindua kuwa tunamwumiza adui, kama anavyotuumiza, lakini sisi tuko zaidi kuliko yeye, kwa sababu sisi twamwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu.

Ama Israel inawategemea wakoloni na ndugu zao mashetani walioitengeneza; wakawasheheni silaha na mali, wakawahimiza kufanya uchokozi na kuwasaidia katika Umoja wa mataifa na katika Baraza la usalama.

Hapana shaka yoyote kuwa kama tukijitegemea na kuwa na msimamo imara wa ikhlasi na tukafanya juhudi zetu zote, kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, ushindi utakuwa wetu tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu, katika Aya nyingine anasema:

﴿فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّـهُ مَعَكُمْ ﴾

Wala msilegee na kutaka suluhu na nyinyi ndio mko juu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja nanyi. (47:35)

Waislamu wako juu kwa itikadi yao historia yao na uwezo wao, Nguvu hizo haziendi wala hazitakwenda bure. Kwa hiyo hapana budi kuwa athari zake zitadhihiri kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, iwe sasa au baadaye.

﴿إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ وَلَا تَكُن لِّلْخَائِنِينَ خَصِيمًا﴾

105.Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu; wala usiwe mtetezi wa wenye kufanya hiyana.

﴿وَاسْتَغْفِرِ اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا﴾

106.Na muombe maghufira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

﴿وَلَا تُجَادِلْ عَنِ الَّذِينَ يَخْتَانُونَ أَنفُسَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ خَوَّانًا أَثِيمًا ﴾

107.Wala usiwatetee wale ambao wamezihini nafsi zao, Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye haini mwenye dhambi.

﴿يَسْتَخْفُونَ مِنَ النَّاسِ وَلَا يَسْتَخْفُونَ مِنَ اللَّـهِ وَهُوَ مَعَهُمْ إِذْ يُبَيِّتُونَ مَا لَا يَرْضَىٰ مِنَ الْقَوْلِ وَكَانَ اللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطًا ﴾

108.Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, na yeye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua vyema muyatendayo.

﴿هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ جَادَلْتُمْ عَنْهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فَمَن يُجَادِلُ اللَّـهَ عَنْهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَم مَّن يَكُونُ عَلَيْهِمْ وَكِيلًا ﴾

109.Nyinyi ndio ambao mnawatetea katika maisha ya duniani, basi ni nani atakayewatetea kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama au ni nani watakayemtegemea?

﴿وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا﴾

110.Na mwenye kutenda uovu au akadhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.

﴿وَمَن يَكْسِبْ إِثْمًا فَإِنَّمَا يَكْسِبُهُ عَلَىٰ نَفْسِهِ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴾

111.Na mwenye kuchuma dhambi, basi anajichumia mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

﴿ وَمَن يَكْسِبْ خَطِيئَةً أَوْ إِثْمًا ثُمَّ يَرْمِ بِهِ بَرِيئًا فَقَدِ احْتَمَلَ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴾

112.Na mwenye kuchuma kosa au dhambi, kisha akamisingizia asiye na kosa, basi hakika amejitwika dhuluma na dhambi iliyo wazi.

﴿وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكَ وَرَحْمَتُهُ لَهَمَّت طَّائِفَةٌ مِّنْهُمْ أَن يُضِلُّوكَ وَمَا يُضِلُّونَ إِلَّا أَنفُسَهُمْ وَمَا يَضُرُّونَكَ مِن شَيْءٍ وَأَنزَلَ اللَّـهُ عَلَيْكَ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَعَلَّمَكَ مَا لَمْ تَكُن تَعْلَمُ وَكَانَ فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكَ عَظِيمًا﴾

113.Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, lingedhamiria kundi katika wao kukupoteza; wala hawazipotezi ila nafsi zao; wala hawatakudhuru na lolote. Na amekuteremshia Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na amekufunza uliyokuwa huyajui. Na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa.

KUWATETEA WAHAINI

Aya 105 - 113

MAANA

Mwenye kufuatilia tafsir, akachunguza Aya hizi na kufikiri vizuri maana yake atakubali kuwa zilishuka kuhusiana na mwislamu mmoja aliyeiba bidhaa, akamsingizia mtu asiyekuwa na hatia; na kwamba jamaa wa mwizi walimwendea Mtume(s.a.w.w) na kujaribu kumkinaisha kwa mbinu mbalimbali wamkinge mtu wao kumwepushia janga la wizi; na kama hakufanya hivyo, basi mtu wao ataangamia.

Karibu Mtume aitikie maombi ya wapotevu hao lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimlinda mchukuzi mwaminifu wa wahyi wake na mfikishaji wa sharia yake. Akamhifadhi na njama zao na kumfichulia uhakika. Akafichuka mwizi na kusalimika yule aliyesingiziwa. Inasemekana pia kuwa aliyesingiziwa alikuwa ni myahudi na mwizi ni ansari; na kwamba yeye baada ya kufichuka alikimbia na kujiunga na washirikina. Dhahiri ya Aya inafungamana kabisa na tukio hili. Ufuatao ndio ubainifu wake:

Hakika tumekuteremshia Kitabu kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu.

Tunasema - Tukimwomba msamaha Mwenyezi Mungu - kwamba msemo huu unatoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Mtume wake mtukufu ukiashiria aina ya lawama.

Kama kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia: Nimekuchagua mimi mwenyewe, nikakuteremshia Qur'an ili uhukumu baina ya watu kwa lile unalojua kwa yakini kuwa ni hukumu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Sasa wadanganyifu wamekurubia kukuhadaa, lakini Mwenyezi Mungu amekulinda na walivyokupangia - kumtia hatiani asiye na makosa - kwa kukufichulia uhakika na njama zao.

Hakuna linalofahamishwa na hali hii zaidi ya kuwa kuhifadhiwa na dhambi (Isma) si jambo la kulazimishwa; kama urefu na ufupi; isipokuwa ni wasifu unaomwepusha huyo maasum kufanya haramu, ingawaje anaweza kufanya, na kumpa msukumo wa kufanya wajibu, ingawaje anaweza kuuacha.

Aya hii ni jibu na kubatilisha kauli ya wasemao kuwa Mtume ana hukumu katika baadhi ya masuala kwa ijtihadi yake. Aya inaonyesha wazi kuwa yeye hahukumu ila kwa wahyi utokao kwa Mwenyezi Mungu. Zaidi ya hayo ni kwamba mwenye kujitahidi anapata na kukosa, na Mtume ni mwamuzi wa tofauti za wenye kujitahidi na kubainisha kosa la mwenye kukosea na usawa wa mwenye kupatia.

Wala usiwe ni mtetezi wa wenye kufanya hiyana.

Mtume hakuwatetea, na ni muhali kwa Mtume kuwatetea wanaofanya hiyana. Na kukatazwa kwake kutetea hakulazimishi kutokea hilo kwake, bali ni kwamba kukatazwa haramu kunatokea kabla ya kuifanya, Lau kungekuwa kunakuja baada ya kutokea lengo la kukatazwa basi litabatilika.

Unaweza kuuliza : Ikiwa kufanya haramu ni muhali kwa Mtume kutokana na kuhifadhiwa kwake na dhambi, kwa nini akakatazwa?

Jibu : Mwenyezi Mungu anaweza kuielekeza amri yake kwa Mtume wake katika hali zote. Kwa sababu ni amri kutoka kwa aliye juu kwenda kwa aliye chini yake. Zaidi ya hayo, ni kwamba amri ya wajibu na katazo la haramu mara nyingi huelekea kwa Mitume kwa kuelewesha hukumu tu.

Na muombe maghufira Mwenyezi Mungu, Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Anasema Tabari katika Tafsir yake kuwa Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kuomba maghufira ya kusamehewa dhambi za kumtetea mhaini, Na sisi tunaomba maghufira kutokana na tafsir hii. Kwani Mtume(s.a.w.w) - kama tulivyotangulia kueleza - hakumtetea mhaini. Kwa dalili ya Aya itakayofuatia (113):

Ama amri ya kutaka maghufira ya dhambi hailazimishi kupatikana dhambi, Tafsiri ya Aya tunavyoiona ni kuwa Mtume(s.a.w.w) kwa kuwa ni mtu, anaweza akadhania vizuri jambo lisilostahiki; ikamdhihirikia hakika kwa njia ya wahyi au nyingine kabla ya kuchukua uamuzi wowote wa dhana yake nzuri. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha kuomba maghufira kutokana na ile dhana nzuri iliyomtokea ambayo haikuwa mahali pake. Makusudio ni kujichunga na kujitoa shakani na kutotegemea lolote ila baada ya yakini.

Wala usiwatetee wale ambao wamezihini nafsi zao, Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye haini, mwenye dhambi.

Kwa dhahiri msemo unaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) , lakini ulazima wake unamhusu kila aliye baleghe mwenye akili, hasa makadhi na mahakimu.

Ama waliozihini nafsi zao ni wale waliofanya dhambi na kuwasingizia watu wengine wasio na hatia; na mwenye kuwatetea basi yeye ni kama wao. Maana ya mtu kujihini yeye mwenyewe ni kujibebesha mzigo wa adhabu kwa kuharibu mambo ya wajibu na kufanya haramu.

Tumetangulia kueleza kuwa Mtume(s.a.w.w) hakutetea wala hatawatetea wahaini, na Aya hii inatilia mkazo kauli yake:Wala usiwe ni mtetezi wa wenye kufanya hiyana ; Vilevile inabainisha kuwa mwenye kumdhulumu mwingine amejidhulumu yeye mwenyewe na kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu atamwadhibu kila haini, mwenye kujidhulumu na anayewadhulumu wengine.

Wanajificha kwa watu wala hawajifichi kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao walipokula njama usiku kwa maneno asiyoyapenda.

Mfanya makosa huficha makosa na kujificha gizani asionekane na watu kwa kutaka sifa au kuogopa shutuma zao. Ambapo ilikuwa afanye kinyume - ajifiche na Mwenyezi Mungu - kama anaweza, na wala asijishughulishe na watu kabisa. Kwa sababu Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye kumiliki madhara na manufaa.

Asiyekuwa Mwenyezi Mungu hawezi kumtosheleza binadamu na kitu chochote. Sifa za watu na shutuma zao ni maneno yanayokwenda na upepo. Ikiwa kujificha na Mwenyezi Mungu hakuwezekani, basi kumtii ni lazima, sio pendekezo.

Nyinyi ndio ambao mnawatetea katika maisha ya duniani, basi ni nani atakayewatetea kwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama au ni nani watakayemtegemeea?

Msemo unaelekezwa kwa watu wa yule mwizi mhaini. Kwa sababu wao peke yao ndio waliomtetea na kumgombea.

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu - ambaye limetukuka neno lake - amewafahamisha kuwa kumtetea mhaini hakuwezi kumfaa mhaini siku atakayofichuliwa na Mwenyezi Mungu:"Na jitengeni leo enyi waovu" (36:59)

Na mwenye kutenda uovu au akadhullumu nafsi yake, kisha akaomba maghufira kwa Mwenyezi Mungu atamkuta Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Huyo ndiye mwenye kutoka katika dhambi mwenye kuikiri na kutubia. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mkali wa adhabu, basi pia ni mwenye kumghufiria mwenye kutubia, mwenye kumrehemu anayekimbilia kwake.

Kuna hadith inayosema:"Hakika Mwenyezi Mungu hachoki, mpaka mchoke; mkiacha naye huacha."

Yaani mkiacha kutubia dhambi naye huacha kusamehe, Kwa hiyo la sawa kwa wale waliomtetea mwenye hatia, ni kumzindua kutokana na kosa lake na kumpa nasaha ya kutubia, kama wangelikuwa ni wanasihi waumin wa kweli.

Katika Aya hizi nne kuna maneno ambayo hapana budi kuyafafanua ili ieleweke tofauti yake ambayo kwa dhahiri inaonekana kama ni moja tu inayokaririka: Neno la kwanza ni dhambi, lilioko katika Aya ya 107, 111 na 112. La pili na la tatu ni uovu na kujidhulumu, yaliyo katika 111. La nne ni kosa, lililotajwa katika Aya ya 112.

Maneno yote haya yanakusanya maana moja ambayo ni maasi. Tofauti ni kuwa uovu ni ule unaofanyiwa mtu mwingine, kujidhulumu ni kujiingiza katika madhara kwa kuacha wajibu au kutenda haramu na kosa ni lile linalofanywa bila ya udhuru wowote; kama vile mzembe asiyejua anayekosea kutekeleza wajibu kwa kutojua ingawaje ana uwezo wa kujifundisha. Hukumu yake ni kama hukumu ya mwenye kukusudia makosa. Kwa sababu amepuuza kufanya utafiti na kuuliza.

Na dhambi ni kufanya kosa pamoja na kujua na kung'angania kulifanya. Dhambi ni ujumla inakusanya uovu na kujidhulumu. Kwa hiyo maana yanakuwa:Mwenye kutenda uovu au akadhulumu nafsi yake… mpaka mwisho " ni kuwa mwenye kumfanyia uovu mwingine kwa kumtukana au ku piga na mengineyo au kuifanyia nafsi yake tu; kama vile yamini ya uongo kisha akatubia, Mwenyezi Mungu humkubalia toba yake; kama vile hakufanya uovu wowote au kudhulumu.

Na maana ya:Mwenye kuchuma dhambi, basi anajichumia mwenyewe . Ni kwamba; mwenye kufanya dhambi, basi amejifanyia uovu mwenyewe, ni sawa awe amefanya uzembe kwa uovu huu yeye peke yake au alimfanyia mwingine.

Maana ya:Mwenye kuchuma kosa au dhambi, kisha akamsingizia asiye na kosa, basi hakika amejitwika dhuluma na dhambi iliyo wazi , ni kuwa mwenye, kumsingizia mtu mwingine kwa kosa asilokuwa nalo, ataadhibiwa adhabu ya uzushi wa makusudi; ni sawa alifanya kosa hilo akamsingizia mwingine kwa makusudi, (hilo linafahamishwa na neno 'dhambi'), au hakulifanya yeye, lakini akamsingizia mwingine kabla ya kuthibitisha, (hilo linafa- hamishwa na neno 'kosa') Lengo ni kuwa haifai kwa yeyote kumbandika mtu mwingine jambo lolote, mpaka awe na yakini nalo kama jua.

Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, lingedhamiria kundi katika wao kukupoteza; wala hawazipotezi ila nafsi zao; wala hawatakudhuru na lolote.

Makusudio ya kundi ni wale waliomtetea mwizi; na dhamiri ya katika wao inawarudia watu wake na wasaidizi wake. Makusudio ya kukupoteza ni kukuhadaa kwa maneno ya makosa na masilahi. Wala hawazipotezi ila nafsi zao, kwa sababu kujaribu kupoteza kunalazimisha upotevu; na mwenye kupoteza ni mpotevu na ziada.

Maana kwa ujumla ni kuwa kundi katika wasaidizi wa mwizi na jamaa zake, walikula njama ya kukuhadaa na haki na kujaribu uwe upande wao katika kumwokoa mtu wao nawe ulikaribia kuwakubalia kwa yale mazuri waliyokudhihirishia, lakini Mwenyezi Mungu akakuhifadhi nao; akakufichulia njama zao na kurudisha vitimbi vyao kwao.

Aya hii ni jibu la wazi kwa wale wanaodai kwamba Mtume(s.a.w.w) aliwatetea wahaini. Kwani kauli yake Mwenyezi Mungu "Na rehema yake" na "Wala hawatokudhuru na chochote," hazikubali taawili yoyote na shaka yeyote kuwa Mtume hakumtetea mwizi na mhaini. Na kwamba aliyefanya haya ni mwingine.

Na amekuteremshia Mwenyezi Mungu Kitabu na hikima na amekufunza uliyokuwa huyajui. Na fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako ni kubwa.

Kitabu ni Qur'an na hekima ni utume. Ikiwa Mwenyezi Mungu amewajibisha Muhammad kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumfanya ni mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume wote na kumfundisha asiyoyajua, basi ni wajibu kwa waarabu kumshukuru Muhammad kwa kuwa wamekuwa ni wenye kutajika baada ya ujinga wao wa wajinga. Vilevile wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumjaalia mtukufu zaidi wa viumbe kuwa ametokana na wao sio kwa wengine.