TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16042
Pakua: 2230


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16042 / Pakua: 2230
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

﴿لَّا يُحِبُّ اللَّـهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَن ظُلِمَ وَكَانَ اللَّـهُ سَمِيعًا عَلِيمًا ﴾

148. Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa mwenye kudhulumiwa; na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mjuzi.

﴿إِن تُبْدُوا خَيْرًا أَوْ تُخْفُوهُ أَوْ تَعْفُوا عَن سُوءٍ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَفُوًّا قَدِيرًا ﴾

149.Mkidhihirisha heri au mkiificha au mkisamehe uovu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwingi wa kusamehe, Muweza.

DHALIMU HAHESHIMIWI

Aya 148 - 149

MAANA

Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuharamisha kusengenya amesema:

﴿وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا﴾

"Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine" (49:12)

Na katika aliyoyasema kuhusu kuharimisha dhulma ni:"Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate madhalimu." (7:44)

Na amesema katika Aya tuliyo nayo: Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa mwenye kudhulumiwa.

Tukiunganisha Aya hii na Aya ya kusengenya, maana yanakuwa ni mtu asitaje aibu na maovu ya mwingine, ila yule aliyedhulumiwa, anaweza kutangaza na kudhihirsha uovu kwa kudhulumiwa.

Maana ya dhulma ni maarufu. Ama kusengenya kuliko haramu, mafakihi wamekueleza kuwa ni kumtaja mwingine kwa jambo analolichukia akiwa hayuko; kama vile kumvunjia heshima yake na watu wamcheke; ni sawa hilo awe analo au ni uongo na uzushi. Wameuondoa uharamu wa kumsengenya dhalimu na mwenye kujidhulumu, kwa kuudhihirisha ule uovu wake na kutojali kwake yanayosemwa na anayoambiwa.

Katika Kitabu Makasib cha Sheikh Ansari, imesemwa kuwa sehemu zinazoondolewa hazina idadi; Kwa sababu kusengenya kunakuwa haramu pale tu ikiwa kutangaza huko hakuna masilahi yenye nguvu, Vinginevyo, basi itakuwa wajibu kutangaza na kueneza kwa kuangalia masilahi yenye nguvu zaidi, kama ilivyo katika kila maasi ya haki za Mwenyezi Mungu na haki za binadamu.

Kwa hali hiyo basi inajuzu kisharia migomo na maandamano dhidi ya serikali dhalimu, bali itakuwa ni wajibu ikiwa hakuna njia nyingine ya kuondoa dhulma isiyokuwa hiyo, kwa sharti ya kuwa isilete ghasia na madhara kwa wengine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hatiiwi pale anapoasiwa. Na Uislamu unachunga hadhi na heshima ya binadamu mpaka aingilie heshima ya mwenzake. Hapo heshima inaondoka na kuwa halali kuvunjwa na kudhalilishwa.

Ilivyo hasa ni kwamba dhuluma haihusiki tu na serikali dhalimu na vibaraka wao. Mtu yeyote aliyemchokoza mwengine kwa kauli au kitendo au akamnyima haki yake au akaichelewesha basi yeye ni dhalimu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: "Kubabaisha deni ni dhulma ". Katika Hadith nyingine anasema: "Mbabaishaji deni ni halali kumvunjia heshiTafsir ma". Mbabaishaji deni hapa ni yule asiyelipa deni na huku ana uwezo wa kuilipa.

Wamepokea Ahlul - Bait kutokana na babu yao amesema:"Mwenye kuishi na watu asiwadhulumu, akizungumza nao hawawadanganyi na akiwaahidi hawakhalifu, basi huyo ni katika ambao umekamilika murua wake, ni wajibu kumfanya ndugu na ni haramu kumsengenya mwongo na mvunja ahadi hana heshima."

Hivi ndivyo ulivyo Uislamu unachunga haki ya mtu maadamu naye anachunga haki za kibinadamu zilizoko kwa wenzake na kwake. Akipuuza basi naye atastahili kupuuzwa na kudharauliwa.

Mkidhirishia kheri au mkificha.

Hili ni himizo la kufanya kheri kwa siri au dhahiri.

Au mkisamehe uovu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwingi wa kusamehe, muweza.

Ni kweli kuwa ni vizuri kusamehe maovu, lakini ni pale utakapokuwa msamaha ni heri kwake wala hauna madhara kwa jamii. Ama ikiwa ni njia ya kumhimiza muovu aendelee na uovu na kueneza ufisadi, basi kumwadhibu ndiko kunakotakikana. Vinginevyo hakutakuwa na nidhamu na maovu yataenea. Mwenyezi Mungu anasema:

"Mna uhai katika kulipiza kisasi enyi wenye akili ili msalimike" (2:179) na amesema tena:"Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna" (2:193)

﴿إِنَّ الَّذِينَ يَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيُرِيدُونَ أَن يُفَرِّقُوا بَيْنَ اللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَيَقُولُونَ نُؤْمِنُ بِبَعْضٍ وَنَكْفُرُ بِبَعْضٍ وَيُرِيدُونَ أَن يَتَّخِذُوا بَيْنَ ذَٰلِكَ سَبِيلًا ﴾

150.Hakika ambao humkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na mitume wake na wakasema: tumeamini baadhi na kukataa baadhi; na wakataka kushika njia iliyo katikati ya haya.

﴿أُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَافِرُونَ حَقًّا وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ عَذَابًا مُّهِينًا﴾

151.Hao ndio makafiri kweli kweli na tumewaandalia makafiri adhabu idhalilishayo.

﴿وَالَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَلَمْ يُفَرِّقُوا بَيْنَ أَحَدٍ مِّنْهُمْ أُولَـٰئِكَ سَوْفَ يُؤْتِيهِمْ أُجُورَهُمْ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴾

152.Na wale ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wala wasifarikishe baina ya yeyote katika wao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.

WANAAMINI BAADHI NA KUKANUSHA BAADHI

Aya 150 - 152

MAANA

Hakika ambao humkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake na wakasema: Tumeamini baadhi na kukataa baadhi.

Mayahudi walimwamini Musa na Taurat, wakamkana Isa na Muhammad. Wakristo walimwamini Isa na Injil wakamkana Muhammad na Qur'an. Na Waislamu wamewaamini wote.

Kwa sababu, imani katika mtazamo wa kiislamu ni moja haigawanyiki wala hakuna njia ya kuigawanya. Imani hiyo ni kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na Malaika wake na Mitume wake wote na vitabu vyake. Mwenye Kukikana kimojawapo basi amekana vyote.

Na wakataka kushika njia iliyo katikati ya haya.

Yaani baina ya ukafiri na imani, ingawaje hakuna njia baina yake; hata mwenye kutia shaka tu anahisabiwa kuwa kafiri. Muulizaji akiuliza kuhusu hukumu ya asiyejua utume wa mmojawapo wa Mitume, basi tumeyafafanua hayo katika kufasiri (3:115) kifungu "Hukumu ya mwenye kuacha Uislamu". Hao ndio makafiri kweli kweli Hata kama wataamini baadhi, kwa sababu imani ni kwa vyote haigawanyiki. Na wale ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wala wasifarikishe baina ya yeyote katika wao, hao atawapa ujira wao.

Hawa ni Waislamu, wafuasi wa Muhammad bin Abdullah, ambaye amewaamrisha kuamini Mitume yote na akasema Mitume yote ni ndugu, dini yao ni moja na umma zao ni mbali mbali. Umetangulia ufafanuzi katika kufasiri Aya 136 ya Sura hii na (2:285).

﴿يَسْأَلُكَ أَهْلُ الْكِتَابِ أَن تُنَزِّلَ عَلَيْهِمْ كِتَابًا مِّنَ السَّمَاءِ فَقَدْ سَأَلُوا مُوسَىٰ أَكْبَرَ مِن ذَٰلِكَ فَقَالُوا أَرِنَا اللَّـهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْهُمُ الصَّاعِقَةُ بِظُلْمِهِمْ ثُمَّ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ مِن بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمُ الْبَيِّنَاتُ فَعَفَوْنَا عَن ذَٰلِكَ وَآتَيْنَا مُوسَىٰ سُلْطَانًا مُّبِينًا ﴾

153.Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshie Kitabu kutoka mbinguni. Hakika walimtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walisema:Tuonyeshe Mwenyezi Mungu waziwazi. Wakapigwa na radi kwa sababu ya dhulma yao. Kisha wakamfanya ndama (kuwa Mungu) baada ya kuwafikia hoja. Na tukawasamehe hayo Na tukampa Musa hoja zilizo wazi.

﴿وَرَفَعْنَا فَوْقَهُمُ الطُّورَ بِمِيثَاقِهِمْ وَقُلْنَا لَهُمُ ادْخُلُوا الْبَابَ سُجَّدًا وَقُلْنَا لَهُمْ لَا تَعْدُوا فِي السَّبْتِ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا ﴾

154.Na Tukanyanyua Tur juu yao kwa ahadi yao. Na tukawaambia: Ingilieni mlangoni kwa unyenyekevu. Na tukawaambia msipetuke mipaka ya Sabato. Na tukachukua kwao ahadi madhubuti.

WALISEMA TUONYESHE MWENYEZI MUNGU WAZIWAZI

Aya 153-154

LUGHA

Neno Taadu lina maana ya kupetuka mpaka. Makusudio yake hapa ni kutofanya kazi siku ya Jumamosi. Na limesomwa Tauddu kwa maana ya kufanya uadui.

MAANA

Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshie Kitabu kutoka mbinguni.

Makusudio ya watu wa Kitabu hapa ni Mayahudi wa Madina waliokuwa na msimamo wa kiadui na ukaidi kwa Mtume na wakamfanyia vitimbi vya kuendelea. Miongoni mwa ukaidi na balaa zao ni yale aliyoyaashiria Mwenyezi Mungu (swt) katika Aya hii - kutaka wateremshiwe Kitabu kutoka mbinguni kitakachomshuhudia na kwamba wakione wao na macho yao.

Kwa dhahiri ni kwamba walisema hivyo kwa njia ya kusumbua na ukaidi na wala sio kutaka hoja na ukweli. Kwa sababu miujiza yake iliyotangulia inatosha kumkinaisha mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki.

Mwenyezi Mungu akamjibia Mtume wake kwa kusema:Hakika walimtaka Musa makubwa kuliko hayo.

Yaani hakuna geni wala ajabu, ewe Muhammad, kukutaka uwateremshie Kitabu kutoka mbinguni, kwani walikwishamuuliza Musa makubwa kuliko hayo, walimtaka awaonyeshe Mwenyezi Mungu hasa. Walisema:

Tuonyeshe Mwenyezi Mungu waziwazi. Wakapigwa na radi kwa sababu ya dhulma yao. Kisha wakamfanya ndama (kuwa Mungu) baada ya kuwafikia hoja.

Imetangulia tafsiri ya matakwa yao haya na kumfanya kwao ndama kuwa Mungu katika (2:54-57) na pia tukazungumzia kauli za madhehebu kuhusu kuonekana Mwenyezi Mungu.

Inajulikana wazi kwamba waliotaka kumwona Mungu waziwazi na kumfanya ndama kuwa Mungu ni Mayahudi wa kwanza na wala sio wa Madina. Lakini hawa waliridhia na kuamini kila walilofanya mababu zao. Kwa hiyo ikafaa kunasibishiwa wao.

Na tukampa Musa hoja zilizo wazi.

Lakini Mayahudi wanadharau kila kitu wala hawalipi umuhimu jambo lolote ila likiwa lina moja kati ya mawili: Ama manufaa au nguvu. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawahofisha kwa jabali ambalo ameliashiria kwa kauli yake:Tukanyanyua Tur juu yao kwa ahadi yao.

Tur ni jina la mlima ambao Musa alizungumza na Mola wake. Mwenyezi Mungu anasema:"Na kwa Tur sininin (95:2)" Sinin na Sinai ni majina ya mahali palipo na mlima huo. Mwenyezi Mungu aliwaamrisha wana wa Israil kupitia kwa Musa waitumie Taurat wakakataa ndipo Mwenyezi Mungu akawainulia mlima juu yao mpaka wakakubali.

Kauli ya Mwenyezi Mungu;kwa ahadi yao , makusudio yake ni kuvunja ahadi yao juu yao wenyewe ya kulazimiana na dini kisha wakaacha.Lau si mlima wasingelirudia.

Kwa hiyo hapana ajabu kwa Israil kuasi nidhamu za kimataifa na kukataa maazimio ya Umoja wa mataifa na Baraza la usalama. Wamevunja ahadi na makubaliano mara kadhaa. Lau si kuwa na hofu wasingelitulia. Hapana ajabu wala geni! Hilo linalingana na historia ya wakale wao ambao Mwenyezi Mungu aliwainulia mlima ili watekeleze ahadi.

Na tukawaambia: Ingieni mlangoni kwa unyenyekevu. Imepita tafsir yake katika (2:58)

Na tukawaambia msipetuke mipaka ya Sabato. Vilevile imepita tafsir yake katika (2:65)

﴿فَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَاقَهُمْ وَكُفْرِهِم بِآيَاتِ اللَّـهِ وَقَتْلِهِمُ الْأَنبِيَاءَ بِغَيْرِ حَقٍّ وَقَوْلِهِمْ قُلُوبُنَا غُلْفٌ بَلْ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَيْهَا بِكُفْرِهِمْ فَلَا يُؤْمِنُونَ إِلَّا قَلِيلًا ﴾

155.Basi (tuliwalaani) kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao, na kuzikufuru kwao ishara za Mwenyezi Mungu, na kuua kwao manabii pasi na haki, na kusema kwao nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa kufuru yao. Basi hawataamini ila wachache tu.

﴿وَبِكُفْرِهِمْ وَقَوْلِهِمْ عَلَىٰ مَرْيَمَ بُهْتَانًا عَظِيمًا ﴾

156.Na kwa kufuru yao na kumsingizia kwao Maryam uwongo mkubwa.

﴿وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّـهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَـٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ وَإِنَّ الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا﴾

157.Na kwa kusema kwao: sisi tumemuua Masih Isa, mwana wa Maryam Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na hawakumuuwa wala hawakumsulubu, lakini alifananishwa kwao. Na hakika wale waliohitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo; hawana ujuzi ila kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini.

﴿بَل رَّفَعَهُ اللَّـهُ إِلَيْهِ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴾

158.Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwake, na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hekima.

﴿وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا ﴾

159.Na hakuna katika watu wa Kitabu ila humwamini yeye kabla ya kufa kwake, na Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.

KUVUNJA KWAO AHADI

Aya 155-159

MAANA

Basi (tuliwalaani) kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi yao.

Yaani tuliwalaani kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi waliyojilazimisha nayo na kuihakikisha katika nafsi zao, ambayo ni kuamini na kuyatumia mafunzo aliyokuja nayo Musa(a.s) . Kisha wakageuza na kubadilisha, wakaharamisha aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu na wakahalalisha aliyoyaharamisha.

Na kuzikufuru kwao ishara za Mwenyezi Mungu

Yaani kuzikataa hoja na dalili juu ya utume wa Isa na Muhammad(s.a.w.w)

Na kuwaua kwao Manabii pasi na haki

Kama vile Zakariya na Yahya, baada ya kuweko hoja ya utume wao.

Na kusema kwao nyoyo zetu zimefumbwa

Yaani zimezibwa haziingii chochote kutokana na wito wa Muhammad.

Waliyasema haya kwa Mtume Mtukufu kwa kukatisha tamaa kuwa wataamini utume wake na kuitikia mwito wake.

Bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa kufuru yao.

Ni jumla iliyoingia kati iliyokuja kujibu kauli yao kuwa nyoyo zetu zimefumbwa. Maana yake ni kuwa, nyoyo zenu hazikufumbika kimaumbile, isipokuwa kwa sababu ya kumkufuru kwenu Muhammad na kubobea kwenu kwenye upotofu ndiko kulikowafanya wagumu kama mawe na wagumu zaidi kuliko mawe.

Baada ya nyoyo zao kufikilia kiwango cha kutofunguka na haki kwa hali yoyote, wamekuwa kama wameumbwa na Mwenyezi Mungu bila ya nyoyo. Kwa kuzingatia hivi ndipo ikafaa kuambiwa kuwa Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri nyoyo zao. Tazama tafsiri (2:7)

Basi hawataamini ila wachache tu.

Kama vile Abdallah bin Salaam, Thaalab bin Saaya, Asad bin Ubaidullah na wengineo.

Na kwa kufuru yao na kumsingizia kwao Maryam uwongo mkubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekariri mara tatu kunasibisha ukafiri kwa Mayahudi:

Kwanza : kwa mnasaba wa kutaja ukanusho wao wa ishara za Mwenyezi Mungu na kuua Mitume.

Pili : Kwa mnasaba wa kusema kwao "Nyoyo zetu zimefumbwa."

Tatu : Kauli yao juu ya Maryam ambayo hawaisemi ila Wayahudi walioingizwa kwenye ukiristo na Amerika, na kuwapa silaha ili waingilie Baitul Maqdis na wavunjie heshima nembo za dini amabazo wanazitukuza Wakristo na Waislamu, hasa makanisa na makaburi ya Wakristo[1] .

1Ninaadikia maneno haya leo hii tarehe 28.4.1968 na Israil imepanga kufanya maonyesho makubwa ya kijeshi mnamo tarehe, 2.5.1968 kwenye mji wa Qudus; ingawaje Baraza la usalama limepitisha kwa kauli moja kutofanyika maonyesho hayo.

Na kwa kusema kwao: Sisi tumemua Masih Isa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Wamemsifu kwa jina la Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa kumchezea tu.

Na hawakumuua wala hawakumsulubu, lakini alifananishwa.

Mayahudi walipong'ang'ania kumua Bwana Masih (Isa), Mwenyezi Mungu alimfananisha mmoja wa wenye makosa anayestahiki kuuliwa. Inasemekana kuwa mkosaji huyo alikuwa ni Yuda ambaye aliongoza shambulio dhidi ya Bwana Masih. Mayahudi wakamkamata wakamwadhibu na kumsulubu kwa kufikiria kuwa ni Bwana Masih. Baada ya kumsulubu wakawa hamwoni mwenzao (Yuda) wakaduwaa na kusema ikiwa aliyesulubiwa ni Masih, basi yuko wapi mwenzetu? Na kama mwenzetu ndiye aliyesulubiwa, yuwapi Masih?

Na hakika wale waliokhitilifiana katika haya, wamo katika shaka nayo. Walihitilafiana Mayahudi na Wakristo kuhusu Bwana Masih(a.s) wakawa na misimamo ya kupingana. Mayahudi wakasema ni mwanaharamu; na Wakristo wakasema ni mwana wa Mungu.

Vile vile Mayahudi walisema: Tumemsulubu na kumzika ardhini bila ya kufufuka; na Wakristo wakasema:

Yeye alisulubiwa na kuzikwa kisha akafufuka baada ya siki tatu.

Mwenyezi Mungu akawajibu wote hawa kwa kusema: Hawana ujuzi wowote ila kufuata dhana tu. Na dhana haitoshelezeki haki kabisa. Na haki ya yakini isiyo na shaka ni ile aliyotuelezea Mwenyezi Mungu katika kauli yake:

Wala hawakumuua kwa yakini, bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwake.

Hii ndiyo hakika, sio kuuwa wala kusulubu. Yamekuja maswali kuhusu hilo: Vipi alivyoinuliwa? Lini? Kabla ya kusulubiwa yule aliyefananishwa au baada.? Je, kulikuwa ni kuinuliwa kwa roho au kwa roho na mwili? Na je, aliinuliwa mbinguni siku ya pili, ya tatu au nyingineyo? Na kwamba je, huko aliko anafanya nini? Na je, atashuka duniani muda mfupi kabla ya Kiyama? Na maswali mengi mengine ambayo wasimulizi wa visa wamejibu kwa majibu yanayofanana na vigano.

Qur'an Tukufu haikuonyesha chochote katika hayo si kwa karibu wala kwa mbali. Lililofahamishwa na Aya ni kwamba Bwana Masih hakuuwawa wala hawakusulubiwa na kwamba Mwenyezi Mungu alimnyanyua kwake na kwamba aliyesulubiwa na kuuawa ni mtu mwengine aliyedhaniwa kuwa ni Masih.

Hakuna katika Qur'an zaidi ya hayo na sisi hatuwezi kutoka nje katika mfano wa maudhui kama haya ila kwa Hadith Mutawatir. Bali hatutilii muhimu maswali haya na majibu yake, madamu hatutaulizwa kesho wala kukalifishwa nayo. Tumetangulia kueleza yaliyosemwa kuhusu Masih katika kufasiri (3:58) kifungu (tofauti kuhusu Isa).

Hebu tuwachekeshe kidogo kwa kunukuu kigano hiki kilichotokana na baadhi ya wafasiri: Hakika Mwenyezi Mungu alimwinua Isa kwake akamvisha vazi la nuru akamwotesha mbawa, akamfanya asile na asinywe, akamchaganya na Malaika akawa anaruka nao pembeni mwa Arsh na akamfanya na tabia mbili ya kibinadamu na Malaika.

Na hakuna katika watu wa Kitabu ila humwamini yeye kabla ya kufa kwake.

Yaani hakuna yeyote katika watu wa Kitabu ila humwamini Isa kabla ya kufa mtu huyo wa kitabu. Makusudio ya watu wa Kitabu ni Mayahudi na Wakristo. Imeelezwa katika baadhi ya Hadith kwamba kila mtu anapokuwa katika maumivu ya kukata roho.

humfunukia haki ya aliyokuwa akiyaitakidi duniani. Aya hii inashuhudia riwaya hizo, ambapo dhahiri yake inafahamishia kuwa kila mtu wa Kitabu awe Myahudi au Mkristo hana budi kumwamini Isa kwa imani sahihi baada ya maumivu ya kukata roho.

Myahudi ambaye alikuwa akisema kwamba Isa ni mchawi na mtoto wa zina, atabadilika na kuamini kwamba yeye ni Mtume aliyetumwa, na kwamba mama yake ni mkweli. Na Mkiristo aliyekuwa akisema kwamba yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu na ni watatu katika utatu ataamini kuwa ni mja miongoni mwa waja wema.

Hili si muhali katika mtazamo wa akili na limeelezewa na wahyi na kila lililoelezewa na wahyi na lisikanushwe na akili ni wajibu kusadikiwa na kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Ama asiyeamini ila yanaonekana kwa darubini hataamini kabisa. Basi na asimwamini yule atakayemwambia: Unayo akili, roho, utambuzi na hisia, kwa sababu zote hizo hazingii katika vipimo vingine. Amesema kweli aliyesema: Mwenye kukosa imani ya kumwamini Mwenyezi Mungu, basi amejikosa yeye mwenyewe.

Unaweza kuuliza : Kuna faida gani ya kuelezea kuwa haki inawafunukia watu wa Kitabu wakati wa maumivu ya kukaa roho ambapo inajulikana kuwa wao katika hali hii hawawezi kufanya lolote?

Jibu : Lengo la hilo ni kuhimiza kufanya haraka kusahihisha imani yao kabla ya kupata hasara ya kupitwa na wakati na maumivu ya kukata roho; sawa na lengo la kuelezea pepo na moto.

Na Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.

Kesho Isa(a.s) atawatolea ushahidi Mayahudi kwamba wao walimfanyia uadui kwa ukafiri na inadi kwa yale aliyokuja nayo kutoka kwa Mwenyezi Mungu; na atawashuhudilia Wakristo kwamba wao walizidi sana kiasi cha kupetuka yale aliyowaamrisha kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake:

﴿مَا قُلْتُ لَهُمْ إِلَّا مَا أَمَرْتَنِي بِهِ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ رَبِّي وَرَبَّكُمْ﴾

"Sikuwaambia ila yale uliyoniamrisha kuwa mwambuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu na Mola wenu" (5:117)

Mitume wote, Muhammad akiwa mstari wa mbele, watamshuhudulia kila mwenye kukengeuka na yale aliyokuja nayo na kuwafikishia:

﴿وَيَوْمَ نَبْعَثُ فِي كُلِّ أُمَّةٍ شَهِيدًا عَلَيْهِم مِّنْ أَنفُسِهِمْ وَجِئْنَا بِكَ شَهِيدًا عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ﴾

"Na siku tutakapompeleka shahidi katika kila umma juu yao kutoka miongoni mwao na wewe tutakuleta uwe shahidi juu ya hawa" (16:89)

﴿فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ لَهُمْ وَبِصَدِّهِمْ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ كَثِيرًا ﴾

160.Basi kwa dhuluma ya ambao ni Mayahudi tuliwaharamisha vitu vizuri walivyohalalishiwa, na kwa sababu ya kuzuilia kwao wengi na njia ya Mwenyezi Mungu.

﴿وَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴾

161.Na kuchukua kwao riba nao wamekatazwa, na kula kwao mali za watu kwa batili, na tumewaandalia makafiri adhabu yenye uchungu.

﴿لَّـٰكِنِ الرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ مِنْهُمْ وَالْمُؤْمِنُونَ يُؤْمِنُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ وَالْمُقِيمِينَ الصَّلَاةَ وَالْمُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالْمُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ أُولَـٰئِكَ سَنُؤْتِيهِمْ أَجْرًا عَظِيمًا﴾

162.Lakini waliobobea katika elimu miongoni mwao na waumini, wanaamini uliyoteremshiwa na yaliyoteremshwa kabla yako. Na wenye kusimamisha Swala na wenye kutoa Zaka na wenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho hao tutawapa ujira mkubwa.

DHULMA YA MAYAHUDI

Aya 160 - 162

IRABU

Neno:wenye kusimamisha Swala ni yambwa (maf'ul) na kiima (fail) yuko kwenye kitendo kililichokadiriwa kuwa ni: Ninakusudia au ninasifu wenye kusimamisha Swala.

Lakini kuna msemaji aliyesema kuwa hili ni kosa la waandishi: Na akajibiwa kuwa Maimamu, wasomaji na maulama hawakubali hata kukosea umma wa Muhammad(s.a.w.w) katika yasiyokuwa maandishi ya Qur'an sembuse, kwenye maandishi yake! Swali hili limekuja kuwa kwa nini neno Muqimin limenasibishwa kwenye kusifiwa, lakini mengine yanayoungana nalo haya kunasibishwa?

Tunajibu: Huenda hilo ni kwa ajili ya kudhihirisha kima cha Swala na utukufu wake, na kwamba hiyo Swala ni nguzo ya dini na imani, ikikubaliwa hukubaliwa mengine na ikirudishwa hurudishwa mengine.

MAANA

Basi kwa dhuluma za ambao ni Mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa, na kwa sababu ya kuzuilia kwao wengi na njia ya Mwenyezi Mungu.

Bado maneno yanaendelea juu ya Mayahudi na uovu wao. Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya zilizotangulia ametaja ufedhuli wao wa kutaka kumuona Mwenyezi Mungu waziwazi, kumwabudu ndama, kukiuka miko ya Jumamosi, kuvunja ahadi na kuzikufuru ishara za Mwenyezi Mungu. Vilevile kuwaua kwao mitume, kusema, nyoyo zetu zimefumbwa, kumzulia Maryam na kujigamba kwao kumuua Masihi.

Na hapa ametaja kuwazuilia kwao watu na njia ya Mwenyezi Mungu na kula riba na rushwa; na kwamba yeye Mwenyezi Mungu kwa sababu ya uovu huu na fedheha hii, amewaharamisha katika duniya baadhi ya vitu vizuri vilivyokuwa halali kwao na kwa wengineo.

Na kuchukua kwao riba nao wamekatazwa.

Hayo yanaungana na 'basi kwa dhuluma.' Inasemekana kuwa Mayahudi ndio wa kwanza kuanzisha riba na kuihalalisha. Tumezungumzia hayo kwa ufafanuzi katika kufasiri Aya (2:275).

Na kula kwao mali za watu kwa batili; kama vile rushwa na njia nyinginezo za haramu. Mwenyezi Mungu amewasifu kuwa wao ni

"Wasikiao sana uwongo, walao sana haramu" (5:42)

Ama vizuri alivyowaharamishia ni vile alivyoviashiria Mwenyezi Mungu kwa kusema kwake:

﴿وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا كُلَّ ذِي ظُفُرٍ وَمِنَ الْبَقَرِ وَالْغَنَمِ حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ شُحُومَهُمَا إِلَّا مَا حَمَلَتْ ظُهُورُهُمَا أَوِ الْحَوَايَا أَوْ مَا اخْتَلَطَ بِعَظْمٍ ذَٰلِكَ جَزَيْنَاهُم بِبَغْيِهِمْ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴾

"Na kwa wale walio Mayahudi tuliharimisha kila (mnyama) mwenye kucha, Na katika ng'ombe na kondoo na mbuzi tukawaharimishia shahamu yao isipokuwa ile iliyobeba migongo yao au matumbo au ile iliyogandamana na mifupa. Tuliwalipa hivyo kwa sababu ya uasi wao. Na hakika sisi ndio wa kweli" (6:146)

Tukilinganisha sera za Mayahudi wa tangu zamani, hasa katika zama za Musa, Isa na Muhammad na njia zao wanazotumia leo, hatuwezi kupata tofauti yoyote baina ya Mayahudi wa jana na wa leo, ikiwa ni pamoja na upotevu, ufisadi, uadui kwa ubinadamu na heshima yake na kuacha kunyenyekea mpaka wanyanyuliwe jabali vichwani mwao.

Hakuna jambo linalofahamishwa na hayo zaidi ya kuwa shari ni tabia ya asili katika uyahudi na ni umbile lisiloepukana nao; kadiri zama zigeukavyo na hali ziendeleavyo, sawa na nge asivyoweza kuacha kuuma na nyoka kudunga sumu yake.

Ikiwa kila mtu ana mwelekeo wa heri na shari, basi tabia ya Mayahudi inahusika na shari tu. Ikiwa utampata katika wao anayeijua haki na kuitumia basi hilo ni nadra sana, na nadra haivunji desturi bali ndio inaiimarisha. Amewavua Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawa wachache kwa kauli yake:

Lakini waliobobea katika elimu miongoni mwao na waumini, wanaamini uliyoteremshiwa na yaliyoteremshwa kabla yako.

Wenye kubobea katika elimu ni wale maulama wanaoitumia elimu yao, sio wale wanaoyajua yaliyoandikwa vitabuni tu, na wahakiki wanaozama katika utafiti wao na nadharia zao tu. Maana haya tumeyatoa katika kauli ya Amirul-muminin Ali(a.s) :"Elimu hukua kwa vitendo, vinginevyo itamuhama."

Unaweza kuuliza : kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameunganisha waumini na wenye kubobea katika elimu na akaeleza kuwa wao kwa pamoja wanaamini Qur'an, Taurat na Injil. Na maelezo hayo yatafaa ikiwa ni kwa Mayahudi, wala hayafai kwa wanaomwamini Muhammad(s.a.w.w) , kwa sababu maana yake yatakuwa ni waumini wanaamini, sawa na kusema waliosimama wamesimama na waliolala wamelala; na Qur'an imetakata na mifano hii, Sasa je, kuna tafsiri gani?

Jibu : Swali hili au mushkeli huu utakuwepo ikiwa tutafasiri waumini kuwa ni waumini katika sahaba wa Mtume na sio katika watu wa Kitabu; kama alivyofanya mwenye Majmaul-bayan na wala asizuiwe na Arrazi na mwenye Al-Manar na wafasiri wengi. Ama tukifasiri waumini kuwa ni Mayahudi wanaowafuata wenye kubobea katika elimu miongoni mwao, basi swali hili halitakuwepo. Kwani maana yatakuwa ni wenye kubobea katika elimu miongoni mwa Mayahudi na wenye kuchukua kauli zao katika watu wa mila zao, wanaamini Qur'an, Taurat na Injil. Wao wanaamini kwa dalili na hawa wanaamini kwa kufuata, Sisi tunapondokea kwenye tafsiri hii kuliko ya kwanza.

Na wenye kusimamisha Swala.

Maneno yamekuwa mengi kuhusu kunasibishwa (kusema Muqimini na sio Muqimun); mpaka ikapokewa kutoka kwa Athman na Aisha kuwa neno hili limekosewa, lakini Razi amebatilisha haya kwa kusema "Msahafu umenukuliwa kwa Mutawatir kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) itawezekana vipi kuthibiti kosa?"

Ilivyo sawa ni kwamba neno hili limenasibishwa na sifa; yaani ninawasifu wanaosimamisha Swala, kwa lengo la kuonyesha fadhila ya Swala na thamani yake; kama tulivyoeleza katika kifungu cha Irabu.

Na wenye kutoa zaka, ni habari ya Mubtada (kianzio) kilichokadiriwa; yaani na hao ni wenye kutoa Zaka. Kwa maana ya kuwa wenye kuswali ambao wanastahiki sifa ni wale wanaoikutanisha Swala na kutoa Zaka. Na wenye kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Inaungana na wenye kutoa Zaka. Ama malipo ya wote ameyaashiria Mwenyezi Mungu kwa kusema: Hao tutawapa ujira mkubwa.

﴿إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَعِيسَىٰ وَأَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا ﴾

163.Hakika sisi tumekuletea wahyi kama tulivyompelekea wahyi Nuh na Manabii baada yake. Na tukampelekea Wahyi Ibrahim na Ismail na Ishaq na Yaqub na wajukuu na Isa na Ayyub na Yunus na Harun na Suleiman; na Daud tukampa Zaburi.

﴿وَرُسُلًا قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا﴾

164.Na mitume tuliokusimulia kabla na mitume ambao hatukukusimulia. Na Mwenyezi Mungu akanena na Musa maneno.

﴿رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ وَكَانَ اللَّـهُ عَزِيزًا حَكِيمًا ﴾

165.(Ni) Mitume wabashiri, waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya mitume; na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

﴿لَّـٰكِنِ اللَّـهُ يَشْهَدُ بِمَا أَنزَلَ إِلَيْكَ أَنزَلَهُ بِعِلْمِهِ وَالْمَلَائِكَةُ يَشْهَدُونَ وَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا﴾

166.Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyokuteremshia, Ameyateremsha kwa elimu yake na Malaika (pia) wanashuhudia; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.

TUMEKULETEAWAHYI

Aya 163 - 166

MAANA

Hakika sisi tumekuletea wahyi kama tulivyompelekea wahyi Nuh na manabii baada yake. Na tukampelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haq naYaaqub na wajukuu na Isa na Ayyub na Yunus na Harun na Suleiman na Daud tukampa Zabur.

Makusudio ya wajukuu hapa ni wajukuu 12 katika watoto kumi na wawili wa Yaqub bin Is-haq bin Ibrahim. Makusudio ya wahyi kwa wajukuu ni mitume katika wao, sio wahyi kwa wao wote.

Aya hii na inayofuatia inaambatana na Aya zilizotangulia: Njia ya kuambatana kwake ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya zilizotangulia ameelezea watu wa Kitabu kwamba wao wanaamini fikra ya utume na wanakubali kwamba Mwenyezi Mungu ana mitume, lakini wao hawawakubali wote, bali wanaamini baadhi na kukanusha baadhi. Muhammad ni miongoni mwa wale wanaowakanusha. Pia amebainisha huko Mwenyezi Mungu kwamba mwenye kukanusha utume wa mmoja katika mitume yake basi ni kama aliyemkufuru Mwenyezi Mungu na kwamba imani sahihi ni kumwamini Mwenyezi Mungu, siku ya mwisho, Malaika wake, vitabu vyake vyote na mitume wake wote.

Kisha akathibitisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya tunayoifasiri na iliyo baada yake, kwamba mwenye kukubali misingi ya utume, akaamini utume wa mmoja wao, basi ni lazima aamini utume wa Muhammad(s.a.w.w) , kwa sababu Mwenyezi Mungu amempelekea wahyi kama alivyowapelekea wengineo katika mitume na akadhihirisha mikononi mwake miujiza, kama alivyoidhihirisha kwa mitume wengine.

"Linalopatikana kwa maafikiano, haliwi ni sababu ya mafarikiano," na mwenye kufarikisha na kugawanya atakuwa amekifarikisha kitu na nafsi yake.

Na mitume tuliokusimulia kabla, na mitume ambao hatukukusimulia.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja majina ya mitume, katika Aya iliyotangulia, alisema kumwambia Mtume wake mtukufu kuwa kuna mitume wengine wasiokuwa hawa tumekusimulia kabla ya kushuka Sura hii na wako wengine hatukukusimulia.

Imeelezwa katika Al-manar kwamba Aya iliyokusanya zaidi majina ya mitume ni ile isemayo:

﴿وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ كُلًّا هَدَيْنَا وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿٨٤﴾ وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿٨٥﴾ وَإِسْمَاعِيلَ وَالْيَسَعَ وَيُونُسَ وَلُوطًا وَكُلًّا فَضَّلْنَا عَلَى الْعَالَمِينَ ﴾

"Na tukampa Is-haq na Yaqub, wote tukawaongoa. Na Nuh tulimwongoa kabla na katika kizazi chake, Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun, Na hivi ndivyo tuwalipavyo wafanyao mema. Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas, wote ni miongoni mwa watu wema. Na Ismail an Al-yasa na Yunus na Lut. Na wote tukawafadhihisha juu ya walimwengu" (6:84.86)

Wengine ni Hud, Saleh na Shuaib nao ni katika waarabu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema:"Na mitume ambao hatukukuhadithia" bila kuishiria idadi ya mitume ambao hakumtajia. Lakini watu wenye kuzidisha mambo wamekataa ila kutoa idadi, nao wakazidisha. Kuna mwenye kusema mia tatu na kumi na tatu (313).

Mwingine akasema ni, milioni moja laki nne na ishirini na nne elfu (1,424,000). Watatu akasema ni elfu nane (8,000), nusu yao wakiwa Waisrail. Na wanne naye akasema ni laki moja na ishirini na nne elfu (124,000). Kauli zote hizi na nyinginezo ni dhana za mbali. Ilivyo hasa ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayejua idadi yao na walivyo.

JE MITUME WOTE NI WA MASHARIKI?

Kuna swali linalomtokea kila mtu nalo ni je mitume wote ni wa Mashariki na wala hakuna aliyetokea Magharibi? Ikiwa wote ni kutoka Mashariki, je yuko Mchina, Mjapani au Mhindi? Au kutoka Mashariki ya mbali? Kisha je, ikichukuliwa kuwa wote ni wa Mashariki, tutaliwekaji hilo pamoja na misingi ya aliyesema:

Hakika Mwenyezi Mungu hawaachi watu bure bure; na kwamba hekima yake na rehema yake inahukumia kupelekea mitume kwa wote,"watakaobashiria na kuonya" (2:213)

Watakaowakumbusha na kuwaonyesha njia ili wasiwe na hoja yoyote kwa Mwenyezi Mungu. Na je, unakubalika msingi huu wa kuhusisha taifa kinyume na mataifa mingine na jinsi kinyume na jinsi nyingine?

Jibu : Hakika msingi huu usemao Mwenyezi Mungu hawaachi watu bure bure, na kwamba Mwenyezi Mungu hana budi kutoa hoja kabla ya hesabu na adhabu, ni msingi wa jumla usiokubali kuhusika na ardhi ya Mashariki au Magharibi, wala kwa jinsi nyeupe, ya njano au nyeusi.

Lakini hoja haifungamani tu na kupatikana Mtume kwa dhati yake katika kila mji na kila kizazi, bali msingi unakuwa kwa Mtume au kwa Kitabu kilichoteremshwa au kwa sharia ya Mwenyezi Mungu inayosimamiwa na manaibu wa mitume; hata pale Mwenyezi Mungu anapomfisha Mtume, bado hoja inakuwa imebaki kwa watu. Amirul-Mumin Ali(a.s) anasema katika hotuba ya kwanza, katika Nahjul-balagha"Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumwacha kiumbe wake asiwe na Nabii mwenye kutumwa au Kitabu chenye kuteremshwa au hoja yenye kulazimiana au hoja iliyosimama."

Hoja yenye kulazimiana ni naibu wa Mtume na hoja yenye kusimama ni sharia iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu. kila moja ya hizi nne, iwe peke yake au pamoja na mwenzake inasimama kuwa ni hoja ya Mwenyezi Mungu kwa watu. Kwa hali hii basi ndio tunapata tafsir ya Aya isemayo:

﴿وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ﴾

"Na hakika tulipeleka Mtume katika kila umma ya kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu na mjiepushe na Taghut." (16:36)

Pia Aya isemayo:"Na hakuna uma wowote ila alipita humo muonyaji." (35:24) Vilevile tunapata tafsiri ya:

﴿فَكَيْفَ إِذَا جِئْنَا مِن كُلِّ أُمَّةٍ بِشَهِيدٍ وَجِئْنَا بِكَ عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ شَهِيدًا﴾

"Basi itakuwaje tutakapowaletea kila umma shahidi na tukakuleta wewe kuwa shahidi juu ya hawa." (4:41)

Makusudio ya Mtume katika Aya ya kwanza, mwonyaji katika Aya ya pili na shahidi katika Aya ya tatu, ni moja kati ya hoja nne: Mtume mwenyewe, naibu wake, Kitabu kilichoteremshwa na Mwenyezi Mungu au sharia. Inajulikana kuwa matatu ya mwisho, yanaishia kwa Mtume hivyo ikafaa kutegemeza shahada kwa Mtume.

Hapa kuna swali linalojitokeza, nalo ni kuwa: kwa nini haikutajwa akili pamoja na hoja nyingine zilizotajwa pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu anaitolea akili hoja kama amtoleavyo hoja Mtume?

Jibu : Akili ni hoja, hilo halina shaka, lakini hiyo ni hoja katika kujua kuweko Mwenyezi Mungu. Ama katika mengine, kama kujua Siku ya mwisho, halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake, hayo yanahitajia mwamshaji na mzinduzi atakayeongoza na kuweka njia sahihi ya kuyafikia. Kazi ya akili katika uwanja huu tulio nao ni kujua yale ayasemayo Mtume ya wajibu wa imani na dalili za uongofu wa heri ya dunia na akhera. Itakapofahamu akili ayasemayo Mtume, basi itakiri bila ya kusita.

Baada ya utangulizi huu ambao hauna budi katika kufahamu maudhui yetu, tunarudi kwenye swali, kuwa je, mitume wote ni wa Mashariki?

Tunajibu : Hapana! Ikiwa hatukupata habari ya mitume waliopelekwa kwa umma wa Magharibi na baadhi ya Mashariki, haina maana kuwa Mwenyezi Mungu hakupeleka Mtume yeyote huko.

Pia sio dharura kwa kupeleka hoja kwa watu wa Magharibi kuwa Mtume lazima awe katika wao, bali anaweza kuwa ni wa Mashariki, lakini ujumbe wake ukaenea Mashariki na Magharibi, na kufikisha ujumbe huo kupita makhalifa wake na manaibu, kama alivyoambiwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) :

﴿وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴾

"Na hatukutuma ila kwa watu wote, uwe mtoaji bishara na muonyaji, lakini watu wengi hawajui" (34:28)

Na akamwambia tena:"Na hatukukutuma ila uwe rehma kwa walimwengu." (21:107).

Vitabu vya dini vya zamani vimeashiria kuwa risala ya Muhammad ni ya wote na kwamba ni rehema kwa viumbe vyote. Zaidi ya hayo, vimetaja jina la Abu Lahab kwa herufi na uadui wake kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) Abdul-haq Vidyarthi, amesema katika Kitabu Muhammad in World Scriptures (Muhammad katika vitabu vya dini za duniani): "Hakika jina la Mtume wa kiarabu limeandikwa kwa tamko lake la kiarabu, Ahmad, katika Sama Veda miongoni mwa vitabu vya Brahamanas[2] .

kwenye sehemu ya sita na ya nane ya juzuu ya pili imeelezwa waziwazi kuwa Ahmad atapokea sharia kutoka kwa Mola wake nayo itakuwa imejazwa hekima, Na sifa za Al-Kaaba zimethibiti katika Kitabu Atharva Veda.

Na katika Kitabu Zand Avesta, ambacho ni mashuhuri kuwa ni Kitabu kitakatifu katika umajusi, imekuja habari ya Mtume akisifiwa kuwa yeye ni rehema kwa walimwengu, atakayelingania kwa Mwenyezi Mungu ambaye hakuwa yeyote mfano wake, na atapingwa na adui anayeitwa Abu Lahab[3] .

Haiwezekani habari hizi zitokee kwa asiyekuwa muumba. Hizo ni wahyi tu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwenda kwa Mtume miongoni mwa mitume yake, hilo halina shaka. Kama si hivyo basi ni nani anayeweza kutoa habari ya utume wake kwamba baada ya maelfu mamia ya miaka atapatikana Mtume atakayeitwa Ahmad, atakayelingania kwenye ibada ya Mungu mmoja tu aliye pekee, na atakayepingwa na adui aitwaye Abu Lahab?

Kwa hivyo basi katika habari hii kuna dalili ya wazi na ya kweli juu ya mambo mawili:

Kwanza : ukweli wa Muhammad katika utume wake na kuenea risala yake.

Pili : kwamba Mwenyezi Mungu alituma mitume hapo zamani ambao hatukuwasikia au visa vyao pia hatukuvisikia; kisha hatujui, pengine maji-

Baada ya yote hayo ni kwamba kutumwa Mtume Mashariki na Magharibi ni maudhui muhimu yanayotaka Kitabu mbali. Ama mnasaba huu, ambao ni tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "na mitume ambao hatukukusi mulia." Hauwezi kuchukua zaidi ya tuliyoyataja; na huenda tukapetuka mpaka.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu kumpa, kwa maudhui haya ya kielimu yenye kunufaisha, elimu na uvumilimivu kila mwenye kufanya utafiti na uchunguzi.

Na Mwenyezi Mungu akanena na Musa maneno.

Mwenyezi Mungu amemtaja Musa peke yake katika jumla hii, kwa sababu yeye ndiye aliyemhusu kusema naye, kinyume na wengine, ingawaje mitume wote walipokea maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Lakini mazungumzo hayo yalikuwa kwa namna aliyoitaja Mwenyezi Mungu:

﴿وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ﴾

"Na haikuwa kwa mtu kwamba Mwenyezi Mungu aseme naye ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia au humtuma mjumbe naye humpa wahyi" (42:51)

Kwa hiyo mazungumzo ya Musa na Mwenyezi Mungu yalikuwa ni nyuma ya pazia. Hakuna yeyote anayejua hali ya pazia hii na ilikuwaje. Mwenyezi Mungu amelinyamazia hilo na sisi tunalinmyamazia, kama alivyolinyamazia Yeye Mwenyewe.

Kwa hali yoyote iwayo, kuhusishwa Musa na kuzungumza na Mwenyezi Mungu hakupunguzi kitu kwa mitume wengine, wala hakufahamishi kuwa yeye ni bora na mkamilifu zaidi ya wengine, hapana! Kwani kumtuma roho mwaminifu kwa wa mwisho wa mitume ni daraja ya juu na ya ukamilifu zaidi.

(Ni) Mitume wabashiri, waonyaji ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya mitume.

Desturi ya 'Hakuna adhabu bila ya ubainifu,' kama wanavyosema mafakihi au 'Hakuna adhabu bila ya kauli wazi,' kama wasemavyo watunga sheria, ni wazi kabisa, isiyohitaji dalili, bali hiyo yenyewe ni dalili. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumwacha binadamu bure bure, bali alimwamrisha na akamkataza, na hapana budi kwake kumfikilizia amri na makatazo haya ili awe na hoja, hata kama atahalifu.

Na hoja zake hazifahamiki ila kwa wahyi; na kwa kuwa mitume ndio kiungo cha kati baina ya Mwenyezi Mungu na viumbe vyake katika kufikisha hukumu zake, na ahadi zake, ndipo Mwenyezi Mungu akawatuma mitume watoao habari njema na waonyaji. Ili kusiweko na nafasi ya kutoa udhuru na sababu. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ وَلَوْ أَنَّا أَهْلَكْنَاهُم بِعَذَابٍ مِّن قَبْلِهِ لَقَالُوا رَبَّنَا لَوْلَا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولًا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ مِن قَبْلِ أَن نَّذِلَّ وَنَخْزَىٰ ﴾

"Na lau kama tungeliwangaamiza kwa adhabu kabla yake wangesema: Ewe Mola wetu! Kwa nini usituletee mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhalilika na kufedheheka?" (20: 134)

Tumezunguzumzia kuhusu ubaya wa adhabu bila ya ubainifu katika kufasiri (2:159)

Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyokuteremshia. Ameyateremsha kwa elimu yake, na Malaika (pia) wanashuhudia; na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.

Ushahidi unakuwa kwa kauli na au kwa vitendo, kama ushahidi wa ulimwengu kwa kuwepo muumbaji na uweza wake, au ushahidi wa kutoa kwa kuwepo mtoaji na ukarimu wake na ushahidi wa ujasiri kwa ushujaa wa mjasiri na nguvu zake. Ushahidi wa vitendo ni dalili zaidi na una nguvu kuliko ushahidi wa kauli ambao unakuwa na shakashaka.

Miongoni mwa ushahidi wa vitendo ni ushahidi wa Mwenyezi Mungu kwa Muhammad(s.a.w.w) alipompa dalili na miujiza ya ukweli.

Mwingine ni Qur'an Tukufu aliyoiteremsha kwa elimu yake. Maana ya 'kwa elimu yake' ni kwamba Qur'an inatokana na elimu ya Mwenyezi Mungu sio elimu ya viumbe ambayo inakuwa na makosa na mapendeleao.

Ama ushahidi wa Malaika, unafuatilia wa Mwenyezi Mungu ambao unatoshelezea ushahidi wote Ndipo Mwenyezi Mungu akasema:"na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi."

Baada ya hayo ni kwamba hakuna asiyependa kusadikiwa na watu katika anayoyasema, lakini mwenye akili huwa hajishughulishi na hilo kabisa hata akifanywa mwongo na kujibiwa maneno yake, maadamu ana yakini ya ukweli wake.

Hilo ndilo linalokusudiwa na Aya. Ni kama kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake. "Usikushughulishe ukadhibishaji wa mwenye kukadhibisha utume wako na upinzani wa mwenye kupinga mwito wako, maadamu kwangu umkweli mwenye kusadikisha"

Aya hii ina makusudio kama yanayokusudiwa na Aya isemayo:

﴿فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ﴾

"Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia, Hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya" (35:8)