TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16190
Pakua: 2342


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16190 / Pakua: 2342
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

Sura Ya Tano: Al - Maidah

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ أُحِلَّتْ لَكُم بَهِيمَةُ الْأَنْعَامِ إِلَّا مَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ غَيْرَ مُحِلِّي الصَّيْدِ وَأَنتُمْ حُرُمٌ إِنَّ اللَّـهَ يَحْكُمُ مَا يُرِيدُ﴾

1.Enyi mlioamini! Tekelezeni mapatano. Mmehalalishiwa wanyama wenye miguu mine, ila wale mnaotajiwa bila kuhalalishiwa mawindo mkiwa katika Ihramu. Hakika Mwenyezi Mungu anahukumu atakavyo.

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحِلُّوا شَعَائِرَ اللَّـهِ وَلَا الشَّهْرَ الْحَرَامَ وَلَا الْهَدْيَ وَلَا الْقَلَائِدَ وَلَا آمِّينَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّن رَّبِّهِمْ وَرِضْوَانًا وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَاصْطَادُوا وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ أَن صَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ أَن تَعْتَدُوا وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَاب﴾

2. Enyi mlioamini! msivunje heshima ya alama za Mwenyezi Mungu wala ya mwezi mtakatifu, wala ya wanyama wa kuchinja, wala ya vigwe, wala ya wale wakusudiao kwenda kwenye nyumba tukufu kutafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi.Na mkishatoka kwenye Ihramu, basi windeni. Wala kule kuwachukia watu waliowazulia kufika Msikiti mtukufu, kusiwapelekee kuwafanyia jeuri, Na saidianeni katika wema na takua wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

KWA JINA LAALLAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU TEKELEZENI MAPATANO

Aya 1-2

MAANA

Aya za Qur'an huzungumzia itikadi, ibada, sharia, maadili, maongozi ya kidini na ya kidunia, hukumu na jihadi. Aya zizungumziazo sharia, ikiwamo ibada, huitwa Aya za hukumu. Nazo zinafikia kiasi cha 500.

Miongoni mwa Aya hizo ni hii isemayo:Enyi mlioamini! Tekelezeni mapatano.

Jumla hii, pamoja na ufupi wake, ina manufaa makubwa. Kwani madhehebu yote yamekongamana kuwa ndio msingi na asili ya wajibu wa kutekeleza mapatano waliyopatana kwa kuridhiana, yakiwa masharti ya sharia yamekamilika, ambayo ni pamoja na kubaleghe na kuwa na akili kwa waliopatana.

Vile vile ustahiki wa kumiliki kilichofanyiwa mapatano na kutowajibisha ya halali kuwa haram na ya haram kuwa halali na mengineyo, ambayo yametajwa katika vitabu vya Fiqhi kama vile Fiqh Imam Jafar as-Sadiq J.3.

Mmehalalishiwa wanyama wenye miguu minne ambao ni ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, wa kufugwa au wa porini. Baada ya Mwenyezi Mungu kuhalalisha kuliwa wanyama hawa, amevua kwa kusema:

Ila wale mnaotajiwa.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ametutajia hapa aina mbili za wanyama:

Kwanza : ni ile aliyoiashiria kwa kauli yake: Bila ya kuhalalisha mawindo mkiwa katika Hija.

Pili ni ile aliyoiashiria katika Aya ya tatu:"Mheramishiwa mfu na damu." Ufafanuzi wake utakuja, inshallah.

Maana ya bila ya kuhalalisha mawindo mkiwa katika Hija, Ni kuwa wanyama ambao Mwenyezi Mungu ametuhalalishia kuwala ni wanyama wa kufugwa au wa porini ambao hatukuwawinda wakati wa Ihramu[7] .

Ama wale tunaowawinda katika hali hii ni haramu kuliwa. Kwa sababu, kila akiwindacho mwenye kuhirimia haifai kukila; ni sawa awe ni katika wanyama wa kufuga au wa porini. Utakuja ufafanuzi katika Tafsiri ya Aya 97 na iliyo baada yake.

Enyi mlioamini! Msivunje heshima ya alama za Mwenyezi Mungu.

Na alama zake Mwenyezi Mungu Mtukufu ni hukumu za dini yake, ambazo miongoni mwa zilizojitokeza zaidi ni ibada ya Hija. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ﴾

"Ndivyo hivyo! Na anayeziadhimisha alama za Mwenyezi Mungu, basi hilo ni katika takua ya moyo" (22:32)

Maana ya kukataza kuvunja miiko ya hukumu za dini ya Mwenyezi Mungu ni kutozipindua na kufanya kama tunavyotaka,Wala ya mwezi mtakatifu.

Yaani msipigane katika miezi mitukufu, Makusudio ya miezi mitukufu ni minne: Dhul-qaada, Dhul-Hijja, Muharam na Rajab[8] .

Wala ya Wanyama wakuchinjwa kwenye nyumba ya Mwenyezi Mungu Mtukufu miongoni mwa Ngamia, Ng'ombe, Mbuzi na Kondoo. Makusudio ni kuwa yeyote asimtaaradhi mnyama kwa kumpora au kumzuia kufika kwenye nyumba tukufu.

Wala ya vigwe, yaani wala heshima ya wale waliofungwa vigwe. Walikuwa wakiwafunga wanyama vigwe ili wajulikane na wasitaaradhiwe na yeyote. Wametajwa wenye vigwe baada ya kutaja wanyama wa kuchinja, pamoja na kuwa hao wanaofungwa vigwe ndio hao watakaochinjwa, kwa sababu ya kutilia umuhimu; kama vile kusema:"Angalieni sana Swala na Swala ya katikati" (2: 238)

Wala ya wale wakusudiao kwenda kwenye Nyumba tukufu kutafuta fadhila za Mwenyezi Mungu na radhi.

Yaani msimuue yeyote anayekusudia nyumba ya Mwenyezi Mungu; ni sawa awe amekusudia ibada au biashara.

Na mkishatoka kwenye Ihramu, basi windeni, kwani kuwinda ni haram katika hali ya Ihram na katika ardhi ya Al-Haram. Ikiwa mtu hayuko katika Ihram wala hayuko katika ardhi ya Haram[9] , basi kuwinda na kula windo ni halali. Neno basi windeni ni kuhalalisha sio kuamrisha, kwa sababu limekuja baada ya makatazo.

Wala kule kuwachukia watu waliowazuilia kufika msikiti mtukufu, kusiwapelekee kupituka mipaka.

Katika mwaka wa sita Hijria, washirikina ndio waliokuwa wakitawala Makka na nyumba tukufu.

Mtume na sahaba zake wakataka kuzuru nyumba tukufu katika mwaka huo, lakini washirikina wakawazuia. Baadaye Makka na nyumba tukufu zikawa chini ya mamlaka ya Waislamu. Ikashuka Aya hii, zikiwa na maana kuwa haifai kwenu nyinyi Waislamu chuki ya washirikina kuwapelekea kuwazuia na nyumba tukufu, kwa kuwa waliwazuilia mwanzo. Hii ilikuwa kabla ya kushuka Aya:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا﴾

"Enyi mlioamini! Hakika washirikina ni najisi kwa hivyo wasiukurubie Msikiti mtakatifu baada ya mwaka wao huu!!" (9:28)

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu si amesema kuwa:

﴿فَمَنِ اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُوا عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَىٰ عَلَيْكُمْ﴾

"Wanaowachokoza nanyi pia wachokozeni kwa kadiri walivyowachokoza?" (2:194)

Jibu : Aya hii imeshuka kuhusu kisasi na kulipiziana katika mambo maalum; kama vile vita na kukatana viungo; yaani mwenye kupigana nanyi piganeni naye, na mwenye kumkata mkono wa mwingine naye akatwe, na mfano wa hayo. Ama mwenye kuzuia ibada ya Mwenyezi Mungu, biashara au kilimo, basi haijuzu kumlipizia hivyo bali atalipizwa kwa kitu kingine.

Kwa ufupi malipo ya mchokozi yanaweza kuwa ni kulipiza alivyofanya au kwa namna nyingine. Sehemu nyingi malipo yanakuwa ni ushindi wa haki sio kuadhibu.

MAPINDUZI NA KUPINGA MAPINDUZI

Na saidianeni katika wema na takua wala msisaidiane katika dhambi na uadui.

Miongoni mwa maneno yanayozunguka leo katika vinywa vya wasemaji na kalamu za waandishi ni mapinduzi na kupinga mapinduzi. Wakiwa na maana ya kuwa mapinduzi ni kuwasaidia wenye ikhlasi na kuwatetea dhidi ya ufisadi.

Na kupinga mapinduzi ni kuwasaidia wahaini na wasio wana mapinduzi katika kujaribu kuleta mageuzi. Dhahiri ya Aya inatupelekea kufuatishia kauli yake Mwenyezi Mungu: wala msisaidiane katika dhambi na uadui, kuwa ni kupinga mapinduzi ya kila heri na maendeleo.

﴿ حُرِّمَتْ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةُ وَالدَّمُ وَلَحْمُ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ وَالْمُنْخَنِقَةُ وَالْمَوْقُوذَةُ وَالْمُتَرَدِّيَةُ وَالنَّطِيحَةُ وَمَا أَكَلَ السَّبُعُ إِلَّا مَا ذَكَّيْتُمْ وَمَا ذُبِحَ عَلَى النُّصُبِ وَأَن تَسْتَقْسِمُوا بِالْأَزْلَامِ ذَٰلِكُمْ فِسْقٌ الْيَوْمَ يَئِسَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن دِينِكُمْ فَلَا تَخْشَوْهُمْ وَاخْشَوْنِ الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا فَمَنِ اضْطُرَّ فِي مَخْمَصَةٍ غَيْرَ مُتَجَانِفٍ لِّإِثْمٍ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾

3.Mmeharamishiwa nyamafu na damu na nyama ya nguruwe, na aliyechinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na aliyekufa kwa kunyongeka, na aliyekufa kwa kupigwa, na aliyeanguka, na aliyepigwa pembe, na aliyeliwa na mnyama ila mliowachinja, na aliyechinjiwa mizimu. Na kuagulia kwa mburuga. Hayo yote ni ufasiki. Leo waliokufuru wamekata tamaa katika dini yenu, basi msiwaogope na mniogope mimi. Leo nimewakamilishia dini yenu na kuwatimizia neema yangu na nimewapendelea Uislamu kuwa dini. Basi aliyefikwa na dharura bila kuelekea kwenye dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye maghufira mwenye kurehemu.

MMEHARAMISHIWA MFU

Aya ya 3

MAANA

Vyakula vyote na vinywaji vyote ni halali ila ambavyo imepatikana nukuu ya kuharamishwa kwa umahususi; kama vile nyamafu na kadhalika, au kwa ujumla; kama vile vitu vinavyodhuru, vikiwemo vitu vichafu. Mwenyezi Mungu anasema:

"Enyi watu kuleni vilivyomo katika ardhi halali na vizuri" (2:168)

Yametangulia maelezo katika Aya ya kwanza katika kauli yake Mwenyezi Mungu ila wale mnaotajiwa. Na Mwenyezi Mungu anatutajia aina mbili, ambapo aina ya kwanza ametutajia katika Aya ya kwanza, aina ya pili ni hii anayotutajia katika Aya hii, navyo ni kumi:

1.Nyamafu : Ni kila mnyama au ndege aliyekufa bila ya kuchinjwa kisheria. Kuchinja huko kunatofautiana kulingana na wanyama: samaki kuchinjwa kwake ni kutolewa hai katika maji; kwa nzige ni kwa kumshika akiwa hai. Vilevile kwa aliye tumboni ni kwa kuchinjwa mama yake. Kwa windo kuchinja kwake ni kwa kutumia mbwa aliyefundishwa, upanga, mkuki, mshale au ala yoyote kali. Na kuchinja mnyama kwa kuelekezwa Qibla na kukata mishipa minne pamoja na kutaja jina la Mwenyezi Mungu. Ufafanuzi umo katika vitabu vya fiqh, kama vile Fiqhul Imam Jafar as-Sadiq.

2.Damu : inayotoka kwa nguvu na kupambanuka na nyama. Kwa sababu ile iliyo katika nyama inasamehewa; vile vile inasamehewa damu iliyogeuka nyama ikawa ini, kwa madhehebu yote; na ni haramu ikiwa ni wengu kwa Shia.

3.Nyama ya nguruwe : Ni haramu kwa Waislamu wote.

4.Aliyechinjwa si kwa ajili ya Mwenyezi Mungu . Washirikina walikuwa wakichinja kwa ajili ya masanamu na kuyataja majina ya Lata na Uzza. Yamekwishatangulia maelezo kuhusu hayo katika Tasfiri (2:173).

5.Aliyekufa kwa kunyongeka : Ni yule anayekufa kwa kunyongwa kwa kamba, mkono au kuingizwa kwenye kitu cha kubana nk.

6Aliyekufa kwa kupigwa kwa fimbo au kitu chochote.

7.Aliyekufa kwa kuanguka : Ni yule aliyeporomoka kutoka juu akafa.

8.Aliyekufa kwa kupigwa pembe : Ni yule aliyepigwa pembe na mwenzake mpaka akafa.

9.Aliyeliwa na mnyama, lakini Mwenyezi Mungu ametoa katika aina hii akiwa hai. Huyo atakuwa halali kuliwa kwa kuchinjwa kisharia. Hii ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu ila mliowachinja. Katika Hadith imeelezwa kuwa kwa uchache wa kuwahi mchinjaji ni kumwahi akitingisha sikio lake, mkia wake au kupepesa jicho lake.

10.Aliyechinjiwa mizimu . Mwenye Kitabu Attashiul-liulumittanzil anasema: Mizimu ni mawe ambayo wakati wa ujahiliya walikuwa wakiyatukuza na kuyachinjia na wala sio masanamu. Kwa sababu masanamu ni yale yenye Sura, na mizimu haina Sura.

Ilivyo ni kwamba uharamu wa vyakula sio aina hizi kumi tu zilizotajwa na Aya tukufu, bali kuna aina nyingine za vyakula vilivyo haramu; kama vile mbwa, wanyama wanaoshambulia, ndege walao nyama; kama vile Kozi na Tai. Pia baadhi ya aina za samaki na vinginevyo viliivyotajwa na Hadith na kukongamana mafakihi. Wala hakuna tofauti baina ya yaliyoelezwa na Qur'an na yale yaliyoelezwa na Hadith.

﴿وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا﴾

"Na anachowapa Mtume kichukueni na anachowakataza kiacheni" (59:7).

Sio mbali kuwa kuhusisha kutaja aina hizi kumi ni kwa kunasibiana na kauli yake Mwenyezi Mungu, "Mmehalalishiwa wanyama."

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja aina hizo, ameunganisha kwa kusema:

Na kuagulia kwa mburuga.

Wakati wa Ujahiliya mtu akitaka kufanya jambo muhimu huchukua mbao tatu: moja huiandika 'Ameniamuru Mola wangu'; Ya pili huiandika 'Amenikataza Mola Wangu'; na ya tatu haiandiki kitu. Kisha huzifunika na kitu na kuingiza mkono wake ili atoe mojawapo. Ikitokea amri hufanya, ikitokea katazo huacha na ikitokea tupu hurudia, mpaka itokee amri au katazo.

Hayo yote ni ufasiki.

Yaani yote hayo yaliyotajwa. Hakuna maana ya kutofautiana wafasiri kuhusu neno 'Hayo' kuwa je ni kuhusisha hayo ya mburuga au yote, maadamu hukumu ya yote ni moja - ufasiki, yaani dhambi kubwa.

Leo waliokufuru wamekata tamaa katika dini yenu, basi msiwaogope na mniogope mimi.

Wafasiri wengi wamesema kuwa makusudio ya leo katika Aya ni siku ile iliyoshuka Aya hiyo. Siku ya Hija ya kuaga (Hijjatul-Wadai) katika mwaka wa kumi Hijriya.

Mwenye Majmaul-bayan anasema: Leo hapa ina maana ya sasa, kama mtu akisema leo umekua, akiwa na maana ya sasa umekua.

Vyovyote iwavyo maana ya Aya ni kuwa makafiri wamekata tamaa ya kuwa Uislamu utakwisha au kuharibika, baada ya kumakinika katika nyoyo za wafuasi wake na kuanza kuenea siku baada ya siku. Kwa hiyo enyi Waislamu msiwaogope makafiri bali muogopeni Mwenyezi Mungu peke yake. Amesema kweli Mwenyezi Mungu katika kila anayoyasema:

﴿يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٣٢﴾ هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ﴾

"Wanataka kuzima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, lakini Mwenyezi Mungu anakataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, wajapochukia makafiri. Yeye ndiye aliyemleta Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili aijalie kushinda dini zote ijapokuwa watachukia washirikina" (9:32-33).

Itakuwa ni jambo la faida kwa mnasaba huu tudokoze maneo kutoka Kitabu Al-Islam Fil-qarnil-Ishirin cha Aqad, amesema: "Uislamu hapo mwanzoni hakuwa na nguvu, lakini ukawa na nguvu imara, baada ya mamia ya miaka. Uimara huu na nguvu ya kiislamu katika hali ya udhaifu ni ya kustaajabisha, lakini uimara wake hivi sasa baada ya kupita karne ishirini ni wa kustaajabisha zaidi. Kwa sababu Uislamu hauna kinga yoyote wala mali, silaha, elimu au maarifa, Bali hata watu wake hawana maafikiano ya kujikinga.

Nguvu ya itikadi ya Kiislamu imeendelea katika pembe zote za ulimwengu ikiwa mbali na vita vya kidola na siasa zake au kuwa katika vyeo. Katika Afrika leo kuna mamilioni ya Waislamu, ambao hawana vyeo vyovyote katika nchi au katika siasa. Hali kama hiyo iko huko Sumatra na Java, na inakurubia hali hiyo katika Pakistan na pengine China na sehemu inayopakana nayo"

KUKAMILISHWA DINI NA KUTIMIZWA NEEMA

Leo nimewakamilishia dini yenu na kuwatimizia neema yangu na nimewapendelea Uislamu kuwa ndiyo dini.

Shia na Sunni wengi wametofautiana kuhusu Aya hii: Tutaelezea kauli za pande zote mbili, kama wanakili tu, sio waungaji mkono wala wakanushaji na kumwachia msomaji na akili yake aamue mwenyewe. Sunni au wengi wao wamesema kuwa makusudio ya Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewakamilishia Waislamu dini yao kwa kushinda kwake na kujitokeza kwake juu ya dini zote pamoja na kupigwa vita. Na ameitimiza neema yake kwa kubainisha itikadi yake na sharia yake kuanzia shina hadi matawi na kubainisha yote wanayoyahitajia katika dini yao na dunia yao.

﴿مَّا فَرَّطْنَا فِي الْكِتَابِ مِن شَيْءٍ﴾

"Hatukupunguza Kitabuni kitu chochote" (6:38)

Shia wamesema kuwa itawezekana kuifasiri Aya hii, kwa maana hayo, ikiwa hatutakukutanisha na tukio lake na kubainisha makusudio yake. Kwani Aya nyingi zinafasiriwa na tukio lililoambatana nalo na muda wa kushuka kwake. Kwa mfano kama ile Aya isemayo kumwambia Mtume wake mtukufu:

﴿وَتَخْشَى النَّاسَ وَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَاهُ﴾

"Na ukachelea watu na hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi ya kumchelea." (33:37)

Lau kama Aya hii tutaiepusha na kisa cha Zaid bin Haritha na tukachukua dhahiri yake, basi maana yatakuwa ni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anaathirika na kuwaridhisha viumbe kuliko muumba wake; jambao ambalo haliwezekani kwa yule ambaye Mwenyezi Mungu amemchagua kuchukua wahyi wake na ujumbe wake.

Kisha wakaendelea kusema Shia kuwa Aya hii imekutanishwa na tukio lake mahsusi linaloifasiri na kubainisha makusudio yake. Hilo wameliTafsir tolea dalili kama ifuatavyo:-

Kwanza : Wameafikiana wanachuoni wa Kishia na Kisunni, wafasiri na wana historia, kuwa Aya za Sura ya Maida zote zimeshuka Madina lakini Aya hii: (Leo nimewakamilishia dini yenu), imeshuka Makka mnamo mwaka wa 10H, mwaka ambao Mtume Muhammad(s.a.w.w) alihiji Hijja ya mwisho. Kwani alielekea kwenye rehema ya Mola (kufariki) katika mwezi wa Rabiul-Awwal (mfungo sita) mwaka wa 11 H.

Pili : Baada ya Mtume kumaliza Hijja yake hii, alielekea Madina. Alipofika Ghadir Khum - sehemu katika Juhfa penye njia nyingi - aliamrisha mnadi Swala anadi, watu wakakusanyika; na kabla ya kutawanyika kushika njia zao, akawahutubia, na miongoni mwa maneno aliyosema ni: "Hakika Mwenyezi Mungu ni mtawala wangu na mimi ni mtaw ala wa waumini na mimi ni bora kwao kuliko nafsi zao. Basi ambaye mimi ni mtawala wake na Ali ni mtawala wake. "Akasema hivyo mara tatu; riwaya nyingine zinasema ni mara nne, Kisha akaendelea kusema "Ewe Mola wangu! Mpende anayempenda na mhasimu anayemha simu, mdhalilishe anayemdhalilisha, ipeleke haki pamoja naye popote atakapokuwa. Haya basi aliyepo na amwambie asiyekuwepo"

Sunni hawaikanushi Hadith hii baada ya kuzidi kiwango cha Mutawatir[10] , na wengi katika Maimamu wao na wanavyuoni wao wameinukuu akiwamo Imam Ahmad Ibn Hanbal katika Musnadi yake, Nasai katika Khasais, Hakim katika Mustadrak, Khawarizami katika Manaqib, Ibn Abdu Rabbih katika Istia'b na Asqalani katika Iswaba. Vilevile Tirmidhi, Dhahabi, Ibn Hajar na wengineo. Lakini wengi wao wamefasiri neno Wilaya kwa maana ya mapenzi badala ya utawala na kwamba makusudio ya kauli ya Mtume(s.a.w.w) ambaye mimi ni mtawala wake, ni ambaye ananipenda na ampende Ali.

Shia wamejibu tafsiri hii, kuwa kauli ya Mtume inafahamisha waziwazi kwamba utawala ulithibiti kwa Mtume juu ya waumini ndio huo ulithibiti kwa Ali(a.s) bila ya kuzidi au kupungua. Na utawala huu ndio utawala wa kidini, hata kama neno Wilaya lina maana elfu.

Kwa hiyo basi maana ya Aya ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameikamilisha dini hii leo kwa kutoa kauli wazi kuwa Ali ni Khalifa.

Unaweza kuuliza : Kukamilisha dini kwa huidhihirisha juu ya dini nyingine na kubainisha hukumu yake kwa ukamilifu, kama wasemavyo Sunni, ni kauli wazi isiyohitaji tafsiri. Ama kukamilisha dini kwa kumweka Ali kuwa Khalifa ni kauli ambayo hapana budi kuweko na tafsiri na ufafanuzi, basi Shia wanaifasiri kwa namna gani?

Katika kufasiri hilo, Shia wamesema: Kukamilika haki hakutimii ila kwa kupatikana utawala wa sharia na utawala wa utekelezaji kwa pamoja, mmoja peke yake hautoshi ikiwa haukuungwa na mwingine.

Utekelezaji ulikuwa mikononi mwa Mtume Mtukufu(s.a.w.w) , Hapo maadui wa Uislamu wakadhani kwamba utawala wa utekelezaji utakwisha kwa kuondoka Mtume.

Na ukiondoka ndio Uislamu umeondoka. Ndipo Mtume akamweka Ali ahifadhi sharia baada yake na aisimamishe dini, kama alivyoisimamisha yeye. Kwa hiyo ikawa makafiri hawana tumaini lolote la kwisha Uislamu au kudhoofika.

Basi aliyefikwa na dharura bila kuelekea kwenye dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusameha mwenye kurehemu.

Imekwishapita tafsiri ya Aya hii katika (2:173) kifungu mwenye dharura na hukumu yake.

﴿يَسْأَلُونَكَ مَاذَا أُحِلَّ لَهُمْ قُلْ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَمَا عَلَّمْتُم مِّنَ الْجَوَارِحِ مُكَلِّبِينَ تُعَلِّمُونَهُنَّ مِمَّا عَلَّمَكُمُ اللَّـهُ فَكُلُوا مِمَّا أَمْسَكْنَ عَلَيْكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهِ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴾

4.Wanakuuliza wamehalalishiwa nini. Sema mmehalalishiwa vilivyo vizuri. Na mlichowafunza mbwa miongoni mwa wanyama wa kuwinda, mnawafunza kama alivyowafunza Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walichowakamatia na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.

NA MLICHOWAFUNZAWANYAMAWA MAWINDO

Aya 4

MAANA

Wanakuuliza wamehalalishiwa nini. Sema mmehalalishiwa vilivyo vizuri.

Kizuri ni kinyume cha kibaya. Vibaya ni vilivyoelezwa waziwazi na kuhusishwa na sharia kuhusu uharamu wake, kama vile nyamafu, nyama ya nguruwe; au vilivyoelezewa kiujumla, ambavyo kwa namna moja au nyingine vina madhara na ufisadi.

Jumla hii Mwenyezi Mungu ameitaja kwa tamko au kwa maana katika sehemu 15 kwenye Kitabu chake kitukufu.

Na mlichowafunza mbwa miongoni mwa wanyama wa kuwinda, mnaowafunza kama alivyowafunza Mwenyezi Mungu. Basi kuleni walichowakamatia na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu.

Madhehebu yote yameafikiana kwa kauli moja kwamba windo la mbwa ni halali kuliwa, likifa bila ya kuchinjwa, kwa masharti yafuatayo:

1. Kuwa mbwa amefundishwa - akiamrishwa na bwana wake anashika amri na akikatazwa anakatazika. Hiyo ndiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:"Mnawafunza kama alivyowafunza Mwenyezi Mungu".

2. Mwindaji awe amemshakiza mbwa kuwinda. Lau atakwenda mwenyewe na akaja na windo, si halali kuliwa.

3. Mwindaji awe Mwislamu, kwa upande wa Shia.

4. Asome Bismillah wakati wa kumshakiza mbwa, aseme: Nenda kwa jina la Mwenyezi Mungu na mfano wa hayo.

5. Mbwa alikute windo liko hai, na life kwa kujeruhiwa naye. Lau akilikuta limekufa basi si halali, au akilikuta hai, lakini likafa sio kwa kujeruhiwa basi si halali.

Hata hivyo wametofautiana kuhusu kuwinda kwa kutumia mnyama mwingine, asiyekuwa mbwa, kama vile: Chui, Kipanga nk. Shia wamesema, si halali na wengineo wamesema ni halali. Shia wametoa dalili kuwa neno'mbwa miongoni mwa wanyama wa kuwinda' katika Aya, linahusika na mbwa tu.

﴿الْيَوْمَ أُحِلَّ لَكُمُ الطَّيِّبَاتُ وَطَعَامُ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حِلٌّ لَّكُمْ وَطَعَامُكُمْ حِلٌّ لَّهُمْ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلَا مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ وَمَن يَكْفُرْ بِالْإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴾

5.Leo mmehalalishiwa vilivyo vizuri na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao; na wanawake wenye kujichunga katika waumini na wanawake wenye kujichunga katika wale waliopewa Kitabu kabla yenu mtakapowapa mahari yao mkafunga ndoa bila ya kufanya uzinzi wala kuwafanya mahawara. Na mwenye kukataa kuamini hakika amali zake zimepomoka na yeye huko Akhera atakuwa miongoni mwa wenye kupata hasara.

UTWAHARAWAWATU WA KITABU

Aya ya 5

LUGHA

Neno ihswan lina maana nne: Uislamu, kuolewa, uhuru na kujichunga na zina ambako ndiko kulikokusudiwa.

MAANA

Leo mmehalalishiwa vilivyo vizuri na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu na chakula chao ni halali kwao.

Wametofautiana Sunni na Shia katika maana ya makusudio ya chakula cha watu wa Kitabu ambao ni Mayahudi na Manaswara (Wakristo). Sunni wamesema makusudio ni walichokichinja. Haya yamenukuliwa kwao kutoka kwa mwenye Tafsir Al-Manar ninamnukuu:

"Wamefasiri kundi kubwa kuwa chakula hapa ni kwa maana ya walichokichinja, kwa sababu vyakula vinginevyo tayari ni halali kwa asili yake."

Mafakihi wengi wa Kishia wamesema kuwa watu wa Kitabu ni najisi wakaharamisha chakula chao, kinywaji chao na hata mkate na maji waliyo yagusa; na wakafasiri chakula katika Aya kwa maana ya nafaka (vyakula vya tembe tembe).

Ama sisi tunaona kuwa watu wa Kitabu ni twahara[11] . Tumeyafafanua haya pamoja na dalili katika Kitabu Fiqhul Imam Jafar as-Sadiq J.1. Na Marja'a wakubwa wengi wamekwenda na rai hii; akiwemo Sayyid Hakim na Sayyid Khui.

Ama kauli ya mwenye kusema kuwa mtu wa Kitabu ni mwenye kunajisika na wala si najisi, hiyo ni kucheza na maneno. Kwa sababu katika sharia vitu viko mafungu mawili Twahara na Najisi, hakuna cha tatu. Ni kweli kuwa kitu twahara kinaweza kuzukiwa na najisi kisha ikaondoka kwa kutwaharishwa; lau najisi inakuwa nacho basi kitakuwa ni najisi, sio chenye kunajisika.

Ama kufasiri chakula kwa kuhusisha nafaka ni umbali wa mbali kabisa na fasihi ya Qur'an na balagha yake. Imetumia neno chakula kwa windo la baharini wala hakuna nafaka baharini. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ ﴾

"Mmehalalishiwa kuvua baharini na chakula chake," (5:96)

Pia ametumia neno hilo katika maji, ambapo maji na nafaka ni tofauti. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿فَمَن شَرِبَ مِنْهُ فَلَيْسَ مِنِّي وَمَن لَّمْ يَطْعَمْهُ فَإِنَّهُ مِنِّي﴾

"Basi atakayekunywa humo si pamoja nami, na asiyekunywa atakuwa pamoja nami" (2:249)

Neno asiyekunywa hapo limetokana na twaam chakula. Vilevile amelitumia katika vyakula mbalimbali, Mwenyezi Mungu anasema:"..Na mnapokwisha kula tawanyikeni" (33:53)

Je, kuna yeyote atakayeweza kupitisha tafsiri yake kwa maana ya mkila shairi tawanyikeni? Kama atapitisha mfano wa tafisiri hii, basi itakuwa ni tafsir ya aina gani hiyo? Bali hata Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametumia chakula kuhusu nyama; akasema:

﴿قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ﴾

"Sema: Sioni katika yale niliyopewa wahyi kitu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa nyamafu au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe" . (6:145)

Kwa ajili hiyo basi tunasema kuwa chinjo la watu wa Kitabu ni halali ikiwa itajulikana kuwa masharti yamekamilika - kuelekea Qibla, kusoma Bismillahi na kukata mishipa minne. Hii ndiyo tofauti baina ya chinjo la mtu wa Kitabu na Mwislam, ambapo kwa mtu wa Kitabu haliwi halali mpaka ijulikane kuwa masharti yalikamilika.

Lakini kwa Mwislamu litakuwa halali bila ya kuweko haja ya kujua kukamilika masharti, ispokuwa kama itajulikana kuwa masharti hayakukamilika.

Tumeyafafanua haya pamoja na dalili katika Kitabu Fiqhul Imam Jafar as- Sadiq J 4.

Kuna riwaya sahihi kutoka kwa Ahlul Bait kuhusu jambo hili, akazitumia shahidi wa pili, Saduq, Ibn Abu Aqil na Ibn Al-Junaid. Mwenye Majmaulbayan amesema katika kufasiri Aya hii: "Wafasiri wengi na mafakihi wengi wamesema kuwa makusudio ya chakula katika Aya ni chinjo la watu wa Kitabu na ni kauli waliyokwenda nayo jamaa katika watu wetu" yaani wanachuoni wa Kishia wanaotegemewa kwa kauli zao.

Na wanawake wanaojichunga katika waumini na wanawake wanaojichunga katika wale waliopewa Kitabu kabla yenu mtakapowapa mahari yao mkafunga ndoa, bila ya kufanya uzinzi wala kuwafanya mahawara.

Makusudio ya uzinzi ni zina ya dhahiri na kufanya uhawara ni zina ya siri siri. Imeshartiwa mahari kwa kutokuzini kwa kutambulisha kwamba anachotoa mwanamume kumpa mwanamke ni lazima iwe ni mahari ya ndoa ya sharia sio hongo ya zina. Maana ni kwamba Mwenyezi Mungu amehalalisha kuwaoa wanawake wanaojistahi katika Waislamu na katika watu wa Kitabu. Na kwamba mwenye kuwaoa ni lazima awape mahari ya sharia kiasi cha mali iliyoafikianwa, sio malipo ya uzinzi.

Wameafikiana mafakihi wa madhehebu yote kwamba si halali kwa Mwislamu kumuoa asiyekuwa na dini kabisa wala wanaoabudu mizimu na moto. Wametofautiana katika ndoa ya mwenye Kitabu, yaani Wakristo na Mayahudi. Madhehebu mane ya Kisunni wamesema; Inajuzu kumuoa na wakatolea dalili kwa Aya hii. Wametofautiana mafakihi wa Kishia baina ya kujuzu na kutojuzu na kutofautisha baina ya ndoa ya daima na ya muda; baadhi wakajuzisha ya muda na kuzuia ya daima.

Sisi tuko pamoja na wasemao kujuzu bila ya chochote kwa kutegemea haya yafuatayo:-

Kwanza : Dalili zihalalishazo ndoa kwa ujumla.

Pili : Kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na wanawake wanaojichunga katika wale waliopewa Kitabu." Tatu: Riwaya nyingi kutoka kwa Ahlu bait(a.s) na kutajwa na mwenye Wasail na Jawahir na kuzisifu kwa Mustafidha, yaani zilizofikilia wingi wa kukurubia kuwa Mutawatir, Tumezinukuu baadhi yake katika Fiqh Imam Jafar as-Sadiq.

Unaweza kuuliza : utasema nini kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Wala msiwaoe washirikina mpaka waamini"(2:221)

na vile vile kauli yake Mwenyezi Mungu:"Wala msifungamane na makafiri katika mshikamano." (60:10)

Jibu : washirikina sio watu wa Kitabu kwa dalili ya kuunganishwa katika Aya isemayo:

﴿لَمْ يَكُنِ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ مُنفَكِّينَ حَتَّىٰ تَأْتِيَهُمُ الْبَيِّنَةُ ﴾

"Hawakuwa wale ambao wamekufuru katika watu wa Kitabu na washirikina ni wenye kuachana na waliyonayo mpaka iwajie hoja." (98:1)

Ama kauli yake "msifungamane na makafiri katika mshikamano" haiko wazi kuwa inahusu ndoa; Kwa sababu mshikamano, kama unavyofumbiwa, ndoa vile vile hufumbiwa isiyokuwa ndoa. Mwenye Masalik anasema: "Aya haiko wazi katika makusudio ya ndoa wala katika makusudio yaliyo kijumla zaidi ya hayo."

Na mwenye kukataa kuamini hakika amali zake zimepomoka na yeye huko Akhera atakuwa miongoni mwa wenye hasara.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja sehemu ndogo ya hukumu zake, halali yake na haramu yake anasema: Mwenye kusikia akatii basi yeye ni Mumin wa kweli, amali yake itakuwa yenye kukubaliwa na malipo yake na thawabu zake ni juu yangu.

Na atakayezikanusha hukumu zangu na sharia yangu basi yeye ni kafiri mwenye kupata hasara Kwa hiyo makusudio ya imani hapa ni zile zile hukumu ambazo ni wajibu kuziamini.

Hiyo ni katika mlango wa kufanya tendo kuwa ndio linatendwa; kama kusema kula kwa maana ya chakula. Kuhusu kupomoka tumekuzungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika (2:217)