TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16223
Pakua: 2355


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16223 / Pakua: 2355
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴾

6.Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu na miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni, na mkiwa wagonjwa au mumo safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara, mpake nyuso zenu na mikono yenu. Mwenyezi Mungu hapendi kuwatia katika taabu lakini anataka kuwatakasa na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.

﴿وَاذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَمِيثَاقَهُ الَّذِي وَاثَقَكُم بِهِ إِذْ قُلْتُمْ سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴾

7.Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu na ahadi yake aliyoifungamanisha nanyi mliposema: Tumesikia na tumetii Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yaliyomo vifuani.

UDHU NA TAYAMMAM

Aya 6 - 7

IRABU

Herufi Ba katika neno Biruu, usikum imesemekana ni ya kuzidi, ikasemekana ni ya kuambatana na ikasemekana ni ya kufanya baadhi. Ufafanuzi utakuja katika kifungu cha maana.

MAANA

Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, yaani mkitaka kuswali.

Basi osheni nyuso zenu

Hakuna tofauti katika hilo, isipokuwa kwamba Shia wamesema ni wajibu kuanzia juu na haifai kufanya kinyume. Wengine wamesema inafaa namna yoyote ingawaje kuanzia juu ni bora.

Na mikono yenu mpaka vifundoni

Vilevile hakuna tofauti isipokuwa Shia wamewajibisha kuanza vifundoni na kutanguliza mkono wa kulia. Sunni wakasema kuwa inafaa kuosha namna yoyote, ingawaje kuanzia vifundoni na kutanguliza kuume ni bora.

Unaweza kuuliza : Sunni na Shia wote wamekhalifu dhahiri ya Aya, kwa sababu vifundo inapasa iwe ni mwishilio wa kuosha kwa sababu ya herufi ilaa (mpaka) ambapo Sunni hawaliwajibishi hilo na Shia hawaliruhusu hilo. Je kuna Taawil gani?

Wengi wamejibu kuwa herufi ilaa hapa ina maana ya mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:"Na awazidishie nguvu mpaka kwenye nguvu zenu." (11:52)

Yaani pamoja na nguvu zenu. Tuonavyo sisi ni kuwa kuwekea mpaka katika Aya ni kuelezea sehemu za kiungo kinachooshwa ambacho ni mkono bila ya kuangalia namna ya kuosha - kuanzia na kuishilia, sawa na mtu anavyosema: Nimekuuzia ardhi kuanzia hapa mpaka huko. Au kata mawaridi ya bustani kuanzia hapa mpaka huko.

Akiwa na maana ya kuelezea kiwango na kiasi sio kubainisha namna na hali.

Na mpake vichwa vyenu.

Hanbal wamesema ni wajibu kupaka kichwa na masikio mawili, na kupaka kunaweza kutoshelezwa na kuosha kwa sharti ya kupitisha mkono kichwani. Malik wakasema ni wajibu kupaka kichwa chote isipokuwa masikio.

Hanafi wakasema ni wajibu kupaka robo ya kichwa; na inatosheleza kukivika kichwa majini au kukimiminia maji. Shafi wakasema ni wajibu kupaka baadhi ya kichwa ijapokuwa ni kidogo; Inatosha kuosha au kunyunyiza.

Shia Imamia wakasema ni wajibu kupaka sehemu ya mbele ya kichwa. Inatosheleza kwa uchache inavyokubalika jina la kupaka; wala haijuzu kuosha au kunyunyiza. Kwa hiyo, maana ya kuwa 'ba' ni kuambatana, ni ya kauli mbili za mwanzo; na kuwa 'ba' ni ya kufanya baadhi, ni ya kauli za mwisho.

Na miguu yenu mpaka vifundoni.

Kisomo (qiraa) cha miguu, kimekuja mara mbili: Kwa Nasb (Arjula) na kingine kwa Khafdh (Arjuli). Sunni wamesema ni wajibu kuosha miguu kwa vile imeungana na mikono kutokana na visomo vyote viwili cha kwanza kiko wazi kwamba inaungana kitamko na mahali. Ama kwa kisomo cha (Khafdh) ni kwa ujirani na kufuata; yaani kwa vile neno Ruusi (Vichwa) lina khafdh basi na jirani yake naye akapata khafdh; sawa na wasemavyo waarabu 'Juhru Dhwabbin Kharibin' ingawaje Kharibin ni wajibu isomewe kwa (raf_u) kwa sababu ni sifa ya Juhr, na wala sio sifa ya dhabbin, lakini imesomwa kwa Khafdh kwa sababu ya ujirani.

Shia wamesema ni wajibu kupaka miguu na wala sio kuosha kwa sababu neno miguu linaungana na vichwa. Kwa kisomo cha Khafdh ni wazi. Ama kwa kisomo cha Nasb[12] ni kuungana na mahali pa neno ruus (vichwa) ambapo ni pa Nasb. Kwa sababu kila kilicho majruri kitamko ni mansub ki mahali.

Kisha Shia wakaendelea kusema: Kuunganisha miguu kwenye mikono hakujuzu kutokana na mambo mawili: Kwanza ni kinyume cha ufasaha kwa sababu ya kuwako kitenganishi baina ya mikono na miguu. Kitenganishi chenyewe ni"na mpake vichwa vyenu." Lau kama miguu ingeunganishwa mikono, basi angelisema Mwenyezi Mungu. "Na mikono yenu mpaka vifundoni na miguu yenu mpaka vifundoni".

Pili : Kuunganisha kwenye mikono kunafanya maana ya kila kisomo kibadilishe maana nyingine. Kwani maana ya kisomo cha Nasb, ni kuosha na kwa kisomo cha jarri ni kwa kupaka. Na hii ni kinyume na kuunganishwa kwenye vichwa ambapo maana inakuwa moja kwa visomo vyote viwili. Zaidi ya hayo kufanya khafdh kwa ujirani si ufasaha wala haijatokea katika maneno ya Mwenyezi Mungu kabisa.

Mkiwa na janaba basi ogeni.

Ni wajibu kuoga janaba kwa mojawapo ya mambo mawili:

Kwanza : kushusha manii, iwe katika usingizini au kuwa macho.

Pili : Kuingiza kichwa cha dhakari katika tupu hasa kuitia yote kamili. Sunni hawakuwajibisha aina maalum ya kuoga, isipokuwa wamewajibisha kuenezwa maji kiwiliwili chochote kwa namna yoyote itakayokuwa.

Shia wameligawanya josho la janaba kwenye aina mbili: Tartib (kimpangilio) na Irtimasi (kujivika). Tartib, ni kujimiminia maji kwa kuanzia kichwa, kisha upande wa kuume wa mwili kisha wa kushoto. Lau ataharibu mpango huo, akatanguliza linalokuja baadae, basi josho litabatilika. Ama Irtimasi ni kukivika kiwiliwili chote katika maji kwa mara moja, lau sehemu itakuwa nje ya maji, basi haitoshi.

Na mkiwa wagonjwa au mko safarini au akawa mmoja wenu ametoka chooni, au mkagusana na wanawake, kisha msipate maji, basi tayamamuni na mchanga ulio twahara, mpake nyuso zenu na mikono yenu.

Imetangulia tafsiri yake katika (4:43)

Mwenyezi Mungu hapendi kuwatia katika tabu; lakini anataka kuwatakasa na kutimiza neema Yake juu yenu ili mpate kushukuru.

Tabu ni dhiki na mashaka; na madhara ni tabu na zaidi; kama vile adha, maradhi na kufilisika. Uislamu hauweki hukumu itakayoleta aina yoyote ya dhiki na mashaka, sikwambii madhara. Haukuamrisha jambo ila litakuwa na kheri na masilahi na haukukataza jambo ila ndani yake mtakuwa na shari na uharibifu.

Iwapo jambo lina yote mawili (manufaa na madhara) itaangaliwa, ikiwa manufaa ni makubwa zaidi basi hutakiwa kufanywa, na ikiwa madhara ni makubwa basi hukatazwa. Daima liangaliwalo ni wingi. Ikiwa yote ni sawa, basi kunakuwa na hiyari. Mwenyezi Mungu anasema:

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ﴾

"Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume wake anapowaitia katika yale yatakayowapa uhai" (8:24)

Na akasema tena:

﴿ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْر﴾

"Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi wala hawataki yaliyo mazito" (2:185)

Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu na ahadi yake aliyofungamanisha nanyi.

Kila mwenye kuingia dini au chama basi anakuwa amejiwekea mkataba wa kukubali misingi yake na mafunzo yake, na afanye hivyo kwa radhi yake, Na hii ndiyo ahadi ambayo tumemfungia Mwenyezi Mungu sisi Waislamu tulipoukubali Uislamu kuwa ndio dini.

Mwenye kuitekeleza ahadi hii kama alivyoamrisha Mwenyezi Mungu atakuwa amemtekelezea Mwenyezi Mungu, Na mwenye kuasi atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu.

Maana yaliyo dhahiri zaidi ya kutekeleza ahadi ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kuwafanyia ikhlasi waja wake na kuamiliana nao kwa ukweli, Na wala sijui alama ya ukweli katika dini zaidi ya kutekeleza ahadi. Namuusia kila binadamu asimwamini yeyote kwa elimu yake au ibada zake au cheo chake na umashuhuri wake, bali amwamini na amtegemee baada ya kuwa na yakini ya ukweli wake na utekelezaje wake wa ahadi.

﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴾

8.Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mtoao ushahidi kwa uadilifu. Wala kuchukiana na watu kusiwapelekee kutofanya uadilifu, Fanyeni uadilifu ndiko kunakokurubisha kwenye takua, Na Mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.

﴿ وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ ﴾

9.Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini na wakafanya mema kuwa watapata maghufira na malipo makubwa.

﴿ وَالَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِآيَاتِنَا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَحِيم﴾

10.Na wale waliokufuru na kuzikadhibisha ishara zetu, hao ndio watu wa motoni.

UADILIFU NDIO UNAOKURUBISHA KWENYE TAKUA

Aya 8 - 10

MAANA

Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, mtoao ushahidi kwa uadilifu.

Imani sahihi inayo mambo ya dhahiri yanayohisiwa. Mwenyezi Mungu ameyapanga na kuyafafanua kwa mifuno mbali mbali katika Aya kadhaa. Mengi yamepita na yanayokuja ni mengi zaidi. Aya tuliyonayo inasema kwa lugha ya wazi wazi kuwa ikiwa nyinyi ni waumini basi muwe wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na mshuhudie uadilifu.

Maana ya kumsimamia Mwenyezi Mungu Mtukufu ni ukweli na ikhlasi katika kauli na vitendo. Ama kushuhudia kwa uadilifu sio makusudio ya kuwatolea ushahidi maadui zetu na walio dhidi yetu kutokana na haki yetu au ya wengine, ingawaje mfumo wa Aya unafahamisha hivyo. Isipokuwa makusudio ni kufanya uadilifu mtu katika mambo yake yote bila ya kuonea.

Akiwa ni mtaalamu wa mambo ya kidunia, elimu yake ataifanya ni nyenzo ya kumaliza sababu za udhaifu, unyonge na kurudi nyuma, na kuleta sababu za kuwa na nguvu na maendeleo. Akiwa ni ulama wa mambo ya dini atalingania neno la Mwenyezi Mungu kufanya uzuri mtu ukhalifa wa Mwenyezi Mungu katika ardhi yake na kumsimamisha kila anayeipeleka kombo njia hii. Na akiwa hajui (sio ulama), basi atawaitikia wenye elimu na dini na kuwa upande wao akiwasaidia na kuwaunga mkono maadamu wako pamoja na haki.

Huu ndio uadilifu aliouamrisha Mwenyezi Mungu katika Aya hii na nyinginezo. Uadilifu ambao ndio matumaini ya ubinadamu na lengo lake, na ambao maisha hayawezi kuwa bila ya huo. Jamii inaweza kuishi bila ya elimu, lakini kuishi bila ya uadilifu katika upande wowote ule ni muhali, hata kama watu wake ni magwiji na wagunduzi. Elimu bila ya uadilifu madhara yake ni mengi kuliko manufaa yake. Ama uadilifu wote ni manTafsir ufaa, na ni muhali kuweko aina ya madhara ndani yake. Na kama ukiyapata, basi itakuwa ni njia ya kuzuia madhara makubwa zaidi na yenye hatari kubwa.

Wala kuchukiana na watu kusiwapeleke kutofanya uadilifu.

Fanyeni uadilifu Makusudio ya watu katika Aya hii ni maadui wa kheri na uadilifu ambao wanakwamisha kila jaribio la kumkomboa binadamu na minyororo ya udhaifu na kutoendelea. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anatuamrisha kufanya uadilifu na kufanya mambo kwa ajili ya maisha ya binadamu bila ya kujali chuki ya wanaokwenda kombo na vitimbi vyao. Kwa maneno mengine, inatakikana tufanye mambo kwa kutumia mfano unaosema: "mbwa anabweka na safari yaendelea"

Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini na wakafanya mema kuwa watapata maghufira na malipo makubwa.

Katika (2:25) Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa bishara waumini wa vitendo kwamba wao wana Pepo ambazo hupita mito chini yake, katika (3:57) akawabashiria kuwa Yeye atawalipa ujira, akaongeza katika (4:56) kwamba wao Peponi watapata Wake watakatifu. Na katika Sura nyingine akatoa ahadi kwa mifumo mingine. Lengo katika Sura zote ni moja tu - kuhimiza imani na matendo.

Na wale waliokufuru na kuzikadhibisha ishara zetu, hao ndio watu wa motoni.

Baada ya kuwaahidi neema waumini wa kimatendo, anawapa kiaga cha moto makafiri, kama kawaida yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kufuatisha kuhimiza na kuhofisha.

Aya hii ni dalili wazi kuwa mwenye kumkanusha Mwenyezi Mungu ni katika watu wa motoni, hata kama hakuambiwa na Mtume au wasii wa Mtume. Kwa sababu dalili zake Mwenyezi Mungu ambazo zinakuwa ni hoja ya kuweko kwake hazihusiki na aliyowateremshia mitume Wake. Ameisimamisha dalili ya kutosha juu ya umoja Wake na ukuu Wake katika nafsi na katika mbingu na ardhini; atakayezikanusha, hoja iko juu yake.

Mwenyezi Mungu anasema:

﴿أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا فِي أَنفُسِهِم مَّا خَلَقَ اللَّـهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ﴾

"Je hawafikirii katika nafsi zao (wakaona kuwa) hakuumba Mwenyezi Mungu mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa haki?". (30:8)

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ هَمَّ قَوْمٌ أَن يَبْسُطُوا إِلَيْكُمْ أَيْدِيَهُمْ فَكَفَّ أَيْدِيَهُمْ عَنكُمْ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴾

11.Enyi mlioamini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, walipoazimia watu kuwanyooshea mikono yao, akaizuia mikono yao kuwafikia. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

KUMBUKENI NEEMA YA MWENYEZI MUNGU

Aya 11

MAANA

Enyi mlioamini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, walipoazimia watu kuwanyooshea mikono yao, akaizuia mikono yao kuwafikia.

Ikisemwa amemnyooshea ulimi ni kumtukana, na amemnyooshea mkono ni kumshambulia.

Makusudio ya watu hapa ni washirikina wa Makka ambao walitaka kuumaliza Uislamu ulipoanza, kwa njia ya kuwashambulia wafuasi wake kwa kuwaua, kuwaadhibu na kuwafukuza kisha kutangaza vita na kuandaa majeshi. Lakini Mwenyezi Mungu hatimaye aliwapa ushindi Waislamu kwa maadui zake na wakawa watukufu baada ya kuwa dhalili na watawala badala ya kutawaliwa. Wala hakuna neema kubwa kuliko uhuru na kuwashinda maadui.

Baada ya Mwenyezi Mungu (swt) kuwakumbusha Waislamu neema hii tukufu, aliwaambia;

Na mcheni Mwenyezi Mungu, na waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

Yaani, tumewapa nguvu hizi ili mzitumie katika kuithibitisha haki na wala sio kuonyesha ushujaa; na katika kueneza amani na uadilifu, sio kuwakandamiza wanyonge kuwakalia na kuwatawala, kama walivyowafanyia washirikina hapo mwanzo na kama wafanyavyo watu wengi.

Wanatafuta uadilifu wawapo wanyonge na wanaukanusha mara tu wawapo na nguvu. Mumin wa kweli humwogopa Mwenyezi Mungu na kumshukuru akiwa na nguvu zaidi kuliko akiwa dhaifu; au angalau sawa katika hali zote mbili. Ama yule anayeamini kwa ulimi bila moyo, basi ni kinyume:

﴿فَإِذَا رَكِبُوا فِي الْفُلْكِ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ فَلَمَّا نَجَّاهُمْ إِلَى الْبَرِّ إِذَا هُمْ يُشْرِكُونَ﴾

"Na wanapopanda katika Jahazi humuomba Mwenyezi Mungu hali ya kuwa wanamtakasia utii, lakini anapowafikisha salama nchi kavu, mara wanamshirikisha" (29:65)

﴿ وَلَقَدْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ بَنِي إِسْرَائِيلَ وَبَعَثْنَا مِنْهُمُ اثْنَيْ عَشَرَ نَقِيبًا وَقَالَ اللَّـهُ إِنِّي مَعَكُمْ لَئِنْ أَقَمْتُمُ الصَّلَاةَ وَآتَيْتُمُ الزَّكَاةَ وَآمَنتُم بِرُسُلِي وَعَزَّرْتُمُوهُمْ وَأَقْرَضْتُمُ اللَّـهَ قَرْضًا حَسَنًا لَّأُكَفِّرَنَّ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَلَأُدْخِلَنَّكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ فَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ مِنكُمْ فَقَدْ ضَلَّ سَوَاءَ السَّبِيلِ ﴾

12.Na hakika Mwenyezi Mungu alifanya agano na wana wa Israil na tukaweka miongoni mwao wakuu kumi na wawili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa hakika mimi niko pamoja nanyi, kama mkisimamisha Swala na mkatoa Zaka na mkaamini mitume yangu na mkawasaidia na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri; hakika nitawafutia maovu yenu na nitawaingiza katika mabustani yapitayo mito chini yake, Basi atakayekufuru baada ya hayo hakika amepotea njia iliyo sawa.

﴿فَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَاقَهُمْ لَعَنَّاهُمْ وَجَعَلْنَا قُلُوبَهُمْ قَاسِيَةً يُحَرِّفُونَ الْكَلِمَ عَن مَّوَاضِعِهِ وَنَسُوا حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا بِهِ وَلَا تَزَالُ تَطَّلِعُ عَلَىٰ خَائِنَةٍ مِّنْهُمْ إِلَّا قَلِيلًا مِّنْهُمْ فَاعْفُ عَنْهُمْ وَاصْفَحْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ﴾

13.Basi kwa sababu ya kuvunja kwao agano, tuliwalaani na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanageuza maneno na mahali mwake na wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa. Na hutaacha kugundua khiyana yao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na uwaache, Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.

﴿وَمِنَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّا نَصَارَىٰ أَخَذْنَا مِيثَاقَهُمْ فَنَسُوا حَظًّا مِّمَّا ذُكِّرُوا بِهِ فَأَغْرَيْنَا بَيْنَهُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ وَسَوْفَ يُنَبِّئُهُمُ اللَّـهُ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ﴾

14.Na kwa wale waliosema: "Sisi ni Wanaswara", tulifanya agano nao, lakini wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa, kwa hiyo tukaweka baina yao uadui na chuki mpaka siku ya Kiyama, Na Mwenyezi Mungu atawaambia waliyokuwa wakiyafanya.

KUFANYAAGANO NAWAISRAIL

Aya 12 - 14

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Kitabu chake kitukufu amezungumzia makafiri na washirikina kwa ujumla, na akazungumzia washirikina wa Kiquraish kwa Sura mahsus, kutokana na aliyoyapata Mtume kutoka kwao.Vilevile amewazungumzia wanafiki, ambao walidhihirisha Uislamu na kuuficha ukafiri, na Mayahudi na Wakristo, lakini Mayahudi amewazungumzia zaidi kuliko wote. Kwa sababu wao ndio waliokuwa na inadi zaidi na chuki juu ya ubinadamu. Yamepita mengi kuwahusu wao katika Sura ya Baqara, Al-Imran na Annisa. Sehemu kubwa ya Sura tuliyonayo (Al-Maida), inawahusu wao na Wakristo.

Na hakika Mwenyezi Mungu alifanya agano na wana wa Israil na tukaweka miongoni mwao wakuuu kumi na wawili.

Mwenyezi Mungu ametaja kuwa amewaweka viongozi kumi na wawili katika wana wa Israil, na wala hakubainisha kuwa je, hawa ni viongozi wa vizazi vyao ambao wanawakilisha matawi kumi na mawili ya Yakub, ambaye ndiye Israil, au ni Mitume au Mawasii? Hakutaja chochote, na sisi tunanyamaza aliyoyanyamizia Mwenyezi Mungu.

Aya inaelezea wazi kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa na ahadi na waisrail, inayowataka watekeleze mambo matano na Mwenyezi Mungu atawalipa mambo mawili wakitekeleza, na wasipotekeleza watastahili adhabu. Mambo yenyewe ni haya yafuatayo:-

1. Kusimamisha Swala (Mkisimamisha Swala )

2. Kutoa Zaka (na mkatoa Zaka )

3. Kuamini Mitume ya Mwenyezi Mungu (Na mkaamini Mitume yangu )

4. Kusaidia Mitume (na mkawasaidia )

5. Kutoa mali Sabili (Na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri ). Kuunganishwa kukopesha na Zaka kunafahamisha kuwa ilikuwa ni wajibu katika mali yao mambo mawili: Zaka na kutoa mali sabili. Wakitekeleza mambo haya matano ambayo ni masharti katika agano lao, basi Mwenyezi Mungu atawalipa mambo mawili yakiwa ni malipo ya masharti hayo. Mambo yenyewe ni:-

1. Kufutiwa maovu (hakika nitawafutia maovu yenu ).

2. Pepo (na nitawaingiza katika mabustani yapitayo mito chini yake ). Hili ndilo agano la Mwenyezi Mungu na waisrail pamoja na masharti yake na malipo, Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaambia: Basi atakayekufuru baada ya hayo hakika amepotea njia iliyo sawa.

Basi kwa sababu ya kuvunja kwao agano, tuliwalaani.

Hakika wao wanavunja kila ahadi isipokuwa ahadi ya kuvunja ahadi, Hii ni nembo isiyowabanduka milele, kama ambavyo laana haiwabanduki, kwa vile kuvunja ahadi kunalazimiana na laana.

Na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu

Kila asiyeogopa shari na maasi basi moyo wake umekufa. Amesema Imam Ali(a.s) ."Ambaye imekuwa chache staha yake basi moyo wake umekufa."

Unaweza kuuliza : Vipi Mwenyezi Mungu amenasabisha kwake ugumu wa nyoyo zao? Je, hii haimanishi kuwa wao hawana jukumu lolote na ugumu huu, kwa sababu unatoka kwa Mungu na sio kwao?

Jibu : Mwenyezi Mungu amewabainshia njia ya heri na akawaamrisha kuifuata hiyo njia; na akawabainishia njia ya sharii, akawakataza kuifuatia; na akachukua kwao ahadi ya kusikiliza na kutii, kisha wakahaini, wakavunja ahadi na wakaendelea kuasi. Kwa hiyo akawaachilia mbali; na asiwaelekeze kwenye amali ya kheri; na kwa kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaelekeza ndio ikasihi kunasibishiwa kwake ugumu. Mwenye kutaka zaidi, na arudie tuliyoyaeleza katika kufasiri Sura (4:88).

Wanageuza maneno na mahala mwake.

Imetangulia tafsiri yake katika Sura (4:46)

Na wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa.

Wamekumbushwa Taurat wakabadilisha yale yanayopingana na matakwa yao na kubakisha wanayoyatamani. Ikiwa wameweza kuvunja ahadi ya Mwenyezi Mungu, na wakakibadilisha Kitabu chake alichowateremshia basi watashindwaje kuvunja ahadi na waarabu na wengineo na kugeuza maazimio ya Umoja wa Mataifa na Baraza la usalama.

Na hutaacha kugundua khiyana yao, isipokuwa wachache miongoni mwao.

Mayahudi wa Bara arabu wakati huo hawakutosheka na kuukanusha utume wa Muhammad(s.a.w.w) bali walikula njama pamoja na maadui zake, ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia hivyo; yaani wewe Muhammad umekutana na mengi kutoka kwao na utaendelea kukutana na mengi, hata kama utawafanyia wema, kwa sababu mwema na mbaya kwao ni sawa, isipokuwa wachache tu katika wao waliosilimu na wakasadikisha Uislamu wao, kama Abdullah bin Salam na waliokuwa pamoja naye. Pamoja na yote hayo, Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kuukabili uovu wao kwa wema.

Basi wasamehe na uwaache.

Unaweza kuuliza : kuwa ni umbali sana kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwasifu kwa sifa mbaya na kwamba haitarajiwi kheri kutoka kwao, kisha amwamrishe Mtume wake awasamehe na kuachana nao.Je Mayahudi wanajua maana ya msamaha? Na je, inafaa kumsamehe nyoka na nge.

Swali hilo limejibiwa kwa majibu kadha ; kama vile kuwa dhamiri ya'wasamehe' inawarudia wachache waliosilimu na kufanya ikhlas. Jengine ni kuwa Aya hii imefutwa hukmu yake na Aya ya upanga.

Majibu yote haya yanawezekana. Ama la kwanza ni kwamba dhamiri kwa dhahiri yake inamrudia aliye karibu. Ama la pili ni kupatikana 'kufuta hukumu' katika Qur'an.

Inawezekana kuwa amri ya kuwasamehe ilishuka baada ya Uislamu kuwa na nguvu ukawa katika ngome madhubuti isiyodhurika na vitimbi vya Mayahudi na wengineo katika makafiri.

Na kwa wale walisema: Sisi ni wanaswara, tulifanya agano nao.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) hali ya Mayahudi ya kuvunja ahadi na kubadilisha, amebainisha hali ya Wakristo, na kwamba wao na Mayahudi hali yao ni moja tu, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya iliyotangulia ametaja aina ya ahadi waliyoivunja Mayahudi, na hapa hakutaja ya Wakristo. Sio mbali kuwa Mwenyezi Mungu ametumia maneno ya kiujumla kwa Wakristo kwa kufafanua ahadi aliyochukua kutoka kwao ambayo ni Tawhid.

Na wakaacha sehemu ya yale waliyokumbushwa.

Waliyokumbushwa ni Injil aliyoiteremsha Mwenyezi Mungu kwa Isa(a.s) inayoelezea wazi wazi Umoja wa Mwenyezi Mungu na utume wa Muhammad(s.a.w.w) kwa jina la Ahmad, lakini wakabadilisha, sawa na Mayahudi walivyobadilisha Taurat.

Dalili ya nguvu zaidi kuwa Injil imebdilishwa ni kwamba viongozi wa kanisa na Maulama wa historia katika Injil nne ambao Wakristo waliwategemea katika karne ya nne, walitofautiana kuhusu nani aliyeandika Injil, imeandikwa lini, kwa lugha gani na vipi imekosekana kopi yake ya asili? Tofauti hizi zinapatikana katika Encyolopidia kubwa ya Kifaransa. Haya na mengine mengi ameyataja mwenye Tafsiri Al-manar.

Kwa hiyo tukaweka baina yao uadui na chuki mpaka siku ya Kiyama.

Hakuna maneno bora yaliyosemwa, katika kufasiri jumla hii, kama yale yalisemwa na Sheikh Abu Zahra katika Kitabu Muhadharat fi Annasraniyya. Kwa hiyo ninamnukuu: "Kumetokea kutoelewana na uadui baina ya wale waliosema: Sisi ni Manaswara, tangu zamani na hivi sasa, kusadikisha yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Kitabu chake kikweli na kitukufu.

Damu zimemwagika baina yao wenyewe, kiasi ambacho hakijawahi katika kupigana kwao na watu wengine katika historia yote. Ni sawa iwe hilo ni kwa sababu ya tofauti za kidini au uongozi wa kidini au hata tofauti za kisiasa, kiuchumi na kijamii. Uadui huu umeendelea muda mrefu na wala hautazimika mpaka siku ya Kiyama, kama alivyosema Mkweli wa wasemaji."

﴿يَا أَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءَكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ كَثِيرًا مِّمَّا كُنتُمْ تُخْفُونَ مِنَ الْكِتَابِ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ﴾

15.Enyi watu wa Kitabu! Amekwishawafikia Mtume wetu, anayewafichulia mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi. Hakika imekwisha wafikia nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinachobainisha.

﴿يَهْدِي بِهِ اللَّـهُ مَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَهُ سُبُلَ السَّلَامِ وَيُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِهِ وَيَهْدِيهِمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴾

16.Mwenyezi Mungu huwaongoza kwacho wenye kufuata radhi yake katika njia za amani na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenya nuru kwa amri yake, na huwaongoza katika njia iliyonyooka.

IMEKWISHAWAFIKIA NURU

Aya 15 - 16

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake(s.a.w.w) na Waislamu wote kujadiliana na watu wa Kitabu kwa uzuri; kisha akatoa mfano wa mjadala huu ili wawe na ubainifu wa maana yake. Miongoni mwa mifano hiyo ni kusema Waislamu kuwaambia watu wa Kitabu:

﴿آمَنَّا بِالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْنَا وَأُنزِلَ إِلَيْكُمْ وَإِلَـٰهُنَا وَإِلَـٰهُكُمْ وَاحِدٌ وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ﴾

"Tunaamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu na Mungu wetu na Mungu wenu ni mmoja, nasi ni wenye kusilimu kwake" (29:46)

﴿قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ أَلَّا نَعْبُدَ إِلَّا اللَّـهَ وَلَا نُشْرِكَ بِهِ شَيْئًا وَلَا يَتَّخِذَ بَعْضُنَا بَعْضًا أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ﴾

"Sema enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno la usawa baina yetu na baina yenu. Kwamba tusimwabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu wala tusimshirikishe na chochote, wala baadhi yetu wasiwafanye baadhi kuwa ni miungu, zaidi ya Mwenyezi Mungu." (3:64)

Na kuna Aya zinazoelezea baadhi ya madhambi ya watu wa Kitabu, kama vile Aya hii tuliyo nayo. Imetaja kugeuza kwao Taurat na Injil na kumfanyia inadi Muhammad aliyewajia na uongofu.

Enyi watu wa Kitabu! Amekwisha wafikia Mtume wetu, anayewafichulia mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi.

Makusudio ya Mtume ni Muhammad(s.a.w.w) kwa sababu yeye amewabainishia Mayahudi na Wakristo, baadhi ya waliyoyaficha katika Kitabu walichonacho. Wakristo walificha Tawhid ambayo ni msingi wa dini na Mayahudi katika itikadi wakaficha habari ya Hisabu na adhabu siku ya Kiyama, na katika sharia wakaficha uharamu wa riba na kurujumiwa mzinifu; kama ambavyo Mayahudi na Wakristo kwa pamoja walificha Utume wa Muhammad:

"Ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurat na Injil." (7:157) Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfichulia Muhammad(s.a.w.w) yote waliyoyaficha na kuyabadilisha Mayahudi katika Taurat na Wakristo katika Injil, kisha Muhammad(s.a.w.w) akawaambia mengi waliyokuwa wakiyaficha na akayanyamazia mengi aliyoyajua. Hii ndio maana ya:

Anayewafichulia mengi mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayesamehe mengi.

Ufichuaji huu kutoka kwa Muhammad umekuwa ni dalili ya mkato ya utume wake na miujiza miongoni mwa miujiza ya Qur'an ambao haifai kwa mwenye akili kuutilia shaka. Kwa sababu Mtume(s.a.w.w) alikuwa ni Ummiy (asiyesoma Kitabu) wala hakuambiwa na yeyote yaliyo katika vitabu vya Mayahudi na Wakristo.

Unaweza kuuliza : Kwa nini Mtume aliwaambia baadhi tu na asiwaambie yote.

Jibu : Lengo ni kuwafahamisha kuwa Mtume anayajua wanayoyaficha; na lengo hilo linafikiwa kwa kuyasema baadhi; kama ambavyo linafikiwa kwa kueleza yote. Zaidi ya hayo ni kwamba walijua kuwa yeye Mtume(s.a.w.w) anajua baadhi ya waliyoyaficha basi ndio wamejua kuwa yeye anayajua yote.

UISLAMU NAWAPIGANIAAMANI

Hakika imekwishawafikia nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Kitabu kinachobainisha.

Imesemwa kuwaNuru ni Muhammad naKitabu ni Qur'an; na ikasemwa kuwa hizo ni sifa za Uislamu, wala hakuna tofauti baina ya kauli mbili ila katika ibara tu, kwa sababu Muhammad, Uislamu, na Kitabu ni maana yanayolazimiana hayaachani.

Mwenyezi Mungu huwaongoza kwacho wenye kufuata radhi yake.

Yaani mwenye kupendelea radhi ya Mwenyezi Mungu peke yake, na akaitafuta haki kwa njia ya haki, atapata katika Uislamu matakwa yake na makusudio yake, Kwa sababu ndani yake kuna faida tatu.

1.Njia za amani : Makusudio ya amani sio ile wanayoihusisha wapigania amani, ya kutaka amani kwenye roho na mali za raia, isipokuwa makusudio ni amani kamili inayowachanganya watu wote, amani ya nyumba na familia kutokana na malezi mabaya. Vilevile Usalama wa akili kutokana na ujinga na imani potofu, na kusalimika nafsi na tamaa, chuki, uongo na hadaa.

2.Na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye Nuru kwa amri yake : Yaani anawatoa Mwenyezi Mungu kwa amri yake kutoka katika giza la kuabudu masanamu kwenye Nuru ya Tawhid ambayo itawakomboa na vifungo vyote isipokuwa kumwabudu Mwenyezi Mungu mwenye nguvu.

3.Na huwaongoza katika njia iliyonyoka : Njia iliyonyoka kwa Mwenyezi Mungu ni ile inayoyafanya maisha haya kuwa ni raha na wema, sio mashaka na uovu. Baada ya yote hayo je, watetezi wa amani wanaopiga kelele za kuongeza mapato yatosheleze watu wote, wanayo njia bora na yenye kufaa zaidi ya ile ya Uislamu? Je, wao wanawapenda waja wa Mwenyezi Mungu zaidi au wao wanajua zaidi masilahi yao kuliko Yeye Mwenyezi Mungu anavyojua kwa viumbe vyake? Au je, katika itikadi ya kiislamu, sharia ya kiislamu na maadili ya Uislamu au katika hukumu za kiislamu, kuna hata moja inayopingana na kuongeza kipato na kukigawanya kwa haki?

Qur'an ndiyo ya kwanza kulingania kwenye maisha bora. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: "Hakika hii Qur'an inaongoza katika njia iliyonyooka kabisa." (17:9)

Wafasiri wanasema kuwa njia iliyonyooka ni hali nzuri. Vyovyote nitakavyotia shaka, lakini nina yakini kwamba hakuna yeyote anayeusoma Uislamu kwa usahihi, yaani kwa uwezo na kutokuwa na kitu kingine, ila atauamini, atake asitake.

﴿لَّقَدْ كَفَرَ الَّذِينَ قَالُوا إِنَّ اللَّـهَ هُوَ الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ قُلْ فَمَن يَمْلِكُ مِنَ اللَّـهِ شَيْئًا إِنْ أَرَادَ أَن يُهْلِكَ الْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ وَمَن فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴾

17.Hakika wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni Masih bin Maryam! Sema: Ni nani anayemiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu kama akitaka kumwangamiza Masih bin Maryam na mama yake na waliomo ardhini wote? Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na vilivyomo baina yake. Huumba atakavyo; na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

﴿وَقَالَتِ الْيَهُودُ وَالنَّصَارَىٰ نَحْنُ أَبْنَاءُ اللَّـهِ وَأَحِبَّاؤُهُ قُلْ فَلِمَ يُعَذِّبُكُم بِذُنُوبِكُم بَلْ أَنتُم بَشَرٌ مِّمَّنْ خَلَقَ يَغْفِرُ لِمَن يَشَاءُ وَيُعَذِّبُ مَن يَشَاءُ وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴾

18.Na Mayahudi na Manaswara wanasema: Sisi ni watoto wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwanini anawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni watu (tu) katika aliowaumba. Humghufiria amtakaye na humwadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake; na marejeo ni kwake.

﴿يَا أَهْلَ الْكِتَابِ قَدْ جَاءَكُمْ رَسُولُنَا يُبَيِّنُ لَكُمْ عَلَىٰ فَتْرَةٍ مِّنَ الرُّسُلِ أَن تَقُولُوا مَا جَاءَنَا مِن بَشِيرٍ وَلَا نَذِيرٍ فَقَدْ جَاءَكُم بَشِيرٌ وَنَذِيرٌ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

19.Enyi watu wa Kitabu! Hakika amewafikia Mtume wetu anayebainishia, katika wakati usio na Mitume, msije mkasema: Hakutufikia mtoaji bishara wala mwonyaji; basi amekwishawafikia mtoaji bishara na mwonyaji na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

WALISEMA MWENYEZI MUNGU NI MASIH

Aya 17 - 19

MAANA

Hakika wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni Masih bin Maryam. Tumefahamu kuwa hukumu za sheria za kutungwa zinabadilika kulingana na wakati. Ama kubadilika misingi ya itikadi ya kidini, kulingana na hali na wakati, ni jambo lisiloingilika akili, Lakini yametokea haya katika itikadi ya Kimasihi (Kikristo).

Itikadi ya Kimasih ilianzia na Tawhid (Umoja wa Mungu) safi; na baadhi ya vikundi vikaenedelea kubaki kwenye Tawhid kwa mda mrefu. Miongoni mwa vikundi hivyo ni kikundi cha Paul, Arius na Apico; kama inavyoeleza Aya 116-117 katika sura hii (Al-Maida), Na Qur'an imeelezea wazi kuwa Isa(a.s) alileta itikadi ya Tawhid (Mungu Mmoja). Kama inavyoeleza Aya 116-117

Ikaendelea itikadi ya Tawhid kwa Wakristo wengi na wala haikutangazwa itikadi ya utatu na kuungwa mkono kwa nguvu hadi mwaka 325 AD, ambapo baraza kuu la Nicaea lilipitisha uamuzi wa kuthibitisha uungu wa Masih na kumkufurisha mwenye kusema kuwa yeye ni mtu; wakachoma vitabu vyote vinavyomsifu kuwa si Mungu, na akautekeleza uamuzi huo, Costantine, Mfalme wa Roma. Akawa Masih ni Mungu kwao baada ya kuwa ni mtu.[13] Amesema kweli mwanafalsafa wa Kichina Lin Yu Tang: "Hakika Wagiriki wamewafanya miungu yao mfano wa watu. Ama Wakristo waliwafanya watu mfano wa Mungu"

Abu Hanifa naye anasema kuwa Mwenyezi Mungu hana hukumu hasa, ispokuwa hukumu yake ni vile anavyoona Mujtahid; yaani hukumu ya Mwenyezi Mungu hasa ni ile aliyoihukumu mtu pekee; si kwambii kundi au baraza kuu.

Kwa hali hiyo, inatubainikia kuwa itikadi ya Uungu wa Isa(a.s) ilikuwa kabla ya kushuka Qur'an kwa kiasi cha karne tatu. Kwa hiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu;

Hakika wamekufuru wale waliosema Mwenyezi Mungu ni Masih bin Maryam.

Maana yanakuwa yako wazi yasiyohitajia taawili ya kuingiliana na umoja; kama walivyofanya wafasiri wengi waliotangulia, wakidai kwamba Wakristo wengi hawasemi kuwa Isa ni Mungu, bali wanasema Mungu ameingia kwake au ameungana naye kwa hiyo hapana idadi. Mwenye Tafsir Al-manar anasema: "Mfano wa Zamakhshari, Baidhawi na Arrazi, hawakuangalia kwa undani kuhusu Ukristo; Kwa sababu hawakuvisoma vitabu vyao wala kuvipitia" Amesema kweli mwenye Al-Manar; kwani mwenye kuviangalia vitabu vyao, atakuta maelezo ya utatu waziwazi.

Amenukuu Sheikh Abu Zahra maelezo mengi kutoka katika vitabu hivyo, katika Kitabu Muhadharat Fi Annasraniyya na akaweka mlango maalum, katika Kitabu hiki, kwa anuani: "Ukristo kama ulivyo kwa Wakristo na katika vitabu vyao!" Miongoni mwa yaliyomo ni kwamba; Kasisi Butar alitunga risala aliyoita Al-usul wal-furuu akisema: "Katika Ungu kuna asili tatu, na kila mmoja ina kazi yake mahsus kwa mtu." Yamekwishatangulia maelezo kuhusu asili tatu, katika kufasiri Sura (4:50)

ASHAIRA NAWAKRISTO

Unaweza kuuliza : Wakristo wanaamini utatu na umoja wakati mmoja, kwa sababu wao wanasema: Kwa jina la baba na la mwana na la roho mtakatifu Mungu Mmoja. Sasa inawezekanaje kuchanganya umoja na utatu? Vipi moja iwe tatu na tatu iwe moja?

Wakristo wenyewe wamejibu hilo, kuwa: itikadi iko juu ya akili na wao wanakuza watoto wao kwenye hilo na kuwaambia: Kama hamkufahamu hakika hii mtaifahamu Siku ya Kiyama.

Kwa mnasaba huu tunaashiria kuwa Ashaira katika Waislamu wanasema: Mwenyezi Mungu anamtakia mja ukafiri, kisha anamwadhibu. Ikiwa kauli ya Wakristo, ya tatu moja haingiliki akilini, basi kauli ya Ashaira, kuwa Mwenyezi Mungu anafanya kitu kisha ana mwaadhibu mja wake haingiliki akilini vile vile.

Ama Waislamu wanaamini kwa imani ya mkato kwamba kila linalothibitishwa na akili, linathibitishwa na dini, na linalokataliwa na akili, linakataliwa na dini. Na wamepokea kutokana na Mtume wao kuwa yeye amesema: "Asili ya dini yangu ni akili." Na kwamba mtu mmoja alimuuliza kuhusu maana ya wema na dhambi; akamwambia: "Utake fatwa moyo wako. Wema ni ule uliotuliza nafsi, na ukatulizana moyo. Na dhambi ni ile iliyotia wasiwasi nafsi na kusitasita moyoni, hata kama watu watakutolea fat-wa.

Sema: Ni nani anayemiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu kama akitaka kumwamngamiza Masih bin Maryam, na mama yake na waliomo ardhini wote?

Aya hii ni dalili kubwa ya kuwajibu Wakristo kuwa Masih si Mungu, Kwa sababu ikiwa Mwenyezi Mungu anaweza kumwamngamiza Masih, basi Masih si Mungu. Na kama hawezi kumwangamiza, basi Yeye sio Mwenyezi Mungu.

Huenda mtu akasema kuwa : Aya hii haifai kuwa ni jibu kwa Wakristo, pia si dalili ya ukweli. Kwa sababu ni madai yasiyokuwa na dalili. Wakristo wanaweza kusema kuwa Mwenyezi Mungu hawezi kumwangamiza Masih wala Masih hawezi kumwangamiza Mwenyezi Mungu, kwa vile kila mmoja ni Mungu?

Jibu : Wakristo wameafikiana kwa kauli moja kwamba Mayahudi walimsulubu Masih, wakamwuudhi na kumwua na kumzika kaburini chini ya ardhi. Vile vile Injil yao imesema: "Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake." (Mat; 27:50). "Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, Mikononi mwako naiweka roho yangu. Alipokwisha kusema hayo akakata roho" (Luka 23:46)

Lakini walipomjia Yesu na kuona kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; Lakini askari mmoja wapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji (Yohana 19: 33-34)

Na Mayahudi na Manaswara wanasema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Kauli yao hii ni sawa na kauli ya waliyozungumziwa na Mwenyezi Mungu aliposema: "Na walisema: Hataingia peponi ila aliye Myahudi au Mnaswara."(2:111) Kwa hakika itikadi ya Kiislamu inasema kuwa hakuna ubora wa binadamu kwa mwanadamu mwingine ila kwa takua, na kwamba kutamka neno Uislamu tu si chochote ila iwe pamoja na matendo mema. Sema: Basi kwanini anawaadhibu kwa ajili ya dhambi zenu?

Unaweza kusema : kuwa hili halitoshi kuwa ni jibu la Mayahudi, kwa sababu wanaweza kusema: Mwenyezi Mungu hatatuadhibu akhera! Ikiwa hawana dalili ya kutoadhibiwa kwao huko Akhera, vile vile hakuna dalili ya kuadhibiwa kwao siku hiyo?.

Jibu : Makusudio ya adhabu ni adhabu ya duniani na akhera. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaadhibu Mayahudi duniani kwa Fir'aun, Nebukadnezzar, Roma na wengineo. Angalia tafsiri ya Sura (2:40).

Ama adhabu ya Wakristo duniani hiyo ni chungu zaidi. Kwa sababu walikuwa wakipigana wenyewe kwa wenyewe na kuadhibiana wenyewe kwa wenyewe. Iilivyo hasa, baba hawezi kuwaadhibu wanawe, na mpenzi hawadhibu wapenzi wake.

Ama dalili ya kuadhibiwa kwao huko akhera ameiashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kauli yake, bali nyinyi ni watu (tu). Hamtofautiana na wengine katika chochote. Watu wote wanatokana na Adam, na Adam ameTafsir tokana na mchanga! Kama alivyosema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Humghufiria amtakaye , ambaye anamwona anastahiki maghufira yake.Na humwadhibu amtakaye , ambaye anamwona kuwa anastahiki adhabu yake.

Hakuna yeyote atakayemlazimisha msamaha au kumzuia kuadhibu. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake. Kwa sababu yeye ni muumba wa ulimwengu, Na mwenye kuwa hivyo hahitajii watoto wala wapenzi.

Na marejeo ni Kwake.

Huko watajua Mayahudi na Wakristo kwamba wao ndio waja wa Mwenyezi Mungu waliochukiwa zaidi na Mwenyezi Mungu na watakuwa na adhabu zaidi kwa kumzulia kwao uongo kuwa wao ni watoto wa Mwenyezi Mungu na wapenzi wake.

Enyi watu wa Kitabu! Hakika amewafikia Mtume wetu, anayewabainishia, katika wakati usio na mitume.

Yaani; baada ya kukatika wahyi kwa muda mrefu na kuhitaji watu mitume na mwongozi. Imam Ali(a.s) anasema:"Alimtuma Mtume na watu wamepotea wamedangana, wanakusanya fitina, wamechotwa na matamanio, wameingiwa na Kibr, wamechanganyikiwa na ujinga, wamedangana katika mgongano wa mambo na balaa la ujinga, Akafikisha Mtume (s.a.w.w) nasiha na kulingania kwa hekima na mawaidha mazuri."

Msije mkasema: Hakutufikia mtoaji bishara wala mwonyaji. Basi amekwishawafikia mtoaji bishara na mwonyaji. Mwenyezi Mungu hakuwaachia hoja wala udhuru. Aya hii iko katika maana ya (4:165)

Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu Anaweza kumnusuru Muhammad(s.a.w.w) na kuliweka juu neno la Uislamu, hata kama Mayahudi na Wakristo watapinga.