TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA0%

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Mwandishi:
: HASANI MWALUPA
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi:

Matembeleo: 16211
Pakua: 2350


Maelezo zaidi:

Juzuu 1 Juzuu 2 Juzuu 3 Juzuu 4 Juzuu 5 Juzuu 6 Juzuu 7 Juzuu 8 Juzuu 12 Juzuu 13 Juzuu 14 Juzuu 15 Juzuu 16 Juzuu 17 Juzuu 18 Juzuu 19 Juzuu 20 Juzuu 21 Juzuu 22 Juzuu 23 Juzuu 24
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 11 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 16211 / Pakua: 2350
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA SITA Juzuu 6

Mwandishi:
Swahili

5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA SITA

﴿وَإِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ يَا قَوْمِ اذْكُرُوا نِعْمَةَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ إِذْ جَعَلَ فِيكُمْ أَنبِيَاءَ وَجَعَلَكُم مُّلُوكًا وَآتَاكُم مَّا لَمْ يُؤْتِ أَحَدًا مِّنَ الْعَالَمِينَ﴾

20.Na pale Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipowafanya manabii kati yenu, na akawafanya watawala, na akawapa ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.

﴿ يَا قَوْمِ ادْخُلُوا الْأَرْضَ الْمُقَدَّسَةَ الَّتِي كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ وَلَا تَرْتَدُّوا عَلَىٰ أَدْبَارِكُمْ فَتَنقَلِبُوا خَاسِرِينَ﴾

21.Enyi watu wangu ingieni katika ardhi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amewaandikia, Wala msirudi nyuma msije mkawa wenye kuhasirika.

﴿قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِنَّ فِيهَا قَوْمًا جَبَّارِينَ وَإِنَّا لَن نَّدْخُلَهَا حَتَّىٰ يَخْرُجُوا مِنْهَا فَإِن يَخْرُجُوا مِنْهَا فَإِنَّا دَاخِلُونَ ﴾

22.Wakasema: Ewe Musa huko kuna watu majabari, Nasi hatutaingia huko mpaka watoke, Wakitoka huko basi tutaingia.

﴿قَالَ رَجُلَانِ مِنَ الَّذِينَ يَخَافُونَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِمَا ادْخُلُوا عَلَيْهِمُ الْبَابَ فَإِذَا دَخَلْتُمُوهُ فَإِنَّكُمْ غَالِبُونَ وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴾

23.Wakasema watu wawili, miongoni mwao wale wanaomwogopa (Mwenyezi Mungu), ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha: Waingilieni kwa mlangoni; mtakapowaingilia hapo, kwa hakika mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini.

﴿قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِنَّا لَن نَّدْخُلَهَا أَبَدًا مَّا دَامُوا فِيهَا فَاذْهَبْ أَنتَ وَرَبُّكَ فَقَاتِلَا إِنَّا هَاهُنَا قَاعِدُونَ﴾

24.Wakasema: Ewe Musa! Sisi hatutaingia kabisa maadamu hao wamo humo, Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa.

﴿قَالَ رَبِّ إِنِّي لَا أَمْلِكُ إِلَّا نَفْسِي وَأَخِي فَافْرُقْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ﴾

25.Akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu; basi tutenge na watu hawa mafasiki

﴿قَالَ فَإِنَّهَا مُحَرَّمَةٌ عَلَيْهِمْ أَرْبَعِينَ سَنَةً يَتِيهُونَ فِي الْأَرْضِ فَلَا تَأْسَ عَلَى الْقَوْمِ الْفَاسِقِينَ ﴾

26.Akasema: Basi wameharamishiwa (ardhi) hiyo kwa miaka arubaini, watatangatanga ardhini, Basi usiwasikitikie watu mafasiki.

MUSA NAWATU WAKE

Aya 20 - 26

MAANA

Aya hizi ni sehemu ya mfululizo wa kisa cha wana wa Israil ambacho Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekitaja sehemu mbali mbali katika Sura za Qur'an, Baadhi ya sehemu za kisa hicho amezirudia. Nazo, kama unavyoziona, maana yake yako dhahiri.

Na pale Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu, alipowafanya manabii kati yenu, na akawafanya watawala na akawapa ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.

Musa aliwakumbusha neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yao, kama utangulizi wa atakayowaamrisha - Jihadi. Alizihesabu neema hizo kuwa ni tatu:

Kwanza : kuwa Mwenyezi Mungu amewafanya mitume katika wao.

Pili : amewafanya wajitawale, wako huru wanajitawala wenyewe; hakuna neema kubwa kama uhuru.

Tatu : kuwa aliwafanyia mambo ambayo hakumfanyia mtu yeyote: Aliwaangamiza adui yao bila jihadi wala kupigana; akawateremshia Manna na Salwa bila ya kulima wala kuvuna; akawatolea maji safi kutoka kwenye jiwe bila ya kufukua wala kuchimba; na akawafunika na kiwingu bila ya kujenga wala tabu yoyote.

Neema hizo tatu, zatupa tafsir ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

﴿يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ﴾

"Enyi wana wa Israil! Kumbukeni neema zangu nilizowaneemesha na nikawatukuza kuliko viumbe wengine" (2:47)

Kutukuzwa kwa watu wa wakati wao kulikuwa ni kwa kutumwa mitume kutokana na wao, kuwa huru, kuteremshiwa Manna na Salwa na mengineyo. Kwa maneno mengine kufadhilishwa kulikuwa hakukuwa ni kwa hulka na sifa, bali kulikuwa ni kwa namna walivyofanyiwa.

Enyi watu wangu! Ingieni katika hiyo ardhi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amewaandikia, wala msirudi nyuma msije mkawa wenye kuhasirika.

Baada ya Musa kuwakumbusha neema ya Mwenyezi Mungu juu yao, aliwaamrisha kuipigania Palestina, na humo walikuwa na Waithi na Wakanaani, akawaamrisha kuwa na uvumiliivu na uthabiti katika vita; Mwenyezi Mungu alikuwa amewaahidi kukaa hapo wakati huo. Kwa hiyo kauli ya Musa: "Ambayo Mwenyezi Mungu amewaandikia," ni kuashiria ahadi hiyo, na wala sio maana yake kuwa Palestina ni milki yao kabisa kama wanavyodai Mayahudi.

Hata hivyo watu wake walimwambia kwa woga na udhaifu: "Ewe Musa! Huko kuna watu majabari, Nasi hatutaingia huko mpaka watoke, Wakitoka huko basi tutaingia" Wanataka ushindi rahisi na wa raha, usiowalazimisha kuuliwa wala kujeruhiwa; sawa na alivyoangamizwa adui yao Firaun.

Lakini kulikuwa na watu wawili katika wao waliosimama kuwaongoza wakiwahimiza kusikiliza na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ndio aliowaashiria Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Wakasema watu wawili, miongoni mwao wale wanaomwogopa (Mwenyezi Mungu), ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha: Waingilieni kwa mlangoni; mtakapowaingilia hapo, kwa hakika mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini.

Yaani washambulieni ndani ya majumba yao watadhalilika na kuvunjika nguvu, huku mkiwa mnamtegemea Mungu kikweli kweli, kama ilivyo kwa waumini wenye ikhlasi. Lakini wao walirudia kwenye umbile lao la inadi na jeuri za kujiona, wakasema:

Ewe Musa! Sisi hatutaingia humo kabisa maadam wao wamo humo, Basi nenda wewe na Mola wako mkapigane, sisi tutakaa hapa.

Je, umeuona ufidhuli wao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Ni Mola wao pale palipo na masilahi yao ya kiutu, ikiwa hatawakalifisha na jambo litakalo wahangaisha na ikiwa atawaua maadui zao huku wenyewe wamekaa wakiwa salama.

Ama akiwaambia litakalowahangaisha hata kwa taklifa ndogo tu, basi huyo ni Mola wa Musa, na wala si Mola wao. Maana yake nikuwa matamanio yao peke yake ndiyo Mungu wao na Mola wao anayestahiki kuabudiwa na kutakaswa. Kwa kweli hali hii haihusiki na Mayahudi tu peke yao, bali inamchanganya kila anayemwabudu Mwenyezi Mungu nchani; na ni wengi katika Waislamu na Wakristo.

Akasema: Ewe Mola Wangu! Hakika mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu.

Huu ni mwelekeo kutoka kwa Musa kwa Mola wake akieleza masikitiko kwa kutengwa kwake na watu wake baada ya juhudi kubwa na taabu nyingi kwa ajili yao. Mimi similiki ila nafsi yangu na ndugu yangu; hakuna milki wala amri kwa asiyetiiwa.

Basi tutenge na hawa watu mafasiki .

Musa akawa hana budi kumwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu awatenge yeye na watu wake baada ya kuvunja kwao ahadi ya Mwenyezi Mungu.

Akasema: Basi wameharamishiwa (ardhi) hiyo kwa miaka arubaini, watatangatanga ardhini, Basi usiwasikitikie watu mafasiki.

Hayo ndiyo malipo yao: Kutangatanga katika jangwa la Sinai lisilo kuwa na chochote, watembea humo bila ya kujua njia ya kutokea na wapi pa kwenda. Watakuwa hivi miaka arubaini mpaka wakubwa wao waishe na kinyanyukie kizazi kingine kipya.

﴿وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ ابْنَيْ آدَمَ بِالْحَقِّ إِذْ قَرَّبَا قُرْبَانًا فَتُقُبِّلَ مِنْ أَحَدِهِمَا وَلَمْ يُتَقَبَّلْ مِنَ الْآخَرِ قَالَ لَأَقْتُلَنَّكَ قَالَ إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّـهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ ﴾

27.Na wasomee habari za watoto wawili wa Adam kwa ukweli, walipotoa Sadaka, ikakuba liwa ya mmoja wao, na ya mwingine haikukubaliwa. Akasema: Nitakuua! Akasema: Mwenyezi Mungu huwapokelea wamchao tu.

﴿لَئِن بَسَطتَ إِلَيَّ يَدَكَ لِتَقْتُلَنِي مَا أَنَا بِبَاسِطٍ يَدِيَ إِلَيْكَ لِأَقْتُلَكَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ رَبَّ الْعَالَمِينَ﴾

28.Kama utaninyooshea mkono kuniua, mimi sitakunyoshea mkono wangu kukuua. Hakika mimi namwogopa Mola wa walimwengu.

﴿إِنِّي أُرِيدُ أَن تَبُوءَ بِإِثْمِي وَإِثْمِكَ فَتَكُونَ مِنْ أَصْحَابِ النَّارِ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الظَّالِمِينَ﴾

29.Mimi nataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako; na kwa hivyo uwe miongoni mwa watu wa motoni, Na hayo ndio malipo ya madhalimu.

﴿فَطَوَّعَتْ لَهُ نَفْسُهُ قَتْلَ أَخِيهِ فَقَتَلَهُ فَأَصْبَحَ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴾

30.Basi nafsi yake ikamfanya kumwua ndugu yake, akamwua; na akawa miongoni mwa wenye kuhasirika.

﴿فَبَعَثَ اللَّـهُ غُرَابًا يَبْحَثُ فِي الْأَرْضِ لِيُرِيَهُ كَيْفَ يُوَارِي سَوْءَةَ أَخِيهِ قَالَ يَا وَيْلَتَىٰ أَعَجَزْتُ أَنْ أَكُونَ مِثْلَ هَـٰذَا الْغُرَابِ فَأُوَارِيَ سَوْءَةَ أَخِي فَأَصْبَحَ مِنَ النَّادِمِينَ ﴾

31.Hapo Mwenyezi Mungu akamleta kunguru anayefukua katika ardhi, ili amwonyeshe jinsi ya kuisitiri maiti ya ndugu yake. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa sawa na kunguru huyu na kuficha maiti ya ndugu yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.

QABIL NA HABIL

Aya 27 - 31

MAANA

Wasimulizi wa visa na wafasiri wengi wamesimulia ngano za kisa cha watoto wawili hawa wa Adam. Lakini hakuna rejea zozote za visa hivyo ila ngano za Kiisrail.

Sisi tutafupiliza yale yanayofahamika kutokana na Aya, kama ifuatayo:- Watoto wawili kutoka katika mgongo wa Adam moja kwa moja, kama inavyoonyesha, walizozana. Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutaja wazi majina yao, lakini wafasiri na wanahistoria walisema kuwa jina la muuaji ni Qabil na la aliyeuawa ni Habil.

Sababu ya mzozo ni kuwa kila mmoja wao alitoa sadaka. Mwenyezi Mungu Mtukufu akakubali sadaka ya Habil na kuikataa ya Qabil. Qur'an haikutaja aina ya sadaka wala aina ya kuikubali na kuikataa.

Qabil akamwonea kijicho nduguye na akatishia kumuua. Habil akamwambia wewe mwenyewe ndiwe mwenye kosa mimi sio wa kulaumiwa, kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anakubali wanaomcha na wewe si katika wao. Na kama unataka kuniua basi mimi sitakukabili kukuua; dhambi za kuniua na za kuacha kukubaliwa sadaka yako zitakutosha.

Hata hivyo maneno haya hayakuathiri nafsi ya Qabil, bali yalizidisha kijicho chake; na akatekeleza makusudio yake, Baada ya ndugu yake kuwa mfu, hakujua namna ya kumsitiri. Ndipo Mwenyezi Mungu akampelekea kunguru akachimbua shimo kwa miguu yake na mdomo wake. Baada ya muuaji kuona vile, Mushkeli wake ukaondoka, akapata mwongozo wa kumzika ndugu yake, kutokana na kazi ya kunguru. Naye akauma vidole kwa majuto ya kufanya dhulma kama ambavyo alijiona yeye anashindwa na kunguru kwa maarifa.

Huu ndio ufupi wa kisa kama kilivyofahamika kutokana na Aya. Kwa mnasaba huu ni vizuri kuelezea kuhitalifiana kuliko maarufu sana baina ya maulama wa maadili, tangu zamani, kuwa je, mtu ni mshari kwa asili na ni mwenye heri kwa asili? Wafasiri wamejaribu kukitolea dalili kisa hiki kuwa ni mshari kwa asili.

Ilivyo hasa ni kuwa kila mtu ana mwelekeo wa heri na shari kwa maumbile yake; hata yule mbora wa wabora na mshari wa washari. Tofauti ni kuwa baadhi ya watu wana akili thabiti iliyo imara au dini yenye nguvu itakayowafunga kupupia shari. Na wengine wanasukumwa na matamanio kwa udhaifu katika dini yao au akili yao.

﴿مِنْ أَجْلِ ذَٰلِكَ كَتَبْنَا عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ أَنَّهُ مَن قَتَلَ نَفْسًا بِغَيْرِ نَفْسٍ أَوْ فَسَادٍ فِي الْأَرْضِ فَكَأَنَّمَا قَتَلَ النَّاسَ جَمِيعًا وَمَنْ أَحْيَاهَا فَكَأَنَّمَا أَحْيَا النَّاسَ جَمِيعًا وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُنَا بِالْبَيِّنَاتِ ثُمَّ إِنَّ كَثِيرًا مِّنْهُم بَعْدَ ذَٰلِكَ فِي الْأَرْضِ لَمُسْرِفُونَ ﴾

32.Kwa ajili ya hayo tukawaandikia wana wa Israil ya kwamba atakayeua nafsi isiyoua nafisi au kufanya ufisadi katika ardhi, basi ni kama amewaua watu wote. Na mwenye kuiacha hai ni kama amewaacha hai watu wote. Hakika waliwafikia mitume wetu kwa hoja zilizo wazi; kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika ardhi.

MMOJA NA WENGI

Aya 32

MAANA

Kwa ajili ya hayo tukawaandikia wana wa Israil

Kisa cha watoto wawili wa Adam kimefichua kuwa watu ni aina mbili; mkosa na mwenye kukosewa. Kwa sababu ya kuhami mwenye kukosea, na kuchunga maisha na nidhamu yake, Mwenyezi Mungu amejaalia kila mkosa na adhabu yake anayostahili; akazingatia kuuwa wasio na hatia ni kosa ya makosa yote.

Kauli yake Mwenyezi Mungu:Kwa ajili ya hayo , ni ishara ya kosa la kuuwa kama lilivyo na wala sio ishara ya kisa cha Qabil na Habil; ingawaje hicho ndiyo sababu ya sharia hiyo; sawa na inavyotunga sharia serikali kwa sababu ya tukio fulani.

Unaweza kuuliza : Adhabu ya kuua inawaenea watu wote, sasa kuna makusudio gani ya kuwahusu wana wa Israil?

Jibu : Ni kweli kuwa adhabu hii inawahusu watu wote, lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kuwataja Mayahudi, kwa sababu wao ndio wanaouwa zaidi waja wake na kumwaga damu zao. Taurat yao inashuhudia hilo kwa kuwahalalishia kuua wanawake na watoto, na historia yao inashuhudia kuua kwao mitume hapo zamani na pia historia yao ya sasa huko Palestina.

Ya kwamba atakayeua nafsi isiyoua nafsi au kufanya ufisadi katika ardhi.

Yaani inajuzu kisheria kumwua aliyeua mtu kwa uadui; vile vile inajuzu kumwua mwenye kufanya ufisadi katika nchi. Ni malipo yenye kulingana na ni kuchunga maisha ya watu na usalama wao.

Ama mwenye kumuua mtu asiyekuwa na hatiabasi ni kama amewaua watu wote.

Wametofautiana wafasiri na wasiokua wafasiri katika wajihi wa kufananisha kuuwa mtu mmoja na watu wote, na kumwacha hai ni kama kuwaacha hai watu wote. Kuna mwenye kusema hilo ni sisitizo la kukanya kosa la kuua na kuhimiza kuiokoa nafsi na kuiepusha na maangamizo, kama vile moto n.k.

Mwingine naye akasema, hiyo ni kubainisha hakika ya muuaji, kwamba mwenye kuweza kuua mtu mmoja basi anaweza kuua watu wengi; sawa na kusema: "Anayeiba yai ataiba ngamia."

Na kwamba mwenye kumfanyia hisani mtu mmoja basi anaweza kuwafanyia wote, Wengine wamesema, hiyo ni kubainisha tabia ya watu kwamba tabia inakuwa sawa tu, haizidi kwa wingi wa watu wala haipungui kwa uchache wao.

Tulivyofahamu sisi kutokana na Aya ni kuwa mtu mmoja katika mtazamo wa Kiislamuu ndio lengo na wala sio nyenzo ya kumfikia mwingine; na kwamba yeye ndio dhahiri ya ubinadamu. Anastahiki yanayostahiki ubinadamu - heshima na karama. Kumfanyia makosa yeye ni kuufanyia makosa ubinadamu ambao unakuwa kutokana naye na watu wote; na kumfanyia wema yeye ni kuwafanyia wema watu wote.

Unaweza kuuliza : Huku si kukazia mawazo kwa mtu mmoja na kujitolea mhanga watu wengi kwa ajili ya mtu mmoja; ambapo sawa ni kuwa kinyume cha hivyo?

Jibu : Makusudio sio masilahi ya mtu mmoja ambayo yanaingilia masilahi ya wengi wala si ya mtu ambaye anajaribu kuishi kwa gharama ya wengine. Huyu haisabiwi kua ni mtu kwa maana yake sahih; bali yeye ndiye adui zaidi wa utu katika mtazamo wa Kiislamu.

Ndipo Mwenyezi Mungu akaashiria kwa kusema:"au ufisadi katika nchi." Makusudio hasa ni mtu mmoja ambaye anayatengeneza masilahi yake na masilahi ya wengi, na anayeona kuwa maisha yake ndiyo maisha ya wote na heshima yake ni ya wote.

Kama ambavyo masilahi ya wote ni masilahi ya mtu mmoja mmoja, kwa sababu wote sio ndege bali wote ni mtu mmoja mmoja. Kundi lolote likiwa na mnyonge asiye na haki basi lote litakuwa ni nyonge, na limeharibika; sawa ulivyo mwili, kama kiungo chake kimoja kikiharibika, au nyumba ikivunjika moja ya nguzo zake. Kwa hali hii ndipo masilahi ya mmoja na wote, yatakuwa yamekamilika.

Hakika waliwafikia mitume wetu kwa hoja zilizo wazi; kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika ardhi.

Yaani mitume waliwafikishia Mayahudi hukumu ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kuwazungumzia kwa wahyi utakao kwake Mungu, kuwa kuua mtu asiye na hatia ni kama kuua watu wote, lakini Mayahudi hawakujali tahadhari hii, na wakaendelea kufanya ufisadi wa kumwaga damu na kuwavunjia watu heshima.

Kauli yake Mwenyezi Mungu baada ya haya ni ishara kuwa waliyafanya waliyoyafanya baada ya kusimamisha hoja na kuondoka nyudhuru zote za kuweza kusamehewa. Huu ndio msimamo wa Qur'an kwa kila mpinzani, inahojiana naye kwa mantiki ya haki na kumlingania kwa hekima, hata kama atang'ang'ania upinzani wake. Utakuwa ni wa kuipinga haki tu, sio kumpinga mwenye kulingania.