MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE 0%

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE Mwandishi:
: SALMANI SHOU
Kundi: Misingi mikuu ya Dini

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

Mwandishi: KIMEANDIKWA NA SAYYID MUJTABAA MUUSAWIY LARI
: SALMANI SHOU
Kundi:

Matembeleo: 27509
Pakua: 2661

Maelezo zaidi:

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 28 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 27509 / Pakua: 2661
Kiwango Kiwango Kiwango
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

Mwandishi:
Swahili

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

KIMEANDIKWA NA

SAYYID MUJTABAA MUUSAWIY LARI

KUHUSU MWANDISHI

Sayyid Mujtaba Mussawi Lari ni mtoto wa marehemu Ayatullah Sayyid Ali Asghar Lari mmojawapo wa wanachuoni na watu mashuhuri katika jamii ya Iran. Babu yake alikuwa marehemu Ayatullah Hajj Sayyid Abd ul- Husayn Lari ambaye alipigania uhuru wakati wa mapinduzi ya kikatiba. Wakati wa kipindi kirefu cha mapambano yake dhidi ya serikali dhalimu ya wakati huo, alijaribu kuanzisha serikali ya Kiislamu na alifaulu kufany hivyo kwa kipindi kifupi huko Larestan.

Sayyid Mujtaba Musawi Lari alizaliwa mwaka 13/4/1935 kwenye jiji la Lar ambako alihitimu elimu yake ya Msingi na masomo ya mwanzo ya Kiislamu. Mnamo mwaka wa 1332/1953, aliondoka Lar na akaenda Qum kuendelea na masomo yake ya elimu ya Kiislamu, akiwa anafundishwa na maprofesa na waalimu wa taasisi ya Kidini, pamoja na wanazuoni wakuu katika maarifa ya sheria (maraji).

Mnamo mwaka wa 1341/ 1962, akawa mshiriki katika Maktabil-Islam, gazeti la kidini na kisayansi lililokuwa lianaandika mfululizo wa makala kuhusu maadili ya Kiislamu. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kuchapishwa kitabu kilichoitwa Ethical and psychological Problems. Matoleo tisa katika kitabu hiki kwa lugha ya kiajemi (Fursi) yamechapishwa, na pia kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu na hivi karibuni kwa Kifaransa.

Mnamo mwaka 1342/1963. Alisafiri kwenda Ujerumani kutibiwa, na alirudi Iran baada ya miezi kadhaa, aliandika kitabu kiitwacho 'The face of Western Civilization'. Kitabu hiki kinajumuisha mazungumzo ya kulinganisha ustaarabu wa Kimagharibi na Kiisilamu, ndani ya kitabu hiki, mwandishi anataka kuthibitisha, kwa njia ya utambuzi, kifikira na ulinganisho kamili, ubora wa utambuzi na mambo mengi ya ustaarabu wa Uislamu kwa ule wa Magharibi. Kitabu hiki hivi karibuni tu kimechapishwa tena kwa mara ya saba. Mnamo 1349/1970, kitabu hiki kilitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na mtaalam wa mambo ya nchi za Mashariki, F.G. Goulding, na kilichochea hisia za watu huko Ulaya. Makala kuhusu kitabu hiki zilionekana kwenye magazeti kadhaa ya kimagharibi na BBC ilifanya mpango wa mahojiano na mtarjumi huyo ambapo sababu za kutafsiri na jinsi kilivyopelekwa hapo Uingereza zilizungumziwa. Tafsiri ya Kiingereza ya kitabu hiki hadi sasa imechapishwa mara tatu huko Uingereza, mara tano Iran na mara mbili Marekani.

Mnamo takriban miaka mitatu baada ya kuchapishwa tafsiri ya Kiingereza, Rudolf Singler, profesa wa chuo Kikuu wa Kijerumani alikitafsiri katika lugha ya Kijerumani, na tafsiri hiyo ilithibitisha kuwa yenye kuvutia huko Ujerumani. Mmojawapo wa viongozi wa chama cha Social Democratic Party alimtaarifu Mtarjumi katika barua kwamba kitabu hicho kimeacha mvuto wa kina juu yake yeye, na kusababisha yeye kubadilisha maoni yake kuhusu Uislamu, na kwamba angelipendekeza Kitabu hicho kisomwe na marafiki zake. Tarjuma ya lugha ya Kijerumani imerudiwa kuchapishwa mara tatu hadi sasa.

Tafsiri za Kiingereza na Kijerumani za kitabu hiki zilichapishwa na Wizara ya Mwongozo wa Kiislamu kwa ajili kuisambaza zaidi nje ya Iran kupitia Wizara ya mambo ya Nje na taasisi ya mafunzo ya Kiislamic nchi za nje. Wakati huo huo ilipochapishwa tafsiri ya kwanza ya lugha ya Kijerumani, mwanachuo Muislamu wa asili ya kihindi aitwaye Maulana Raushan Ali alikitarjumi kitabu hiki katika lugha ya Urdu kwa lengo la kukisambaza India na Pakistani. Tarjumi hii ya Urdu imechapishwa mara tano hadi sasa. Sayyid Mujtaba Musawi Lari pia ameandika kijarida kuhusu Tawhid (upweke wa Mwenyezi Mungu), ambacho kilitafsiriwa Uingereza na kuchapishwa mara kadhaa Marekani.

Mnamo mwaka 1343/1964, aliasisi taasisi ya kutoa msaada huko Lar kwa madhumuni ya kueneza Uislamu, kutoa mafunzo ya Kiislamu kwa vijana walioko vijijini, na kuwasaidia wasiojiweza. Taasisi hii iliendelea kufanya kazi hadi 1346/1967. Taasisi hii ilitekeleza mambo makuu kama kuwapeleka wanafunzi wa sayansi za Kidini vijijini kufundisha Uislamu kwa watoto na vijana, kuwagawia maelfu ya watoto wa shule nguo, vitabu, vifaa vya kuandikia, kujenga idadi ya misikiti, mashule, zahanati mijini na vijijini, na huduma nyingine nyingi.

Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliyaandama matakwa yake katika maadili ya Kiislamu, akiandika makala mpya kuhusu somo hilo. Mnamo mwaka wa 1353/1974, mkusanyiko wa makala hizi, zilizopitiwa upya na kuongezewa maneno, zilitoka katika muundo wa kitabu kilichoitwa 'The Function of Ethics in Human Development.' Kitabu hiki kimechapishwa mara sita hadi sasa.

Mnamo mwaka 1357/1978, alisafiri hadi Marekani kwa mwaliko wa Taasisi ya Kiislamu nchini humo. Halafu akaenda Uingereza, Ufaransa na baada ya kurudi Iran alianza kuandika mfululizo wa makala kuhusu itikadi za Uislamu kwa ajili ya gazeti la Sorouch. Makala hizi baadaye zilikusanywa na kutengenezwa kitabu chenye juzuu nne kuhusu imani za misingi za Uislamu (tauhid, uadilifu wa Mwenyezi Mungu, utume, uimamui, na ufufuo) kwa jina la 'The Foundations of Islamic Doctrine.' Kitabu hiki chenye juzuu nne kimetafsiriwa katika lugha ya Kiarabu, sehemu zake zingine zikiwa tayari zimekwisha chapishwa mara tatu. Tafsiri ya Kiingereza ya juzuu ya kwanza ya kazi hii ndio imetengeneza kitabu hiki cha sasa; juzuu zilizosalia pia zitatafsiriwa na kuchapishwa. Tafsiri za Urdu, Hindi na Kifaransa pia zimo katika mpango wa kutayarishwa; juzuu mbili za lugha ya Kifaransa zimekwishatokea.

Mnamo mwaka wa 1359/1980, Sayyid Mujtaba Musawi Lari aliasisi Taasisi huko Qum iitwayo 'Office for The Diffusion of Islamic Culture Abroad.' Husambaza bure nakala za vitabu vyake vilivyotafsiriwa kwa watu wapendao kuzisoma duniani pote. Taasisi hii pia imechukua shughuli ya kuchapisha Qur'ani kwa lengo la kuisambaza kwa Waislamu binafsi, Taasisi na shule za Kidini hapa Afrika.

NENO LA MCHAPISHAJI

Kitabu kilichoko mikononi mwako, ni tarjuma ya kitabu cha Kiingereza, kwa jina la: "God and His Attributes." Sisi tumekiita: "Mwenyezi Mungu na Sifa Zake." Kitabu hiki, "Mwenyezi Mungu na Sifa Zake" ni kazi ya kielimu iliyofanywa na Mwanachuoni mahiri, Sayyid Mujtaba Musawi Lari. Mwandishi wa kitabu hiki ameichambua itikadi ya Kiislamu na Umoja wa Mungu (tawhid) kwa kutumia uhojaji wa kifilosofia na maneno mepesi. Ili kukamilisha kazi yake hii ametegemea sana juu ya Sunna na nukuu nyingi kutoka kwenye Qur'an Tukufu.

Kitabu hiki ni chenye manufaa sana, hususan wakati huu wa maendeleo makubwa ya elimu katika nyanja zote. Kutokana na ukweli huu, Taasisi yetu ya 'Al-Itrah Foundation' imeona ikitoe kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, kwa madhumuni yake yale yale ya kuwahudumia Waislamu, hususan wazungumzaji wa Kiswahili, ili kuongeza ujuzi wao katika masuala ya dini na ya kijamii.

Tunamshukuru ndugu yetu, Salman Shou kwa kukubali jukumu hili la kukifanyia tarjuma kitabu hiki. Vilevile tunawashukuru wale wote walioshiriki kwa njia moja au nyingine hadi kufanikisha kuchapishwa kwa kitabu hiki.

Mchapishaji:

Al-Itrah Foundation

S. L. P. 19701

Dar-es-Salaam, Tanzania.

UTANGULIZI

Ombwe la kielimu na kiitikadi linazidi kumsogeza mwanadamu mbali na utambuzi wa ukweli kuelekea kwenye dimbwi la upotovu. Leo tunashuhudia nguvu nyingi za ubunifu wa mwanadamu zikipotea bure pale anapofumbia macho ile bahari yenye utajiri na mawimbi ya utamaduni na fikra ambayo dini inaitengeneza na vile anavyoyaruhusu maisha yake ya kisomi kunyongwa na itikadi za dunia ya kisasa.

Leo, mawazo mbali mbali yanawasilishwa kwenye kizazi cha wakati wetu chenye kiu na ambacho kimechanganyikiwa, mawazo ambayo yanatokana na dhana potovu za juu juu za wanafalsafa na wanazuoni wenye peo finyu. Mawazo haya yanajifanya kujaribu kujibu mahitaji ya kizazi cha sasa, lakini hayapendekezi maana yoyote au lengo la maisha. Muundo wa mwelekeo mmoja wa fikira ambao ndio msingi wa mawazo haya sio malezi yanayofaa kwa ajili ya akili nyeti za zama zetu hizi, na wala haustahili hata kufikiriwa katika mazingira yoyote yale ambamo akili na busara bado vinakuwa na mshiko juu ya uhai.

Hapawezi kuwa na wasiwasi kwamba tofauti mbalimbali kubwa, ukatili, mateso na ghasia ambayo yanaweza kuonekana katika historia yote, yanatokana na ikhtilafu ambazo zinaitawala dunia yenyewe na maisha ya mwanadamu.

Tunaamini kwamba Uislamu na itikadi yake, iliyoegemea kwenye tawhiid, ikiwa na, kama ilivyo, mlolongo mpana wa chambuzi za kifalsafa na kisayansi za kina za dunia yenye madhumuni na uhalisia wa nje, na kumfahamisha mwanadamu juu ya mielekeo yote ya uhai wake, una uwezo wa kutatua kimsingi ikhtilafu zote na kutowiana kote na kummuongoza mwanadamu katika mwelekeo wa kitendo cha ubunifu kilichokubalika cha kumhakikishia mustakabali wake.

Kila mfumo wa imani, ingawa kanuni zake zinaweza kuwa zimeenea na misingi yake ikawa ya kudumu, inahitaji kuwasilishwa upya kwa kila kizazi kwa mujibu wa mazingira ya zama hizo. Wenye fikra na walezi wa kiroho, ambao wamezoena na ari ya wakati na wenye kuelewa haja ya utafiti zaidi katika shughuli za msingi ili kukabiliana na mageuzi yanayoletwa na falsafa na sayansi za kisasa, ni lazima kwa hiyo, watoe mazingatio ya uangalifu, makini na yenye upeo mpana juu ya maswali haya, wakichukua vyanzo vya Kiislamu. Ni lazima wawasilishe ukweli, kama mwelekeo mpana na endelevu wa Uislamu unavyotaka kwamba uwasilishwe, na kuizoesha dunia na kanuni za kimantiki za Uislamu.

Kitabu hiki cha sasa ni juhudi za kuwasilisha, kwa njia fupi na hai, uchunguzi wa misingi ya kiimani ya Uislamu, kwa kuchanganya mantiki ya kifalsafa kwa urahisi wa maneno. Kwa vile lengo letu limekuwa ni kuwasilisha kazi fupi kiasi, tumejizuia kutokana na kunukuu maoni ya wanafalsafa na wanasayansi mbalimbali kwa kirefu. Sehemu ya kwanza ya kazi yetu inashughulika na mada za tawhid na uadilifu. Tunategemea kwamba itakuwa ni mchango wa kufanya yajulikane maoni ya Uislamu juu ya maswali haya ya msingi. Sayyid Mujtaba Musavi Lari, Qum, Julai 15, 1981.

1

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

SOMO LAKWANZA

USTAWI WA IMANI KATIKA VIPINDI MBALIMBALI

Miongoni mwa mada za msingi za kielimu zinazohusu maisha ya binadamu, masuala ya kidini yanachukua umuhimu wa pekee. Kwa kweli, kila mara zimekuwa zinazingatiwa kama tatizo la msingi kwa ustawi na hatima ya mwanadamu na zimetengeneza utambuzi wa kina sana na ujuzi mkubwa. Wanachuo na watafiti wamefanya uchunguzi mpana sana kuhusu sababu za asili zilizomfanya binadamu ajihusishe na mambo ya Kidini, kufuatilia utafiti wao kwa mtazamo wa pekee na utaratibu ambao hutawala maamuzi na maoni yao.

Ukweli wa jambo hili ni kwamba tangu nyakati za kabla ya historia, itikadi na imani kila mara vimekuwa ndio sehemu ya mtindo wa jamii ya wanadamu; sio zamani au wakati huu ambapo inawezekana kukuta jamii ambayo ndani yake masuala ya kidini hayakulelewa. Qur'ani Tukufu imetaja kwenye Aya kadhaa kuhusu ukweli wa kihistoria kwamba Mitume waliotumwa toka mbinguni siku zote walijitokeza kwenye umma zilizopita ambako, pamoja na athari zao za kiroho zenye manufaa, vile vile walichukua nafasi muhimu katika kubuni ustaarabu wa kibinadamu.

Uchunguzi wa jinsi ambavyo maisha ya mwanadamu yameendelea taratibu na ujuzi kupanuka, pamoja na ujuzi uliotokana na upeo wa mbali sana wa historia, unaonyesha kwamba binadamu aliambatana na imani ya kidini kabla hajawa na utambuzi kamili wa mbinu za maamuzi ya busara. Kipindi cha kwanza cha ujuzi na utendaji wa mwanadamu, kwa hiyo, hakuchukui ubora juu ya vipindi vya mwanzoni kabisa vya dini na imani. Inawezekana hata kudaiwa kwamba jitihada za mwanadamu katika nyanja

za dini na imani zimeonyesha bidii kubwa sana na za kudumu zaidi kuliko juhudi zake katika eneo la ujuzi na sanaa, kwani elimu ya ukweli unaokuvuka mipaka ambao ndio kiini cha cha dunia ya uhai ni mgumu zaidi na inayopatikana kwa taabu kuliko kiini cha vitu vile ambavyo ujuzi na sanaa daima huhangaikia kuvipata. Hali halisi ya msingi ya jua lenye utukufu, ambalo ndio kitu dhahiri kuliko vitu vyote, ilibakia bila kujulikana kwa binadamu kwa karne nyingi na mwenendo na athari zake vilipewa tafsiri za kila aina; ingawa hapana mtu aliyeweza kukanusha kuhusu kung'ara kwa miale yake, akili za watu wengi zilibakia gizani kuhusu kujulikana kwake.

Kwa hiyo, utambuzi wa ukweli mkubwa hauwezekani bila uchunguzi wa kimantiki, maamuzi na kusoma kunakoeleweka. Endapo ushirikina na visa-asili (hekaya) vya kidini vinaweza kupatikana miongoni mwa watu wa kale, na muda wote vikiingizwa kwenye tabia mpya kwa sababu ya upungufu na udhaifu wa kifikira na mipaka finyu ya ujuzi, hii haimaanishi kwamba dini pamoja na kiwango chake cha nadharia, ni udanganyifu. Kwa usahihi zaidi, dini huonyesha ubora na uhuru wa matamanio ya Kidini katika vina vya nafsi na moyo wa mwanadamu. Zaidi ya hayo, kutoka kwenye sayansi ambayo inatafuta kuchunguza nyakati za kabla ya historia, hatuwezi kutegemea kwamba itagundua zaidi kuhusu dini za kale kuliko masalia ya hekaya na ushirikina unaoweza kufumbulika kwenye mabaki ya mtu wa kale na chini ya ardhi.

Kwa kuwa mwenendo wa binadamu na shughuli zake daima huambatana na sifa mbili zilizo wazi; ubora na uhuru, kwa upande moja, na ufahamikaji na ueneaji pote duniani miongoni mwa jamii ya spishi, kwa upande mwingine - kimantiki, moja kwa moja inaonyesha kwamba tunatakiwa tutoe namna ya chimbuko kwa ajili ya mwenendo na shughuli hiyo kutoka katika kina cha moyo wa mwanadamu. Kuwepo kwa jambo endelevu la aina hiyo kwenye hali ya umilele na kilimwengu, muda wote wa historia na kabla ya historia haliwezi kuchukuliwa kama athari za desturi na mazoea; ni udhihirashaji wa kiu ya dahari na silika ya lazima kwa ajili ya ukweli. Imani zote za kidini na vipengele na aina zao zinazotofautiana zinatoka kwenye chanzo kimoja kinachobubujika na chenye hazina kubwa - ni asili ya dahari ya mwanadamu, ambao haukulazimishwa kutoka nje wala haikuwa ajali.

Kwanza kunakuja kuwepo katika moyo wa binadamu, uwezo wa kukubali imani, na halafu imani yenyewe kuchukua muundo wake. Mwelekeo huo huo wa ndani unaomlazimisha mtu kufanya uchunguzi na utafiti wa kisomi ili aweze kufahamu ukweli ndio dalili ya binadamu kuhitaji elimu ya kidini. Hii, kwa kweli, haina maana kwamba hali ya ndani na maelekezo ni lazima yaambatane na imani sahihi na iliyoundwa kikamilifu. Kama vile ambavyo mwili unavyohitaji viini rutubishi bila ya tamaa hii, haionyeshi uzuri na ukamilifu wa chakula, roho nayo pia hutafuta chakula chake - yaani imani na itikadi - kwa msisitizo ikitafuta utambuzi wa Mola wake na kutamani kuomba kwenye lango lake. Lakini silika ambayo inailazimisha roho kutafuta haiwezi kutambua na kutathmini imani na kanuni za imani, kubainisha ukweli na uwongo.

Wanachuo wanakubaliana kwamba imani za kidini kila mara zimefungamanishwa na maisha ya binadamu. Hata hivyo, maoni yao yanatofautiana kuhusu viini vya misingi vya dini na mambo ambayo yameshika nafasi muhimu katika kuanzishwa na kuendelea kwake. Uamuzi wao katika jambo hili, kwa ujumla umetegemezwa kwenye uchunguzi wa dini za kishirikina na imani za kale, na matokeo yake ni kwamba, maamuzi yao, kwa uchambuzi wa mwisho, yanakuwa na mapungufu na bila mantiki. Ni kweli kwamba dini fulani, zisizofungamana na kanuni za ufunuo wa ki- Mwenyezi Mungu, zimeathiriwa katika muonekano na kukua kwao na mazingira ya kijamii na mambo mengine yanayofanana na hayo. Hata hivyo, haina mantiki kuhusisha misingi yote ya imani na mielekeo ya kidini na mazingira ya kinyenzo au hali ya kiuchumi na mahitaji, kwa hofu ya nguvu zinazoogofya za kiasili, kwa ujinga au kwa fikira zilikataliwa na sayansi.

Bila shaka, moja wapo ya mambo katika kujitokeza kwa mawazo ya kinyume na dini na kundi la watu wanaomkana Mwenyezi Mungu, ni mafundisho ya udanganyifu, upungufu na upotovu wa kiakili wa wafuasi wa baadhi ya dini. Upekee na tofauti za tabia za kila dini, kwa hiyo lazima zichambuliwe moja baada ya nyingine wakati wa kuchunguza sababu ambazo zimemfanya binadamu kuwa mfuasi wa dini hiyo.

Katika matukio mengi ya kihistoria, dini inaweza kuonekana kutawala mahusiano yote. Endapo dini ingekuwa si jambo la msingi, ingekuwa imefungika moja kwa moja kwenye dhamira za kimaada. Hata hivyo, ni jambo gani ambalo lingewapa watu wa dini uimara na ushupavu wa aina hiyo kwa ajili ya kukidhi malengo yao ya kidini? Je, ilikuwa ni kwa sababu ya mategemeo ya manufaa ya utajiri wa kidunia na manufaa mengine ya kibinafsi ambayo yalifanya matatizo machungu yaliyotokana na balaa na shida kuwa na ladha tamu katika nafsi zao? Kinyume chake, tunaona kwamba walitoa utajiri wao wote, maendeleo yao na utashi wa kibinafsi, kwenye hisia na maadili ya kidini, hadi kufika kiasi cha kujitolea nafsi zao kwa mapenzi makubwa.

Kwenye hadithi inayomhusu Firauni na wachawi wake, tunasoma kwamba aliwaita waganga wake wote wa mazingaombwe ili wamshinde Musa(a.s) yule mtu aliyesemeshwa na Mwenyezi Mungu, wakiwa na matumaini kwamba kwa werevu na uwezo wao wa kichawi, wangeweza kumlazimisha kusalimu amri. Lakini shukurani kwa uwezo wa kimiujiza aliopewa Musa, walishindwa na wakarejea kwenye imani ya kweli. Firauni mwenye hasira, ambaye kiburi chake kilivunjwa, akaanza kuwakashifu na kuwatishia, akiwaambia kwamba angewaadhibu kwa mateso mabaya kuzidi yote - yaani kuwakata miguu yao. Lakini, mageuzi ya kina sana yalikwisha kufanyika katika nyoyo zao; walibakia kuwa imara na madhubuti mbele ya vitisho na kurairai kwa Firauni na mateso yake makali. Wachawi hao wakajibu, kwa ushupavu sana;

فَاقْضِ مَا أَنتَ قَاضٍ إِنَّمَا تَقْضِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٧٢﴾

"....basi fanya unavyotaka kufanya, unaweza kutoa hukumu inayohusiana na maisha haya ya dunia tu." (Surat-Twaha; 20:72).

Hili lilikuwa ni onyesho la wazi la nguvu ya utashi wa asili wa kutaka kupata ukweli na uhalisi ndani ya binadamu anapokabiliwa na dhuluma uonevu na nguvu za kikatili. Watu ambao waliishi kati kati ya chombo cha Firauni na walikuwa wanafaidika nacho, walinyanyua vichwa vyao na kuasi na walikuwa tayari kujitoa mhanga. Mwelekeo maalum wa mtu kwenye masuala ya kidini, kwa hiyo hauwezi kuelezwa kwa kigezo cha tafsiri ya manufaa ya kidunia; kinyume chake matukio kama lile la wachawi huonyesha ubora wa maana za kidini kwa binadamu.

Imani zisizo na mantiki hazifungamani na masuala ya kidini tu. Kabla hazijasafishwa sawasawa, elimu nyingi zilikuwa zimechanganywa na ushirikina. Watu waliona njia yao kutoka kwenye upandisha mashetani na uchawi kwenda kwenye tiba za kweli na zenye manufaa na kutoka kwenye alkemi za uongo kuja kwenye kemia halisi. Hapana mtu anayeweza kudai kwamba endapo mtu alifanya kosa mara moja wakati wa kutafuta kitu, kwa hiyo, analazimika kubakia kwenye makosa wakati wote na kamwe hatapata njia ya kuufikia ukweli. Wale watu wanaoamini katika falsafa za kisayansi na ubora na mbinu ya majaribio, wanakubali kwamba majaribio yao yanaweza kuleta matokeo yasiyo sahihi ingawa kwa namna moja au nyingine watayapatia hadhi ya ukweli.

Watu wanaomkana Mwenyezi Mungu husisitiza uamuzi wa kwamba Mwenyezi Mungu ni matokeo ya fikira ya mwanadamu. Kwa mfano, mwanafalsafa Mwingereza, Betrand Russell, anauona woga wa nguvu za asili kutokea kuwa chanzo cha dini. "Kwa maoni yangu, dini zaidi ya yote imetokana na woga wa kisichojulikana, woga wa kifo, woga wa kushindwa, hofu ya mambo ya siri na yaliyofichikana. Kwa nyongeza, kama ambavyo imekwisha kuandikwa, hisia hujitokeza na kumwezesha kila mtu kudhani kwamba anaye msaidizi katika matatizo yake yote na jitihada zake."[1]

Haya ni madai tu, ambayo hayaungwi mkono na ushahidi wowote. Samuel King anasema, "Chanzo cha dini kimegubikwa na usirisiri. Miongoni mwa nadharia zisizo na idadi za wasomi kuhusu somo hili, baadhi huonekana zenye mantiki kuzidi zingine, lakini hata ile bora kuliko zote inakabiliwa na upinzani kutoka katika mta zamo wa uthibitisho wa kisayansi. Haziwezi kuvuka mipaka ya mazingira ya makisio ya kimantiki. Kwa hiyo, kupo kutokukubaiana kukubwa sana miongoni mwa wataalamu wa elimu ya jamii kuhusu chanzo cha dini."[2] Hata hivyo, tunaweza kujibu kwamba hata kama tunakubali chanzo na msingi wa hamasa ya imani ya binadamu juu ya kuwepo muumba imeonekana kuwa ni hofu, hii haithibitishi kwa vyovyote vile kwamba kuwepo kwa Mwenyezi Mungu ni mzaha mzaha usio na ukweli.

Endapo hofu ilimsukuma binadamu kutafuta kimbilio na kama katika kutafuta huko aligundua ukweli yakini, yaani Mwenyezi Mungu, je, kuna haja ya kufanya upinzani wowote dhidi ya hilo? Kama hofu ni sababu ya ugunduzi wa kitu fulani, hivi tunaweza kusema kwamba kitu hicho ni cha kubuni na si cha kweli kwa sababu woga ndio uliomsukuma binadamu kukitafuta kitu hicho? Kwa hakika haingekuwa na mantiki kushikilia, kwa mfano, kwamba elimu ya tiba haina ukweli kwa sababu binadamu ameitafuta na kuivumbua kwa sababu ya woga yaani hofu ya maradhi na kifo? Ukweli wa jambo hili ni Katika mambo yote na matukio ya maisha, kuamini Mungu Mmoja aliye na hekima ni hifadhi halisi na msaada madhubuti.

Hili ni jambo tofauti kabisa mbali na kama ndivyo au sivyo kwamba msukumo wa binadamu kutafuta kitu hiki ni woga wa mabadiliko ya maisha na kutafuta kimbilio au hapana. Mambo haya mawili yapo mbali mbali kabisa na lazima yachunguzwe kila moja kwa upande wake. Bila shaka katika hatua za zamani za maisha yake, binadamu kwa kweli alikuwa mateka wa hofu ya kufedhehesha na kuumiza alipokabiliwa na matukio ya kimaumbile ya kutisha kama vile mafuriko, matetemeko ya ardhi na maradhi. Jinamizi la hofu lilitupa kivuli chake chenye kisirani katika vipengele vyake vyote vya maisha yake na fikira zake, na katika mapambano yasiyoisha aliyoyaendesha dhidi ya udhaifu na hofu, alitafuta msaada ambapo angeweza kupata hifadhi kutoka kwenye mazingira yake ya kuogofya na kupata amani ya kina. Hatimaye, kwa bidii kali, alilishinda jinamizi la unyonge na hofuna akapata ushindi wa dhahiri.

Uchunguzi wa hatua tofauti tofauti kuhusu maisha ya binadamu wa kale, na ugunduzi wa ushahidi kwamba woga ulikuwepo katika fikira za binadamu, hauthibitishi kwamba woga na ujinga ndio tu mambo ya msingi yaliyomfanya binadamu aielekee dini. Dai la aina hii litakuwa ni matokeo ya kuona eneo moja tu la jambo hili. Uamuzi wa jumla unaweza tu kufanywa kutokana na utafiti na uchunguzi wa kihistoria ambapo utimilifu wa historia, pamoja na vipindi tofauti vyote katika maisha ya binadamu, umechunguzwa na kufanyiwa utafiti, si pembe moja ya kihistoria yake pana na yenye sura mbalimbali.

Hofu kutawala mambo ya binadamu na unyonge wao katika vipindi maalum na vyenye mipaka si lazima vifanywe kuwa msingi wa uamuzi wa jumla kuhusu vipindi vyote. Haitakuwa ni uamuzi wa haraka mno kusema kwamba fikira zote za kidini na hisia ya mwanadamu, mwelekeo wa kumwabudu Mwenyezi Mungu katika nyakati zote tangu zama za kale pamoja na huu wa sasa, zimesababishwa hivi hivi tu na hou, kwa kuogopa ghadhabu ya maumbile, ya vita na magonjwa? Kwa kweli hasa, wale ambao wameridhika kwa uthabiti hasa miongoni mwa watu kwa hali yoyote ile sio wale wanyonge mno. Wale ambao, jinsi wakati unavyopita, wamenyanyua juu bendera ya dini ni wale wenye nguvu sana na imara katika watu. Imani ya mtu kamwe haiongezeki kwa kuwiana na unyonge wake, na kiongozi wa watu katika mambo ya imani ya kidini si mtu wa mbele sana miongoni mwao katika udhaifu, unyonge na kuishiwa nguvu.

Je, Imani katika dini ya maelfu ya wanachuo na wanafikra ni matokeo ya woga wao juu ya dhoruba, matetemeko ya ardhi na magonjwa? Inawezekana mwelekeo wao kwenye dini, uchunguzi wa kisomi, wa mantiki na uthibitisho madhubuti, kudhaniwa kuwa ni kwa sababu ya ujinga wao na kutokutambua kwao sababu asilia za matikio? Ni lipi litakuwa jibu la mtu mwenye akili?

Zaidi ya hayo mtu kuingia kwenye dini si kwa sababu ya kupata amani ya aina fulani. Badala yake, mtu huanza kufurahia matunda mazuri ya dini - amani na utulivu, baada ya kupata imani na kusadikisha. Kwa maoni ya wanazuoni waliongozwa Ki-Mungu, dunia ni ufupisho kamili wa sababu na hoja zilizopangwa uzuri, mfumo sahihi wa ulimwengu unaoshuhudia kuwepo kwa chanzo kitambulikanacho kwa elimu na uwezo. Michirizi ya upakaji rangi usioeleweka na unaotatiza haiwezi kuchukuliwa kuwa dalili ya msanii stadi, lakini michirizi iliyo sahihi na ubunifu wenye maana huo ndio ushahidi wa hakika wa kuwepo kwa fundi rangi mwenye ujuzi.

Pia wapo watu wanaoiangalia imani katika ukweli ulioko nje ya mipaka ya asili kuwa kama matokeo ya mambo ya uchumi. Hufanya juhudi kubwa kuanzisha uhusiano fulani baina ya dini na uchumi. Wanadai kwamba wakati wote dini imekuwa katika huduma ya ubeberu na unyonyaji na kwamba ilikuwa uvumbuzi wa tabaka utawala na unyonyaji kama njia ya kuvunja upinzani wa umma unaonyonywa. Wanadai kwamba, dini imekuwa ikitumiwa kuwapumbaza wavuja jasho wasiojiweza na kuwahimiza waendelee kuridhia kutojiweza kwao. Hapana shaka kwamba, kama kwa kitu kingine chochote kile hapa duniani, dini inaweza kutumiwa vibaya. Inapobadilishwa kutoka kwenye malengo yake ya kweli, inakuwa ni silaha mikononi mwa wenye kufaidika ambao wanataka kuyaweka mataifa utumwani. Hata hivyo, huku kutumika vibaya kwa dini kusiwape wabinafsi kisingizio cha kushambulia kidhalimu kila kitu chenye jina la dini. Lazima pawepo na utenganisho uliowazi baina ya dini potovu zilizobuniwa na ubeberu kwa lengo la kuwapumbaza watu, na zile halisi za kweli na zenye kujenga.

Inawezekana kwamba katika jamii nyingi za binadamu, hali mbaya ya kiuchumi, kuvia na kukosa maendeleo vinaweza kuwepo sambamba na imani ya kidini. Lakini, kuwepo pamoja huku hakuwezi kulazimisha kuwepo uhusiano wa kawaida; mmoja hauwezi kuwasilishwa kama sababu ya mwingine. Wakati fulani tunaona jamii inafaidi maendeleo na ustawi kiuchumi ambao umeambatana kwa kina sana na dini, ambapo jamii nyingine ambayo inafaidi vivyo hivyo hali nzuri ya kiuchumi iko kinyume kabisa na dini. Vivyo hivyo, kwenye mazingira ya umasikini na kukosa maendeleo, nuru ya dini inaweza kutoweka ambapo kwenye mazingira mengine kama hayo, mvuto wa dini unaweza kuwa kwenye kilele chake. Kutokuwepo kwa ulingano wa wazi baina ya hali ya uchumi na kuwepo au kuanguka kwa mvuto wa kidini na uthibitisho uliowazi wa ukweli kwamba kutokea kwa wakati mmoja (kwa mambo mawili) hakutoshi kuanzisha uhusiano wa kawaida. Jambo fulani maalum lazima liwepo kusababisha kutokeza au kutoweka kwa mojawapo kuunganishwa na kuwepo au kutokuwepo kwa jingine.

Tunaweza kuona wazi kabisa huku kutokuwepo kwa ulingano katika jamii mbili ambazo zote zipo kwenye utawala dhalimu wa tabaka la wanyonyaji. Katika mojawapo ya hizo jamii mbili, dini imeondoka kabisa kwenye mazingira yake, ambapo kwenye jamii nyingine mvuto wake umepanuka. Uhalisi wa lengo unatuonyesha kwa hiyo kwamba, mtu anavutwa kwenye dini na mazingira mbalimbali ya nje. Popote pale ambapo dini inaonyesha mvuto wake, mtu lazima atafute dhamira ya msingi ya ndani kabisa katika hali asili hususia ya dini, sio katika mazingira ya uchumi. Kwa nyongeza, tunapoyachunguza yale malengo ya dini za ki-Mungu, tunafikia uamuzi kwamba mahitaji ya kuwepo kwa ustawi na kuanzishwa kwa mfumo wa uchumi wa haki ambao unaegemezwa kwenye dini yamekuwa mojawapo ya sababu za kutumwa Mitume. Hii, pia ni sababu mojawapo ambayo imewafanya watu wamevutiwa kwenye dini na ni moja wapo ya manufaa ambayo jamii ya binaadamu imepata kutoka humo.