MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE 0%

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE Mwandishi:
: SALMANI SHOU
Kundi: Misingi mikuu ya Dini

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

Mwandishi: KIMEANDIKWA NA SAYYID MUJTABAA MUUSAWIY LARI
: SALMANI SHOU
Kundi:

Matembeleo: 27530
Pakua: 2662

Maelezo zaidi:

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE
Tafuta ndani ya kitabu
  • Anza
  • Iliyopita
  • 28 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 27530 / Pakua: 2662
Kiwango Kiwango Kiwango
MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

Mwandishi:
Swahili

20

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

SOMO LA ISHIRINI

MIUNDO YA RIDHAA ZA MWENYEZI MUNGU NA HIARI

Majaaliwa na hatima ni mojawapo ya hizo mada zinazoelekea kuleta ubishi na ambazo mara nyingi zinatafsiriwa vibaya kwa sababu ya kukosa kuelewa kwa usahihi au, wakati mwingine, kwa nia mbaya. Ili tuweze kuigundua mada hii, tutaifanyia uchambuzi hapa kwa muhtasari kwa kadiri iwezekanavyo.

Kila kitu hapa duniani kimeegemezwa kwenye mpango uliokadiriwa kwa usahihi, mantiki na kanuni. Kimewekwa mahali pake kwa mujibu wa kipimo sahihi, na kinapata tabia zake bainifu kutoka kwenye vyanzo na vipengele kinavyovitegemea. Kama vile ambavyo kila kiumbe hupata uhai wake muhimu kutoka kwenye chanzo chake maalum, pia hupata sifa zake zote za nje na ndani kutoka kwenye chanzo hicho hicho; kinapata umbo lake na ukubwa kutoka kwenye chanzo hicho. Kwa kuwa kuna hali ya ulinganifu baina ya chanzo na athari, hicho chanzo bila kipingamizi hupitisha kwenye athari tabia zile yenye uhusiano na asili yake chenyewe.

Filosofia ya maisha ya Uislamu, majaaliwa na hatima, ni mambo yenye maana ya amri ya Mwenyezi Mungu kuhusu kudhihiri kwa mambo ya dunia, ukubwa na mipaka yao. Matukio yote ambayo hutokea kwenye utaratibu wa maumbile, pamoja na matendo ya mwanadamu, yanakuwa yamepangwa na kuwa ya uhakika kwa njia ya vyanzo vyao; kuwa kwao ni matokeo ya uhalali ulimwenguni kote wa kanuni ya usababisho. Majaaliwa (qada') ina maana ya kitu kilichofikishwa mwisho wake na kisichogeuzika, na marejeo yake ni kwenye ubunifu na matendo ya Mwenyezi Mungu. Hatima (qadar) ina maana ya ukubwa au uwiano na inaashiria asili na sifa ya utaratibu wa maumbile, mwenendo wake wenye utaratibu; maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu ameupatia ulimwengu wa viumbe muundo uliopangwa wenye utaratibu. Kwa maneno mengine, hatima ni matokeo ya usanifu Wake kama inavyoacha athari zake kwenye vitu vyote vilivyoumbwa.

Kwa kuelezea kwa namna tofauti, maana ya hatima ni uwekaji mipaka na uwiano wa nje na ya busara ya kitu sio kiakili. Kabla hajatekeleza mpango wake, msanifu majengo atatayarisha kichwani mwake ubora na vipimo vya jengo analotaka kujenga. Qur'ani inasema kuhusu miundo hii iliyopangwa, tabia na uwiano wa vitu kama Qadar:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾

"Kwa hakika sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo." (54:49),

قَدْ جَعَلَ اللَّـهُ لِكُلِّ شَيْءٍ قَدْرًا ﴿٣﴾

"Mwenyezi Mungu amekijaalia kila kitu na kipimo chake." (65:3).

Neno, majaaliwa (qadar) kwenye Qur'ani maana yake ni mahitaji yenye uwiano na ya kawaida, sehemu zote za chanzo zinazoelekeza katika kutokeza kitu. Inamaanisha kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu utajitekeleza wenyewe pale tu ambapo kadiri, mazingira na vyanzo vya kitu vinafungamanishwa na kila kimoja chao.

Mwenyezi Mwenyezi Mungu anazingatia hali ya nafasi na muda ya matukio yote, pamoja na mipaka na uwiano wao, na halafu hutoa hukumu Yake katika misingi ya hayo. Jambo lolote lile au chanzo chochote kile kinachoonekana hapa duniani ni udhihirisho wa utashi wa Mwenyezi Mungu na ujuzi na chombo cha kutimiza kile alichokijaalia.

Uwezo wa ukuaji na maendeleo umekadiriwa kwenye kiini chenyewe hasa cha kila kitu. Mata, ambayo hutegemea sheria ya msogeo, ina uwezo wa kujitwalia maumbo tofauti na kupita kwenye taratibu tofauti nyingi. Chini ya athari ya mambo tofauti, hujitwalia jamii nzima ya hali na sifa tofauti. Hupata nishati kutoka kwenye vipengele fulani asilia ambayo huiwezesha kusonga mbele, lakini inapokutana na vipengele vingine fulani, hupoteza uhai wake na kutoweka kabisa. Wakati mwingine huendelea kusonga mbele kupitia hatua tofauti hadi inapokaribia kwenye kiwango cha juu zaidi cha maendeleo; wakati mwingine, inakosa ile kasi muhimu ya kuendelea kwenye hatua zingine zaidi za maendeleo na kusonga kwa kujikongoja. Kwa hiyo, matokeo ya mambo hayakuunganishwa moja kwa moja na majaaliwa na hatima kwa sababu chanzo ndio kinacho bainisha namna ya athari. Kwa kuwa vitu vinauhusiano na aina mbali mbali za vyanzo, ni lazima kwamba vitafuata njia mbalimbali; kila chanzo hukiweka kile kiumbe kilicho chini yake kwenye njia maalum.

Fikiria mtu anasumbuliwa na maradhi ya kidole tumbo. Hii ni 'hatima' itokanayo na chanzo maalum. 'Hatima' zingine tofauti mbili za ziada zinamngojea mgonjwa huyu; ama anakubali kufanyiwa upasuaji, ambapo matokeo yanayo tarajiwa ni kupona, au akatae kufanyiwa upasuaji ambapo matokeo yake ni kifo. Chaguzi zote hizi mbili zinawakilisha aina ya hatima.

Hatima zinaweza kubadilishana lakini uamuzi wowote utakaochukuliwa na mgonjwa na kuzitekeleza hautakuwa nje ya upeo ambao Mwenyezi Mungu ameujaalia. Mtu hawezi akakaa na kukunja mikono na kujiambia mwenyewe; 'kama haya ndio majaaliwa yangu, nitabakia hai, na kama sio majaaliwa yangu, nitakufa, hata kwa juhudi ya kiasi chochote nitakazofanya ili kutibiwa.' Kama ukitafuta tiba na ukapona, huu ndio mustakabali wako, na kama unakataa tiba na unakufa, pia huo, ndio mwisho wako. Popote uendako na lolote ufanyalo, upo katika kuzungukwa na hatima. Watu ambao ni wavivu na hukataa kufanya kazi, kwanza huamua kutokufanya kazi na halafu wanapokosa fedha, wanatupia lawama zote kwenye majaaliwa. Endapo wangekuwa wameamua kufanya kazi, fedha walizopata zingekuwa sawa na matokeo ya majaaliwa. Hivyo basi, hata kama wewe ni mtu mwenye bidii na jitihada au mvivu, kwa jinsi yoyote ile hujavunja kanuni ya majaaliwa.

Mabadiliko katika hatima, hayana maana ya kipengele fulani kuasi dhidi ya majaaliwa au upinzani dhidi ya kanuni ya usababisho. Hakuna jambo linalosababisha athari hapa duniani ambalo linaweza kusamehewa kuepukana na kanuni ya usababisho ya kilimwengu. Kitu kinachosababisha mabadiliko kwenye hatima, chenyewe ni kiunganishi katika mlolongo wa usababisho, udhihirishao mmoja wa majaaliwa na hatima. Kusema kwa namna nyingine tofauti, hatima moja hubadilishwa kwa njia ya hatima nyingine.

Tofauti na elimu ambazo huelekea upande mmoja tu na kutoa mwelekeo fulani tu wa vipengele vya matukio, sheria za metafizikia hazihusiki na matukio katika mtizamo wa muungano wa matukio ingawa sheria hurekebisha matukio, hayajali uhusiano wa mwelekeo yanaouchukua. Kwa kweli, matukio yenyewe na mwelekeo wao yanategemea sheria pana na nyingi za metafizikia: mwelekeo wowote ule matukio yatayochukua, bado yapo kwenye mjumuiko wa sheria ambamo haviwezi kuepuka. Hali ni kama ile ya uwanda mpana na mkubwa sana; hata zile sehemu zake za upeo wa kaskazini na kusini zimejumuishwa kwenye uwanda huu.

Kwa ufupi, majaaliwa na hatima haziwakilishi chochote zaidi ya ueneaji wa kanuni ya usababisho ulimwenguni kote, huwakilisha ukweli wa metafizikia ambao haupimiki kama takwimu za sayansi. Kanuni ya usababisho husema tu kwamba kila tukio lina chanzo chake, yenyewe haiwezi kufanya utabiri, hii ikiwa ni tabia ambayo haipo kabisa kwenye utambuzi wa kimetafizikia. Kwa sheria za metafizikia, ambao ni muundo wa ujuzi unaojieleza na msingi madhubuti na imara kwa ajili ya matukio mbali mbali ya dunia, hautofautishi ni tukio gani mahsusi linatokea. Hii ni njia kuu ambayo wanadamu hupita katika safari yao kwa sababu umadhubuti na uimara wake haujali kabisa ni upande gani wanakoelekea.

Amirul-Mu'minin Ali(a.s) , alikuwa anapumzika kwenye kivuli cha ukuta uliovunjika ambao ulielekea kuanguka. Ghafla alinyanyuka na akaenda kuketi kwenye kivuli cha ukuta mwingine. Aliulizwa: "Unakimbia lile ambalo Mwenyezi Mungu amelikadiria?" Alisema, "Ninakimbilia kwenye hifadhi ya Mwenyezi Mungu kutokana na lile ambalo Amelikadiria," akimaanisha, "Ninakimbia kutoka kwenye jaala moja na kwenda kwenye jaala jingine. Vitendo vyote viwili kuketi na kunyanyuka vilikuwa vipo kwenye majaaliwa sawa. Endapo ukuta uliokatika ukiniangukia na nikaumia, hayo yatakuwa majaaliwa na hatima, na kama nikiondoka kutoka kwenye eneo la hatari na kuepuka madhara yote, hayo pia ni majaaliwa na hatima."

Qur'ani Tukufu imeeleza kama kanuni, mifumo na sheria za asili ambazo hutawala juu ya dunia na kufuata njia zisizobadilika na zisizoepukika:

وَلَن تَجِدَ لِسُنَّةِ اللَّـهِ تَبْدِيلًا ﴿٦٢﴾

"..........wala hutapata mabadiliko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu." (33:62).

Kanuni ya hukmu ya Mwenyezi Mungu isiyoepukika, miongoni mwa mambo mengine, inahukumu kwamba:

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ﴿٥٥﴾

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakafanya matendo mema, bila shaka atawafanya makhalifa katika ardhi....." (24:55).

Kwa mujibu wa Qur'ani, hii pia ni kanuni ya Mwenyezi Mungu isiyoepukika:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ... ﴿١١﴾

".....Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili yaliyomo katika nafsi zao....." (13:11).

Kwa mtazamo wa kidini wa falsafa ya maisha, ukweli haukuwekewa mipaka kwenye eneo la usababishaji wa vitu. Matukio hayatakiwi kufikiriwa katika uhusiano wa utambuzi wa hisia tu na ukubwa wa mambo. Vipengele, visivyo vya kimaada vinaweza kufika kwenye nyanja ambazo vipengele vya maada vimefungiwa kabisa, na vina wajibu huru na wenye maamuzi katika kutokea kwa matukio.

Kwa hali yoyote ile dunia haijiingizi katika utofautishaji baina ya wema na uovu; matendo ya mtu hutoa athari fulani wakati wa maisha yake. Wema na ukarimu kwa wenzake wengine na upendo na huduma kwa viumbe vya Mwenyezi Mungu ni mambo ambayo kupitia njia zisizokuwa za kimaada, hatimaye husababisha mabadiliko ya hatima ya binadamu na huchangia kuwepo kwa utulivu furaha, na neema nyingi. Ukandamizaji, unyang'anyi, ubinafsi, uvamizi pia huzaa matokeo machungu na matokeo yake lazima yawe mabaya. Kwa hiyo, kwa mtazamo huu, aina fulani ya kulipa kisasi ni asili katika maumbile, kwani dunia ina utambuzi na ufahamu, inaona na kusikia. Namna ambayo hulipa matendo ni mojawapo ya udhihirisho wa majaaliwa na hatima, haiwezekani kulikimbia hilo, kwani popote utakapokwenda litakukamata.

Mtaalamu mmoja wa sayansi anasema: "Usiseme dunia haina utambuzi, kwani utakuwa umejishutumu mwenyewe kwa kukosa utambuzi. Wewe umekuja kuwepo kama sehemu ya dunia, na endapo hakuna utambuzi duniani pia wewe huna utambuzi." Kuhusu wajibu wa mambo yasiyo ya kimaada katika kuunda hatima. Qur'ani inasema yafuatayo:

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِن كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٦﴾

"Na kama watu wa miji wangeamini na kuwa wacha-mungu, lazima tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi, lakini walikadhibisha, tutawaangamiza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma."(7:96)

وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَىٰ حَتَّىٰ يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولًا يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَىٰ إِلَّا وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ ﴿٥٩﴾

"Na Mola wako haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika mji wao mkuu, awasomee Aya zetu: Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe wamekuwa madhalimu." (28:59).

Dhana za majaaliwa na hatima zinatolewa na watetezi wa kadari kama mojawapo ya uthibitisho wao. Kwa maoni yao, haiwezekani kwa tendo lolote kufanywa na mtu yeyote kwa uhuru, kwani Mwenyezi Mungu amekwisha yakadiria matendo ya mtu, ya jumla na ya hususia, mabaya na mema, hivyo kwamba hakuna nafasi inayobakia kwa ajili ya matendo ya hiari upande wake.

Kuna tofauti baina ya kadari na hatima isiyobadilika. Kila tukio litaelekea kutokea pindi sababu zake zote zitakapokuwepo. Kiunganishi kimoja katika mlolongo wa sababu hizo ni hiari ya mtu, ambayo ina nafasi ya wazi ya kipekee. Mwanadamu kiumbe ambaye amepewa hiari, kwa hiyo, matendo yake kufuatilia malengo yaliyo wazi, na katika kufuatilia malengo hayo, hafuati sheria fulani za asili zinazojiendesha zenyewe, kama ilivyo kwa matone ya mvua ambayo huanguka kwa mujibu wa kanuni ya nguvu ya uvutano. Kama ingekuwa vinginevyo, mwanadamu asingeweza, kwa kweli, kufuatilia malengo aliyonayo akilini mwake kama kiumbe chenye hiari.

Hii ni kinyume na fikra ya takdiri, ambayo inaiona hiari ya mtu kama isiyotumika na inahusisha sababu zote kwa Mwenyezi Mungu na mambo yaliyoko nje ya asili yake. Imani katika majaaliwa na hatima huishia kwenye takdiri hapo tu ambapo inapochukuliwa kuwa badala ya uwezo na hiari ya mtu, hivyo kwamba hakuna wajibu au athari inayohusishwa na matakwa yake katika matendo ayafanyayo. Kwa uhalisi, hata hivyo majaaliwa na hatima si vinginevyo isipokuwa ni mfumo wa asili na athari. Qur'ani inasema kwamba baadhi ya wale waliowapinga Mitume na wakanyanyua bendera ya uasi dhidi ya wateule wa Mungu wametafsiri majaaliwa na hatima katika namna ya takdiru. Hawakutaka hali iliopo ibadilike kwa namna ambayo utaratibu wa kijamii wa imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja ingeshika nafasi ya desturi zilizooza ambazo waliambatana nazo.

Hizi ndiyo Aya zinazostahili:

وَقَالُوا لَوْ شَاءَ الرَّحْمَـٰنُ مَا عَبَدْنَاهُم مَّا لَهُم بِذَٰلِكَ مِنْ عِلْمٍ إِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿٢٠﴾ أَمْ آتَيْنَاهُمْ كِتَابًا مِّن قَبْلِهِ فَهُم بِهِ مُسْتَمْسِكُونَ ﴿٢١﴾

"Nao husema: Angelipenda Mwingi wa rehema tusingewaabudu sisi. Hawana ujuzi wowote wa hayo! Hawana ila kusema uwongo tu! Kwani tuliwapa Kitabu kabla ya hiki, na ikawa wao wanakishikilia hicho?" (43:20-21).

Kinyume na wafuasi wa makaadiru, wajumbe wa Mwenyezi Mungu na wafuasi wa mafundisho ya matakatifu hawakuhusika na kulinda hali kama ilivyokuwa lakini wao walihusika na kubadilisha desturi na kuangalia hali ya siku za baadaye.

Qur'ani Tukufu inaahidi jamii ya wanadamu mwisho wenye ushindi katika mapambano yake dhidi ya madikteta na inasisitiza kwamba serikali ya mwisho kutawala hapa duniani itakuwa ni serikali ya haki; upotofu utatoweka na matokeo ya mwisho ya mambo yote yatakuwa mikononi mwa wale wanaomuogopa Mwenyezi Mungu. Hii ndio ahadi ya Qur'ani:

وَنُرِيدُ أَن نَّمُنَّ عَلَى الَّذِينَ اسْتُضْعِفُوا فِي الْأَرْضِ وَنَجْعَلَهُمْ أَئِمَّةً وَنَجْعَلَهُمُ الْوَارِثِينَ ﴿٥﴾

"Na tukataka kuwafadhili wale waliodhoofishwa katika ardhi na kuwafanya viongozi na wawe warithi."(28:5),

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾

"Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya makhalifa wale wa kabla yao, na kwa yakini atawasimamishia Dini yao aliyowapendelea, na atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na watakaokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.

(24:55),

وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذِينَ كَانُوا يُسْتَضْعَفُونَ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ الْحُسْنَىٰ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ بِمَا صَبَرُوا وَدَمَّرْنَا مَا كَانَ يَصْنَعُ فِرْعَوْنُ وَقَوْمُهُ وَمَا كَانُوا يَعْرِشُونَ ﴿١٣٧﴾

"Na tukawarithisha watu waliokuwa wanadharauliwa mashariki na magharibi mwa ardhi tuliyoibariki. Na likatimia neon jema la Mola wako juu ya wana wa Israili, kwa vile walivyosubiri. Na tukayaangamiza aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake, na waliyokuwa wakiyajenga." (7:137).

Kwa hiyo Qur'ani inaoyesha upinzani kati ya imani na kutoamini, kati ya walionyang'anywa na madikteta, na inatuambia kwamba dunia inaelekea kwenye ushindi wa ukweli dhidi ya batili, wa walioonewa dhidi ya wakandamizaji, vuguvugu la kimapinduzi liko mbioni ambalo linayoendana na msogeo wa maumbile yote kuelekea kwenye ukamilifu.

Wito wa Mitume, thawabu na adhabu, pepo na moto wa jahanamu - yote haya yanathibitisha kwamba mwanadamu anazo kazi na wajibu, na kwa sababu hiyo Qur'ani inaunganisha ukombozi wa mwanadamu hapa duniani na baada ya hapa duniani kwenye matendo yake. Kwa mujibu wa kanuni ya majaaliwa na hatima, mtu yu huru na anawajibika kwa hatima yake na anaidhibiti. Majaaliwa na hatima kwa kweli hufanya kazi endapo watu fulani wanao uwezo na wengine wanyonge na dhaifu, kama jamii moja ina ushindi na inajivuna, na nyingine, imeshindwa na ni dhaifu. Hii ni kwa sababu tu kwamba majaaliwa na hatima huamua kwamba watu fulani hutumia uwezo wa kusonga mbele na kuendelea na kutembea kwenye njia ya heshima na hadhi, ambapo kundi lingine huchagua kujinyima na kutojali, na haliwezi kutegemea lolote isipokuwa kushindwa, fedheha na unyonge.

Qur'ani inasema wazi:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٥٣﴾

"Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizowaneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao......"(8:53).

Bila shaka inaweza kutokea kwamba matakwa yetu hayatimizwi kama tunavyotegemea, lakini hii kwa hali yoyote haithibitisha kwamba mwanadamu analazimika na kukadiriwa katika vitendo vyake. Ukweli kwamba nafasi ya matendo ya hiari ya mwanadamu imewekewa mipaka kwa namna yoyote ile haipingani na kuwa kwake na hiari kuliko wazi; kukubali kwamba mwanadamu anayo hiari kwa namna yoyote ile kunamaanisha kwamba hiari yake haina mipaka. Mwenyezi Mungu ameweka mambo mengi sana ili yafanye kazi kwenye uwazi mpana wa maumbile. Wakati mwingine mambo haya, pamoja na matukio ambamo hutokea, yanadhihirika kwa binadamu na wakati mwingine hayaonekani. Tafsiri ya uangalifu ya fikra ya majaaliwa na hatima itamhamasisha mwanadamu kujitahidi zaidi kujua na kutambua mambo yote hayo, ili kwamba kwa kuyazingatia, anaweza bado kutumainia mafanikio makubwa zaidi. Kwa kwa sababu hasa ya ufinyu wa uwezo wa binadamu kwamba hawezi kupata mambo yote yanayohitajika kwa ajili ya kufuzu ili kwamba matamanio yake, matakwa yake yanabakia hayajatimizwa.

Kwa mujibu wa kanuni ya jumla ya usababisho, hatima ya kila kiumbe imefungamana na vyanzo vinavyo kitangulia. Kama mtu atakubali kuwepo kwa kanuni ya ki-Mungu au hapana hana mwelekeo kwenye suala la uhuru na hatima ya binadamu, kwa sababu mtu anaweza ama kuhusisha mfumo wa chanzo na athari kwenye utashi wa Mwenyezi Mungu, au adhani kwamba inajitegemea na haina uhusiano na kanuni ya ki-Mungu. Hali ikiwa ni hivyo, pia haiwezi kufikiriwa kwamba majaala yanatokana na kuamini katika misinngi ya majaaliwa na hatima. Tunachomaanisha kwa majaaliwa ni kiunganishi kisichoachanishwa cha kila kiumbe na vyanzo vyake, pamoja na hiari na chaguo la mtu; kwa hakika hatukanushi usababisho.

Majaaliwa na hatima husababisha kuwepo kwa kila tukio kwa njia ya chanzo chake maalum. Utashi wa Mwenyezi Mungu hutawala pote duniani kama kanuni na sheria ya ulimwengu. Badiliko lolote linalofanyika pia ni katika msingi wa utaratibu au kanuni ya ki-Mungu. Kama mambo yasingekuwa hivyo, majaaliwa na hatima yasingekuwa na mwonekano wa nje kamwe. Taasisi yoyote ya fikra ya kisayansi inayokubali kanuni ya usababisho wa kijumla inalazimika kukubali ukweli wa uhusiano baina ya matukio na chanzo chake, ikiwa imma ni ya imani ya kuwepo kwa Mwenyezi Mungu au ya kiyakinifu katika matarajio yake.

Sasa, kama kiungo dhahiri kati ya kutokea kwa jambo - pamoja na matendo ya wanadamu - na sababu zake zinaelekezea kwa mwanadamu kuwa ni roboti, aliyekwishakadiriwa katika matendo yake, yote ya imani ya Mungu mmoja na ya kiyakinifu yako wazi kwa pingamizi, kwa kadiri yote yanavyokubali usababisho. Lakini kama hakielekezi kwenye mwisho huo (kama ambavyo kwa kweli kisingefanya hivyo), swali bado linajitokeza: ni tofauti gani, katika hali hii, kati ya uabudu Mungu mmoja na uyakinifu?

Tofauti ni kwamba mtazamo wa dunia wa kiimani ya Mungu mmoja ukilinganishwa na ule wa uyakinifu, unachukulia mambo ya kidhanifu na yasiyokuwa ya maada kuwa yanaweza kusababisha athari. mambo hayo kwa kweli ni yenye kutatiza sana na magumu katika utando wa maumbile kuliko yalivyo mambo ya kimaada. Falsafa ya maisha yenye msingi juu ya imani kwa Mwenyezi Mungu inatia moyo, lengo na maana kwenye maisha. Humpatia mwanadamu ujasiri, uimara, upana wa mawazo, kuzama katika umaizi na ushupavu wa akili; humzuia asiangukie kwenye lindi kuu la kutokuwa na lengo; na humchukua juu kwenye tao lisilo na ukomo wa kwenda juu.

Kwa hiyo, mtu anayemwamini Mwenyezi Mungu ambaye anasadiki kikamilifu kuhusu majaaliwa na hatima, ambaye anatambua kwamba kuna makusudio ya busara yanayofanya kazi kwenye uumbaji wa binadamu na ulimwengu, ataelekea kwenye njia iliyonyooka kupitia kumtegemea kwake Mwenyezi Mungu; akijijua mwenyewe kwamba anasaidiwa na kulindwa na Mwenyezi Mungu, atakuwa mwenye kujiamini zaidi na mwenye matumaini ya matokeo ya shughuli yake.

Lakini mtu ambaye amenasa kwenye falsafa ya maisha ya uyakinifu, ambaye mfumo wa akili yake humwelekeza kuamini katika majaaliwa ya kimaada na hatima, hapati yoyote kati ya manufaa haya. Anakosa msaada wa uhakika na usioshindika katika kujitahidi kufanikisha malengo yake. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba kuna tofauti kubwa kati ya mifumo miwili ya fikra kwa kiasi ambacho athari zao za kijamii na kisaikolojia zinavyohusika. Anatole France anasema: "Ni athari ya manufaa ya kidini ambayo humfundisha mwanadamu sababu ya kuwepo kwake na matokeo ya matendo yake. Mara tunapozikataa kanuni za falsafa za kiimani ya Mungu mmoja, kama wafanyavyo sasa karibu watu wote katika kipindi hiki cha sayansi na uhuru, hatuna tena njia ya kujua kwa nini tumekuja hapa duniani na nini tunatakiwa kufanikisha baada ya kukanyaga dunia hii.

"Mwujiza wa hatima umetukumbatia kwa siri zake zenye uwezo mkubwa, na kama tunataka kuepuka kabisa kukutana na kusikitisha kwa utata wa maisha, lazima tusifikiri kabisa.

Kwani mzizi wa huzuni zetu upo kwenye ujinga wa kutokujua kwetu sababu ya kuwepo kwetu. Maumivu ya kimwili na kiroho, mateso ya roho na akili - yote yangeweza kuvumilika endapo tungetambua sababu yao na kuamini kwamba Mwenyezi Mungu ameyaridhia. "Muumini wa kweli hufurahia mateso ya kiroho anayoyavumilia. Hata dhambi anazofanya hazimnyang'anyi matumaini. Lakini kwenye dunia ambamo mwale wa imani umezimwa, maumivu na ugonjwa hupoteza maana na huwa utani mbaya, aina ya dhihaka ya kisirani."

21

MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

SOMO LA ISHIRINI NA MOJA

TAFSIRI ISIOFAA YA MAJAALIWA NA HATIMA

Baadhi ya wasomi bandia wanazo fikra potofu kuhusu majaaliwa na hatima na hudhani kwamba msingi huu husababisha kuvia na kutojishughulisha, humzuia binadamu na juhudi za aina yoyote za kuboresha maisha yake. Chanzo cha fikra hii katika nchi za Magharibi ni kutokuelewa vya kutosha kuhusu dhana hii, hususan kama inavyofafanuliwa katika mafundisho ya Kiislamu. Huko nchi za Mashariki fikra hii imepata athari kwa sababu ya kufifia na kurudi nyuma kimaendeleo.

Inajulikana vya kutosha kwamba wakati wowote watu au jamii za kihistoria zinaposhindwa kufikia malengo na mawazo yao, kwa sababu yoyote ile, hujifariji kwa maneno kama vvile 'bahati' 'ajali', 'hatima', 'majaaliwa'. Mtume mtukufu kabisa(s.a.w.w) alijieleza kwa ufasaha sana kuhusu jambo hili: "Wakati utakuja kwa watu wa umma wangu ambapo watafanya dhambi na dhuluma, na ili waweze kuhalalisha uovu na uchafu wao, watasema: 'majaaliwa na hatima yametuamulia kwamba tufanye hivi.' Ukikutana na watu kama hao, waambie mimi siwatambui, ninawakana hao."

Kuamini majaaliwa na hatima haimzuii mtu kufanya jitihada kufikia malengo yake katika maisha yake. Kama wale wenye ujuzi muhimuwa kidini wanavyotambua, Uislamu unawataka wanadamu kujitahidi sana katika kuboresha maisha yao, kimaadili na kimali. Peke yake hiki ni kipengele madhubuti katika kuongeza juhudi anayofanya mwanadamu. Mmoja wa mabingwa wa nchi za Magharibi ambaye anao uelewa mfinyu wa majaaliwa na hatima ni Jean- Paul Sartre. Anadhani haiwezekani kwa wakati moja kuamini majaaliwa na hatima chini ya uamuzi wa Mwenyezi Mungu na katika uhuru wa binadamu, na kwa hiyo, ni muhimu ama kuchagua kumwanini Mwenyezi Mungu au hiari ya mwanadamu: "Kwa sababu mimi ninaamini katika uhuru, siwezi kumwamini Mwenyezi Mungu, kwa sababu endapo ninamwamini Mwenyezi Mungu, lazima nikubali dhana ya majaaliwa, na kama nikikubali majaaliwa, nitalazimika kukana uhuru.

Kwa kuwa mimi ninaambatana na uhuru, simwamini Mwenyezi Mungu." Hata hivyo, hakuna ukinzani kati ya kuamini majaaliwa kwa upande moja, na uhuru wa mtu, kwa upande mwingine. Wakati inapochukulia utashi wa Mwenyezi Mungu kuwa wa kila mahali kiuwezo, Qur'ani Tukufu pia inahusisha wajibu huru na hai kwa binadamu, ikimwelezea kama mwenye uwezo kutengeneza hatima yake mwenyewe akiwa na utambuzi wa wema na uovu, ubaya na uzuri, na uwezo wa kuchagua kati ya hayo:

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا ﴿٣﴾

"Hakika sisi tumemuongoza njia, imma awe ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru." (76:3),

وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾

"Na aliyeitaka Akhera na akaifanyia juhudi, ile inayopasa, naye ni mwenye kuamini, basi hao ndio juhudi zao zitakubaliwa." (17:19).

Wale ambao mnamo siku hiyo ya Hukumu wataitafuta hifadhi kwenye uamini majaaliwa na kusema:

لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ ﴿٣٥﴾

"Mwenyezi Mungu angetaka tusingeliabudu chochote badala yake....." (16:35).

Wanashutumiwa kwa kuhusisha utendaji dhambi wao na upotovu kwenye utashi wa Mwenyezi Mungu na majaaliwa.

Hakuna hata ndani ya Aya moja kwenye Qur'ani ambamo ufisadi na matendo maovu ya mtu au jamii yamehusishwa kwenye majaaliwa na hatima. Hivyo, majaaliwa na hatima ni mambo ambayo hayakuonyeshwa kama vikwazo kwa jamiii fisadi na ya kiuovu inayojirekebisha. Hakuna hata Aya moja inayoweza kupatikana ambayo kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu umeshika nafasi ya hiari ya binadamu au ambamo inasemekana kwamba mtu alianza kuteseka kwa sababu ya majaaliwa na hatima.

Qur'ani imetamka kwa kurudia rudia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ambayo itawakumba madikteta na mafisadi, kwa kuleta adhabu kali baada yake. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye mapenzi na huruma sana kwa waja wake, akiwa ametoa neema zisizohesabika juu yao na wakati huo huo ni mpole na yu tayari kukubali toba, wakati wote Ameacha wazi njia kwa mwenye dhambi anayetaka kurudi kwenye utakaso na unyofu. Kukubali toba kwa Mwenyezi Mungu, kwenyewe peke yake ni mfano mkubwa sana wa huruma Yake.

Ingawa upeo wa hiari ya binadamu ni mkubwa na mpana zaidi kuliko ule wa viumbe hai vingine vijulikanavyo na huchukua nafasi kubwa sana ya ubunifu zaidi, hiari yake ina athari kwenye maeneo yale tu ambayo yamewekewa mipaka na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya shughuli na matendo yake. Kwa hiyo, binadamu hawezi kutimiza kila kitu anachotaka katika maisha yake. Mara nyingi hutokea kwamba mtu huamua kufanya jambo lakini kila atakavyojitahidi, anakuwa hawezi kulitimiza. Sababu yake hili sio kwamba utashi wa Mwenyezi Mungu unajipinga wenyewe kuhusu hiari ya mwanadamu na kumzuia kufanya atakavyo. Ni kwamba hasa katika masuala kama hayo, vipengele vya nje visivyojulikana vilivyopo nje ya upeo wa ujuzi na udhibiti wa binadamu huzusha vikwazo kwenye njia yake na kumzuia kufanikisha malengo yake.

Watu binafsi na jamii wakati wote hukabiliana na vikwazo vya aina hii. Kuzingatia ukweli kwamba katika uwanja wa maumbile hakuna chanzo bila athari na hakuna athari bila chanzo, na kwamba uwezo wetu wa kutambua umewekewa mipaka katika dunia hii na kwenye milki ya binadamu, isiwe vigumu sisi kukubali kwamba matumaini yetu yanaweza yasitimie kama tunavyotaka.

Mwenyezi Mungu ameweka mabilioni ya vipengele katika utaratibu wa uhai. Wakati mwingine vipengele hivyo vipo dhahiri kwa mwanadamu, wakati mwingine havijulikani kwa binadamu na haviwezi kushirikishwa katika kufikiri kwake. Hali hii pia ina uhusiano na majaaliwa na hatima lakini sio tu kwamba haishii katika kumnyima mwanadamu hiari au kumzuia kujaribu kupata hali ya kujitosheleza katika maisha; pia humwongoza kifikra na kishughuli na humjaza ndani kabisa ya nafsi yake na matumaini makubwa. Binadamu hutafuta kuongeza ujuzi wake na utambulisho wake, kwa usahihi kadiri iwezekanavyo, mambo ambayo humnyooshea njia ya kupata mafanikio makubwa zaidi katika maisha. Imani ya majaaliwa na hatima kwa hiyo ni mambo yenye nguvu katika kumwendeleza binadamu kuelekea kwenye malengo yake na ubora wake.

Suala la ukombozi au kulaaniwa kwa mwanadamu limetafutiwa ufumbuzi kwenye mazungumzo yaliyotangulia, kwani ukombozi na kulaaniwa hutokana na matendo ya mwanadamu si kutoka kwenye mambo ambayo yapo nje ya upeo wa hiari zao au kutoka kwenye matukio ya asili ambayo yamepandikizwa na Muumbaji kwenye uhai wa mwanadamu. Wala sio mambo ya kimazingira na urithi ama uwezo wa kimaumbile uliopo ndani ya mwanadamu ambavyo vina athari zozote kuhusu ukombozi wa mtu au laana yake; hayawezi kutengeneza hatima yake. Kile kinachokadiria mambo ya binadamu ya siku za usoni, ni ule mhimili ambamo ukombozi au kulaaniwa kwake huzunguuka na chanzo cha kupanda au kushuka kwake, ni kiwango ambacho mwanadamu kama kiumbe ambacho kimepewa hiari ya kuchaga, hutengeneza matumizi yanayofaa ya akili yake na ujuzi na uwezo mwingine.

Furaha na ukombozi havitegemei wingi wa uwezo wa kimaumbile. Hata hivyo, ni kweli kwamba mtu ambaye ana uwezo mkubwa zaidi kuliko wengine pia huwa na wajibu mkubwa zaidi. Kosa dogo kwa upande wake ni la wazi zaidi kuliko kosa hilo hilo ambalo limefanywa na mtu dhaifu na asiye na uwezo. Kila mtu ataitwa kuwasilisha mahesabu yake kwa mujibu wa vipaji na uwezo aliokuwa nao.

Inawezekana kabisa kwamba mtu ambaye uwezo wake wa asili na maarifa ni madogo anatakiwa kuendesha maisha yake kwa mujibu wa kazi zake na wajibu wake, alizopewa na kufikia hiyo furaha ya kweli ambayo hiyo peke yake inastahili ya kituo cha juu sana cha mwanadamu. Kitakachomwezesha kupata matokeo hayo ni ukubwa wa juhudi zake anazotumia ili kufanya matumizi sahihi ya uwezo mdogo aliopewa.

Kinyume chake, mtu ambaye amepewa maarifa ya ndani mwengi sana na uwezo mkubwa, sio tu anaweza kutozitumia kwa kujinufaisha mwenyewe, anaweza kutumia vibaya na kufedhehesha hadhi yake ya ubinadamu; na kujitumbukiza kwenye dimbwi la uovu na dhambi. Mtu kama huyu, bila shaka ni mwovu anayetegemewa kulaaniwa na kamwe hatapata hata sekunde moja ya kuona ukombozi. Qur'ani inasema:

"Kila nafsi itafungika (motoni) kwa (maovu) iliyoyachuma." (74:38).

Kwa hiyo, ukombozi au laana ya mtu hutegemeana na matendo yake ya hiari, sio katika hali yake ya kimaumbile au kisaikolojia. Huu ni udhihirisho wa wazi mno wa uadilifu wa Mwenyezi Mungu.

Moja ya kanuni bainifu za madhehebu ya Shia ni badaa, neno lenye maana kwamba hatima za wanadamu hubadilika pale ambapo mambo na vyanzo vinavyoyarekebisha hubadilika; kile kinachoonekana kama cha milele na kisichobadilika, hubadilika kwa mujibu wa mabadiliko ya tabia ya mtu na matendo yake. Kama ambavyo vipengle vya kimaada vinavyoweza kubadili hatima ya mtu, vipengele visivyo vya kimaada pia vinaweza kuchochea matukio mapya.

Inawezekana kwamba vipengele visivyo vya kimaada kama hivi vinaweza kudhihirisha wazi yale yaliyofichika na kinyume na mkondo uliowazi wa matukio. Kwa kweli, kupitia kwenye mabadiliko ya sababu na mazingira, Mwenyezi Mungu ataamua kwamba tukio jipya litatokea, lenye manufaa zaidi ya lile lililobadilishwa. Hii inalingana na ile kanuni ya kutangua sheria iliyofunuliwa. Kama sheria ya mwanzo inatanguliwa kwa ajili ya nyingine, hii haionyeshi ujinga au kujuta kwa upande wa mtungaji-sheria za ki-mungu ila tu ni kwamba uhalali wa ile sheria iliyofutwa umefikia mwisho wake.

Hatuwezi kutafsiri dhana ya badaa kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu anabadili mawazo Yake baada ya ukweli wa kitu ambacho mwanzoni hakukijua na akaja kukijua baadae. Hii itakuwa inapingana na kanuni ya ujuzi wa Mwenyezi Mungu unaojumuisha ulimwengu wote na kwa hiyo haiwezi kukubaliwa na Muislamu yeyote.

Maombi ya dua ni kipengele kingine, ambacho kwamba athari yake isidhalilishwe. Ni dhahiri kwamba Mwenyezi Mungu anatambua siri za ndani kabisa za kila mwanadamu, lakini katika uhusiano wa mtu na Mwenyezi Mungu, maombi ya dua huchukua nafasi kama ile ya juhudi na matendo katika uhusiano wake na maumbile. Mbali kabisa na athari zake za kisaikolojia, dua husababisha athari inayojitegemea.

Kila sekunde matukio mapya hutokea katika maumbile katika kutokea ambako sababu zinazotangulia hutoa mchango. Vivyo hivyo, katika fani moja mashuhuri sana ya maisha maombi ya dua yana athari kubwa sana katika kumwendeleza mtu kuelekea kwenye malengo yake. Kwa namna ileile tu ambayo Mwenyezi Mungu ameweka wajibu kwenye mfumo wa usababisho kwa kila kitu cha asili, vivyo pia, Ameweka wajibu kwenye maombi ya dua.

Mtu anapozungukwa na matatizo, asije akaangukia kwenye fikra za kukosa matumaini na kukataa tamaa. Milango ya huruma za Mwenyezi Mungu kamwe haikufungwa kwa yeyote yule. Inawezekana kwamba kesho hali mpya inatokea ambayo haiendani na vile alivyotegemea. Kwani, kama isemavyo Qur'ani:

".....Kila siku Yeye yumo katika mambo tofauti tofauti." (55:29).

Kwa hiyo, mtu anatakiwa asiache juhudi zake kamwe. Maombi ya dua ambayo hayaunganishwi na jitihada zinazofaa, kama Ali (a.s) Mkuu wa Wamwogopao Mwenyezi Mungu alivyosema, "Kama mtu anayetaka kuachia mshale kutoka kwenye upinde usiokuwa na kamba." Wakati anapofanya juhudi mfululizo, mtu anatakiwa kuweka matakwa yake mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kutumaini na kuamini, na kuomba msaada kwa moyo wote kutoka kwenye kile chanzo cha uwezo wa milele. Mwenyezi Mungu, kwa hakika atamshika mkono mhusika na kumsaidia.

Qur'ani inasema:

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾

"Na waja wangu watakapokuuliza juu yangu basi hakika mimi nipo karibu, nayaitikia maombi ya muombaji anapoomba. Basi waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka." (2:186).

Roho ya binadamu itapaa juu kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na kumtosa kwenye furaha ya kweli ikiwa atakwepa lindi la kuhitaji kwa kuvunja uhu- siano na vyanzo vyote na kumgeukia Mwenyezi Mungu. Hapo atajiona ameungana moja kwa moja na dhati ya Mwenyezi Mungu na kuhisi kuguswa na neema na baraka Zake zisizo na ukomo. Imamu Sajjad(a.s) anamuomba Mwenyezi Mungu ifuatavyo katika dua yake ijulikanayo kama Dua ya Abu Hamza:

"Ee Muumba! Naona njia za kuombea na kulalamikia zinazoelekea Kwako zikiwa wazi na zilizosawazishwa, na sababu za matumaini Kwako zikiwa nyingi sana. Naona inaruhusiwa kuomba msaaada kutoka kwenye neema Yako na huruma Yako, na ninaiona milango ya dua ipo wazi kwa wote wanaokujia Wewe na kuomba msaada Wako. Ninao uhakika kwamba Wewe upo tayari kujibu maombi ya wale wanaokuomba Wewe na kutoa hifadhi kwa wale wanaoitafuta kutoka Kwako."[46]

Pia ipo hadithi kuhusu athari za dhambi na matendo mema: "Wale wanaokufa kwa sababu ya dhambi ni wengi zaidi kuzidi wale wanaokufa kwa sababu za kawaida, na wale wanaoishi kwa sababu ya kutenda matendo mema ni wengi zaidi kuliko wale wanaoishi kwa sababu ya umri wao wa kawaida."[47]

Ilikuwa ni athari za dua zilizomwezesha Zakariya, Mtume wa kweli ambaye alikuwa amekata tamaa ya kupata mtoto, kufanikiwa matakwa yake; ilikuwa athari ya toba iliyomwokoa Mtume Yunus na watu wake kutokana na janga na kuangamia. Sheria ambazo Mwumbaji Mkuu amezipandikiza kwenye mfumo wa ulimwengu, kwa namna yoyote ile haziwezi kuwa mipaka ya uwezo Wake usio na ukomo au kupunguza upeo wake. Anao uamuzi ule ule wa uhakika katika kubadilisha sheria hizo, katika kuthibitisha au kutangua athari

zao, kama Alivyofanya katika kuziasisi. Hiyo dhati ya Pekee, Ambayo usimamizi wake wenye uangalifu na mpana unajumuisha mfumo wote wa uhai, haiwezi kutiishwa kabisa na sheria na viumbe ambavyo Ameviumba Mwenyewe, au Apoteze madaraka na uwezo wa kufanya Atakavyo. Tunaposema kwamba Mwenyezi Mungu anao uwezo wakati wowote kubadili jambo ambalo Ameliumba katika dunia, hatuna maana kwamba Huharibu utaratibu wa dunia na kanuni zake zilizowekwa au anabadilisha sheria na kanuni za maumbile. Kutendeka hasa kwa mabadiliko hutokea kwa kulingana na kanuni fulani zisizojulikana na vigezo ambavyo vinaupita uelewa na utambuzi wetu mfinyu. Endapo mtu analitazama kwa uangalifu na umakini jambo lenyewe na akaufikiria wigo mpana wa uwezekano ambao unamkabili, utamzuia kufanya majaribio makubwa kwa shauku kabisa, ya kutabiri vitu vyote kwa msingi wa kanuni zile chache ambazo ameweza kuzichunguza katika nyanja ya maumbile.

ORODHAYA VITABU VILIVYO CHAPISHWA NA AL-ITRAH FOUNDATION

1. Qur'an Al-Kariim - Tafsir Al-Kashif Juzuu ya kwanza mpaka kumi na tatu

2. Uharamisho wa Riba

3. Uharamisho wa uwongo Juzuu ya kwanza

4. Uharamisho wa uwongo Juzuu ya pili

5. Hekaya za Bahlul

6. Muhanga wa Imamu Husein (A.S.)

7. Mikingamo iliyomzunguka Imamu Ali (A.S.)

8. Hijab vazi Bora

9. Ukweli wa Shia Ithnaashari

10. Madhambi Makuu

11. Mbingu imenikirimu

12. Abdallah Ibn Saba

13. Khadijatul Kubra

14. Utumwa

15. Umakini katika Swala

16. Misingi ya Maarifa

17. Kanuni za Ndoa na maadili ya Familia

18. Bilal wa Afrika

19. Abudharr

20. Usahihi wa Historia ya Uislamu na Waislamu

21. Salman Farsi

22. Ammar Yasir

23. Qur'an na Hadithi

24. Elimu ya Nafsi

25. Yajue Madhehebu ya Shia

26. Ukusanyaji na Uhifadhi wa Qur'an Tukufu

27. Al-Wahda

28. Ponyo kutoka katika Qur'an.

29. Mashukio ya Akhera

30. Nafasi ya Ahlul Bayt

31. Uislamu mfumo wa maisha

Mwenyezi Mungu na sifa zake

258

32. Haki za wanawake

33. Adhana

34. Amateka

35. Udhuu kwa mujibu wa kitabu na sunna

36. Al-Amali

37. Nyuma yaho naje Kuyoboka

38. Amavu namavuko by ubushiya

39. Dua Kwa Mujibu Wa Ahlulbayt(as)

BACK COVER MWENYEZI MUNGU NA SIFA ZAKE

Uislamu ni dini ya elimu na mtu hatakiwi afuate tu kibubusa bila kuelewa kile anachokifua na kukiamini. Misemo inayotumiwa na watu wavivu wakusoma kama vile; "mimi nina swali, ninafunga Mwezi wa Ramadhani na ninashiriki katika masuala yanayo husu dini, hivyo sina haja ya kujua mambo mengine ya dini," kauli kama hizi hazikubaliki katika Uislamu. Mtu lazima ajifundishe na ailewe dini yake vilivyo. Na kitu cha kwanza kwa Mwislamu ni kumjua Mwenyezi Mungu na Sifa Zake ili aweze kufanya ibada zake vizuri na kwa usahihi.

Kitabu hiki huelezea mtazamo wa imani ya Kiislamu ya Mungu Mmoja asiye na mshirika. Mwandishi wa kitabu hiki ameichambua itikadi ya Kiislamu na Umoja wa Mungu (tawhid) kwa kutumia uhojaji wa kifilosofia na maneno mepesi. Ili kukamilisha kazi yake hii ametegemea sana juu ya Sunna na nukuu nyingi kutoka kwenye Qur'an Tukufu. kwa uhodari mkubwa na ujuzi ameyapinga mawazo na mitazamo ya wakana Mungu na wale wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na viumbe vyake.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU