TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS 40%

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS Mwandishi:
Kundi: tafsiri ya Qurani

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS
  • Anza
  • Iliyopita
  • 10 /
  • Inayofuata
  • Mwisho
  •  
  • Pakua HTML
  • Pakua Word
  • Pakua PDF
  • Matembeleo: 12906 / Pakua: 3878
Kiwango Kiwango Kiwango
TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

Mwandishi:
Swahili

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

UTANGULIZI

Makala hizi zimekusanywa kutoka radio ya kiswahili ya iran, na lengo hasa la kuzikusanya makala hizi, ni kueneza na kusambaza utamaduni wa kiislamu ulimwenguni. kwa hiyo basi ukusanyaji huu haukulenga malengo ya aina yeyote isipokua ni kama ilivyotajwa hapo juu.

MKUSANYAJI WA MAKALA HIZI NI:

SALIM SAID AL-RAJIHIY

1

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

MWANZO WA MAKALA

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Ifuatayo ni tarjumi na maelezo mafupimafupi ya Sura ya 10 ya Qur'ani Tukufu ambayo inaitwa Surat Yunus.

Jina la sura hii linatokana na jina la Nabii Yunus(a.s) , ambaye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu aliyekuja baada ya Manabii: Nuh na Musa(a.s) .

AYA YA KWANZA NA YA PILI

Tunaianza basi darsa letu hili kwa aya ya kwanza na ya pili za sura hiyo ambazo zinasema:

الر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْحَكِيمِ ﴿١﴾

1. Alif lam Ra. Hizi ni aya za kitab chenye hikima.

أَكَانَ لِلنَّاسِ عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِّنْهُمْ أَنْ أَنذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا أَنَّ لَهُمْ قَدَمَ صِدْقٍ عِندَ رَبِّهِمْ قَالَ الْكَافِرُونَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ مُّبِينٌ ﴿٢﴾

2. Je ni ajabu kwa watu ya kwamba tumemfunulia wahyi mtu miongoni mwao kuwa: Waonye watu na wape walioamini habari njema ya kwamba watakuwa na cheo kikubwa mbele ya Mola wao?. Wakasema makafiri: "Hayakuwa haya ila ni kiini macho.

Kama tulivyowahi kueleza wakati tulipoizungumzia sura ya pili ya al Baqarah, ni kwamba kati ya sura zote 114 za quran tukufu, sura 29 kati yao zinaanza kwa herufi za mkato kama alif lam mim, hamim, yasin n.k. Na tukasema kuwa kwa kuwa aya zinazofuatia baada ya aya hizo mara nyingi huzungumzia adhama ya quran, baadhi ya wafasiri wanasema lengo lililokusudiwa katika kutanguliza aya hizo ni kutolewa changamoto kwa wasioiamini quran, kwa maana kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha quran kwa kutumia herufi hizo, hivyo nanyi pia kama mnao uwezo teremsheni quran mfano wa hiyo.

Mojawapo ya sifa ambazo Mwenyezi Mungu ameitaja kuwa kimepambika nayo kitabu chake kitukufu cha quran ni hikima. Na hii ni kwa sababu hukumu za dini zilizokuja ndani ya kitabu hicho zimesimama juu ya hoja madhubuti na yale yaliyomo ndani yake ni mafunzo yenye hekima kubwa.

Baada ya kueleza hadhi na nafasi ya quran, katika aya ya pili Mwenyezi Mungu anabainisha nafasi na hadhi ya Mtume wake na kueleza kuwa watu wanatarajia kuona Mwenyezi Mungu akiteremsha Malaika kwa ajili ya kuwafikisha wao uongofu ,wakati kwa kuwa wao ni wanaadamu akili inahukumu kwamba Mtume atakayetumwa kwao lazima naye awe ni mtu kama wao, na anayezungumza lugha yao ili matendo na mwenendo wake wa maisha uweze kuwa kigezo kwao.

Kazi ya Mitume hao ni kutoa bishara njema kwa wafanyao mema na kuwaonya wale watendao mabaya. Lakini kutokana na baadhi ya wakati kuonyesha miujiza ya kuthibitisha ukweli wa unabii wao, baadhi ya watu wasiokuwa tayari kuiamini haki huwasingizia Mitume hao kuwa ni wachawi. Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa quran ni kitabu imara na cha milele, kiasi kwamba kupita kwa wakati hakuwezi kupunguza hata chembe thamani na itibari ya kitabu hicho.

AYA YA TATU

Ifuatayo sasa ni aya ya 3 ya sura hiyo ambayo inasema:

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ مَا مِن شَفِيعٍ إِلَّا مِن بَعْدِ إِذْنِهِ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣﴾

3. Bila shaka Mola wenu ni Mwenyezi Mungu ambaye ameziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Arshi. Yeye ndiye anayepitisha mambo yote. Hakuna muombezi ila baada ya idhini yake. Huyu ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu, basi Muabuduni yeye. Je hamkumbuki?.

Moja kati ya taratibu alizojiwekea Mwenyezi Mungu s.w.t ni kuumba ulimwengu hatua kwa hatua. Na ndiyo maana pamoja na kuwa na uwezo wa kuuumba ulimwengu na kila kiumbe wakati mmoja, Allah s.w.t aliamua kuziumba mbingu na ardhi katika nyakati sita tofauti. Na hivyo ndivyo alivyojaalia pia katika maumbile ya viumbe wengine akiwemo binaadamu ambaye pia uumbwaji wake ni wa hatua kwa hatua, toka tone la manii, pande la damu na hadi mwishowe kufikia kiumbe kamili.

Kama tunavyoona kitoto kichanga kabla ya kuja duniani hupitisha kipindi cha miezi tisa tumboni mwa mama kikiwa katika umbo na hali tofauti hadi kuwadia wakati wa kuja duniani, hali ya kuwa kama angetaka, yeye Mola aliye Muweza wa kila kitu angeufanya uumbaji wote huo katika lahadha moja tu.

Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa uumbaji wa ulimwengu umetokana na ratiba na wakati maalumu na si jambo lililotokea kwa sadfa tu. Aidha aya inatuonyesha kuwa ulimwengu ni kitu kinachofuata kanuni na malengo maalumu. Na sababu ni kuwa mumbaji wake ni mmoja tu.

AYA YA NNE

Darsa hii ya 306 inahitimishwa na aya ya 4 ambayo inasema:

إِلَيْهِ مَرْجِعُكُمْ جَمِيعًا وَعْدَ اللَّـهِ حَقًّا إِنَّهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ لِيَجْزِيَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ بِالْقِسْطِ وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ شَرَابٌ مِّنْ حَمِيمٍ وَعَذَابٌ أَلِيمٌ بِمَا كَانُوا يَكْفُرُونَ ﴿٤﴾

4. Kwake ndiyo marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika yeye ndiye aliyeanzisha viumbe na ndiye atakayewarejesha (baada ya kufa kwao) ili awalipe kwa uadilifu wale walioamini na kufanya vitendo vizuri. Na wale waliokufuru wao watapata vinywaji vya maji yanayochemka na adhabu inayoumiza kwa sababu ya kukataa kwao.

Aya iliyotangulia imeashiria uwezo wa Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi. Aya hii ya nne inazungumzia uumbaji wa mara ya pili wa viumbe, yaani kufufuliwa kwao siku ya kiyama; na katika kuliondolea shaka suala hilo inasema, hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu isiyo na shaka ambapo wale waliomwamini Mola wao wakatenda mema watapata jaza ya kheri, na wale waliomkufuru, malipo yao yatakuwa ni adhabu. Tabaan yote hayo yatafanyika kwa uadilifu ambayo ni miongoni mwa sifa kuu za Allah s.w.t

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa falsafa ya kufufuliwa viumbe ni kuthibiti kwa uadilifu wa Mwenyezi Mungu mtukufu. Kwani dunia hii ndogo na ya kupita tunayoishi haitoshi kuwa ni mahali pa kuwalipa kiadilifu wale waliomwamini Allah na kutenda mema na pia kuwapa adhabu wanayostahiki wale waliomkufuru Mwenyezi Mungu na kufanya kila aina ya dhulma. Aidha aya inatuelimisha kuwa kama dunia na kila kilichomo ndani yake kimeumbwa kwa ajili ya mwanaadamu, huko akhera pia kuwepo kwa ulimwengu huo na neema na nakama zake vitakuwepo kwa ajili ya kutoa malipo kwa sisi wanadamu kutokana na yale yaliyotangulizwa na mikono yetu. Darsa ya 306 imefikia tamati.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa na mwisho mwema na kutunusuru na adhabu ya moto. Amin.

SURAT YUNUS 5-10

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa letu hii.

AYA YA 5 NA 6

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na tunaianza kwa aya ya 5 na 6 za sura hiyo ambazo zinasema:

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا وَقَدَّرَهُ مَنَازِلَ لِتَعْلَمُوا عَدَدَ السِّنِينَ وَالْحِسَابَ مَا خَلَقَ اللَّـهُ ذَٰلِكَ إِلَّا بِالْحَقِّ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ

5. Yeye (Mwenyezi Mungu) ndiye aliyelifanya jua kuwa muanga, na mwezi kuwa nuru na akaupimia vituo(huo mwezi) ili mujue idadi ya miaka na hisabu (nyinginezo). Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo ila kwa haki. Anazipambanua ishara (zake) kwa watu wanaotaka kujua.

﴿٥﴾ إِنَّ فِي اخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَّقُونَ ﴿٦﴾

6. Hakika katika mfuatano (wa daima) wa usiku na mchana ; na katika alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi ziko ishara kwa watu wanaomcha Mungu.

Baada ya aya za mwanzoni mwa sura hii kuashiria juu ya kufufuliwa, kama tulivyoona katika darsa iliyopita, aya hizi tulizosoma zinagusia sehemu ndogo tu ya madhihirisho ya adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji kwa kuzungumzia nafasi ya jua na mwezi.

Uhai wa wanaadamu na sayari yenyewe ya dunia vinategemea nuru na joto litokanalo na jua kama ambavyo nuru ya kupendeza ipatikanayo kupitia kwenye mwezi huwa mithili ya mwanga wa kulalia kwa viumbe mbali mbali wakiwemo wanadamu na pia hutumiwa kama kurunzi ya kuongozea njia katika safari za majangwani na baharini za viumbe hao.

Lakini pia kama tunavyojua mwendo wa sayari ya dunia wa kulizunguka jua na ule wa mwezi wa kuizunguka dunia ndivyo vinavyotuwezesha kuwa na hesabu za siku na pia mwaka kulingana na kalenda ya jua yaani shamsia.

Aidha kutokana na mabadiliko ya umbo la mwezi kuanzia hilali hadi mwezi kamili, ndivyo tunavyoweza kupata pia hesabu ya miezi 12 kulingana na kalenda ya Hijria.

Aya zinamalizia kwa kutilia mkazo nukta hii kwamba yote hayo yaani mfumo kamili wa uumbaji vimefanywa kwa ajili ya kuthibitisha kuwa Mwenyezi Mungu ni wa haki na yote hayo ameyafanya kwa hikma kubwa na kwamba mabadiliko tunayoshuhudia kila siku ya kubadilika kwa usiku na mchana ambayo wengi wetu tunayachukulia kuwa ni kitu cha kawaida, ni dhihirisho la uwezo na hikma ya Allah s.w.t ambalo wanalidiriki na kulihisi wale wamchao yeye Mola Mwenyezi.

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa idadi, hesabu na tarakimu ni vitu vyenye umuhimu katika maisha ya mwanadamu, na quran inatuonyesha kuwa kuhesabu masiku ya mwezi na mwaka kwa kutumia jua na mwezi ni miongoni mwa njia za kutumia kwa ajili ya kufanyia hesabu hizo.

Funzo jengine na ambalo ni la kuzingatiwa sana katika aya hizi ni kuwa haifai kwa muislamu kuvipita vivi hivi vitu vya kimaumbile vilivyomzunguka, kwani katika vitu hivyo anaweza kushuhudia kwa karibu adhama yake Mola Muumba.

AYA 7 NA 8

Zifuatazo sasa ni aya 7 na 8 ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ ﴿٧﴾

7. Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua kwa hayo, na walioghafilika na ishara zetu.

أُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمُ النَّارُ بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨﴾

8. Hao makaazi yao ni motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha ishara za kuwepo Allah s.w.t kupitia uumbaji wa mbingu na ardhi aya hizi zinasema wale walioghafilika na ishara hizo na kushindwa kuzidiriki ishara za kuwepo Mwenyezi Mungu, uwezo wake na hikma yake huishia katika kuikumbatia dunia ya kupita wakidhani kuwa kila kitu kinaishia hapa.

Hivyo huwa hawafikirii juu ya kukutana na Mola wao siku ya Kiyama, na ndiyo maana mwisho wa watu hao unakuwa ni kwenda kutumbukizwa kwenye moto wa jahannam huko akhera.

Moja kati ya mafunzo muhimu tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa kughafilika na Kiyama na kuipaparikia dunia ndiyo mambo yanayomfanya mtu atumbukie kwenye ufuska na maasi.

AYA 9 NA 10

Darsa yetu tunaihitimisha kwa aya 9 na 10 ambazo zinasema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ تَجْرِي مِن تَحْتِهِمُ الْأَنْهَارُ فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٩﴾

9. Hakika wale walioamini na wakatenda mema Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya imani yao. Itakuwa inapita mito mbele yao katika mabustani yenye neema.

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ وَآخِرُ دَعْوَاهُمْ أَنِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠﴾

10. Wito wao humo utakuwa utakuwa: Subhanakallahumma! Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu. Na maamkiano yao humo ni salamun (Alaykum). Na wito wao wa mwisho ni: Alhamdulillahi Rabbil Aalamin" Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu. Mola Mlezi wa walimwengu wote.

Wakati aya zilizotangulia zimebainisha hali ya adhabu itakayowapata wale walioamua kuiabudu dunia, aya hizi zinaashiria hali ya waumini watakaoingizwa peponi na kusema kuwa kupata uongofu wa Allah ndiyo hazina kubwa waliyokuwa nayo watu hao tabaan waliipata kutokana na kumwamini Mola wao na kufanya amali njema.

Kisha aya zinaashiria dua na dhikri za watu wa peponi na kusema kuwa utajo wa Subhanallah na Alhamdulillah ni miongoni mwa alama za watu hao, lakini kama tujuavyo dhikri hizo haziishii katika kuzitamka kwa ulimi tu bali mtu anatakiwa awe anaitakidi kwa dhati kuwa Allah s.w.t ametakasika na kila kasoro na upungufu, na ni kwa kufahamu hivyo ndipo mja humhimidi na kumshukuru kwa dhati Mola Mwenyezi kwa sifa zake zote za ukamilifu.

Aya hizi wapenzi wasomaji zinatuoyesha kuwa uongofu wa Allah ni kitu anachokihitajia katika lahadha ya uhai wake. Aidha aya zinatuonyesha kuwa maamkizi ya amani, ndiyo yatakayotawala katika anga ya peponi. Maamkizi ya amani yatakyotoka kwa Mwenyezi Mungu, yatakayotoka kwa Malaika, na pia watakayopeana watu wa peponi wao kwa wao. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa watu hao. Amin.

2

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

SURAT YUNUS 11-14

Bismillahir Rahmanir Rahim. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 11

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hapa tunaianza kwa aya ya 11 ambayo inasema:

وَلَوْ يُعَجِّلُ اللَّـهُ لِلنَّاسِ الشَّرَّ اسْتِعْجَالَهُم بِالْخَيْرِ لَقُضِيَ إِلَيْهِمْ أَجَلُهُمْ فَنَذَرُ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿١١﴾

11. Na lau kama Mwenyezi Mungu angeliwafanyia watu haraka kuwaletea shari, kama wanavyojihimizia kuletewa kheri, bila shaka wangelisha timiziwa ajali yao. Lakini tunawaacha wale wasiotumainia kukutana nasi, wakihangaika katika upotovu wao.

Moja ya utaratibu ambao Allah s.w.t ameuweka kuhusiana na waja wake ni kutoa muhula na fursa kwao, ili kila mmoja aamue na kuchagua kwa hiyari yake njia gani anayotaka kufuata, ikiwa ni ya kuiamini haki au kuikufuru. Kwa bahati mbaya akthari ya watu huwa hawaitumii kwa njia sahihi fursa hiyo adhimu wanayotunukiwa na Mola wao, na badala yake huogelea kwenye dimbwi la maasi na maovu. Pamoja na hayo Mola aliye mrehemevu huendelea kuamiliana kwa upole na ukarimu na waja wake kwa kuwapa fursa nyingine ya kutubia kwa madhambi waliyoyafanya ili wapate maghufira na msamaha wake.

Ama ikiwa hata baada ya kupata fursa hiyo mja ataamua kuselelea katika kutenda maovu na kumwasi Mola Muumba, mja wa aina hiyo huachwa kama alivyo aendelee kufuata njia hiyo ya upotofu hadi kipindi cha uhai wake kinapomalizika, ambapo hapo huelekea ulimwengu mwingine wa akhera na huko hupata jaza na malipo ya maovu na maasi aliyoyafanya hapa duniani.

Aya hii pamoja na mambo mengine inatufunza kuwa kutoangamizwa kwa makafiri na madhalimu hapa duniani hakumaanishi kuwa yale wayafanyao ni ya sawa au kwamba Mwenyezi Mungu sw anashindwa kuwateremshia adhabu. Bali hiyo inatokana na ile fursa na muhula ambao Allah ameamua kuwapa waja wake hao.

AYA YA 12

Ifuatayo sasa ni aya ya 12 ambayo inasema:

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ الضُّرُّ دَعَانَا لِجَنبِهِ أَوْ قَاعِدًا أَوْ قَائِمًا فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُ ضُرَّهُ مَرَّ كَأَن لَّمْ يَدْعُنَا إِلَىٰ ضُرٍّ مَّسَّهُ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْمُسْرِفِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢﴾

12. Na mtu akiguswa na shida hutuomba, naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tukimwondoshea shida yake huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumwondoshee shida iliyompata. Namna hivi wamepambiwa warukao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda.

Raha na neema za kidunia wapenzi wasomaji humfanya mtu aghafilike na Mola wake na kuikumbatia dunia. Ama shida, masaibu na matatizo mara nyingi humfumbua macho mtu huyo na kumfanya aelewe kuwa binadamu ni kiumbe dhaifu kiasi kwamba pale anapotingwa na matatizo hutambua jinsi ya kumwomba na kumlingana Mwenyezi Mungu kutaka msaada, awe kitandani anaugua maradhi akiomba aponywe, au baharini na angani pale mauti yanapomkabili akawa hana njia nyingine yoyote ya kujiokoa, na hivyo kutaka nusra ya Mwenyezi Mungu s.w.t

Ya laiti baada ya mja kuitikiwa kilio chake hicho angeweza walau kumshukuru tu Mola wake na kuendelea kumkumbuka japo kwa siku chache.

Lakini wapi! Akthari ya watu humsahau haraka Mwenyezi Mungu kana kwamba hawakuwa wametingwa na masaibu na ni yeye Mola aliyetukuka ndiye aliyewaondolea masaibu hayo.

Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa imani ya kuwepo na Mungu mmoja imekita ndani ya nafsi ya kila mwanadamu, na kwa kweli maafa, shida na misukosuko huwa ndiyo chachu ya kuiamsha fitra na maumbile hayo yaliyolala ya kukiri kuweo kwa yule aliye na uwezo mutlaki wa kila kitu.

AYA YA 13 NA 14

Aya ya 13 na 14 ndizo zinazotuhitimishia darsa letu hii. Aya hizo zinasema:

وَلَقَدْ أَهْلَكْنَا الْقُرُونَ مِن قَبْلِكُمْ لَمَّا ظَلَمُوا وَجَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ وَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْقَوْمَ الْمُجْرِمِينَ ﴿١٣﴾

13. Na kwa yakini tumekwisha ziangamiza uma nyingi kabla yenu walipodhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa hoja zilizowazi; lakini hawakuwa wenye kuamini. Namna hivi tunawalipa watu wanaofanya waovu.

ثُمَّ جَعَلْنَاكُمْ خَلَائِفَ فِي الْأَرْضِ مِن بَعْدِهِمْ لِنَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ ﴿١٤﴾

14. Kisha tukakufanyeni nyinyi ndio wenye kushika mahala pao baada yao katika ardhi ili tuone jinsi mtakavyotenda.

Ijapokuwa kama tulivyotangulia kunena katika aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu huwapa muhula wale wanaomwasi na kufanya madhambi na kutowaangamiza papa hapa duniani, lakini hili huwa ni tofauti linapohusu umma au kaumu nzima ya watu, pale watu hao wanapokithirisha dhulma na madhambi, kwani hatima ya kaumu za aina hiyo ni kuangamizwa. Kisha baada ya kuangamizwa kaumu hizo huletwa mahala pao kaumu ya watu wengine ambao wanatakiwa kuyachukulia yale yaliyowasibu waliowatangulia kuwa ni ibra na funzo kwao, vinginevyo na wao pia watapatwa na majaaliwa kama yao.

Miongoni mwa mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa dhulma na uonevu ni mambo yanayoandaa mazingira ya kuangamizwa watu, tabaan wale watu ambao hakuna matumaini tena kwa wao kuamini na kuifuata haki.

Halikadhalika aya zinatuelimisha kuwa hatima na majaaliwa ya watu yako mikononi mwao wenyewe, na kwa kweli ni matendo yao mabaya na maovu ndiyo yanayoainisha wawe na hatima gani.

Na pia aya zinatufunza kwamba endapo mtu atajiona amepata madaraka au mamlaka ya utawala, ajue kuwa huo ni mtihani ambao Mwenyezi Mungu amempa kumjaribu. Tunamwomba Allah atuwafikishe kufuzu mitihani yake na atuzindue kila pale tunapoghafilika na kumkumbuka yeye. Amin.

SURAT YUNUS 15-18

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa letu hii.

AYA YA 15

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hili ni darsa la 309, tunayoianza kwa aya ya 15 ambayo inasema:

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا ائْتِ بِقُرْآنٍ غَيْرِ هَـٰذَا أَوْ بَدِّلْهُ قُلْ مَا يَكُونُ لِي أَنْ أُبَدِّلَهُ مِن تِلْقَاءِ نَفْسِي إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ إِنِّي أَخَافُ إِنْ عَصَيْتُ رَبِّي عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٥﴾

15. Na wanaposomewa aya zetu zilizo wazi, wale wasiotaraji kukutana nasi husema: Lete quran isiyokuwa hii au ibadilishe. Sema: Siwezi kuibadilisha kwa hiyari ya nafsi yangu. Mimi sifuati ila ninayofunuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi naogopa nikumuasi Mola wangu adhabu ya siku iliyo kuu.

Washirikina na waabudu masanamu ambao walikuwa walinganiwa wa wito wa tauhidi aliokuja nao Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) , badala ya kuachana na itikadi na ibada zao hizo potofu, ni wao ndio waliomtaka bwana Mtume akidhi matakwa yao kwa kuzifuta katika Quran zile aya zinazokataza na kukemea ibada ya masanamu, au hata ikiwezekana kuleta kitabu kingine kabisa kisicho na aya za aina hiyo, ili hapo ndipo wao wamwamini Mtume huyo wa Allah.

Hali ya kuwa lengo la Mitume ni kuwaelekeza watu kwenye uongofu na si kutaka kujipatia wafuasi wengi zaidi. Kwa maana kwamba katu hawawezi kukubali matakwa yasiyo ya kimantiki ya watu kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya wafuasi.

Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hii ni kuwa hakuna mtu yeyote yule hata Mtume aliye na haki ya kuibadilisha hata aya moja ya vitabu vya mbinguni vilivyoteremshwa na Allah, bali manabii hao, wao wenyewe ni wenye kujisalimisha na kutii kikamilifu kila kilichokuja katika risala ya wahyi walioteremshiwa na Mola wao.

Aidha aya inatuelimisha kuwa msingi wa mafundisho ya Uislamu ni kushikamana nayo kama yalivyo yale yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu, na wala hakuna thamani yoyote kuifanya dini iwe na wafuasi wengi zaidi kwa gharama ya kubadilisha na kupotosha mafundisho yake ya asili.

AYA ZA 16 NA 17

Zifuatazo sasa ni aya za 16 na 17 ambazo zinasema:

قُل لَّوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا تَلَوْتُهُ عَلَيْكُمْ وَلَا أَدْرَاكُم بِهِ فَقَدْ لَبِثْتُ فِيكُمْ عُمُرًا مِّن قَبْلِهِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٦﴾

16. Sema: Mwenyezi Mungu angeli taka nisingeli kusomeeni, wala nisingeli kujuvyeni. Kwani nilikwisha kaa nanyi umri mzima kabla yake! Basi, je hamzingatii?

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أَوْ كَذَّبَ بِآيَاتِهِ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْمُجْرِمُونَ ﴿١٧﴾

17. Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu na akazikanusha aya zake? Hakika hawafaulu wale wafanyao maovu.

Aya hizi wapenzi wasomaji zinaendelea kutoa jibu kwa wale watu waliomtaka Bwana Mtume Muhammad(s.a.w.w) aibadilishe quran na kuwaambia, Mtume huyu ameishi na nyinyi kwa miaka arubaini.

Lau quran hii ingekuwa imetokana na fikra zake yeye mwenyewe bila shaka katika kipindi hicho chote mungeweza kushuhudia maneno mithili ya hayo katika fikra zake. Isitoshe ni kuwa yeye Muhammad hakuwahi kusoma popote wala kufunzwa na yeyote hata mseme labda hii quran itakuwa ni matunda ya elimu hiyo aliyokuwa amejifunza hapo kabla.

Hivyo wale wanomtaka yeye aibadilishe quran hakika wanachofanya ni kuzikadhibisha aya za Mwenyezi Mungu na kumzulia uwongo yeye Mola Muumba, jambo ambalo ni sawa na kumfanyia dhulma kubwa kabisa yeye Mola, Mtume wake na kitabu chake cha quran.

Baadhi ya tunayojifunza katika ya hizi ni kuwa vitabu vya mbinguni ni wahyi utokao moja kwa moja kwa Allah na wala si kitu kinachotokana na fikra za Mitume au mtu mwengine yoyote.

Aidha zinatutaka tuelewe kuwa dhulma kubwa kabisa ni ile ya kupotosha na kuyabadilisha mafundisho asili ya dini.

AYA YA 18

Tunaihitimisha darsa yetu hii kwa aya ya 18 ambayo inasema:

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُمْ وَلَا يَنفَعُهُمْ وَيَقُولُونَ هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ قُلْ أَتُنَبِّئُونَ اللَّـهَ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١٨﴾

18. Nao wanaabudu (waungu) wasiokuwa Mwenyezi Mungu wasioweza kuwadhuru wala kuwanufaisha. Na wanasema: "Hao ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu". Sema:"Je Mnamwambia Mwenyezi Mungu asiyoyajua katika mbingu wala katika ardhi?".Ameepukana na upungufu (wa kutaka mshirika), na ametukuka na hao wanaowashirikisha naye.

Washirikina walikuwa wakiyaabudu masanamu ambayo si kwamba yalikuwa yana uwezo wa kuwadhuru hata kwa kukhofia hilo wahisi kuwa hawana budi ila kuwaabudu, na si kwamba pia kuna faida walikuwa wakipata kwa masanamu hayo hata tamaa ya kupata faida hiyo iwe sababu ya kuwafanya wawapigie magoti na kuwaomba.

Ama hoja waliyokuwa wakiitoa washirikina hao ni kuwa masanamu hayo yalikuwa ni wasita na kiunganishi kati yao na Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo hoja hii haikubaliki kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuyafanya masanamu hayo ni wasita, kiunganishi na waombezi wa waja wake kwake yeye. Hii ni tofauti na wala haiwezi kulinganishwa na suala la tawasul wanayofanya watu kwa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu na kuomba wawatakie shufaa mbele ya Mola, kwani hao wako katika maisha maalumu ya barzakhi waliyojaaliwa na Allah na vile vile ni yeye Mola mwenyewe aliyewaelekeza watu watumie wasita wa waja wake hao walio wateule kwa ajili ya kumfikia yeye.

Funzo moja muhimu tunalolipata kutokana na aya hii ni kuwa tujihadhari na kukifanya kitu au mtu yeyote yule kuwa mshirika wa Allah katika uungu, au kukifanya kitu au mtu kuwa na hadhi ya kuweza kutushufaia na kutuombea mbele ya yeye Mola, ghairi ya wale yeye Allah mwenyewe aliowapa daraja hiyo ya kuwa waombezi kwa waja wake.

Darsa ya 309 imefikia tamati. Tunamwomba Allah atulinde na kila aina ya shirki. Amin.

3

TAFSIRI YA SUURAT YUUNUS

SURAT YUNUS 19-23

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an.

AYA YA 19

Hii ni darsa ya 310, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya ya 19 ambayo inasema:

وَمَا كَانَ النَّاسُ إِلَّا أُمَّةً وَاحِدَةً فَاخْتَلَفُوا وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ فِيمَا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿١٩﴾

19. Wala watu hawakuwa ila umma mmoja tu. Kisha wakakhitalifiana. Na lau kuwa si neno lililo kwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka hukumu ingelikwisha katwa baina yao katika hayo wanayo khitalifiana.

Mwenyezi Mungu sw amewaumba wanaadamu wote wakiwa na fitra yaani maumbile safi ya tauhidi ya kukubali kuwepo kwa Mungu mmoja.

Hivyo hapo awali wanaadamu wote walikuwa ni sawa na umma mmoja. Lakini kwa kupita muda, na kuzainiwa na shetani kundi miongoni mwa watu wakatumbukia kwenye upotofu wa shirki na hivyo watu wakagawika katika makundi mawili ya wampwekeshao Allah na Mushrikina. Ama Mwenyezi Mungu hakutaka kuwateza nguvu waja wake, bali alitaka kila mtu achague kwa hiyari yake njia anayoamua kufuata. Na ni kwa sababu hiyo ndipo akaamua kuwapa fursa na muhula wale waliokhitari upotofu kufanya lolote lile watakalo.

Na lau si utaratibu huo aliouweka Mwenyezi Mungu basi angewaadhibu papa hapa duniani na kumaliza hitilafu kati ya waumini na makafiri. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa thamani na utukufu wa mwanadamu unapatikana kwa kule kufanya ayatakayo ikiwa ya thawabu au ya madhambi kwa hiyari yake. Vinginevyo hakuna fakhari yoyote kwa mtu kuamini na kufuata njia ya haki kwa kulazimishwa.

AYA YA 20

Ifuatayo sasa ni aya ya 20 ambayo inasema:

وَيَقُولُونَ لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَقُلْ إِنَّمَا الْغَيْبُ لِلَّـهِ فَانتَظِرُوا إِنِّي مَعَكُم مِّنَ الْمُنتَظِرِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na wanasema: Kwa nini hakuteremshiwa kutoka kwa Mola wake miujiza (tunayoitaka)? Sema: Mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu.Basi nyinyi ngojeni, na mimi ni pamoja na nanyi katika wanaongoja.

Nabii Muhammad(s.a.w.w) alikuja na miujiza mbali mbali kama walivyokuwa Manabii waliomtangulia. Tabaan muujiza mkuu wa Mtume huyo wa mwisho ni quran tukufu ambao washirikina walishindwa kukabiliana nao hata kwa kuleta walau aya moja mfano wake.

Lakini katika kutafuta visingizio, washirikina hao kila siku walikuwa wakitaka waonyeshwe muujiza mpya ikiwa ni pamoja na kumtaka Bwana Mtume awaletee kila wanachotaka. Ndipo katika kuwajibu Bwana Mtume akawaambia muujiza ni suala lililoko kwenye mamlaka ya Mwenyezi Mungu na wala haliko mikononi mwangu mimi, na ni kila pale anapotaka yeye ndipo muujiza unapoletwa, ama mnachotaka nyinyi si kitu kingine ghairi ya kutafuta visingizio tu.

Ukweli wa haya wapenzi wasomaji unashuhudiwa pia kama tulivyoona katika aya zilizotangulia pale washirikina wa kikureishi walipomtaka Bwana Mtume azibadilishe aya za quran au hata ikiwezekana awaletee qurani nyingine mpya badala ya ile aliyoteremshiwa na Mola wake.

Pamoja na mambo mengine aya hii inatufunza kuwa chanzo na chimbuko la shirki na ukafiri si kutokuwepo muujiza na hoja za kuthibitisha ukweli wa risala ya haki, isipokuwa ni tabia ya ukaidi, inda na inadi mbele ya haki.

AYA YA 21

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 21 ambayo inasema:

وَإِذَا أَذَقْنَا النَّاسَ رَحْمَةً مِّن بَعْدِ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُمْ إِذَا لَهُم مَّكْرٌ فِي آيَاتِنَا قُلِ اللَّـهُ أَسْرَعُ مَكْرًا إِنَّ رُسُلَنَا يَكْتُبُونَ مَا تَمْكُرُونَ ﴿٢١﴾

21. Na tunapowaonjesha watu rehma baada ya shida iliyowapata, mara huanza kutunga hila (za kutaka kupinga) Aya zetu. Sema: Mwenyezi Mungu ni mwepesi zaidi wa kupanga. Hakika wajumbe wetu wanayaandika mnayoyapanga.

Historia inasimulia kuwa ilitokea wakati mmoja mji wa Makka ulikumbwa na ukame mkubwa lakini Mwenyezi Mungu kwa baraka ya kuwepo Nabii Muhammad(s.a.w.w) akateremsha mvua zake za rehma na kuuletea faraja mji huo.

Ama washirikina wao walidai kuwa kunyesha kwa mvua hizo kulitokana na baraka za masanamu yao.

Ndipo aya tuliyoisoma ikashuka na kuwatanabahisha kuwa kama nyinyi ni wenye kutaka hakika ya mambo, basi tambueni kuwa mvua hizo ilikuwa ni muujiza utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo inadi yenu imekufanyeni muzue hila hizi na zile za kuzinasibisha na masanamu yenu rehma hiyo iliyotoka kwa Mola wenu.

Pamoja na hayo tambueni kuwa malaika wa Mwenyezi Mungu ambao hutumwa kwa watu wanayanakili na kuyarekodi yote yanayotendwa na waja na hivyo mushirikina wajiandae na majibu ya kwenda kumpa Mola wao siku ya kiyama kwa yote wanayoyatenda.

Tabaan katika dunia hii pia Mwenyezi Mungu atawapa jaza ya vitimbi na hila zao, nao katu hawawezi kusimama dhidi ya irada ya Allah s.w.t.

AYA ZA 22 NA 23

Aya za 22 na 23 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

هُوَ الَّذِي يُسَيِّرُكُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ حَتَّىٰ إِذَا كُنتُمْ فِي الْفُلْكِ وَجَرَيْنَ بِهِم بِرِيحٍ طَيِّبَةٍ وَفَرِحُوا بِهَا جَاءَتْهَا رِيحٌ عَاصِفٌ وَجَاءَهُمُ الْمَوْجُ مِن كُلِّ مَكَانٍ وَظَنُّوا أَنَّهُمْ أُحِيطَ بِهِمْ دَعَوُا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ لَئِنْ أَنجَيْتَنَا مِنْ هَـٰذِهِ لَنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ ﴿٢٢﴾

22. Yeye ndiye anayekuendsheni bara na baharini. Hata mnapokuwa majahazini na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri wakaufurahia, mara upepo mkali ukawazukia na yakawajia mawimbi kutoka kila upande na wakaona wameshatingwa, hapo ndipo wanapomwomba Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia utii (wakisema): Ukituokoa na haya bila shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

فَلَمَّا أَنجَاهُمْ إِذَا هُمْ يَبْغُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّمَا بَغْيُكُمْ عَلَىٰ أَنفُسِكُم مَّتَاعَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ثُمَّ إِلَيْنَا مَرْجِعُكُمْ فَنُنَبِّئُكُم بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٣﴾

23. Lakini akishawaokoa mara wanafanya jeuri tena katika ardhi bila ya haki.Enyi watu! Jeuri zenu zitakudhuruni wenyewe. Ni starehe (chache tu) za maisha ya dunia. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutakuambieni mliyokuwa mkiyatenda.

Bila shaka mngali mnakumbuka wapenzi wasomaji kuwa tulisema mwanzoni mwa darsa yetu hii kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu wote katika fitra na maumbile safi ya tauhidi ya laa ilaha illa llah, yaani kukana waungu wengine wote bandia na kuthibitisha hakika ya kuwepo kwa Mola mmoja tu wa haki.

Baada ya kueleza hayo, aya hizi tulizosoma hivi punde zinabainisha kuwa mapumbao haya na yale ya kidunia huwa mithili ya utando unaogubika na kufililiza nuru hiyo ya tauhidi ndani ya nafsi ya mtu na kumfanya mja aghafilike na Mola wake.

Ama pale mtu anapotingwa na kupatwa masaibu yanayomfanya akate tamaa ya kupata nusra kupitia njia yoyote ile hapo ndipo utando ule unapotoweka mithili ya vumbi lililosukumwa na upepo na kuiamsha fitra na maumbile ya tauhidi, na kumshuhudia mja akimlingana na kumwomba kwa ikhlasi na unyenyekevu Mola wake aliyemuumba msaada wa nusra na uokozi.

Lakini kama tulivyowahi kuashiria katika moja ya darsa zilizopita baada ya kupata nusra ya Allah mwanadamu husahau kila kitu mara moja, akighafilika kwamba maisha haya ya dunia ni mafupi na ya kupita tu, na kwamba sisi sote mwisho wetu na marejeo yetu ni kwa Mwenyezi Mungu, na huko kila mmoja atasimamishwa mbele ya mahakama ya uadilifu ili kuwajibika kwa yote aliyoyafanya hapa duniani.

Aya hizi zinatuoenyesha kuwa majanga ya kimaumbile husaidia kuondoa ghururi na kiburi cha mwanadamu na kuamsha hisia za kumtambua na kumnyenyekea Mola wake.

Aidha aya zinatutaka tuelewe kuwa imani ya msimu na ya mazingira fulani haina faida; imani ya kweli ni ya kudumu na ya katika kila hali, awe mtu katika raha na neema au shida na nakama.

Darsa ya 310 inaishia hapa. Tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaomwamini na kuikiri tauhidi katika hali zote. Amin. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 24-27

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 24

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 311 tunayoianza kwa aya ya 24 ambayo inasema:

إِنَّمَا مَثَلُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا كَمَاءٍ أَنزَلْنَاهُ مِنَ السَّمَاءِ فَاخْتَلَطَ بِهِ نَبَاتُ الْأَرْضِ مِمَّا يَأْكُلُ النَّاسُ وَالْأَنْعَامُ حَتَّىٰ إِذَا أَخَذَتِ الْأَرْضُ زُخْرُفَهَا وَازَّيَّنَتْ وَظَنَّ أَهْلُهَا أَنَّهُمْ قَادِرُونَ عَلَيْهَا أَتَاهَا أَمْرُنَا لَيْلًا أَوْ نَهَارًا فَجَعَلْنَاهَا حَصِيدًا كَأَن لَّمْ تَغْنَ بِالْأَمْسِ كَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mawinguni, kisha mimea ya ardhi wanayoila watu na wanyama ikachanganyika nayo (maji hayo, ikastawi). Hata ardhi ilipokamilika uzuri wake na ikapambika, na wenyewe wakadhani wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana na tukaifanya kama iliyofyekwa, kama kwamba haikuwako jana. Namna hivi tunazipambanua aya (zetu) kwa watu wanaofikiri.

Katika kubainisha baadhi ya masuala, Mwenyezi Mungu ametumia ndani ya quran lugha ya tamthili na tashbihi. Aya tuliyoisoma ni miongoni mwa aya hizo ambayo imelinganisha na kushabihisha hali ya kupita na kumalizika haraka dunia kuwa ni sawa na ardhi iliyonawiri kutokana na kunyeshewa na mvua lakini pale inapokuja kukumbwa na kimbunga au mafuriko tahamaki kila kitu kilichopandwa katika ardhi hiyo kinatoweka kana kwamba havukiwepo hapo kabla.

Aya hii wapenzi wasomaji inatuelimisha kuwa umri wa mwanadamu katika dunia hii ni mfupi mithili ya umri wa mimea na maua hivyo tusihadaike tukadhani kuwa tutabaki milele katika ulimwengu huu.

AYA YA 25

Ifuatayo sasa ni aya ya 25 ambayo inasema:

وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَىٰ دَارِ السَّلَامِ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٢٥﴾

25. Na Mwenyezi Mungu anaita kwendea nyumba ya amani, na humuongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka (maadamu anakubali uwongofu).

Mkabala wa maisha haya ya mafupi na ya kupita ya dunia kuna maisha mengine ya milele ya akhera ambayo Mwenyezi Mungu amewataka waja wake wayapiganie hayo na akawapelekea Mitume pia wa kuongoza watu kuelekea kwenye makazi ya utulivu wa kweli.

Ni wazi kuwa watu wanaoshikamana na kamba ya uongofu ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewahisi kuwa wana ustahili wa kufikia makazi hayo na ambao matendo na amali zao hapa duniani hazikuwa sababu ya kujiweka mbali na njia iliyonyooka.

Aya hii inatufunza kuwa raha na uzima wa dunia ni vitu vya kupita tu, kinyume chake raha na uzima wa akhera ni za kudumu na za milele. Funzo jengine tunalolipata katika aya hi ni kuwa njia pekee ya kufikia kwenye utulivu na raha za kweli ni kupiga hatua kuelekea kwenye njia ya iliyonyooka ya Allah, ambayo hapa duniani huupa moyo wa mja utulivu na huko akhera humuongoza kuelekea kwenye pepo ya saada.

AYA YA 26

Tuitegee sikio sasa aya ya 26 ambayo inasema:

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ وَلَا يَرْهَقُ وُجُوهَهُمْ قَتَرٌ وَلَا ذِلَّةٌ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٦﴾

26. Wale waliofanya wema watapata (jaza ya) wema (wao) na ziada; Wala vumbi halitawafunika nyuso zao wala madhila. Hao ndio watu wa Peponi; humo watakaa milele.

Baada ya aya iliyotangulia kuashiria juu ya pepo, aya hii inasema Mwenyezi Mungu ameiandaa pepo hiyo kwa wale waja wake waliofanya mema, na kwamba jaza na malipo watakayopata waja hao iwe ni kwa sura ya wingi au ubora, yatakuwa makubwa na bora zaidi kuliko amali walizotenda hapa duniani, .kama ambavyo katika aya nyinginezo Allah s.w.t anasema yeyote atendaye jema moja hupata thawabu na malipo mara kumi ya jema hilo, ambapo kwa upande wa utoaji, malipo ya mja hufikia hata mara mia saba ya kile alichotoa.

Baadhi ya yale tunayojifunza katika aya hii ni kuwa ikiwa Mwenyezi Mungu ametuita tuifuate njia yake ya uongofu kisha akatuonyesha njia ya kuifikia, na kisha akatushajiisha na hata kuwalipa thawabu na malipo bora kabisa wale wanaoifikia njia hiyo, ni kitu gani basi cha kutufanya tuache kuitikia mwito wa Mola wetu na kuwafuata wengine wasiokuwa yeye?

AYA YA 27

Aya inayotuhitimishia darsa yetu ni aya ya 27 na ambayo inasema:

وَالَّذِينَ كَسَبُوا السَّيِّئَاتِ جَزَاءُ سَيِّئَةٍ بِمِثْلِهَا وَتَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ مَّا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِنْ عَاصِمٍ كَأَنَّمَا أُغْشِيَتْ وُجُوهُهُمْ قِطَعًا مِّنَ اللَّيْلِ مُظْلِمًا أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٧﴾

27. Na wale waliochuma maovu, malipo ya uovu ni mfano wake vile vile; na yatawafika madhila. Hawatakuwa na awezaye kuwalinda na (adhabu ya) Mwenyezi Mungu. Zitakuwa nyuso zao kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio watu wa Motoni; humo watakaa daima.

Wakati ambapo wale waliotenda matendo mazuri watakuwa na mwisho mwema huko akhera, wale waliokhitari kufuata upotofu kwa kumkufuru na kumwasi Mola wao hawatapata jaza nyingine ghairi ya adhabu ya Allah, na wala hawatoweza, wala kupata pa kukimbilia, ambapo ukali wa adhabu watakayopata utazifanya nyuso zao zititie na kupiga weusi.

Tabaan adhabu hiyo italingana kabisa na uzito na kiwango cha madhambi waliyofanya, ama kwa upande wa watenda mema wao watapata fadhila zake Mola za kulipwa malipo ya kheri yaliyo makubwa zaidi ya mema waliyotenda.

Aya hii pamoja na mambo mengine inatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu amewaumba wanaadamu akiwa amewapa uhuru na hiyari ya kuchagua njia ya kufuata. Na ndiyo maana kundi moja linaamua kufuata mema na jengine linakhitari kufuata maovu.

Halikadhalika aya inatufunza kuwa katika mfumo wa malezi wa Uislamu siku zote ushajiishaji kwa kutoa hidaya na zawadi unapewa kipaumbele kuliko utiaji adabu na utoaji adhabu.

Darsa ya 311 inaishia hapa. Tunamwomba Allah ajaalie bora ya amali zetu ziwe ni zile za lahadha ya mwisho ya uhai wetu, na siku bora kwetu iwe ni ile ya kukutana na yeye. Amin

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 28-33

Assalaamu Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni katika mfululizo mwingine wa Darsa ya Qur'an.

AYA ZA 28 NA 29

Hii ni darsa ya 312, na tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus, tunaianza darsa yetu kwa aya za 28 na 29 ambazo zinasema:

وَيَوْمَ نَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا ثُمَّ نَقُولُ لِلَّذِينَ أَشْرَكُوا مَكَانَكُمْ أَنتُمْ وَشُرَكَاؤُكُمْ فَزَيَّلْنَا بَيْنَهُمْ وَقَالَ شُرَكَاؤُهُم مَّا كُنتُمْ إِيَّانَا تَعْبُدُونَ ﴿٢٨﴾

28. Na siku tutakapowakusanya wote, kisha tutawaambia wale walioshirikisha: 'Simameni mahali penu nyinyi na wale mliowafanya washirika wa Mungu.' Kisha tutawatenga baina yao. Na hao waliowashirikisha watasema: 'Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi.

فَكَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ إِن كُنَّا عَنْ عِبَادَتِكُمْ لَغَافِلِينَ ﴿٢٩﴾

29. Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yetu na baina yenu. Hakika sisi tulikuwa hatuna habari ya ibada yenu.

Aya hizi zinabainisha jinsi hali itakavyokuwa siku ya Kiyama, ambapo Mwenyezi Mungu atawasimamisha mushirikina na wale waliokuwa wakiwaabudu na kuliuliza kila kundi peke yake; kwa nini nyinyi mlikuwa mkiyaabudu masanamu na miungu wa kubuni? Na nyinyi pia ilikuwaje mkaridhia kuabudiwa na watu hawa? Hapo ile miungu ya masanamu isiyo na uhai itapewa uhai kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuwakana wale waliokuwa wakiwaabudu na kutamka kuwa, "sisi hatukuwa tukijihesabu kuwa washirika wa Mwenyezi Mungu, bali nyinyi mlijitengenezea taswira akilini mwenu, na kuziabudu na sisi kutufanya kama kisingizio tu".

Aya ya 41 ya suratu Sabaa pia imeashiria maudhui hii na kueleza kuwa malaika nao ambao walikuwa wakiabudiwa wanadhihirisha, kuchukizwa kwao na kitendo hicho cha Mushrikina.

Nukta yenye mguso wa aina yake hapa ni kuwa katika aya hizi Allah s.w.t amewataja waabudiwa hao kuwa ni washirika wa Mushrikina kwa maana kwamba, hao hawakuwa waungu wanaoshirikishwa na Mwenyezi Mungu, bali ni washirika wenu nyinyi mushirikina mliojibunia na kujitengenezea wenyewe.

Miongoni mwa yale tunayojifunza katika aya hizi ni kuwa siku ya Kiyama, mbali ya wanaadamu, miungu na waabudiwa bandia yakiwemo masanamu yatapewa uhai ili kutoa ushahidi katika mahakama ya uadilifu dhidi ya mushirikina.

AYA YA 30

Ifuatayo sasa ni aya ya 30 ambayo inasema:

هُنَالِكَ تَبْلُو كُلُّ نَفْسٍ مَّا أَسْلَفَتْ وَرُدُّوا إِلَى اللَّـهِ مَوْلَاهُمُ الْحَقِّ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٣٠﴾

30. Huko kila mtu atayajua aliyoyatanguliza. Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki. Na yatawapotea yale waliyokuwa wakiyazua.

Baada ya masanamu na waabudiwa wengine kuwakana mushirkina, hapo makundi mawili hayo yatatenganishwa na mushirikina hawatoweza kuwaomba msaada hao waliokuwa wakiwafanya washirika wa Mwenyezi Mungu hapa duniani, na badala yake watarejea kwa Mola wao wa haki yaani Allah sw na hapo ndipo watapata jaza na malipo ya amali zao.

AYA YA 31

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 ambayo inasema:

قُلْ مَن يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ أَمَّن يَمْلِكُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَمَن يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ وَيُخْرِجُ الْمَيِّتَ مِنَ الْحَيِّ وَمَن يُدَبِّرُ الْأَمْرَ فَسَيَقُولُونَ اللَّـهُ فَقُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣١﴾

31. Sema: 'Ni nani anayekuruzukuni kutoka mbinguni na katika ardhi. Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani amtoaye mzima katika mfu na kumtoa mfu katika mzima?Na nani anaye yadabiri mambo yote?' Watasema: 'Ni Mwenyezi Mungu.' Basi sema: 'Je Hamuogopi?

Baada ya aya zilizotangulia ambazo zimeonyesha unyonge na udhalili utakaowapata washirikina siku ya Kiyama, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume wake awaulize watu hao kuwa nyinyi ambao mnamkubali Mwenyezi Mungu, na mnajua kuwa ni yeye ndiye anayekuruzukuni, na ni yeye ndiye anayesimamia mambo yenu yote, kwa nini basi badala ya kumwabudu yeye mnayaabudu masanamu na kuyafanya wasita na waunganishi wa mambo yenu kwa Mwenyezi Mungu?

Kama ambavyo katika aya nyingine za quran imeelezwa kuwa mushirikina wa enzi za ujahiliya walikuwa wakikubali kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wao na Muumba wa ulimwengu, ama katika suala la kuendesha mambo, mamlaka hayo yako mikonnoni mwa malaika na vitu vingine vya maumbile, kama kwamba Mwenyezi Mungu ameumba tu kisha akakaa kando na kulikabidhi kwa viumbe hao suala la uendeshaji wa ulimwengu.

Fikra ya aina hii imeelezwa na quran tukufu kuwa ni batili na aina mojawapo ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu. Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa uendeshaji wa ulimwengu unahitajia tadbiri isiyobadilika, na hili halingewezekana kama kungekuwepo na Muumba zaidi ya mmoja.

AYA ZA 32 NA 33

Aya za 32 na 33 ndizo zinazotuhitimishia darsa yetu hii. Aya hizo zinasema:

فَذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمُ الْحَقُّ فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ فَأَنَّىٰ تُصْرَفُونَ ﴿٣٢﴾

32. Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki isipokuwa upotofu tu? Basi huwaje mkageuzwa?

كَذَٰلِكَ حَقَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ عَلَى الَّذِينَ فَسَقُوا أَنَّهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٣﴾

33. Hivi ndivyo kauli ya Mola wako itakavyowathubutikia wale walioasi, ya kwamba hawataamini.

Baada ya aya zilizotangulia kubainisha mifano ya ishara za adhama ya Mwenyezi Mungu katika uumbaji wa mbingu na ardhi pamoja na kukiri kwa washirikina kuhusu uumbaji wa Mwenyezi Mungu.

aya hizi zinabainisha wazi kuwa Mungu huyu ndiye Mola wenu, na vile vile ndiye muendeshaji mambo yenu; na si kwamba yeye ni muumba wenu lakini masanamu yakawa ndio waendeshaji wa mambo yenu.

Kisha aya zinaendelea kwa kutoa kauli ya mkato kwamba, hakuna hali ya tatu baada ya haki na batili. Kwa maana kwamba kila kitu ima ni haki au ni batili, na kwa hivyo kwa kuwa Mwenyezi azza wa jal ndiye haki, basi bila shaka masanamu na miungu wenu wengine wa kubuni hawawezi kuwa haki, na hivyo wale watu wanaoamua kuipa mgongo haki kwa inadi, ubishi na ukaidi hawawezi kupata taufiki ya kuufikia uongofu.

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa hakuna njia ya tatu baada ya haki na batili. Na kwa hivyo yanapothibitika mawili hayo, hakuna nafasi ya mtu kudai kuwa yeye hayuko huku wala huku bali ni mtu wa kati na kati.

Kwa haya machache tunaifunga darsa yetu hii. Tunamwomba Allah atuepushe na shirki na kuijenga imani kamili na safi ya tauhidi ndani ya nyoyo zetu. Amin

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 34-38

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA ZA 34 NA 35

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 313 tunayoianza kwa aya za 34 na 35 ambazo zinasema:

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ قُلِ اللَّـهُ يَبْدَأُ الْخَلْقَ ثُمَّ يُعِيدُهُ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ ﴿٣٤﴾

34. Sema: Je Yupo katika miungu yenu ya ushirikina, aliyeanzisha kuumba viumbe kisha akavirejesha? Sema: Mwenyezi Mungu ameanzisha kuumba viumbe kisha ndiye atakayevirejesha. Huwaje basi mkadanganywa?.

قُلْ هَلْ مِن شُرَكَائِكُم مَّن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ قُلِ اللَّـهُ يَهْدِي لِلْحَقِّ أَفَمَن يَهْدِي إِلَى الْحَقِّ أَحَقُّ أَن يُتَّبَعَ أَمَّن لَّا يَهِدِّي إِلَّا أَن يُهْدَىٰ فَمَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ ﴿٣٥﴾

35. Sema: Je Yupo katika miugu yenu ya ushirikina anayeongoa kuendea Haki? Sema: Mwenyezi Mungu anaongoa kwendea Haki. Basi je anayestahiki kufuatwa ni yule Mwenye kuongoa kwendea Haki au asiyeongoa ila aongozwe yeye? Basi nyinyi mna nini? Mnahukumu namna gani?.

Zikiendelea kuzungumzia yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu kutoa changamoto kwa mushrikina ya kuwaonyesha jinsi miungu yao bandia isivyo na uwezo wa kufanya lolote, aya tulizosoma zinasema, ikiwa mtatupia jicho na kuzingatia uumbaji ulivyo mtabaini kuwa hakuna yeyote ghairi ya Mungu Mmoja awezaye kuumba kila kilichopo na kukipa uhai mpya, na hayo masanamu yenu mnayoyaabudu na viumbe vingine vyote vilivyoko, vyote hivyo vimeumbwa na vinamhitajia Muumbaji, basi yawaje vitu hivyo viweze navyo kuwa waumbaji wa ulimwengu?

Kama nyinyi ni wenye kutafuta uongofu na kutaka kuifikia saada tambueni kuwa miungu wenu hao wenyewe hawana cha kumuongoza mtu hata muweze kupata muongozo wa kufuata kutoka kwao, na kama ni suala la kupata uongofu, inalazimu wao wenyewe kwanza wawe na sifa hiyo ya kuweza kuufikia huo uongofu kisha ndipo waweze kukuonyesheni nyinyi pia njia ya kuufikia. Hali ya kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muongozaji wenu wa kukufikisheni kwenye njia iliyonyooka. Tabaan uongofu wa Mwenyezi Mungu unapatikana kupitia Mitume wake na vitabu vya mbinguni walivyokuja navyo ambavyo kila kilichomo ndani yake ni maneno yake Mola Muumba.

Miongoni mwa yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa kutumia mfumo wa masuali na majibu ni mojawapo ya mbinu bora kwa ajili ya kujadiliana na wapinzani wa kiitikadi na kifikra, mbinu ambayo Allah sw amewafunza Mitume wake. Aidha aya zinatuelimisha kuwa Mwenyezi Mungu si Muumbaji wa ulimwengu tu, bali baada ya kuwaumba viumbe wake hakuwaacha kama walivyo, ila amewaonyesha pia njia yao ya uongofu itakayowafikisha kwenye saada ya duniani na akhera.

AYA YA 36

Ifuatayo sasa ni aya ya 36 ambayo inasema:

وَمَا يَتَّبِعُ أَكْثَرُهُمْ إِلَّا ظَنًّا إِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٣٦﴾

36. Na wengi wao hawafuati ila dhana tu. Na dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua yote wanayoyatenda.

Aya hii wapenzi wasomaji inaashiria chanzo na chimbuko la upotofu wa kifikra la wale wanaomkanusha na kumkufuru Mwenyezi Mungu na kueleza kuwa kufuata dhana na mambo ya udhanifu yasiyo na msingi ambayo kwa hakika ni njozi za kifikra ndiyo yaliyowafanya watu hao waipe mgongo haki na kung'ang'ania fikra na itikadi batili.

Hali ya kuwa katika masuala ya kifkra na kiitikadi, dhana na mambo ya udhanifu hayana nafasi wala itibari yoyote, na ukweli ni kuwa hakika na yakini ndiyo mambo yanayoweza kumfikisha mtu kwenye haki.

Mbali na hayo chimbuko la itikadi nyingi za zama za ujahilia lilikuwa ni watu kufuata yale waliyowakuta nayo babu zao na kushikilia na kuyanng'ang'ania mambo kwa sababu ya taasubi tu za kikabila, mambo ambayo hayakuwa na thamani wala itibari yoyote ya kielimu na kifikra.

Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hii ni kuwa katika masuala ya kiitikadi na kimaadili wingi hauwi kipimo cha kuonyesha haki. Kwani si hasha walio wengi katika watu wakawa wamepotoka kifikra na kimatendo.

AYA ZA 37 NA 38

Tunaihitimisha darsa yetu ya juma hili kwa aya za 37 na 38 ambazo zinasema:

وَمَا كَانَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ أَن يُفْتَرَىٰ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ الْكِتَابِ لَا رَيْبَ فِيهِ مِن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٣٧﴾

37. Na haiwezekani Qurani hii kuwa imetungwa, na haitoki kwa Mwenyezi Mungu. Bali inayasidikisha yaliyotangulia, na ni mfafanuo wa Kitabu kisicho na shaka ndani yake kutoka kwa Mola wa walimwengu wote.

أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّثْلِهِ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٣٨﴾

38. Je! Ndiyo wanasema ameizua? Sema:" Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite (kukusaidieni) muwawezao isipokuwa Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi mnasema kweli.

Quran tukufu imetoa changamoto mara kadhaa ya kuthibitisha kuwa ni maneno ya mbinguni na kuonyesha kwamba si majini wala binaadamu walio na uwezo wa kuleta kitu kilicho mfano wake.

Bali ikafika mbali zaidi na kueleza kwa kujiamini kwamba, si kuleta mfano wa Quran yote au moja ya sura zake tu, bali kama wana uwezo, wapinzani wa muujiza huo wa Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu na walete walau aya moja tu iliyo mfano wa Quran.

Hata hivyo licha ya maadui na wapinzani wengi ambao Uislamu na Quran imekabiliana nao katika kipindi cha karne 14 zilizopita, hadi leo hii hakuna aliyethubutu kujitokeza kukabiliana na changamoto hiyo iliyotolewa na kitabu hicho cha Mwenyezi Mungu.

Magwiji wa kila zama wa nahau na balagha pamoja na fani nyinginezo za lugha ya kiarabu wasio waislamu, wote hao wameshindwa kubuni walau aya moja tu iliyo na sifa za aya ya Quran tukufu.

Wapenzi wasomaji quran tukufu ina miujiza na maajabu ya aina kwa aina, machache kati ya hayo ni haya yafuatayo:

Kwanza : ni utamu wa maneno yake na mvuto wa ajabu yalionao, kiasi kwamba hata kama mtu ataisoma mara elfu hahisi kuwa amesoma kitu cha kushosha na kilichopitwa na wakati. Si hayo tu, bali vibwagizo vya maneno yake, mianguko yake ya sauti na mahadhi yake yamejipambanua na maneno mengine yote ya lugha ya kiarabu.

Ujumuishaji wa quran wa kila kipengele cha maisha ya mwanadamu vikiwemo vya masuala ya mtu binafsi, familia, jamii, masuala ya kisheria, kiuchumi, kisiasa na kiakhalqi ni wa namna ambayo, ni muhali kwa mwanaadamu yeyote kuweza kuufikia upeo wake.

Wapenzi wasomaji darsa ya 313 imefikia tamati. Tunamwomba Mwenyezi Mungu aturuzuku kuisoma quran usiku na mchana, kwa namna airidhiayo yeye, na kutuwafikisha kutekeleza kivitendo yaliyomo ndani yake ili tuweze kupata uombezi wa quran siku ya kiyama. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 39-44

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Karibuni katika mfululizo huu wa 314 wa darsa ya quran, tukiwa tunaendelea kuizungumzia sura ya 10 ya Yunus.

AYA ZA 39 NA 40

Tunaianza darsa yetu kwa aya za 39 na 40 ambazo zinasema:

بَلْ كَذَّبُوا بِمَا لَمْ يُحِيطُوا بِعِلْمِهِ وَلَمَّا يَأْتِهِمْ تَأْوِيلُهُ كَذَٰلِكَ كَذَّبَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الظَّالِمِينَ ﴿٣٩﴾

39. Bali wameyakanusha wasiyoyaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Namna hivi walikanusha waliokuwa kabla yao. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa madhalimu hao.

وَمِنْهُم مَّن يُؤْمِنُ بِهِ وَمِنْهُم مَّن لَّا يُؤْمِنُ بِهِ وَرَبُّكَ أَعْلَمُ بِالْمُفْسِدِينَ ﴿٤٠﴾

40. Na miongoni mwao wapo wanaoiamini. Na miongoni mwao wapo wasioiamini. Na Mola wako anawajua vyema waharibifu.

Katika darsa iliyopita tulisema kuwa kutokana na dhana tu na bila kuwa na ushahidi mushirikina na makafiri walikuwa walivurumiza tuhuma kuwa Quran ni maneno ya Bwana Mtume na kukanusha kwa kudai kuwa kitabu hicho kitukufu hakina uhusiano wowote na Mwenyezi Mungu.

Aya tulizosoma zinasema kuwa kinachofanywa na makafiri na mushirikina hao ni kukariri yale yaliyosemwa na wenzao waliotangulia, kwani mitume wa kabla ya Nabii Muhammad(s.a.w.w) walikabiliwa na tuhuma sawa na hizo.

Hii ni pamoja na kuwa ukadhibishaji wao hauna mashiko yoyote ya kielimu, hivyo kitendo chao hicho ni sawa na kujidhulumu nafsi zao na pia ni dhulma kwa dini ya haki ya mbinguni na mitume waliotumwa na Allah kuitangaza dini hiyo kwa watu.

Lakini katika upande mwingine, kuna watu wanaoitambua na kuiamini haki, na hivyo, kama tulivyowahi kuashiria mara kadhaa, ndivyo alivyokadiria Allah s.w.t, kwamba: kila mtu kwa hiyari mwenyewe aamue ima kuwa muumini au kafiri. Baadhi ya yale tunayojifunza kutokana na aya hizi ni kuwa chanzo cha ukafiri, ukanushaji na ukadhibishaji haki ni kukosa utambuzi wa kuielewa haki hiyo. Kwani wale wanaokusudia kwa dhati kuitafuta na kutaka kuijua haki hufika mahali wakaitambua risala ya tauhidi waliyokuja nayo Mitume wa Mwenyezi Mungu na wakaiamni.

Aidha aya zinatuelimisha kuwa kuyakanusha na kuyapa mgongo mafundisho ya manabii wa Allah ndiyo chanzo cha dhulma na ufisadi tunaoushuhudia ulimwenguni.

AYA YA 41

Ifuatayo sasa ni aya ya 41 ambayo inasema:

وَإِن كَذَّبُوكَ فَقُل لِّي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ أَنتُم بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٤١﴾

41. Na wakiendelea kukukadhibisha sema: Mimi nina amali yangu na nyinyi mna amali yenu. Nyinyi hamna dhima kwa niyatendayo, wala mimi sina dhima kwa mnayotenda nyinyi.

Aya hii inabainisha jinsi ya kuamiliana na makafiri na wapinzani wa haki na kueleza kuwa jukumu lenu nyinyi kwa watu hao ni kuwaonyesha tu na kuwatambulisha uongofu; si kuwalazimisha wao waufuate kwa nguvu, wala nyinyi kutaka kuwakumbatia wao ili kiwe kishawishi cha kuwafanya wavutiwe na haki.

Ikiwa wao watakuwa wamekaidi na kukataa kata kata kuiamini haki, dhima yenu kwao imeshaondoka, kwani imani ni jambo la moyoni na la hiyari, na hivyo watu hao ni kwamba wameshaamua hawataki kuielewa haki, na kama wameielewa, basi hawataki kuiamini.

Katika suala hili hutokezea baadhi ya Waislamu wakahisi kuwa labda ikiwa wao wenyewe wataamua kuacha kushikamana na baadhi ya mambo ya msingi ya dini huenda hilo linaweza kuwavutia wale wanaowalingania waikubali haki. Hali ya kuwa mtu hana haki yoyote ya kufanya hivyo kwa sababu tu ya kutaka kupata idadi kubwa zaidi ya watu walioukubali uongofu.

Na ndiyo maana tunaona katika aya hizi Bwana Mtume Muhammad saw anatakiwa awaambie makafiri kwamba, madamu nyinyi hamko tayari kuyaamini maneno yangu, tambueni kuwa mimi najiweka mbali kabisa na matendo yenu na wala sina dhima wala jukumu lolote kwenu.

Funzo mojawapo tunalolipata katika aya hii ni kuwa Uislamu ni dini ya hoja, maadili na msimamo. Inatangaza na kuweka wazi msimamo wake; na kama ambavyo haimlazimishi mtu kuifuata, ndivyo vivyo hivyo nayo haiko tayari kulegeza msimamo katika misingi ya mafundisho yake.

AYA ZA 42, 43 NA 44

Darsa ya 314 inahitimishwa na aya za 42, 43 na 44 ambazo zinasema:

وَمِنْهُم مَّن يَسْتَمِعُونَ إِلَيْكَ أَفَأَنتَ تُسْمِعُ الصُّمَّ وَلَوْ كَانُوا لَا يَعْقِلُونَ ﴿٤٢﴾

42. Na wako miongoni mwao wanaokusikiliza. Je wewe unaweza kuwafanya viziwi wasikie ijapokuwa hawafahamu?.

وَمِنْهُم مَّن يَنظُرُ إِلَيْكَ أَفَأَنتَ تَهْدِي الْعُمْيَ وَلَوْ كَانُوا لَا يُبْصِرُونَ ﴿٤٣﴾

43. Na wapo miongoni mwao wanaokukodolea macho. Je wewe utawaongoa vipofu ingawa hawaoni?

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٤﴾

44. Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu chochote; lakini watu wenyewe wanajidhulumu nafsi zao.

Katika kuendeleza yale yaliyokuja katika aya zilizotangulia kuhusu jinsi wapinzani wa haki walivyokuwa wakiamiliana na Bwana Mtume, aya hizi zinasema, si hasha baadhi ya wapinzani hao wakawa ni watu wanaohudhuria vikao vya Bwana Mtume, wakimwona kwa macho yao mtukufu huyo na kuyasikia yale anayoyasema; lakini yote hayo hayazipi athari yoyote nafsi zao. Na sababu ni kuwa yote hayo waliyokuwa wakiyashuhudia na kuyasikia hayakuwa yakipenya kweli kwenye masikio yao na kukita kwenye fikra na nyoyo zao.

Kana kwamba watu hao walikuwa ni vipofu wasioona au viziwi wasioweza kusikia chochote. Kimsingi ni kwamba kitu kinachompambanua mwanadamu na mnyama ni uwezo wake wa kufikiri na kutafakari, vinginevyo mnyama naye anaona na anasikia, bali hata uwezo na nguvu zake zake za kuona na kusikia ni kubwa zaidi kuliko za binaadamu. Hivyo linalomstahikia mwanadamu ni kuyatia kwenye tafakuri yale ayaonayo na ayasikiayo, kwa kupambanua la haki na la batili, kisha kushikamana na lile la haki na kujiweka mbali na lile la batili. Funzo mojawapo tunalolipata kutokana na aya hizi ni kuwa kuona na kusikia, ni utangulizi wa kutafakari na kuifahamu haki.

Wapenzi wasomaji darsa yetu ya juma hili inaishia hapa. Tunamwomba Allah atuwafikishe kuitambua haki na kuifuata, na kuielewa batili na kuiepuka. Amin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

SURAT YUNUS 45-49

Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwafikisha kukutana tena katika darsa yetu hii.

AYA YA 45

Sura ya 10 ya Yunus ndiyo tunayoizungumzia kwa sasa, na hii ni darsa ya 315 tunayoianza kwa aya ya 45 ambayo inasema:

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ كَأَن لَّمْ يَلْبَثُوا إِلَّا سَاعَةً مِّنَ النَّهَارِ يَتَعَارَفُونَ بَيْنَهُمْ قَدْ خَسِرَ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِلِقَاءِ اللَّـهِ وَمَا كَانُوا مُهْتَدِينَ ﴿٤٥﴾

45. Na siku atakapowakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa (duniani) ila saa moja tu ya mchana. Watatambuana. Hakika wamekhasirika wale waliokanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.

Ijapokuwa makafiri wamekadhibisha na kukanusha kuwepo kwa siku ya kiyama, hata hivyo watake wasitake ni kwamba wao pia kama ilivyo kwa wanaadamu wote watafufuliwa tu na kuishuhudia siku hiyo.

Uzito wa siku hiyo utakuwa hauna mfano wake kiasi cha kuwafanya wale waliokufuru wahisi kwamba umri wao wote walioishi hapa duniani, pamoja na kipindi chote cha maisha ya barzakh huko makaburini, ulikuwa ni sawa na muda wa saa moja tu ya mchana mzima.

Pamoja na wanaadamu kupitiwa na miaka bali pengine karne nyingi za baada ya kufa kwao, lakini watahisi kana kwamba wameamka tu kutoka kwenye usingizi wa kawaida. Katika hali hiyo watu watatambuana vizuri na wala hawatokumbwa na usahaulifu.

Ni wazi kwamba katika lahadha hiyo wale ambao hapa duniani walikanusha kuwepo kwa kiyama, wakati kweli itakapodhihiri na kujiona wamesimamishwa katika uwanja wa siku ya kiyama, hapo ndipo watakapobaini kuwa wao ni watu waliokhasirika kwa kufika mahala hapo wakiwa mikono mitupu, huku kukiwa hakuna tena fursa ya kurudi walikotoka.

Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kuwa umri tunaoishi hapa duniani ni mfupi, kiasi kwamba siku ya kiyama mtu atajuta na kujihisi amekhasirika na kupata hasara kubwa kwa kutoitumia fursa hiyo ya uhai wa kupita aliojaaliwa hapa duniani.

Halikadhalika inatubainikia kutokana na aya hii ni kuwa hasara ya kweli ni ile ya mtu kuhitari na kufadhilisha starehe za kupita za hapa duniani kwa raha na neema za milele za huko akhera.

AYA YA 46

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 46 ambayo inasema:

وَإِمَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِلَيْنَا مَرْجِعُهُمْ ثُمَّ اللَّـهُ شَهِيدٌ عَلَىٰ مَا يَفْعَلُونَ ﴿٤٦﴾

46. Na vyovyote vile, tukikuonyesha baadhi ya tunayowaahidi au tukakufisha kabla yake, marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni shahidi wa wanayoyafanya.

Aya hii inamliwaza Bwana Mtume na waumini kwa kuwaambia kuwa ikiwa mnaona Mwenyezi Mungu hawashushii adhabu kamili makafiri hapa duniani ni kwa sababu malipo hasa ya waja iwe ni adhabu ya moto au neema ya pepo wataipata huko akhera pale wote watakaporejea kwa Mola wao.

Hata hivyo sio kwamba adhabu ya kila ovu itasubiri huko akhera tu bali baadhi ya adhabu zitawashukia wakanushaji hapo papa hapa duniani, nawe Mtume utashuhudia kwa macho yako; na baadhi ya adhabu zitawashukia hata baada ya wewe kuaga dunia.

Funzo mojawapo tunalopata katika aya hii ni kuwa waislamu wasikate tamaa kuona muda unapita bila makafiri kupatwa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mtimizaji wa ahadi anayotoa, tabaan kulingana na hikima yake mutlaki.

AYA YA 47

Ifuatayo sasa ni aya ya 47 ambayo inasema:

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ فَإِذَا جَاءَ رَسُولُهُمْ قُضِيَ بَيْنَهُم بِالْقِسْطِ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٤٧﴾

47. Na kila umma una Mtume. Alipowajia Mtume wao walihuhukumiwa baina yao kwa uadilifu; wala hawakudhulumiwa.

Mitume wa Mwenyezi Mungu walikuwa katika makundi mawili. Wale waliopewa vitabu na sheria, na wale ambao walikuwa wafikishaji na walinganiaji tu wa risala za Mitume waliopewa vitabu na sheria. Kutokana na aya za quran inabainika kuwa katika kipindi cha historia, na katika umma na kaumu mbali mbali za wanaadamu wamekuwepo watu waliokuwa wakiwafikishia wanadamu wenzao mafundisho ya mitume na yale yaliyokuja katika vitabu vya mbinguni.

Na ujumbe mkuu katika risala za manabii ulikuwa ni kusimamisha haki na uadilifu na kupambana na dhulma na uonevu. Na hivyo siku ya kiyama Allah sw ataawafufua watu wa kila kaumu na umati pamoja na Mtume wao na kuwasimamisha na kuwahukumu kwa uadilifu katika mahakama ya siku hiyo ya malipo.

Funzo mojawapo tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa: hakuna uma au kaumu yoyote ambayo Mwenyezi Mungu ameiwacha vivi hivi bila ya kuhakikisha imefikiwa na ujumbe wa mafundisho ya Mitume wake.

AYA ZA 48 NA NA 49

Tunaihitimisha darsa yetu kwa aya za 48 na na 49 ambazo zinasema:

وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾

48. Na wanasema: Ni lini ahadi hii ikiwa mnasema kweli?

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ لِكُلِّ أُمَّةٍ أَجَلٌ إِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَلَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٤٩﴾

49. Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao waliowekewa. Ukifika muda wao hawakawii saa moja wala hawatangulii.

Makafiri ambao waliamua kukanusha hakika ya kuwepo kwa siku ya kiyama waliamua kuzusha visingizio vya kila aina alimradi kuutia shaka uhakika huo.

Hivyo wakaibuka na suali kwamba ikiwa ni kweli kiyama kitatokea na wewe Muhammad unayoyasema ni kweli kuhusu hilo, tuambie basi kujiri kwake kutakuwa lini hasa! Walizusha hoja hiyo ilhali uhakika wa kutokea jambo haushurutishi kujua wakati halisi wa kutokea kwake. Mfano wa hili ni sawa na mauti.

Kila mmoja wetu ana hakika kuwa iko siku ataiaga dunia tu, lakini hakuna yeyote kati yetu ajuaye ni lini hasa atafikwa na mauti. Kwa upande wa Bwana Mtume, naye pia kupitia wahyi alioushushiwa na Mola wake aliwapa khabari watu wa umati wake kwamba baada ya kumalizika dunia itawadia siku ya Kiyama, hata hivyo Allah s.w.t hakumbainishia Mtume wake ni wakati gani hasa litajiri tukio hilo kubwa kabisa la kutikisa nyoyo.

Baadhi ya mafunzo tunayoyapata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume walikuwa ni waja wateule wanaozungumza na watu kwa uwazi na ukweli mtupu; na hivyo wakiwaeleza bayana kuwa binafsi hawana nguvu na uwezo usio wa kawaida wala mamlaka ya kujiamulia kupata manufaa fulani au kujilinda na kujiepusha na shari yoyote ile ila kwa uwezo na idhini ya Allah s.w.t

Wapenzi wasomaji, kwa haya machache tunaifunga darsa hii ya 315. Inshaallah Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoyakinisha kiimani juu ya kuwepo kwa siku ya kiyama kutokana na amali zao na matendo yao.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh


3

4

5